MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI

Uendelezaji wa Sekta Binafsi
Masuala Maalum Yanayohusu Sekta Zote

Maendeleo ya Juhudi za Kupambana na Umasikini

     
    UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI    
UWEKEZAJI

Uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC)

127. Katika mwaka 2003, Kituo cha Uwekezaji kiliendelea kuboresha huduma zake kwa wawekezaji kwa mtindo wa kituo kimoja cha uwezeshaji (one-stop facilitation center). Kituo kilikamilisha mapitio ya Mpango wa Maendeleo wa Kituo wa miaka mitano (2001 – 2006) ambao ulirekebishwa kutoka Mpango wa Maendeleo wa Kituo wa miaka mitano (2003 – 2008). Vile vile kituo kilishiriki kikamilifu kukamilisha uanzishwaji wa Mpango wa Uimarishaji wa Mazingira ya Biashara Tanzania (BEST).

128. Idadi ya wawekezaji waliohudumiwa kwa kupatiwa vibali mbalimbali kupitia Kituo katika mwaka 2003 ni; 272 kwa masuala ya TRA; 196 kwa masuala ya uanzishaji wa makampuni, na 218 leseni za biashara; ikilinganishwa na masuala 296 ya TRA, 257 uanzishwaji wa makampuni, na 206 leseni za biashara yaliyoshughulikiwa mwaka 2002. Pia, vibali 473 vya kufanya kazi nchini vya daraja B vilitolewa ikilinganishwa na vibali 1,043 vilivyotolewa mwaka 2002. Aidha, wawekezaji 82 kwa masuala ya ardhi walihudumiwa ikilinganishwa na wawekezaji 50 mwaka 2002. Maombi ya kufanya kazi nchini yaliyopokelewa na kupitishwa na Wizara ya Kazi ni 1,298.

129. Katika mwaka 2003, Kituo kiliidhinisha miradi 372 yenye thamani ya Sh. 1,669.4 bilioni, inayokadiriwa kutoa nafasi za ajira 198,458, sawa na ongezeko la miradi 61 au asilimia 19.6 ikilinganishwa na miradi 311 iliyokuwa na thamani ya sh.1,024 bilioni na nafasi za ajira 33,000 iliyoidhinishwa mwaka 2002 . Miradi 229 kati ya hii ilikuwa mipya, ambapo miradi 143 ilikuwa ya ukarabati na upanuzi wa shughuli zilizopo. Mchanganuo wa umiliki wa hii miradi unaonyesha kuwa miradi 155 ilikuwa ya wawekezaji wa ndani, miradi 109 ya wawekezaji wa nje na miradi 108 ikiwa ni ya ubia. Sekta ya viwanda ndio iliyopata miradi mingi zaidi, ikiwa na miradi 127 (asilimia 34) yenye thamani ya Sh. 239.6 bilioni. Sekta nyingine zilizovutia wawekezaji wengi ni pamoja na sekta ya utalii iliyopata miradi 81 (asilimia 22), sekta ya ujenzi miradi 48 (asilimia 13), sekta ya usafirishaji miradi 28 (asilimia 8), sekta ya maliasili miradi 21 (asilimia 6) na sekta ya kilimo miradi 20 (asilimia 5). Sekta nyingine zilizovutia miradi ni mawasiliano miradi 12, uendelezaji rasilimali watu miradi 10, huduma miradi 8, miundombinu miradi 6, madini na mafuta miradi 4, tarakilishi miradi 4 na huduma za kibenki miradi 3.

130. Mgawanyo wa miradi kimkoa unaonyesha kuwa mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kupata miradi 231. Mikoa mingine iliyopata wawekezaji ni Arusha-miradi 55, Mwanza-miradi 15, Kilimanjaro-miradi 13, na Tanga-miradi 11. Mikoa ya Mara, Pwani na Shinyanga ilipata kila mmoja miradi 8 wakati mkoa wa Morogoro ulipata miradi 7. Mikoa iliyopata miradi kwa kiasi kidogo ni mkoa wa Iringa miradi 6, mkoa ya Kagera 5, mikoa ya Lindi na Mtwara miradi mitatu kila mmoja, wakati mikoa ya Mbeya, Dodoma, Tabora, Rukwa na Ruvuma miradi miwili kila mmoja. Mikoa ambayo ilipata mradi mmoja mmoja tu ambao ni mtandao wa simu kwa nchi nzima ni Kigoma na Singida. Jedwali Na.34 linaonyesha miradi iliyosajiliwa na Kituo mwaka 2003, na Jedwali Na. 7.1 linaonyesha mgawanyo wa miradi kimikoa katika mwaka 2003.

Uhamasishaji wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
131. Kituo kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kiliratibu semina ya uwekezaji mkoa wa Kilimanjaro (Agosti 2003); Vile vile, semina za kukuza ujasirimali na uwekezaji zilifanyika kwa vijana wa mikoa ya Mwanza na Tabora. Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Biashara la Jumuiya ya Madola (CBC), taasisi ya sekta binafsi (Tanzania, Private Sector Foundation, TPSF), na Kituo cha Uwekezaji iliratibu mkutano wa uwekezaji nchini mwezi Mei 2003 ambao ulikutanisha viongozi, wafanyabiashara na wawekezaji wa nje na ndani katika kuitangaza Tanzania na kuweka wazi fursa za uwekezaji nchini. Kituo kiliandaa na kufanikisha mpango wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi za kusini mwa Ulaya mnamo Oktoba 2004 kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Duniani (UNIDO), Taasisi ya sekta binafsi (TPSF), na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Mpango huu uliwezesha kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa Ulaya ili kukuza biashara baina yao, kutafuta ubia, na kutafuta masoko. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2003, Kituo cha Uwekezaji kilikuwa tayari kimeratibu miradi 400 ya ngazi ya chini na ya kati (SMEs) iliyobuniwa na watanzania iliyokuwa katika ngazi mbalimbali za kutafuta wabia, mitaji na teknolojia. Katika mwaka 2003, watanzania wapatao 30 walijigharamia wenyewe kwenda Ulaya na Asia kunadi miradi yao na kuzungumza na wabia muafaka.

Uwekezaji wa Miradi ya Moja kwa Moja (FDI)
132. Katika mwaka 2003, thamani ya mitaji ya kigeni ya moja kwa moja (Foreign Direct Investments) iliongezeka kufikia dola 300.00 milioni ikilinganishwa na thamani ya dola 240.4 millioni mwaka 2002. Jedwali Na. 1 linaonyesha mwenendo wa mitaji ya kigeni ya moja kwa moja katika kipindi cha mwaka 1997 – 2003.

 

Jedwali Na.7.2: Uwekezaji wa Mitaji ya Kigeni ya  moja kwa moja (FDI),

1997 – 2003

Mwaka

Thamani ya Mitaji iIiyowekezwa

(Dola za Marekani Milioni)

1997

157.8

1998

172.2

1999

516.7

2000

463.4

2001

327.4

2002

240.4

2003

300.0

 

   
Uboreshaji wa Mazingira ya Uwekezaji

133. Ili kuendeleza miradi ya watanzania katika mwaka 2003, Kituo cha Uwekezaji kilianzisha idara maalum ya kuwahudumia wawekezaji wa ndani kuwaunganisha na wawekezaji wa nje kwa ajili ya ubia; kuwasaidia katika utayarishaji wa michanganuo ya miradi inayokubalika ili kusaidia upatikanaji wa mikopo kutoka benki; kufanya semina na mikutano mbalimbali kwa wawekezaji wa ndani na wananchi kwa ajili ya kukuza ujasiriamali; na kuwaelimisha juu ya Kituo na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini.

134. Katika kutekeleza azma ya kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji wa ndani na nje, serikali imeanza utekelezaji wa Programu ya Kuimarisha Mazingira ya Biashara Tanzania (Business Environment Strengthening for Tanzania - BEST). Lengo ni kujenga uwezo wa ushindani wa kibiashara ili kuwezesha uchumi kukua kwa kasi zaidi. Utekelezaji rasmi umeanza mwezi Desemba 2003 kwa kuunda Kitengo cha Kurekebisha Mazingira Bora ya Biashara (Better Regulation Unit - BRU), chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji. Aidha Kitengo kimejishughulisha na maandalizi ya awali ya kurekebisha mfumo wa sheria na taratibu za kibiashara katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hususan; mfumo wa leseni za biashara, sheria za ajira na kazi, utekelezaji wa Sheria ya Ardhi na marekebisho ya muundo wa utendaji wa wakala wa uandikishaji wa biashara (Business Registration and Licensing Agency-BRELA).

Baraza la Taifa la Biashara
135. Baraza la Taifa la Biashara liliendelea kutekeleza majukumu yake ya kuendeleza mashauriano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuboresha hali ya biashara hapa nchini na uwekezaji wa mitaji ya ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi. Baraza limeunda kamati saba za kushughulikia masuala ya viwanda na usindikaji wa mazao ya kilimo, utalii na utangazaji nchi, uendelezaji wa wataalam, fedha, kilimo, ushauri kwa Rais, na biashara. Katika mwaka 2003, Baraza lilifanya mikutano miwili yenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji na kujifunza njia bora za kisasa za uwekezaji wa mitaji na kufanya biashara. Pia, Baraza liliendelea na kuandaa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Ardhi kwa lengo la kurahisisha utoaji wa mikopo kwa biashara ndogondogo kwa kutumia ardhi kama dhamana, sheria ya ajira kwa lengo la kuboresha ajira, kurekebisha mfumo wa kodi, na kuondoa adha ya utozaji wa kodi nyingi.

UREKEBISHAJI NA UBINAFSISHAJI WA MASHIRIKA YA UMMA

136. Hadi kufikia Desemba 2003, jumla ya mashirika 289 yamebinafsishwa na mali za mashirika (non-core assets) zipatazo 328 zimeuzwa ikilinganishwa na mashirika 265 na mali za mashirika (non-core assets) zipatazo 265 hadi 2002. Katika mwaka 2003, jumla ya mashirika 101 yalibinafsishwa yakijumuisha Mashirika 26 na uuzaji wa mali za mashirika zipatazo 75 ikilinganishwa na jumla ya mashirika 124 yakijumuisha mashirika 9 na mali za mashirika 115 mwaka 2002. Mashirika hayo yamebinafsishwa kwa Watanzania na kwa wawekezaji kutoka nje kwa utaratibu wa kuuza hisa, kuuza mali, kukodisha na kufilisi.

137. Katika mwaka 2003, juhudi kubwa zilielekezwa katika kutekeleza uandaaji wa mamlaka za udhibiti pamoja na kufanya marekebisho ya sheria za kisekta zinazolenga kudhibiti mamlaka hizo. Vile vile, kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na ukamilishaji wa taratibu za ukodishaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) kwa mikoa ya Dar es salaam na Pwani; taratibu za ukodishaji wa TRC zilifikia hatua ya kuandaa utaratibu wa kuitisha zabuni; tafiti mbili za kuligawa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zilikamilika, na maandalizi ya kuunda mfumo mpya wa utendaji wa soko la nishati na umeme na usimamizi wa utendaji wa menejimenti ya mkataba unayoiongoza TANESCO kwa kipindi maalum, yalikamilika. Pia ubinafsishaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Benki ya NMB, na vitengo vya kibiashara vya Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA) ulianza kushughulikiwa. Kadhalika Serikali ilifanya maandalizi ya ubinafsishaji wa mashamba makubwa kama NAFCO, ranchi za taifa na viwanda 12 vya kubangulia korosho. Pia, Serikali iliendelea na ukamilishaji wa sheria za mamlaka za udhibiti katika maeneo husika. Vyombo hivyo ni Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA); Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA) na Kamisheni ya Ushindani wa Haki. Aidha, marekebisho ya sheria za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) za mwaka 2001 yalifanyika.

138. Zoezi la kubinafsisha mashirika ya umma limekuwa na mafanikio ikiwa ni pamoja na: ongezeko la uzalishaji mali; tija; ajira isiyo ya moja kwa moja viwandani; kupatikana kwa teknolojia mpya na mitaji mipya ya wastani wa dola 725.9 milioni na shilingi 52.65 bilioni; kuongezeka kwa ubora wa bidhaa za viwandani; kuongezeka kwa mapato ya kodi kwa Serikali kutokana na kodi inayolipwa na mashirika yaliyobinafsishwa; na zaidi ya mashirika 70 yaliyokuwa yamefungwa kabla ya kubinafsishwa sasa yanafanya kazi kwa ufanisi.

139. Katika mwaka 2003, serikali iliendelea kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa zoezi la ubinafsishaji ikiwemo; ugumu wa kuwapata wawekezaji mahiri wenye sifa na uwezo unaotakiwa; baadhi ya mashirika kuwa na wafanyakazi wengi kuliko kazi zilizopo jambo lililosababisha wengine kulazimika kupunguzwa; baadhi ya bodi za wakurugenzi na menejimenti kushindwa kutoa ushirikiano unaostahili katika juhudi za ubinafsishaji wa mashirika wanayoyaongoza; baadhi ya mashirika kutowasilisha makato ya michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya pensheni; na baadhi ya mashirika yalikuwa na madeni makubwa na hivyo kushindwa kuvutia wawekezaji.

140. Changamoto nyingine katika ubinafsishaji ni pamoja na baadhi ya wawekezaji kushindwa au kuchelewa kufufua mashirika waliyokabidhiwa kwa mfano viwanda vya ngozi; mashirika mengi yaliyonunuliwa na watanzania kushindwa kufufuliwa kutokana na ukosefu wa mitaji ya kuendeshea mashirika hayo; na mashirika mengi yaliyobinafsishwa kuwa na kesi mahakamani na hivyo kuchelewesha zoezi la ubinafishaji. Hivi sasa zipo zaidi ya kesi 170 mahakamani dhidi ya mashirika ya umma. Aidha, kati ya hatimiliki za mashirika yanayobinafsishwa 700, hatimiliki 400 zimepatikana, na zilizosalia zinafuatiliwa.

141. Serikali imechukua hatua zifuatazo ili kukabiliana na matatizo yaliyojitokeza: kufuatilia utendaji wa mashirika yaliyobinafsishwa kwa kushirikiana na wizara husika na Kamati za Bunge; kutumia wataalam wa kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa sugu; kuendelea kuwaelimisha wadau mbali mbali kuhusu sera ya ubinafsishaji kupitia, warsha, vyombo vya habari, vipeperushi, na matangazo; kuanzisha utaratibu wa dhamana za benki kwa nia ya kuwadhibiti madalali na wawekezaji wasio waaminifu; kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wawekezaji walioshindwa kutekeleza mikakati ya ubinafsishaji; kuajiri wanasheria kushughulikia kesi zilizo mahakamani; na kuajiri mtaalamu wa masuala ya ardhi kufuatilia hati miliki zenye matatizo.

Jedwali Na.34(KITUO CHA UWEKEZAJI TANZANIA (TIC): MIRADI ILIYOPITISHWA)

Back Top