HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA

MHESHIMIWA ANNA MARGARETH ABDALLAH, MBUNGE, KUHUSU MAKADIRIO YA

MATUMIZI YA FEDHA

KWA MWAKA 2005/2006

 

 

 

UTANGULIZI

 

1.                 Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyochambua bajeti ya Wizara ya Afya, naomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako likubali kupokea na kujadili taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Afya kwa mwaka 2004/2005 na malengo ya bajeti ya mwaka 2005/2006.  Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Kawaida na ya Mpango wa Maendeleo kwa ajili ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2005/2006.

 

2.                 Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa, Makamu wa Rais, Mhe. Dr. Ali Mohamed Shein na Waziri Mkuu, Mhe. Frederick Tluway Sumaye, (Mb.), kwa uongozi wao wa busara ambao umewezesha kupatikana kwa maendeleo makubwa katika Serikali ya awamu ya tatu hasa katika kufufua na kukuza uchumi na kutoa huduma bora za jamii ikiwemo Afya.  Hapana shaka  kuwa mafanikio haya yataendelea kukipatia Chama cha Mapinduzi ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao. Aidha wameonyesha mfano wa kuigwa katika suala zima la kupunguza umaskini na kuhakikisha kuwa amani inadumishwa hapa nchini.

 

3.       Mheshimiwa Spika, nawapongeza kwa dhati Mheshimiwa Dr. Abdallah Omari Kigoda (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji na Mheshimiwa Basil Pesambili Mramba, (Mb.), Waziri wa Fedha kwa hotuba zao nzuri za Hali ya Uchumi Nchini, Mipango ya Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2005/2006.  Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Frederick Tluway Sumaye, Mbunge wa Hanang, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake inayoonyesha jinsi Serikali ya Awamu ya Tatu ilivyotekeleza majukumu yake na kuonyesha jinsi Serikali ya Awamu ya Nne itakavyotekeleza majukumu yake katika mwaka 2005/2006. Ninampongeza Mheshimiwa Brigedia Jenerali (Mstaafu) Hassan Ngwilizi, (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambaye kwa pamoja tunashirikiana kutoa huduma za afya kwa wananchi. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hotuba  zilizotangulia, michango yao imesaidia sana kuboresha hotuba yangu.  Ninawaahidi kwamba Wizara itazingatia ushauri wao katika kutekeleza bajeti ya Wizara yangu.

 

4.                 Mheshimiwa Spika,  napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge wote walionitangulia kusema, kuwapongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Mbunge wa Chalinze, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kuchaguliwa na Chama cha Mapinduzi kuwa Mgombea Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  Mhe. Dr. Ali Mohamedi Shein, Makamu wa Rais kwa kuchaguliwa kuwa Mgombea Mwenza.  Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Amani Abeid Karume, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi kuwa mgombea wa Urais na Uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar.  Sote tuna imani kuwa kuteuliwa kwao na Chama cha Mapinduzi kupeperusha bendera ya Chama    kutaleta ushindi mkubwa kwa Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi ujao.

 

5.       Mheshimiwa Spika,  tangu mwaka jana niliposimama hapa kuwasilisha bajeti yangu baadhi ya Wabunge wenzetu wamefariki dunia.  Natoa rambirambi kwa familia za wafiwa na namwomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira kwa yote yaliyowafika.  Waheshimiwa Wabunge waliofariki dunia ni Mheshimiwa Captain (Mstaafu) Theodorus James Kasapira, aliyekuwa Mbunge wa Ulanga Mashariki,  Mheshimiwa Frank Michael  Musati aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mashariki.  Mheshimiwa Balozi Ahmed Hassani Diria,  aliyekuwa Mbunge wa Raha Leo na Mheshimiwa Abu-Towegale Kiwanga, aliyekuwa Mbunge wa Kilombero. Tukio la ghafla la kifo cha mwenzetu Mheshimiwa Magreth Bwana, aliyekuwa Mbunge wa CCM Viti Maalum limetutia simanzi sio tu sisi Wabunge bali hata Watanzania wote hasa wananchi wa Sumbawanga.  Kwa kuwa hakina mwenyewe lililobaki kwetu sote ni kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peoponi.  Amina.

 

 

6.       Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru kwa dhati Kamati ya Huduma za Jamii ya Bunge lako Tukufu, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Omar Shaban Kwaangw’, Mbunge wa Babati Mashariki kwa ushauri walioutoa ambao umeendelea kuboresha huduma za Sekta ya Afya pamoja na matayarisho ya bajeti ya Wizara yangu ambayo naiwasilisha mbele ya Bunge lako tukufu.  Kwa kuwa hiki ni kikao cha mwisho cha Bunge la Serikali ya Awamu ya Tatu, ninawatakia wajumbe wote wa kamati hii kila la kheri katika uchaguzi ujao na ni matumaini yangu kuwa watachaguliwa tena kurudi Bungeni kutokana na kazi nzuri waliyoifanya.

 

7.                 Mheshimiwa Spika, hotuba yangu imegawanyika katika maeneo

yafuatayo:-

 

·        Muhtasari wa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tatu kuanzia Novemba 1995 hadi 2005,

 

·        Muhtasari wa utekelezaji  wa Serikali kuhusu  Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2000-2005,

 

·        Taarifa ya utekelezaji wa majukumu pamoja na mipango ya maendeleo iliyoidhinishwa katika bajeti ya mwaka 2004/2005,

 

·        Kuelezea mipango, majukumu na malengo  ya bajeti ya Wizara, kwa mwaka 2005/2006,

 

·        Maombi ya fedha kwa mwaka 2005/06.

 

 

MUHTASARI WA MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TATU NOVEMBA 1995 HADI SASA

 

8.                 Mheshimiwa Spika, katika  miaka 10 ya Serikali ya Awamu ya Tatu, Wizara imefanikiwa kutekeleza Mabadiliko katika Sekta ya Afya kwa lengo  la  kuinua kiwango cha ubora wa huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi na kuongeza kiwango cha uwajibikaji kwa wasimamizi na watoaji wa huduma hizo.  Mabadiliko hayo yameleta mafanikio katika nyanja mbalimbali za utoaji huduma za afya zikiwemo kinga, tiba, mafunzo na utawala. Aidha, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita toka 1995/1996 hadi 2004/2005, Wizara imefanya mapitio ya Sera ya Afya na kuainisha marekebisho ya sheria, miongozo, kanuni, taratibu na viwango vya ubora wa huduma mbalimbali.

 

Huduma za Kinga

 

9.       Mheshimiwa Spika, Wizara iliimarisha na kuboresha huduma za kinga. Matokeo ya uimarishaji huo ni kama ifuatavyo:-

 

Magonjwa ya watoto yanayozuilika kwa chanjo ambayo ni polio, homa ya ini, kifua kikuu/dondakoo, surua na pepopunda yamepungua.  Hali hii imetokana na   kuimarika kwa huduma za chanjo kulikoongezeka kutoka asilimia 30 mwaka 1995 na kufikia wastani wa zaidi ya asilimia 90 mwaka 2004.  Aidha ugonjwa wa polio umedhibitiwa kiasi kwamba hajapatikana mgonjwa wa polio tangu mwaka 1996.  Sasa tunasubiri cheti cha uthibitisho kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ili Tanzania iwe miongoni mwa nchi ambazo zimetokomeza ugonjwa wa Polio.  Vile vile ugonjwa wa Surua uliokuwa tishio kwenye miaka ya 90 ulipungua kutoka wagonjwa 14,609 hadi 687 mwaka 2003.  Kutokana na kuimarika kwa huduma ya chanjo na usimamizi mzuri wa Serikali ya Awamu ya Tatu tumefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka watoto 99 mwaka 1996 hadi kufikia watoto 68 mwaka 2005 kwa kila watoto 1,000  wanaozaliwa hai.

 

10.     Mheshimiwa Spika, kutokana na uongozi mzuri wa Serikali ya Awamu ya Tatu uliopelekea kuimarika kwa uchumi, Serikali kuanzia miaka 3 iliyopita inagharamia kwa asilimia 100 ununuzi wa chanjo za Homa ya Ini, Polio na Pepopunda hivyo kuondokana na utegemezi wa wahisani uliokuwepo kwa kipindi kirefu cha nyuma.

 

11.     Mheshimiwa Spika, huduma za afya ya uzazi na mtoto zimeendelea kuboreshwa na kutolewa bila malipo. Idadi ya wanawake wanaotumia huduma za kliniki, iliongezeka kutoka asilimia 70 mwaka 1995 hadi asilimia 90 mwaka 2005. Idadi ya kinamama wanaotumia huduma ya uzazi wa mpango nayo iliongezeka kutoka asilimia 12 mwaka 1995 hadi 22 mwaka 2005.  Vile vile mafunzo ya kuzuia ukeketaji kwa wanawake yalifanyika kwa  viongozi 1,227 wa ngazi ya Vijiji, Kata na Tarafa nchini na hivyo kuongeza uelewa kwa viongozi wa jamii juu ya madhara ya  mila hii mbaya na kuhamasisha jamii kuachana na mila hiyo.

 

12.     Mheshimwa Spika, Wizara imefanikiwa kukabiliana na magonjwa ya milipuko hasa ugonjwa wa Kipindupindu ambao ulipungua kutoka wagonjwa 12,266 mwaka 1999 hadi wagonjwa 6,254 mwaka 2004. Ugonjwa wa Tauni ulipungua kutoka wagonjwa 831 na vifo 74  mwaka 1995 hadi kufikia  wagonjwa 4 bila kifo mwaka 2004. Katika Halmashauri ya Lushoto, vijiji vilivyoathirika na ugonjwa huu vimepungua kutoka 47 mwaka 1995 hadi kufikia vijiji 5 mwaka 2004.

 

Wizara imeanzisha Kitengo cha Kukabiliana na Dharura kwa kushirikiana na Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu ili kukabiliana na matukio ya ajali na magonjwa ya milipuko kama vile EBOLA, na Homa ya Mafua Makali (SARS). Aidha, kila mkoa umeanzisha Kamati ya Kukabiliana na Dharura/Maafa.

 

 

 

Huduma za Tiba

 

13.     Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa dawa muhimu na vifaa tiba vinawafikia wananchi katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya. Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umetokana na uamuzi wa Serikali yetu kutoa kipaumbele kwa huduma za afya na hivyo kuendelea kuiongezea Wizara yangu bajeti.  Kiasi cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 10 kwa mwaka 2000 hadi kufikia shilingi bilioni  30 kwa mwaka 2004/2005.  

 

Aidha, Wizara imeanzisha utaratibu ambapo kituo cha kutolea huduma za afya huagiza dawa kulingana na mahitaji halisi (indent system) kwa kuzingatia mgao wa fedha na mzigo wa magonjwa (burden of disease).  Hadi sasa, zahanati 1,498 na vituo vya afya 179 zinapatiwa dawa kwa kufuata mfumo huo. Mfumo huu unasaidia kupunguza matumizi mabaya ya rasilimali.

 

14.     Mheshimiwa Spika, Hospitali 98 za Wilaya, Mikoa, Rufaa na Maalum zilipatiwa vifaa na mashine mbalimbali zikijumuisha eksirei, Hadubini (microscope) na mashine za “Ultra Sound”, kulingana na mahitaji yao.  Vifaa na mashine hizi zimetolewa na mpango wa ORET. ORET pia ilitoa magari maalum katika kanda zote kwa ajili ya matengenezo ya vifaa hivyo.  Serikali pia ilinunua vifaa vifuatavyo “CT-Scan” kwa ajili ya  hospitali za rufaa,  mashine moja aina ya  “Cobalt 60”,  mashine moja ya eksirei inayohamishika (Mobile X-Ray unit),    “Gama cameras”, tatu na “Intracavity Radio therapy machine” moja,  kwa ajili ya Hospitali ya Ocean Road.

 

15.     Mheshimiwa Spika,  kutokana na mabadiliko yanayoendelea katika huduma za afya, hadi kufikia mwaka 2004, hospitali 184, vituo vya afya 298,  zahanati 992 na nyumba za waganga 583 zimefanyiwa ukarabati.  Jumla ya zahanati 790, vituo vya afya 90, hospitali 39 na nyumba za waganga 826 mpya zilijengwa nchini kote.  Aidha, hospitali zimeongezeka kutoka 194 mwaka 1995 hadi 233 mwaka 2004, vituo vya afya kutoka 343 mwaka 1995 hadi 433 mwaka 2004 na zahanati zimeongezeka kutoka 3,832 mwaka 1995 hadi 4,622 mwaka 2004. 

 

16.     Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua mchango unaotolewa na Waganga wa Tiba za Jadi imetunga Sheria namba 23 ya mwaka 2002 itakayosimamia na kuratibu shughuli zote za Tiba Asili nchini.  Aidha, Baraza la kusimamia maadili na mienendo ya Waganga wa Tiba za Jadi limekwishaundwa.

 

 

Huduma ya Mafunzo

 

17.     Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutoa mafunzo kwa wataalam mbalimbali ili kupata wataalamu wa kutosha.  Wataalam wa tiba  waliohitimu kwa mwaka waliongezeka kama ifuatavyo:- Madaktari wa Uzamili na Shahada mwaka 1995 waliohitimu 83 na  mwaka 2004 walihitimu 212,  Madaktari Wasaidizi mwaka 1995 walihitimu 118 na  mwaka 2004 walihitimu 134, Madaktari wa Meno hapakuwa na mhitimu mwaka 1995 na  mwaka 2004 wahitimu  12. Wauguzi wenye Shahada mwaka 1995 wahitimu 3 na mwaka 2004 wahitimu 40,  Wauguzi waliopata Stashahada mwaka 1995 walihitimu 205 na mwaka 2004 walihitimu 457 na Wauguzi waliopata Cheti waliongezeka kutoka 989 mwaka 1995 hadi 1,162 mwaka 2004.   Hata hivyo, ongezeko hili bado halijakidhi mahitaji halisi ya wataalamu hao nchini mwetu.   Katika kuendelea kuimarisha huduma za mafunzo vituo 43 vya mafunzo ya afya viliboreshwa kwa kufanyiwa ukarabati, na kupatiwa vifaa vya kufundishia.

 

18.     Mheshimiwa Spika, idadi ya wanafunzi wanaosomea udaktari katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Afya Muhimbili imeongezeka  maradufu.  Chuo hicho kimeanzisha shahada mpya za uuguzi na  Afya ya Mazingira (Bsc-Nursing and Bsc-Environmental Health).   Shahada ya Uzamili ya Afya ya Jamii (Masters in Public Health) imeanzishwa katika vyuo vya Muhimbili na Tumaini University (KCMC).  Aidha, Chuo Kikuu cha Agha Khan kimeanzisha masomo ya Shahada ya Uuguzi.  Vyuo vipya vilivyoanzishwa vina uwezo wa kutoa shahada ya Udaktari.  Vyuo hivyo ni Tumaini (KCMC),  Mtakatifu Augustino (Bugando, Mwanza), Kumbukumbu ya Hurbert Kairuki (Mikocheni, Dar es Salaam), International Medical and Techological  University (IMTU  Dar es Salaam).  Katika mwaka 2004 wanafunzi waliohitimu ngazi ya shahada katika vyuo hivi ni kama ifuatavyo:-

 

·        Madaktari – Muhimbili 103, KCMC 11, Kairuki 12, IMTU 5,

·        Madaktari wa Meno – Muhimbili 13,

·        Wauguzi – Muhimbili 19.

·        Maafisa Afya – Muhimbili 19.

·        Wafamasia – Muhimbili 32.

 

Napenda kuliarifu  Bunge lako tukufu kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tumepata daktari mmoja katika fani ya maumbile na mimba tete (Anatomy and Embryology) kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Afya Muhimbili.

 

Hospitali ya KCMC imeanzisha kituo cha ushauri nasaha cha ANGAZA na hospitali hiyo inashirikiana na chuo kikuu cha Tumaini katika kutoa mafunzo katika taaluma mbalimbali za afya katika hospitali hiyo. Aidha, huduma za upasuaji wa moyo zimeanza kutolewa katika hospitali hii.

 

 

Huduma za Utawala na Utumishi

 

19.  Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kuwapandisha vyeo watumishi mbalimbali wa kada za afya 32,994 ambao ni sawa na asilimia 94 ya lengo la kuwapandisha vyeo watumishi 35,100.

 

Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya

 

20.     Mheshimiwa Spika, mafanikio ya Taasisi zilizo chini ya  Wizara ya Afya ni pamoja na:-

 

·        Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali ulinunua mtambo wa uchunguzi wa “Deoxyribo Nucleic Acid (DNA) na vifaa vingine vya kisasa na kufungua maabara mpya ya kwanza ya kanda jijini Mwanza.

 

·        Katika kuboresha utendaji Serikali iliunganisha iliyokuwa Bodi ya Madawa na Tume ya Kudhibiti Vyakula na kuunda Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) chini ya sheria No. 1 ya mwaka 2003.

 

·        Aidha, Mamlaka imejenga maabara mpya ya kisasa yenye uwezo wa kupima ubora wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba na kuanzisha Mpango wa kuhakiki ubora wa dawa, vyakula na vipodozi (Quality Assurance program).

 

·        Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu imefanya na inaendelea kufanya tafiti nyingi za kuimarisha huduma za afya ikiwa ni pamoja na usugu wa vimelea vya malaria, utokomezaji wa magonjwa ya matende, mabusha na usubi.

 


MUHTASARI KUHUSU UTEKELEZAJI WA SERIKALI KUHUSU ILANI YA UCHAGUZI YA CCM 2000-2005

 

21.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2000 mpaka 2005 Ibara ya 57 imefanikiwa kutekeleza yafuatayo:

 

·        Madaraka, majukumu na rasilimali zaidi za afya zilipelekwa kwa jamii na hivyo kufanikisha uhamasishaji wa uanzishaji wa Bodi za Huduma za Afya za Halmashauri 113 na Kamati za Vituo vya kutolea huduma za afya.  Bodi hizi zinasimamia utoaji wa huduma bora za afya pamoja na kusimamia matumizi ya fedha ya uchangiaji wa huduma za afya. Hadi kufikia Aprili 2005,  Halmashauri 61 zilikwisha zindua Bodi za Huduma za Afya na 51 kati ya hizo zilishazindua Mfuko wa Afya ya Jamii.  Halmashauri 52 zilizobaki ziko katika hatua mbalimbali za kuzindua Bodi na Mfuko wa Afya ya Jamii. Mfuko wa Afya ya Jamii umewasaidia wananchi kupunguza matatizo ya uhaba wa dawa na vifaa, ukarabati wa majengo  na pia umeziwezesha baadhi ya Halmashauri kama vile Mbinga kuajiri wataalamu wanaotoa huduma za Afya.  Wanachama hupatiwa kadi na hupata matibabu bila kutoa fedha taslimu wakati wa kupata matibabu na hivyo kuziba mianya ya rushwa.

 

·        Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao unatoa huduma za matibabu kwa watumishi wa umma na wategemezi wao ulianzishwa na umeonyesha mafanikio makubwa.  Walengwa wameongezeka kutoka 691,774 mwaka 2002 hadi 1,141,637 mwaka 2004. Vituo vyote vya Serikali   na 518 vya sekta binafsi  vinatoa huduma za matibabu.  Aidha,  maduka ya dawa 32 ya sekta binafsi yamesajiliwa kutoa huduma kwa wanachama. Makusanyo ya mfuko yameongezeka kutoka shilingi milioni 12,546.1 mwaka 2001/2002 hadi shilingi milioni 22,007.7 mwaka 2003/2004. Katika kikao hiki cha Bunge la Bajeti kinachoendelea, Bunge  lako Tukufu  limefanya marekebisho ya sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya namba  8 ya mwaka 1999  ibara ya 17 na kumpa Waziri mwenye dhamana, madaraka zaidi ya kuandaa na kuongeza orodha ya huduma ambazo zinazotolewa na mfuko.

 

·        Hospitali zimeongezeka kutoka 203 mwaka 2000 hadi 233 mwezi Mei 2005, vituo vya afya vimeongezeka kutoka 367 mwaka 2000 hadi vituo 433 Mei, 2005 na zahanati zimeongezeka kutoka 4,232 mwaka 2000 hadi 4,622 Mei, 2005. Vituo hivi vya huduma vimejumuisha vile vya Serikali, Mashirika ya dini na binafsi.

 

·        Kiwango cha chanjo kimeongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 90 ya lengo. Kwa mlinganisho mafanikio yalikuwa kama ifuatavyo: -

 

-         Chanjo za kawaida DPT- HB ziliongezeka kutoka asilimia 90 mwaka 2000 hadi asilimia 91 mwaka 2004.

-         Chanjo ya pepopunda TT2+ kwa wanawake wajawazito kutoka asilimia 77 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 88 mwaka 2004.

 

-         Chanjo ya polio kiwango kiliongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2000 hadi asilimia 96 mwaka 2004.

 

-         Chanjo ya surua kiwango kiliongezeka kutoka asilimia 78 mwaka 2000 Hadi asilimia 94 mwaka 2004.

 

·        Katika kuimarisha huduma za chanjo, majokofu 2,287 ya mafuta ya taa yalibadilishwa na majokofu mapya ya kutumia gesi kwenye vituo vya mikoa 17 na majokofu 125 ya mionzi ya jua yalifungwa katika mikoa 7.

 

·        Ununuzi na usambazaji wa dawa za uzazi wa mpango nchi nzima ulifanyika. Pia huduma za mama wajawazito ziliendelea kuboreshwa kwa kutoa vifaa vya kujifungulia.  Aidha Halmashauri 9 zenye kiwango cha juu cha vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi walipewa magari ya kubebea wagonjwa ili kupunguza tatizo hilo.   Halmashauri hizo ni Bariadi, Maswa, Kahama, Kasulu, Ngara, Karagwe, Manyoni, Igunga na Tarime.   Ninazipongeza Halmashauri nyingine zilizoamua kununua magari ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya kupunguza tatizo la akina mama wajawazito na wagonjwa wengine wanaohitaji rufaa.    Halmashauri hizo ni Geita, Urambo, Korogwe, Lushoto, Manispaa za Iringa, Tanga, Ilala, Temeke   na Kinondoni.  Aidha, simu za upepo (redio call) 20 zimenunuliwa na kusambazwa katika Wilaya za Bariadi, Kahama na Maswa ili kurahisisha mawasiliano.

 

·        Idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano waliopata matone ya vitamini A iliongezeka kutoka watoto 1,457,000 mwaka 2000 hadi watoto 5,746,299 mwaka 2005 sawa na ongezeko la asilimia 294.

 

·        Tatizo la upungufu wa madini joto nchini limepungua kutoka asilimia 25 ya miaka ya tisini hadi asilimia  7 hivi sasa. Aidha, asilimia 95 ya kaya za Tanzania sasa wanatumia chumvi yenye madini joto.

 

·        Katika kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI na kuhakikisha upatikanaji wa damu salama, Serikali ilinunua na kusambaza vipimo vya damu (HIV Test Kits) 1,100,000 katika hospitali zote zinazotoa damu kwa wagonjwa nchini. Ushauri nasaha ulitolewa katika vituo zaidi ya 400 vya Serikali na visivyo vya Serikali. Ununuzi wa mashine za kupimia chembe chembe za CD4 kwa waathirika ulifanyika na kusambazwa katika hospitali za rufaa, mikoa na  hospitali za Manispaa 3 za Dar es Salaam.

 

·        Mpango wa kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI toka kwa Mama mjamzito kwenda kwa mtoto (PMCT) umeonyesha mafanikio.  Baada ya mafanikio ya majaribio ya awali, sasa Wizara imepanua mpango huu ili uweze kufikia mikoa yote ya Tanzania Bara kwa awamu.  Mpango huu sasa unaendeshwa sambamba na utoaji wa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) kwa wagonjwa wale wenye sifa za kupewa dawa hizi.

 

·        Mpango wa kutoa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) umeanza na dawa zinatolewa katika vituo 96 vya hospitali za Serikali, mashirika ya dini na binafsi. Dawa hizi hutolewa bila malipo. Hadi kufikia Mei 2005 wagonjwa 6,000 wa jinsia zote wakiwemo watoto wananufaika na mpango huu.   Aidha, wagonjwa 44,000 wanatarajiwa kunufaika na mpango huu ifikapo Desemba 2005.

 

·        Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imefanikiwa kusambaza na kufunga vifaa vya Tiba ya Meno (Dental Units) katika hospitali zote za Mikoa na Wilaya.  Hii ilikuwa ni katika mpango wa awamu ya kwanza ambao ulianza mwaka 2002/2003 na umekamilika katika mwaka 2004/2005.

 

·        Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na hospitali za Mashirika ya Dini na hasa mahali ambapo hakuna kituo cha kutolea huduma cha Serikali.  Aidha, Wizara imekuwa ikiongeza ruzuku kwa kitanda kutoka shilingi 7,500/= mwaka 2002/2003 hadi kufikia shilingi 30,000/= mwaka 2004/2005.

 

·        Udhibiti wa Uwiano wa magonjwa ya watoto (Integrated Management of Childhood Illnesses – IMCI)

 

 Wizara iliendeleza mafunzo kwa watumishi wa afya wa ngazi zote jinsi ya kutoa matibabu kwa magonjwa yale yanayosababisha vifo zaidi kwa watoto kwa pamoja.  Magonjwa hayo ni Malaria, Kichomi, Kuharisha, Surua, Utapiamlo na upungufu wa damu.  Pia jamii ilihamasishwa kuzingatia mambo yanayohusu makuzi na maendeleo ya watoto ikijumuisha kuhamasisha akina mama wakamilishe unyonyeshaji na kuwapa watoto virutubisho muhimu,   kuzuia maradhi yanayozuilika kwa chanjo,   kuhimiza matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu,   kuwapeleka watoto kliniki wapate chanjo na kuchunguzwa afya zao.  Mpango huu na mpango wa Chanjo kwa pamoja umesaidia kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga.  (Infant Mortality Rate).

 

·        Dawa za kifua kikuu na ukoma zilinunuliwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kipindi chote cha miaka 5 bila upungufu.    Kampeni kuhusu ukoma ilifanyika katika mikoa 11 na wagonjwa wapatao 23,067 walitambuliwa na kupewa dawa, viatu na viungo bandia.  Utafiti wa maambukizi ya kifua kikuu ulifanyika katika shule za msingi 731 katika mikoa 20 na wanafunzi 110,243 walifanyiwa uchunguzi kati yao wanafunzi 4,617 sawa na asilimia 4.2 walikuwa na maambukizi na kuanzishiwa matibabu. 

 

·        Wizara iliendelea kuhamasisha na kuhimiza jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora, usafi wa mazingira na matumizi bora ya vyoo.  Aidha, Wizara imeanzisha mashindano ya utunzaji mazingira kwa Halmashauri zote nchini. 

 

·        Katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria, dawa mpya ya Sulphadoxine Pyrimithmine (SP) ilianza kutumika kuanzia mwaka 2001 baada ya Klorokwini kuonyesha usugu mkubwa dhidi ya vimelea vya malaria.  Hata hivyo, utafiti umeonyesha kuwa vimelea vya malaria vimekuwa sugu kwa dawa ya SP kwa asilimia 25.  Kwa sasa yanafanyika maandalizi ya kubadili matibabu ya malaria kutoka dawa ya SP kwenda dawa ya mseto iitwayo Arthemether/Lumefantrine.  Serikali pia imeanzisha mpango wa Hati punguzo ili kuwawezesha watoto wenye umri chini ya miaka mitano na mama wajawazito kupata vyandarua vyenye viuatilifu kwa bei nafuu.

 

·        Wizara hadi kufikia mwaka 2004/2005 ilijenga matanuru 56 ya kuteketeza taka zinazozalishwa na hospitali katika hospitali za rufaa, maalumu, mikoa na wilaya.

 

·        Wizara imeanzisha Mfuko wa Pamoja (Basket Fund) ambao umechangia katika kuimarisha huduma za afya katika ngazi za wilaya. Mfuko umekuwa ukinunua magari mapya kwa ajili ya kubadilisha magari machakavu kwa Halmashauri.  Magari haya yanatumika katika shughuli za chanjo na huduma nyingine za afya ili ziweze kuwafikia wananchi wote hasa walioko vijijini.

·        Huduma za tiba ziliendelea kuimarika na yafuatayo yamefanyika:  Kununua na kusambaza makasha ya dawa (drug kits) kwenye zahanati 2,033 na vituo vya afya 206.  Zahanati na Vituo vya Afya vingine vimepewa dawa kwa kutumia mfumo wa (Indent system) yaani  utaratibu wa kuagiza dawa kulingana na mahitaji halisi kwa kila kituo kwa kuzingatia mgao wa fedha na mzigo wa mgonjwa (Burden of disease – BOD).  Mpango huu umewezesha Zahanati 1,498 na Vituo vya Afya 179 kununua dawa.  Jumla ya zahanati zote za Serikali pamoja na za Mashirika ya Dini zilipatiwa makasha ya dawa na zilizonunua kwa mfumo wa ‘indent’ ni  3,531 na vituo vya afya ni 385.  Serikali pia ilianzisha utaratibu unaowawezesha wagonjwa kununua dawa kwa nusu ya bei (Capitalization of Hospital Pharmacies). 

 

·                    Mradi wa Uimarishaji Huduma Muhimu za Afya (MUHUMA) umekuwa ukitekelezwa katika wilaya mbili za Morogoro vijijini na Rufiji toka Mwaka 1997 mpaka mwaka 2004 ulipofikia kikomo kama mradi.  Utafiti umeonyesha kuwa kumekuwa na upunguaji wa kasi ya vifo katika wilaya zote mbili kwa asilimia zaidi ya 55 kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na asilimia 18 kwa watu wazima. Kupungua huku kumeziweka wilaya hizo mbili kwenye matumaini ya kufikia moja ya malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza kasi ya vifo miongoni mwa watoto wadogo kwa theluthi mbili ifikapo mwaka 2015. Aidha, uzoefu uliopatikana katika wilaya hizi utasaidia kupanga mbinu sahihi ya kukabiliana na kupunguza vifo vya watoto wachanga na watu wote kwa ujumla.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU  NA MIPANGO YA MAENDELEO ILIYOIDHINISHWA KATIKA BAJETI YA MWAKA 2004/2005

 

22.  Mheshimiwa Spika, ifuatayo ni taarifa ya utekelezaji wa bajeti katika mwaka 2004/2005. Utekelezaji huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili, Miradi ya Maendeleo na Matumizi ya Fedha za Kawaida.

 

Miradi ya Maendeleo

 

23.     Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2004/05, Wizara ya Afya ilitengewa kiasi cha shilingi 91,215,753,600/= kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Jumla ya shilingi 3,552,448,200/= zilitolewa na Serikali ya Tanzania na shilingi 87, 663, 305,400/=  zilitolewa na  wahisani mbalimbali, wakiwemo wahisani wanaochangia Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund). Fedha hiyo imetumika kutekeleza miradi ifuatayo: -

 

Ukarabati wa Hospitali ya Taifa Muhimbili

 

·        Wizara  kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) inaendelea na ukarabati mkubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.  Ukarabati wa Wodi ya Sewahaji, ujenzi wa tanuru la kuchomea taka (incinerator) na karakana umekamilika. Pia mashine 10 mpya za kufulia, moja ya kutakasia vifaa na ya kuchomea taka hatari zimefungwa na zinafanya kazi. Ukarabati wa jengo la wodi za Kibasila, upasuaji, eksirei na  chumba cha upasuaji wa akinamama wenye matatizo ya kujifungua ulianza na unaendelea vizuri.  Ukarabati wa majengo mengine uko katika hatua za mwisho ikiwa ni pamoja na nyumba ya kuhifadhia maiti, vibanda vya mitambo ya umeme na majenereta. Ukarabati wa njia za maji safi, maji taka, umeme, na barabara unaendelea. Ukarabati huu unaenda sambamba na ununuzi na ufungaji wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya Hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali za Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni.

 

·        Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni Abbott/Axios wametoa msaada uliotumika kujenga uzio kuzunguka hospitali, kufanya ukarabati mkubwa wa jengo la maabara (Central Pathology Laboratory) na ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje  (OPD).  Ujenzi wa uzio na ukarabati wa maabara umekamilika. Ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) lenye vyumba 35 vya matibabu  liko kwenye hatua za mwisho na linatarajiwa kukabidhiwa mwezi Agosti, 2005.  Pia Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Taasisi ya Kuzuia Magonjwa ya Marekani (CDC) imekamilisha ujenzi wa jengo jipya la ushauri nasaha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na limeanza kutumika.

 

·        Ujenzi wa jengo la huduma kwa watoto (Paediatric Complex) uliendelea vizuri.  Ujenzi wa Ghorofa ya msingi (basement), Ghorofa ya chini (ground floor) na Ghorofa ya kwanza (first floor) ulikamilika.  Ghorofa ya chini inatumika kwa wagonjwa waliohamishwa kutoka kwenye wodi zinazofanyiwa ukarabati, vyumba vya upasuaji, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na Maabara ya Kifua Kikuu. Ukarabati utakapokamilika jengo hili litaendelea kutumika kwa ajili ya huduma za watoto kama ilivyokusudiwa.  Ujenzi wa kuta na nguzo kwa ajili ya ghorofa ya pili na ya tatu umekamilika na mkandarasi anaendelea kupaua. 

 

 

Kuimarisha Hospitali, Taasisi na vyuo vya Afya

 

Kazi zifuatazo zilifanyika:

 

·        Ukarabati wa majengo ya huduma ya wagonjwa wa nje, upasuaji, mfumo wa maji taka katika hospitali ya  META iliyoko Manispaa ya Mbeya, pamoja na ukarabati wa kijiji cha wagonjwa wa akili.

 

·        Michoro kwa ajili ya ujenzi wa hosteli mpya ya madaktari wanafunzi imekamilika na taratibu za kumpata mjenzi zinaendelea na ujenzi wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Rufaa Mbeya umekamilika.

 

·        Taratibu za ununuzi wa vifaa vya tiba kwa ajili ya hospitali za rufaa na maalum zimekamilika.  Vifaa hivyo ni “Oxygen concentrator, Electroencephalograph (EEG) machine, Autoclave (High pressure steam sterilizer),  Gynaecological beds,  Automatic film processor machine, Mammograph machine,  Electro-Cardiograph (ECG) machine, Mortuary refrigerator (12 bodies),  Defibrillator, Cardiac monitor, Orthopaedic Operating Table, Basic Neuro-Surgical instrument na Basic Laminectomy instrument set”.

 

·        Serikali  imetoa mchango wake wote (counterpart fund) wa kununulia vifaa vya Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili –MOI.

 

·         Ujenzi wa jengo la ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Tukuyu ulikamilika na kukabidhiwa.  Kwa sasa ununuzi wa vifaa unaendelea.

 

·        Ukarabati wa mifumo ya njia za umeme kwenye jengo la ofisi za Huduma za Mama na Mtoto Dar es Salaam umekamilika.

 

·          Ukarabati wa ofisi, mabweni na madarasa katika vyuo 32 vya afya vilivyo chini ya Wizara umekamilika kwa asilimia 80.  Pia ujenzi wa nyumba za watumishi, maktaba na vyumba vya mazoezi ya vitendo umefanyika katika vyuo vyote 21 vya uuguzi vya Serikali.

 

Udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza

 

24.     Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza mambo yafuatayo yalifanyika:-

·         Vituo vyote vya huduma za afya vimepata dawa na vifaa kwa ajili ya kukinga na kutibu magonjwa ya zinaa – STIs.

 

·        Serikali iliendelea kutoa mchango wake kwa ajili ya kugomboa na kusambaza dawa za ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma.  

 

25.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea na juhudi za kuelimisha na kuhamasisha wananchi na jamii kuhusu mabadiliko yanayoendelea katika Sekta ya Afya.  Katika uelimishaji huu, Halmashauri ambazo ni kitovu cha utekelezaji wa mabadiliko haya, zimehamasishwa kukamilisha uanzishwaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).    Uelimishaji na uhamasishaji huo umekwenda pamoja na maelekezo ya kuunda Bodi za Huduma ya Afya za Wilaya na Kamati za Afya kuanzia ngazi ya Zahanati, Kata, Kituo cha Afya na Hospitali ya Wilaya.  Kazi hii inakwenda sambamba na awamu za mabadiliko ya Serikali za Mitaa.  Hadi Desemba 2004, Halmashauri zote 113 nchini zilikwishahamasishwa kuhusu uundaji wa Bodi za Afya za Wilaya na Kamati mbalimbali za afya katika ngazi zote. Aidha Halmashauri 61 kati ya 113 zimeshazindua Bodi za Huduma za Afya na zinafanya kazi.

 

26.     Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanatekeleza kwa ufanisi malengo na majukumu yaliyokusudiwa na Mabadiliko katika Sekta ya Afya, Wizara yangu imeendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha  wajumbe wa Timu za Uendeshaji na Usimamizi wa Huduma za Afya mkoani na wilayani ili wawaeleweshe wafanyakazi wanaowasimamia,  mabadiliko katika Sekta ya Afya na wajibu wao kwa wateja wanaowahudumia.   Aidha viongozi wafawidhi wa vituo vya Afya na Zahanati zote katika Halmashauri 66 nao wamekwisha hamasishwa.  

 

27.     Mheshimiwa Spika, jamii pia imeendelea kuelimishwa na kuhamasishwa kuhusu mabadiliko, haki na wajibu wao katika kumiliki Huduma za Afya kwa njia mbalimbali zifuatazo:

 

·        Vipindi na matangazo katika redio na televisheni,

 

·        Mabango na vipeperushi,

 

·        Mabadiliko katika huduma za afya kupitia michezo ya kuigiza (TV),

 

·        Mikutano ya Bodi na Kamati mbalimbali za Afya.

 

Mfuko wa Afya ya Jamii

 

28.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/05 Wizara ilifanikiwa kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa Halmashauri za wilaya 92 za Tanzania Bara na kuziwezesha kuandaa na kupitisha Sheria ndogo ya kuanzisha Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).  Halmashauri hizo hazijumuishi Halmashauri za wilaya 8  mpya kwa kuwa Wizara bado inazisubiri zipate mabaraza ya Madiwani mwezi Oktoba 2005. Halmashauri za wilaya 51 kati ya 92 zilizohamasishwa, zimekwishazindua Mfuko wa Afya ya Jamii na zilizobaki 41 ziko katika hatua mbalimbali za uzinduzi. 

 

29.     Mheshimiwa Spika, Serikali hutoa kiasi cha fedha kinacholingana na kiasi cha fedha kinachongwa na wananchi katika mfuko wa Afya ya Jamii (Tele kwa Tele).  Ili Halmashauri iliyokwisha kuanzisha Mfuko wa Afya ya Jamii iweze kupata fedha za tele kwa tele, inatakiwa kuwekeana mkataba na Wizara ya Afya.  Mkataba huo unatoa mwongozo wa matumizi ya fedha za CHF.  Halmashauri 15 kati ya 51 zilizoanzisha CHF zimekwisha wekeana mkataba na Wizara ya Afya.  Hadi sasa jumla ya shilingi milioni 500 za tele kwa tele zimekwishalipwa.  Tunazihimiza Halmashauri zilizobaki zikamilishe taratibu za mikataba ili nazo ziweze kulipwa fedha za tele kwa tele.

 

30.     Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Hati rasmi na miongozo ya kufundishia jinsi ya kutekeleza mpango wa TIKA yamekamilika.  Halmashauri ya Mwanza, Iringa na Mji wa Mtwara wataanzisha mfuko huu. Aidha, Umoja wa Matibabu katika Sekta isiyo Rasmi (UMASIDA) ulioanzishwa katika Jiji la Dar es Salaam, Manispaa za Moshi na Arusha umeweza kutoa huduma ya matibabu kwa mafanikio makubwa kwa wananchi wasio katika sekta rasmi waishio mijini.  Kutokana na mafanikio makubwa ya mpango huu natoa wito kwa wakazi wa mijini walioko katika sekta isiyo rasmi  kuiga au kujiunga na mpango huu.

 

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya

 

31.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake ya mwaka 2004/2005 Mfuko huu hadi kufikia tarehe 2 Aprili 2005 ulitekeleza yafuatayo:-

 

·        Kusajili wanachama wapya 6,321 na hivyo kuufanya Mfuko kufikisha jumla ya wanachama 248,829 ikilinganishwa na wanachama 242,508 waliokuwepo kipindi kama hicho mwaka jana. Kati ya wanachama hao asilimia 56 ni wanaume na asilimia 44 ni wanawake. Idadi ya wanaonufaika na mpango huu imeongezeka kutoka 1,115,537 kipindi cha mwaka 2003/2004 hadi kufikia 1,144,614 katika mwaka 2004/2005. Hii ni sawa na asilimia nne (4%) ya Watanzania wote. Ninafurahi kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa kati ya wanaonufaika na Mpango huu, kundi la wazee nalo lipo ambapo wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 walioandikishwa na watoto wao kama wategemezi ni 468,148. 

 

·        Jumla ya shilingi bilioni 7.35 zimelipwa kwa watoa huduma wa Serikali na wa asasi zisizo za Serikali tangu utaratibu huu ulipoanza kutumika miaka minne iliyopita, ikiwa ni marejesho kwa huduma walizotoa kwa wanachama.

 

32.     Mheshimiwa Spika, jumla ya vituo 3,558 vya matibabu vilisajiliwa na Mfuko ili kuhudumia wanachama, ambapo asilimia 70 ya vituo hivyo viko vijijini. Kati ya vituo hivyo vituo 518 vinamilikiwa na madhehebu ya dini na asasi zisizo za Serikali na maduka ya dawa 36 yanamilikiwa na wamiliki binafsi. Usajili wa vituo zaidi vya matibabu umesaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu karibu zaidi na wanapoishi wanachama na hivyo kuongeza ushindani miongoni mwa watoa huduma. Wanachama wana uhuru wa kuchagua wapi wakapate huduma za matibabu kati ya vituo vinavyomilikiwa na Serikali au vile vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini na mashirika ya kujitolea.

 

33.     Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa dawa umeendelea kuridhisha japo bado kuna tatizo katika baadhi ya maeneo ambayo yana usimamizi hafifu. Mfuko uko katika hatua za mwisho za kusajili baadhi ya maduka ya dawa muhimu (ADDO – “ Accredited Drug Dispensing Outlet”) yaliyoanza kutoa huduma mkoani Ruvuma na ambayo yanaonyesha  ufanisi.

 

34.     Mheshimiwa Spika,   Mfuko umetoa elimu kwa wadau 96,414 wakiwemo Viongozi wa vyama vya wafanyakazi, watoa huduma na  kwa wanahabari.

 

35.     Mheshimiwa Spika,   Mfuko uliimarisha ofisi zake saba za kanda kwa kuzipatia nyenzo na madaraka zaidi.  Katika kipindi hicho jumla ya watumishi 37 waliajiriwa katika Ofisi za Kanda wengi wao wakiwa ni wakaguzi na hivyo kufanya Mfuko kuwa na watumishi 121 nchi nzima.  Uimarishaji huu umeuwezesha Mfuko kuzisogeza huduma karibu zaidi na wadau.

 

36.     Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2004/05, Mfuko umeimarisha shughuli zake kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano.  Hii ni pamoja na kuziunganisha ofisi zote saba za kanda na Makao Makuu, na kurahisisha uandaaji wa malipo kwa watoa huduma na mawasiliano ya haraka na wateja. Aidha, mfuko ulizindua tovuti yake yenye anwani ifuatayo ya www.nhiftz.com ambapo shughuli nyingi sasa zinafanyika kupitia mfumo huo.

 

Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya (MTUHA) na Utafiti

 

37.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/05 Wizara yangu imeendelea kutoa kipaumbele kwa upatikanaji wa takwimu katika Sekta ya Afya.  Pamekuwepo na mikakati ya makusudi ili kuhakikisha kuwa takwimu zinazohitajika zinapatikana kwa ajili ya mipango, kutoa tathmini ya utoaji wa huduma za afya, kufuatilia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kisekta na kuboresha sera na miongozo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba huduma za afya zinatolewa katika ubora unaostahili.

 

38.     Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha mipango ya upatikanaji wa takwimu sahihi mikakati ifuatayo imetekelezwa:- 

 

·        Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya (MTUHA), umezidi kuboreshwa katika ngazi ya wilaya,    baada ya kuweka kompyuta na programu ya kuchambua takwimu hizo.  Hii imesaidia kuongeza kasi ya upatikaji wa takwimu katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.

 

·        Takwimu zinazopatikana kupitia mfumo wa tafiti mbalimbali nazo  zimeimarishwa zaidi (Operational Research).

 

·        Mafunzo yametolewa kwa wajumbe wa Kamati za Afya za Uendeshaji wa Huduma wilayani na mikoani.  Lengo la mafunzo hayo lilikuwa kuwapa uwezo na mbinu za kufanya utafiti ili kukusanya takwimu zilizo sahihi,   kuchambua na kutumia matokeo yake kuboresha huduma za afya ngazi ya mkoa,  wilaya na jamii kwa ujumla.

 

·         Kutayarisha na kusambaza vitabu vya mfumo wa taarifa za uendeshaji wa Huduma za Afya nchi nzima.

 

 

MATUMIZI  YA   KAWAIDA

 

HUDUMA ZA KINGA

 

Udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza (Epidemiologia)

 

39.     Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza Wizara iliendelea kutumia mbinu zifuatazo:-

 

·       Wilaya zilihamasishwa na kuweza kutumia mbinu shirikishi (Participatory Hygiene and Sanitation Transformation – PHAST) ili kuwezesha jamii kubuni, kupanga, kutekeleza na kusimamia mipango ya afya ya mazingira ili kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na milipuko.

 

·       Fremu za mabamba ya vyoo 490 zilitengenezwa na kugawanywa katika Wilaya ili ziweze kutumika kwa mafunzo na ujenzi wa vyoo bora.

 

·       Matanuru 4 ya kuteketekeza taka yalijengwa katika hospitali maalum ya Kibong’oto, hospitali ya Saratani Ocean Road, hospitali za Wilaya za Kilosa na Mahenge.

 

·       Mashindano ya usafi wa mazingira katika Halmashauri za Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya yalifanyika.

 

Mbinu zote hizi ziliwezesha kuboreshwa kwa usafi wa mazingira na hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wa kipindupindu kutoka wagonjwa 6,254 na vifo 217 mwaka 2003/2004 hadi kufikia wagonjwa 3,462 na vifo 93 mwaka 2004/2005.

 

 

40.     Mheshimiwa Spika, tatizo la watu kuumwa na mbwa au wanyama wanaohisiwa kuwa na kichaa cha mbwa limekuwa likiongezeka kila mwaka.  Mwaka 2004 watu 16,750 waliumwa na mbwa au wanyama wanaohisiwa kuwa na kichaa cha mbwa na kati yao watu 97 walifariki ikilinganishwa na mwaka 2003 ambapo watu 12,587 waliumwa na kati yao 77 walifariki.  Kuanzia Januari hadi Aprili, 2005, walioumwa ni 6,350 na waliofariki ni 34.  Katika kupambana na tatizo hili, Wizara yangu ina jukumu la kununua dawa za kuchanja wagonjwa walioumwa na mbwa.  Jumla ya shilingi milioni  259.35 zilitumika kununua dawa ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika kipindi cha Julai 2004 hadi Mei, 2005.  Gharama za kumchanja mtu aliyeumwa na mbwa ni dola za kimarekani 24 na gharama ya kumchanja mbwa ni dola za kimarekani 0.4.  Kwa kuwa kuchanja mbwa ni rahisi, Wizara yangu ikishirikiana na Wizara ya Maji na Mifugo imeandaa taarifa yakinifu (concept paper) inayopendekeza kubadilisha kifungu cha sera ya Kilimo ya mwaka 1997 sehemu ya 3, kifungu kidogo cha 3, kipengele cha 1, sehemu D, kibadilishwe na jukumu la kuchanja mbwa liwe la Serikali badala ya kuachiwa jukumu hilo mfugaji.  Aidha, Wizara yangu inashirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kupanua wigo wa ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza na milipuko hasa sehemu za mipakani.

 

Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria

 

41.     Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa malaria bado ni tatizo kubwa nchini na linahitaji jitihada za pamoja katika kukabiliana nalo. Katika kipindi cha 2004/2005, Wizara yangu ilitekeleza majukumu mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria. Utekelezaji ni kama ifuatavyo:-

 

·        Kutoa mafunzo kwa wataalam mbalimbali wa afya kuhusu tiba sahihi,

 

·        Kuhamasisha umma juu ya utumiaji wa vyandarua vyenye viuatilifu hasa kwa mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya  miaka mitano,

 

·        Kutafiti   usugu wa vimelea vya malaria,

 

·        Kuendeleza utafiti wa tiba ya dawa mseto,

 

·        Kutoa tiba ya tahadhari kwa vipindi (Intermittent Preventive Treatment) kwa mama wajawazito,

 

·        Kutoa tahadhari ya kudhibiti milipuko ya malaria katika wilaya zenye milipuko ya mara kwa mara ya malaria na kuimarisha udhibiti wa malaria ngazi ya jamii.

 

42.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea na uhamasishaji wa jamii katika kutumia vyandarua vyenye viuatilifu. Tarehe 22 Oktoba mwaka 2004, Wizara yangu ilizindua Mpango wa Taifa wa Hati Punguzo. Mpango ambao unawawezesha mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kupata vyandarua vyenye viuatilifu kwa bei nafuu.  Kwa hivi sasa, mpango wa Taifa wa Hati Punguzo unatekelezwa katika mikoa ya Dar-es-salaam, Dodoma, Morogoro, Tanga, Pwani, Kilimanjaro na Arusha. Mpango huu utajumuisha mikoa yote ya Tanzania Bara ifikapo Desemba, 2005.

 

43.     Mheshimiwa Spika, mwaka huu Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliadhimisha Siku ya Malaria Afrika iliyofanyika Kitaifa tarehe 25 Aprili, 2005 mkoani Singida.  Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa “Tushirikiane kwa pamoja tushinde malaria”.  Kauli mbiu hii inatukumbusha na kusisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wadau wote katika  Sekta ya Afya kupiga vita malaria, hii ikiwa ni pamoja na jamii, Serikali kuu, Serikali za mitaa, wahisani mbalimbali, mashirika ya dini na watu binafsi.

 

Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma

 

44.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2004 mpaka Juni 2005,  Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma ulifanya ufuatiliaji wa watoto wa shule 1,048 waliobainika kuwa na uambukizo wa ugonjwa wa Kifua Kikuu katika mikoa ya Singida, Iringa, Mbeya, Kigoma na Kagera.  Asilimia 48 ya watoto hao walipata uambukizo ndani ya kaya zao na jumla ya watoto 75 yaani  asilimia 3 walikuwa tayari na ugonjwa wa kifua kikuu (active TB) na walipewa dawa za matibabu.

 

45.     Mheshimiwa Spika, kampeni za kutokomeza ugonjwa wa ukoma zilifanyika katika mikoa ya Kagera, Rukwa na Tabora ambako jumla ya wagonjwa wapya 836 waligunduliwa na kuanzishiwa tiba. Aidha katika juhudi za kurekebisha ulemavu (prevention and rehabilitation of disabilities) unaotokana na ukoma, watu walioathirika na ukoma wenye ulemavu 175 walifanyiwa upasuaji wa aina mbalimbali na wengine 5,811 walipewa viatu maalumu na watu 37 walipewa miguu bandia. Vile vile madaktari bingwa wa upasuaji 5 walipewa mafunzo rejea juu ya upasuaji wa wagonjwa waliopata ulemavu kutokana na ukoma.  Kutokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani, ili nchi ihesabiwe kuwa imetokomeza ukoma inatakiwa kufikia mgonjwa 1 kwa kila watu 10,000.  Hadi hivi sasa Tanzania imefikia wagonjwa 1.3 kwa kila watu 10,000.  Mafanikio haya ni makubwa lakini tunatakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji ili hatimaye kutokomeza ugonjwa huu kabisa.

 

46.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2004/2005, jamii iliendelea kuelimishwa kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa matangazo kwa kutumia vyombo vya habari, kusambaza vipeperushi na mabango yenye ujumbe wa jinsi ya kutambua dalili, kujikinga na matibabu ya kifua kikuu na ukoma. Aidha dawa za kutosha za kifua kikuu na ukoma ziliendelea kusambazwa katika mikoa, wilaya na vituo vyote vya matibabu. Dawa hizo zilitolewa kwa wagonjwa wote bila malipo.

 

Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI:

 

47.     Mheshimiwa Spika,   katika kutekeleza Mkakati wa Sekta ya Afya wa Kudhibiti UKIMWI 2003-2006,  Wizara yangu inaendelea kutekeleza yafuatayo:-

 

Huduma ya kutoa elimu ya UKIMWI

 

48.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 huduma ya  elimu ya UKIMWI iliendelea kutolewa kwa kutumia mbinu na njia mbalimbali,   kama kalenda, vipeperushi, majarida,   michezo ya kuigiza, magazeti, matangazo katika redio na televisheni na mabango.  Vielelezo hivyo vilikuwa na ujumbe mbalimbali kama vile ushauri nasaha, lishe bora kwa wagonjwa wa UKIMWI na matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa UKIMWI.  Pamoja na kwamba asilimia kubwa ya Watanzania wana viwango vya juu vya uelewa kuhusu UKIMWI uelewa huo, hauendi sambamba na kubadilisha tabia, kwa hiyo bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu zaidi ili tujifunze, tukubali na tufanye uamuzi sahihi wa jinsi ya kujikinga.

 

Huduma za Ushauri Nasaha na Upimaji wa Hiari

 

49.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 huduma za Ushauri Nasaha na upimaji wa afya kwa hiari ziliendelea kutolewa katika vituo 521 vinavyotoa huduma hiyo nchini kote. Aidha, idadi ya watu waliohudhuria katika vituo hivyo walikuwa 227,973 ukilinganisha na mwaka 2003/2004 ambapo watu 139,972 walipata huduma hii. Ongezeko hili linatokana na kuongezeka kwa idadi ya vituo vinavyotoa ushauri huo kutoka 332 mwaka 2003 hadi 521.  Hata hivyo pamoja na ongezeko hili idadi ya watu wanaojitokeza kwa ajili ya upimaji bado ni ndogo sana.  Hivyo napenda kutoa wito  kwa wananchi kujitokeza kwa wingi zaidi ili  waweze kufahamu hali yao ya afya kuhusiana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI ili waweze kuchukua hatua zinazostahili.

 

50. Mheshimiwa Spika, mafunzo kuhusu ushauri nasaha yalitolewa kwa watumishi wa afya 165 na kufanya idadi ya wataalam wa ushauri nasaha kufikia 12,000.

 

Huduma ya Damu Salama

 

51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI uliendelea kuhakikisha kuwa damu inayotolewa kwa wagonjwa ni salama. Vifaa vya kupima damu (Rapid Tests) 755,908 vilisambazwa nchini kote.

 

 

Usambazaji wa Kondomu

 

52.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005, Wizara yangu ilipokea jumla ya kondomu millioni 52. Wizara ilisambaza kondomu za kiume millioni 21 kati ya hizo na milioni 21 nyingine za kiume na 10,000 za kike zilizobaki    zilisambazwa kupitia mashirika yasiyokuwa ya kiserikali chini ya utaratibu wa  ‘social marketing’.

                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                

Huduma ya Magonjwa ya Ngono

 

53. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI unaendelea kuratibu upatikanaji wa huduma za kutibu magonjwa ya ngono nchini kote. Tiba ya magonjwa ya ngono ni njia mojawapo ya kudhibiti kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Sasa hivi huduma hii inapatikana mikoa yote nchini.

 

Huduma za kuzuia Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (Prevention of Mother to Child Transmission – PMTCT)

 

54.     Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2004/2005  Wizara imesambaza huduma ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika mikoa 9 zaidi ya Tanzania Bara. Mikoa hiyo ni Lindi, Dodoma, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Mara, Shinyanga, Tanga na Singida na kufanya huduma hii kupatikana katika hospitali zote za Mikoa na hospitali 82 za Wilaya. Vile vile Wizara inashirikiana na wadau mbalimbali ili kuweza kusambaza huduma hii katika hospitali na vituo vya kutolea huduma vinavyomilikiwa na mashirika ya dini.

 

55.     Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na mpango wa kutoa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa UKIMWI kwa akina mama wajawazito, wazazi wenzao na watoto wao.  Mpango huu ambao unaitwa “PMTCT – Plus” unaenda sambamba na mpango wa Taifa wa kutoa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ART programe) na hivyo umeanza kutekelezwa katika vituo 96 vilivyo katika mpango wa ART.

 

Dawa za Kupunguza Makali ya Ugonjwa wa UKIMWI (Anti-  Retro Viral – ARVs)

 

56.     Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2004/2005, shilingi bilioni 8.3 zilitumika kununua dawa za kupunguza makali ya UKIMWI. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.5 zilitolewa na Serikali, dola za Canada millioni 4.5 sawa na shilingi bilioni 3.5 zilitolewa na Serikali ya Canada kupitia Shirika lake la Misaada la Kimataifa (Canadian International Development Agency - CIDA) na Serikali ya Norway ilitoa Euro millioni 1.0 sawa na shilingi bilioni 1.3.  Dawa zilizonunuliwa zitatosheleza kuingiza wagonjwa 44,000 kwa makisio yaliyopo toka wagonjwa 500,000 wanaohitaji tiba ya dawa za kupunguza makali ya UKIMWI.  Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na uwezo wetu.  Huduma ya kutoa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa UKIMWI zitaendelezwa kwa awamu kulingana na uwezo wa kifedha wa Serikali.   Aidha, Serikali itaendelea kuongeza idadi ya wagonjwa wanaopata huduma hii kwa awamu mpaka wagonjwa wote wafikiwe.

 

Huduma ya Tiba ya Wagonjwa wa UKIMWI Nyumbani (Home Based Care)

 

57.     Mheshimiwa Spika, huduma ya tiba kwa wagonjwa wa UKIMWI nyumbani ni ya muhimu sana kama sehemu ya tiba na matunzo kwa wagonjwa wa UKIMWI. Huduma hii hutolewa kwa kushirikiana na jamii na ndugu za wagonjwa. Katika mwaka 2004/2005, huduma hii ilianzishwa katika wilaya 65 za Tanzania Bara ambapo wagonjwa 20,000 (wanaume 9,150 na wanawake 10,850) walifaidika na huduma hii. Aidha, watoa huduma wa jamii 814 walipata mafunzo na vifaa vya kuhudumia wagonjwa nyumbani.

 

 

 

Huduma ya Kufuatilia Mwenendo wa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI katika Jamii

 

58.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 Wizara yangu kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI ilifuatilia vidokezo vifuatavyo katika mwenendo wa ugonjwa wa UKIMWI: Kiwango cha maambukizi ya UKIMWI na magonjwa ya ngono, njia za maambukizi, maambukizi ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa wajawazito na tabia za maambukizi ya UKIMWI miongoni mwa vijana. Utafiti wa tabia nchini Tanzania ulifanyika katika mikoa miwili ya Mbeya na Lindi ukiwalenga vijana wa kike na kiume wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 24. Uchambuzi wa taarifa kuhusu utafiti huo bado unaendelea. Aidha, ufuatiliaji wa viwango vya mambukizi ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa wanawake wajawazito uliendelea katika mikoa kumi hapa nchini. Matokeo ya ufuatiliaji huo yanaonyesha kuwa viwango vya maambukizi kwa wanawake waja wazito ni asilimia 8.7.

 

Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho

 

59.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2004/2005  Tanzania imekuwa ni nchi mojawapo ya kwanza kuandaa na kukamilisha Mpango Mkakati wa miaka mitano (2004-2008) wa Huduma za Macho unaoelekeza kutokomeza upofu unaozuilika ifikapo mwaka 2020.  Mpango Mkakati huu unatoa dira na mwelekeo wa Huduma za Macho katika jitihada za kudhibiti upofu unaozuilika.

 

60.     Mheshimiwa Spika,  Wizara yangu kwa msaada wa shirika la Kitamaifa la kudhibiti ugonjwa wa vikope  imeainisha Wilaya 50 zenye tatizo la ugonjwa wa vikope.  Aidha, utafiti wa kina wa ugonjwa huu umekamilika katika Wilaya thelathini (30) na kuthibitisha kwamba Wilaya 26 kati ya 30 zina ugonjwa huu kwa zaidi ya asilimia 10 ya wakazi.  Kutokana na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani, inapogundulika kuwa jamii imeathirika na ugonjwa huu kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 10, jamii yote inatakiwa kupewa dawa.   Kutokana na matokeo hayo, tumeanza kutoa dawa ya Zithromax katika Wilaya 6 kati ya 26 za Sikonge, Handeni, Dodoma Vijijini, Tunduru, Ruangwa na Magu.  Utafiti katika wilaya 20 zilizobakia unaendelea.  Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kufanya utafiti kama huu kwa nchi zenye ugonjwa huu na kuifanya kuwa nchi ya mfano.  Dawa ya Zithromax ni msaada kutoka Kampuni ya Pfizer kupitia Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Ugonjwa wa Vikope (International Trachoma Initiative – ITI).  Kampuni ya Pfizer iko tayari kutoa dawa ya kiasi chochote tunachohitaji kulingana na mahitaji yetu.

 

61.   Mheshimiwa Spika, Mpango wa Taifa wa kudhibiti ugonjwa wa Usubi uligawa dawa ya mectizan katika vijiji 650 vilivyoko katika wilaya 14 ambazo ni Ulanga, Kilombero, Kilosa, Songea, Mbinga, Tunduru, Ludewa, Rungwe, Kyela, Muheza, Mvomero, Morogoro, Korogwe, na Lushoto. Jumla ya wananchi 2,948,862 walipatiwa dawa hii.

 

Huduma ya Elimu ya Afya Kwa Umma

 

62.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imetoa mafunzo kwa Kamati za Uendeshaji Huduma za Afya za Halmashauri 32 ili ziweze kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini huduma za elimu ya afya kwa umma.  Msisitizo uliwekwa katika kuongeza ubunifu wa mikakati na njia za mawasiliano zenye uwezo wa kuhimiza na kuleta mabadiliko ya tabia na mienendo inayolenga kuboresha afya katika jamii yetu.

 

 

Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto

 

63.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2004/2005 huduma maalum kwa wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ziliendelea kutolewa bila malipo katika vituo vyote vya kutolea huduma vya Serikali. Huduma hizo ni pamoja na huduma kwa wanawake wajawazito, huduma za kujifungua, chanjo, matibabu kwa watoto wagonjwa wenye umri chini ya miaka 5 na uzazi wa mpango. Aidha Wizara yangu ilihakikisha upatikanaji na usambazaji wa dawa mbali mbali za uzazi wa mpango unafanyika nchini kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali.

 

64.     Mheshimiwa Spika, tathmini ya kina ya kutambua hali halisi ya uwezo wa vituo vyetu katika kukabiliana na dharura ya uzazi pamoja na rufaa imefanyika. Taarifa kamili itakuwa tayari mwaka 2005/2006. Matokeo yatatumika katika kuimarisha mikakati iliyopo ya kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi ambapo wilaya zitakuwa ni watekelezaji wakuu. Aidha tathmini ya kitaifa kuhusu hali halisi za Afya (Tanzania Demographic Health Survey) iliyoanisha takwimu za Uzazi na Mtoto imefanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (National Bureau of Statistics). Matokeo ya awali yaliyopatikana mwezi Mei, 2005 yameonyesha kuwa vifo vinavyotokana na uzazi vimeongezeka kutoka 529 mwaka 1996 hadi 578 mwezi Mei 2005 kwa kila kinamama 100,000 wanaojifungua.  Kutokana na matokeo haya ya awali imeonekana kuwa tatizo hili bado linaongezeka.  Wizara yangu itaendelea kuwaelimisha watoa huduma pamoja na jamii kuhusu mbinu za kutambua vidokezo vya hatari na kuimarisha huduma za rufaa.

65.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2004/2005 watoa huduma na wakufunzi 130 walipata mafunzo rejea kuhusu uzazi wa mpango kutoka mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Morogoro, Tanga, Lindi, Mbeya, Pwani na Mwanza. Pia watoa huduma 100 kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Dodoma, Tanga, Mtwara, Morogoro, Lindi, Mbeya, Mwanza na Pwani walipata mafunzo rejea ya utoaji huduma kwa wajawazito ikijumuisha matibabu ya tahadhari kutoa kinga kwa wajawazito dhidi ya malaria na upimaji wa ugonjwa wa Kaswende.

 

Mkakati wa Kutibu Magonjwa ya Watoto kwa Uwiano (Intergrated Management of Childhood Illness-IMCI)

 

 66.    Mheshimiwa Spika,  katika kipindi 2004/2005 Wilaya 87 zinaendelea kutekeleza mkakati wa IMCI. Jumla ya watoa huduma za Afya  300 wamepata mafunzo kuhusu stadi za kumtibu mtoto. Watoa huduma za afya 40 kutoka hospitali 7 za Amana, Temeke, Mwananyamala, Morogoro, Tumbi, KCMC pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamepata mafunzo juu ya utoaji wa huduma ya dharura na kuboresha utoaji huduma kwa mtoto aliyezidiwa. Aidha jamii imeendelea kuelimishwa juu ya mienendo inayoboresha afya ya mtoto. Mienendo hii inakazia lishe kwa mtoto, makuzi ya mwili na akili, pamoja na uzuiaji wa magonjwa ya watoto kwa njia ya chanjo. Mafunzo haya yametolewa katika ngazi ya kaya katika wilaya 13 za Mtwara, Masasi, Hai, Musoma vijijini, Magu, Ngara, Kilosa, Mbinga, Makete, Songea Vijijini, Kisarawe, Kibaha na Mbarali.

 

 

Mpango wa Taifa wa Chanjo

 

67.     Mheshimiwa Spika, huduma za chanjo zimeendelea kutolewa nchi nzima kwa watoto  ikiwa ni juhudi ya Serikali ya kupunguza vifo na magonjwa ya watoto yanayozuilika kwa chanjo. Magonjwa hayo ni kifua kikuu, dondakoo, kifaduro, pepopunda, polio, surua na homa ya ini. Viwango vya chanjo vimeendelea kuongezeka vikilinganishwa na viwango vya mwaka uliopita; chanjo ya DPT- Hepatitis B kutoka asilimia 89 hadi 91,  Surua kutoka asilimia 90 hadi 94, Polio kutoka asilimia 92 hadi 96, Kifua Kikuu kutoka asilimia 94 hadi 95. Mafanikio haya yametokana na juhudi ya Serikali, jamii na wadau mbalimbali wakiwemo Global Alliance for Vaccine and Immunisation (GAVI), ambao tunawashukuru sana.

 

 

 

 

Huduma ya Afya Shuleni

 

68.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 Wizara yangu ilisambaza kadi za kuwekea kumbukumbu ya afya ya wanafunzi kwa kuanzia katika manispaa za IIala, Temeke na Kinondoni.  Waratibu 150 kutoka ngazi ya mkoa na wilaya walipatiwa mafunzo juu ya udhibiti wa magonjwa ya kichocho na aina nyingine za minyoo. Aidha utafiti kuhusu ugonjwa wa kichocho katika shule za msingi umefanyika katika wilaya zote nchini. Matokeo ya utafiti huu yatatolewa katika kipindi cha 2005/2006.  Vile vile Waratibu 75 wa Afya Shuleni wakiwemo wa mikoa yote, na wa Wilaya 17 za Kanda ya Kaskazini walipata mafunzo ya Huduma ya Kwanza (First Aid).

 

Afya ya Mazingira

 

69.     Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma za Afya ya Mazingira na kuinua kiwango cha usafi, Wizara yangu ilianzisha mashindano ya usafi wa mazingira nchini.  Katika kipindi cha 2004/2005 mashindano yalifanyika katika makundi matatu ambayo ni Jiji na Manispaa, Halmashauri za Miji na Halmashauri za Wilaya.  Washindi katika makundi yote matatu ni kama ifuatavyo:-

 

Washindi katika kundi la kwanza la Manispaa na Jiji walikuwa ni  Manispaa ya Moshi ambayo imekuwa mshindi wa kwanza, Jiji la Mwanza limeshika nafasi ya Pili na Manispaa ya Tanga imeshika nafasi ya Tatu.  Kundi la pili washindi walikuwa Halmashauri za Singida Mjini mshindi wa kwanza, Songea Mjini mshindi wa pili na Sumbawanga Mjini mshindi wa tatu na kundi la tatu  washindi walikuwa Halmashauri ya Arumeru mshindi wa kwanza, Lushoto mshindi wa pili na Njombe mshindi wa tatu.

 

70.  Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2004/2005 Wizara iliandaa na kusambaza miongozo ya utekelezaji wa huduma za afya ya mazingira nchini. Miongozo na mikakati iliyoandaliwa ni pamoja na:-.

 

·        Mwongozo wa Mafunzo ya Mbinu Shirikishi Jamii katika kuboresha tabia za Afya na Usafi wa Mazingira,

 

·        Mwongozo wa Udhibiti wa Taka (Waste Management Policy Guideline),

 

·        Mwongozo wa Afya ya Mazingira (National Environmental Health Policy Guideline),

 

·        Na rasimu ya Mkakati wa Kitaifa wa Afya na Usafi wa Mazingira (National Environmental Health, Hygiene and Sanitation Strategy).

 

71. Mheshimiwa Spika, ili kuinua kiwango cha usafi na ubora wa vyoo, kalibu (moulds) za kutengenezea mabamba (slab) 560 zilitengenezwa na kusambazwa katika Wilaya za Rungwe, Bagamoyo, Kisarawe, Monduli na Mufindi na Mkoa wa Kigoma ili zitumike kujengea vyoo bora.

 

72. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia imeimarisha udhibiti wa taka zinazozalishwa katika hospitali (Health Care Waste Management) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuendesha mafunzo juu ya udhibiti wa taka hizo, na ujenzi wa matanuru katika hospitali za Wilaya za Kilosa, Mahenge, Hospitali ya Ocean Road na Hospitali ya Rufaa ya Kibongoto.

 

 

Afya katika Sehemu ya Kazi

 

73.     Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa afya ya Wafanyakazi hususan maeneo ya viwanda, ujenzi na mashamba, Wizara yangu imefanya ufuatiliaji na uhamasishaji wa Bodi za Afya za Halmashauri za wilaya 48 jinsi ya  kuainisha  huduma za afya sehemu za kazi na huduma za afya ya msingi.   Aidha mafunzo ya Afya kazini ya kukabiliana na athari mbalimbali za kiafya kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini katika Mikoa ya Arusha na Mwanza yametolewa kwa wachimbaji 70.

 

 

Taasisi ya Chakula na Lishe

 

74.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2004/2005 Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe iliendelea kutoa ushauri wa kitaalam kwa wilaya na kushirikiana na Taasisi na wadau mbali mbali katika kuboresha hali ya lishe ya jamii nchini.

 

75.     Mheshimiwa Spika, Taasisi iliendelea kuimarisha uwekaji wa madini joto kwenye chumvi katika wilaya 25 zenye wazalishaji chumvi wadogo wadogo kwa kuhamasisha viongozi 285. Aidha Taasisi ilitoa mafunzo kwa wakaguzi wa chumvi 451 na kuunda timu za wakufunzi wa wazalishaji wa chumvi katika wilaya za; Mtwara, Lindi, Kilwa, Rufiji, Mkuranga, Temeke, Kinondoni, Bagamoyo, Dodoma, Manyoni, Singida, Iramba, Kigoma, Njombe na Mbozi. Wilaya nyingine ni Tanga, Pangani, Muheza, Korogwe, Same, Mwanga, Meatu, Babati, Hanang na Karatu. Juhudi zilielekezwa katika wilaya hizo kwa sababu takwimu zinaonyesha kwamba kati ya wazalishaji hao wadogo ni asilimia 30 tu ndio wamekuwa wakiweka madini joto kwenye chumvi. Wizara iliendelea kusambaza vifaa mbalimbali vya kuwekea madini joto kwenye chumvi kwa wazalishaji. Vifaa hivyo ni pamoja na kilo 5,000 za madini joto na pampu 4,650 za kunyunyuzia madini joto kwenye chumvi na jumla ya chupa 93,750 za kemikali ya kupima uwepo wa madini joto kwenye chumvi (iodine test solution).

 

76.     Mheshimiwa Spika, Taasisi iliendelea kuratibu utoaji wa matone ya vitamini A kwa watoto wa umri kati ya miezi sita hadi miaka mitano na vidonge vya kutibu minyoo ya tumboni kwa watoto wa umri kati ya mwaka mmoja hadi miaka mitano katika mikoa yote ya Tanzania Bara; ambapo hadi Desemba, 2004  asilimia 93 ya watoto walengwa walipata matone ya vitamini A na asilimia 90 walipata vidonge vya kutibu minyoo.

 

77.     Mheshimiwa Spika, mkakati wa kitaifa unaoelekeza jinsi ya kusimamia lishe na afya ya mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano umeandaliwa na kuzinduliwa. Aidha, Mwongozo wa kitaifa kuhusu lishe bora kwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI umeandaliwa. Jumla ya nakala 10,000 za mwongozo huo zilichapishwa na kusambazwa kwenye Wizara hospitali za rufaa, hospitali za mkoa na wilaya, vyuo vya afya na taasisi mbalimbali zinazoshughulika na tatizo la UKIMWI hapa nchini.

 

78.     Mheshimiwa Spika, Mpango wa Hospitali Rafiki kwa Mama na Mtoto unaotekelezwa nchini toka mwaka 1992 unalenga katika kuboresha hali ya afya na lishe ya watoto wachanga. Chini ya mpango huu hospitali zinatakiwa kutekeleza na kuboresha Huduma ya Afya na Uzazi kwa wanawake wajawazito na waliojifungua.  Hadi kufikia mwaka 2005 katika kufuatilia Hospitali Rafiki kwa Mama na Mtoto, hospitali 68  nchini zilifanikiwa kuwa rafiki kwa Mama na Mtoto kwa vigezo vya kimataifa.  

 

Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (National Institute for Medical Research – NIMR)

 

79.     Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2004/2005, Taasisi ilishughulikia usimamizi, uratibu, udhibiti, uenezi, utangazaji wa matokeo na ukuzaji wa utafiti nchini. Magonjwa yaliyofanyiwa utafiti ni Malaria, Matende na Mabusha, Usubi, Kichocho, Minyoo ya Tumbo, Kuhara, Magonjwa ya Zinaa, Malale, Kifua Kikuu na UKIMWI.

 

80.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi 2004/2005 tafiti mbalimbali za malaria zimetoa matokeo ambayo yanaonyesha kuwa usugu wa vimelea vya malaria kwa dawa ya SP unakua na umefikia asilimia 25. Hatua hii ya usugu iliyofikiwa inahitaji mabadiliko ya tiba dhidi ya malaria itakayoweka viwango vipya vya dawa za kutibu malaria na kuweka bayana mabadiliko ya sera ya tiba ya malaria. Kiutafiti pendekezo linalotolewa kukabiliana na usugu huu ni matumizi ya dawa mchanganyiko (combination therapy). Taasisi pia inafuatilia kuona kama kuna uwezekano wa mbu kuwa na usugu kwa viuatilifu vinavyotumika katika vyandarua hapa nchini. Ufuatiliaji huo umefanyika katika wilaya za Muheza, Tanga, Korogwe, Lushoto, Babati, Arumeru, Magu, Tabora, Kyela, Moshi, Ifakara, Kinondoni na Pangani. Aidha ujenzi wa jengo la kituo cha kuimarisha mikakati thabiti ya kudhibiti malaria kilichoko NIMR, Dar es Salaam (Center for Enhancement of Effective Malaria Interventions - CEEMI) lilikamilika na kufunguliwa rasmi na Mhe. Naibu Waziri wa Afya Dk. Hussein Ali Mwinyi (Mb.) Septemba, 2004.

 

81.     Mheshimiwa Spika, Wizara pia kwa kupitia Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu imefanya utafiti ili kutathmini kiwango cha dawa kinachopatikana katika mmea wa Artemisia annua na pia kufanya utafiti katika ngazi ya kimaabara ya namna ya kutengeneza dawa itokanayo na mmea huo. Kutokana na utafiti huu, Wizara imefanikiwa kupata mtiririko wa namna ya kutengeneza “Artemisinin” na baadaye kuibadilisha “Artemisinin” kuwa “Dihydro-artemisinin”, dawa inayofaa kwa kutibu malaria.  Aidha, watafiti wa Kituo cha Utafiti cha Ifakara kwa kutumia tabia ya maumbile ya mbu ya kupenda kupumzika gizani baada ya kufyonza damu, wameweza  kutumia njia za asili za kibaolojia kutengeneza dawa ambayo itawaangamiza mbu bila ya kuharibu mazingira.  Utafiti huu bado unaendelea na utakapokamilika tutalijulisha Bunge lako tukufu.

 

82.     Mheshimiwa Spika, uchunguzi juu ya nguvu za viuatilifu ya kuulia wadudu wanaosababisha usubi ulifanyika katika wilaya za Rungwe na Kyela. Matokeo yalionyesha mafanikio mazuri, kwa kuua wadudu hao kama ilivyotarajiwa.  Wizara itayatumia matokeo haya na kuendelea kutumia nguvu za viuatilifu kuua wadudu wanaosababisha usubi.

 

83.     Mheshimiwa Spika, Utafiti wa kuangalia ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa matende umeonyesha kuwa asilimia 6.6 ya watanzania wameathirika na ugonjwa huu. Tathmini pia imegundua kwamba watu wenye vimelea vya ugonjwa wa matende wapo katika wilaya zote za nchi yetu isipokuwa wilaya ya Babati na Chunya. Aidha, katika jitihada za kupambana na tatizo la matende na mabusha Wizara yangu katika mwaka 2004/2005 iligawa dawa kwa watu 900,000 katika mkoa wa Tanga na hivyo kufanya jumla ya watu 5,000,000 waliofikiwa na mradi huu tangu ulipoanza mwaka 2000 katika wilaya 24. Huduma ya upasuaji wa mabusha inaendelea katika mkoa wa Pwani hususan katika hospitali za wilaya za Mafia na Kibaha. Jumla ya watu 2000 walifanyiwa upasuaji katika mkoa wa Pwani.

 

84.     Mheshimiwa Spika, taasisi ilifanya utafiti kwa wagonjwa walioathirika na kifua kikuu pamoja na UKIMWI mkoani Mwanza. Wagonjwa hawa walipewa virutubisho na dawa za kutibu kifua kikuu. Matokeo yalionyesha kwamba idadi ya vifo ilipungua kwa asilimia 72 ikilinganishwa na wakati walipopewa dawa za kifua kikuu peke yake. Aidha kwa kushirikiana na kituo cha Munufu kilichopo Ubungo Dar es Salaam,  Taasisi imeifanyia utafiti wa awali dawa ya tiba ya asili ya Muhanse inayotumiwa na baadhi ya wagonjwa wa UKIMWI na kuiona haina madhara ya kuhatarisha maisha ya mtumiaji. Taasisi itaendelea  kuifanyia utafiti  zaidi ili kujua uwezo wake wa kutibu.

 

85.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa ushirikiano na Taasisi imefanya  tathmini ya magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo katika Ukanda wa Ziwa kwa wanafunzi 8,580 wa shule 143 za msingi za mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Tabora na  Kagera. Matokeo ya tathmini hii yatasaidia kupata njia muafaka za kupambana na magonjwa haya.

 

Kuimarisha Huduma za Afya Wilayani

 

86.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2004/2005 Wizara yangu imebadilisha magari machakavu na kutoa mapya 19 kwenye Halmshauri za Monduli, Kiteto, Mbeya, Songea, Nkasi, Rufiji, Muleba, Singida, Mbinga, Rombo, Magu, Kibondo, Kigoma, Urambo, Kyela, Rungwe, Manispaa ya Tabora, Jiji la Mwanza na ofisi ya Mganga Mkuu Kagera kwa ajili ya ufuatiliaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na kinga kwenye vituo vya kutolea huduma.

 

 

HUDUMA ZA TIBA

 

Huduma ya Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba

 

87.     Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2004/05, kiasi cha shilingi 30,660,128,899.37/= zilitumika kununua dawa, vifaa na vifaa tiba kwa matumizi ya hospitali, zahanati na vituo vya afya. Aidha, hospitali za wilaya, mikoa na rufaa ziliendelea na utekelezaji wa uchangiaji wa gharama za dawa chini ya mfumo wa ‘Capitalization of Hospital Pharmacies’ ambapo wananchi wanalipa nusu ya bei halisi ya dawa. Fedha kutokana na mauzo ya dawa ziliingizwa kwenye mfuko wa dawa (Drug Revolving Fund) kuwezesha hospitali hizo kununua dawa nyingine zilizohitajika.

 

88.     Mheshimiwa Spika, Bohari ya Madawa ndicho chombo kikuu cha Serikali cha ununuzi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba vikiwemo vinavyotolewa kwa kupitia misaada mbalimbali ya miradi misonge (vertical programme). Katika kipindi hicho, Bohari ya Madawa ilisambaza dawa za chanjo, dawa za kutibu kifua kikuu na ukoma, usubi, uzazi wa mpango, matende, mabusha na magonjwa ya mtegesheo kwa watu waishio na virusi vya UKIMWI.

 

89.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005, zahanati mpya 526 na vituo vya afya 36 vilivyojengwa na Halmashauri na kwa nguvu za wananchi vilipewa masanduku ya dawa. Aidha, zahanati 716 na vituo vya afya 88 katika mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza na Shinyanga vilianza kuagiza dawa na vifaa kwa kutumia mfumo wa kuagiza dawa kulingana na mahitaji (indent). Kutokana na hatua hiyo, Bohari ya Mwanza sasa imeondokana na mfumo wa usambazaji wa masanduku ya dawa.

 

90.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia ilitoa mafunzo ya utekelezaji wa mfumo wa kuagiza dawa kulingana na mahitaji kwa wajumbe wa Kamati za Uendeshaji wa Huduma za Afya katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga. Wajumbe hawa watatoa mafunzo kwa watumishi katika zahanati na vituo vya afya katika mikoa yao ili kuwezesha uagizaji wa dawa na vifaa kulingana na mahitaji na kwa kuzingatia mgao wa fedha na mzigo wa magonjwa katika sehemu zao.

 

 

Huduma za Uchunguzi wa Magonjwa

 

91.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005, Mradi wa uimarishaji wa huduma za eksirei na ultrasound (Overseas Related Export Trade – ORET) ulikabidhiwa kwa Serikali na kampuni ya “Philips Medical Systems” ya Uholanzi.  Makabidhiano hayo yalifanyika Jijini Mwanza katika hospitali ya Bugando tarehe 22 Februari 2005.  Katika makabidhiano hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alipewa zawadi ya  mashine kubwa na maalum ya Ultrasound yenye thamani ya shilingi millioni 88.  Naye Mheshimiwa Rais alitoa mashine hiyo kwa hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.  Mashine hiyo imekwishakabidhiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar kama Mheshimiwa Rais alivyoagiza. Katika kuboresha huduma za mionzi, Wizara yangu inatayarisha muswada wa sheria wa usajili wa wanataaluma ya mionzi.

 

92.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 Wizara yangu, imezipa Karakana za kanda vipuli, na nyenzo za utekelezaji wa matengenezo ya mashine za kutolea huduma za afya. Wizara pia imetoa mafunzo kwa mafundi ili kuhakikisha kuwa mashine hizo pamoja na vifaa na vifaa tiba vinadumu kwa muda mrefu zaidi.

 

93.     Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za maabara za hospitali ili ziweze kufuatilia wagonjwa wanaopatiwa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa UKIMWI, Wizara yangu imeweka mashine  za kupima CD4 katika hospitali zote za rufaa, mikoa yote pamoja na hospitali za manispaa za Dar es Salaam.  Vile vile, mashine kwa ajili ya vipimo vingine (Clinical Chemistry & Haematology) kwa ajili ya hospitali 10 za mikoa na 13 za wilaya zimekwisha agizwa.  Vipimo hivyo ni kwa ajili ya kufuatilia athari zinazoweza kuwapata wagonjwa kutokana na kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa UKIMWI.

 

Damu Salama

 

94.     Mheshimiwa Spika, mwaka 2004/2005 Wizara yangu imeimarisha upatikanaji wa damu salama kwa kukamilisha mwongozo wa utoaji wa huduma za damu salama na kukamilisha vituo 3 vya kanda (Zonal Blood Transfusion Centres- ZBTC) katika kanda za Ziwa, Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini.   Vituo hivyo vya Kanda vitahudumia hospitali zote zilizoko katika kanda hizo.

 

Kwa upande wa Kanda ya Mashariki, ujenzi wa kituo umekwisha anza Dar es Salaam  eneo la Mchikichini.  Hadi hivi sasa Mkandarasi amemaliza asilimia 30 ya kazi.  Kituo hiki kitakapokamilika kitahudumia hospitali zote zilizoko katika Kanda ya Mashariki.

 

 Huduma ya Afya ya Kinywa

 

95.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 Wizara ya Afya imefunga vifaa  vya Tiba ya Meno (Dental Units) katika  hospitali zilizobakia katika awamu ya kwanza katika Halmashauri za Wilaya zifuatazo:  Mbarali, Karatu, Ngorongoro, simanjiro, Kiomboi, Morogoro Vijijini, Mbozi, Hanang, Sikonge, Mpanda, Mvomero, Bariadi, Bukombe, Kilombero, Liwale, Njombe, Ludewa, Sengerema, Geita, Ukerewe, Misungwi, Newala, Mwanga, Kwimba na Manispaa ya Morogoro.  Aidha,  hospitali za mikoa ya  Iringa, Bombo, Mawenzi, Mt. Meru na hospitali ya rufaa ya KCMC nazo zilipata vifaa hivyo.

 

Huduma ya Afya ya Akili na Vita dhidi ya Madawa ya kulevya

 

96.     Mheshimiwa Spika, mwaka 2004/2005 Wizara imeendelea kusimamia uboreshaji wa huduma za afya ya akili ngazi ya msingi.  Shughuli hizo zinaendelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara, Mtwara na Mwanza. Pia vitabu vya kiswahili vinavyobainisha na kutibu magonjwa ya akili yanayojitokeza kwa wingi ndani ya jamii  vimechapishwa na kusambazwa.

 

Huduma za Hospitali za Mashirika ya kujitolea,  Makampuni na Watu Binafsi

 

97.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 ruzuku ya kitanda ilipandishwa kutoka Tshs 15,000/= hadi TShs 30,000/= kwa mwaka. Aidha, hospitali mbili za Mashirika ya Dini (Karatu na Mugana) ziliombwa na Halmashauri za Wilaya ya Karatu na Bukoba Vijijini zitumike kama Hospitali Teule. Hospitali hizo tayari zimeanza kutumika kama hospitali Teule za wilaya hizo. Katika mwaka huo kulikuwa na ongezeko la vitanda 174 kwa ajili ya kupewa ruzuku na kufanya jumla ya vitanda vinavyopewa ruzuku hadi sasa kufikia 5,623. Wizara yangu pia ilisajili vituo vya kutolea huduma za afya  53 kati ya 73 vlivyoombewa usajili.

 

Huduma ya Tiba Asili

 

98.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sheria namba 23 ya mwaka 2002 inayosimamia Dawa, Tiba Asili na Tiba Mbadala, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala tayari limekwisha teuliwa na mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria hiyo. Wizara ya Afya imeandaa Kanuni na Miongozo ya usajili wa Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, usajili wa vituo vya kutolea huduma,   nidhamu na maadili, usimamizi na usajili wa bidhaa nyinginezo za Asili zinazotumika kwa ajili ya afya ya binadamu. 

 

Huduma ya Matibabu Nje ya Nchi

 

99.     Mheshimiwa Spika,  kama nilivyoahidi katika hotuba ya mwaka jana, Wizara yangu imefanya mazungumzo na shirika la TOKUSHUKAI kutoka Japan na limeahidi kutusaidia kujenga hospitali ya ubora wa hali ya juu itakayotumika kutibu magonjwa mbalimbali yaliyokuwa yakitibiwa nje ya nchi yakiwemo magonjwa ya moyo. Aidha, tunaendelea na mazungumzo na Serikali ya China na India ili tupate hospitali nyingine za kiwango kama hicho.

 

Hospitali za Rufaa na Hospitali Maalumu

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili

 

100.   Mheshimiwa Spika, hospitali iliendelea kutoa huduma kwa wagonjwa huku ukarabati mkubwa ukiendelea katika hospitali hiyo. Aidha, hospitali hiyo ilianzisha matibabu kwa wagonjwa 1,211 wa UKIMWI. Hata hivyo, huduma za     upasuaji na  maabara ya pathologia  zilipungua kutokana na ukarabati unaoendelea katika hospitali hiyo.

 

101.   Mheshimiwa Spika,  kufuatia kukamilika kwa kazi ya Kamati ya Mpito, wafanyakazi wa lililokuwa Shirika la Afya Muhimbili walipangwa ama Hospitali ya Taifa Muhimbili au chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Afya (Muhimbili University College of Health Sciences – MUCHS).  Hivi sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili imeandaa muundo mpya wa utumishi unaolingana na hali ya sasa na mabadiliko yanayoendelea katika hospitali hiyo ya taifa.

 

102.   Mheshimiwa Spika, hospitali hiyo, imeweza kutoa huduma muhimu bila ya kulimbikiza madeni ya malipo ya kazi za ziada (overtime). Hospitali hiyo pia imefanikiwa kulipa madeni ya kazi za ziada kwa watumishi ya tangu 2001. Hayo yaliwezekana kwa sababu hospitali hiyo kutokana na juhudi za hospitali  kuongeza ufanisi. Kuhusu makusanyo katika mwaka 2004/2005 hospitali hiyo ya taifa ilikusanya zaidi ya shilingi bilioni moja kutokana na huduma binafsi na uchangiaji wa huduma za afya.

 

 

Hospitali ya Bugando

 

103.   Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa maboresho ya huduma za afya uliendelea katika hospitali ya Bugando katika mwaka 2004/2005.  Maboresho hayo yalilenga katika ukarabati, utoaji mafunzo, utoaji wa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) na ujenzi wa kituo cha kanda cha kuhifadhi damu salama (zonal blood bank) pamoja na kutoa  huduma ya kutembelea hospitali za nje (outreach services). Aidha hospitali imeanzisha chumba cha kisasa cha kuhudumia wagonjwa mahututi (intensive care unit).

 

 

104.   Mheshimiwa Spika, hospitali hii yenye jengo kuu la hospitali lenye ghorofa 11 imefanya ukarabati wa ghorofa 5, kwenye maeneo yanayotumika kwa kutoa huduma kwa wagonjwa.  Ukarabati huo uliojumuisha wodi na chumba cha upasuaji wa wazazi wenye matatizo uliogharimu shilingi 142,153,250 zilizopatikana  kwa msaada  wa Japan/Tanzania Food Counterpart Fund. Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa  Serikali ya Japan kwa msaada wao.

 

105.   Mheshimiwa Spika, mafunzo mahali pa kazi yalitolewa kwa wafanyakazi wa hospitali wa vitengo mbalimbali ili kuboresha huduma zinazotolewa.  Aidha wafanyakazi 45 walipelekwa kwenye mafunzo ya kujiendeleza vyuoni.  Ili kuinua kiwango cha elimu kwa wafanyakazi wasio na elimu ya sekondari Hospitali imeanzisha masomo ya sekondari kwa wauguzi na watumishi wengine ili waweze kujipatia elimu hiyo katika sehemu yao ya kazi.

 

106.   Mheshimiwa Spika, hospitali ya Rufaa ya Bugando ilianza kutoa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI mwezi Oktoba 2004.  Wananchi wengi wamejitokeza na zoezi linaendelea vizuri.  Wagonjwa 1,000 wanahudhuria kliniki kati ya hao 300 ndio wako kwenye matibabu ya dawa za kupunguza makali ya UKIMWI.  Aidha huduma za kuzuia maambukizi ya UKIMWI toka kwa mama kwenda kwa mtoto   zinaendelea  kutolewa.

 

107.   Mheshimiwa Spika, hospitali ya Bugando imeanzisha mpango maalum kwa kushirikiana na AMREF wa kupeleka Madaktari Bingwa kwenye hospitali za mikoa ya Kagera, Kigoma, Shinyanga na Mwanza kila mwezi kutoa huduma za ubingwa.

 

Hospitali ya KCMC

 

108.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/05, hospitali ya KCMC ilikamilisha awamu ya kwanza ya upanuzi wa jengo la Idara ya Wagonjwa wa Dharura. Jengo hilo pia linatumika kwa huduma za wagonjwa wa nje, vipimo vya ubongo  mionzi (eksirei), famasia, kutunza kumbukumbu za wagojwa na huduma ya afya kazini (occupational therapy). Aidha, hospitali hiyo imepata wafadhili kutoka Marekani kwa ajili ya upanuzi wa wodi, chumba cha upasuaji na jengo la idara ya magonjwa ya njia ya mkojo ambao uligharimu shilingi millioni 170.

 

109.   Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba katika kipindi cha mwaka 2004/05 nilizindua maabara kubwa ya Bio-Technolojia kwa ajili ya utafiti wa malaria katika hospitali ya KCMC. Aidha, hospitali hiyo ilipokea vifaa vipya kwa ajili ya Kitengo cha “Endoscopy” vyenye thamani ya shilingi millioni 300 kupitia Bohari Kuu ya Madawa pamoja na kununua mashine ya kufulia. Vifaa hivyo vimefungwa na vinatumika. Katika kipindi hicho, hospitali hiyo ilianza uzalishaji wa hewa muhimu ya “oxygen” na hivyo kuondokana na gharama za ununuzi wa hewa hiyo na ina uwezo wa kutoa huduma hiyo ya oxygen kwa hospitali za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.

 

110.   Mheshimiwa Spika, hospitali hiyo ilifanya upasuaji wa kwanza kwa wagonjwa wa moyo 13. Upasuaji huo ulifanywa na madaktari wa hospitali hiyo kwa kushirikiana na madaktari kutoka Chuo Kikuu cha Florida, Marekani.

 

111.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/05, mafunzo ya uganga yaliendelea kuongezeka kama ifuatavyo: wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tiba (KCMC College) walikuwa mwaka wa kwanza 38, mwaka wa pili 27, mwaka wa tatu 24, mwaka wa nne 26 na mwaka wa tano 15. Pamoja na madaktari wanafunzi, pia kumekuwa na ongezeko la madaktari wanaochukua mafunzo ya ubingwa katika fani mbali mbali. Jumla ya madaktari wa masomo ya ubingwa walikuwa 87.  Aidha, katika kipindi hicho, kulikuwa na wahitimu 49 kama ifuatavyo: madaktari 11, madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto 2, madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama 2, daktari bingwa wa magonjwa ya macho 1, madaktari bingwa wa upasuaji mifupa 2, daktari bingwa wa magonjwa ya masikio na koo 1, madaktari bingwa wa afya ya jamii 9, shahada ya uuguzi (b.sc. nursing) 5, shahada katika taaluma ya viungo bandia (b.sc in prosthetics and orthotics) 2, stashahada ya occupational therapy 4 na stashahada fundi sanifu maabara (laboratory technologists) 10.

 

112.   Mheshimiwa Spika,  Wizara yangu ilianza kutoa fedha kwa ajili ya huduma za akina mama wenye matatizo ya VVF mwaka 2003/2004.  Hadi hivi sasa jumla ya akina mama ………………. wamefaidika na huduma hii muhimu.  Wizara yangu itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya huduma hii.

 

Huduma hii inatolewa na hospitali za Serikali pamoja na Mashirika ya Dini nay a kujitolea ambayo ni Bugando, CCBRT, Selian Arusha na Peramiho.

 

Hospitali ya Rufaa Mbeya

 

113.   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2004/05 hospitali ya Rufaa Mbeya iliendelea kutoa huduma za tiba ngazi ya rufaa kwa mikoa ya nyanda za juu kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma, katika majukumu yake ya kutoa huduma za tiba za rufaa (tertiary care) kwa wananchi.  Hospitali pia iliendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya na kufanya utafiti unaosadia kutatua matatizo ya kiafya kwa wananchi. Mafunzo yaliyotolewa kwa kipindi hicho yalikuwa katika fani za Madaktari Wasaidizi, (assistant medical officers), Tabibu wa Meno (dental assistants) na uendeshaji wa huduma katika vyumba vya kupasulia kwa wauguzi (theatre management course for nurses).  Aidha, hospitali ilitoa mafunzo ya kazi kwa vitendo kwa wanafunzi waliofuzu mafunzo ya shahada ya udaktari (intern doctors).

 

114.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 hospitali ilitekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na:

 

·        Ujenzi wa kitengo cha kuhudumia wagonjwa mahututi (intensive care unit),

 

·        Ukarabati wa wodi za hospitali kuu,

 

·        Uwekaji wa mfumo wa maji moto unaotumia mionzi ya jua kwa ajili ya kitengo cha wazazi META,

 

·        Uanzishaji wa ukusanyaji wa damu salama, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha kanda,

 

·        Kuongeza idadi ya madaktari wanaofanya mafunzo ya vitendo kwa mwaka mmoja (intern doctors) kutoka 20 mpaka 45.

 

 

Taasisi ya Tiba ya Magonjwa ya Mifupa  (MOI)

 

115.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/05, Taasisi ya Tiba ya Magonjwa ya Mifupa (MOI) iliendelea kutoa huduma za kibingwa za Tiba kwa wagonjwa wa mifupa na upasuaji wa mishipa ya fahamu kwa ufanisi zaidi. Taasisi hii ilihudumia jumla ya wagonjwa 1,811 ambapo wagonjwa 1,577 sawa na asilimia 86 walikuwa wa kawaida, na wagonjwa 234 sawa na asilimia 14 walikuwa wa kulipia (private). Aidha, kutokana na kuendeleza mfumo wa kutibu wagonjwa wa kawaida na wa kulipia (Public/Private Mix) Taasisi ilikusanya jumla ya shilingi 442,615,161 ambayo ni asilimia 13 ya mapato yote ya Taasisi.  Fedha hii ilitumika kutoa motisha kwa wafanyakazi, kusaidia uendeshaji wa Taasisi. 

 

116.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 Taasisi ilianzisha huduma za upasuaji ambazo awali hazikuwepo na ilibidi wagonjwa waende kutibiwa nje ya nchi na hivyo kuigharimu Serikali fedha nyingi.  Upasuaji huu ni pamoja na ubadilishaji wa mifupa ya nyonga (total hip replacement) na pia upasuaji wa ubongo.  Aidha ili kufanikisha upasuaji huo muhimu,  Serikali ilinunua na kufunga vitendea kazi katika vyumba vitano (5) vya upasuaji, vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU), majeruhi (casualty) na dharura.  Huduma ya ubadilishaji wa mifupa ya nyonga (total hip replacement),   ilitolewa na hadi hivi sasa wagonjwa 32 wamebadilishiwa mifupa ya nyonga, na viungo bandia 446 vilitengenezwa na kutolewa kwa wagonjwa. Aidha, tanuru (incinerator) la kuchomea taka lilijengwa.

 

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (The Ocean Road Cancer Institute)

 

117.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kushirikiana na wahisani imeendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa wa Saratani nchini. Aidha Taasisi imekamilisha ujenzi wa vyumba maalum vya mashine zinazotumika kutibu saratani, kuendeleza huduma ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, kuwatibu na kuwapatia nafuu wagonjwa waliozidiwa wa saratani majumbani kwao, na kufanya tafiti za saratani.   Aidha katika kipindi hicho Taasisi kwa kushirikiana na wahisani iliwasomesha nje ya nchi  wataalamu wawili wa kutibu saratani.

 

Hospitali ya Kibong’oto

 

118.   Mheshimiwa Spika, hospitali ya Kibong’oto ni hospitali maalum kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Kifua Kikuu ulioshindikana kutibiwa katika hospitali nyingine. Hospitali pia hutoa huduma kwa wananchi wenye magonjwa ya kawaida.  Katika mwaka wa 2004/05 hospitali ya Kibong’oto imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu waliopewa rufaa toka hospitali za mikoa hasa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dodoma, Shinyanga, Dar es Salaam na Singida. Hospitali pia imejenga wodi kwa ajili ya wagonjwa wa Kifua Kikuu wenye vimelea sugu vya Kifua Kikuu (Multi Drug Resistant – TB – MDRT).   Aidha, hospitali imekamilisha taratibu za manunuzi ya mashine za kufulia na   ya kutakasia vifaa vikiwemo vikombe vya makohozi.  Mashine hizi zitagharamiwa kwa msaada wa Shirika la Kimataifa la AXIOS.

 

 

 

 

 

Hospitali ya Mirembe na Taasisi ya Isanga

 

119.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2004/2005 Hospitali ya Mirembe na Taasisi ya Isanga ilitekeleza miradi ya maendeleo na shughuli za kawaida kama ifuatayo:

 

·        Ukarabati wa wodi tatu za wagonjwa,

 

·        Ukarabati wa mfumo wa maji taka katika Taasisi ya Isanga,

 

·        Ujenzi wa ukuta wa ngome ya wanawake katika Taasisi ya Isanga pamoja na kuweka taa za usalama/ulinzi,

 

·        Ukarabati wa jengo la kutolea huduma za kinywa na meno,

 

·        Ujenzi wa tanuru la kuchomea taka ngumu (incinerator).

 

·        Utoaji wa mafunzo ya kuboresha ujuzi wa watumishi wa kuzuia maambukizi yanayotokana na kuchomwa na vitu vyenye ncha kali kama sindano.

 

·        Ununuzi wa dawa muhimu, vifaa tiba na vifaa vya usafi vya kutosha,

 

·        Wauguzi 70 walipatiwa mafunzo ya kuzuia maambukizi, kwa wagonjwa wanapokuwa wodini (Hospital Acquired Infecious).

 

·        Chuo cha uuguzi Mirembe kilitoa stashahada kwa wataalamu 40 wenye taaluma ya kuhudumia wagonjwa wenye magonjwa ya akili.

 

·        Kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa wanafunzi wa shule zilizofanyiwa utafiti,

 

·        Makusanyo ya fedha za uchangiaji huduma za afya yaliongezeka kutoka shilingi millioni 3.6 mwaka 2003/04 hadi shilingi millioni 5.1 mwaka 2004/05. Fedha hii ilitumika kufanyia ukarabati wa majengo pamoja na kununulia dawa muhimu  za ziada.

 

 

 

 

HUDUMA ZA UTAWALA NA UTUMISHI

 

120.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2004/2005, Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza sera ya menejimenti na ajira katika utumishi wa umma ya mwaka 1999, kwa kuajiri jumla ya watumishi 148 wa kada mbalimbali za afya. Aidha katika kushughulikia maslahi na maendeleo ya watumishi ili kuimarisha utendaji kazi Wizara ya Afya imewapandisha vyeo watumishi 6,587. Hili ni ongezeko la asilimia 65 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuwapandisha vyeo watumishi 4000.

 

121.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 watumishi 110 wa kada na ngazi tofauti walifanyiwa upekuzi (vetting) kwa madhumuni ya kuwawezesha kuelewa na kuzingatia misingi ya maadili mema katika utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Msisitizo mkubwa uliowekwa katika mafunzo hayo ulihusu suala zima la matumizi sahihi ya taarifa za Serikali na utii kwa Serikali. Aidha Wizara iliendelea kutoa mafunzo ya jinsia kwa watumishi ili kuendelea kudumisha Utawala Bora. Jumla ya watumishi 744 walipatiwa mafunzo hayo.

 

122.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2004/2005 Wizara ya Afya ilitoa mafunzo kwa maafisa waandamizi na wa ngazi ya kati kuhusu misingi ya Utawala Bora na mapambano dhidi ya rushwa ili kuzuia matukio ya rushwa na kuziba mianya ya rushwa. Mafunzo haya yaliwahusisha Wakurugenzi wa Wizara ya Afya, Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Vyuo vyote vya Afya nchini na Maafisa wengine. Jumla ya watumishi 1,169 walipatiwa mafunzo hayo.

 

123.   Mheshimiwa Spika, sambamba na mapambano dhidi ya rushwa, Wizara ilichapisha vijarida vya Mkataba wa Huduma kwa Mteja na kuvisambaza kwa wadau. Lengo lilikuwa kuwafahamisha wateja wetu mahusiano na majukumu yetu kwao pamoja na haki na wajibu wao. Mkataba huu unaelekeza pia namna mteja anavyoweza  kutoa malalamiko/maoni kuhusu huduma zetu.

 

 

HUDUMA YA MAFUNZO

 

124.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi 2004/2005, jumla ya wanafunzi 214 walihitimu mafunzo katika ngazi ya Shahada wakiwemo Madaktari, Madaktari wa Meno, Wafamasia Maafisa Afya Mazingira na Wauguzi. Mchanganuo wake ni kama ifuatavyo: Madaktari  103 walihitimu kutoka Muhimbili; 11 KCMC; 12 Hubert Kairuki na 5 IMTU.  Madaktari wa meno 13; wauguzi 19; Wafamasia 32 na Maafisa Afya Mazingira 19.  Aidha jumla ya Watumishi 83 walihitimu mafunzo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili kama ifuatavyo;  Madaktari bingwa tiba 21, Afya ya jamii 30 na Famasia 32.

 

125.   Mheshimiwa Spika, Jumla ya wanafunzi 2,803 walihitimu fani za Sayansi ya Afya na Uuguzi katika vyuo vyote vya mafunzo hapa nchini. Jumla ya wanafunzi  1,481 walihitimu kutoka vyuo vya Serikali na 1,322 walihitimu kutoka vyuo vya Mashirika ya dini na Binafsi.  Wanafunzi 2,820 walipata nafasi ya mafunzo katika vyuo vya Sayansi ya Afya na Uuguzi.  Wakati huo huo wanafunzi 1,490 kati ya hao walipata nafasi katika vyuo vya Serikali na 1,330 walipata nafasi katika vyuo vya Mashirika ya Dini na Binafsi.  Aidha, jumla ya Waganga Wasaidizi Vijijini 52 walihitimu mafunzo ya Maafisa Tabibu (Clinical Officer)  kwa kupita mafunzo yanayotolewa kwa njia ya posta na 253 walihitimu kupitia vyuo vya serikali na vya Mashirika ya dini.  Jumla ya wahitimu wa Maafisa Tabibu walikuwa 305.

 

126.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa mafunzo ya kujiendeleza mahali pa kazi kwa watumishi wake ili kuinua na  kutoa huduma bora   kwa wateja.  Katika kipindi 2004/2005 jumla ya watumishi 492 wa kada mbalimbali za afya wamepata mafunzo ya stadi ya kuwahudumia wagonjwa wanaotumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (Anti-Rentro Viral).   Aidha, Watumishi katika hospitali 68 wakiwemo madaktari wafawidhi wa hospitali, Wauguzi waandamizi na Wafamasia walipata mafunzo ya kujiendeleza kuhusu matumizi sahihi ya dawa hizo. 

 

127.   Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa ngazi ya mkoa katika usimamizi na utoaji huduma kwa Halmashauri, Wizara ya Afya imetoa mafunzo ya kuimarisha utendaji kwa ujumla kwa watumishi 72 kutoka katika timu za afya za mikoa ((RHMT) 9 ya Tanga, Ruvuma, Rukwa, Iringa, Shinyanga, Singida, Kilimanjaro, Manyara na Arusha.

 

128.   Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya Afya hapa nchini, Wizara imevifanyia ukarabati vyuo 32 na kuanza ujenzi wa majengo ya Chuo cha CEDHA. Sambamba na ukarabati wa vyuo, huduma ya ukaguzi wa vyuo unaozingatia usafi wa mazingira, ubora wa viwango vya masomo yanayotolewa, mafunzo ya vitendo ulifanyika kwa vyuo 54.  Katika kipindi 2004/2005 vyuo 7 kati ya vyuo vya mafunzo 110 vimepatiwa ithibati (accreditation) na Baraza la Elimu ya Ufundi (National Council for Technical Education – NACTE).  Aidha, vyuo vilivyobaki 103 viko katika hatua mbalimbali za kupata ithibati.

 

OFISI YA MGANGA MKUU KIONGOZI

 

Huduma za Dharura na Maafa

 

129.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kujiandaa kukabiliana na dharura na maafa mbalimbali yanayoweza kutokea katika nchi yetu wakati wowote. Katika kipindi cha mwaka 2004/2005, Wizara yangu imefanya ufuatiliaji wa huduma za dharura na maafa katika mikoa ya Singida, Iringa, Manyara, Pwani, Mtwara na Ruvuma. Mikoa mingine ni Kilimanjaro, Arusha na Tanga.

 

130.   Mheshimiwa Spika, mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na dharura na maafa yalitolewa kwa wajumbe wa Kamati za Uendeshaji za Huduma za Afya za Mikoa (RHMT) katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara na Pwani. Mafunzo haya pia yametolewa kwa baadhi ya wafanyakazi wa afya, walioko katika hospitali za mikoa ya Mwanza, Mara, Pwani na Singida. Aidha mafunzo maalumu ya jinsi ya kutumia mwongozo wa kukabiliana na dharura na maafa (emergency operations plan) yalitolewa kwa watumishi wa afya, walioko katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Singida, Iringa, Manyara, Pwani, Mtwara na Ruvuma. Mikoa mingine ni Kilimanjaro, Arusha na Tanga. Wizara pia ilichapisha na kusambaza vitabu viwili vya miongozo ya utoaji wa huduma za dharura na maafa (health sector guidelines and protocol on emergency and disaster management) na  mpango wa uendeshaji huduma za dharura (emergency operations plan - EOP) nakala 1,000 kila kimoja.

 

Huduma za Uuguzi

 

131.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005, Wizara ya Afya imetayarisha Mwongozo wa  kuzuia maambukizi kwa watoaji wa huduma kutoka kwa wagonjwa walioathirika na virusi vya UKIMWI. Nakala 8,000 za mwongozo huu  zimetayarishwa na zitasambazwa katika Halmashauri zote nchini.  Aidha, Wizara imefanya ukaguzi wa huduma za afya za uuguzi na ukunga katika mikoa ya  Morogoro, Ruvuma, Tabora, Mtwara, Lindi, Mbeya, Shinyanga na Singida. Taarifa ya usimamizi huo ilionyesha kuwa kuna upungufu wa vifaa na watumishi katika hospitali zote.  Wizara inaitumia taarifa hii kuwasiliana na Halmashauri husika kuhusiana na upungufu huu.

 

Mabaraza ya Kitaaluma

 

132.   Mheshimiwa Spika, mwaka 2004/2005 Baraza la Madaktari na Baraza la Wauguzi na Wakunga yalifanya uchunguzi (inquiries) wa makosa ya ukiukwaji wa maadili na miiko katika utendaji kazi kwenye hospitali nne (4) za Morogoro, Mt Meru Arusha, Temeke na hospitali ya Ligula Mtwara. Watumishi 5 waliobainika na makosa walichukuliwa hatua za kinidhamu, wawili walipewa onyo, wawili walisimamishwa na mmoja alifutiwa usajili.  Aidha Baraza la Famasia liliandaa mwongozo wa kusajili wafamasia wa ndani na nje ya nchi),  na mwongozo wa mafunzo kwa Wafamasia wanaofanya mazoezi ya vitendo baada ya kuhitimu mafunzo ya shahada ya Ufamasia.  Mabaraza mengine yakiwemo Hospitali Binafsi, Mafundi Sanifu Maabara na Waganga wa Tiba Asili yaliendelea kufanya kazi za kitaaluma na kuisaidia Wizara katika kuboresha huduma za afya.

 

 

WAKALA ZILIZO CHINI YA WIZARA YA AFYA

 

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)

 

133.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2004/2005 jumla ya aina 279 za dawa  za binadamu aina 12 za dawa za mifugo na aina 22 ya bidhaa za vyakula zilisajiliwa.  Katika jitihada ya kuhakikisha kuwa vyakula, vipodozi na vyakula dawa vimesajiliwa kwa kuhakiki usalama wake kwa watumiaji.  Mamlaka imebaini aina 5066 za vyakula, aina 26 za dawa na aina 921 za vipodozi  havijasajiliwa.  Jumla ya maombi 17 ya kusajili dawa zitokanazo na mimea yalipokelewa na yanaendelea kufanyiwa tathmini.  Sampuli 767 zilizofanyiwa uchunguzi wa kimaabara, sampuli 608 zilikidhi viwango na 159 hazikukidhi viwango.  Bidhaa ambazo hazikukidhi viwango ziliondolewa katika soko na kwa zile ambazo zilikuwa zinaombewa usajili, cheti cha usajili hakikutolewa na hivyo kutokuruhusiwa kuingizwa katika soko la Tanzania. 

 

Aidha, Mamlaka imeendelea kuhakikisha kuwa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI kwa wagonjwa wa UKIMWI, zinazoingizwa nchini ni bora, salama na zina ufanisi unaofikia viwango vinavyotambulika kimataifa. Aidha matukio 42 ya madhara yaliyoshukiwa kutokana na matumizi ya dawa yametolewa taarifa kwa usahihi na kufanyiwa tathmini ili kutambua madhara yaliyotokea kama yamesababishwa na dawa au la.  Iwapo madhara yatagundulika kuwa yamesababishwa na dawa, dawa hiyo itaendelea kufanyiwa utafiti wa kuiondoa kwenye soko.

 

134.   Mheshimiwa Spika, Mamlaka imefanya ukaguzi katika jumla ya maduka 630 ya dawa, 70 ya vipodozi, maduka 39 ya vyakula, viwanda 183 vya chakula na 72 vya dawa   (66 vya nje, na 6 vya ndani). Jumla ya maombi 3,474 ya vibali vya kuingiza bidhaa nchini yalipokelewa. Vibali 3117 kwa ajili ya kuingiza vyakula na dawa vilitolewa.  Maombi 357  yalikataliwa.

135.   Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la ukiukwaji wa sheria unaofanywa katika maduka ya dawa baridi, Mamlaka imeanzisha maduka 41 ya dawa muhimu (Accredited Drug Dispensing Outlets – ADDO) mkoani Ruvuma katika vijiji na miji midogo ikiwa ni nyongeza kwa maduka 110 yaliyokwishafunguliwa tangu mpango huo uanzishwe mnamo Agosti 2003. Tathmini ya mpango wa ADDO imefanyika na kuonyesha mafanikio makubwa.    Kutokana na mafanikio hayo Serikali imepanga kueneza mpango huu kwa awamu.

 

136.   Mheshimiwa Spika, katika kuelimisha wadau na kuboresha upashanaji habari mwaka 2004 Mamlaka ilizindua tovuti www.tfda.or.tz.  Pia mafunzo ya wadau 515 yanayofafanua sheria na majukumu ya TFDA yalifanyika katika kanda za Kusini na Kaskazini.

 

137.   Mheshimiwa Spika, ili kusogeza huduma karibu na wananchi Mamlaka imefungua ofisi za kanda katika mikoa ya Mwanza na Arusha. Mamlaka pia imeimarisha maabara kwa kununua vifaa vya kisasa vya maabara na kusomesha  baadhi ya wafanyakazi wake ili kuongeza ufanisi na uwezo wao wa kuchunguza na kupima vipimo mbalimbali vya vyakula, dawa na vipodozi kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.

 

Huduma za Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali

 

138.   Mheshimiwa Spika, Wakala ulichunguza jumla ya sampuli 8,147  na kutoa matokeo katika wastani wa siku 14 kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Huduma kwa Mteja na kupata jumla ya shillingi 193,344,842. Kati ya sampuli zilizochunguzwa sampuli 3,934 zilikuwa ni za vyakula, dawa, maji, maji taka, kemikali na mazao yake. Sampuli 4,213 zilikuwa ni za madawa ya kulevya  na makosa mengine ya jinai. Idadi ya sampuli za madawa ya kulevya na makosa mengine ya jinai zilizochunguzwa iliongezeka kutoka sampuli 3,718 mwaka 2003, hadi 4,213 mwaka 2004 ambazo ni  ongezeko la  asilimia 13. Matokeo ya uchunguzi huo yamesaidia mamlaka zinazohusika kuchukua hatua zinazostahili na  kuharakisha usikilizaji wa kesi na utoaji haki.

 

139.   Mheshimiwa Spika, katika kusimamia na kudhibiti kemikali zinazotumika Viwandani na Majumbani, Wakala  umepokea na kushughulikia maombi 150 ya usajili wa kemikali kutoka kwa wadau mbalimbali wa Tanzania Bara.  Vibali 365  kwa ajili ya uagizaji na uingizaji wa kemikali kutoka nje ya nchi vilivyotolewa.  Mafunzo kwa wakaguzi 92 wa kemikali nchini yalifanyika.

 

140.   Mheshimiwa Spika, ili kusogeza huduma karibu na wananchi, Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa  Serikali tarehe 7/01/2005 ilizindua rasmi maabara ya kwanza  ya kanda jijini Mwanza. Kuanzishwa kwa Maabara hii kumesaidia   kuondoa kero ya kusafirisha sampuli na gharama kubwa inayohitajika kwa mteja kufika Dar es Salaam ili kufuatilia matokeo ya uchunguzi.

 

 

MIPANGO, MAJUKUMU NA MALENGO YA BAJETI YA MWAKA 2005/2006

 

MIRADI YA MAENDELEO

 

141.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2005/2006, Wizara yangu inaomba kiasi cha shilingi 90,862,748,400 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.  Kati ya fedha hiyo shilingi 5,000,000,000 ni fedha za ndani na  shilingi 85,862,748,400 ni kutoka Taasisi za Kimataifa na Wahisani wanaochangia  Mfuko wa Pamoja wa Afya (Basket Fund – BF) na wale walioko nje ya mfuko.

 

142.   Mheshimiwa Spika, fedha zilizoainishwa hapo juu zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo ifuatavyo:-

 

·        Kuendeleza ukarabati na upanuzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali za Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam urban health facilities).

 

·        Ukarabati wa wodi, maabara, chumba cha upasuaji na kuendeleza ujenzi wa hosteli ya madaktari wanafunzi (intern’s doctors) katika hospitali ya Rufaa Mbeya.

 

·        Kuendeleza ukarabati wa wodi, nyumba za watumishi na jiko katika hospitali maalum ya Mirembe na Taasisi ya Isanga.

 

·        Kukarabati wodi 6, nyumba za watumishi 3, mfumo wa maji taka, kuanza kujenga nyumba 3 za watumishi na kuendeleza ujenzi wa maabara ya kuchunguza vimelea sugu vya ugonjwa wa Kifua Kikuu, kuandaa eneo kwa ajili ya kusimika mashine za kutakasia vikombe vya makohozi ili kuzuia uambukizo wa magonjwa ndani ya hospitali na ununuzi wa vifaa kwa ajili ya hospitali maalum ya Kifua Kikuu ya Kibong’oto.

 

·        Kuendeleza ujenzi wa wodi ya watoto katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 

·        Kukarabati wodi za wagonjwa hospitali ya Saratani Ocean Road.

 

·        Kutoa mchango wa Serikali (counterpart funds) kwa ajili ya kuendeleza ukarabati wa majengo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, ujenzi wa hospitali mpya maalum Dar es Salaam itakayojengwa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na Shirika la TOKUSHUKAI la Japani na maandalizi ya ujenzi wa hospitali ya rufaa Kanda ya Kusini – Mtwara.

 

·        Kukamilisha ujenzi wa maabara ya kudhibiti ubora (quality control laboratory) Makao Makuu ya Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na ununuzi wa vifaa na kemikali kwa ajili ya maabara mpya ya Mwanza. 

 

·        Ukarabati wa vituo vya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Amani, Gonja, Mwanza,  Tukuyu na ofisi za Makao Makuu – Dar es Salaam.

 

·        Ukarabati wa jengo la Ofisi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

 

·        Kuendeleza ukarabati wa vyuo vya afya 35.

 

·        Kununua vifaa tiba kwa hospitali za Rufaa na hospitali maalum.

 

 

SERA NA MIPANGO

 

Mabadiliko katika Sekta ya Afya

 

143.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kuelimisha na kuhamasisha Halmashauri na jamii kuhusu haki na wajibu wao katika mabadiliko yanayoendelea kwa njia  zifuatazo:

 

·        Vipindi na matangazo katika redio na televisheni, mkazo  utawekwa zaidi katika kutumia redio za kanda zilizoko mikoani. 

 

·        Kuziwezesha Halmashauri kujenga uwezo wa vyombo vya uwakilishi wa jamii (Bodi na Kamati za Vituo vya huduma za Afya) wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi, ili jamii iendelee kuunga mkono mabadiliko, kuelekeza juhudi zao katika Mfuko wa Afya ya Jamii – CHF, umiliki, usimamizi na ufuatiliaji wa utoaji huduma za Afya katika maeneo yao.

 

·        Kutengeneza na kusambaza nyenzo na vielelezo mbalimbali (vipeperushi, vijitabu, mabango, na majarida) vyenye ujumbe wa kuelimisha na kuhamasisha mabadiliko katika Sekta ya Afya kwa Halmashauri, vituo vya kutoa huduma za afya na Watendaji wa Kata, Mitaa na Serikali za Vijiji. 

 

144.   Mheshimiwa Spika, Mabadiliko katika Sekta ya Afya, yanahitaji mabadiliko ya tabia, mwenendo, mwelekeo, mazoea, desturi na masuala yote yanayohusu mwenendo mzima wa mfanyakazi. Kwa kuwa utaratibu wa mabadiliko ya kitabia huchukua muda mrefu, Wizara yangu itaendelea kuwaelimisha  na kuwahamasisha wafanyakazi wa afya watambue umuhimu wa mabadiliko, wajibu na majukumu yao katika ngazi zote za utekelezaji kwa njia za:  mafunzo, mikutano na majadiliano, mapitio ya utekelezaji wa mabadiliko, vijitabu, majarida na vipeperushi.

  

Mfuko wa Afya ya Jamii

 

145.   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2005/06 Wizara, itatekeleza yafuatayo:

·        Kutoa mafunzo ya njia bora za kufanya makisio ya makusanyo,

 

·         Kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu CHF,

 

·        Kutoa mafunzo yanayohusu utunzaji na matumizi bora ya fedha za CHF kwa kufuata miongozo, 

 

·        Kushirikiana na mikoa kuteua waratibu wa CHF wa mikoa na Halmashauri chini ya Kamati za uendeshaji huduma za afya za mikoa  -  (RHMT) na  za Halmashauri (CHMT) ili wawe kiungo kati ya Wizara, Mikoa na Halmashauri.

 

146.   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2005/06 Wizara imepanga kuhamasisha na kuziwezesha Halmashauri zote za Miji/Manispaa/Jiji kuanzisha mpango wa Tiba kwa Kadi – TIKA.

 

 

 

 

 

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya

 

147.   Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka wa 2005/06, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya utatekeleza yafuatayo:

 

·        Kuanza kutekeleza mpango mkakati wa miaka mitano ambao umetoa kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za matibabu hususani vijijini ambako zaidi ya asilimia 70 ya wanachama wa Mfuko huu wanaishi.

 

·        Kuongeza idadi ya wanufaika wa Mpango huu hadi kufikia asilimia 5 ya Watanzania wote.

 

·        Kuboresha kitita cha mafao pamoja na kurahisisha upatikanaji wa mafao hayo.

 

·        Kushughulikia suala zima la upatikanaji wa dawa hasa vijijini kwa ushirikiano na wadau na mamlaka husika.

 

·        Kuanzisha mashindano na kutoa tuzo kwa vituo vya matibabu vitakavyotoa huduma bora kwa wanachama.

 

 

Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya (MTUHA) na Utafiti

 

148.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006, Wizara yangu itaunganisha mfumo wa kompyuta uliopo makao makuu ya Wizara na mifumo iliyopo mikoani na katika hospitali za mikoa na za rufaa.  Lengo kuu ni kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo takwimu za afya.

 

149.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaboresha mfumo wa kukusanya takwimu za afya katika ngazi ya Wilaya.  Mfumo huu unalenga kuhakikisha kuwa takwimu zinazokusanywa kutoka vituo vya kutolea tiba zinaingizwa kwenye kompyuta  Wilayani na kupelekwa moja kwa moja Makao Makuu.  Aidha, kukusanya takwimu kutoka vituo vya afya peke yake hakutupatii taswira halisi ya hali ya afya nchini.  Kutokana na umuhimu wa ukusanyaji wa takwimu kutoka katika Jamii, Wizara yangu itaboresha mfumo huu ili  matokeo ya mifumo hii miwili ya ukusanyaji takwimu iweze kutoa taswira ya hali halisi ya nchi nzima.

 

 

MATUMIZI  YA KAWAIDA

 

IDARA YA KINGA

 

150.   Mheshimiwa Spika,  kwa mwaka 2005/2006 Wizara yangu inaomba kiasi cha shilingi 180,305,853,900.  Kiasi cha shilingi 6,406,945,600 ni kwa ajili ya mishahara na kiasi cha shilingi 173,898,908,200 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.  Fedha hii itatumika kutekeleza kazi zifuatazo:

 

Udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza (Epidemiologia)

 

151.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/06 Wizara itaendeleza udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza magonjwa ya milipuko na kutoa mfunzo ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa kwa wataalamu wa afya.

 

Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria

 

152.   Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada kubwa zinazofanyika ili kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini, kuna wilaya 24 ziko katika hatari ya kupata milipuko ya ugonjwa wa malaria. Wilaya hizo ni Mufindi, Makete, Njombe, Rungwe, Mbozi, Ileje, Mbinga, Ilolo, Ludewa, Same, Hai, Dodoma, Mpwapwa, Kongwa, Lushoto, Korogwe, Hanag, Babati, Karatu, Ngorongoro, Nkasi, Sumbawanga, Karagwe na Muleba. Wizara yangu katika mwaka wa fedha 2005/06 imeandaa mikakati ya kuziweka wilaya hizo zenye uwezekano wa kupata milipuko ya malaria katika hali ya tahadhari ya kutabiri milipuko na kudhibiti milipuko hiyo kwa kuwafundisha watendaji wa Wilaya jinsi ya kutumia takwimu za wagonjwa, kuangalia kuzaliana kwa mbu na kiasi cha mvua na hali ya joto.

 

153.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2005/06 Wizara yangu itaendelea na  maandalizi ya kubadilisha matibabu ya malaria kutoka dawa ya SP kwenda dawa mseto ya Artemether/Lumefantrine (ALU/Coartem). Shughuli zitakazofanyika katika maandalizi hayo ni kubadili mwongozo wa matibabu pamoja na kuendesha mafunzo kwa watoa huduma za afya kuhusu tiba mpya na kuelimisha jamii. Baada ya maandalizi hayo kukamilika, tutaanza kutumia dawa mseto mara moja.

 

Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma

 

154.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2005/06 Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma utaendeleza kampeni za kutokomeza ukoma katika mikoa ya Ruvuma, Morogoro na Tanga. Aidha shughuli za kuhuisha rejesta za wagonjwa wa ukoma zitaendelea  sambamba na kampeni ya kutokomeza ukoma ili kufikia lengo la kimataifa  la mgonjwa mmoja kwa kila watu 10,000 ili kufikia lengo hilo ifikapo Desemba mwaka 2005. Mpango utaendelea kuimarisha huduma za pamoja za kudhibiti Kifua Kikuu na UKIMWI na zile za kudhibiti Kifua Kikuu sugu ili kisienee nchini.

 

155.   Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuagiza na kusambaza dawa za kutosha za Kifua Kikuu na Ukoma katika vituo vyote vya matibabu nchini. Aidha Mpango utaendelea kuelimisha jamii kwa kutumia njia zote za upashanaji habari.  Aidha, mpango utaendelea kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga na maambukizi, kutambua mapema dalili za ugonjwa  na taratibu za kufuata wakati wa matibabu ya magonjwa ya kifua kikuu na ukoma.

 

156.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaanzisha huduma kwa wagonjwa wenye Kifua Kikuu sugu (Multi Drug Resistant - TB) katika hospitali ya Kibong’oto iliyoko wilayani Hai. Aidha, Wizara yangu itaanzisha mpango wa kutumia dawa za mseto (four Fixed Dose Combinations) kutibu Kifua Kikuu.  Mpango huu  utaanzishwa katika wilaya 6 za mwanzo kwa majaribio. Mabadiliko haya yana lengo la kupunguza wingi wa dawa anazotumia mgonjwa na kupunguza usugu wa vimelea vya Kifua Kikuu. Aidha tutaendelea na utekelezaji wa mpango wa pamoja wa kudhibiti uambukizo wa kifua kikuu na UKIMWI katika wilaya za Temeke, Korogwe na Manispaa ya Iringa.

 

Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI

 

157.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu katika mwaka wa fedha 2005/2006 itaendelea kufuatilia mwenendo wa maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika jamii kwa kuwafuatilia wajawazito katika kliniki 93 zilizopo kwenye mikoa 15 ya Tanzania Bara. Matokeo ya ufuatiliaji huu yatatoa taswira ya kuenea kwa virusi vya UKIMWI katika jamii na kusaidia kuimarisha  mikakati  ya udhibiti.

 

158.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2005/06 Wizara yangu itakamilisha mwongozo wa ufuatiliaji wa usugu wa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa UKIMWI kwa dawa zinazotumika hivi sasa kupunguza makali ya UKIMWI, na kuanzisha ufuatiliaji wa wagonjwa  katika mkoa wa Dar es Salaam ambapo dawa za kupunguza makali ya UKIMWI zilianza kutumika kabla ya Serikali kuanza mpango wa kutoa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI kwa wagonjwa wa UKIMWI. Matokeo yake yatasaidia katika kujua aina ya  dawa ambazo tayari virusi vya UKIMWI  vinaonyesha kuwa sugu kwa dawa hizo na hivyo kutopunguza tena makali ya ugonjwa wa UKIMWI kwa watumiaji na hivyo kusaidia wataalamu kutoa maelekezo ya dawa zinazofaa.

 

159.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itanunua na kusambaza dawa za kupunguza makali ya UKIMWI katika vituo 198 vilivyoteuliwa kutoa huduma hiyo vikijumuisha vituo 96 vya mwaka jana na 102 vipya ili kuwafikia wagonjwa wapya 56,000 kwa nia ya kufikia lengo jipya lililowekwa na mpango la kuwafikia wagonjwa 100,000 nchini kote ifikapo Desemba 2006. Vituo vipya vitakavyohusishwa katika mpango huu ni pamoja na hospitali zote za wilaya na hospitali zisizo za Serikali zilizoko kwenye mikoa ya pembezoni na mikoa iliyo na viwango vya maambukizi ya UKIMWI zaidi ya asilimia saba.  Mikoa hiyo ni Tabora, Mwanza, Kilimanjaro, Pwani, Mtwara, Dar es Salaam, Iringa na Mbeya. Aidha Serikali kwa mwaka 2004/2005 imetenga shilingi 20,000,000,000/= kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI na shilingi 4,291,856,000 kwa ajili ya ununuzi, usambazaji wa vifaa tiba pamoja na kazi zote za kudhibiti ugonjwa wa UKIMWI.

 

160.   Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kutoa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa hiari katika vituo 521 vinavyotoa huduma hii ili kutoa ushauri nasaha kwa wagonjwa wote 100,000 watakaokuwa kwenye tiba ya dawa za UKIMWI ifikapo Desemba, 2006.  Aidha mafunzo kwa wataalam wa kutoa huduma ya dawa za kupunguza makali ya UKIMWI katika kila kituo yanatolewa kwa wataalam wanne ambao wanatakiwa kuwa katika kila kituo cha kutolea huduma hii.

 

161.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kutoa huduma kwa magonjwa ya zinaa katika mikoa yote 21.  Pia itaendelea kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa UKIMWI,  kupiga vita unyanyapaa na kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa UKIMWI.

 

 

Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho

 

162.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2005/2006, Wizara yangu inatarajia kuongeza wilaya 10 zaidi katika mpango wa kudhibiti ugonjwa wa vikope nchini kwa kutumia mtindo mpya wa “District Wide-Approach”. Wilaya 8 kati ya hizo zinatarajiwa kutoa dawa ya Zithromax kwa wananchi. Wilaya zitakazojumuishwa katika mpango huo ni Kongwa, Kilosa, Meatu, Iramba, Singida vijijini, Igunga, Simanjiro, na Mkuranga. Wananchi wapatao 2,300,000 wanatarajiwa kupata matibabu na kinga ya ugonjwa wa vikope.

 

163.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2005/2006, Wizara yangu inatarajia kugawa dawa ya “Mectizan” kwa ajili ya tiba ya ugonjwa wa usubi (mass treatment) kwa wananchi wapatao 3,000,000 katika vijiji 690 vilivyopo katika wilaya 15 za Ulanga, Kilombero, Kilosa, Songea, Mbinga, Tunduru, Ludewa, Rungwe, Kyela, Muheza, Mvomero, Morogoro vijijini, Korogwe, Lushoto, na Ileje.

 

Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto

 

164. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006, Wizara yangu itaendelea kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto bila malipo katika vituo vya Serikali vya kutolea huduma na zitatolewa bila malipo.  Huduma hizi ni pamoja na matibabu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, chanjo, uzazi wa mpango, huduma kwa wanawake wajawazito watakaohudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma.  Aidha, Wizara yangu itaendelea kununua na kusambaza dawa za uzazi wa mpango nchi nzima. Wizara imetenga fedha kiasi cha shilingi billioni 6.8 kwa ajili ya  kununulia dawa za uzazi wa mpango na kuzisambaza.

 

165.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006, Wizara yangu imepanga kutoa mafunzo mbalimbali katika maeneo ya uzazi wa mpango,  uzazi salama na afya ya uzazi kwa vijana katika mikoa ya Kilimanjaro, Dodoma, Tanga, Mtwara, Morogoro, Lindi, Mbeya, Mwanza na Pwani.

 

Udhibiti wa Magonjwa ya Watoto kwa Uwiano (IMCI)

 

166.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006  Wizara yangu itatekeleza mkakati wa IMCI ili kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano.  Wizara inatarajia kutoa mafunzo ya stadi za kutibu watoto kwa watoa huduma za afya katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya. Pia mafunzo maalum yatatolewa kwa watoa huduma za afya kwa wakufunzi 60 na watoa huduma za afya 220.   Aidha, wakufunzi 60 watakaofundishwa wataendelea kutoa mafunzo katika Halmashauri zao. Mkakati huu pia unalenga kuendeleza mienendo inayoboresha afya ya mtoto katika ngazi ya jamii na kaya. 

 

Mpango wa Taifa wa Chanjo

 

167.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006, Wizara yangu kwa kushirikiana na mikoa itaendelea kusimamia huduma ya chanjo katika ngazi ya wilaya.  Wizara yangu itaendelea kutoa vitendea kazi na chanjo ili kuhakikisha watoto wote wanaostahili chanjo wanapata chanjo.  Aidha juhudi zaidi zitaelekezwa katika kutokomeza polio, kupunguza ugonjwa wa surua, kufuta pepopunda kwa watoto wachanga na hivyo kupunguza vifo. Wizara yangu pia itaendelea kufanya tathmini ya magonjwa mengine yanayozuilika kwa chanjo ambayo chanjo zake hazijaanza kutumika hapa nchini.

 

Huduma za Afya Shuleni

 

168.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 Wizara itatoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa waratibu 80 wa afya shuleni wa ngazi ya wilaya na mikoa kwa mikoa ya Rukwa, Mbeya na Iringa. Aidha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Elimu na Utamaduni tutachapisha na kusambaza kadi za kupima afya za wanafunzi wa shule za awali na sekondari.  Mpango wa utoaji dawa za kichocho /minyoo kwa wanafunzi  utatekelezwa katika mikoa 7 iliyoathirika zaidi ya Mwanza, Mara, Tabora, Kagera, Shinyanga, Kigoma na Tanga.

 

 

Afya ya Mazingira

 

169.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006, Wizara inakusudia kuanzisha mashindano ya kupata vijiji bora katika wilaya 5, kila wilaya itatoa kijiji bora kimoja kitakachokidhi  mahitaji yote ya kiafya.  Vijiji vyote katika wilaya  moja vitashindanishwa ili kupata kijiji bora kimoja kwa kila wilaya. Aidha Wizara itaendelea kushirikiana na Wizara mbali mbali, jumuia za kimataifa, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) na jamii katika kupanga mipango shirikishi jamii ili kuboresha hali ya afya na usafi wa mazingira katika mikoa yote.

 

170.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendeleza mashindano ya afya na usafi wa mazingira nchini, ambayo yataendelea kujumuisha Halmashauri zote nchini (Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya). Lengo kuu la mashindano haya ni kushirikisha wananchi, sekta binafsi katika kuboresha hali ya usafi wa mazingira katika maeneo yao. 

 

171.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu katika kipindi cha 2005/2006 itaanza kutekeleza Mpango Maalum wa muda wa miaka mitano 2005/2006 – 2009/2010.  Mpango maalum wa kudhibiti taka zinazozalishwa  hospitalini  utaanzishwa  ili kudhibiti hali ya uambukizo wa magonjwa kwa watoa huduma, wateja na jamii kwa jumla.  Mpango huu  utazihusisha hospitali zote nchini.

 

 

Afya Bandarini na Mipakani

 

172.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kuimarisha utendaji wa vituo vya mipakani ili kuhakikisha kuwa magonjwa ya kuambukiza yanadhibitiwa kwa kufuata sheria za afya. Vituo hiyo vya mipakani vitapatiwa usafiri.  Vituo hivyo ni Kabanga, Kasumulo, Holili, Kigoma, Kyaka na Tunduma.  Pia udhibiti wa uingizwaji wa vyakula, dawa na vipodozi visivyokidhi viwango vya afya utaimarishwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.  

 

Afya Kazini

 

173.   Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi, Wizara yangu itashirikiana na wadau wote kikamilifu kuendeleza mpango wa kuzuia maambukizi ya UKIMWI mahali pa kazi. Ili kufikia azma hii watumishi wa afya 118 wa Halmashauri za wilaya watapatiwa mafunzo juu ya uboreshaji wa afya ya wafanyakazi sehemu za kazi. Wizara pia itahakikisha kuwa watumishi wote wanashiriki kwenye michezo ili kuboresha afya zao. Katika bajeti ya mwaka 2005/06 Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kujenga chumba cha mazoezi cha kisasa ili kuwawezesha watumishi wote wa Wizara kufanya mazoezi kila siku.

 

Taasisi ya Chakula na Lishe

 

174.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe itaendelea kuratibu shughuli za kitaifa za utoaji matone ya vitamini A na vidonge vya kutibu minyoo kwa watoto walio na umri  chini ya  miaka mitano katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Wizara itaendelea kufuatilia na kutoa mafunzo na mkazo juu ya uwekaji wa madini joto kwenye chumvi, kufikia asilimia 90 kiwango kinachopendekezwa na Shirika la Afya Duniani, Tanzania kwa sasa imefikia asilimia 84.

 

175.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 Taasisi pia itafanya utafiti kuhusu tatizo la upungufu wa damu kwa nchi nzima ili kuwa na takwimu sahihi za hali halisi ya tatizo hilo. Kupatikana kwa takwimu hizo kutasaidia katika kupanga mikakati na programu za kupunguza tatizo hili. Aidha, Taasisi itaandaa na kuchapisha vitabu nakala 10,000 zaidi vya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu lishe bora kwa wenye UKIMWI. Pia Wizara itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu lishe bora ili kuepukana na magonjwa sugu yenye uhusiano na ulaji usiozingatia lishe bora  kama vile  kiriba tumbo (obesity), magonjwa ya mfumo wa mishipa ya  damu, moyo, na mengineyo.

 

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu

 

176.   Mheshimiwa Spika, Taasisi hii inashughulikia utafiti wa magonjwa ya binadamu yakiwemo malaria, usubi, matende na mabusha, malale, kichocho/minyoo na kifua kikuu. Utafiti utaofanyika utalenga maeneo yafuatayo;

 

177. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006, Taasisi itaendelea kufanya utafiti zaidi wa aina za dawa mchanganyiko dhidi ya malaria ili kutoa ushauri sahihi juu ya dawa  zitakazoweza kuhimili usugu wa vimelea vya malaria. Aidha Taasisi  itaendeleza utafiti wa dawa  zinazotokana na mimea zinazoweza kuua na kufukuza mbu wa aina mbalimbali.  

 

178.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2005/06, Taasisi itafanya utafiti wa kupima kiwango cha usubi katika jamii inayoishi kando kando ya mito inayonyunyiziwa dawa ya kuuwa wadudu wanaoeneza ugonjwa wa usubi.  Aidha, utafiti wa uelewa wa ugonjwa wa UKIMWI utaendelezwa katika Wilaya za Korogwe, Kibaha na Iringa. Pia utafiti wa kutathmini maendeleo ya wagonjwa wanaopewa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI  (ARVs) utaendelea katika wilaya  ya Muheza.

 

179.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 Mpango  wa Taifa wa Kudhibiti Matende na Mabusha unatarajia kuwafikia walengwa 2,800,000 katika  Manispaa tatu za mkoa wa Dar-es-Salaam. 

 

Huduma za Afya Wilayani (District Health Services)

 

180.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/06 tutakamilisha uzinduzi wa Bodi za Afya katika Halmashauri 52 zilizobaki kati ya 113 mara Hati Rasmi (instrument) za Bodi hizo zitakapotangazwa kwenye Gazeti la Serikali. Kwa kuwa uanzishwaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii unatanguliwa  na uzinduzi wa Bodi za Afya za Halmashauri, mwaka 2005/06 tutazisaidia Halmashauri za Wilaya 41 zilizobakia nazo zizindue Mfuko huu.  Halmashauri mpya za Wilaya  zitakazoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu zitahamasishwa ili ziunde Bodi na kuanzisha Mfuko wa Afya ya Jamii.

 

181.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/06 Wizara itaendelea kutoa usimamizi wa kitaalamu kwa Halmashauri juu ya uendeshaji wa huduma za afya katika ngazi ya wilaya ili kuboresha huduma. Pia itapeleka gari mpya 15 kwenye Halmashauri kwa ajili ya kazi ya ufuatiliaji na usambazaji wa dawa na vifaa muhimu vya afya.

 

182.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itatoa mafunzo ya kuainisha Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA), unavyohusiana na Kitita cha Huduma Muhimu za Afya (National Essential Package of Health Interventions), Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa miaka mitano (Health Sector Strategic Plan) 2003 - 2008 na Mipango Kabambe ya afya ya Halmashauri (Comprehensive Council Health Plans).  Aidha mafunzo yatatolewa kwa Maafisa  Mipango wa Wilaya jinsi ya kutayarisha bajeti na mipango ya Afya ya Halmashauri (comprehensive council health plans) inayozingatia mzigo.

 

 Huduma ya Elimu ya Afya kwa Umma

 

183.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 Wizara yangu itaendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii ishiriki katika kutambua na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya ki-afya yanayoisibu.  Wizara yangu itashirikiana na wadau mbali mbali kuelimisha wananchi mbinu za kubadili tabia na mitindo ya maisha inayohatarisha afya zao. Aidha Wizara yangu itaimarisha uratibu na kupanua wigo wa shughuli za utoaji elimu ya afya kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari vilivyopo katika jamii yetu na kuimarisha matumizi ya sanaa kwa maendeleo, ili kuweza kufikisha ujumbe wa afya kwa wananchi wengi.

 

HUDUMA ZA TIBA

 

184.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2005/06, Wizara ya Afya imetengewa jumla ya shilingi 47,394,729,600 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba kwa matumizi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali teule, hospitali za mikoa, rufaa, maalum na  hospitali ya taifa ya Muhimbili. Wizara pia imetenga shilingi 6,000,000,000/= zitakazotumika kulipa sehemu ya deni la MSD.

 

185.   Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya kupitia Bohari ya Madawa (MSD), itasambaza dawa na vifaa katika zahanati 3,706 na vituo vya afya 410. Kati ya hivyo, zahanati 175 na vituo vya afya 25 vitakuwa vipya vilivyojengwa na Halmashauri na nguvu za wananchi na kuthibitika kuwa vina ubora unaofaa. Aidha, katika kuboresha usambazaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, Wizara ya Afya itaendesha majaribio ya mfumo wa ‘Integrated Logistics System’ katika mikoa ya Dodoma na Iringa. Mfumo huu utawezesha zahanati, vituo vya afya na hospitali kuagiza dawa na vifaa vya kawaida, na vya miradi ya misaada kwa mfumo mmoja. Mfumo  utaiwezesha Wizara ya Afya kukusanya takwimu za mahitaji na matumizi halisi ya dawa, vifaa na vifaa tiba.

 

186.   Mheshimiwa Spika, Wizara itaingia mkataba wa miaka mitano (5) na kampuni ya Philips Medical Systems katika kuhakikisha kuwa, mashine za eksirei, Ultrasound na vifaa vingine chini ya mradi wa kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa nchini zinadumu kwa miaka mingi ili ziendelee kutoa huduma kwa wananchi.  Katika mkataba huo mafunzo maalum hasa yale ya mashine zenye teknolojia ya hali ya juu yatatolewa kwa watumiaji, Wahandisi na mafundi waliopo katika karakana za kanda.  Wizara pia itaendelea kutoa utaaalam wa matengenezo ya mara kwa mara ya vifaa tiba kupitia karakana za kanda kwa maeneo yote yanayotoa huduma ya afya kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa. 

 

187.   Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuimarisha huduma za maabara kwa kuagiza mashine nyingine, na vifaa vya maabara kwa ajili ya kufuatilia wagonjwa wanaopatiwa dawa za kusaidia kupunguza makali ya UKIMWI.  Wizara itakamilisha ujenzi wa kituo cha Kanda ya Mashariki  cha damu salama pamoja na kuanza mipango ya ujenzi wa Kanda za Kusini (Mtwara) na Kati (Dodoma).  Wakati huo huo Kanda za Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini zitaendelea na kazi ya kukusanya damu salama, kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania. Aidha, maabara 13 za mikoa na 8 za Wilaya zitaboreshwa kwa kufanyiwa ukarabati ili kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma bora.

 

Huduma za kuzuia Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto

 

188.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/06 Wizara imepanga kupanua huduma za kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) katika hospitali zote za Wilaya zilizokuwa bado hazijaanza kutoa huduma hiyo na kufanya Hospitali zote za  Wilaya  kuwa na huduma hii.  Vile vile Wizara itaendelea kuimarisha huduma ya PMTCT – Plus.  Kwa lengo la kuhakikisha akina mama wajawazito walioathirika na Virusi vya UKIMWI – VVU na wenye vigezo vya kupata “ART” wanapata huduma hiyo na wale ambao hawana vigezo wakishajifungua waendelee kufuatiliwa. 

 

 

 

Huduma za Hospitali za Mashirika ya kujitolea, Makampuni na Watu Binafsi

 

189.   Mheshimiwa Spika, ili kupeleka madaraka zaidi kwa wananchi, Halmashauri zimepewa mamlaka ya kuingia  makubaliano ya kutoa huduma za afya (Service Agreement)   na Hospitali za Mashirika badala ya mfumo wa zamani ambapo mikataba ya huduma ilikuwa kati ya hospitali hizo na Wizara ya Afya.  Halmashauri  zitaingia mkataba na hospitali hizo baada ya kupata ridhaa ya Wizara ya Afya.  Wizara pia itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na ile ya umma katika utoaji wa huduma za afya.  Aidha, kwa kuthamini mchango unaotolewa na Mashirika ya Dini katika kuboresha huduma za afya,  Serikali imeongeza ruzuku ya kitanda kutoka shilingi 30,000 mwaka 2004/05 hadi shilingi 50,000 kwa mwaka 2005/06.

 

Huduma za Afya ya Kinywa

 

190.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 itaanza awamu ya pili ya ufungaji vifaa vifuatavyo vya meno katika kliniki za meno za Hospitali za Wilaya, Mkoa, rufaa na za mashirika.  Vifaa hivyo ni:- viti (dental chairs), taa maalum (operating lights) na viti vya kukalia. Hospitali zitakazopatiwa vifaa hivyo ni; Muheza, Korogwe, Chunya, Ileje, Mbeya Vijijini, Mbarali, Rungwe, Kyela, Karatu, Ngorongoro, Simanjiro, Iramba, Morogoro Vijijini, Mbozi, Hanang, Sikonge, Mpanda, Musoma, Kilombero, Mvomero, Bariadi, Bukombe, Kishapu, Liwale, Njombe, Ludewa, Karagwe, Sengerema, Geita, Ukerewe, Misungwi, Newala, Mwanga, Kwimba, Tarime, Bunda, Biharamulo, Mbinga, Morogoro, Dodoma na Tabora.  Pia hospitali nyingine zitakazopatiwa vifaa hivyo ni; Kibosho, Mbeya Rufaa, Mawenzi, Mount Meru, Bombo, Iringa, Mbeya Mkoa, Mirembe, Kilema, Bugando, Dareda, Ligula, Maweni, Singida na Bukoba.

 

Huduma za Afya ya Akili na Madawa ya Kulevya

 

191.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 shughuli za kueneza stadi za kutoa huduma za magonjwa ya akili katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara na Shinyanga zitaendelea. Pia vijitabu vya mwongozo wa utambuzi na matibabu ya  magonjwa ya akili ngazi ya msingi vitasambazwa mikoa yote.

 

 

 

 

 

Hospitali za Rufaa

 

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili

 

192.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/06 huduma za tiba kwa wananchi zitaimarishwa ikiwa ni pamoja na waathirika wa UKIMWI. Jengo jipya la kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje lenye vyumba 35 litaanza kutumika na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano na pia litawezesha kuchujwa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma maalum za rufaa.  Wagonjwa wote watalazimika kupitia katika jengo hili kwanza kabla ya kupata huduma za afya.

 

Hospitali ya Bugando

 

193.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/06 hospitali ya Bugando itaendelea na ukarabati wa wodi za wagonjwa, kuimarisha utoaji huduma na kuendelea kutafuta Madaktari Bingwa na wa kawaida,  ili kutosheleza mahitaji ya hospitali.

 

Hospitali ya KCMC

 

194.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006, hospitali ya KCMC inatarajia kuwapeleka madaktari wa upasuaji, nusu kaputi na wauguzi kwenye mafunzo ya muda mfupi ili kupata taaluma zaidi ya upasuaji wa moyo. Aidha, hospitali hiyo kwa kushirikiana na mashirika ya nje na hapa nchini, itaendelea kuimarisha utafiti wa magonjwa ya malaria na UKIMWI. 

 

195.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/06, hospitali itaimarisha huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya kwa kuteua mratibu ambaye ataratibu shughuli zote za mfuko. Aidha, itapanua huduma kwa wagonjwa wa UKIMWI kufuatia kukamilika kwa majengo ya wagonjwa wa nje.

 

196.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/06, hospitali ya KCMC itatoa nafasi ya masomo kwa madaktari katika Chuo Kikuu cha Tumaini (KCMC)  ili kuongeza idadi ya madaktari bingwa katika fani mbali mbali. Aidha, Chuo hiki  kitaongeza    nafasi za masomo ya udaktari ili kuongeza idadi yao hapa nchini. 

 

 

 

 

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Muhimbili Orthopaedic Institute (MOI)

 

197.   Mheshimiwa Spika, baada ya ununuzi wa vifaa    muhimu, katika kipindi cha 2005/06 Taasisi itapanua huduma za upasuaji katika fani ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu ambazo awali zilikuwa hazipatikani nchini.

 

198.   Mheshimiwa Spika,  Taasisi ya MOI, itaendelea kutoa tiba ya mazoezi ya viungo kwa wagonjwa wa nje na wa ndani, huduma ya viungo bandia, huduma kwa wagonjwa mahututi, huduma za maabara na mionzi (X-ray).  

 

 

Hospitali ya Rufaa Mbeya

 

199.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 hospitali ya Rufaa Mbeya itaendelea kutoa huduma kwa ajili ya wagonjwa wa nje na ndani wanaopata rufaa kutoka mikoa yote ya Kanda za Nyanda ya Juu Kusini.  Aidha hospitali itaendelea na utafiti wa chanjo   ya ugonjwa wa UKIMWI (Vaccine Trial Centre) kwa msaada wa Serikali ya Ujerumani.  Hospitali itaendelea kuboresha sehemu ya kuhifadhi kumbukumbu za wagonjwa na kuanza kutumia huduma kutoka sekta binafsi katika maeneo ya ulinzi, usafi wa nje na ufuaji nguo.

 

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road

 

200.   Mheshimiwa Spika, mwaka 2005/2006 Taasisi itaendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wa saratani wa ndani na nje.   Aidha, Taasisi itafunga mashine mpya 2 za mionzi. Mashine hizo 2 zikifungwa zitafanya Taasisi kuwa na mashine 5 na hivyo kutoa uwezo zaidi wa kumudu kuhudumia ongezeko la asilimia 10 ya wagonjwa.  Taasisi  kwa kushirikiana na shirika la Mionzi Duniani (International Atomic Energy Agency – IAEA) litakamilisha maandalizi ya uanzishaji wa mafunzo ya  kufundishia mafundi wa kuendesha mashine za mionzi yaani “Radiotherapy Technologists”

 

Hospitali ya Mirembe na Taasisi ya Isanga

 

201.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 hospitali ya Mirembe itaendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili wa ndani na nje.  Kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti madawa ya kulevya, itaendelea kutoa huduma kwa waathirika wa pombe na madawa ya kulevya.  Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Taasisi ya Isanga itaendelea kutoa huduma kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai yaliyotendeka kutokana na matatizo ya afya ya akili.

 

Hospitali ya Kibong’oto

 

202.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 hospitali itaendelea kutoa huduma za tiba kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu na wagonjwa wengine.  Aidha, hospitali itaendelea na uchunguzi wa vimelea sugu vya kifua kikuu.

 

HUDUMA ZA UTAWALA NA UTUMISHI

 

203.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2005/2006 Wizara ya Afya itaendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha na kuboresha uwezo wa utendaji kazi kwa watumishi wake ili kuimarisha na kuongeza tija.  Aidha, Wizara itaendelea kuajiri watumishi wapya kwa mujibu wa ikama iliyoidhinishwa.  Wizara pia itawapandisha vyeo watumishi  waliopo kwa kuzingatia sifa, vigezo na ikama.  Ili kwenda sambamba na mabadiliko yanayoendelea kufanyika katika Sekta ya Afya, Wizara imejiwekea mpango wa kutoa mafunzo ya Huduma kwa Mteja kwa watumishi wake wote (Client Service Charter). Mafunzo haya yatawahusisha watumishi wapatao 3,336 kutoka Makao Makuu ya Wizara, Hospitali za Rufaa maalum, na Vyuo vya Afya 110. 

 

HUDUMA YA MAFUNZO

 

204.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imedhamiria kuboresha na kupanua huduma ya mafunzo ili kuongeza idadi ya watoa huduma za afya nchini.   Hivyo chuo kipya cha madaktari wasaidizi (Assistant Medical Officers) kitaanzishwa huko Ifakara.  Chuo hiki awali kilikuwa kinatoa mafunzo ya Maafisa Tabibu. Aidha, Mapitio ya mitaala ya vyuo vya Sayansi ya Afya na Uuguzi yatafanyika ili kuboresha mafunzo yanayotolewa vyuoni. Mafunzo ya Matibabu ya Watoto kwa uwiano (Integrated Management of Chilhood Illness – IMCI) kwa waalimu 40 wa vyuo vya Mafunzo yatatolewa.

 

205.   Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya kujiendeleza ili kutoa huduma bora. Mafunzo yatatolewa kwa timu 12 za mikoa ikiwa ni watumishi 96 watakaopatiwa mafunzo hayo. Lengo ni kuzipatia timu za afya za mikoa uwezo wa kusimamia na kuziekeleza timu za Wilaya ili zitoe huduma sahihi. Aidha wahitimu 136 wa ngazi ya Shahada wakiwemo Madaktari, Madaktari wa meno, Wauguzi na Wafamasia watapatiwa mafunzo ya kuwaandaa kuanza kazi katika vituo vya kazi watakavyopangiwa yaani “Induction Course”. Jumla ya Waganga Wasaidizi Vijijini 21 wanatarajia kuhitimu mafunzo ya Maafisa Tabibu kupitia mafunzo kwa njia ya Posta na 253 wanatarajia kuhitimu katika vyuo vya mafunzo.  Aidha, Waganga Wasaidizi vijijini 190 wako katika hatua mbalimbali za masomo kwa njia ya posta.

 

 

OFISI YA MGANGA MKUU KIONGOZI

 

Huduma za Kupambana na Maafa

 

206.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2005/06, Wizara inakusudia kufanya kazi zifuatazo:

 

·        Usimamizi wa huduma za dharura na maafa katika mikoa 9 kila mkoa wilaya 2, kwa lengo la kutathmini utoaji wa huduma za afya na kutoa ushauri wa kitaalam na maelekezo ili kuboresha huduma.

 

·        Kutoa mafunzo ya namna ya kukabiliana na dharura na maafa kwa wajumbe 40 wa Timu za Uendeshaji wa Huduma za Afya za Mikoa na mafunzo maalum kwa watumishi 36 wa hospitali za Mikoa na Rufaa. Mafunzo haya yatawawezesha watumishi kuongeza ufanisi katika kusimamia utendaji wa kazi wakati itokeapo dharura kwenye hospitali zao.

 

Ukaguzi wa Huduma za Afya

 

207.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu katika mwaka 2005/2006 itaendelea kufanya ukaguzi kwa ajili ya kuhakikisha ubora wa huduma za afya zinazotolewa kwa ngazi zote.

 

Huduma za Uuguzi

 

208.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2005/06 Wizara itasambaza nakala 8,000 za  mwongozo wa jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa walioathirika  na UKIMWI katika Halmashauri zote nchini. Wizara itafanya  ufuatiliaji na usimamizi wa huduma za uuguzi na ukunga katika mikoa ya Mwanza, Pwani, Kilimanjaro, Kigoma, Kagera, Dodoma, Arusha,  na Rukwa.  Aidha,  Wizara yangu itaandaa  Mpango Mkakati  wa utoaji huduma za uuguzi na ukunga wa miaka mitatu.

 

 

 

Mabaraza ya Kitaaluma

 

209.   Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa mabaraza ya kitaaluma, katika kusimamia maadili, Wizara yangu kwa mwaka 2005/2006 itatekeleza yafuatayo: -

 

·        Kutayarisha na kukamilisha mwongozo wa Maadili na Kanuni kwa taaluma za Madaktari na Madaktari wa Meno, Wafamasia, Mafundi Sanifu wa Maabara, Wataalam wa Macho na Wauguzi/Wakunga.

 

·        Kuandaa Mpango Mkakati (strategic plan) kwa mabaraza ya Famasia, Fundi Sanifu wa Maabara na Wauguzi/Wakunga.

 

 

WAKALA  ZILIZO CHINI YA WIZARA YA AFYA

 

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)

 

210.   Mheshimiwa Spika, mwaka 2005/06 Mamlaka ya Chakula na Dawa inatarajia kutekeleza yafuatayo:-

 

·        Kusimamia ubora na usalama wa vyakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na kuimarisha mfumo wa usajili.  Aidha, ukaguzi wa maduka, viwanda vya nje na ndani na vituo vya mipakani utaendelea. 

 

·        Kuimarisha maabara kuu na ndogo zinazohamishika zilizoko katika vituo vya mipakani na mikoani ili ziwe na uwezo wa kupima vipimo mbali mbali kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika. 

 

·        Kuandaa miongozo na kanuni ili kuwezesha utekelezaji  bora wa Sheria.

 

·        Kutoa mafunzo kwa watumishi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

 

·        Kutoa elimu kwa wadau na wananchi kwa njia za  vyombo vya habari na tovuti.       

 

·        Kufungua Ofisi ya Kanda  Mbeya ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

 

 

 

Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali

 

211.   Mheshimiwa Spika, mwaka 2005/2006 Wizara yangu itaendelea kuimarisha uwezo wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili utoe huduma za uchunguzi wa kimaabara kwa ufanisi zaidi.  Wizara itanunua kemikali na vitendea kazi. Wizara itatoa mafunzo kwa wataalamu 19 wa Wakala katika nyanja mbalimbali zitakazosaidia kuimarisha utoaji huduma.

 

212.   Mheshimiwa Spika, ili kusogeza huduma za Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali karibu na wananchi, Wizara itakamilisha  taratibu za kupata eneo kwa ajili  ya ujenzi wa Maabara  ya Kanda ya Kaskazini.

 

213.   Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza usimamizi wa sheria ya Kemikali za Majumbani na Viwandani, Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali utaendelea kuimarisha na kusimamia usajili, ukaguzi na utoaji wa habari kuhusu kemikali mbalimbali.  Kutayarisha miongozo mbalimbali ya utekelezaji wa sheria na kutangaza kazi zake kwa njia ya vyombo vya habari na vipeperushi ili kuelimisha umma juu ya sheria yenyewe, madhara na faida zinazoletwa na kemikali.

 

 

USHIRIKIANO WA NDANI NA NJE YA NCHI

 

214.   Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu na nchi rafiki na mashirika ya kimataifa yanayosaidia sekta ya afya. Wizara ya Afya, pia imepata ushirikiano mzuri kutoka sekta nyingine ambazo zinasaidia kuboresha huduma za afya.

 

215.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuadhimisha siku mbali mbali za Afya zinazodhimishwa  Kitaifa na Kimataifa.  Naomba kuchukua nafasi hii kuwashukuru viongozi mbalimbali wa kitaifa, mikoa, wilaya na wananchi wote kwa ujumla kwa kufanikisha maadhimisho ya siku hizo.

 

216.   Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kipekee kuzishukuru nchi za Denmark, Uswisi, Uholanzi, na Ujerumani na mashirika ya Benki ya Dunia, UNFPA, Development Cooperation of Ireland (DCI) kwa kutoa misaada yao katika Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Afya (Basket Fund) ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya. Pia napenda kuzishukuru nchi nyingine za China, Cuba, Canada, Hispania, India, Ireland, Italia, Japan, Korea Kusini, Marekani, Misri, Sweden, Ufaransa, Norway na Uingereza,ambazo zimeendelea kuisaidia sekta ya Afya kwa njia mbali mbali.

 

217.   Mheshimiwa Spika, Mashirika ya Kimataifa pia yanastahili shukrani kwa ushirikiano wao mzuri na Wizara yangu.  Naomba kuchukua tena nafasi hii kutoa shukrani kwa Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU), Shirika la Umoja wa Kimataifa la Maendeleo (UNDP), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Uzazi wa Mpango (UNFPA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti UKIMWI (UNAIDS), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Benki ya Nchi za Kiarabu kwa ajili ya Maendeleo ya Uchumi ya Nchi za Afrika (BADEA), Umoja wa Nchi zinazotoa Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC), na Madaktari Wasio na Mipaka (Medicine Sans Frontieres – MSF).   Wengine ni CIDA (CANADA), CUAMM, DANIDA, DFID, GTZ, IDRC,  JICA, KFW, MISERIOR, SAREC, SDC, CDC, SIDA (SWEDEN), Engender Health (USA), CORDAID (Netherlands) BASIC NEED (UK) na USAID.  Tunawashukuru pia Wafadhili wa mradi wa kudhibiti magonjwa ya usubi na vikope ambao ni African Programme for Orchorcerciasis Control, International Eye Foundation, Merk, Pfizer, Hellen Keller Foundation na International Trachoma Initiative.  Taasisi nyingine za Kimataifa ni Axios International, US President’s Initiative, Bill Clinton Foundation, Bill and Melinda Gates Foundation, Abbot Laboratories, London School of Hygiene and Tropical Medicine, John Hopkins University, Global Fund for HIV/AIDS, TB and Malaria, University of Columbia, CMB, Germany Leprosy Relief Association, Gabriel Project ya Marekani, Citi Bank, General Electric (GE – USA), Havard University na Duke University za Marekani, Community of Saint Egidio (DREAM) na Glasgow Smith Kline (GSK).

 

218.   Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali kuwashukuru watu binafsi, vyama vya hiari, na mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani ya nchi kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia uimarishaji wa huduma za afya.  Mashirika hayo ni pamoja na Aga Khan Foundation, AMREF, Lions Club, Rotary Club International, BAKWATA, CCBRT, Christian Social Services Commission (CCT), ELCT, TEC, Msalaba Mwekundu, Shree Hindu Mandal, Hubert Kairuki Memorial Hospital, Regency Hospital, TPHA, USADEFU, NSSF, PASADA, PSI, Women Dignity Project, Tanzania Diabetic Association, MEHATA, TANESA na vyama vyote vya kitaaluma vya Sekta ya afya. Napenda pia kuwapongeza Tanzania Heart Institute kwa hatua waliyofikia katika kuanzisha huduma za upasuaji wa moyo hapa nchini.

 

 

 

MWISHO

 

219.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi chote cha mwaka wa fedha 2004/2005 nimefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na viongozi wenzangu wa Wizara ya Afya.  Nachukua fursa hii ya pekee kuwashukuru wafuatao Mheshimiwa Dr. Hussein Ali Mwinyi (Mb.) Naibu Waziri wa Afya, Ndugu Mariam Joy Mwaffisi, Katibu Mkuu, Dr. Gabriel Upunda, Mganga Mkuu Kiongozi, Wakurugenzi wa Idara zote katika Wizara ya Afya, Wakurugenzi wa Hospitali za Rufaa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Hospitali, Vituo vya Afya, Zahanati na Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo ya Afya na wafanyakazi wote wa sekta ya afya.  Nawaomba waendelee kufanya kazi kwa nguvu zote na kwa moyo wa kujitolea kwa manufaa ya wananchi na taifa letu kwa ujumla.

 

220.   Mheshimiwa Spika, sitaweza kumaliza hotuba yangu bila kuwashukuru wafuatao, mume wangu Mheshimiwa Pius Msekwa na watoto wetu, pamoja na wananchi wa Jimbo la Lulindi ambao mimi ninawawakilisha katika Bunge hili tukufu.  Nawashukuru sana kwa uvumilivu wao. Mara nyingi sipo pamoja nao kwa ajili ya majukumu yangu ya kitaifa.  Wamenisaidia na wamenipa imani na ushirikiano mkubwa.  Kwa wananchi wa Jimbo la Lulindi, nawashukuru kwa heshima mliyonipa kwa kunichagua mara mbili niwe Mbunge wenu. Kwa kuwa sitagombea tena Ubunge wa Jimbo katika uchaguzi ujao, naahidi kushirikiana na Mbunge ajaye na wananchi wa Lulindi kwa ujumla katika kulijenga jimbo letu na Wilaya yetu.

 

 

MAOMBI YA FEDHA MWAKA 2005/06

 

221.   Mheshimiwa Spika, ili kuiwezesha Wizara ya Afya kutekeleza kazi zilizopangwa mwaka 2005/06 naliomba Bunge lako tukufu litafakari, lijadili, na kuidhinisha makadirio ya Wizara ya Afya  na Asasi zake yenye jumla ya Shilingi 271,168,602,300 kati ya fedha hiyo, Shilingi 180,305,853,900 ni kwa ajili ya mishahara na matumizi ya kawaida, shilingi 90,862,748,400 ni kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.  Kati ya fedha za maendeleo shilingi 5,000,000,000 ni fedha ya ndani na shilingi 85,862,748,400 ni fedha ya nje.

 

222.   Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. 

         


 

VIAMBATANISHO

Kiambatanisho Na.1

 

KIREFU CHA MAJINA YA MASHIRIKA YA KITAIFA NA KIMATAIFA YANAYOSAIDIA HUDUMA ZA AFYA

 

ADB            -        African Development Bank       

AMREF      -        African Medical and Research Foundation

BADEA       -        Bangue Arabe pour Development Economique en                                          Afrique

BAKWATA -        Baraza Kuu la Waislamu Tanzania      

CBM           -        Christoffel Brinden Mission

CCBRT       -        Comprehensive Community Based Rehabilitation in     Tanzania     

CCT            -        Christian Council of Tanzania

CDC           -        Centre for Disease Control and Prevention Atlanta                                         Georgia

CIDA          -        Canadian International Development Agency

CSSC                   -        Christian Social Services Commission

CUAMM     -        International College for Health Cooperation in                                              Developing Countries

DANIDA     -        Danish International Development Agency

DFID           -        UK Department for International Development

DSE            -        Deusche stiftung fur Internationale Entwicklung

ELCT                   -        Evangelical Lutheran Church of Tanzania

EU              -        European Union

FINNIDA    -        Finnish International Development Agency

GSF            -        Good Samaritan Foundation     

GTZ            -        Gesellschaft fuer Technische Zusammenarbeit

IDRC          -        International Development Research Centre of Canada

IMA            -        International Missionary Association

JICA           -        Japan International Cooperation Agency

MDP           -        Mectizan Donation Programme

MSF           -        Medicine Sans Frontiers

NBC            -        National Bank of Commerce

NIMR          -        National Institute for Medical Research

NORAD      -        Norwegian Agency for Development

NSSF          -        National Social Security Fund

OPEC                   -        Organisation of Petroleum-Producing Countries

SADC         -        Southern Africa Development Cooperation

SAREC       -        Swedish Agency for Research Cooperation in                                               Development Countries

SDC            -        Swiss Agency for Development and Cooperation

SIDA           -        Swedish International Development Authority

TAC-AIDS  -        Tanzania Commission for AIDS

TAMWA     -        Tanzania Media Women Association

TANESA     -        Tanzania Netherlands Support to AIDS Control

TANESCO  -        Tanzania Electric Supply Company

TBL            -        Tanzania Breweries Limited

TEC            -        Tanzania Episcopal Conference

TPDC                   -        Tanzania Petroleum Development Corporation

TRA            -        Tanzania Revenue Authority

TTCL                   -        Tanzania Telecommunication Company Limited

UNDP         -        United Nations Development Programme

UNFPA       -        United Nations Fund for Population Activities

UNHCR      -        United Nations High Commission for Refugees

UNICEF      -        United Nations Children Fund

USADEFU  -        Usambara Development Fund

USAID        -        United States Agency for International Development

WHO          -        World Health Organisation

PSI              -        Population Service International

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kiambatanisho Na.2

 

VIREFU VYA VIFUPISHO VILIVYOTUMIKA NDANI:

 

ADB            -        African Development Bank

ARV           -        Anti Retro Viral

BOD           -        Burden of Diseases

CDC           -        Centre for Disease Control

CHF            -        Community Health Fund

DNA           -        Deoxyribo NucleicAcid

DPT-HB      -        Diptheria, Pertussis Tetanus, Hepatitis B

GAVI          -        Global Alliance for Vaccine and Immunisation

HIV             -        Human Immuno Deficiency Virus

ICU             -        Intensive Care Unit

ILO             -        International Labour Organisation

IMCI           -        Integrated Management of Childhood Illness

KCMC        -        Kilimanjaro Christian Medical Centre

MOI            -        Muhimbili Orthopaedic Institute

MTUHA      -        Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji Huduma za Afya

MUCHS      -        Muhimbili University College of Health Sciences

NHIF           -        National Health Insurance Fund

NIMR          -        National Institute for Medical Research

ORCI          -        Ocean Road Cancer Institute

ORET         -        Overseas Related External Trade

PMTCT      -        Prevention of Mother To Child HIV Transmission

SP               -        Sulphadioxine Pyrimithmine

STI             -        Sexual Transmitted Infections 

TAMISEMI -        Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

TIKA          -        Tiba kwa Kadi

TPRI           -        Tanzania Pesticides Research Institute

TT              -        Tetanus Toxoid

TV              -        Television

UKIMWI     -        Upungufu wa Kinga Mwilini

 

 

 

 

 

 

 

Kiambatanisho Na.3

 

ORODHA YA HALMASHAURI 61 ZILIZOKWISHAZINDUA BODI ZA HUDUMA ZA AFYA

 

                                                                  


1.                 Wilaya ya Hai

2.                 Manispaa ya Tanga

3.                 Wilaya ya Shinyanga

4.                 Mji wa Singida

5.                 Wilaya ya Mbulu

6.                 Wilaya ya Mpwapwa

7.                 Manispaa ya Kinondoni

8.                 Wilaya ya Mufindi

9.                 Wilaya ya Monduli

10.             Wilaya ya Kiteto

11.             Wilaya ya Hanang

12.             Wilaya ya Lushoto

13.             Wilaya ya Kigoma

14.             Manispaa ya Temeke

15.             Manispaa ya Arusha

16.             Manispaa ya Tabora

17.             Mji wa Songea

18.             Wilaya ya Ngara

19.             Wilaya ya Igunga

20.             Wilaya ya Mwanga

21.             Wilaya ya Ulanga

22.             Wilaya ya Masasi

23.             Wilaya ya Sumbawanga

24.             Wilaya ya Babati

25.             Wilaya ya Geita

26.             Wilaya ya Sengerema

27.             Wilaya ya Iringa

28.             Manispaa ya Iringa

29.             Wilaya ya Njombe

30.             Wilaya ya Makete

31.             Wilaya ya Handeni

32.             Wilaya ya Arumeru

33.             Wilaya ya Mbozi

34.             Wilaya ya Rombo

35.             Wilaya ya Kasulu

36.             Manispaa ya Moshi

37.             Manispaa ya Mbeya

38.             Wilaya ya Newala

39.             Wilaya ya Mtwara

40.             Wilaya ya Kilwa

41.             Wilaya ya Lindi

42.             Wilaya ya Liwale

43.             Manispaa ya Morogoro

44.             Jiji la Mwanza

45.             Wilaya ya Kondoa

46.             Wilaya ya Singida

47.             Wilaya ya Morogoro

48.             Wilaya ya Serengeti

49.             Wilaya ya Muheza

50.             Wilaya ya Biharamulo

51.             Wilaya ya Karagwe

52.             Wilaya ya Bukoba

53.             Mji wa Bukoba

54.             Wilaya ya Ngara

55.             Wilaya ya Muleba

56.             Wilaya ya Kibondo

57.             Wilaya ya Magu

58.             Mji wa Musoma

59.             Wilaya ya Bunda

60.             Manispaa ya Shinyanga

61.             Wilaya ya Korogwe.


 

 


Kiambatanisho Na.4

 

ORODHA YA HALMASHAURI 51 AMBAZO ZIMEANZISHA MFUKO WA AFYA YA JAMII

 

 

  1. Nzega                                                              42.  Lindi Mjini
  2. Igunga                                                              43.  Bukombe
  3. Singida                                                 44.  Meatu
  4. Iramba                                                             45.  Bariadi
  5. Kilosa                                                              46.  Muheza
  6. Hanang                                                 47. Kisarawe
  7. Iringa Vijijini                                                     48.  Pangani
  8. Songea Vijijini                                      49.  Same
  9. Mbinga                                                             50.  Serengeti
  10. Kigoma                                                            51. …………….
  11. Ulanga
  12. Mufindi
  13. Masasi
  14. Mwanga
  15. Sumbawanga Vijijini
  16. Urambo
  17. Mbulu
  18. Kilwa
  19. Songea Mjini
  20. Mpwapwa
  21. Kondoa
  22. Karatu
  23. Kiteto
  24. Simanjiro
  25. Babati
  26. Monduli
  27. Kasulu
  28. Sikonge
  29. Uyui
  30. Manyoni
  31. Geita
  32. Sengerema
  33. Hai
  34. Newala
  35. Liwale
  36. Arumeru
  37. Kibondo
  38. Bunda
  39. Handeni
  40. Njombe
  41. Rombo

Kiambatanisho Na.5

 

MIKOA 17 ILIYOBADILISHIWA MAJOKOFU YA MAFUTA YA TAA KWA MAJOKOFU MAPYA YA KUTUMIA GESI

 

1.     Tanga                                       11.  Arusha                              

2.     Pwani                                       12.  Manyara

3.     Dodoma                                   13.  Mwanza

4.     Morogoro                                14.  Mara

5.     Lindi                                        15.  Kagera

6.     Mtwara                                     16.  Shinyanga

7.     Iringa                                        17.  Tabora

8.     Mbeya

9.     Ruvuma

10. Singida

 

 

 


Kiambatanisho Na.6

 

 

HALMASHAURI 15  ZILIZOWEKEANA MKATABA NA WIZARA NA KUPEWA FEDHA ZA TELE KWA TELE KUANZIA  MWAKA 2000 - 2005

 

 

JINA LA HALMASHAURI

KIASI KILICHOKWISHALIPWA (TSHS.)

  1.  

Singida Vijijini

46,747,500.00

  1.  

Iringa Vijijini

66,665,000.00

  1.  

Kilosa

14,055,000.00

  1.  

Igunga

87,630,000.00

  1.  

Hanang

28,640,000.00

  1.  

Karatu

11,130,000.00

  1.  

Iramba

20,677,262.60

  1.  

Nzega

16,190,000.00

  1.  

Sumbawanga

19,255,000.00

  1.  

Masasi

80,000,000.00

  1.  

Mufindi

7,910,000.00

  1.  

Kigoma Vijijini

13,390,000.00

  1.  

Songea Mjini

56,772,000.00

  1.  

Mbulu

16,782,000.00

  1.  

Mwanga

16,205,000.00

 

JUMLA

502,048,762.60

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kiambatanisho Na.7

 

Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Vikope (Trachoma)

 

A. Wilaya 30 zilizokwisha fanyiwa utafiti wa awali wa kujua kiwango cha ugonjwa wa vikope mwaka 2004:

1. Tunduru            9.  Monduli            17.Kiteto                         24. Lindi vijijini

2. Iramba               10. Igunga             18.Singida vijijini             25. Simanjiro

3. Dodoma vijijini   11. Masasi             19.Nachingwea                26. Handeni

4. Kondoa             12. Manyoni          20.Kilosa                        27. Meatu

5. Ruangwa           13. Mpwapwa        21.Sikonge                      28. Kongwa

6. Mkuranga          14.Rufiji                22.Magu                         29. Shinyanga

7. Kishapu             15.Nzega               23.Rombo                      30.Singida mjini

8. Hai                    16. Iringa vijijini

 

B. Wilaya 26 zilizogundulika kuwa na ugonjwa wa vikope kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 10

 

1. Monduli             8. Tunduru            15. Kiteto                        21. Lindi vijijini

2. Iramba               9. Igunga               16. Singida vijijini            22. Simanjiro

3. Dodoma vijijini   10. Masasi             17. Nachingwea               23. Handeni

4. Kondoa             11. Manyoni          18. Kilosa                       24. Meatu

5. Ruangwa           12. Mpwapwa        19. Sikonge                     25. Kongwa

6. Mkuranga          13. Rufiji               20.Magu                         26.Shinyanga

7. Kishapu             14. Nzega

 

C. Wilaya 4 zilizogundulika kuwa na ugonjwa wa vikope kwa kiwango cha

     chini ya asilimia 10

 

1. Rombo              2. Singida mjini      3. Hai                              4. Iringa vijijini

 

D. Wilaya 10 ambazo zitafanyiwa utafiti wa awali wa kujua kiwango cha

     ugonjwa wa vikope mwaka huu 2005.

 

1. Songea vijijini     4. Karagwe            7. Newala              9. Mtwara Vijijini

2. Liwale               5. Bagamoyo         8.Kilwa                  10.Mbarali

3. Kilindi               6. Tandahimba

 

 

 

Kiambatanisho Na.8

 

Halmashauri 32 Zilizopata Mafunzo Ili ziweze kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini huduma za Elimu ya Afya Kwa Umma kwa Kamati za Uendeshaji

 

Morogoro

1. Kilosa                         3. Kilombero                   5. Morogoro Vijijini

2. Ulanga                        4. Morogoro Manispaa    6. Mvomero.

 

Kilimanjaro

7. Same                          9. Rombo                       11. Mwanga

8. Moshi Manispaa          10. Moshi Vijijini             12. Hai

 

Mbeya

13. Kyela                        16. Mbarali                      18. Mbeya Vijijini

14. Ileje                           17.Rungwe                      19. Mbozi

15. Mbeya Manispaa

 

Iringa

20. Iringa Manispaa         22. Mufindi                     24. Ludewa

21. Njombe                     23. Iringa Vijijini              25. Makete

 

Arusha

26. Arumeru                    27. Arusha Manispaa       28. Monduli

 

Dodoma

29. Dodoma Manispaa     30.Dodoma Vijijini 31. Kongwa

 

Manyara

32. Babati

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kiambatanisho Na.9

 

HALMASHAURI ZA WILAYA, MIJI, MANISPAA NA JIJI

ZILIZOSHIRIKI KATIKA MASHINDANO YA AFYA

NA USAFI WA MAZINGIRA 2005

 

HALMASHAURI ZA WILAYA (VIGEZO VILIKUWA NA ALAMA 157)

 

                                                ALAMA                     ASILIMIA

 

1. ARUMERU                         137                              87.2%

2. LUSHOTO                                      134                              85.4%

3. NJOMBE                                        132                              84.0%

4. MBINGA                                        129                              82.1%

5. KAHAMA                                       120                              76.4%

6. MOSHI VIJIJINI                             117                              74.5%

7. MPANDA                                       115                              73.8%

8. MPWAPWA                                   114                              72.6%

9. KYELA                                           112                              71.3%

10. NZEGA                                         109                              69.4%

11. GEITA                                           107                              68.1%

12. MANYONI                                   102                              64.2%

13. HANANG                                     96                                61.1%

14. NGARA                                        92                                58.5%

15. KILOSA                                        87                                55.0%

16. RUANGWA                                  82                                52.2%

17. BAGAMOYO                               66                                42.0%

18. KIGOMA VIJIJINI                       50                                31.8%

19. NEWALA                                     46                                29.2%

20. MUSOMA VIJIJINI                      44                                28.0%                                     

 

 

HALMASHAURI ZA MIJI (VIGEZO VILIKUWA NA ALAMA 110)

 

                                                ALAMA                     ASILIMIA

 

1. SONGEA                                        95                                84.6%

2. SINGIDA                                        92                                83.6%

3. SUMBAWANGA                           90                                81.8%

4. BUKOBA                                        83                                75.5%

5. MTWARA                                       69                                62.7%

6. LINDI                                              68                                61.8%

7. KIGOMA                                        61                                55.5%

8. MUSOMA                                      54                                49.1%

9. KIBAHA                                         51                                46.0%

10. BABATI                                        44                                40.0%

 

HALMASHAURI ZA MANISPAA NA JIJI (VIGEZO VYOTE VILIKUWA NA ALAMA 110)

 

                                                            ALAMA                     ASILIMIA

 

1. MOSHI                                           90                                82.0%

2. MWANZA                                      83                                75.0%

3. TANGA                                           80                                73.0%

4. IRINGA                                           78                                71.2%

5. MBEYA                                          77                                70.0%

6. DODOMA                                      76                                69.1%

7. ARUSHA                                        73                                66.4%

8. ILALA                                             72                                65.5%

9. TABORA                                        71                                64.6%

10. KINONDONI                               69                                62.7%

11. TEMEKE                                       68                                62%

12. MOROGORO                               56                                51%

13. SHINYANGA                               45                                41%

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kiambatanisho Na.10

 

Wilaya 48 ambapo Ufuatiliaji wa Afya Kazini katika Maeneo ya Viwanda, Ujenzi na Mashamba Ulifanyika

 

1. Hanang                       15. Kibaha                                27. Kisarawe         

2. Tanga                         16. Muheza                               28. Korogwe        

3. Rombo                       17. Arumeru                             29. Mwanga          

4. Sumbawanga               18. Mbeya Manispaa                 30. Mbarali           

5. Kondoa                       19. Mpwapwa                           31. Kongwa          

6. Morogoro Vijijini         20.Morogoro Manispaa             32. Kilosa   

7. Kilombero

8. Lushoto                      21. Moshi Manispaa                  33.MoshiVijijini     

9. Babati                         22. Monduli                              34.Same               

10. Mufindi                     23. Iringa Vijijini                        35.IringaManispaa 

11. Rungwe                     24. Mbeya Vijijini                      36. Ilala       

12. Kinondoni

13. Temeke                     25. Shinyanga                           37. Kahama 

14. Nzega                        26.Igunga                                 38. Pangani

                                                                                      39. Hai

40.     Arusha

41.     Dodoma

42.     Mvomero

43.     Dodoma

44.     Mbozi

45.     Tukuyu

46.     Tabora

47.     Nzega

48.     Manispaa ya Tabora

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kiambatanisho Na.11

 

HOSPITALI 68 ZILIZOPITISHWA KUWA RAFIKI KWA MAMA NA MTOTO KUANZIA 1992 HADI 2005

 

MKOA

NA.

JINA LA HOSPITALI

Arusha

1.

2.

Babati

Mount Meru

Dar es Salaam

3.

4.

5.

6.

7.

8.

Hindu Mandal

Dr. Khan

Ilala (Amana)

Mwananyamala

Temeke

Muhimbili

Dodoma

9.

10.

11.

Dodoma

Kondoa

Mpwapwa

Iringa

12.

13.

14.

15.

16.

17.

Iringa

Ilembula

Tosamaganga

Mafinga

Makete

Njombe

Kilimanjaro

18.

19.

20.

21.

22.

23.

24.

Huruma

KCMC

Hai

Machame

Mawenzi

Same

Usangi

Mbeya

25.

26

27.

28.

29.

30.

Chimala

Igongwe

Kyela

Mbeya Rufaa

Mbozi Vwawa

Tukuyu

Kagera

31.

32.

33.

34.

35.

Ndolage

Biharamulo

Nyakahanga

Mugana

Rubya

Mwanza

36.

37.

38.

39.

40.

41.

42.

Bugando

Geita

Mugumu

Ngudu

Sekou Toure

Sengerema

Magu

Mara

43.

Bunda

 

44.

45.

Musoma

Tarime

Pwani

46.

47.

48.

Bagamoyo

Kibaha

Kisarawe

Singida

49.

50.

51.

52.

Kilimatinde

Makiungu

Manyoni

Singida

Tanga

53.

54.

55.

56.

57.

58.

Bombo

Handeni

Korogwe

Lushoto

Muheza

Pangani

Ruvuma

59.

60.

61.

62.

Songea

Mbinga

Litembo

Peramiho

Mtwara

63.

64.

Ligula

Ndanda

Shinyanga

65.

66.

67.

Mwadui

Meatu

Shinyanga

Kigoma

68.

Kasulu

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kiambatanisho Na.12

 

ORODHA YA VYUO 32 VILIVYOFANYIWA UKARABATI

S/N

JINA LA CHUO

KAZI / MRADI

1

Tanga AMO

Rehabilitation of administration block and domitories

2

Sumbawanga COTC

Rehabilitation of domitories, 3 staff houses, class rooms, laboratory and office, kitchen and dinning

3

Kiomboi NTC

Finalization of rehabilitation of buildings

4

Newala NTC

Rehabilitation of administration block, domitories and dinning hall

5

Mpwapwa HO

Construction of staff quarters, laboratory and kitchen

6

Same PHN

Rehabilitation of administration block, class rooms and fence

7

Kahama PHN

Extention of 2 staff quarters,recreation room, construction of laundry and library

8

Mtwara PHN

Rehabilitation of domitory, dinning room and kitchen

9

Mbozi NTC

Rehabilitation of school buildings

10

Geita PHN

Construction of toilets, laundry, library,demonstration room, corridor, wardens house and rehabilitation of staff quarters and deep well

11

Tanga NTC

Rehabilitation of school buildings

12

Kagemu HT

Rehabilitation of 5 domitories

13

Maswa COTC

Rehabilitation of administration block, 2 class rooms, laboratory, kitchen and dinning hall and semidetached wardens house

14

Ngudu HT

Construction of library

15

Mkomaindo NTC

Rehabilitation of 2 class rooms, demonstration rooms, 4 offices, dinning hall, 4 domitories, 2 staff houses, library, recreation hall and  kitchen

16

Tukuyu NTC

Rehabilitation of domitory, principals,quarter and finalization of construction of fencing wall

17

Mtwara COTC

Finalization of construction of fencing

18

Musoma COTC

Rehabilitation of drainage, water systems and school buildings

19

Mafinga COTC

Rehabilitation of domitories

21

Njombe PHN

Completion of security fence and rehabilitation of toilets

22

Tarime PHN

Rehabilitation of school buildings

23

Songea COTC

Completion of rehabilitation of domitories

24

Kilosa COTC

Rehabilitation of school buildings

25

Bagamoyo PHN

Rehabilitation of students domitory and construction of shallow wells

26

Kibaha COTC

Rehabilitation of school buildings

27

CEDHA

Constuction of multipurpose bilding ( office, laboratory, theatre rooms)

28

Mirembe NTC

Construction of class rooms, dorminories and staff quarter

29

Tanga HO

Construction of sttudents hostel

30

Vector Control

Rehabilitation of school buildings

31

Kondoa PHN

Construction of library and demonstration room

32

Kigoma COTC

Rehabilitation of class rooms domitories

Kiambatanisho Na.13

 

 

ORODHA YA AINA ZA DAWA ZILIZOLETA MADHARA KWA WATUMIAJI

 

 

1.  SP                           -           16

2.  Contrimoxazole       -             6

3.  Metranidazole          -             1

4.  Amodiaquine           -             2

5.  Seprin                     -             2

6.  Annate                    -             2

7.  6 Norplant Implant  -             1

8.  Ampclox                 -             1

9.  Nevirapine               -             2

10. Thiabendazole        -             1

11. Diclofenac              -             1

12. Quinine                   -             1

13. Amolin                   -             1

14. Tramadol                -             1

15. Depoprovera          -             1

16. Asprin                    -             1

17. Methyldopa            -             1

18. PPF                       -             1

                                                42

 

 

 


 

Kiambatanisho Na.14

 

 

ZAHANATI NA VITUO VYA AFYA VIPYA VITAKAVYOPATA DAWA 2005/06

Mkoa

Halmashauri

Zahanati

Vituo vya Afya

Arusha

Arumeru

 Olkeriani

 

 Ngyani

 

 Terrati

 

 Kipandenkoavele

 

 

 

 

Arusha Manispaa

 

 Themi

 

 

 

Monduli

 Matale

 Engarenaibor

 Lendikinya

 

 Meserani

 

 Ilorionito

 

 Oldonyondoroboni

 

 

 

 

Karatu

 Oldeani

Aya - Labe

 

Gyekrum - Lambo

 

 

 

Ngorongoro

Irkeekpusi

 

Oloipiri

 

Oloirien/Magaiduru

 

Esere

 

 

 

 

DSM

Ilala Manispaa

 Ukonga Ogombolwa

 

 

 

 

Kinondoni Manispaa

Msewe

 

Mlalakuwa

 

Makongo Juu

 

 

 

 

Temeke Manispaa

 

 

 

 

 

Dodoma

Dodoma Manispaa

 Ntuba

 

 Zuzu

 

 Chahwa

 

 Michese

 

 Ntyuka

 

 Gawaye

 

 

 

 

Dodoma Vijijini

 Ndembwe

 

 

 Mpamantwa

 

 

 

 

Mpwapwa

 Chinyanguku

 

 Tambi

 

 Matonya

 

 Chitemo

 

 Nghambi

 

 Ikuyu

 

 Kiboriani

 

 Kimagai

 

 Mtamba

 

 Kidenge

 

 

 

 

 

 

Kondoa

 

 

 

 

 

Kongwa

Ihanda

 

Nghumbi

 

Chiwe

 

Lenjulu

 

Chamkoroma

 

Mbagilwa

 

Pingalane

 

Ndurugumi

 

 

 

 

Iringa

Iringa Manispaa

 

 

 

 

 

Iringa Vijijini+Kilolo

 Masisiswe

 Kimande

 

 Idegenda

 

 Ngongwa

 

 

 

 

Ludewa

 

 

 

 

 

Makete

Ibanga

 

 Ilungu

 

 Ivirikinge

 

 Ukange

 

 Kipagalo

 

 Kinyika

 

 

 

 

Mufindi

 Bumilainga

 Mgololo

 Igombavanu

 Sadani

 Ilogombe

 

 Mninga

 

 Mtambula

 

 Mtula

 

 Mkonge

 

 Ihanzikwa

 

 Kilolo

 

 

 

 

Njombe

 

 Makoka

 

 

 

Kagera

Biharamulo

 

 

 

 

 

Bukoba Mjini

 

 

 

 

 

Bukoba Vijijini

Bulembo

 

Kibirizi

 

Kashenye

 

Buzi

 

Nyakato

 

 

 

 

Karagwe

 

 

 

 

 

Muleba

 

 

 

 

 

Ngara

 

 

 

 

 

 

 

Kigoma

Kasulu

 Nyanchenda

 Janga

 Kanazi

 

 Muhunga

 

 Songambele

 

 Mugera

 

 Kajana

 

 Nyamugali

 

Rusaba

 

 

 

 

 

 

Kibondo

 

 

 

 

 

Kigoma - Ujiji

 

 

 

 

 

Kigoma Vijijini

 

 

 

 

 

Kilimanjaro

Hai

 

 

 

 

 

Moshi Manispaa

 

 

 

 

 

Moshi Vijijini

 Mdawi

 

 Mahoma

 

 Leghomulo

 

 Kindi

 

 Kimangara

 

 Marangu Kiraracha

 

 

 

 

Mwanga

 

 

 

 

 

Rombo

 

 

 

 

 

Same

 Karamba

 

 Bwambo

 

 Mhezi

 

 

 

 

Lindi

Kilwa

 

 

 

 

 

Lindi Mjini

 

 

 

 

 

Lindi Vijijini

 

 

 

 

 

Liwale

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Nachingwea

 Namalongo

 Marando

 

 Kihuwe

 

 

 Nakaloji

 

 

 

 

Ruangwa

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Manyara

Hanang

 Endasaki

 

 Waranga

 

 Genuwasi

 

 Simbai

 

 

 

 

Mbulu

Bargish

 

Gehandu

 

Ngorat

 

Hasama

 

Tsawa

 

Endaharghadat

 

Diyomat

 

 

 

 

Kiteto

 

 

 

 

 

Babati

Minjingu

 Gallapo

 

Dohom

 

 

Qash

 

 

Gendamar

 

 

Arri

 

 

Dabir

 

 

 Mayoka

 

 

 

 

Simanjiro

Kwitai B

 Mererani

Lemukuna

 

Loibor Soit A

 

Nomeuti(Kambi ya Chokaa)

 

Narakau

 

Mara

Bunda

 Kunzugu

 

 Wariku

 

 

 

 

Musoma Mjini

 

 

 

 

 

Musoma Vijijini

 Mirwa

 

 

 

 

Serengeti

 Bwitegi

 Nata

 

 

 

Tarime

 Ochuna

 Sirari