HOTUBA YA WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA MASOKO MHE. NAZIR MUSTAFA KARAMAGI (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MATUMIZI YA  FEDHA KWA MWAKA 2006/2007

 

A.      UTANGULIZI

 

Mheshimiwa Spika,

1.       Kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara iliyochambua bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kwa mwaka 2006/07.

 

Mheshimiwa Spika,

2.                 Awali ya yote napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kwao kwa ushindi mkubwa wa kishindo.  Aidha, nampongeza kwa namna ya kipekee Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Kitaifa.  Napenda pia, kumpongeza Mhe. Amani Abeid Karume kwa kuchaguliwa kwake kwa kipindi cha pili kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Vile vile, nampongeza Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.), kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mbunge na hatimaye kuteuliwa na kuthibitishwa na Bunge kwa kura nyingi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

3.                 Aidha, napenda kukupongeza wewe mwenyewe Mheshimiwa kwa kuchaguliwa kwako kwa kura nyingi kuwa Spika na Mhe. Anna Makinda (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika katika Bunge la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawapongeza pia Mawaziri wenzangu wote pamoja na Manaibu Waziri kwanza kwa kuchaguliwa kuwa Wabunge na pili kwa kuteuliwa kwao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Vile vile, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Uwekezaji na Biashara ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. William Shellukindo (Mb.), kwa kutupatia ushauri na maelekezo wakati wa kujadili muhtasari wa hotuba hii.  Aidha, ninawashukuru wale wote tulioshirikiana nao katika maandalizi ya Hotuba hii ninayowasilisha leo. Mwisho napenda niwapongeze Wabunge wote kwa kuchaguliwa au kuteuliwa kwao kuingia katika Bunge hili Tukufu.  Aidha, mimi pamoja na Naibu waziri Mhe. Dkt. David Mathayo David (Mb.), tunawashukuru kipekee wapiga kura wa Majimbo yetu waliotuwezesha kuwa miongoni mwa Wabunge katika Bunge lako Tukufu.

 

Mheshimiwa Spika,

4.                 Napenda kuchukua nafasi hii kuwapa pole Waheshimiwa Wabunge waliopata mikasa ya kufiwa na jamaa zao.  Tunaomba Mungu awape faraja na azilaze roho za marehemu mahali pema peponi – Amina.

 

B.                 MAJUKUMU NA MUUNDO WA WIZARA

 

Majukumu

 

Mheshimiwa Spika,

5.                 Majukumu ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko yamezingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa (National Development Vision 2025) ambayo imeweka bayana kwamba sekta za Viwanda, Biashara na Masoko ndiyo ziwe mihimili mikuu ya kuuwezesha uchumi wa nchi yetu kukua na kufikia kiwango cha kati cha Maendeleo ya uchumi wa Viwanda. Majukumu ya msingi ya Wizara ni pamoja na:-

a)                  Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera za kuendeleza sekta za Viwanda, Biashara na Masoko;

b)                  Kuandaa mipango na mikakati ya kushirikisha na kuimarisha Sekta Binafsi katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia uendelezaji wa uwekezaji katika sekta za Viwanda, Biashara na Masoko;

c)                  Kusimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko;

d)                  Kusimamia utekelezaji wa mikakati mahsusi ya uendelezaji wa mauzo ya mazao na bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje;

e)                  Kubaini na kutekeleza mikakati ya kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na nchi nyingine ili kuhakikisha kwamba Taifa linapata manufaa kwa kiwango cha juu hususan kupitia sekta ya Viwanda, Biashara na Masoko; na

f)                    Kuimarisha uwezo wa Wizara na Asasi zilizo chini yake ili kutekeleza majukumu yake kwa kiwango cha ufanisi wa hali ya juu.

 

Muundo

 

Mheshimiwa Spika,

6.                 Kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Awamu ya Nne, sekta ya Masoko imeunganishwa na sekta za Viwanda na Biashara na kuunda Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko.  Kwa hiyo, muundo mpya wa Wizara sasa una Idara nne zenye majukumu muhimu ya kisekta na Idara mbili za huduma na uratibu. Idara za majukumu kisekta ni Idara ya Viwanda, Idara ya Biashara ya Kimataifa, Idara ya Maendeleo ya Masoko na Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo. Idara za huduma na uratibu ni Idara ya Utawala na Utumishi na Idara ya Sera na Mipango. 

 

Ushirikiano na Sekta Binafsi

 

Mheshimiwa Spika,

7.                 Wizara inashirikiana kikamilifu na Sekta Binafsi kwa kuzingatia azma ya Serikali kwamba Sekta Binafsi ndio mhimili mkuu katika kutekeleza majukumu yake mbalimbali ya uwekezaji na biashara katika mkakati mzima wa kukuza uchumi na kuondoa umaskini.  Baadhi ya taasisi zinazoshirikiana na Wizara yangu ni Tanzania Private Sector Foundation - TPSF, Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture - TCCIA, Confederation of Tanzania Industries – CTI pamoja na Asasi Zisizo za Kiserikali – AZISE. Aidha, hushiriki katika mikutano ya kila mwaka inayoshirikisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na kupata michango yao kuhusu mikakati mbalimbali ya kuendeleza viwanda, biashara na masoko.  Mkutano huu wa pamoja hufanyika chini ya utaratibu wa Baraza la Taifa la Biashara ambalo Mwenyekiti wake ni Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ya viwanda huandaa maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya maendeleo ya viwanda barani Afrika kila mwaka tarehe 20 Novemba ambapo hujumuika na Sekta binafsi kutafakari mikakati ya kuharakisha maendeleo ya viwanda nchini. 

 

C.      UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CHAMA TAWALA KATIKA KIPINDI CHA MIEZI SITA

 

Mheshimiwa Spika,

8.                 Wakati tukiendelea kutekeleza mpango wa MKUKUTA, uongozi wa Serikali ya awamu ya nne ulipoingia madarakani, Wizara yangu ilioanisha MKUKUTA na utekelezaji wa ahadi za Chama Tawala (CCM) zilizobainishwa katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005.

 

Mheshimiwa Spika,

9.                 Ilani ya Chama Tawala imebainisha wazi kinachotakiwa kufanyika katika sekta zinazosimamiwa na Wizara yangu ili kuleta maendeleo katika nchi yetu.  Katika sekta ya Viwanda, Ilani imeelekeza kuwa ifikapo mwaka 2010 kiwango cha ukuaji wa sekta kifikie asilimia 15 kwa mwaka. Hii ni changamoto na hatua muhimu katika mikakati ya kuwezesha kufikia kiwango cha Maendeleo ya kati ya Uchumi na Viwanda ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoonyeshwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa.  Aidha, katika sekta za Biashara na Masoko, Ilani imeelekeza kuandaa mikakati itakayouwezesha uchumi wa Taifa kuhimili ushindani na kulifanya Taifa letu liwe na uwezo madhubuti wa kushiriki na kufaidika katika mfumo wa biashara kwenye masoko ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa katika mazingira ya utandawazi.  Hii inatarajiwa kuwa kichocheo cha kuongeza uwezo wa  uwekezaji na uzalishaji katika uchumi wa ndani kwa kuzingatia fursa zilizopo za malighafi na masoko. Aidha, Ilani imesisitiza kipaumbele kiwekwe katika shughuli za kupanua ajira kwa kuendeleza rasilimali watu na wajasiriamali katika viwango vya viwanda vidogo na biashara ndogo.

 

Mheshimiwa Spika,

10.            Katika kipindi ambacho uongozi wa awamu ya nne umekuwa madarakani, Wizara yangu imeweza kutekeleza yafuatayo kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi:-

a)       Zoezi la kumpata mwekezaji wa Mradi wa Kuzalisha Magadi wa Ziwa Natron limekamilika.  Uzalishaji wa magadi kwa ajili ya matumizi ya mbolea, vioo, madawa na vigae unatarajiwa kuanza mwaka 2008.  Aidha, Mradi unatarajiwa kutoa ajira kwa watu wasiopungua 500;

b)       Maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na mradi wa chuma wa Liganga yamefikia hatua ya kuanza kubainisha wawekezaji;

c)       Teknolojia mbalimbali zinazofaa kutumika vijijini na mijini kwa kurahisisha kazi, kuendeleza viwanda vidogo mijini na vijijini, kuhifadhi na kusindika mazao, pamoja na kuchangia hifadhi ya mazingira zimeendelezwa na taasisi zilizo chini ya wizara.  Teknolojia hizo zinajumuisha yafuatayo:-

·              Ukamilishaji wa maandalizi ya mradi wa wachimbaji wadogo wa madini hadi hatua ya ufungaji wa mitambo Igunga, Tabora;

·              Majembe ya kukokotwa na ng’ombe yapatayo 5,352 katika Mikoa tisa inayojumuisha Mwanza, Kagera, Arusha, Rukwa, Iringa, Dodoma, Singida, Mbeya na Shinyanga yalitengenezwa;

·              Viwanda Vidogo 199 ambavyo vimeajiri watu 406 vilianzishwa;

·              Mafunzo mbali mbali ya ufundi yamefanyika katika kozi 59 kwa washiriki 2,254; kozi nane za usindikaji wa vyakula kwa wajasiriamali 160; utengenezaji wa zana za kilimo na uchukuzi vijijini kwa wajasiriamali 23 pamoja na utumiaji udongo-saruji katika ujenzi wa nyumba bora zenye gharama nafuu vijijini kwa wajasiriamali 10.

·              Mashine ndogo 101 zilitengenezwa katika karakana za Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO); na

·              Jumla ya mikopo 831 yenye thamani ya shilingi milioni 556 ilitolewa   katika Mikoa 11 na kutoa nafasi za ajira kwa watu 4,100.

d)    Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (Copyright Society of Tanzania - COSOTA) cha kulinda maslahi ya wasanii kimejisajili katika taasisi ya kulinda maslahi ya wasanii duniani (International Confederation of Authors and Composers - CISAC). Kwa kujiandikisha huko, muziki  wa Tanzania utalindwa katika nchi mbalimbali ambazo ni wanachama wa CISAC;

e)   Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeanza kutumia sheria mpya (New Company Act No. 12 of 2002) tangu tarehe 1 Machi 2006. Sheria hii inatoa fursa kwa wafanyabiashara kusajili kampuni bila kulazimika kuorodhesha shughuli zote kwenye “Memorandum” kama ilivyokuwa awali. Aidha, wale wanaotaka kubadilisha orodha ya biashara hawawajibiki kwenda mahakamani kama ilivyokuwa awali;

f)    Kituo cha kutoa taarifa za kibiashara kwa wananchi na wadau mbali mbali kuhusu haki za ubunifu kimeanzishwa ndani ya BRELA;

g)      Ujenzi wa tembe bora 5 za ukaushaji wa tumbaku huko Mkoani Ruvuma zimekamilika na tayari zinatumiwa na wakulima;

h)      Viwango vya Ubora vya Taifa 38 vimekamilishwa kwa bidhaa za huduma zikijumuisha nne katika nyanja mbalimbali za uhandisi; 32 za vyakula, kemikali na nguo; na viwili vya ufungashaji; na

i)        Leseni za ubora wa bidhaa saba zenye alama ya “tbs”

zikijumuisha saba kwa viwanda vidogo 21 kwa viwanda vikubwa na 163 kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje.

 

 

D.      UTEKELEZAJI WA MALENGO YA BAJETI YA MWAKA 2005/06

 

Mheshimiwa Spika,

11.            Sehemu kubwa ya bajeti ya mwaka 2005/06 ililenga katika kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania maarufu kwa jina la MKUKUTA. Wizara yangu ilielekeza nguvu katika kuwaongezea uwezo wanaviwanda na wafanyabiashara wadogo kushiriki katika juhudi za kukuza uchumi na kuondoa umaskini wa kipato. Msisitizo uliwekwa katika kuendeleza wajasiriamali kwa kuwawezesha katika nyanja za kiufundi, masoko, mawasiliano na huduma za kifedha hususan vyanzo vya mtaji. Ili kufikia malengo hayo, Wizara yangu ilishirikiana na Taasisi zilizo chini yake na Sekta Binafsi katika kuboresha mazingira wezeshaji katika sekta za Viwanda, Biashara na Masoko.

 

D.1:   Sekta ya Viwanda

 

Mheshimiwa Spika,

12.            Katika kipindi cha mwaka 2005/06, sekta ya viwanda ililenga kufanya yafuatayo: -

 

a)                 Kutekeleza sera na mikakati ya kuendeleza sekta ya viwanda ili kukuza mchango wa sekta katika pato la Taifa;

b)                 Kuendelea kuwaongezea uwezo wanaviwanda na wafanyabiashara wadogo ushiriki wao katika shughuli za kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato;

c)                  Kutoa huduma za kiufundi na kuendeleza ujasiriamali, masoko, mawasiliano na huduma za kifedha kwa ajili ya mitaji;

d)                 Kushirikiana na Taasisi zilizo chini ya Wizara (SIDO, CAMARTEC, TEMDO, TIRDO, TBS na NDC) katika kuendeleza sekta ya viwanda chini ya bajeti ya MKUKUTA; na

e)                 Kushirikiana kwa karibu na wenye viwanda ili kujua matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi.

 

Utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda

 

Mheshimiwa Spika,

13.            Wizara iliendelea na utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda (1996 – 2020) kwa kutekeleza programu mbali mbali ikiwa ni pamoja na awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Viwanda.  Mpango huu unalenga katika kuhamasisha, kuwezesha na kuelekeza wawekezaji binafsi katika kujenga viwanda vya usindikaji wa mazao na bidhaa za kilimo ili kuongeza thamani, nafasi za ajira na kupunguza uharibifu baada ya mavuno.  Mradi wa majaribio wa kusindika matunda ulioanzishwa huko Muheza, Tanga ni mmojawapo wa baadhi ya miradi katika lengo kuu la kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa ndani ya nchi. Kazi nyingine iliyotekelezwa chini ya mpango huu wa awamu ya pili ni kutoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa watu wenye ulemavu ambapo vijana 10 walipatiwa mafunzo hayo yaliyoendeshwa na “Leather Association of Tanzania - LAT”, kwa ushirikiano kati ya Wizara na UNIDO kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha miradi ya kujiajiri wenyewe.

 

Mheshimiwa Spika,

14.            Katika kipindi cha 2005/06, yamekuwepo maendeleo ya kutia moyo katika sekta ya viwanda vya kuyeyusha chuma baada ya Serikali kuzuia uuzaji nchi za nje chuma chakavu kinachoweza kuyeyushwa na viwanda vya hapa nchini. Kutokana na hatua hiyo, viwanda sita vipya vimeanzishwa na kutoa nafasi mpya za ajira kwa wananchi wasiopungua 1,000 na hivyo kuwaongezea kipato na kupunguza umaskini.  Aidha, Wizara imewakutanisha wadau wa sekta ya chuma chakavu kwa lengo la kupata maoni yao na mapendekezo yatakayosaidia katika kukamilisha utaratibu wa kudumu wa biashara ya chuma chakavu. Utaratibu huu unalenga kuhakikisha upatikanaji wa malighafi ya kutosha kwa viwanda vya kuyeyusha chuma na kuuza tu nje chuma chakavu ambacho hatuna uwezo wa kuyeyusha. Vile vile, tathmini ya sekta ya viwanda vya mkonge ilifanyika na mapendekezo kutolewa na wataalam yenye lengo la kukwamua sekta hiyo ambapo yanajadiliwa na Serikali kubainisha hatua za kuchukua.

 

Mheshimiwa Spika,

15.            Wizara pia iliandaa semina za kuhamasisha wamiliki wa viwanda kuhusu masuala ya kuhifadhi na kulinda mazingira katika uzalishaji viwandani ambapo watendaji wakuu viwandani wapatao 30 waliohudhuria semina hiyo walijifunza mengi yenye manufaa ikiwa ni pamoja na Sera ya Mazingira, Sheria ya Mazingira, “Cleaner Production Technology’’, ‘‘Environmental Impact Assessment’’ na ‘‘Environmental Audit”. Aidha, walitoa maoni yao yatakayozingatiwa katika kuandaa miongozo ya kisekta kuhusu mazingira.

 

Mheshimiwa Spika,

16.            Baada ya marekebisho ya Sheria ya Maeneo Huru ya Uzalishaji wa Bidhaa za Kuuza Nje (Export Processing Zone - EPZ) kukamilika na kupitishwa na Bunge tarehe 15 Februari 2006, Wizara imeunda Mamlaka ya EPZ.  Kuhusu upatikanaji wa wawekezaji katika programu ya EPZ katika kipindi cha 2005/06, wawekezaji watano walipewa leseni za uzalishaji (EPZ Operators’ Licence) ambao ni: Tsubasa Renew Car (EA) Ltd, Dar es Salaam; Net Health Ltd, Arusha; Vector Health International Ltd, Arusha; African Packaging International Ltd, Dar es Salaam; na Metrec International Ltd, Dar es Salaam.  Aidha, wawekezaji watatu, Fruit Kin Concentrates Ltd, Kibaha; Net Health Ltd, Arusha; na Vector Health Ltd, Arusha walipewa leseni ya ujenzi wa miundombinu ya EPZ (EPZ Developers’ Licence). Jumla ya mtaji uliowekezwa katika EPZ hadi sasa ni Dola za Kimarekani milioni 121.98.       

 

Mheshimiwa Spika,

 

Ili kubaini hali ya maendeleo ya viwanda nchini, katika kipindi cha mwaka 2005/06, Wizara ilifanya ziara ya kutembelea viwanda katika kanda tatu ambazo ni Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Mashariki ambayo ilisaidia katika kudumisha ushirikiano na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda.  Aidha, ziara hizo zilisaidia kutathimini mafanikio na changamoto zinazokabili viwanda na kuwezesha Serikali kubuni mikakati ya kutatua matatizo na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya viwanda.

 

Mheshimiwa Spika,

17.            Kwa ujumla uwekezaji katika viwanda unaendelea kuongezeka na kutoa nafasi za ajira. Kati ya viwanda vipya vilivyoanzishwa ni pamoja na China Paper Corporation cha Kilimanjaro (ajira 60), Kahama Ginnery and Oil Mill Ltd cha Shinyanga  (ajira 120) na Merchandise Products Group cha Kibaha (ajira 20) na viwanda vingine vya kusindika samaki katika Mikoa ya kanda ya ziwa. Aidha, kati ya viwanda vya zamani vilivyokarabatiwa na kufanyiwa upanuzi ni pamoja na Kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI) ambacho sasa kinaitwa Tanzania Steel Pipes (TSP), Dar es Salaam; Kiwanda cha Nyuzi Tabora (TABOTEX); Tanzania Dairy Ltd, cha Tanga; Tanganyika Instant Coffee (TANICA), Kagera na Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI), Arusha. 

 

 

Mheshimiwa Spika,

18.            Kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Wizara kama nilivyoeleza hapo awali, mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa katika mwaka 2005/06 uliongezeka. Katika kipindi cha mwaka 2005, sekta ya viwanda ilikua kwa asilimia 9 ikilinganishwa na asilimia 8.6 mwaka wa 2004. Mchango wa sekta ya viwanda kwa pato la Taifa kwa mwaka 2005 ulikuwa asilimia 9 ikilinganishwa na asilimia 8.8 mwaka 2004.  Aidha, mauzo ya bidhaa za viwanda nchi za nje yalikuwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 156.1 mwaka 2005 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 110.1 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 41.8.  Ajira katika sekta ya viwanda iliongezeka kufikia watu 88,713 mwaka 2005 kutoka 83,712 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 6 kama ilivyonyeshwa katika Jedwali Na. 2.  Ukiondoa uzalishaji wa nguo, rangi na chuma, uzalishaji wa bidhaa nyingine kama vile nyuzi za katani, ‘‘aluminium’’, mabati, saruji, unga, biskuti, sigara na vinywaji baridi na vikali uliongezeka katika kipindi cha mwaka 2005 ukilinganisha na mwaka 2004 ona Jedwali Na. 1.

 

Mheshimiwa Spika,

19.      Katika kipindi cha mwaka 2005, sekta ya viwanda ilikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa umeme usio na uhakika na gharama kubwa ya nishati; miundombinu duni hususan barabara za vijijini zinakotoka malighafi; kuporomoka kwa thamani ya shilingi kulikochangia kuongezeka kwa gharama za malighafi na vipuri kutoka nje pamoja na gharama kubwa za usafirishaji kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa za petroli. Kama yasingekuwepo hayo matatizo, mchango wa sekta ya viwanda ungekuwa mkubwa zaidi katika pato la Taifa kuliko ulivyokuwa.  Aidha, matatizo haya yanachangia kwa kiwango kikubwa kupanda kwa gharama za uzalishaji na bei za bidhaa hizo kwa mlaji na hivyo kuvifanya viwanda vingi vishindwe kuhimili ushindani katika soko la ndani na nje.

 

D.2:   Sekta ya Biashara

 

Utekelezaji wa Sera ya Biashara

 

Mheshimiwa Spika,

20.            Sera ya Taifa ya Biashara iliyozinduliwa rasmi mwezi Agosti 2003, ina madhumuni ya kujenga uwezo wa Sekta Binafsi, Asasi na Taasisi za Umma katika ushindani wa biashara.  Aidha, Sera ya Taifa ya Biashara inabainisha nyenzo zitakazotumika katika kupanua na kukuza biashara kwa kuzingatia misingi ya kuongeza tija na ushindani katika sekta za uzalishaji mali pamoja na utoaji huduma.  Sera imetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili na vile vile maandalizi yamefanyika ya kuchapisha nakala katika lugha rahisi inayotumia viponzo (Cartoons) ili kutoa ujumbe kwa urahisi na kuwafikia wananchi wengi zaidi. 

 

Mheshimiwa Spika,

21.            Sera ya Taifa ya Biashara imeendelea kutekelezwa kwa kuendesha mafunzo kwa wadau mbalimbali kutoka Wizara, Idara za Serikali, Taasisi na Sekta Binafsi katika jitihada za kuwajengea uwezo wa kuchambua na kushiriki kwa manufaa katika majadiliano ya Kimataifa.  Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Kitengo cha Usimamizi wa Miradi (Project Management Unit – PMU) iliendesha mafunzo maalum ya wiki sita kwa kutumia wataalam kutoka Taasisi ya Biashara Duniani (World Trade Institute).  Mafunzo hayo maalumu yalilenga kuboresha uwezo wa kushiriki majadiliano katika Shirika la Biashara la Dunia (WTO), kwenye maeneo ya kilimo, bidhaa za viwandani, biashara ya huduma, hakimiliki, biashara na uwekezaji na utatuzi wa migogoro ya kibiashara.  Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kwa mwaka wa fedha 2005/06 imefadhili watumishi 24 wa Wizara, Idara za Serikali, Sekta Binafsi na Asasi nyingine kusomea Shahada ya Uzamili ya Biashara ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  Katika mwaka wa fedha 2006/07, jumla ya wanafunzi 26 watajiunga na mafunzo hayo. Lengo la mafunzo hayo ni kujenga uwezo wa wataalam kushiriki katika masuala ya biashara ya Kimataifa ikiwa ni pamoja na kuwaongezea uwezo mahiri katika ujuzi wa mbinu za kushiriki katika majadiliano ya biashara.

 

Mheshimiwa Spika,

22.            Dunia ya sasa ya utandawazi imeegemea sana kwenye Biashara ya Kimataifa.  Kwa kutambua hili, Sera ya Biashara ya Taifa imeweka msukumo madhubuti katika kukuza mauzo ya bidhaa zetu katika soko la nje.

 

Mauzo ya Nje

 

Mheshimiwa Spika,

23.            Kutokana na utekelezaji wa msukumo huu, mauzo nje yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka. Mauzo ya nje yaliongezeka toka Dola za Kimarekani milioni 682.9 mwaka 1995 hadi Dola za Kimarekani milioni 1,549.3 mwaka 2005.  Aidha, kiwango cha ukuaji wa sekta ya biashara kiliongezeka toka asilimia 3.1 mwaka 1995 hadi asilimia 16.5 mwaka 2005, angalia Jedwali Na. 3 na Kielelezo Na. 2.

 

Mheshimiwa Spika,

24.            Katika jitihada za kukuza biashara ya nje, Wizara imewezesha Halmashauri ya Biashara ya Nje (BET) chini ya mpango wa MKUKUTA kuchangia zoezi la kuongeza msukumo wa mauzo ya nje kwa kubuni mikakati mbalimbali. BET ikishirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) iliviunganisha vikundi mbalimbali vya Sanaa za Mikono na kuunda Chama cha Kitaifa cha Sanaa za mikono (Tanzania Handcraft Association – TanCraft).  Katika mchakato huu, yaliandaliwa maonesho ya bidhaa hizo na kuhudhuriwa na wanunuzi wa bidhaa  kutoka Marekani, Canada na Ulaya.  Wanunuzi hawa walipata fursa ya kubainisha mahitaji ya masoko yao na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wajasiriamali wa Tanzania.  Aidha, katika jitihada za kuendeleza na kuongeza uzalishaji wa mazao ya viungo kwa ajili ya soko la nje, BET ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine imeanzisha mpango wa kuendeleza zao la iliki katika Tarafa ya Turiani Wilaya ya Mvomero na mazao ya mdalasini na pilipili manga katika Tarafa ya Mkuyuni Wilaya ya Morogoro Vijijini.  Dhana ya utekelezaji ni ile ya kuwa na “Export Production Villages” ambayo inahimiza aina moja ya zao kuzalishwa katika eneo moja kwa lengo la kuongeza uzalishaji.  Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, kinatoa mafunzo na pia kusambaza mbegu bora kwa wakulima wa mfano bora walioteuliwa ili hatimaye ujuzi huo uigwe na wakulima wengine.

 

Mheshimiwa Spika,

25.            BET imefanikiwa kupata wakufunzi washauri 11 katika mpango wa pamoja wa Taasisi za Afrika Mashariki zinazokuza Biashara ya Nje kwa ushirikiano na Kituo cha Kukuza Uagizaji Bidhaa kutoka Nchi Zinazoendelea (Centre for Promotion of Imports from Developing Countries) cha Uholanzi. Wakufunzi washauri watatumiwa na BET katika programu zake za mafunzo kwa wajasiriamali na makundi mengine.

 

Mheshimiwa Spika,

26.            BET iliratibu ushiriki wa Tanzania katika maonesho mbalimbali ya Kimataifa, kama vile ‘‘Nairobi International Trade Fair’’, ‘‘9th China Investment and Trade Fair’’, ‘‘Rwanda EXPO’’, ‘‘Cairo International Trade Fair’’ na ‘‘Zimbabwe International Trade Fair’’ ambapo BET iliwadhamini wajasiriamali 30 kushiriki maonesho hayo kwa kuwalipia gharama za pango la mabanda pamoja na usafirishaji wa mizigo yao.  Fursa hii inawapa nafasi ya kujua mwenendo wa masoko na mahitaji yake na kujua namna ya kuongeza mauzo katika masoko ya nje.  Katika mwaka wa fedha 2005/06, BET ilikiongezea uwezo kituo chake cha Zanzibar kwa kuwapa vifaa na vitendea kazi kama vile mashine ya “photocopier”, kompyuta, “scanner”, viyoyozi, samani, majarida na kuunganisha mtandao wa mawasiliano katika ofisi.

 

Mheshimiwa Spika,

27.            Katika mkakati wa kutafuta masoko kwa bidhaa zetu, BET ilifanya utafiti wa soko la asali na nta ya Tanzania katika nchi za Oman na Muungano wa Nchi za Falme za Kiarabu.  Utafiti umetoa matokeo mazuri kwa asali hiyo kukubaliwa katika soko hilo na tumepata oda ya tani 30 zenye thamani ya Dola za Kimarekani 45,000.  Taarifa za utafiti huu zimesambazwa katika vijiji vya Mikoa ya Singida na Tabora kwa lengo la kuhamasisha uundaji wa vikundi vya wafuga nyuki ili waweze kutumia fursa za soko hilo la Uarabuni. 

 

Mheshimiwa Spika,

28.            Manunuzi ya bidhaa kutoka nje yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 1,340.5 mwaka 1995 hadi kufikia Dola za Kimarekani  milioni 2,677.8 mwaka 2005.  Kadhalika, manunuzi ya bidhaa kutoka nje yaliongezeka toka asilimia 2.38 mwaka 1995 hadi kufikia asilimia 7.2 mwaka 2005, kama ilivyoonyeshwa katika Jedwali Na. 3 na Kielelezo Na.2.  Katika mwaka 2005, urari wa biashara ya bidhaa ulikuwa na nakisi ya Dola za Kimarekani milioni 985.5, ikilinganishwa na nakisi za Dola za Kimarekani milioni 866.6 mwaka 2004 sawa na asilimia 13.7. Kuongezeka kwa nakisi katika urari wa biashara ya bidhaa kulichangiwa zaidi na ongezeko la thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ikilinganishwa na mauzo ya bidhaa nje. Aidha, urari wa biashara ya huduma ulikuwa na ziada ya Dola za Kimarekani milioni 35.2 mwaka 2005 ikilinganishwa na ziada ya Dola za Kimarekani milioni 151.9 mwaka 2004. Kupungua huko kulichangiwa na ongezeko kubwa la malipo ya huduma, hasa malipo ya gharama za uingizaji mizigo pamoja na safari za nje ikilinganishwa na ongezeko la mapato yaliyotokana na biashara ya huduma.

 

Fursa za masoko ya masharti nafuu kwa nchi zinazoendelea

 

Mheshimiwa Spika,

29.            Kuwepo kwa fursa nyingine za masoko, kutawawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kwa ujumla kuuza bidhaa nyingi na bora. Ili kukuza na kupanua wigo wa biashara baina ya Tanzania na nchi mbalimbali, Wizara yangu ikishirikiana na Sekta Binafsi ilifanya makongamano ya biashara na uwekezaji katika nchi za Falme za Kiarabu, China, Jamhuri ya Korea Kusini, Japan, Vietnam na Urusi. 

 

Mheshimiwa Spika,

30.            Tanzania ilifanikiwa kuingia katika mpango maalum wa “African Growth and Opportunity Act – AGOA” Februari 2002. Mpango huu umewezesha kuvutia wawekezaji hususan katika uzalishaji wa nguo na mavazi.  Kwa sasa waliofanikiwa kushiriki katika mpango huu ni: Sunflag (T) Ltd; Tanzania - China Friendship Textile Mills Ltd; A to Z Textile Mill Ltd; Footlose Ltd na Marvelous Batik. Mpaka sasa Dola za Kimarekani  milioni 12.4 zimepatikana kutokana na mpango wa AGOA. Aidha, fursa nyingine za masoko yenye masharti nafuu ni mfumo unaoruhusu nchi maskini kuuza bidhaa mbali mbali kwenye soko la Ulaya isipokuwa silaha unaojulikana kama “Everything But Arms - EBA”. Vile vile, China, Japan na Canada wanatoa masharti nafuu kwa  nchi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Tanzania. Katika mwaka wa fedha wa 2005/06 kupitia bajeti ya MKUKUTA, BET ilifanya semina katika Mikoa ya Mwanza, Tanga, Morogoro na Arusha ambazo zililenga kuwaelimisha wafanyabiashara katika Mikoa husika juu ya fursa za masoko nafuu yakiwemo ya EAC, SADC, China, AGOA na EBA.  Wafanyabiashara 300 waliweza kunufaika na mafunzo haya muhimu na baadhi wameshaanza kufanya mawasiliano na wanunuzi ili kuweza kufanya biashara. Vile vile, BET imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali 15 katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2005/06 ambayo yanafadhiliwa na taasisi ya Ujerumani iitwayo INWENT.  Mafunzo haya yanalenga kuwafundisha wajasiriamali wa Kitanzania ambao wameonyesha uwezo wa kuuza bidhaa nje juu ya mbinu za kushiriki katika biashara ya Kimataifa.

 

Ushirikiano Kikanda; EAC na SADC

 

Mheshimiwa Spika,

31.            Mwenendo wa biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umekuwa wa kuridhisha kiasi. Mauzo ya Tanzania yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 24.4 mwaka 1997 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 96.4 mwaka 2005. Aidha, manunuzi ya bidhaa yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 97.6 mwaka 1997 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 160.4 mwaka 2005 kama inavyonyeshwa kwenye Jedwali Na. 6 na Kielelezo Na. 5.  Hali kadhalika, katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mauzo yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 22.3 mwaka 1997 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 322.3 mwaka 2005. Aidha, manunuzi yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 139.94 mwaka 1997 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 425.5 mwaka 2005 angalia Jedwali Na. 7 na Kielelezo Na.6.  Tangu kuanza utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 1 Januari 2005, wafanyabiashara wa Tanzania wameanza kutumia fursa hii. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2005/06, BET ilifanya utafiti nchini Kenya kubainisha uwezekano wa kutumia Mfumo wa Maghala (Warehousing Scheme) wenye nia ya kusogeza karibu bidhaa za Tanzania katika soko la Kenya, kuongeza ushindani na kukuza mauzo nje.   Hivi sasa, Jumuiya hii  imeanza matayarisho ya kuingia katika mazungumzo ya awali kwa ajili ya Itifaki ya Soko la Pamoja (Protocol Common Market) na yale ya kuwezesha “Free Movement of Labour” na uwekezaji kuwa huru katika nchi wanachama. Aidha, utafiti wa kina umefanyika kuangalia uwezekano wa kuwa na sarafu moja kwa nchi za Jumuiya.   Pia, kwa ajili ya ushiriki wa Sekta Binafsi, Mkakati wa Maendeleo ya Sekta Binafsi wa Nchi za Afrika Mashariki 2006-2010, umeandaliwa na unasubiri uzinduzi ili uweze kutekelezwa. Kwa upande wa biashara ya kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wizara yangu inaendelea na programu ya ulegezaji wa masharti ya biashara katika Wigo wa Pamoja wa Ushuru wa Forodha (Common External Tariff – CET) ikiwa ni nyenzo za kuendeleza uwekezaji, kukuza uzalishaji na biashara.

 

Mheshimiwa Spika,

32.            Mabadiliko ya kimuundo katika SADC yamewezesha kuanzishwa kwa mpango kamambe wa kimkakati ujulikanao kama ”Regional Indicative Strategic Development Plan – RISDP” kwa ajili ya kuhitimisha azma yake ya kuwa ni chombo cha muungano wa kina, kupunguza umaskini na kuleta maendeleo endelevu. Masuala muhimu yanayoshughulikiwa na nchi zote kwa sasa ni yale ya taratibu za kulinda Afya ya Wanyama, Binadamu na Mimea (Sanitary and Phytosanitary – SPS) na yale ya vizuizi visivyo vya kibiashara “Technical Barriers to Trade - TBT” ili bidhaa katika soko zifikie kiwango cha Kimataifa. Aidha, majukumu yanayosimamiwa na Tanzania yanajumuisha Biashara ya Huduma na Sera ya Uwekezaji na Ushindani.

 

Ushirikiano na nchi za ACP na EU

 

Mheshimiwa Spika,

33.            Majadiliano ya utaratibu mpya wa kudumu wa ushirikiano (Economic Partnership Agreements – EPAs) baina ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific (ACP) na Jumuiya ya Ulaya (EU) yanaendelea.  Mpango huu ni wa kubadilishana fursa za biashara yaani “nipe nikupe” (reciprocity) na unatarajiwa kuanza kutumika ifikapo Januari 2008, kwa misingi ya Mkataba mama wa Cotonuo.  Majadiliano ya kibiashara kati ya SADC na Jumuiya ya Ulaya yanaendelea.  Kwa upande wa SADC, katika majadiliano ya SADC/EPA na EU, Tanzania imepewa jukumu la kuratibu majadiliano hayo katika Biashara ya Huduma na Sera ya Uwekezaji na Ushindani.  Maandalizi haya yanaendeshwa na Serikali ikishirikiana na wadau katika kuweka misimamo ya Kitaifa na Kikanda kuhusu maeneo yote yanayohusika katika majadiliano.

 

Utandawazi

 

Mheshimiwa Spika,

34.            Serikali iliazimia kushiriki kikamilifu katika michakato ya Kimataifa kwa lengo la kuboresha mazingira ya Biashara ya Kimataifa na utandawazi kwa ujumla yakiwamo majadiliano ya Doha. Katika mkutano wa Mawaziri wa biashara wa nchi wanachama wa Shirika la Biashara Duniani uliofanyika Hong Kong, China mwezi Desemba 2005, ilitarajiwa kuwa majadiliano ya Doha yangekamilika ifikapo Desemba 2006. Hata hivyo, kutokana na kuahirishwa kwa majadiliano kuna uwezekano kwamba yanaweza yasikamilike kama ilivyotarajiwa. Wizara yangu, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaratibu zoezi la kuainisha jinsi gani wote kwa pamoja tutatekeleza kwa manufaa ya Taifa makubaliano yatakayofikiwa. Masuala muhimu yaliyopewa kipaumbele katika mkutano wa Mawaziri Hong Kong ni upatikanaji wa misaada inayolenga kuinua biashara, masuala ya uwezeshaji wa biashara, huduma na haki miliki.  Katika utekelezaji wa makubaliano hayo, ni lazima kwenda sambamba na matakwa ya wanachama wengine wa Shirika la Biashara Duniani.  Tanzania ikiwa mojawapo ya nchi maskini za kundi la LDC ilifanikiwa kutetea maslahi yake katika maeneo mawili: la kwanza, ni lile la kusamehewa majukumu ya kulegeza masharti ya soko la biashara ya huduma; na la pili, ni lile kusamehewa kutumia kanuni ya kupunguza ushuru wa forodha kwa kiwango kikubwa.  Aidha, Tanzania itanufaika na kufanya biashara na nchi wanachama na kuendelea kupata misaada ya kiufundi na kisheria pale itakapohusika katika mgogoro wa kibiashara unaohitaji kutatuliwa katika bodi ya usuluhishi ya WTO.

 

 

 

 

Mchango wa Taasisi za Uwezeshaji katika Sekta ya Biashara

 

Mheshimiwa Spika,

35.            Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kinatoa mafunzo ya taaluma za Uhasibu, Masoko, Ununuzi na Ugavi ambayo yanawezesha watu mbalimbali kupata utaalamu wa kushiriki nyanja mbalimbali za kuanzisha na kuendeleza biashara. Aidha, Chuo kina mpango wa kupanua mtandao wa mafunzo ya elimu ya biashara kwa kuanzisha tawi jingine Kanda ya Ziwa jijini Mwanza kwa lengo la kusogeza huduma zake karibu na wananchi. Vile vile, CBE inaendesha mafunzo kwa mfumo wa masomoya jioni.

 

Mheshimiwa Spika,

36.            Uboreshaji wa mitaala katika CBE kulingana na mahitaji ya soko unazingatiwa hasa katika michepuo ya masoko, uhasibu, ununuzi na ugavi. Aidha, uenezaji wa elimu ya biashara ya ujasiriamali, uendeshaji na usimamizi bora wa biashara ndogo na za kati unatolewa na Chuo hiki. Pia, mafunzo ya ushauri na utafiti ya Ujasiriamali yanatolewa kwa wafanyabiashara katika stadi za uhasibu, fedha, utunzaji kumbukumbu za biashara na ukuzaji wa masoko na mauzo.  Vile vile, Chuo kinatoa mafunzo ya ushauri wa kitaalamu na utafiti vijijini kupitia Kitengo cha ujasiriamali. 

 

Mheshimiwa Spika,

37.            Kituo cha Kibiashara cha Tanzania kilichoko London kwa kushirikiana na Ubalozi wetu nchini Uingereza, kiliendelea kuitangaza Tanzania katika nchi za Ulaya.  Katika kipindi cha mwaka 2005/06, kituo kilikusanya na kutoa taarifa za fursa za biashara na uwekezaji, kuhudumia misafara ya kibiashara, kutangaza vivutio vya utalii katika maonesho yaliyofanyika katika miji ya London, Manchester na Glasgow.  Aidha, kituo kilishiriki mikutano mbalimbali ya mashirika na taasisi ambazo Tanzania ni mwanachama. 

 

Mheshimiwa Spika,

38.            Changamoto zinazoikabili sekta ya biashara ni pamoja na:

a)                 Gharama kubwa za uzalishaji;

b)                 Ufungashaji wa bidhaa usiofikia viwango vya ubora wa Kimataifa;

c)                  Ukosefu wa taarifa za masoko na taaluma ya utumiaji wa teknolojia ya mawasiliano;

d)                  Mwitikio mdogo wa wawekezaji;

e)                 Ukosefu wa teknolojia zinazoinua ufanisi wa uzalishaji wa bidhaa nyingi na za viwango vya ubora unaokidhi mahitaji ya soko la Kimataifa;

f)                   Kutokuwepo Maafisa Biashara Waambata katika Balozi zetu nje ambao  wangetafiti na kutoa taarifa za ‘‘Market intelligence” na kuwa kiungo kati ya Serikali na wafanyabiashara;

g)                 Mfumo wa ushindani wa Biashara ya Kimataifa usio wa haki;

h)                 Kushindwa kuongeza thamani katika bidhaa zetu;

i)                   Kushindwa kupanua wigo wa bidhaa na masoko; na

j)                   Miundombinu hafifu.

 

Mheshimiwa Spika

39.            Hatua zifuatazo zimechukuliwa ili kukabili changamoto hizo:

a)                  Wizara inawezesha wadau kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya biashara ya kikanda na Kimataifa;

b)                  Kupitishwa kwa sheria ya EPZ mwanzoni mwa mwaka 2002 na marekebisho ya mwaka 2006 kutawezesha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuzalisha bidhaa bora kwa ajili ya soko la nje;

c)                  Katika kutatua tatizo la ukosefu wa taarifa za masoko, tayari kituo cha taarifa za masoko (Trade Portal) kimeanzishwa BET, ikiwa ni pamoja na vituo vya kupokea na kutoa taarifa za biashara (Reference Centres) vilivyoko CBE, TCCIA, TBS, WVBM na Wizara ya Kilimo, ambapo wafanyabiashara wanaweza kupata taarifa mbalimbali za masoko;

d)                  Mchakato wa kuboresha maabara za Tanzania na kuzifanya zitambulike (Accredited) na asasi za Kimataifa za viwango unaendelea;

e)                  Katika kuimarisha Ofisi ya Geneva Wizara imeongeza mtaalamu wa biashara katika ubalozi wa Tanzania Geneva, ikiwa ni pamoja na mtaalamu mmoja kupata mafunzo kazini katika ubalozi huo; na

f)                    Pamoja na kuimarisha Kituo cha Biashara cha Tanzania kilichoko London; katika mwaka huu wa Fedha, Wizara itafungua kituo kingine Dubai kwa ajili ya soko la Mashariki ya Kati.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

D.3:   Sekta ya Masoko

 

Sera na Mkakati wa Maendeleo ya Masoko

 

Mheshimiwa Spika,

40.            Kwa kuwa maendeleo ya sekta ya kilimo hutegemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao yanayozalishwa, Serikali imekuwa ikifanya mabadiliko ya kisera na kimkakati ili kukuza masoko ya mazao ya kilimo tangu mwanzoni mwa miaka ya tisini.  Baadhi ya matokeo ya mabadiliko haya yanajumuisha kuimarika kwa bei za mazao; kuongezeka kwa uzalishaji na mauzo ya nje kwa baadhi ya mazao; kuongezeka kwa vyanzo vya mikopo pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu ya masoko na mfumo wa upatikanaji wa taarifa za masoko. Aidha, mafanikio mengine yanajumuisha yafuatayo:-    

a)                 Wizara kwa kushirikiana na Programu ya Kuendeleza Mifumo ya Masoko ya Mazao imeviunganisha vikundi vya wakulima na masoko maalum ikiwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha mkataba kwa mazao ya mboga mboga kati ya wakulima wadogo na Kampuni zinazouza  mboga mboga katika soko la Jumuiya ya Ulaya;

b)                 Kufanya utafiti wa zao la Vitunguu Wilayani Kilosa; utafiti kuhusu biashara ya zao la Kahawa Mkoani Kagera ili kuainisha chanzo cha kuwepo kwa biashara isiyo rasmi kati ya Mkoa huo na nchi za jirani unaoendelea na uchunguzi wa vipimo vinavyotumika kununulia mazao kutoka kwa wakulima;

c)                  Mafunzo ya ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa taarifa za masoko yalitolewa kwa wakusanyaji wa taarifa za masoko kutoka Wilaya 75.  Vile vile, wakusanyaji wa taarifa hizo katika ngazi ya Mkoa walipatiwa vitendea kazi zikiwemo kompyuta sita;

d)                 Wizara imepanua wigo wa usambazaji wa taarifa za bei za mazao kwa  kupitia ujumbe mfupi wa maneno katika simu za mikononi za Kampuni ya Vodacom Tanzania Limited; na

e)                 Wizara imeboresha mfumo wa kuhifadhi na kuchambua taarifa za masoko kwa kutumia kompyuta na programu maalumu kwa taarifa za masoko ya mazao.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kumekuwepo na changamoto zinazowakabili wazalishaji, wasindikaji na wafanyabiashara wa mazao.  Ili kuweka mwongozo wa kisera na kimkakati katika kushughulikia changamoto za masoko ya mazao na bidhaa za kilimo, Serikali iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo.

 

Ununuzi wa Mazao Asilia

 

Mheshimiwa Spika,

41.            Mazao ambayo ununuzi wake uliongezeka katika msimu wa mwaka 2005/06 ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2004/05, yanajumuisha pamba mbegu, tumbaku ya mvuke, korosho, mkonge, maua ya pareto na miwa.  Jedwali Na. 8 na Kielelezo Na.7 vinatoa takwimu za ongezeko kwa kila zao.   Kuongezeka kwa ununuzi wa mazao hayo kulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji.  Aidha ununuzi wa mazao ya tumbaku ya moshi, kahawa na chai ulipungua kama Jedwali Na. 8 na Kielelezo Na.7 vinavyodhihirisha.   Kushuka kwa ununuzi wa kahawa na chai kulisababishwa na kushuka kwa uzalishaji ambao kwa kiasi kikubwa kulisababishwa na ukame.

 

Bei ya Mkulima (Producer Price)

 

Mheshimiwa Spika,

42.            Bei ya mkulima iliongezeka kwa mazao ya kahawa ya robusta, kahawa ya arabica, chai pamoja na zao la miwa kwa mkataba (outgrowers) kama Jedwali Na. 10a linavyoonyesha.  Kuongezeka kwa bei ya mkulima kwa mazao ya kahawa na chai kulisababishwa na kuimarika kwa bei ya mazao hayo katika soko la dunia na kuongezeka kwa ubora wa mazao. Kwa mfano, bei ya kuuzia nje kahawa aina ya arabica iliongezeka kwa asilimia 13 na bei ya chai iliongezeka kwa asilimia 2.  Aidha, bei ya mkulima kwa zao la pamba ilishuka kutoka wastani wa Shilingi 250 kwa kilo msimu wa 2004/05 hadi Shilingi 220 kwa kilo msimu wa 2005/06 ikiwa ni anguko la asilimia 12, ona Jedwali Na. 10a.

 

Bei ya Kuuzia Nje (FoB Price)

 

Mheshimiwa Spika,

43.            Bei ya kuuzia nje kahawa aina ya arabica iliongezeka kwa asilimia 13, pamba asilimia 10, tumbaku ya moshi asilimia 25, chai asilimia 2 na mkonge asilimia 7. Bei ya kuuzia nje korosho ghafi na tumbaku ya mvuke ilipungua kwa asilimia 17 na 20 sawia. Bei ya kuuzia nje korosho ghafi ilishuka kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo duniani. Uzalishaji wa korosho duniani umeongezeka maradufu kutoka tani milioni 0.8 mwaka 1995 hadi tani milioni 1.6 mwaka 2005. Zao jingine lililoonyesha kushuka kwa bei ya kuuzia nje ni kahawa aina ya robusta ambayo ilishuka kwa asilimia moja kama ilivyoonyeshwa kwenye Jedwali Na. 10b.

 

Mauzo ya Ndani

Mheshimiwa Spika,

44.            Mauzo ya korosho kwa wabanguaji wa ndani yaliongezeka kutoka tani 7,070 msimu wa 2004/05 hadi tani 20,000 msimu wa 2005/06. Aidha, jumla ya tani 381 za kahawa safi ziliuzwa kwa wasindikaji wa ndani msimu wa 2005/06 ikilinganishwa na tani 229  msimu wa 2004/05. Jumla ya tani 363 za kahawa zilisindikwa katika viwanda vya ndani msimu wa 2005/06 ikilinganishwa na tani 214 msimu wa 2004/05.

 

Mheshimiwa Spika,

45.            Jumla ya tani 3,000 za chai zenye thamani ya Shilingi bilioni 3.6  zinatarajiwa kuuzwa katika soko la ndani msimu 2005/06 ikilinganishwa na tani 4,329 zilizouzwa msimu wa 2004/05 zilizokuwa na thamani ya Shilingi  bilioni 4.3. Aidha, mauzo ya pamba kwa viwanda vya ndani msimu wa 2005/06 yamefikia tani 25,100 ikilinganishwa na tani 30,475 zilizouzwa msimu wa 2004/05. Msimu wa mauzo wa 2005/06 bado unaendelea.

Mauzo ya Nje

 

Mheshimiwa Spika,

46.            Katika msimu wa 2005/06 mauzo ya nje kwa mazao makuu ya biashara yalipungua kwa mazao mengi isipokuwa zao la tumbaku na pareto kama Jedwali Na. 9 linavyoonyesha.  Aidha, mauzo ya mkonge yalilingana na mauzo ya msimu uliotangulia ambapo tani 11,693 ziliuzwa. Hata hivyo, thamani ya mauzo hayo iliongezeka kwa asilimia 8 kutoka Dola za Kimarekani 8,214,505 hadi Dola za Kimarekani 8,899,694.  Aidha, mauzo ya korosho ghafi nje yalishuka kutokana na kuongezeka kwa wasindikaji wa ndani. Jumla ya tani 20,000 ziliuzwa kwa wasindikaji wa ndani msimu wa 2005/06 ikilinganishwa na tani 7,070 msimu 2004/05.

 

Mheshimiwa Spika,

47.            Hadi kufikia mwezi Mei 2006, mauzo ya kahawa safi nje ya nchi yalikuwa tani 31,356 na kuliingizia Taifa Dola za Kimarekani 59,406,628. Msimu wa mauzo ya kahawa bado unaendelea. Jumla ya tani 42,517 za kahawa safi zenye thamani ya Dola za Kimarekani 74,792,907 ziliuzwa nje ya nchi msimu wa 2004/05.  Wanunuzi wakuu wa kahawa ya Tanzania msimu wa 2005/06 walikuwa ni Japan (33%), Ujerumani (22%), Italia (19%), Marekani (6%), Uswis (4%), Ubeligiji (4%), Uholanzi (4%) na nchi nyingine (8%).

 

Mheshimiwa Spika,

48.            Mauzo ya nje kwa zao la pamba msimu wa 2005/06 hadi Aprili 2006 yalifikia tani 83,362 ikilinganishwa na tani 84,021 zilizouzwa msimu wa 2004/05. Msimu wa mauzo unaendelea na hivyo kuna uwezekano wa kuzidi kiwango cha mauzo yaliyopatikana msimu wa 2004/05.

 

Mauzo ya Nje kwa Mazao ya Biashara Yasiyokuwa Asilia

 

Mheshimiwa Spika,

49.            Thamani ya mauzo ya maua na mboga nchi za nje yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 14.3 kipindi cha msimu wa 2004/05 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 18.3 msimu wa 2005/06. Ongezeko hili ni asilimia 28 na kwa kiasi kikubwa limetokana na kuongezeka kwa wastani wa bei na matumizi katika soko la dunia pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji nchini.

 

Bei ya Mazao Makuu ya Chakula

 

Mheshimiwa Spika,

50.            Wastani wa bei ya mazao makuu ya chakula hususan mahindi, mchele na maharage ulipanda mwishoni mwa mwaka 2005 na mwanzoni mwa mwaka 2006 kutokana na kupungua kwa ugavi wa mazao hayo, kulikosababishwa na kuchelewa kwa msimu wa mvua za vuli na masika. Kwa mfano, bei ya jumla ya gunia la mahindi la kilo 100 katika jiji la Dar es Salaam ilipanda kutoka wastani wa Shilingi 15,438 mwezi Septemba 2005 hadi Shilingi 20,700 mwezi Desemba 2005 na kuendelea kupanda hadi kufikia wastani wa Shilingi 30,000 mwezi Machi 2006. Katika Jiji la Mbeya bei ya jumla ya mahindi iliongezeka kutoka Shilingi 12,041 mwezi Septemba 2005 na kufikia Shilingi 29,916 mwezi Machi 2006. Bei ya mchele Jijini Dar es Salaam iliongezeka kutoka Shilingi 52,958 mwezi Septemba 2005 na kufikia Shilingi 82,500 mwezi Machi 2006. Jijini Mbeya, bei ya jumla ya mchele iliongezeka kutoka Shilingi 44,833 mwezi Septemba 2005 na kufikia Shilingi 64,166 mwezi Machi 2006.

 

Mheshimiwa Spika,

51.            Tofauti kubwa ya bei ya mazao makuu ya chakula kati ya masoko mbalimbali nchini ni kiashirio cha kuendelea kuwepo kwa matatizo ya miundombinu duni ya masoko kama barabara za vijijini, magulio au vituo vya kuuzia na kununulia mazao. Gharama kubwa za kusafirisha mazao kutoka maeneo yanakozalishwa kwenda kwa walaji husabisha kushuka kwa bei anayopata mzalishaji. Aidha, soko la mazao ya chakula bado linakabiliwa na matatizo ya kiwango cha chini cha usindikaji wa mazao hayo, kukosekana kwa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na udhaifu katika usimamizi wa uuzaji wa mazao kulingana na madaraja, ubora na vipimo.

Mifugo na Mazao Yake

 

Mheshimiwa Spika,

52.            Sekta ya mifugo imeendelea kutegemea soko la ndani kwa maendeleo yake. Sababu kubwa ya mifugo na bidhaa zake kuendelea kutegemea soko la ndani ni pamoja na kuwepo kwa magonjwa ya mifugo na ubora usiokidhi mahitaji na masharti katika masoko ya nchi za nje. Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha bidhaa hizo ziweze kuuzwa katika masoko ya Kimataifa. Tanzania huuza  mifugo katika nchi za Ghuba na Visiwa vya Comoro ingawaje biashara hii siyo kubwa. Aidha, biashara ya mifugo isiyo rasmi hufanyika kati ya nchi yetu na  nchi za jirani. 

 

Mheshimiwa Spika,

53.            Ununuzi wa ngozi za ng'ombe, mbuzi na kondoo katika msimu wa 2005/06 uliongezeka kwa asilimia 4 ikilinganishwa na msimu wa 2004/05. Mapato ya wafugaji kutokana na mauzo hayo yaliongezeka kwa asilimia 24 kutoka Shilingi bilioni 5.5 hadi Shilingi bilioni 6.2 msimu wa 2005/06 kama inavyoonyeshwa kwenye Jedwali Na 11 na Kielelezo Na.8. Aidha, mauzo  ya ngozi nje ya nchi katika kipindi hicho yaliongezeka kwa asilimia 8 kutoka vipande milioni 3.2 hadi vipande milioni 3.7 na mapato kutokana na mauzo hayo yaliongezeka kwa asilimia 86 kama inavyonyeshwa kwenye Jedwali Na. 12 na Kielelezo Na.8.

 

Mheshimiwa Spika,

54.            Pamoja na kuwepo kwa fursa mbalimbali za masoko ndani na  nje ya nchi, Tanzania haijazitumia fursa hizo kikamilifu kutokana na matatizo ambayo bado yanaukabili mfumo wa masoko ya mazao ya kilimo nchini. Matatizo hayo ni pamoja na:

 

a)                  Gharama kubwa za kufanya biashara ya mazao kutokana na uduni wa miundombinu ya kusafirisha, kuhifadhi na kusindika mazao ya kilimo;

b)                  Uduni wa ubora na uchache wa mazao yanayozalishwa na hivyo kushindwa kushindana na bidhaa kutoka nchi nyingine hasa katika soko la dunia;

c)                  Upungufu  wa taarifa sahihi za masoko kwa wazalishaji, wasindikaji na wafanyabiashara;

d)                  Uwezo mdogo wa kuyaongezea thamani mazao ambao pamoja na sababu zingine unatokana na ukosefu wa mtaji;

e)                  Udhaifu katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa mazao na hasa yale yasiyosimamiwa na Bodi za Mazao; na

f)                    Kuongezeka kwa ushindani usiokuwa wa haki wa mazao na bidhaa za kilimo zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

 

Mheshimiwa Spika,

55.            Ili kukabiliana na matatizo yanayoikabili sekta ya masoko ya mazao na bidhaa za kilimo, Wizara ilichukua hatua zifuatazo: -

a)       Kuandaa, kusimamia, kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa Sera, Sheria na kanuni zinazohusu masoko ya mazao na bidhaa za kilimo kwa kutekeleza yafuatayo:-

·        Kukamilisha Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo;

·        Kukamilisha Kanuni za Utekelezaji wa Sheria ya Stakabadhi za Mazao Ghalani ya mwaka 2005; na

·        Kuhamasisha wadau mbalimbali (wakulima, wafanyabiashara, taasisi za fedha) kuhusu matumizi ya Mfumo huo.

b)       Kuanzisha na kuendeleza mikakati ya kukuza masoko ya mazao na bidhaa za kilimo ndani na nje ya nchi. Utekelezaji wa jukumu hili ulihusisha yafuatayo:-

·        Kuhamasisha wakulima na wasindikaji kuzalisha kulingana na mahitaji ya soko ili kuifanya shughuli ya kilimo kuwa na manufaa;

·        Kuhamasisha uwekezaji katika miundombinu ya masoko na uongezaji thamani wa mazao na bidhaa za kilimo;

·        Kuhamasisha na kuendeleza matumizi ya mbinu mbalimbali za kukinga athari zinazojitokeza katika masoko;

·        Kuhamasisha na kuendeleza soko la ndani kwa mazao na bidhaa za kilimo zinazozalishwa nchini;

·        Kuhamasisha wakulima na wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo za masoko ya kikanda na Kimataifa; na

·        Kufanya tafiti mbalimbali za masoko ili kuainisha matatizo kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi.

c)       Kuboresha upatikanaji na usambazaji wa taarifa za masoko ya mazao na bidhaa za kilimo. Utekelezaji wa hatua hii ulihusisha:-

 

·        Kuandaa Kitabu cha Orodha ya Wanunuzi na Wasindikaji wa Mazao ya Kilimo (Agribusiness Directory);

·        Kuimarisha na kuendeleza mfumo wa ukusanyaji, uchambuzi, hifadhi na usambazaji wa taarifa za masoko ikiwa ni pamoja na kuwezesha Halmashauri kutekeleza jukumu hilo.

d)       Kusimamia utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Mifumo ya Masoko. Utekelezaji wa jukumu hili unahusisha Wilaya 38 katika Mikoa nane kwa kutekeleza yafuatayo:-

·        Kuwezesha maandalizi ya Sera ya Masoko ya Mazao kwa kugharamia wataalamu, washauri waelekezi na mafunzo;

·        Programu ilitoa mafunzo kwa Wahandisi na Mafundi kutoka Wilaya 18 na kukamilisha ujenzi wa masoko ya kisasa katika maeneo ya Kikatiti (Arumeru), Matai (Sumbawanga) na Kwasadala (Hai). Pia ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao katika mji mdogo wa Magugu (Babati) umekamilika na ukarabati wa maghala katika vijiji vya Qash (Babati), Chimala (Mbarali) na Iwindi (Mbeya) umefanyika. Aidha, jumla ya kilomita 210 za barabara za vijijini zilijengwa katika Wilaya nane (Arumeru, Hai, Babati, Muheza, Mufindi, Mbeya, Sumbawanga na Songea);

·        Mafunzo ya matumizi ya mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani yalitolewa kwa wanachama wa vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), pamoja  na kuunganisha vyama hivyo na mabenki yanayotoa mikopo kwa ajili ya mfumo wa stakabadhi za mazao; Benki za CRDB na Exim ndizo zilizokubali kutoa mikopo chini ya Mfumo wa Stakabadhi za Mazao. Mfumo huu umeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima kupata bei nzuri za mazao yaliyojaribiwa katika mfumo huo;

·        Kuboresha upatikanaji wa mitaji na mbinu za kujikinga na maanguko ya bei za mazao kwa kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani; na

·        Kujasirisha wakulima na wafanyabiashara wa mazao na bidhaa za kilimo na  kuwaunganisha na masoko.

e)       Kusimamia Mradi wa Kuendeleza na Kuboresha Biashara ya Pamba na Kahawa kwa kufanya kazi zifuatazo katika mwaka 2005/06: -

 

·        Kujadili na kupokea maoni ya wadau kuhusu Rasimu ya Kanuni za Sheria ya Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani;

·        Kushiriki katika mikutano ya wadau wa mazao ya pamba na kahawa kwa lengo la kuboresha masoko ya mazao hayo na kufuatilia utekelezaji wa mradi; na

·        Kuandaa stakabadhi zitakazotumika katika Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani na kuendeelea kuhamasisha matumizi ya mfumo huo.

 

D.4:  Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo.

Utekelezaji wa Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo

 

Mheshimiwa Spika,

56.            Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo imeendelea kutoa mchango  muhimu katika ukuaji wa uchumi. Maendeleo ya sekta hii ni muhimu hasa kwa vile pamoja na kuongeza ajira, inasaidia kutoa msingi wa ujuzi na uzoefu kwa wanaviwanda na wafanyabiashara  wadogo. Katika kuchochea  maendeleo ya sekta hii, Wizara iliandaa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo katika mwaka 2003. Sera hii inalenga kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha uanzishaji wa miradi mipya na wakati huo huo kuwezesha miradi iliyopo kuimarika na kuongeza mchango wa sekta hii katika pato la Taifa. Mikakati iliyoainishwa katika sera ni pamoja na kuboresha mfumo wa sheria na taratibu; kuimarisha miundombinu; kuboresha huduma za masoko, ujasiriamali, upatikanaji wa taarifa na teknolojia na pia kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha.

 

Mheshimiwa Spika,

57.            Semina za kikanda zilifanyika ili kuendelea kuelimisha wananchi juu ya Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo na pia kuwafahamisha juu ya fursa zilizopo. Vile vile, nakala ya sera katika lugha rahisi inaandaliwa. Wizara imekwishaanza kuchukua hatua mbali mbali za utekelezaji wa sera, hii ikiwa ni pamoja na maandalizi yaliyofanyika kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ya kuanzisha programu ya kuendeleza viwanda vidogo na biashara ndogo vijijini. Kwa kuanzia, programu hii itatekelezwa katika Mikoa ya Pwani, Tanga, Manyara, Mwanza, Iringa na Ruvuma. Vile vile, Mfuko maalum wa kuchochea ukuaji wa viwanda vidogo na biashara ndogo (SME competitiveness Facility) umeanzishwa kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA). Madhumuni ya mfuko huu ni kuwezesha wajasiriamali wadogo kuimarisha ubora wa bidhaa zao ili kuweza kuyafikia masoko ya nje. Vile vile, Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kufuatilia utekelezaji wa mfuko wa kudhamini miradi ya viwanda vidogo na biashara ndogo. Pia, Wizara inashirikiana na Shirika la Kazi  Duniani (ILO) kutekeleza mradi wa kuendeleza wajasiriamali wanawake kwa kuwapatia mafunzo yanayochochea ujasiriamali, uimarishaji wa vikundi vya uzalishaji na utafutaji wa masoko. Aidha, Wizara imeendelea kuimarisha taasisi zinazohudumia sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo, hii ikiwa ni pamoja na SIDO ili taasisi hizi ziimarishe utoaji wa huduma kwa wajasiriamali wadogo.

 

Mheshimiwa Spika,

58.            Katika kipindi cha 2005/06, Wizara kupitia SIDO iliendelea kutoa huduma za kiufundi kwa wajasiriamali wadogo ambapo, jumla ya mashine 383 zilitengenezwa na wajasiriamali 540 walipatiwa mafunzo ya kiufundi. Pia, jumla ya wajasiriamali 4,926 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na mbinu za biashara, wajasiriamali 1,066 walipatiwa mafunzo ya usindikaji  na uhifadhi wa vyakula na wajasiriamali 4,200 walipatiwa ushauri. Aidha, wajasiriamali wadogo 968 walipata fursa ya kushiriki katika maonesho ya kikanda yanayoendeshwa na SIDO ambapo waliweza kufanya mauzo ya shs. 120 millioni  na pia kupata oda za Shilingi milioni 160.

 

Mheshimiwa Spika,

59.            Miradi ya kuendeleza ardhi na miundombinu kwa ajili ya viwanda vidogo na biashara ndogo inayotekelezwa ni pamoja na:- vituo vya biashara vya Songea na Moshi; uimarishaji wa kituo cha mafunzo na uzalishaji cha Njombe; ujenzi wa majengo ya wafanyabiashara wadogo katika miji ya Makambako na Babati; ujenzi na uimarishaji wa majengo kwa ajili ya viatamizi kwa ajili ya Dar es Salaam na Mbeya; na ujenzi wa vituo vya wajasiriamali kuoneshea bidhaa zao. Aidha, kwa kutumia utaratibu wa kushirikisha Sekta Binafsi kuendeleza maeneo, ujenzi wa majengo ya viwanda unaendelea katika mitaa ya viwanda iliyoko Mikoa ya Mwanza na Ruvuma.

 

Mheshimiwa Spika,

60.            Serikali iliendelea kusambaza teknolojia mbalimbali zilizobuniwa, kuzalishwa na kujaribiwa ili ziwafikie walengwa na ziweze kuchangia katika kuongeza ufanisi wa uzalishaji mali, kuongeza ajira na kipato na hatimaye kupunguza umaskini. Mashine za kuwasaidia wakulima katika kilimo na usindikaji wa mazao ya kilimo zilitengenezwa na Taasisi za TEMDO, CAMARTEC, TIRDO, ‘‘Technology  Development and Transfer Centre’’  na SIDO.

Mheshimiwa Spika,

61.            Mfuko wa Wafanyabiashara Wananchi – NEDF ulioanzishwa mwaka 1994 hadi kufikia mwezi Machi, 2006 ulikuwa umetoa mitaji yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.34 kwa wajasiriamali 23,578 na kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa wananchi 33,404.  Mwaka 2005/06 mfuko ulitoa mikopo ya thamani ya Shilingi milioni 285.  Aidha, wajasiriamali wadogo 268 walipatiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 481 kutoka Mfuko wa Mitaji ya Mikoa unaosimamiwa na SIDO na wengine 44 walipatiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 243 kutoka mfuko ulioanzishwa na SIDO kwa kutumia fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki.

 

Mheshimiwa Spika,

62.            Sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo nchini bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali. Hii ni pamoja na mwamko mdogo wa wananchi kuzitumia fursa zilizopo, uwezo mdogo wa taasisi zinazoihudumia sekta, ukosefu wa taarifa muhimu hususan kuhusu masoko, matumizi ya teknolojia na miundombinu duni, pamoja na kushindwa kunufaika na mitaji inayotolewa na taasisi za fedha, ikijumuisha kushindwa kumudu masharti ya mikopo.

 

D.5:   Utafiti na Maendeleo.

 

Mheshimiwa Spika,

63.            CAMARTEC iliendelea kueneza teknolojia ya ‘‘biogas’’, majiko sanifu na teknolojia ya udongo-saruji.  Katika kipindi hicho, mafunzo na ujenzi wa mtambo wa ‘‘biogas’’ wenye mita za ujazo 16 vilifanyika mjini Dar es Salaam kwa mafundi waashi watano.  Pia mtambo mmoja wenye ukubwa wa mita 50 za ujazo ulitengenezwa kituoni CAMARTEC.  Mafunzo kuhusu Teknolojia ya majiko sanifu yalitolewa kwa wajasiriamali 20 waliofundishwa katika Wilaya za Rombo na Ulanga.  Katika Wilaya ya Kondoa mafunzo ya teknolojia ya udongo–saruji yalitolewa kwa wajasiriamali sita kwa ajili ya ujenzi wa nyumba bora vijijini.

 

 

Mheshimiwa Spika,

64.            TEMDO katika mwaka 2005 ilibuni teknolojia ambazo zililenga katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi walio wengi pamoja na kuendeleza ujasiriamali na kuongeza ajira.  TEMDO katika kipindi hicho iliendeleza teknolojia za kukamua mafuta ya alizeti, kusindika matunda na kupukuchua mahindi.  Lengo ni kueneza teknolojia hizo vijijini ili kurahisisha kazi na kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo.

 

Mheshimiwa Spika,

65.            TIRDO katika kipindi cha mwaka 2005 ilibuni teknolojia ambazo zililenga katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi, kuendeleza ujasiriamali na kuongeza ajira. TIRDO katika kipindi hicho imetoa mafunzo ya uchomeleaji vyuma kwa wazalishaji wadogo na wajasiriamali 75 huko Morogoro, Dar es Salaam, Songea na Ulanga wanaotengeneza mashine za kusindika vyakula na matunda. Aidha, kwa mwaka 2005/06 idadi ya watu waliofundishwa kusindika matunda na nyanya ni 35 katika maeneo ya Dar es salaam, Njombe, Iringa na Tanga. Pia, jumla ya wakulima 58 wa Mikoa ya Pwani na Mtwara wamefundishwa juu ya utengenezaji wa wanga unaotumika katika viwanda vya nguo na unga wa mihogo usio na sumu.  Katika kuongeza thamani ya mwani, TIRDO imefundisha wakulima 85 katika Wilaya za Muheza na Pangani.  Vile vile, ufuatiliaji wa mazao toka shambani, viwandani  hadi kwa mlaji kwa lengo la kuwa na ubora na kumbukumbu umefanyika kwa msaada wa DANIDA na wametoa mafunzo kwa wajasiriamali 649 katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Ruvuma na Kagera na utaratibu wa kumbukumbu umewekwa na mazao husika ni kahawa, korosho, chai, samaki, maua na viungo.

 

Mheshimiwa Spika,

66.            TIRDO imeendelea kutoa mafunzo ya kilimo cha uyoga kwa wakulima 237 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro na Dar es Salaam. Wazalishaji wadogo 20 wamefundishwa jinsi ya kutumia mtambo wa majaribio wa kutengeneza chumvi wenye uwezo wa kuzalisha tani nne kwa wiki katika Mkoa wa Singida. Kuhusu utengenezaji wa chaki wajasiriamali 154 wamefundishwa katika Wilaya za Nzega, Ulanga (Mahenge) na Songea. Mafunzo hayo yanaendelea katika Mikoa ya Morogoro na Mtwara. Katika kuongeza thamani ya mwani, Shirika limefundisha wakulima wa mwani 85 katika Wilaya za Muheza na Pangani. Aidha, vikundi vinne vya wajasiriamali 82, vimefundishwa juu ya ukusanyaji, usafishaji na kurejea taka za plastiki na karatasi kwa lengo la kutunza mazingira na kuongeza ajira.

 

Mheshimiwa Spika,

67.            Katika kutekeleza majukumu yao, taasisi hizi za utafiti zimekuwa zikikabiliwa na matatizo kama vile uwezo mdogo kifedha kwa ajili ya kufanya tafiti, uwezo mdogo wa wajasiriamali kuzalisha kibiashara teknolojia zilizopasishwa kwa matumizi, uwezo mdogo wa kutangaza teknolojia zilizopasishwa, uwezo mdogo wa walengwa kununua na kutumia teknolojia zinazobuniwa, na kupanda kwa gharama za malighafi. Aidha, viwanda vinavyomilikiwa na Makampuni ya Kimataifa hupendelea kutumia kampuni mama katika utafiti na hivyo kutotumia huduma za taasisi zetu.

Mheshimiwa Spika,

68.            Hatua zilizochukuliwa ili kukwamua matatizo ya Taasisi hizo ni pamoja na serikali kuzitengea fedha kutokana na bajeti ya MKUKUTA ili kuziwezesha kufanya tafiti mbalimbali na kutangaza teknolojia zilizokwisha pasishwa ziweze kufikia walengwa. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea kufanya marekebisho ya sheria zilizoanzisha taasisi hizi ili ziendane na wakati.

 

D.6:   Usimamiaji wa Sheria za Udhibiti

 

Mheshimiwa Spika,

69.            BRELA iliendelea kutekeleza majukumu yake ya usajili na kusimamia sheria ya makampuni, majina ya biashara, alama za biashara, hataza, na sheria ya leseni ya viwanda. Katika mwaka 2005/06, ufanisi wa utendaji kazi wa wakala ulikuwa na matokeo na mabadiliko mazuri ambapo uandikishaji wa shughuli zitolewazo na Wakala uliongezeka, usajili wa kampuni ambao haukuwa na muda maalum kwa sasa usajili unapatikana kati ya siku tatu hadi tano kuanzia siku maombi yalipopokelewa.  Vivyo hivyo, kazi ya usajili wa majina ya biashara hukamilika ndani ya siku moja hadi tatu. Muda anaotumia mteja kupata huduma ulipungua, kiwango cha kutii sheria kwenye makampuni na kufuata taratibu zake uliongezeka na mapato ya wakala.

 

Mheshimiwa Spika,

70.            BRELA imefanikiwa kupunguza kero za wateja na washitiri wake katika kusubiri muda mrefu kuandikisha kampuni, jina la biashara na kupata leseni ya viwanda kwa kuondoa masharti yasiyokuwa ya lazima. Mafanikio mengine ni pamoja na Sheria mpya ya Makampuni Na.12 ya mwaka 2002 kuanza kutekelezwa mwezi Machi 2006.  Mafanikio hayo yamewezesha kuongezeka kwa majina ya biashara zinazosajiliwa kutoka 5,890 mwaka 2004/05 hadi 7,409 mwaka 2005/06 na makampuni yaliyoandikishwa kutoka 3,347 mwaka 2004/05 hadi 3,791 mwaka 2005/06. Ongezeko hilo pia limetokana na uelimishaji wa wadau kuhusu taratibu za usajili kwa njia ya vyombo vya habari, warsha na vipeperushi.

Mheshimiwa Spika,

71.            Wakala wa Vipimo (WMA) uliendelea kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Sheria na Kanuni ili kuhakikisha kuwa kuna biashara ya haki kati ya wadau.  Katika mwaka 2005/06, Wakala ulichukua hatua madhubuti ya kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vipimo. Kwa kuanzia, mafunzo hayo yalitolewa katika Mikoa ya nyanda za juu kusini. Vile vile, wafanyabiashara wameendelea kupewa ushauri kuhusu vipimo wanavyostahili kuvitumia.  Elimu hiyo pia ilitolewa kupitia matangazo katika vyombo vya habari kama vile luninga, redio, magazeti na majarida; na kwenye maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam.

 

Ubora

 

Mheshimiwa Spika,

72.            TBS iliendelea na majukumu ya uwekaji viwango vya ubora wa bidhaa na usimamiaji wake.  Hadi kufikia mwezi Machi 2006, Shirika lilikuwa limetayarisha Viwango vya Taifa 957 katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo na chakula, nguo, kemikali, uhandisi na mazingira.  Aidha, Shirika liliendelea kusimamia utekelezaji wa Viwango vya Taifa kwa kutumia mifumo iliyopo ya kuhakiki ubora (certification scheme).  Hadi kufikia mwezi Machi 2006, Shirika lilikuwa limetoa jumla ya leseni 706 za ubora wa bidhaa mbalimbali katika viwanda 433 vya humu nchini.

 

Mheshimiwa Spika,

73.            Pamoja na mafanikio hayo, TBS inakabiliwa na uchakavu wa vifaa vya maabara na uhaba wa nyenzo nyingine zinazotumika kupima na kudhibiti viwango vya ubora wa bidhaa mbalimbali. Pia, uelewa mdogo wa umma na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa viwango vya ubora katika kulinda afya na usalama wa mlaji na kuzifanya bidhaa zikubalike katika soko la Kimataifa.

 

Mheshimiwa Spika,

74.            TBS kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo DANIDA, Sida, UNIDO, UNFPA na FAO, ilifanikisha upatikanaji wa vyombo na mahitaji mbalimbali ya maabara. Aidha, TBS kwa msaada wa Sida waliweza kutoa mafunzo kwa umma na jumuiya ya wafanyabiashara juu ya umuhimu wa viwango vya ubora wa bidhaa.

 

Ushindani wa Haki

 

Mheshimiwa Spika,

75.            Katika kipindi cha mwaka 2005/06, maandalizi ya utekelezaji wa Sheria mpya ya Ushindani 2003, yalifikia hatua ya kuteua Mwenyekiti, Mkurugenzi Mkuu, Makamishna wa Tume ya Ushindani pamoja na Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Ushindani mwezi Novemba 2005. Baada ya uteuzi huo, Makamishna wa Tume na Wajumbe wa Baraza la Ushindani walipata mafunzo ya awali mwezi Desemba 2005 kuhusu sheria na wajibu wao.  Vyombo hivi sasa vinakamilisha ajira ili kuweza kutekeleza vyema majukumu yake. Aidha, Baraza la Taifa la Ushauri kwa Mlaji lilianzishwa mwezi Julai 2005.

 

E.       MWELEKEO KATIKA SEKTA ZA VIWANDA, BIASHARA NA MASOKO KWA MWAKA 2006/07

 

Mheshimiwa Spika,

76.            Katika kipindi cha mwaka 2006/07, Wizara yangu itaendelea kutekeleza MKUKUTA na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2005.  Kama nilivyokwishasema, Ilani hiyo, imebainisha wazi mwelekeo wa Sekta za Viwanda, Biashara na Masoko kama ifutavyo: - Sekta ya Viwanda ikue kwa asilimia 15 ifikapo 2010; Sekta za Biashara na Masoko zijenge uwezo wa kushiriki na kufaidika na mfumo wa Biashara ya Kikanda na Kimataifa katika mazingira ya utandawazi. Katika hili Wizara inalenga kutekeleza kama ifuatavyo kisekta: -

 

E.1:   Sekta ya Viwanda

 

Mheshimiwa Spika,

77.            Katika mwaka 2006/07, mkazo umewekwa katika juhudi za kuanzisha viwanda mama, kwa kutafuta wabia wa kuwekeza katika mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma, mradi wa chuma wa Liganga na tafiti za miradi mingine iliyo katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara. Kipaumbele kingine ni kuendelea na utekelezaji wa programu inayolenga katika kuimarisha usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo na maliasili; kuendelea kuhamasisha uanzishaji wa maeneo ya uzalishaji kwa ajili ya uuzaji nje (EPZ) pamoja na uwekezaji katika viwanda ndani ya maeneo hayo. 

 

Mheshimiwa Spika,

78.            Changamoto kubwa ambazo zinaikabili sekta ya Viwanda ni pamoja na ukosefu wa vyanzo vya mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya Viwanda, Ufinyu wa soko la ndani unaotokana na kasumba ya wananchi kuthamini na kupendelea kununua bidhaa kutoka nje badala ya zinazotengenezwa na viwanda vya hapa nchini hata kama vina ubora wa juu ikilinganishwa na bidhaa za aina hiyo toka nje.  Vile vile, kutokana na wananchi wengi kuwa na kipato kidogo uwezo wao wa kununua bidhaa za viwandani ni mdogo. Changamoto nyingine ni kushindwa kufikia viwango vya ubora wa bidhaa na mbinu za utafutaji masoko ya bidhaa ili kuweza kushindana vema katika soko la Kimataifa na la ndani.  Vile vile, upungufu wa wataalamu hasa katika fani ya taaluma maalum kwa mfano wataalam wa nguo (textiles technologists) na ngozi (leather technologists).  Tanzania haina vyuo vinavyotoa wataalamu wa fani hizo, hivyo viwanda vingi vinategemea wataalam kutoka nje. Changamoto nyingine ni ukosefu wa nishati nafuu na ya kuaminika.

 

Mheshimiwa Spika,

79.            Ili kukamilisha malengo ya mwelekeo huo na kukabili changamoto, kazi zifuatazo zimepangwa kutekelezwa katika kipindi cha mwaka 2006/07: -

a)                 Kuandaa taarifa kuhusu fursa za uwekezaji katika miradi ya maendeleo ya viwanda (project profiles);

b)                 Kuendelea kutekeleza mkakati wa kuimarisha sekta ya ngozi na viwanda vya ngozi;

c)                  Kuwezesha na kuhamasisha uanzishaji wa viwanda  vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, maliasili na viwanda vya msingi;

d)                 Kuimarisha Mamlaka ya EPZ pamoja na BET ili kuongeza juhudi za kuongeza mauzo ya nje;

e)                 Kutekeleza mkakati wa kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji na kufuatilia utekelezaji wa tamko la serikali la kupiga marufuku utengenezaji wa mifuko laini ya plastiki;

f)                   Kuweka utaratibu wa kudumu wa biashara ya chuma chakavu;

g)                 Kuimarisha taasisi za utafiti na maendeleo ya viwanda hususan, CAMARTEC, TEMDO, TIRDO; na

h)                 Kushirikiana na Sekta Binafsi katika kubuni mikakati ya kuendeleza sekta ya viwanda kwa lengo la kukuza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

 

Mheshimiwa Spika,

80.            Wizara itaendelea kushirikiana na Wizara na Taasisi nyingine pamoja na Sekta Binafsi katika kubainisha na kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na matatizo ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu kwa wawekezaji. Aidha, Serikali itaendelea kuvutia na kuhamasisha wawekezaji wa nje na wa ndani kwa kubainisha fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali za viwanda na fursa za mitaji.  Pia, Wizara itaendelea kuhamasisha wananchi kwa kufanya kampeni ya ‘NUNUA BIDHAA ZA TANZANIA JENGA TANZANIA’. Aidha, wawekezaji watahamasishwa kuwekeza katika teknolojia mpya za kisasa ili kuzalisha bidhaa bora zinazoweza kuhimili ushindani.  Vile vile, Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi nyingine za kiafrika kupitia EAC na SADC ili kufungua masoko ya bidhaa za Tanzania katika nchi hizo. 

 

 

E.2:       Sekta ya Biashara

 

Mheshimiwa Spika,

81.              Katika mwaka 2006/07, Sekta ya Biashara inaandaa mikakati itakayouwezesha uchumi wa Taifa kuhimili ushindani na kuweza kushiriki kikamilifu na kufaidika na mfumo wa biashara katika mazingira ya utandawazi kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya uchaguzi.  Vile vile, Wizara itaendelea na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Biashara, katika kutekeleza malengo ya MKUKUTA. Aidha, masuala muhimu ni pamoja na kukuza na kuendeleza biashara na nchi mbalimbali, kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na nchi za Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati kwa lengo la kupanua wigo wa masoko badala ya kuendelea kutegemea masoko asilia ya nchi za Ulaya Magharibi. Aidha, Wizara yangu itatoa elimu kwa wananchi juu ya kanuni za masoko na biashara nchi za nje hususan Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki (EAC Customs Union) na nchi nyingine ambazo zinatoa upendeleo kwa bidhaa zinazozalishwa katika nchi zinazoendelea  kwa lengo la kupanua soko la bidhaa zetu na kuvutia wawekezaji.

 

Mheshimiwa Spika,

82.            Katika kuendeleza biashara, changamoto zinazoikabili sekta ya biashara ni uwezo mdogo wa uzalishaji wa bidhaa kukidhi mahitaji ya soko, kupanua wigo wa bidhaa tunazozalisha, kuhakikisha Tanzania inafaidika na fursa zinazotokana na majadiliano ya EPAs pamoja na fursa za masoko kikanda. Vile vile, kujenga na kudumisha mshikamano kati ya nchi maskini na zinazoendelea kushikilia msimamo wa kupinga vitendo vinavyosababisha biashara isiyo ya usawa na haki.  Kujenga na kudumisha mshikamano na nchi zilizoendelea kiviwanda ili zisaidie katika mchakato wa kutatua matatizo ya uzalishaji wa bidhaa na huduma zinazohimili ushindani wa soko. Kwa ujumla changamoto ni kuboresha urari kati ya mauzo na manunuzi nje nchi.

 

Mheshimiwa Spika,

83.            Katika kuitangaza Tanzania nje, Kituo cha Biashara cha Tanzania kilichopo London kitaendelea kushirikiana na Makampuni Binafsi, Mashirika na Mamlaka mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa mauzo ya bidhaa na mazao ya asili kwa lengo la kuliongezea Taifa mapato ya fedha za kigeni.  Kituo hiki cha biashara kitaendeleza mkakati wa kuitangaza Tanzania kiutalii katika vyombo vya habari nchini Uingereza. Aidha, Wizara yangu kupitia Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki cha Tanzania (COSOTA) itaendelea kuboresha zoezi la ukusanyaji wa mirabaha kutoka maeneo mbali mbali baada ya kuchapisha Kanuni za Usajili wa Wanachama na Kazi Zao ya mwaka 2005 (The copyright Registration of Members and their works Regulations 2005).

 

Mheshimiwa Spika,

84.            Katika kipindi cha mwaka 2006/07, BET itaboresha Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ambayo sasa yanatambulika na Chama Kinachosimamia Maonesho Duniani (Union des Foires Internationale - UFI).  Lengo ni kuendeleza viwanja vya maonesho vya Mwalimu J.K.Nyerere kufikia kiwango cha ubora wa Kimataifa.  Vile vile, BET itaendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wapatao 100, kuhusu ubora wa bidhaa, utaalamu wa kuuza nje kwa ujumla na jinsi ya kuzitumia fursa za upendeleo zinazopatikana katika masoko kadhaa. Aidha, Wizara itaendeleza kampeni ya “NUNUA BIDHAA ZA TANZANIA JENGA TANZANIA”.  Vile vile, nachukua fursa hii kuzipongeza Wizara zilizoshiriki kwenye Maonesho ya 30 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam na hasa Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ambazo zimeshiriki kwa mara ya kwanza. Natoa mwito kwa Wizara nyingine nazo kushiriki kwani hii ni fursa nzuri ya kuwaonyesha na kueleza umma wa Watanzania kuhusu fursa mbali mbali za shughuli za serikali kwa maendeleo ya wananchi. BET pia, itaendelea kufikisha huduma za kutoa habari za biashara “Tele-Centres” katika Mikoa ya Morogoro na Mbeya.  Kwa upande wa Zanzibar BET itaimarisha na kuongeza wafanyakazi na vitendea kazi.  Aidha, Serikali inakusudia kuiunda upya BET kuwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tanzania Trade Development Authority) yenye jukumu la kuendeleza biashara na wafanyabiashara.  Hatua hiyo inalenga kuiwezesha Mamlaka hiyo kusimamia maendeleo ya biashara vizuri zaidi.

 

Mheshimiwa Spika,

85.            Sekta ya Biashara katika kipindi cha mwaka 2006/07 itaendelea kutekeleza yafuatayo:-

 

a)                 Kuendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Biashara;

b)                 Kuainisha na kuandaa mkakati wa utekelezaji wa fursa zitokanazo na  makubaliano ya WTO;

c)                  Kuendelea kufanya mashauriano na wadau kuhusu programu ya kuainisha matatizo yanayokwamisha biashara (Diagnostic Trade Integration Study - DTIS);

d)                 Wizara  kwa kushirikiana na DANIDA itafadhili watumishi 26 wa Wizara, Idara za Serikali, Sekta Binafsi na Asasi  zingine kuchukua mafunzo ya Shahada ya Uzamili ya Biashara ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

e)                  Kuendeleza shughuli za vituo vya kupokelea na kutolea taarifa mbalimbali zilizoanzishwa na mpango wa pamoja (UNCTAD/WTO/ITC) wa kujenga uwezo wa kitaalamu katika muasuala ya biashara;

f)                   Kuendelea na majadiliano ya EPAs baina ya nchi zinazoendelea na Jumuiya ya Ulaya;

g)                 Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwa ni pamoja na kukamilisha utaratibu wa uandikishaji wa biashara badala ya utaratibu wa utoaji wa leseni;

h)                 Kuendeleza mkakati wa kurasimisha biashara; na

i)                   Kamati ya Kitaifa ya kusimamia utekelezaji wa mpango wa AGOA itaimarishwa kwa madhumuni ya kutoa ushauri katika masuala ya utekelezaji na uenezaji wa taarifa za masoko kwa Sekta Binafsi ili waweze kuuza zaidi kupitia mpango wa AGOA;

 

 

 

 

E.3:   Sekta ya Masoko

 

Mheshimiwa Spika,

86.            Malengo ya sekta ya Maendeleo ya Masoko ya mazao na bidhaa za kilimo kwa mwaka 2006/07 ni kuendelea na jitihada za kuwezesha mazao ya wakulima kuuzwa kwa bei ya kuridhisha kulingana na mahitaji ya ubora wa soko la ndani na nje. Vile vile, mwelekeo wa sekta ya masoko ya mazao ya kilimo ni kuendeleza usindikaji wa mazao yanayozalishwa hapa nchini ili kuongeza thamani na nafasi za ajira. Pia, kuhakikisha upatikanaji wa masoko kwa bidhaa zisizokuwa za kilimo.

 

Mheshimiwa Spika,

87.            Changamoto zinazoendelea kukabili masoko ya mazao na bidhaa za kilimo nchini ni pamoja na kuporomoka mara kwa mara kwa bei za mazao katika masoko ya Kimataifa; miundombinu duni ya masoko ya mazao; uzalishaji mdogo usiokidhi wingi na viwango vya ubora unaohitajika katika masoko ya Kimataifa; kuongezeka kwa ushindani wa Kimataifa usiokuwa wa haki; kuongezeka kwa matumizi ya mazao na bidhaa mbadala; na kuwepo kwa magonjwa ya mifugo na mimea yanayoathiri Biashara ya Kimataifa.

 

Mheshimiwa Spika,

88.            Ili kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika, Wizara imepanga kufanya mambo yafuatayo katika kipindi cha mwaka 2006/07:-

 

a)                 Kukamilisha Sera na Mkakati wa Masoko ya Mazao ya Kilimo nchini;

b)                 Kuimarisha na kuendeleza mfumo wa ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa taarifa za masoko;

c)                  Kuwezesha mchakato wa ujenzi wa masoko ya Kimataifa ya mazao ya kilimo na bidhaa zake;

d)                 Kufanya tathmini ya uboreshaji wa miundombinu ya masoko;

e)                 Kukamilisha Kitabu cha Orodha ya Wanunuzi na wasindikaji wa mazao;

f)                   Kuelimisha wadau kuhusu maendeleo ya masoko ya mazao na bidhaa ndani ya nchi na katika Jumuiya za Ushirikiano wa Kibiashara (EAC, SADC, EU) na nchi nyingine;

g)                 Kuimarisha uwezo wa Halmashauri na Manispaa kukusanya na kusambaza taarifa za masoko;

h)                 Wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na wadau wengine kuratibu na kusimamia Programu ya Kuendeleza Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo;

i)                   Kuendelea kutekeleza Mradi wa Kuendeleza na Kuboresha Biashara ya Pamba na Kahawa hususan utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani; na

j)                   Kuendeleza soko la ndani kwa kukuza matumizi ya mazao na bidhaa mbali mbali zinazozalishwa nchini.

 

 

 

 

E.4:   Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo

 

Mheshimiwa Spika,

89.            Katika kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo kwa mwaka 2006/07, msukumo utawekwa katika kuhamasisha uanzishaji na uimarishaji wa viwanda vidogo na biashara ndogo. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma zinazolenga kuchochea uanzishaji na uimarishaji wa viwanda vidogo na biashara ndogo. Huduma hizi zitatolewa katika nyanja za ufundi, mafunzo, ushauri, masoko, habari na mitaji.

 

Mheshimiwa Spika,

90.            Mikakati mbalimbali italenga kutoa huduma kwa wajasiriamali wadogo hususan wanawake na vijana kwa lengo la kuongeza nafasi za ajira na kipato. Msukumo wa huduma za ufundi katika mwaka 2006/07 utalenga kujenga uwezo wa wajasiriamali kuzalisha kwa tija kwa kutafuta na kusambaza teknolojia zilizotengenezwa na kujaribiwa na taasisi mbalimbali za hapa nchini. Aidha, SIDO itawawezesha wajasiriamali kuanzisha miradi ya usindikaji wa vyakula na kutoa huduma za ushauri wa kiufundi kwa wajasiriamali. Kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa, SIDO itatafuta maeneo na kuratibu ujenzi wa miundombinu na majengo kwa matumizi ya wajasiriamali wadogo.

 

Mheshimiwa Spika,

91.            Wizara itahamasisha zaidi huduma zitakazoweka msisitizo katika kusaidia maendeleo ya shughuli za uzalishaji na biashara vijijini hasa kujenga na kuimarisha uwezo wa wahunzi na makundi mengine. Aidha, huduma za kiatamizi zitaendelea kutolewa pamoja na huduma kwa wachimbaji wadogo wa madini katika maeneo mbalimbali ya nchi. Uzalishaji wa bidhaa za ngozi utahamasishwa kwa kutoa mafunzo na huduma kwa wazalishaji. Wizara yangu kupitia SIDO itaendesha kozi za ujasiriamali na uongozi wa biashara na kutoa mafunzo kwa wasindikaji wa vyakula na matunda. Pia, Shirika litatumia mbinu ya kuwaendeleza wazalishaji wadogo kwa kuwatumia wazalishaji na wafanyabiashara waliofanikiwa (mentorship program).

Mheshimiwa Spika,

92.            Wizara yangu itaendelea kuilea mifuko ya mitaji iliyopo na kuhakikisha kuwa mitaji inatolewa na kutumika kwa ufanisi. Aidha, Shirika litaendelea kutoa mitaji kwa wajasiriamali wadogo na kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya mitaji ya wajasiriamali.  Wizara itaendelea na juhudi zake za kuwawezesha wajasiriamali kushiriki katika masoko ya ndani na nje ya nchi na pia litaandaliwa kongamano la Kitaifa litakalowakutanisha wadau mbali mbali wa sekta kwa madhumuni ya kuzungumzia maendeleo ya sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo, hii ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo nchini.

 

E. 5:  Utafiti na Maendeleo

 

Mheshimiwa Spika,

93.            Katika kipindi cha mwaka 2006/07, taasisi za utafiti yaani CAMARTEC, TEMDO na TIRDO, zinalenga katika kubuni teknolojia zitakazokwamua matatizo yanayokabili sekta ya kilimo na viwanda hususan, viwanda vidogo na vya kati ambavyo havina uwezo wa kufanya utafiti vyenyewe. Hii ni pamoja na kuongeza uwezo wa taasisi hizi kwa kufundisha wataalamu wake. Lengo ni kuboresha na kuinua maendeleo ya sekta hizi muhimu.  Vile vile, taasisi hizi zinalenga katika kutangaza teknolojia wanazobuni na kuzitengeneza ili ziweze kufahamika na wengi na kupata wajasiriamali watakaozitengeneza kwa wingi na kuzisambaza kwa wananchi, kwa matumizi katika shughuli zao hususan, kilimo vijijini na kuanzisha viwanda vidogo huko vijijini vya kusindika mazao yanayozalishwa. Aidha, eneo lingine jipya litakaloshughulikiwa katika utafiti wa mashirika haya ni teknolojia ya mawasiliano.

 

Mheshimiwa Spika,

94.            Serikali itaendelea kuzitengea Taasisi hizi fedha za bajeti kupitia MKUKUTA na kutafuta wafadhili kwa lengo la kuziwezesha kuendelea na shughuli zao.  Vile vile, taasisi zenyewe zitaongeza nguvu katika kutangaza teknolojia walizobuni na kutengeneza ili kupata soko na kujipatia fedha.  Aidha, zitazingatia kubuni teknolojia kulingana na soko (demand driven) badala ya kuzitengeneza ndipo watafute soko.

 

E.6:   Usimamiaji wa Sheria za Udhibiti

 

Ubora

 

Mheshimiwa Spika,

95.            Katika mwaka 2006/07, TBS inalenga kukamilisha ununuzi wa vifaa muhimu vya Kituo cha Ufungashaji kwa lengo la kuongeza ubora wa ufungashaji wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kuhakiki vifungashio kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi.  Pia, Shirika linatarajia kuanza utekelezaji wa kiwango cha mita za teksi na kukamilisha ujenzi wa maabara ya kemikali. Pia, Shirika litaendelea na hatua za kuthibitisha maabara za shirika na mifumo ya utendaji wa Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO certification) pamoja na kuhakikisha kuwa maabara zake zinaboreshwa ili kuweza kutoa huduma nzuri zaidi kwa wananchi.

Ushindani wa Haki

 

Mheshimiwa Spika,

96.            Tume ya Ushindani, baada ya zoezi la uteuzi wa wataalamu, katika kipindi cha mwaka 2006/07, itaendelea kutoa mafunzo kwa wataalam wake, kuelimisha umma na utekelezaji wa Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003.

 

Vipimo

 

Mheshimiwa Spika,

97.            Katika mwaka 2006/07, Wakala wa Vipimo unategemea kutekeleza majukumu yake yakiwemo: -

 

a)                 Kuhakiki vipimo vinavyotumika kwenye biashara;

b)                 Kutangaza majukumu ya Wakala ili wadau waweze kuelewa huduma zinazotolewa; 

c)                  Kushirikiana na taasisi nyingine hususan Wizara ya Kilimo, Chakula na Maendeleo ya Ushirika na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kuhakikisha wauzaji wa mazao ya kilimo wanatumia vipimo sahihi; na

d)                 Kuhakikisha mianya yote ya wizi na udanganyifu wa kutumia vipimo visivyokuwa sahihi na rasmi katika biashara vinakomeshwa.

 

Usajili

 

Mheshimiwa Spika,

98.            Katika mwaka 2006/07, BRELA itatekeleza yafuatayo:-

 

a)                 Kuanza kutekeleza mpango wa awamu ya tatu wa mwaka 2006/07-2008/09.  Katika kutekeleza mpango huu mambo ambayo yatazingatiwa ni kuboresha na kusimamia sheria, kuelimisha na kuhamasisha wadau wake kwa kutangaza huduma zake kupitia redio na luninga, kujenga uwezo wa ndani, kujenga na kutumia mbinu za kisasa za utekelezaji na kupanua wigo ili kupeleka huduma karibu na wananchi;

b)                 Kuboresha na kuzingatia mkataba wa huduma kwa wateja;

c)                  Kupunguza kero za wadau kwa kuanzisha mtandao wa kuratibu matatizo yanayojitokeza wakati wa kuwahudumia; na

d)                 Kuendelea kujijengea uwezo wa utendaji kazi na ufanisi wa utekelezaji kwa msaada wa MKUMBITA.

 

E.7:   Uendeshaji wa Wizara na Taasisi Zilizo Chini Yake

 

Mheshimiwa Spika,

99.            Wizara yangu inaweka mkazo katika kuzingatia misingi ya utawala bora na uwajibikaji. Wizara imeunda Kamati ya Uadilifu kufuatilia ukiukwaji wa maadili sehemu za kazi. Aidha, Kamati ya Ukaguzi wa matumizi na mapato ya Serikali imeundwa  ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma.

 

 

Vita Dhidi ya Rushwa

 

Mheshimiwa Spika,

100.       Katika juhudi za kupambana na rushwa, Wizara yangu imeendesha warsha nne za utawala bora na huduma kwa mteja kwa watumishi wake na watumishi wa wakala wa vipimo. Aidha, juhudi hizo zitaendelezwa katika mwaka wa fedha wa 2006/07 ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mkakati wa Wizara wa Vita dhidi ya Rushwa.

 

Mapambano Dhidi ya UKIMWI

 

Mheshimiwa Spika,

101.       Wizara yangu iliendelea kutekeleza mpango mkakati wa kudhibiti UKIMWI sehemu za kazi, ikiwa ni pamoja na kuandaa vipeperushi na kuendesha semina sita juu ya mbinu za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu kwa watumishi wa Wizara na Taasisi zake. Vile vile, katika mwaka 2006/07, Wizara yangu kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) itaendeleza juhudi hizo kwa lengo la kupambana na kupunguza athari zitokanazo na ugonjwa huu hatari. Wizara itapitia na kuboresha Mkakati wake wa kupambana na UKIMWI, ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya hali halisi ya maambukizi kwa watumishi wake.

 

Masuala ya Jinsia

 

Mheshimiwa Spika,

102.       Katika mwaka wa fedha 2005/06, Wizara yangu ilianzisha Dawati la Jinsia na Kuunda Kamati ya Jinsia ya Wizara pamoja na kuandaa mkakati wa kushughulikia masuala ya jinsia ambayo yanapaswa kuingizwa kwenye Sera, mipango, programu na katika utendaji wa kila siku. Aidha, Kamati za Jinsia zilianzishwa kwenye Mashirika, Taasisi na Wakala chini ya Wizara yangu, ili ziweze kuzingatia uingizaji wa masuala ya jinsia katika mafunzo na uzalishaji. Katika mwaka 2006/07, Wizara yangu imepanga kuendesha semina za uhamasishaji kuhusu masuala ya jinsia ili wafanyakazi waweze kuwa na uelewa wa jinsi ya kuyahusisha katika kazi zao za kila siku.

 

Mheshimiwa Spika,

103.       Katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuwa na utendaji kazi bora katika Utumishi wa Umma, Wizara yangu imeajiri jumla ya watumishi 20 kwa mwaka 2005/06. Aidha, Wizara imewapatia watumishi 35 mafunzo ya muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi kwa nia ya kuinua viwango vyao vya utendaji kazi.  

 

F:       MAKADIRIO YA BAJETI YA 2006/2007

 

Shukrani

 

Mheshimiwa Spika,

104.       Napenda kutumia nafasi hii kuzishukuru Nchi rafiki na Mashirika ya Kimataifa ambayo yamekuwa yakitoa misaada iliyoiongezea Wizara uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija zaidi.  Napenda kuzishukuru nchi za Austria, Canada, China, Denmark, Finland, Ireland, Uswis, India, Japan, Marekani, Sweden, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na nchi nyingine ambazo zimeendelea kuisaidia Wizara.  Aidha, napenda kuyashukuru Mashirika ya Sida, UNIDO, DANIDA, DFID, GTZ, ILO, IFAD, NORAD, WTO, UNCTAD, OECD, USAID, UNDP, OPEC Fund, JICA, WIPO, ARIPO, SECO na ITC.  Nazishukuru pia Taasisi za Kimataifa za Benki ya Dunia, Shirika la  ‘‘Common Fund for Commodities – CFC’’ na African Development Bank (ADB) kwa misaada na michango yao ya fedha na utaalamu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu na malengo ya Wizara.

 

Mheshimiwa Spika,

105.       Hoja hii ni matokeo ya kazi nzuri na ushirikiano wa karibu nilioupata kutoka kwa wenzangu katika Wizara, Mashirika, Wakala, Asasi, Taasisi na Makampuni yaliyo chini ya Wizara.  Naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Mhe. Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, Bw. Wilfred L. Nyachia, Katibu Mkuu, Bw. Godfrey Mkocha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara, Mashirika, Wakala, Asasi, Taasisi na Makampuni yaliyo chini ya Wizara kwa michango yao katika kufanikisha kazi za Wizara na kwa kuhusika na maandalizi ya Bajeti ninayoiwasilisha leo.  Nazishukuru pia Jumuiya na Taasisi za Sekta Binafsi, ikiwemo CTI, TCCIA na TPSF.  Aidha, nazishukuru taasisi za elimu ya juu na utafiti, hasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Chuo Kikuu Mzumbe na ESRF kwa michango yao ya mawazo wakati wa mikutano, warsha, semina na makongamano mbalimbali kuhusu Sekta za Viwanda, Biashara na Masoko.  Ushirikiano huu ni muhimu katika kuendeleza na kuimarisha Sekta za Viwanda, Biashara na Masoko kwa maendeleo ya Taifa letu.  Natoa pia shukrani za dhati kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa huduma muhimu ya kuchapa hotuba hii.

 

 

 

 

MAOMBI YA FEDHA

Mahitaji ya Fedha kwa Matumizi ya Maendeleo

 

Mheshimiwa Spika,

106.       Katika mwaka wa 2006/2007, Wizara inaomba Shilingi 3,002,000,000.00 kwa ajili ya shughuli za miradi ya maendeleo ya Viwanda, Biashara na Masoko.  Kati ya fedha hizi, Shilingi 326,000,000.00 ni fedha za ndani ambazo zitatumika katika shughuli za maendeleo ya Taasisi zilizo chini ya Wizara na Shilingi 2,676,000,000.00 ni fedha za nje kutoka kwa wahisani ambazo zitatumika kulipia tafiti za kitaalamu na vifaa kwa miradi mbalimbali itakayotekelezwa na Wizara.

 

Maombi ya Fedha kwa Matumizi ya Kawaida

 

Mheshimiwa Spika,

107.       Ili kutekeleza malengo na majukumu ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, katika kipindi cha mwaka 2006/2007 ninaomba Shilingi 15,654,086,000.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.  Kati ya fedha hizi, kiasi cha Shilingi 6,120,846,000.00 ni matumizi ya Wizara yenyewe na Shilingi 9,533,240,000.00 ni ruzuku kwa ajili ya mishahara na shughuli za kuondoa umaskini zinazofanywa na mashirika ya umma yanayosimamiwa na Wizara. 

 

Mheshimiwa Spika,

108.       Pamoja na hotuba hii, nimeambatisha majedwali na vielelezo mbalimbali ambavyo kwa pamoja vinatoa takwimu zitakazowezesha Waheshimiwa Wabunge kutafakari vizuri zaidi maendeleo na utendaji katika sekta za Viwanda, Biashara na Masoko.  Ninaomba takwimu hizi zichukuliwe kama sehemu ya vielelezo vya hoja hii.

 

G.      KUTOA HOJA

109.       Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.