MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI
   

Kilimo
Maliasili na Utalii
Madini
Viwanda na Biashara
Ujenzi wa Maendeleo ya Ardhi
Mawasiliano na Uchukuzi
Nishati
Maji
Elimu na Mafunzo
Afya
Maendeleo ya Jamii

           
KILIMO NA MIFUGO
KILIMO

Ukuaji wa Sekta

189. Sekta ya kilimo katika mwaka 2003 ilikua kwa asilimia 4.0 ikilinganishwa na asilimia 5 mwaka 2002. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji kulitokana na ukame uliojitokeza sehemu nyingi za nchi hasa mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga Pwani, Arusha, Manyara na Tabora ambayo iliathiriwa sana na ukame. Mikoa ya Mbeya, Iringa, Lindi, Mara, Mwanza, Tanga, Kilimanjaro na Mtwara pia iliathirika na ukame lakini kwa kiasi tu. Mchango wa sekta ya kilimo katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 46.8.

Mazao ya Chakula
190. Mwaka 2003 uzalishaji wa mazao ya chakula ulikuwa tani 12,432,000 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.0 kutoka tani 11,599,000 mwaka 2002. Uzalishaji wa mazao aina ya nafaka yakijumuisha mahindi, mpunga, mtama, uwele na ngano ulikuwa tani 5,108,000 ikilinganishwa na tani 5,373,000 mwaka 2002, sawa na upungufu wa asilimia 4.9. Upungufu huu ulitokana na hali ya hewa isiyotabirika hususan ukame uliyoyakumba maeneo mengi ya nchi. Uzalishaji wa mazao yasiyo ya nafaka (maharage, ndizi, mihogo, viazi na mengineyo) ulifikia jumla ya tani 7,781,000 ikilinganishwa na tani 6,740,000 mwaka 2002, sawa na ongezeko la asilimia 15.4 kutokana na wakulima kujihami kwa kulima mazao yanayostahimili ukame, magonjwa na wadudu na yanayokua haraka. Jedwali Na. 11.1 linaonyesha uzalishaji wa mazao ya chakula mwaka 2002 na 2003.

 
 

Jedwali Na. 11.1: Uzalishaji wa Mazao ya Chakula Mwaka 2002 Na 2003

Zao (tani)

2002 (‘000)

2003(‘000)

Badiliko %

Mahindi

3,480

3,129

(10)

Mpunga

1,069

921

(14)

Ngano

67

72

7.5

Mtama/ulezi

757

986

30

Muhogo

2,058

2,656

29

Maharage

574

517

(10)

Ndizi

2,067

2,501

21

Viazi

1,527

1,650

8

Jumla

11,599

12,432

7

  Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu

 

 
Mazao ya Biashara

191. Uzalishaji wa mazao mengi makuu ya biashara katika mwaka 2003 uliongezeka kama ifuatavyo: uzalishaji wa pamba uliongezeka kutoka tani 149,000 mwaka 2002 hadi tani 188,000 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 26. Uzalishaji wa chai uliongezeka kutoka tani 25,000 mwaka 2002 hadi tani 30,000 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 20. Uzalishaji wa korosho uliongezeka kutoka tani 78,000 mwaka 2002 hadi tani 92,000 mwaka wa 2003, sawa na ongezeko la asilimia 18. Uzalishaji wa mkonge ulibakia tani 24,000 mwaka 2003 kama ilivyokuwa mwaka 2002 kutokana na wawekezaji kuwa na mitaji midogo na wengine kushindwa kupata hati za mashamba husika. Uzalishaji wa tumbaku ulipungua kutoka tani 59,000 mwaka 2002 hadi tani 20,000 mwaka 2003, sawa na upungufu wa asilimia 66 kutokana na kuwepo kwa ukame na kupatikana kiwango kisichoridhisha cha mbolea za kupandia na kukuzia. Uzalishaji wa pareto ulipungua kutoka tani 2,000 mwaka 2002 hadi tani 1,000 mwaka 2003, sawa na upungufu wa asilimia 50. Uzalishaji wa kahawa ulipungua kutoka tani 67,000 mwaka 2002 hadi tani 53,000 mwaka 2003, sawa na upungufu wa asilimia 21 kutokana na upungufu wa mvua za vuli ambazo ni muhimu katika kukomaza na kusaidia kuchanua kwa maua. Uzalishaji wa mazao ya biashara mwaka 2003 unaonyeshwa kwenye Jedwali Na. 11.2.

Jedwali Na. 11.2:  Uzalishaji wa Mazao Mbalimbali ya Biashara 2001 –2003

Aina ya zao

Uzalishaji (tani)

Badiliko %

2001

2002

2003

2003

Pamba

125,000

149000

188,000

26.0

Tumbaku

28,000

59,000

20,000

(66)

Sukari

135,534

190000

248000

30.0

Chai

26,385.5

25,000

30,000

20.00

Pareto

1,850

2,000

1,000.00

(50)

Kahawa

58,134

67,000

53,000.00

(21)

Mkonge

20.5

24,000

24,000.00

1.0

Korosho

122,283

78000

92000.00

18.0

Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu

MIFUGO

192. Tanzania inakadiriwa kuwa na kiasi cha ng'ombe wapatao 17.7 milioni, mbuzi 12.5 milioni, kondoo 3.5 milioni, kuku 47.0 milioni na nguruwe 880,000. Hatua zilizochukuliwa ili kuboresha mifugo na mazao yake yaweze kukubalika katika masoko ya ndani na ya nje (kikanda na kimataifa) mwaka 2003 zilikuwa ni pamoja na kuzalisha dozi 65,995 za mbegu bora za ng'ombe, kuhamilisha ng'ombe 51,398, kusambaza mitamba 3,937 kwa ajili ya wafugaji wadogo wadogo wa ng'ombe wa maziwa nchini, kuchimba malambo 171 katika mikoa 16 kwa kushirikisha wilaya 49, ujenzi wa minada 52, vituo 15 vya kukagulia afya ya mifugo, vituo 78 vya kupumzikia mifugo, vituo 12 vikubwa vya kupakilia ng'ombe, vituo vya reli vya kupakilia na kupakulia mifugo kwenye mabehewa, kukarabati mabehewa 50 ya kubebea mifugo na kuendesha kampeni za kitaifa za kuhamasisha ulaji mazao ya mifugo ili kuinua matumizi ya mazao ya mifugo.

193. Uzalishaji wa mazao ya mifugo ulikuwa kama ifuatavyo:- Nyama kutoka tani 332,000 mwaka 2002 hadi tani 341,500 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 2.78; maziwa kutoka lita 900 milioni mwaka 2002 hadi lita 980,500 milioni mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 8.21; na mayai ya kuku kutoka 650 milioni mwaka 2002 hadi 790 milioni mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 17.72. Ongezeko katika uzalishaji lilitokana na upatikanaji wa kuridhisha wa malisho, maji na juhudi za ukusanyaji na usindikaji na kupanuka kwa wigo wa soko la ndani la bidhaa. Hali ya uzalishaji wa mazao na bidhaa za mifugo inaonyeshwa kwenye Jedwali 3.

Jedwali Na. 11.3:Uzalishaji wa Mazao ya Mifugo Msimu 2000/01 Hadi 2002/03

Uzalishaji/Msimu

Kipimo

2000/01

2001/02

2002/03

Badiliko %

NYAMA

 

 

 

 

 

   Ng’ombe

Tani

181,000

182,000

   182,500

0.27

   Kondoo/Mbuzi

Tani

72,100

74,000

    74,500

0.67

   Nguruwe

Tani

20,000

21,000

    23,000

8.70

   Kuku

Tani

50,000

55,000

    61,500

10.57

      Jumla - Nyama

Tani

323,100

332,000

  341,500

2.78

MAZIWA

 

 

 

 

 

    Ng’ombe wa Kienyeji

Lita (000)

492,500

578,000

 620,700

6.88

    Ng’ombe wa Kisasa

Lita (000)

321,500

322,500

   359,800

10.37

         Jumla - Maziwa

 

814,000

900,000

  980,500

8.21

MAYAI

 

 

 

 

 

    Mayai ya kuku

Idadi  (000)

600,000

650,000

   790,000

17.72

NGOZI

 

 

 

 

 

   Ngozi za Ng’ombe

Idadi

1,400,000

1,400,000

1,400,000

0.00

    Ngozi za mbuzi

Idadi

750,000

700,000

   800,000

12.50

    Ngozi za kondoo

Idadi

400,000

350,000

   460,000

23.91

          Jumla - Ngozi

 

2,550,000

2,450,000

2,660,000

7.89

Chanzo: Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo

Ughani na Mafunzo

194. Katika mwaka 2003, wakulima 932 walipatiwa mafunzo ya aina mbalimbali yanayohusu kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga. Aidha, jumla ya wataalamu wa kilimo wapatao 250 wenye astashahada katika fani mbalimbali za kilimo walifadhiliwa kwa masomo ya stashahada. Mabwana shamba 22 kutoka wilaya 10 za Serengeti, Babati, Bunda, Mbinga, Ngara, Mbeya Vijijini, Arumeru, Muheza, Magu na Musoma walipatiwa mafunzo ya Mbinu Shirikishi na Shamba Darasa ili kueneza matumizi ya mbinu hizo. Kazi ya kuboresha mitaala ya uzalishaji mazao na lishe ilikamilika. Mitaala ya mafunzo ya mboga, maua na matunda, matumizi bora ya ardhi na hifadhi ya udongo imefanyiwa marekebisho. Mbinu mbalimbali zilibuniwa na kutumiwa na wataalamu wa ughani katika kufikisha ujumbe sahihi kwa wakulima zikiwa ni pamoja na mbinu shirikishi jamii kwa timu za kata na wilaya husika, vipindi 13 vya ukulima wa kisasa viliandaliwa na kurushwa na Redio Tanzania Dar Es Salaam. Aidha, Gazeti la Mkulima wa Kisasa limechapishwa mara mbili na kusambazwa.

Maendeleo ya utafiti
195. Huduma za utafiti katika mwaka 2003 zililenga katika kupata mbegu zinazozaa kwa wingi, zinazostahimili ukame na kumudu mashambulizi ya wadudu na magonjwa. Vituo vya utafiti viliendelea na utafiti wa mazao ya jamii ya nafaka, mikunde, matunda na mboga. Utafiti pia ulifanyika kwa mazao ya viungo, mizizi na mbegu za mafuta zinazostahimili ukame, magonjwa, ushambulizi wa wadudu na ambazo zinatoa mavuno mengi kwa eneo. Matokeo ya tafiti zilizofanyika ni kuzalishwa kwa mbegu mpya kwa mazao ya kunde, mbaazi, mboga, matunda, migomba, viazi vitamu, mihogo na mananasi.

Vyama vya Ushirika na Masoko
196. Mwaka 2003 kulikuwa na vyama vya ngazi nne, vikiwemo vyama vya msingi 4903, vyenye wanachama 650,000, vyama vikuu vya ushirika 48, vyama vya kilele 3, na shirikisho moja la vyama vya ushirika. Aidha, kulikuwepo na vyama vya kuweka na kukopa 1,264 vyenye hisa zenye thamani ya shilingi 11.8 bilioni na amana zenye thamani ya shilingi 13.9 bilioni ikilinganishwa na vyama 4,778 vyenye wanachama 644,796 na vyama vya kuweka na kukopa vilikuwa 1,048 vyenye wanachama 142,700 wenye hisa zenye thamani ya shilingi 7.6 bilioni na amana zenye thamani ya shilingi 11.4 bilioni mwaka 2002. Mafanikio yaliyofikiwa yametokana na utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Ushirika 2002, kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushirika ya mwaka 1991 na kuandaa rasimu ya Mkakati wa Maendeleo ya Ushirika unaozingatia mabadiliko ya mfumo wa uchumi, siasa na jamii ili kuweza kukabiliana na nguvu za soko huria na utandawazi.

Upatikanaji wa Mikopo kwa Ajili ya Ununuzi wa Mazao na Pembejeo
197. Benki ya Ushirika Kilimanjaro na Benki ya Ushirika wa Wakulima Kagera zilindelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kununulia mazao na pembejeo kwa vyama vya ushirika na watu binafsi. Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro ilitoa mikopo yenye jumla ya shilingi 12.82 bilioni kwa watu binafsi mwaka 2003 ikilinganishwa shilingi 8.81 bilioni zilizotolewa mwaka 2002. Aidha, Benki ya Ushirika wa Wakulima Kagera ilitoa mikopo kwa watu binafsi yenye thamani ya shilingi 850 milioni na jumla ya shilingi 950 milioni zilizotolewa kwa vyama vya ushirika mwaka 2003 ikilinganishwa na jumla ya shilingi 11 bilioni zilizotolewa kwa watu binafsi mwaka 2002. Mbinu nyingine zilizotumika kupata mikopo kwa wauzaji nje ni pamoja na mpango wa kukopesha wauzaji mazao nje ambapo jumla ya shilingi 13.3 bilioni zilitolewa na Benki ya CRDB kwa Vyama Vikuu vya Ushirika vifuatavyo; Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza, Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga; Chama Kikuu cha Ushirika Karagwe; Chama cha Ushirika wa Biharamulo, Chama cha Ushirika Arusha, Chama cha Ushirika wa Wakulima Kilimanjaro, Chama cha Ushirika ISAYULA, Chama cha Ushirika Mbozi, Chama cha Ushirika Ruvuma na Chama cha Ushirika Kahama. Aidha, vyama vya msingi vitano vya kahawa vya Malindindo, Pilikano, Kimuli, Luwaita na Mahenge vilipata jumla ya shilingi 2.2 bilioni. Uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa njia ya mikataba kati ya wakulima na makampuni yanayokopesha pembejo za kilimo, kutoa mitaji na kuhakikisha upatikanaji wa soko ulitumika kwenye maeneo mengi nchini.

Masoko na Mazao
198. Katika mwaka 2003, maandalizi ya Sera ya Taifa ya Masoko ya Mazao ya Kilimo yaliendelea. Ushiriki katika maonyesho mbalimbali yaliyofanyika mwaka 2003 ulitoa fursa kwa wakulima, wafugaji, wafanya biashara kujionea na kujifunza juu ya bidhaa zinazozalishwa humu nchini, aina ya pembejeo zinazotumika na masoko ya mazao yaliyopo nje ya nchi. Mwenendo wa bei za mazao ulikuwa kama ifuatavyo: bei ya maharage iliongezeka kutoka shilingi 31,500 mwaka 2002 hadi shilingi 40,000 kwa kilo 100 mwaka 2003; bei ya mchele iliongezeka kutoka shilingi 27,436 mwaka 2002 hadi shilingi 41,995 kwa kilo 100 mwaka 2003, na bei ya mahindi iliongekeza kutoka shilingi 9,653 mwaka 2002 hadi shilingi 18,313 kwa kilo 100 mwaka 2003. Kwa ujumla bei za mazao ya biashara walizolipwa wakulima mwaka 2003 zilikuwa nzuri ikilinganishwa na bei kwa mwaka 2002. Bei ya kilo moja ya kahawa iliongezeka kutoka shilingi 450 mwaka 2002 hadi shilingi 600 mwaka 2003. Bei ya kilo moja ya pamba iliongezeka kutoka shilingi 190 mwaka 2002 hadi shilingi 280 mwaka 2003. Bei ya kilo moja ya korosho iliongezeka kutoka shilingi 377 mwaka 2002 hadi shilingi 462 mwaka 2003. Bei ya kilo moja ya tumbaku iliongezeka kutoka shilingi 567 mwaka 2002 hadi shilingi 600 mwaka 2003, na bei ya kilo moja ya chai iliongezeka kutoka shilingi 80 mwaka 2002 hadi shilingi 85 mwaka 2003.

Jedwali Na.35(UZALISHAJI WA MIWA NA SUKARI NCHINI)

Jedwali Na.36( PAMBA ILIYONUNULIWA NA MAUZO NCHINI)

Jedwali Na.38(KAHAWA ILIYONUNULIWA NA MAUZO NCHINI)

Jedwali Na.39(ENEO LILILOPANDWA MKONGE NA KATANI ILIYOPATIKANA )

Jedwali Na.40(TUMBAKU ILIYONUNULIWA NA MAUZO NCHINI)

Jedwali Na.41(MAUA YA PARETO YALIYONUNULIWA NA MAUZO YA BIDHAA ZA PARETO NCHINI)

Jedwali Na.42(KOROSHO ZILIZONUNULIWA NA MAUZO NCHINI)

Jedwali Na.43(MUHTASARI WA KIASI CHA MAZAO MUHIMU YA BIASHARA YALIYONUNULIWA)

Back Top