MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI
 

Kilimo
Maliasili na Utalii
Madini
Viwanda na Biashara
Ujenzi wa Maendeleo ya Ardhi
Mawasiliano na Uchukuzi
Nishati
Maji
Elimu na Mafunzo
Afya
Maendeleo ya Jamii

       
MAENDELEO YA JAMII
 

Elimu na Mafunzo

285. Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ambavyo madhumuni yake ni kujenga uwezo wa wanavijiji wa kutambua, kuamua kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, vilitoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi. Mafunzo ya muda mrefu yalitolewa kwa wanakijiji 7,489 ambapo wanaume walikuwa 4,738 na wanawake 2,751. Mafunzo ya muda mfupi yalitolewa kwa wanavijiji 10,007 na kati ya hawa wanawake walikuwa 5,144 na wanaume walikuwa 4,863. Aidha, Mafunzo yalitolewa nje ya vyuo kwa wananchi 4,872 wakiwemo wanaume 2,331 na wanawake 2,541. Jumla ya wananchi 13,263 walipewa mafunzo kuhusu kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI. Kati ya hao wanawake walikuwa 6,215 na wanaume walikuwa 7,048.

286. Vyuo vya Maendeleo ya Jamii hutoa mafunzo katika ngazi ya cheti na stashahada. Wanafunzi 163 kati ya hao 92 wanawake na 71 wanaume walihitimu ngazi ya cheti. Aidha, wanafunzi 60 kati ya hayo 23 wanawake na 37 wanaume walihitimu ngazi ya stashahada. Pia, mitaala minne, mitatu ya stashahada ya juu na mmoja wa ngazi ya Cheti ilichapishwa na kukubalika na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Maendeleo ya Wanawake
287. Mwaka 2003 wanawake waliendelea kupewa mikopo inayotokana na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) unaotolewa kila mwaka na Serikali. Wilaya zote zilipewa kiasi cha shilingi 4 milioni kila mmoja kwa ajili ya kuwakopesha wanawake. Asasi zisizokuwa za kiserikali nazo ziliendelea kutoa mikopo ikiwemo CREW Tanzania ambayo ilitoa jumla ya mikopo 754 yenye thamani ya sh. 228,830,000. Wanawake wapatao 135 waliwezeshwa kushiriki katika maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar-es-Salaam na wanawake 60 wafanyabiashara walipewa mafunzo ya namna ya kuendesha biashara, kutafuta masoko na namna ya kunakshi bidhaa.

288. Mafunzo ya muda mfupi kwa wanawake wa kada mbalimbali yaliendelea kutolewa kwa lengo la kuongeza uwezo wao wa kiutendaji. Baada ya Serikali kukubali kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika wizara na taasisi mbalimbali za umma, mafunzo ya watendaji wapatao 34 yalifanyika, ambapo wizara 20 na Idara 4 zinazojitegemea zilishiriki. Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wapatao 40 walipewa mafunzo kuhusu jinsia. Aidha, watumishi 40 wa Wizara ya Maliasili na Utalii, na Tume ya Ualimu walipewa mafunzo ya namna ya kuingiza maswala ya jinsia katika shughuli mbalimbali.

Maendeleo ya Watoto
289. Mwaka 2003, rasimu ya ripoti ya pili ya nchi kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto iliandaliwa. Aidha, mwongozo ulitolewa wa kuandaa mpango wa Taifa wa utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele kulingana na tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu dunia ifaayo watoto. Bunge la Tanzania liliridhia Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto na Itifaki za Nyongeza za CRC kuhusu biashara ya kuuza watoto, ukahaba wa watoto, upigaji wa picha za udhalilishaji wa watoto, na watoto katika migogoro ya kivita.

 
Back Top