MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

SUALA MAALUM KATIKA MAENDELEO    
             

UHUSIANO KATI YA MWENENDO WA UCHUMI

JUMLA NA HALI YA UMASKINI


Utangulizi

161. Kwa zaidi ya miongo miwili sasa, Tanzania imekuwa ikifanya mabadiliko makubwa katika kuendesha uchumi jumla na kuboresha sekta za huduma za jamii. Mabadiliko haya yametokana na hali mbaya ya kiuchumi na jamii iliyoikumba nchi mwishoni wa miaka ya sabini na mwanzoni wa miaka ya themanini. Sababu za hali mbaya ya uchumi na huduma za kijamii mwanzoni wa miaka ya themanini ni kutokana na udhaifu wa sera na uendeshaji uchumi wa taifa pamoja na sababu nyingine zilizokuwa nje ya uwezo wake.

162. Hata hivyo, tangu mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yamefanywa hadi sasa yameiwezesha Tanzania kupata mafanikio makubwa katika maendeleo ya uchumi jumla kama vigezo vya uchumi jumla vinavyoonyesha. Pato la Taifa kwa wastani limekuwa likikua kwa asilimia 4.8 toka mwaka 1990 hadi sasa na mwaka 2002, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.2. Kasi ya upandaji bei imekuwa ikishuka toka asilimia 30 miaka ya tisini hadi chini ya asilimia 4.5 mwishoni mwa mwaka 2002. Kwa sababu ya mabadiliko ya kiuchumi, masoko yanafanya kazi kwa ufanisi na mapato ya serikali yameongezeka mara nne zaidi katika kipindi cha miaka saba mfululizo toka sh. 25 bilioni mwaka 1995 hadi sh. 100 bilioni mwaka 2002. Uwiano wa uwekezaji vitega uchumi na Pato la Taifa uliongezeka toka asilimia 14.8 mwaka 1997 hadi asilimia 17.4 mwaka 2001 na vitega uchumi toka nje ya nchi pekee viliongezeka toka dola za Marekani 20 milioni mwaka 1994 hadi kufikia dola za Marekani 327.2 milioni mwaka 2001. Akiba ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagizia bidhaa nje iliongezeka kutoka mwezi mmoja na nusu mwaka 1995 hadi kufikia karibu miezi 9 mwaka 2002. Kutokana na mafanikio hayo, ushirikiano kati yetu na wafadhili umeongezeka na kupelekea kuongezeka kwa misaada na kupata unafuu katika mzigo wa madeni.

163. Wakati viashiria mbalimbali vya uchumi vinaonyesha ukuaji mzuri na mafanikio makubwa ya uchumi jumla kufuatia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, baadhi ya watu nchini wanahoji kwamba maisha ya Mtanzania wa kawaida yameendelea kuwa duni na umaskini umezidi kuongezeka. Lengo la sura hii ya kitabu ni kujaribu kuhusisha mafanikio ya vigezo vya uchumi jumla na hali ya umaskini nchini.

MAPITIO YA MWENENDO NA MABADILIKO YA UCHUMI

164. Tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, uchumi wetu umepitia katika sera kuu mbili za kiuchumi na kijamii. Kuanzia mwanzoni mwa miaka ya sitini hadi kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967, mfumo wa uchumi ulikuwa ule uliorithiwa kutoka kwa wakoloni na ulioendeleza soko huria na sekta binafsi. Baada ya Azimio la Arusha, sera ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ilifuatwa ambayo ilikuwa na malengo ya kuweka njia kuu za uzalishaji mali na huduma chini ya umma. Sekta ya umma ilichukua uongozi wa uendeshaji uchumi na kupelekea huduma za msingi za kijamii kutolewa bure kwa wote. Uchumi ulitegemea zaidi uzalishaji katika sekta ya kilimo, ambayo ilichangia kwa wastani wa asilimia 50 ya Pato la Taifa. Nchi ilishuhudia ukuaji mzuri wa uchumi na kwa ujumla kiwango cha ukuaji uchumi kilikua karibu asilimia 5, kutoka katikati ya miaka ya sitini hadi mwanzoni mwa miaka ya sabini. Katika kipindi hiki Tanzania ilifanikiwa kuimarisha na kuboresha hali za maisha ya kijamii.

Sababu za Mabadiliko ya Sera za Kiuchumi

165. Mfumo wa uwekaji wa shughuli zote za uchumi na jamii chini ya dola, kama vile uwekezaji mkubwa wa fedha za taifa katika mashirika ya umma, uhamishwaji wa watu vijijini, ukiritimba wa kuhodhi na uendeshaji mbaya wa uchumi, pamoja na hali mbaya ya hewa, upandaji wa bei ya mafuta miaka ya sabini, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kushuka kwa bei za mazao ya wakulima kwenye soko la kimataifa na vita vya Kagera vilisababisha mwishoni mwa miaka ya sabini kuyumba kwa uchumi. Matatizo ya kiuchumi na kijamiii yalifikia hali mbaya sana mwanzoni mwa miaka ya themanini kusababisha serikali kupunguza juhudi zake katika kutoa huduma za msingi kwa wananchi. Kufuatia hali hiyo, mipango ya kufufua uchumi (NESP I na II) ilianzishwa kwa madhumuni ya kufufua uchumi na kuboresha hali ya maisha ya jamii kama ilivyokuwa hapo awali.

166. Mageuzi mapya ya kiuchumi na kijamii yalianza katikati ya miaka ya themanini (Economic Recovery Programme, ERP 1986). Sekta binafsi ilianza kuchukua nafasi ya sekta ya umma katika kuendesha uchumi hivyo kuondokana na uchumi uliotawaliwa na kumilikiwa na umma kwenda kwenye mfumo wa uchumi huria. Madhumuni hasa yalikuwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na pato la uuzaji nje ya nchi kutokana na bidhaa za biashara. Mabadiliko yalikuwa ni pamoja na: kuhakikisha bei huru za bidhaa, kuondoa ruzuku za serikali katika uzalishaji, kuongeza uzalishaji viwandani, kupunguza nakisi ya urari wa biashara, kupunguza kasi ya upandaji bei, kupunguza nakisi ya mapato na matumizi ya serikali, kuongeza fedha za kigeni na kuboresha huduma za kijamii. Kufuatia mageuzi ya kiuchumi na kijamii, hadi mwanzoni mwa mwaka 1995, Tanzania ilianza kufanikiwa kurejesha hali yake ya kuwa na uchumi imara na endelevu, sambamba na kuongezeka kwa mapato ya serikali, kudhibiti kasi ya upandaji bei, ukuaji endelevu wa Pato la Taifa, kupungua kwa viwango vya riba, viwango imara vya ubadilishaji fedha, na kupungua kwa nakisi ya mapato na matumizi ya serikali katika bajeti. Mageuzi zaidi ya kiuchumi na kijamii yamekuwa yakiendelea kutekelezwa nchini. Mageuzi hayo ni pamoja na: ubinafsishaji wa mashirika ya umma; mageuzi ya sekta ya fedha; urekebishaji wa mfumo wa kodi; mabadiliko katika sheria za uwekezaji; mageuzi ya sekta ya umma na mageuzi mengine katika sekta mbalimbali za uchumi na jamiii.


Mafanikio ya Vigezo vya Uchumi Jumla

Ukuaji wa Pato la Taifa

167. Mara baada ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kufufua uchumi, ukuaji wa uchumi ulianza kuimarika katika kipindi cha mwaka 1986 hadi 1996. Katika kipindi hicho, uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 3.0. Kuanzia kipindi cha mwaka 1997 hadi 2002, Pato la Taifa liliendelea kukua kutoka asilimia 3.3 hadi kufikia asilimia 6.2 mwaka 2002. Ukuaji huo endelevu ulichangiwa na uzalishaji mzuri katika sekta za kilimo, viwanda, biashara (ikijumuisha utalii), na madini. Wastani wa pato kwa kila mwananchi uliongezeka kutoka sh. 147,134 mwaka 1997 hadi sh. 256,490 mwaka 2002. Sekta ya kilimo ambayo inatoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa, pamoja na kutegemea hali ya hewa na matatizo ya kiutendaji, iliendelea kukua kutoka ukuaji wa asilimia 2.4 mwaka 1997 hadi asilimia 5.5 mwaka 2001.

Mwenendo wa Bei

168. Kasi ya upandaji bei kama kiashiria cha ukuaji imara wa uchumi, iliendelea kushuka kutoka wastani wa asilimia 21.0 mwaka 1996 hadi wastani wa asilimia 4.5 mwaka 2002. Kasi hii ya ushukaji imechangiwa kwa kiasi kikubwa na upatikanaji na ugavi mzuri wa chakula, na sera za makusudi za serikali katika kudhibiti mwenendo wa mapato na matumizi ya serikali na ujazi wa fedha nchini.

Mapato na Matumizi ya Serikali

169. Juhudi za serikali katika kukusanya mapato zimezidi kuongezeka kwa kukusanya zaidi ya sh. 100 bilioni kwa mwezi ikilinganishwa na sh. 25 bilioni kwa mwezi mwaka 1995. Kuongezeka kwa ukusanyaji mapato kunatokana na uboreshaji wa ukusanyaji kodi na kupungua kwa mianya wa ukwepaji kodi. Kwa upande wa matumizi, serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa matumizi yake kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Fedha kwa ajili ya kudhibiti matumizi (Integrated Financial Management System - IFMS) na kuanzishwa kwa Mfumo wa Muda wa Kati wa Matumizi ya serikali (MTEF) na matumizi kulingana na mapato ya ndani (cash budget system). Mfumo wa MTEF unatoa kipaumbele katika sekta muhimu za maendeleo kiuchumi na kijamii. Pamoja na kuongezeka kwa ukusanyaji mapato ya ndani, uwiano wa mapato ya ndani kwa Pato la Taifa ulipungua kutoka asilimia 13.2 mwaka 1995/96 hadi asilimia 12.2 mwaka 2001/02, wakati uwiano wa matumizi kwa Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 13.1 mwaka 1995/96 hadi asilimia 19.0 mwaka 2001/02.


Ujazi wa Fedha, Karadha na Akiba ya Fedha za Kigeni

170. Katika kipindi chote cha mageuzi ya uchumi, ujazi wa fedha uliendelea kuimarika kutoka asilimia 26.1 mwaka 1995/96 hadi asilimia 12.3 mwaka 2001/02. Lengo ni kuwa na ujazi wa fedha wenye kuendana na ukuaji wa uchumi. Wastani wa riba za amana na mikopo unaotolewa na mabenki ya biashara kuanzia mwaka 1997 hadi 2002, ulionyesha ifuatavyo: viwango vya riba za amana viliendelea kupungua kutoka asilimia 12.0 mwaka 1995/96 hadi asilimia 3.1 mwaka 2002/03. Kiwango hiki ni cha chini mno katika kuchochea uwekaji amana. Aidha, kiwango cha riba ya mikopo kilipungua kutoka asilimia 28.0 mwaka 1995/96 hadi asilimia 15.7 mwaka 2002/03. Kwa upande wa akiba ya fedha za kigeni (foreign exchange reserves), akiba iliendelea kuongezeka kutoka miezi 3.8 ya uagizaji nje mwaka 1997 hadi miezi 8.9 mwaka 2002.

Deni la Taifa

171. Deni la Taifa ni miongoni mwa vigezo vinavyochangia kuwepo kwa uchumi thabiti na endelevu. Kiwango cha deni kina athari katika bajeti ya serikali. Hadi kufikia mwaka 2001/02 Deni la Taifa lilifikia dola 7,482.1 milioni kutoka dola 7,754.1 milioni mwaka 1995/96. Hali hii inaonyesha kuwa Deni la Taifa limepungua kwa asilimia 3.5 katika kipindi cha mwaka 1995/96 hadi 2001/02. Kupungua kwa Deni la Taifa kunawezesha fedha zaidi za matumizi ya serikali kuelekezwa katika maeneo muhimu ya uzalishaji na utoaji huduma bora za jamii.

172. Kama viashiria vya uchumi jumla vinavyoonyesha, Tanzania imepata mafanikio makubwa na yakuridhisha katika mageuzi yake ya kiuchumi na jamii ambayo imekuwa ikiyatekeleza kwa takribani miongo miwili sasa. Serikali na wahisani wanahisi mabadiliko na mafanikio haya yameleta maendeleo na manufaa kwa wananchi wote na yataendelea kuleta mafanikio makubwa zaidi siku za mbeleni hivyo hayana budi kuendelezwa. Wakati hivyo ndivyo inavyoonekana na wengi, bado kuna malalamiko kwamba mabadiliko na mafanikio haya hayajamsaidia mwanachi wa kawaida kwani hali duni na umaskini umekuwa ukiongezeka miongoni mwa wananchi wengi. Kabla ya kuhusisha mafanikio haya ya uchumi jumla na hali ya umasikini nchini, ni vyema kutazama kwa ufupi hali halisi ya umaskini Tanzania.

HALI YA UMASKINI NCHINI

173. Mikakati mbalimbali iliainishwa na serikali katika kupambana na umaskini tangu uhuru. Katika kipindi cha 1967 hadi 1983, serikali ilikuwa ikifuata siasa ya ujamaa na kujitegemea yenye lengo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuongeza ubora wa maisha kwa walio wengi. Njia kuu za uchumi ziliwekwa chini ya umma kwa lengo la kugawa kwa ufanisi rasilimali za taifa. Huduma muhimu za jamii kama vile maji, afya, elimu nk zilitolewa bure kwa wananchi. Pia ajira ziliongezeka, na vyama vya ushirika/bodi za mazao zilirahisisha uuzaji wa mazao ya wakulima. Mageuzi ya kiuchumi yaliyotekezezwa katika kipindi cha kuanzia miaka ya 1986 hadi sasa yalikuwa na lengo la kuinua kipato cha watu maskini. Katika kufanikisha hili, Dira ya Taifa ya maendeleo 2025 iliandaliwa na kuainisha malengo mbali mbali ya kimaendeleo ikiwemo mikakati ya kupambana na umaskini uliokithiri nchini. Mikakati hii iliandaliwa kwa dhamira ya kuwezesha ukuaji wa uchumi na kuinua kipato cha wananchi walio wengi hususan wale waishio maeneo ya vijijini. Mikakati hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kupunguza Umaskini; Mkakati wa Maendeleo Vijijini; na Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo.


174. Aidha, kumekuwepo na jitihada nyinginezo katika kukabiliana na umaskini ikiwa pamoja na kuanzishwa kwa mifuko mbalimbali kusaidia upatikanaji wa zana na pembejeo muhimu za uzalishaji, ununuzi wa mazao, usindikaji, uhifadhi, vifungashio na upatikaji wa teknolojia ya kisasa. Mifuko iliyoanzishwa ni kama Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (Agricultural Input Trust Fund), Mfuko wa Kusaidia Sekta Binafsi katika Kilimo, na Mfuko wa Wafanyabishara Wadogo, na Mfuko wa Jamii.

175. Sera ya Viwanda Vidogo na vya Kati (SME’s) imeweka msukumo katika viwanda ambavyo ni rahisi kumilikiwa na kuendeshwa na Watanzania wenyewe bila kuhitaji misaada ya kiufundi na mitaji kutoka nje ya nchi, hususan katika usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo ili kuwa na ubora unaoweza kuhimili ushindani wa masoko ya kikanda na kimataifa, kuongeza thamani na pato, kuongeza nafasi za ajira, na hivyo kuchangia katika kupambana na umaskini. Pia, Sera ya mikopo midogo (Micro Finance Policy) imeweka misingi ya uanzishwaji wa benki za ushirika na jamii, vyama vya kuweka na kukopa, na kuundwa kwa vikundi vya kijamii na asasi zisizokuwa za kiserikali. Sera hizi zimeweka mazingira yanayowezesha ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji mali.

176. Katika kuhakikisha kuwa teknologia, mitaji na masoko inapatikana kwa wawekezaji wa ndani, Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kimeanzisha zoezi la kuwatambua na kuwaendeleza wawekezaji wadogo na wakubwa wa ndani. Jumla ya wawekezaji wadogo wenye miradi 600 wametambuliwa na kusaidiwa kutayarisha taarifa muhimu za miradi.

177. Serikali imeanzisha na kuendeleza majadiliano na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara lililoanzishwa mwaka 2001 likiwa chini ya uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majadiliano yamewezesha kurekebisha mfumo wa kodi na ujenzi wa misingi ya utawala bora na kubaini vikwazo vinavyoathiri uwekezaiji na biashara na namna ya kushughulikia vikwazo hivyo. Kutokana na mikakati iliyowekwa na kuanza utekelezaji, zipo dalili za awali za kuelekea kupata mafanikio katika kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya jamii nchini.

178. Pamoja na jitihada zote hizo, umaskini bado ni tatizo kubwa kwa wananchi wa Tanzania hasa wale waishio vijijini. Matokeo ya Utafiti wa Matumizi ya Kaya (HBS) mwaka 2000/01 yanaonyesha kwamba, asilimia 18.7 ya watanzania hawawezi kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula (food poverty line) na asilimia 35.7 wanashindwa kukidhi mahitaji yao ya msingi (Basic needs poverty line). Hata hivyo kiwango cha umaskini ni kikubwa mno katika maeneo ya vijijini kuliko mijini. Kwa jumla, uwiano wa watu maskini katika miji ni asilimia 13 pekee ikilinganishwa na asilimia 87 ya wanaoishi vijijini.

Umaskini wa Kipato

179. Viashiria vya umaskini nchini vinaonyesha kuwa bado umaskini ni tatizo kubwa linalowakumba wananchi mbalimbali hususan wale wa vijijini. Kwa upande wa mahitaji ya chakula (food poverty) kiwango kimepungua kutoka asilimia 21.6 mwaka 1991/92 hadi asilimia 18.7 mwaka 2000/01 kitaifa. Kwa upande wa mahitaji muhimu kiwango kimepungua kutoka asilimia 38.6 mwaka 1991/92 hadi asilimia 35.7 mwaka 2002/03. Katika viashiria vyote viwili inaonyesha kuwa ni maeneo ya mijini tu ambako viwango hivi vya umaskini ndiyo vimepungua kwa hali ya kuridhisha, hususan Dar es Salaam.

 

 

Jedwali Na. 10.2:  VIWANGO VYA VIASHIRIA VYA UMASKINI KATIKA TANZANIA

 asilimia

Eneo

Chakula

Mahitaji yote muhimu

1991/92

2000/01

1991/92

2000/01

Dar es salaam

13.6

7.5

28.1

17.6

Miji mingine

15.0

13.2

28.7

25.8

Vijijini

23.1

20.4

40.8

38.7

Kitaifa

21.6

18.7

38.6

35.7

Chanzo: HBS 2000/01
Tofauti ya Kipato

180. Kiwango cha tofauti ya kipato kitaifa kimeongezeka kwa asilimia 0.1 kutoka asilimia 0.34 mwaka 1991/92 hadi asilimia 0.35 mwaka 2000/01. Tofauti ya kipato imeongezeka kwa kiwango kikubwa katika jiji la Dar es Salaam wakati maeneo mengine ya nchi utofauti ulikuwa ni kidogo.

 

Jedwali Na. 10.3:  KIWANGO CHA TOFAUTI YA KIPATO (GINI COEFFICIENT)

 

Eneo

Kiwango cha tofauti ya kipato

1991/92

2000/01

Dar es salaam

0.30

0.36

Miji mingine

0.35

0.36

Vijijini

0.33

0.33

Kitaifa

0.34

0.35

Chanzo:  HBS 2000/01

Ajira

181. Kiwango cha ukosefu wa ajira kiliongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 1990/91 hadi asilimia 26 mwaka 2000/01, wakati katika maeneo ya vijijini kiwango cha ukosefu wa ajira hakikubadilika. Maeneo mengine ya miji kiwango cha ukosefu wa ajira kiliongezeka kutoka asilimia 6 mwaka 1990/91 hadi asilimia 10 mwaka 2000/01. Hii inaonyesha tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa katika maeneo ya mijini. Rika ambalo linaloathirika zaidi ni vijana kati ya umri wa miaka 15 hadi 34 hasa waishio mijini.

 

Jedwali Na. 10.4:  KIWANGO CHA UKOSEFU WA AJIRA KIJINSIA KATIKA

 MAENEO MBALIMBALI

 

 

Dar es salaam

Miji mingineyo

Vijijini

1990/91

2000/01

1990/91

2000/01

1990/91

2000/01

Wanaume

11

19

4

8

2

2

Wanawake

39

35

7

15

2

2

Jumla

22

26

6

10

2

2

Chanzo: ILFS 2000/01

Umaskini Usio wa Kipato

182. Viashiria vya umaskini usio wa kipato vinaonyesha mafanikio kidogo kwa kipindi cha mwaka 1991/92 hadi mwaka 2000/01. Kwa upande wa elimu, matokeo ya Utafiti wa Matumizi ya Kaya (HBS) 2000/01, yanaonyesha kwamba, asilimia ya wanawake walio na elimu imebaki pale pale (asilimia 68 kutoka mwaka 1991/92). Umbali kutoka shule hadi anapoishi mtoto umepungua kutoka asilimia 66 mwaka 1991/92 hadi asilimia 63 mwaka 2000/01, umbali wa kutoka shule si zaidi ya kilomita 2. Kwa upande wa wasiojua kusoma na kuandika, takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa asilimia 28.6 ya idadi ya watu wote nchini hawajui kusoma na kuandika. Tatizo hili linajitokeza sana kwa upande wa wanawake (asilimia 36) kuliko wanaume (asilimia 20.4), wakati ambapo maeneo ya vijijini kiwango ni kikubwa zaidi ikilinganishwa na mijini. Uandikishaji katika shule za msingi, uliongezeka kutoka asilimia 54.2 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 65.5 mwaka 2001.

183. Kwa upande wa huduma za afya, idadi ya watu wanaopata huduma ya afya katika vituo mbalimbali imeongezeka hadi asilimia 66.6 mwaka 2000/01 wakati kaya ambazo zimo katika umbali usiozidi kilomita 6 imebaki asilimia 75 katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

 

 Jedwali Na. 10.5:  KIWANGO CHA WASIOJUA KUSOMA NA KUANDIKA

 

Wasiojua kusoma na kuandika (wanaume)

Wasiojua kusoma na kuandika (wanawake)

Jumla ya Wasiojua kusoma na kuandika

Dar es salaam

5.7

11.7

8.7

Miji mingine

8.5

19.0

14.2

Vijijini

23.9

41.2

33.1

Jumla

20.4

36.0

28.6

Chanzo: HBS 2000/01


184. Matokeo ya Utafiti wa Matumizi ya Kaya (HBS) mwaka 2000/01 yanaonyesha kuwa huduma za maji zimeimarika zaidi mijiji kuliko maeneo ya vijijini. Asilimia 86 na 76 za kaya za Dar es salaam na miji mingine zinapata maji ya bomba, wakati ni asilimia 28 ya kaya za vijijini ndizo zinazopata maji safi. Hata hivyo, asilimia ya watu wanaopata maji vijijini kutokana na vianzio visivyo salama imepungua kutoka asilimia 64 mwaka 1991/92 hadi asilimia 53 mwaka 2000/01.

185. Kwa upande wa makazi, kumekuwepo na ongezeko kubwa la makazi bora. Nyumba zisizo na sakafu za udongo zimeongezeka kutoka asilimia 21 mwaka 1991/92 hadi asilimia 26 mwaka 2000/01. Asilimia ya kaya zenye nyumba zilizo na kuta madhubuti imeongezeka kutoka 16 mwaka 1991/92 hadi kufikia asilimia 25 mwaka 2000/01. Nyumba zenye bati zimeongezeka kutoka asilimia 36 mwaka 1991/92 hadi asilimia 43 mwaka 2000/01.

186. Viashiria vya uchumi vinaonyesha mwelekeo uliotengemaa katika ukuaji wa uchumi. Licha ya mafanikio hayo, changamoto muhimu inayojitokeza katika hili ni kiwango kidogo kilichofikiwa katika kupunguza umaskini nchini hasa katika maeneo mengi ya vijijini. Ni dhahiri kuwa ukuaji wa uchumi bado ni wa kiwango kidogo katika kupunguza umaskini nchini. Mkazo zaidi unahitajika katika kuongeza uzalishaji kwenye sekta zote zenye kutoa ajira kwa watu wengi ambao ni maskini na zile zinazoonyesha ukuaji endelevu kama vile madini na utalii. Sekta binafsi ndio imekuwa mhimili wa uchumi. Kinachohitajika ni kuwepo mazingira bora ya kukuza sekta hii.

Uhusiano Kati ya Maendeleo ya Uchumi Jumla na Kupungua kwa Umaskini

187. Ukuaji wa uchumi jumla ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa taifa lolote lile. Na ni muhimu zaidi kwa mataifa yale maskini kama Tanzania kwa ajili ya kuvutia uwekezaji, kukuza biashara ya ndani na nje, kutoa nafasi za kazi, kuboresha maisha ya jamii na kupunguza umaskini. Pamoja na hayo, ukuaji wa uchumi jumla hautegemewi moja kwa moja kusababisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, isipokuwa unaweka mazingira muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na hatimaye kupunguza umaskini.

188. Kuimarika kwa bei ni kigezo kizuri cha uchumi thabiti (macroeconomic stability) katika kuwavutia wawekezaji pamoja na kuongeza uwezo wa kununua bidhaa na huduma mbali mbali kwa watu walio wengi. Kukua kwa Pato la Taifa kuna maana ya kuongezeka kwa pato la wastani la kila mtu. Kuongezeka kwa pato la wastani kwa watu inawezesha watu kujipatia mahitaji yao muhimu, kupeleka watoto shule, kujipatia huduma za afya na kuboresha afya zao, kujenga nyumba bora na kuishi katika makazi bora zaidi. Hivyo, ukuaji wa uchumi unachangia kwa kiasi kikubwa kuboreka kwa maisha ya jamii.

189. Aidha, ukuaji wa Pato la Taifa unasaidia kuongezeka kwa shughuli za kibiashara. Kutokana na kuongezeka kwa biashara, mapato ya serikali yanaongezeka kupitia kodi zinazokusanywa kutoka katika makampuni/mashirika na shughuli mbalimbali za watu. Mapato ya serikali yakitumika vizuri katika kuboresha miundo mbinu ya kiuchumi na kijamii hasa barabara, maji, umeme, mawasilianao, mashule, mahospitali, mabenki, n.k. yatachangia katika kupunguza umaskini uliokithiri nchini.

190. Riba katika mabenki ni kiashirio cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii. Riba za amana zikiimarika zitachochea uwekaji akiba ambao ni muhimu sana katika ulimbikizaji wa mitaji. Upatikanaji wa mitaji katika mabenki pamoja na riba nzuri za kukopa zitaharakisha uwekezaji vitega uchumi, utakaosukuma kasi ya ukuaji uchumi na hivyo kupunguza umaskini.

191. Kuimarika kwa biashara ya nje kunaongeza fedha zaidi za kigeni na kupunguza nakisi ya urari wa biashara. Fedha za kigeni zitawezesha serikali na wawekezaji kuagiza bidhaa muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo kuchangia moja kwa moja katika kupunguza umaskini.

192. Hiyo ni mifano michache tu inayoonyesha ni namna gani mafanikio ya uchumi jumla ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambayo moja kwa moja yanachangia katika kupunguza umaskini katika nchi yoyote ile na mfano mzuri hapa ni nchi za kusini-mashariki mwa Asia katika miaka ya themanini (Asian Tigers). Baada ya maelezo na uchambuzi hapo juu inafaa kuangalia namna gani mafanikio ya vigezo vya uchumi jumla vinavyoweza kutafsiriwa katika maendeleo ya jamii na kupunguza wa umaskini.

UHUSIANO KATI YA MAFANIKIO YA VIASHIRIA VYA UCHUMI JUMLA NA HALI YA UMASKINI NCHINI

193. Ukuaji wa uchumi endelevu na imara unatarajiwa utoe fursa kwa jamii nzima kuweza kushiriki katika uzalishaji mali na kuboresha hali ya maisha yao kwa: kuongeza ajira, kupanua wigo wa ujasirimali na kuongeza mapato na hatimaye kupunguza kasi ya umaskini miongoni mwao. Kutokana na mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea kufanyika, hali ya maisha ya Mtanzania katika baadhi ya maeneo imeanza kuboreka, ingawa kwa kiasi kidogo. Huu ni mwanzo tu wa matunda ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii. Hali ya umaskini wa leo Tanzania ni tofauti na ule wa miaka ya themanini kabla ya mageuzi. Kama ilivyoelezwa katika sehemu iliyotangulia, hakuna uhusiano wa moja kwa moja (direct linkage) kati ya kukua kwa uchumi na kuondoa umaskini. Ni vyema kuelezea zaidi ni kwa namna gani mageuzi ya kiuchumi na kijamii ambayo Tanzania imekuwa ikiyatekeleza na mafanikio iliyoyapata katika ukuaji wa uchumi jumla, yamesaidia kupunguza umaskini. Pia, ni sababu zipi mafanikio haya yameshindwa kupunguza umaskini katika maeneo mengine.

Kutengemaa kwa Mwenendo wa Bei

194. Kutokana na mageuzi ya kiuchumi, mwenendo wa bei za bidhaa umezidi kuimarika mwaka hadi mwaka toka asilimia 30 mwaka 1990 hadi chini ya asilimia 4.5 mwaka 2002. Kushuka ambako kumelinda uwezo wa manunuzi ya Mtanzania, wengi wao walio maskini. Uimarikaji wa bei pia ni mzuri sana katika kuharakisha ukuaji wa uchumi na hivyo kuondoa umaskini. Kutokana na uimara wa bei, gharama za uzalishaji zimetengemaa na hivyo kuchochea uzalishaji mali. Hii imepelekea kuongezeka kwa Pato la Taifa na hivyo, pato la wastani la kila mtu. Uimara wa bei, pia umevutia wawekazaji toka ndani na nje ya nchi kwa sababu ya kutopanda mara kwa mara kwa gharama za uzalishaji na riba za mitaji. Hali hii imesababisha ukuaji wa biashara na hivyo kuongezeka kwa mapato ya serikali ambayo ni muhimu katika matumizi yanayowalenga maskini.

Kuongezeka kwa Pato la Taifa

195. Kuongezeka kwa Pato la Taifa kunatokana na kukua kwa uchumi kwa sababu ya kuongezeka uwekezaji, kukua kwa biashara, kuimarika mwenendo wa kasi ya bei za bidhaa na huduma, na kadhalika, hivyo kuongezeka kwa pato la wastani la kila Mtanzania. Pato la wastani lilikuwa asilimia –1.5 kati ya mwaka 1979 - 1985, na liliongezeka hadi asilimia 2 kati ya mwaka 1986 - 1998. Pamoja na mafanikio hayo madogo lakini ni dalili nzuri kwa Mtanzania. Kuongezeka kwa Pato kumemwezesha mwananchi kupata mahitaji muhimu kiuchumi na kijamii, hivyo, kupunguza umaskini. Kuongezeka kwa pato la Taifa hakuna budi kwenda sambamba na mgawanyo mzuri wa mali kwa watanzania wote.

Kuboreka kwa Masoko

196. Kutokana na mageuzi ya kiuchumi yaliyofanyika Tanzania, masoko ya bidhaa za walaji, huduma, na upatikanaji wa bidhaa unazidi kuboreka katika maeneo ya mijini na vijijini. Kabla ya mabadiliko haya katika miaka ya themanini, watu walikuwa walishindwa kupata baadhi ya mahitaji kama vile; chakula, sabuni, madawa, elimu, n.k. Hii haikuwa kwa sababu ya kukosa pesa bali mahitaji hayo yalikosekana. Hivi leo mahitaji muhimu ya kijamii yanapatikana kwa urahisi na katika bei za ushindani, tatizo lililopo ni uwezo wa kifedha. Kwani mageuzi haya ya kiuchumi yanatoa fursa nyingi za watu kujitafutia kipato kupitia sekta rasmi na isiyo rasmi.

Kuboreka kwa Mapato na Matumizi ya Serikali
197. Kutokana na mafanikio mbalimbali ya kiuchumi, ikiwemo ukuaji wa uchumi na kutengamaa kwa uchumi, kuongezeka kwa mapato ya ndani, kuongezeka kwa akiba za fedha za kigeni, kushuka kwa bei, kuimarika kwa usimamizi wa matumizi ya fedha za serikali, sehemu kubwa ya bajeti ya matumizi ya serikali imeelekezwa kwenye sekta au maeneo ya kipaumbele na imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kuongezeka kwa matumizi katika maeneo muhimu yaliyoainishwa katika Mkakati wa Kupunguza Umaskini, kumechochea kasi ya ukuaji uchumi na utoaji huduma za jamii (elimu, afya, maji, mahakama), huduma za uchumi (barabara hasa za vijijini), na kilimo.

198. Mkakati wa Kupunguza Umaskini uliainisha sekta za kipaumbele sita za kuondoa umaskini ambazo ni elimu, maji, mahakama, afya, barabara na kilimo. Serikali tangu kipindi hicho imekuwa ikitekeleza azma ya kuondoa umaskini kwa kutumia bajeti yake ya mwaka wa fedha kupitia Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF) kwa kuongeza bajeti ya matumizi katika sekta hizo muhimu na pia kufanya mapitio na ufuatiliaji wa matumizi (PER).

Sekta ya Elimu

199. Kutokana na serikali kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu, bajeti ya matumizi imeongezeka hadi kufikia sh. 414.8 bilioni mwaka 2002/03 kutoka sh. 164.9 bilioni mwaka 1998/99, sawa na ongezeko la asilimia 151.6. Maendeleo yaliyofikiwa katika sekta hii yanatokana na kuongezeka kwa sehemu ya bajeti katika sekta hiyo pamoja na kuanzishwa na kutekelezwa kwa programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) na Programu ya Maendeleo ya Elimu ya Shule za Msingi (PEDP). Matokeo ya utekelezaji wa programu hizi ni kuongezeka kwa uandikishwaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule na kufutwa kwa ada katika shule za misingi; kukamilika kwa zoezi la upimaji maeneo ya shule za misingi katika wilaya 82 nchini; kuongezeka kwa kiwango cha wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kwenda elimu ya sekondari toka asilimia 19.5 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 21.7 mwaka 2002; na serikali kuajiri walimu wapya wenye grade A wapatao 7,277 katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 -2002. Pia, serikali iliendelea kutoa mafunzo kwa walimu ili kuwapatia ujuzi zaidi na idadi ya nyumba za walimu zipatazo 2,228 zimejengwa na madarasa mapya 12,868 yalijengwa katika kipindi cha 2000 - 2002.

Sekta ya Barabara

200. Bajeti ya matumizi katika sekta ndogo ya barabara imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka tangu Mkakati wa Kupunguza Umaskini uanze kutekelezwa mwaka 2000/01. Ujenzi na uboreshwaji wa barabara vijijini umekuwa ukifanyika chini ya Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa. Kwa mfano, kati ya kilometa 6,599 za barabara vijijini mwaka 2001/2002 zilifanyiwa matengenezo ya kawaida na ya muda na Mfuko Maalum wa miradi maalum ya barabara ulianzishwa mwaka 2001/02 ili kuboresha usafirishaji kati ya mikoa ya kaskazini magharibi na mikoa ya kusini.

Sekta ya Maji

201. Kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya matumizi ya serikali katika sekta ya maji, huduma za usambazaji maji mjini zimeongezeka kutoka asilimia 68 mnamo Desemba 2000 hadi asilimia 73 mwaka 2002. Ukarabati na upanuzi wa usambazaji huduma ya maji ulifanyika katika mikoa ya Morogoro, Tabora, Dodoma, Tanga, Arusha na Kilimanjaro. Pia, uendelezaji na upanuzi wa vyanzo vipya vya maji ukihusisha visima virefu umekuwa ukifanyika katika maeneo mbalimbali nchini. Utoaji wa huduma ya maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 48.5 mnamo mwezi Desemba 2000 hadi asilimia 50 mwezi Juni 2002, ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya Mwanyiha na Maswa katika mkoa wa shinyanga, ukarabati na upanuzi wa miradi 12 ya maji vijijini.

Sekta ya Sheria na Mahakama

202. Bajeti ya sekta hii iliongezeka kutoka sh. 5.5 bilioni mwaka 1998/99 hadi sh. 23.8 bilioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 332.7. Mwaka 2001/02 mahakimu wakazi 22, mahakimu wa mahakama za mwanzo 26, na wanasheria wa serikali 16 nchini waliajiriwa. Taasisi ya Uongozi wa Mahakama (IJA) iliyoko Lushoto ilianzishwa kwa lengo la kuwafundisha na kuwapatia ujuzi zaidi mahakimu wa mahakama ya mwanzo. Hadi mwaka 2002, jumla ya watumishi wa mahakama 30 walikuwa wamehitimu mafunzo. Aidha, Serikali ilianzisha Mahakama ya Biashara mwezi Agosti mwaka 1999, na taratibu za utatuzi wa kesi au migogoro ya kibiashara umeimarika, na kesi zimekuwa zikikamilika kati ya miezi 3 na 6. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo ilianzishwa mwezi Machi 2002.

Sekta ya Kilimo

203. Kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani ya serikali, mgawo wa bajeti ya matumizi kupitia Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati kwenye sekta hii umeongezeka kutoka sh. 14.9 bilioni mwaka 1998/99 hadi sh. 62.6 bilioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 320.1 katika kipindi hicho. Mwaka 2001, Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo ulipitishwa. Utafiti wa mazao ya kilimo umeendelea kufanyika katika taasisi za utafiti za kilimo. Hatua mbalimbali za kuimarisha uzalishaji na uboreshaji wa sekta ya kilimo zimeshafanywa na serikali, hatua hizo ni pamoja na kusambazwa kwa madawa ya kuua ndege na wadudu waharifu, ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji endelevu wa mazao ya kilimo. Baadhi ya miradi ya umwagiliaji ni pamoja na Usimamizi wa Mabonde ya Mito na Uboreshaji Umwagiliaji wa wakulima wadogowadogo (RBMNSIIP) – hekta 1,169, Programu ya Ushirikishwaji katika Maendeleo ya Umwagiliaji (PIDP) – miradi 18 ilianzishwa mwaka 2002/03, Programu ya Kusaidia Sekta ya Kilimo (ASPS) – miradi 5 yenye hekta 3,830 ilikarabatiwa kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya, na hekta 560 za miradi midogomidogo ya umwagiliaji zilikarabatiwa.

Sekta ya Afya

204. Mgawo wa bajeti ya matumizi katika sekta hii umeongezeka kutoka asilimia 7.5 ya bajeti mwaka 2000/01 na kufikia asilimia 8.7 mwaka 2002/03. Kuongezeka kwa mgawo wa bajeti ya matumizi katika sekta ya afya, kumeongeza na kuboresha utoaji wa huduma ya afya. Uchambuzi wa utendaji katika sekta hii unaonyesha kuwa matumizi yanayoelekezwa kwenye huduma za afya ya msingi yameongezeka kwa asilimia 184 kati ya kipindi cha mwaka 1999/2000 na mwaka 2002/03. Kuongezeka kwa mgawo wa fedha za matumizi katika sekta ya afya hasa afya ya msingi kunalenga katika kushughulikia matatizo ya kiafya katika maeneo muhimu matano ambayo ni afya ya uzazi wa mama na mtoto, kuthibiti magonjwa ya kuambukiza na kuimarisha muundo wa uongozi na utawala. Programu mbalimbali za kuboresha na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi zimeshaanzishwa na kutekelezwa ikiwemo pamoja na Mradi wa Kitaifa wa Kudhiti Malaria, Mfuko wa Kuimarisha upatikanaji madawa (Drug Revolving Funds) katika hospitali zote za wilaya, programu za TV na Radio iliandaliwa na kusambaza taarifa kwa ajili ya kutangaza Programu ya mabadiliko katika sekta ya afya mwaka 2001/02.

Virusi Vya Ukimwi (VVU)/UKIMWI

205. Madhara ya VVU/UKIMWI katika uchumi ni pamoja na: kupunguza nguvu kazi na tija; kuongezeka kwa utegemezi; na kuongeza gharama za matumizi ya fedha za serikali kwa kuwatunza na kuwatibu walioathirika na UKIMWI. Ili kudhibiti kuenea kwa UKIMWI, upo Mkakati wa Taifa Unaojumuisha Sekta mbalimbali (NMSF) wa kupambana na UKIMWI. Aidha, Tume ya Kudhibiti VVU/UKIMWI (TACAIDS) iliundwa mwaka 2001. Mafanikio ya uanzishwaji wa mikakati hiyo yameanza kuonekana. Kiwango cha ueneaji Virusi vya UKIMWI kimeshuka kutoka asilimia 24 mwaka 1994 hadi kufikia asilimia 11 mwaka 2001. Kuongezeka kwa mgawo wa fedha katika kampeni za weledi, sekta zote katika ngazi mbalimbali tayari zimeshaandaa mipango mbalimbali ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu. Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wengine imeishaanzisha mpango wa kutoa na kusambaza dawa za kupunguza makali ya UKIMWI kwa walioathirika.

 

Jedwali Na. 10.6:   MATUMIZI YA SERIKALI KUU KATIKA SEKTA ZA KIPAUMBELE,

   MWAKA 1998/99 – 2002/03

Sh.  bilioni                  

 

1998/99

1999/00

2000/01

2001/02

2002/03

Halisi

Halisi

Halisi

Halisi

Matarajio

Jumla ya Matumizi

338.9

414.3

494.6

753.8

945.0

Elimu

164.9

218.0

254.9

344.9

414.8

Afya

72.5

81.2

100.7

142.1

172.3

Maji

14.4

14.5

18.3

32.5

58.6

Kilimo

14.9

21.6

19.1

31.9

62.6

Barabara

66.7

70.8

92.5

179.6

208.4

Mahakama

5.5

8.3

9.2

18.8

23.8

TACAIDS

0.0

0.0

0.0

4.0

4.5

Matumizi ya Kawaida

233.0

282.0

347.5

490.2

676.7

Elimu

117.6

158.9

189.2

282.1

400.0

Afya

50.7

53.9

70.3

90.9

128.6

Maji

7.1

5.4

8.1

15.5

16.9

Kilimo

8.6

13.7

10.3

17.2

34.2

Barabara

43.9

42.

60.7

65.7

73.6

Mahakama

5.

7.9

8.8

14.8

18.9

TACAIDS

0.0

0.0

0.0

4.0

4.5

Matumizi ya Maendeleo

105.9

132.4

147.1

263.5

268.3

Elimu

47.3

59.1

65.7

62.8

14.8

Afya

21.9

27.3

30.4

51.2

43.7

Maji

7.3

9.1

10.1

17.0

41.6

Kilimo

6.3

7.9

8.7

14.7

28.4

Barabara

22.8

28.6

31.7

113.9

134.8

Mahakama

0.3

0.4

0.4

4.0

4.9

TACAIDS

0.0

0.0

0.0

0.0

0.0

Chanzo:  Wizara ya Fedha
Kutengemaa kwa ujazi wa Fedha,

206. Kuongezeka kwa ufanisi wa mabenki kufuatia mageuzi ya sekta ya fedha kunatoa fursa kwa watanzania kuongeza amana, mitaji na hivyo uzalishaji mali. Mbali na mikakati mingi inayochukuliwa na serikali katika eneo hili, bado jamii ya watanznia iko nyuma sana katika kutumia mabenki kwenye kuweka akiba zao na kukopa kwa ajili ya biashara na uzalishaji.

Kuimarika kwa biashara ya Nje na Fedha za kigeni

207. Mageuzi ya kiuchumi na mafanikio ya uchumi yameleta mazingira mazuri nchini ambayo yamepelekea kukua kwa biashara ya nje na hivyo, kuongezeka kwa akiba ya kigeni. Pamoja na kwamba mpaka sasa hakuna mafanikio makubwa katika eneo hili, lakini kilichofanyika mpaka sasa ni kuongezeka kwa msingi imara wa kipato cha watanzania na serikali kwa ujumla na hivyo kuwa na nafasi ya kuondoa umaskini hatimaye.

Kuongezeka kwa Misaada toka Nje

208. Kutokana na mafanikio ya serikali katika mageuzi ya kiuchumi na kijamii na mafanikio yaliyofikiwa katika kiwango cha ukuaji uchumi, Tanzania imeweza kuwashawishi wahisani kwa kuwa makini na dhati katika kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi. Hii imewezesha Tanzania kuongezewa misaada na wahisani na kupunguziwa baadhi ya madeni yake, ambapo inaelekezwa kwenye kuondoa umaskini chini ya Mkakati wa Kupunguza Umaskini.


209. Mbali na mafanikio ya uchumi jumla Tanzania iliyoyapata, Tanzania bado ni nchi maskini kama zilivyo nchi nyingine nyingi duniani. Ila kama baadhi ya viashiria vya mafanikio ya uchumi jumla vinavyoonyesha hapo juu, Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo kama kupunguza umaskini kwa kiasi. Umaskini unaoikabili Tanzania leo sio kama ule wa kabla ya mageuzi ya kiuchumi na jamii. Uchumi thabiti na endelevu ni muhimu sana kwa kuweka mazingira ambayo yatawezesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii na hivyo kufuta umaskini.

MAJUMUISHO NA MWELEKEO

210. Tanzania imepiga hatua kubwa na ya kuridhisha katika utekelezaji wa mageuzi yake ya kiuchumi na kijamii. Mafanikio haya yamedhihirishwa zaidi katika mafanikio yake katika uchumi jumla. Kama maelezo na takwimu zinavyoonyesha, mafanikio haya hayajapelekea kwa kiasi kikubwa kupungua kwa umaskini nchini. Lakini mambo matatu ni wazi: kwanza, kuboreka na kuimarika kwa uchumi jumla hakusababisha moja kwa moja kupatikana kwa mafanikio ya kiuchumi na jamii na hivyo kuondoa kabisa umaskini, ila ni muhimu sana kwa kutengeneza mazingira na kutoa fursa ambazo kama ikitumika vilivyo itachochea na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii na hatimaye kuondoa umaskini. Pili ni kwamba, hoja ya baadhi ya watu siyo sahihi kwamba mafanikio ya mageuzi ya kiuchumi na jamii na kukua kwa uchumi jumla hayajapunguza bali yameongeza umaskini. Ni dhahiri mafanikio haya yameanza kuzaa matunda, yanajenga fursa nzuri sana ya kuondoa umaskini na pia, bado ni mapema sana kwani hayana muda mrefu wa kuyapima. Tatu, kwa upande wa Tanzania, mafanikio haya madogo katika kuondoa umaskini mbali na mafanikio makubwa katika ukuaji wa uchumi jumla yanasabishwa na sababu nyingine nyingi kama: miundombinu hafifu ya kiuchumi na kijamii, uchanga wa mfumo wa uendeshaji uchumi wa soko huria, kukosekana kwa utamaduni wa kuweka akiba, kutojituma kwa jamii kufanya kazi kwa bidii, utumiaji mbaya wa rasilimali, binafsi na hata zile za serikali kwa matumizi yasiyo lazima, tija ndogo ya uzalishaji, mfumo mzima wa elimu na mafunzo, mfumo mzima wa afya na huduma, janga la UKIMWI, tatizo la mikopo nafuu, na kukosekana kwa ujuzi katika biashara, na majanga mengine yaliyo nje ya uwezo wa nchi.


211. Mafanikio yaliyopatikana kutokana na mageuzi ya kiuchumi nchini yamesababisha kuwepo kwa uchumi thabiti na ukuaji endelevu. Hata hivyo, mafanikio bado hayajafikiwa kwa kiwango kinachowezesha wananchi kujikwamua kiuchumi hasa wale wanaoishi vijijini na wenye vipato vya chini. Ili mafanikio hayo yawe na manufaa na kuwafikia wananchi walio wengi na kuboresha hali zao za maisha na kipato, hakuna budi kuendeleza juhudi katika maeneo muhimu yafuatayo:


Mageuzi katika sekta ya kilimo ambayo yatatoa ajira kwa wananchi walio wengi hasa wale waishio vijijini hususan katika kilimo cha umwagiliaji katika mashamba makubwa na madogo ili kuepukana na kilimo kinachotegemea mvua. Aidha, teknolojia ya kisasa zaidi inahitajika katika kusukuma sekta hii.

• Kujenga na kuendeleza shughuli ndogo ndogo za uzalishaji na biashara (small and micro enterprises) zinazojumuisha: usindikaji wa bidhaa asilia; viwanda vidogo vidogo; na utoaji wa huduma mbalimbali. Katika kufanikisha azma hii, juhudi zinahitajika katika utoaji wa mikopo midogo midogo (micro finance) na kuendelea ujasiri mali kwa makundi mbalimbali.

• Marekebisho zaidi katika mfumo wa kodi yanahitajika ili kupunguza mzigo wa kodi kwa wakulima hasa wale wadogo wadogo na kuboresha usimamizi katika ukusanyaji kodi.

• Uimarishaji wa miundombinu ya kiuchumi kama vile barabara hasa zile za vijijini kwa lengo la kusaidia maendeleo ya sekta ya kilimo na uimarishaji wa masoko ya ndani.

• Kuangalia upya sheria ya umilikaji ardhi na sera iliyopo ili kuweza kutatua matatizo yanayoambatana na matumizi ya ardhi kama dhamana kwa ajili ya mikopo.

• Kujenga misingi ya fikra ya kimaendeleo na za kujituma katika jamii ili kuondokana na fikra tegemezi.

Back Top