MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

                 
MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA

Hali ya Uchumi wa Taifa
Hali ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa
Sekta ya Nje
Fedha za Serikali
Fedha na Taasisi za Fedha
Rasilimali Watu

       
FEDHA NA TAASISI ZA FEDHA

Ujazi wa Fedha na Karadha

95. Katika mwaka 2002/03, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) uliongezeka kwa sh. 225.3 bilion, sawa na ongezeko la asilimia 16.9 kutoka sh. 1,333.5 bilioni mwezi Juni 2002 hadi sh. 1558.8 bilioni mwezi Juni 2003. Ongezeko la ujazi wa fedha mwaka 2002/03 lilizidi lengo lililopangwa la kati ya asilimia 10 hadi 12 kwa mwaka..Ongezeko hilo lilichangiwa zaidi na ongezeko la amana za hundi, amana za akiba na amana za muda maalum. Ongezeko la amana za akiba lilikuwa dogo ikilinganishwa na ongezeko la amana za aina nyingine. Aidha, kiwango cha ukuaji wa akiba katika amana za hundi kiliongezeka kwa asilimia 31.4 ikilinganishwa na asilimia 22.1 mwaka 2001/02, wakati ambapo akiba katika amana za muda maalum na amana za akiba vilipungua kwa asilimia 12.9 na 10.5, kwa mpangilio huo, vikilinganishwa na viwango vya mwaka 2001/02, vya asilimia 27.4 na 26.7, kwa mpangilio huo.

96. Katika kipindi cha Julai – Desemba 2003, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) uliongezeka hadi kufikia sh. 1,719.7 bilioni, kutoka shs. 1,558.8 bilioni mwezi Juni 2003, sawa na ongezeko la asilimia 10.3. Katika kipindi hicho mchango wa amana za muda maalum katika ujazi wa fedha ulikuwa mdogo, ikilinganishwa na mchango wa fedha zilizo kwenye mzunguko nje ya mabenki, amana za hundi, na akiba.

97. Katika mwaka 2002/03, karadha nchini iliongezeka kwa sh. 173.3 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 25.3, kutoka sh. 684.9 bilioni mwezi Juni 2002 hadi sh. 858.2 bilioni mwezi Juni 2003. Ongezeko hilo lilitokana na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Karadha kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 36.6 katika mwaka 2002/03, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 27.4 mwaka 2001/02. Jedwali Na. 27 linaonesha mchanganuo wa ujazi wa fedha na karadha nchini na Jedwali Na. 28 linaonyesha viwango vya mabadiliko ya mchanganuo huo.

Mikopo ya Benki za Biashara kwa Sekta Mbalimbali
98. Katika mwaka 2002/03, mikopo iliyotolewa kwa sekta mbalimbali iliongezeka kwa sh. 176.5 bilioni na kufikia sh. 658.5 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 36.6 kutoka sh. 482 bilioni zilizotolewa katika mwaka 2001/02. Sekta zilizopata viwango vikubwa vya mikopo ni pamoja na madini na viwanda na biashara nyinginezo. Kulikuwa na ongezeko la kiwango cha mikopo kwa sekta ya uzalishaji katika kilimo, kulikowezeshwa na serikali kutoa dhamana kwa mikopo iliyotolewa kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya kilimo kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi (Export Credit Guarantee Scheme). Serikali imepanga kuupanua mpango huo kwenye miradi maalum inayolenga katika kukuza uchumi, kuongeza ajira, na uuzaji wa mazao nje ya nchi.

99. Katika mwaka 2002/03, serikali iliendelea kuchukua hatua katika kuondoa vikwazo vya kimfumo kwa mabenki kukopesha zaidi sekta binafsi, hususan wakulima na wajasiriamali wadogo na wa kati. Sheria ya mikopo midogo midogo ilipitishwa (Microfinance) na Bunge mwezi Februari 2003 ili kuwezesha mabenki na taasisi za fedha kutoa mikopo midogo midogo.

100. Mikopo kwa serikali katika mwaka 2002/03, toka benki za biashara, kupitia mauzo ya dhamana za serikali, ilifikia sh. 347,166 milioni, ikijumuisha hawala za hazina za sh. 190,446.1 milioni na dhamana nyingine za serikali za sh. 156,719.9 million, ikilinganishwa na jumla ya sh. 2,671,025.3 milioni zilizopatikana kwa utaratibu huo mwaka 2001/02. Kwa mauzo hayo katika mwaka 2002/03 kulikuwa na ongezeko la sh. 80,140.7 milioni sawa na ongezeko la asilimia 30, ikilinganishwa na mwaka 2001/02. Katika kipindi hicho hawala za hazina ziliongezeka kutoka sh. 95,665.6 milioni mwaka 2001/02 hadi kufikia sh. 190,446.1 milioni, wakati ambapo dhamana nyingine za serikali zilipungua kutoka sh. 171,359.7 mwaka 2001/02 hadi kufikia sh. 156,719.9 milioni. Aidha, katika kipindi hicho, mikopo iliyotolewa na mabenki ya biashara kwa sekta binafsi iliongezeka kutoka sh. 482,043.1 milioni mwaka 2001/02 hadi sh. 658,524.6 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 36.6. Kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi kumetokana na kuongezeka kwa ushindani kati ya mabenki ya biashara nchini baada ya idadi yake kuongezeka na fursa ya kuwekeza katika hawala za hazina kupungua.

Amana katika Benki za Biashara
101. Katika mwaka 2002/03, jumla ya amana katika benki za biashara ziliongezeka kutoka sh. 1,368,506 milioni mwaka 2001/02 hadi sh. 1,732,190.4 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 26.6. Mchango wa amana za fedha za kigeni katika amana zote ulikuwa asilimia 37.4, amana za muda maalum asilimia 14.3; amana za hundi asilimia 29.3, na amana za akiba asilimia 19.1. Viwango vidogo vya riba za amana vilivyotolewa na benki za biashara, hususan amana za akiba, pamoja na ada mbalimbali zinazotozwa kwenye akaunti za akiba za wateja, kama vile ada ya kuchukua fedha kutoka kwenye akaunti na ada ya kuacha salio dogo kwenye akaunti viliendelea kupunguza hamasa ya wateja kuwekeza katika amana za aina hiyo. Jedwali Na.31 linaonyesha mwenendo wa amana za aina mbalimbali katika benki za biashara.

102. Katika mwaka 2002/03, benki za biashara ziliendeleza ushindani katika kutoa huduma mbalimbali za kibenki. Kati ya benki zilizofungua matawi mapya ya biashara ni pamoja na Akiba Commercial Bank na Benki ya Taifa ya Biashara (National Bank of Commerce Limited). Aidha, wafanyakazi serikalini walianza kupokea mishahara yao kupitia benki ya biashara, na hivyo kuziwezesha benki hizo kupata faida zaidi kutokana na ada mbalimbali zinazotozwa wafanyakazi hao katika kuendesha akaunti zao.

Mwenendo wa Viwango vya Riba
103. Riba ya mikopo ya Benki Kuu kwa benki za biashara na serikali iliongezeka kutoka asilimia 9.4 mwezi Juni 2002 hadi asilimia 10.6 mwezi Juni 2003. Kiwango hicho kiliendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia 12.3 mwezi Desemba 2003. Wastani wa riba zilizotolewa na benki za biashara kwa amana za akiba ulishuka kutoka riba ya wastani wa asilimia 3.5 mwezi Juni 2002 hadi asilimia 2.5 mwezi Juni 2003. Riba hiyo iliendelea kubaki kama ilivyo hadi ilipofika mwezi Desemba 2003. Wastani wa riba za amana za muda maalum ulishuka kutoka wastani wa asilimia 4 mwezi Juni 2002 hadi wastani wa asilimia 3.5 mwezi Juni 2003. Ilipofika Desemba 2003 wastani wa riba hizo uliongezeka hadi kufikia asilimia 3.9.

104. Riba zilizotozwa na benki za biashara kwa mikopo ya muda mfupi ziliongezeka kutoka wastani wa asilimia 14.8 mwezi Juni 2002 hadi wastani wa asilimia 16.4 ilipofika mwezi Juni 2003, lakini baada ya hapo, riba hizo zilianza kushuka hadi kufikia wastani wa asilimia 15.7 ilipofika Desemba 2003. Mikopo ya muda wa kati na mrefu ilitozwa riba ya wastani wa asilimia 13.5 mwezi Juni 2003 ikiwa imepungua kutoka wastani wa riba ya asilimia 16.8 mwezi Juni 2002. Riba hiyo ilishuka zaidi hadi kufikia asilimia 13.4 ilipofika mwezi Desemba, 2003. Katika mwaka 2002/03 benki za biashara ziliendelea kutoza riba tofauti kwa aina moja ya mikopo kwa wakopaji tofauti (negotiated lending rate). Mwenendo wa riba katika mabenki ya biashara unaonesha kwamba bado tofauti kati ya riba za amana na za mikopo ni kubwa sana. Jedwali Na. 32 linaonesha mchanganuo wa viwango vya riba.

Mwenendo wa Thamani ya Shilingi
105. Katika mwaka 2002/03, kiwango rasmi cha kubadilisha dola ya Marekani kwa shilingi ya Tanzania (wastani wa kiwango cha kuuzia) kiliongezeka kutoka sh. 946.9 mwezi Juni 2002 hadi sh. 1,047.4 ilipofika mwezi Juni 2003, sawa na kupungua kwa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa asilimia 10.6, ikilinganishwa na kupungua thamani kwa asilimia 6.6 katika mwaka 2001/02. Katika kipindi hicho, kiwango cha kubadilisha dola kwa shilingi ya Tanzania katika maduka ya fedha za kigeni (wastani wa kiwango cha kuuzia) kiliongezeka kutoka sh. 975.0 mwezi Juni 2002, hadi sh. 1,053.0 ilipofika mwezi Juni 2003, sawa na kupungua kwa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa asilimia 8. Kuanzia mwezi Julai 2003 shilingi ya Tanzania iliendelea kushuka thamani dhidi ya dola ya Marekani katika soko la fedha za kigeni (IFEM) hadi kiwango cha sh. 1,061.7 ilipofika Desemba, 2003. Katika kipindi hicho, kiwango cha kubadilisha dola ya Marekani kwa shilingi ya Tanzania katika maduka ya fedha za kigeni (wastani wa kiwango cha kuuzia) kilifika sh. 1,074 kwa dola moja. Jedwali Na. 29 linaonesha mwenendo wa viwango vya kubadilisha dola kwa shilingi ya Tanzania.

Benki Kuu ya Tanzania
106. Katika mwaka 2002/03, amana za serikali katika Benki Kuu ziliongezeka kwa sh. 79.6 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 44.1 kutoka sh. 180.6 bilioni mwezi Juni 2002, hadi sh. 260.2 bilioni mwezi Juni 2003. Kuongezeka kwa amana za serikali katika Benki Kuu ya Tanzania kulitokana na ongezeko katika ukusanyaji wa mapato ya ndani lililotokana na mabadiliko katika mfumo wa usimamizi wa kodi kulikoboresha mazingira ya ulipaji wa kodi. Katika kipindi hicho, amana za benki za biashara katika Benki Kuu nazo ziliongezeka kutoka sh. 106.6 bilioni mwezi Juni 2002, hadi sh. 117.1 bilioni mwezi Juni 2003, sawa na ongezeko la asilimia 9.8.

107. Jumla ya mapato yote ya Benki Kuu katika mwaka 2002/03 yalifikia sh. 98.3 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 28.3, toka mapato ya sh. 76.6 bilioni mwaka 2001/02. Shughuli za fedha za kigeni ziliingizia Benki Kuu mapato ya sh. 75.1 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 31.5, ikilinganishwa na mapato ya sh. 57.1 bilioni mwaka 2001/02. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa shughuli za wawekezaji wa nje pamoja na riba katika soko la ndani. Mapato kutokana na shughuli za ndani yaliongezeka kutoka sh. 19.5 bilioni mwaka 2001/02 hadi sh. 23.2 bilioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 19.

108. Katika mwaka 2002/03, jumla ya matumizi ya Benki Kuu yalifikia sh. 78.3 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 36.4, ikilinganishwa na matumizi ya sh. 57.4 bilioni mwaka 2001/02. Ongezeko hilo la matumizi lilitokana na kuongezeka kwa gharama za utoaji wa noti mpya, zilizoongezeka kwa asilimia 79 pamoja na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kwa sh. 5.5 bilioni. Shughuli za ndani ya nchi ziliigharimu Benki Kuu sh. 10.4 bilioni, ikilinganishwa na sh. 6.6 bilioni mwaka 2001/02, sawa na ongezeko la asilimia 57.6.

109. Kutokana na mwenendo huo wa mapato na matumizi ya Benki Kuu, faida iliyopatikana katika mwaka 2002/03 ilifikia sh. 20 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.2, ikilinganishwa na faida ya sh. 19.2 bilioni iliyopatikana katika mwaka 2001/02. Benki Kuu ilitoa gawio la sh. 5 bilioni katika mwaka 2002/03, sawa na upungufu wa asilimia 60 ikiliganishwa na gawio la sh. 8 bilioni lililotolewa mwaka 2001/2002.

Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF)
110. Katika mwaka 2003, Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma uliendelea kukusanya michango na kutoa mafao kwa wanachama wake. Aidha, Mfuko huu uliendelea kupanua huduma zake kwa makampuni binafsi. Hadi kufikia Desemba 2003, makampuni 362 yalikuwa yamejiunga na Mfuko huo, ikilinganishwa na makampuni 320 mwaka 2002. Mafao yatolewayo na PPF ni pamoja na mafao ya uzeeni, mafao ya kiinua mgongo, mafao ya kifo, na mafao ya wategemezi.

111. Thamani ya vitega uchumi vya PPF iliongezeka kutoka sh. 112.71 bilioni mwaka 2002, hadi sh. 123.2 bilioni mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 9.4. Uwekezaji katika hawala za hazina na dhamana nyingine za serikali uliongezeka kutoka sh. 8 bilioni mwaka 2002, hadi sh. 23.4 bilioni mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 190.5. Makusanyo kutoka kwa wananchama yalipungua kidogo kutoka sh. 35.6 bilioni mwaka 2002, hadi sh. 33.7 bilioni mwaka 2003. Jumla ya mafao yaliyotolewa kwa wanachama yalikuwa sh. 16.8 bilioni mwaka 2003 ikilinganishwa na sh. 14.3 bilioni mwaka 2002. Idadi ya wanachama mwaka 2003 ilipungua hadi kufikia 72,755 ikilinganishwa na wanachama 78,000 mwaka 2002, hali iliyotokana na ubinafsishaji wa mashirika ya umma ulioandamana na upunguzaji wa wafanyakazi.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
112. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ni moja ya mifuko inayokusanya michango ya wafanyakazi kutoka kwa waajiri ikiwa ni akiba ya kuwalipa mafao wafanyakazi hao hapo baadaye. Waajiri ambao ni wanachama wa mfuko huu ni pamoja na mashirika ya umma, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) na waajiri wengine katika sekta binafsi. Katika mwaka 2002/03, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii uliendelea kuwekeza michango ya wanachama wake katika vitega uchumi mbalimbali, zikiwemo dhamana za serikali, hisa na majengo ya kupangisha, kwa madhumuni ya kutunisha mfuko huo ili kuuwezesha kulipa mafao manono kwa wanachama wake. Mafao yanayotolewa na Mfuko huu ni pamoja na mafao ya uzeeni/kustaafu, ulemavu, urithi, msaada wa mazishi, na mafao ya kujitoa uanachama katika mfuko. Katika mwaka 2002/03, jumla ya mafao yaliyotolewa kwa wanachama yalikuwa sh.18,305.1 milioni, ikilinganishwa na sh. 13,322.9 milioni mwaka 2001/02.

113. Idadi ya wanachama mwaka 2002/03 ilifikia 327,609, ikilinganishwa na wanachama 351,975 mwaka 2001/02. Thamani ya vitega uchumi vya NSSF ilifikia sh. 230,778.5 milioni mwaka 2002/03 ikilinganishwa na sh. 186,799.5 milioni mwaka 2001/02. Uwekezaji katika dhamana za serikali uliongezeka kutoka sh. 83,628.9 milioni mwaka 2001/02, hadi sh. 111,234.6 milioni mwaka 2002/03. Makusanyo kutoka kwa wanachama yaliongezeka kutoka sh. 49,909.3 milioni mwaka 2001/02, hadi kufikia sh. 64,352.9 milioni mwaka 2002/03. Aidha, idadi ya waajiri wanaochangia mfuko wa NSSF ilipungua kutoka wanachama 15,535 mwaka 2001/02 hadi wanachama 15,097 mwaka 2002/03.

Benki ya Posta Tanzania
114. Katika mwaka 2003, Benki ya Posta Tanzania iliendelea kutoa huduma zake kwa wateja kama ilivyoainishwa katika mpango wake maalum. Benki inatoa huduma mbalimbali za amana, ikiwa ni pamoja na akaunti ya kawaida ya akiba, ijulikanayo kama Quick Account, akaunti ya call account na akaunti ya muda maalum wa kati ya mwezi mmoja na miezi 24. Benki ya Posta Tanzania inafanya kazi kupitia mtandao wake wenye kujumuisha matawi kamili ya benki, vituo vinavyofanya shughuli za benki mikoani na ofisi za Posta zilizo chini ya Shirika la Posta Tanzania.

115. Benki ya Posta Tanzania ni wakala pekee nchini wa shirika linalotoa huduma za kusafirisha fedha za kimataifa lijulikanalo kama Western Union Financial Services International. Kwa kupitia huduma ya shirika hilo wateja wanaweza kutuma na kupokea fedha popote ulimwenguni. Vituo vilivyokuwa vinatoa huduma hiyo nchini viliongezeka kutoka vituo 20 mwaka 2002 hadi 21 mwaka 2003, baada ya Benki kufungua ofisi mpya kwa ajili ya kutoa huduma hiyo Dar es Salaam. Jumla ya vituo vya mawakala wadogo wa huduma hiyo chini ya Shirika la Posta Tanzania, iliongezeka kutoka 33 katika mwaka 2002, hadi 79 katika mwaka 2003, na hivyo kuongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma za kusafirisha fedha kwa kutumia Western Union Money Transfer nchini kufikia 100, ikilinganishwa na vituo 63 katika mwaka 2002.

116. Amana za wateja wa Benki ziliongezeka kutoka sh. 45,127.6 milioni mwishoni mwa mwaka 2002, hadi sh. 49,650.8 milioni mwishoni mwa mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la sh. 4,523.2 milioni au asilimia 10, ikilinganishwa na ongezeko la sh. 3,658 milioni au asilimia 8.8 mwaka 2002. Idadi ya wateja wenye amana iliongezeka kutoka wateja 1,079,225 mwaka 2002 hadi wateja 1,104,954 mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la wateja 25,729. Akaunti ya aina ya Quick Account ndiyo iliyovutia wateja wengi katika mwaka 2003.

117. Sehemu kubwa ya vitega uchumi vya Benki viliendelea kuwa hawala za hazina na hati fungani. Vitega uchumi vingine vipo katika amana za muda maalum katika benki nyingine na mikopo. Jumla ya thamani ya vitega uchumi vya benki katika mwaka 2003 ilifikia sh. 43,153.2 milioni ikilinganishwa na sh. 41,666.5 milioni mwaka 2002, ikiwa ni ongezeko la sh. 1,486.7 au asilimia 4. Uwekezaji katika dhamana za serikali ulipungua kidogo kutoka sh. 26,781 milioni au asilimia 64.3 ya vitega uchumi vyote vya mwaka 2002, hadi sh. 24,359.5 milioni au asilimia 61.1 ya vitega uchumi vyote vya mwaka 2003. Vitega uchumi katika benki nyingine kupitia amana za muda maalum vilipungua mwaka 2003 kutoka sh. 6,540 milioni mwaka 2002 hadi sh. 4,750.4 milioni. Mchango wa amana za muda maalum katika jumla ya vitega uchumi vyote pia ulipungua kutoka asilimia 15.7 mwaka 2002 hadi asilimia 11.0 mwaka 2003.

118. Benki ilianzisha utoaji wa mikopo midogomidogo mwaka 2001 na hadi kufikia mwaka 2003 vikundi vilivyopata mikopo hiyo viliongezeka hadi kufikia 827, vilivyokopa jumla ya sh. 1067.4 milioni ikilinganishwa na vikundi 676 vilivyopata mikopo yenye thamani ya sh. 1,731 milioni mwaka 2002.

Jedwali Na. 27(MWENENDO WA KARADHA NA UJAZI WA FEDHA - TANZANIA BARA)

Jedwali Na. 28(VIWANGO VYA UKUAJI WA KARADHA NA UJAZI WA FEDHA - TANZANIA BARA)

Jedwali Na. 29(MWENENDO WA VIWANGO VYA UBADILISHAJI KATI YA SHILINGI NA DOLA YA MAREKANI)

Jedwali Na. 30(MIKOPO YA BENKI ZA BIASHARA KWA SEKTA MBALIMBALI)

Jedwali Na. 31(MWENENDO WA AMANA KATIKA BENKI ZA BIASHARA)

Jedwali Na. 32( VIWANGO VYA WASTANI VYA RIBA)

 
Back Top