HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA FREDERICK TLUWAY SUMAYE, MBUNGE, KUHUSU MAPITIO YA KAZI ZA SERIKALI MWAKA 2000/2001, MPANGO WA KAZI 2001/2002 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA 2001/2002
UTANGULIZI
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili mapitio ya kazi za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2000/2001, na mpango wa kazi kwa mwaka 2001/2002. Aidha, kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kisekta inayohusu Ofisi ya Waziri Mkuu, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako sasa likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2001/2002 ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake na Ofisi ya
Spika.
- Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze Mheshimiwa Basil Mramba, (Mb.), Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Dr. Abdallah Kigoda, (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji, kwa hotuba zao nzuri ambazo zimeelezea kwa muhtasari Hali ya Uchumi nchini na Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2001/2002. Napenda pia kuwashukuru kwa dhati Waheshimiwa Wabunge kwa uchambuzi wa kina, michango yao ya mawazo na kwa kukubali kuipitisha Bajeti hiyo ya Serikali. Serikali inaahidi kuzingatia kwa makini ushauri wote uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika mipango na utekelezaji wake.
- Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa matayarisho ya Bajeti ya Serikali ni matokeo ya juhudi kubwa ya uongozi na wafanyakazi wa Serikali, taasisi zake na wawakilishi wa taasisi binafsi. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya. Napenda pia kuishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge lako Tukufu kwa kuchambua Bajeti na Mpango wa Maendeleo wa Serikali wa mwaka 2001/2002. Aidha, Kamati za Kisekta za Bunge lako Tukufu zimepitia makadirio ya matumizi ya kila Wizara, Ofisi na Idara za Serikali zinazojitegemea. Napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati zote kwa kazi yao nzuri. Ni matarajio yangu kuwa utaratibu huu utaleta ufanisi zaidi katika kuliwezesha Bunge lako Tukufu kushiriki kikamilifu katika kuandaa sera na mipango inayolenga kuondoa kero za wananchi kwa kukuza uchumi, kupambana na umaskini na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma muhimu kwa jamii.
- Mheshimiwa Spika, katika muda mfupi tu wa uhai wa Bunge lako Tukufu tumewapoteza Wabunge wenzetu marehemu Ernest Nyanda, aliyekuwa Mbunge wa Busega, marehemu Bhiku Mohammed Bhiku, aliyekuwa Mbunge wa Solwa, marehemu Profesa Crispin Hauli, aliyekuwa Mbunge wa Ludewa na Naibu Waziri wa Fedha na marehemu Abbas Gulamali, aliyekuwa Mbunge wa Kilombero. Ninapenda kutoa pole kwa wananchi wa majimbo yao na kwa familia za marehemu. Tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amin.
HALI YA SIASA NCHINI
- Mheshimiwa Spika, nchi yetu ilifanya uchaguzi mkuu wa pili chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kama ilivyopangwa Oktoba, 2000. Katika uchaguzi huo nafasi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Ubunge, Baraza la Wawakilishi na nafasi za udiwani ziligombewa na vyama mbalimbali. Vyama vyote 13 vyenye usajili wa kudumu vilishiriki katika uchaguzi huo na vyama vinne tu yaani CCM, CUF, TLP na UDP vilitoa wagombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jumla ya Watanzania 10,088,484 walijiandikisha kupiga kura wakati waliopiga kura ni 8,517,598 sawa na asilimia 84.43 ya walioandikishwa. Kati ya kura halali 8,172,284 mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, alipata ushindi mkubwa wa kura 5,863,201, sawa na asilimia 71.7 ya kura hizo. Mgombea wa CUF, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba, alipata kura 1,329,077 sawa na asilimia 16.3; Mheshimiwa Augustino Lyatonga Mrema wa TLP alipata kura 637,115 sawa na asilimia 7.8 na Mheshimiwa John Momose Cheyo wa UDP alipata kura 342,891 sawa na asilimia 4.2 ya kura zote halali zilizopigwa. Kwa upande wa Tanzania Visiwani, kulikuwa na wagombea wawili wa kiti cha Urais. Kutokana na matokeo ya kura, Mheshimiwa Amani Abeid Karume wa CCM aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 67.1 ya kura zote halali na Mheshimiwa Seif Shariff Hamad wa CUF aliyeshindwa alipata asilimia 32.9 ya kura halali zilizopigwa.
- Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Wabunge, CCM ilishinda kwa kupata viti vya majimbo 202, CUF viti 17, TLP viti 4, CHADEMA viti 4, UDP viti 3 na NCCR-Mageuzi kiti 1. Kutokana na uwiano huo, Tume ya Uchaguzi iliwateua Wabunge wa viti maalum kutoka CCM 41, CUF 4, TLP 1, CHADEMA 1 na UDP 1. Kwa upande wa madiwani, CCM ilishinda kwa kupata asilimia 94.8 ya kata zote.
- Mheshimiwa Spika, kwa ujumla Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu mkubwa. Huo ni ushahidi wa kutosha kwamba mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini unazidi kuimarika siku hadi siku. Hivyo, waliopata nafasi mbalimbali iwe ya urais, ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi au udiwani wajue wamepewa ridhaa hiyo na wapiga kura kwa uamuzi wao wenyewe wa demokrasia. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Watanzania wote kwa kushiriki katika hatua zote muhimu za uchaguzi huo. Nawapongeza kwa dhati, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Mheshimiwa Dr. Omar Ali Juma na Mheshimiwa Amani Abeid Karume kwa ushindi mkubwa walioupata. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waheshimiwa Madiwani waliochaguliwa kuwakilisha wananchi. Navipongeza pia vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi huo. Vilevile, naipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi nzuri iliyofanya katika kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na chaguzi ndogo zilizofuata.
- Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, CCM ilishinda kwa kura nyingi na Serikali zote mbili zilizoundwa ziko madarakani. Pamoja na kwamba kuna viongozi au wanachama wa baadhi ya vyama wanaosema hawayatambui matokeo ya uchaguzi na hawawatambui viongozi waliochaguliwa na wananchi, ukweli ni kuwa uchaguzi wa mwaka 2000 umekwisha na sote tujiandae kwa uchaguzi wa mwaka 2005. Ninaviomba vyama vyote vya siasa sasa kwa pamoja tujielekeze katika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwahamasisha, kuwaelekeza na kushirikiana nao. Wananchi hawahitaji vurugu, mapambano, maandamano wala matembezi yasiyoisha. Watanzania wanachotaka kuona ni umasikini unaondoka, maendeleo yanakuwepo, kero zao zinashughulikiwa na amani yao inadumishwa. Tufanye kazi zetu za kisiasa ili kutimiza malengo hayo ya wananchi kwani ndivyo vigezo Watanzania watakavyovitumia kutuchagua mwaka 2005. Tujenge maelewano, tujenge upendo na tuwe na uvumilivu. Navipongeza vyama vya CCM na CUF kwa juhudi zao zinazoendelea za mazungumzo ili kufikia muafaka kati yao.
HALI YA UCHUMI
- Mheshimiwa Spika, wakati wa Bunge la Bajeti la mwaka 2000/2001, Serikali ilitoa mwelekeo wa sera, malengo na mikakati ya kusukuma ukuaji wa uchumi wetu na kuboresha maisha ya Watanzania walio wengi kwa kipindi cha 2001/2002 - 2003/2004. Mikakati hiyo ilizingatia shabaha na malengo ya Mpango wa Taifa wa Kupambana na Umasikini na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo imeweka vipaumbele vifuatavyo:
i. Kuboresha maisha ya wananchi,
ii. Kuendeleza rasilimali watu,
iii. Kuwepo na uhakika wa chakula,
iv. Kuongeza mapato ya fedha za kigeni na
v. Kukuza ajira.
Sambamba na vipaumbele hivyo, mkazo umewekwa katika kujenga mazingira mazuri kwa wawekezaji na washikadau mbalimbali katika maeneo ya uzalishaji, miundombinu, huduma za jamii na hifadhi ya mazingira. Aidha, mikakati yetu ya marekebisho ya uchumi na kupambana na umasikini inaungwa mkono na wahisani ambao wameahidi kutusaidia ikiwa ni pamoja na kutufutia madeni chini ya Mpango wa Misamaha kwa Nchi Masikini zenye Madeni Makubwa (HIPC).
- Mheshimiwa Spika, Mpango wa Misamaha kwa Nchi Masikini zenye Madeni Makubwa ambao Tanzania inautekeleza utatoa nafuu kubwa katika bajeti ya Serikali. Hivi sasa nchi yetu imekamilisha makubaliano ya awali (decision point) na tunatarajia kufikia hatua ya mwisho (completion point) baadaye mwaka huu. Hata hivyo, bado tunayo kazi kubwa ili kufikia hatua hiyo. Lazima tuwe na mipango kamili ya kupambana na umasikini na UKIMWI, tuendelee na usimamizi mzuri wa ufufuaji uchumi, tuwe na mipango kamili na mahsusi ya kuendeleza sekta za huduma za jamii na kilimo na tuendelee kusimamia mapato na matumizi mazuri ya fedha za Serikali. Utekelezaji wa mambo haya yote unahitaji nidhamu ya hali ya juu sana. Mpango huu wa kusamehewa madeni uwe ni kichocheo kwa Watanzania kujikwamua katika umasikini na kufanya kazi kwa bidii.
- Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mipango hii umeanza kutoa matunda. Katika mwaka 2000, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 1999. Ongezeko la ukuaji huo limechangiwa zaidi na ukuaji mkubwa katika sekta za madini, bidhaa za viwandani, maji, umeme, biashara na utalii. Kasi ya upandaji bei imeshuka kufikia asilimia 5.1 mwezi Machi 2001, hali ambayo imechangiwa zaidi na hatua za Serikali za kuendelea kudhibiti ongezeko holela la fedha katika uchumi, kupungua kwa uhaba wa chakula nchini na kubana matumizi ya Serikali. Mauzo ya bidhaa nje pia yaliongezeka kutoka Dola za Marekani 543.3 milioni mwaka 1999 hadi Dola za Marekani 662.1 milioni mwaka 2000. Ongezeko hili la asilimia 21.9 lilitokana na ongezeko la mauzo ya bidhaa zisizo asilia, madini hususan dhahabu na almasi, mauzo ya minofu ya samaki na bidhaa za viwandani.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na dalili za mafanikio haya, Serikali inatambua kwamba hakuna mabadiliko makubwa ya hali za maisha kwa wananchi wengi. Huduma za elimu na afya zimeendelea kuwa duni, idadi ya wananchi wanaopata maji safi na salama bado ni asilimia 45 tu ya wananchi wa vijijini na asilimia 68 kwa wanaoishi mijini. Aidha, idadi ya watoto wanaokufa chini ya umri wa miaka 5 bado ni kubwa, yaani watoto 150 mwaka 1999 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa. Hali hii inatokana na ongezeko dogo sana la Pato la Taifa na uwezo mdogo wa Serikali kuboresha utoaji wa huduma za msingi za elimu, afya na maji. Kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa cha asilimia 4.9 mwaka 2000, bado ni cha chini sana kutuwezesha kuondokana na umasikini. Ongezeko hili dogo linatokana na ukuaji mdogo wa sekta ya kilimo ambayo ni chanzo kikuu cha Pato la Taifa na kipato kwa wananchi wengi waishio vijijini. Vivyo hivyo, sekta binafsi ambayo tunaitegemea kuongoza katika uzalishaji na biashara na kutoa ajira, bado haijaimarika. Sambamba na udhaifu huu, UKIMWI umeendelea kupunguza nguvukazi ya Taifa na kuathiri ukuaji wa uchumi.
- Mheshimiwa Spika, linalojitokeza hapa ni kuwa uchumi wetu bado ni tegemezi. Hivi leo asilimia 42 ya bajeti yetu inategemea fedha za wengine. Kiwango chetu cha ukusanyaji kodi ambacho ni asilimia 12 ya Pato la Taifa, ni cha chini sana ukilinganisha na nchi jirani ambacho ni wastani wa asilimia 20 ya Pato la Taifa kwa nchi hizo. Hii maana yake ni kuwa watu wanaolipa kodi ni wachache sana. Tunahitaji kupanua wigo wa kodi ili Serikali ipate mapato ya kutosha kuwahudumia vizuri raia wake. Baada ya makusanyo, fedha za umma lazima zitumike vizuri. Nidhamu yetu katika matumizi ya fedha bado haijawa nzuri sana ndio maana taarifa za ukaguzi wa hesabu za Serikali zina kasoro kila mwaka. Maofisa wahasibu wamekwisha agizwa kurekebisha kasoro hizo haraka na kanuni za fedha zitumike ipasavyo. Suala hili lipewe kipaumbele cha juu na ngazi zote za Serikali, kuanzia Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na taasisi zote za Serikali.
- Mheshimiwa Spika, Serikali itaendeleza utekelezaji wa mikakati yote ya kurekebisha uchumi ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo katika kutatua matatizo yanayokwamisha ukuaji wa sekta ya kilimo hususan uzalishaji wa mazao na mifugo na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwandani. Aidha, Serikali itakamilisha utayarishaji na kuanza utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo Vijijini ambao unaweka mkazo katika maendeleo ya sekta ya kilimo. Mkakati huu unalenga kuboresha mazingira ya uzalishaji na utoaji huduma za jamii vijijini. Aidha, sekta ya viwanda ambayo ndiyo inayotarajiwa kuongoza uchumi siku za usoni itapewa uzito unaostahili. Ubinafsishaji utaendelea kwa viwanda na makampuni yaliyobaki ikiwa ni pamoja na mashirika ya huduma. Hata hivyo, udhibiti mkubwa utawekwa katika kutathmini hali na viwango vya uwekezaji katika viwanda na mashirika yanayobinafsishwa.
- Mheshimiwa Spika, Serikali vilevile itaendeleza juhudi za kukuza ajira kwa kuwawezesha wananchi kupata nyenzo na mitaji ya kuendeshea shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuwawezesha kupata kipato cha kukidhi mahitaji yao ya kila siku. Kwa mfano, Serikali imeanzisha Mfuko wa Kuongeza Uwezo wa Wananchi katika Maendeleo ya Jamii (TASAF) kutokana na fedha za mkopo wa Benki ya Dunia. Mfuko huu unachangia gharama za miradi iliyobuniwa na wananchi wenyewe ya kuboresha elimu, huduma za afya, maji, na ujenzi wa miundombinu ya uchumi kama vile umwagiliaji maji mashamba, ujenzi wa maghala ya mazao na ujenzi wa masoko madogo. Katika maeneo ya mradi, Mfuko huu husaidia kupunguza umasikini kwa kutoa ajira kwa wananchi wanapotumia nguvu kazi zao kutekeleza miradi hiyo. Hivi sasa shughuli za Mfuko huu zinatekelezwa katika wilaya 45 zilizoteuliwa kwenye mikoa yote nchini. Napenda kusisitiza tena kuwa kero ya umasikini haitaondoka ikiwa wananchi hawatakubali kushika hatamu ya maendeleo yao wenyewe. Ni lazima kila mmoja wetu akatae umasikini na sote kama jamii tukatae umasikini.
MAJUKUMU YA OFISI YA WAZIRI MKUU
- Mheshimiwa Spika, majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Serikali, kuratibu na kusimamia masuala ya Bunge na Siasa, kuratibu shughuli za vyombo vya habari nchini, kuratibu shughuli za maafa, kusimamia na kuratibu vita dhidi ya UKIMWI, kusimamia na kuratibu Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma na vilevile kusimamia uchapaji wa nyaraka za Serikali.
Uratibu wa Shughuli za Siasa na Bunge
- Mheshimiwa Spika, demokrasia ya vyama vingi imeendelea kukua na kuimarika. Idadi ya vyama vya siasa vilivyopata usajili wa kudumu bado ni 13 na havijaongezeka tangu mwaka 1995. Hii ni dalili kuwa Watanzania sasa tunaanza kuona mantiki ya kuwa na vyama vya siasa vichache ambavyo vitaweza kutoa ushindani wenye lengo la kuimarisha demokrasia na utawala bora nchini. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2000 hadi Aprili 2001, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imepokea maombi ya kusajiliwa kutoka kwa vyama vipya viwili vya National Liberal Party (NLP) na The Forum for Restoration of Democracy (FORD). Serikali kupitia Ofisi ya Msajili imeendelea kutoa ruzuku kwa vyama vinavyostahili kwa madhumuni ya kuviimarisha. Hata hivyo, kwa baadhi ya vyama, ruzuku imekuwa kichocheo cha migogoro na mitafaruku baina ya viongozi. Hii ni kasoro kubwa inayodhoofisha juhudi za kuimarisha demokrasia ya vyama vingi nchini. Katika kipindi cha mwaka 2001/2002 Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kukamilisha usajili wa kudumu kwa vyama vilivyokamilisha masharti ya usajili wa muda, kupokea maombi mapya ya usajili, kupokea na kuchambua taarifa za fedha na mali za vyama vya siasa, kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya vyama na kuvisaidia kujenga uwezo wao wa kutumia Katiba zao kutatua migogoro yao.
- Mheshimiwa Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Ofisi ya Spika ilikuwa na jukumu kubwa la kuhudumia Bunge Jipya kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Kazi ya kupanua ukumbi kukidhi ongezeko la Wabunge imefanyika na huduma muhimu za Wabunge kama za mafunzo, usafiri, vitendea kazi na mawasiliano ziliimarishwa. Huduma hizo zimesaidia kupitishwa kwa miswada ya sheria 12, maazimio 6 na kanuni mpya za Bunge zilitungwa. Baadhi ya kamati za kudumu za Bunge zilifanya ziara na vikao mbalimbali na kutoa ushauri kwa Serikali. Katika kipindi cha mwaka 2001/2002, Ofisi ya Spika itaendelea kuboresha huduma za kiutawala, kuongeza elimu ya kibunge, kuendeleza mahusiano na Mabunge mengine na kudumisha mahusiano na Vyama vya Kimataifa vya Kibunge.
- Mheshimiwa Spika, katika muda mfupi wa uhai wa Bunge lako Tukufu, Wabunge 15 wa Chama cha CUF wamepoteza viti vyao baada ya kushindwa kuhudhuria mikutano mitatu mfululizo bila ruhusa ya Mheshimiwa Spika na hivyo kukiuka matakwa ya Katiba. Mbunge ni mwakilishi wa wananchi wote wa jimbo lake, anawakilisha wale waliompa kura na wale ambao hawakumpa kura. Anawakilisha wanachama wa chama chake na wale wasio wa chama chake. Kwa msingi huo, kitendo cha kususia Bunge ambalo ndicho chombo cha uwakilishi ni kuwanyima haki wananchi na hakisaidii kujenga na kudumisha demokrasia nchini.
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2000/2001, Tume ya Uchaguzi ilifanikisha maandalizi na hatimaye kukamilisha zoezi la uchaguzi mkuu katika hali ya amani na utulivu. Tume pia imesimamia kwa ufanisi chaguzi ndogo katika majimbo ya Busega, Solwa na Ludewa. Katika mwaka 2001/2002, Tume ya Uchaguzi itaanza taratibu za kuanzisha Daftari la Taifa la Kudumu la Wapiga Kura. Aidha, Tume itaendelea kuimarisha shughuli za ukusanyaji na utunzaji wa takwimu za uchaguzi, kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa kutoa mafunzo kwa watumishi na kuwapatia mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Uratibu wa Sekta ya Habari
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2000/2001 sekta ya habari imeendelea kuelimisha wananchi juu ya mambo yanayohusu siasa, uchumi, maendeleo ya jamii, burudani na kuwapa habari za matukio mbalimbali. Sekta hii inategemewa sana katika kufanikisha malengo tuliyojiwekea ya kuondoa umaskini, kupiga vita rushwa, kupambana na UKIMWI na kuimarisha demokrasia na utawala bora. Vyombo vya habari vimeongezeka hadi kufikia vituo 17 vya radio, 8 vya televisheni ya wazi na 18 vya televisheni ya kulipia.
- Mheshimiwa Spika, Idara ya Habari (Maelezo) iliendelea kuratibu utoaji wa habari kuhusu shughuli za Serikali kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Aidha, Idara hii ilianzisha utaratibu wa kuhariri na kuweka habari na matukio ya Serikali katika mtandao wa Taifa (National Website). Mtandao huu una maelezo ya sekta zote za Serikali, na ni jukumu la kila sekta kuhakikisha kuwa yale yaliyoandikwa katika mtandao huo yanaboreshwa na yanakwenda na wakati. Mtandao huu unasimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji.
- Mheshimiwa Spika, ili kupanua huduma za matangazo ya radio na televisheni katika maeneo yao, baadhi ya Halmashauri za Manispaa, Miji, na Wilaya zimeanzisha vituo vya radio na vya kurushia matangazo ya televisheni kwa lengo la kuhamasisha maendeleo. Nazipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Mbeya, Halmashauri za Miji ya Iringa, Songea na Musoma, na Halmashauri za Wilaya za Rungwe, Mbozi, Iramba, Njombe na Masasi, kwa kuanzisha vituo hivyo. Hii ni changamoto kwa Halmashauri nyingine na watu binafsi kuanzisha huduma ya utangazaji katika maeneo ambayo hayana huduma hii. Utaratibu huu utarahisisha kufikisha matangazo ya radio na televisheni kwa wananchi wote.
- Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha vyombo vya habari vya umma ili viweze kuwafikia wananchi wengi zaidi. Kwa upande wa Radio Tanzania, mitambo mipya ya kurushia matangazo imefungwa Mwanza, Arusha na Mbeya. Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Japan, Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa kupunguza tatizo la usikivu kwa kujenga mtambo mkubwa wa kurushia matangazo na jengo jipya la utangazaji ambalo litakuwa na studio za kisasa. Kwa upande wa Televisheni ya Taifa, Serikali inatafuta fedha ili kufikisha huduma hiyo nchini kote mapema iwezekanavyo. Kuhusu Kampuni ya Magazeti ya Serikali, Serikali imeipatia jengo la ofisi la kudumu na inaendelea kuimarisha mtaji wa Kampuni hiyo ili kuongeza uwezo wake wa kukabiliana na ushindani mkubwa uliopo katika sekta ya habari. Hali kadhalika, suala la kuboresha taaluma ya wanahabari litatiliwa mkazo kwa kukamilisha taratibu za kukiwezesha Chuo cha Uandishi wa Habari kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na ongezeko la vyombo vya habari binafsi na uboreshaji wa huduma ya utangazaji unaofanywa na vyombo vya umma, bado huduma hii haiwafikii wananchi walio wengi vijijini, na hata katika baadhi ya miji. Maombi mengi ya kuanzisha vyombo vya habari yanalenga kutoa huduma katika miji mikubwa tu michache, ambako tayari kuna msongamano mkubwa wa vyombo hivyo. Natoa wito kwa wawekezaji katika sekta hii kujitokeza kutoa huduma hii hususan katika yale maeneo ambayo hivi sasa hayana huduma hiyo.
- Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha na kuboresha sekta hii, katika mwaka 2001/2002, Serikali kwa kushirikiana na washikadau wote wa sekta ya habari, itakamilisha sera mpya ya habari itakayowezesha vyombo vya habari kuendelea kutekeleza kazi zao kwa uhuru na kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao. Aidha, sera hii itaainisha wajibu wa Baraza la Habari katika kusimamia taaluma na utendaji katika vyombo vya habari. Vilevile, sheria mbalimbali zinazotawala vyombo vya habari zitaangaliwa upya ili ziende na wakati.
Uratibu wa Maafa
- Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu shughuli mbalimbali zenye lengo la kuzuia maafa; kuwasaidia wananchi walioathirika kutokana na maafa mbalimbali na kusimamia miradi yenye lengo la kuwawezesha wananchi kukabiliana na tatizo la mara kwa mara la upungufu wa chakula. Katika mwaka 2000/2001, Serikali iliratibu usambazaji wa tani 20,000 za mahindi ambayo yaliuzwa kwa bei nafuu kwa wananchi wale tu waliokuwa na upungufu wa chakula. Vilevile, iliratibu na kusimamia usambazaji wa chakula cha msaada kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani na misaada iliyotolewa na taasisi mbalimbali, nchi marafiki na watu binafsi.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/2002 Serikali itakamilisha uandaaji wa Sera ya Maafa pamoja na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Maafa Na. 1 ya mwaka 1990. Ili kujenga uwezo zaidi, Serikali itatoa mafunzo kwa washikadau mbalimbali na vilevile itaendelea kutekeleza mradi wa kuimarisha uwezo wa Taifa kukabiliana na maafa nchini, unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani - USAID. Aidha, hatua zitachukuliwa za kuanzisha Mfuko wa Maafa utakaochangiwa na watu binafsi, taasisi na mashirika mbalimbali.
Uhamiaji Makao Makuu - Dodoma
- Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Serikali kuhamishia makao yake makuu Dodoma bado haujabadilika. Katika mwaka 2000/2001, Serikali imechukua hatua za kuimarisha uongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu, Dodoma, pamoja na kufanya matayarisho muhimu ya kuwezesha Wizara mbili kuhamia Dodoma katika mwaka 2001/2002. Wizara hizo ni Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo na Ushirika na Masoko. Serikali itaendelea na utaratibu huo wa kuhamisha shughuli za Wizara nyingine hatua kwa hatua ili hatimaye Wizara zote zihamie Dodoma. Serikali vilevile, itaangalia upya sheria na majukumu ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu, Dodoma kwa lengo la kuboresha utendaji na kuleta ufanisi zaidi.
URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI
- Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu na kufuatilia utendaji wa kazi za kila siku za Serikali katika kutekeleza malengo mbalimbali ya Taifa. Taarifa na nyaraka mbalimbali za Serikali zimechambuliwa na kutolewa maamuzi. Aidha, kamati mbalimbali zimeundwa katika ngazi ya mawaziri na wataalam kusukuma na kufuatilia utekelezaji wa mambo muhimu hasa yale ambayo utekelezaji wake sio jukumu la Wizara moja. Kamati zilizoundwa ni kama zifuatazo:-
i. Kamati ya Mawaziri ya kusukuma mabadiliko ya maisha ya wananchi ngazi ya familia,
ii. Kamati ya Mawaziri ya kushughulikia huduma za jamii na kero za wananchi,
iii. Kamati ndogo ya Mawaziri ya kushughulikia ubinafsishaji wa mashirika yenye ardhi kubwa na mashamba ya Taifa.
iv. Kamati ya Mawaziri ya kuangalia namna ya kuwapa uwezo Watanzania ili washiriki katika uchumi na ubinafsishaji.
v.Kamati ya Wataalam ya kutayarisha Mkakati wa Maendeleo Vijijini ambao utaweka mkazo katika maendeleo ya sekta ya kilimo.
vi.Kamati ya Wataalam ya kuandaa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu.
Utaratibu huu umeimarisha ushirikiano na uwajibikaji, umefupisha urasimu wa kufanya maamuzi, umepunguza misuguano kati ya watendaji na hivyo kurahisisha utekelezaji wa kazi za Serikali katika sekta mbalimbali. Taarifa za Kamati hizo zinaendelea kufanyiwa kazi na Serikali.
Sekta ya Uzalishaji Mali
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2000, sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 3.4 tu ikilinganishwa na asilimia 4.1 mwaka 1999. Uzalishaji wa takriban mazao yote ulishuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo mabadiliko ya hali ya hewa. Hali hii inalifanya Taifa kutokuwa na uhakika wa chakula na kupunguza uwezo wa kupata fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi. Sekta ya kilimo pia inakabiliwa na matatizo ya matumizi ya teknolojia duni, ukosefu wa mitaji hususan kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa mikopo kwa wakulima, uwekezaji mdogo wa rasilimali ambao haukidhi mahitaji ya utafiti na mafunzo na huduma za ugani. Matatizo mengine ni kutozingatiwa kwa kanuni za kilimo bora, mfumo dhaifu wa usambazaji wa pembejeo, hali duni ya miundo mbinu na upotevu mkubwa wa mazao.
- Mheshimiwa Spika, tija katika kilimo itaongezeka pale wakulima wetu wengi watakapoongeza matumizi ya pembejeo na kutumia kilimo cha kitaalam. Serikali itaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo kuzifikisha kwa wakulima vijijini ili waweze kuzinunua pale wanapozihitaji. Aidha, Mfuko wa Pembejeo utaimarishwa ili uweze kutimiza malengo yake. Halmashauri za Wilaya zitahusishwa katika kuteua wasambazaji wa pembejeo hizo na kuhakikisha kuwa mikopo inatumika ipasavyo na inarejeshwa. Ni lazima wote waliopewa dhamana ya kusimamia Mfuko huu watimize wajibu wao kikamilifu.
- Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine muhimu ni kuanzisha mradi wa kurutubisha udongo na kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo. Mradi huu unalenga katika kuboresha mazingira ya uzalishaji wa mazao ikiwa ni pamoja na kumwezesha mkulima kupata na kutumia pembejeo sahihi, kwa wakati na kwa bei nafuu. Hivi sasa, maandalizi ya mradi huu yamefikia hatua za kuridhisha. Mazungumzo kati ya Serikali na wahisani waliokubali kusaidiana nasi katika kuuanzisha na kuusimamia mradi huu yanaendelea na tunatarajia kuwa utekelezaji rasmi utaanza katika msimu wa kilimo wa 2001/2002.
- Mheshimiwa Spika, hatua nyingine muhimu ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji. Nchi yetu ina hekta zaidi ya milioni moja ambazo zinafaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, lakini ni hekta 157,000 tu ndizo zilizokwisha endelezwa. Ili kuendeleza kilimo cha umwagiliaji mkazo utawekwa kwenye kuendeleza umwagiliaji wa jadi, kutoa ushauri wa kitalaam juu ya uendeshaji wa skimu zilizopo na zitakazoendelezwa kwa kushirikiana na wakulima wenyewe. Aidha, sekta binafsi itahamasishwa ili kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuwa na mashamba makubwa ya uzalishaji wa uhakika.
- Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mwaka 2000/2001, wakulima wamekumbana na matatizo ya soko la mazao yao ambayo yamesababisha kushuka kwa bei ya mazao. Hali hii imesababishwa na ubovu wa miundo mbinu, kushuka kwa bei ya mazao katika soko la dunia, uhaba wa mikopo ya ununuzi wa mazao, ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao ya chakula, upungufu wa taarifa za masoko na vikwazo vya kibiashara. Ili kukabiliana na matatizo haya, Wizara ya Ushirika na Masoko itaimarisha Kitengo cha Uendelezaji wa Masoko ili wataalam wa ugani na wakulima waweze kuwa na taarifa sahihi za masoko. Aidha, kanuni na taratibu za ununuzi wa mazao zitasimamiwa kikamilifu na suala la usindikaji wa mazao litapewa kipaumbele kwa kuishirikisha sekta binafsi kikamilifu.
- Mheshimiwa Spika, ingawa nchi yetu inayo rasilimali kubwa ya mifugo, sekta hii imechangia asilimia 4.6 tu ya Pato la Taifa kwa mwaka 2000. Katika sehemu mbalimbali nchini mifugo inatumika kama nguvu kazi, inatoa mbolea kwa ajili ya kilimo na kutupatia lishe. Hata hivyo, sekta hii imekumbana na matatizo ya ukosefu wa aina bora ya mifugo na mifumo ya uzalishaji, malisho na maji, ukosefu wa tiba na milipuko ya mara kwa mara ya magonjwa, ukosefu wa viwanda vya usindikaji na masoko ya mifugo na ukosefu wa elimu kwa wafugaji. Katika kipindi cha mwaka 2000/2001, Serikali imeimarisha huduma za ugani, kutoa chanjo kwa mifugo na pia imeandaa mkakati wa kupambana na matatizo sugu yanayoikumba sekta hii. Katika mwaka wa fedha wa 2001/2002, Serikali itaweka mkazo katika utafiti na uzalishaji wa mifugo bora, kuboresha huduma za tiba, kuboresha taratibu za masoko na kuimarisha elimu kwa wafugaji.
- Mheshimiwa Spika, Vyama vya Ushirika ni vyombo vya kuwaunganisha wanaushirika na kuwapatia mitaji, soko, pembejeo na elimu ya ushirika na uzalishaji bora kwa wanachama wake. Baadhi ya vyama vyetu vya ushirika vimedhoofika au kufa kwa sababu ya wizi, ubadhirifu, rushwa, uongozi mbovu na elimu duni ya ushirika. Aidha, uchache wa wanachama uliopo hivi sasa katika Vyama vya Ushirika unachangiwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma duni ya vyama vyenyewe na umma kutohamasishwa vya kutosha ili wautambue na kuukubali ushirika kama silaha ya wanyonge. Chini ya mfumo wa biashara huria, umuhimu wa ushirika nchini sasa ni mkubwa zaidi kuliko awali. Kwa hiyo, inatubidi tujenge ushirika mpya na ulio imara ambao mkazo wake utakuwa katika ngazi ya vyama vya msingi. Ushirika huu utawawezesha na kuwaelimisha wakulima, wafugaji, wavuvi na vikundi mbalimbali vya uzalishaji kuondokana na umaskini. Aidha, utawawezesha wanachama kuchagua viongozi wao wenyewe na pia kuhimiza ushirikishwaji wao katika maamuzi mbalimbali ya uendeshaji wa vyama vyao.
- Mheshimiwa Spika, ukosefu wa mitaji ni miongoni mwa vikwazo vinavyodhoofisha uwezo wa Vyama vya Ushirika kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Ukuaji wa mitaji ya ndani na nje unahitaji muda mrefu na unategemea viwango vya mafungu na limbikizo la ziada ambalo ni matokeo ya ufanisi katika biashara. Kwa kutambua umuhimu wa mitaji hiyo, Serikali itafanya utafiti wa kina ili kushauri viwango vya viingilio, mafungu na hisa vitakavyofaa kwa chama husika. Katika juhudi hizi, maeneo yatakayopewa kipaumbele ni uimarishaji na uanzishaji wa Vyama vya Akiba na Mikopo, Benki za Ushirika, na Mifuko ya Mazao na Pembejeo. Sambamba na malengo hayo, Serikali inaangalia upya Sera ya Maendeleo ya Ushirika, Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 1991 na mfumo wa sasa wa ushirika ili kuona mapungufu yanayokwamisha utendaji wake kufikia upeo wa ufanisi unaohitajika ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kutumika kwa Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Vyama vya Ushirika.
- Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Sera Endelevu ya Viwanda inayolenga kuongeza kasi ya ukuaji wa viwanda nchini ili kukuza Pato la Taifa, kuongeza nafasi za ajira, na kukuza mauzo ya bidhaa za viwanda nchi za nje imeanza kuleta mafanikio. Aidha, kukamilika kwa ukarabati wa baadhi ya viwanda vilivyobinafsishwa, na ukamilishwaji wa viwanda vipya kumeongeza ajira kwa wananchi wetu. Katika mwaka 2000/2001, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) ilitekeleza mpango utakaowezesha Serikali na sekta binafsi kuendeleza viwanda na biashara ndogo na za kati ili kuboresha mazingira na taratibu za uwekezaji. Hali hiyo imewezesha sekta ya viwanda kukua kwa asilimia 4.8 mwaka 2000 ikilinganishwa na asilimia 3.6 mwaka 1999. Ongezeko hili liliiwezesha sekta hii kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 8.4. Hata hivyo, uzalishaji katika viwanda uliathiriwa na mgao wa umeme, ukosefu wa mitaji ya kutosha, na ushindani usio wa haki unaotokana na uingizaji nchini wa bidhaa hafifu zinazouzwa kwa bei ya chini. Moja kati ya vyombo muhimu vya kuendeleza viwanda na biashara nchini ni Baraza la Taifa la Biashara. Baraza hili litawezesha kuwepo kwa mashauriano kati ya Serikali na sekta binafsi, katika masuala ya kuendeleza shughuli za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na zile za sekta ya viwanda.
- Mheshimiwa Spika, sekta ya biashara ilikua kwa asilimia 6.5 mwaka 2000 ikilinganishwa na asilimia 6 mwaka 1999. Pamoja na mwelekeo huu mzuri, kiwango cha ufanisi katika biashara ya ndani hakiridhishi kutokana na hali duni ya ushindani wa sekta binafsi katika mfumo wa soko huria. Aidha, mauzo ya bidhaa zetu nje yameendelea kupungua, na hivyo kukuza nakisi iliyopo kati ya thamani ya bidhaa zilizouzwa nje na zilizoagizwa kutoka nje. Ili kuleta ufanisi katika biashara ya ndani, Serikali imeanza kutekeleza hatua kadhaa ikiwemo ya kulinda baadhi ya viwanda vinavyozalisha bidhaa muhimu. Hata hivyo, hatua hii isitafsiriwe kuwa tunarudisha mfumo wa ukiritimba kinyume na mwenendo wa soko huria. Bidhaa za nje zitaendelea kuagizwa ili mradi ziwe za ubora unaokubalika na zinalipiwa kodi zote zinazohusika. Tusipovilinda viwanda vyetu vitaathirika, hali ambayo itasababisha Taifa kupoteza ajira, mapato na nchi kuwa soko la watu wengine. Vivyo hivyo, wenye viwanda nchini wanao wajibu wa kupunguza gharama za uzalishaji ili bidhaa za ndani ziweze kuhimili ushindani. Katika mwaka 2001/2002, Serikali itakamilisha Sera ya Biashara inayolenga kujenga mfumo wa ushindani katika uchumi, kukuza mauzo nje kwa njia ya kupanua wigo wa bidhaa na kuingia katika masoko mapya.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2000 sekta ya utalii nchini iliendelea kutoa mchango mkubwa katika mapato na ajira hivyo kusaidia kukuza uchumi na kuleta maendeleo. Mchango huu ungeweza kuwa mkubwa zaidi kama tungepanua na kuendeleza wigo wa bidhaa katika utalii, ikiwa ni pamoja na utalii wa utamaduni, hasa ule wa vijijini na wa maeneo ya mambo ya kale. Nchi yetu imejaa vivutio hivi na tayari utalii wa aina hii umeanza Amani, Lushoto na Gezaulole, Dar es Salaam. Sambamba na vivutio hivyo, sekta ya utalii ni eneo mojawapo kubwa lenye fursa nyingi za uwekezaji hususan katika mahoteli, migahawa, usafirishaji wa anga, nchi kavu na majini, wakala wa masoko, mafunzo na huduma nyingine nyingi zinazoendana na shughuli za utalii. Serikali imeshatoa sera inayoongoza sekta hii na inaendelea kuweka miundo mbinu katika sehemu mbalimbali ili kuvutia wawekezaji. Ili kukuza sekta hii, itabidi tuendelee kujitangaza zaidi na kutumia mbinu za kisasa za kuendesha utalii. Serikali itaendelea kuhimiza sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta hii.
- Mheshimiwa Spika, sekta ya madini imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wetu. Mchango wa sekta hii kwenye Pato la Taifa kwa mwaka 2000 ulifikia asilimia 2.3 ukilinganisha na asilimia 2.1 mwaka 1999. Katika kipindi hiki pia kumekuwepo na ongezeko la asilimia 130.2 la mauzo ya madini na vito vya thamani nje ya nchi yaani kutoka Dola za Marekani 80.4 milioni mwaka 1999 na kufikia Dola za Marekani 185.1 milioni mwaka 2000. Madini ya dhahabu yamechangia asilimia 65, almasi asilimia 25, na madini ya vito yamechangia asilimia 10 ya mauzo yote ya madini nchi za nje. Katika mwaka 2001/2002, tunatarajia mauzo ya madini nje yataongezeka kutokana na uzalishaji wa dhahabu wa mgodi wa Kahama Mining Corporation Ltd ambao ulianza uzalishaji Aprili 2001. Kutokana na kupanuka kwa sekta ya uchimbaji wa madini, Serikali itaongeza uwezo wake katika kusimamia na kudhibiti shughuli za madini. Aidha, Kamati ya Ushauri ya Madini imeundwa ili kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali ya sekta ya madini yakiwemo: utoaji na ufutaji wa leseni za madini, utengaji wa maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo, uingiaji mikataba na wawekezaji katika sekta ya madini na hifadhi ya mazingira. Serikali pia itaendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata mitaji, zana za kisasa za kuchimbia, soko na mafunzo.
- Mheshimiwa Spika, sera yetu ya madini inatambua kuwepo kwa wachimbaji wadogo na wakubwa wa madini. Kila mmoja anayo nafasi katika kuendeleza sekta hii muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Pamoja na umuhimu huu, lazima tuendelee kuhakikisha kuwa tunazingatia sheria na taratibu tulizojiwekea katika kutenga maeneo ya utafutaji na uchimbaji wa madini kwa makundi hayo mawili makubwa. Ni vyema tujiepushe na matumizi ya fujo na vurugu katika kutatua migogoro kwenye maeneo ya madini. Serikali itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye utaalamu na teknolojia za kisasa ambazo zitatuwezesha kufaidika na rasilimali hii kubwa tuliyonayo nchini.
Sekta ya Huduma za Kiuchumi
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2000/2001 uzalishaji wa umeme nchini uliongezeka na hasa baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa Kihansi, na kufikia uniti 2,412.4 milioni, ukilinganisha na uniti 2,324.6 milioni zilizozalishwa mwaka 1999. Mitambo ya gesi na ya dizeli kwenye gridi ya Taifa iliendelea kuzalisha umeme kwa muda wote wa ukame hadi kipindi cha mvua kilipoanza. Aidha, ulifanyika ukarabati wa mitambo ya umeme katika vituo vya Songea, Lindi na Sumbawanga. Mradi wa kutoa umeme Mbala, Zambia hadi mjini Sumbawanga uliendelea kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka wa fedha 2001/2002.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2000/2001, miji mikuu 4 ya wilaya za Meatu, Igunga, Tandahimba, na Ruangwa na mji mdogo wa Kibakwe ilipatiwa umeme. Katika mwaka 2001/2002, miji ya Biharamulo na Geita na miji midogo ya Kanyigo na Nassa itapatiwa umeme. Lengo la Serikali baada ya kuweka umeme kwenye miji mikuu ya wilaya, ni kuendeleza upelekaji umeme kwenye viwanda vya mazao ya kilimo na katika miji mingine ambayo ni vitovu vya maendeleo. Utekelezaji wa malengo haya utategemea upatikanaji wa fedha.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/2001, Serikali imeendelea kuimarisha taratibu za kusimamia ujenzi, utunzaji na matengenezo ya barabara kupitia Mfuko wa Barabara na kuanzisha Wakala wa Barabara. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2000 hadi Machi 2001, Mfuko wa Barabara umekusanya na kugawa jumla ya Shilingi 20.1 bilioni. Ni dhahiri kuwa hiki ni kiwango kikubwa cha fedha za ndani ambazo zimetolewa kwa ajili ya matengenezo ya barabara. Katika kipindi kifupi tangu uanze kazi, Wakala wa Barabara umeonyesha maendeleo mazuri. Kwa mfano, umeingia mikataba takriban 700 na makandarasi kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja. Huu ni mwanzo mzuri, hivyo tuvipe vyombo hivi ushirikiano wa karibu ili viimarike na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Katika mwaka 2001/2002 lengo la Mfuko wa Barabara ni kukusanya jumla ya Shilingi 35.5 bilioni ambazo zitagawanywa kwa Mamlaka zote zinazohusika na matengenezo ya barabara nchini.
- Mheshimiwa Spika, miradi ya ujenzi huhitaji utaalam mkubwa na fedha nyingi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka wa fedha 2001/2002, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuimarisha uwezo wake wa kujenga na kutunza barabara kwa kutenga fedha kutoka katika bajeti yake kwa kuanzisha Mfuko Maalum wa Kujitegemea kwa ajili hiyo. Katika mwaka wa fedha wa 2001/2002, Mfuko huu umetengewa Shilingi 12 bilioni. Pamoja na fedha kutoka vianzo vingine, Mfuko huu pia utatumika kujenga barabara za Somanga-Masaninga hadi Matandu, Nangurukuru hadi Lindi, Lindi hadi Mingoyo, Dodoma hadi Manyoni na Manyoni hadi Singida. Serikali pia itaendeleza azma yake ya kukaribisha sekta binafsi katika ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kwa mpango wa jenga, endesha, kabidhi (Build, Operate and Transfer).
- Mheshimiwa Spika, usafiri katika miji yetu mbalimbali hapa nchini umeendelea kutolewa kwa kiwango cha kuridhisha. Ushindani unaotolewa na sekta binafsi umechangia sana katika kuboresha huduma hii kwa wananchi. Azma ya Serikali ni kuendelea kubaini njia bora za kuhudumia wasafiri wote nchini. Hata hivyo, bado ipo haja ya kuboresha taratibu na mipango ya kudhibiti tabia ya baadhi ya madereva na makondakta ambao hawataki kuzingatia sheria za usalama barabarani. Ajali nyingi zimetokea na maisha ya watu yamepotea kwa sababu sheria na taratibu hazifuatwi. Kutokana na hali hii, napenda kutoa wito kwa wale wote wanaohusika na usimamiaji wa sheria na taratibu za uchukuzi hapa nchini, wakiwemo askari wa usalama barabarani, kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa ipasavyo ili kuepuka ajali ambazo zinaweza kuepukika.
- Mheshimiwa Spika, huduma za simu ni nyenzo muhimu katika kuinua uchumi wa Taifa letu. Ili kuboresha huduma hii, Serikali iliuza asilimia 35 ya hisa zake za Kampuni ya Simu Tanzania. Kwa mujibu wa mkataba, njia mpya za simu 800,000 zitaunganishwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2003. Vivyo hivyo, ukamilishaji wa mradi wa Telecommunications Restructuring na ule wa Wireless Local Loop umeongeza huduma zinazotolewa na Kampuni ya Simu Tanzania ukilinganisha na miaka ya nyuma. Huduma ya simu za mkononi pia imeendelea kutolewa katika viwango vya kuridhisha na makampuni ya MOBITEL, TRITEL, ZANTEL na VODACOM. Pamoja na kazi nzuri zinazofanywa na kampuni za simu nchini napenda nitoe changamoto kwamba ni vyema makampuni hayo yakaendelea kupanua huduma zao nchini ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hasa walioko vijijini kunufaika na huduma za simu.
- Mheshimiwa Spika, ardhi ni rasilimali muhimu na ni mojawapo ya misingi mikuu ya maendeleo ya sekta zote za uchumi wa Taifa. Sheria ya Ardhi, Na. 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 zimeanza kutumika kuanzia tarehe 1 Mei 2001. Ili sheria hizi ziweze kueleweka vizuri kwa wananchi walio wengi, Serikali kwa kushirikiana na washikadau wote inawaelemisha wananchi kuhusu maudhui ya sheria hizo kupitia vikundi mbalimbali visivyokuwa vya kiserikali, na pia vyombo vya habari. Aidha, ili kuhakikisha matumizi bora ya ardhi hasa huko vijijini, Serikali imesambaza katika makao makuu ya wilaya vitabu vifuatavyo:-
i. Miongozo ya Ushirikishwaji katika Mipango na Usimamizi wa Matumizi Bora ya Ardhi Vijijini na
ii. Kiongozi cha Mwanakijiji katika Utumikaji wa Sheria ya Ardhi Vijijini.
Pamoja na juhudi hizo, bado kuna vikundi au watu wachache ambao wamekuwa wakiupotosha umma kwa kutoa tafsiri potofu ya maudhui ya sheria mpya ya ardhi. Nawasihi wote wasome kwa uangalifu na kuelewa maudhui ya sheria hizo ili waweze kutoa elimu sahihi kwa wananchi kwa maslahi ya Taifa zima.
- Mheshimiwa Spika, ipo migongano katika matumizi ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji inayotokana na kutokuwepo kwa maeneo yaliyotengwa maalum kwa kila shughuli. Baadhi ya wilaya nchini zimeanza kuchukua hatua kwa kutenga maeneo kwa ajili ya mifugo na kilimo. Aidha, Serikali imetoa maelekezo kwa Halmashauri za Wilaya kuandaa na kuweka mipango ya matumizi ya ardhi, kutoa wataalam wa fani zote zinazohusika na mipango ya matumizi ya ardhi ili waweze kusaidia Serikali za Vijiji kuandaa mipango hiyo. Vilevile, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya zimeagizwa kuwa na agenda za kudumu kujadili masuala ya migogoro ya mipaka baina ya Vijiji au Wilaya.
- Mheshimiwa Spika, maendeleo ya sekta ya ardhi yanaenda sambamba na suala la hifadhi ya mazingira. Sera yetu ya Taifa ya Mazingira inatoa mwongozo ambao ndiyo dira yetu katika hifadhi na utunzaji wa mazingira. Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhimiza upandaji miti, utengaji wa maeneo mapya yanayofaa kwa hifadhi ya misitu na mbuga za Taifa, kupambana na uchomaji wa misitu, udhibiti wa uharibifu wa vyanzo vya maji, uanzishwaji wa elimu ya mazingira na mashindano ya hifadhi ya mazingira vijijini. Ingawa hatua hizi zimechukuliwa, bado Taifa letu linakabiliwa na tatizo la uharibifu na uchafuzi wa mazingira. Ili tuweze kukabiliana na tatizo hili Serikali itashirikiana na washikadau wengine ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi zaidi na kutunza mazingira. Kila mkoa uwe na programu yake ya upandaji miti itakayozingatia hali ya hewa ya kila mkoa. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinao wajibu wa kutunga sheria ndogo kuhusu hifadhi ya mazingira na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira.
Huduma za Jamii
- Mheshimiwa Spika, moja ya malengo makuu ya mpango wetu wa kurekebisha uchumi ni kujenga uwezo wa Serikali wa kutoa huduma bora za jamii kwa wananchi. Mpango wa Misamaha kwa Nchi Masikini zenye Madeni Makubwa ambao nchi yetu inautekeleza una lengo la kutuwezesha kufutiwa madeni ili fedha tutakazookoa kutokana na msamaha huo tuzitumie katika kuchangia nguvu za wananchi kuboresha huduma za jamii za elimu, afya, maji na makazi. Pamoja na hayo, Serikali nayo imeanza kuchukua hatua kwa kuongeza fedha katika bajeti za elimu, afya na maji. Aidha, Mfuko wa Elimu unaotarajiwa kuchangiwa na washikadau wote umeanzishwa na Serikali. Katika mwaka wa fedha wa 2001/2002, Serikali imetenga Shilingi 5 bilioni kwa ajili ya Mfuko huo.
- Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha elimu hususan ya msingi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuondoa umaskini. Eneo muhimu ambalo Serikali imeanza kulishughulikia ni kuongeza uandikishaji watoto wenye umri wa kwenda shule kutoka asilimia 77 ya sasa hadi asilimia 85 ifikapo mwaka 2003. Ili kufanikisha lengo hili, Serikali imeamua kuwa elimu ya msingi itatolewa bure kwa watoto wote kuanzia mwaka wa fedha wa 2001/2002. Serikali pia imeanza kuchukua hatua za kuinua ubora wa elimu hususan ya msingi na sekondari kwa kuboresha mazingira ya utoaji elimu, kuweka uwiano mzuri wa wanafunzi, mikondo na walimu na kupiga vita vitendo vyote vinavyosababisha watoto wetu hususan wale wa kike wasimalize elimu ya msingi na/au sekondari. Aidha, Serikali itaanza kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Elimu ambayo itashughulikia upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunza; ukarabati wa shule na ukamilishaji wa majengo ya shule chini ya utaratibu wa kuwashirikisha wananchi.
- Mheshimiwa Spika, kuhusu elimu ya juu, Serikali imeendelea kusimamia uanzishwaji wa vyuo vikuu vya umma na binafsi ili jamii yetu iendelee kuelimika na iendane na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mikakati mbalimbali ilitekelezwa ya kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika vyuo vikuu vya umma, na kutatua matatizo sugu yanayokabili vyuo hivyo yakiwemo uhaba wa madarasa, ukosefu wa hosteli, uhaba wa walimu, na uhaba wa huduma nyingine muhimu. Aidha, wazazi na jamii imeendelea kuhamasishwa kuchangia gharama za elimu ya juu. Serikali inahimiza sekta binafsi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuwekeza rasilimali nyingi zaidi katika elimu ya juu ili kuongeza ubora wa elimu na udahili wa wanafunzi.
- Mheshimiwa Spika, katika sekta ya afya, Serikali inaendelea kutekeleza mabadiliko ya uendeshaji wa huduma za hospitali za Serikali ambapo hospitali hizo zinapewa madaraka zaidi ya kusimamia rasilimali zote za hospitali. Hivi sasa ipo sheria inayoongoza uanzishwaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila wilaya nchini inaanzisha Mfuko wa Afya ya Jamii. Katika wilaya za Igunga, Nzega, Iramba, Singida Vijijini, Hanang, Kilosa, Iringa Vijijini, Songea Mjini, Songea Vijijini na Mbinga ambako huduma za Mifuko ya Afya ya Jamii imeanzishwa mafanikio makubwa yamepatikana. Hali ya upatikanaji wa madawa imekuwa bora zaidi na majengo ya huduma yamekarabatiwa na familia zinazochangia Mifuko hiyo zimepata huduma katika kipindi chote cha mwaka.
- Mheshimiwa Spika, mazingira machafu na lishe duni ni vyanzo vikubwa vya magonjwa. Pamoja na kuhimizwa kwa umuhimu wa kuzingatia kanuni bora za afya, bado wapo baadhi ya wananchi wanaopuuza maelekezo ya wataalamu wa afya. Serikali itaendelea kuweka msukumo zaidi katika huduma za kinga kwani zitawasaidia wananchi wetu kuepukana na magonjwa yanayoweza kuzuilika. Viongozi na Watalaam katika ngazi mbalimbali tusimamie utunzaji na usafi wa mazingira yetu na kuweka sheria ndogo zitakazowabana wale watakaopuuza maelekezo ya kanuni bora za afya.
- Mheshimiwa Spika, UKIMWI ni tishio kubwa la uhai na maendeleo ya Taifa letu. Ugonjwa wa UKIMWI unaenea kwa kasi sana katika jamii yetu. Kulingana na takwimu za mwaka 1999 zilizotolewa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, asilimia 20 - 24 ya mama wajawazito katika miji na asilimia 7 - 10 vijijini wana virusi vya UKIMWI. Aidha, inakisiwa kuwa zaidi ya watoto 72,000 wanaozaliwa wanakuwa wameambukizwa ugonjwa huo. Takwimu hizo pia zinaonyesha kwamba asilimia 70.5 ya wagonjwa wapya ni wenye umri kati ya miaka 25 - 49. Hivyo, Taifa linapoteza idadi kubwa ya watu wanaotegemewa kuzalisha mali na pia wale ambao wamesomeshwa kwa gharama kubwa na kuwa mabingwa katika fani mbalimbali.
- Mheshimiwa Spika, kwa kutambua athari za UKIMWI, Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa, katika salamu zake za mwaka mpya wa 2001 kwa Taifa, alitamka kwamba UKIMWI ni janga la Taifa. Ili kukabiliana na janga hili aliunda Tume ya UKIMWI (Tanzania Commission for AIDS - TACAIDS) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tume hiyo ina jukumu la kuratibu na kusimamia vita dhidi ya UKIMWI katika mitandao iliopo ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Jumuiya za Wananchi. Aidha, itahamasisha juhudi za kila mmoja wetu, kila kikundi, vyama, taasisi mbalimbali na wafadhili katika vita dhidi ya UKIMWI.
- Mheshimiwa Spika, juhudi hizi pekee haziwezi kuleta mafanikio ikiwa hatutakubali kubadili tabia, mila na desturi zinazoendekeza kuambukizana UKIMWI. Wazazi tusione aibu kuzungumza na watoto na vijana wetu njia za kujikinga kuambukizwa UKIMWI. Elimu mashuleni katika ngazi zote itumiwe ili kunusuru vijana na janga hili. Ni wajibu wa kila wizara, idara na mashirika ya aina zote, kuweka katika mipango yao ya kazi, mikakati itakayochangia kuupiga vita UKIMWI. Sambamba na mikakati hiyo, ni lazima sasa tukubali kupimwa ili tufahamu hali ya afya zetu. Ni robo moja tu ya watu walio na UKIMWI wanaojijua kuwa wameathirika. Robo tatu nyingine hawajui kuwa wana UKIMWI, na hivyo wanaendelea kueneza UKIMWI. Pengine wangejijua, wangebadili tabia na mienendo yao, na hivyo kuzuia maambukizo zaidi. Juhudi za Serikali na washikadau wengine za kusaidia walioathirika hazitakuwa na manufaa kama hatufahamu hali za afya zetu. Pamoja na kuwa ugonjwa huu hauna dawa wala tiba, Serikali itawezesha kuwepo mfumo mzuri wa upatikanaji wa dawa za kurefusha maisha kwa waathirika.
- Mheshimiwa Spika, malaria ni ugonjwa mwingine unaongoza kwa kusababisha vifo vya wananchi wengi nchini. Kulingana na takwimu zilizotolewa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, asilimia 30 hadi 40 ya mahudhurio ya wagonjwa wa nje na asilimia 24 ya vifo vinavyotokea hospitalini husababishwa na malaria. Chini ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Serikali imekuwa ikihimiza kinga zaidi hususan usafi wa mazingira yetu, kuharibu mazalio ya mbu na kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa. Pamoja na juhudi hizi ugonjwa huu hivi sasa umeonyesha kuwa hauwezi kutibiwa kikamilifu kwa dawa ya Klorokwini ambayo tumeitumia kwa takriban miaka 50 iliyopita. Kwa hiyo, imebidi mabadiliko ya tiba yafanyike ili kutoa dawa nyingine ambayo itaweza kutibu ugonjwa huu. Ugonjwa unakuwa sugu pale tunaposhindwa kuzingatia maelekezo ya madaktari. Natoa wito kwa wananchi kuzingatia maelekezo ya madaktari kikamilifu wakati wa matibabu ili kuepuka madawa kuwa sugu.
- Mheshimiwa Spika, huduma ya maji ni muhimu kwa wananchi wetu. Mahitaji ya maji nchini kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo, kilimo, viwanda na umeme ni makubwa na yanazidi kuongezeka. Katika miji mikuu ya mikoa 18 zipo Mamlaka za Maji Safi na Maji Taka ambazo zimeonyesha mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma hii. Kwa mfano, Mamlaka za Maji katika miji ya Arusha, Moshi, Mwanza, Morogoro, Mbeya na Tanga zinajitegemea katika kugharimia maji na huduma zote za maji katika miji hiyo. Aidha, huduma za maji kwa Jiji la Dar es Salaam.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/2002, Serikali itaimarisha na kuhamasisha utumiaji wa teknolojia ya kuvuna maji ya mvua katika miji na vijiji vyetu. Aidha, itawashirikisha wananchi katika kazi za kusafisha, kufufua na kuchimba malambo. Vilevile, Serikali katika ngazi zote itaendelea kusimamia matumizi ya maji na kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinahifadhiwa na kwamba wananchi wanaoishi karibu na mabonde ya mito mikubwa wanashiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira katika mabonde hayo. Kwa vile mipaka ya nchi yetu inapita katika mabonde ya mito na maziwa ambayo yanachangiwa na nchi jirani, tutaendelea kushirikiana na nchi hizo ili tuweze kutumia maji hayo kwa uwiano unaozingatia maslahi ya nchi zetu zote.
- Mheshimiwa Spika, moja ya mahitaji muhimu ya binadamu ni nyumba. Katika kipindi cha takriban miezi saba tangu achaguliwe tena kuiongoza nchi yetu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, ameahidi kuwa Serikali yake itashirikiana na vyombo na taasisi mbalimbali nchini ili kuanzisha utaratibu wa ukopeshaji wa nyumba na kuanzisha soko la rehani za nyumba. Hivi sasa mawasiliano yanaendelea ili tupate utaratibu mzuri na endelevu wa kukuza sekta hii. Katika maeneo ya miji, Mamlaka za Serikali za Mitaa nazo zinao wajibu wa kuhakikisha kuwa viwanja vingi zaidi vinapimwa na kugawiwa kwa wananchi ili kupunguza tatizo la ujenzi holela katika miji yetu.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kuwa mwajiri, vilevile hutoa huduma mbalimbali za ajira zenye lengo la kukuza ajira, kusimamia na kukagua huduma za afya na usalama wa wafanyakazi na kudumisha mahusiano mazuri sehemu za kazi. Serikali imekamilisha utafiti kuhusu ukubwa wa tatizo la ajira ya mtoto nchini na matayarisho yamekamilika ya kufufua ofisi za huduma za ajira. Ili kudumisha usalama na afya ya wafanyakazi, kaguzi 2,625 za kawaida zinazohusu mazingira ya sehemu za kazi, kaguzi za aina mbalimbali 401 na kaguzi maalum za umeme 108 zilifanyika. Aidha, Serikali imeendelea kuwaelimisha wafanyakazi na waajiri taratibu za sheria za kazi kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri yenye kuongeza tija. Katika mwaka 2001/2002, Serikali itahuisha sera ya ajira ili iweze kuzingatia mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.
- Mheshimiwa Spika, moja ya taasisi ambayo tunaweza kuitumia kikamilifu katika kuwawezesha vijana wetu kupata ujuzi, stadi na maarifa ya kuwawezesha kujiajiri wenyewe ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Serikali imeamua kuwa shughuli za kuwapokea vijana wanaojiunga na JKT zianze tena rasmi katika mwaka wa fedha wa 2001/2002. Chini ya utaratibu mpya, Jeshi la Kujenga Taifa litaendeshwa katika muundo, dhana na taswira itakayolenga kuliwezesha kujiendesha lenyewe. Pamoja na kutoa mafunzo ya ukakamavu kwa vijana itawatayarisha vilevile kwa mafunzo ya awali ya ulinzi wa Taifa na kuwapa ujuzi wa kiufundi na kilimo.
- Mheshimiwa Spika, michezo ni fani ya utamaduni wetu inayopendwa na kuthaminiwa sana na wananchi wengi. Serikali, vyama mbalimbali vya michezo nchini, na washikadau wengine wanashirikiana kuimarisha michezo kwa kutoa mafunzo kwa vikundi mbalimbali, kushiriki katika mashindano ndani na nje ya nchi; na kuweka hali ya utulivu na maelewano katika vilabu na vyama vya michezo. Hata hivyo, inabidi tutatue matatizo yanayoikabili sekta hii, na ambayo naamini mengi yako ndani ya uwezo wetu. Baadhi ya matatizo hayo ni pamoja na uongozi mbovu, uhaba wa viwanja, gharama kubwa za vifaa vya michezo, upungufu wa waataalam na uwezo mdogo wa kumudu gharama za michezo. Katika mwaka 2001/2002, Serikali itakabiliana na baadhi ya matatizo hayo kwa kuhimiza Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Jiji kutenga na kulinda maeneo ya michezo, kushirikisha wananchi na sekta binafsi katika kujenga viwanja vya kisasa. Halikadhalika, Serikali itaendelea kuhamasisha watu binafsi, makampuni na taasisi mbalimbali kujenga viwanda vya kutengeneza vifaa vya michezo na kuendelea kufadhili michezo.
- Mheshimiwa Spika, dhana ya jinsia imeanza kueleweka na kutekelezwa katika mipango yetu mbalimbali ya maendeleo na uendeshaji wa kazi. Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia imezinduliwa na kusambazwa nchini kote. Sera hii ni matokeo ya kutambua kuwa tukiacha tofauti zilizopo za kiuchumi na kijamiii kati ya wanawake na wanaume ziendelee, Taifa letu halitakuwa na maendeleo ya kweli. Hatuna budi kuhakikisha kuwa sera, sheria na taratibu zinazotawala ajira, kuondoa umaskini, haki za kisheria, siasa, elimu na mafunzo, vinatoa fursa na nafasi sawa kwa jinsia zote. Aidha, hatua za makusudi na marekebisho zitachukuliwa ili kurekebisha pale ambapo jinsia moja ilipunjika kupata haki stahili kwa sababu tu za mila na desturi zilizokuwepo. Mkazo utaelekezwa kuingiza masuala ya jinsia katika mikakati na programu mbalimbali za Serikali, na kuwawezesha wanawake kupata mitaji kupitia mikopo inayotolewa kutoka mifuko mbalimbali ya maendeleo. Kwa kuthamini umuhimu wa wanawake kitaifa na kimataifa, viti maalum vya wanawake vimeongezwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, kati ya Wabunge tisa wanaowakilisha nchi yetu katika Bunge la Afrika Mashariki, watatu ni wanawake.
Utawala Bora
- Mheshimiwa Spika, kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, utawala bora ni ule wenye kuzingatia sheria, haki, uhuru wa raia, uwajibikaji wenye kuenzi utendaji mzuri wa kazi, wenye kuzingatia demokrasia na ushirikishwaji, na ule wenye kupiga vita rushwa na maovu mengine ya jamii. Ili kuleta mabadiliko katika utendaji kazi Serikalini hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Mabadiliko katika Utumishi wa Umma wenye lengo la kuwawezesha viongozi na watumishi wa umma kuwajibika zaidi kwa wananchi na kutatua matatizo yao. Mpango huu utaongeza tija katika sehemu za kazi na kutakuwepo utaratibu wa kupima matokeo ya kazi kwa kila taasisi na kila mtumishi ili tuweze kuwatunza watendaji wazuri na kupiga vita uzembe, rushwa na maovu mengine katika utumishi wa umma. Serikali pia imeanzisha mtandao wa mawasiliano na teknolojia ya kompyuta wa kisasa unaosimamia kumbukumbu zote za watumishi katika malipo ya mishahara. Mtandao huu utaimarishwa ili uweze kufanikisha uwekaji wa kumbukumbu za utendaji kazi, nidhamu na upandishwaji vyeo. Serikali vilevile imechukua hatua za kuwapandisha vyeo watumishi wake ambao kwa muda mrefu hawakuwa wamepandishwa vyeo. Ili kukabiliana na upungufu wa baadhi ya kada za utumishi, Serikali itaanza tena kuajiri watumishi katika kada maalum katika mwaka 2001/2002. Marekebisho ya viwango vya mishahara kwa watumishi wa umma yataendelea kufanyika hatua kwa hatua ili kuongeza ari, ufanisi na tija katika utendaji kazi, na kuondoa kero za watumishi Serikalini.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi kubwa iliyofanywa na Serikali na Watanzania kwa jumla katika kupambana na rushwa, bado hili ni tatizo kubwa katika jamii yetu. Ili kukabiliana na tatizo hili, katika kipindi cha mwaka 2000/2001, Serikali ilikamilisha Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa na kila Wizara na Idara za Serikali zinaandaa mpango wa utekelezaji wake. Aidha, Bunge lako limepitisha sheria mbalimbali zitakazosaidia kuziba mianya ya rushwa. Baadhi ya sheria muhimu zilizopitishwa katika mwaka 2000/2001 ni Sheria ya Uagizaji na Ununuzi wa Vifaa vya Serikali ya mwaka 2001, Sheria ya kurekebisha Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 2001 na Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali ya mwaka 2001. Harakati za upigaji kura za maoni zinaendelea na taarifa za wanaojihusisha na vitendo vya rushwa zinaendelea kutolewa kwa wingi. Watumishi wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa wanaendelea kuchukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini, kuvuliwa madaraka na kushitakiwa mahakamani.
- Mheshimiwa Spika, vita dhidi ya rushwa ni vita vya kila mwananchi. Ushindi wake unahitaji kila mmoja wetu kuwa na nia thabiti ya kuikataa rushwa. Viongozi wawe mstari wa mbele na wawasimamie vyema walio chini yao, na walio chini wazingatie kanuni na maadili ya utumishi wa umma. Hivi sasa kila kiongozi wa sekta yoyote ahakikishe kuwa moja ya majukumu yake makubwa ni kusimamia maadili katika sekta yake. Kama unasimamia sekta ambayo inatuhumiwa kwa rushwa, basi ukubali umeshindwa kazi. Kupambana na rushwa sasa iwe ni sharti la kazi kwa kila kiongozi na mtendaji. Aidha, wananchi washiriki kuwafichua wala rushwa na hatimaye wadhibitiwe na kuadhibiwa ipasavyo. Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2001/2002, Serikali itaendelea kutoa msukumo zaidi katika mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha Ofisi za Taasisi ya Kuzuia Rushwa katika ngazi ya Wilaya.
- Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya kero za wananchi zinatokana na kutowajibika kikamilifu kwa baadhi ya watendaji na viongozi wenye dhamana katika Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali. Hali hii imesababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kuhusu kucheleweshwa kwa haki za msingi kama mafao ya wastaafu na ya watumishi waliopunguzwa kazi Serikalini na katika Mashirika ya Umma yaliyobinafsishwa, kucheleweshwa kwa hukumu za kesi mbalimbali kunakosababisha haki kutotendeka, kucheleweshwa kwa malipo ya fidia yatokanayo na bima za ajali, mirathi na migogoro ya ardhi. Viongozi na watendaji wakuu katika ngazi zote za Serikali wameelekezwa kuzingatia sheria na taratibu za utendaji kazi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi katika maeneo yao. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2001/2002, Tume ya Haki za Binadamu itaanza kazi zake rasmi. Tume hii itasaidia kuongeza nguvu za Serikali kupunguza kero za wananchi na kulinda haki zao za msingi. Hata hivyo, Tume hii haitafanya kazi badala ya Mahakama zetu. Mahakama zitaendelea kuwa mhimili mkubwa katika kuendeleza haki za wananchi na Tume itatumia nguvu ya Mahakama kulinda haki za wananchi.
- Mheshimiwa Spika, ili kuziwezesha Mahakama kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha Idara ya Mahakama. Kwa mfano, ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa Mahakimu pamoja na kutoa mafunzo kwa mahakimu, Serikali imewezesha Chuo cha Mahakama cha Lushoto sasa kuanza kazi. Vilevile, Serikali imeipatia Idara ya Mahakama majengo ya kudumu kwa ajili ya Mahakama ya Rufaa. Aidha, imeendeleza mpango wa kuboresha mfumo wa utoaji haki kwa kuimarisha utaratibu wa usuluhishi na Kamati za kusukuma mashauri. Serikali pia, imewezesha kuendeshwa kwa mafunzo kwa Mahakimu wa Wilaya, Mahakimu Wakazi na Majaji wote wa Mahakama Kuu kuhusu utaratibu wa kuwasuluhisha wadaawa. Kwa sasa utaratibu huu unatumika Dar es Salaam, Mwanza na Arusha peke yake, lakini tunatarajia kuueneza katika kanda nyingine za Mahakama Kuu, kwa lengo la kupunguza muda na gharama za kesi na kuongeza kasi ya kuendesha mashauri ya madai.
Uboreshaji wa Serikali za Mitaa
- Mheshimiwa Spika, katika kuboresha utendaji na utoaji huduma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Programu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa imeendelea kutekelezwa. Kazi zinazotekelezwa chini ya programu hii zina lengo la:
i. Kuwahamasisha wananchi ili waweze kuelewa na kushiriki katika kutekeleza programu hii na kukuza kanuni za utawala bora,
ii. Kuongeza ufanisi wa Serikali za Mitaa katika kutoa huduma bora na kujenga misingi ya kupambana na umaskini,
iii. Kuongeza mapato ya Serikali za Mitaa na kuimarisha usimamizi wa matumizi yake,
iv. Kuinua ufanisi wa utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi kwa Halmashauri,
v. Kuandaa na kupendekeza mabadiliko ya sheria ili kuwezesha utekelezaji wa uboreshaji kwa mujibu wa Sheria na
vi. Kujenga uwezo wa wizara yenye dhamana ya Serikali za Mitaa ili iweze kuratibu shughuli za uboreshaji wa mfumo wa Serikali za Mitaa.
- Mheshimiwa Spika, hadi sasa hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuandaa mazingira ya kuboresha mfumo wa Serikali za Mitaa ni pamoja na kupitisha Sheria ya Tawala za Mikoa Na. 19 ya mwaka 1997, Sheria Na. 6 ya mwaka 1999 na Sera ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1998. Kazi ya utekelezaji wa programu katika Halmashauri inaendelea vizuri. Mafunzo mbalimbali yaliyotolewa kwa watendaji wa Halmashauri pamoja na madiwani yamewezesha Programu hii kueleweka kwao na hivyo kuweza kupata mafanikio ya kuridhisha. Programu sasa inatarajia kuingia katika Halmashauri 45 za awamu ya pili hivyo kufanya jumla ya Halmashauri zilizopo katika Programu kufikia 82. Serikali itawasilisha katika Bunge lako Tukufu muswada wa marekebisho mbalimbali ya baadhi ya sheria za wizara za kisekta ili ziende sambamba na utekelezaji wa Programu hii. Jambo la msingi ni kuwa Halmashauri zinapewa uwezo zaidi wa kusimamia maendeleo ya wananchi.
- Mheshimiwa Spika, Halmashauri zina majukumu ya kushughulikia kero za wananchi, kuboresha huduma za jamii, kuleta maendeleo katika maeneo yao na kupunguza umasikini kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, hazitaweza kutekeleza majukumu hayo kama hazitaimarisha ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali. Aidha, Manispaa zilizoainishwa kwenye Mradi wa Kurekebisha Miundombinu za Miji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia zichukue hatua thabiti za kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo vilivyothibitishwa na mradi huo na kupiga vita ubadhirifu wa aina yoyote. Bila kuchukua hatua za dhati za kuimarisha mapato na kudhibiti matumizi ni wazi kuwa miundombinu mipya ya barabara, mifereji ya majitaka, dampo, mifumo ya maji safi ambayo karibu inakamilishwa haitakuwa endelevu.
Uhusiano wa Kimataifa
- Mheshimiwa Spika,Tanzania imeendelea kuwa na mahusiano mazuri na mataifa yote duniani, na vilevile kuendeleza uanachama wake katika jumuiya mbalimbali, kama vile Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Madola, Umoja wa Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi, Umoja wa Nchi Huru za Afrika, Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara, na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, Tanzania imekuwa ikiunga mkono hatua zinazochukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kuleta amani na kutatua migogoro mbalimbali duniani.
- Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeridhia mkataba wa ushirikiano baina ya nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania. Aidha, nchi zote tatu zimedhamiria kujenga taasisi za ushirikiano ambazo zitawasaidia wananchi wa nchi hizi kushirikiana katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Moja kati ya taasisi hizo ni Bunge la Afrika Mashariki ambalo litazinduliwa katika kipindi cha mwaka 2001/2002. Nawapongeza Wabunge waliochaguliwa na Bunge lako Tukufu kuiwakilisha nchi yetu katika Bunge hilo. Watanzania wote tunalo jukumu la kutumia fursa inayojitokeza katika ushirikiano huu kushiriki kikamilifu katika shughuli za biashara na uwekezaji. Haitusaidii kulalamika au kujiona wanyonge, bali tuondoe vikwazo vyote vinavyotukwamisha ili tuwe washiriki wa kweli katika jumuiya hii. Vilevile, Tanzania imeendelea kuwa mwanachama hai wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Tumeshiriki kikamilifu katika jumuiya hii ili kuunganisha nguvu zetu na zile za nchi wanachama katika kutatua matatizo na kuondoa vikwazo vya maendeleo katika Bara letu la Afrika. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa umoja na ushirikiano wa nchi za Afrika, Tanzania imeridhia mkataba wa kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika.
- Mheshimiwa Spika, hali katika eneo la Maziwa Makuu bado haijawa ya kuridhisha sana. Kutokuwepo kwa amani na utulivu katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumeendelea kusababisha wimbi la Wakimbizi wanaoingia nchini mwetu. Hivi sasa inakadiriwa kuwa wapo wakimbizi takriban 700,000 nchini. Mikoa ya mipakani ya Kagera, Kigoma na Rukwa ndiyo inayoathirika zaidi na vitendo vya uhalifu vinavyotokana na wimbi la wakimbizi. Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, inaimarisha ulinzi na usalama ili kudhibiti athari hizo. Hata hivyo, suluhisho la kudumu ni kupatikana kwa amani katika nchi hizo na wakimbizi kurudi makwao. Aidha, Serikali inaendelea kusisitiza kuwa hatutairuhusu nchi yetu kutumiwa na wakimbizi kuhujumu nchi wanamotoka. Maelezo yoyote yanayotolewa kuwa Tanzania inavisaidia vikundi vinavyoipinga Serikali ya sasa ya Burundi ni ya uzushi na uongo.
- Mheshimiwa Spika, kufuatia mabadiliko ya sera zetu za ndani zinazotufanya tuwe na uchumi huria, ni dhahiri msisitizo katika sera zetu za nje utakuwa kwenye diplomasia ya uchumi. Katika mwaka 2001/2002, Serikali itakamilisha maandalizi ya sera mpya ya mambo ya nje ambayo msisitizo wake utakuwa ni kukuza sekta za uzalishaji mali hususan utalii, biashara na uwekezaji.
MAJUMUISHO
- Mheshimiwa Spika, Bara la Afrika bado limegubikwa na matatizo mengi. Kuna matatizo ya uchumi duni na dhaifu usiokua vizuri na kukidhi mahitaji muhimu ya wananchi wetu. Kuna matatizo ya huduma duni za jamii likiwemo tatizo kubwa la ugonjwa wa UKIMWI. Kuna matatizo ya ongezeko kubwa la watu, matatizo ya kisiasa, matatizo ya amani na usalama, matatizo ya njaa, ukame na mafuriko, matatizo ya umasikini uliokithiri n.k. Baadhi ya matatizo haya yanatupata kwa sababu ya mfumo mbaya wa uchumi duniani na kwa sababu tusizoweza kuzizuia kama vile majanga au mabadiliko ya hali ya hewa. Hata hivyo, matatizo yaliyo mengi yanasababishwa na sisi wenyewe.
- Mheshimiwa Spika, kisiasa Afrika bado ni eneo la matatizo makubwa. Tatizo moja kubwa ni la baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kujipangia nafasi za uongozi kabla ya kura za wananchi. Matokeo ya kura yanapokuwa tofauti na walivyojipangia, basi hukataa matokeo ya uchaguzi na kuanzisha vurugu. Hali hii husababisha vurugu ndani ya nchi zetu na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe jambo ambalo husababisha uharibifu mkubwa wa mali na upotevu wa maisha. Ni vyema viongozi wa kisiasa wa Kiafrika wakajifunza kuiheshimu demokrasia na kukubali matokeo ya matakwa ya wengi.
- Mheshimiwa Spika, hali hii pia imetukumba Tanzania tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 na hata ule wa mwaka 2000. Wote bado tunakumbuka vurugu za tarehe 27 Januari 2001 ambapo watu 23 walipoteza maisha. Tunaomba aibu ya namna hiyo isitokee tena Tanzania. Viongozi wa kisiasa lazima tukubali kuwa katika mashindano kuna kushinda na kushindwa na ni wajibu wetu kukubali matokeo ya mashindano hayo na baada ya hapo tujiandae kwa mashindano mengine yanayofuata.
- Mheshimiwa Spika, ninapenda kuvihakikishia vyama vyote vya siasa viwe vya upinzani au chama tawala kuwa vinao uhuru wa kufanya shughuli zao za kisiasa ili mradi havivunji sheria za nchi na taratibu za jamii yetu. Wanachama wa vyama vya siasa wanaweza kufanya mikutano, maandamano, au matembezi ya kuchangisha fedha kwa kadri wanavyoona inafaa ili mradi hawavunji sheria au kupata kizuizi cha polisi. Lakini pale mikutano, maandamano au matembezi yanapotumika kuvunja amani au kutolea kauli za uchochezi, Serikali haitakaa kimya eti kwa sababu ya haki za binadamu na uhuru wa vyama vya siasa. Uhuru na haki hiyo lazima viwe na mipaka na kuhakikisha kuwa havitishii amani na utulivu nchini mwetu. Aidha, tukumbuke kuwa Serikali iliyoko madarakani popote duniani ina jukumu na wajibu wa kwanza kabisa wa kulinda usalama wa raia wake.
- Mheshimiwa Spika, moja ya matatizo makubwa ya nchi zinazoendelea duniani ni umasikini. Tanzania ni moja ya nchi masikini sana duniani. Ili kuondoa umasikini uliokithiri kwa wananchi wetu, Serikali kwa kushirikiana na washikadau wote ilitayarisha Dira ya Maendeleo 2025 yenye lengo la kukabiliana na tatizo hili. Katika miaka mitano iliyopita jitihada kubwa zimefanywa na zimeleta mafanikio makubwa katika kuimarisha na kukuza uchumi wetu. Pamoja na matatizo makubwa tuliyokuwa nayo ya hali ya hewa, yaani ukame na mvua za El Nino, tuliweza kupunguza sana mfumuko wa bei, Pato la Taifa liliongezeka, mapato ya Serikali yaliongezeka, uwekezaji uliongezeka n.k. Kazi kubwa katika kipindi kilichoko mbele yetu ni kuimarisha mafanikio haya na kuhakikisha yanawafikia wananchi kwa kuhakikisha umasikini unapungua, huduma za afya, elimu, maji, usafiri, nishati, barabara, biashara n.k. zinakuwa bora zaidi na kero mbalimbali za wananchi zinashughulikiwa. Kazi hii imekwisha anza.
- Mheshimiwa Spika, ili tuondokane na uchumi duni na tegemezi, ni lazima wananchi wote tushirikiane kujenga uchumi. Tukumbuke hakuna taifa linaloweza kujengewa uchumi endelevu na taifa lingine au kwa njia ya misaada kutoka nje. Watanzania tunayo nafasi nzuri sana ya kuleta mabadiliko katika maisha yetu na uchumi wetu kama tutatumia rasilimali tulizonazo kikamilifu na hasa ardhi. Jawabu la uduni wa uchumi wetu ni kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya jamii yetu inajihusisha na shughuli za uzalishaji mashambani na viwandani. Hivi sasa tija ya Watanzania bado ni ndogo sana. Hali hii isipobadilika ipo hatari kwa Watanzania kutupwa nje ya soko la ajira hasa milango ya mahusiano ya kiuchumi inavyozidi kufunguka kwa kuanzia na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni lazima tuongeze tija na ubora wa bidhaa zetu za kilimo na viwanda ili tuweze kuingia na kushindana katika mkondo wa biashara za kimataifa. Aidha, ni muhimu kuwavutia na kushirikiana na wawekezaji wa nje na ndani ili kukuza mitaji na uchumi wetu.
- Mheshimiwa Spika, jambo lingine muhimu ni kuendelea kuhimiza wananchi kubuni na kushiriki katika utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo. Moyo wa kujitegemea ambao tayari umejitokeza ni lazima uhimizwe na kuendelezwa. Jambo hili lisipohimizwa na kuendelezwa kikamilifu litaleta tofauti kubwa ya maendeleo baina ya maeneo ya nchi yetu hasa wakati huu ambapo fedha nyingi za HIPC zinaelekezwa katika huduma za jamii kusaidiana na nguvu za wananchi. Ni dhahiri kuwa wale watakaojituma zaidi watanufaika zaidi na fedha hizo. Aidha, Serikali itapambana na vitendo vyote vinavyowakatisha tamaa wananchi katika kuchangia nguvu na mali zao katika miradi ya maendeleo. Sambamba na kujenga miradi hii ni muhimu kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuitunza miradi hiyo pamoja na ile ya Serikali iliyoko katika maeneo yao. Wapo baadhi ya watu wanaoharibu miradi ya umma kwa faida zao binafsi. Kwa mfano, alama za barabara hunyofolewa, bomba za maji na vyuma vya madaraja huondolewa, nguzo za taa huharibiwa, nyaya za umeme huibwa, mafuta ya transfoma huibwa n.k. Kamati zetu za ulinzi na usalama katika vijiji vyetu zitumike kudhibiti hali za aina hii. Aidha, suala la uharibifu wa mazingira nalo lisimamiwe kikamilifu. Miti huangamizwa katika maeneo ya vijiji bila kupanda miti mipya, mapori na misitu yetu huchomwa moto na hakuna hatua zinazochukuliwa na Serikali zetu ngazi za vitongoji, vijijiji, mitaa au ngazi nyingine za juu zaidi. Ni vyema tukatambua kuwa haya yote yapo kwa ajili yetu na tusipoyalinda, watakaoathirika ni sisi na vizazi vyetu vijavyo.
- Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia ningependa kusisitiza mambo yafuatayo:-
i. Ni lazima maisha ya Watanzania yabadilike na kuwa bora zaidi. Kazi ya kuleta mabadiliko hayo itafanywa na Watanzania wenyewe na jambo hili halina miujiza bali ni kwa kila mmoja wetu kufanya kazi kwa bidii. Kwa bahati nzuri bado tunayo ardhi kubwa na nzuri ambayo inaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali ya maendeleo kama vile kilimo, ufugaji, viwanda n.k. Suala la watu kukimbilia mijini kwa matumaini eti kila mtu atapata kazi ya ajira ni kudidimiza uchumi wetu na kujichimbia katika umasikini uliokithiri.
ii. Tuwe na mipango yenye malengo thabiti ya kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, na kuwe na tathmini ya utekelezaji. Baadhi ya maeneo muhimu ya kutiliwa mkazo
ni:
- Uboreshaji wa huduma za jamii.
- Kuongeza tija katika kilimo ili kukidhi mahitaji ya chakula na bidhaa za kuuza
nje.
- Usindikaji wa mazao utiliwe mkazo.
- Ushirika sahihi ufufuliwe.
- Uzalishaji katika viwanda uongezeke na kuboreshwa kukidhi soko la ndani na la
nje.
- Tuendelee kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani ili kupata mitaji, teknolojia na masoko.
iii. Bajeti hii imeondoa au kupunguza kodi nyingi kwa matumaini kuwa watu wengi sasa watalipa kodi na mapato ya Serikali hayatapungua. Naomba kila mmoja wetu aone ni wajibu wake kulipa kodi na kutoa taarifa kuhusu wanaokwepa kulipa kodi. Tuanzie kwa kudai stakabadhi kila tunaponunua bidhaa. Kwa upande wa Serikali, tuhakikishe kuwa fedha zinakusanywa na zinatumika kama zilivyoidhinishwa na Bunge.
iv. Watumishi na watendaji wote wawajibike ipasavyo kwa umma. Nidhamu, uadilifu na uaminifu viwe vigezo muhimu katika utumishi. Huduma zinazopaswa kutolewa bure zitolewe bure na kwa uwazi na zile za kulipiwa zilipiwe kwa uwazi. Matangazo ya kuonesha bei za huduma zinazolipiwa yawekwe wazi katika mbao za matangazo na stakabadhi zitolewe.
v. Rushwa na UKIMWI ni matatizo makubwa sana katika jamii yetu. Mambo haya mawili tusiyaonee haya wala tusioneane haya. Tuelezane ukweli waziwazi. Yote haya ni magonjwa mabaya. Hivyo basi, jamii kwa ujumla ishiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya magonjwa haya. Aidha, kuanzia kipindi hiki, sekta zote za Serikali na taasisi zake, zitenge muda muafaka kuzungumzia namna ya kukabiliana na magonjwa haya mawili makubwa yanayoikabili Taifa letu.
SHUKRANI
- Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Mawaziri wote na Naibu Mawaziri wote kwa ushauri wao ambao umemwezesha Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yao ya kitaifa kwa ufanisi. Aidha, nawashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na taasisi zake chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Marten Lumbanga pamoja na vyombo vyote vya dola kwa kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuiwezesha kukamilisha maandalizi yote ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2001/2002 pamoja na makadirio ya matumizi ya fedha ya kila wizara. Nawashukuru wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara na wengine wote kwa mchango wao ambao ndio unaoiwezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
- Mheshimiwa Spika, napenda vilevile kuwashukuru Mheshimiwa William Lukuvi, Waziri wa Nchi (Sera) na Mheshimiwa Omari Ramadhani Mapuri, Waziri wa Nchi (Habari na Siasa) kwa msaada mkubwa na ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu niliyokabidhiwa ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru vilevile wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Bwana Raphael Mollel, kwa ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na Mawaziri wa Nchi. Aidha, nawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2001/2002.
- Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limeweka utaratibu mpya wa kupitisha bajeti za wizara zetu, utaratibu ambao umewezesha ushirikishwaji zaidi wa Wabunge katika kupitia bajeti hizo. Napenda kukupongeza wewe Mheshimiwa Pius Msekwa, Spika, Mheshimiwa Juma Jamaldin Akukweti, (Mb.) Naibu Spika, kwa kutuongoza vyema. Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Anne Makinda, (Mb.) na Mheshimiwa Eliakim Simpasa, (Mb.) kwa kuchaguliwa kwa kauli moja kuwa Wenyeviti wa Bunge na kwa kuwasaidia kuongoza shughuli za Bunge. Ninawashukuru pia watumishi wa Ofisi ya Spika chini ya uongozi wa Katibu wa Bunge Bwana Kipenka Msemembo Mussa, kwa ushirikiano wao na huduma nzuri wanazotoa kwa Waheshimiwa Wabunge.
- Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kupata misaada na mikopo kutoka kwa Wahisani mbalimbali. Misaada na mikopo hii imechangia sana katika kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Napenda kuwashukuru wote kwa dhati na kuwahakikishia kuwa Watanzania tunathamini misaada na mikopo yao na tutaendelea kushirikiana nao katika harakati za maendeleo ya Taifa letu.
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA TAASISI ZAKE PAMOJA NA OFISI YA SPIKA KWA MWAKA 2001/2002
- Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2001/2002, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake pamoja na Ofisi ya Spika, inaomba jumla ya Shilingi 19,040,937,700 kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo. Kati ya fedha hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaomba jumla ya Shilingi 11,758,992,900 na Ofisi ya Spika inaomba jumla ya Shilingi 7,281,944,800. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaomba jumla ya Shilingi 2,500,000,000 kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo. Kati ya hizo, Shilingi 700,000,000 ni fedha za hapa na Shilingi 1,800,000,000 ni fedha za nje.
- Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili mpango wa kazi za Serikali kwa mwaka 2001/2002 na kujadili na kuzingatia taarifa ya kamati ya kisekta iliyojadili Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Ofisi ya Spika kwa mwaka 2001/2002.
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
MAJEDWALI
Jedwali
Na.
1
IDADI YA WABUNGE WA KUCHAGULIWA
|
Na.
|
Chama
|
Idadi ya Wabunge
|
Asilimia
|
|
1.
|
CCM
|
202
|
87.45%
|
|
2.
|
CUF
|
17
|
7.36%
|
|
3.
|
CHADEMA
|
4
|
1.73%
|
|
4.
|
TLP
|
4
|
1.73%
|
|
5.
|
UDP
|
3
|
1.30%
|
|
6.
|
NCCR-MAGEUZI
|
1
|
0.43%
|
Jumla
|
231
|
100%
|
Jedwali
Na. 2
IDADI YA MADIWANI WA KUCHAGULIWA
|
Na.
|
Chama
|
Idadi
ya Madiwani
|
Asilimia
|
|
1.
|
CCM
|
2,327
|
91.72%
|
|
2.
|
TLP
|
59
|
2.33%
|
|
3.
|
CHADEMA
|
50
|
1.97%
|
|
4.
|
CUF
|
49
|
1.93%
|
|
5.
|
UDP
|
30
|
1.18 %
|
|
6.
|
NCCR-MAGEUZI
|
20
|
0.79%
|
|
7.
|
TADEA
|
2
|
0.08%
|
|
8.
|
UMD
|
0
|
0.00%
|
|
9.
|
TPP
|
0
|
0.00%
|
|
10.
|
PONA
|
0
|
0.00%
|
|
11.
|
NRA
|
0
|
0.00%
|
|
12.
|
NLD
|
0
|
0.00%
|
|
13.
|
UPDP
|
0
|
0.00%
|
|
|
|
2,537
|
100%
|
Jedwali Na. 3
SHERIA ZILIZOPITISHWA NA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 200/2001
1. The Community Health Act, 2001 (Act. No. 1/2001)
2. The Cotton Industry Act, 2001 (Act. No. 2/2001)
3. The Public Procurement Act, 2001 (Act. No. 3/2001)
4. The Treaty for Establishment of the East African Community Act, 2001
(Act. No. 4/2001)
5. The Public Leadership Code of Ethics (Amendment) Act, 2001
(Act. No. 5/2001)
6. The Public Finance Act, 2001 (Act. No. 6/2001)
7. The Commission for Human Rights and Good Governance Act, 2001
(Act. No. 7/2001)
8. The Education Fund Act, 2001 (Act. No. 8/2001)
9. The Surface and Marine Transport Regulatory Authority Act, 2001
(Act. No. 9/2001);
10. The Written Laws (MSC Amendment) Act, 2001 (Act. No. 10/2001)
11. The Energy and Water Utilities Authority Act, 2001 (Act. No. 11/2001)
12. The Dar Es Salaam Water and Sewerage Authority Act, 2001 (Act. No. 12/2001).
Jedwali Na. 4
VYOMBO
VYA UTANGAZAJI
|
|
JINA
|
MMILIKI
|
MAKAO
MAKUU
|
MWAKA
ILIPOANZA
|
|
1.
|
Radio
Tanzania Dar es Salaam
|
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
|
Dar es
Salaam
|
1952
|
|
2.
|
Radio One
|
Reginald
Mengi & Agapitus Nguma
|
Dar es
Salaam
|
1994
|
|
3.
|
Radio
Tumaini
|
Catholic
Archdiocese Dar es Salaam
|
Dar es
Salaam
|
1994
|
|
4.
|
Radio
Kwizera
|
Jestus
Refugee Service, Diocese of Rulenge
|
Ngara
|
1995
|
|
5.
|
Radio
Free Africa
|
Anthony
M. Dialo
|
Mwanza
|
1996
|
|
6.
|
Radio
Maria
|
Catholic
Archdiocese, Songea
|
Songea
|
1996
|
|
7.
|
Radio
Sauti ya Injili
|
Evangelical
Lutheran Church of Tanzania
|
Moshi
|
1996
|
|
8.
|
Radio 5
Arusha
|
Didas
Kavishe
|
Arusha
|
1997
|
|
9.
|
United
Radio Service
|
Elisario
Urio
|
Arusha
|
1997
|
|
10.
|
Tanzania
Radio FM
|
Wilfred
Munuve & Athman Majengo
|
Arusha
|
1997
|
|
11.
|
Clouds
Entertainment Radio FM
|
Joseph
Kussaga
|
Dar es
Salaam
|
1998
|
|
12.
|
Classic
F.M 103.1 Radio
|
Cablevision
Africa Ltd.
|
Dar es
Salaam
|
1999
|
|
13.
|
Radio
Uhuru
|
Uhuru
Publications Ltd.
|
Dar es
Salaam
|
2000
|
|
14.
|
Chechemi
Radio Sumbawanga
|
Diocese
of Sumbawanga
|
Sumbawanga
|
2000
|
|
15.
|
Times
Radio FM
|
Business
Times Ltd.
|
Dar es
Salaam
|
2000
|
|
16.
|
Radio
Ukweli (RU)
|
Catholic
Diocese of Morogoro
|
Morogoro
|
2000
|
|
17.
|
Abood
Radio
|
Abood
Media
|
Morogoro
|
2001
|
TELEVISHENI
|
JINA
|
MMILIKI
|
MAKAO
MAKUU
|
MWAKA
ILIPOANZA
|
|
1.
|
Coastal
Television Network (CTN)
|
Shabir
Abji, Tayesh Shah, Ramesh Patel, Girish Chande, Bud Kassam, Mohmood Mawji
|
Dar es
Salaam
|
1994
|
|
2.
|
Dar es
Salaam Television (DTV)
|
Shabbir
Dewji & Murtaza Dewji
|
Dar es
Salaam
|
1994
|
|
3.
|
Independent
Television
|
Reginald
Mengi & Agapitus Nguma
|
Dar es
Salaam
|
1994
|
|
4.
|
Cable
Entertainment Network (CEN)
|
Jitendra
P. Ganatra & Ramesh V. Savajiani
|
Dar es
Salaam
|
1997
|
|
7.
|
Sokoine
University of Agriculture Television
(SUA –
TV)
|
SUA
|
Morogoro
|
1995
|
|
7.
|
Abood
Television
|
Aziz M.
Abood
|
Morogoro
|
1998
|
|
8.
|
Televisheni
ya Taifa (TVT)
|
Serikali
ya Muungano wa Tanzania
|
Dar es
Salaam
|
2000
|
TELEVISHENI ZA KULIPIA
(CABLE TELEVISION NETWORK)
|
JINA
|
MMILIKI
|
MAKAO
MAKUU
|
MWAKA
ILIPOANZA
|
|
1.
|
Bharat
Video Centre
|
Bharat
Unadkati
|
Mwanza
|
1994
|
|
2.
|
Mwanza
Satellite Communication Ltd. (MSCTN)
|
Rizwani
Kanji, Hino/Moihin Barmeda
|
Mwanza
|
1994
|
|
3.
|
Millan
Video Centre
|
Sudha
Millan, Millan T. Majithia, Mohamed Hassan
|
Arusha
|
1994
|
|
4.
|
Star
Cable Television Ltd.
|
Jahajir
Hassan Dalvi, Karim A. Ladha & Hassan S. Khan
|
Dar es
Salaam
|
1995
|
|
5.
|
Cable
Television Network (CTV)
|
Hitesh
Tanna, B.S. Rughan & H. Mgome
|
Tanga
|
1995
|
|
6.
|
Ayoub
Cable Television Co. Ltd.
|
Ayoub
Azizi
|
Shinyanga
|
1996
|
|
7.
|
Tabora
Television Broadcasting Co. Ltd.
|
Shashikant
M. Patel & Jagdish M. Patel
|
Tabora
|
1996
|
|
8.
|
Bahman
Satellite Cable
|
Ally H.
Said & Ahmed H. Said
|
Tanga
|
1996
|
|
9.
|
Dodoma
Cable Television
|
Alkarim
Sadrudin Jaffer
|
Dodoma
|
1996
|
|
10.
|
Arusha
Cable Television (ACTV)
|
Abdi
Abdulrasul
|
Arusha
|
1996
|
|
11.
|
International
Entertainment Cable Television Network
|
Shobhag
D. Shah
|
Moshi
|
1996
|
|
12.
|
Dhandho
Cable Network
|
Karim
Dharsi
|
Mbeya
|
1997
|
|
13.
|
Space
Satellite Cable Television Network
|
Godfrey
Kajanja
|
Musoma
|
1997
|
|
14.
|
Cable
Television Network
|
Hitesh
Tanna, Basker Rughan & Harold Ngoma
|
Dar es
Salaam
|
1998
|
|
15.
|
Morogoro
Cable Network
|
A. R.
Pandya & K. A. Adam
|
Morogoro
|
1998
|
|
16.
|
Television
Burudani (Wireless Cable TV)
|
Didas D.
Kavishe
|
Arusha
|
1999
|
|
17.
|
Tarime
Satellite TV Network
|
-
|
Tarime
|
2000
|
|
18.
|
Ghana
Cable TV Services
|
Patrick
Pius
|
Mwanza
|
2000
|
mwisho