HOTUBA YA WAZIRI WA UJENZI MHESHIMIWA JOHN P. MAGUFULI (MB.) WAKATI AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO WA MAENDELEO NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2002/03

 

UTANGULIZI

 

1.                Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2002/03.

 

2.                Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea napenda kwanza kabisa kuipongeza Kamati nzima ya miundombinu ambayo kwa umoja wao wameweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Wizara yangu itaendelea kuzingatia na kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo, na yatakayotolewa na Bunge lako Tukufu katika kipindi hiki cha mwaka 2002/03 kwa kadri ya uwezo tutakaopewa tayari kutekeleza majukumu yaliyopangwa.

 

3.                Mheshimiwa Spika, Napenda pia kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Frederick Tluway Sumaye, Mbunge wa Hanang, kwa hotuba yake katika Bunge hili la Bajeti ambayo kwa kiasi kikubwa imefafanua masuala ya barabara na  imetupa upeo wa majukumu ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi kijacho. Hali kadhalika nawapongeza Waziri wa Fedha Mheshimiwa Basil P. Mramba, na Mheshimiwa Abdallah M. Kigoda, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Ubinafsishaji) kwa hotuba zao ambazo sio tu zimechambua na kuelezea kwa kina maendeleo, matatizo na matarajio ya uchumi wetu, bali pia zimeweka wazi sera, malengo na mikakati ya utekelezaji wa mipango ya Serikali.

 

DIRA YA WIZARA

 

4.                Mheshimiwa Spika, Dira ya Wizara ya Ujenzi ni kuendeleza Sekta ya Ujenzi ili kuchochea na kuleta ufanisi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi na hivyo hatimaye kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

 

Maeneo yanayosimamiwa na kuendelezwa na Wizara ya Ujenzi ni yale ya Ujenzi, Ukarabati, na Matengenezo ya Barabara, Madaraja na Majengo ya Serikali.  Maeneo mengine ni ya kutoa Huduma za Ufundi na Umeme na Huduma za Ugavi.

 

Kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi mwaka 2025 (vision 2025), malengo na matazamio ya Wizara ifikapo mwaka 2025 ni kama ifuatavyo:

 

·        Kuwa na mtandao mzuri na salama wa barabara ambapo nchi zote jirani zitakuwa zimeunganishwa kwa barabara za lami, makao makuu ya Mikoa yote yatakuwa yameunganishwa kwa barabara za lami wakati makao makuu ya Wilaya yatakuwa yameunganishwa na barabara za kuaminika zinazopitika wakati wote.

·        Kuwepo kwa Makandarasi na Wahandisi Washauri wengi wazalendo watakaokuwa na sifa na uzoefu wa kutosha wa kuwawezesha kufanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilisha kazi katika muda uliopangwa kwa mujibu wa Sheria zetu.

·        Kuwa na Sekta ya ujenzi inayochangia katika kupunguza utegemezi, kuondoa umaskini na kutoa ajira kwa wananchi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya raslimali za ndani ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu kazi iliyopo hasa katika matengenezo ya barabara.

·        Kuandaa mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji binafsi kuwekeza katika miradi ya barabara.

·        Kuwa na maeneo ya miliki ya barabara (Roads Reserve) yanayotambulika na kuheshimika.

·        Kuwa na ushiriki mkubwa wa wanawake katika kazi za barabara katika ngazi zote za utungaji sera, upangaji mipango, utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi ya barabara.

·        Kuwa na Sekta ya Barabara inayotekeleza shughuli zake bila kuathiri mazingira.

 

MAJUKUMU YA WIZARA

 

5.                Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumekuwa tunalieleza Bunge lako Tukufu, majukumu ya Wizara ya Ujenzi ni kama ifuatavyo:

·        Kuandaa sera, mipango na mikakati inayolenga katika ukuzaji, uimarishaji na uendelezaji wa sekta ya ujenzi nchini katika muda mfupi, wa kati na mrefu.

·        Kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya Barabara, Madaraja na Majengo ya Serikali.

·        Kusimamia uendeshaji wa shughuli za Bodi ya Mfuko wa Barabara, Wakala wa Barabara, Wakala wa Nyumba pamoja na Wakala zingine zinazotarajiwa kuundwa chini ya Wizara zinazohusu Idara ya Ufundi na Umeme na Idara ya Ugavi na Huduma.

·        Kuratibu shughuli za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ambazo ni Baraza la Taifa la Ujenzi na Bodi za Usajili wa Makandarasi, Wahandisi, Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Usimamizi wa Vifaa.

·        Kutafuta fedha za nje na za ndani za kugharamia miradi iliyo chini ya Wizara.

·        Kuandaa na kusimamia viwango vya ubora wa kazi za ujenzi, ukarabati pamoja na matengenezo ya barabara.

·        Kuandaa mazingira yatakayovutia wawekezaji binafsi katika ujenzi wa barabara na madaraja.

·        Kusimamia na kuratibu shughuli za upembuzi yakinifu wa barabara kuu na za vijijini.

·        Kusimamia shughuli za Usalama wa Barabara (Road Safety).

·        Kuboresha ufanisi wa Wahandisi Washauri na Makandarasi wazalendo katika ujenzi na matengenezo ya barabara nchini kwa kuwapatia mafunzo.

·        Kusimamia na kuendesha shughuli zote za ununuzi, ukarabati na matengenezo ya magari, vivuko, mitambo, viyoyozi na vifaa vya elektroniki vya Serikali.

·        Kuhakikisha mali za Serikali kama Magari, Pikipiki na Mitambo inasajiliwa kwa namba za Serikali kwa mujibu wa Sheria ya barabarani ya mwaka 1973.

·        Kutekeleza utaratibu wa kujenga na kuwauzia Watumishi wa Serikali nyumba za kuishi kupitia Wakala wa Majengo.

·        Kusimamia ukodishaji wa magari, mitambo ya kokoto na ukodishaji wa mitambo ya Serikali (Road Workshops).

·        Kusimamia maendeleo ya Watumishi wa Wizara.

 

 

 

MIKAKATI YA UTEKELEZAJI

 

6.                Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu haya, Wizara imezingatia maelekezo yaliyotolewa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2000-2005, Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi mwaka 2025, mikakati ya kupunguza umaskini na Sera nyingine za Ujumla za Taifa za kukuza uchumi na kuboresha maendeleo ya Jamii. Aidha Wizara imejiwekea Mikakati ifuatayo katika kutekeleza majukumu haya:-

 

·        Kufanya mapitio ya mfumo wa utendaji ili shughuli za kiutendaji zifanywe na taasisi zinazojitegemea (Wakala) na Wizara ibaki na majukumu yake ya msingi ya uandaaji wa sera na mikakati inayolenga katika ukuzaji na uimarishaji wa sekta ya ujenzi.

·        Kutoa kipaumbele katika ukarabati na ujenzi wa barabara kwa kufuata Kanda Kuu za usafirishaji, barabara za Mikoa na za Wilaya ambazo ni muhimu kwa huduma za usafirishaji wa mazao ya kilimo na huduma nyingine muhimu za kitaifa.

·        Kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa zana za ujenzi kwa kuimarisha karakana za Serikali na kuhamasisha watu binafsi kuanzisha kampuni za kukodisha mitambo.

·        Kuendeleza mafunzo kwa Wahandisi Washauri na Makandarasi wazalendo ili wasimamie na kutekeleza vizuri mikataba ya ujenzi na matengenezo ya barabara.

·        Kutafuta vyanzo vingine vya fedha za Mfuko wa Barabara ili ukidhi mahitaji ya ujenzi na matengenezo ya barabara.

·        Kuendeleza mazungumzo na wawekezaji binafsi wanaoonyesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa barabara na madaraja.

·        Kuhakikisha usanifu wa barabara mpya unazingatia hifadhi ya mazingira, usalama wa watumiaji wote na viwango vya mahitaji halisi ya matumizi ya magari.

·        Kuandaa utaratibu mzuri wa kusimamia Sheria ya Udhibiti wa Uzito wa magari na matumizi bora ya barabara kwa kuwashirikisha wadau wote.

·        Kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani na Mawasiliano na Uchukuzi katika kuimarisha utaratibu mzima wa utoaji mafunzo na leseni kwa madereva na kutoa elimu na hamasa ya Usalama Barabarani.

·        Kuwasaidia wananchi, mamlaka mbalimbali na Umma kwa ujumla kutambua mipaka ya maeneo ya barabara (Road Reserve) na kutayarisha ramani za barabara zitakazoonyesha mipaka ya miliki ya barabara zote za Umma.

·        Kuendeleza teknolojia ya nguvu kazi ili kuwapa uwezo wananchi wengi zaidi kushiriki katika kazi za matengenezo ya  barabara katika maeneo yao bila kusubiri msaada kutoka Serikalini.

 

UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2001/02 NA MALENGO YA MWAKA 2002/03

 

7.                Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo kuhusu Dira, Majukumu na Mikakati ya utekelezaji ya Wizara, naomba sasa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa malengo ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2001/02 na malengo ya mwaka 2002/03.

 

Mifumo ya Taasisi zilizo chini ya Wizara

 

8.                Mheshimiwa Spika, kama nilivyolieleza Bunge lako Tukufu katika hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2001/02 kuhusu uundwaji wa Wakala, nafurahi kutamka kuwa pamoja na Wakala wa Barabara (Tanzania Roads Agency - TANROADS) ambao umeanzishwa tangu mwaka 2000,  Wakala wa Nyumba za Serikali (Tanzania Building Agency -TBA) pia umeundwa tangu mwezi Mei mwaka 2002, kwa kutumia Sheria Na. 30 ya mwaka 1997.  Majukumu yake muhimu ni pamoja na:-

·        Kutunza nyumba za Serikali zinazomilikiwa na Wakala.

·        Kuwapatia nyumba bora za kuishi Watumishi wa Serikali wakiwa kazini na baada ya kustaafu.

·        Kutekeleza utaratibu wa kujenga na kuwauzia Watumishi wa Serikali nyumba kwa kutumia fedha zitakazolipwa na waliokopeshwa nyumba, na pia kutokana na mapato mengine.

·        Kutoa huduma za ushauri (Consultancy Services) kuhusiana na majengo.

·        Kuhakikisha kuwa majengo ya Serikali yanajengwa na kutunzwa kwa kuzingatia viwango(standards) vilivyowekwa.

 

Aidha, hatua mbalimbali zinachukuliwa ili Idara za Ufundi na Umeme na Ugavi na Huduma nazo ziwe Wakala.

 

Mpango wa Taifa wa kuendeleza Mtandao wa Barabara

 

9.                Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekamilisha kuandaa rasimu ya awali ya Mpango wa Miaka Kumi wa kuendeleza Mtandao wa Barabara hapa nchini kwa kipindi cha 2001-2010.  Mpango huu utatumika kama mwongozo wa kuteua barabara kuu na za vijijini za kufanyiwa ukarabati katika kipindi hiki.  Wizara kwa sasa inafanya mapitio ya rasimu hiyo ili kuandaa mapendekezo ya mwisho ya mpango.  Aidha, Wizara imepanga kufanya mkutano na wahisani wa sekta ya barabara mwaka 2002/03 ili kuwasilisha Mpango huo kwao kwa madhumuni ya kuwaomba kugharamia baadhi ya miradi inayopendekezwa.

 

USHIRIKIANO WA KIKANDA

 

Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor - MtDC)

 

10.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ikiwa ndiyo mratibu wa shughuli za Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara inaendelea kushirikiana na Wizara nyingine nchini ili kusimamia na kutekeleza malengo yaliyowekwa kwa kushirikiana na nchi wanachama wa Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor  – MtDC). 

 

Baada ya mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Makaa ya Mawe ya Mchuchuma-Katewaka kupata wawekezaji na kuweka saini Mkataba wa Makubaliano ya Awali (Agreement of Intent) kati ya Serikali na Wawekezaji mwezi Julai, 2001, hatua iliyofikiwa mpaka sasa ni kwamba majadiliano ya pamoja kwa pande zote zinazohusika yanaendelea vizuri.  Aidha, wadau mbalimbali kama vile Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TANESCO na Benki ya Dunia wanashirikishwa katika majadiliano hayo.  Hadi sasa Mkakati wa utekelezaji (Project Development Programme) umekwisha tayarishwa na Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na kwa ushirikiano na wawekezaji na majadiliano ya jinsi ya kuanza utekelezaji yanaendelea.

 

Mradi mwingine unaohusika ni ujenzi wa barabara ya Mtwara-Masasi-Songea-Mbamba Bay.  Mradi huu umepata fedha za msaada kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait kwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni moja (US.$1.0million). Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kufanyia upembuzi yakinifu (feasibility study).  Kazi hii inatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2002/03 mara baada ya kumpata Mtaalam Mshauri.

 

11.    Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Machi 2002, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara yangu na Serikali ya Msumbiji kupitia Wizara ya Ujenzi na Nyumba ziliwekeana saini Mkataba wa Maelewano (Memorandum of Understanding) juu ya ujenzi wa Daraja la Umoja (Unity Bridge) katika mto Ruvuma.  Daraja hilo litakuwa ni kiungo muhimu kwani litaweza kuziunganisha nchi hizi mbili kwa njia ya barabara.  Katika mkataba huo nchi zote mbili zinawajibika kutafuta fedha na wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.

 

12.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2002/03 lengo kuu kuhusu maendeleo ya Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara ni kukamilisha Rasimu ya Mkataba wa Maelewano (Memorandum of Understanding) kati ya nchi wanachama.  Tunaamini kwamba kusainiwa kwa Mkataba wa Maelewano kwa nchi wanachama kutakuwa ni kiunganisho chenye nguvu za kisheria kwa nchi wanachama wa ukanda huu na kuwa kichocheo kikubwa cha kupata wawekezaji na wahisani katika miradi ya Ukanda huu.  Pili, hali hii itawezesha kuandaliwa kwa miradi mama (Regional Anchor Projects) ambapo nchi zote zitaweza kuiwasilisha kwa pamoja kwenye makongamano mbalimbali ya wawekezaji.

 

Ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

 

13.    Mheshimiwa Spika, kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki ningependa niongelee zaidi miradi ya barabara iliyomo kwenye ukanda wa Jumuiya hiyo (East African Road Network Projects).  Miradi hii iko kwenye kanda tano (five corridors) ambazo zimeunganisha nchi za Afrika Mashariki.  Miradi hiyo na hatua za utekelezaji wake hadi sasa ni kama inavyoonyeshwa katika Kiambatanisho Na. 1.

 

14.    Mheshimiwa Spika, ili kutafuta fedha za kuendeleza barabara kwenye kanda hizo Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inaandaa kongamano/mkutano wa wafadhili (EAC / Development Partners Road’s Consultative Meeting) Mwezi Oktoba mwaka 2002.  Madhumuni ya mkutano huo ni kuwafahamisha wahisani wa miradi ya barabara kuhusu maendeleo na utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kuwahamasisha katika kuendeleza sekta hii ya barabara.  Vile vile, zimeanzishwa juhudi za pamoja kwa nchi zote za Afrika ili kuweka mkakati wa pamoja wa kuondoa umaskini  (New Partnership for Africa’s Developemnt-NEPAD).  Kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, maandalizi haya yamekwishaanza na Wizara yangu imekwishaainisha miradi ya barabara itakayoingizwa katika mkakati huu kama ilivyofafanuliwa kwenye Kiambatanisho Na. 2(a).

 

BODI YA MFUKO WA BARABARA

 

15.    Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2001/2002 nililiarifu Bunge lako Tukufu juu ya hatua mbalimbali zilizofikiwa na Bodi ya Mfuko wa Barabara katika utekelezaji wa majukumu yake pamoja na malengo ya siku zijazo.  Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2001/2002 Bodi imefanya yafuatayo:-

·        Bodi imetathimini upya viwango vya tozo mbalimbali zinazoingia katika mfuko na kutoa mapendekezo kwa ajili ya kuhakikisha fedha za kutosha zinapatikana za kutunza barabara zetu.  Lengo ni Mfuko wa Barabara uweze kutosheleza mahitaji ya matengenezo ya barabara Kuu na za Mikoa pamoja na barabara muhimu za Wilaya na Mijini ifikapo mwaka 2008/2009.  Mapendekezo hayo yanaendelea kufanyiwa kazi na Wizara yangu kwa lengo la kuyawasilisha Serikalini ili yatolewe maamuzi ya mwisho.

·        Bodi imepitia upya na kuboresha mikataba ya kazi (Performance Agreements) kati ya Bodi na watekelezaji kwa kuweka vigezo vya utekelezaji (performance indicators) vinavyopimika.

·        Bodi imefuatilia matumizi ya fedha za mfuko kwa kukagua kazi zinazofanywa na taasisi zinazotumia fedha hizi kwa kutumia wakaguzi wa fedha na ubora wa kazi (Financial and Technical Audits).

 

16.    Mheshimiwa Spika, kati ya mwezi Agosti na Desemba, 2001, Bodi ya Mfuko wa Barabara iliendesha ukaguzi wa hesabu kwa taasisi zilizopokea fedha kwa mwaka wa fedha 2000/01.  Ripoti ya Ukaguzi inaonyesha Bodi ya Mfuko ilipata ripoti safi.  Ripoti inaonyesha  Wizara ya Ujenzi, TANROADS, Halmashauri za Miji na Wilaya zilifanyiwa ukaguzi.  Hatua zimekwishaanza kuchukuliwa kwa watendaji waliobainika kutumia vibaya fedha hizi. Halikadhalika hatua kali zitachukuliwa dhidi ya makandarasi waliobainika kufanya kazi mbovu kwa mujibu wa Sheria Na.17 ya mwaka 1997. Ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mwaka 2000/01, Bodi imeamua kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2001/02 ukaguzi wa hesabu ufanyike mara mbili kwa mwaka ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha mapema iwezekanavyo. Taasisi husika zitaendelea kutoa ripoti za kazi mara nne kwa mwaka.

 

17.          Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, katika mwaka wa fedha 2001/02, hadi kufikia tarehe 25/6/2002, Bodi ya Mfuko wa Barabara ilipokea na kugawa jumla ya Shilingi 48,519.18 milioni ambazo ni asilimia 96 ya lengo la mwaka ambalo ni Shilingi 50,790 milioni.  Kati ya fedha hizo, Shilingi 3,352.9 milioni zimetolewa kwa Wizara ya Ujenzi, Shilingi 30,176.243 milioni kwa TANROADS, Shilingi 620.384 milioni kwa ajili ya matumizi ya Bodi yenyewe na Shilingi 14,369.639 milioni kwa Serikali za Mitaa.

 

18.          Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Bodi ya Mfuko wa Barabara imepanga kutekeleza malengo yafuatayo katika mwaka 2002/03:-

 

·            Kufuatilia matumizi ya fedha zilizotolewa kwa kufanya ukaguzi wa hesabu na ubora wa kazi kwa kutumia Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali, Mhandisi Mshauri na Bodi yenyewe.

·            Kutayarisha kitabu cha mwongozo wa Mfuko wa Barabara ambacho kitajumuisha utaratibu wa usimamzi wa fedha za mfuko na mikataba ya kazi, kuelimisha juu ya mabadiliko  yanayoendelea katika sekta ya barabara, majukumu ya Bodi ikiwemo utaratibu wa kugawa na kufuatilia fedha za mfuko.  Sheria iliyoanzisha Bodi nayo itaambatanishwa.  Kijitabu hicho kitasambazwa kwa Wabunge wote, Makatibu Tawala wa Mikoa yote, Wakurugenzi Watendaji na Umma kwa ujumla.

·            Kuelimisha wadau juu ya fomula mpya ya kugawa fedha kwenye Halmashauri na kusisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika kutunza barabara kwa njia ya kuchangia gharama.

·            Kushirikiana na wadau ili waunge mkono juhudi za kupanua wigo wa Mfuko wa Barabara na juhudi za kupambana na tatizo la magari kuzidisha uzito kwenye barabara.

·             Kushirikiana na Bodi nyingine za nchi mbalimbali ili kujifunza kutokana na uzoefu wao.

 

19.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2002/03 Serikali imeweka malengo ya kukusanya jumla ya Shilingi 64,341 milioni kwa ajili ya Mfuko wa Barabara ambazo zitagawiwa kwa TANROADS Shilingi 40,154.866 milioni,  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Shilingi 19,070.02 milioni, Wizara ya Ujenzi Shilingi 4,449.67 milioni na Bodi ya Mfuko wa Barabara Shilingi 674.27 milioni.

 

WAKALA WA BARABARA (TANROADS)

 

20.    Mheshimiwa Spika, miaka miwili imetimia tangu Wakala wa Barabara, (TANROADS) uliopoanzishwa hapo tarehe 1 Julai, 2000.  Katika miaka hii miwili, TANROADS imekuwa ikiweka na kuendeleza mifumo ya kisasa ya menejimenti na mawasiliano katika ngazi zote za Makao Makuu ya Mikoa ili kuweza kukabili majukumu yake katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia.  Matokeo ya juhudi hizo yanadhihirishwa na dalili za kuboreka kwa utendaji wa kazi za barabara na nidhamu katika matumizi ya fedha.

 

Aidha, Wakala umeongeza kasi ya kufanya kazi kwa kutumia makandarasi na kupunguza mfumo wa kufanya kazi kwa kutumia vikosi vyake (Force Account).  Uamuzi wa kutumia makandarasi umewezesha kuwepo kwa ongezeko la kandarasi za matengenezo ya barabara zinazotekelezwa kutoka wastani wa kandarasi 50 -100 kwa kila robo katika mwaka 1999/2000 hadi kufikia kandarasi 500-700 kwa robo katika mwaka 2001/2002.  Aidha, katika kipindi cha 2002/03 Wizara itapitia muundo wa TANROADS ili kuwa na Wakala wenye Watumishi wachache lakini wenye ufanisi zaidi na hii itasaidia kuelekeza fedha nyingi za Mfuko wa Barabara kwenye matengenezo ya barabara badala ya fedha nyingi kuishia kwenye matumizi ya uendeshaji/utawala.

 

21.    Mheshimiwa Spika, napenda kusisitizia tena mwito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuendelea kufuatilia kwa karibu utendaji wa TANROADS katika maeneo yao na kuzipa taasisi hizi mbili (TANROADS na Bodi ya Mfuko wa Barabara) ushirikiano wa karibu ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

 

Ukusanyaji wa mapato

 

22.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Wizara ilipanga kukusanya jumla ya Shilingi 4,789.636 milioni kupitia idara zake zinazokusanya maduhuli ambazo ni Bohari Kuu, Ufundi na Umeme, Majengo na Utawala. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2002, jumla ya Shilingi 3,528.56 milioni zilikusanywa sawa na asilimia 73.7 ya malengo yaliyowekwa.

 

Katika mwaka 2002/03

Wizara ya Ujenzi inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 2,089,985,000 kutokana na vianzio vyake mbalimbali.

 

Wakala wa Nyumba, Idara ya Ufundi na Umeme pamoja na Bohari Kuu ziko chini ya “Retention Scheme” hivyo huruhusiwa kutumia kiasi fulani cha makusanyo yao kugharamia matumizi ya kawaida na kiasi kingine kinachobakia hupelekwa HAZINA.

 

Utekelezaji Miradi ya Maendeleo na kazi za matengenezo mwaka 2001/02

 

 

23.    Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kutekeleza miradi ya ukarabati na ujenzi wa barabara kuu katika mfumo wa kanda kuu za usafirishaji kama zilivyofafanuliwa kwenye Kiambatanisho Na.2(b).  Katika mwaka wa fedha 2001/2002 Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi 91,799 milioni kwa miradi ya maendeleo ambapo Shilingi 16,554 milioni zilikuwa fedha za hapa na Shilingi 75,245 milioni zilikuwa fedha za kigeni zilizotokana na michango ya wahisani mbalimbali.  Aidha, Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi 3,488 milioni toka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya miradi ya maendeleo.  Kwa hiyo jumla ya fedha zote za hapa zilizotengwa kwa miradi ya maendeleo ni Shilingi 20,042 milioni. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2002 jumla ya Shilingi 19,906.92 milioni fedha za hapa zilikwishatolewa. Viambatanisho Na. 3 na 4 vinaonyesha utekelezaji halisi wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2001/02.

 

Katika mwaka 2001/02 Wizara yangu ilitengewa jumla ya Shillingi milioni 58,908.162 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.  Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 31,390.28 ni za hapa toka Mfuko wa Barabara na Shilingi 27,517.882 ni za nje toka kwa wahisani mbalimbali.  Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2002, jumla ya kandarasi 1,365 za kazi za matengenezo zilitolewa kama Kiambatanisho Na. 2(c) kinavyoonyesha.

 

24.    Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mipango ya mwaka 2001/02, utekelezaji wa kazi za barabara uliathirika kutokana na sababu zifuatazo:

·        Ufanisi duni wa baadhi ya Makandarasi katika kutekeleza kazi za barabara.

·        Upungufu wa mitambo ya kuwawezesha Makandarasi wazalendo kumudu utekelezaji wa kazi za barabara.

·        Baadhi ya Wahisani kuchelewa kutoa fedha kufuatana na ratiba iliyowekwa hivyo kuchelewesha miradi kuanza ama kuchelewesha malipo kwa makandarasi kwa muda uliokubaliwa katika mikataba.

·        Upungufu wa fedha kulinganisha na mahitaji halisi ya miradi ya maendeleo na kazi za matengenezo ya barabara.

·        Utaratibu mrefu wa kutoa zabuni (hasa kwa miradi ya Wahisani) umechelewesha kuanza kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi.

 

MIRADI MAALUM YA KUBORESHA BARABARA KUU

 

 

25.          Mheshimiwa Spika, ili kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara nchini, Serikali imeanzisha Mpango Maalum wa kutekeleza miradi ya barabara kwa kutumia fedha za ndani kama Waraka wa Baraza la Mawaziri Na.5 wa 2001 unavyoeleza.  Katika Mpango huu Serikali itakuwa inatenga Shilingi 1,840 milioni kila mwezi kwa ajili ya ujenzi wa barabara.  Wizara yangu imeanza kutekeleza miradi ifuatayo katika mwaka wa fedha wa 2001/02 mpaka 2005/06 kupitia mpango huu maalum:-

 

·        Barabara ya Somanga¾Masaninga na Daraja la Matandu (km.33)

·        Barabara ya Nangurukuru¾Mbwemkulu (km. 95)

·        Barabara ya Mbwemkulu¾ Mingoyo (km 95)

·        Barabara ya Dodoma¾Manyoni (km 124)

·        Barabara ya Manyoni¾Singida (km122)

 

26.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2001/2002 Shilingi 12,000 milioni zilitengwa kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huu. Kazi ambazo zilipangwa kufanyika ni kuteua Mkandarasi wa ujenzi wa Barabara ya Somanga¾Masaninga kwa kiwango cha lami na daraja la Matandu, kufanya usanifu, kuitisha zabuni na kuanza ujenzi sehemu ya Nangurukuru¾Lindi¾Mingoyo na Dodoma ¾ Manyoni na Manyoni¾Singida.  Mkandarasi wa sehemu ya Somanga-Masaninga pamoja na daraja la Matandu ameteuliwa.  Mkataba kati ya Wizara ya Ujenzi na Kampuni ya Ujenzi inayoitwa China Geo Engineering kwa ujenzi wa barabara ya Somanga¾Masaninga ulitiwa saini tarehe 22/2/2002.  Kazi hiyo itagharamu Shilingi 12,286,602,742.00. Hivi sasa Mkandarasi anaendelea na kazi ya kupeleka vifaa katika eneo la mradi.  Maandalizi ya kuanza ujenzi yanatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 9/7/2002 na ujenzi rasmi kuanza. Tarehe 11/06/2002 Mkataba wa usimamizi wa ujenzi wa barabara hiyo ulisainiwa kati ya Wizara na Kampuni ya Parkman Limited ya Uingereza inayoshirikiana na Kampuni ya M-Konsult ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi 1,041,952,476.00 Mhandisi Mshauri huyu anatazamiwa kuanza kazi ya usimamizi mara moja.

 

Tarehe 3/6/2002 Wizara ya Ujenzi iliingia Mkataba na Kampuni ya BKS Group ya Afrika ya Kusini inayoshirikiana na Kampuni ya Co-Architecture ya Tanzania kama Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kuandaa nyaraka za zabuni hadi kumpata Mkandarasi wa kujenga barabara ya Nangurukuru¾Mingoyo baadaye kusimamia ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo ya Nangurukuru hadi Mbwemkulu (95 km).  Kazi hiyo itagharimu Shilingi 1,038,144,000.00

 

Tarehe 12/06/2002 Wizara ya Ujenzi imeingia pia Mkataba na Kampuni iitwayo Roughton International ya Uingereza ambayo inashirikiana na Kampuni iitwayo Data Consult Ltd ya Tanzania kuwa Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kuandaa nyaraka za zabuni hadi kumpata Mkandarasi wa kujenga barabara ya Dodoma¾Singida na baadaye kusimamia ujenzi wa sehemu ya Dodoma hadi Manyoni.  Mkataba huu utagharimu Paundi za Kiingereza 500,978.00 na Shilingi 426,412,500.00 za Tanzania.

 

27.          Mheshimiwa Spika, malengo ya mwaka wa fedha 2002/03 ni kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Somanga-Masaninga na Daraja la Matandu na kukamilisha nyaraka za Zabuni na kuteua Makandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara za Nangurukuru¾Mbwemkulu, Mbwemkulu¾Mingoyo, Dodoma¾Manyoni na Manyoni-Singida.  Jumla ya Shilingi 22,000 milioni za ndani zimetengwa katika mwaka wa fedha wa 2002/03 kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa mpango huu kama Kiambatanisho Na.5 (b) kinavyoonyesha.

 

Miradi ya maendeleo mwaka 2002/03

 

28.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2002/03 jumla ya Shilingi 160,169.32 milioni zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo Shilingi 38,968.67 milioni ni fedha za hapa na Shilingi 121,200.9 milioni ni fedha za kigeni.

 

Aidha, katika fedha za hapa, jumla ya Shilingi 4,449.67 milioni zinatoka Mfuko wa Barabara na Shilingi 34,519 milioni zinatoka kwenye bajeti ya maendeleo. Muhtasari wa Mpango huu umeonyeshwa katika Viambatanisho Na. 5 na Na.6.

 

Mpango wa matengenezo ya Barabara mwaka 2002/03

 

29.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002/03 jumla ya Shilingi milioni 51,445.913 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara Kuu na za Mikoa. Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 40,154.866 ni fedha za hapa toka Mfuko wa Barabara na Shilingi milioni 11,291.047 ni fedha za nje.  Muhtasari wa kazi zote za matengenezo zilizopangwa kwa mwaka 2002/03 ni kama zilivyoonyeshwa katika Kiambatanisho Na.7.

 

Matumizi ya kawaida mwaka 2002/03

 

30.          Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2002/03 Wizara ya Ujenzi imetengewa jumla ya Shilingi milioni 9,075.9569 fedha za hapa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.  Fedha hizi zinajumuisha, mishahara ya Wizara, mishahara ya TANROADS, mishahara ya Taasisi nyingine na fedha za retention.

 

Muhtasari wa makisio ya Matumizi ya Kawaida pamoja na mapato ya fedha za Mfuko wa Barabara kwa mwaka 2002/03 umeonyeshwa katika Kiambatanisho Na.8.

 

MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA NGUVU KAZI

31.          Mheshimiwa Spika, katika harakati za kupambana na hali ngumu ya upatikanaji wa nyenzo na vitendea kazi, Wizara yangu inatekeleza mradi huu wenye lengo la kuendeleza teknolojia inayoruhusu na kutilia mkazo matumizi ya nguvu kazi na nyenzo zinazopatikana kwa urahisi hususan hapa hapa nchini (Labour Based Technology) katika ukarabati, matengenezo na ujenzi wa barabara. Katika mwaka wa fedha wa 2001/02, Wizara yangu iliendelea kufuatilia, kutathmini na kuratibu matumizi ya teknolojia hii katika kazi za barabara kwenye miradi mbalimbali mikoani na wilayani. Aidha, Wizara imeendelea kusambaza vitabu vya miongozo na maelekezo ya matumizi ya teknolojia hii kwa watumiaji na watendaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wakandarasi na Wahandisi Washauri.

 

32.          Mheshimiwa Spika, Wizara ina Chuo kinachotoa mafunzo ya matumizi sahihi ya teknolojia hii (Appropriate Technology Training Institute – ATTI) ambacho kipo Kiwira mkoani Mbeya. Wizara inaendelea na juhudi zake za kuhakikisha Chuo hiki kinaimarishwa ili kiendelee kutoa mafunzo na huduma nyinginezo kwa walengwa wote hususan ofisi za Halmashauri za Wilaya na Miji, Wakala wa Barabara (TANROADS), Makandarasi na Wahandisi Washauri kwa kuchangia gharama kiasi kidogo.

 

33.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2002/03, Wizara yangu imepanga kutekeleza yafuatayo:-

·        Kuendelea kutoa miongozo na maelekezo ya utumiaji wa teknolojia ya nguvu kazi kwa walengwa na kutathmini mwenendo mzima wa utekelezaji wa kazi za barabara kwa kutumia teknolojia hii.

·        Kuchapisha na kusambaza kitabu cha mwongozo (Labour Based Technical Manual Volume IV).

·        Kukiendeleza na kukipatia nyenzo na vitendea kazi chuo cha ATTI kwa kushirikiana na wataalamu kutoka ILO ili kiweze kutoa mafunzo kwa watu wote ikiwa ni pamoja na Makandarasi.

·        Kuhamasisha kupatikana kwa mwelekeo mmoja (National Framework) utakaofuatwa na watu wote wanaojihusisha kwa njia moja au nyingine na matumizi ya teknolojia hii katika kazi za barabara.

·          Kuiendeleza ‘Labour Based Documentation Center’ kwa kukusanya na kusambaza takwimu na taarifa mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya teknolojia hii katika kazi za barabara.

 

USHIRIKISHWAJI WA WANAWAKE KATIKA KAZI ZA BARABARA

 

34.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Kitengo cha Wanawake inaendelea kuhamasisha na kuwaelimisha wanawake ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi katika kazi za barabara. Lengo kuu la kuanzishwa kwa Mpango huu ni kuhakikisha kuwa wanawake nao wanashiriki katika kazi za ukarabati na matengenezo ya barabara kwa ajili ya kujipatia pato, kuchangia maendeleo nchini na kujikwamua na umasikini. Wizara kupitia mikoa inayotekeleza mpango huu inaendelea kuhamasisha na kuwaelimisha wanawake ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi katika kazi hizi. Mpango huu umekuwa ukikua mwaka hadi mwaka kutoka mikoa 5 ya majaribio katika mwaka 1993 hadi mikoa 14 hivi sasa. Hadi sasa mikoa inayotekeleza Mpango huu ni Mtwara, Lindi, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, Kagera, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Shinyanga na Mbeya. Katika mikoa hii asilimia 20 ¾ 35 ya nguvu kazi za barabara ni wanawake.

         

35.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/2002 Wizara yangu ilitoa mafunzo ya upangaji mipango yenye mtazamo wa kijinsia kwa washika dau wa Wizara, Mikoa na Wilaya ili kujenga msingi imara wa ushirikishwaji wanawake katika sekta ya ujenzi. Aidha ili kujenga msingi imara wa ushiriki wa wanawake katika kazi za barabara, Wizara yangu kwa kushirikiana na vyombo vingine itaendelea kufanya uhamasishaji kwa wanawake waweze kuunda vikundi vya ukandarasi ili kuweza kufaidika na zabuni za barabara ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira ya nguvu kazi kwa wanawake. Pia, Wizara yangu kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) imeweza kutoa mafunzo ya jinsia na uongozi kwa viongozi wa ngazi za juu wa Wizara (Wakurugenzi na Wakurugenzi wasaidizi) wapatao 35. Lengo la mafunzo haya ni kuwawezesha kupanga mipango yenye mtazamo wa kijinsia, kuelewa mikataba mbalimbali ambayo imeridhiwa na Serikali yetu kwa lengo la kumwendeleza mwanamke katika nyanja mbalimbali, usawa wa kijinsia na kuangalia/kuweka mikakati ya kuendeleza dhana ya ushirikishwaji wa wanawake katika sekta ya ujenzi. Kwa kushirikiana na mikoa ya Mtwara na Lindi, inayofadhiliwa na Finnida, Morogoro (SDC), Pwani (DANIDA), Iringa na Ruvuma (EDF) na Mwanza (UNDP), kitengo cha ushirikishwaji wa wanawake cha Wizara yangu kimeweza kuunda vikundi vya makandarasi wadogowadogo hivyo kuhamasisha wanawake kujiunga na kuongeza ajira ya nguvu kazi kwa asilimia 35%.

 

36.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2002/2003 Wizara yangu itaendelea kutoa mafunzo ya upangaji mipango yenye kuzingatia jinsia katika ngazi mbalimbali ili kuongeza kasi ya ushirikishwaji wanawake katika sekta ya ujenzi kutoka asilimia 35% ya sasa hadi 50%. Aidha, Kitengo cha wanawake cha Wizara yangu kwa kushirikiana na Mameneja wa Mikoa wa Wakala wa Barabara kitaendelea kufanya uhamasishaji kwenye Mikoa ile ambayo haijaanza utekelezaji wa mpango huu ili mpango uweze kutekelezwa nchi nzima kama ilivyokusudiwa.

 

KITUO CHA USAMBAZAJI WA TEKNOLOJIA KATIKA SEKTA YA USAFIRISHAJI (TANZANIA TECHNOLOGY TRANSFER (T2) CENTRE)   

 

37.          Mheshimiwa Spika, Kituo hiki kilianzishwa mwaka 1997 kutokana na juhudi za Wizara yangu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es salaam pamoja na msaada wa Shirika la Barabara la Marekani (US FHWA). Madhumuni ya kituo hiki  ni kuimarisha/kuboresha sekta ya usafirishaji kwa kutumia mbinu ya usambazaji wa Teknolojia. Kwa kuanzia kituo kinajihusisha na usambazaji wa teknolojia katika sekta ya barabara.

 

38.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/2002, Wizara yangu kwa kupitia Kituo hiki iliendelea kusambaza Teknolojia katika sekta ya usafirishaji hapa nchini kwa kusambaza kwa wadau makala zinazoelezea teknolojia mbalimbali katika sekta ya usafirishaji na kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kuhamasisha wanafunzi wa shule za Sekondari kuchukua masomo ya Sayansi (TRAC Programme) kwa shule za Sekondari za Jangwani, Mzizima na Azania ziliziko jijini Dar es Salaam.  Aidha, Kituo kimefanya utafiti unaolenga kuboresha utendaji kazi wake, kukiwezesha kuwa endelevu na kutayarisha Mpango wa muda mfupi na mrefu kuhusu usambazaji wa teknolojia hapa nchini. Pia, kiliandaa na kukamilisha makubaliano ya ushirikiano (Memorandum of Understanding) na Shirikisho la Barabara Duniani (World Road Association) litakalowezesha kituo kupata misaada na kubadilishana teknolojia katika masuala ya sekta ya barabara, na kuimarisha huduma za kituo kwa kununua vifaa mbalimbali.

39.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2002/03, Wizara yangu ina mpango wa kukiendeleza kituo hiki ili kiweze kusambaza teknolojia katika sekta ya barabara na usafirishaji, kukamilisha utafiti kuhusu uboreshaji wa huduma za Kituo na kuanza utekelezaji wa mapendekezo yake, kuandaa kozi, semina na warsha zinazohusu sekta ya usafirishaji, kwa wadau. Pia kituo kitaendelea kutekeleza mradi wa kuhamasisha wanafunzi wa shule za Sekondari kuchukua masomo ya Sayansi na Teknolojia (TRAC Programme).  Aidha kituo kitaendelea kuboresha njia za kisasa ya upashanaji habari na nyaraka mbalimbali kitaalamu kupitia mtandao wa kompyuta (Website), uboreshaji wa huduma za maktaba ya Kituo na kukiimarisha kwa kununua vifaa mbalimbali.

 

 

CHUO CHA UJENZI MOROGORO

40.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina Chuo cha Ujenzi Morogoro kilichoanzishwa kwa madhumuni ya kuwapa mafunzo kazini Mafundi Sanifu (Technicians) na Wahandisi wa Wizara ya Ujenzi na Halmashauri za Miji/Wilaya. Katika mwaka wa fedha 2001/02 Chuo kilipanga kutoa mafunzo kwa Mafundi Sanifu na Wahandisi 75. Hadi kufikia Juni 2002, Mafundi Sanifu 87 wamepata mafunzo mbalimbali chuoni. Aidha, Chuo kimeweza kukarabati baadhi ya majengo yake.

 

41.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2002/03 Chuo kimepanga kutoa mafunzo kwa idadi ya Wahandisi na Mafundi Sanifu 90 kutoka Idara na Wakala mbalimbali. Aidha, Chuo kimepanga kuendelea kuyafanyia ukarabati majengo ya Chuo pamoja na ununuzi wa samani na gari kwa ajili ya kurahisisha mafunzo.

 

USALAMA BARABARANI NA UDHIBITI WA UZITO

WA MAGARI.

 

 

42.          Mheshimiwa Spika, ajali za barabarani limekuwa tatizo kubwa hapa nchini. Taifa limekuwa likipoteza watu wengi kutokana na ajali za barabarani. Aidha Serikali hutumia fedha nyingi zikiwemo za kigeni katika ununuzi wa dawa, vipuri kwa ajili ya kutengeneza magari yaliyopata ajali au kununua mengine mapya baada ya kuharibika kabisa. Tathmini inaonyesha kuwa gharama hizi hufikia asilimia kati ya 1 na 2 ya pato la Taifa kwa mwaka.

 

43.          Mheshimiwa Spika, kutokana na utafiti, ajali nyingi husababishwa na mambo yafuatayo; uendeshaji mbaya wa magari, baadhi ya magari kuendeshwa yakiwa mabovu na uzembe wa watumiaji wengine wa barabara. Aidha uzidishaji wa uzito katika magari makubwa huchangia sana uharibifu wa barabara kabla ya muda wake uliokadiriwa wakati wa kusanifiwa na hivyo kuongeza gharama za matengenezo.

 

44.          Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekuwa nikilieleza Bunge lako Tukufu, Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zinazolenga kupunguza ajali pamoja na uharibifu wa barabara unaotokana na uzidishaji uzito. Katika mwaka wa 2001/02, Kitengo cha Usalama Barabarani kimeweza kutekeleza kazi zifuatazo: -

·        Kuimarisha mfumo wa kisasa wa uwekaji takwimu za ajali kwenye kompyuta kwa kuwapa mafunzo zaidi wataalam husika ili iwe rahisi kufahamu sehemu sugu za ajali na kuzirekebisha ipasavyo.

·        Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Utamaduni na Taasisi ya Elimu Tanzania inalenga kuendeleza elimu ya usalama barabarani katika shule zote za msingi na sekondari pamoja na vyuo vya Walimu hapa nchini. Mitaala ya Elimu ya Usalama Barabarani imeshaandaliwa na majaribio ya kufundisha somo hili yanafanywa katika baadhi ya shule za msingi na sekondari katika mikoa ya Pwani, Dar es salaam na Morogoro.

·        Wizara imeandaa mfumo bora wa ukaguzi wa magari unaoendana na mapendekezo ya Umoja wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).

·        Wizara kwa kupitia redio, magazeti na televisheni imekuwa ikiendesha kipindi cha “Barabara zetu”, ili kuwaelemisha wananchi juu ya utumiaji bora na salama wa barabara zetu na ubebaji wa mizigo.

·        Ili kudhibiti uzito na kuondoa tatizo la rushwa, Wizara kupitia Wakala wa Barabara imekuwa ikiwashirikisha wadau wote kuanzia wanaoagiza na wanaosafirisha mizigo mfano Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Mapato (TRA), Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Leseni za Usafirishaji, Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) pamoja na Kitengo cha Vipimo (Weights and Measures) ili kuhakikisha kwamba mizigo inayoagizwa na kusafirishwa katika barabara zetu inakuwa katika viwango vinavyoruhusiwa kwa mujibu wa Sheria ya Road Traffic Act. Na. 30 ya mwaka 1993, Regulation 2001 – Section 114.1P. (Max. Vehicle Weight) na hivyo kupunguza mianya ya rushwa.

45.          Mheshimiwa Spika, Mpango wa mwaka wa fedha 2002/03 ni :-

·        Kujenga vituo vipya vya mizani za kisasa katika maeneo ya Mikese (Morogoro), Mpemba (Tunduma) na Mutukula (Kagera).

·        Kuendelea kuwaelimisha wananchi, madereva, wamiliki wa vyombo vya usafiri umuhimu wa kuzingatia kanuni bora za utumiaji wa barabara.

·        Wizara itaendelea kusimamia majaribio ya elimu ya usalama barabarani katika baadhi ya shule za msingi, sekondari na vyuo katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro na kupanua majaribio haya katika kanda nyingine.

·        Kutoa mafunzo kwa Askari wa Usalama barabarani na Wahandisi mbalimbali juu ya uingizaji wa takwimu za ajali kwenye kompyuta na uchambuzi wake wa vyanzo vya ajali.

·        Kukamilisha rasimu ya mfumo wa shule za udereva, upimaji na utoaji wa leseni kwa madereva.

·        Mapendekezo yaliyo kwenye mifumo ya Ukaguzi wa magari, uendeshaji wa kozi za madereva pamoja na utoaji leseni kwa madereva itawasilishwa katika vyombo husika kuomba ridhaa ya Serikali kuanza kutekelezwa.

·        Kuendelea kutoa mafunzo kwa Wahandisi na Watumishi wengine wa Wizara jinsi ya kufanya Road Safety Audit.

 

IDARA YA UFUNDI NA UMEME

 

46.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Idara ya Ufundi na Umeme iliendelea kutekeleza majukumu yake ya kuratibu, kutathmini, kusajili, kufuta, kukodisha na kufanya matengenezo ya magari na mitambo ya Serikali, uendeshaji wa Vivuko na Mitambo ya kusaga mawe, ushauri, usimamizi wa miradi, usimikaji na matengenezo ya mitambo ya umeme, majokofu, viyoyozi na vifaa vya Elektroniki.

 

47.          Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma zitolewazo na Idara hii,  Wizara yangu katika mwaka 2001/02 ilitekeleza yafuatayo:

·        Zabuni zimetangazwa kwa lengo la kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na baadaye kuandaa zabuni kwa ajili ya matengenezo ya vivuko vitano kwa kugharimiwa na fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (IDA). Vivuko hivyo ni MV. Sengerema, MV. Pangani, MV. Kigamboni, MV. Rufiji, MV. Ulanga.

·        Ununuzi wa vifaa vya kisasa na uimarishaji wa huduma za utengenezaji wa magari na mitambo katika karakana zote za Idara ya Ufundi na Umeme.

·        Magari madogo (Saloon) mapya kumi  (10) yamenunuliwa kwa nia ya kuimarisha kitengo cha kukodisha magari ya Serikali yaani GTA. Aidha magari manne ya kuimarisha ukaguzi wa kazi yamenunuliwa. Vilevile gari moja maalum (Bucket Wagon) limenunuliwa kwa lengo la kuboresha huduma za ubadilishaji taa za kuongozea magari pamoja na taa za barabarani.

·        Kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba tani 50 kimenunuliwa kwa ajili ya mto Kilombero.

·        Ukarabati wa mitandao ya umeme (Electrical systems) ulifanyika katika majengo ya Wizara ya Ulinzi na Mahakama ya Rufaa Dar es Salaam.  Aidha ukaguzi wa mtandao wa umeme ulifanyika kwenye majengo ya Wizara ya Elimu na Utamaduni na Wizara ya Afya.

·         Kusajili magari ya Serikali yenye namba za kiraia.

Kwa muda mrefu sasa, Serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa kutokana na kulipia Bima na matumizi mabaya ya magari ya Serikali ambayo yamesajiliwa kwa namba za kiraia.  Katika kutekeleza Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 na Waraka Na.1 wa Rais wa mwaka 1998 unaohusu kubana matumizi ya Serikali, Wizara imetekeleza zoezi maalum la kusajili magari 3,139; pikipiki 1,407; na mitambo 120 iliyokuwa na namba za kiraia kuanzia Februari, 2002 hadi tarehe 29/6/2002.  Zoezi hili linaendelea hadi magari, mitambo na pikipiki zote zitakaposajiliwa na tunategemea kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 10 za Serikali.

 

48.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002/03 Wizara yangu kupitia Kitengo cha Ufundi na Umeme kitatembelea Mikoa yote, Wilaya zote na miradi yote ya Serikali ili kufanya uhakiki wa kusajili mali za Serikali ikiwa ni pamoja na Magari, pikipiki na Mitambo na hii itasaidia kujua Mitambo halisi ya Serikali.  Ningeomba Waheshimiwa Wabunge na Wananchi  kwa ujumla waisaidie Idara hii katika kupata taarifa ya vifaa hivi vya Serikali katika maeneo yao.  Katika mwaka wa Fedha wa 2002/03 Idara hii inalenga kutekeleza kazi zifuatazo:-

·        Ununuzi wa kivuko kipya chenye uwezo wa kupakia tani 25 kwa ajili ya Bugolora¾Ukara (Mwanza).

·        Kuendelea na ukarabati wa vivuko na kununua vifaa vya uokoaji majini kwa ajili ya vivuko (Life Saving Equipments and Life Jackets).  Aidha mafunzo ya uokoaji kwa wafanyakazi wa vivuko vyote nchini yataendeshwa.

·        Kuimarisha Karakana za viyoyozi, majokofu na elektroniki zilizopo katika Mikoa ya Dodoma, Arusha na Tanga ili ziweze kutoa huduma nzuri zaidi.

·        Kuendelea kununua vitendea kazi vya kisasa (Workshop Tools) zaidi ili kuboresha huduma zitolewazo na Wizara hii.

·        Kuendelea kukagua na kukarabati mitambo ya umeme kwenye majengo na Taasisi za Serikali kwa nia ya kuepusha majanga yatokanayo na hitilafu za umeme kama vile moto.

·        Kuendelea kujiandaa ili Kitengo hiki nacho kiwe Wakala kwa mujibu wa Sheria Na. 30 ya Mwaka 1997.

 

IDARA YA UGAVI NA HUDUMA

 

49.          Mheshimiwa Spika, Idara ya Ugavi na Huduma chini ya Wizara yangu inalenga katika kuhakikisha kunakuwepo na mfumo imara wa kuendesha shughuli za ununuzi na Ugavi Serikalini zenye ufanisi unaolenga matumizi bora ya fedha za Serikali. Umuhimu wa fani ya Ugavi hasa katika mazingira ya sasa ya uchumi unaotegemea nguvu za soko unaendelea kudhihirika kwani utaalamu wa fani hii huleta thamani kwa kila Shilingi inayotumika katika ununuzi.

 

50.          Mheshimiwa Spika, Wataalamu wa Ugavi wanahusika na shughuli za kupanga kwa ufanisi upatikanaji wa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya shughuli za Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.  Ili kufanikisha shughuli hizi Idara husimamia wataalamu ili kuhakikisha kuwa ununuzi wa vifaa, kazi na huduma, utunzaji wa vifaa na mali za Serikali pamoja na kumbukumbu zake unafanywa kwa ufanisi.

 

51.          Mheshimiwa Spika, Idara pia husimamia shughuli za Bohari Kuu ya Serikali, Wakala wa Ugomboaji na Usafirishaji wa mizigo ya Serikali pamoja na maendeleo ya Watumishi wa kada ya Ugavi Serikalini.

 

52.          Mheshimiwa Spika, takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa, kati ya asilimia 60 hadi 70 ya Bajeti ya Serikali hutumika kila mwaka katika ununuzi wa vifaa, kazi na huduma (goods, works & services).  Hii ina maana kwamba wataalamu hawa wanapaswa kuwajibika zaidi kusimamia matumizi ya fedha za Serikali na kwa ufanisi. Kutokana na jukumu hilo watumishi hao wanapaswa kuzingatia maadili ya taaluma yao ili kuepuka hasara ambazo hutokea kutokana na usimamizi dhaifu katika shughuli za Ugavi. Wizara yangu ikizingatia hasara ipatikanayo kutokana na udhaifu huo haiwezi kuacha hali hii iendelee, hasa ikizingatiwa kwamba Serikali ina jukumu la kujenga uchumi imara ili kuleta maendeleo kwa wananchi wake kwa kuondoa umaskini na kuongeza pato la Taifa.

 

53.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002/03 Wizara yangu inalenga katika kuongeza ufanisi ili Serikali ipate vifaa na huduma zenye ubora ambao utalingana na thamani ya fedha zinazotumika. Ili kufanikisha azma hii wizara yangu inatarajia kufanya yafuatayo:-

·        Kuandaa orodha ya viwango (standard specifications) ya vifaa ambavyo vitatumika Serikalini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

·        Kuhakikisha kuwa Watumishi wa Ugavi Serikalini wanafanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kama zilivyoainishwa na Sheria ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2001 na Sheria Namba 9 ya NBMM ya mwaka 1981.

·        Kuhakikisha kwamba watumishi wa Ugavi wanapewa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi katika taaluma yao ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.

·        Kuimarisha shughuli za Wakala wa Ugomboaji na Usafirishaji wa shehena za Serikali ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa gharama nafuu.

·        Kuendelea kuboresha mfumo wa Ununuzi na Utunzaji wa vifaa (Procurement and Supply Management Systems) katika Wizara, Idara, kuhakikisha kuwa Taasisi na Mikoa ili kuleta ufanisi katika uagizaji, upokeaji, utunzaji na utoaji wa vifaa.

 

54.          Mheshimiwa Spika, ili kuleta ufanisi, Wizara yangu katika mwaka 2002/03 itafuatilia suala la ajira ili kuhakikisha kuwa Taasisi zote za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zinaajiri wataalamu wa Ugavi ambao wamesajiliwa na Bodi ya Taifa ya Usimamizi wa Vifaa kama Sheria inavyotaka. Ni matarajio ya Wizara yangu kuwa utekelezaji wa mkakati huu utaweza kuleta ufumbuzi kwa matatizo ya upotevu wa fedha na mali za Serikali katika harakati za kupunguza umaskini ili kuleta maendeleo ya nchi .

BARAZA LA TAIFA LA UJENZI (NCC)

 

55.          Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Ujenzi lina jukumu la kuendeleza sekta ya ujenzi nchini.  Jukumu hili linatekelezwa kwa njia ambazo zinajumuisha ushauri kuhusu mipango ya sera na mikakati ya kukuza sekta, ushauri wa kiufundi ikiwa ni pamoja na tathmini ya kiufundi yaani (technical audit), mafunzo, takwimu, upashanaji habari wa shughuli za sekta, na utoaji miongozo ya kiufundi na kanuni za zabuni.

 

56.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02, Baraza lililenga kutoa msukumo katika kukamilisha Sera ya Taifa ya Ujenzi, kuendelea na shughuli za mafunzo kwa Makandarasi, Washauri, Watendaji Wakuu hasa wa Serikali za Mitaa kuhusu sheria mpya ya Manunuzi ya Umma (Public Procurement Act No. 3 of 2001), usimamizi wa mikataba ya ujenzi; kuboresha upatikanaji wa takwimu za shughuli za ujenzi; utayarishaji wa miongozo ya kiufundi; huduma za ushauri, ukaguzi wa miradi, na usuluhishi wa migogoro.  Aidha Baraza lilipanga kukamilisha uundaji wa Mfuko wa fedha wa Maendeleo ya Sekta ya Ujenzi  (Construction Industry Development Fund – CIDF).

 

57.          Mheshimiwa Spika, huduma ya mafunzo imeendelea kuwa miongoni mwa mambo muhimu yaliyoshughulikiwa na Baraza katika mwaka huu wa fedha. Mafunzo yafuatayo yalitolewa:-

 

·        Matengenezo na ujenzi wa barabara kwa kutumia nguvu kazi (labour based technology) yalitolewa kwa wahandisi na mafundi 21 wa mradi wa kilimo wa “Participatory Irrigation Development Programme (PIDP)” na pia kwa makandarasi 6 wa Wilaya ya Muheza.

·        Kanuni za zabuni na mikataba ya ujenzi yalitolewa kwa wahandisi kutoka Halmashauri za Wilaya 29.

·        Udhibiti wa mikataba na sheria mpya ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2001 yalitolewa kwa makandarasi 30 na wahandisi 18 wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

·        Baraza lilishiriki katika kutoa mafunzo kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi juu ya sheria mpya ya Manunuzi ya Umma. Mafunzo haya yaliandaliwa na Wizara ya Fedha.

·         Tathmini za zabuni (tender evaluation), ukaguzi wa kiufundi (technical audit), mambo ya kisheria yahusuyo zabuni na mikataba na masuala ya madai katika kandarasi za ujenzi kwa washiriki wapatao 140.

·        Matengenezo na ujenzi wa barabara kwa Kanda ya Kati na Nyanda za Juu Kusini yameendelea kutolewa kwa makandarasi 32. Zabuni na usimamizi wa mikataba ya ujenzi yalitolewa kwa wahandisi 30 wa TANROADS wa mikoa ya Iringa na Ruvuma.

 

58.          Mheshimiwa Spika, Baraza limepiga hatua kubwa katika kuanzisha Mfuko wa Fedha wa Maendeleo ya Sekta ya Ujenzi.  Mfuko huu umeshaanzishwa na Kamati ya Uendeshaji imeshateuliwa.  Mfuko huu unategemewa kutoa huduma za dhamana na ukopeshaji wa fedha kwa walengwa ambao ni wadau wote wa Sekta ya Ujenzi.

 

59.          Mheshimiwa Spika, nafurahi kulitangazia Bunge lako kwamba Baraza lilitoa huduma za ushauri zipatazo 34 ikiwa ni pamoja na usuluhishi wa migogoro mitano. Aidha Baraza limetengeneza miongozo ya taratibu za zabuni kwa miradi ya Wizara za Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Kilimo – Mradi wa Programu ya kilimo (Agricultural Sector Programme Support).

 

60.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2002/2003 Baraza litaendelea kutoa Huduma za Ushauri wa Kiufundi kwa wateja wake kuhusiana na tathmini za zabuni, uteuzi wa washauri, utayarishaji wa makabrasha ya zabuni, madai, usuluhishi wa migogoro, usimamizi wa miradi na uchapishaji wa majarida.

 

BODI YA TAIFA YA USIMAMIZI WA VIFAA (NBMM)

 

61.          Mheshimiwa   Spika, Bodi ya Taifa ya Usimamizi wa Vifaa (National Board for Materials Management – NBMM) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na 9 ya mwaka 1981 kwa lengo la kukuza na kuendeleza taaluma ya Ugavi. Bodi katika kutekeleza majukumu yake hutoa miongozo mbalimbali, mafunzo na ushauri wa kitaalamu kwenye taaluma ya Ugavi, aidha huratibu mafunzo na kuendesha mitihani ya taaluma ya Ugavi. Bodi pia, husimamia na kudhibiti mienendo ya wataalamu wafanyao kazi za Ugavi kupitia njia ya usajili, ambapo hadi mwezi Juni 2002 wataalamu wapatao 1,379 wameshasajiliwa na Bodi.

 

62.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa 2001/02 Bodi imefanya ukaguzi katika sehemu mbalimbali za kazi kwenye Serikali na Taasisi zake pia Mashirika mbalimbali ya Umma na binafsi kwa mikoa ya Dar es salaam na Mbeya kwa madhumuni ya kuwaelimisha na kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Bunge Namba 9, ya mwaka 1981. Aidha katika ukaguzi huo Waajiri walitakiwa kuajiri Wataalamu wenye sifa katika fani ya Ugavi na ununuzi na kusisitiza juu ya uzingatiaji wa miiko ya maadili (ethical code of conduct) ili kuepuka hasara kwa Taasisi na Mashirika hayo na Taifa kwa ujumla kutokana na ununuzi usiokuwa wa kitaalamu.  Bodi imepanga kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka utekelezaji wa sheria hiyo. Kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha Bodi imesajili wataalamu wapya wapatao 220, pia ni azma ya Bodi kuwafutia usajili wataalamu watakaobainika kukiuka miiko ya maadili ya taaluma. Katika kipindi hiki Bodi haikuwasajili waombaji wawili waliokuwa na vyeti vya kughushi na wamefikishwa kwenye vyombo vya dola kujibu mashtaka hayo. Aidha, Bodi imetahini watahiniwa 1996 katika ngazi mbalimbali za taaluma, kati yao watahiniwa 502 sawa na asilimia 25.1 walifaulu mitihani yao, 42 wamefutiwa matokeo ya mitihani yao kutokana na kukiuka taratibu na kanuni za mitihani na waliosalia ama wanarudia mtihani au baadhi ya masomo. Hadi kufikia Juni 2002 jumla ya watahiniwa 10,108 sawa na asilima 40.6 ya watahiniwa wote 24,896 wamefuzu mitihani yao katika ngazi mbalimbali.

 

63.          Mheshimiwa Spika, Bodi imeanza kufanya marekebisho makubwa katika mtaala wa kufundishia ili kwenda na wakati. Aidha Bodi inaandaa utaratibu utakaowezesha kuimarisha kitengo cha Ushauri na Utafiti wa kitaalamu (Research and Consultancy Unit) ili kuboresha ushauri unaotolewa kwenye Serikali na Taasisi zake hasa katika masuala yote yanayohusiana na shughuli za Ugavi.

 

64.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2002/03, Bodi imeweka majukumu yafuatayo kwa ajili ya utekelezaji:-

 

·    Kusajili wataalam 200 na kuwatahini watahiniwa 2,500 katika ngazi mbalimbali.

·    Kwa kushirikiana na Waajiri, kuwachukulia hatua mbalimbali za kinidhamu Wataalamu wote watakaobainika wanakiuka miiko ya maadili ya taaluma, kusababisha matumizi mabaya ya fedha katika ununuzi na utunzaji vifaa, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi katika njia ya uwazi na ukweli na kupambana na rushwa.

·    Kuendelea kutoa mafunzo kwa njia ya warsha na makongamano juu ya umuhimu wa matumizi ya njia bora za kisasa katika ununuzi na ugavi.

·    Kuendelea na ukaguzi na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola Waajiri na Wataalamu mbalimbali Serikalini, kwenye Taasisi na Mashirika ya Umma na binafsi wanaoajiri Wataalam ambao hawajasajiliwa na Bodi. Ukaguzi huo utahusu mikoa yote ya Tanzania bara.

·    Kufanya marekebisho katika mtaala wa kufundishia kwa lengo la kupata wataalamu wenye sifa na upeo mkubwa zaidi hasa wakati huu wa utandawazi na mabadiliko ya tekinolojia.

·    Kushirikiana na Bodi zingine pamoja na taasisi mbalimbali katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayoathiri utendaji bora wa wataalamu wa ugavi.

·    Kuendelea kuwaelimisha waajiri juu ya namna bora za utunzaji na usimamizi wa vifaa na uwekaji sahihi wa kumbukumbu za manunuzi, pia taratibu bora za ununuzi.

·    Kubuni mbinu mbalimbali za kuwezesha kuongeza idadi ya wanaofaulu mitihani kwa kiwango kikubwa zaidi.

 

BODI YA USAJILI WA WAHANDISI (ERB)

 

65.          Mheshimiwa Spika, majukumu ya Bodi hii ni pamoja na kusajili, kuendeleza ubora na kudhibiti mwenendo wa kitaaluma wa Wahandisi na Makampuni ya ushauri wa kihandisi.  Aidha katika kipindi cha mwaka 2001/02 Bodi ya Usajili wa Wahandisi imetekeleza yafuatayo:-

·        Hadi mwishoni mwa Juni 2002, Bodi ilikuwa imesajili Wahandisi 447 na Makampuni ya ushauri wa kihandisi 13, hivyo kufanya idadi ya Wahandisi waliosajiliwa nchini kufikia 4,435 na Makampuni ya ushauri wa kihandisi kufikia 84 yakiwemo makampuni 20 ya kigeni.

·        Bodi ilitembelea mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mbeya Ruvuma, Kilimanjaro na Arusha ili kukagua shughuli za kihandisi viwandani, kwenye miradi na mashirika ya Umma.

·        Bodi iliandaa mitihani ya kitaalamu kwa ajili ya kuwapandisha daraja “Technician Engineers” kufikia kiwango cha “Professional Engineers”. Jumla ya Technician Engineers 58 walifanya mitihani hiyo na watahiniwa 35 kufaulu.

·        Bodi imechapisha majarida, kuandaa miongozo ya mafunzo kwa vitendo (Internship) kwa fani 11 za uhandisi, mihadhara ya kitaalam (Professional Lectures) na kozi fupi za ujenzi.

 

66.          Mheshimiwa Spika, Bodi imewafuta kwenye orodha Wahandisi 189 na Makampuni mawili (2) ya ushauri wa kihandisi kutokana na kukiuka miiko ya taaluma hii. Narudia wito wangu wa siku zote kwamba wataalamu wote wa Sekta ya Ujenzi lazima watekeleze kazi zao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za taaluma husika. Huu ni msingi muhimu wa kujenga na kuendeleza wazalendo.

 

67.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2002/03 Bodi inakusudia kufanya yafuatayo:

·        Kuendelea kusajili Wahandisi.

·        Kuhakikisha kuwa Wahandisi wote wa kigeni pamoja na Makampuni ya kigeni ya ushauri wa kihandisi yanayofanya kazi katika miradi iliyofadhiliwa na nchi zao wanasajiliwa na Bodi.

·        Kutoa mafunzo kwa vitendo (internship) kwa wahandisi wanaomaliza mafunzo yao vyuoni.

·        Kuendelea kuuelimisha Umma juu ya athari za kutumia wataalam wasio na sifa za kihandisi.

·        Kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara juu ya mienendo na shughuli za kihandisi.

·        Kuendeleza mikakati ya kupambana na rushwa katika fani ya uhandisi.  

 

BODI YA USAJILI WA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI (AQSRB)

 

68.          Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2001/02 Bodi ya AQSRB ilipanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-

 

·        Kuendelea kusajili Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi.

·        Kuendeleza kuimarisha ukaguzi katika maeneo ya ujenzi

·        Kuendelea kuhamasisha watu wote waone umuhimu wa kutumia Wataalam waliosajiliwa na Bodi.

·        Kushirikiana na Serikali, Bodi nyinginezo na Taasisi mbalimbali katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoathiri utendaji bora wa kazi katika sekta ya ujenzi.

 

 

 

69.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2001/02 Bodi ilifanya ukaguzi katika maeneo ya Ujenzi katika mikoa 13 ambayo ni: - Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Pwani, Singida, Mbeya, Kagera na DSM. Katika ziara hii, pamoja na ukaguzi, Bodi iliwakumbusha Wajenzi umuhimu wa kufuata sheria Aidha Bodi, iliendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusu umuhimu wa kutumia wataalam waliosajiliwa na Bodi.

 

70.          Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa Juni 2002, Bodi ilikuwa imeshasajili jumla ya wataalam 270 katika fani za Wabunifu Majengo (Wazalendo) 133, Wakadiriaji Majenzi (Wazalendo) 83, Wabunifu Majengo (Wageni) 41 na Wakadiriaji Majenzi (Wageni) 13. Aidha, makampuni 95 yalikuwa yamesajiliwa na yanafanya kazi. Katika mwaka huo huo wataalam 92 waliomba kufanya mitihani na 81 walitahiniwa. Ili kuimarisha nidhamu ya wataalam waliosajiliwa Bodi iliwafutia usajili wataalam wake kumi(10) na kampuni moja.

 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002/03 Bodi itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwa ni pamoja na :

·        Kusajili wataalam wapya

·        Kufanya ukaguzi wa maeneo ya majenzi

·        Kusimamia kwa makini sheria Na. 16 ya mwaka 1997 pamoja na taratibu zake

·        Kuendelea kuuelimisha Umma kuhusu umuhimu wa kutumia Wataalam wa majenzi katika kazi za ujenzi

·        Kuboresha utaratibu wa mitihani ya Bodi

·        Kuanzisha maktaba kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za rejea na habari nyingine muhimu kwa wataalam.

·        Bodi itatoa miongozo ya mara kwa mara, yenye lengo ya kufafanua na kuelekeza mfumo wa utendaji kazi za kila siku za kitaalam.

·        Bodi itaendelea na mpango wa kutayarisha Sheria ya Majengo ambayo itakuwa sheria mama.

·        Kuanzisha mpango wa Elimu Endelevu (CPD) ambao lengo lake kuu ni kuwanoa wataalam waliosajiliwa.

 

 

BODI YA USAJILI WA MAKANDARASI (CRB)

 

 

71.          Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria ya Bunge Na. 17 ya mwaka 1997, Bodi ya Usajili wa Makandarasi ina jukumu la kusajili Makandarasi wa aina zote za ujenzi. Aidha Bodi inawajibika kuhakikisha kwamba Makandarasi wote wanasajiliwa baada ya kuthibitisha kuwa wana sifa, uwezo wa kitaalam na fedha za kufanyia kazi za ujenzi katika madaraja (class of registration) watakayosajiliwa. Aidha Bodi ina jukumu la kujenga uwezo wa Makandarasi wazalendo.

 

72.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2001/02 Bodi ilisajili Makandarasi 551 katika fani na madaraja mbalimbali na kufanya jumla ya Makandarasi waliosajiliwa kuwa 2,428.

 

73.          Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu lake la msingi, Bodi ilifanya ukaguzi katika miradi ya ujenzi 160 na kutathmini utendaji wa Makandarasi katika miradi hiyo.  Hadi mwishoni mwa Juni 2002, Bodi ilifuta makandarasi 301 na kufanya jumla ya Makandarasi waliofutwa tangu mwaka 1998 kwa kushindwa masharti ya sheria na utendaji mbaya wa kazi kuwa 1,195.  Aidha Bodi imepeleka Makamani Kampuni 20 zilizofanya kazi ya Ukandarasi bila kusajiliwa na Bodi.

 

74.          Mheshimiwa Spika, kama nilivyokuwa nalieleza Bunge lako Tukufu, Bodi ya kusajili Makandarasi ina jukumu kubwa la kujenga uwezo wa Makandarasi wazalendo. Bodi imeshaendesha warsha 16 kwa kushirikisha Makandarasi 2,423.  Katika mwaka 2001 Bodi ilitekeleza Mpango wake wa Mafunzo Endelevu (Sustainable Structured Training Programme – SSTP).  Kozi 10 zimeshafanyika na Makandarasi 291 wameshiriki katika mafunzo mbalimbali ikiwemo misingi ya biashara, uandaaji wa zabuni na jinsi ya kutekeleza vema mikataba. 

 

Aidha, Bodi imeanzisha Mfuko wa kusaidia Makandarasi wadogo (daraja v ¾ vii) kwa kuwadhamini katika benki ili waweze kupewa dhamana zinazotakiwa bila kuwa na haja ya kuweka rehani kitu chochote. Kwa kuanzia mpango huu utatoa dhamana kwa ajili ya zabuni (Bid Bonds) na malipo ya awali (Advance Payment Guarantees).

 

Utaratibu huu utawawezesha Makandarasi wadogo ambao ndio wengi kupata dhamana na pesa za kuanzia kazi kwa urahisi zaidi. Vile vile Bodi inajenga uwezo wa uwakilishi wa Makandarasi kwa kuratibu uanzishwaji wa Chama cha Kitaifa cha Makandarasi ambao utalenga kujenga mfumo mzuri wa ushirikiano katika kutatua matatizo yanayowakabili Makandarasi.

 

75.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2002/03 Bodi itaendelea kusajili, kuratibu na kujenga uwezo wa Makandarasi kwa kufuata sheria.  Lengo ni kuwa na Makandarasi wa Tanzania wenye uwezo kimitambo, ujuzi, mtaji, wanaozingatia sheria, usalama, kanuni na maadili ya ujenzi ili kulinda haki na usalama wa watumiaji wa Makandarasi hapa nchini na kufanya kazi nzuri kwa muda uliopangwa.

 

UBINAFSISHAJI WA PEHCOL

 

76.          Mheshimiwa Spika, PEHCOL ni Shirika la Umma lililoundwa chini ya Wizara yangu kwa madhumuni ya kuboresha upatikanaji wa mitambo na magari kwa ajili ya shughuli za ujenzi na matengenezo ya barabara.  Idara na Taasisi za Serikali na Makandarasi binafsi ambao hawana uwezo wa kununua mitambo hutumia mitambo na magari kutoka kwenye Shirika hili kwa kukodi.

 

Mheshimiwa Spika, kama nilivyolieleza Bunge lako Tukufu katika Hotuba yangu ya mwaka 2001/2002, taratibu za kuibinafsisha PEHCOL bado zinaendelea chini ya PSRC.

 

MAENDELEO YA WATUMISHI

 

77.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2001/02 Watumishi 511 wa kada mbalimbali wamepandishwa vyeo, 80 wamethibitishwa kazini na 6 wameajiriwa. Wizara yangu itaendelea na zoezi hili kwa Watumishi watakaostahili kutokana na miundo ya Utumishi ya kada zao. Katika mwaka wa fedha 2001/02 Watumishi 40 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na Watumishi 222 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali. Lengo la kuwapatia mafunzo Watumishi ni kuwaongezea ujuzi na ufanisi katika kazi zao. Wizara yangu itaendelea na juhudi za kuwapatia mafunzo zaidi Wafanyakazi wake katika mwaka wa fedha 2002/03.

 

78.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2001/02 Wizara yangu imeunda na kuzindua rasmi Baraza la Wafanyakazi tarehe 06/05/2002 ambalo limeshajadili na kupitisha Miundo ya Utumishi ya Kada zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi.

 

79.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2002/03 Wizara yangu itaendeleza azma yake ya kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wake. Aidha, Watumishi 293 wa kada mbalimbali watapata mafunzo ya ndani katika fani mbalimbali.  Watumishi 1,247 watapandishwa vyeo.

 

80.          Mheshimiwa Spika, kutokana na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ni muhimu Watumishi wote hasa viongozi wakuu wawe na elimu ya kompyuta.

 

 

 

 

MIKAKATI YA KUPAMBANA NA UKIMWI

 

81.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imechangia juhudi za Kitaifa za kupambana na kudhibiti maambukizo ya ukimwi.

 

Katika kipindi cha mwaka 2001/02 Wizara ilizindua rasmi mkakati wa kupambana na ukimwi katika Wizara ya Ujenzi Makao Makuu na Mikoani.

 

Aidha, Wizara imeanzisha kitengo maalum cha kubuni, kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mikakati ya kupambana na ukimwi kwa watumishi wake na wananchi kwa ujumla waliopo kwenye maeneo ambayo shughuli za ujenzi zinaendelea.  Ni matarajio yetu kuwa mkakati tulioanzisha wa kupambana na ukimwi utasaidia kwa kiwango kikubwa kudhibiti maambukizo ya ugonjwa wa ukimwi.

 

VITA DHIDI YA RUSHWA

 

82.          Mheshimiwa Spika, kama nilivyolieleza Bunge lako Tukufu katika Hotuba yangu ya mwaka 2001/02, Watumishi wa kada mbali mbali wakiwemo Wahandisi, Makandarasi, Wabunifu Majengo, Wakadiriaji Majenzi, Wahandisi Washauri, Wahasibu na kadhalika walihudhuria Semina juu ya kupiga vita rushwa katika Sekta ya Ujenzi.  Aidha kutokana na Semina hiyo wajumbe walitoa maazimio ya mikakati ya kupiga vita rushwa katika Sekta ya Ujenzi ambayo Wizara yangu inaendelea kuyatekeleza.

 

Mheshimiwa Spika, kama njia mojawapo ya kupiga vita rushwa, Wizara yangu inatekeleza kikamilifu Sheria Na. 3 ya mwaka 2001 (Public Procurement Act. No. 3) ambayo inapunguza sana mianya ya rushwa katika utoaji zabuni za ujenzi, ushauri na ununuzi wa vifaa.

 

Vile vile katika kupunguza rushwa kwenye vituo vya Mizani, Wizara inabadilisha mizani ya kizamani na kuweka mipya ambayo inatumia kompyuta na imeongeza idadi ya mizani inayohamishika (Portable Weigh Bridges).  Aidha, Wizara yangu inaelimisha Umma matumizi bora ya barabara na haki za watumiaji barabara kwa njia ya vipeperushi na matangazo magazetini.

 

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa usimamizi wa ubora wa kazi za barabara Wizara imeimarisha maabara ya vifaa vya ujenzi mikoani na kusisitiza matumizi yake katika kudhibiti ubora wa kazi.  Pia Wizara inashirikiana na Idara ya Ukaguzi (Technical Audit) ya Wizara ya Fedha katika kukagua miradi inayoendelea na iliyokamilika.

 

HITIMISHO

 

83.          Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha eleza hapo awali, Wizara yangu inatekeleza malengo yake kwa kutumia Bajeti ya Serikali, kushirikiana na wananchi pamoja na misaada ya Wahisani mbalimbali. Napenda nitumie nafasi hii kuzishukuru Serikali za nchi za Denmark, Finland, Italia, Japan, Kuwait, Marekani, Norway, Saudi Arabia, Switzerland, Uholanzi, Uingereza na Ujerumani ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia sana sekta ya Ujenzi.  Pia nayashukuru mashirika ya kimataifa ya ADB, EU, IDA na Mfuko wa Maendeleo wa OPEC kwa kuendelea kusaidia sekta ya ujenzi. Jitihada zao wote zimechangia katika mafanikio na maendeleo ya Wizara yangu. Tunawashukuru sana kwa msaada wao.

 

84.          Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kuishukuru tena Kamati ya Bunge ya Miundo Mbinu chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Prof. Daimon Mwaga, Mbunge wa Kibakwe, kwa ushauri mzuri waliotupa katika kuandaa bajeti hii. Nawashukuru pia viongozi wenzangu katika Wizara ya Ujenzi ambao ni Naibu Waziri, Mheshimiwa Hamza Mwenegoha (Mb), Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Katibu Mkuu, Eng. John Kijazi, Mwenyekiti wa RFB Mama Mang’enya, Wenyeviti wa Bodi za NCC, CRB, ERB, AQSRB, NBMM na PEHCOL.  Aidha, nawashukuru Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Wakala zote zilizo chini ya Wizara yangu pamoja na Wahandisi na Watendaji wote wa Wizara.

 

Makadirio ya Bajeti ya Wizara 2002/03

 

85.   Mheshimiwa Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na malengo yake ya mwaka 2002/03, naliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe Bajeti ya jumla ya Shilingi 221,365.084 milioni ambapo kati ya hizo Shilingi 88,873.763 milioni ni za hapa na Shilingi 132,491.321 milioni ni za nje.

Fedha za hapa zinajumuisha:

 

(i)    Shilingi 45,278.80 milioni za Mfuko wa Barabara ambapo Shilingi 40,154.866 milioni ni kwa ajili matengenezo ya barabara, Shilingi 4,449.67 milioni ni kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa barabara Kuu na za Mikoa na Shilingi 674.27 milioni ni kwa ajili ya gharama za usimamizi na uendeshaji Bodi ya Mfuko wa Barabara.

(ii)   Shilingi 9,075.96 milioni kwa ajili ya mishahara (Personal Emoluments) na matumizi mengineyo (Other Charges).

(iii)  Shilingi 22,000.0 milioni kwa ajili ya mradi maalum wa barabara kuu (Special Trunk Roads Project).

(iv)  Shilingi 12,519.0 milioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Barabara Kuu na za Mikoa.

 

Fedha za nje zinajumuisha:

 

(i)    Shilingi 121,200.9 milioni za miradi ya maendeleo ya Barabara Kuu na za Mikoa.

(ii)   Shilingi 11,291.047 milioni za matengenezo ya Barabara Kuu na za Mikoa.

 

85.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

 

Viambatisho

Kiambatisho 1

Kiambatisho 2A, 2B

Kiambatisho 3

Kiambatisho 4

Kiambatisho 5

Kiambatisho 6, 6B

Kiambatisho 7, 7A na 7B, 7C na 7D, 7E, 7F na 7G, 7H, 7I, 7J, 7K, 7L, 7M, 7N

Kiambatisho 8