HOTUBA YA WAZIRI
WA FEDHA
MHESHIMIWA BASIL P. MRAMBA (MB.),
AKIWASILISHA KATIKA BUNGE MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI
KWA MWAKA 2004/05
UTANGULIZI:
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge likubali
kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali katika mwaka
wa fedha wa 2004/05. Takwimu
zinazoelezea kwa undani Bajeti hii ziko kwenye vitabu vinne (4) ambavyo ni
sehemu ya Bajeti hii. Kitabu cha kwanza
kinahusu makisio ya mapato, Kitabu cha pili na cha tatu vinahusu makisio ya
matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara, Mikoa pamoja na Halmashauri za Miji na
Wilaya. Kitabu cha nne kinaelezea
makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara, Mikoa, na Halmashauri. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa
mwaka 2004/05.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kutoa
shukrani zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine
kufanikisha matayarisho ya bajeti, hususan Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge
na Kamati za Kisekta; kwa kazi zao nzuri za kuchambua makisio yote kwa
kina. Ushauri uliotolewa na Kamati hizo
umesaidia sana kuboresha bajeti ninayowasilisha leo.
3. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya bajeti hii yamehusisha wadau
wengi ndani na nje ya Serikali. Napenda kuwashukuru wote waliochangia ambao ni
pamoja na wafanyakazi wa Wizara mbalimbali, Idara zinazojitegemea, Mikoa na
Halmashauri zote za Wilaya, Miji, Manispaa na Jiji, Asasi zisizo za Kiserikali
pamoja na sekta binafsi, kwa michango yao iliyosaidia kufanikisha utayarishaji
wa bajeti hii. Aidha, napenda kuchukua
nafasi hii kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha
Miswada na Nyaraka mbalimbali za Sheria ambazo ni sehemu ya bajeti hii. Nawashukuru pia wenzangu wa Wizara ya Fedha, Manaibu
Waziri, Mheshimiwa Abdisalaam Issa Khatibu (Mb.) na Mheshimiwa Dr. Festus Limbu
(Mb.); Makatibu Wakuu Bw. Gray S. Mgonja na Bw. Peniel M. Lyimo, Manaibu Katibu Mkuu Bw. Ramadhani Khijjah na
Bw. Wilfred Nyachia, Wakuu wa Idara, na wafanyakazi wengine wote kwa michango
yao iliyowezesha bajeti hii kukamilika.
Vile vile, namshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha kwa
wakati hotuba hii, vitabu vya bajeti pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu
bajeti hii. Mwisho, nawashukuru wale wote waliowasilisha kwangu mapendekezo yao
ya kodi mpya au ya kurekebisha kodi zilizopo na pia wataalam wote waliotoa
ushauri kuhusu sera na namna ya kutoza kodi mbali mbali nchini, pamoja na
matumizi ya mapato yetu ambapo mengi yamezingatiwa katika kuandaa bajeti hii.
4. Mheshimiwa Spika, mwaka huu wa fedha tumeshuhudia kuundwa rasmi
kwa Bunge la Afrika. Napenda kuchukua
fursa hii kuwapongeza Wabunge wote waliochaguliwa kutuwakilisha katika Bunge
hilo ambao ni Mhe. Gertrude
Mongella, Mbunge wa Ukerewe, Mhe. Dr. William F.
Shija, Mbunge wa Sengerema, Mhe. Dr. Amani W. A. Kabourou,
Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Dr.
Remigius Edington Kissassi, Mbunge wa Dimani Zanzibar, na Mhe. Athumani Janguo,
Mbunge wa Kisarawe. Aidha, pongezi za
pekee nazitoa kwa Mhe. Mongella kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa
5. Napenda kuchukua fursa hii pia kumpongeza Mhe. Arcado Ntagazwa,
Mbunge wa Muhambwe, kwa kuteuliwa kwake kuwa Rais wa Baraza la Kimataifa la
Mazingira. Naamini kwamba uteuzi huo si
wa kubahatisha bali unaonyesha imani waliyo nayo Wajumbe wa Baraza hilo kwa
Mhe. Ntagazwa na kwa nchi yetu. Vile
vile, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Sophia Simba, Mbunge Viti Maalum na pia
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Maendeleo ya Jamii kwa kuteuliwa
kuiwakilisha Tanzania katika Baraza la Wabunge wa SADC, yaani “SADC
Parliamentary Forum”. Narudia tena kuwapongeza wote na ninawatakia kazi njema
katika majukumu hayo mapya.
6. Mheshimiwa Spika, tunakumbuka kwamba, tarehe 30 Mei, mwaka huu
kulifanyika uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Bariadi Mashariki, Mkoa wa
Shinyanga, ambao umemrudisha Bungeni Mheshimiwa Danhi Makanga kwa kishindo na
kwa tiketi ya CCM. Uchaguzi huo
ulifuatia mtafaruku baina yake na chama chake cha UDP ambapo ilibidi akihame
chama hicho na kurejea tena kwenye Chama cha Mapinduzi. Nampongeza Mheshimiwa Makanga kwa ushindi
wake katika uchaguzi huo, na pia wananchi wa Bariadi Mashariki kwa kutorudia
kosa la kutokiri umaarufu wa CCM na kukubalika kwa Mheshimiwa Makanga miongoni
mwa wapiga kura wa Bariadi Mashariki. Aidha, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka
kwamba katika mwaka huu wa fedha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, alimteua Mhe. Makongoro Nyerere kuwa Mbunge. Napenda pia kumpongeza Mhe. Makongoro Nyerere
kwa uteuzi huo na kwa kurejea kwenye Chama alicho asisi hayati baba yake ambaye
ni Baba wa CCM na wa Taifa letu.
7. Mheshimiwa Spika, matukio mengine muhimu yaliyotokea mwaka huu
wa fedha ni pamoja na kuteuliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na
pia Mtanzania mwenzetu, Profesa Anna Tibaijuka, kuwa Makamishna katika Kamisheni ya Afrika iliyoundwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Mhe.
Tony Blair. Kamisheni hii ina
jukumu la kutathmini vikwazo ambavyo vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya
Bara la Afrika na kupendekeza nini kifanywe kuondokana navyo. Uteuzi wa Rais Mkapa umetokana na juhudi zake
za kuyapa kipaumbele matatizo ya Bara la Afrika, hususan matatizo ya maendeleo
na umaskini uliokithiri pamoja na ufahamu wa Rais Mkapa wa masuala ya
utandawazi. Uzoefu wake kama
Rais wa nchi ya Kiafrika inayojizatiti kupiga vita umaskini na kuleta maendeleo
ya wananchi wake unatambulika duniani.
Sote tunajivunia uteuzi huo wa Rais Mkapa na wa Profesa Tibaijuka ambae
ni Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi duniani. Tunawapongeza Watanzania hao kwa kazi nzito
wanazoufanyia ulimwengu na heshima kubwa wanayo iletea nchi yetu katika
kutekeleza majukumu hayo mazito mazito.
UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2003/04:
8. Mheshimiwa Spika,
tathmini ya hali ya uchumi katika mwaka 2003/04 inaonyesha maendeleo ya
kuridhisha, licha ya ukame ulioikumba nchi yetu. Takwimu za awali zinaonyesha kwamba uchumi
ulikua kwa asilimia 5.6 mwaka 2003 badala ya lengo letu la asilimia 6.3. Kasi ya mfumuko wa bei iliongezeka kidogo
kutoka asilimia 4.0 mwezi Julai 2003 hadi asilimia 4.6 mwezi Machi 2004. Mfumuko wa bei ulitokana na upungufu wa
chakula kutokana na ukame, pamoja na ongezeko kubwa la bei ya mafuta ya
petroli. Akiba ya fedha za kigeni
mwishoni mwa Machi, 2004 ilifikia uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu kutoka
nje kwa kipindi cha zaidi ya miezi minane ambayo ni zaidi ya lengo la miezi
sita.
9. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Bajeti ya
Serikali ya mwaka 2003/04, umekuwa wa kuridhisha, licha ya dharura iliyoletwa
na ukame, hasa katika kuongeza mahitaji ya fedha ya bajeti kwa ajili ya kununua
na kusambaza chakula, pamoja na kulazimika kutoa ruzuku kwa TANESCO kwa ajili
ya kununulia mafuta ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme, na kununua umeme
wa mtambo wa IPTL.
10. Katika bajeti ya mwaka 2003/04 Serikali ililenga kukusanya mapato
ya ndani yasiyopungua asilimia 13.3 ya Pato la Taifa. Ili kufanikisha lengo hili, Serikali
ilikusudia kutekeleza hatua kadhaa za kurekebisha mfumo na utawala wa
kodi. Marekebisho hayo yalilenga kupanua
wigo wa kodi, kuongeza uwajibikaji kwa watoza kodi na walipa kodi, kuondoa kodi
za kero, kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuongeza ufanisi wa
utendaji katika Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Aidha Sheria mpya ya Kodi ya Mapato iliwasilishwa na kupitishwa Bungeni
mwezi Aprili mwaka huu wa fedha.
11. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya
mwaka huu wa fedha yaani kuanzia Julai, 2003 hadi Aprili, 2004 ukusanyaji wa
mapato ya ndani umevuka lengo kwa kila mwezi. Aidha, misaada ya bajeti kutoka kwa Nchi
Wafadhili, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Umoja wa Ulaya, ilivuka
lengo. Sehemu kubwa ya misaada hiyo
ilipatikana katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa fedha na hivyo kutupa uwezo
zaidi wa kumiliki bajeti hiyo.
Inatarajiwa kwamba malengo ya mapato ya ndani na misaada ya bajeti kwa
mwaka huu yatafikiwa ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha.
12. Mheshimiwa Spika, mapato halisi ya ndani kwa
kipindi cha Julai, 2003 hadi Machi, 2004 yalifikia shilingi trilioni moja,
bilioni themanini na tisa, milioni mia mbili sitini na mbili (1,089,262
milioni) sawa na asilimia 3.7 au shilingi milioni 38,396 zaidi ya makisio
ya bajeti ya shilingi trilioni moja, bilioni hamsini, mia nane sitini na sita
milioni (1,050,866 milioni). Kodi ya
VAT kwenye mauzo ya ndani ya nchi ilikadiriwa kuwa shilingi milioni 142,242
katika kipindi hicho, lakini makusanyo halisi yalifikia shilingi milioni 148,632,
ambayo ni ziada ya shilingi milioni 6,390 au asilimia 4.5 juu ya makisio
kwa kipindi hicho. Kwa upande wa Kodi
ya Mapato, makusanyo halisi yalifikia shilingi milioni 256,888
ikilinganishwa na makisio ya shilingi 227,382 milioni, sawa na ziada ya shilingi
milioni 29,506 au asilimia 13 juu ya makadirio. Ukusanyaji wa Ushuru wa Forodha
ulifikia shilingi milioni 95,239 ukilinganishwa na makadirio ya shilingi
milioni 93,562, na hivyo kuwa na ziada ya shilingi milioni 1,677 sawa na
asilimia 1.8 juu ya makadirio.
Aidha, mapato yasiyo ya kodi (non-tax revenue) yakijumuisha mapato
ya Wizara, Idara mbali mbali na Mikoa, yalifikia shilingi milioni 87,368 ikiwa
ni chini ya lengo la shilingi milioni 96,951.
13. Mheshimiwa
Spika, sababu kuu zilizochangia kuongezeka kwa Mapato ya
Serikali ni pamoja na usimamizi na utawala bora wa ukusanyaji wa kodi, hasa
Kodi ya Mapato na Kodi ya Ongezeko la Thamani, (VAT). La muhimu zaidi ni zile hatua tulizochukua kudhibiti ukwepaji wa kodi katika
biashara ya mafuta ya petroli.
14. Kwa muhtasari matokeo mazuri ya hatua
zilizochukuliwa na Serikali kwa lengo la kuongeza
ukusanyaji wa mapato ya Serikali ni pamoja na haya yafuatayo:-
Marekebisho ya viwango vya ushuru wa forodha ambayo yameipatia Serikali mapato
ya shilingi milioni 1,717 kwa kipindi cha Julai 2003 hadi Machi 2004
ikilinganishwa na lengo la shilingi milioni 133.8 kwa mwaka 2003/04. Hii ni sawa na ziada
ya asilimia 1,183.
Pili:
Marekebisho ya Ushuru wa bidhaa katika bidhaa
mbali mbali, yaliyoipatia Serikali mapato ya ziada ya shilingi milioni 758.5
katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2003.
Tatu:
Kupunguzwa kwa ushuru wa bidhaa kwa gesi ya kupikia (LPG) kutoka
shilingi 228 hadi shilingi 114 kwa kilo, kulikoongeza uagizaji wa gesi hiyo
kwa asilimia 52.6
Nne:
Msamaha wa kodi uliotolewa kwa mitambo ya kuchimbia Visima vya Maji ambao umeonyesha matokeo mazuri. Mitambo ya aina hii iliyoagizwa imeongezeka
kwa asilimia 68 kutoka shilingi milioni 12,602.1 mwaka 2002 hadi shilingi
milioni 21,187.8 mwaka 2003.
Tano:
Nafurahi
kuliarifu Bunge hili tukufu kwamba hatua zilizochukuliwa kudhibiti ukwepaji wa kodi katika biashara ya mafuta ya petroli zimezaa matunda
yaliyotarajiwa. Jumla ya shilingi milioni
226,036 zimekusanywa kwa kipindi cha Julai 2003 hadi Aprili 2004,
kulinganisha na lengo la shilingi milioni 208,002. Kiasi hiki ni asilimia
25 zaidi ya kodi za mafuta zilizokusanywa katika kipindi
Sita:
Nasikitika kwamba kodi
ya mauzo ya nje ya asilimia 15 kwa ngozi ghafi
iliyoanzishwa mwaka huu wa fedha ili kuvutia usindikaji wa bidhaa hiyo hapa
nchini, haijawa na matokeo yaliyo kusudiwa, kwani mapato yaliyopatikana
katika nusu mwaka ya kwanza ni shilingi milioni 413 kulinganisha na lengo la
shilingi milioni 1,080 katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2003. Eneo hili litachunguzwa zaidi mwaka huu kwa lengo la kuwezesha kusindika ngozi zote hapa nchini, kwa
manufaa ya wafugaji na uchumi wa taifa kwa ujumla.
15. Mheshimiwa Spika, matokeo kamili ya hatua mbali
mbali zilizochukuliwa na Serikali kuongeza mapato
yatafahamika baada ya mwisho wa mwezi huu, lakini mifano michache
niliyoielezea ni ushahidi tosha kwamba sera nzuri, utawala bora na usimamizi
imara katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, huongeza mapato. Serikali itaendelea
kusimamia mambo haya na mengine mapya ambayo nitaelezea hivi
punde. Aidha, Sheria mpya ya Kodi ya
Mapato iliyotungwa na Bunge hili tukufu mwezi Aprili mwaka huu itaanza kutumika
mwezi Julai 2004 kama ilivyo pangwa.
Zoezi la kutayarisha Kanuni za Sheria hii pamoja na maelezo ya kina ya
vifungu mbali mbali vya sheria hiyo linaendelea vizuri. Sheria hiyo inatarajiwa kupanua wigo wa kodi
na kuanzisha utaratibu mpya wa walipa kodi kujikadiria kodi wenyewe. Aidha, Idara ya Walipa Kodi Wakubwa katika
Mamlaka ya Mapato Tanzania imeimarishwa na malalamiko yaliyokuwepo ya walipa
kodi hao yamepungua kwa kiwango kikubwa.
16. Mheshimiwa Spika, kama
nilivyo kwisha elezea hapo awali, mwenendo wa upatikanaji wa misaada na mikopo
nafuu umekuwa wa kuridhisha kwa mwaka huu wa fedha wa 2003/04. Katika kipindi cha Julai 2003 hadi Mei 2004
jumla ya misaada na mikopo kwa ajili ya bajeti ya
kawaida ilifikia shilingi milioni 490,253 sawa na asilimia 121 ya makisio
tuliyojiwekea ya shilingi milioni 405,047. Fedha hizi pia zilitolewa mapema
ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo hadi kufikia Desemba 2003, asilimia 90
ya fedha hizo ilikwisha patikana na hivyo kutoa mchango mkubwa kwa Serikali
katika kukabiliana na matatizo ya kibajeti yaliyotishia kujitokeza, kutokana na
ukame. Mafanikio yote haya ni matokeo ya
utekelezaji wa mkakati wetu wa kupokea misaada na mikopo (Tanzania Assistance
Strategy – TAS) na wa kurahisisha utawala wa misaada (aid harmonisation) ili
kupunguza urasimu na umimi kama ilivyo kuwa huko nyuma. Utaratibu huu pamoja na ule wa kujadiliana na
Wafadhili katika vikao vya pamoja na pia kujadili matumizi ya bajeti hadharani
kila mwaka umeimarisha sana imani ya Wafadhili kwa Tanzania kuliko nchi nyingi
Afrika.
17. Pamoja na uhusiano huo unaoivumisha Tanzania
katika duru za Wafadhili, bado tunalo tatizo la kuimarisha zaidi uhuru wa
Tanzania kuelekeza misaada hiyo kikamilifu na bado liko tatizo kubwa zaidi kuwa
nchi karibu zote zingali bado kutimiza ahadi zao za kuongeza misaada chini ya
makubaliano ya Monterrey, Mexico ili ifikie asilimia 0.7 au zaidi ya Pato la
Taifa la nchi tajiri katika kutekeleza mkakati wa kuondoa umaskini duniani
karne hii (Millenium Development Goals).
Tunazipongeza hasa Serikali za Uingereza na Ufaransa kwa kuongoza mijadala
ya suala hili kwenye vikao vya kimataifa na hata kupendekeza kuanzishwe mfuko
maalum wa kimataifa wa kuziwezesha nchi maskini sana duniani kupata misaada
zaidi ya kupambana na umaskini, jambo ambalo baadhi ya wakubwa wenzao
wanalichenga au wanalikwepa kwa kuanzisha mifuko yao ya aina isiyo lenga
kikamilifu kukabiliana na umaskini kwa misingi iliyo kubalika tayari duniani.
18. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendeleza majadiliano na Wafadhili mwaka ujao wa fedha kuhakikisha
kuwa misaada na mikopo nafuu inaelekezwa katika maeneo yanayolenga kutekeleza
dira na matakwa ya nchi (complete ownership of aid utilization) ili kukuza
uchumi, hususan kwenye kilimo, elimu, viwanda, na miundo mbinu, hasa madaraja
na barabara za lami za kuunganisha wilaya, mikoa, mikoa na mikoa, maeneo ya
uzalishaji mkubwa na baina yetu na nchi majirani. Maeneo haya ndiyo yatatuondoa kwenye ujinga
na umaskini kwa haraka zaidi kuliko mengineyo ambayo ni ya ulaji (consumption)
kuliko uzalishaji (production). Kupanga ni kuchagua
pale panapo weza kulivusha taifa letu haraka haraka. Tutaweza kulima kwa wingi, kusindika mazao
hayo kwa wingi na kusafirisha mazao ya kilimo na viwanda hadi nchi jirani, za
kanda na ng’ambo kwa barabara za kuaminika hadi bandarini au nchi majirani,
hasa kaskazini, magharibi na kusini mwa Tanzania. Na hatuwezi kufanya hayo na mengineyo bila
kuwa na wasomi wa nyanja zinazo endana na ulimwengu huu wa elimu ya juu,
sayansi, na utandawazi.
19. Mheshimiwa Spika, kwa
niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kushukuru nchi Wafadhili, Jumuiya
ya Ulaya, pamoja na Mashirika yote ya Kimataifa yaliyotoa fedha kusaidia bajeti
yetu kwa mwaka huu wa fedha. Nchi na
mashirika hayo ni Australia, Austria, Canada, China, Denmark, Finland,
Hispania, Ireland, Italia, Japan, Marekani, Norway, Sweden, Ubeligiji,
Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uswisi Benki ya Maendeleo ya Afrika
(ADB), BADEA, Benki ya Dunia, EIB,
Jumuiya ya Ulaya, Kuwait Fund, NDF, OPEC Fund na Taasisi za Umoja wa
Mataifa.
20. Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea kudhibiti ukuaji holela wa madeni chini ya Mkakati wa Madeni wa
Taifa. Sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada ya Mwaka 1974 pamoja na marekebisho
ya mwaka 2003 inaendelea kutekelezwa kikamilifu. Kwa sasa, mikopo inatafutwa
kutoka vianzio vyenye masharti nafuu sana na kuelekezwa kwenye maeneo muhimu ya
kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
Aidha, udhamini wa Serikali kwa mikopo ya nje umesitishwa na hakuna
ruksa kwa mtumishi au mamlaka yoyote kukopa kwa niaba ya Serikali au kufikia
mapatano yanayo husu fedha bila idhini rasmi ya Waziri wa Fedha ambaye naye
lazima ashauriwe kwanza na Kamati iliyoundwa chini ya sheria hiyo.
21. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na juhudi za kupata misamaha ya
madeni toka nchi wanachama na zile zisizokuwa wanachama wa Kundi la Paris kwa
mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika mpango wa kuzipunguzia madeni nchi
masikini. Nchi za Kundi la Paris, isipokuwa Brazil, zimefuta sehemu kubwa ya
madeni yetu kwao, na nyingine zimeyafuta kabisa madeni hayo. Juhudi za kufanya majadiliano na Brazil
zitaendelea mwaka ujao wa fedha. Aidha,
katika mwaka huu wa fedha, tumepata msamaha wa deni kiasi cha dola za Marekani
milioni 15.1 toka Bulgaria na mazungumzo ya awali yamekamilika kwa Iran na
karibu kukamilika kwa Mfuko wa Abu Dhabi na mashirika ya kibiashara ya India
ambayo tayari imetufutia madeni ya kiserikali.
Juhudi zitaendelea kuwa na mazungumzo na nchi nyingine zinazotudai ili
zitufutie madeni kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa kwa nchi maskini sana
duniani. Majadiliano na nchi na
mashirika yasiyo ya Kundi la Paris yamekuwa magumu kwa wao kutokubali kutii
makubaliano ya Paris, suala linalo zua mijadala katika mikutano ya kimataifa
ambapo baadhi ya nchi zimeshitakiwa na mali zao kufilisiwa.
22. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa utekelezaji wa Bajeti ya mwaka huu wa
fedha unaonyesha kwamba kwa kiasi fulani kumekuwa na ongezako la ufanisi na
udhibiti wa matumizi, hasa katika Serikali Kuu, kama ilivyo kwenye ukusanyaji
wa mapato. Hii inamaanisha kwamba
Serikali inaanza kuona matunda (ingawa ya awali) ya hatua ilizochukua kwa
kipindi cha miaka nane iliyopita za kupanga na kusimamia bajeti, kuondoa
matumizi yasiyo ya lazima, na kujifunza kutumia kile tulicho nacho. Ni ishara nzuri pia kwamba sasa taratibu na
kanuni za ununuzi kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma (Na. 3 ya 2001)
zinaeleweka. Aidha, licha ya matumizi
makubwa yaliyosababishwa na ukame katika maeneo ya chakula na umeme, matumizi
ya Serikali kwa ujumla yamedhibitiwa na hakuna athari kwenye bajeti ya mwaka
huu. Serikali imehakikisha kwamba sekta
za kuondoa umaskini yaani afya, elimu, maji, barabara, kilimo, mahakama na
sheria zimepata fedha kulingana na bajeti zao, hata pamoja na kwamba kumekuwa
na matumizi makubwa kwa ajili ya TANESCO na chakula. Kigezo kikubwa cha uimara wa utekelezaji wa
bajeti ya mwaka huu ni kwamba, Serikali haikukopa kutoka Benki Kuu nje ya
lengo. Badala yake, hata kiwango cha
kukopa Benki Kuu kilichowekwa katika makubaliano na IMF chini ya mpango wa
PRGF, hakikuvukwa. Hili limewezekana
kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani, misaada ya bajeti kutoka kwa
Nchi Wafadhili ambayo pia imepita lengo kidogo, udhibiti wa matumizi ya
Serikali, na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi.
23. Mheshimiwa Spika, Katika
kipindi cha Julai 2003 hadi Machi 2004, matumizi kwa ujumla yalifikia shilingi
trilioni moja, bilioni mia saba ishirini na mbili na mia sita kumi na mbili
milioni (1,722,612 milioni) ikilinganishwa na makisio ya shilingi trilioni
moja, bilioni mia nane themanini na tisa na milioni mia mbili na saba
(1,889,207 milioni) katika kipindi hicho.
Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 422,559 ni kwa ajili ya miradi ya
maendeleo na shilingi trilioni moja, bilioni mia tatu na milioni hamsini na
tatu (1,300,053 milioni) ni kwa matumizi ya kawaida.
24. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba kutokana na hali ya ukame
ulioikumba nchi yetu mwaka 2003, Serikali ililazimika kuandaa Bajeti ya Ziada
na kupata kibali cha Bunge cha kutumia fedha kiasi cha shilingi milioni 176,784
zaidi ya zilizoidhinishwa awali katika bajeti ya 2003/04. Mahitaji ya nyongeza
ya shilingi milioni 176,784
yalikuwa ni pamoja na ununuzi na usambazaji wa chakula cha njaa, msaada kwa TANESCO kuiwezesha kumudu gharama za
uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta badala ya nguvu za maji, fidia kwa
Halmashauri za Wilaya na Miji kufuatia kufutwa kwa kodi zenye kero, mchango
katika Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali pamoja na malipo kwa Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), kufidia michango ambayo haikuwa imewasilishwa na mashirika hayo
kabla ya kubinafsishwa. Mahitaji mengine
ya ziada yalihusu maandalizi ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ukaguzi wa
dhahabu, na ununuzi wa ndege mpya ya Serikali.
Mahitaji haya yaligharamiwa kwa njia mbili; kwanza shilingi 87,250 milioni
zilitokana na mapato mapya, na pili, shilingi 89,534 milioni zilitokana na
uhamisho wa fedha ambazo zilikuwa ndani ya bajeti iliyoidhinishwa. Matumizi hayo ya nyongeza yalifanyika na
yanaendelea kufanyika kama yalivyopangwa.
25. Mheshimiwa Spika, kulingana
na mwenendo wa mapato na matumizi hadi sasa inatarajiwa kwamba kwa mwaka wote
wa fedha mapato yatavuka lengo kwa shilingi bilioni 74
na milioni 210 (74,210 milioni) sawa na asilimia 5.3 zaidi ya lengo. Inategemewa pia
kwamba misaada na mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya bajeti nayo itazidi
lengo. Mapato
kutokana na ubinafsishaji ambayo yalikadiriwa kufikia shilingi bilioni 17
(17,000 milioni), yaelekea hayatapatikana yote.
Kuhusu
malengo ya matumizi, mwelekeo ni kwamba, maeneo mengi ya matumizi ya maendeleo
na ya kawaida hususan Matumizi Mengine (OC)
hayatafikia malengo kwa sababu zilizoelezwa awali. Aidha, kuna mwelekeo wa malengo kufikiwa
katika sekta za kipaumbele za kupunguza umaskini na kukuza uchumi.
26. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuboresha usimamizi
wa fedha za umma, Serikali imechukua hatua mbalimbali ambazo ni pamoja na
kuanzisha kamati za ukaguzi wa ndani wa hesabu za Serikali katika Wizara, Idara
na Wakala zote za Serikali. Mafunzo hivi
sasa yanaendelea ya kuelimisha Wakaguzi hao kuhusu kazi za kamati hizo. Kanuni na taratibu za ukaguzi wa ndani wa
hesabu zimekamilishwa na zitachapishwa hivi punde na kutangazwa kwa wadau
wote. Aidha, Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa
(NAO) inaimarishwa kwa kupatiwa makao mapya ya ofisi, na sasa inakamilisha
mpango wa kurekebisha muundo wake wa ndani na kujaza nafasi za kazi zilizo wazi
ili kuongeza tija katika utendaji wake.
Vile vile, maandalizi yamekamilika ya kuifanyia marekebisho Sheria ya
Ununuzi wa Umma Na. 3 ya 2001 ili kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji
wa bajeti ya Serikali, hasa kuhusu miradi ya maendeleo. Marekebisho hayo yatawasilishwa katika Kikao
hiki cha Bunge kwa kusomwa kwa mara ya kwanza.
27. Mheshimiwa
Spika, katika sekta ya huduma za kibenki, kuna maendeleo ya kuridhisha
pia. Ujazi wa fedha ulidhibitiwa na
kuongezeka kwa asilimia 18.7 kati ya Julai 2003 na Machi 2004 kulinganisha na
asilimia 22.7 mwaka uliotangulia.
Mwenendo huu wa ujazi wa fedha unathibitisha kwamba tumeweza kweli
kuweka msingi thabiti wa kuzuia mfumuko wa bei.
Mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi iliongezeka kwa kiwango
kikubwa cha asilimia 41.8 kati ya Julai 2003 na Machi 2004. Ongezeko hili limetokana hasa na kampuni
kubwa hapa nchini kuacha kukopa kutoka benki za nje ya Tanzania, badala yake
sasa zinakopa kutoka benki za hapa nchini.
Hali hii inatokana na sababu kadhaa, kubwa zikiwa, kwanza kuepuka hasara
inayotokana na kubadilika kwa bei ya fedha za kigeni (exchange rate); na pili
kushuka kwa gharama za kukopa hapa Tanzania hasa kutokana na ongezeko la
ushindani katika sekta ya kibenki. Kwa
hiyo riba ya mikopo sasa imeshuka na kufikia wastani wa asilimia 13.5. Riba ya amana kwa upande mwingine imepanda na
kufikia wastani wa asilimia 4.1.
Sasa tofauti kati ya riba ya mikopo na riba ya amana imeshuka kutoka
kiwango cha 10.6 mwezi Juni 2003 hadi 9.4 mwezi Machi 2004. Ingawa riba ya amana bado ni ndogo na ile ya
mikopo bado ni kubwa, mwenendo huu unatia moyo, na ni dalili nzuri kwamba benki
sasa zimepata uelewa mkubwa wa soko la Tanzania, hasa mahitaji ya huduma za
benki, na kwamba riba zitaendelea kubadilika kulingana na mahitaji ya soko. Serikali inaamini kwamba hili litatokea kwa
kuzingatia mabadiliko ambayo Serikali imefanya ili kuboresha mazingira
yanayotoa motisha kwa benki kama vile kurekebisha Sheria ya Ardhi, kuimarisha
Kitengo cha Mahakama Kuu kinacho shughulikia Mashauri ya Biashara, kuanzisha
mifuko ya kudhamini mikopo (credit guarantee schemes), na maendeleo yanayotokea
katika miundo mbinu.
28. Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa urari wa malipo ya nje (balance of payments),
kumekua na ongezeko la uagizaji wa bidhaa kutoka nje, na pia ongezeko la
mauzo ya nje, hasa ya bidhaa zisizo asilia.
Uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi umeongezeka kwa asilimia 26.6
katika mwaka wa 2003, kutokana na mafuta ya petroli na chakula na hasa
mchele. Uagizaji wa mafuta ya petroli
umeongezeka kutokana na mahitaji makubwa ya TANESCO kwa ajili ya kuzalisha
umeme kwa kutumia mitambo ya mafuta badala ya maji. Usafirishaji nje wa bidhaa uliongezeka kwa
asilimia 16 ukitokana hasa na dhahabu, na bidhaa za viwandani. Usafirishaji wa mazao asilia uliendelea
kuzorota ingawa kuna dalili za kupanda tena kwa bei za kahawa, pamba, chai,
na korosho katika soko la dunia. Mapato
yatokanayo na utalii yaliongezeka katika mwaka huu. Kwa ujumla, kwa mara ya kwanza, urari wa
malipo ya nje ulikuwa na ziada (surplus) ya dola za Marekani 243.9 milioni. Kwa kuzingatia misamaha ya Madeni na ongezeko
la misaada na mikopo ya bajeti, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za
Marekani 1,973.2 milioni (dola bilioni moja, milioni mia tisa sabini na tatu,
laki mbili) sawa na shilingi trilioni 2.2.
Mambo Mengine Muhimu Yaliyojitokeza Katika Utekelezaji wa Bajeti ya
Mwaka 2003/04:
29. Mheshimiwa Spika, ingawa
tunapata mafanikio makubwa kutokana na marekebisho ya sera na utawala, bado
tuna kazi kubwa ya kufanya kuweza kujitegemea, na la muhimu zaidi kuondoa
umaskini. Baadhi ya mambo mengine muhimu
yaliyo jitokeza katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha unaoisha
ni:-
La
kwanza:
Bajeti ya Serikali bado
ni tegemezi kwa kiasi kikubwa, ingawa kiwango cha utegemezi
kinapungua. Katika mwaka 2003/04,
Wafadhili pamoja na Mashirika ya Fedha ya Kimataifa wamechangia asilimia 45
ya Bajeti ya Serikali ikilinganishwa na asilimia 47 mwaka 2002/03. Hivyo, ingawa mapato ya ndani yanaongezeka, pengo la kujitegemea bado
ni kubwa.
La
pili:
Pamoja na kupewa upendeleo
maalum, fedha zinazotengwa kwa sekta za kuondoa umaskini bado hazitoshelezi
mahitaji; na
La
tatu:
Ingawa ufanisi na nidhamu
Serikalini vimeongezeka kiasi, uwezo wa utendaji hasa katika maeneo ya uhasibu,
mawasiliano, utibabu n.k. bado ni duni, na ndio sababu miradi ya maendeleo
haitekelezwi kwa wakati na hata hesabu za Serikali haziko sahihi wakati wote.
MISINGI, SERA, NA MALENGO YA BAJETI YA MWAKA 2004/05
30. Mheshimiwa Spika, mfumo wa bajeti ya mwaka 2004/05 unazingatia
malengo muhimu ya uchumi ambayo ni pamoja na:-
(i)
Uchumi kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2004 na
asilimia 6.5 mwaka 2005. Kukua huku
kutatokana na kilimo, uzalishaji viwandani na uzalishaji kwa mauzo ya nje.
(ii)
Mapato ya ndani yanalengwa kufikia shilingi
trilioni moja, bilioni mia saba thelathini na tisa, na milioni mia mbili
themanini na nane (1,739,288 milioni) sawa na asilimia 13.8 ya Pato la Taifa.
(iii)
Mfumuko wa bei utakuwa katika kiwango cha
asilimia 4 ifikapo Juni 2005 na baadaye kulingana na viwango vya wastani katika
nchi tunazofanya nazo biashara na zile tunazoshindana nazo katika biashara ya
nje.
(iv)
Akiba ya fedha za kigeni inalengwa iwe katika
kiwango ambacho kinatosha kulipia mahitaji muhimu ya uagizaji wa bidhaa na
huduma kutoka nje kwa muda usiopungua miezi sita.
(v)
Kupunguza kiwango cha utegemezi wa
bajeti ya Serikali hadi asilimia 41 mwaka 2004/05.
(vi)
Kusimamia utekelezaji wa sera ya mikopo midogo
midogo (micro-finance) na mpango wa dhamana kwa wawekezaji wadogo wadogo (SMEs)
na miradi mikubwa ili kuwezesha wananchi walio wengi kujiendeleza kiuchumi kwa
kujipatia mikopo zaidi ya kibenki.
31. Mheshimiwa Spika,
muhula wa kwanza wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini umemalizika, na taarifa ya
tatu ya utekelezaji wa Mkakati huo imechapishwa. Taarifa hiyo imeainisha matokeo ya tafiti
mbalimbali zilizofanywa kuhusu hali ya umaskini nchini. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
anayesimamia Mkakati wa kuondoa umaskini ataelezea kwa kina maudhui ya taarifa
hiyo. Taarifa hiyo imebainisha, pamoja
na mambo mengine, kwamba maendeleo ya kilimo ambayo ni sekta muhimu kuliko zote
Tanzania yanakwamishwa na mambo mengi.
Vikwazo hivyo ni pamoja na ukosefu wa mikopo ya pembejeo na mitaji,
ukosefu wa huduma za ugani, mazingira mabaya ya uwekezaji, ubovu wa
miundombinu, na mengine mengi. Wakati
huo huo, sekta ya kilimo bado inabakia kuwa sekta kuu katika uchumi wa
Tanzania. Udogo
wa mashamba, teknolojia duni na utegemezi kwa mvua ni baadhi ya orodha ya
matatizo yanayokwamisha maendeleo ya kilimo na pia maendeleo ya wananchi wanao
kitegemea. Serikali
imekua ikichukua hatua mbali mbali kila mwaka katika jitihada za kuondoa
matatizo haya lakini hayaja tokomezwa bado.
32. Mheshimiwa Spika, ili
kuinua kilimo, Serikali imechukua hatua za ziada zenye lengo la kuvutia
uwekezaji katika sekta hii, na papo hapo kuwezesha wakulima wadogo kuongeza
tija ya jasho lao, na kujiondolea umaskini.
Hatua hizo ni pamoja na hizi zifuatazo:-
Moja: Chini
ya Sheria ya Kodi ya Mapato ya 2004
(a)
Kuna punguzo la mara moja (100% expensing) la
gharama za kusafisha pori, ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji, kupanda mazao ya
kudumu na kutunza mazingira au kudhibiti mmomonyoko katika ardhi inayotumika
kwa kilimo. Kwa taratibu za kawaida za
kiuhasibu, gharama hizi ni za rasilimali (capital expenditures) na
zingepunguzwa kwa kipindi kirefu sana.
(b)
Gharama ambazo mtu ametumia kuhifadhi mazingira
kwenye ardhi inayotumiwa kwa kilimo, ufugaji wa wanyama au samaki, au
kuirejeshea ardhi hiyo hali yake baada ya kuharibiwa, zinapunguzwa katika
kukadiria mapato ya mhusika kwa minajili ya kodi ya mapato.
(c)
Gharama za utafiti na uendelezaji wa mashamba ya
kilimo na mifugo zinapatiwa punguzo hilo kwa ajili ya kodi ya mapato.
(d)
Vifaa vya umwagiliaji maji mashambani vimeingizwa
katika kundi moja na magari makubwa ili kupata punguzo la uchakavu kwa kiwango
cha juu zaidi cha asilimia 25 kwa mwaka.
(e)
Matrekta na mitambo mingine inayotumiwa katika
kilimo, ufugaji na uvuvi imeingizwa katika kundi la mitambo ya viwandani na
kupatiwa punguzo la uchakavu la asilimia 50 katika mwaka wa kwanza na asilimia
25 miaka inayofuata.
(f)
Wafanyabiashara wa mazao ya kilimo hawatakiwi
kulipa kodi ya awali kwa awamu sawa (equal quarterly instalments), bali mwisho
wa robo ya tatu ya mwaka baada ya kuvuna.
Mbili: Chini ya
Sheria ya Ushuru wa Forodha:
Zana
na pembejeo za kilimo kama vile matrekta, madawa ya kuua wadudu na mbolea hivi
sasa hazitozwi Ushuru wa Forodha. Ikiwa
kuna kodi zilizosalia bado katika maeneo haya zitafutwa.
Tatu: Chini ya
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT)
(a)
Mazao ghafi ya kilimo na mifugo yanapata msamaha
wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ikiwa ni pamoja na nyama isiyosindikwa,
mazao ya mifugo ambayo hayajasindikwa, samaki zisizosi-ndikwa, na mazao mengine
yote ya kilimo ambayo hayajasindikwa.
(b)
Hakuna Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye
pembejeo za kilimo na uvuvi kama vile madawa ya kuua wadudu, mbolea, madawa na
vifaa vya mifugo, vifaa vya kilimo kama matrekta, majembe, sururu, nyavu,
mashine na vifaa vya uvuvi.
(c)
Kuna unafuu wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
pia kwa mazao ya kilimo yanayouzwa nje na wakulima waliojiunga kwenye Vyama Vya
Ushirika au Umoja wa wazalishaji (Associations) na kujisajili chini ya Sheria
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani.
Nne: Chini
ya Sheria ya Ushuru wa Stempu
Mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi yamesamehewa ushuru wa stempu.
Aidha, ushuru wa stempu haukusanywi katika magulio, ambapo mazao haya
huuzwa kwa wingi.
Tano: Chini
ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa
(a)
Bado sheria inakataza Serikali za Mitaa kutoza
kodi inayozidi asilimia tano (5%) ya bei ya shambani au chama cha msingi au cha
wakulima kwenye mazao ya kilimo. Aidha,
kodi hiyo inatakiwa kutozwa pale ambapo mazao husika yamelimwa au
yanaponunuliwa kwa mara ya kwanza kutoka kwa wakulima na siyo katika Wilaya
yanakopitia yakielekea sokoni au Wilaya nyingine au nchi jirani.
(b)
Kodi na ada
zinazoruhusiwa kutozwa ni zile tu zilizo orodheshwa katika Sheria ya Fedha ya
Serikali za Mitaa na Sheria ya Fedha ya Taifa ya mwaka 2003.
Sita: Katika
Bajeti ya Matumizi ya Serikali
(a)
Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya
mipango ya maendeleo ya kilimo katika ngazi ya Wilaya.
(b)
Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya
kufidia gharama za usafirishaji wa mbolea kwa ajili ya Mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini na mikoa mingine yenye mvua za uhakika itakayo tangazwa na Waziri wa
Kilimo na Chakula.
(c)
Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa vyama vya ushirika
na vyombo vingine vinavyonunua mazao ya wakulima utaimarishwa kwa kuongezewa
fedha katika bajeti hii. Mfuko huu umekuwa na
mafanikio makubwa.
33. Mheshimiwa Spika, Hatua hizi za
kufuta kodi au kutoa unafuu mkubwa wa kodi na fidia ya mbolea iliyotangazwa
mwaka tunao malizia kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, hasa wadogo na wa kati
ambao wengi ni wananchi, zikiunganishwa na mpango wa Serikali wa kudhamini
wakulima wadogo wadogo ili waweze kukopa kutoka mabenki kibiashara na mipango
inayoendelea ya kuchimba na kuimarisha barabara vijijini hadi taifani, na pia
hatua za kuondoa kero za kodi za leseni, ni ushahidi imara wa utekelezaji wa
sera na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Ni hatua madhubuti za
kuwawezesha Watanzania vijijini kuzalisha
mali na kujitajirisha kwa kujituma na kuwa wabunifu; ni msumari muhimu kwenye
jeneza la kuuzika umaskini kisayansi.
Atakayesema kwamba bajeti hii haimsaidii maskini au mkulima, mfugaji na
mvuvi atakuwa anapotosha tu ukweli.
Aliye na macho haonyeshwi njia!
34. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2004/05, hatua za kuimarisha
na kuboresha vyanzo vya akiba za pamoja za wananchi zitachukuliwa, ambapo “Unit
Trust of Tanzania” (UTT) itauza hisa
(Units) kwa wananchi. Uanzishwaji wa ‘Collective Investment Schemes’ ambapo wananchi watashirikiana
kuweka akiba kwa pamoja na hivyo kushiriki katika masoko ya mitaji nchini
litakuwa jambo geni sana.
UTT itashirikiana pia na
benki za biashara katika kuanzisha chombo cha kuweka kumbukumbu za wakopaji
(credit reference bureau) ili kuboresha mazingira ya benki kukopesha. Aidha, hatua zinazochukuliwa kuimarisha
mifuko ya dhamana ya mikopo na mitaji zinalenga pia kuwawezesha wananchi
kushiriki kikamilifu katika uendeshaji wa uchumi wa Taifa.
MWELEKEO WA BAJETI YA MWAKA
2004/05
Mapato
35. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha wa 2004/05, Serikali inalenga kukusanya mapato ya
ndani yasiyopungua shilingi trilioni moja, bilioni mia saba thelathini na tisa
na milioni mia mbili themanini na nane (milioni 1,739,288) sawa na asilimia
13.8 ya Pato la Taifa. Kiwango hiki ni ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na mapato
yanayotarajiwa kukusanywa mwaka huu wa 2003/04.
Azma ya Serikali kwa mwaka 2004/05 na muda wa
kati ujao itaendelea kuwa ya kuongeza mapato, kupunguza utegemezi, kugharamia
mpango wa kuondoa umaskini, na kuhakikisha kwamba hatubebi tena mzigo
tusiouweza wa madeni. Hatua kuu
zitakazochukuliwa katika kuongeza mapato ni pamoja
na:-
Moja: Kuimarisha
usimamizi na utawala wa Mamlaka ya Mapato, hasa kwa
kupanua Idara ya Walipa Kodi Wakubwa.
Mbili: Kutekeleza
Sheria Mpya ya Kodi ya Mapato, 2004 na kukamilisha
mapitio ya sheria nyingine za kodi kwa lengo la kuziboresha.
Tatu: Kuanza
utekelezaji wa Mkataba wa Kuanzishwa Umoja wa Forodha
wa Afrika Mashariki.
Nne: Kuingiza mapato
yatakayotokana na mauzo ya gesi ya Songo Songo katika maduhuli ya
Serikali. Mategemeo ni
kwamba gesi hii itaanza kupatikana kunako mwezi Julai 2004.
Tano: Kufanya
marekebisho ya mfumo wa kodi katika baadhi ya maeneo
ili kuuboresha zaidi pamoja na kuweka vivutio kwa baadhi ya sekta ili kukuza
Pato la Taifa.
Sita: Kuimarisha makusanyo ya
mapato kutoka Wizara na Idara, hasa zile zilizo kwenye utaratibu wa
“retention”.
Saba: Kusimamia kikamilifu biashara
ya bidhaa ya mafuta ya petroli ikiwemo kufungwa kwa “Flow Meter” bandarini ili kudhibiti ukwepaji kodi. “Flow Meter” inategemewa kufungwa mwezi Julai
2004.
Nane: Kuendeleza utaratibu wa utawala
wa misamaha ya kodi kwa njia ya “Treasury Voucher” na kuangalia uwezekano wa
kuingiza katika utaratibu huu vifaa vinavyoingizwa nchini kwa miradi
inayogharamiwa na Wafadhili.
Tisa: Kuimarisha utendaji wa TRA
kwa kuongeza matumizi ya teknolojia, tija ya watumishi, mafunzo, na huduma bora
kwa walipa kodi.
Kumi: Kuanzia Julai 2004 ukaguzi wa
mizigo utafanywa baada ya kuwasili nchini (destination inspection) badala ya
utaratibu wa sasa wa kabla ya kuwasili (preshipment inspection). Utaratibu huu utaboresha mazingira ya
biashara, utaondoa kero kwa waagizaji wa bidhaa, na utaboresha mazingira ya
uwekezaji.
Kumi na moja: Kuongeza saa za kazi za shughuli za forodha
ili kuondoa msongamano wa mizigo bandarini.
Vyombo vyote vinavyotoa huduma katika maeneo ya Forodha vitatakiwa
kushirikiana kwa karibu zaidi na Idara ya Forodha ili kufanikisha azma hii.
Kumi na mbili: Zoezi limeanza la kuainisha maeneo ya Sheria ya
Uwekezaji ya mwaka 1997 ambayo yanahitaji kurekebishwa ili kuondoa mianya ya
ufujaji wa mapato ya Serikali.
Kumi na tatu: Imeundwa Kamati ya kutathmini sheria na kanuni
zinazotawala uwekezaji katika sekta ya madini kwa lengo la kutoa mapendekezo ya
kuziboresha ili Serikali isipoteze yale mapato ambayo ni halali yake.
36. Mheshimiwa Spika, inaeleweka wazi kuwa misaada kutoka nje sio
njia nzuri ya kuendeleza uchumi imara na wa kudumu (sustainable). Hata hivyo katika kipindi hiki ambacho
tunafufua uchumi wetu na Kuondoa Umaskini, michango ya Wafadhili ni muhimu
katika kusaidia Serikali yetu. Sera safi
tulizo nazo pamoja na usimamizi imara wa uchumi vimewezesha Wafadhili na
Mashirika ya Fedha ya Kimataifa kupenda kuendelea kutoa misaada yao kuchangia
bajeti ya taifa. Kama nilivyosema awali,
ni muhimu kutumia nafasi hii vizuri na kuhakikisha kuwa michango hii inatumika
vizuri kutuwezesha kuondoa umaskini na kuleta maendeleo kama ilivyokuwa kwa
nchi nyingi za Bara la Asia. Mkakati wetu
wa Kusimamia Misaada (TAS) utazidi kutuongoza ili kuhakikisha misaada na mikopo
ya masharti nafuu inatumika vizuri kukuza uchumi wa taifa.
37. Mheshimiwa Spika, kutokana na majadiliano
tuliyofanya na nchi Wafadhili na Mashirika ya Fedha ya Kimataifa, katika mwaka
wa fedha 2004/05 tunatarajia kupata misaada na mikopo ya masharti nafuu
kiasi cha shilingi trilioni moja, bilioni mia tatu sitini na saba na milioni
ishirini na tano (shilingi 1,367,025 milioni) ambacho kitakuwa asilimia 41
ya matumizi yote ya Serikali. Kati
ya fedha hizo, shilingi 509,140 milioni ni misaada ya bajeti, na shilingi
857,885 milioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kiwango hiki cha misaada na mikopo
kinaonyesha ongezeko la shilingi 191,204 milioni au asilimia 16
ikilinganishwa na matarajio ya misaada na mikopo kwa mwaka huu wa fedha wa
2003/04. Ni mategemeo yetu kwamba Nchi
Wafadhili zitaendelea kuongeza misaada yao kwa Tanzania na kutekeleza
kikamilifu ahadi za Monterrey (Monterrey Consensus), ya kuhakikisha kuwa
tunawezeshwa kufikia malengo ya Maendeleo ya Milenia Mpya ( “Millenium
Development Goals” - MDG).
38. Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kutumia akiba yake Benki
Kuu pamoja na kukopa katika vyanzo vya ndani kiasi cha shilingi 231,110 milioni
kwa kutumia dhamana za muda mfupi na mrefu.
Sehemu kubwa ya mikopo hiyo itatumika kulipia madeni yaliyoiva
(rollover) na madeni mengine yanayotokana na mikataba. Kiasi kingine kitatumika kuchangia mfuko wa
dhamana ya mikopo kwa bidhaa za kuuza nje.
Matumizi
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
fedha 2004/05, Serikali imedhamiria kuendelea kusimamia vyema nidhamu katika
matumizi ya fedha za umma. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha mtandao wa
kompyuta wa kutayarisha na kutekeleza bajeti ya Serikali. Hatua hii ni pamoja
na kupanua teknolojia hii ili ifike kwenye Serikali za Mitaa.
40. Mheshimiwa Spika, mgao wa fedha kwa mwaka 2004/05 umezingatia
mambo yafuatayo:-
Kwanza: Sekta za kipaumbele katika Mkakati wa Kupunguza Umasikini zimeendelea
kupewa upendeleo. Hata hivyo kwa
kuzingatia mahitaji mapya ya fedha kugharamia matayarisho ya Uchaguzi Mkuu, na
pia mahitaji ya sekta ya nishati, hasa kuhusu umeme, nyongeza katika sekta hizo
za kuondoa umaskini haitakuwa kubwa, isipokuwa kwa zile ambazo zinapata misaada
mikubwa ya Wafadhili.
Pili: Utaratibu wa kutoa ruzuku kupunguza
gharama za usafirishaji wa mbolea kwenda Mikoa iliyoteuliwa utaendelezwa mwaka
wa 2004/05.
Tatu: Utaratibu wa kutoa fedha
kulingana na mapato yaliyopo (cash budget) utaendelea.
Nne: Fedha zaidi zimetengwa kwa
ajili ya Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Wauzaji wa bidhaa nchi za nje (ECGS) na Mfuko wa Dhamana kwa Biashara
ndogo na za kati (SME Credit Guarantee
Scheme).
Tano: Mipango ya kuendeleza kilimo katika ngazi ya Wilaya kwa utaratibu wa angalao Zao moja la Chakula
na zao moja la biashara utaendelezwa.
Sita: Mheshimiwa spika, katika miaka ya hivi
karibuni tumeshuhudia juhudi za Serikali za kutumia mapato yake ya ndani katika
ujenzi wa barabara muhimu. Mwaka 2004/05, Serikali itaendelea na utaratibu huo
ambapo fedha zaidi ya zile zilizotolewa mwaka huu zimetengwa, kama
atakavyoeleza zaidi Waziri wa Ujenzi atakapo-wasilisha bajeti ya Wizara yake.
Saba: Serikali itaendelea kutekeleza
mpango wa kuboresha mishahara ya watumishi wake, ili kufikia asilimia 4.8 ya
Pato la Taifa kama ilivyodhamiriwa katika mpango huo. Aidha, Serikali inaandaa utaratibu maalum wa
kushughulikia kwa haraka malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa Serikali
wakiwemo walimu. Malipo ya malimbikizo hayo yalisitishwa kutokana na matukio ya
wizi wa kalamu wa mishahara ulio fanywa na watumishi wachache wasioaminika
ambao sasa umefanyiwa uchunguzi na hatua za kisheria zinachukuliwa kwa
wanaohusika.
Nane: Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa
kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Umuhimu wa kwanza unawekwa kwa
miradi ambayo tayari ina mikataba.
Tisa: Bajeti imeendelea kutenga
asilimia 4.5 ya mapato yatokanayo na misaada (grants) isiyo ya miradi kwa ajili ya bajeti ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Utaratibu huu utaendelea hadi hapo mapendekezo
ya Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint
Finance Commission) yatakapopa-tikana.
Kumi: Katika mwaka wa fedha
2004/05, Serikali itawarejesha katika daftari la Pensheni wastaafu waliokuwa
wamepokea mafao yao kwa mkupuo. Wastaafu hawa wanategemewa kuanza kupokea
malipo yao mwezi Januari, 2005, ili kujipa muda wa matayarisho baada ya sheria
husika kurekebishwa.
Kumi na moja: Kutokana
na ongezeko la matukio ya ujambazi nchini, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
ujao, na vitendo vingine vya uhalifu, bajeti ya mwaka 2004/05 imeongeza mgao wa
fedha kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kumi na mbili: Katika
mwaka 2004/05, Serikali imetenga fedha
zaidi kwa ajili ya chakula cha dharura endapo hali ya hewa itakuwa mbaya
pamoja na kugharamia Mfuko wa Hifadhi ya Chakula (SGR).
Kumi na tatu: Kama
ilivyokuwa katika mwaka 2003/04, bajeti ya 2004/05 imetenga fedha kwa ajili ya
kulipia mahitaji ya sekta ya Nishati na hasa TANESCO kuisaidia katika mpango
wake wa dharura, pamoja na malipo ya “capacity charge” kwa IPTL na Songas.
Kumi na nne: Kwa
kuzingatia ukweli kuwa idadi ya Wabunge inategemea kuongezeka baada ya uchaguzi
mkuu wa mwakani, Mifuko ya Hifadhi za Jamii imekubali kwa ridhaa yao wenyewe,
kujenga Ukumbi mpya kwa utaratibu wa kujenga, kukodisha na hatimaye kuikabidhi
Serikali. Kwa sababu hii, mradi huu
hauko kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka huu. Serikali pia inafikiria kutumia utaratibu
kama huu kwa miradi mingine mikubwa ya ujenzi ikiwemo miradi ya barabara.
Kumi na tano: Kwa
kuzingatia umuhimu wa michezo, bajeti ya mwaka 2004/05 imetenga fedha kwa ajili
ya ujenzi wa uwanja wa michezo wa kisasa.
Sehemu kubwa ya fedha hiyo ni msaada wa Serikali ya China.
Kumi na sita: Mgao
wa Ruzuku kwa Halmashauri za Wilaya kwa mwaka 2004/05 umezingatia utaratibu
mpya ambao umebuniwa kufuatia zoezi la kina lililoshirikisha wadau wa aina
zote. Utaratibu mpya umetumika katika
kutenga fedha za bajeti ya kawaida kwa sekta za afya na elimu kwa Halmashauri,
na umetumika kwa sekta zote katika fedha za bajeti ya maendeleo. Utaratibu huu mpya unajibu hoja za
Waheshimiwa Wabunge kuhusu usawa wa mgao wa bajeti Kimkoa na Kiwilaya. Maelezo zaidi yatatolewa na Waziri wa
TAMISEMI atakapowasilisha bajeti ya Wizara yake.
MFUMO WA MAKISIO YA BAJETI YA MWAKA 2004/05
41. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, Serikali imelenga kukusanya
mapato ya ndani ya jumla ya shilingi trilioni moja, bilioni 739 na milioni 288
(1, 739, 288 milioni) mwaka wa fedha wa 2004/05 kwa msingi wa mfumo wa kodi wa
sasa, pamoja na marekebisho yanayopendekezwa katika eneo la kodi. Kiwango hiki cha mapato ni
sawa na asilimia 13.8 ya Pato la Taifa.
Serikali inakusudia pia kuingiza katika mapato yake shilingi 10,115
milioni mapato yatakayotokana na uuzaji wa hisa za Serikali katika baadhi ya
Mashirika ambapo Serikali ni mbia.
42. Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kutumia
jumla ya shilingi trilioni tatu, bilioni mia tatu arobaini na saba, milioni mia
tano thelathini na nane (shs. 3,347,538, milioni) katika mwaka wa fedha wa
2004/05. Kwa kuzingatia mapato ya
shilingi trilioni moja, bilioni mia saba thelathini na tisa, milioni mia mbili
themanini na nane (shs. 1,739,288 milioni) na yale ya kuuza hisa za shilingi
bilioni kumi, milioni mia moja kumi na tano (shs. 10,115 milioni), bajeti
inakuwa na pengo la shilingi trilioni moja, bilioni mia tano tisini na nane, na
milioni mia moja thelathini na tano (shs. 1,598,135 milioni). Sehemu kubwa ya pengo hili itajazwa na
misaada ya Nchi Wafadhili, Jumuiya ya Ulaya, mikopo yenye masharti nafuu kutoka
kwa Mashirika ya Fedha ya Kimataifa, hususan Benki ya Dunia na Benki ya
Maendeleo ya Afrika. Kwa mujibu wa
makubaliano tuliyofikia kati ya Serikali ya Tanzania na hawa Wafadhili na
Mashirika kwa pamoja, tumekadiria kupata misaada na mikopo ya masharti nafuu,
jumla ya shilingi trilioni moja, bilioni mia tatu sitini na saba, milioni
ishirini na tano (shs. 1,367,025 milioni) mwaka wa 2004/05. Kwa hiyo pengo linapungua hadi shilingi
bilioni mia mbili thelathini na moja, milioni mia moja na kumi (shs. 231,110
milioni). Pengo hili litazibwa kwa njia
ya kupunguza akiba ya Serikali katika Benki Kuu na kukopa kutoka soko la fedha
la ndani kama nilivyosema hapo awali.
MAREKEBISHO YA MFUMO WA KODI, ADA MBALIMBALI NA HATUA
NYINGINE ZA MAPATO
43. Mheshimiwa Spika, hapo mwanzo nimetoa
maelezo kuhusu matokeo mazuri ya hatua zilizochukuliwa na Serikali mwaka huu wa
fedha unaoisha za kuongeza tija na kuziba mianya katika ukusanyaji wa mapato ya
Serikali. Aidha, kama nilivyoeleza awali, Serikali
ina dhamira ya dhati ya kuona kuwa tija katika sekta ya kilimo inaongezeka ili
kupanua ajira, kujitosheleza kwa chakula, kupunguza umaskini, na kuongeza mauzo
yetu nje ya nchi. Pamoja na hatua mbalimbali zilizokwishachukuliwa, Serikali
itachukua hatua za ziada mwaka wa fedha ujao. Serikali imeona kuna haja ya kutoa vivutio
zaidi ili kuhamasisha uwekezaji wa miradi mikubwa na ya kati katika sekta hii
ili kutumia ardhi kubwa ambayo hivi sasa haitumiki ipasavyo na kuongeza nafasi
za ajira vijijini. Aidha, tunalenga kuongeza
tija kwa viwanda vinavyozalisha pembejeo au kusindika mazao ya kilimo. Hatua hizo ambazo ni nyongeza ya zile nilizoelezea
awali ni pamoja na hizi zifuatazo:-
(a)
Kwa Wakulima na Wafugaji Wakubwa:
Kwanza: Katika Mfumo wa Kodi ya
Mapato, utatolewa unafuu wa asilimia mia moja (100% expensing) ya gharama za
mtaji katika mwaka wa kwanza wa kutumia rasilimali inayotokana na gharama
hizo. Unafuu huu pia utahusu
mitambo ya usindikaji wa mazao ghafi ya kilimo mashambani au uvuvi. Nia ni kuongeza uwekezaji katika teknolojia
ya kilimo.
Pili: Katika Mfumo wa Ushuru wa Stempu,
utawekwa ukomo wa Shilingi 500 kwa kiwango cha ushuru unaolipwa wakati
wa kuhamisha milki (conveyance) ya ardhi ya kilimo. Nia ni kupunguza gharama za
kubadilisha milki ya ardhi ya kilimo.
Tatu: Katika Mfumo wa Tozo ya Mafunzo ya
Ufundi Stadi (Skills Development Levy), tozo hiyo kwa ajira za mashambani
itafutwa.
(b)
Kwa Wakulima na Wafugaji Wadogo Wadogo:
Hatua zilizotangazwa mwaka
jana za kuboresha mazingira na mapato ya
wakulima na wafugaji wadogo wadogo zinapaswa kutekelezwa kwa ukamilifu. Napenda kukumbusha kwamba Halmashauri za
Wilaya, Miji, Manispaa na Jiji zina fursa ya kutoza kodi na tozo
zilizoorodheshwa katika Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa kufuatia
marekebisho yaliyofanywa mwaka jana. Aidha, Halmashauri zinakumbushwa
kuzingatia ukomo wa asilimia 5 ya bei ya mazao kwa mkulima kwa ajili ya Ushuru
wa Mazao unaotozwa, na iwapo tu mazao husika yamezalishwa katika eneo la
Halmashauri hiyo. Aidha, imedhihirika kwamba Halmashauri
nyingi bado zinatoza michango mabalimbali kwenye mazao kwa maelezo kuwa ni ya
hiari! Inasisitizwa kwamba michango
ya namna hiyo inakubalika tu pale ambapo wanakijiji wameshirikishwa na michango
iwe kwa ajili ya miradi maalumu inayotekelezwa ndani ya kijiji husika au kwa
ushirikiano wa vijiji kadhaa.
(c)
Kwa Viwanda vya Pembejeo za Kilimo na Uvuvi:
Kwa kuwa pembejeo za kilimo
na uvuvi hazitozwi VAT, wazalishaji wa ndani wa bidhaa hizo wanapata ushindani
usio wa haki kutoka kwa bidhaa za namna hiyo zinazotoka nje. Ili kuondoa kasoro hii, inapendekezwa kuwa
bidhaa husika zijumuishwe kwenye kundi la kutozwa VAT kwa kiwango cha sifuri
(zero rate) zinapouzwa na wazalishaji wa ndani ili kuwezesha wazalishaji hao
kurejeshewa kodi wanayolipa kwenye nyenzo na malighafi. Aidha, hatua hii itaboresha
mazingira ya uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha pembejeo.
(d)
Kwa Viwanda vya Mazao ya Kilimo na Uvuvi:
Pamoja na hatua zilizotangazwa chini ya Sheria ya Kodi ya Mapato,
inapendekezwa kuwa:
Kwanza:
Mvinyo na brandi vitakavyo-tengenezwa kutokana na zabibu za hapa nchini
visitozwe Ushuru wa Bidhaa. Lengo ni
kupanua soko la zabibu hapa nchini, ili kupanua kilimo cha zao hilo, hasa
Mkoani Dodoma.
Pili: Inapendekezwa
kusamehe kodi ya VAT kwa chai iliyosindikwa (black tea) na iliyofungashwa
(packaged tea) ili kuhimili ushindani baada ya soko la chai kufunguliwa. Lengo
kubwa hapa ni kulinda pato la wakulima wadogo wa chai.
Uwezeshaji Wananchi katika Biashara Ndogo na za Kati
44. Mheshimiwa Spika, eneo jingine litakalo patiwa msukumo maalum katika
bajeti hii ni la biashara ndogo na za kati (SMEs). Baada ya sekta ya kilimo, inafuata sekta ya
biashara ndogo na kati kuwa tegemeo kubwa la ajira kwa wananchi wengi. Aidha, sekta hii ni muhimu sana katika juhudi
za Serikali za kuwawezesha wananchi kujiondolea umaskini. Kwa hiyo mkazo mwingine wa bajeti hii ni
kuboresha mazingira kwa ajili ya kukua kwa sekta ya biashara ndogo na za kati.
45. Mheshimiwa Spika, hivi sasa biashara ndogo na za kati zenye mauzo
(turnover) isiyozidi shilingi milioni 20 kwa mwaka hulipa aina mbili kubwa za
kodi kwa TRA, ambazo ni Ushuru wa Stempu na Kodi ya Mapato kwa utaratibu wa
kodi ya makadirio (presumptive tax). Kodi hizo mbili zinakadiriwa kwa msingi wa
thamani ya mauzo ya biashara husika. Ili
kupunguza gharama kwa biashara hizi, inapendekezwa kufuta Ushuru wa Stempu na
kufidia sehemu ya mapato yatakayopungua kwa kuongeza kidogo viwango vya kodi ya makadirio (presumptive
tax rates). Viwango vipya vya kodi ya
makadirio vitakuwa kama ifuatavyo:
|
Thamani ya Mauzo (Shilingi) |
Kodi iwapo kuna kumbukumbu za kuridhisha |
Kodi iwapo hakuna kumbukumbu za kuridhisha |
|
0 -
3,000,000 |
1.2% ya mauzo kwa mwaka |
35,000 kwa mwaka |
|
3,000,001 - 7,000,000 |
Tshs.35,000 na 1.5% ya mauzo yanayozidi
Tshs3,000,000 kwa mwaka. |
95,000 kwa mwaka |
|
7,000,001 - 14,000,000 |
Tshs.95,000 na 2.8% ya mauzo yanayozidi
Tshs7,000,000 mwaka. |
291,000 kwa mwaka |
|
14,000,001 - 20,000,000 |
Tshs.291,000 na 5.0% ya mauzo yanayozidi
Tshs.14,000,000 kwa mwaka. |
589,000 kwa mwaka |
Pamoja na kuwapunguzia mzigo wa kodi, utaratibu
huu utatoa hamasa kwa wenye biashara hizi kutayarisha na kutunza kumbukumbu na
hivyo kuongeza uwezekano wa kujenga mahusiano mazuri na wakopeshaji. Aidha, viwango vya kawaida vya Kodi ya Mapato
kwa msingi wa faida halisi vitatumika pale ambapo
hesabu kamili zitakuwa zimeandaliwa na kuwasilishwa TRA.
46. Mheshimiwa
Spika, vile vile inapendekezwa kuongeza kiwango cha chini (threshhold) cha
mauzo kwa ajili ya usajili wa VAT kutoka shilingi
milioni 20 hadi milioni 40 kwa mwaka.
Lengo la hatua hii ni kuondoa biashara ndogo
ndogo katika wigo wa VAT kwa kuzingatia gharama za kutunza mahesabu na pia
gharama za kusimamia na kutawala ukusanyaji wa kodi hii. Hata hivyo, biashara
zenye kiwango hiki cha mapato zitaweza kujisajili
47. Mheshimiwa
Spika, pendekezo la tatu linalolenga kuboresha mazingira na
kuondoa kero kwa biashara, hasa ndogo na za kati linahusu ada za leseni za
biashara chini ya Sheria ya Leseni za Biashara ya mwaka 1972. Kwa kuwa nia
ya leseni za biashara ni kusimamia tu kanuni za
biashara kwa kutoa leseni (regulatory) na wala siyo chanzo cha mapato,
hatua zifuatazo zinapendekezwa:
Pili: Kufuta
ada ya leseni inayotozwa chini ya Sheria ya Leseni za Biashara ya 1972 kwa biashara zenye
mauzo yasiyozidi shilingi milioni 20 kwa mwaka ili kupunguza gharama na
kuwezesha vijana na wafanyabiashara wadogo kuanzisha biashara kwa njia
halali. Biashara
hizi zitapewa leseni bila kulipia ada.
Tatu: Biashara
zenye mauzo yanayozidi Shilingi milioni 20 kwa mwaka
zitozwe ada ya leseni ya shilingi 20,000/= tu ili kupunguza gharama
zinazoambatana na kuanza biashara, na kuweka mazingira mazuri ya kuingiza
biashara nyingi katika Uchumi Rasmi.
Nne: Kufuta ada za leseni
zinazotozwa chini ya Sheria ya Leseni za Biashara, pale ambapo biashara husika
inasimamiwa chini ya Sheria nyingine ya kisekta ambapo leseni nyingine
hutolewa chini ya sheria hizo. Mfano ni biashara ya kibenki, bima, hoteli n.k.
Tano: Leseni
ya biashara chini ya Sheria ya Leseni za Biashara itolewe mara moja tu
wakati biashara inapo-anzishwa.
Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa, na Jiji
zitakiwe kutayarisha na kutoa takwimu sahihi za leseni za biashara kwa mamlaka
husika ili kuwa na takwimu pale zinapotakiwa kufanya hivyo. Kwa kuwa wenye biashara wanasajiliwa pia na TRA kupitia Namba ya Utambulisho ya Kodi (TIN), hakuna
haja ya kukata leseni ya biashara kila mwaka.
Sita: Pamoja
na hatua hizi zinazohusu kodi na tozo nyingine
mbalimbali, ningependa kueleza kwamba Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa ajili ya
Biashara Ndogo na za Kati ulioanzishwa mwaka huu wa fedha umeongezewa fedha
katika bajeti hii. Kanuni na taratibu za kutawala mfuko huo zimeshakamilika.
48. Mheshimiwa
Spika, pamoja na hatua hizi za kuboresha sekta za kilimo na
biashara ndogo na za kati, marekebisho mengine mapya katika kodi mbalimbali
yanapendekezwa
(i)
Mfumo wa Kodi ya Mapato
Sheria
ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 iliyopitishwa katika kikao cha Bunge cha mwezi
Aprili itaanza kutumika kuanzia Julai 2004.
Inapendekezwa kwamba uandishi wa Sheria hiyo urekebishwe ili kufafanua
kwamba Sheria hii itatumika kuanzia Julai 2004 kwa walipa kodi wote isipokuwa
wale ambao wanatengeneza mahesabu na ambao mwaka wao wa mapato ulianza kabla ya
Julai 2004.
(ii)
Mfumo wa Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT)
(a) Ili kuwezesha wazalishaji
wa ndani kurejeshewa VAT wanayolipa kwa malighafi, inapendekezwa kujumuisha
madawa ya binadamu na mifugo, vyandarua, na vifaa maalum vya walemavu katika
Jedwali la I ili zisilipiwe kodi kwa kuwa kwenye kiwango cha sifuri (zero rate).
(b) Kurekebisha msamaha wa
kodi kwa magari kwa wale wenye msamaha huo, ili kujumuisha magari yaliyomo
kwenye HS Code 8703, 8702.10.20 na 8702.90.20 yenye injini zenye uwezo zaidi ya
CC 3000.
Pamoja na hatua
nilizoeleza awali, marekebisho haya katika mfumo wa Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) yatapunguza mapato ya Serikali kwa shilingi 4,954 milioni.
Hatua
mpya nilizozitaja zina lengo la
kuimarisha kilimo na biashara na kuwezesha wananchi, hasa wale wa kipato kidogo
kuingia katika uchumi rasmi na kujitafutia
riziki ili wajiondolee umaskini. Aidha, marekebisho katika
ada za leseni yanajibu pia hoja za wawekezaji na Wafadhili wetu ambao ni pamoja
na taasisi za dini zinazotoa huduma ya jamii Nchini mwetu.
(iii)
Mfumo wa Ushuru wa Bidhaa
Mheshimiwa Spika,
inapendekezwa kufanya marekebisho kadhaa katika eneo la ushuru wa bidhaa kama
ifuatavyo:
Kwanza, kurekebisha viwango vya
Ushuru wa Bidhaa kulingana na mfumuko wa bei kwa bidhaa zifuatazo:
Moja: Vinywaji baridi. Ushuru
unaongezwa kutoka shilingi 37.50 kwa lita hadi shilingi 40.0 kwa lita.
Mbili: Bia. Ushuru unaongezwa kutoka
shilingi 232.0 kwa lita hadi shilingi 243.0 kwa lita.
Tatu: Mvinyo. Unaotengenezwa kwa kiwango kisichozidi asilimia
75 ya zabibu inayozalishwa hapa nchini.
Ushuru unaongezwa kutoka shilingi 743.40 kwa lita hadi shilingi 780.00
kwa lita.
Nne: Vinywaji vikali. Ushuru unapanda kutoka shilingi 1,102.50 kwa
lita hadi shilingi 1,158 kwa lita.
Tano: Sigara zenye urefu usiozidi
milimita 70 na zinazotengenezwa kwa tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango
kinachozidi asilimia 75. Ushuru
unaongezwa kutoka shilingi 3,781.05 kwa sigara 1000, hadi shilingi 3,970 kwa
sigara 1000.
Sita: Kwa sigara zenye urefu wa
milimita 70 au zaidi zilizotengenezwa kwa kiwango cha tumbaku
inayozalishwa nchini inayozidi asilimia 75.
Ushuru unaongezwa kutoka shilingi 8,920.30 kwa sigara 1000 hadi shilingi
9,367 kwa sigara 1000.
Saba: Sigara nyingine zenye sifa
tofauti na nilizozitaja katika vifungu vya (tano) na (sita) hapo juu, ushuru
utaongezeka kutoka shilingi 16,206.75 kwa sigara 1000 hadi shilingi 17,017 kwa
sigara 1000
Nane: Tumbaku ambayo iko tayari
kutengeneza sigara “cut rug/filler” ushuru wake unaongezeka kutoka shilingi
8,183.70 kwa kilo hadi shilingi 8,593.
Tisa: Ushuru wa “Cigar” unabaki kuwa
asilimia thelathini (30%).
Pili, kuweka ushuru wa bidhaa (excise) kwenye huduma ya
televisheni kupitia satelaiti (DSTV) kwa kiwango cha asilimia 5 kwa mauzo ya huduma hiyo.
Mwisho, kurekebisha msamaha wa
ushuru wa bidhaa kwa magari ili kuingiza magari yaliyomo kwenye HS Code 8703,
8702.10.20, na 8702.90.20 yenye injini zenye uwezo zaidi ya CC 3000.
Marekebisho haya ya Ushuru
wa Bidhaa yataiongezea Serikali mapato ya shilingi milioni 6,143.
(iv)
Sheria ya Fedha ya
Serikali za Mitaa
Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya
marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ili kuzipa uwezo
Halmashauri kukusanya mrahaba kwenye madini ya Jasi (Gypsum), Pozzolana, na Chokaa, ambayo yanatumiwa na viwanda kama
malighafi.
(v)
Ada ya Leseni za Biashara
zinazokusanywa na Wizara na Vyombo Vingine vya Serikali.
Mheshimiwa Spika, hatua nilizoainisha
awali katika eneo hili kwa pamoja zitaipunguzia Serikali mapato kwa kiasi cha shilingi milioni 14,000, ambazo
zimegawanyika kama ifuatavyo:-
q
shilingi milioni 11,200 kwa Halmashauri za
Wilaya, Miji, Manispaa na Jiji, na
q
shilingi milioni 2,800 kwa Wizara ya Viwanda na
Biashara. Bajeti hii imetenga fedha hizo
kufidia Halmashauri na Wizara hiyo.
(vi)
Ada ya Viza na Utaratibu
wa kutoa Viza
Mheshimiwa Spika, hivi sasa wageni
wanaoingia Tanzania kama wafanya-biashara wanalipa ada ya viza ya dola za
Marekani 200, na wale wanaoingia kama Watalii au wasafiri wa kawaida wanalipa
ada ya viza ya dola za Marekani 50. Kwa
kuwa dola 200 ni nyingi na kwa kuzingatia tofauti kubwa kati ya dola 200 na 50,
wageni wengi waingiapo nchini wanajitambulisha kama wasafiri au watalii wa
kawaida. Hivyo ni wachache sana
wanaolipa ada hiyo ya dola za Marekani 200.
Aidha, kuna ufujaji mkubwa wa mapato yatokanayo na ada ya viza
unaosababishwa na utaratibu unaotumika wa kutoa viza kwa wageni wanaokuja
nchini kwetu. Utaratibu unaotumika ni wa
kupiga mhuri kwenye pasi ya kusafiria, ambao imedhihirika hauna udhibiti, na ni
wa kizamani. Kwa sababu hizi,
inapendekezwa kama ifuatavyo:-
(i)
Ada ya “viza ya biashara” ya dola za Marekani
200 ipunguzwe hadi dola za Marekani 50 ili kuondoa tofauti hiyo ambayo haina
faida kwa Nchi yetu ambayo inataka itembelewe na wawekezaji wengi,
wafanyabiashara wengi na watalii kemkem.
(ii)
Utaratibu mpya wa kutumia “visa stickers”
uanzishwe badala ya huu wa sasa wa mihuri, ili kudhibiti mapato yatokanayo na
viza nchini na katika Balozi zetu.
Hatua hizi mbili kwa
pamoja zitaipatia Serikali mapato mapya ya shilingi milioni 19,823.
(vii)
Mfumo wa Ushuru wa Forodha
Lengo la Marekebisho ya Mfumo wa Kodi mwaka 2004/05
49. Mheshimiwa Spika, Lengo
la marekebisho yote yanayo pendekezwa ni kuboresha
mazingira ya kukuza uchumi wetu, kuwawezesha wananchi kufanya shughuli mbali
mbali za kujiendeleza na kujiondolea umaskini, na kupanua wigo wa ajira na
kodi. Aidha, baadhi ya hatua hizi
zitaongeza na nyingine zitapunguza mapato ya Serikali katika mwaka ujao wa
fedha, kama ifuatavyo:
|
|
Eneo la Hatua |
Nyongeza/Punguzo la
Mapato (shilingi milioni) |
|
(i) |
Mfumo wa Kodi ya
Ongezeko la Thamani |
(4,954) |
|
(ii) |
Mfumo wa Ushuru wa
Bidhaa |
6,143 |
|
(iii) |
Mfumo wa Kodi ya Mapato |
13,189 |
|
(iv) |
Mfumo wa Ushuru wa
Forodha |
1,138 |
|
(v) |
Mfumo wa Ushuru wa Stempu |
(19,263) |
|
(vi) |
Mfumo wa Tozo ya Ufundi
Stadi |
(2,076) |
|
(vii) |
Mfumo wa Leseni za
Biashara |
(14,000) |
|
(viii) |
Mfumo wa Viza |
19,823 |
|
|
JUMLA |
0 |
SURA YA BAJEI YA MWAKA 2004/05
50. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa
bajeti nilioueleza hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2004/05 inakuwa kama
ifuatavyo:
Mapato
Shilingi Milioni
A. Mapato
ya Ndani 1,739,288
(i) Mapato ya Kodi 1,603,886
(ii) Mapato yasiyo ya Kodi 135,402
B. Mikopo
na Misaada ya Nje
ikijumuisha
HIPC 1,367,025
C. Mapato kutokana na uuzaji Hisa 10,115
D. Kupunguza
akiba (reserve) pamoja na
mikopo
ya ndani 231,110
Jumla ya Mapato Yote 3,347,538
E. Matumizi ya Kawaida 2,239,000
(i)
Deni la Taifa 481,175
(ii)
Wizara (sekta mbali mbali) 1,293,467
(iii)
Mikoa 33,473
(iv)
Serikali za Mitaa
386,768
(v)
Matumizi Maalum 44,117
a)
Mishahara (taasisi)
6,000
b) Mishahara (Serikali Kuu) 32,699
c) Tansort escrow account 561
d) Vita Dhidi ya Rushwa 857
e) Mafao ya Watumishi 4,000
F. Matumizi ya Maendeleo 1,091,590
a) Fedha za Ndani 233,705
b) Fedha za Nje 857,885
G. Dharura 16,948
JUMLA YA MATUMIZI YOTE 3,347,538
51. Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, bajeti ya mwaka
2004/05 imeandaliwa kwa msingi wa kuendeleza juhudi za Serikali katika
kutekeleza:
(i)
Shabaha za Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ya
Chama Cha Mapinduzi;
(ii)
Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi 2025;
(iii)
Mkakati wa
Kupunguza Umaskini;
(iv)
Sera za
Kijumla za Kiuchumi kwa mwaka 2004/05.
52. Mheshimiwa Spika,
53. Mheshimiwa Spika,
katika yote haya, mafanikio halisi ya kukuza uchumi na
kuondoa umaskini yatapatikana pindi tutakapoweza kuunganisha Nchi yetu kwa njia
ya miundo mbinu ya barabara, reli, mawasiliano na nishati. Pili tunahitaji kujenga uwezo wa utaalam ambao ni lazima katika dunia hii ya
utandawazi. Tatu, kwa
kuwa wananchi wengi wanaishi vijijini na wanategemea kilimo kwa chakula na
ajira, ni lazima mkakati wetu wa kuinua kilimo uwe imara zaidi – na uunganishe
kilimo, viwanda na biashara, ndipo tutaweza kugeuza sekta hiyo iwe ya
kisasa. Pengine tuna haja ya kuangalia
tena vipaumbele vyetu ili tupate tija ya uhakika kwa
kutumia uwezo mdogo tulio nao wa fedha kwa maeneo machache kwanza kuliko kugawa
kidogo kidogo bila mafanikio ya maana.
Nitafurahi kupata ushauri wa Waheshimiwa
Wabunge juu ya wazo hili wakati wa mjadala wa hoja hii.
54. Mheshimiwa Spika,
Bajeti hii ni mfululizo wa jitihada za Serikali ya
awamu ya tatu za kurekebisha uchumi na kupambana na umaskini. Inaendeleza matakwa ya uchumi tulivu,
endelevu na unaokua hatua kwa hatua, mwaka hadi
mwaka. Inaweka mazingira mazuri ya
kujiajiri, kuwekeza, na kujiendeleza. Inatoa fursa kwa
kila mtu kufanya kazi kwa tija, hasa za kilimo na shughuli ndogo ndogo. Inawezesha Wananchi walio kwisha anza safari ya kujiajiri na kujitegemea kiuchumi kupiga
hatua zaidi, kwa kuwaondolea urasimu, kuwadhamini wakikopa benki, kuwapunguzia
kodi, leseni na ushuru wa aina aina na kuwaondolea kero ya kufukuzana na wakata
leseni, hasa wa mijini. Naamini kuwa
hotuba zifuatazo za Mawaziri wa kisekta zitatangaza
hatua zaidi za kuwawezesha Watanzania kujiendeleza kiuchumi na kijamii katika
sekta zao kwa mujibu wa sera iliyo wekwa.
Pamoja na hayo Mheshimiwa Spika, hakuna
Serikali inayo weza kumlisha au kumtajirisha mwana kaya ambaye hachukii
umaskini na kufanya kazi kwa bidii.
Uchumi wa kaya na wa taifa unakuzwa na wanakaya
na wananchi kwa ujumla wao. Serikali
itaendelea kuweka mazingira bora ya kumwezesha mwenye nia na
dhamira ya kupiga hatua ya maendeleo ya kaya yake na ya taifa lake. Naamini kabisa kwamba Waheshimiwa Wabunge
wanaelewa
55. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.