MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA

Hali ya Uchumi wa Taifa
Hali ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa
Sekta ya Nje
Fedha za Serikali
Fedha na Taasisi za Fedha
Rasilimali Watu

   
HALI YA UCHUMI WA TAIFA
Ukuaji wa Uchumi

1.Katika mwaka 2003, Pato la Taifa halisi lilikua kwa asilimia 5.6 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.2 mwaka 2002. Upungufu huu ulitokana na kushuka kwa viwango vya ukuaji wa sekta za kilimo; uuzaji jumla, reja reja na mahoteli (ikijumuisha utalii); mawasiliano na uchukuzi; na fedha na huduma za bima. Hata hivyo, viwango vya ukuaji wa sekta za madini na uchimbaji mawe; bidhaa za viwandani na umeme na maji viliongezeka. Viwango vya ukuaji wa sekta za ujenzi na uendeshaji serikali na huduma nyingine viliendelea kubaki kama vile vya mwaka 2002.

2.Pato la Taifa mwaka 2003 lilikuwa sh. 9,811,553 milioni kwa bei za mwaka huo au sh. 1,962,040 milioni kwa bei za mwaka 1992. Idadi ya watu Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa milioni 34.2 mwaka 2003 kutokana na ongezeko la watu la asilimia 2.9 kwa mwaka. Pato la wastani la kila mtu lilikuwa sh. 286,887 kwa bei za mwaka 2003 au sh. 57,370 kwa bei za mwaka 1992. Ongezeko halisi la Pato la wastani kwa kila mtu (kwa bei za mwaka 1992) lilikuwa sh. 2,097, sawa na asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 4.0 mwaka 2002.

3. Sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 4.0 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 5.0 mwaka 2002. Kupungua kwa ukuaji wa sekta hii kulitokana hasa na kushuka kwa uzalishaji katika sekta ndogo ya mazao, (baadhi ya mazao ya chakula – mahindi, mpunga na maharage na baadhi ya mazao ya biashara tumbaku, pareto na kahawa) ambapo sekta hii ndogo ilikua kwa kiwango cha asilimia 3.6 ikilinganishwa na asilimia 5.3 mwaka 2002. Kushuka kwa uzalishaji wa sekta ndogo ya mazao kulisababishwa na ukame katika maeneo mengi ya nchi. Aidha, sekta ndogo ya uvuvi nayo pia ukuaji wake ulishuka kutoka asilimia 6.5 mwaka 2002 hadi asilimia 6.4 mwaka 2003. Kiwango cha ukuaji wa sekta ndogo ya misitu na uwindaji kiliongezeka kutoka asilimia 3.0 mwaka 2002 hadi asilimia 4.2 mwaka 2003. Sekta ndogo ya mifugo ilikua kwa asilimia 5.0 ikilinganishwa na asilimia 3.5 mwaka 2002. Kwa upande wa sehemu ya sekta ya kilimo isiyouzika, ilikua kwa asilimia 3.8 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 3.9 mwaka 2002. Pamoja na kushuka kwa kiwango cha ukuaji wa sekta ya kilimo bado mchango wake katika uchumi wa nchi ulikuwa mkubwa ikilinganishwa na sekta nyingine. Katika mwaka 2003, sekta ya kilimo ilichangia asilimia 46.8 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 47.5 mwaka 2002.

4. Sekta ya bidhaa za viwandani ilikua kwa asilimia 8.6 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 8.0 mwaka 2002. Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika baadhi ya viwanda mbalimbali kama saruji, chuma, aluminiamu, rangi, bati na vyakula (tambi, biskuti, unga wa ngano). Aidha, kuongezeka huku kunatokana pia na kupungua kwa gharama za uzalishaji na kuimarika kwa baadhi ya viwanda vilivyobinafsishwa pamoja na ongezeko la viwanda vipya katika uchumi. Mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa umeongezeka hadi kufikia asilimia 8.6 mwaka 2003 kutoka asilimia 8.4 mwaka 2002.

5. Sekta ya madini na uchimbaji mawe ilikua kwa asilimia 17.0 mwaka 2003 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 15.0 mwaka 2002. Kuongezeka kwa ukuaji wa sekta hii kunatokana na kukamilika kwa uwekezaji katika baadhi ya miradi mikubwa ya uchimbaji na utafutaji madini hivyo kuimarika kwa uzalishaji. Mchango wa sekta ya madini na uchimbaji mawe mwaka 2003 uliongezeka hadi kufikia asilimia 3.0 kutoka asilimia 2.9 mwaka 2002.

6. Sekta ya biashara (ikijumuisha mahoteli, utalii, uuzaji jumla na reja reja) ilikua kwa asilimia 6.5 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2002. Kushuka kwa sekta hii kulitokana na hali ya wasiwasi kiusalama ulimwenguni kulikosababishwa na matishio ya ugaidi katika nchi mbalimbali. Mchango wa sekta katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 16.8 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 16.6 mwaka 2002.

7. Sekta ya ujenzi ilikua kwa asilimia 11.0 mwaka 2003, kiwango ambacho ni sawa na kile cha mwaka 2002. Ukuaji huu ulitokana na ujenzi wa majengo yasiyo ya kuishi, ujenzi wa barabara, uendelezaji ardhi ikijumuisha ujenzi wa nyumba za kuishi. Mchango wa sekta ya ujenzi katika Pato la Taifa mwaka 2003 ulikuwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 5.0 mwaka 2002.

8. Sekta ya mawasiliano na uchukuzi ilikua kwa asilimia 5.1 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 6.4 mwaka 2002. Kushuka huku kwa ukuaji wa sekta hii kulitokana na ukuaji mdogo katika sekta ndogo za uchukuzi na mawasiliano kwa asilimia 5.7 na 4.0 mwaka 2003 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.9 na 7.3 mwaka 2002, kwa mtiririko huo. Mchango wa sekta ya mawasiliano na uchukuzi katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 5.4 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 5.5 mwaka 2002.

9. Sekta ya umeme na maji ilikua kwa asilimia 4.9 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 3.1 mwaka 2002. Kuongezeka kwa ukuaji kulitokana na kukua kwa sekta ndogo ya umeme kutoka asilimia 3.0 mwaka 2002 hadi kufikia asilimia 5.0 mwaka 2003 kulikosababishwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta. Sekta ndogo ya maji ilikua kwa asilimia 3.7 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 3.8 mwaka 2002. Kupungua huku kwa ukuaji wa sekta ya maji kulitokana na ukame katika baadhi ya maeneo ya nchi katika kipindi cha mwaka 2003. Mchango wa sekta ya umeme na maji katika Pato la Taifa kwa mwaka 2003 ulikuwa asilimia 1.6, sawa na ilivyokuwa katika mwaka 2002.

10. Sekta ya huduma za fedha, bima na mali ilikua kwa asilimia 4.4 mwaka 2003 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 mwaka 2002. Kupungua kwa ukuaji wa sekta hii kulitokana na kushuka kwa sekta ndogo za fedha na bima na upangishaji majengo kwa asilimia 3.2 na 5.1 mwaka 2003 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.0 na 5.3 mwaka 2002, kwa mtiririko huo. Kwa upande wa sekta ndogo ya huduma za kibiashara, ukuaji uliongezeka kidogo kutoka asilimia 5.4 mwaka 2002 hadi asilimia 5.5 mwaka 2003. Sekta hii ilichangia kiasi cha asilimia 9.9 katika Pato la Taifa mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 10.0 mwaka 2002.

11. Sekta ya uendeshaji serikali na huduma nyingine ilikua kwa asilimia 4.1 mwaka 2003, kiwango ambacho ni sawa na ilivyokuwa mwaka 2002. Pamoja na kiwango cha ukuaji kuwa sawa katika miaka miwili mfululizo, sekta ndogo za utawala na afya zilikuwa kwa asilimia 2.5 na 6.5 kwa mwaka 2003 kutoka ukuaji wa asilimia 2.3 na 6.0 mwaka 2002, kwa mtiririko huo. Sekta ndogo za elimu na huduma nyinginezo zilikua kwa asilimia 7.0 na 5.4, viwango ambavyo ni pungufu ya vile vilivyofikiwa katika mwaka 2002 vya asilimia 8.0 na 5.5, kwa mtiririko huo. Mchango wa sekta ya uendeshaji serikali na huduma nyingine katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 7.2 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 7.3 mwaka 2002. Majedwali 1 – 4D yanaonyesha mchanganuo wa ukuaji wa Pato la Taifa.

Kasi ya upandaji bei

12. Kasi ya upandaji bei iliendelea kushuka hadi wastani wa asilimia 4.4 mwaka 2003 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 4.5 mwaka 2002, licha ya kupanda kwa bei ya mafuta, ukame na kushuka kwa thamani ya shilingi. Kushuka huko kwa sehemu kubwa kunatokana na kudhibiti ujazi wa fedha na matumizi ya serikali. Kiwango kidogo cha kushuka kwa kasi ya upandaji bei mwaka 2003 kimetokana na uhaba wa chakula uliojitokeza nchini kufuatia kuwepo kwa mvua zisizotosheleza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula hasa ikizingatiwa kuwa chakula huchukua sehemu kubwa (asilimia 71.2) katika kapu la bidhaa za walaji.

13. Pamoja na kwamba kasi ya upandaji bei iliendelea kupungua, fahirisi ya bei kwa baadhi ya bidhaa na huduma ziliongezeka. Hata hivyo, ongezeko hilo halikuweza kuathiri wastani wa kitaifa kutokana na bidhaa hizo kuwa na uzito mdogo katika kapu la walaji. Bei za bidhaa na huduma katika makundi ya kodi ya nyumba, huduma za afya, na mahitaji ya nyumbani ziliongezeka na kuzidi wastani wa kitaifa kutoka asilimia 1.6, 3.5 na 1.4 mwaka 2002 hadi asilimia 4.5, 5.9 na 5.3 mwaka 2003, kwa mtiririko huo. Viwango vya ongezeko la bei katika makundi ya usafiri, michezo na starehe, fenicha na vyombo vya nyumbani, vinywaji na sigara, na chakula pia viliongezeka kuwa asilimia 2.5, 2.1, 4.4, 3 na 4.2 mwaka 2003 ikilinganyishwa na asilimia 2.1, 1.8, 3.9, 2.7 na 4.1 mwaka 2002, kwa mtiririko huo. Kwa makundi yaliyobaki, viwango vya ongezeko la bei vilipungua mwaka 2003 ikilinganishwa na mwaka 2002 kama ifuatavyo (ongezeko la mwaka 2002 katika mabano): Maji, mafuta ya taa na umeme-asilimia 8.6 (14.5), nguo na viatu asilimia 3.8 (6.4), na elimu asilimia 3.5 (3.7).

14. Uchambuzi wa mabadiliko katika fahirisi za bidhaa na huduma kwa tabaka mbalimbali za wananchi kimapato unaonesha kuwa fahirisi hiyo iliongezeka kwa kiwango karibu sawa katika kundi la watu wa kipato cha juu. Katika kundi hili, fahirisi ya bei iliongezeka kwa asilimia 6.6 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2002. Katika makundi ya watu wa kima cha chini na kati, fahirisi ya bei ilipanda kwa asilimia 4.8 na 7.1 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 7.3 na 9.9 mwaka 2002 kwa mtiririko huo.

15. Kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, kasi ya upandaji bei ilishuka katika huduma za afya kwa wakazi wote bila kujali vipato vyao. Fahirisi ya vinywaji na sigara ilipanda kwa watu wa kipato cha kati na juu kutokana na kupanda kwa bei ya bia ambayo hutumiwa kwa wingi na watu hao. Pamoja na ukame uliokuwepo, bado bei ya chakula haikuweza kuathirika sana kutokana na juhudi za serikali kusaidia kupatikana na kusambaza chakula. Fahirisi ya bei ya chakula kwa wakazi wa Dar es Salaam wa kima cha chini na kati iliongezeka kwa asilimia 3.3 na 6.6 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 7.1 na 11.9 mwaka 2002, kwa mtiririko huo. Kima cha juu, fahirisi ya bei ya chakula ilipanda kwa asilimia 4.7 mwaka 2003 ikilinganishwa na mwaka 2002 ambapo fahirisi ya bei ilishuka kwa asilimia 2.8

Ukuzaji rasilimali

16. Ukuzaji rasilimali uliongezeka kutoka sh. 454,214 milioni mwaka 2002 hadi sh. 481,328 milioni mwaka 2003, kwa bei za mwaka 1992. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 6.0 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 19.0 mwaka 2002. Mwaka 2003, uwiano wa ukuzaji rasilimali na Pato la Taifa ulikuwa asilimia 24.5 kwa bei za mwaka 1992, sawa na ilivyokuwa katika mwaka 2002. Ukuzaji rasilimali kwa bei za miaka husika uliongezeka kwa kiasi cha asilimia 10.2 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 28.5 mwaka 2002.

17. Ukuzaji rasilimali katika shughuli za ujenzi wa majengo uliongezeka kutoka sh. 137,647 milioni mwaka 2002 hadi sh. 181,775 milioni mwaka 2003. Kiwango cha ukuaji katika shughuli za ujenzi wa majengo kilikua kutoka asilimia 15.5 mwaka 2002 hadi asilimia 32.1 mwaka 2003. Ongezeko hili kubwa lilitokana na ukuzaji rasilimali katika sekta ndogo ya majengo yasio ya kuishi ulioongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 21.8 mwaka 2002 hadi asilimia 75.4 mwaka 2003, kutokana na ujenzi wa majengo ya shule za msingi, na nyumba za kibiashara. Ukuzaji rasilimali katika sekta ndogo za majengo ya kuishi na ujenzi vijijini ulipungua kwa asilimia 3.5 na 7.0 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 10.7 na 12.7 mwaka 2002, kwa mtiririko huo.

18. Shughuli nyingine za ujenzi (barabara na madaraja, uendelezaji ardhi, na maji) ziliongezeka kutoka sh. 86,470 milioni mwaka 2002 hadi sh. 96,674 milioni mwaka 2003 kwa bei za mwaka 1992, sawa na ongezeko la asilimia 11.8 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 68.4 mwaka 2002. Kushuka kwa ongezeko katika shughuli nyingine za ujenzi kulitokana na kupungua kwa ukuaji katika shughuli za uendelezaji ardhi, barabara na madaraja na maji kutoka asilimia 312.3, 68.0 na 103.6 mwaka 2002 hadi asilimia 62.3, 30.6 na 17.7 mwaka 2003, kwa mtiririko huo.

19. Uagizaji vifaa nchini ulipungua kutoka sh. 225,356 milioni mwaka 2002 hadi sh. 198,234 milioni mwaka 2003. Thamani ya ununuzi wa vifaa vya usafiri ilipungua kwa kiwango cha asilimia 16.5 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 14.5 mwaka 2002. Aidha, ununuzi wa mitambo na vifaa vinginevyo ulipungua kwa asilimia 8.5 mwaka 2003 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.8 mwaka 2002.

20. Uwekezaji katika rasilimali ya kudumu ambayo inajumuisha rasilimali za majengo, shughuli nyingine za ujenzi na vifaa uliongezeka kutoka sh. 449,474 milioni mwaka 2002 hadi sh. 476,683 milioni mwaka 2003, kwa bei za mwaka 1992, sawa na ongezeko la asilimia 6.1.

21. Limbikizo la rasilimali kwa bei za mwaka 1992 lilipungua kwa asilimia 2.0 mwaka 2003, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 15.0 mwaka 2002. Thamani ya limbikizo ilikuwa sh. 4,739 milioni mwaka 2002 ikilinganishwa na sh. 4,645 milioni mwaka 2003. Limbikizo la rasilimali kwa bei za miaka husika lilipungua kutoka sh. 17,854 milioni mwaka 2002 hadi shs. 17,498 milioni mwaka 2003, sawa na upungufu wa asilimia 2.0 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 14.9 mwaka 2002.

22. Ukuzaji rasilimali katika sekta binafsi uliongezeka kutoka sh. 1,073,938 milioni mwaka 2002 hadi sh. 1,184,036 milioni mwaka 2003 kwa bei za miaka husika, sawa na ongezeko la asilimia 10.3. Mchango wa sekta binafsi katika ukuzaji rasilimali ulikuwa asilimia 59.5 mwaka 2003 ikilinganishwa na asilimia 59.4 mwaka 2002. Ukuzaji rasilimali katika sekta ya umma uliongezeka kutoka sh. 715,958 milioni mwaka 2002 hadi shs. 790,018 milioni mwaka 2003 kwa bei za miaka husika, sawa na ongezeko la asilimia 10.3. Mchango wa sekta ya umma katika ukuzaji rasilimali kwa mwaka 2003 ulikuwa asilimia 39.7 ikilinganishwa na asilimia 39.6 mwaka 2002.

Jedwali Na. 1 (PATO LA TAIFA (GDP) KISEKTA KWA GHARAMA ZAKE)

Jedwali Na. 1A( PATO LA TAIFA (GDP) KISEKTA, KWA GHARAMA ZAKE - SEHEMU INAYOUZIKA NA ISIYOUZIKA( Kwa bei za miala inayohusika))

Jedwali Na. 2(MCHANGO WA SEKTA KWA PATO LA TAIFA (% of GDP) KWA GHARAMA ZAKE)

Jedwali Na. 2A(MCHANGO WA SEKTA KWA PATO LA TAIFA (% of GDP) KWA GHARAMA ZAKE - SEHEMU INAYOUZIKA NA ISIYOUZIKA( Kwa bei za miaka inayohusika))

Jedwali Na. 2B(PATO LA TAIFA NA MATUMIZI YAKE KWA BEI ZA SOKO)

Jedwali Na. 3(PATO LA TAIFA (GDP) KISEKTA KWA GHARAMA ZAKE )

Jedwali Na. 3A(PATO LA TAIFA (GDP) KISEKTA KWA GHARAMA ZAKE - SEHEMU INAYOUZIKA NA ISIYOUZIKA)

Jedwali Na. 4(UKUAJI WA PATO LA TAIFA (PTL) KISEKTA, KWA GHARAMA ZAKE )

Jedwali Na. 4A(UKUAJI HALISI WA PATO LA TAIFA (REAL GDP GROWTH) KI SEKTA KWA GHARAMA ZAKE - SEHEMU INAYOUZIKA NA ISIYOUZIKA)

Jedwali Na. 4B(MCHANGO WA SEKTA KWA PATO LA TAIFA (PTL), Kwa gharama zake ( Bei za mwaka 1992))

Jedwali Na. 4C(MCHANGO WA SEKTA KWA PATO LA TAIFA (% of GDP) KWA GHARAMA ZAKE - SEHEMU INAYOUZIKA NA ISIYOUZIKA)

UKUAJI WA PATO LA TAIFA

Jedwali Na. 5(UKUZAJI RASILIMALI KWA AINA YA SHUGHULI)

Jedwali Na. 6(UKUZAJI RASILIMALI KWA AINA YA SHUGHULI)

Jedwali Na. 7(UKUZAJI WA RASILIMALI KATIKA SEHEMU ZA UCHUMI WA KITAIFA NA BINAFSI)

Jedwali Na. 8( FAHIRISI YA BEI ZA REJAREJA YA BIDHAA ZITUMIWAZO NA WATU WA KIPATO CHA CHINI DAR-ES-SALAAM (1994=100))

Jedwali Na. 9(FAHIRISI YA BEI ZA REJAREJA YA BIDHAA ZITUMIKAZO NA WATU WA KIPATO CHA CHINI DAR ES SALAAM (1994 =100))

Jedwali Na. 10( FAHIRISI YA BEI YA BIDHAA NA HUDUMA ZITUMIWAZO NA WAFANYAKAZI WA KIMA CHA KATI - DAR-ES-SALAAM (1994 =100))

Jedwali Na. 11( FAHIRISI YA BIDHAA NA HUDUMA ZITUMIWAZO NA WAFANYAKAZI WA KIMA CHA KATI DAR-ES-SALAAM (1994 =100))

Jedwali Na. 12(FAHIRISI YA GHARAMA YA MAISHA YA WENYE KIPATO CHA JUU DAR-ES-SALAAM (1994 =100))

Jedwali Na. 13(FAHIRISI YA GHARAMA YA MAISHA YA WENYE KIPATO CHA JUU DAR-ES-SALAAM (1994=100))

Jedwali Na. 14( FAHIRISI YA BEI YA BIDHAA NA HUDUMA ZITUMIWAZO NA WAKAZI WA MIJINI - TANZANIA BARA (DEC.1994=100))

MWENENDO WA KASI YA UPANDAJI BEI-Tanzania Bara