MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI
   

Kilimo
Maliasili na Utalii
Madini
Viwanda na Biashara
Ujenzi wa Maendeleo ya Ardhi
Mawasiliano na Uchukuzi
Nishati
Maji
Elimu na Mafunzo
Afya
Maendeleo ya Jamii

         
   
MALIASILI NA UTALII
 
 
Ukuaji wa sekta

199. Sekta ya maliasili inajumuisha sekta ndogo za misitu na nyuki, uvuvi, na wanyamapori. Sekta ndogo ya misitu na wanyamapori ilikua kwa asilimia 4.2 ikilinganishwa na asilimia 3.0 mwaka 2002 na sekta ndogo ya uvuvi ilikua kwa asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 6.5 mwaka 2002. Kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji katika sekta ndogo ya misitu na wanyamapori kulitokana na kukua kwa biashara ya wanyamapori pamoja na mazao yake katika soko la nje, uzuiaji wa biashara haramu ya wanyamapori hai na mazao yake na uhamasishaji wananchi katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake. Aidha, kushuka kwa kiwango cha ukuaji katika sekta ndogo ya uvuvi kulitokana na ukosefu wa mitaji kwa wavuvi wadogo, mbinu na teknolojia duni katika utunzaji na usindikaji wa mazao ya uvuvi pamoja na matumizi ya zana haramu katika uvuvi ambazo zinaharibu mazingira ya viumbe wa majini.

Misitu na Nyuki
200. Shughuli zilizofanyika katika mwaka 2003 ni pamoja na kukuza miche 7,3776,733 ikilinganishwa na miche 8,265,000 mwaka 2002; hekta 2,275 kupandwa miti, hekta 881 kupunguzwa na kupogoa matawi hekta 1,650. Pia, misitu ya asili iliendelea kuwekewa doria na kuwekewa vibao vya utambulisho ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera na sheria za misitu. Maandalizi ya kanuni za utekelezaji wa sheria ya misitu yaliendelea ili kuiwezesha sheria mpya ya misitu Na. 14 ya mwaka 2002 kutumika. Mipango ya usimamizi iliandaliwa katika misitu ya hifadhi ya Maisome na Kome mkoani Mwanza. Aidha, Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kitaifa na kimataifa, ilianzisha mradi wa matumizi ya mianzi asili kwa ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu Mkoani Mbeya. Vile vile, usimamizi shirikishi wa misitu umepewa kipaumbele katika sera ya misitu na nyuki na kuzingatiwa kwa sheria husika. Hekta 1,085,306 za misitu ziko chini ya usimamizi shirikishi katika ardhi ya jumla na hekta 1,863,623 katika misitu ya hifadhi. Vijiji 15 katika wilaya za Kibondo, Tabora, Manyoni, Kondoa na Handeni vilianzisha hifadhi za nyuki za vijiji. Mpango wa uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki unaohusisha wilaya za Mtwara Vijijini, Liwale, Muheza, Nachingwea, Handeni na Korogwe umeandaliwa na wilaya 24 ziliwezeshwa kuandaa mipango yake ya utekelezaji. Halikadhalika, katika mwaka 2003, jumla ya miti 68.3 milioni ilipandwa katika mikoa yote nchini ikilinganishwa na miti 82.7 milioni iliyopandwa mwaka 2002. Kushuka kwa kiwango cha idadi ya miti iliyopandwa kulitokana na kutopatikana kwa takwimu za miti iliyopandwa katika mikoa ya Mara, Mbeya na Rukwa. Jedwali Na. 45 linaonyesha idadi ya miche iliyopandwa nchini katika mwaka 2003. Aidha, wakala wa Mbegu za Miti Tanzania ulizinduliwa na kupewa majukumu ya kukusanya na kuuza mbegu bora za miti.

Uvunaji na Uuzaji wa Mazao ya Misitu na Nyuki
201. Katika mwaka 2003, magogo yenye mita za ujazo 19,020 katika misitu ya asili na mita za ujazo 315,853 katika mashamba ya miti yalivunwa ikilinganishwa na magogo ya mita za ujazo 4,556.3 katika mwaka 2002. Mazao ya misitu na nyuki yaliyouzwa nje yalikuwa na thamani ya shilingi 7.2 bilioni mwaka 2003 ikilinganishwa na shilingi 6.018 bilioni zilizopatikana katika mwaka 2002. Jedwali Na. 47 linaonyesha mwenendo wa mapato na mauzo ya bidhaa za misitu na nyuki nje katika mwaka 2003.

Wanyamapori
202. Katika mwaka 2003, udhibiti wa matumizi haramu ya wanyamapori uliendelea na miundombinu iliongezwa kuwezesha shughuli za watalii. Mapori mawili ya akiba ya Kitulo na Saadan yalipandishwa hadhi na kuwa hifadhi za taifa na Misitu ya Meru na Kilimanjaro. Vile vile jumla ya kilometa 85 za barabara mpya zilitengenezwa na kilometa 756 za barabara zilikarabatiwa katika mapori ya akiba ya Mkomazi/Umba, Mpanga/Kipengere, Lukwila/Lumesulu/Msanjesi, Usangu, Swagaswaga, Rungwa/Kizigo/Muhesi, Pande, Ibanda/Rumanyika, Maswa, Burigi/Biharamulo na Moyowosi ikilinganishwa na kilometa 636 mwaka 2002. Kadhalika viwanja viwili vipya vilitengenezwa katika mapori ya akiba ya Selous na Mpanga/Kipengere na viwanja 11 vilikarabatiwa. Aidha, jumla ya kilometa 680 ziliwekewa alama ya mipaka ya mapori ya akiba 10, ikilinganishwa na kilometa 838 mwaka 2002. Mipaka ya mapori ya akiba matano ilipitiwa upya na ramani zake kuchorwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

203. Katika kupambana na ujangili dhidi ya rasilimali ya wanyamapori na mazingira yao, doria ziliendelea kuwekwa ndani na nje ya hifadhi ambapo idadi ya kesi za ujangili ziliongezeka hadi 780 ikilinganishwa na kesi 520 mwaka 2002. Hadi Desemba 2003, kesi 102 zilimalizika na majangili 180 kufungwa jela. Aidha, doria za upelelezi na ukaguzi wa wafanyabiashara ya nyara ziliendeshwa ambapo nyara zenye thamani ya shilingi 188,092,536 zilikamatwa ikilinganishwa na nyara zenye thamani ya shilingi 219,785,118 zilizokamatwa mwaka 2002. Nyara zilizokamatwa ni pamoja na meno ya tembo 80 na vipande 140 vya meno ya tembo, meno ya kiboko 218, ndege hai 166, wadudu 300, wanyama 33 na kobe 44.

204. Katika mwaka 2003, waombaji 388 walipewa leseni za nyara ikilinganishwa na waombaji 278 mwaka 2002, sawa na ongezeko la asilimia 28.3. Ada za leseni hizo ziliingizia Serikali mapato ya shilingi 131,398,445. Vile vile, mapato kutokana na biashara ya nyara na viumbe hai yameongezeka kwa shilingi 56,969,412 sawa na ongezeko la asilimia 77 ikilinganishwa na shilingi 74,429,033 zilizopatikana mwaka 2002. Ongezeko hili linatokana na wafanyabiashara wengi kutumia ‘quota’ zao kikamilifu. Ushirikishwaji wa sekta binafsi na wananchi katika shughuli za ufugaji wanyamapori ziliendelea kuimarika ambapo jumla ya kobe 2,816 walisafirishwa nchi za nje na kuwapatia wafugaji kiasi cha shilingi 56,320,000.

205. Katika mwaka 2003 kulikuwepo na vitalu 142, ikilinganishwa na vitalu 131 mwaka 2002, sawa na ongezeko la asilimia 7.7. Biashara ya uwindaji wa kitalii ililiingizia Taifa mapato ya dola 8.8 milioni ikilinganishwa na mapato ya dola 9.3 milioni ya mwaka 2002, mapato haya yameonyesha upungufu wa dola 0.5 milioni sawa na upungufu wa asilimia 5.04. Upungufu huu ulitokana na watalii wengi kukatisha safari zao kufuatia kuzuka kwa vita vya Iraq, mlipuko wa homa ya mapafu (SARS) na homa ya kuku (Bird flu).

Uvuvi
206. Katika mwaka 2003, ukuaji wa sekta ya uvuvi ulipungua kwa asilimia 0.1, kutokana na ukosefu wa mitaji kwa wavuvi wadogo, teknolojia duni katika utunzaji na usindikaji wa mazao ya uvuvi pamoja na matumizi ya zana haramu katika uvuvi ambazo huharibu mazingira ya viumbe wa majini (samaki). Vyombo vya uvuvi kwa ajili ya uvuvi wa kamba vilikuwa 25 na jumla ya tani 36,689,405 za sangara na mazao yake zilivunwa. Kwa ujumla, uvuvi wa kamba, sangara na mazao yake ndio yanayoliingizia taifa mapato makubwa ya fedha za kigeni. Kiuzalishaji na kibiashara katika soko la nje, samaki wengi wanatoka zaidi katika maeneo ya maziwa na mito. Biashara ya minofu ya sangara katika mwaka 2003 iliongezeka hadi kufikia kilo 28,568,979. Uzito huu ni ongezeko la kilo 4,740,878 ikilinganishwa na mwaka 2002.

207. Mapato ya mazao ya uvuvi katika soko la nje yalipanda kutoka karibu shilingi 99,294,249 mwaka 2002 hadi shilingi 132,502,001,939 katika mwaka 2003, ikiwa ni ongezeko la shilingi 33,207,752,036. Majedwali Na. 16, 17 na 18 yanaonyesha biashara na mapato yatokanayo na mauzo ya mazao ya uvuvi. Ili kuimarisha utekelezaji wa sera ya uvuvi, mwaka 2003 Sheria Na. 6 ya uvuvi ya mwaka 1970 ilirekebishwa na sheria na. 22 ya mwaka 2003 ilitungwa. Azma ya marekebisho haya ni kuhakikisha kuwa jamii inayojishughulisha na uvuvi inazingatia kanuni na taratibu zilizopo.

208. Katika hatua ya kudhibiti uvuvi haramu, doria 26 zilifanyika katika maeneo ya ukanda wa pwani na ukanda wa uchumi wa bahari ikilinganishwa na doria 135 mwaka 2002. Jumla ya wahalifu 9 na meli 3 zilikamatwa. Mafanikio hayo yalipatikana kwa kupitia mradi wa uthibiti na ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi kwa kutumia meli ya chuo cha uvuvi Mbegani na kutumia ndege. Aidha, kanuni za uvuvi katika Ziwa Victoria zimeainishwa na zile za Kenya na Uganda ili kwa pamoja nchi zinazomiliki ziwa hili ziweze kukabiliana na uvuvi haramu.

Utalii
209. Idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka kufikia watalii 576,198 ikilinganishwa na watalii 575,296 mwaka 2002, sawa na ongezeko la asilimia 0.2. Mapato yatokanayo na biashara ya utalii, nayo yaliongezeka kutoka dola 730.0 milioni mwaka 2002 hadi dola 731.0 milioni mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 0.1. Tahadhari za usafiri zilizokuwa zinatolewa na baadhi ya nchi za magharibi kuhusiana na ugaidi zilisababisha ukuaji mdogo wa mapato ya sekta hii ya utalii.

210. Vivutio vipya vilivyoko sehemu mbalimbali nchini vilitathiminiwa ili kuhakikisha kwamba barabara zinazoelekea kwenye vivutio na hoteli zinapitika muda wote. Barabara kuu ya utalii kutoka Makuyuni hadi Ngorongoro yenye urefu wa km 77 ilijengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, utangazaji wa vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi ulifanyika kwa kutumia usambazaji wa majarida, vipeperushi, mabango, Digital Video Disc (DVD) kwenye balozi zetu na sehemu mbalimbali za maonyesho mwaka 2003. Vile vile, katika kuitangaza kauli mbiu inayotumika ya “Afrika Halisi ni Tanzania”, tovuti ya utalii ilianzishwa (www.tourismtanzania.go.tz).

Utalii wa Mambo ya Kale
211. Katika mwaka 2003, mipango kabambe ya uhifadhi na uendelezaji wa maeneo na vituo vya mambo ya kale ilifanyika: maeneo ya makumbusho ya Dr. Livingstone-Ujiji-Kigoma na kimondo cha Mbozi yaliweza kupimwa na kuwekewa mipaka; mradi wa kuuandaa mji mkongwe wa Bagamoyo ili uwekwe kwenye orodha ya urithi wa Dunia ulianzishwa; uendelezaji wa utafiti wa mambo ya kale uliendelezwa ambapo watafiti wa ndani na nje ya nchi walishirikishwa; na kiasi cha shilingi 12,874,843.94 zilikusanywa kama ada na vibali vya utafiti. Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na maandalizi ya kanuni za uhifadhi wa miji na majengo ya kihistoria hususani majengo ya kihistoria katika jiji la Dar es Salaam. Ukusanyaji wa maduhuli ya sekta uliongezeka na kufikia shilingi 132.6 milioni katika mwaka wa 2003, ikilinganishwa na shilingi 96.5 milioni mwaka 2002, sawa na ongezeko la asilimia 37.4. Makusanyo ya maduhuli yalipatikana katika vituo vya kale vifuatavyo; Olduvai, Bagamoyo Kaole Ruins, Isimila. Kalenga, Amboni, Tongoni, Kilwa, Kuihara (Tabora) na makao makuu.

Jedwali Na.45(UPANDAJI WA MITI (MICHE ILIYOOTESHWA))

Jedwali Na.47(MAUZO YA BIDHAA ZA MISITU NCHI ZA NJE)

Jedwali Na.48(MWENENDO WA BIASHARA YA NDEGE, WANYAMAPORI NA VIPUSA NCHI ZA NJE)

Jedwali Na.48A(MWENENDO WA BIASHARA YA WANYAMA HAI NA UWINDAJI WA KITALII)

Jedwali Na.48B(IDADI YA WAWINDAJI (TOURIST HUNTERS))

Jedwali Na.49(MAUZO YA WANYAMA HAI NA PEMBE NCHI ZA NJE)

Jedwali Na.50(UZALISHAJI KATIKA SEKTA YA UVUVI 1993-2000)

Jedwali Na.51(MAUZO YA MAZAO YA UVUVI NCHI ZA NJE (2000-2002))

Jedwali Na.51A(MUHTASARI WA MAUZO YA MAZAO YA UVUVI NCHI ZA NJE - 1996-2002)

Jedwali Na.51B(MWELEKEO WA MAUZO YA SANGARA NJE YA NCHI -1996-2002)

Jedwali Na.52(IDADI YA WATALII, SIKU ZAO HOTELINI NA MAKADIRIO YA FEDHA ZA KIGENI ZILIZOPATIKANA)

Jedwali Na.53(IDADI YA WATALII WALIOINGIA NCHINI NA KIASI CHA FEDHA ZILIZOPATIKANA (1990-2002))

Jedwali Na.54(SAFARI KATIKA HIFADHI ZA TAIFA)

Jedwali Na.55(NAFASI KATIKA HOTELI NA MATUMIZI YAKE+)

 
Back Top