HOTUBA
YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA FREDERICK
TLUWAY SUMAYE, MBUNGE, KUHUSU MAPITIO
NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI, 2002/2003 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA
OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE, 2002/2003
1. Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo Bungeni
na Mwenyekiti wa Kamati ya Kisekta ya Utawala iliyochambua bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili mapitio ya utekelezaji wa kazi
za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2001/2002 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa
mwaka 2002/2003. Aidha, naliomba Bunge
lako tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya
Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake pamoja na yale ya Ofisi ya Bunge kwa
mwaka 2002/2003.
2. Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze Mheshimiwa Dk. Abdallah Omar Kigoda, (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji na Mheshimiwa Basil Pesambili Mramba, (Mb), Waziri wa Fedha kwa hotuba zao nzuri ambazo zimeelezea kwa muhtasari hali ya uchumi nchini na mpango wa maendeleo na bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2002/2003. Kwa takriban siku tano Waheshimiwa Wabunge wamejadili hotuba hizo na kutoa michango yao ya mawazo na hatimaye kukubali kuipitisha bajeti hiyo ya Serikali. Ninapenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao na pia ninapenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kuwa Serikali itazingatia kwa makini ushauri wote uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika mipango mbalimbali na utekelezaji wake.
3. Mheshimiwa Spika, napenda vilevile kuishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge lako tukufu kwa kuchambua kwa makini bajeti na mpango wa maendeleo wa Serikali wa mwaka 2002/2003. Aidha, Kamati za Kisekta za Bunge lako tukufu zimepitia makadirio ya matumizi ya kila Wizara, Ofisi na Idara za Serikali zinazojitegemea. Napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa kamati zote kwa kazi kubwa na nzuri walizofanya.
4. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2001/2002 nchi yetu imempoteza kiongozi wetu mpendwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Dk. Omar Ali Juma. Aidha, Bunge lako tukufu limepata pengo kubwa baada ya kufariki kwa Mheshimiwa John Mangwangwa, aliyekuwa Mbunge wa Mpanda Magharibi na Mheshimiwa Sebastian Rukiza Kinyondo aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Vijijini. Vilevile, tumempoteza Mwandishi Mkuu wa Sheria marehemu Sigfried Lushagara ambaye sote tunakiri alikuwa mchapa kazi makini sana asiyechoka, aliyefanya kazi kwa muda mrefu na kwa tabasamu hata pale ambapo kazi yenyewe ni ngumu sana. Kwa hakika ametuachia pengo kubwa sana. Napenda nitumie fursa hii kutoa pole kwa wafiwa wote. Kwa marehemu wote hawa na wengine ambao sikuwataja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi.
9. Mheshimiwa Spika, Serikali zetu mbili zimeendelea kujenga mazingira ya kuwawezesha Watanzania kuimarisha Muungano. Mashirikiano kati ya Serikali zetu mbili yamezidi kukua na mawasiliano kati ya viongozi wa ngazi zote na kati ya wananchi yameongezeka. Wizara na Idara za Serikali zetu zimeendelea kubadilishana mawazo na uzoefu katika shughuli zao za kutoa huduma kwa wananchi. Wananchi wameongeza ushirikiano katika nyanja za michezo, utamaduni na biashara hivyo kuzidi kudumisha udugu. Aidha, viongozi wetu wa pande zote mbili za Muungano wameshirikiana kuhakikisha kuwa maelewano ya kisiasa yanapatikana ili kudumisha amani na utulivu nchini kote. Serikali zetu zote mbili zitaendelea kushirikiana kuondoa vikwazo vinavyokwamisha kuimarika kwa Muungano ili tuweze kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika.
10. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2001/2002 Bunge lako tukufu limepitisha jumla ya miswada ya sheria 30. Aidha, maazimio 28 yahusuyo masuala ya kitaifa na kimataifa yaliridhiwa. Serikali ilipokea na kuyafanyia kazi maoni na maagizo mbalimbali ya Kamati za Kudumu za Bunge na yale ya Kamati za Bunge za Kisekta. Taarifa za utekelezaji wa maoni na maagizo ya kamati hizo zimewasilishwa na nyingine zitaendelea kuwasilishwa katika Bunge lako tukufu. Vilevile, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali Bungeni nayo itawasilishwa kwenye mkutano huu wa Bunge lako tukufu. Katika mwaka 2002/2003, Ofisi ya Bunge itaendelea kusimamia mipango ya kuongeza elimu ya kibunge na mafunzo kwa watendaji, kuendeleza mahusiano ya mabunge na nchi nyingine na kuboresha huduma mbalimbali za kiutawala. Aidha, Serikali itaendelea kufanya matengenezo ya ofisi za Waheshimiwa Wabunge. Wizara ya Fedha imekwisha agizwa kutenga fedha za kufanya matengenezo hayo na fedha hizo zitaonyeshwa katika hati za fedha wanazopelekewa Makatibu Tawala wa Mikoa.
12. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/2002 idadi ya vyama vya siasa imeongezeka na kufikia kumi na saba baada ya vyama vinne vya siasa yaani Chama cha Ustawi Tanzania (CHAUSTA), Demokrasia Makini, The Forum for Restoration of Democracy (FORD) na Democratic Party (DP) kupata usajili wa kudumu. Hata hivyo, kutokana na masharti ya sheria inayosimamia vyama vya siasa, Chama cha Tanzania People’s Party (TPP) na Popular National Alliance (PONA) vilifutwa kwa kushindwa kutimiza baadhi ya masharti muhimu yanayowezesha chama chochote cha siasa kuwa hai. Hatua hiyo itapunguza idadi ya vyama vyenye usajili wa kudumu kuwa kumi na tano. Katika kipindi cha mwaka 2002/2003, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kuhakiki vyama vyenye usajili wa muda ili kukamilisha usajili wa kudumu. Aidha, itaendelea kupokea maombi mapya ya usajili, kuchambua taarifa za fedha na mali za vyama vya siasa na kutoa ushauri wa ufumbuzi wa migogoro ndani ya vyama.
13. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2001/2002, ukiondoa matukio ya uhalifu yaliyotishia usalama wa raia na mali zao, hali ndani ya nchi ilikuwa shwari. Majeshi yetu ya ulinzi na usalama yameendelea kutekeleza wajibu wao kikamilifu wa kulinda maisha ya raia na mali zao. Jeshi letu la ulinzi kwa kushirikiana na majeshi ya nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika pamoja na mataifa ya Marekani na Ufaransa yameshirikiana kwenye mazoezi na mafunzo ya kulinda amani kimataifa. Vilevile, kama kichocheo cha kuleta amani nchini, uzalendo, uwezo wa kujiajiri na nidhamu kwa vijana, Serikali imerejesha utaratibu wa kutoa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Vijana takriban 2,600 wa awamu ya kwanza kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani walianza rasmi mafunzo mwezi Oktoba 2001 katika kambi za Makutopora mkoani Dodoma na Ruvu mkoani Pwani.
14. Mheshimiwa
Spika, usalama wa maisha na mali za wananchi wa mikoa ya magharibi mwa nchi
yetu bado unatishiwa na idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi jirani. Hadi kufikia Mei 2002, nchi yetu ilikuwa na
wakimbizi wasiopungua 650,000. Idadi
hiyo ya wakimbizi nchini inaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi hususan wale
wanaoishi katika maeneo hayo. Tatizo
hilo la wakimbizi linaambatana kwa
karibu sana na kuzagaa kwa silaha zinazotumika katika ujambazi. Serikali
itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo
hayo ili kudhibiti athari zinazotokana na wakimbizi. Ili kuwawezesha wakimbizi wanaopenda kurudi makwao wafanye hivyo,
mazungumzo yamefanyika kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali za Rwanda na
Burundi kuhusu urejeshwaji wa wakimbizi hao.
Hadi kufikia mwezi Mei, 2002 jumla ya wakimbizi 79,265 walikuwa
wamerejeshwa makwao.
15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002/2003 Serikali itaendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kuboresha uwezo na kununua vitendea kazi vya kisasa ili kupambana na uhalifu nchini. Wahalifu ni watu wanaoishi miongoni mwa wananchi wema na mienendo yao inafahamika vizuri. Jeshi la Polisi ni dogo mno kuweza kudhibiti uhalifu wote uliopo nchini na hali halisi ni kwamba askari mmoja anahudumia wastani wa watu 1,300. Katika hali hiyo, mchango wa wananchi ni muhimu sana kuliko kutegemea polisi pekee. Nawahimiza wananchi wote kuwafichua wahalifu na kushirikiana na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola katika jukumu hilo kwani msingi wa ulinzi na usalama wa Watanzania ni Watanzania wenyewe. Hata hivyo, Serikali imeamua kuliongezea nguvu Jeshi la Polisi kizana ili liweze kupambana na wimbi la ujambazi.
Vilevile, Jeshi la Polisi litaangaliwa zaidi kinidhamu ili kuwatambua baadhi ya askari wanaoshirikiana na wahalifu na walio wazembe kazini ili kuwachukulia hatua kali.
16. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2001/2002 Serikali imeendelea kupambana na tatizo la madawa ya kulevya. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2001 madawa ya kulevya ya aina mbalimbali yalikamatwa yakiingizwa nchini. Aidha, matumizi ya bangi yaliongezeka katika baadhi ya maeneo nchini. Kwa mfano, katika operesheni maalum iliyofanyika katika kipindi cha Juni hadi Julai 2001 jumla ya kilo 249,000 za bangi zilikamatwa, ekari 106 za mashamba ya bangi zilitekelezwa na watuhumiwa 1,132 walifikishwa mahakamani. Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti ongezeko la madawa ya kulevya nchini kwa kuimarisha ukaguzi, doria, kutoa mafunzo, na kufanya operesheni za kudhibiti na kukamata wahalifu wanaohusika na utengenezaji, uingizaji na usambazaji wa madawa ya kulevya.
17. Mheshimiwa
Spika, pamoja na kujenga uvumilivu wa kisiasa Watanzania tunao pia wajibu wa
kudumisha uvumilivu wa kidini. Katiba
ya nchi yetu inamruhusu kila Mtanzania kuamini dini yoyote ili mradi
anazingatia sheria za nchi. Pale
yanapojitokeza matatizo ya kutoelewana kwa makundi ya imani moja au kati ya
makundi yenye imani tofauti njia za majadiliano zitumike kutatua matatizo
hayo. Aidha, pale inapojitokeza kuwa
katika utekelezaji wa majukumu ya mamlaka mbalimbali za Serikali panatokea
mgongano kati ya mamlaka hizo na vyombo na taasisi za dini, hatua za
majadiliano zitumike kufikia maelewano kwa kuzingatia sheria za nchi. Napenda kusisitiza kuwa imani ya dini
inamhusu mtu binafsi na sio busara kutumia imani hiyo kuanzisha chuki miongoni
mwa Watanzania.
Hali ya Chakula Nchini
18. Mheshimiwa
Spika kwa ujumla msimu wa mwaka 2000/2001 ulikuwa ni mzuri kwa uzalishaji wa
mazao ya chakula ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita. Mikoa yote ilipata chakula cha kutosha ukiondoa
maeneo machache ambayo hayakupata mvua za kutosha. Uzalishaji wa chakula ulikuwa takribani tani 7.69 milioni
ukilinganisha na mahitaji ya tani 8.14 milioni. Hivyo, tulijitosheleza kwa chakula kwa asilimia 94. Aidha, baadhi ya maeneo ya mikoa sita ya
Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Shinyanga, Singida na Iringa ndiyo yaliyokuwa na
upungufu kidogo wa chakula kutokana na kutopata mvua za kutosha. Hata hivyo, mikoa hiyo ilipata chakula toka
mikoa mingine kwa taratibu za soko.
19. Mheshimiwa
Spika, pamoja na hali ya kuridhisha ya chakula nchini, Serikali imekuwa
ikifuatilia hali ya chakula katika maeneo yaliyoainishwa kuwa na upungufu kwa
kufanya tathimini za mara kwa mara.
Kutokana na tathimini hizo, ilibainika kuwa baadhi ya familia katika
wilaya kumi zilikuwa zinahitaji msaada wa chakula. Wilaya hizo zilipatiwa msaada huo kupitia Shirika la Chakula
Duniani. Jumla ya tani 5,800
zilisambazwa katika wilaya za Ngorongoro, Simanjiro, Kiteto, Monduli, Mbulu,
Karatu, Same, Mwanga na Iringa Vijijini.
20. Mheshimiwa
Spika, mvua za kutosha zimenyesha mwaka huu katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa msingi huo,
tunategemea maeneo mengi yatajitosheleza kwa chakula, ingawa upo uwezekano wa baadhi ya maeneo kuwa na
upungufu kutokana na mvua zilizonyesha kupita kiasi au kukatika mapema. Kwa hali hiyo, napenda kuchukua fursa hii
kuwashauri wananchi kutumia kwa uangalifu chakula watakachokipata na kuweka
akiba.
21. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya mageuzi ya sera za uchumi na ustawi wa jamii ili kurekebisha na kufufua uchumi wetu. Katika mwaka 2001, uchumi wetu ulikua kwa asilimia 5.6 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.9 mwaka 2000. Mwenendo wa ukuaji huo unaonyesha dalili nzuri ya kuondoa kabisa umaskini nchini ifikapo mwaka 2020. Matokeo ya juhudi hizo ni pamoja na nchi yetu kuwa moja ya nchi nne duniani kufaulu kuingia katika mpango wa kusamehewa madeni (HIPC). Ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa kwa kuongoza juhudi hizo za kufufua uchumi wetu.
22. Mheshimiwa Spika, mojawapo ya vigezo vya kutuletea mafanikio katika kufufua uchumi ni uwezo wetu wa kuingia katika ulimwengu wa mashindano ya kibiashara. Mazingira ya utandawazi ni ya mashindano ambapo tusipojitahidi ama tutaachwa nyuma au tutabakia soko la wengine. Mazuri na mabaya ya utandawazi yamezungumzwa kwa kirefu katika vikao vya Shirika la Biashara Duniani ili kukinga kwa kiwango fulani viwanda na bidhaa za nchi maskini. Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya nchi maskini katika mfumo wa utandawazi. Kwa kutambua mchango huo Rais wetu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa aliteuliwa kuwa Mwenyekiti mwenza wa Tume ya Kimataifa ya kuangalia athari za jamii zinazoweza kuletwa na utandawazi. Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.
23. Mheshimiwa
Spika, Tanzania inayo nafasi nzuri ya kukuza uchumi ikiwa sote kwa pamoja
tutaelekeza nguvu zetu katika sekta za uzalishaji mali na zile za huduma za
kiuchumi.
Ili uchumi wetu uweze kukidhi gharama muhimu za
huduma za jamii za elimu, afya, maji na zile za kiuchumi ni lazima mambo
yafuatayo yafanyike:
· Kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuuza nje;
· Kuongeza ubora wa bidhaa ili kukidhi ushindani katika masoko;
· Kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vipya au kubinafsisha vilivyopo;
· Kuongeza ajira;
· Kuongeza mapato ya Serikali na
·
Kusimamia
na kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali.
24. Mheshimiwa Spika, kwa kiwango kikubwa, ukuaji wa uchumi umekuwa ukitegemea kilimo ambacho bado ni duni, na kina tija ndogo isiyolingana na jasho la mkulima. Kilimo chetu kimekuwa cha kutegemea mvua, zana duni na matumizi hafifu ya pembejeo na hivyo kwa kiasi kikubwa hakitabiriki kwa mavuno. Hivyo, upatikanaji wa chakula na mauzo ya bidhaa za kilimo zisizosindikwa nje ya nchi yamekuwa hayawezi kutabirika. Kwa hali hiyo, Serikali imeandaa Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ambao programu zake za utekelezaji zitaanza mwaka 2002/2003. Mkakati huo unalenga kuongeza uzalishaji, uhakika wa upatikanaji wa chakula, kuongeza kipato kwa kuboresha thamani ya mazao, na kuwawezesha wakulima wadogo kupata soko la kuaminika. Maeneo mengine ambayo yatapewa kipaumbele ni pamoja na upatikanaji wa uhakika wa mbegu bora za mazao ya chakula na biashara, upatikanaji wa mbolea kwa wingi na kwa utaratibu utakaomwezesha mkulima kuipata, kupanua matumizi ya wanyamakazi na matrekta na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Aidha, huduma za ugani kwa wakulima zitaimarishwa kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe, wataalam wa kilimo na viongozi wa utawala.
25. Mheshimiwa Spika, matumizi ya maarifa, yaani sayansi na teknolojia, ni lazima yaongezeke ili kutuwezesha kuwa na uchumi wa kisasa. Ongezeko la tija na upatikanaji wa ziada ya mazao ndiyo njia pekee ya kupiga vita umaskini vijijini, kupunguza mtiririko wa vijana kukimbilia mijini na kuongezeka kwa mauzo yetu nchi za nje. Ni vyema pia tuimarishe uhusiano kati ya sekta ya kilimo na ile ya viwanda kwa kuwianisha maendeleo ya sekta hizo ili sekta ya viwanda iweze kuwa kichocheo cha maendeleo ya sekta ya kilimo. Tunapokuwa na viwanda vya kusindika mazao yetu tunaongeza ajira kwa Watanzania, thamani ya mauzo nchi za nje inaongezeka na pia tunaongeza hamasa na motisha ya uzalishaji kwa vile kunakuwepo na soko la uhakika kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wetu. Serikali itaendelea kuhamasisha, kuwezesha na kuelekeza wawekezaji kujenga viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo ili kuinua sekta hiyo na kuondokana na utaratibu wa kuuza nje mazao yetu yakiwa ghafi.
26. Mheshimiwa
Spika, Tanzania ina rasilimali kubwa ya mifugo. Katika mwaka 2001/2002, jumla ya mitamba bora ya maziwa 950
ilizalishwa na kusambazwa kwa wananchi.
Kati ya hiyo, mitamba 75 ilipelekwa Zanzibar. Serikali iliendelea kuzishauri Halmashauri za Wilaya kutenga
maeneo ya mifugo na kuhakikisha wafugaji wanamilikishwa maeneo hayo na
wanayaendeleza. Aidha, ilikamilisha
ukarabati wa masoko ya mifugo ikiwa ni pamoja na minada ya mwanzo mitano, mnada mmoja mkubwa, ujenzi wa machinjio
ya kisasa na chuo cha ukataji nyama katika Manispaa ya Dodoma. Katika kipindi cha mwaka 2002/2003 mafunzo
ya ufugaji bora yatatolewa kwa wafugaji 300, kati yao 200 ni wanawake. Uimarishaji, usimamizi na uendelezaji wa nyanda za malisho utafanyika katika
maeneo 50 nchini na kutafuta vyanzo vya maji kwa ajili ya mifugo katika kanda
zenye ukame na kujenga malambo 100 katika mikoa minane. Vilevile, mashamba ya kuzalisha mbegu za
malisho ya Vikuge mkoani Pwani na Langwira mkoani Mbeya yataendelezwa.
27. Mheshimiwa Spika, soko la mazao ya kilimo na mifugo litaimarika na kutabirika ikiwa patakuwepo na ushirika imara wa wazalishaji. Wengi wa wakulima wetu ni wadogo na wanyonge ambapo nguvu ya unyonge wao ni umoja. Kuwekeza mitaji na rasilimali pamoja kwa wanyonge kunaongeza nguvu, uwezo wa kufanya shughuli za kiuchumi, kushindana katika mfumo wa soko na hivyo kujiletea maendeleo. Kwa kuelewa umuhimu huo, Serikali imeandaa upya Sera ya Maendeleo ya Ushirika ambayo imeweka mazingira mazuri zaidi ya kutekeleza mikakati mbalimbali ya kufufua, kuimarisha na kuendeleza ushirika nchini. Mkazo katika sera hiyo umewekwa katika kujenga vyama vya msingi na kupanua wigo wa ushirika ili kuhusisha sekta nyingine kama uvuvi, ufugaji, na biashara ndogo ndogo. Serikali itaendeleza juhudi zake za kujenga upya ushirika kwa kuanzia na vyama vya msingi kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe katika kuunda, kumiliki, kuendesha na kuhakikisha kwamba viongozi wanakuwa mstari wa mbele kujiunga na ushirika ili kuonyesha mfano kwa wengine. Aidha, Serikali itaandaa sera na mkakati wa kuimarisha mfumo wa masoko ya mazao ya kilimo na mifugo nchini ikiwa ni pamoja na miundo mbinu ya masoko.
28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/2002 uzalishaji katika baadhi ya viwanda vyetu umeongezeka. Sekta ya viwanda ilikua kwa asilimia 5.0 katika mwaka 2001 ikilinganishwa na asilimia 4.8 mwaka 2000. Uzalishaji umeonyesha maendeleo mazuri katika viwanda vya madawa ya binadamu, sabuni, usagishaji wa nafaka, sigara, mafuta ya kupikia, saruji, nondo, vinywaji baridi na bia. Mafanikio hayo ni matokeo ya sera yetu ya ubinafsishaji. Hata hivyo, kumekuwa na mapungufu katika ufuatiliaji wa viwanda na mashirika yaliyobinafsishwa. Kumekuwa na ugumu wa utoaji taarifa kutoka kwenye mashirika na viwanda vilivyobinafsishwa kwa dhana potofu kwamba jukumu la Serikali linakoma baada ya kutiliana saini mikataba ya mauzo. Nia ya Serikali katika kufuatilia mashirika na viwanda vilivyobinafsishwa ni kwanza, kutambua mafanikio ya sera yetu ya ubinafsishaji na pili, kubaini matatizo na hivyo kwa kushirikiana na wawekezaji kutafuta ufumbuzi.
29. Mheshimiwa Spika, lengo kubwa la ubinafsishaji ni kupanua uzalishaji, kuingiza teknolojia mpya, kuongeza mapato ya Serikali, kuongeza tija, ajira na kuingiza mbinu mpya za uongozi. Bila kufuatilia mashirika na viwanda hivyo, Serikali haitaweza kufahamu kama malengo hayo yamefikiwa na kwa kiwango gani. Natoa wito kwa wawekezaji wote walionunua mashirika na makampuni ya umma watoe ushirikiano wa karibu kwa Wizara zinazohusika ili wapate taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu ufanisi wa viwanda walivyonunua. Kwa wale wawekezaji ambao hawatatoa ushirikiano huo, basi masharti ya mikataba ya mauzo yatachukua mkondo wake. Wizara zote kwa kushirikiana na Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma zimekwisha agizwa kutoa kipaumbele kwa kazi hiyo ya ufuatiliaji.
30. Mheshimiwa Spika, sheria kuhusu uanzishwaji na uendelezaji wa maeneo maalum ya uzalishaji kwa ajili ya kuuza bidhaa nje ya nchi imeanza kufanya kazi. Kutokana na sheria hiyo, Tanzania sasa imejiwekea mazingira mazuri ya kuinua viwango vya mauzo nje kwa sababu bidhaa zitakazozalishwa katika mfumo huo zitaweza kuhimili ushindani katika soko la kimataifa kutokana na kutoa vivutio mbalimbali ambavyo vitapunguza gharama za uzalishaji. Maeneo maalum ya uzalishaji yamegawanywa katika sehemu mbili: moja ni mitaa ya viwanda na pili ni uteuzi wa kiwanda kimoja kimoja kuwa eneo maalum la uzalishaji. Kwa sasa kiwanda cha nguo cha URAFIKI kimekwishateuliwa kama eneo maalum la uzalishaji. Kimsingi, maeneo haya maalum yatawezesha Taifa kukuza mauzo nje na pia kuiwezesha nchi yetu kushiriki katika biashara inayochochewa na utandawazi na hivyo kunufaika na masoko ya Afrika Mashariki, Nchi za Kusini mwa Afrika, Soko la Marekani kupitia mpango wa AGOA na Soko la Ulaya kupitia makubaliano ya Cotonou. Viwanda vitakavyokuwa chini ya maeneo maalum ya uzalishaji vitakuwa pia soko la ndani la uhakika kwa bidhaa za sekta za kilimo, mifugo, madini, misitu na uvuvi na hivyo kuwa na ongezeko la ajira na kipato cha mwananchi. Hata hivyo, ni vyema wazalishaji wetu wakafahamu kuwa masoko hayo hayapokei bidhaa hizo kwa sababu tu zimetengenezwa katika nchi inayoendelea. Ni lazima bidha zetu ziwe bora na zenye uwezo wa kushindana katika soko.
31. Mheshimiwa Spika, mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi na kiteknolojia yametokea duniani ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mfumo huria wa biashara na maendeleo ya kasi ya teknolojia kwa kutumia kompyuta. Mabadiliko hayo yanalenga katika kupanua wigo wa masoko na biashara. Ili Tanzania iweze kunufaika kikamilifu na mabadiliko hayo, Serikali inaandaa sera mpya ya biashara ambayo lengo lake ni kuchochea mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa Taifa kutoka uchumi wenye mfumo duni wa uzalishaji na ugavi kuelekea mfumo imara wa uchumi wenye uwezo wa kuhimili ushindani wa biashara kimataifa na ule wa kushiriki na kufaidika na mfumo wa biashara na utandawazi. Sera hiyo itazingatia fursa zinazojitokeza, changamoto zinazoendelea na mfumo wa sasa duniani na mabadiliko tunayopaswa kufanya kimkakati ili kuwezesha Tanzania kuhimili mwenendo wa uchumi kimataifa. Sambamba na utekelezaji wa Sera hiyo, Serikali pia itaendelea kuzuia nchi yetu kugeuzwa soko la bidhaa hafifu au duni kutoka nje. Serikali itawasilisha kwenye Bunge lako tukufu mapendekezo ya sheria ya kuzuia uingizaji wa bidhaa hafifu nchini na uuzaji wa bidhaa kwa bei za chini kuliko bei za bidhaa hizo katika nchi zilikozalishwa. Aidha, itachukua hatua za kulinda bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu ili kuondoa ushindani usio wa haki. Hata hivyo, ieleweke kuwa viwanda vyetu vina wajibu wa kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kuongeza ubora wa bidhaa zao. Viwanda havitalindwa dhidi ya ushindani halali.
32. Mheshimiwa Spika, Tanzania inaanza kujulikana duniani kama kivutio mahsusi cha watalii. Utalii ni moja ya sekta za biashara ambayo inakua kwa kasi kubwa. Katika mwaka 2001 idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka kufikia watalii 525,122 ikilinganishwa na watalii 501,669 waliofika mwaka 2000. Aidha, hoteli zenye hadhi ya kitalii ziliongezeka kwa asilimia 2 kutoka 326 mwaka 2000 hadi 329 mwaka 2001. Hali kadhalika, sekta hiyo ilitoa ajira mpya za moja kwa moja kwa Watanzania 450 kutoka nafasi za ajira 156,050 mwaka 2000 hadi 156,500 mwaka 2001. Napenda niwapongeze wote kutoka Serikalini na sekta binafsi wanaofanya bidii kutangaza utalii wetu na kuhudumia watalii. Wananchi pia wanayo nafasi kubwa kuchangia uendeshaji wa sekta hiyo kwa kushiriki katika biashara hiyo kwa kujenga mahoteli ya kisasa, kuendesha kampuni za kitalii, kampuni za uwindaji na kuendeleza utalii wa kitamaduni hasa ule wa vijijini na wa maeneo ya mambo ya kale. Hata hivyo, ili tufikie malengo hayo ni lazima tuongeze juhudi katika kujitangaza na pia kuweka miundo mbinu bora katika sehemu mbalimbali ili kuvutia wawekezaji. Aidha, tuwahamasishe wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za utalii, kwa kulinda vivutio vyetu kama vile wanyama na kwa wao wenyewe kutalii katika mbuga za wanyama, maeneo ya kale na kupanda milima.
33. Mheshimiwa
Spika, sekta ya madini imeendelea kutoa mchango mkubwa katika Pato la
Taifa. Mauzo ya madini nje ya nchi
yameongezeka kwa asilimia 69 kutoka Dola za Marekani 185.06 milioni mwaka 2000
hadi Dola za Marekani 311.9 milioni mwaka 2001. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2001 sekta hiyo imetoa ajira ya
kudumu kwa Watanzania 3,300 katika makampuni makubwa manne ya uchimbaji wa
dhahabu ya Geita Gold Mining, Kahama Mining
Corporation Limited, Afrika
Mashariki Gold Mines na East Africa Gold Mines Limited. Ni dhahiri kwamba sekta hiyo
imekuwa ni kielelezo kizuri cha mafanikio ya uwekezaji yanayoweza kupatikana
kutokana na sera nzuri, vivutio vya kutosha na mfumo mzuri wa kisheria,
kiutawala na wa kodi. Serikali
itaendeleza sekta hiyo ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa
uchumi, ajira na pia kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapa mafunzo, kuwakopesha
zana za kisasa na kuwapa soko la uhakika.
Aidha, utaratibu mzuri wa biashara na masoko ya madini unaandaliwa kwa
kuanzia na vito vya thamani na hatimaye kwa madini yanayochimbwa na makampuni
makubwa ili kudhibiti hitilafu mbalimbali katika biashara hiyo.
34. Mheshimiwa Spika, kutokana na nchi
yetu kuwa na eneo kubwa na ili tuweze kuharakisha ukuaji wa uchumi wetu hatuna
budi kuwekeza katika ujenzi wa miundo mbinu ya kisasa. Barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari,
simu, posta, kompyuta na nishati ni mambo muhimu sana kwa ujenzi wa uchumi wa
kisasa. Kwa upande wa barabara,
taratibu za kusimamia ujenzi na utunzaji wa barabara kupitia Mfuko wa Barabara
na Wakala wa Barabara zimekamilika.
Hivyo, ni vyema sasa tuendelee kuimarisha uwezo wa kuhimili matengenezo
ya mara kwa mara ili misaada na mikopo mipya kutoka kwa wafadhili itumike
kujenga kule ambako bado hakuna barabara nzuri. Wizara ya Ujenzi, Bodi na Menejimenti ya Mfuko wa Barabara
zisimamie ipasavyo matumizi ya Mfuko huo ili fedha zake zitumike kikamilifu katika
kufanya ukarabati, matengenezo ya kawaida, ya muda maalum na yale ya dharura ya
barabara kuu za mikoa na zile za wilaya na miji. Aidha, taarifa za utekelezaji na matumizi ya fedha za Mfuko huo
ziwasilishwe kwa wakati. Kutokana na
uwezo mdogo wa Serikali katika kukidhi haja ya matengenezo ya barabara nchini
na hasa zile za vijijini ni muhimu wananchi washirikishwe katika matengenezo ya
barabara katika maeneo yao. Serikali
itaimarisha ushirikishwaji huo kwa kutoa mafunzo ya teknolojia ya nguvu-kazi ili
wananchi waweze kuongeza uwezo wao wa kufanyia marekebisho barabara zilizoko
katika maeneo yao mara zinapoharibika bila kusubiri Serikali.
35. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kutekeleza utaratibu wa kujenga na kutunza barabara kwa kutumia
uwezo wetu wenyewe. Serikali ilianzisha Mfuko Maalum wa kujitegemea kwa ajili
ya kugharamia ujenzi wa mradi maalum wa barabara kuu kiwango cha lami mwaka
2001/2002. Katika kipindi cha miaka
mitano kuanzia mwaka 2001/2002, Serikali itajenga barabara zifuatazo kwa
kiwango cha lami: Somanga-Matandu, Nangurukuru-Lindi, Lindi-Mingoyo,
Dodoma-Manyoni na Manyoni-Singida. Katika kipindi cha mwaka 2001/2002, usanifu
wa barabara ya Somanga-Matandu pamoja na daraja la Mto Matandu ulikamilika na
kazi ya ujenzi itaanza mwezi Julai 2002.
Kuhusu barabara ya Dodoma-Singida na Nangurukuru-Lindi-Mingoyo tayari
Wahandisi Washauri wameteuliwa na wamekwishaanza kazi. Ujenzi wa barabara hizo utaanza katika mwaka
wa fedha 2002/2003. Pamoja na utaratibu huo wa kujenga uwezo wetu na kuanza
kujitegemea, Serikali itaendeleza azma yake ya kukaribisha sekta binafsi katika
ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kwa mpango wa Jenga, Endesha na
Kabidhi. Maeneo ambayo utaratibu huo
unaweza kutumika ni pamoja na Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara, Ukanda wa Kati,
ujenzi wa daraja la Kigamboni na maeneo mengine ambayo yatawavutia wawekezaji
wa aina hiyo.
36. Mheshimiwa
Spika, pamoja na juhudi hizo, Serikali bado inaendelea kushirikiana na wahisani
mbalimbali katika kujenga baadhi ya barabara zetu kuu. Kwa mfano, Barabara ya Singida – Shelui iko
katika hatua ya kukamilisha usanifu na nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi
kwa mkopo wa fedha za Benki ya Dunia.
Barabara ya Shelui – Nzega iko
katika hatua ya ujenzi kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya
Afrika. Tathmini ya zabuni ya ujenzi wa
barabara ya lami ya Ilula – Shinyanga – Tinde – Nzega na Tinde – Isaka iko katika hatua za mwisho kukamilika na
ujenzi wa barabara hiyo utagharimiwa kwa fedha za msaada kutoka Jumuiya ya Nchi
za Ulaya. Ujenzi wa barabara ya
Mutukula – Muhutwe – Kagoma unaendelea kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya
Maendeleo ya Afrika na OPEC. Aidha,
maandalizi ya nyaraka za kuitisha zabuni ya ujenzi wa barabara ya Kagoma –
Biharamulo – Lusahunga kwa mkopo wa
fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika yanaendelea. Hizo ni baadhi ya barabara zinazotengenezwa chini ya mpango wa
Serikali wa kujenga barabara kuu nchini.
37. Mheshimiwa Spika, sekta ya mawasiliano nchini ilikua kwa asilimia 6.3 mwaka 2001 ikilinganishwa na asilimia 6.1 mwaka 2000. Teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo hivi sasa ndiyo chimbuko la mageuzi makubwa ya kiuchumi duniani imeanza kupewa nafasi inayostahili nchini. Teknolojia hiyo ni nyenzo muhimu inayotumika duniani katika kupunguza pengo lililopo katika nyanja zote baina ya mtu na mtu, jamii na jamii, nchi na nchi na makundi ya nchi. Teknolojia hiyo ikitumika ipasavyo inaweza kuunganisha nguvu za watu, nchi na makundi ya nchi kushirikiana kikamilifu kuainisha ujuzi na rasilimali zilizopo kwa lengo la kupambana na umaskini, ujinga na maradhi. Kwa kuzingatia manufaa hayo na ukweli kwamba teknolojia hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya shughuli za sayansi, kijamii, utamaduni, siasa na uchumi, Serikali inakamilisha maandalizi ya Sera ya Taifa kuhusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
38. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2002/2003, Serikali itasimamia uandaaji wa Programu ya Taifa kuhusu utekelezaji wa shughuli za teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kuandaa mazingira mazuri ya uanzishwaji wa Taasisi ya Kitaifa itakayoshughulikia masuala yote yanayohusiana na teknolojia hiyo. Aidha, Serikali itashirikiana na wadau wengine katika kutekeleza miradi ya kuweka mitandao ya mawasiliano katika maeneo ya utawala bora Serikalini, kilimo, biashara, elimu, afya na utalii. Miradi mingine itakayopewa msukumo wa pamoja ni ile ya kupeleka huduma za simu na umeme hadi vijijini ambayo ndiyo uti wa mgongo wa huduma za teknolojia ya habari na mawasiliano.
39. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
mwaka 2001/2002, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine imewaelimisha
wananchi kuhusu sera na sheria mpya ya ardhi. Ili kuhakikisha matumizi bora ya
ardhi yanakuwepo huko vijijini, Serikali imetoa mafunzo kwa wananchi katika
wilaya saba kuhusu miongozo ya ushirikishwaji katika mipango na usimamizi wa
matumizi bora ya ardhi vijijini. Wilaya hizo ni Kiteto, Ngorongoro, Bagamoyo,
Kibaha, Kilosa, Handeni na Morogoro Vijijini. Katika mwaka 2002/2003, Serikali
itaendelea na utayarishaji wa matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo kwa
ajili ya uwekezaji katika utalii, mashamba makubwa, ranchi, viwanda na maeneo
huru ya uzalishaji mazao ya biashara.
Vilevile, hatua zitachukuliwa kuzuia uharibifu wa ardhi na maliasili
zake kwa kuelekeza matumizi endelevu ya kilimo, ufugaji, makazi, misitu na
uchimbaji madini kwa ajili ya mahitaji ya matumizi ya sasa na baadaye. Aidha, Serikali itahakikisha kuwa migongano
na migogoro ya matumizi ya ardhi katika wilaya na vijiji vyake baina ya watumiaji
mbalimbali hususan kati ya wafugaji na wakulima inapungua. Serikali pia itaendelea kuwaelimisha
wananchi hasa walio vijijini kuwa mtaji wao mkubwa ni ardhi ambayo ina thamani
na inaweza kutumika katika kupata mikopo kutoka vyombo vya fedha au kama hisa
kwenye miradi ya uwekezaji. Ili kufanikisha
suala hilo, maeneo yenye utata katika sheria husika yataangaliwa upya kwa lengo
la kuyafanyia marekebisho. Vivyo
hivyo, Serikali itawashirikisha kikamilifu wananchi na sekta binafsi katika
utayarishaji wa matumizi bora ya ardhi vijijini.
40. Mheshimiwa Spika, ili ardhi iweze kuendelea kuwa na thamani hatuna budi kuchukua hatua madhubuti za kulinda na kuhifadhi mazingira. Umuhimu wa hifadhi ya mazingira hasa katika mazingira ya soko huria wenye ushindani wa kibiashara unapaswa kupewa msukumo unaostahili kwani shughuli za kijamii na za kiuchumi ambazo hazizingatii hifadhi ya mazingira zina athari kubwa kwenye maji, udongo, hewa na pia afya ya viumbe wengine. Serikali imelipa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira madaraka na mamlaka ya kusaidiana na wadau wote katika kuratibu hifadhi ya mazingira. Katika mazingira ya kiuchumi na kisiasa tuliyonayo hivi sasa ni wajibu wetu kama Taifa kuhakikisha kuwa miradi yote inayoanzishwa nchini inafanyiwa tathmini ya athari ya mazingira. Aidha, ni muhimu kwa wenye miradi inayoanzishwa au ile ambayo tayari inafanya kazi kuzingatia na kutekeleza ushauri unaotolewa na Baraza kila mara. Kwa upande wa wananchi ni vyema sote kwa pamoja tupige vita uchomaji moto ovyo na tuendeleze hifadhi ya vyanzo vya maji. Kwa maeneo ya mijini, Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe kuwa mifumo ya maji machafu haiwi chanzo cha uchafuzi wa mazingira. Ukaguzi wa mara kwa mara ufanyike na kuwaadhibu wale wote wasio zingatia masharti ya ujenzi katika miji.
41. Mheshimiwa Spika, uzalishaji umeme
mwaka 2001 iliongezeka kwa asilimia 9.5 kutoka saa za gigawati (GWh) 2,484
milioni mwaka 2000 hadi saa za gigawati (GWh) 2,746 milioni mwaka 2001. Ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa
mahitaji ya umeme na kupatikana kwa mvua za kutosha. Hata hivyo, ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa TANESCO
hususan katika kuboresha mapato yake, huduma kwa wateja, uendeshaji na hatimaye
kuiandaa TANESCO kubinafsishwa, Serikali ilibadilisha menejimenti ya Shirika
hilo kwa kuajiri Kampuni ya NETGroup Solutions ambayo ilianza kazi mwezi Mei
2002. Napenda nitoe wito kwa
wafanyakazi wote wa TANESCO na wananchi kwa ujumla watoe ushirikiano mzuri kwa
Kampuni hiyo ili tuweze kufikia malengo yetu kama yalivyopangwa. Serikali
itahakikisha kuwa wafanyakazi wanaelimishwa, wanafahamishwa na wanashirikishwa
katika kila hatua ambayo itakuwa imefikiwa wakati zoezi la ubinafsishaji
linafanyika ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima. Napenda kusisitiza kuwa zoezi la ubinafsishaji halihusiani na
menejimenti mpya na wala halifanyiki sasa hivi.
42. Mheshimiwa Spika, ili kuwapatia wananchi nyenzo nafuu za nishati pasipo kuathiri mazingira, Serikali itaendeleza juhudi zake za kupeleka umeme vijijini. Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika inatayarisha Mpango Kamambe wa Umeme Vijijini ambao utaainisha njia mbalimbali za kupeleka umeme vijijini katika kipindi cha miaka kumi na tano. Mshauri Mwelekezaji ataanza kazi kabla ya mwisho wa mwaka 2002 na itamchukua kipindi cha miezi kumi na saba kukamilisha kazi yake. Sambamba na mpango huo, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Sweden inaandaa taratibu za kuanzisha kitengo maalum kitakachojulikana kama Rural Energy Agency ambacho kitajihusisha na utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini. Aidha, mfuko wa Rural Energy Fund utaanzishwa kwa ajili ya miradi hiyo. Pamoja na juhudi hizo za Serikali, wananchi waendelee kuelimishwa na kuhamasishwa kutumia nishati mbadala kama zile zinazotokana na mionzi ya jua, upepo na gesi ya kinyesi cha wanyama kwani zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wanatumia nishati ya kuni na mkaa, jambo ambalo linaathiri mazingira.
43. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2001/2002 Serikali imechukua hatua za kuimarisha
huduma za jamii kwa kuhakikisha kuwa sekta hizo zinapata kiasi kikubwa cha
fedha. Kuhusu sekta ya afya, Serikali
imeendelea kutekeleza mabadiliko katika sekta hiyo kwa kusimamia uanzishwaji wa
Bodi za Afya za Wilaya; kamati za afya na vituo vya afya na zahanati. Aidha,
imeendelea kuzijengea uwezo zaidi kamati za uendeshaji wa huduma za afya za
wilaya ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfuko wa pamoja wa afya. Serikali pia imechukua hatua za kuimarisha
huduma za Mfuko wa Bima ya Afya ambazo zilianza kutolewa rasmi tarehe 1 Oktoba,
2001. Katika utekelezaji wa huduma za mfuko huo imedhihirika kuwa pamoja na
matatizo ya awali, wadau wote wanakubaliana kuhusu dhana ya bima ya afya. Wanachama wamebaini manufaa makubwa yakiwemo
ya familia kupata huduma bora bila kulazimika kuzilipia papo kwa papo.
Hospitali pia zinaanza kutambua kuwa kuwahudumia wanachama wa mfuko ni chanzo
kizuri cha kuinua kipato chao. Hadi
mwezi Mei 2002 jumla ya shilingi 9.45 bilioni zimepatikana katika Mfuko huo
kama michango ya wanachama na mwajiri wao, yaani Serikali. Aidha, jumla ya
shilingi 52.4 milioni zimetumika kulipia gharama za matibabu ya watumishi na
familia zao. Hata hivyo, Mfuko
unaendelea kufanyia kazi mapungufu machache yaliyodhihirika katika muda huo
mfupi wa mwanzo.
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2002/2003 Serikali itaanza kutekeleza mpango wa ukarabati katika sekta ya afya. Awamu ya kwanza ya mpango huo itahusisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali tatu na zahanati thelathini na mbili na ujenzi wa kituo kimoja cha afya katika Jiji la Dar es Salaam na ununuzi wa vifaa vya hospitali na samani. Aidha, utafiti wa kuimarisha huduma za matibabu katika mikoa ya Mara, Mtwara na Tabora utafanyika.
45. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa maendeleo wa elimu ya msingi wa miaka mitano yaani 2002 hadi 2006. Lengo kuu la mpango huo ni kurejesha elimu ya msingi kwa watoto wote. Moja ya maamuzi muhimu yaliyotolewa na Serikali ni kuhakikisha kuwa watoto wote waliofikisha umri wa kuanza darasa la kwanza yaani miaka saba wanaandikishwa kuanzia Januari 2002. Hali ya utekelezaji wa uamuzi huo ni nzuri kwani idadi ya wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2002 imefikia watoto 1,558,480 ambao ni ongezeko la asilimia 40 ukilinganisha na watoto 1,100,000 walioandikishwa mwaka 2001. Serikali vilevile,
imeanzisha utaratibu maalum wa kuwapa elimu ya msingi watoto wote wa umri wa miaka zaidi ya saba hadi miaka kumi na tatu.
46. Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa maelekezo kwa wote wanaosimamia mpango huo katika ngazi za Halmashauri za Wilaya na Mikoa kuzingatia taratibu za kuandikisha na kufundisha katika shule za msingi. Kwa mfano, pale idadi ya wanafunzi inapozidi watoto 45 katika chumba kimoja uongozi wa shule uanzishe mikondo mipya. Aidha, Serikali imepeleka kiasi kikubwa cha fedha katika Halmashauri ili kusaidia nguvu za wananchi. Hadi mwezi Mei, 2002 kiasi cha Shilingi 69.9 bilioni kimetolewa kwa ajili ya mpango huo. Jumla ya walimu wapya wa shule za msingi wapatao 6,437 wameajiriwa ambao ni asilimia 70.7 ya lengo. Zoezi la kuajiri walimu bado linaendelea. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo ya kazini kwa walimu wa shule za msingi mashuleni na kwenye vyuo vya walimu.
47. Mheshimiwa Spika, pamoja na azma ya Serikali ya kupanua na kuimarisha elimu ya msingi ni vyema kila Halmashauri ikaunga mkono juhudi hizo kwa kutayarisha mkakati wake wa utekelezaji utakaozingatia mazingira yao. Zipo Halmashauri ambazo zimepiga hatua nzuri katika ujenzi wa madarasa. Wakati huo huo, zipo Halmashauri nyingine ambazo hazijaweza kutekeleza ujenzi huo pamoja na kuwa Serikali imeshatoa mwongozo wa utekelezaji. Fedha zilizopelekwa kwenye Halmashauri ni nyingi na ni vyema sote tuhakikishe kuwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Pale ambapo hazikutumika kama ilivyokusudiwa wahusika wawajibishwe ipasavyo. Viongozi na watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia utaratibu huo wazingatie taratibu zote za matumizi ya fedha za Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za utekelezaji kwa wakati. Hii ni changamoto kubwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na wataalam wao wote. Serikali itachukua hatua za kisheria pale itakapobainika kuna ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha hizo.
48. Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeendelea kutekeleza mpango wake wa kupanua na kuboresha elimu ya juu. Miradi iliyokamilika ni ujenzi wa Hosteli ya kulaza jumla ya wanafunzi 4,309 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ununuzi wa jengo la iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara, Morogoro kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi wa elimu ya juu. Ili kuongeza idadi ya nafasi za wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu vya umma, Serikali imekigeuza Chuo cha Maendeleo Mzumbe kuwa Chuo Kikuu. Aidha, marekebisho yamefanywa kwenye mitaala ili izingatie mahitaji ya Watanzania na ya soko. Serikali imeendelea kutoa mafunzo maalum kwa wanafunzi wa kike ili kuweza kuinua viwango vyao vya masomo katika fani za sayansi na ufundi na hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu na ufundi. Katika mwaka wa fedha wa 2002/2003, Serikali itakamilisha mpango kamambe wa elimu ya juu, elimu ya ufundi na sayansi na teknolojia. Aidha, zoezi la uhuishaji matumizi ya taasisi za elimu ya juu litaendelea na mabaraza ya elimu ya juu na ufundi yataendelezwa ili yaweze kusimamia ubora wa elimu nchini.
49. Mheshimiwa
Spika, mafunzo ya ufundi stadi ni mafunzo muhimu yanayoweza kuwasaidia vijana
wengi kupambana na tatizo la ajira nchini.
Hivi sasa Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi imeanzisha mfumo mpya wa
mafunzo ambao unalenga katika kutoa mafunzo yanayolingana na mahitaji ya soko
la ajira na hasa sekta isiyo rasmi ambao unatekelezwa katika vyuo vyote 20 vya
Mamlaka. Tuwahimize vijana wa jinsia
zote wajiunge na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vilivyopo katika mikoa yao
ili wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri wenyewe. Ili kuwawezesha wasichana vilevile kupata mafunzo hayo, Mamlaka
imeandaa mwongozo kuhusu jinsi ya kuongeza idadi ya wasichana katika mafunzo ya
ufundi stadi na kuusambaza kwa vyuo vyote vinavyotoa mafunzo hayo. Aidha, imeweka na kutekeleza mikakati ya
mafunzo ya ufundi stadi kwa watu wenye ulemavu kulingana na mahitaji yao ikiwa
ni pamoja na kuandaa mazingira yanayozingatia mahitaji maalum ya walemavu.
50. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2001/2002, Serikali kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali, Halmashauri za Wilaya na wananchi imejenga miradi mbalimbali ya huduma za maji vijijini katika mikoa ya Pwani na Mtwara na uchimbaji wa visima katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Tanga, Pwani na Jiji la Dar es Salaam. Serikali imekarabati miradi ya maji isiyofanyakazi vijijini katika mikoa ya Shinyanga, Singida, Lindi, Mtwara, Mbeya, Ruvuma, Tabora na Iringa. Kwa kutumia mkopo wa Benki ya Dunia na msaada wa Serikali ya Japan, Serikali imekamilisha matayarisho ya mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ambao utatekelezwa katika baadhi ya wilaya katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Morogoro, Singida, Tabora, Mtwara, Lindi na Arusha. Aidha, mradi wa uchimbaji visima virefu katika baadhi ya vijiji katika mikoa ya Tabora na Arusha umetekelezwa. Serikali pia imekamilisha utafiti wa awali wa maji chini ya ardhi katika mikoa ya Mtwara na Lindi. Wananchi wameanzisha na kuendeleza vyombo huru vya watumiaji maji kwa lengo la kuimarisha huduma za maji vijijini na kuzifanya ziwe endelevu. Hadi Aprili 2002, vyombo arobaini na moja vya watumiaji maji vimeanzishwa, Wilaya tisa zimeanzisha mamlaka za maji katika makao makuu yake na Wilaya ishirini na saba zipo katika hatua mbalimbali za kuanzisha mamlaka za maji katika miji mikuu yake.
51. Mheshimiwa Spika, kuhusu maeneo ya mijini miradi ya upanuzi wa mifumo ya maji safi ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika miji ya Arusha, Moshi, Tanga, Dodoma, Lindi, Mtwara, Shinyanga na Sumbawanga. Serikali pia imeendelea kufanya uchunguzi na usanifu wa mifumo ya maji safi katika miji ya Songea na Mbeya na kufanya mapitio ya usanifu wa miradi ya maji safi na majitaka katika Jiji la Mwanza na Manispaa ya Iringa. Aidha, Serikali imeendelea kufanya uchunguzi na usanifu wa miradi ya kuimarisha huduma ya maji katika miji ya Dodoma, Morogoro, Tabora, Bukoba, Mwanza, Musoma na Singida. Mpango wa kuleta maji ya Ziwa Viktoria ili kuondoa tatizo sugu la uhaba wa maji katika miji ya Kahama na Shinyanga pamoja na vijiji na migodi iliyo kusini mwa Ziwa hilo umeendelea katika hatua za awali. Mradi huo utakapokamilika utakuwa muhimu kwa wananchi wa maeneo ya Ziwa Viktoria na utapunguza uhaba wa maji.
52. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha jamii kupitia vyombo wa habari, na mikutano mbalimbali kubadili fikra na mtazamo kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii. Vilevile, imeshirikiana na Asasi zisizo za Serikali katika kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya jinsia. Aidha, mila potofu ambazo zinawadhalilisha na kuwanyanyasa wanawake zimeendelea kupigwa vita. Kazi ya kubadili fikra na mtazamo ni ngumu kwani zimejikita katika utamaduni wetu. Serikali itaendelea kusaidiana na Asasi zisizo za Serikali katika kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu kuachana na mila potofu. Aidha, sheria zinazowalinda wanawake dhidi ya unyanyasaji na udhalilishwaji wowote zitaendelea kusimamiwa kikamilifu.
53. Mheshimiwa Spika, watoto ni rasilimali yenye thamani kwa sababu ndiyo tunaowakabidhi rasilimali zote tulizo nazo, hazina ya maarifa, maadili na matarajio ya baadaye ya Taifa letu. Wananchi wote hatuna budi kuweka msukumo mkubwa wa kuwapatia maendeleo, haki na ustawi katika maeneo ya elimu, afya, na malezi na kuepuka tabia za kuwanyanyasa. Kwa kuzingatia mkataba wa Shirika la Kazi Duniani unaokataza aina zote za ajira mbaya ya watoto, Serikali kwa kushirikiana na mataifa mengine itapiga vita kabisa unyanyasaji wa watoto katika eneo la ajira. Aidha, itaendelea kudurusu na kusimamia utekelezaji wa sheria nyingine zinazolinda watoto na kuchukua hatua kali kwa wanaozikiuka ili kuwaandaa vyema na kulijenga taifa madhubuti la kesho.
54. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/2002 Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma katika ngazi ya Serikali za Mitaa. Hivi sasa zipo Halmashauri thelathini na nane za awamu ya kwanza ya mpango wa uboreshaji wa Serikali za Mitaa ambao utekelezaji wake ulianza mwezi Januari, 2000. Tathmini ya utekelezaji wa programu iliyofanyika mwezi Juni, 2001 ilibaini kuwa Sera na Mpango wa Uboreshaji havitekelezwi kulingana na maamuzi, mwelekeo na kauli mbiu kuhusu Serikali za Mitaa tunazotaka kuzijenga. Hali hiyo imesababisha kulegalega kwa shughuli za kupeleka madaraka kwa Halmashauri ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa zoezi la kuwianisha sheria za kisekta ili ziendane na maamuzi ya kupeleka madaraka kwa wananchi. Kwa upande wa Halmashauri zenyewe, uzoefu umeonyesha kuwa tatizo hilo linasababishwa na usimamizi hafifu wa Baraza la Madiwani na Watendaji Wakuu. Pale ambapo Baraza la Madiwani limekuwa makini na likashiriki kikamilifu katika zoezi hilo, mafanikio ya kuridhisha yameonekana. Pale ambapo Baraza la Madiwani halikusimamia mpango huo ipasavyo kasi ya utekelezaji imepungua. Napenda kusisitiza kuwa suala la usimamizi imara wa mpango huo ni muhimu sana katika kutuwezesha kuendelea na awamu ya pili ili hatimaye tuweze kujenga Mamlaka za Serikali za Mitaa imara nchi nzima.
55. Mheshimiwa Spika, uimarishaji wa Serikali za Mitaa hautakuwa na maana kama wananchi nao hawataona mabadiliko katika utoaji wa huduma mbalimbali zinazowagusa katika harakati za maendeleo yao. Kwa hiyo, jukumu la awali kabisa la Halmashauri yoyote ni kusimamia shughuli za maendeleo za wananchi yaani zile za uzalishaji mali na utoaji huduma za jamii. Siyo sahihi wataalamu wa Halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi wawe mstari wa mbele kufuatilia masuala ya kodi na kupuuza kusimamia masuala ya uzalishaji mali. Kama tunataka kupata mapato zaidi katika Halmashauri zetu, hatuna budi kuchukua hatua madhubuti za kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujishughulisha na uzalishaji na hivyo kuongeza uwezo wa kulipa kodi. Kwa mfano, shughuli za kufikisha utaalam wa kilimo kwa wananchi, kazi za kufufua na kujenga ushirika imara zitawezekana pale ambapo Wakurugenzi watachukua hatua za dhati za kuwawezesha wataalamu kuwafikia wananchi. Hivyo, kila Halmashauri ihakikishe kuwa katika bajeti yake zinatengwa fedha za kuwawezesha wataalamu mbalimbali kuwafikia wananchi. Katika bajeti ya mwaka 2002/2003, Serikali imeelekeza rasilimali nyingi kwenye shughuli zinazowagusa wananchi hasa elimu, afya, maji, kilimo na barabara. Hivyo, ni lazima Halmashauri nazo zitoe kipaumbele kwa njia ya fedha na wataalamu ili mwelekeo huo ulete manufaa kwa kuwajenga wananchi kiuchumi na kihuduma ili waweze kujitegemea zaidi.
56. Mheshimiwa
Spika, Halmashauri za Jiji, Manispaa na Miji zimeendelea kuwapatia
wafanyabiashara ndogo ndogo na viwanda vidogo vidogo maeneo ya kufanyia kazi
japo kwa kasi ndogo. Hata hivyo, ni vyema Halmashauri hizo zitambue kuwa kwa
kuwapatia maeneo ya kazi na kuwasajili, zitaweza kuwapatia huduma muhimu na
hivyo kuziwezesha kukusanya kodi kwa ufanisi zaidi. Serikali itaendelea kuzihimiza Halmashauri za Mji, Manispaa na
Jiji zitazame upya mpangilio wa huduma mbalimbali kwenye miji na maeneo yao ili
kukabiliana na mahitaji makubwa ya sekta isiyo rasmi ambayo inajumuisha makundi
makubwa ya wafanyabiashara ndogo ndogo na wenye viwanda vidogo vidogo. Aidha, pale maeneo rasmi ya biashara
yanapotengwa, wafanyabiashara hawa nao wakubali maeneo wanayopewa na mamlaka na
wasing’ang’anie katika maeneo kwa sababu ya mazoea tu. Wapo waliojengewa masoko mazuri ya kisasa
lakini wao wakang’ang’ania utaratibu wao wa zamani ambao siyo salama hata kwa
afya za walaji.
57. Mheshimiwa Spika, katika miaka ya karibuni baadhi ya watu wamepatwa na matatizo ya kuvunjiwa nyumba zao kwa sababu mbalimbali hasa za maendeleo. Hali hiyo imewakumba wengine bila kufahamu lakini wengine kwa kufahamu kuwa nyumba zao haziko katika maeneo halali ya ujenzi wa makazi. Ninapenda kuwatahadharisha wananchi waache kabisa utaratibu wa kuvamia maeneo yasiyo ya ujenzi wa makazi, kupata vibali kwa njia zisizo halali au kujenga bila vibali. Aidha, utaratibu wa kuuziana viwanja, mashamba au nyumba bila ya kushirikisha mamlaka husika inachangia sana katika kushamirisha tatizo hilo. Mara nyingi watu wameuziwa nyumba au viwanja vilivyolipwa fidia au ambavyo mwenyewe alikwisha pewa notisi ya kuvunja jengo au kuhama kutoka eneo hilo. Serikali itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma mbalimbali za maendeleo kwa wananchi. Pale ambapo baadhi ya wananchi wamejenga kwenye maeneo yenye mahitaji ya shughuli za umma itabidi wananchi hao wabomoe majengo hayo na kuhama. Natoa wito kwa wananchi kujenga mazoea ya kutafuta uhalali wa maeneo wanayoishi au majengo wanayotaka kuyanunua kutoka katika mamlaka zinazotambulika kisheria.
58. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa Halmashauri za Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya ili ziweze kuzifanyia matengenezo barabara. Kuwepo kwa barabara nzuri katika maeneo ya vijiji kutawapa wananchi uwezo wa kupata huduma mbalimbali. Katika mpango wake wa miaka kumi ijayo Serikali imedhamiria kuzifanyia matengenezo kilometa 12,767 za barabara za wilaya na zile zinazounganisha barabara hizo na barabara nyingine. Katika awamu ya kwanza ya mpango huo, kilometa 6,290 zitafanyiwa matengenezo. Pamoja na kutayarisha mpango huo, Serikali imeendelea kupeleka kwenye Halmashauri fedha kutoka katika Mfuko wa Barabara ili ziweze kuongeza uwezo wake wa kutengeneza barabara zao. Hadi mwezi Mei, 2002 kiasi cha Shilingi 12.75 bilioni zimepelekwa kwenye Halmashauri zote nchini kwa ajili hiyo.
59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2001/2002 Serikali imeendelea kutekeleza zoezi la mabadiliko katika utumishi wa umma ili kujenga kada ya utumishi wa umma yenye kuwajibika na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Zipo programu zinazotekelezwa katika ngazi mbalimbali za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zenye lengo la kujenga uwezo wa watumishi wa umma kutoa huduma kwa ufanisi na tija zaidi. Programu za uboreshaji wa maslahi ya watumishi, uundaji wa mfuko wa bima ya afya kwa watumishi wa Serikali, uunganishaji wa marupurupu katika mishahara na uanzishaji wa mfuko wa pensheni wa wafanyakazi wa Serikali ni baadhi ya hatua muhimu zilizochukuliwa.
60. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali ilitangaza kuuza baadhi ya nyumba zake kwa watumishi wake kwa kutoa kipaumbele kwa watumishi wanaoishi katika nyumba hizo. Kati ya watumishi wa Serikali 265,700 ni watumishi wapatao 6,000 tu au asilimia 2.26 ndiyo wanaoishi katika nyumba za Serikali. Aidha, hao waliobahatika kupanga katika nyumba hizo chache, huishi katika mazingira yasiyoridhisha kwa sababu Serikali haina uwezo wa kuzitengeneza au kuzihudumia. Katika utaratibu huo mpya, nyumba 3,000 kati ya nyumba 6,000 za Serikali zitauzwa. Kwa vile lengo ni kuwasaidia wafanyakazi walioko katika nyumba hizo, mauzo yamefanyika kwa bei ya tathmini iliyotolewa na Wakala wa Majengo ya Serikali na Mtathmini wa Mali za Serikali na siyo kwa njia ya tenda ambayo ingekuwa sawa na kuwanyima watumishi hawa nyumba hizo.
61. Mheshimiwa Spika, vita dhidi ya rushwa imeendelea kupewa msukumo unaostahili ndani ya Serikali na taasisi zake. Ili kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa, Wizara, Idara na Wakala wa Serikali ziliainisha maeneo yenye mianya ya rushwa na kuandaa mbinu za kuiziba mianya hiyo. Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara na Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali wamepewa jukumu la kusimamia na kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu kwa Katibu Mkuu Kiongozi jinsi wanavyotekeleza mkakati huo. Taasisi ya Kuzuia Rushwa itaendelea kuimarishwa kwa kuboresha muundo wake, kuongeza vitendea kazi, kuongeza idadi ya watumishi na kuwapatia mafunzo maalum ili kuongeza ujuzi na ufanisi katika kuchunguza vitendo vya rushwa. Serikali itaendelea na juhudi za kupambana na rushwa kwa kurekebisha sheria, sera, kanuni na taratibu za kazi ili kuziba mianya yote pamoja na kubaini mbinu zinazotumiwa na wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa.
62. Mheshimwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma ili wananchi wafahamu haki na wajibu wao katika mapambano dhidi ya rushwa. Hatua hiyo itasaidia kuwaondoa wasiwasi wananchi na kuwawezesha kutoa taarifa kuhusu watendaji waonevu na wanaotumia madaraka yao vibaya. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo imeshaanza kazi rasmi itasaidia sana kuwawezesha wananchi kuwafichua watendaji wa aina hiyo na kudai haki zao. Hata hivyo, nguvu ya pamoja ni muhimu katika ushindi wa vita dhidi ya rushwa kwa sababu juhudi za Serikali pekee haziwezi kuzaa matunda bila ya kushirikisha wananchi. Napenda niwahakikishie wananchi wote kwamba, Serikali itawalinda wale wote watakaokuwa wanatoa taarifa za wala rushwa.
63. Mheshimiwa
Spika, bado yapo malalamiko toka kwa wananchi kuhusu huduma zisizoridhisha,
vitendo vya uonevu na unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali
Kuu na Serikali za Mitaa. Hali hiyo
imechangia kero mbalimbali zikiwemo za uchelewesho wa haki za msingi za malipo,
fidia mbalimbali, pensheni, kucheleweshwa kwa uendeshaji kesi, migogoro ya
ardhi na kadhalika. Watendaji wote wa
Serikali na hasa viongozi katika ngazi zote ni lazima wazingatie maadili,
sheria na taratibu za utendaji kazi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
64. Mheshimiwa
Spika, maandalizi ya Sera ya Habari yapo katika hatua za mwisho. Sera hiyo inatarajiwa kujibu malalamiko ya muda mrefu
ya wadau mbalimbali wa sekta ya habari kwa kubainisha uhuru, haki na wajibu wa
kila mdau wa sekta hiyo. Lengo la sera
hiyo mpya ni kutoa mchango mahsusi katika:
· Kuiwezesha Tanzania kuwa na vyombo vingi vya habari vilivyo huru na vinavyowajibika kwa jamii;
· Kuimarisha demokrasia kwa kuwa na jamii iliyo na mwamko na hamasa inayotokana na ubora na wingi wa mawazo yanayotolewa na vyombo tofauti vya habari; na
· Kueneza huduma za vyombo vya habari vijijini ili kuondoa tofauti ya upatikanaji wa huduma hizo kati ya wananchi wa mijini na wale wa vijijini.
65. Mheshimiwa Spika, ili kupanua upeo wa upatikanaji wa habari kwa wananchi, jumla ya magazeti na majarida hamsini na tatu yalisajiliwa katika mwaka 2001/2002. Hata hivyo, katika hatua ya kuendeleza maadili mema ya jamii za taifa letu, Serikali iliyafungia kwa vipindi tofauti magazeti matatu yaliyokuwa yanachapisha matusi na vitendo vya ngono. Serikali pia ilifungia kwa muda wa mwezi mmoja kipindi kimoja cha televisheni kilichokuwa kinaonyesha picha za matusi na ngono bila kujali athari zake kwa jamii, hasa watoto na vijana wa umri mdogo. Serikali imetoa maagizo kwa vituo vyote vya televisheni nchini kubadili muda wa kuonyesha vipindi visivyofaa kuonyeshwa watoto ili vionyeshwe baada ya saa 4.00 usiku.
66. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2001/2002 Serikali ilikamilisha mradi wa
uimarishaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) uliogharimu zaidi ya shilingi
10 bilioni kwa msaada wa Serikali ya Japan.
Chini ya mradi huo, jengo jipya la utangazaji lenye studio tano za
kisasa na mtambo mkubwa wa kisasa wenye nguvu ya kilowati (Kw) 100 wa kurushia
matangazo wa Kunduchi vimejengwa.
Kukamilika kwa mradi huo kumeongeza ubora wa matangazo na kuongeza
usikivu wa RTD kufikia asilimia 80. Mradi huo pia ulitoa mafunzo ya ndani kwa
mafundi na wahandisi wa RTD.
67. Mheshimiwa Spika, Televisheni ya Taifa (TVT) nayo imeendelea kurusha matangazo yake katika baadhi ya maeneo nchini. Katika mwaka wa fedha 2002/2003 Serikali itakamilisha ujenzi wa mitambo ya kurushia matangazo ya TVT kupitia satelaiti na baadhi ya vituo vya kupokelea na kurushia tena matangazo hayo katika baadhi ya maeneo nchini. TVT itakapoanza kurusha matangazo yake kupitia satelaiti, Halmashauri za Miji na Wilaya zenye vituo vya kupokelea na kurushia matangazo ya televisheni zitaweza kusaidia kusambaza matangazo ya TVT kwa wananchi wa maeneo yao.
68. Mheshimiwa Spika, ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kujenga miundo mbinu mipya kwa kila chombo pekee, Serikali imeamua kuunganisha huduma za RTD na TVT chini ya chombo kitakachoitwa Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TUT). Hatua hiyo itaiwezesha taasisi itakayoanzishwa kutumia miundo mbinu iliyopo katika maeneo mbalimbali kwa ufanisi zaidi. Taratibu za kuunda taasisi hiyo mpya zimekamilika na kisheria itaanza kazi tarehe 1 Julai 2002.
69. Mheshimiwa Spika, kuhusu Kampuni ya Magazeti ya Serikali, mtaji wa Kampuni hiyo umeimarishwa kwa kuipatia jengo la ofisi za kudumu. Hatua hiyo imeiwezesha Kampuni kuimarisha uwezo wake kiutendaji na hivyo kuongeza ufanisi katika utoaji magazeti. Katika mwaka wa fedha 2002/2003 Kampuni itaendelea kujiimarisha na kuongeza ubora wa magazeti yake ili kukabiliana na ushindani mkubwa uliopo katika sekta ya habari.
70. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/2002 Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania kilishughulikia taratibu za kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa, Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam limekubali Chuo cha Uandishi wa Habari kijiunge na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia tarehe 1 Septemba, 2002 kama Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma. Mapendekezo ya marekebisho ya sheria iliyoanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ile ya Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania, yanakamilishwa ili yaweze kuwasilishwa kwenye Bunge lako tukufu ili kukidhi mabadiliko hayo. Taratibu za kujiunga na Chuo Kikuu zitakapokamilika wanafunzi waliopo hivi sasa watatunukiwa vyeti na stashahada za juu za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mujibu wa sheria. Aidha, wanafunzi walioomba kujiunga na mafunzo kwa mwaka 2002/2003 watachaguliwa kwa mujibu wa taratibu za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
71. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/2002 Tume ya Utangazaji iliendelea kusimamia maendeleo ya sekta ya utangazaji hapa nchini. Msisitizo mkubwa ulikuwa kuruhusu vituo vya radio na televisheni vya jamii ili kuwawezesha wananchi walio wengi waweze kupata habari. Halmashauri za Manispaa za Mbeya na Iringa, Halmashauri za Miji ya Mtwara Mikindani na Songea, na Halmashauri za Wilaya za Masasi, Njombe, Mbozi na Rungwe zilipatiwa leseni za kuanzisha vituo vya radio na televisheni. Katika kipindi cha mwaka 2002/2003, Tume itaendelea kuhamasisha uanzishwaji wa vituo vya kijamii katika maeneo mbalimbali nchini na kukagua vituo vya radio na televisheni ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapokea matangazo yaliyo bora. Aidha, Tume itafuatilia malalamiko kuhusu ubora wa vipindi vinavyotangazwa na kuchukua hatua zinazostahili ili kupunguza mmomonyoko wa maadili katika jamii.
72. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
fedha 2001/2002, Idara ya Kupigachapa ya Serikali iliendelea kusimamia shughuli
zote za uchapaji wa nyaraka za Serikali.
Aidha, ilitoa mafunzo ya kitaalam kwa watumishi na kununua mitambo mipya
ya kisasa. Katika mwaka wa fedha
2002/2003, mitambo ya kisasa zaidi itaongezwa na programu ya mafunzo kwa
watumishi itaandaliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitengo cha mipango na
masoko.
Aidha,
matawi ya maduka ya vitabu na nyaraka za Serikali yatafunguliwa mikoani ili
kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo.
Ushirikiano wa Kimataifa
73. Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba marekebisho ya Sera mpya ya Mambo ya Nje hivi sasa yamekamilika na ilianza kutumika rasmi tangu Desemba, 2001. Mbali na kuendelea kulinda na kukuza misingi yote iliyotuletea heshima kubwa kama taifa nje ya nchi tangu tupate uhuru, sera hiyo mpya inasisitizia diplomasia ya uchumi kama njia ya kuleta maendeleo endelevu na kukuza uchumi wa taifa letu. Ni matarajio yetu kwamba kuanza rasmi kutumika kwa sera hiyo kutaongeza chachu katika kukuza uwekezaji rasilimali, biashara, utalii na maendeleo ya wananchi wetu kwa ujumla.
74. Mheshimiwa Spika, shughuli za kujenga Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea vizuri. Mikutano ya kisekta imefanyika ili kutekeleza masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyoainishwa katika Mkataba na Mkakati wa Maendeleo wa Afrika Mashariki, 2001-2005. Kazi ya kuunda asasi za Jumuiya imekamilika baada ya Mahakama na Bunge kuzinduliwa rasmi tarehe 30 Novemba, 2001. Mheshimiwa Abdulrahman Kinana alichaguliwa kuwa Spika wa kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati. Kazi hiyo ni nzito, lakini sina shaka ataimudu vyema na kuitekeleza kwa uadilifu mkubwa. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochaguliwa katika Bunge la Afrika Mashariki. Nawapongeza kwa dhati Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani kwa kuteuliwa kuwa miongoni mwa majaji sita wa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki.
75. Mheshimiwa Spika, kazi ya kuandaa mapendekezo ya kuanzishwa kwa Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki bado inaendelea. Makubaliano ya kimsingi yamefikiwa katika maeneo kadhaa kuhusu namna ya kuondoleana ushuru wa forodha wa ndani kwa bidhaa zitokazo katika nchi wanachama na viwango vya wigo wa pamoja wa ushuru wa forodha kwa bidhaa zitokazo nchi nyingine duniani. Matumaini yetu ni kuwa kazi hiyo itakamilika kwa wakati muafaka na kwa manufaa sawia kwa nchi zote wanachama. Changamoto kubwa kwetu Watanzania ni kujipanga vizuri, kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili tuweze kutumia vizuri fursa zote zinazotokana na soko hilo jipya.
76. Mheshimiwa Spika, katika eneo la Maziwa Makuu bado hali siyo ya kuridhisha. Katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Watu wa Kongo vita vya wenyewe kwa wenyewe bado vinaendelea. Tanzania imeendelea kushiriki na kuunga mkono juhudi za kimataifa za kujaribu kutafuta suluhisho la migogoro katika nchi hizo. Hivi karibuni baadhi ya vikundi vya Burundi ambavyo havikuwa vimekubali kushiriki katika juhudi za kuleta amani nchini humo vimekubali kusitisha vita. Kwa upande wa Jamhuri ya Watu wa Kongo, Serikali ya Tanzania inaunga mkono kwa dhati juhudi za kujaribu kuvipatanisha vikundi vyote vinavyopigana nchini humo kwa kupitia msuluhishi Rais Mstaafu wa Botswana, Mheshimiwa Ketumile Masire.
77. Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi. Sensa ya watu na makazi itafanyika mwezi Agosti, 2002 kama ilivyopangwa. Kadiri tunavyokaribia muda wa zoezi hilo, sote tunao wajibu wa kuelimishana na kukumbushana kuhusu umuhimu wa zoezi hilo kwa mustakabali wa Taifa letu. Kamisheni ya Sensa inaendelea kukamilisha taratibu zote muhimu zinazohitajika ili kufanikisha zoezi hilo. Kwa sehemu kubwa walimu wa shule za msingi ndiyo watakaotekeleza zoezi hilo. Uamuzi wa kuwatumia walimu katika zoezi hilo umezingatia uwezo wao na urahisi wao wa kuwa karibu na watu kwenye vijiji na mitaa yetu. Viongozi wote wa mikoa na wilaya wazingatie na kutekeleza maagizo yote yaliyopo katika Waraka wa Serikali Na. 1 wa mwaka 2002 kuhusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002. Wito wangu kwa viongozi wote, vyombo vya habari na wadau wengine ni kuwa kadiri tunavyokaribia muda wa sensa sote tunao wajibu wa kuongeza bidii katika kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi ili wawe tayari kuwapokea wale wote watakaohusika na kuhesabu watu na kuwapa ushirikiano wa kutosha. Aidha, tuwaeleze wananchi umuhimu wa sensa ili tuwatoe woga na tuwashawishi washiriki vizuri katika zoezi hilo. Zoezi la Sensa ni la kitaifa kwa malengo ya kiuchumi na kijamii. Kwa vyovyote vile lisitumiwe kwa dhamira zenye utashi wa kisiasa. Kama tujuavyo, takwimu zitakazopatikana ndizo zitatumika katika mipango yetu ya maendeleo kwa miaka kumi ijayo, hivyo ni muhimu sote tukashiriki kikamilifu ili kupata takwimu sahihi.
Matukio ya Maafa
78. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2001/2002 nchi yetu imeendelea kukumbwa na matukio mengi ya
ajali za majini na nchi kavu. Matukio
hayo ni pamoja na ajali ya kuzama kivuko cha Mto Kilombero, ajali za magari
zilizotokea katika mikoa mbalimbali nchini na tetemeko la ardhi lililotokea
katika maeneo ya wilaya za Rungwe na Bariadi.
Kwa ujumla ajali hizo zimesababisha upotevu wa maisha, mali na kuwafanya
watu wengi kupata ulemavu. Kuhusu ajali
ya kivuko katika Mto Kilombero napenda kutoa taarifa kuwa Serikali iliunda Tume
ya Wataalamu ya kuchunguza ajali hiyo.
Tume imekamilisha kazi yake na kubaini kuwa ajali hiyo ilisababishwa na
maji yaliyoongezeka sana mtoni na kwa kasi kubwa na hivyo kusababisha kamba ya
upande yanapotokea maji kushindwa
kuhimili nguvu ya maji na kukatika.
Hivyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo hapakuwa na uzembe katika ajali
hiyo. Nachukua nafasi hii tena kwa
niaba ya Serikali kuwaombea malazi mema peponi waliofariki na kuwapa pole wale
waliofikwa na misiba, kupata ulemavu, kujeruhiwa na kupoteza mali kutokana na
ajali hizo. Serikali itaendelea
kuchukua hatua za kuimarisha usalama wa raia na shughuli za uokoaji katika aina
zote za usafiri. Kama nilivyoahidi,
Serikali itawalipa kifuta machozi wale wote walioathirika. Aidha, taratibu za uagizaji wa kivuko kipya
cha Mto Kilombero zimekamilika na kitapatikana mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa
2002/2003.
79. Mheshimiwa
Spika, vilevile, katika mwaka wa 2001/2002 nchi yetu imekumbwa na majanga
makubwa ya moto. Baadhi ya majanga hayo
ni pamoja na yale ya kuungua kwa jengo linalotumiwa na Wizara za Maji na
Maendeleo ya Mifugo na ya Nishati na Madini, Jengo la Makao Makuu la Jeshi la
Kujenga Taifa, Chuo cha Sanaa Bagamoyo, Jengo la Kitega Uchumi la Shirika la
Bima la Taifa, baadhi ya viwanda na makazi ya watu. Matukio yote haya
yamesababisha hasara kubwa kwa Taifa. Ili kukabiliana na matukio hayo, Serikali
inaimarisha ukaguzi katika majengo kwa lengo la kuainisha kasoro za kiufundi
zilizopo. Moto umekuwa ni tishio kubwa
kwa mali na maisha ya wananchi. Ajali
ya moto inaweza kuangamiza kwa muda mfupi raslimali zilizojengwa kwa gharama
kubwa na kwa muda mrefu. Kwa msingi
huo, ni vyema taasisi zote na wananchi
kuchukua tahadhari zinazopasa ili kujikinga na ajali za moto.
80. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza uwezo wa kusimamia na kuratibu maafa nchini, Serikali imeanzisha kituo cha mafunzo ya udhibiti wa maafa katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi. Katika mwaka wa fedha 2002/2003 Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya kujikinga na maafa kwa wadau mbalimbali katika ngazi zote na kufanya utafiti juu ya madhara ya maafa. Hatua hizo zitasaidia kuimarisha uwezo wetu wa kupunguza athari za maafa.
81. Mheshimiwa
Spika, UKIMWI bado ni tishio kwa ustawi na maendeleo yetu. Katika mwaka wa fedha 2001/2002, Serikali
imeendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari zinazostahili
kujikinga na ugonjwa huo. Aidha, Tume
ya Kudhibiti UKIMWI imewashirikisha wadau mbalimbali katika kujadili na
kutafuta njia mbalimbali za kuwafikia wananchi wa rika zote na makundi yote
katika vita hiyo. Tatizo hivi sasa siyo
uelewa wa Watanzania kuhusu ugonjwa huo bali dhamira ya dhati ya kubadili tabia
ili tuweze kupunguza kasi ya maambukizo.
Uundaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI hivi sasa umekamilika baada ya
makamishna kuteuliwa na muundo wake kukamilishwa. Serikali itaendelea kuimarisha Tume hiyo ili iweze kuratibu
shughuli za wadau mbalimbali katika vita dhidi ya ugonjwa huo. Hata hivyo, napenda kusisitiza kuwa ushindi
dhidi ya ugonjwa huo utapatikana kama Watanzania wote watabadili tabia na
kuonyesha kuwa wanajali.
82. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na majirani zetu na jumuiya ya kimataifa katika vita dhidi ya UKIMWI. Hivi sasa katika Eneo la Maziwa Makuu tunashirikiana kupitia The Great Lakes Initiative for AIDS (GLIA) inayoshirikisha nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya. Tunashirikiana vilevile na Umoja wa Afrika kupitia vikao mbalimbali na International Partnership Against AIDS in Africa (IPAA). Tunashiriki pia katika harakati zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa. Ushirikiano huo umetuwezesha kupata taarifa mbalimbali kuhusu juhudi za kimataifa za kupambana na ugonjwa huo. Aidha, tumeweza kujifunza mafanikio na matatizo ya wenzetu katika vita hivyo. Ili kuendelea kutoa msukumo katika vita hivyo umeanzishwa Mfuko Maalum wa Kimataifa wa Kudhibiti UKIMWI , Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund for HIV/AIDS, TB and Malaria). Nchi yetu imeanza kufaidika na huduma za Mfuko huo na hivi karibuni umetoa kiasi cha Dola za Marekani 9 milioni kwa ajili ya kuongeza nguvu zetu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria na Dola za Marekani 5 milioni kwa ajili ya kupambana na UKIMWI. Serikali itashirikiana na wadau wote nchini ili tuweze kutumia uzoefu unaotokana na ushirikiano huo kuongeza kasi ya vita dhidi ya ugonjwa huo.
83. Mheshimiwa Spika, baada ya juhudi za kuimarisha uongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu katika kipindi cha 2001/2002, Mamlaka hiyo itaendelea na jukumu la kusimamia huduma zilizopo ili Dodoma ifanane na Makao Makuu ya nchi yetu. Juhudi zitaelekezwa katika upangaji na upimaji wa viwanja, usimamizi wa huduma za barabara, mifereji na uboreshaji mazingira ili kutoa huduma bora kwa wakazi. Msukumo pia utawekwa katika uhamishaji wizara hatua kwa hatua kulingana na uwezo wa fedha. Hatua za kuhamishia shughuli za Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, zimeshaanza kuchukuliwa na zitaendelea katika mwaka wa fedha 2002/2003. Waziri Mkuu na baadhi ya watumishi wamehamia Dodoma na wengine wataendelea kuhamia kadri hali ya fedha itakavyoruhusu.
MAJUMUISHO
84. Mheshimiwa Spika, kama tulivyoelezwa katika hotuba za Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji na wa Fedha, kuwa pamoja na unafuu wa bajeti ulioonekana, bado ni tegemezi kwa kiwango kikubwa. Bado hatujawa na uwezo hata wa kujitegemea kwa matumizi ya kawaida kwa sababu bajeti yetu inakidhi asilimia 78 tu ya matumizi hayo. Kwa upande wa bajeti ya maendeleo hali ni mbaya zaidi kwa sababu tunajitegemea kwa asilimia 13.3 tu. Katika mwaka wa fedha 2001/2002 hali haikuwa tofauti sana na hali ya sasa. Bajeti ilitegemea misaada na mikopo. Hata hivyo, kama tulivyojulishwa na Waziri wa Fedha, asilimia 40.6 ya fedha hizo za nje kwa upande wa miradi ya maendeleo hazikupatikana. Tafsiri ya hali hiyo ni kuwa baadhi ya miradi tuliyoipitisha hapa Bungeni haikuweza kutekelezwa kutokana na ukosefu wa fedha.
85. Mheshimiwa Spika, hali hiyo ya utegemezi katika bajeti ya Serikali tunaweza kuipunguza kwa kiwango kikubwa endapo tutajenga na kuimarisha maeneo muhimu ya uzalishaji. Eneo la kwanza ni kilimo ambacho ndiyo shughuli kuu ya uchumi kwa wananchi wengi nchini na kwa sehemu kubwa kinachangia ukuaji wa pato la Taifa. Serikali imeongeza fedha katika eneo hilo ili lilete mabadiliko kwa wananchi wetu na uchumi kwa ujumla. Matumaini yetu ni kuwa sasa tutawaona mabwana na mabibi shamba mashambani na tutawaona watafiti wetu wakishughulikia utafiti wa kutatua matatizo ya wakulima na wafugaji. Aidha, tunatarajia kuona matumizi ya pembejeo na zana za kilimo yanaongezeka baada ya ushauri kuboreka na masoko ya mazao ya wakulima kuwa na utaratibu mzuri ili wapate bei nzuri na kwa wakati muafaka. Hatutarajii kuona utitiri wa semina na kongamano zisizoisha kwa sababu tu
fedha zipo. Mawaziri wanaohusika wameagizwa kuwa fedha hizo zielekezwe zaidi kwa wakulima na zisiishie makao makuu ya wizara.
86. Mheshimiwa Spika, eneo lingine muhimu ni la uzalishaji viwandani ambalo limegawanyika katika sehemu tatu muhimu. Kwanza, ni viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi ili kupata bei nzuri na mapato zaidi kwa wakulima na wavuvi wetu. Pili, ni viwanda vya kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko la ndani ili tujenge uwezo wetu, kuwa na ajira na nchi isiwe soko la wengine. Tatu, ni viwanda vya uzalishaji kwa ajili ya soko la nje. Ni lazima tuwavutie wawekezaji washiriki kuwekeza upya, kununua amana na kukodisha mashirika yetu. Bila ya kujenga sekta binafsi imara katika mazingira haya ya ushindani na utandawazi mafanikio yetu yatakuwa madogo sana.
87. Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya sasa ya ushindani mkali, ni lazima bidhaa zetu ziwe bora. Tukumbuke tunapozungumza masoko ya Marekani kwa utaratibu wa AGOA, ya Ulaya kwa makubaliano ya Cotonou, ya SADC au ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, maana yake ni kuwa na wao pia unawapa fursa ya kuingia katika soko lako. Hivyo, ninawaomba Watanzania tutumie changamoto hiyo kuzalisha kwa wingi viwandani ili tufaidi ipasavyo biashara hiyo. Kwa mantiki hiyo, ni vyema sote tulio katika nafasi zinazohusiana na uwekezaji tusiwe kikwazo kwa wawekezaji.
88. Mheshimiwa Spika, eneo lingine ninalotaka kulizungumzia ni la mapato ya Serikali. Mapato yetu ya ndani bado ni madogo sana. Tunakusanya asilimia12.2 tu ya Pato la Taifa. Kuna sababu mbalimbali zinazosababisha hali hiyo ikiwa ni pamoja na watu wengi kutokulipa kodi, ukwepaji mkubwa wa kodi, vitendo vya rushwa katika ukusanyaji wa kodi, udanganyifu wa njia mbalimbali hasa kwa kutumia mizigo inayodaiwa ni ya nchi jirani na mizigo inayokwenda katika maduka yanayouza bidhaa zisizo na ushuru. Serikali itaendelea kupanua wigo wa kodi na kuwahamasisha wananchi waelewe umuhimu wa kulipa kodi ili mapato ya Serikali yaongezeke. Hata hivyo, Serikali itapambana vikali na vitendo vya ukwepaji kodi hasa vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara vya kuuza katika soko la ndani bidhaa zinazotakiwa kusafirishwa nje ya nchi au kuuzwa katika maduka ya bidhaa zisizotozwa ushuru. Vilevile, wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao bado hawatoi stakabadhi kwa bidhaa wanazouza. Pale wateja wao wanapodai stakabadhi bidhaa hupandishwa bei. Hawa wote ni wahujumu wa uchumi wetu. Serikali haitasita kuleta kwenye Bunge lako tukufu mapendekezo ya mabadiliko ya sheria zinazohusika ili kuongeza adhabu kwa wakwepa kodi wote.
89. Mheshimiwa Spika, baada ya kuongeza mapato ya Serikali ni vyema usimamizi wa matumizi ya fedha za umma uwe makini zaidi kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa. Ni matumaini ya Serikali kuwa utaratibu mpya unaotumika hivi sasa chini ya Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali ya mwaka 2001 na ile ya Uagizaji na Ununuzi wa Vifaa vya Serikali ya mwaka 2001 utawezesha kudhibiti matumizi mabaya ya fedha, vifaa, magari na mitambo ya Serikali kwa kiwango kikubwa. Aidha, Maafisa Wahasibu wawe waangalifu zaidi na wizi unaotokea katika ofisi na taasisi mbalimbali za Serikali. Utaratibu wa kutunza fedha nyingi katika ofisi uachwe isipokuwa pale ambapo pana uwezo huo. Uchukuaji wa fedha za umma na hata za makampuni binafsi ufuate taratibu zinazokubalika ili kusiwe na vishawishi vya wizi.
90. Mheshimiwa Spika, suala jingine ninalotaka kulisemea ni malalamiko yanayotolewa kuhusu viwango vya mishahara na vile vya malipo ya mafao. Kwa upande wa mishahara, Serikali imejitahidi kupandisha mishahara kutegemeana na uwezo wa bajeti. Watumishi wangependa walipwe mishahara mizuri zaidi na Serikali pia ingependa hali iwe hivyo. Tatizo letu ni uwezo! Kama nilivyosema, hata bajeti ya matumizi ya kawaida ambayo ni pamoja na mishahara inachangiwa na fedha za watu wengine. Katika bajeti ya mwaka 2002/2003, mishahara ya watumishi wa umma inachukua zaidi ya asilimia 35. Ufumbuzi wa tatizo hilo ni kukuza uchumi na mapato ya Serikali ili mishahara iongezeke. Kwa upande wa watumishi wa mashirika ya umma wanaodai mafao makubwa zaidi ya yale ya kisheria ni lazima tukubaliane kuwa fedha hizo lazima ziwepo katika shirika kama faida iliyolimbikizwa na siyo kutoka penginepo. Katika bajeti ya 2002/2003 hatuna fedha za mkono wa heri ila tumetenga fedha kwa ajili ya mafao ya kisheria kwa wale watakaoachishwa kazi.
91. Mheshimiwa
Spika, zoezi la ubinafsishaji wa mashirika makubwa ya huduma limeingia katika
hatua muhimu na yenye kuhitaji ushirikiano wa karibu wa wadau wote. Wito wangu kwa Watanzania ni kwamba tujenge
hoja zenye maslahi kwa Taifa kwanza na binafsi baadaye. Aidha, Watanzania tuna hulka ya kistaarabu. Pale ambapo tuna hoja tofauti na hatua
zinazochukuliwa na Serikali ni vyema tutumie taratibu zilizowekwa kuzifikisha
kwenye meza ya majadiliano. Watanzania
tunakumbuka enzi za wingi wa Mashirika ya Umma ambapo wakati mwingine ajira
haikutazama uwezo wa shirika bali ilizingatia zaidi matashi ya viongozi. Leo katika dunia ya utandawazi na ushindani
hali ni tofauti, ajira hutegemea uwezo wa uzalishaji na faida. Jeuri ya Shirika la Umma hivi sasa siyo
umiliki wake bali uwezo wake wa kushindana na kutoa huduma kwa ufanisi na kwa
gharama nafuu. Milango ya biashara ipo
wazi na utandawazi umeleta ushindani mkubwa ambapo ili tuweze kuuhimili ni budi
tujizatiti na kujijenga kiteknolojia.
Ubinafsishaji ni mbinu mojawapo ya kutuwezesha kuingiza teknolojia mpya
kwenye shughuli za uchumi nchini.
Tushirikiane basi ili tuwezeshe mashirika ambayo bado tunayarekebisha yafikie
malengo na hivyo kuanza kujijenga na kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo yetu. Serikali inawahakikishia
wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kuwa kwa vyovyote vile haki itakuwa
inatendeka kulingana na sheria zetu.
92. Mheshimiwa
Spika, napenda kuwashukuru Mawaziri wote na Naibu Mawaziri wote kwa ushauri wao
ambao umewawezesha Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa
Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yao ya kitaifa kwa ufanisi. Aidha, nawashukuru wafanyakazi wote wa
Serikali na taasisi zake chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Marten
Lumbanga pamoja na vyombo vyote vya dola kwa kuiwezesha Serikali kutekeleza
majukumu yake ipasavyo na kuiwezesha kukamilisha maandalizi yote ya bajeti ya
Serikali ya mwaka 2002/2003 pamoja na makadirio ya matumizi ya fedha ya kila
wizara, mikoa na taasisi zinazojitegemea. Nawashukuru Watanzania wote na
Washirika wetu wa Maendeleo mbalimbali kwa mchango wao ambao ndiyo unaoiwezesha
Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
93. Mheshimiwa Spika, napenda vilevile kuwashukuru Mheshimiwa William Lukuvi, Waziri wa Nchi (Sera) na Mheshimiwa Omar Ramadhan Mapuri, Waziri wa Nchi (Habari na Siasa) kwa msaada mkubwa na ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu niliyokabidhiwa ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru vilevile wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Bwana Raphael Mollel, kwa ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na Mawaziri wa Nchi. Aidha, nawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2002/2003.
94. Mheshimiwa Spika, nchi yetu katika mwaka wa fedha 2001/2002 imepata misaada na mikopo kutoka kwa wahisani wetu mbalimbali. Misaada na mikopo hiyo imetoka kwa nchi rafiki, nchi fadhili, taasisi za fedha duniani, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mifuko mbalimbali duniani, madhehebu ya dini mbalimbali na mashirika yasiyo ya Serikali. Misaada na mikopo hiyo imechangia sana katika kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Napenda kuwashukuru wote kwa dhati na kuwahakikishia kuwa Watanzania tunathamini misaada na mikopo yao na tutaendelea kushirikiana nao katika harakati za maendeleo ya Taifa letu.
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA
WAZIRI MKUU NA TAASISI ZAKE PAMOJA NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2002/2003
95. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2002/2003, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake pamoja na Ofisi ya Bunge, inaomba jumla ya Shilingi 35,682,928,400 kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo. Kati ya fedha hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaomba jumla ya Shilingi 25,274,261,000 na Ofisi ya Bunge inaomba jumla ya Shilingi 10,408,667,400. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaomba jumla ya Shilingi 6,235,420,000 kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo. Kati ya hizo, Shilingi 2,000,000,000 ni fedha za hapa na Shilingi 4,235,420,000 ni fedha za nje.
96. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.