MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA

Hali ya Uchumi wa Taifa
Hali ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa
Sekta ya Nje
Fedha za Serikali
Fedha na Taasisi za Fedha
Rasilimali Watu

   
HALI YA UCHUMI NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
 
HALI YA UCHUMI DUNIANI
Ukuaji wa Uchumi Duniani

23. Katika mwaka 2003, pato la dunia lilikua kwa asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 3.0 mwaka 2002. Hali ya wasiwasi kuhusu ugaidi na usalama haikuathiri mwenendo wa ukuaji wa uchumi duniani. Ongezeko la pato la dunia mwaka 2003 lilichangiwa zaidi na ukuaji uwekezaji rasilimali, kukua kwa biashara na ongezeko la uzalishaji viwandani. Aidha, kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Marekani na nchi za Asia kumechangia mwenendo huo. Kwa nchi zilizoendelea, pato lilikua kwa asilimia 2.1 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2002. Pato la nchi zinazoendelea lilikua kwa asilimia 6.1 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2002. Ongezeko hili kubwa mwaka 2003 lilitokana na kuongezeka kwa uwekezaji wa rasilimali pamoja na kuimarika kwa sera za uchumi. Pato la Afrika lilikua kwa silimia 4.1 mwaka 2003 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.5 mwaka 2002.

Jedwali 2.1:Pato la Dunia 2001 – 2003 (Badiliko %)

 

2001

2002

2003

Pato la Dunia

2.4

3.0

3.9

Nchi Zilizoendelea

1.1

1.7

2.1

Nchi Zinazoendelea

4.1

4.6

6.1

Nchi za Asia zinazoendelea

 

6.4

7.8

Amerika ya Kusini

 

-0.1

1.7

Afrika

3.6

3.4

4.1

Chanzo: Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)

24. Kiwango cha biashara ya bidhaa na huduma duniani kiliongezeka kwa asilimia 4.5 mwaka 2003 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 3.1 mwaka 2002. Uagizaji bidhaa kwa nchi zilizoendelea uliongezeka kwa asilimia 3.5 mwaka 2003 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 2.3 mwaka 2002. Kwa upande wa nchi zinazoendelea, uagizaji wa bidhaa uliongezeka kwa asilimia 8.9 mwaka 2003 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 6.2 mwaka 2002 wakati ambapo kwa nchi zilizoendelea uliongezeka kwa asilimia 2.7 mwaka 2003 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 1.9 mwaka 2002. Kwa nchi zinazoendelea, uuzaji nje wa bidhaa uliongezeka kwa asilimia 8.7 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 6.5 mwaka 2002.

25. Fahirisi ya bei ya bidhaa za viwanda iliongezeka kwa asilimia 14.5 mwaka 2003 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 2.4 mwaka 2002. Bei ya mafuta yasiyosafishwa iliongezeka kwa asilimia 15.8 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 2.5 mwaka 2002. Bei ya bidhaa asilia iliongezeka kwa asilimia 7.1 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 0.5 mwaka 2002. Katika nchi zilizoendelea, bei ziliongezeka kwa asilimia 1.2 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 1.5 mwaka 2002. Kwa upande wa nchi zinazoendelea, bei ziliongezeka kwa asilimia 6.1 mwaka 2003, sawa na ilivyokuwa mwaka 2002. Katika nchi za Afrika, bei ziliongezeka kwa asilimia 10.3 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 9.6 mwaka 2002.

Hali ya Uchumi wa Bara la Afrika
26. Nchi nyingi za Afrika zimepata mafanikio kutokana na utekelezaji wa sera thabiti za kukuza uchumi, ambazo zimesaidia kupunguza kasi ya upandaji bei, na kuleta nafuu ya madeni ya nje. Pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika bara la Afrika, nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, hali ya umaskini imezidi kuongezeka na imekuwepo tofauti kubwa katika hali ya ukuaji wa uchumi baina ya nchi kutokana na sababu mbalimbali, hususan, hali ya hewa, usalama na fursa za uwekezaji.

27. Pamoja na kuimarika kwa hali ya amani na usalama katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pato la nchi za Maziwa Makuu lilikua kwa asilimia 3.7 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2002. Ukuaji huo mdogo umetokana na ukame uliosababishwa na hali mbaya ya hewa iliyoathiri ukuaji wa sekta muhimu za uzalishaji, hususan, kilimo. Kwa upande wa Nchi za Pembe ya Kaskazini Mashariki, pato lilikua kwa asilimia 1.9 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 3.9 mwaka 2002. Ukuaji huo mdogo umesababishwa hasa na ukame na njaa katika nchi ya Ethiopia. Pamoja na matatizo ya uchumi yanayoikabili nchi ya Zimbabwe, pato la nchi za Kusini mwa Afrika lilikua kwa asilimia 2.4 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 2.3 mwaka 2002. Ongezeko kidogo la pato katika eneo hili limechangiwa hasa na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini Angola kutokana na kugundulika kwa maeneo mapya ya uzalishaji mafuta, pamoja na kuimarika kwa hali ya amani na usalama.

28. Nchi za Afrika ya Kati na Magharibi zilipata mafanikio makubwa kiuchumi katika mwaka 2003. Pato la nchi hizi lilikua kwa asilimia 6.4 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 3.4 mwaka 2002. Ukuaji huo mkubwa umetokana na ongezeko kubwa la uzalishaji wa mafuta nchini Nigeria. Kwa upande wa nchi za Kaskazini mwa Afrika, pato lilikua kwa asilimia 6.2 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 3.4 mwaka 2002. Ongezeko hilo la pato limechangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo kutokana na hali nzuri ya hewa, kuongezeka kwa matumizi ya serikali ya kuijenga upya Algeria baada ya kukumbwa na janga la tetemeko la ardhi, pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa mafuta nchini Algeria. Jedwali Na. 2.2 linaonyesha mwenendo wa viashirio muhimu katika uchumi jumla wa baadhi ya nchi za Afrika.

 

Jedwali Na.2.2:  Mwenendo wa Pato la Taifa, Kasi ya Upandaji Bei na Urari wa Malipo ya Kawaida kwa Baadhi ya Nchi za Afrika.

Nchi

Pato la Taifa

(Badiliko %)

Bei kwa Mlaji

 (Badiliko %)

Urari wa Malipo ya  Kawaida

(% ya Pato la Taifa)

2001

2002

2003

2001

2002

2003

2001

2002

2003

AFRIKA

3.6

3.4

4.1

13.0

9.6

10.3

-0.1

-1.7

-0.7

Kaskazini

Algeria

Morocco

Tunisia

4.1

3.4

6.2

2.6

2.1

2.2

7.2

4.5

6.0

2.1

4.1

6.7

4.2

1.4

2.6

12.9

7.8

11.3

6.5

3.2

5.5

0.6

2.8

1.2

4.8

4.1

3.1

5.2

1.7

6.1

1.9

2.8

2.7

-4.3

-3.5

-2.9

Kusini mwa Jangwa la Sahara

3.8

3.4

4.4

21.6

14.0

17.4

-3.9

-5.6

-4.0

Pembe ya Afrika

Ethiopia

Sudan

6.1

3.9

1.9

1.8

1.3

10.5

-7.4

-8.5

-7.3

7.7

1.2

-3.8

-7.1

-7.2

15.1

-4.2

-5.7

-4.7

5.3

6.0

5.8

4.9

8.3

7.7

-10.3

-9.7

-8.3

Nchi za Maziwa Makuu

DRC

Kenya

Tanzania

Uganda

2.3

4.6

3.7

54.6

8.8

7.7

-3.9

-3.0

-3.3

-2.1

3.5

5.0

356.7

27.7

9.1

-4.7

-2.7

-2.0

1.2

1.0

1.5

5.8

2.0

9.7

-3.5

-

-2.3

5.6

6.3

5.5

5.2

4.6

5.0

-1.5

-4.0

-2.6

5.5

6.7

4.9

4.5

5.7

5.9

-6.8

-6.3

-6.0

Kusini mwa Afrika

Angola

Zimbabwe

2.9

2.3

2.4

35.2

44.3

54.3

-4.8

-3.5

-3.7

3.2

15.3

4.5

152.6

108.9

98.3

-2.0

-5.8

-6.2

-8.8

-12.8

-13.2

76.7

140.0

431.7

-9.7

-2.2

-4.5

Afrika ya Kati na Magharibi

Ghana

Nigeria

4.0

3.4

6.4

12.0

8.4

9.7

-2.7

-7.0

-3.6

4.2

4.5

4.7

32.9

14.8

26.4

-6.6

0.5

-0.4

2.8

1.5

10.6

18.9

13.7

14.4

2.7

-10.7

-2.8

CFA franc zone

Cameroon

Cote d’ Ivoire

4.9

4.4

4.1

4.2

3.8

2.0

-6.7

-4.7

-4.1

5.3

6.5

4.2

2.8

6.3

1.2

-1.7

-7.2

-3.1

0.1

-1.6

-3.8

4.4

3.1

3.8

-2.0

6.2

4.9

Afrika ya Kusini

2.8

3.6

1.9

5.7

8.9

6.0

-0.1

0.3

-1.2

Nchi zinazonunua mafuta

3.8

3.1

3.0

11.9

8.9

9.6

-2.4

-1.9

-2.2

Nchi zinazouza mafuta

3.0

4.6

8.0

16.8

12.3

12.6

6.2

-1.1

3.4

Chanzo: Shirika la Fedha la Kimataifa, (IMF)

   
 
USHIRIKIANO WA KIUCHUMI KIMATAIFA  
 
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

29. Katika mwaka 2003, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeendelea kutekeleza mkakati wa maendeleo wa miaka mitano (2001-2005) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi wanachama na kutekeleza programu zilizopewa kipaumbele kama inavyoainishwa katika mwongozo wa utekelezaji. Juhudi zilielekezwa zaidi katika kukamilisha itifaki ya ushuru wa pamoja wa forodha. Maeneo muhimu yaliyokamilika katika itifaki hiyo ni pamoja na uondoaji wa ushuru wa bidhaa kwa biashara za ndani na utaratibu wa kuhakiki uasili wa bidhaa, uanzishaji wa mfumo mmoja wa ushuru wa forodha ambapo viwango vitakavyotumika ni asilimia 0, 10 na 25.

30. Mkutano wa nchi wanachama kuhusu maendeleo ya barabara za nchi za Afrika Mashariki ulifanyika mwezi Aprili, 2003 ambapo nchi wanachama na wahisani walikubaliana kuongeza juhudi katika kuendeleza miradi iliyoainishwa katika mtandao wa barabara. Upembuzi yakinifu kuhusu mpango wa miaka mitano wa kuendeleza na kuwekeza katika sekta ya hali ya hewa umeshaanza uwekezaji kwa miaka mitano ijayo. Utekelezaji wa Mpango Kamambe wa Nishati wa Afrika Mashariki uliendelea. Itifaki ya Maendeleo Endelevu ya Bonde la Ziwa Victoria ilisainiwa Novemba, 2003. Nchi wanachama zilikubaliana na mkakati wa utekelezaji na unasubiri kuridhiwa. Vilevile, mradi wa usimamizi na uendelezaji uvuvi katika ziwa Victoria ulizinduliwa Oktoba, 2003 mjini Jinja, Uganda. Mradi huu unalenga katika kuweka vifaa vya kuimarisha uvuvi endelevu katika ziwa Victoria.

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
31. Katika mwaka 2003, Tanzania ilikuwa mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC uliofanyika Dar es salaam Agosti, 2003. Wakuu wa Nchi na Serikali waliidhinisha mkakati wa mpango wa maendeleo (Regional Indicative Strategic Development Plan-RISDP) wa ushirikiano kwa kipindi cha miaka kumi na mitano ijayo. Ili kufanikisha ufuatiliaji na utekelezaji, mpango wa “RISDP” umeweka malengo na muda wa utekelezaji wa malengo hayo katika sekta mbalimbali za ushirikiano.

32. Nchi wanachama wa SADC walitia saini mkataba wa Ulinzi na Usalama ili kudumisha mahusiano, kuunganisha nguvu za utekelezaji wa malengo yaliyowekwa, pamoja na kuweka moja ya misingi imara katika suala zima la ulinzi na usalama katika bara la Afrika. Hali ya Kisiasa katika umoja wa nchi za SADC ilizidi kuimarika katika mwaka 2003 baada ya kusainiwa kwa mkataba wa kuleta amani Angola Aprili, 2002 na kuwekwa madarakani kwa serikali ya mpito katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Juni, 2003.

33. Pamoja na jitihada zilizochukuliwa na Nchi wanachama wa SADC kupunguza umaskini na kukuza maendeleo ya kijamii kikanda, bado changamoto ni kubwa. Kasi ya kupungua kwa umaskini bado hailingani na malengo ya kimataifa ya kupunguza umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015. Ongezeko la umaskini katika nchi za SADC limechangiwa na sababu nyingi zikiwa ni pamoja na ukame wa mara kwa mara, mafuriko, ukosefu wa amani na usalama, pamoja na magonjwa kama UKIMWI, malaria na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Mpango Mpya wa Ushirikiano wa Kusukuma Maendeleo ya Nchi za Afrika (NEPAD)
34. Katika mkutano wa pili wa Umoja wa Afrika uliofanyika Maputo, Msumbiji Julai, 2003 viongozi wa Afrika walikubaliana kuendelea kutimiza malengo ya NEPAD ili kuondoa umaskini na kukuza uchumi wa bara la Afrika. Tayari nchi 15 za Afrika zimeshajiunga na utaratibu unaotoa fursa kwa nchi kufanyiwa ukaguzi na kupimwa ufanisi wake katika kutekeleza vigezo vya uchumi na utawala bora (NEPAD Peer Review Mechanism). Mpango huo unasisitiza uimarishaji na uzingatiaji wa masuala ya uwazi, utawala bora, utekelezaji wa haki za binadamu na ufanisi katika uendeshaji uchumi. Mafanikio ya NEPAD katika mwaka 2003 yalionekana pia katika ushirikiano ulioonyeshwa na nchi zote za Afrika na jumuiya ya kimataifa. Aidha, wakuu wa Nchi na Serikali wa Ukanda wa Mashariki ya Afrika walikutana mjini Nairobi, Kenya Oktoba 2003 kujadili, kuchambua na kukubaliana kuhusu vigezo vya programu na miradi ya kupewa kipaumbele chini ya mpango wa NEPAD, utaratibu wa kuratibu programu na miradi ya kikanda, na jinsi ya kushirikisha sekta binafsi kwenye utekelezaji wa mpango wa NEPAD. Ili kuongeza ufanisi katika kuratibu programu na miradi ya kimaendeleo katika ukanda wa mashariki ya Afrika, Wakuu wa Nchi waliridhia Kenya kuwa mratibu wa programu na miradi ya kimaendeleo kikanda.

Ushirikiano wa Kiufundi baina ya Nchi Zinazoendelea (TCDC)
35. Mkutano wa 13 wa kamati ya ushirikiano wa kiufundi baina ya nchi zinazoendelea ulifanyika New York, Marekani Mei, 2003. Mkutano huu ulifanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya utekelezaji wa mpango mahsusi wa “Buenos Aires Plan of Action”. Ili kufuatilia maamuzi ya mkutano huo, kundi la nchi zinazoendelea (Group 77) pamoja na China zilikutana Desemba, 2003 nchini Morocco na kulikubali azimio la “Marrakesh” kama moja ya misingi ya makubaliano ya utekelezaji wa mpango wa Havana. Kuhusu ushirikiano wa kubadilishana ufundi, Serikali ilifaidika kutokana na misaada ya serikali ya China ambapo wataalam wa Kitanzania walihudhuria mafunzo nchini China katika maeneo yanayohusu utumiaji na utengenezaji wa vyombo vya hali ya hewa, utunzaji wa mazingira, utunzaji wa nafaka, ukulima wa mboga, teknolojia ya tarakishi, nishati ya maji, usindikaji wa vyakula na bidhaa, na teknolojia ya upimaji wa viwango.

Ushirikiano wa kirafiki kati ya nchi za Afrika na China
36. Mkutano wa pili wa mawaziri wa nchi za Afrika na China ulifanyika Addis Ababa, Ethiopia Desemba, 2003 kwa lengo la kuendeleza ushirikiano kati ya Afrika na China kiuchumi, kijamii na kisiasa. Katika mkutano huo, mpango wa utekelezaji wa Addis Ababa kwa mwaka 2004-2006 (Addis Ababa Action Plan 2004-2006) ulipitishwa. Katika mpango huo nchi ya China imepanga kutoa mafunzo kwa wataalamu zaidi ya 10,000 kutoka katika bara la Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kuongeza ujuzi wa wafanyakazi katika bara la Afrika. Pamoja na hayo, China iliahidi pia kuondoa kodi kwa baadhi ya bidhaa zinazoingia ndani ya nchi hiyo kutoka Afrika.

Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kwa ajili ya Maendeleo ya Afrika (TICAD)
37. Mwaka 2003, TICAD ilitimiza miaka kumi kwa mkutano wa TICAD III kufanyika Tokyo, nchini Japan. Maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na; usalama, utawala bora, kilimo, maendeleo ya sekta binafsi, miundombinu, rasilimali watu, afya, maji, ushirikiano wa kikanda na ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Asia. TICAD III ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia juhudi za Afrika za kuleta maendeleo. Mikakati ya Tanzania ya maendeleo kama ilivyoanishwa katika Dira ya Taifa 2025 inawiana na maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mpango wa TICAD. Hivyo, agenda ya Serikali katika utekelezaji wa TICAD inawiana pia na mpango wa taifa wa kupunguza umaskini.

Mpango wa Marekani wa Kusaidia Maendeleo ya Afrika (AGOA)
38. AGOA ni mpango ulioanzishwa na serikali ya Marekani mwaka 2000 kwa lengo la kusaidia nchi za Kiafrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara kuongeza mauzo ya bidhaa zao kwenye soko la Marekani kwa kutotozwa ushuru au kutowekewa kiwango. Mpango huu umebuniwa ili kuziwezesha nchi hizi kuongeza mapato yao ya fedha za kigeni na hivyo kuimarisha uwezo wao wa kupunguza umaskini. Tanzania kwa upande wake bado haijaweza kunufaika vizuri kutokana na fursa hii ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine zilizoko katika mpango huu. Matatizo yanayochangia hali hii ni kutokuwepo kwa uzalishaji wa bidhaa nyingi na zenye ubora unaotakiwa na soko la Marekani, udhaifu wa miundombinu, na ufahamu mdogo wa wadau kuhusu soko lenyewe. Kwa kufahamu matatizo hayo, Serikali ikishirikiana na sekta binafsi imebuni na kutekeleza mikakati ambayo italetea kufanikisha azma hii. Baadhi ya mikakati iliyobuniwa na kutekelezwa ni pamoja na kuwaelimisha wadau juu ya masharti na mbinu za kujipenyeza kwenye soko hilo, kutoa vivutio kwa wawekezaji wenye nia ya kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko hilo, na kuanzisha na kuendeleza maeneo huru ya uzalishaji bidhaa za kuuza nje (EPZ). Kutokana na mikakati hii, tayari baadhi ya wadau wameshaanza kunufaika na fursa hii. Viwanda vya Sunflag na Star Apparel vimeshaanza kuuza bidhaa za nguo Marekani. Kwa mwaka 2003, bidhaa zenye thamani ya dola 1.5 milioni ziliuzwa Marekani. Vile vile, kumekuwepo na mauzo ya nyuzi Mauritius kwa ajili ya utengenezaji wa nguo za kuuza Marekani chini ya mradi wa AGOA.

Shirika la Kimataifa la Biashara (WTO)
39. Mkutano wa tano wa Mawaziri wa Shirika la Kimataifa la Biashara (WTO) ulifanyika Cancun Mexico Septemba 10 – 14 mwaka 2003 na lengo likiwa ni kuendeleza na kukamilisha majadiliano ya biashara yaliyotokana na mkutano wa nne yajulikanayo kama Agenda ya Maendeleo ya Doha. Hata hivyo, mkutano huo ulifungwa bila kufikia makubaliano katika mambo mengi muhimu. Mambo yaliyokwamisha mafanikio ya mkutano huo yalikuwa ni pamoja na masuala ya ruzuku katika kilimo ambapo nchi zinazoendelea zilitaka nchi zilizoendelea kuondoa ruzuku zinazotoa kwa wakulima wao ili bidhaa zao ziwe na ushindani sawa katika soko. Nchi zilizoendelea hazikukubaliana na matakwa ya nchi zinazoendelea katika suala hili. Jambo la pili na la msingi lililokwamisha majadiliano lilikuwa ni juu ya kuendeleza majadiliano kwa masuala ya Singapore yanayojumuisha biashara na vitega uchumi, biashara na sera ya ushindani, uwazi katika manunuzi ya Serikali na usaidizi wa kibiashara. Katika masuala haya, nchi zinazoendelea hazikutaka majadiliano yaanze wakati zile zilizoendelea zilitaka kuendeleza majadiliano. Mkutano ulivunjika baada ya nchi zinazoendelea kutokubaliana na mpango wa kuanza majadiliano katika mambo haya. Kutokana na msimamo ulionyeshwa na nchi zinazoendelea huko Cancun Mexico, nchi zilizoendelea zimekubali kuondoa katika meza ya majadiliano masuala matatu ya Singapore hasa biashara na vitega uchumi, pamoja na biashara na sera za ushindani. Hata hivyo, juhudi kubwa zinafanyika katika ngazi ya WTO ili kuhakikisha kuwa majadiliano katika mambo muhimu yanaendelea kwa lengo la kufikia makubaliano yatakayoboresha mazingira ya biashara duniani. Tanzania kwa upande wake iliendelea kushirikiana na nchi nyingine zinazoendelea katika kudai maslahi mazuri zaidi kutoka kwa nchi zilizoendelea.