MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI
   

Kilimo
Maliasili na Utalii
Madini
Viwanda na Biashara
Ujenzi wa Maendeleo ya Ardhi
Mawasiliano na Uchukuzi
Nishati
Maji
Elimu na Mafunzo
Afya
Maendeleo ya Jamii

         
ELIMU NA MAFUNZO
Utangulizi

266. Katika mwaka 2003, Serikali iliendelea kuimarisha ubora wa elimu kwa kutoa vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia; kukarabati madarasa na kujenga mapya. Aidha, ilitoa mafunzo kwa walimu ambao hawajahitimu, kuongeza uwezo kwa wale walioko kazini, na kuajiri walimu wapya ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi. Pia, iliimarisha uongozi na utawala wa shule na asasi zake, na kufundisha walimu, wanafunzi na wafanyakazi wengine juu ya kinga dhidi ya UKIMWI, na utunzaji wa mazingira ya shule. Vile vile, wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya dini na watu binafsi walijitolea kwa njia mbalimbali katika utoaji wa elimu katika ngazi zote (elimu ya awali, msingi, sekondari, ualimu, na elimu ya juu).

Elimu ya Awali
267. Katika mwaka 2003, shule za awali zilikuwa 11,846, kati ya hizo shule 6,948 zilikuwa za serikali na 4,898 zilikuwa za watu binafsi. Katika mwaka 2002, shule za awali zilikuwa 9,569 ambapo shule 5,261 zilikuwa za serikali na 4,308 zilikuwa za watu binafsi. Sambamba na ongezeko la shule, idadi ya wanafunzi ilifikia 774,750 mwaka 2003 kutoka 313,310 mwaka 2002, ikiwa ni ongezeko la asilimia 147.3.

Elimu ya Msingi
268. Mwaka 2003 ulikuwa ni mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) na mafanikio yalikuwa yameanza kuonekana. Idadi ya shule za msingi iliongezeka na kufikia 12,815 mwaka 2003 kutoka 12,211 mwaka 2002. Kati ya shule hizo 166 zilikuwa za watu binafsi ikiwa zimeongezeka kutoka shule 59 mwaka 2002. Pia, idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 5,981,338 mwaka 2002 hadi 6,562,772 mwaka 2003, kati yao wanafunzi 6,531,769 walikuwa katika shule za serikali na 31,003 shule za watu binafsi. Aidha, kati yao, wasichana walikuwa asilimia 48.7 na wavulana asilimia 51.3. Vile vile, kiwango cha jumla cha uandikishaji kiliongezeka kutoka asilimia 98.6 mwaka 2002 hadi asilimia 105.3 mwaka 2003. Kiwango halisi cha uandikishaji kiliongezeka kutoka asilimia 80.7 mwaka 2002 hadi asilimia 88.5 mwaka 2003.

269. Katika mwaka 2003, kulifanyika ujenzi wa madarasa 13,342; ofisi za walimu 226; nyumba za walimu 997; vyoo vya shimo 14,700; na kuajiri walimu wapya 15,921 ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Jumla ya walimu katika shule za msingi ilifikia 114,660 mwaka 2003 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.3 kutoka walimu 112,109 waliokuwepo mwaka 2002. Wastani wa uwiano kati ya mwalimu na wanafunzi ulikuwa 1:57. Pia uwezo wa kamati za shule mbalimbali uliimarishwa kwa kushiriki katika warsha juu ya utawala, usimamizi wa fedha, usimamizi wa vifaa vya shule na uandaaji wa mipango ya shule.

Elimu ya Sekondari
270. Katika mwaka 2003 kulikuwa na shule za sekondari 1,083 ambapo 649 zilikuwa za serikali na 434 za watu binafsi, sawa na ongezeko la asilimia 6 kutoka shule 1,059 mwaka 2002. Idadi ya wanafunzi wa kidato cha I – IV ilikuwa ni 186,055 katika shule za serikali na 133, 432 katika shule binafsi; ambapo kwa kidato cha V-VI ilikuwa 14,665 katika shule za serikali na 11,289 katika shule binafsi. Idadi ya wanafunzi wa kidato I-IV iliongezeka kutoka 296,529 mwaka 2002 hadi 319,487 mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.7. Idadi ya wanafunzi wa kidato cha V-VI ilipungua kutoka 26,789 mwaka 2002 hadi 25,954 mwaka 2003. Aidha, mgawanyo wa wanafunzi wavulana kwa wasichana wa kidato I-IV ulikuwa asilimia 53.4 kwa wavulana na asilimia 46.6 kwa wasichana. Mgawanyo wa wavulana kwa wasichana kwa wanafunzi wa kidato cha V – VI ulikuwa asilimia 65.5 kwa wavulana na asilimia 34.5 kwa wasichana.

271. Katika mwaka 2003, kulikuwa na walimu 16,399, kati yao 9,896 walikuwa shule za serikali na walimu 6,503 walikuwa shule za watu binafsi. Hili ni ongezeko la asilimia 3.4 kutoka walimu 15,837 mwaka 2002. Aidha, uwiano kati ya walimu na wanafunzi kwa kidato cha I - VI ulibakia ule ule wa 1:20 kwa shule za sekondari za serikali na uliongezeka kwa shule za binafsi kutoka 1:21 mwaka 2002 hadi 1:22 mwaka 2003. Mwaka 2003, serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ya elimu waliandaa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) kwa ajili ya kipindi cha 2004-2009. Lengo kuu la MMES ni kuboresha utoaji wa elimu ya sekondari ili wanafunzi wengi watakaomaliza elimu ya msingi waweze kujiunga na elimu ya sekondari.

Mafunzo ya Walimu
272. Katika mwaka 2003, idadi ya vyuo vya ualimu ilikuwa 41 ambapo 34 vilikuwa vya serikali na 7 vya watu binafsi. Idadi ya walimu – wanafunzi daraja IIIA katika vyuo mbalimbali ilikuwa 22,487 katika vyuo vya serikali na 503 katika vyuo binafsi. Kati ya hawa, wanafunzi wanaume walikuwa 10,880 na wanawake 12,110. Mgawanyo kati ya walimu-wanafunzi wa kiume na kike ulikuwa asilimia 47.4 kwa wanaume na asilimia 52.6 kwa wanawake kwa vyuo vya ualimu vya serikali na asilimia 42.5 kwa wanaume na asilimia 57.5 kwa wanawake katika vyuo vya watu binafsi. Kwa upande wa vyuo vya Stashahada kulikuwa na walimu wanafunzi 4,930, kati yao 4,693 walikuwa katika vyuo vya serikali na 237 walikuwa katika vyuo vya watu binafsi. Katika vyuo hivyo idadi ya walimu-wanafunzi wa kiume walikuwa 3,108 na wa kike 1,822. Aidha, katika jitihada za kuongeza uwezo wa walimu, serikali iliendesha mafunzo ya kuwainua walimu wa daraja B na C na ililipia mafunzo ya wakufunzi 103 waliojiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mwaka 2003.

Ufundi na Elimu ya Juu
273. Katika mwaka 2003, kulikuwa na ongezeko la wanafunzi katika vyuo vya ufundi kutoka 2,223 mwaka 2002 hadi 2,292 mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1. Idadi ya wanafunzi wa kike ilikuwa 158 sawa na asilimia 7.1 ya wanafunzi wote mwaka 2002 ikilinganishwa na wanafunzi 202 sawa na asilimia 8.8 ya wanafunzi wote mwaka 2003. Aidha, katika vyuo vikuu vya Serikali idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 16, 396 mwaka 2002 hadi kufikia 21,391 mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30. Idadi ya wanafunzi wa kike iliongezeka kutoka 3,935 au asilimia 24 ya wanafunzi wote mwaka 2002 hadi 5,990 sawa na asilimia 28 ya wanafunzi wote mwaka 2003. Katika vyuo binafsi, idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 1,779 mwaka 2002 hadi 1,931 mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9. Idadi ya walimu katika vyuo vya ufundi ilipungua kutoka walimu 186 mwaka 2002 hadi 172 mwaka 2003, ikiwa ni upungufu wa asilimia 8. Katika vyuo vikuu vya Serikali, walimu waliongezeka kutoka 1,256 mwaka 2002 hadi 1,300 mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la asilima 4. Katika vyuo vikuu binafsi idadi ya walimu iliongezeka kutoka 278 mwaka 2002 hadi 307 mwaka 2003. Aidha, wastani wa uwiano wa walimu kwa wanafunzi ulikuwa 1:13 kwa vyuo vya ufundi, 1:16 kwa vyuo vikuu vya Serikali na 1:06 kwa vyuo vikuu vya watu binafsi.

Jedwali Na.A(MATUMIZI YA SERIKALI KATIKA SEKTA YA ELIMU)

Jedwali Na.B(IDADI YA TAASISI ZA ELIMU)

Jedwali Na.C(IDADI YA WANAFUNZI NA WALIMU KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI KWA JINSIA)

Jedwali Na.D(MAFUNZO YA WALIMU KATIKA VYUO VYA UALIMU)

Jedwali Na.E(IDADI YA WANAFUNZI KATIKA TAASISI ZA ELIMU YA JUU KWA JINSIA)

Jedwali Na.80(SHULE ZA SEKONDARI ZA SERIKALI: IDADI YA WANAFUNZI KWA KIDATO)

Jedwali Na.81(SHULE ZA SEKONDARI ZA BINAFSI: IDADI YA WANAFUNZI KWA KIDATO)

Jedwali Na.82(WANAFUNZI WATANZANIA KATIKA VYUO VIKUU VYA DAR ES SALAAM, SOKOINE NA CHUO KIKUU HURIA)

Jedwali Na.83(MUHTASARI WA TAKWIMU ZA ELIMU)

 
Back Top