HOTUBA YA WAZIRI WA
USALAMA WA RAIA, MHESHIMIWA H. BAKARI MWAPACHU (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2006/07
HOJA
1. Mheshimiwa
Spika, kutokana na taarifa
iliyowasilishwa Bungeni mapema leo na
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa William
Kusila, Mbunge wa Bahi, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa
likae kama Kamati ya Matumizi ili liweze kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato
na Matumizi ya Wizara ya Usalama wa Raia kwa mwaka wa fedha wa 2006/07.
UTANGULIZI
2. Mheshimiwa
Spika, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa
kwa kura nyingi za kishindo, za asilimia 80.2 katika Uchaguzi Mkuu
uliofanyika mwezi Desemba 2005. Napenda
pia kumpongeza Mheshimiwa Dr. Ali Mohamed Shein aliyekuwa Mgombea
Mwenza, kwa ushindi mkubwa walioupata.
3. Mheshimiwa
Spika, nampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa
Amani Abeid Karume kwa ushindi mkubwa alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2005, ambao katika mazingira ya Zanzibar ni ushindi wa kishindo. Aidha, nampongeza
Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa kwa kuteuliwa kushika
wadhifa huo. Kuteuliwa kwake na kuthibitishwa
kwa kura nyingi na bunge hili ni ishara ya imani kubwa aliyonayo Mheshimiwa
Rais na Waheshimiwa Wabunge juu ya utendaji wake wa kazi.
4.
Mheshimiwa Spika, nakupongeza kwa dhati wewe binafsi Mheshimiwa
Samuel Sitta na Naibu Spika Mheshimiwa Anne Makinda kwa kuchaguliwa
kutuongoza. Vile vile nampongeza Spika Mstaafu, Mhe. Pius Msekwa kwa
usimamizi madhubuti wa shughuli za Bunge ambao umetuwezesha kupata jengo jipya
na la kisasa. Nawapongeza pia Wenyeviti, Mheshimiwa Jenista Mhagama
Mbunge wa Peramiho na Mheshimiwa Job Ndugai, Mbunge wa Kongwa kwa kuteuliwa
kuwa wenyeviti. Aidha, nawapongeza Wenyeviti
wote na Makamu Wenyeviti wa Kamati zote za Kudumu za Bunge kwa
kuchaguliwa kuongoza kamati hizo.
5.
Mheshimiwa Spika, napenda
pia kutoa pongezi nyingi za
dhati kwa Chama changu cha CCM kwa kupata viongozi wapya wa kitaifa. Nampongeza sana Mwenyekiti wa CCM Taifa Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa kwa kishindo kushika wadhifa
huo. Ushindi wa kura 1,812 kati
ya kura 1,813 zilizopigwa ni ushindi wa kihistoria.
6. Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kumpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa
Benjamin William Mkapa na Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Frederick
Tulway Sumaye kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuendeleza amani na utulivu nchini.
Aidha, nawapongeza kwa kusimamia
utungaji mzuri wa sera za kiuchumi zilizoweza kuwavutia wawekezaji wa ndani na
nje ya nchi na hivyo kuufanya uchumi wetu uwe wenye ushindani na endelevu.
7.
Mheshimiwa Spika,
nampongeza Mheshimiwa Yusuph Rajab Makamba kwa kuteuliwa na baadaye
kuthibitishwa na NEC kuwa Katibu Mkuu wa CCM.
Nampongeza Mheshimiwa Jaka Mwambi kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu
Mkuu wa CCM (Bara). Nawapongeza sana Waheshimiwa
Wabunge wenzangu kwa nyadhifa walizopata, Mheshimiwa Aggrey Mwanri, Mheshimiwa
Dr. Asha Rose Migiro, Mheshimiwa Kidawa Salehe na Mheshimiwa Rostam Aziz.
8. Mheshimiwa
Spika, wote hawa tunawaombea kheri, afya njema na baraka tele za Mwenyezi
Mungu katika kutekeleza majukumu yao mapya.
Napenda kuwathibitishia kuwa, mimi binafsi pamoja na wananchi wa Jimbo
la Tanga tunawaahidi kuwapa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao.
9. Mheshimiwa Spika, natoa pongezi
kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango, Uchumi na
Uwezeshaji kwa hotuba zao nzuri ambazo zimetoa mwelekeo wa bajeti ya Serikali,
hali ya uchumi wa nchi kwa jumla na masuala ya msingi yanayopaswa kutekelezwa
mwaka ujao wa fedha wa 2006/07.
10.
Mheshimiwa Spika, natoa
shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kwa
kuyapitia na kuyachambua makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yangu tarehe
30 Mei 2006, pamoja na kuchambua masuala
mbalimbali ya Wizara ya Usalama wa Raia na kuyatolea maoni na ushauri. Michango
iliyotolewa na kamati kwa ujumla imetusaidia kwa kiwango kikubwa kuiboresha
hotuba yangu.
11. Mheshimiwa
Spika, napenda pia kutoa shukrani kwa ushirikiano wa karibu, ushauri na
maelekezo fasaha ambayo nimekuwa nikiyapata kutoka Kamati ya Bunge ya Ulinzi
na Usalama. Ushauri na maelekezo yao unasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha
utendaji kazi katika Wizara yangu.
12. Mheshimiwa
Spika, namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuniteua kuwa Waziri wa kwanza wa Wizara
mpya ya Usalama wa Raia na kunipatia Naibu Waziri wa Usalama wa Raia Mheshimiwa
Mohamed Aboud Mohamed, ambaye ameonesha umahiri na uwezo mkubwa katika
kunisaidia kusimamia shughuli za Wizara na za Bunge.
13. Mheshimiwa
Spika, napenda kuchukua fursa hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa uteuzi
wa Katibu Mkuu wa Wizara Bw. Bakari Mahiza ambaye ni hazina kubwa kwa
Wizara yetu kutokana na uzoefu alioupata akiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
ambayo wakati huo Jeshi la Polisi lilikuwa chini yake.
14. Mheshimiwa Spika, aidha,
napenda kumshukuru Inspekta Jenerali Mstaafu, Alhaj Omar Iddi Mahita,
ambaye yeye pamoja na Makamishna wake wote walifanya kazi nzuri na
walijitahidi sana kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa Polisi. Ninawashukuru na kuwapongeza sana.
15. Mheshimiwa
Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wa Inspekta Jenerali mpya Ndugu Said Mwema,
pamoja na Makamishna wapya ambao kwa kipindi kifupi wameweza kuleta
mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kukabiliana na uhalifu nchini, na hivyo
kurejesha heshima ya Serikali na kuwapa imani wananchi, wageni na wawekezaji,
kwamba nchi yetu bado ina amani na utulivu.
16. Mheshimiwa
Spika, napenda kutoa pongezi nyingi kwa Makamanda wote wa Polisi wa
Mikoa, Vikosi na Wilaya; Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa, Vikosi na Wilaya
na askari wote kwa ujumla kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya ya kulinda
amani na usalama nchini. Juhudi zao
tunazitambua na kuzithamini.
17. Mheshimiwa
Spika, Wizara ya Usalama wa Raia ilianzishwa na Mheshimiwa Rais kwa Tangazo la Serikali
Na. 1 la mwezi Januari 2006 kwa lengo la kusimamia usalama wa raia na mali
zao wakiwemo wageni na wawekezaji. Kuundwa
kwa Wizara hii ni kutekeleza Ilani
ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya
111 inayozungumzia Ulinzi na Usalama. Ilani ya Uchaguzi inataka uwezo wa
Taifa wa kupambana na ujambazi na uhalifu kwa ujumla wake uongezwe na pia
kuwahamasisha wananchi kushiriki katika ulinzi wa maeneo yao ili kuhakikisha
usalama wao na wa mali zao.
18.
Mheshimiwa Spika, wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu Mheshimiwa
Rais alisisitiza umuhimu wa kuendeleza amani na utulivu uliopo nchini
ili kuimarisha uchumi wa nchi na kuongeza kasi ya maendeleo, na hivyo kuleta
maisha bora kwa kila Mtanzania. Kunapokuwa na amani na utulivu wananchi
wanaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa
ili kujiletea maendeleo yao.
19. Mheshimiwa
Spika, hali ya amani na utulivu pia itawavutia wawekezaji wa ndani na
nje ya nchi kuwekeza kwenye maeneo mbali mbali nchini na hivyo kuongeza
nafasi za ajira na Pato la Taifa. Ni
katika mazingira hayo ya amani na utulivu, mipango na mikakati ya Kitaifa kama
vile Mipango ya Muda wa Kati na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini
Tanzania (MKUKUTA), inaweza kutekelezwa na malengo ya Millenia 2015
na hatimaye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inaweza kufanikiwa.
20.
Mheshimiwa Spika, wakati
Mheshimiwa Rais alipotembelea
Wizara hii mara baada ya kuunda Baraza la Mawaziri, alizitaja sababu kuu za
kuundwa kwa Wizara hii kama ifuatavyo:
a.
Ongezeko la idadi
ya watu kutoka milioni 10.3 wakati wa Uhuru mwaka 1961 hadi
milioni 35 hivi sasa.
b. Kuongezeka kwa uhalifu na maarifa ya
uhalifu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kufanya
uhalifu.
c. Kukua kwa Jeshi la Polisi na shughuli za
Polisi kuongezeka.
d. Kupunguza ukubwa wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi kwani ilikuwa kubwa mno, kiasi cha kupunguza umakini wa kazi.
e. Kumpa nafasi
Waziri kushughulikia masuala yanayohusu Polisi tu ili kukabiliana na
ongezeko la vitendo vya uhalifu, hasa uhalifu wa kutumia silaha.
MAJUKUMU YA WIZARA
21.
Mheshimiwa Spika, muundo wa Wizara uliidhinishwa na Mheshimiwa
Rais tarehe 18 Aprili 2006. Baadhi ya majukumu ya Wizara ya Usalama wa Raia
kulingana na muundo huo ni kama ifuatavyo:
a. Kusimamia
na kufuatilia masuala yote yanayohusu usalama wa raia na mali zao ikiwa ni pamoja na wageni kama vile watalii na wawekezaji kutoka nje.
b. Kuandaa Sera
ya Usalama wa Raia
na
kusimamia utekelezaji wake.
c.
Kuandaa mikakati ya muda mfupi, muda wa kati
na muda mrefu ya kukabiliana na uhalifu nchini.
d. Kushirikisha jamii katika kuweka mikakati
ya kuzuia uhalifu kupitia utaratibu wa Polisi Jamii.
e.
Kushughulikia
malalamiko mbali mbali ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi.
f.
Kusimamia
maendeleo ya watumishi wa Wizara.
g.
Kuzuia uhalifu wa kimataifa kwa
kushirikiana na nchi jirani pamoja na Mashirika ya Kimataifa na kikanda kama
vile Shirikisho la Polisi la Kimataifa (INTERPOL), Shirikisho la
Polisi la Nchi za SADC (SARPCCO), na Shirikisho la Polisi la Nchi
za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (EAPCCO).
DIRA YA WIZARA
22. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu
imejizatiti kutekeleza majukumu niliyoainisha hapo juu kwa kuongozwa na Dira ya
“Kuwa na Wizara yenye uwezo endelevu wa kuhakikisha kuwa usalama wa raia na
mali zao unakuwepo”. Lengo la dira hii ni kuhakikisha usalama wa raia na
mali zao wakiwemo wageni kama vile watalii na wawekezaji.
HALI YA UHALIFU NCHINI
23. Mheshimiwa
Spika, kwa ujumla idadi ya matukio ya uhalifu nchini, Tanzania Bara na
Visiwani, hasa makosa makubwa ya jinai kitakwimu imeendelea kushuka
kuanzia mwaka 2000 hadi kufikia Desemba 2005.
Mfano, kipindi cha Januari hadi Desemba 2000, jumla ya matukio 87,973
yaliripotiwa katika vituo vya Polisi nchini, ikilinganishwa na jumla ya matukio
73,555 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2001.
24. Mheshimiwa
Spika, idadi hiyo ilishuka zaidi mwaka 2002 ambapo jumla ya matukio 67,371
yaliripotiwa. Takwimu zinaonyesha pia
kwamba, idadi ya matukio hayo yalipungua zaidi mwaka 2003 na kufikia matukio 58,516. Mwaka 2004 kulikuwepo na ongezeko kidogo la
idadi ya matukio yaliyoripotiwa Polisi ambapo jumla ya matukio 61,376
yaliripotiwa. Hata hivyo, idadi hiyo ya
matukio kwa kipindi kilichoishia mwezi Desemba 2005 ilishuka sana hadi kufikia
matukio 46,650, ikiwa ni upungufu wa matukio 14,726 ambao ni sawa
na asilimia 24.
25. Mheshimiwa
Spika, makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika vituo vya Polisi
kuanzia Julai 2005 hadi Aprili 2006 katika mikoa yote nchini yalikuwa 48,265
ikilinganishwa na matukio 51,820 kipindi cha Julai 2004 hadi Aprili
2005. Kuna upungufu wa matukio 3,555
sawa na asilimia 6.8. Hata
hivyo, bado juhudi zaidi zinahitajika kupambana na uhalifu kote nchini, Bara na
Visiwani.
26. Mheshimiwa
Spika, makosa ya Usalama Barabarani yaliyosababisha ajali ambayo
yaliripotiwa Polisi kati ya Julai 2005 hadi Aprili 2006 yalikuwa 17,062
ikilinganishwa na 14,710 katika kipindi cha Julai 2004 hadi Aprili 2005.
Kuna ongezeko la makosa 2,352 sawa na asilimia 16. Kati ya Julai
2005 hadi Aprili 2006 watu waliofariki kutokana na ajali za barabarani walikuwa
1,896 na wengine 12,349 walijeruhiwa ikilinganishwa na kipindi
kama hiki mwaka 2004/05 ambapo watu 2,159 walifariki na wengine 16,523
walijeruhiwa.
27. Mheshimiwa Spika, idadi ya watu
waliofariki ilipungua kwa watu 263 sawa na asilimia 12.2 na
waliojeruhiwa walipungua kwa watu 4,174
sawa na asilimia 25.3 kama inavyoonyesha katika Jedwali Na. 1.
Pamoja na takwimu hizo kuonyesha kupungua, lakini bado tatizo la ajali za
barabarani ni kubwa, hivyo jitihada zaidi za Jeshi la Polisi katika kukabiliana
na makosa ya usalama barabarani zinahitajika.
28. Mheshimiwa
Spika, sababu za kuwepo ajali nyingi
za barabarani ni pamoja na uzembe wa madereva, ubovu wa magari, ubovu wa barabara, magari kujaza
kupita kiasi, uendeshaji mbaya na wa hatari,
ulevi, mwendo wa kasi, kulegeza vidhibiti mwendo, utembeaji mbaya wa waenda kwa
miguu, upandaji mbaya wa pikipiki na baiskeli, ukosefu wa alama za barabarani,
n.k.
29. Mheshimiwa
Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, tatizo la ajali za barabarani
bado ni kubwa na linahitaji mikakati thabiti ya pamoja ya wadau wote wa sekta
hii. Ajali za barabarani zinasababisha vifo kwa abiria na waenda kwa miguu, zinaacha
majeruhi, vilema na wengine kubaki yatima.
Ajali pia husababisha upotevu na uharibifu wa mali.
30. Mheshimiwa Spika, kulingana na takwimu
za mwaka 2005, mikoa inayoongoza kwa kuwa na ajali nyingi za barabarani ni Dar es Salaam, Mwanza,
Mjini Magharibi, Pwani, Iringa, Arusha, Tanga, Mbeya, Morogoro na Kilimanjaro
kama inavyoonyesha kwenye Jedwali Na. 2(f).
31. Mheshimiwa Spika, matukio ya ajali
mbaya za barabarani ya hivi karibuni ni yale yaliyotokea Mkoani Kagera
na kuua watu 28 na Mkoani Arusha, ambapo watu 54 walipoteza
maisha yao. Nachukua fursa hii kuwapa pole familia, ndugu na jamaa za marehemu,
na kuwatakia wapone haraka majeruhi wote ambao bado wamelazwa. Aidha, narudia
kutoa wito kwa madereva wote, kuwa waangalifu na kufuata sheria zote za barabarani. Abiria kwa upande wao, wasikubali kabisa
kupanda magari yaliyojaa na yanayokwenda mwendo wa kasi kwani ni hatari kwa
maisha yao wenyewe.
32 Mheshimiwa
Spika, kama ilivyo kwenye matukio mengine ya uhalifu ambapo wananchi hutoa
taarifa kwa Jeshi la Polisi, Wizara yangu inaomba ushirikiano kutoka kwa abiria
kwa kutoa taarifa Polisi kuhusu magari ya abiria yanayokiuka sheria za Usalama
Barabarani.
33. Mheshimiwa Spika,
Majedwali Na. 2(a) hadi 2(e) na 2(g) yanatoa mchanganuo wa makosa ya
jinai kimkoa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 2005. Kwa
muhtasari kwa makosa dhidi ya binadamu mikoa inayoongoza ni Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Kagera,
Mwanza, Shinyanga na Arusha. Makosa
dhidi ya mali, mikoa inayoongoza ni Dar es salaam, Kagera, Tanga,
Morogoro, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Mara na Kigoma. Aidha kwa
upande wa makosa dhidi ya maadili ya jamii, mikoa inayoongoza ni Dar es
Salaam, Mwanza, Mara, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Shinyanga, na Kagera.
BAADHI YA MATUKIO
MAKUBWA YA UHALIFU YALIYOTOKEA NCHINI
34. Mheshimiwa Spika, ufuatao ni muhtasari
wa baadhi ya matukio makubwa ya uhalifu yaliyotokea katika kipindi cha Januari
hadi Julai, 2006. Matukio hayo yalileta
hofu kubwa kwa wananchi kiasi cha kujenga hisia kwamba Jeshi la Polisi
limeshindwa kukabiliana na wimbi la ujambazi hapa nchini na wengine walithubutu
hata kusema kwamba kazi hii wapewe Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
35. Mheshimiwa Spika, kazi ya kulinda
usalama wa raia na mali zao ni yenye taaluma maalum na wenye taaluma hiyo ni
Jeshi la Polisi. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa
jumla kuwa Jeshi la Polisi lina uwezo wa kuwalinda wananchi na mali zao.
36. Mheshimiwa Spika, tarehe 7 Januari
2006 majambazi yakiwa na silaha yalivamia Benki ya NBC (T) LTD Tawi la Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam na kupora Tsh. 8,762,915, mali ya benki hiyo
na kutoweka.
37. Mheshimiwa Spika, tarehe 14 Januari 2006
ilisemekana majambazi manne yakiwa na silaha yalivamia gari la Kampuni ya
BIDCO lililokuwa na makusanyo ya fedha za mauzo Tsh. 5,775,000 na
kupora kisha kutoweka. Hata hivyo,
ilisemekana wakati huo kwamba majambazi hayo yalikamatwa na Polisi muda mfupi
baadaye na kuuawa wakati wakirushiana risasi.
Tukio hili la kuuawa watu hao lilisababisha hisia tofauti miongoni mwa
wananchi ambapo yalikuwepo madai kwamba waliouawa hawakuwa majambazi bali raia
wema. Malalamiko hayo yalisababisha
Mheshimiwa Rais kuunda Tume ya Jaji Kipenka Mussa ili kufanya
uchunguzi.
38. Mheshimiwa Spika, tayari Tume
imewasilisha ripoti yake Serikalini, na katika uchunguzi wake ilibaini kwamba
waliouawa hawakuwa majambazi bali raia wema na kupendekeza askari 15
waliohusika katika tukio hilo washtakiwe kwa mauaji. Askari 12 wamekwishakamatwa na kufikishwa
mahakamani ambapo kesi yao bado inaendelea.
Askari waliobakia bado wanasakwa na Jeshi la Polisi.
39. Mheshimiwa
Spika, tarehe 2 Februari, 2006 majambazi yanayokadiriwa kufikia 10 yakiwa
na silaha yalivamia Benki ya NBC Tawi la Ubungo na kufanikiwa kupora
Tsh. 123,000,000, Dola za Kimarekani 16,128 na EURO 50
mali ya benki hiyo na kisha kutoweka.
40. Mheshimiwa Spika, tarehe 6 Machi 2006 majambazi yakiwa na silaha
yalivamia benki ya Standard Chartered Tawi la Life House na kufanikiwa
kupora fedha taslimu Shilingi Milioni 300 kutoka kwa mteja ambaye
alikuwa anataka kuweka fedha hizo benki.
41. Mheshimiwa
Spika, tarehe 20 Aprili, 2006 katika
makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Nelson Mandela, majambazi
kadhaa yaliyokuwa na silaha nzito za kivita yalishambulia msafara wa magari ya
benki ya NMB Tawi la Bank House ambayo yalikuwa yanasafirisha
fedha Shilingi bilioni 1 kutoka tawi la NMB Bank House Dar es Salaam kwenda Tawi
la NMB Wami Morogoro. Katika tukio hilo askari mmoja kati ya askari wanne
waliokuwa wanasindikiza fedha hizo pamoja na mfanyakazi mmoja wa benki ya NMB
waliuawa na majambazi hayo.
42. Mheshimiwa Spika, askari wengine
watatu, dereva na wananchi wengine wapita njia walijeruhiwa kwa risasi
zilizopigwa na majambazi hayo. Fedha shilingi milioni 150 ziliporwa na
majambazi hayo na Polisi waliweza kuokoa shilingi milioni 850.
43. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kisiwani
Zanzibar mwanzoni mwa mwezi Julai, yametokea matukio ya ujambazi wa kutumia
silaha ambapo kiasi kikubwa cha fedha kimeibiwa na mtu mmoja kuuawa. Hali hii imesababisha hofu kubwa kwa
wafanyabiashara na wananchi wa Visiwani
kwa sababu siyo kawaida matukio ya aina hii kutokea huko.
44. Mheshimiwa Spika, tarehe 4 Julai,
2006 eneo la Darajani Mjini Unguja,
majambazi yakiwa na silaha yalivamia dukani kwa Ndugu Mohamed Nassoro na kupora
fedha taslimu Sh.12,000,000 na kadi za simu zenye thamani ya Sh.5,000,000. Majambazi hayo yalifyatua risasi na kumpiga
kichwani Ndugu Mohamed Bakari Mrisho na kufariki.
45. Mheshimiwa Spika, tarehe 6 Julai, 2006
eneo la Kisiwandui, majambazi yenye silaha yalivamia duka la Al-Habbys na
kufanikiwa kupora fedha taslimu Sh.30,000,000 baada ya kutishia kwa silaha.
46. Mheshimiwa Spika, kufuatia matukio
haya ya ujambazi kutokea kwa mfululizo, Jeshi la Polisi lilijipanga upya kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama na kukamata idadi kubwa ya
majambazi yaliyohusika kwenye matukio haya pamoja na silaha walizotumia. Miongoni mwa majambazi yaliyokamatwa wapo
raia wa nchi jirani na raia wa humu humu nchini. Watuhumiwa wamekwishafikishwa
mahakamani. Majambazi hayo yaliweza kukamatwa
kutokana na ushirikiano wa wananchi. Kwa
kupitia Waheshimiwa Wabunge, napenda kuwashukuru wananchi waliotoa ushirikiano
wao uliowezesha majambazi kukamatwa.
Aidha napenda kuwapongeza askari wote walioshiriki kupambana na
majambazi na kufanikisha kuokolewa kwa mali na kukamatwa kwa majambazi.
SABABU ZA KUWEPO KWA
UHALIFU NCHINI
47. Mheshimiwa Spika, zipo sababu nyingi
zinazosababisha kutokea kwa uhalifu nchini.
Sababu za jumla ni kama vile kuongezeka
kwa idadi ya watu nchini, tatizo la wimbi la watu kuhamia mijini toka vijijini, kupanda kwa gharama za maisha
na ukosefu wa ajira, na kuongezeka kwa wakimbizi
ambao baadhi yao huingia na silaha kinyume cha sheria. Sababu hizo za jumla kwa namna moja au
nyingine zimechangia ongezeko la vitendo vya uhalifu nchini na hasa uhalifu wa
kutumia silaha.
48. Mheshimiwa
Spika, uchambuzi umeonyesha kwamba zipo sababu nyingine zinazochangia
kuwepo kwa vitendo vya uhalifu kama ifuatavyo:-
a.
Utandawazi
na Mageuzi katika Mfumo wa Mawasiliano
Sera ya Utandawazi imesababisha na
kurahisisha mwingiliano wa watu wa mataifa mbali mbali. Wahalifu wa Kimataifa
nao wametumia mwanya huu na kuweza kufanya uhalifu nje ya mipaka ya nchi
zao. Aidha, mageuzi katika mfumo wa
mawasiliano yamerahisisha sana na kuongeza kasi ya utendaji makosa. Wahalifu hivi sasa wanaweza kuwasiliana kwa
haraka na kwa mawasiliano bora zaidi popote wanapokuwa, wakati mwingine kupita
yale waliyonayo Polisi kwa sasa. Mfano,
matumizi ya Computer, Internet na simu za mkononi za kisasa.
Aidha, pale
ambapo Polisi wanahitaji kufuata utaratibu wa kisheria na Kidiplomasia wa kuvuka
mipaka kufuatilia wahalifu, wahalifu hao hawalazimiki kufanya hivyo wanapokwepa
mkono wa sheria.
b.
Uchache
wa askari na nyenzo za kutendea kazi
Upo uhaba mkubwa wa askari ikilinganishwa
na idadi ya wananchi wanaohitaji huduma ya Polisi. Kwa upande mwingine, upo uhaba wa vitendea
kazi muhimu kwa ajili ya doria za miguu, magari, vifaa vya majini na vifaa vya
mawasiliano. Kukosekana kwa vitendea
kazi hivi kumeathiri sana uwezo wa Idara kukabiliana kikamilifu na tishio la
uhalifu nchini. Mfano, imekuwa ni vigumu
kuwahi kwenye baadhi ya matukio ya uhalifu kwa sababu ya ama kukosekana gari au
gari kutokuwa na mafuta.
Aidha, imekuwa
vigumu kukabiliana na uhalifu wa kuteka nyara magari kwenye barabara kuu
kutokana na kutokuwa na magari ya kufanyia doria kwenye barabara hizo (Highway
Patrol).
c.
Kutokuwa
na Mfumo wa Kisasa wa Uwekaji Kumbukumbu na Upashanaji Taarifa
Upo umuhimu wa kuwa na njia za kisasa za
uwekaji kumbukumbu, mawasiliano kwa njia ya mtandao wa ‘Computer’ na
umuhimu wa kuwa na ‘Electronic Surveillance System’ kama ‘Closed
Circuit Televisions (CCTV), ambayo hunakili matukio yote ya uhalifu. Kukosekana kwa mfumo huo wa
kisasa wa uwekaji kumbukumbu na mawasiliano kwa Jeshi letu kumedhoofisha kwa kiasi kikubwa
jitihada za kukabiliana na uhalifu.
d.
Uhaba wa
Elimu na Taaluma za Upelelezi
Uhaba wa askari wenye taaluma ya upelelezi
umechangia kwa kiasi fulani kupunguza kiwango cha mafanikio ya kudhibiti
uhalifu kwa baadhi ya maeneo. Ukweli ni
kwamba aina, muundo na mbinu za makosa ya jinai kwa jumla hubadilika siku hadi
siku.
Mbinu hizo ni
matumizi ya teknolojia ya kisasa kama vile matumizi ya mifumo ya kisasa na ya
haraka ya kusafirisha fedha pamoja na kujenga mtandao wa magenge ya wahalifu
ambao unahusisha wahalifu wa nchi za jirani.
Hali hii inahitaji kupata askari ambao wamepata taaluma kuhusu
mabadiliko hayo ili kuweza kukabiliana kikamilifu na matishio ya uhalifu wa
kisasa na yenye sura ya Kimataifa.
e.
Udhibiti
hafifu wa Mipaka yetu
Upo upungufu wa nyenzo na watendaji wa
kutosha katika maeneo muhimu ya mipaka yetu.
Matukio yaliyotokea hivi karibuni hasa ya unyang’anyi wa kutumia silaha,
wizi wa magari, madawa ya kulevya, n.k. yametudhihirishia kwamba wahalifu
kutoka nchi jirani wamehusika katika matukio hayo.
Hali hii inaashiria
kwamba kumekuwepo na udhaifu katika kuwachunguza wageni mbalimbali wanaoingia
nchini mwetu. Udhaifu huu umetokana na
ama ukosefu wa vifaa muhimu na vya kisasa kama vile detecting/screening machines,
kumbukumbu sahihi za wahalifu wa Kimataifa na upungufu wa watendaji wenye
taaluma inayostahili kwenye vituo vya mipakani.
f.
Ukosefu
wa Vyumba/Ofisi Maalumu za Upelelezi
Tatizo la uhaba wa ofisi kwa ajili ya
askari wa Upelelezi na hasa vyumba maalum vya kufanyia mahojiano (Interview
Rooms) pia linaathiri kwa kiasi kikubwa ufanisi katika upelelezi hasa wa
kesi kubwa. Hali hii inachangia
kuharibika au kuchelewa na hatimaye kushindwa mahakamani katika baadhi ya kesi.
g.
Mabenki
na Taasisi za Fedha Kutojikinga kwa Njia
za Kisasa
Kukataa ushauri wa Polisi wa kuweka mifumo mizuri ya ulinzi inayotumia teknolojia
ya kisasa katika Benki na Taasisi nyingine za fedha hapa nchini, kumechangia sana wahalifu wa ndani na nje ya
nchi kufanya vitendo vya uporaji kwenye taasisi hizo kwa urahisi na kuondoka
bila kugundulika na hivyo kufanya kazi ya upelelezi kuwa ngumu zaidi.
HATUA ZINAZOCHUKULIWA KUIMARISHA UTENDAJI
49. Mheshimiwa
Spika, kuanzia mwaka 2002/03 Serikali imekuwa ikichukua hatua za kuboresha Bajeti
ya Jeshi la Polisi. Bajeti hiyo
imewezesha upatikanaji wa baadhi ya vitendea kazi kama vile magari, vifaa vya
mawasiliano, mashua za doria n.k na upatikanaji wa makazi ya askari.
50. Mheshimiwa
Spika, bajeti ya Jeshi la Polisi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka kama
ifuatavyo: Mwaka 2006/07 bajeti ya matumizi ya kawaida ya Jeshi
la Polisi imeongezeka kwa asilimia 40.1 na ile ya maendeleo imeongezeka
kwa asilimia 36.2 ukilinganisha na mwaka 2005/06 ambapo bajeti ya
matumizi ya kawaida iliongezeka kwa asilimia 18.7 na ile ya maendeleo
iliongezeka kwa asilimia 1.9. Kwa mwaka 2006/07 bajeti ya
matumizi ya kawaida na ya maendeleo kwa pamoja imeongezeka kwa asilimia 39.8
ukilinganisha na asilimia 17.6 mwaka 2005/06 kama inavyoonyesha
kwenye Jedwali Na. 4(a). Hata
hivyo kutokana na matatizo ya Jeshi la Polisi kuwa makubwa, kama yalivyotajwa
bado juhudi zaidi zinahitajika kuboresha bajeti yake.
51. Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa
kuiangalia Wizara hii kwa jicho la huruma.
Mheshimiwa Rais akiwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama ameona umuhimu wa kuisaidia Wizara hii ili iweze kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu. Pamoja na ukweli kuwa safari bado ni ndefu,
lakini namshukuru sana kwa hatua zinazochukuliwa. Aidha, namshukuru Waziri wa Fedha na Waziri wa
Mipango, Uchumi na Uwezeshaji kwa kuyaelewa matatizo ya Wizara yangu na
kuendelea kuyapatia ufumbuzi kulingana na uwezo uliopo.
52. Mheshimiwa Spika, baada ya
Serikali kufanya mabadiliko ya uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi, ambapo
aliteuliwa Inspekta Jenerali mpya na Makamishna, hatua mbali mbali
zimechukuliwa kwa lengo la kuimarisha utendaji kama ifuatavyo:-
a.
Kufanya
mabadiliko ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa. Aidha, baadhi ya Wakuu wa Polisi Usalama
Barabarani wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya pia wamebadilishwa.
b.
Kuanzishwa Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, ambapo Wilaya za Kinondoni, Ilala na
Temeke zimepewa hadhi ya Mikoa Kipolisi ili kuongeza ufanisi, kwani
Jiji la Dar es Salaam lilikuwa linaongoza kwa matukio ya uhalifu.
c. Kutangazwa hadharani namba za simu za IGP,
Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa na Wakuu wa Upelelezi
wa Wilaya kumewezesha upatikanaji wa taarifa nyingi za uhalifu kutoka kwa
wananchi. Matukio mengi ya uhalifu
yalizuiwa kutokea kutokana na Polisi kupata taarifa mapema.
d. Uwekaji wa masanduku ya maoni nje ya Vituo
vya Polisi umewezesha upatikanaji wa taarifa muhimu za uhalifu.
e.
Uhamasishaji wa wananchi kwa njia ya mazungumzo na viongozi wa Serikali za
Mitaa, wananchi na vikundi binafsi vya ulinzi ili kuwaelimisha juu ya utoaji
taarifa za uhalifu.
f. Kufanya misako ya kushtukiza na yenye
malengo maalum baada ya kupata taarifa za uhalifu ili kuzuia uhalifu usitokee.
g. Kuwasaka wafadhili wa uhalifu, ambapo baadhi
yao wanaotuhumiwa wameshafikishwa mahakamani na zoezi linaendelea.
h. Kila Mkoa unaendelea kuimarisha kitengo cha
Intelijensia ambacho kazi yake ni kutafuta na kukusanya taarifa za uhalifu kwa
nia ya kuzuia, kufuatilia, kuwatambua na kuwakamata watu wanaofanya uhalifu
huo.
i. Kuimarisha ulinzi katika Mabenki na Maduka
ya fedha nchini.
j. Kuwahamasisha wananchi wanaosafirisha
fedha nyingi kutumia huduma ya Polisi ya kusindikiza fedha.
k. Kuongeza juhudi katika upelelezi wa
matukio ya uhalifu yaliyotokea hasa ya ujambazi wa kutumia silaha. Jitihada hizo ambazo ziliwezesha Polisi kufika
hata nchi za jirani kuwafuatilia wahalifu, zimeleta mafanikio makubwa ambapo
wahalifu wengi wamekamatwa na mitandao yao kuvunjwa.
l. Kuimarisha
doria za miguu, magari, pikipiki na operesheni mbalimbali.
m. Kufanya
ukaguzi mara kwa mara kwenye nyumba za kulala wageni na maeneo yanayohisiwa
kuwa maficho ya wahalifu.
n. Kuwapa askari, hasa wa Upelelezi, mafunzo ya ndani
na nje ya nchi kwa lengo la kuwaongezea ujuzi.
o. Kufanya uchunguzi
wa kuwabaini askari wote wa Polisi na wa vyombo
vingine vya ulinzi na usalama wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kwa lengo
la kuwachukulia hatua za kisheria.
p. Kusindikiza
magari
ya
abiria
kwenye
maeneo ambayo ni hatari kama vile Milima ya
Kitonga Mkoani Iringa, Mapori ya
Biharamulo Mkoani Kagera na Mlima wa Koro (Kondoa) Mkoani Dodoma.
q. Kuimarisha ushirikiano wa vyombo vya dola
vyote nchini na kupanga mikakati ya pamoja ya kupambana na uhalifu nchini.
r. Kuimarisha
ushirikiano wa Kimataifa na kikanda wa
Kipolisi kwa kupitia INTERPOL, SARPCCO, EAPCCO, EAC na kuimarisha
ushirikiano na nchi nyingine kwenye ukanda wetu na hata duniani kote.
MATARAJIO YA WANANCHI KWA JESHI LA POLISI
53. Mheshimiwa
Spika, baada ya mabadiliko ya uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi, wananchi
na wadau wengine wamejenga imani na kuwa na matarajio makubwa kwa Jeshi la
Polisi. Kutokana na hali hiyo, Jeshi la
Polisi linajitahidi kufanya yafuatayo:
a. Kuboresha Huduma ya Polisi Kwa Wananchi
54. Mheshimiwa
Spika, utendaji kazi wa Polisi usiojali na kuheshimu haki za raia, Polisi
kushindwa kushughulikia kero za wananchi kikamilifu na ukiukwaji wa haki za
binadamu ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wananchi kukosa imani na Jeshi hilo
na hivyo kuacha kutoa ushirikiano. Kufuatia hatua mbali mbali zinazochukuliwa
na Jeshi hivi sasa kupambana na uhalifu nchini, wananchi na wadau wengine
wanatarajia huduma ya Polisi kwao itaboreshwa. Hivyo, kazi kubwa ya Jeshi la
Polisi itakuwa ni kuboresha huduma kwa wananchi.
b.
Jeshi la Polisi Kuwa Karibu Zaidi na Wananchi
55. Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia kwamba wahalifu ni watu waishio miongoni mwa
wananchi, na kwamba waathirika wakubwa ni wananchi wenyewe, raia wapenda amani
na watiifu wa sheria wanatarajia kwamba Jeshi la Polisi litashirikiana nao kwa
karibu zaidi katika kukabiliana na uhalifu.
Katika ushirikiano huo, Jeshi la Polisi litazingatia utunzaji wa siri za
raia wema wanaotoa taarifa za kuisaidia Polisi.
Askari watakaobainika kuvujisha siri za raia hao watachukuliwa hatua
kali za kinidhamu.
c. Kufanya Kazi kwa Kuzingatia Sheria na Haki za Binadamu
56. Mheshimiwa
Spika, wananchi wanatarajia Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa ukweli, uwazi
na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Pia wananchi wanatarajia
Polisi kujiepusha na vitendo vyovyote
vya ukiukaji wa haki za binadamu, kama vile kutumia nguvu ya ziada kwa
mtuhumiwa, kuwabambikiza watu kesi, kuchelewesha upelelezi wa kesi, kuwanyima
watu dhamana ya Polisi hata kwa kesi ndogo na kuepuka itikadi na ushabiki wa
vyama vya siasa. Aidha, askari Polisi
wanatakiwa kujiepusha na kuwakamata wananchi siku za mwisho wa wiki bila ya sababu
za msingi na kuwashikilia watu hasa wafanyabiashara hata pale wanapoonyesha
vielelezo vyote vya biashara zao.
57. Mheshimiwa
Spika, napenda kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara yangu kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuwasimamia
askari kwa lengo la kupunguza
vitendo hivi na wale watakaobainika kukiuka, hatua kali za kisheria zitachukuliwa
dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
d. Polisi
Kujiepusha na Vitendo Vyote vya Rushwa
58. Mheshimiwa
Spika, wananchi wanawatarajia askari Polisi wa ngazi zote kujiepusha na vitendo
vyote vya rushwa, hasa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani na askari wa
upelelezi. Polisi wanatarajiwa kuwa mstari wa mbele kupambana na vitendo vya
rushwa, na siyo kuonekana wanashiriki kwa namna moja au nyingine.
e. Askari
Kufika Mapema Eneo la Tukio
59. Mheshimiwa
Spika, changamoto kubwa ya Wizara hii ni kuwahakikishia Watanzania usalama
wao pamoja na mali zao. Katika hili, matarajio ya wananchi ni Polisi kufika
mapema eneo la tukio. Sanjari na hili, wananchi wanatarajia kwamba Polisi
watayashughulikia matukio yote ya uhalifu kwa ufanisi kwa kuwakamata na
kuwafikisha mahakamani wahalifu wote wanaohusika. Inapotokea askari wamechelewa
kufika kwenye tukio na hakuna wahalifu wanaokamatwa kuhusiana na tukio hilo,
wananchi hubaki na tafsiri tofauti, ikiwa ni pamoja na tafsiri kwamba Polisi imeshindwa
kazi au Polisi nayo inashiriki katika vitendo vya uhalifu.
MATARAJIO YA WIZARA
60. Mheshimiwa
Spika, ili Jeshi la Polisi liweze kukidhi matarajio ya Serikali na ya
wananchi, lazima liwezeshwe. Serikali kwa upande wake, italipatia Jeshi la
Polisi vitendea kazi vya kutosha na kuboresha mazingira ya utendaji kazi. Wananchi kwa upande wao, wanatarajiwa
kulipatia Jeshi la Polisi ushirikiano mkubwa, hasa wa kuwapatia taarifa sahihi
na kamilifu za uhalifu na wahalifu zitakazotumika kukabiliana na uhalifu. Wananchi
pia wanatarajiwa kushiriki kikamilifu
katika kutafuta mbinu za kukabiliana na uhalifu katika maeneo yao. Pande zote mbili ni lazima sio tu zinapaswa
kuwa na mawasiliano mazuri bali pia zinapaswa kuaminiana kwa kiwango kikubwa
katika kufanikisha azma hii. Aidha, mambo
yafuatayo yanatarajiwa kufanywa na Wizara:-
a. Kuandaa
Sera ya Usalama wa Raia
61. Mheshimiwa
Spika, Wizara ya Usalama wa Raia inatarajia kuanza mchakato wa kuandaa Sera
ya Usalama wa Raia ambayo itaongoza pamoja na mambo mengine, mahusiano ya kiutendaji
kati ya Wizara na Jeshi la Polisi, wananchi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu,
Mahakama, Magereza, Usalama wa Taifa, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Taasisi ya
Kuzuia Rushwa, Uhamiaji, Idara ya Forodha, Taasisi zisizo za Kiserikali, Vyuo,
Sekta Binafsi, Makampuni Binafsi ya Ulinzi, pamoja na mashirikisho ya Kipolisi
ya Kikanda na Kimataifa.
b. Kuangalia Upya Mfumo wa Jeshi la
Polisi
62. Mheshimiwa Spika, baada ya
muundo wa Wizara ya Usalama wa Raia kuidhinishwa, hatua inayofuata ni kuangalia
upya muundo na mfumo wa Jeshi la Polisi. Lengo ni kuuboresha mfumo wa Jeshi la
Polisi ili kuliwezesha kukabiliana na uhalifu
wa sasa kulingana na mabadiliko ya hali
ya uchumi, jamii na utamaduni nchini na duniani kwa jumla ambapo sasa sera za
utandawazi zinatawala dunia.
63. Mheshimiwa
Spika, upo mpango wa kupunguza zaidi watendaji wanaoripoti moja kwa moja
kwa Inspekta Jenerali ili kutawanya madaraka katika kanda kwa ajili ya kupunguza
urasimu, kuharakisha maamuzi na kubwa zaidi ni kumpa muda wa kutosha Inspekta
Jenerali wa Polisi kufikiria maandalizi
ya mipango ya mikakati ya kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi. Kanda ya Dar es Salaam ni kama kanda ya majaribio;
itakapofanya vizuri, zitaanzishwa Kanda nyingine na Makamanda wa Mikoa wa Kanda
husika wataripoti kwa Kamishna wa Kanda.
64. Mheshimiwa
Spika, hivi sasa idadi ya Makamanda wanaoripoti moja kwa moja kwa Inspekta
Jenerali ni 35, ikijumuisha Makamanda wa Mikoa na Vikosi. Huu sio mfumo mzuri wa kiutendaji. Watateuliwa
Wataalamu (Consultants) kuchambua masuala haya yote na kutupa
mapendekezo ya muundo na mfumo mpya wa Jeshi la Polisi.
65. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu inakusudia pia kulifanyia maboresho Jeshi la Polisi ili
muundo na mfumo wake uwe imara kutoka ngazi ya Makao Makuu hadi ngazi ya Kituo
cha Polisi. Hii ni pamoja na kugawa
madaraka na raslimali husika Mikoani, Wilayani na Vituoni na kukasimu madaraka
ya uongozi kwa watendaji bila kuathiri udhibiti ili kuongeza ufanisi zaidi.
c. Kuzipitia Upya Sheria na Kanuni za Jeshi la Polisi
66. Mheshimiwa Spika, baadhi ya
sheria zinazoongoza Jeshi la Polisi zilitungwa wakati wa ukoloni. Sheria hizo
zilitungwa kukidhi mahitaji ya ulinzi na usalama wa wakoloni. Baadhi ya sheria na kanuni hizo hivi sasa
zimepitwa na wakati na kuhitaji marekebisho kwani hazijazingatia kikamilifu
Haki za Binadamu na hata za askari wa kawaida ndani ya Jeshi lenyewe. Lengo ni
kuziboresha ili ziendane na wakati na zisikwamishe kwa namna moja au nyingine utekelezaji
wa majukumu ya Polisi.
67. Mheshimiwa
Spika, taratibu, kanuni na sheria zinazokusudiwa kupitiwa upya ni Taratibu
za Kudumu za Polisi (Police General Orders (PGO), Kanuni za Utumishi za
Jeshi la Polisi (Police Force Service Regulations), Muundo wa Utumishi
(Scheme of Service), Muundo wa Kamisheni ya Polisi. Aidha, utawasilishwa
Bungeni muswada wa Sheria kwa lengo la kuibadilisha sheria ya sasa ya Jeshi la
Polisi yaani Police & Auxilliary Services Act na kutengeneza sheria
ya Polisi yaani ‘Police Act’.
68. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu
imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa askari wanaostaafu wakilalamikia
utaratibu wa malipo ya Bakshishi (Gratuity). Pamoja na ukweli kwamba askari huchagua kwa
hiari yake kuingia utaratibu wa Pensheni au Bakshishi, inaelekea askari hapati
elimu ya kutosha ili kumwezesha kuchagua vizuri utaratibu unaomfaa. Kwa utaratibu
uliopo ukishachagua kuingia katika Pensheni au Bakshishi huruhusiwi tena
kubadilisha. Hivyo, kanuni zinazoongoza
taratibu za malipo ya Bakshishi na Pensheni zitapitiwa upya ili kuona uwezekano
wa kuweka utaratibu mmoja
d. Kuifanyia Maboresho Idara ya Upelelezi
69. Mheshimiwa Spika, Serikali ipo
kwenye mchakato wa kuhamisha shughuli za uendeshaji mashtaka kutoka Jeshi la
Polisi na taasisi nyingine zilizokuwa zinafanya kazi hiyo na kuzipeleka Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini. Ili kuweza kufanikisha mchakato huo, Idara ya
Upelelezi inahitaji kufanyiwa maboresho ili iweze kuhimili mabadiliko hayo. Maboresho hayo yatakuwa na lengo la kuweka
mahusiano mazuri ya kiutendaji kati ya ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini.
70. Mheshimiwa
Spika, maboresho hayo pia yatalenga kumpatia Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai nchini uwezo wa kuratibu shughuli zote za upelelezi wa makosa
ya jinai zinazofanywa na taasisi mbali mbali ili hatimaye iweze kuwa rahisi
kupata takwimu zote na kumbukumbu sahihi za makosa ya jinai nchini. Aidha, utaratibu huu utamwezesha Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuandaa taratibu zinazofanana za upelelezi
zitakazotumiwa na taasisi zote (Standard Operating Procedure).
71. Mheshimiwa
Spika, sanjari na hayo, Wizara yangu inatarajia kuigawa Idara ya Upelelezi
katika vitengo kulingana na utaalamu wa makosa mbali mbali ya jinai. Kwa mfano, vitaundwa vitengo vya Makosa dhidi
ya Binadamu, Makosa dhidi ya Mali, Uhalifu wa Kimataifa (Transnational/Cross
Border Crimes), Makosa ya Uhujumu Uchumi (Serious Economic Crimes). Kitengo cha Intelijensia pia
kitaimarishwa ili kiweze kutoa mchango mkubwa katika uzuiaji wa uhalifu.
e. Kuboresha Utendaji Kazi wa Askari wa
Kikosi cha Usalama Barabarani
72. Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia kwamba ajali za barabarani bado ni kero kubwa na
tishio kwa maisha ya wananchi, na kwa kuelewa madhara ya malalamiko ya vitendo
vya rushwa dhidi ya askari wa usalama barabarani, Jeshi la Polisi limeanzisha
utaratibu wa usimamizi madhubuti wa askari wa usalama barabarani. Kwa sasa
Wakuu wa Polisi wa Vituo na Wilaya wanakofanya kazi askari hawa watawajibika
kuwasimamia moja kwa moja tofauti na zamani ambapo usimamizi ulikuwa unafanywa
na Makamanda wa Kikosi hicho.
73. Mheshimiwa Spika, vile vile Kikosi cha
Usalama Barabarani hivi sasa kinafanyiwa mageuzi makubwa. Sehemu ya mageuzi hayo inahusu maandalizi ya
mtaala mpya, ambapo askari watakapoenda chuoni siku zijazo, watakuwa
wanajifunza pia Sheria ya Usalama Barabarani na hivyo kila askari atakuwa na
elimu hiyo. Lengo ni kuwafanya askari wote kufahamu kazi za Usalama
Barabarani ili pale inapolazimu kuweza kuwabadilisha bila kulazimika kuwapeleka
kwanza chuoni.
74. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Makamanda
wa Polisi wa Mikoa wamepewa mamlaka ya kuwabadili askari wa Usalama Barabarani
wakati wowote watakapoona inafaa bila kulazimika kuwasiliana kwanza na Makao Makuu. Hivyo,
hakutakuwa na askari wa kukaa katika kikosi hicho mpaka anastaafu, bali askari
hao watakuwa wakibadilishwa mara kwa mara kulingana na mahitaji.
75. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu
inatarajia kupendekeza marekebisho ya baadhi ya Sheria za Usalama
Barabarani, ikiwemo Sheria ya kutoa leseni, ambapo sasa madereva wa
magari makubwa, hasa magari ya abiria watalazimika kujaribiwa upya ili kupima
uwezo wao wa kuendelea kubeba roho za
watu. Aidha, sifa zinazotakiwa
ili mtu aruhusiwe kuendesha magari ya abiria zimepitiwa upya na leseni
daraja C inayoruhusu madereva kuendesha magari yote, sasa itatumika kwa
kuendesha magari ya abiria tu. Aidha, tunatarajia pia kubadili leseni
za udereva ili zifanane na za nchi za SADC zenye mfano wa kadi za
Benki ambazo siyo rahisi kughushiwa.
76. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya kutunga sheria ya ukaguzi wa
lazima wa magari (Mandatory Vehicle Inspection) yanaendelea. Vile vile,
faini na adhabu kwa makosa ya usalama barabarani zinatazamwa upya kwa lengo la
kuziongeza ili kuwadhibiti madereva wasio waangalifu. Aidha Wizara inatarajia kupendekeza kutungwa
kwa sheria zifuatazo : Sheria ya
kuwashitaki wamiliki wa magari, madereva, makondakta na abiria wanaozidi
kwenye magari ya abiria ; Sheria ya kuwaadhibu madereva na makondakta wanaonyanyasa
wanafunzi na watu wengine wasio na uwezo; Sheria ya kuzuia magari kuweka
vioo vya giza (tinted) ; Sheria ya kuwazuia madereva kuendesha
magari wakati wanaongea na simu za mkononi na Sheria ya kuruhusu
taasisi za Serikali, Makampuni binafsi na magereji yenye uwezo kukagua
magari kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kudhibiti magari mabovu.
f. Kuanzisha Kikosi Maalum kwa
Ajili ya Ulinzi na Usalama Kwenye
Vituo Vya Kuingilia Nchini
77. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuongezeka
kwa kasi kwa tatizo la wahamiaji haramu nchini na hali ya vitendo vya uhalifu
vinavyofanywa na wahamiaji hao, na vile vile kwa kuelewa kwamba upo uwezekano
wa biashara haramu ya watu (Human Trafficking) kushamiri hapa nchini,
Wizara inaangalia uwezekano wa kuanzisha Kikosi Maalum ndani ya Jeshi la Polisi
kwa ajili ya kuboresha ulinzi na usalama
kwenye vituo vyote vya kuingilia nchini.
Aidha Wizara inaangalia sababu zilizofanya Jeshi la Polisi kujiondoa
kwenye ulinzi wa bandari zetu na kuachia Mamlaka ya Bandari jukumu hilo. Lengo ni kurudisha ulinzi wa Bandari kwa
Jeshi la Polisi kwa vile huo ni mlango wa kuingilia nchini kama ilivyo
Viwanja vya Ndege na Mipaka ya nchi kavu.
g. Kuanzisha Kikosi Maalum kwa
Ajili ya Ulinzi wa Watalii
78. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu
wa sekta ya utalii katika kuchangia Pato
la Taifa na kwa kuzingatia hali ya kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu dhidi ya
watalii, Wizara inaangalia uwezekano wa
kuanzisha Kikosi Maalum ndani ya Jeshi la Polisi ambacho jukumu lake
kubwa litakuwa ni kuimarisha ulinzi na usalama wa watalii, wanaotembelea nchi
yetu, Bara na Visiwani. Mawasiliano yanaendelea hivi sasa baina ya Wizara yangu
na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wengine muhimu katika suala hili. Kwa upande wa Zanzibar, Wizara yangu
inaendelea na mazungumzo na Wizara ya Biashara, Uwekezaji na Utalii kuhusu
suala hili.
h. Kuanzisha Utaratibu wa Polisi Jamii
79. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ukweli kwamba wahalifu wa kila
namna, yakiwemo majambazi yanayotumia silaha ni watu waishio miongoni mwa
jamii, utaanzishwa utaratibu wa Polisi Jamii (Community Policing). Polisi Jamii
ni utaratibu wenye lengo la kuweka mazingira ya ushirikiano wa dhati
baina ya Polisi na wananchi. Katika
utaratibu huu Jeshi la Polisi litasambaza huduma zake kwa jamii kwa kutumia
askari Polisi wa Kata au Shehia kwa upande wa Zanzibar. Askari huyu atapangwa katika kata/shehia kwa
utaratibu wa kudumu na atakuwa kichocheo cha mabadiliko ndani ya kata/shehia
hiyo.
80. Mheshimiwa Spika, kwa kumpanga
askari Polisi katika kata/shehia kama
sehemu yake ya kazi, Jeshi la Polisi litakuwa na mtazamo wa muda mrefu wa
kutatua matatizo ya uhalifu katika kata/shehia hiyo badala ya kusubiri kutatua
tatizo moja moja kila
linapojitokeza. Aidha, kwa utaratibu
huu, raia wa kawaida atakuwa na kauli katika uwekaji wa malengo ya Polisi
badala ya kuwa mpokeaji tu wa maelekezo kutoka Polisi juu ya namna ya kuzuia
uhalifu.
81. Mheshimiwa Spika, lengo ni kuondoa dhana iliyokuwepo kuwa Jeshi la
Polisi ni chombo cha mabavu, badala yake kuwa chombo rafiki na cha utoaji huduma. Hili litawezekana kwa kuwa na taratibu zilizobuniwa
makusudi kuruhusu mashauriano baina ya
Polisi na wananchi. Taratibu hizi zitawawezesha wananchi kuwaarifu Polisi
kuhusu kuridhika au kutoridhika kwao na huduma ya Polisi. Kwa njia hii uwajibikaji wa Polisi kwa
wananchi utaongezeka. Aidha, utaratibu
huu utasaidia sana kupunguza kero ya rushwa ya Polisi kwa sababu Polisi
Kata/Shehia ambaye ni sehemu ya jamii ya Kata/Shehia husika inatarajiwa
hataweza kuwadai rushwa wanajamii wenzake ili atoe huduma ya Polisi maana
mipango yenyewe ya kazi wanapanga wote.
82. Mheshimiwa Spika, ili utekelezaji wa
utaratibu wa Polisi Jamii (Community Policing) uweze kufanyika kwa
mafanikio, Wizara yangu inaandaa mkakati maalum kwa lengo hilo. Mkakati huo pia utaelekeza namna ambavyo
Polisi Kata atashirikiana na Vikundi vya Ulinzi wa Jadi katika utekelezaji wa
utaratibu wa Polisi Jamii. Suala la kutoa
elimu ya Polisi Jamii kwa wananchi na Polisi wenyewe nalo litapewa
kipaumbele. Elimu hii ni muhimu sana ili
kuondoa migongano baina ya wananchi na Polisi ambayo inaweza kujitokeza wakati
wa utekelezaji.
i. Kushirikiana na Idara Nyingine za Serikali
83. Mheshimiwa
Spika, Serikali inatambua mchango wa vyombo vingine vya dola katika suala
zima la ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Hivyo, Wizara inakusudia kukuza na kuendeleza ushirikiano uliopo hivi
sasa baina ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vikiwemo Idara ya
Usalama wa Taifa, Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania,
pamoja na wadau wengine muhimu, hasa
katika ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia na kufanya operesheni za
pamoja.
j. Kutoa
Ushauri wa Kiusalama Kwa Taasisi za
Fedha
84. Mheshimiwa Spika, ni jukumu la
Jeshi la Polisi kutoa ushauri wa kiusalama kwa taasisi mbalimbali za kibiashara
kama vile mabenki juu ya namna bora ya kuimarisha mifumo ya ulinzi katika
maeneo yao. Kwa hivi sasa Jeshi la Polisi linaendelea kuwasiliana
na Benki Kuu kuhusu kuweka utaratibu wa kisheria wenye lengo la kuwalazimisha
wamiliki wa benki na taasisi za fedha nchini kuweka mifumo ya kisasa ya ulinzi katika benki zao kama CCTV Cameras
kwa lengo la kudhibiti uporaji wa fedha katika taasisi hizo.
k. Taratibu
za Ajira
85.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwepo kwa mapungufu katika zoezi
la ajira ya askari Polisi, Wizara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi
inachambua taratibu za ajira zinazotumika sasa ili kubuni utaratibu bora zaidi wa ajira.
l. Upandishwaji
Vyeo
86.
Mheshimiwa Spika, upandishwaji vyeo ndani ya Jeshi la Polisi
unapaswa kufanyika kwa mujibu wa maelekezo yaliyopo kwenye Taratibu za Kudumu
za Polisi (Police General Orders). Hata
hivyo, kwa kuwa yamejitokeza malalamiko miaka ya hivi karibuni kuhusiana na upandishwaji vyeo hasa kwa askari wa vyeo vya
chini, Wizara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inaangalia upya utaratibu
uliopo, iwapo bado unafaa au umepitwa na wakati ili askari wapandishwe vyeo
kulingana na sifa na utendaji kazi.
m. Msongamano
wa Wafungwa na Mahabusu
87. Mheshimiwa Spika, kwa kuelewa tatizo la
msongamano wa mahabusu katika magereza yetu na kwa kutambua kwamba msongamano
huo wakati mwingine unasababishwa na utendaji usioridhisha wa baadhi ya askari
wa Jeshi la Polisi, Makamanda wa Polisi wa Mikoa wameelekezwa kushirikiana na
wenzao wa Jeshi la Magereza katika kuendesha zoezi la kukagua magereza kwa
lengo la kuelewa sababu za watuhumiwa
kuendelea kukaa ndani na ucheleweshaji wa kesi zao.
88. Mheshimiwa Spika, itakapodhihirika hakuna
sababu za msingi za kuendelea kukaa magerezani, taratibu za kisheria
zitafuatwa ili mahabusu hao waachiwe ama
kwa dhamana au kwa kesi zao kumalizika haraka iwezekanavyo. Zoezi hili litaenda
sanjari na uendeshaji wa mara kwa mara wa vikao vya Kamati za Kusukuma Kesi
Nchini.
89. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itawasiliana
na Wizara za Katiba na Sheria, na Mambo ya Ndani ya Nchi kwa lengo la kuweka
utaratibu ambao Maafisa wa Polisi, Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Majaji
Wafawidhi wa Kanda husika na Mahakimu Wakazi wataenda magerezani kuwasikiliza mahabusu
na kufanya uamuzi wa haraka kwa mujibu wa sheria. Lengo ni kushirikiana na wizara hizo kupunguza
msongamano wa mahabusu magerezani, hasa
kwa kesi ndogo ndogo.
n. Udhibiti wa Silaha Ndogo Ndogo
90. Mheshimiwa Spika, ujambazi wa kutumia
silaha nchini bado ni tatizo kubwa ambalo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na
tatizo la kuzagaa silaha. Hivyo, pamoja na juhudi na mikakati mingine, Jeshi la
Polisi litazikagua, kuziorodhesha
na kuzisajili upya silaha zote za kiraia nchini ili kuhakiki umiliki na
matumizi yake. Zoezi kama hili pia
litafanyika kwa silaha ndogo ndogo zinazomilikiwa na Taasisi/Idara za Serikali
ili hatimaye ziwepo kumbukumbu za silaha zote ndogo ndogo nchini na udhibiti
wake uweze kuwa rahisi.
91. Mheshimiwa Spika, sanjari na uhakiki huu wa miliki ya silaha na
risasi, yanafanyika mapitio ya Sheria ya umiliki wa silaha ili hatimaye ifanyiwe marekebisho kwa lengo la
kuongeza udhibiti wa silaha na risasi. Katika marekebisho hayo, suala la
utengenezaji na miliki ya Magobore litaangaliwa kwa lengo la kuyapiga
marufuku. Uzoefu umeonyesha kwamba watengenezaji na wamiliki wanakiuka taratibu
za utengenezaji, umiliki na matumizi ya silaha hizo. Kwa mfano, sasa hivi Magobore mengi
yanayotengenezwa yanatumia risasi za kisasa kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Vile vile sheria za Kimataifa zimekwishapiga
marufuku utengenezaji na umiliki wa silaha za aina hii.
92. Mheshimiwa Spika, udhibiti na
utaratibu wa magobore unafanywa na Halmashauri za Wilaya/Manispaa chini ya sheria
ndogo ya ‘Arms and Ammunition Native Authorities Regulations’ iliyo
chini ya Sheria za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Chini ya sheria hii, Halmashauri za Wilaya
ndizo zinazotoa leseni za kutengeneza magobore, kuweka alama au namba kwenye
magobore yanayotengenezwa na kuwatoza kodi watengenezaji na wamiliki wa
magobore.
93. Mheshimiwa Spika, kazi hii itaenda
pamoja na juhudi za makusudi za kuendesha misako ya mara kwa mara kuhakikisha
kuwa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria zinakamatwa pamoja na wamiliki wa
silaha hizo kama moja ya mikakati ya kupunguza ujambazi nchini.
o. Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi
94. Mheshimiwa
Spika, katika jitihada za kuzuia uhalifu nchini, Jeshi la Polisi
linatarajia kujenga ubia na sekta binafsi. Lengo ni kuwahamasisha wafanya
biashara wakubwa, makampuni binafsi, taasisi na mashirika mbalimbali kuchangia
na kutunisha mfuko wa Ulinzi wa Umma ambao tayari umeshaanzishwa na
Jeshi la Polisi. Hili limeanza kufanyika kwa Benki ya CRDB kuchangia
fedha kwa ajili ya kufungua akaunti Makao Makuu ya Polisi pamoja na Mikoani kwa
ajili hiyo.
95. Mheshimiwa
Spika, hivi karibuni Jeshi la Polisi limepokea michango mbalimbali ya
vitendea kazi na fedha taslimu toka kwa Kampuni za Ulinzi za Ultimate
Security Ltd, Vodacom, Kampuni ya Simu ya Alphatel, Umoja
wa Kampuni za Ulinzi Nchini, Riki Hill Hotel, Kampuni ya CMC Motors,
Kampuni ya Sigara nchini (TCC) pamoja na wafanyabiashara mbalimbali. Napenda kutumia fursa hii kuyashukuru
makampuni haya na watu wote waliochangia.
Ninatoa wito kwa sekta binafsi kwa ujumla, kuchangia mfuko huo kwa lengo
la kuunganisha nguvu za Serikali pamoja
na za sekta binafsi katika kukabiliana na uhalifu nchini.
96. Mheshimiwa Spika, vitendea kazi
vilivyopokelewa ni pamoja na magari, pikipiki, simu za mkononi na simu za upepo.
Mawasiliano yatafanyika na taasisi zinazohusika ili kuandaa taratibu madhubuti za
matumizi ya fedha zinazopatikana kwenye mfuko huu.
97. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu imekuwepo
dhana kwamba kazi ya kudhibiti uhalifu na ujambazi ni jukumu la Serikali au
Jeshi la Polisi peke yake. Mtazamo huu
siyo sahihi. Kudhibiti uhalifu, na hasa
wakati huu wa utandawazi ni lazima kuishirikisha sekta binafsi, wafanyabiashara
na wananchi wote kwa ujumla wao.
98. Mheshimiwa Spika, Mzee Nelson Mandela
alipokuwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini aliwahi kusema, na
ninamnukuu :
|
|
«The business
sector could make a valuable contribution in supporting Government in
combating crime and the causes of crime by transfer of knowledge and the
development of skills and capacity through a public - private
partnership » mwisho wa
kunukuu. |
|
99. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi
limefungua milango kwa sekta binafsi na wananchi na kuwa wazi katika kuandaa
mikakati ya ushirikiano wa hali na mali baina yao ili kwa pamoja watokomeze
vitendo vya uhalifu. Tayari baadhi ya Mikoa kama vile Dar es Salaam,
Arusha na Mbeya imekwishajitokeza kuchangia juhudi za Polisi. Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Mikoa
hiyo. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa mingine kushirikiana
na sekta binafsi kuanzisha programu ya kupambana na wahalifu na hivyo kuwa
karibu na Wakuu wa Polisi wa Mikoa yao katika kubuni mikakati na kuitekeleza.
100. Mheshimiwa Spika, ili kuufanya utaratibu
huu wa sekta binafsi kuchangia shughuli za Polisi uwe endelevu na wa kisheria,
Wizara yangu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inawasiliana na Wataalamu wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili waweze kushauri namna ya kuufanya mfuko huu
kuwa endelevu na wa kisheria.
p. Udhibiti wa Simu za Mkononi
101. Mheshimiwa Spika, mawasiliano ya simu
za mkononi yanachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la matukio ya uhalifu nchini,
kwa kuwa simu hizo zimerahisisha mawasiliano kufanyika wakati wowote, mahali
popote na kwa haraka zaidi. Wahalifu
wameweza kutumia njia hii ya mawasiliano na kufanikiwa kufanya uhalifu bila
kugundulika kwa urahisi.
102. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu imekwishaanza kushauriana na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini
pamoja na makampuni yote ya simu za mkononi, ili kuhakikisha unakuwepo udhibiti
wa simu zote za mkononi, ambapo wamiliki wote wa simu watasajiliwa na
kuondokana na utaratibu wa sasa wa kuuza namba za simu (line) kiholela.
Utaratibu huu una lengo la kuweka kumbukumbu za wamiliki wote wa simu ili iwe
rahisi kuwapata pindi wanapohitajika.
q. Askari Polisi Kutokaa Katika
Kituo Kimoja Muda Mrefu
103. Mheshimiwa
Spika, kazi za kupambana na uhalifu na wahalifu zinahitaji kufanywa
kwa uadilifu mkubwa ili kuepuka uvujaji
wa taarifa. Ili lengo hili lifanikiwe unahitajika mkakati utakaohakikisha
kwamba askari Polisi hawakai kituo kimoja muda mrefu na kuzoeleka. Jeshi la
Polisi litaendelea kufanya uhamisho mara kwa mara wa askari wote, ili kudumisha
nidhamu na kuboresha utendaji kazi.
r. Kuboresha Maslahi ya Askari
104. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge na
wananchi ni mashahidi wa juhudi kubwa zinazochukuliwa na Amiri Jeshi Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete katika
kuboresha maslahi ya askari na kuwapatia vitendea kazi. Kupitia Bunge lako Tukufu, napenda nimshukuru
pia Mhe. Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma kwa kuliangalia suala la mishahara ya watumishi wa umma pamoja
na Askari Polisi ambapo mishahara yao
imeongezwa.
105. Mheshimiwa
Spika, kutokana na kipato kidogo cha askari Polisi, inawawia vigumu kukopa
katika mabenki nchini kutokana na riba
kuwa kubwa na kukosa dhamana za uhakika.
Hivyo, askari Polisi hawana mahali popote wanapoweza kupata fedha za kujiendeleza
kiuchumi. Aidha, mishahara na posho wanayolipwa askari bado haikidhi hali
halisi ya mahitaji yao na familia zao.
106. Mheshimiwa Spika, ili kupunguza ukali wa
maisha kwa askari, Maduka ya Polisi yenye utaratibu wa kuwakopesha askari
mahitaji muhimu (Kantini) yatafufuliwa na kusimamiwa kwa karibu ili yaweze
kutoa mikopo midogo midogo na huduma nyingine muhimu kwa askari na familia zao.
Aidha, Serikali itaendelea kuwadhamini askari
na watumishi wengine wa Wizara kupata mikopo kutoka Benki kama vile CRDB,
NMB, AZANIA BANCOP, BENKI YA POSTA na makampuni binafsi, kama vile TUNAKOPESHA Limited n.k.
107. Mheshimiwa Spika, ili kujenga utamaduni wa askari kujiwekea akiba
kwa njia ya kuweka na kukopa, inatarajiwa kuanzishwa Chama cha Kuweka na Kukopa (SACCOS) cha Wizara ambacho askari Polisi watajumuika na watumishi
wengine kukopa kwa masharti nafuu. Mikopo hii itawasaidia askari kustaafu kwa heshima wakiwa
na makazi yao na hali nzuri ya maisha.
108. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za
kuboresha maslahi ya askari, Serikali ilipandisha kiwango cha posho ya resheni
kutoka Sh.28,000 kwa mwezi kuwa Sh.50,000. Aidha, askari wanaidai Serikali Sh. bilioni
8.5 zikiwa ni stahili mbali mbali kama posho za safari nk. Baada ya mazungumzo
kati yangu na Wizara ya Fedha, deni hili litalipwa katika mwaka huu wa fedha ili kuondoa kero
hiyo ya muda mrefu na askari hao kupata stahili zao.
109. Mheshimiwa Spika, zaidi ya askari 18,000
wa Jeshi la Polisi wanaishi nje au ndani ya makambi katika mazingira ya
makazi yasiyofaa. Baadhi ya askari
wanaishi katika nyumba za kupanga uraiani. Hali hii huathiri utendaji wao wa kazi kwa
kiasi kikubwa. Jitihada zinafanyika ili kuhakikisha kwamba askari Polisi wote
wanaishi kambini katika mazingira ya kuridhisha. Wizara yangu inafanya mazungumzo na Mifuko
ya Fedha ya NSSF na PPF na Wizara ya
Fedha kwa lengo la kuanzisha mradi wa
ujenzi wa nyumba za Polisi nchini kote.
Kwa kuanzia ujenzi utafanyika Dar es Salaam na Zanzibar.
110. Mheshimiwa
Spika, katika kujali afya za askari, hivi sasa yanafanyika mazungumzo na Bima
ya Afya ili askari Polisi nao wajumuishwe katika mpango huo. Awali askari
Polisi hawakuwa wamejumuishwa katika Bima ya Afya kama ilivyo kwa
watumishi wengine. Mawasiliano na Mfuko
wa Bima ya Afya tayari yameshaanza na mweleko ni mzuri. Baada ya taratibu zote kukamilika, askari
Polisi na familia zao watanufaika kutokana na kupata matibabu wakati wote.
111. Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Askari ni
mahali ambapo askari hupata fursa ya kueleza kwa viongozi wao, matatizo mbali mbali yanayowakabili. Hivyo, Makamanda wote wa Mikoa, Vikosi na
Wilaya wameelekezwa kuhakikisha kwamba Mabaraza hayo yanafanyika ipasavyo kwa
malengo yaliyokusudiwa. Kila Kamanda wa
Mkoa, Kikosi na Wilaya ahakikishe kwamba Baraza la Askari linafanyika walau
mara moja kwa mwezi, na askari wanapata fursa kamili ya kueleza matatizo yao.
s. Kuwapatia Mafunzo askari wa
Vyeo vya Chini na Maofisa
112. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeandaa
mpango wa mafunzo kazini ambapo askari watapatiwa mafunzo na mbinu mbali mbali
za utendaji kazi. Hivi sasa walimu wa
mafunzo hayo wako chuoni CCP Moshi wakipata mafunzo ili nao waweze kuwafundisha
askari wenzao waliopo kazini. Aidha,
unaandaliwa utaratibu ili walimu kutoka nje ya nchi waje kuwafundisha askari
hapa nchini ili kupata askari wengi
zaidi wenye ujuzi. Aidha, Wizara yangu
imeandaa mpango wa mafunzo ya uongozi wa askari wa vyeo vya juu wakiwemo
Makamanda wa Mikoa ili kuwaongezea ujuzi kuhusu dhana ya menejimenti na ufahamu
wa sera za maboresho mbalimbali yanayofanyika hapa nchini.
113. Mheshimiwa
Spika, ili kuimarisha maendeleo ya Jeshi la Polisi Mikoani, Makamanda wa
Mikoa watashirikishwa kikamilifu katika kupanga mipango na maboresho ya Mikoa
yao na kushirikishwa katika mipango ya maboresho. Matarajio ni kwamba, kila Kamanda wa Mkoa ataweza kuandaa na kuitetea
bajeti yake, ikiwa ni pamoja na kusimamia matumizi mazuri ya raslimali.
UTEKELEZAJI WA
BAJETI YA 2005/06
114. Mheshimiwa Spika, naomba sasa kutoa
tathmini ya utekelezaji wa malengo ya Jeshi la Polisi katika kipindi cha mwaka 2005/06. Kwa ujumla utekelezaji wa malengo ya
mwaka 2005/06 ulikuwa wa mafanikio. Hali halisi ya utekelezaji kwa maeneo
muhimu ilikuwa kama ifuatavyo:
115. Mheshimiwa
Spika, Jeshi la Polisi lilikadiria kukusanya mapato ya Serikali ya jumla ya
Sh.4,247,940,000 kwa mwaka 2005/06.
Hadi kufikia Aprili, 2006, Jeshi lilikuwa limekusanya jumla ya Sh. 3,825,584,105
sawa na asilimia 90 ya lengo la mwaka mzima. Hadi tarehe 31 Mei, 2006 Wizara ilivuka lengo
lililowekwa kwa kiasi cha Shilingi 10,563,419.21.
116. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi liliidhinishiwa
jumla ya Sh. 102,161,080,300 kwa matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Hadi kufikia Aprili, 2006, jumla
ya Sh. 91,860,947,158 zilikwishatumika ikiwa ni sawa na asilimia 90
ya lengo la mwaka. Kati ya fedha hizo Tsh. 58,449,119,797 ni Matumizi
Mengineyo, Tsh. 30,782,827,361 ni Mishahara na Tsh. 2,629,000,000
ni za Matumizi ya Bajeti ya Maendeleo.
a.
Ujenzi wa nyumba 124 kati ya 131
katika Kambi
ya Kunduchi umekamilika.
b. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa maabara ya
kisasa ya uchunguzi (Forensic Laboratory) imekamilika. Ujenzi wa awamu ya pili ulikwishaanza na bado
unaendelea.
c.
Ujenzi wa Kituo cha Polisi Katesh – Hanang
upo katika hatua za mwisho.
d. Ujenzi wa mabweni mawili Kambi ya FFU
Finya Pemba umekamilika.
e. Ukarabati wa mabweni
mawili Chuo cha
Polisi
Dar es Salaam umekamilika.
f Mashua
mbili za doria zimenunuliwa kwa ajili ya ukanda wa Bahari ya Hindi. Mashua moja
iko Unguja na nyingine iko Dar es Salaam.
g. Ujenzi wa Ofisi za
Makamanda wa Polisi
wa Mikoa uko katika hatua mbali mbali katika
mikoa ya Tabora, Ruvuma, Mwanza na Iringa.
h. Ujenzi wa Kituo
cha Polisi Morogoro
upo
hatua za mwisho.
i. Ukarabati
wa
Chuo cha Polisi
Zanzibar
unaendelea.
j. Mafunzo ya askari wapya 2000
yameendeshwa na yalimalizika tarehe 21 Aprili, 2006. Mafunzo kazini yanaendelea
kufanyika.
k. Doria na Operesheni
mbalimbali za Polisi
zilifanyika Kiwilaya,
Kimkoa, Kitaifa na Kimataifa ambapo nchi tatu za Afrika Mashariki zilishiriki.
l.
Mawasiliano ndani ya Jeshi la Polisi
yaliendelea kuimarishwa kwa ununuzi wa mitambo, simu n.k.
m.
Mkutano wa
Maofisa wa Polisi ulifanyika CCP
Mjini Moshi kwa mafanikio makubwa, ambapo mikakati mbali mbali ya utendaji
iliwekwa na sasa inaendelea kutekelezwa .
n.Kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya dola, Jeshi la Polisi lilifanikisha Uchaguzi
Mkuu mwezi Desemba, 2005 kwa amani na utulivu.
VITA DHIDI YA UKIMWI
118. Mheshimiwa
Spika, juhudi za kupambana na janga la ukimwi ndani ya Jeshi la Polisi
zimeendelea kwa mwaka uliopita ikiwa ni pamoja na kuendesha semina tatu za
uelimishaji zilizohusisha Maofisa, askari na wakufunzi. Juhudi hizi
zitaendelezwa mwaka wa fedha wa 2006/07.
MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
119. Mheshimiwa Spika, Jeshi la
Polisi limeendeleza vita dhidi ya rushwa
ndani na nje ya Jeshi. Mafunzo mbali mbali kwa maafisa na askari wa
kawaida yameendeshwa nchi nzima ambapo wadau mbali mbali wa mapambano dhidi ya
rushwa walishirikishwa. Hatua za
kinidhamu zimeendelea kuchukuliwa dhidi ya askari/maofisa wanaojiingiza katika
vitendo vya rushwa au kuvunja maadili ya kazi zao.
120. Mheshimiwa Spika, pamoja na
mafanikio yaliyotajwa, baadhi ya matatizo yaliyoathiri utekelezaji ni pamoja na
haya yafuatayo:
a. Ufinyu wa bajeti kwa kiasi kikubwa umeathiri
utekelezaji wa mipango mbali mbali ya Jeshi
na hivyo kutofanya kazi kwa ufanisi na tija kama inavyotarajiwa.
b. Upungufu
wa vitendea kazi kama vile magari, pikipiki, vifaa vya mawasiliano, mbwa,
farasi, karatasi, vifaa vya kunasia sauti, Fomu mbali mbali, mfano PF.3 n.k.
c. Upo upungufu mkubwa wa nyumba za kuishi
askari. Zaidi ya askari 18,000 wanaishi nje ya Makambi katika nyumba za kupanga
uraiani na wengine wanaishi katika mazingira magumu sana makambini.
d. Upo
upungufu mkubwa wa vituo vya Polisi katika wilaya mbali mbali nchini, ambapo
Wilaya 24 hazina kabisa vituo vya Polisi. Aidha, katika wilaya 73
Vituo vya Polisi vipo kwenye majengo chakavu, ambapo baadhi yalirithiwa kutoka kwa
wakoloni.
e. Upo upungufu wa askari unaochangiwa na
askari kustaafu, kuacha kazi, kufukuzwa kazi, kufariki n.k.
121. Mheshimiwa
Spika, changamoto zinazolikabili Jeshi la Polisi ni nyingi. Ni azma ya
Serikali kuendelea hatua kwa hatua kulipunguzia matatizo na kulipatia mahitaji
Jeshi la Polisi ili kulijengea uwezo wa kukabiliana na uhalifu nchini.
122. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2006/07, Wizara inatarajia
kutekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-
a.
Kuandaa Sera
ya Usalama wa Raia na kusimamia utekelezaji wake.
b.
Kuandaa Muundo
mpya wa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kutazama upya Sheria na Kanuni za
Jeshi hilo.
c.
Upatikanaji wa
Ofisi na Makazi kwa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam.
d.
Kuboresha
maslahi ya askari
e.
Kuboresha
mazingira ya kufanyia kazi, upatikanaji wa vitendea kazi na miundombinu.
f.
Kuwapatia
askari mafunzo mbali mbali ya taaluma zao na ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora na Kuimarisha Vyuo vya Polisi vya Moshi, Dar es Salaam na Zanzibar na
kuanza maandalizi ya ujenzi wa chuo cha CID Dodoma.
g.
Kwa
kushirikiana na Mifuko ya Fedha nchini na Makampuni kutoka nje ya nchi, itaanzishwa
Programu ya ujenzi wa Makambi nchini kote, kwa kuanzia nyumba za Kambi ya Barabara
ya Kilwa, Dar es Salaam na Ziwani Zanzibar.
h.
Jeshi la
Polisi kuendelea kushiriki kikamilifu katika maboresho ya Sekta ya Sheria (Legal
Sector Reform Programme).
i.
Kuharakisha
upelelezi wa kesi ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka na hivyo kupunguza
msongamano wa mahabusu katika magereza.
j.
Kupambana na
uhalifu kwa kubuni mbinu na mikakati ya kisasa maeneo ya mijini, vijijini, mipakani
na katika maeneo ya kitalii.
k.
Kuendeleza
miradi ya maendeleo katika mikoa na Wilaya na ukarabati wa majengo ya Ofisi.
123. Mheshimiwa Spika, kabla ya
kumalizia hotuba yangu naomba kutoa shukrani za pekee kwa Naibu Waziri wa
Usalama wa Raia, Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Usalama wa Raia Bwana Bakari A. Mahiza, Inspekta Jenerali wa Polisi Bwana Said
A. Mwema, Wakuu wa Idara, Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Askari na wafanyakazi
wa Wizara ambao kwa ushirikiano wao wamewezesha hotuba hii kuandaliwa na
kukamilika katika wakati unaotakiwa. Aidha, napenda kumshukuru Mpiga Chapa Mkuu
wa Serikali Bw. Cassian Chibogoyo kwa kufanikisha uchapaji wa hotuba hii.
124. Mheshimiwa
Spika, napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa wahisani wote ambao
misaada yao imeiongezea nguvu Wizara yangu katika kutekeleza baadhi ya majukumu
yake. Wahisani hao ni
pamoja na Serikali za Jamhuri ya Watu wa China, Marekani, Afrika
Kusini, Misri na Uingereza.
125. Mheshimiwa Spika, napenda pia
kuyashukuru Mashirika ya Kimataifa ya INTERPOL,
SAFER AFRICA, UNDP na EU
na wafadhili wa hapa nchini ikiwa ni pamoja na Kampuni ya Ulinzi ya Ultimate
Security Ltd, Kampuni ya Simu ya Alphatel, Vodacom, Umoja wa
Kampuni za Ulinzi hapa nchini, Riki Hill Hotel, CMC Motors, Kampuni
ya Sigara (TCC) wafanyabiashara pamoja na wote ambao kwa njia moja au
nyingine wanaendelea kuisaidia Wizara ya Usalama wa Raia.
126. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukrani
za pekee kwa nchi wahisani za Canada, Sweden, Denmark na Belgium
na Mashirika ya UNDP na WB ambao wamechangia fedha kwenye mfuko (
Basket Funding) wa kutekeleza
programu ya maboresho ya Sekta ya Sheria (Legal Sector Reform Programme) ambapo
Wizara yangu ni mdau katika sekta hiyo. Jeshi la Polisi litanufaika na programu
hii katika maeneo ya mafunzo, kuimarisha upelelezi, marekebisho ya sheria,
uboreshaji mazingira ya kazi n.k.
127. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya,
sasa naliomba kwa heshima na taadhima Bunge lako Tukufu likubali kupitisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Usalama wa Raia ya jumla ya shilingi
142,908,007,300 kwa mwaka wa fedha wa 2006/07 kama ifuatavyo:-.
FUNGU 28: WIZARA YA
USALAMA WA RAIA
|
|
SH. |
|
Mishahara (PE) |
52,728,751,000 |
|
Matumizi Mengineyo
(OC) |
82,826,000,000 |
|
Matumizi ya
Maendeleo |
7,353,256,300 |
|
Jumla |
Sh.
142,908,007,300 |
128. Mheshimiwa
Spika, nakushukuru wewe binafsi pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa
kunisikiliza.
129.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.