HOTUBA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII

MHESHIMIWA ZAKIA HAMDANI MEGHJI (MB),

WAKATI AKIWASILISHA BUNGENI,

MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA

KWA MWAKA 2004/2005

 

 

UTANGULIZI

 

Mheshimiwa Spika,

1.    Kutokana na taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Maliasili na Mazingira, naomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako tukufu likubali kupitisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2004/2005.

 

Napenda kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Mazingira kwa kujadili makadirio ya matumizi ya fedha ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2004/2005. Wizara yangu itazingatia na kutekeleza mapendekezo ya Kamati hiyo. 

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA WIZARA MWAKA 2003/2004 NA MALENGO YA MWAKA 2004/2005

 

Mheshimiwa Spika,

2.    Katika mwaka 2003/2004, Sekta ya Maliasili na Utalii iliendelea kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.  Kwa kutumia vigezo vya kawaida vya mafanikio, wananchi wengi wameendelea kupata ajira ya moja kwa moja katika shughuli za maliasili na utalii na vile vile wengine kujiajiri wenyewe katika biashara mbalimbali kutokana na mazao ya maliasili hasa uvuvi, misitu na shughuli zinazoimarisha utalii.

 

Mheshimiwa Spika,

3.    Kwa kutumia kigezo cha mapato ya fedha za kigeni, katika mwaka 2003, ukiachia mbali mapato kutokana na utalii, uuzaji wa mazao ya samaki pekee nchi za nje uliingizia Taifa Dola 129.6 milioni ikilinganishwa na Dola 121 milioni mwaka 2002 na Dola 95.4 milioni mwaka 2001. Ili kufaidika na ufanisi huu, Serikali imeamua kwamba kuanzia mwaka 2004/2005, samaki wakubwa wa mapezi wa maji ya chumvi wasioliwa sana na wananchi wa mwambao nao watachakatwa (process) na kuuzwa nchi za nje kama vile ilivyo Sangara. Hatua hii itatoa fursa kwa wananchi wa mwambao kuboresha zana zao za uvuvi ili kuwavua samaki hao kwa wingi, na muhimu zaidi, kuwapanulia wigo wa uvuvi na kuongeza mapato yao katika vita ya kupambana na umaskini.

 

Mheshimiwa Spika,

4.    Eneo lingine lililoonyesha mafanikio mazuri ni katika ukusanyaji wa maduhuli katika maeneo yanayosimamiwa na Wizara. Lengo la mwaka 2003/2004 lilikuwa kukusanya Sh.21.3 bilioni. Hadi mwezi Mei, 2004 Wizara ilikwishakusanya Sh.22.9 bilioni. Makusanyo ya maduhuli yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kwani katika mwaka 2002/2003 lengo lilikuwa Sh. 17.7 bilioni lakini makusanyo halisi yalikuwa Sh. 22.4 bilioni. Maongezeko haya, bila kubadilisha viwango vya ushuru pia ni ishara ya kuboresha utoaji huduma na kusimamia uhifadhi.

 

 

Mheshimiwa Spika,

5.    Baada ya kusema hayo ni lazima nikiri kuwa pamoja na mafanikio hayo, pametokea pia changamoto ambazo Wizara yangu inalazimika kuzishughulikia. Kwa mfano, tumefanikiwa katika kuboresha uhifadhi wa wanyamapori na hivyo idadi ya wanyama imeongezeka kama vile tembo, simba n.k.  Hali ya usalama na wingi wa wanyama hao umewafanya wasogelee zaidi sehemu chache za makazi na mashamba ya wananchi na kuwaondolea amani. Suala hili linashughulikiwa. Matatizo mengine yaliyoendelea katika mwaka 2003/2004 ni pamoja na uchomaji ovyo wa misitu, uvunaji haramu wa mazao ya maliasili, uvamizi wa maeneo ya hifadhi ya wanyamapori na misitu kwa ajili ya kilimo, makazi na malisho ya mifugo, ubovu wa miundo mbinu katika maeneo ya hifadhi na uchache wa vitendea kazi.

 

Mheshimiwa Spika,

6.    Baada ya kutoa maelezo hayo ya utangulizi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba pamoja na mafanikio na matatizo niliyoyaeleza, katika kusimamia uhifadhi endelevu, Wizara iliendelea kufanya mapitio katika Sera, Sheria na Kanuni za sekta zake ndogo na kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha sekta hizo.  Vile vile, utangazaji wa utalii uliimarishwa kwa kutafuta masoko mapya na kuongeza ushirikiano na sekta binafsi.

 

Mheshimiwa Spika,

7.    Naomba sasa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji ya mwaka 2003/2004 na malengo ya Wizara kwa mwaka 2004/2005 kama ifuatavyo:

 

SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI

 

Mheshimiwa Spika,

8.    Sekta hii ni msingi wa biashara ya utalii nchini na inachangia maendeleo ya wananchi kwa kutoa asilimia ya mapato kugharamia miradi ya kijamii.  Sekta imetekeleza majukumu yake kwa kuzingatia ushirikishaji wa wananchi katika kuhifadhi na kunufaika na uhifadhi huo.

 

 

 

Kuandaa na Kusimamia Sera

 

Mheshimiwa Spika,

9.    Katika mwaka 2003/2004 moja ya kazi za sekta hii ilikuwa kufanya mapitio ya Sera ya Wanyamapori pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Wanyamapori ili iendane na marekebisho yaliyoko kwenye sera.

 

Katika kipindi cha 2004/2005 sekta hii itakamilisha mapitio ya sera na sheria husika.

 

Kuanzisha Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori

 

Mheshimiwa Spika,

10.  Katika mwaka 2003/2004, Wizara yangu kwa kutumia wataalamu wake ilitoa elimu juu ya Kanuni za Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (Wildlife Management Areas Regulations – WMAs) za mwaka 2002 kwa baadhi ya viongozi Watendaji wa vijiji na Halmashauri za Wilaya 13 kati ya 16 ambazo zimo kwenye majaribio ya matumizi ya Kanuni hizo. Wilaya hizo ni Monduli, Kiteto, Ngorongoro, Kilolo, Morogoro, Rufiji, Tunduru, Songea, Tarime, Urambo, Sikonge, Namtumbo na Babati ambazo zimehusisha jumla ya vijiji 73.  Katika wilaya ya Serengeti elimu ilitolewa pia kwa wananchi kwenye mikutano ya hadhara katika vijiji vitano vinavyounda eneo la Majaribio la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori la Ikona.

 

Mheshimiwa Spika,

11.  Maeneo ya Majaribio ya Wilaya za Rufiji na Morogoro tayari yameshawasilisha maombi rasmi ya kutangazwa na Jumuiya za Jamii kutambuliwa kisheria kuwa zitasimamia wanyamapori katika ardhi za vijiji vya Tapika na Ngarambe kwa Wilaya ya Rufiji na eneo la Ukutu linalohusisha vijiji 23 kwa Wilaya ya Morogoro.  Wilaya zilizobaki zenye vijiji vilivyomo kwenye mpango wa Majaribio ya WMA, zimo katika hatua za kuandikisha Jumuiya za Jamii (Community - based Organisation - CBO) kwa mamlaka husika. Aidha, Wilaya 10 kati ya 17 zimeunda Bodi za Wilaya za Ushauri wa Masuala ya Maliasili.

 

Wizara imeandaa viashiria na mpango wa utekelezaji wa viashiria hivyo kwa ajili ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa Kanuni za Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori, ili kuwezesha tathmini ya utekelezaji wa Kanuni ifikapo miaka mitatu tangu zianze kutumika.

 

Katika kuendeleza uhamasishaji na elimu kwa umma vipindi vya radio 20 vilirushwa hewani na Redio Tanzania, picha za video 14 zilioneshwa katika Mikoa 7 na kipindi kimoja kilirushwa kupitia Televisheni ya Taifa.

 

Mheshimiwa Spika,

12.  Katika mwaka 2004/2005 Wizara itatoa mafunzo kwa watumiaji viashiria kuhusu ufuatiliaji wa mabadiliko kwenye WMA na utekelezaji wa mpango wa viashiria. Wizara itaendelea kutoa mafunzo kuhusu Kanuni za WMA katika vijiji na Jumuiya za Jamii na itaendelea kufuatilia kwa karibu uendeshaji na usimamizi wa Maeneo 16 ya Majaribio ya kanuni za Hifadhi ya Wanyamapori.

 

 

Ulinzi wa Wanyamapori

 

Mheshimiwa Spika,

13.  Ulinzi wa Wanyamapori uliimarishwa kwa kuwapatia watumishi mafunzo maalum pamoja na kuwapatia vitendea kazi. Hadi Aprili 2004, Doria zilizofanyika zilinasa watuhumiwa 1,700 na nyara mbalimbali za Serikali ikiwemo kilo 587.8 za meno ya tembo, kilo 79 za meno ya kiboko na ngozi 64 za wanyama. Vile vile, bunduki 349 za aina mbalimbali zilikamatwa.

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara itaendelea kuimarisha ulinzi kwa kuimarisha doria, kuwapatia watumishi 160 mafunzo kuhusu kupambana na ujangili pamoja na kuongeza vitendea kazi.

 

Ulinzi wa Maisha na Mali za Wananchi

 

Mheshimiwa Spika,

14.  Katika mwaka 2003/2004, siku 1,122 za doria zilitumika kusaka wanyamapori waharibifu katika Wilaya 24. Risasi 23,350 za aina mbalimbali zilinunuliwa kwa ajili ya kudhibiti wanyama waharibifu na kati ya hizo 3,080 zilitolewa kwa Halmashauri za wilaya 24.

 

Mheshimiwa Spika,

15.  Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itaendeleza ulinzi wa maisha na mali za wananchi dhidi ya wanyamapori kwa kuhakikisha upatikanaji wa risasi na kuwapatia mafunzo ya mbinu mbalimbali za kuthibiti wanyama waharibifu askari wa vijiji kwenye maeneo ya majaribio ya Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori.

 

Usimamizi na Uendelezaji wa Mapori ya Akiba

 

Mheshimiwa Spika,

16.  Mwaka 2003/2004, Wizara ilikamilisha mipango ya Uendeshaji wa Mapori ya Akiba ya Burigi/Biharamulo, na Ibanda/Rumanyika. Kazi ya kupitia mipango ya uendeshaji wa mapori ya akiba ya Ugalla na Mkomazi/Umba inaendelea. Barabara mpya zenye urefu wa kilometa 1,753 zilitengenezwa na nyingine zenye urefu wa kilometa 2,756 zilifanyiwa ukarabati. Viwanja vipya vya ndege vitano vilijengwa katika mapori ya akiba ya Selous, Moyowosi/Kigosi, Mpanga/Kipengere, Lukwika/Lumesule na Ugalla. Vile vile, viwanja 17 vilifanyiwa matengenezo ya kawaida. Mipaka ya mapori ya Lukwika/Lumesule, Rungwa/Kizigo, Ugalla, Mpanga/Kipengere, Moyowosi/Kigosi na Liparamba imepitiwa na kuchorwa upya. Kilometa 1,033 za mipaka ya mapori zimefanyiwa ukarabati. Katika mapori ya Usangu na Mpanga/Kipengere mipaka iliwekwa alama za kudumu. Aidha, nyumba 10 za watumishi zimejengwa na 42 kukarabatiwa katika vituo mbali mbali.

 

Vile vile, Wizara iliwahamisha wafugaji waliokuwa wanaishi ndani ya Pori la Akiba la Moyowosi.

 

Mheshimiwa Spika,

17.  Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itaendelea kupanua mtandao wa barabara katika mapori ya akiba kwa kulima barabara mpya zenye urefu wa kilomita 350 na kukarabati barabara zenye urefu wa kilomita 1,000. Aidha, Wizara itakamilisha kupitia mpango wa uendeshaji kwa mapori ya Akiba ya Ugalla na Mkomazi na itaandaa mipango ya Uendeshaji mapori ya Rukwa/Lukwika na Mpanga/Kipengele. Mpango wa uwekezaji wa pori la Akiba la Rungwa/Kizigo utafanyiwa mapitio na maandalizi ya mipango ya uendeshaji ya mapori ya Lukwika/ Lumesule, Swagaswaga na Mkungunero yataanza.

 

Usimamizi wa Ardhioevu

 

Mheshimiwa Spika,

18.  Katika mwaka wa 2003/2004, Wizara ilikamilisha kuorodhesha eneo la Bahari la Rufiji–Kilwa-Mafia kuwa eneo la ardhioevu yenye umuhimu wa kimataifa (Ramsar site). Hivyo tangu nchi yetu iliporidhia mkataba wa Ramsar mwaka 2002 ilishatenga maeneo manne muhimu yenye hadhi kama hiyo.  Vile vile, katika kuratibu masuala ya ardhioevu Wizara iliunda chombo cha juu kabisa cha kutoa maamuzi kuhusiana na uendelezaji wa ardhioevu kinachowahusisha Makatibu Wakuu wanane. Katika mwaka 2004/2005, wizara itaanza hatua za awali za kuorodhesha vinamasi (swamps) vya Bonde la Mto Kagera kuwa eneo lenye umuhimu wa kitaifa na itakusanya maoni ya wadau ili kuandaa mkakati wa kitaifa wa Ardhioevu.

 

Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori

 

Mheshimiwa Spika,

19.  Utafiti wa Wanyamapori umelenga kutathmini wingi wa rasilimali pamoja na kubaini magonjwa kwa lengo la kuwa na rasilimali endelevu ya wanyamapori.

 

20.  Katika kipindi cha 2003/2004, Taasisi ilifanya sensa za wanyamapori katika maeneo ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mapori ya Akiba ya Moyowosi/Kigosi na Ugalla. Aidha, Taasisi iliendelea na utekelezaji wa miradi ya utafiti wa ufugaji nyuki katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Dar es Salaam na Tabora, utafiti wa magonjwa ya wanyamapori, na utafiti wa wanyama wanaokula nyama.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Taasisi itaendelea kufanya sensa ya wanyamapori na ndege wa majini (water birds) pamoja na kuendeleza miradi ya utafiti. Taasisi pia itakarabati majengo ya kituo cha Tabora pamoja na kujenga ofisi ya makao makuu.

 

Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori

 

Mheshimiwa Spika,

21.  Mfuko umekuwa ukitegemea mapato toka kwa wahisani na wakereketwa wa uhifadhi wa wanyamapori. Fedha zinazopatikana zinatumika kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori.

 

Mheshimiwa Spika,

22.  Katika mwaka 2003/2004, Mfuko ulitarajia kukusanya shilingi bilioni 3.9.  Hadi kufikia Aprili 2004, Mfuko ulikuwa umekusanya shilingi bilioni 3.7.  Fedha hizo zilitumika kuimarisha doria za uzuiaji ujangili, miradi ya maendeleo, kugharimia utafiti na mafunzo ya uhifadhi.

 

Katika mwaka 2004/2005, Mfuko umekadiria kukusanya shilingi bilioni 3.8. Fedha hizo zitatumika kuimarisha na kuboresha usimamizi wa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira pamoja na ushirikishaji wananchi katika uhifadhi wa wanyamapori.

 

Shirika la Hifadhi za Taifa

 

Mheshimiwa Spika,

23.  Hifadhi za Taifa zimekuwa zikisimamia mbuga za wanyama zilizotengwa maalum kwa ajili ya utalii wa kuona na kupiga picha.

 

Katika kipindi cha 2003/2004 hadi Februari 2004, Shirika liliendesha doria za kuzuia ujangili na kufanikiwa kukamata majangili 1,799 na silaha mbalimbali 36 na mbao 2,104. Aidha, wanyama 326 wa aina mbalimbali waliuawa na majangili. 

 

Mheshimiwa Spika,

24.  Hadi kufikia Februari 2004, Watalii 304,105 walitembelea hifadhi za taifa. Idadi hii ni pungufu kwa asilimia 11.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2002/2003. Kupungua kwa watalii kunatokana na tishio la ugaidi na vita vya Iraq. Licha ya idadi ya watalii kupungua, mapato yaliongezeka ambapo Shirika lilikusanya shilingi bilioni 17.6 kutokana na shughuli za utalii ikilinganishwa na shilingi bilioni 17.5 zilizopatikana kufikia Februari 2003. Ongezeko hili linatokana na kuanzishwa kwa shughuli mpya za utalii kama utalii wa mitumbwi katika hifadhi ya Arusha pamoja na utalii wa kutembea kwa miguu kwenye hifadhi za Tarangire na Ruaha. Jumla ya kampuni 107 za utalii ziliendesha biashara ya utalii katika hifadhi za taifa.

 

Chini ya Mpango wake wa Ujirani Mwema, Shirika lilitumia Shilingi milioni 102.5 kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo.

 

Mheshimiwa Spika,

25.  Katika mwaka 2003/2004, Shirika liliendesha warsha tatu kwa ajili ya kupata maoni ya wadau ili kuandaa mipango ya uendeshaji ya Hifadhi za Serengeti na Mahale. Aidha, Wizara itawasilisha muswada kwa ajili ya kuanzisha hifadhi za Saadani na Kitulo pamoja na kupandisha hadhi ya Misitu ya Meru/Ngrudoto, Kilimanjaro/Marang na mashamba namba 1 – 3 ya Manyara kuwa sehemu za hifadhi.

 

Mheshimiwa Spika,

26.  Mipango na matarajio ya Shirika kwa mwaka 2004/2005, itaelekezwa katika kuboresha miundo mbinu kwa ajili ya utalii, kupanua wigo wa shughuli za utalii na kukamilisha mipango ya uendeshaji wa hifadhi za Mahale, Serengeti na Gombe. 

 

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro

 

Mheshimiwa Spika,

27.  Mamlaka inasimamia uhifadhi wa bonde la Ngorongoro ambalo ni kivutio maarufu cha utalii duniani. Eneo hilo linajumuisha hifadhi ya wanyamapori na makazi ya watu.

 

28.  Hadi kufikia Aprili 2004, watalii 219,761 walitembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.  Kati ya hao, 160,541 walitoka nje na 59,220 walikuwa watalii wa ndani ya nchi. Jumla ya Shilingi bilioni 8.5 zilikusanywa kutokana na watalii hao na kuvuka lengo la shilingi bilioni 6.9 la mwaka 2003/2004.

 

Mheshimiwa Spika,

29.  Katika mwaka wa 2003/2004, Mamlaka ilikamilisha ujenzi wa barabara kutoka Makao makuu ya Hifadhi hadi Kata ya Naiyobi, Olbalbal na Kakesio pamoja na barabara kutoka kata ya Endulen hadi kijiji cha Olpiro.

 

Mheshimiwa Spika,

30.  Katika kipindi cha 2004/2005, Mamlaka inatazamia ongezeko la asilimia 10% ya watalii watakaotembelea Hifadhi ambao wataingiza Shilingi bilioni 7.7. Ili kuhakikisha mapato endelevu, Mamlaka itajenga jengo la kitega uchumi mjini Arusha, pamoja na kununua vitendea kazi kwa ajili ya ujenzi na kuimarisha barabara.

 

Aidha, Mamlaka itakamilisha ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Embarway kwa kujenga madarasa nane na nyumba tano za watumishi.

 

SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI

 

Mheshimiwa Spika,

31.  Sekta hii katika kutekeleza majukumu yake imetoa kipaumbele katika kutekeleza Sera na marekebisho ya sheria, usimamizi shirikishi wa misitu pamoja na uendelezaji wa mashamba ya miti na hifadhi za nyuki. Ili Sera ya Taifa ya Misitu ya 1998 na Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya 1998 ieleweke kwa wadau, Wizara iliweka sera hizi katika tovuti ya Wizara ili wadau wengi waweze kuzipata.

 

Usimamizi Shirikishi wa Misitu

 

Mheshimiwa Spika,

32.  Katika mwaka 2003/2004, Wizara iliendesha mafunzo ya usimamizi shirikishi wa misitu katika wilaya 15.  Vile vile, vijiji 39 katika wilaya za Mpwapwa, Same, Kondoa, Dodoma Vijijini, Lindi na Kilwa viliwezeshwa kuandaa Mipango ya Usimamizi Shirikishi wa misitu na hifadhi za nyuki.  Katika kuboresha uhifadhi wa Misitu ya Hifadhi ya vyanzo vya maji na mikoko, uhamasishaji ulifanyika katika vijiji 72 kwenye wilaya 28. 

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara itatekeleza mpango wa usimamizi shirikishi wa misitu katika wilaya 37 kwenye Mikoa ya Morogoro, Lindi, Iringa, Mbeya, Mtwara, Ruvuma, Pwani, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma, Tabora, Kigoma, Rukwa, Mwanza, Kagera na Shinyanga. 

 

Uvunaji wa Mazao ya Misitu

 

Mheshimiwa Spika,

33.  Katika mwaka 2003/2004 hadi Aprili 2004, magogo yenye mita za ujazo 24,866 yalivunwa katika misitu ya asili, na mita za ujazo 309,100 katika mashamba ya miti. 

 

Mwaka 2004/2005, magogo yenye mita 25,000 za ujazo katika misitu ya asili na mita za ujazo 350,000 katika mashamba ya miti yatavunwa.  Ili kuboresha usimamizi wa uvunaji wa mazao ya misitu, utoaji wa leseni za kuvuna miti utashirikisha wilaya na serikali za vijiji.  Utaratibu huu utaanza katika wilaya 20 ambazo zitaunda kamati za kujadili maombi ya leseni.

 

Biashara ya Nje ya Mazao ya Misitu na Nyuki

 

Mheshimiwa Spika,

34.  Mwaka 2003/2004, Wizara ilikadiria kuwa sekta binafsi itauza mazao ya misitu yenye thamani ya shilingi bilioni 9.8.  Hadi kufikia Aprili 2004, mazao ya misitu na nyuki yenye thamani ya shilingi bilioni 11.6 yaliuzwa.

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara inatarajia sekta binafsi itauza mazao ya misitu na nyuki yenye thamani ya shilingi bilioni 10.9. Aidha, kuanzia tarehe 1 Julai 2004, usafirishaji wa magogo nje ya nchi hautaruhusiwa.  Madhumuni ni kuendeleza sekta ya viwanda, kuongeza ajira na thamani ya bidhaa.

 

 

 

 

Usimamizi na Uendelezaji wa Mashamba ya Miti

 

Mheshimiwa Spika,

35.  Maandalizi ya upigaji picha za anga katika mashamba ya Sao Hill, Kiwira, Buhindi, Meru na Kilimanjaro Kaskazini yalikamilika ikiwa ni sehemu ya kukamilisha taratibu za kuwashirikisha wadau katika kusimamia mashamba hayo.

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara itakuza miche milioni 7.5 na kupanda miti hekta 5,000.  Vile vile, itapogoa miti katika hekta 3,000 na kupunguza miti katika hekta 1,000.

 

Kuendeleza Ufugaji Nyuki

 

Mheshimiwa Spika,

36.  Mwaka 2003/2004, Wizara iliwezesha kutenga na kuchora ramani za Hifadhi za vijiji vya Tura na Kizengi katika wilaya ya Uyui.  Shughuli za ugani zilifanyika katika Wilaya za Newala, Lindi, Masasi, Kahama, Songea, Dodoma, Manyoni, Mpanda na Uyui. 

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara itatoa huduma za ugani katika wilaya 10 na kutangaza hifadhi 4 za nyuki za vijiji.

 

Taasisi ya Utafiti wa Misitu

 

Mheshimiwa Spika,

37.  Taasisi ililenga kuendeleza usimamiaji na uratibu wa utafiti wa misitu kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kitaifa na kimataifa, pamoja na kutoa ushauri ili kuendeleza rasilimali za misitu.

 

Katika mwaka 2004/2005, Taasisi itapanua na kuimarisha utafiti wa kilimo misitu katika mikoa ya Pwani, Shinyanga, Mwanza, Tabora na Tanga, kwa lengo la kuwafikia wakulima 1,000.  Vile vile, itafanya utafiti wa kuzalisha vyahuso (cloning) ya mikaratusi inayokua haraka katika vitalu vya majaribio vilivyoko Arusha, Lushoto, Mombo, Korogwe, Kibaha, Morogoro, Dodoma na Mufindi.

 

 

 

Wakala wa Mbegu za Miti

 

Mheshimiwa Spika,

38.  Madhumuni ya Wakala ni kuwezesha upatikanaji endelevu wa mazao ya misitu na utunzaji wa mazingira kwa kuzalisha na kusambaza mbegu bora za miti pamoja na vipandikizi vingine.

 

39.  Hadi kufikia Aprili 2004, Wakala ulikusanya kilo 13,500 za mbegu, ambapo kilo 10,582 ziliuzwa nchini na 38 nchi za nje.  Vile vile, miche 20,000 ilikuzwa.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wakala inalenga kupanua upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora za miti kwa kukusanya kilo 12,500 za mbegu za miti, kuuza kilo 10,000 nchini na kilo 50 nchi za nje. 

 

 

 

 

 

SEKTA NDOGO YA UVUVI

 

Mheshimiwa Spika,

40.  Sekta Ndogo ya Uvuvi ina mchango mkubwa katika upatikanaji chakula nchini. Katika kuzingatia hilo, mpango kamambe wa kutekeleza Sera ya Uvuvi umeanza kwa kuanzisha miradi mbalimbali. Sekta ndogo ya uvuvi imelenga kuimarisha masoko na vituo vya kupokelea samaki, kuhamasisha ufugaji wa samaki na mazao ya baharini pamoja na kudhibiti ubora wa mazao.

 

Utekelezaji wa Mpango Kamambe

 

Mheshimiwa Spika,

41.  Mwaka 2003/2004, Wizara ilianza kutekeleza Mpango Kamambe wa kuendeleza Sekta ya Uvuvi kwa kuanza ujenzi wa soko la kisasa la Kirumba katika Manispaa ya Mwanza.  Vile vile, ilianza kutekeleza mradi wa kuhifadhi mazingira ya Ziwa Tanganyika pamoja na kuendeleza huduma za kiuchumi kwa wavuvi na huduma za jamii, ambao unahusisha nchi zinazomiliki ziwa hilo. 

Ufugaji wa Samaki na Ukulima wa Mwani

 

Mheshimiwa Spika,

42.  Katika mwaka 2003/2004, Wizara yangu iliendeleza juhudi za kuboresha ufugaji samaki pamoja na ukulima wa mwani.  Wizara ilitoa mafunzo ya uhamasishaji juu ya ufugaji bora wa samaki kwa wananchi 1,472. Aidha, Wizara ilitoa mafunzo kwa wasimamizi wa vituo vya kuzalisha mbegu bora ya samaki aina ya perege katika Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.  Jumla ya wananchi 153 walinufaika na mafunzo hayo.

 

Mheshimiwa Spika,

43.  Katika kuendeleza kilimo cha Mwani, katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itatoa mafunzo kwa wakulima wa mwani 70.

 

Udhibiti wa Ubora wa Mazao na Masoko

 

Mheshimiwa Spika,

44.  Mwaka 2003/2004, Wizara ilikagua viwanda 26 vya kusindika mazao ya samaki na meli za uvuvi 25.  Washiriki 4,838 kutoka sekta binafsi walipewa semina kuhusu njia bora za kusindika na kusafirisha mazao ya uvuvi.

 

Katika mwaka 2004/2005, sampuli 2,842 za minofu zitachukuliwa kuhakiki ubora, 562 za minofu na maji zitapimwa kuchunguza uchafuzi utokanao na dawa za kuua wadudu wa mimea. Vile vile, sampuli 2,000 za minofu zitapimwa kudhibiti uchafuzi utokanao na mionzi viwandani. Kaguzi 16 zitafanyika viwandani kuhakiki kiwango cha usafi unaokubalika kimataifa.  Pia, Watumishi 40 watapatiwa elimu ya ukaguzi wa mazao ya uvuvi na wadau 1,480 watapata mafunzo ya uzalishaji bora wa mazao ya uvuvi.  Vituo vitano vya ukaguzi wa mazao vya Mafia, Kilwa, Bukoba, Musoma na Mwanza vitaimarishwa na maabara ya Nyegezi itakamilishwa.

 

Mheshimiwa Spika,

45.  Serikali imeamua kwa mara ya kwanza kuanzia Juni 2004 kuruhusu kuuza nje ya nchi samaki wa mapezi wa baharini ili kuinua kipato cha wavuvi wadogo wadogo na pato la Taifa.  Uamuzi huu ulifikiwa kutokana na matakwa ya wananchi wa Ukanda wa Pwani.  Mawasiliano ya kina yalifanywa na wadau kabla ya kufikia uamuzi huu.

 

Udhibiti wa Uvuvi Bora

 

Mheshimiwa Spika,

46.  Mwaka 2003/2004, doria zilifanyika kwenye maeneo mbalimbali ambapo watuhumiwa 31na nyavu 2,143 zenye ukubwa tofauti zilikamatwa na kuharibiwa kwa amri ya Mahakama.

 

Doria 12 zilifanyika pia kwenye Bahari ya Ndani na kwenye Ukanda wa Uchumi ambapo 6 zilikuwa ni kwa meli na 6 ni kwa ndege, na meli tatu zilishikwa kwa tuhuma ya kukiuka masharti ya leseni na kusafirisha mizigo kinyume na sheria. 

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itaendesha doria ya siku 12,500 za kazi ili kudhibiti uvuvi haramu na kuzuia biashara ya magendo.  Mtambo maalum wa Kompyuta utanunuliwa kwa madhumuni ya kuratibu mwenendo wa meli zinazovua kwenye Ukanda wa uchumi wa Bahari.

Elimu kwa Umma

 

Mheshimiwa Spika,

47.  Mwaka 2003/2004, Wizara ilitoa elimu kwa umma kuhusu uvuvi bora kwa kurusha vipindi 160 vya redio na 10 vya televisheni.  Ukusanyaji wa takwimu uliimarishwa kwa kuwapa masomo ya muda mfupi watumishi 86 na kuongeza vitendea kazi.

 

Mwaka 2004/2005, Wizara itatoa elimu kuhusu uvuvi bora kwa umma kwa kurusha hewani vipindi 138 vya redio na 10 vya televisheni. Sensa ya wavuvi na zana itafanyika kwenye Ukanda wa Pwani na Maziwa Makubwa pamoja na kutoa mafunzo kwa wakusanya takwimu 60 ili kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali.

 

Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu

 

Mheshimiwa Spika,  

48.  Mwaka 2003/2004, Wizara yangu kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ilikamilisha upembuzi yakinifu kuona jinsi gani Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, pamoja na rasilimali za Bahari na mwambao zinavyoweza kuchangia katika juhudi za kuondoa umaskini.  Matokeo ya upembuzi huo ni utayarishaji wa mpango ambao utahusika na usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na mwambao. Mpango huu vile vile utahusisha sehemu ya Tanzania Visiwani (Zanzibar). Aidha, Wizara yangu ilikamilisha ujenzi wa kituo cha taifa (Visitors Information Centre) katika Maeneo Tengefu ya Visiwa vya Bongoyo na Mbudya. 

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara itakamilisha utayarishaji wa Mpango wa mchakato wa muda mrefu (Long Term Strategic Plan). Aidha, Wizara itakamilisha utayarishaji wa Mkakati wa usimamizi wa fukwe za bahari na visiwa vidogo, Hifadhi za Bahari ya Ghuba ya Mnazi na maingilio ya Mto Ruvuma na Maeneo Tengefu ya Dar es Salaam Kaskazini.

 

Kadhalika, Wizara itakamilisha Kanuni za kutekeleza Sheria ya Hifadhi za Bahari Na. 29 ya 1994 katika Hifadhi za Bahari ya Mafia na Ghuba ya Mnazi.

 

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi

 

Mheshimiwa Spika,

49.  Utafiti wa Uvuvi umekuwa ukifanyika kwa lengo la kubaini wingi wa rasilimali na kutoa ushauri kuhusu matumizi endelevu.

 

Katika mwaka 2003/2004, Taasisi ilifanya utafiti wa Kamba katika maeneo ya Pwani ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara ili kubaini wingi wa samaki katika maeneo hayo.  Kutokana na utafiti huo msimu wa uvuvi wa kamba ulipangwa kuanza rasmi tarehe 01 Aprili 2004 na utaishia Septemba 2004 badala ya Machi - Novemba ya kila mwaka.

 

Mheshimiwa Spika,

50.  Samaki “kisukuku” anayesadikika kuishi miaka takribani milioni 60 iliyopita alipatikana kwa mara ya kwanza kwenye maji ya Tanzania.   Taarifa za kuaminika ni kwamba tokea samaki huyu apatikane huko Kilwa Masoko, idadi ya watalii imeanza kuongezeka. Taasisi za Utafiti za nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi zimeweka mkakati wa kufanya utafiti wa samaki huyo.

 

Mheshimiwa Spika,

51.  Katika mwaka 2004/2005, ujenzi wa Makao Makuu ya Taasisi na Kituo cha Utafiti cha Dar es Salaam utaanza.

 

SEKTA NDOGO YA UTALII

 

Mheshimiwa Spika,

52.  Utalii ni sekta ambayo inaweza kuchangia ukuaji wa kasi wa pato la taifa.  Katika kutekeleza majukumu yake, sekta hii itakamilisha maandalizi ya utekelezaji wa Sera ya Utalii na pia itatilia mkazo kukuza na kuimarisha utalii wa ndani.

 

Mheshimiwa Spika,

53.  Mwaka 2003/2004, biashara ya utalii ulimwenguni iliathiriwa na vita vya Iraq, ugonjwa wa mafua (SARS) na ugaidi. Mataifa mbalimbali hasa yale ambayo ni masoko ya utalii duniani yalitoa tahadhari ya usafiri kwa wananchi wake kutotembelea maeneo fulani kwa hofu ya kutokuwa salama.  Kutokana na hali hii, watalii 576,198 waliingia nchini ikilinganishwa na matarajio ya watalii 603,990 na kuliingizia taifa Dola za Kimarekani milioni 731.

 

Watalii wa ndani waliongezeka kutoka 270,934 mwaka 2002 hadi 297,077 mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, lengo ni kupokea watalii 607,000 kutoka nje ya nchi, watakaoliingizia Taifa Dola za Kimarekani milioni 750.

 

Uendelezaji Utalii

 

Mheshimiwa Spika,

54.  Katika mwaka 2003/2004, Wizara ilibaini na kutathmini vivutio na maeneo ya uendelezaji utalii katika mikoa ya Singida, Mtwara, Mwanza na Mara.  Aidha, taarifa na picha za vivutio mbalimbali katika mikoa hiyo ziliandaliwa.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itafanya semina za uhamasishaji katika mikoa ya Singida, Lindi na Mtwara na kuandaa taarifa na picha za vivutio vya utalii katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.

 

Ushirikiano katika Utalii

 

Mheshimiwa Spika,

55.  Katika mwaka 2003/2004, Wizara ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Amani kupitia Utalii uliohudhuriwa na washiriki 350. Vile vile, Wizara ilishiriki kwenye mikutano ya Shirika la Utalii ya nchi za Jumuiya ya Madola na “Africa Travel Association” iliyofanyika Malaysia na Cameroon sawia kwa madhumuni ya kukuza ushirikiano.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itakuwa mwenyeji wa semina ya Shirika la Utalii Duniani kuhusu Maendeleo ya Utalii na Kupunguza Umaskini (Regional Seminar on Tourism Development and Poverty Alleviation) itakayofanyika Septemba 2004.

 

 

Uwekezaji katika sekta ya Utalii

 

Mheshimiwa Spika,

56.  Mwaka 2003/2004, Wizara iliteua Kampuni ya “DCDM Consulting Group” kutoa ushauri kuhusu masuala ya uwekezaji katika sekta ya utalii. Randama (Memorandum) ya maeneo yanayofaa kwa uwekezaji na ripoti ya Mpango wa Kudhamini Wawekezaji wadogo vimekamilika. Vile vile, Wizara ilitayarisha Kanzidata ya wawekezaji watarajiwa.

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara itatayarisha jarida litakalotoa habari za kina za fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii.

 

Kuboresha Huduma za Utalii

 

Mheshimiwa Spika,

57.  Mwaka 2003/2004, Wizara kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ilikamilisha rasimu ya vigezo vya kupanga hoteli, migahawa na loji za kitalii katika daraja. Aidha, watumishi wanne wamepata mafunzo kuhusu taaluma ya kusimamia zoezi hilo nchini Afrika ya Kusini. 

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itaendesha semina kwa wadau kuhusu vigezo hivyo na kuanza kuendesha zoezi hilo. 

 

Kuboresha Takwimu za Utalii

 

Mheshimiwa Spika,

58.  Mwaka 2003/2004, Wizara ilikamilisha ripoti ya matokeo ya utafiti wa wageni wanaotoka nje. Vile vile, iliendelea na ukusanyaji wa takwimu mbalimbali kutoka kwa watoa huduma za kitalii kwa ajili ya kutengeneza mfumo mpya wa ukusanyaji takwimu unaojulikana kama “Tourism Satellite Account”. Utafiti huo ulifanyika katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Iringa, Singida na Mtwara. Aidha, Wizara ilianzisha tovuti inayoitwa www.tourismtanzania.go.tz ambayo inatoa taarifa muhimu za sekta ya utalii.

 

Kwa mwaka 2004/2005, Wizara itaendelea kukusanya takwimu za watoa huduma za utalii katika vituo vyote vya maingilio ya watalii pamoja na kuboresha tovuti.

 

Bodi ya Utalii

 

Mheshimiwa Spika,

59.  Bodi imekuwa na jukumu la kutangaza utalii kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuharakisha ukuaji wa sekta ya utalii.

 

Katika mwaka 2003/2004, Bodi ilifanya ziara 22 za kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi. Vile vile, ilichapisha nakala 75,000 za majarida na 150,000 za vipeperushi.

 

Mwaka 2004/2005, Bodi itaendelea kutafuta masoko mapya ya watalii hasa kutoka Bara la Asia, China na Urusi kutokana na matatizo ya ugaidi yanayozikumba nchi za magharibi.

 

Wakala wa Serikali wa Chuo cha Taifa cha Utalii

 

Mheshimiwa Spika,

60.  Wakala unatoa mafunzo ya Cheti katika fani ya utalii na hoteli. 

 

Mwaka 2003/2004, Wizara ilipata milki ya viwanja viwili vilivyopo Mtaa wa Shaaban Robert Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Utalii kitakachotoa mafunzo katika ngazi ya Stashahada. Aidha, Serikali imesaini Mkataba wa Ushirikiano na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho ambacho kitatoa elimu ya ngazi ya juu zaidi.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara inatarajia kuanza ujenzi huo utakaogharimu Shilingi bilioni tano. Chuo kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kutoa wahitimu wa ngazi ya usimamizi katika fani ya hoteli ili kupunguza waajiriwa wageni katika hoteli nyingi hapa nchini.

 

 

SEKTA NDOGO YA MAMBO YA KALE

 

Mheshimiwa Spika,

61.  Sekta ya Mambo ya Kale ina jukumu la kulinda, kutafiti na kuhifadhi urithi wa Mambo ya Kale.  Utekelezaji wa jukumu hili umezingatia mwono na wito wa Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997, Sheria ya Mambo ya Kale ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya 1979.  Kutokana na Sekta ya Mambo ya Kale kutokuwa na Sera yake, katika mwaka 2004/2005 Wizara yangu itaandaa Sera ya Mambo ya Kale.

 

Utafiti wa Mambo ya Kale

 

Mheshimiwa Spika,

62.  Mwaka 2003/2004, Wizara iliendelea kufanya utafiti wa akiolojia huko Kinole na Kola Hill, Mkoani Morogoro. Aidha, Wizara iliratibu na kusimamia utafiti wa akiolojia huko Ngorongoro katika Bonde la Olduvai, eneo la Laitoli, Engaruka, Ziwa Eyasi, Hifadhi ya Taifa Serengeti na Ziwa Natron.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itafanya utafiti wa kuboresha historia ya maeneo ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara. Aidha, Wizara itakamilisha mpango wa uhifadhi endelevu wa mji mkongwe wa Bagamoyo na kuanza kuboresha baadhi ya vivutio vilivyoko kwenye njia ya kati ya utumwa kutoka Ujiji hadi Bagamoyo.

 

Uhifadhi na Uendelezaji wa Vituo vya Mambo ya Kale

 

Mheshimiwa Spika,

63.  Katika mwaka 2003/2004, Wizara ilikamilisha ujenzi wa vituo vya kumbukumbu na habari vya Isimila Mkoani Iringa na Kolo Mkoani Dodoma. Vile vile, Wizara ilikamilisha ukarabati wa jengo la Caravan Serai, Bagamoyo Mkoani Pwani litakalotumika kama kituo cha habari na kumbukumbu.

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara itaendelea na ujenzi wa vituo vya kumbukumbu na taarifa vya Ujiji, Mkoani Kigoma na Kaole, Mkoani Pwani.

Uhifadhi wa Eneo la Kilwa Kisiwani

 

Mheshimiwa Spika,

64.  Katika mwaka 2003/2004, Wizara ilikamilisha ukarabati wa nyumba ya Kijerumani, uimarishaji wa gofu la Msikiti Mkuu na jengo la Kireno huko Kilwa Kisiwani.  Aidha, Wizara ilikamilisha ujenzi wa gati, kuweka umeme wa mionzi ya jua na mawasiliano ya redio ya upepo.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itafanya tafiti za kiakiolojia, historia, usanifu majengo, elimu jamii na kuandaa mpango wa uendeshaji wa Kilwa Kisiwani.

 

Uhifadhi wa Mji wa Kihistoria, Bagamoyo

 

Mheshimiwa Spika,

65.  Katika mwaka 2003/2004, Wizara iliingia mkataba na serikali ya Sweden kugharimia mradi wa uboreshaji njia ya kati ya biashara ya utumwa, vipusa na meno ya tembo ili iingizwe kwenye orodha ya Urithi wa Dunia. Katika mwaka 2004/2005, Wizara itaanza kutekeleza mkataba huo.

SHIRIKA LA MAKUMBUSHO YA TAIFA

 

Mheshimiwa Spika,

66.  Shirika linatekeleza jukumu la kukusanya, kuhifadhi na kutafiti vitu vyote vya urithi wa kihistoria, kiutamaduni, kisayansi na kiteknolojia. Taarifa za urithi huo huhifadhiwa na kutumika kuelimisha Umma.

 

Mheshimiwa Spika,

67.  Katika mwaka 2003/2004, Shirika lilifanya uhamasishaji wa jamii ili zihifadhi na kuuenzi utamaduni wao. Jamii ya Wamwera ilihamasishwa na kufanya tamasha la Siku ya Utamaduni wa Mtanzania katika Kijiji cha Makumbusho. Aidha, katika mwaka 2003/2004, Shirika liliendelea na maandalizi ya ujenzi wa Jumba la Utamaduni kwa kuwashirikisha wadau ambapo warsha mbili zilifanyika kupata maoni yao. Watendaji wa Makumbusho pia walipata fursa ya kutembelea nchi nyingine kupata uzoefu wa uendeshaji wa majumba ya Makumbusho.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Shirika litaendelea na Mpango wa maandalizi ya ujenzi wa jumba la utamaduni na kutafuta wafadhili wa ujenzi wa jumba hilo. 

 

Mheshimiwa Spika,

68.  Mwaka 2003/2004, Shirika lilianza kufanya utafiti wa akiolojia wilaya ya Iringa na utafiti wa Viumbe Bahari huko Kaole, Wilayani Bagamoyo. 

 

Katika mwaka 2004/2005, Shirika litaendeleza utafiti wa akiolojia katika Wilaya ya Iringa na utafiti wa viumbe bahari katika Wilayani Mafia.

 

UTAWALA NA UTUMISHI

 

Maendeleo ya Watumishi na Mafunzo

 

Mheshimiwa Spika,

69.  Katika kipindi cha 2003/2004, Wizara ilikuwa na watumishi 3,484.  Pamoja na idadi hiyo, bado kuna upungufu wa watumishi. Matarajio yalikuwa ni kuajiri watumishi 166 lakini watumishi walioajiriwa katika ajira mbadala ni 20.

 

Katika Mwaka 2004/2005, Wizara inatarajia kuajiri watumishi wapya 152.

 

Mheshimiwa Spika,

70.  Katika mwaka wa fedha 2003/2004, Wizara ilitegemea kuwapandisha cheo watumishi 286 wa kada mbalimbali.  Hadi mwezi Aprili 2004, watumishi 150 walikuwa wamepandishwa cheo. Mapendekezo mengine yako Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara inatarajia kuwapandisha cheo watumishi 326.

 

Mheshimiwa Spika,

71.  Jumla ya watumishi 323 walipatiwa mafunzo ya taaluma mbalimbali ya muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi katika mwaka 2003/2004. Aidha, katika kuendana na mabadiliko ya teknolojia na utandawazi Wizara imefanya zoezi la kubaini mahitaji ya mafunzo kwa watumishi na kuandaa Mpango wa Mafunzo. 

 

Katika mwaka wa fedha 2004/2005, Wizara itaanza kutekeleza Mpango wa Mafunzo.

 

Ustawi wa Watumishi

 

Mheshimiwa Spika,

72.  Katika kuboresha Ustawi wa Watumishi Wizara imeingia Mkataba na Benki mbalimbali unaowawezesha watumishi kukopa fedha. Hata hivyo, tatizo lililojitokeza ni riba kubwa inayotozwa kwa mikopo. Wizara pia ina mipango ya kukabiliana na janga la ukimwi.

 

Vyuo vya Wizara

 

Mheshimiwa Spika,

73.  Mwaka 2003/2004, Wizara iliendelea kuboresha vyuo kwa kukarabati majengo na kuboresha mitaala pamoja na kuvipatia vifaa vya kufundishia ili vilingane na mahitaji ya soko.

 

Aidha, hatua mbalimbali zilichukuliwa na vyuo ili vipate usajili wa kudumu kutoka Baraza la Taifa la Usajili wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi. Chuo cha Wanyamapori Mweka ambacho kilithibitishwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa kituo cha mafunzo bora ‘Centre of Excellence’ katika fani ya wanyamapori, kinatarajia kupanua soko lake kwenye nchi za maziwa makuu na kupanua wigo wa mafunzo ya muda mfupi pamoja na kuridhia mikataba ya ushirikiano na vyuo, taasisi za elimu na utafiti ndani na nje ya nchi. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vyuo vya Elimu ya Ufundi Stadi itakamilisha mtaala wa kitaifa wa fani ya Utalii ambao utawezesha kudhibiti na kuboresha kiwango cha elimu kinachotolewa na vyuo vya utalii hapa nchini.

 

Chuo cha Uvuvi Mbegani kimefikia katika hatua za mwisho za kupata usajili wa awali wa Baraza la Taifa la Usajili wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi. Pamoja na mafunzo ya kawaida, lengo la Wizara ni kuinua hadhi ya Chuo hiki ili kiwe taasisi ya kuendeleza shughuli za uvuvi katika Ukanda wa Bahari (Fisheries Development Centre) kama kilivyokuwa hapo awali.

 

Mkataba wa Huduma kwa Mteja,

 

Mheshimiwa Spika,

74.  Katika kutekeleza Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao ulizinduliwa mwaka juzi, kila Idara imeandaa mkataba wake wa jinsi ya kuwahudumia wateja kwa ufanisi. Katika mwaka 2004/2005 Wizara itaendelea kutekeleza mkataba huo. Aidha, Taasisi na Mashirika yaliyo chini wa Wizara yametakiwa kuandaa mikataba ya Huduma kwa wateja wao.

 

Utawala Bora

 

Mheshimiwa Spika,

75.  Mwaka 2003/2004, Wizara iliandaa mafunzo ya utawala bora kwa viongozi wa vyuo, taasisi, mashirika na wakala wa serikali.  Wakuu wa vyuo na Maafisa Maliasili wa Mikoa walipata mafunzo hayo yaliyolenga kubaini namna na kuzuia vitendo vya rushwa na kuimarisha utendaji unaozingatia misingi ya utawala bora. Kila Taasisi, Mashirika na Wakala wameagizwa kuwa na mipango ya kupambana na rushwa na kuimarisha utawala bora katika maeneo yao. 

 

Katika mwaka 2004/2005, Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya utawala bora kwa watumishi katika ngazi mbalimbali.

 

Kurekebisha Mashirika ya Umma

 

Mheshimiwa Spika,

76.  Hadi Aprili 2004, Mashirika 27 kati ya 33 yaliyokuwa chini ya Wizara yalikuwa yamerekebishwa au kubinafsishwa. Mashirika 19 yamesaini mikataba ya mauzo na 8 yamesaini makubaliano ya awali. Kati ya Mashirika 6 yaliyobaki, 4 yamefilisiwa, moja shughuli zake zimefungwa na moja bado halijafanyiwa marekebisho.

 

Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara itaendeleza urekebishaji wa mashirika yaliyosalia pamoja na kufuatilia maendeleo ya uendeshaji kwa yale yaliyorekebishwa.

 

MWISHO

 

Mheshimiwa Spika,

77.  Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, Wananchi na Wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Wizara yangu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake.

 

Aidha, natoa shukurani kwa washirika wetu wa maendeleo wafuatao kwa michango yao ya kifedha na kitaalamu kama ifuatavyo: Norway, Denmark, Finland, Marekani, Sweden, Japan, Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Uingereza, Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU), ADB, AWF, FAO, FZS, GTZ, IUCN, KfW, Trade Aid, MIGA, AFRICARE, UNESCO, UNDP, World Bank, WWF, ICCROM na mengineyo.

 

 

 

Mheshimiwa Spika,

78.  Naomba kutoa shukurani zangu za dhati kwa Katibu Mkuu, Bw. Salmon Odunga, Wakurugenzi na wafanyakazi wote wa Wizara na Taasisi zake, kwa ushirikiano walionipa na kuiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake katika mwaka 2003/2004.

 

Mheshimiwa Spika,

79.  Ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na malengo yake katika kipindi cha 2004/2005, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe makadirio ya matumizi ya Shilingi 47,123,892,100. Kati ya fedha hizo, Shilingi 18,970,499,400 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Shilingi 28,153,392,700 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.

 

Mheshimiwa Spika,

80.  Naomba kutoa hoja.