HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA MHESHIMIWA BASIL P. MRAMBA (MB) KATIKA BUNGE TAREHE14 JUNI, 2001 AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2001/2002

UTANGULIZI:

1.            Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2001/2002.   Pamoja na hotuba hii vimetayarishwa vitabu vinne vinavyoelezea kwa undani takwimu mbalimbali za bajeti.  Kitabu cha kwanza kinahusu makisio ya mapato.  Kitabu cha pili na cha tatu vinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara na Idara pamoja na Mikoa na Halmashauri za Miji na Wilaya.   Kitabu cha nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara na Mikoa pamoja na Halmashauri.  Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2001/2002.  

2.            Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya Bajeti hii.  Napenda kuishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge kwa kazi nzuri iliyofanya ya kuchambua makisio yote kwa kina.  Ushauri uliotolewa na Kamati hiyo umesaidia sana kuboresha bajeti hii.  

3.            Mheshimiwa Spika, maandalizi ya bajeti yamehusisha washikadau wengi na vyombo mbalimbali.  Kwa msingi huo, nawashukuru pia wafanyakazi wa Ofisi ya Rais Mipango na Ubinafsishaji, Wizara nyingine zote, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Halmashauri zote, pamoja na Taasisi za Kitaifa kwa michango yao iliyosaidia kufanikisha utayarishaji wa bajeti hii.  Naomba pia niishukuru Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba kwa kutayarisha miswada na nyaraka mbalimbali za sheria kama sehemu ya zoezi hili. Aidha, napenda kuwashukuru wafanyakazi wenzangu wa Wizara ya Fedha, nikianzia na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Abdisalaam Issa Khatibu (Mb); Katibu Mkuu Peter J. Ngumbullu, Manaibu Katibu Mkuu Peniel Lyimo na Gray Mgonja, Viongozi wengine wa Hazina na wafanyakazi wote.  Namshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha kwa wakati hotuba hii, vitabu vya bajeti, pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu bajeti hii.  Mwisho nawashukuru kipekee wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera na namna ya kutoza kodi mbalimbali nchini ambayo yamezingatiwa sana katika kuandaa bajeti hii.  

4.            Mheshimiwa Spika, tunamaliza mwaka wa fedha wa 2000/2001 tukiwa na majonzi kwa kufiwa na Wabunge wenzetu kadhaa.  Katika kipindi hiki cha Bunge jipya Wabunge watano (5) waliaga dunia.  Wabunge hao ni Hayati John Ndugulile Mgeja aliyekuwa Mbunge wa Solwa; Hayati Ernest Nyanda aliyekuwa Mbunge wa Busega; Hayati Biku Mohamed Biku aliyekuwa Mbunge wa Solwa; Hayati Prof. Chrispin Hauli aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Ludewa na Hayati Abbas Gulamali aliyekuwa Mbunge wa Kilombero.  Mwenyezi Mungu aziweke roho za Marehemu hawa mahali pema peponi.  

5.            Mheshimiwa Spika, kikao hiki cha Bajeti ni cha kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge uliofanyika mwezi Oktoba, mwaka 2000.  Chama cha Mapinduzi kilishinda uchaguzi huo kwa kishindo.  Hotuba hii ni ya kwanza katika kutekeleza  Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha CCM.  Naomba Waheshimiwa Wabunge muipokee kwa imani na matumaini makubwa.  

UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2000/2001:

6.            Mheshimiwa Spika, tathmini inaonyesha kwamba sera na malengo  ya  bajeti  ya  Serikali ya mwaka wa fedha unaoisha yamepata   mafanikio ya kuridhisha.    Mwaka   wa   kalenda   wa  2000,     uchumi ulikua kwa asilimia 4.9  ukilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 1999.  Mfumuko wa bei uliendelea kupungua na kufikia asilimia 5.3 kwa mwaka ulioishia Machi 2001 na  unatarajiwa  kuwa  asilimia  4.9  ifikapo  mwisho  wa  mwezi  huu  wa Juni 2001.  Akiba ya fedha za kigeni iliongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni moja mwisho wa mwezi Machi 2001, ambayo inatosha kulipia bidhaa na huduma za kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi mitano.  Kiwango hiki hakijawahi kufikiwa katika historia ya Tanzania.  

7.            Mheshimiwa Spika, makusanyo ya mapato ya Serikali kwa kipindi cha Julai 2000 hadi mwezi Machi 2001, yalifikia shilingi 686.316 bilioni ikilinganishwa na makisio ya shilingi 647.209 bilioni, kwa kipindi hicho. Kiasi hicho kinaonyesha ongezeko la shilingi 39.107 bilioni zaidi ya lengo.  Aidha, mwelekeo unaonyesha kwamba hadi Juni 30, 2001, makusanyo yatafika kiasi cha shilingi 912.906 bilioni yakilinganishwa  na  kiasi kilichokisiwa katika bajeti cha shilingi 861.402 bilioni.  Hili ni ongezeko la shilingi 51.504 bilioni sawa na asilimia 6 zaidi ya lengo.  

8.            Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi katika mwaka 2000/2001, Serikali imeendelea na utaratibu wa 'Cash Budget' kwa lengo la kudhibiti matumizi yake. Utaratibu huu umesaidia sana kuboresha nidhamu ya matumizi katika vyombo vya Serikali.  Katika mwaka huu wa fedha kuanzia Desemba 2000 Serikali ilitoa mgao wa fedha za matumizi kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu badala ya kila mwezi kwa sekta zinazopewa  kipaumbele (Priority Sectors).  Hatua hii imesaidia sekta hizo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha na hivyo kupanga vizuri matumizi yao.  Aidha, katika mwaka huu wa fedha Bunge lako lilipitisha sheria mbili za kudhibiti mapato na matumizi.  Sheria ya kwanza ni ya kusimamia fedha za Serikali (Mapato na Matumizi pamoja na Ukaguzi wa Hesabu  za  Serikali)  na  Sheria  ya pili inahusu taratibu za manunuzi ya vifaa na huduma serikalini. 

Sheria hizi mbili mpya ambazo zitaanza kutumika rasmi mwezi ujao,  zimechukua nafasi ya sheria ya 'Exchequer and Audit Ordinance' ya mwaka 1961 ambayo imefutwa. Madhumuni ya sheria hizi ni kuboresha zaidi usimamizi, udhibiti na ukaguzi wa fedha, na ununuzi wa vifaa na huduma. Aidha, hesabu za Wizara zote sasa zimeingizwa katika mtandao wa kompyuta ili kudhibiti matumizi. Serikali hivi sasa iko mbioni kuingiza ofisi zote za Hazina Ndogo zilizoko mikoani katika mtandao huo na tunategemea zoezi hilo litakamilika katika miezi michache ijayo.  Aidha, Halmashauri za Wilaya 28 zimeshaingia katika mtandao na nyingine 29 zinafanyiwa majaribio ya kuingia katika mfumo huo kwa lengo la kuziingiza Halmashauri zote upesi iwezekanavyo.  

9.                  Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/2001, mgao wa fedha za matumizi uliendelea kuzingatia Sera ya Serikali ya kutoa upendeleo maalumu kwa Sekta za huduma ya jamii (Elimu, Afya na Maji),na huduma za kiuchumi kama vile barabara.  Shughuli za Uchaguzi Mkuu pia zilipatiwa fedha za kutosha na hivyo hapakuwa na matatizo kama yaliyotokea mwaka 1995.  Aidha, Serikali imeendelea kulipa deni la ndani lililohakikiwa, na hadi Machi 2001, kiasi cha shilingi 7.630 bilioni kililipwa kwa wazabuni, na shilingi 45.008 bilioni zililipwa kwa wadai wengine ambao ni pamoja na TANESCO, DAWASA, na vyombo vya fedha.  

10.             Mheshimiwa Spika,   ningependa kutoa taarifa kwamba madeni yote ya nyuma kati ya Serikali ya Muungano na TANESCO na DAWASA yamesawazishwa.    Hivyo kuanzia Januari mwaka huu, TANESCO na DAWASA haziidai Serikali Kuu.  Kuanzia Julai 2000, kila Afisa Mhasibu alitakiwa kulipia matumizi ya umeme, maji, na simu, kinyume na huko nyuma ambapo HAZINA ilikuwa inabeba mzigo huo kwa niaba ya Maafisa Wahasibu hao.  

11.             Mheshimiwa Spika,  matumizi halisi kwa kipindi cha  Julai 2000  hadi  Machi 2001,  yalifikia shilingi 906.905 bilioni  yakilinganishwa  na  makisio ya shilingi 985.394 bilioni.  Kati ya fedha hizo shilingi 736.024 bilioni ni matumizi ya kawaida na shilingi 170.881 bilioni ni matumizi ya maendeleo.  Mwelekeo unaonyesha kwamba matumizi yote yatafikia shilingi 1,493.899 bilioni (1.49 trilioni) kwa mwaka mzima wa 2000/2001 ikilinganishwa na makisio ya awali ya shilingi 1,394.588 bilioni (1.39 trilioni).   

MISAADA NA MIKOPO NAFUU YA NJE:

12.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2000 hadi Machi, 2001, mwenendo wa upatikanaji wa misaada kutoka Jumuiya ya Kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mashirika ya Fedha na Nchi Wafadhili, ulikuwa wa kuridhisha kwa ujumla.  Katika kipindi hicho cha miezi tisa, jumla ya misaada iliyopatikana ni shilingi 353.063 bilioni.  Kati ya misaada iliyopokelewa, shilingi 198.218 bilioni zilikuwa za urari wa malipo ya nje (balance of payments), msaada wa kulipia madeni ya Mashirika ya Fedha ya Kimataifa (multilateral debt fund), msaada wa mpango wa kusaidia bajeti kwa ajili ya kupunguza umaskini (poverty reduction budget support – PRBS) na msaada wa kapu kwa sekta za afya na serikali za mitaa (basket funds).  Kiasi hicho kilichopatikana chini ya programu hizi katika kipindi cha Julai 2000 – Machi 2001, ni kikubwa kuliko kile kilichokuwa kimekadiriwa cha shiling 154.456 bilioni.  Aidha, shilingi 118.974 bilioni zilipatikana kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi hicho, ikiwa ni chini ya makadirio ya shilingi 248.889 bilioni.  Hali kadhalika, chini ya mpango wa kufutiwa madeni wa HIPC, tulipata msamaha wa awali wa kufutiwa madeni (interim relief) kwa kiasi cha shilingi 46.062 bilioni.

MBINU ZA KUKUZA UCHUMI:

13.             Mheshimiwa Spika, katika miaka mitano iliyopita, Serikali ilichukua hatua muhimu mbalimbali za kurekebisha sera na mfumo wa uchumi na fedha, kwa lengo la kujenga msingi wa maendeleo ya taifa linalojitegemea.  Dira ya taifa (vision 2025) inaainisha dhamira hiyo, ambayo kwayo, mikakati mingi imetayarishwa na inaendelea kutekelezwa, ikiwa ni pamoja na mbinu za kuhamasisha uwekezaji, mkakati wa kuondoa umaskini, na mingine mingi.  

14.             Mheshimiwa Spika, njia kuu za kuondoa umaskini ni kuongeza kipato cha wananchi, na kuboresha huduma za msingi za jamii.  Njia pekee ya kuongeza kipato ni uchumi  wetu  kukua  kwa  kiwango  kikubwa  kuliko  cha  sasa  cha  asilimia 5  hivi.   Tunahitaji uchumi ukue kwa asilimia zaidi ya 8 kwa mwaka, ndipo tuwe na uhakika wa kupata matokeo endelevu ya kuondoa umaskini.  Uchumi ukikua kwa kiwango cha juu, wigo wa kodi kwa ajili ya mapato ya ndani utapanuka, na uwezo wa Serikali kugharamia shughuli za kuondoa umaskini na nyingine za maendeleo ya Taifa, utaongezeka.  

15.            Mheshimiwa Spika, njia kuu kuliko zote ya kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi, ni kufufua kilimo, ambacho kinabeba asilimia 80 ya Watanzania. Tukiweza kufikia na kuvuka asilimia 5 ya ukuaji endelevu katika kilimo, umaskini utapungua kwa kasi kubwa.  Mbinu mpya za kufufua kilimo ziko mbioni kukamilishwa, na Waziri wa sekta husika atazungumzia hili kwa undani katika maelezo yake hapa Bungeni.  

16.            Mheshimiwa Spika, mbinu nyingine muhimu ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi ni kuendeleza upanuzi na uimara wa sekta binafsi ya ndani na nje.  Serikali imekuwa ikisaidia maendeleo ya sekta binafsi tangu mwaka 1993, kwa njia mbalimbali, zikiwemo:-

(i)                 Marekebisho ya uchumi (macroeconomic reforms)  

(ii)               Sheria ya uwekezaji (1993 na 1997)

(iii)             Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma

(iv)              Uundaji upya wa Kituo cha Uwekezaji (TIC)  

(v)               Marekebisho ya Mfumo wa Kodi

(vi)             Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika kubuni na kutafakari sera za Serikali za maendeleo, ambazo ni pamoja na sera za sekta muhimu kama fedha (kodi), mawasiliano na uchukuzi, nishati (umeme), n.k.

17.            Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na sera hizo, licha ya kuchukua hatua nyingine zenye lengo la kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji ili sekta binafsi ikue na itoe mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya taifa na kupunguza umaskini.  Maeneo ambayo utekelezaji wake unaendelea ni pamoja na:-

·                    kuboresha zaidi mfumo wa kodi

·                    kuongeza mgao wa fedha katika bajeti kwa miundo mbinu kama vile barabara,

·                    kufanya mabadiliko ambayo yatapunguza gharama za uzalishaji,

·                    kutekeleza kwa haraka mabadiliko muhimu ya utawala bora,

·                    kuweka mazingira bora yanayoimarisha biashara kubwa, ndogo, za kati, na isiyo rasmi,

·                    kuendeleza sera ya kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha ili kudhibiti mfumuko wa bei,

·                    kuweka mazingira bora ya ushindani katika sekta ya benki ili kupunguza riba, na kuongeza uwezo wa vyombo vya fedha kutoa mikopo kwa wakopaji wadogo na wakubwa.  Hii ni pamoja na kukamilisha kanuni za usimamiaji wa taasisi za mikopo kwa wakopaji wadogo wadogo (micro-finance regulation);

·                    kuweka mazingira yatakayowezesha uanzishwaji wa vyombo vya uwekezaji wa pamoja (collective investment schemes);

·                    kuendeleza programu za ushirikiano chini ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kupanua soko na kuongeza biashara na uwekezaji.

  MKAKATI WA KUONDOA UMASKINI

18.            Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha mkakati wa kitaifa wa kupunguza umaskini kwa kushirikisha jamii ya Watanzania na nchi zinazotufadhili.   Mkakati  huo  uliwasilishwa  kwa Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia na kupitishwa na Bodi zao mwezi Novemba mwaka 2000.  Wakati tunatayarisha mkakati huo wa kupunguza umaskini (Poverty Reduction Strategy Paper - PRSP), tumekuwa pia tukikamilisha vigezo kadhaa kuhusu vita dhidi ya umaskini, vikiwemo kuboresha takwimu juu ya hali halisi ya umaskini nchini, kuboresha uwezo wetu wa kufuatilia mipango yetu, kuhakikisha Bajeti ya Serikali inaonyesha wazi tunalenga katika kupambana na umaskini, kufanya tathmini ya mtandao wa shule, kuendeleza chanjo kwa watoto, na vita dhidi ya Ukimwi, na kuendelea kuzungumza na wadai wetu wengine ili nao washiriki katika kutupunguzia madeni.  Wakati huo pia, katika kipindi cha mpito, Tanzania imepata msamaha wa awali wa madeni (Interim Debt Relief) kutoka Benki ya  Dunia,  Shirika  la  Fedha  la  Kimataifa, Benki ya  Maendeleo  ya  Afrika,  na  Wadai  wa  kundi  la nchi  tajiri  la  Paris  Club.  Hadi kufikia Aprili 2001, msamaha huo wa awali ulifikia dola za Kimarekani 54.6 milioni, sawa na shilingi 46.062 bilioni, ambazo nimezitaja hapo awali.  

19.            Mheshimiwa Spika, uamuzi wa mwisho wa kupatiwa msamaha kamili wa madeni (Completion Point) utafikiwa kabla ya Desemba mwaka huu.  Hivi sasa Serikali inakamilisha taarifa ya utekelezaji wa vigezo mbalimbali vya PRSP kwa ajili ya kufikia uamuzi huo wa mwisho wa kupunguziwa madeni.  Dalili zinaonyesha kwamba, mara uamuzi wa mwisho ukifikiwa, nchi zinazotudai za kundi la Paris Club, zitatufutia  madeni  yote,  na  Mashirika  ya  Fedha ya Kimataifa,   na   Benki   ya   Maendeleo   ya   Afrika    kwa   pamoja   yatatupunguazia  mzigo  wa  madeni kwa zaidi ya asilimia 70.  

20.            Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa vigezo muhimu vya programu ya kuondoa umaskini, tunapaswa tuendelee na sera sahihi za uchumi, fedha, na utawala bora.  Vigezo  vya  kuzingatia  hapa  ni  pamoja  na  usimamizi  bora  wa  bajeti  ya  Serikali, ikiwemo kuendelea kuwa makini na waadilifu katika kukusanya na kutumia mapato ya Serikali, kuendelea kuboresha mfumo wa kodi, kuboresha mazingira ya uwekezaji mitaji na biashara, miundo mbinu na huduma nyingine za uchumi.  

21.             Mheshimiwa Spika, mpango wa Taifa wa kupunguza umaskini unahitaji kupewa msukumo mkubwa kwa kushirikisha jamii yote ya Watanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa hususan nchi na mashirika yanayotufadhili.  Katika kuweka msukumo huo, mambo matatu hayana budi yafanyike:  

(i)                 Kuweka malengo ya Kitaifa yaliyo wazi,

(ii)               Kubuni mazingira ya kiuchumi ya Kitaifa ambayo yatachochea maendeleo, na

(iii)             Kujenga mfumo wa usimamizi na tathmini.

Mambo haya yameainishwa katika Dira ya Taifa (Vision 2025), na katika Mkakati wa Kuondoa Umaskini (PRSP).  

22.            Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, malengo, shughuli na viashirio vya mkakati wetu wa kupunguza umaskini vinazingatia maeneo matatu makubwa:- 

(i)                 kupunguza umaskini wa kipato,

(ii)               kuendeleza ubora wa maisha na ustawi wa jamii, na

(iii)             kupunguza madhara yanayoweza kuwapata watu maskini.

Njia ya kupunguza umaskini wa kipato ni kuwezesha shughuli za kuzalisha mapato ya aina mbalimbali kustawi.  Uwezesho huo utatokana na ukuaji wa kilimo,  upanuzi  wa  vitega  uchumi  vya   asilia  na vya kisasa vya uzalishaji, uimarishaji wa miundo mbinu hasa vijijini, kuendeleza nyenzo za uchumi mdogo, na kuboresha mfumo wa utawala na sheria ulio thabiti na unaochochea maendeleo.  

Umaskini wa kutokuwa na kipato unatokana pia na elimu ndogo, afya mbaya, na ustawi wa jamii ambao ni wa mashaka.  Hivyo, njia ya kuboresha maisha ya watu ni kuhakikisha kwamba kila mtu anapata nafasi sawa ya kupata elimu angalu ya msingi, anajua kusoma na kuandika, anapata afya bora, maji salama, chakula bora, lishe bora, na kwa hali ya sasa, kwamba anajikinga na madhara, hasa ya Ukimwi.  

23.            Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hali ya umaskini ya wananchi wetu, na kwa kutambua kwamba sekta ya binafsi bado ni changa, sehemu kubwa ya gharama za kutekeleza mkakati wa kuondoa umaskini itaendelea kubebwa na Serikali kwa kupitia bajeti yake.  Kiasi kikubwa cha fedha kitatokana na mapato yetu ya ndani, na kingine kitatokana na misaada ya wafadhili wetu, pamoja na mikopo nafuu kutoka vyombo vya fedha vya kimataifa.  Uwezo wetu wa kugharamia programu hiyo pia utasaidiwa na kufutiwa madeni chini ya mpango wa HIPC.  

24.            Mheshimiwa Spika, kwa sasa bado hatuna uhakika tutahitaji fedha kiasi gani miaka ijayo kwa kugharamia za mahitaji muhimu ya kuondoa umaskini.  Hii ni kwa sababu programu kabambe za kufufua kilimo na maendeleo vijijini hazijakamilishwa vilivyo.  Hata hivyo, ni wazi kwamba mahitaji yatakuwa makubwa kuliko uwezo wetu, na hivyo, itatubidi tuimarishe juhudi za kuongeza mapato ya ndani, tutumie mapato yetu kwa uangalifu mkubwa, na tuendeleze uhusiano mzuri tuliuonao sasa na wafadhili wetu na wengine wote wanaotuunga mkono katika vita dhidi ya umaskini.  

MALENGO YA BAJETI YA MWAKA 2001/2002:

25.            Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, sera ya bajeti ya mwaka 2001/2002 ni ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, ambayo kwa ujumla inalenga kuendeleza ustawi wa uchumi, na wakati huo huo kuongeza matumizi katika sekta na maeneo yaliyobainishwa ya kupunguza umaskini.  Malengo ya jumla ya uchumi, mapato na matumizi kwa mwaka 2001/2002 ni haya yafuatayo:-

(i)                 Kuongeza ukuaji wa uchumi kwa asilimia 5.9, mwaka huu wa 2001 na asilimia 6.2 mwaka 2002.  Ongezeko hili litatokana hasa na hali nzuri ya hewa, na kuchukuliwa kwa hatua nilizozieleza hapo awali.

(ii)               Kudhitibi mfumuko wa bei yaani upandaji wa gharama za maisha kwa kiasi cha kufikia asilimia 4.4 badala ya 4.9 kwa mwaka unaomalizika sasa.

(iii) Kulenga nakisi ya bajeti (bila misaada ya nje) kuwa asilimia 3.1 ya Pato la Taifa.  Nakisi hiyo ni kubwa kuliko ya mwaka huu wa fedha ya asilimia 1.2 ya Pato la Taifa kutokana na nia ya Serikali ya kuongeza matumizi chini ya mpango wa kupunguza umaskini.  Matumizi hayo ni kwa ajili ya elimu ya msingi, afya, maji, barabara vijijini, kilimo, mahakama, na vita dhidi ya Ukimwi.

(iv) Kuongeza matumizi yote ya Serikali (bila kujumuisha miradi inayogharamiwa na wafadhili) kutoka asilimia 13 ya Pato la Taifa kwa mwaka wa fedha unaomalizika na kufikia asilimia 15.2 ya Pato la Taifa mwaka ujao wa fedha.  Matumizi yasiyo ya mishahara (non-wage) yataongezeka kwa asilimia 28 kwa sekta zinazopewa kipaumbele.  Vile vile gharama za mishahara (wage bill) zitaongezeka kwa asilimia 10.

(v) Kupanua wigo wa kodi ili mapato ya kodi yafikie asilimia 12.1 ya Pato la Taifa.  

(vi) Kuendelea kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni katika kiwango kinachoweza kununua toka ng’ambo mahitaji ya bidhaa na huduma za kutosheleza miezi minne.  Hivi sasa kiasi hiki ni shilingi bilioni takribani 900 sawa na dola bilioni moja za kimarekani.  

SERA ZA MAPATO:

26.            Mheshimiwa Spika, sera za mapato zinalenga kuendeleza hatua zilizoanza miaka ya hivi karibuni za kupanua wigo wa kodi, na pia kuboresha mfumo na usimamizi wa kukusanya kodi, ili kuongeza ari ya wananchi ya kulipa kodi na kuondoa ukwepaji wa kodi wa watu wasio waaminifu.  

27.            Mheshimiwa Spika, sababu za msingi za nchi yetu kulazimika  kuwa na sera sahihi ya kodi ni pamoja na:-

(i)                 Kukusanya mapato ya kutosha kuiwezesha  Serikali  kugharamia huduma za uchumi, jamii, usalama na ulinzi, na kulipa madeni ya Serikali.

(ii)               Kuweka mazingira sahihi ambayo hayaongezi gharama kwa walipa kodi na wanaokusanya kodi (cost of compliance).

(iii)             Kuweka mazingira yatakayoiwezesha Tanzania kushindana katika ulingo wa biashara ya Kimataifa, ambayo ni pamoja na kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi.

(iv)             Kuwa na mfumo wa kodi ambao unatabirika.

(v)               Kutoa upendeleo maalum kwa baadhi ya sekta (kwa mfano kilimo) ambazo zinapewa kipaumbele cha juu katika maendeleo ya nchi, katika kuondoa umaskini.

 

28.            Mheshimiwa Spika, misingi hii ya sera za kodi imeainishwa katika hatua mpya za mapato nitakazopendekeza hivi punde.     

SERA ZA MATUMIZI:

29.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa  2001/2002, sera za matumizi zinalenga katika kutekeleza azma ya Serikali ya  kupunguza umaskini niliyoielezea hapo awali.  Hata hivyo, kutenga mgao mkubwa wa fedha kwa sekta zinazopewa kipaumbele kutakuwa na matokeo yanayotarajiwa iwapo tu, fedha hizo zitasimamiwa vizuri.  Kwa mantiki hii, Serikali kuanzia mwezi Julai itatekeleza kikamilifu Sheria ya Fedha za Umma (Public Finance Act) na ile ya Ununuzi wa Vifaa vya Umma (Public Procurement Act).  Aidha, mianya inayofanya vyombo vya Serikali kukopa bidhaa na huduma bila idhini na kusababisha Serikali kulimbikiza madeni itazibwa. Mfumo wa Kompyuta wa IFMS sasa umeanza kutumika kwa kila Wizara na pia umesambazwa hadi Mikoani ili kuwezesha taarifa za mapato na matumizi kupatikana Hazina moja kwa moja katika mtandao wa kompyuta.   Nia ni kuwa na mtandao huo hadi ngazi ya Halmashauri za Wilaya.   Aidha, utaratibu wa matumizi kwa fedha taslim  'Cash Budget' utaendelezwa lakini kwa kutoa fedha kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu  badala ya kila mwezi kwa sekta muhimu (priority sectors) . Sekta nyingine zitaendelea kupewa fedha kila mwezi, pamoja na maelezo kuhusu matarajio ya miezi mitatu inayofuata. Marekebisho haya ya utaratibu wa cash budget' yana lengo la kusaidia Maafisa Wahasibu kuwa na uhakika wa kiasi cha fedha wanazotegemea ili waweze kupanga matumizi yao kwa ufanisi zaidi na kwa kiasi kile tu cha mgao uliopo.  Utaratibu huu umeongeza sana nidhamu ya matumizi kuliko ilivyokuwa awali ambapo tabia ya ponda mali’  ilishamiri.  

30.            Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo linafuja fedha za serikali na ambalo halina budi kupatiwa ufumbuzi ni lile la mifuko mbalimbali iliyoundwa kusaidia vikundi au sekta maalum.  Mifuko hiyo ni pamoja na ule wa pembejeo, mfuko wa vijana, mfuko wa wanawake na mingine.  Sote tunajua kwamba fedha zinazotolewa kupitia mifuko hii hazirudi,  na  hivyo matarajio ya kufanya mifuko hii iwe mifuko endelevu, hayapo.  Utaratibu mpya wa kuendesha mifuko hii unatayarishwa.  Njia nzuri ni kutumia benki za hapa nchini kusimamia mifuko hiyo chini ya kanuni za huduma za mikopo midogo midogo (microfinance regulations).  Kwa hivyo fedha za mifuko hiyo hazitatolewa mpaka hapo utaratibu mzuri utakapobuniwa na kuamuliwa.  

31.            Mheshimiwa Spika, ili nchi iweze kupanga mipango yake ya maendeleo kwa uhakika zaidi,  ni  muhimu kuwa na takwimu sahihi za idadi ya wananchi wake.  Nchi yetu  haijafanya  sensa  kwa  zaidi  ya miaka kumi sasa.  Kwa kuzingatia ukweli huu, mwezi Agosti mwaka 2002, tunategemea kufanya sensa ya watu nchini kote.  Ili kufanikisha zoezi hilo maandalizi yanatakiwa yaanze sasa.  Kwa hivyo, Bajeti ya 2001/2002 imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 8.0 kugharamia maandalizi yanayotakiwa.   Nachukua fursa hii kuwaomba wananchi kujiandikisha itakapotangazwa kwani ni zoezi muhimu sana ambalo limeahirishwa mno.  

MASLAHI YA WATUMISHI

32.            Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua hali isiyoridhisha ya maisha ya watumishi wake kutokana na mishahara midogo.  Hali hii imesababisha baadhi ya watumishi wasio waadilifu kushawishika kujihusisha na vitendo vya wizi, rushwa au hujuma na pia kuwa na ufanisi mdogo katika sehemu zao za kazi.  Ili kurekebisha hali hii, Serikali katika mwaka huu wa fedha yaani 2001/2002, imetenga fedha kwa ajili ya nyongeza ya mishahara ya watumishi wake.  Kiasi kilichotengwa kwa zoezi hilo ni shilingi bilioni 30.  Idara Kuu ya Utumishi itatoa maelezo kuhusu marekebisho hayo mara itakapokamilisha uchambuzi.   Aidha, kwa upande wa wastaafu, Serikali inatarajia kuongeza kiwango cha chini cha pensheni kwa asilimia 20.  Vile vile katika mwaka wa fedha wa 2001/2002, Serikali itaanza kutekeleza uamuzi wake wa kuanzisha bima ya matibabu kwa watumishi wa umma baada ya kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa.  Chini  ya  utaratibu   huo,            mwajiri atachangia asilimia tatu  (3%) ya mshahara wa mtumishi na mtumishi mwenyewe atachangia kiasi kama hicho.   Utaratibu huu utaanza mwezi Julai, 2001 na tayari shilingi bilioni 11 zimetengwa katika bajeti hii.  

Mfuko wa Elimu

33.            Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili, 2001 Bunge lilipitisha sheria ya kuanzisha mfuko wa elimu wenye lengo la kusaidia kugharamia elimu ya juu.  Pamoja na mambo mengine mfuko huo utatumika kusomesha watoto ambao wazazi wao hawana uwezo.  Waziri mwenye dhamana ya elimu ya juu atatoa kanuni na taratibu za matumizi ya mfuko huo.  Kwa kuanzia, bajeti hii imetenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya mfuko huo.  

MISAADA NA MIKOPO NAFUU YA NJE

34.            Mheshimiwa Spika, ingawa juhudi zitaimarishwa za kuongeza mapato ya ndani, kiasi kinachotarajiwa kukusanywa bado hakitaweza kutosheleza mahitaji ya msingi ya bajeti ya Serikali.  Serikali bado itahitaji kupata mikopo nafuu na misaada kutoka nje.  

35.            Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua za Serikali za kusimamia sera za kukuza uchumi na kuondoa umasikini, Wafadhili wana nia ya kuendelea kuisaidia Tanzania. Mpango wa PRGF unaogharimiwa na Shirika la  Fedha la Kimataifa - IMF umeingia mwaka wa pili. Katika mwaka 2001/2002, tunategemea kupata jumla ya dola za Kimarekani 51.6 milioni sawa na shilingi  bilioni 46.440.   Fedha hizo zitasaidia kutunisha akiba ya fedha za kigeni kwa ajili ya uagizaji bidhaa kutoka nje na kulipa madeni ya nje.  Aidha, Benki ya Dunia - World Bank, chini ya Mpango wa kurekebisha uchumi, (PSAC) inatarajiwa kutoa mkopo nafuu kiasi cha dola za Kimarekani 80.0 milioni sawa na shilingi bilioni 72.0  katika mwaka 2001/2002.   Tunategemea pia kupata kiasi cha dola za Kimarekani 25 milioni, sawa na shilingi bilioni 22.5 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).  

36.            Mheshimiwa Spika, pamoja na mikopo nafuu tunayotegemea kupata kutoka Mashirika ya Fedha ya Kimataifa, tukifanikiwa kufikia hatua ya mwisho ya kusamehewa madeni chini ya mpango wa HIPC (completion point) wadai wetu watatupa msamaha mkubwa zaidi wa madeni, unaokadiriwa kuwa dola za Kimarekani 100 kwa mwaka, sawa na shilingi 90.0 bilioni.   Aidha, tunategemea katika mwaka 2001/2002, Wahisani marafiki wataendelea kuchangia katika programu mbalimbali kwa ajili ya kupunguza umaskini.

Makisio yanaonyesha kwamba Wafadhili wetu, Nchi marafiki, na Jumuiya ya Ulaya watatupatia misaada (grants) kiasi cha dola za Kimarekani 225 milioni sawa na shilingi  202.5  bilioni, kupitia kwenye mpango wa kusaidia bajeti kwa ajili ya kupunguza umaskini (PRBS), na misaada maalum kwa programu za kapu la sekta (basket funding).  Tunakadiria pia kupata dola za Kimarekani 336 milioni sawa na shilingi 302.272 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.  

37.            Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge waungane nami kumpongeza kwa dhati, kwa niaba ya wananchi, hasa maskini, Mheshimiwa Rais Benjam William Mkapa kwa mchango wake mkubwa wa kutupatia misaada na misamaha hiyo.  Haya ni matokeo ya juhudi zake makini katika kusimamia uchumi, kuinadi nchi yetu ng’ambo na kuiletea Tanzania sifa kubwa kama nchi inayo piga hatua nzuri ya maendeleo, inayotawaliwa kwa msingi wa demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, na ambayo mambo yake ni ya ukweli, uwazi na yenye kutabirika.  Tanzania ni miongoni mwa nchi za HIPC nne tu duniani ambazo zimekamilisha mkakati kabambe unaokubaliwa na jumuiya ya kimataifa na hivyo kuwa na sifa ya kusamehewa madeni.  

MFUMO WA MAKISIO YA BAJETI YA MWAKA 2001/2002:

38.            Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo awali  bajeti  ya mwaka 2001/2002, inalenga kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, ambayo imeweka kipaumbele kikubwa katika kuondoa umaskini uliokithiri nchini mwetu.  Kwa kuzingatia sera za uchumi zilizoelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji, pamoja na zile nilizoelezea hapo awali, kwa msingi wa mfumo wa kodi wa sasa bila ya marekebisho  yoyote,  Serikali  inatarajia  kukusanya  mapato  ya  ndani  ya jumla ya shilingi  991.198  bilioni katika mwaka wa 2001/2002.  Kwa upande wa matumizi, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi 1,764.737 bilioni (trilioni 1.76).   

39.            Mheshimiwa Spika,             kwa kuzingatia makisio ya kukusanya shilingi 991.198 bilioni kulingana na mfumo wa sasa wa kodi, na matumizi ya jumla ya shilingi 1,764.737 bilioni, (1.76 trilioni) pengo la shilingi 773.539 bilioni linajitokeza. Kama nilivyoeleza hapo awali, katika mwaka 2001/2002, Wafadhili mbali mbali wanatarajia kutupatia misaada na mikopo nafuu (ikijumuisha misamaha ya madeni) ya jumla ya shilingi 649.643 bilioni.  Kati ya fedha hizo, shilingi 283.770 bilioni ni mikopo na misaada itakayopitia kwenye bajeti chini ya programu mbali mbali, shilingi 63.600 bilioni ni kutokana na misamaha ya madeni, na shilingi 302.272 bilioni ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo.  Ni muhimu kueleza hapa kuwa baadhi ya wafadhili bado wameendelea kutoa misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo nje ya bajeti ya Serikali.  Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa misaada yote toka  kwa  wafadhili  itatolewa  katika  utaratibu  wa  ‘exchequer’  yaani kujumuishwa katika bajeti ya Serikali.  Kiwango hiki cha mchango wa wafadhili kinapunguza pengo hadi kufikia  shilingi 123.896 bilioni.

40.            Mheshimiwa Spika,  serikali inategemea kupunguza akiba yake (reserve) ya ndani kwa kiasi cha shilingi 69.910 bilioni.  Aidha, Serikali katika mwaka 2001/2002, inatarajia kupata shilingi 20 bilioni kutokana na uuzaji wa sehemu ya hisa katika mashirika ambayo Serikali ni mbia.  Maeneo haya mawili ya vianzio vya fedha yanapunguza pengo hadi kufikia shilingi 33.986 bilioni ambazo inabidi zipatikane kwa kuchukua hatua mpya za mapato.  

MAREKEBISHO YA MFUMO WA KODI NA HATUA MPYA ZA MAPATO

41.            Mheshimiwa Spika,  katika jitihada za kuboresha mfumo wa kodi, ada, na taratibu za kukusanya mapato ya Serikali, inapendekezwa kufanya marekebisho ya aina mbalimbali katika kodi.  Lengo la marekebisho haya ninayopendekeza ni kufanikisha malengo niliyoyaeleza hapo awali, ambayo ni pamoja na kuipatia Serikali mapato yaliyopangwa katika bajeti hii, kuleta uwiano mzuri wa kodi katika uchumi, na kupunguza adha na kero kwa wananchi, kuweka mazingira mazuri zaidi ya kutumia nguvu kazi na rasilimali nyingine katika maeneo muhimu ya uchumi kama vile kilimo, viwanda, utalii, madini, na biashara.  Aidha, hatua hizi za kodi zitasaidia sana mkakati wetu wa kupiga vita umaskini.   

42.            Mheshimiwa Spika,  Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika maeneo yafuatayo:-  

(a)               Mfumo wa ushuru wa forodha;

(b)               Mfumo wa kodi ya mapato;

(c)               Mfumo wa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT);

(d)               Mfumo wa kodi ya ushuru wa bidhaa;

(e)               Kuanzisha kodi mpya katika michezo ya kubahatisha;

(f)                 Kodi za Serikali za Mitaa;

(g)               Marekebisho ya baadhi ya sheria;

(h)               Marekebisho ya kodi ya huduma za viwanja vya ndege;

(i)                 Kodi ya pango la ardhi kwa mashamba; na

(j)                  Kodi na ada zinazokusanywa na Serikali Kuu.

 

Mfumo wa Ushuru wa Forodha

43.            Mheshimiwa Spika, kuhusu mfumo wa ushuru wa forodha, marekebisho yafuatayo yanapendekezwa:-

(a)          Viwango vya ushuru wa forodha (tariff bands) vipunguzwe kuwa vitatu (ukiacha cha sifuri) badala ya vinne vya sasa.  Kutokana na pendekezo hili, viwango vipya vya ushuru wa forodha vikilinganishwa na vya sasa vitakuwa kama ifuatavyo:-

            

Viwango Vya sasa

Viwnago VinavyoPendekezwa  

Husika  
0%   0% (i)         Pembejeo na zana za kilimo, ufugaji, uvuvi, madawa ya mifugo na binadamu, malighafi za kutengeneza madawa.  
5% 0% (ii)   Malighafi, bidhaa za uzalishaji na ukarabati  
10% 10% (iii)    Malighafi zilizosindikwa kiasi na vipuri mbali ya vile vya magari (semi-processed input and spares)  
20%   15%   (iv)  Malighafi zilizosindikwa kikamilifu  yaani (fully  processed inputs)  na vipuri vya magari
25%   25% v)   Bidhaa za walaji (consumer goods)  

44.            Mheshimiwa Spika, matokeo ya marekebisho haya ni kwamba ushuru wa forodha sasa utatozwa katika viwango vitatu tu – yaani asilimia 10, 15 na 25.  Bidhaa ambazo sasa hivi zinatozwa asilimia 5 ya ushuru, hazitalipa ushuru wa forodha.  Matumaini ya Serikali ni kwamba hatua hii itapunguza gharama za uzalishaji hasa kwa viwanda na wawekezaji wengine wanaoagiza kutoka nje malighafi na bidhaa za uzalishaji.  

45.            Mheshimiwa Spika, marekebisho haya ya mfumo wa ushuru wa forodha yanakadiriwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 18.791 bilioni.  Sambamba na punguzo hilo la mapato, mfumo mpya wa viwango vya ushuru unategemewa kupunguza mapato ya VAT, kwa kiasi cha shilingi 1.939 bilioni kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

 
Kufuta Tangazo la Serikali Na. 433 la Mwaka 2000

46.           Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia marekebisho ya mfumo wa ushuru wa forodha niliyoyaelezea hapo juu, hakuna haja ya kuendelea kuwa na Tangazo la Serikali Na. 433 (Government Notice No. 433). Tangazo hilo liliweka viwango tofauti na vile vilivyomo katika kitabu cha Ushuru (Tariff Book) kwa baadhi ya malighafi za viwanda vya ndani ili kuvipa upendeleo maalum.  Viwango vipya vya ushuru vinavyopendekezwa tayari vimezingatia azma hiyo.   Hatua hii inategemewa kupunguza mapato kwa kiasi cha shilingi 3.5 bilioni.  

Kutoza Ushuru wa Muda (Suspended Duty) kwa Baadhi ya Bidhaa Zinazoagizwa Kutoka Nje

47.            Mheshimiwa Spika, Ili kuhakikisha kuwa kuna ushindani wa haki katika soko la ndani kati ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na zile zinazotoka nje, inapendekezwa kutoza ushuru wa muda  (suspended duty) kwa baadhi ya bidhaa kutoka nje.  Bidhaa hizo zimeorodheshwa katika Muswaada wa sheria ya Fedha ya mwaka 2001.   Hatua hii itaongeza mapato ya Serikali kwa shilingi 2.4 bilioni.  

Utaratibu Mpya wa Kutathmini Bidhaa kutoka Nje:

48.            Mheshimiwa Spika, ili kuzingatia matakwa ya Shirika la Biashara la Kimataifa (World Trade Organisation) ambako Tanzania ni mwanachama, utaratibu wa kutathmini bidhaa kutoka nje kwa ajili ya kutoza kodi, umebadilika. Utaratibu ujulikanao kama "Agreement on Customs Valuation" (ACV) ndio unatumika sasa.  Kutokana na badiliko hili hakuna tena matumizi ya mtindo wa “bei ya chini ya kukadiria kodi” (minimum dutiable value -MDV) isipokuwa kwa Sukari inayoagizwa kutoka nje ambayo inatawaliwa na mkataba maalum kati ya Serikali na wawekezaji.  

49.            Mheshimiwa Spika,            napendekeza kulifanyia marekebisho Tangazo la Serikali No. 133 la mwaka 1996 ili kuweka ukomo (Cap) wa kiwango cha ushuru wa forodha wa asilimia 5 kwa mwezi kitakachotozwa waingizaji kwa muda mfupi wa vifaa na zana za uwindaji wa kitalii.  Hatua hii inalenga kuondoa kero na lawama zilizokuwa zinatolewa na sekta ya utalii, na haina madhara kwa mapato ya Serikali.

Marekebisho ya Mfumo wa Kodi ya Mapato

50.            Mheshimiwa Spika, inapendekezwa pia kufanya marekebisho kadhaa katika eneo la kodi ya mapato kama ifuatavyo:-

(a)          Kodi ya zuio kwenye bidhaa na huduma (withholding tax) on goods and services) inafutwa kwa wale wote ambao wana kitambulisho cha walipa kodi (tax payer identification number - TIN).  Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato kwa kiasi cha shilingi 12.179 bilioni.

(b)          Kwamba kipengele cha "additional 15% capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure"  kwenye Sheria ya Madini ya mwaka 1998 (The Mining Act, 1998) sasa kitumike kwa wawekezaji wa zamani tu. Wawekezaji wapya wasipewe unafuu huo.  Hatua hii inafuatia  ukweli  kwamba,  sehemu ya 17 ya Sheria hiyo tayari inaruhusu punguzo la asilimia 100 (100% capital allowance).   Aidha, hatua hii itasaidia pia kurahisisha usimamizi wa kodi katika sekta ya madini. Pendekezo hili halitaathiri mapato ya Serikali.  

(c)               Kurekebisha kifungu cha 87(1) cha Sheria ya madini ya mwaka 1998 ambacho kinaruhusu mchimbaji madini kuahirisha ulipaji wa mrahaba (royalty) au kurejeshewa mrahaba aliolipa endapo atakuwa na matatizo ya ukwasi.  Napendekeza kwamba kifungu hiki cha sheria kiwahusu wawekezaji wa zamani tu.  Marekebisho haya hayategemewi kuipatia au kuipotezea Serikali mapato.

(d)              Napendekeza kuunganisha kodi za “Housing Levy” na ile ya “VETA” na kuwa kodi moja ya kuendeleza ufundi stadi (skills development levy).  Kiwango cha    kodi  hiyo  kitakuwa   asilimia         sita (6%) ya gharama za mishahara (wage bill).  Kadhalika, kodi hii sasa itakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kugawanywa kama ifuayavyo: theluthi mbili ya kodi itawasilishwa Hazina, na theluthi moja itawasilishwa Taasisi ya VETA.  Hatua hii itapunguza gharama kwa waajiri (cost of labour) na haipunguzi mapato ya Serikali wala ya VETA.  

(e)              Napendekeza kuondoa kodi ya zuio kwenye riba (interest) kwa mikopo iliyokopwa nje ya nchi.  Pendekezo hili lina lengo la kuhuisha kodi hiyo ya riba na kuboresha mazingira ya uwekezaji.  Hatua hii itapunguza mapato kwa shilingi 378 milioni.  

(f)                 Napendekeza kufuta kipengele cha gawio hisia (deemed dividend) kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato. Pendekezo hili linalenga kumwondolea mamlaka Kamishna wa Kodi ya Mapato ya kujitangazia gawio endapo kampuni haitafanya hivyo ili kuondoa kero iliyopo hivi sasa kwa kampuni zinazolipa kodi.  

(g)              Napendekeza kufuta malipo ya awali ya kodi ya mapato ambayo mfanya biashara hutakiwa kulipa kabla hajaanza biashara. Pendekezo hili linalenga kuwawezesha hasa  wafanyabiashara ndogo ndogo kupata leseni na kuanza biashara halali, badala ya utaratibu wa sasa ambao wengi wanashindwa kulipa kodi hiyo ya awali na hivyo kulazimika kufanya biashara bila leseni. Hatua hii inategemewa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 3.179 billioni.   

Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)

51.            Mheshimiwa Spika, katika eneo la kodi ya VAT, napendekeza kufanya marekebisho yafuatayo:-

(i)     Nafuta msamaha wa kodi ya VAT kwa Serikali na taasisi zake.  Kwa maana hiyo basi, Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Taasisi zinazotegemea Serikali Kuu kwa bajeti zao sasa zitalipa  Kodi  ya  Ongezeko  la  Thamani  (VAT).  Hata hivyo, misamaha hii ya kodi itaendelea kutolewa kwa vifaa na huduma kwa ajili ya miradi inayofadhiliwa na wafadhili na mashirika na taasisi za kujitolea, kulingana na sheria na mikataba maalum iliyopo.  Hatua hii inategemewa kuipatia Serikali jumla ya shilingi 56.0 bilioni kwa mwaka 2001/2002.

(ii)                Kwa kuzingatia pendekezo nitakalotoa hivi punde la kuanzisha kodi mpya ya michezo ya kubahatisha (gaming tax), napendekeza pia kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye michezo yote ya kubahatisha ili kurahisisha utozaji wa kodi hiyo mpya. Hatua hii inategemewa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 2.0 bilioni, ambayo yatafidiwa na kodi mpya inayopendekezwa.  

(iii)             Naondoa  kodi ya VAT kwa usafiri wa barabara (ground transport) kwa watalii (tour operators).  Lengo la hatua hii ni kuleta usawa na haki katika biashara ya utalii.  Hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Shs. 500 milioni.  

(iv)             Napendekeza kuondoa kodi ya VAT kwa vifungashio vya maziwa (milk packaging materials).  Hatua hii ina lengo la kusaidia kupunguza  gharama za viwanda vya kutengeneza maziwa ili yaweze kuuzwa kwa bei nafuu na pia kumpatia mfugaji soko la maziwa ghafi.  Pendekezo hili litapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Shs. 400 millioni. Aidha, inapendekezwa kufuta uingizaji wa maziwa ya unga na kuweka ushuru wa ziada "suspended duty" wa asilimia ishirini na tano (25%) kwa aina nyingine zote za maziwa kutoka nje isipokuwa maziwa ya watoto (infant formula).   

(v)               Napendekeza kuondoa kodi ya VAT katika ‘Computers’, ‘Printers’ zake na ‘Accessories’ zake.   Hatua hii inalenga kuharakisha kasi ya Tanzania kuingia katika karne ya 21 ya mawasiliano na uchumi unaotegemea mtandao wa kompyuta katika zama za sasa za utandawazi.  Hii ni pamoja na kutoa motisha kwa vijana washawishike kujihusisha na shughuli za Kompyuta, kama wenzao wanavyofanya ulimwenguni kote.   Ni tegemeo langu kuwa shule, vyuo na taasisi za elimu zitachukua fursa hii kuanza kufundisha masomo ya kompyuta na hasa kutumia kompyuta zaidi kuliko sasa.  Hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 1.544 bilioni.

(vi)             Napendekeza kuondoa kodi ya VAT kwenye vifaa vya hospitali, na kodi zote kwa madawa ya walioadhirika na ukimwi, malaria na kifua kikuu.  Pendekezo hili linalenga kuongeza idadi na aina ya mashine na vifaa vya kuchunguza magojwa na kutibu wagonjwa ili kutoa unafuu kwa sekta ya tiba na hivyo kusaidia kupunguza gharama ya vifaa hivyo na madawa ambavyo hata bila ya kodi bado ni aghali sana.  Hatua hii pia inajibu lawama ambazo zimetolewa kwa Serikali kutoka mashirika na taasisi za kujitolea kwamba kodi katika vifaa vya kuokoa maisha ya binadamu ni kero kubwa.  Hatua hii pia itapunguza gharama kubwa mno za kupeleka watu kutibiwa nje ya nchi na haitegemewi kupunguza mapato ya Serikali. Aidha, pendekezo kuhusu dawa za ukimwi lina lenga kumwongezea uhai mgonjwa na linaenda sambamba na fikra za kitaifa na kimataifa.  Ieleweke kuwa bado hakuna dawa za kuponyesha kabisa ugonjwa huu na kuwa zilizopo bado ni aghali sana sana.

(vii)           Napendekeza kuondoa kodi ya VAT kwa nyuzi (yarn) zinazosokotwa nchini.  Pendekezo hili linalenga kupunguza gharama ya nyuzi hizi na kuongeza ajira kwa wafumaji wadogo wadogo wanaotumia mikono (hand looms).  Hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh.9 milioni.

(viii)         Napendekeza kuondoa kodi ya VAT kwenye vifaa vya uwekezaji katika miradi ya elimu.  Pendekezo hili linalenga kuvutia wawekezaji wa shule, vyuo na taasisi zenye hadhi ya kimataifa badala ya kupeleka wanafunzi nje ya nchi, hasa nchi jirani.  Hatua hii pia inajibu malalamiko yanayotolewa kwamba sera ya kodi inakwamisha uwekezaji katika elimu ya kisasa.   Hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa Sh.88.7 milioni.  

Mfumo wa Kodi ya Ushuru wa Bidhaa (Excise)        

52.            Mheshimiwa Spika, kuhusu mfumo wa Ushuru wa Bidhaa inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo:

(a)       Napendekeza kufanya marekebisho ya  viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa za mafuta ya petroli ili viwe kama ifuatavyo:-                   

Shs. Kwa Lita  
(i) Liquified Petroleum Gas (LPG) 228.0  
(ii)  Motor Spirit Premium (MSP)  146.0 
(iii)  Motor Spirit Regular (MSR) 135.0  
(iv) JET A I    56.0 
(v) Illuminating kerosine (IK) 122.0  
(vi) Gas Oil (GO) 127.0  
(vii) Industrial Diesel Oil (IDO)  201.0  
(viii) Heavy Furnace Oil (HFO) 35.0  

            Hatua hii ina lengo la kulinda mapato yatakayopotea kutokana na kufuta ushuru wa forodha wa asilimia tano (5) kufuatia marekebisho niliyotaja awali ya mfumo wa ushuru wa forodha.  Kutokana na marekebisho hayo, mafuta ya petroli sasa yatakuwa na kodi tatu tu, ambazo ni ushuru wa bidhaa (excise duty), VAT na ada ya barabara (fuel levy).  Hatua hii italinda mapato ya Serikali kwa kiasi cha  shilingi  8.311 bilioni.  Napenda kusisitiza kwamba pendekezo hili haliongezi kodi katika bidhaa za mafuta ya petroli, ila linapunguza idadi ya kodi hizo.

(b)               Napendekeza pia kupunguza ushuru wa bidhaa (excise duty) kwa mvinyo  unaotengenezwa kwa zabibu za hapa nchini kutoka  shilingi 700 kwa lita za sasa hadi shilingi 350  kwa lita.  Pendekezo hili lina nia ya kuhamasisha upya kilimo cha zabibu na kupanua viwanda vya mvinyo Mkoani Dodoma na hivyo kuondoa umaskini humo.  Hatua hii itapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi kidogo sana cha  shilingi milioni moja na nusu tu.  

(c) Sambamba na hatu hii, napendekeza pia kuanzisha utaratibu wa kuweka stampu ya kodi ‘tax stamp’ kwenye mvinyo unaoagizwa kutoka nje ili kudhibiti ukwepaji kodi katika bidhaa hii na kulinda viwanda vya mvinyo nchini.  Utaratibu  huo wa kuweka ‘tax stamp’ kwenye  mvinyo kutoka nje utaanza kutekelezwa mwezi Januari 2002.  

(d) Napendekeza kurekebisha ushuru wa bidhaa ‘excise duty’ kwa asilimia 5 (5%) kwenye bidhaa za sigara, bia na soda ili kuhuisha kodi hiyo kulingana na mfumuko wa bei.  Pendekezo hili linategemewa kuipatia Serikali mapato ya ziada ya shilingi 3.624 bilioni katika mwaka 2001/2002.  

Kodi Mpya kwenye Michezo ya Kubahatisha:

53.             Mheshimiwa Spika, kutokana na uzoefu ambao Serikali sasa inao kuhusu michezo ya kubahatisha, napendekeza kuanzisha kodi ya michezo ya kubahatisha (gaming tax).  Napendekeza kodi hiyo mpya iwe katika viwango vifuatavyo:-  

(i)               Casino:  (a)  shilingi 500,000 kwa meza moja kwa mwezi.

(b) shilingi 100,000 kwa mashine kwa mwezi.

(ii) Bahati nasibu binafsi (private lotteries) – asilimia 60 ya mauzo yote (gross sales)

(iii)             Mashine za Sloti (slot machines) shilingi 20,000 kwa mashine kwa mwezi.  

Kodi hii mpya inatarajiwa kuipatia Serikali mapato ya kiasi cha shilingi 7.0 bilioni katika mwaka 2001/2002.  Napendekeza kwamba asilimia 92 ya mapato hayo iingie Serikalini na asilimia 8 iliyobaki iende kwa chombo cha usimamizi (regulator).  

Kodi za Serikali za Mitaa:

54.            Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, nakumbushia na kusisitizia:  

(i)                 Utekelezaji wa dhati wa sheria inayotaka Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kushauriana na Waziri wa Fedha kabla ya kufanya marekebisho katika sheria za kodi na ada mbalimbali za Serikali za Mitaa.  Hii ni kutokana na kudhihirika kuwa bado kuna mgongano kati ya Sera za Kodi Kitaifa ambazo hutangazwa na Waziri wa Fedha na kodi au ada mbalimbali zinazoanzishwa na Serikali za Mitaa.  Hatua hii ina lengo la kuondoa kero ya kuwepo kwa kodi nyingi mno na hasa kwa wakulima, wafanya biashara na wenye viwanda.

(ii)               Ukomo wa kiwango cha asilimia 5 cha ushuru wa mazao ya mkulima, na mfugaji uzingatiwe ili kuondoa utata uliopo sasa wa baadhi ya Halmashauri za Wilaya kutoza viwango zaidi ya hicho na hivyo kuleta lawama kutoka kwa wananchi wa vijijini na vyama vya ushirika.

(iii)             Napendekeza kuhamisha utoaji leseni za biashara zifuatazo kutoka Serikali za Mitaa kwenda Serikali Kuu:-

(a)               Biashara za uingizaji  bidhaa (import trade)

(b)               Wakala wa kulipwa (commission agents)

(c)               Uwakilishi wa Wana-viwanda (manufacturers’  representatives)

(d)               Wakala wa Wasafiri (travel agents)

(e)               Kambi za Watalii (tourist camps)

(f)                 Wauza Magari (motor vehicle dealers)

(g)               Wahudumu kwa Watalii (tour operators); na mwisho

(h)               Masonara (goldsmith)  

Leseni hizo zitatolewa na mamlaka zinazosimamia maeneo husika.  Hatua hii ina lenga kuhuisha usimamizi (regulation) wa maeneo hayo ambayo yana upeo wa kitaifa na wa kimataifa.  

(iv)             Napendekeza kuhamishia Halmashauri za Wilaya uandikishaji na utozaji leseni za biashara  na  viwanda  vidogodogo, na shughuli zote ndogo ndogo (micro  enterprises).  Lengo la hatua hii ni kuoanisha (rationalise) leseni mbali mbali kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na pia kuondoa usumbufu na gharama kwa walipa kodi husika.  Inalenga pia kupunguza gharama na usumbufu kwa wahusika.

(v)               Napendekeza pia kwamba masharti ya kutoa leseni za biashara yapunguzwe sana.  Njia moja ya kupunguza masharti hayo na kuondoa kero ni kuwa na kituo kimoja (one stop centre) cha kuandikishia na kutolea leseni za biashara vijijini, wilayani, mikoani, na wizarani.  

(vi)             Napendekeza kuwa leseni za utaalam (professional licence) kwa watu walioajiriwa zifutwe, kwani ni kero, zinaongeza gharama za ajira, na kupunguza ajira hasa za wananchi wasomi.  

(vii)           Inapendekezwa pia kwamba sheria ya Uhamiaji ihuishwe na ile ya Biashara ili kuondoa kero na  utata uliopo sasa hasa kuhusu wawekezaji.  

Marekebisho Mengine ya Baadhi ya Sheria

55.            Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, napendekeza kufanya marekebisho yafuatayo:-  

(i)                 Kuhusu Sheria ya Ushuru wa Barabara yaani, (Road Toll Act, 1985).  Napendekeza kubadilisha jina la kodi ya “road toll” liwe “fuel levy”.   Madhumuni ya hatua hii ni kuondoa utata uliojitokeza kwa baadhi ya walipa kodi hiyo ambao hutumia mafuta ya petroli katika vyombo visivyotumia barabara kama vile reli na vyombo vya majini au katika mitambo.  Hawa wanadai kwamba wasingetakiwa kulipa kodi isiyo wahusu.  Kwa hiyo sheria ya “road toll” (Road Toll Act, 1985) irekebishwe ili kuondoa utata huo na kila anayetumia “fuel” alipe kodi hiyo.

(ii)               Napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa  Stempu (Stamp Duty Act No. 20 of 1972) kama ifuatavyo:

(a)               Ushuru wa Stempu kwa mikataba ya ukodishaji (lease agreements) uwe asilimia 0.96 au shilingi 10.0 milioni kutegemea  ipi ni ndogo.  Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za mikataba ya ukodishaji ambazo zimelalamikiwa sana na washika dau kwamba zinaathiri uwekezaji.

(b)               Ushuru wa Stempu kwa mapato yatokanayo na mazao ya kilimo unafutwa.  Ushuru huu umekuwa  kero  kubwa  kwa   wakulima.  Kuondolewa kwake kutalinda pato la mkulima na kusaidia kupunguza umaskini.

(c)               Ushuru wa stempu kwa mapato yanayotokana na kodi ya pango (rental income) unapunguzwa na kuwa asilimia 1.5.   Lengo ni kuweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya makazi,  na  kuzuia  ukwepaji  wa  kodi  hiyo.  Hatua hii itapunguza mapato kwa kiasi cha shilingi 896 milioni.  

Marekebisho ya Kodi ya Huduma za Viwanja vya Ndege (Airport Departure Charges):

56.            Mheshimiwa Spika, katika eneo hili inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo:  

(i)                 Kuongeza kidogo kiwango cha kodi kwa wasafiri waendao nje ya nchi kuwa dola za Kimarekani 30 badala ya 20 za sasa.  

(ii)               Kuongeza kiwango cha kodi kwa wasafiri wa ndani kutoka shilingi 3,000/= hadi shilingi 5,000/=.

Hatua hii inategemewa kuipatia Serikali jumla ya shilingi 2.64 bilioni. Lengo la hatua hii ni kuvihuisha viwango hivyo ili viwiane na hali halisi ya sasa.  

Kodi Ya Pango La Ardhi Kwa Mashamba

57.            Mheshimiwa Spika, napendekezwa kurekebisha kodi ya Pango la Ardhi (Land Rent)  kwa Mashamba ya kibiashara  kutoka shilingi 600 kwa ekari hadi shilingi 200  kwa  ekari  kwa  mwaka,  kwa  mashamba  ya  kilimo, mifugo na misitu.  Hatua hii haitegemewi kupunguza mapato ya Serikali kwa sababu hivi sasa kodi hii haikusanywi – kwani wenye mashamba wanasema hawaimudu.   Lengo ni kuhimiza upanuzi wa mashamba makubwa kwa kutohodhi ardhi na kusisitiza umuhimu wa kulipia kodi raslimali hiyo.  

Kodi na Ada Zinazokusanywa na Serikali Kuu

58.            Mheshimiwa Spika,  inapendekezwa kufanya marekebisho ya mfumo wa ada mbali mbali zinazokusanywa na Serikali Kuu.  Madhumuni ya marekebisho hayo ni kuhuisha viwango vya ada hizo ili viwiane na hali halisi ya sasa.   Maelezo kuhusu viwango hivyo vya ada yapo kwenye muswaada wa sheria ya fedha wa mwaka 2001.  

Biashara ya Mipakani

59.            Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikubaliana kuweka mazingira bora zaidi ya kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta za uchumi, miundo mbinu, na biashara kati ya nchi na nchi ndani ya Jumuiya hiyo.  Moja ya maeneo yaliyopewa msukumo ni kurahisisha biashara ya mipakani ili wananchi wa nchi hizi waongeze biashara kati yao kwa njia  halali.  Kwa mantiki hiyo, ushuru wa forodha mipakani umepunguzwa sana.  Bidhaa kutoka Tanzania na Uganda kwenda Kenya zinapata punguzo la ushuru wa forodha kwa asilimia 90.  Kwa maneno mengine, kama ushuru Kenya ni asilimia 25, Mtanzania akiuza Kenya analipa asilimia 2 tu.  Bidhaa za Tanzania zikiingia Uganda zinapata punguzo la ushuru la asilimia 80.  Maana yake ni kwamba kama ushuru Uganda ni asilimia 25, Mtanzania akiuza Uganda analipa ushuru asilimia 5 tu.  Kwa upande mwingine, chini ya makubaliano hayo, bidhaa za Kenya zikiingia Tanzania na Uganda zinapata punguzo la ushuru la asilimia 80.  

60.            Mheshimiwa Spika, punguzo hili la ushuru ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ni changamoto kubwa kwa wananchi wetu.  Nimeagiza ofisi za Idara ya Forodha mikoani kuwaelimisha wananchi kuhusu changamoto hii, kwa kuweka matangazo kwa njia ya mabango na nyingine, na pia wao wenyewe kurahisisha taratibu za forodha, na kuhamasisha watu wafanye biashara halali, kwa kulipa huo ushuru mdogo sana. 

Muda wa Kodi Mpya Kutumika

61.            Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zitaanza kutumika tarehe 1 Julai, 2001 isipokuwa pale ilivyoelezwa vinginevyo.  

Majumuisho

62.            Mheshimiwa Spika,  mapendekezo haya ya marekebisho ya kodi na tozo nyingine, yamelenga katika kuboresha mfumo wa kodi, ili kupanua wigo kwa kuongeza utii (compliance), kuondoa kero hasa katika eneo la kilimo na mifugo, kuboresha mazingira ya ushindani, kuweka mazingira bora na ya wazi ya uwekezaji, kusaidia kusukuma maendeleo ya jamii kulingana na programu ya kupunguza umaskini, na mengine mengi.  Kwa ufupi, mapendekezo haya ni ya kuchochea uchumi ukue kwa kasi na kupunguza umaskini.  

MUHTASARI  

63.            Mheshimiwa Spika, muhtasari wa hatua zinazopendekezwa na matokeo yake kimapato ni kama ifuatavyo:

        

Shilingi bilioni  
(i)                Mfumo wa Ushuru wa Forodha -21.830
(ii)               Marekebisho ya Mfumo wa Kodi ya Mapato -15.737  
(iii)             Mfumo wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) 51.458  
(iv)              Mfumo wa Ushuru wa Bidhaa 11.934
(v)                Kodi Mpya ya Michezo ya Kubahatisha 6.417  
(vi)             Marekebisho ya Kodi ya Viwanja vya Ndege 2.640
(vii)            Mfumo wa Ushuru wa Stempu -0.896
Jumla 33.986  

Mapato haya ya shilingi 33.986 bilioni yanaziba pengo la bajeti ya mwaka 2001/2002 lililoelezwa hapo awali.  

SURA YA BAJETI YA MWAKA 2001/2002:

64.            Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2001/2002 inakuwa kama ifuatavyo

          Mapato                              Shilingi bilioni

A.         Mapato ya Ndani             1.025184 trilioni

           

(i)            Mapato ya Kodi 892.228  
(ii)            Mapato yasiyo ya Kodi 98.970  
(iii)            Mapato Mapya 33.986

       

B.         Mikopo na Misaada ya Nje   ikijumuisha HIPC    649.643 bilioni  
C.         Kupunguza akiba (Reserve)   69.910 bilioni  
D.         Mapato kutokana na uuzaji Hisa  20.000 bilioni  

Jumla ya Mapato yote           

1.764737 trilioni  

                     Matumizi

E.            Matumizi ya Kawaida                         1.412225 trilioni

(i)                  Deni la Taifa                         332.590

(ii)                 Wizara                                    625.610

(iii)               Mikoa                                         20.519

(iv)                Matumizi Maalum                  232.387

(a)   Bima ya Afya              (10.973)

(b)   Marejesho ya Kodi          (56.000)

(c)   Kampeni ya Ukimwi         (4.443)

(d)   Karo za Shule za Msingi  (11.000)

(e)   Malipo ya Wazabuni       (41.900)

(f)    Mengineyo                         (108.071)

 

(v)                 Serikali za Mitaa          201.119

     (a)  Miji                    37.039

                        (b)  Wilaya                  164.080

 

F.            Matumizi ya Maendeleo          352.512 bilioni

                                (a)    Fedha za Ndani     47.240

(b)      Fedha za Nje     302.272

(c)    Songosongo        3.000                     

Jumla ya Matumizi yote   1.764737 trilioni

 
MWISHO

65.            Mheshimiwa Spika, sura hii ya bajeti inaonyesha kwamba nchi yetu bado ni tegemezi kwa kiwango kikubwa.  Mapato yetu wenyewe yanatosha kugharamia asilimia 58 tu ya matumizi yote.  Hii ina maana kwamba karibu asilimia 42 ya bajeti yetu inategemea wafadhili, na mikopo nafuu kutoka nje.  Huu ni ushahidi tosha kwamba uchumi wetu haujakua kwa kiwango kinachotakiwa.  Tunahitaji kukuza uchumi kwa kiwango cha asilimia 8 na zaidi kwa mwaka ili kuongeza uwezo wetu wa kujitegemea na kuondoa umaskini.  

66.             Mheshimiwa Spika, bajeti ninayo pendekeza leo ni bajeti ya kuelekeza juhudi za taifa kwenye kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa na hivyo kupambana na umaskini wa mali; ambapo kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya taifa, ifikapo mwaka 2010  idadi ya watu maskini kupindukia  nchini  itakuwa  imepungua kutoka asilimia  48  ya    sasa    hadi    asilimia    24.

Maskini vijijini watapungua toka asilimia 57 sasa hadi asilimia 29 ifikapo mwaka 2010.  Njia ya uhakika ya kufikia viwango hivyo ni kutekeleza kwa nguvu zote sera na mikakati iliyowekwa katika kilimo, mifugo, utalii, viwanda vya msingi na uchimbaji madini.  Aidha, wananchi wenyewe ndio pekee watakaoweza kujikwamua kwa kufanya  kazi  hasa  za  kilimo  kwa  juhudi  na  maarifa  makubwa.   Hii  ni  kutokana  na ukweli  kwamba  umaskini  uko  katika  kaya  moja  moja  na  wala  si  jambo la kinadharia.  Tujikumbushe tena kwamba ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi na siasa bora.  Bajeti hii imeweka mazingira bora ya kila mtu kufanya kazi kwa kujipatia maendeleo katika hali ya utulivu na amani.  

67.            Mheshimiwa Spika, bajeti hii, kama itakavyo dhihirika katika kamati za kisekta wakati Mawaziri mbalimbali watakapofafanua sera na mikakati ya Wizara zao, ni mwanzo wa kupambana kwa dhati na umaskini wa hali.  Mpango wa HIPC ukitekelezwa inavyokusudiwa utaleta unafuu mkubwa kwenye kuelimisha watoto wetu; utaongeza chakula na lishe bora; utapunguza makali ya madhara ya gonjwa hatari la ukimwi, na utaimarisha haki za binadamu na utawala bora wenye kuzingatia demokrasia na sheria.  Bilevile mpango huo utapunguza vifo vya watoto chini ya miaka 5 na vya mama wajawazito.  Utaongeza kasi ya kuwapatia wananchi maji safi na salama mijini na vijijini, utaongeza idadi ya barabara za lami na morum zenye kupitika wakati wote kwa faida ya wakulima, wazalishaji mali wengineo na wafanyabiashara.  

68.            Mheshimiwa Spika, yote hayo yatawezekana kama watekelezaji watafanya kazi kwa ufanisi na uadilifu mkubwa, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa tena na tena, kwani bado lipo tatizo la uwezo “capacity” katika Wizara na Halmashauri za Wilaya.  Bado upo ubadhirifu na wizi wa mali za umma; bado wapo wavivu na wazembe katika utumishi wa umma.  Natoa rai kwa viongozi na hasa Waheshimiwa Wabunge, kuwa makini na wakali katika kusimamia na kuchunguza matumizi ya fedha na mali za umma.  Haipendezi kusikia kazi hii ikifanywa na mabalozi wanapokagua miradi wakati sisi tupo.  

69.            Mheshimiwa Spika,  hali kadhalika bajeti hii imejitahidi kuwasaidia wanyonge, wakiwemo wafanyakazi, wakulima wadogo wadogo, wafanyabiashara ndogo ndogo na masikini wasio na uwezo wa kusomesha watoto wao.  Imewapa fursa wasomi, wahitimu walio tayari kuingia kwenye usomi na biashara za kompyuta na mtandao wake ambazo zinasisimua vijana wengi kote duniani leo.  Imetoa nafuu kwa viwanda vidogo vidogo na biashara  ndogo ndogo  kwa  ujumla  hasa  pale  wanapoweza kuanza biashara bila kwanza  kutanguliza  kodi  kama  ilivyokuwa.   Imepunguza  sana ushuru kwa biashara za mipakani ili kuondoa aibu ya kutumia “njia za panya”, ambazo natumaini sasa zitaota nyasi kwa kukosa watumiaji, wapita njia!  

70.            Mheshimiwa Spika, bajeti hii imesikiliza sana mawazo na mapendekezo ya wataalamu mbalimbali, wafanyabiashara wa kati na wakubwa, imewasikiliza wana-utalii hasa wasafirishaji wa ndege na magari ya kitalii na wawindaji; imewasikiliza sana wana-viwanda, na wakulima wakubwa na imewasikiliza hata wafadhili na washauri wa kimataifa.  Na imewasikiliza sana Waheshimiwa Wabunge, hasa wakati wa kikao cha Kamati ya Fedha na Uchumi.  Nawashukuru wote hao walionipa mawazo na ushauri ulioniwezesha kufikia hatua hii ya bajeti.  

71.            Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kukiri kwamba ingawa tumepiga hatua kubwa sana na ya kujivunia  katika kukusanya kodi na ushuru wa aina aina, hadi kufikia wastani wa shilingi 76 bilioni kwa mwezi, bado kodi nyingi haikusanywi kutokana na ukwepaji wa makusudi.  Si siri kwa mfano, kwamba wenye maduka wana bei kwa VAT na bei bila VAT ambayo ni ya chini.  Wateja wengi hawadai risiti wanaponunua mali, kwa kutotambua kuwa wanashiriki katika kukwepa kodi.  Napenda kuwakumbusha wananchi wote kwamba wanaponunua bidhaa madukani wasisitize kupewa risiti, kwani huo ndio utaratibu wa kisheria unaotakiwa kuzingatiwa.  Hivi sasa Serikali imefanikiwa kwa kiasi kuziba mwanya uliokuwepo kwenye mafuta ya petroli ambapo udanganyifu umeanza kutoweka na ambapo adhabu kali sana zitawakabili watakao kamatwa wakiuza mafuta yasiyo na alama ya siri.  Serikali inayafanyia kazi maeneo mengine ya ukwepaji kodi kwa lengo la kuziba mianya iliyopo.  Kama nilivyoeleza, kuifanya Serikali yenyewe kulipia kodi manunuzi yake ni hatua ya kupambana na wakwepa kodi waliokuwa wakitumia vibaya mianya ya manunuzi ya mahitaji ya Serikali.  

72.            Mheshimiwa Spika, tatizo la pili ni katika sera za kodi; kuwepo kwa mamlaka tofauti za utozaji na ukusanyaji kodi, yaani Serikali za Mitaa, Waziri wa Fedha na Bunge. Malalamiko  mengi  kuhusu wingi wa kodi na leseni yanatokana na mgongano huo ambapo baada ya Waziri wa Fedha na Bunge kuidhinisha viwango vya kodi, hutokea eneo hilo likawekewa tena viwango vya ziada kutokana na maamuzi ya Halmashauri za Wilaya.  Nakusudia kusawazisha hali hii mwaka ujao wa fedha na nitafurahi kupata maoni ya Waheshimiwa Wabunge.  

73.            Mheshimiwa Spika, eneo lingine lenye utata katika kodi ni la misamaha.  Baada ya kuyumba yumba miaka ya karibuni, Serikali sasa imeamua kurejesha tena misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini na taasisi za kujitolea yanayotoa huduma bila faida (not for profit; NGO).   Uamuzi huu utatangazwa kisheria kwa njia ya Tangazo la Serikali (Government Notice) na hivyo kuondoa kero iliyojitokeza kuhusiana na misamaha  kwa makundi hayo.  Lakini utakuwepo udhibiti zaidi, kwa nia ya kuondoa udanganyifu. 

74               Mheshimiwa Spika,  naomba kutoa hoja.