| |
Hali
ya Magonjwa kwa Jumla
274. Kumekuwa na ongezeko la wagonjwa
wa kifua kikuu kutoka wagonjwa 63,048 mwaka 2002 hadi wagonjwa 63,211
mwaka 2003, sawa na ongezeko la chini ya asilimia 1. Upande wa ukoma wagonjwa
wamepungua kwa asilimia 17.6 kutoka wagonjwa 7,007 mwaka 2002 hadi wagonjwa
5,771 mwaka 2003. Ugonjwa wa malaria unaendelea kuwa tatizo kubwa na unahitaji
jitihada za ziada ili kuukabili kikamilifu. Msisitizo umekuwa katika utoaji
wa tiba sahihi kwa wagonjwa wa malaria kwa kutumia dawa ya SP (sulfadoxine/pyrimethamine)
na kufanya utafiti wa dawa nyingine za kuutibu. Aidha, mpango wa kuongeza
matumizi ya vyandarua kwa bei nafuu kwa mama wajawazito na watoto walio
chini ya mwaka mmoja umekamilika. Utekelezaji wa majaribio wa mpango huo
unaendelea katika wilaya ya Kilosa na Kibaha.
UKIMWI
275. Ugonjwa wa UKIMWI bado unaendelea kuwa tatizo kubwa hapa nchini na
katika nchi jirani. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2002 watu takribani
milioni 2 walikuwa wakiishi na virusi vya UKIMWI. Kati yao, watu 400,000
– 500,000 wapo katika hatua ya ugonjwa ya kuhitaji madawa ya kupunguza
makali ya UKIMWI. Tatizo hili la UKIMWI linaongezea mzigo mkubwa kwa huduma
za afya nchini kwa vile asilimia 40-50 ya vitanda vya hospitalini vimekaliwa
na wagonjwa hao. Mwaka 2002, wagonjwa wa UKIMWI wapatao 12,675 walipata
huduma mbalimbali kwenye vituo vya huduma za afya nchini kote.
Elimu
ya Afya kwa Wananchi na Afya ya Mazingira
276. Elimu ya afya imeendelea kutolewa kwa wananchi kwa njia ya radio,
magazeti na televisheni. Aidha, tafiti zimefanyika juu ya athari ziwapatazo
wafanyakazi viwandani, mashambani na katika sekta za ujenzi na kubaini
kuwa athari za afya na magonjwa mengi huwapata wafanyakazi ambao hutumia
kemikali. Kwa hiyo, miongozo ya utekelezaji wa huduma za afya ya mazingira
iliandaliwa ili kuleta changamoto kwa wadau wa afya ya mazingira katika
utoaji huduma.
Afya
ya Mama na Mtoto
277. Jitihada za kupunguza vifo vya watoto, hasa wenye umri wa chini ya
miaka mitano na mama wajawazito ziliendelea. Huduma zilitolewa kwa wanawake
wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ikiwemo chanjo na uzazi wa
mpango pamoja na kujifungua. Aidha, mafunzo yalitolewa kuhusu afya ya
mama na mtoto kwa watoa huduma mbalimbali zikiwepo zile za matibabu ya
tahadhari na kutoa kinga kwa wajawazito dhidi ya malaria, matibabu ya
dharura kwa wazazi na mafunzo rejea kuhusu uzazi wa mpango ambapo kwenye
vituo vya kutolea huduma vya serikali zilitolewa bila malipo. Mafunzo
hayo yanalenga kuongeza stadi za matibabu ya magonjwa yale yanayosababisha
zaidi vifo kwa watoto ambayo ni malaria, vichomi, kuharisha, surua, upungufu
wa damu na utapiamlo. Kufikia mwaka 2003, wilaya 72 zinatekeleza mkakati
huo na zaidi ya wahudumu 1,226 katika wilaya 46 walipatiwa mafunzo.
278. Viwango vya chanjo katika mwaka 2003
vilikuwa vya kuridhisha. Chanjo ya kifua kikuu ilifikia asilimia 88, polio
asilimia 91, kifaduro, pepopunda na homa ya ini asilimia 89, na surua
asilimia 89. Jumla ya majokofu mapya 1,003 yanayotumia gesi yalinunuliwa
na kupelekwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Singida, Mbeya, Iringa na Ruvuma
badala ya majokofu ya zamani yaliyokuwa yanatumia mafuta ya taa.
Chakula
na Lishe
279. Taasisi ya Chakula na Lishe iliendelea kutoa ushauri wa kitaalam
kwa wilaya na kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini ili kuboresha
afya na lishe ya jamii. Utafiti uliofanyika nchi nzima ulionyesha kwamba,
tatizo la uvimbe wa tezi la shingo kwa sasa linaathiri asilimia 8 ya Watanzania.
Aidha, utafiti huo pia uliangalia upatikanaji wa chumvi yenye madini joto
katika ngazi ya kaya na kuonekana ya kuwa asilimia 83.8 ya kaya zinatumia
chumvi yenye madini joto. Kiwango hiki kipo chini ya kigezo cha Shirika
la Afya Duniani (WHO) ambacho ni asilimia 90.
UKIMWI
na Lishe
280. Mafunzo na ushauri nasaha kuhusu unyonyeshaji na ulishaji watoto
kwa wakati huu wa UKIMWI yalitolewa kwa wafanyakazi 39 wa Afya katika
mikoa ya Arusha, Manyara na Iringa. Aidha, vijitabu, vipeperushi na mabango
vinavyoelezea njia mbadala za ulishaji watoto vilichapishwa na kusambazwa.
Vile vile, kutokana na tafiti mbalimbali kuonyesha uhusiano mkubwa kati
ya lishe na uambukizo wa virusi vya UKIMWI, mwongozo wa kitaifa wa lishe
kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ulitayarishwa.
Mfuko
wa Afya ya Jamii (CHF)
281. Utaratibu wa kuelimisha na kuhamasisha halmashauri za wilaya kuanzisha
CHF unaendelea. Wilaya 88 zimeelimishwa na kuhamasishwa kuunda bodi za
afya za halmashauri na kamati mbalimbali za afya kama vyombo vya usimamizi
wa huduma za afya wilayani. Halmashauri 23 zinatekeleza utaratibu huu
wa CHF na nyingine 17 zinakamilisha taratibu ili waanze utekelezaji. Faida
zilizopatikana kwa kuanzisha mfuko huu ni pamoja na upatikanaji wa dawa,
ukarabati wa majengo na vifaa vya tiba, ulinzi wa dawa toka kwa wananchi
wenyewe, na uimarishaji wa ushirikishwaji wa wananchi kuhusu afya zao.
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
282. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya uko katika mwaka wake wa tatu wa utekelezaji.
Idadi ya wanachama wa mfuko ilifikia 242,508 mwaka 2003 ikilinganishwa
na 167,989 mwaka 2002, sawa na ongezeko la asilimia 44.4. Jumla ya wananchama
210,152 kati ya 242,508 tayari walikwisha kamilisha taratibu za ujazaji
wa fomu ikiwa ni asilimia 86.7 ya wanachama wote na hivyo kustahili kupatiwa
vitambulisho. Aidha, vituo 3,551 vya matibabu vilisajiliwa na Mfuko kuhudumia
wanachama, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na vituo 3,415
vilivyokuwepo mwaka 2002. Vituo hivi vinajumuisha vituo 3,060 vya serikali,
na 491 vya madhehebu ya dini. Jumla ya maduka ya dawa 33 yamekwisha sajiliwa
kutoa huduma za dawa katika mikoa 20 ikilinganishwa na maduka mawili 2
yaliyosajiliwa katika mwaka wa fedha wa 2002/03.
Vituo
vya Kutolea Tiba
283. Katika harakati za kuboresha utoaji wa huduma za afya, kumekuwa na
mtandao mzuri wa vituo vya kutolea huduma nchi nzima. Katika mwaka 2003,
kumekuwa na ongezeko la zahanati 233 na vituo vya afya 16 vilivyojengwa
na halmashauri na nguvu za wananchi. Pia, masanduku ya dawa yalipelekwa
kwenye vituo hivyo. Jumla ya vituo 87 vilivyo chini ya mashirika ya kujitolea
na watu binafsi vimesajiliwa katika mwaka 2003. Aidha, serikali imeongeza
ruzuku ya vitanda kwa hospitali za mashirika ya dini kutoka sh. 7,500
mpaka sh.15,000 kwa kitanda kwa mwaka.
Mafunzo
ya Afya
284. Katika jitihada za kuongeza ufanisi katika fani mbalimbali za afya,
Wizara imepeleka mafunzoni Madaktari Wasaidizi 154, Waganga 694, Wauguzi
daraja “A” 454, daraja “B” 429, Wauguzi wakunga
184, Mabwana Afya 11 pamoja na Mabwana Afya Wasaidizi 62.
Jedwali
Na.84(VYOMBO VYA AFYA NCHINI)
Jedwali
Na.85(WALIOFAULU MAFUNZO)
Jedwali
Na.86(MATUMIZI YA VYOMBO VYA AFYA)
Jedwali
Na.87(IDADI YA WATAALAM WA AFYA )
Jedwali
Na.87A(IDADI YA VITANDA KATIKA HOSPITALI ZOTE NCHINI - 2002)
|
|