MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUMU KATIKA MAENDELEO |
MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

SUALA MAALUM KATIKA MAENDELEO    
             

MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2025 NA MKAKATI WA KUPUNGUZA UMASKINI

UTANGULIZI

164. Serikali ya Tanzania imeweka sera, mipango na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha ukuaji wa uchumi na kuinua hali ya maisha ya Watanzania. Mifumo mbalimbali ya ufuatiliaji iliwekwa kwa ajili ya kufuatilia mabadiliko, na kutathmini mafanikio na mambo yanayokwamisha utekelezaji. Hata hivyo, imebainika kuwa mfumo wa ufuatiliaji nchini hautoshelezi matarajio kwa vile bado haujazingatia ushiriki wa sekta zote. Kila sekta ina mfumo wake wa ufuatiliaji bila kuwa na uhusiano na sekta nyingine. Hivyo, panahitajika utaratibu utakaowezesha kuratibu mifumo mbalimbali ya ufuatiliaji iliyopo. Lengo kuu la mada hii ni kubainisha mwelekeo wa mfumo thabiti wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo inayozingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mkakati wa Kupunguza Umaskini.

Maana ya Ufuatiliaji na Tathmini Katika Muktadha wa Maendeleo
165. Ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango/programu za maendeleo ni michakato inayoenda pamoja. Ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango/programu unahusu taratibu za mameneja wa miradi za kuhakiki kama shughuli za mradi zinaenda kufuatana na ratiba ya utekelezaji na kama rasilimali au njia za utekelezaji zinatumika kwa usahihi na ufanisi. Taratibu za ufuatiliaji hazina budi kumpa msimamizi (meneja) wa miradi mtiririko endelevu wa taarifa za utekelezaji katika kipindi chote cha mradi ili iwezekane kufanya maamuzi sahihi ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza. Ufuatiliaji unatawaliwa na mahusiano kati ya shughuli za utekelezaji na matokeo ya shughuli hizo, ambapo matokeo yanatokana moja kwa moja na shughuli za mradi tu.

166. Tathmini ya utekelezaji wa mipango/programu inajaribu kueleza mabadiliko katika maisha na ustawi wa walengwa. Tathmini inalinganisha hali iliyokuwepo kabla ya mpango/programu na baada ya utekelezaji, na inachambua matokeo mazuri na mabaya ya mabadiliko. Mara kwa mara, tathmini inachangia katika kufanya maamuzi ya kusimamisha shughuli fulani za mpango/programu au kuongeza shughuli nyingine. Katika mchakato wa kutathmini, hali zilizo nje ya mipango/programu ambazo zinaweza kuathiri shughuli za kuleta matokeo fulani katika hali za walengwa, pia zinaangaliwa.

MUHTASARI WA MAPITIO YA MCHAKATO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI NCHINI

Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini Kabla ya Mwaka 1995
167. Serikali ya Tanzania tangu uhuru mwaka 1961 ilianza juhudi za kuweka mfumo mzuri wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango. Kutokana na hilo, mipango ya maendeleo iliwekewa mfumo wa ufuatiliaji na programu zote za kisekta zilikuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa kuangalia mwenendo wa bajeti ya maendeleo na kupima hatua zilizofikiwa na programu hizo.

168. Mpango wa kwanza wa maendeleo wa miaka mitano ambao ulizinduliwa mwaka 1964 ulikuwa ni awamu ya kwanza katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa miaka kumi na tano. Ili kufikia madhumuni na malengo yaliyokuwa katika mpango wa muda mrefu ililazimika kukusanya nguvu za sekta zote kwa njia ya taratibu zilizohitajika na kwa makusudi kabisa ili kuendeleza viwango vikubwa vya ukuaji wa uchumi. Mchakato huu ulitumia mapitio ya katikati ya kipindi cha mpango ambayo yalibaini masuala ya kisera na kiutekelezaji yaliyohitaji kuangaliwa kwa makini zaidi katika kipindi cha mpango kilichosalia.

169. Mpangilio wa kiasasi kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji wa mpango wa miaka mitano uligawanywa katika utaratibu ufuatao; Wizara ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo (sasa Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji) ilikuwa ndiyo yenye jukumu la jumla la kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mipango. Ili kusaidia juhudi za kuleta maendeleo katika ngazi za mikoa, wilaya na vijiji, kamati za maendeleo ziliundwa ili kusaidia kazi na kutoa urahisi wa mawasiliano kati ya ngazi mbalimbali za utawala. Mchoro ufuatao unaonyesha mfumo uliokuwepo.

Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mipango na Utekelezaji: Mpangilio wa Kiasasi katika Miaka ya Sitini na Sabini

Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mipango na Utekelezaji: Mpangilio wa Kiasasi  katika Miaka ya Sitini na Sabini

 

170. Pamoja na kuwepo kwa mfumo bayana wa ufuatiliaji wa mipango na programu, kulikuwepo na vikwazo vifuatavyo: kwanza, majukumu ya kila mtendaji hayakueleweka vizuri; pili, kulikuwepo na tatizo la uhaba wa wafanyakazi katika mazingira ya kazi nyingi, tatu, kutokana na kutokuwa na vitengo vya mipango katika baadhi ya wizara, Wizara ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo haikuwa inapokea taarifa za miradi katika wakati unaotabirika, matokeo yake ilikuwa kwa kiasi kikubwa si rahisi kuchukua hatua za kuondoa vikwazo vya utekelezaji.

Mapitio ya Mchakato wa Ufuatiliaji na Tathmini Baada ya Mwaka 1995

Muhtasari wa Utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla na Uhusiano Wake na Mchakato wa Ufuatiliaji na Tathmini tangu mwaka 1995
171. Tangu mwaka 1995, Tanzania imepata mafanikio makubwa katika masuala ya maendeleo ya uchumi jumla. Mwenendo wa fedha za Serikali, unaohakikisha kuwepo kwa utengamano wa uchumi jumla na viwango vikubwa vya ukuaji, umeimarika. Kiwango cha wastani cha ukuaji wa Pato la Taifa katika kipindi cha mwaka 1995 hadi 2003 kilikuwa asilimia 4.7. Katika mwaka 2003, ukuaji ulikuwa asilimia 5.6 ambao ni chini kidogo ya kiwango cha malengo ya Mkakati wa Kupunguza Umaskini cha asilimia 6.0 katika mwaka 2003. Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 30 mwaka 1995 hadi kufikia kiwango kinachodhibitika cha wastani wa asilimia 4.4 mwaka 2003 ikilinganishwa na lengo la upandaji bei uliochini ya asilimia 4. Kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kimeongezeka na kuzidi kiwango kilichotarajiwa (miezi 4) kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje na kuwa zaidi ya miezi 6 katika miaka minne iliyopita. Hayo ni maeneo machache muhimu yenye mafanikio yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni. Jedwali Na. 10.1 linaonyesha mwenendo wa baadhi ya viashiria vya uchumi jumla katika miaka ya karibuni. Pamoja na mafanikio katika mwenendo wa uchumi jumla ni wazi kuwa juhudi za kuendeleza mwenendo huu zinahitajika katika miaka ijayo. Hii itarahisishwa kwa kuwa na mchakato wa ufuatiliaji na tathmini inayopima mafanikio yaliyopatikana kwa kulinganisha na malengo au shabaha zilizowekwa. Kwa kufanya hivyo, nchi itakuwa katika nafasi ya kubaini matatizo ya utekelezaji ya msingi na kuyatafutia njia za kuyaondoa. Viwango hivyo vya viashirio vinaonyesha mafanikio katika utekelezaji wa sera za uchumi jumla. Viashirio hivi haviwezi kutayarishwa bila kuwa na mfumo thabiti wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa sera hizo.

Mwenendo wa Baadhi ya Viashirio vya Uchumi Jumla Mwaka 1996 - 2003

 

1996

1997

1998

1999

2000

2001

2002

2003

Ukuaji wa Pato la Taifa - %

4.2

3.3

4.0

4.7

4.9

5.7

   6.2

5.6

Kasi ya upandaji bei  - %

21.0

16.1

12.9

7.8

6.0

5.2

    4.5

4.4

Ubadilishaji wa fedha (Tshs/USD) – wastani wa mwaka

580.0

612.1

664.7

744.8

808.4

876.4

966.6

1038.6

Ubadilishaji wa fedha (Tshs/USD) – mwisho wa mwaka

595.6

624.6

668.0

797.3

803.3

916.3

976.3

1063.6

Uuzaji nje (mil. US$) – FOB

763.8

752.6

588.5

543.3

663.3

776.4

902.5

1142.4

Uagizaji bidhaa (mil. US$) – FOB

1212.6

1148.0

1382.2

1415.4

1367.6

1560.3

1511.3

1973.0

Uwiano kati ya uuzaji/uagizaji nje  (Bidhaa)-%

63.0

65.6

42.6

39.7

49.6

52.0

58.7

57.9

Urari wa biashara (mil. USD)

-265.1

-403.4

-905.4

-829.5

-498.6

-480.0

-251.1

-337.2

Uwiano wa uwekezaji/Pato la Taifa - %

16.5

14.7

16.0

15.4

17.6

17.0

18.9

18.5

Uwekezaji wa moja kwa moja  (FDI) - mil. USD

148.5

157.8

172.2

516.7

463.4

327.2

240.4

247.8

Akiba za fedha za kigeni (miezi)

2.4

3.8

3.0

4.1

5.6

6.3

8.3

8.9

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

1996/97

1997/98

1998/99

1999/00

2000/01

2001/02

2002/03

2003/04 [1]

Mapato (%  ya GDPmp)

13.5

12.6

12.5

11.3

12.2

12.1

12.8

13.4

matumizi [2]    (% ya GDPmp)

17.3

17.4

17.6

18.3

20.6

19.1

23.4

24.9

Uwiano wa mapato na matumizi (kabla ya ruzuku) - % ya GDPmp

-1.7

-2.3

-2.3

-5.8

-4.6

-5.6

-8.2

-11.2

Uwiano wa mapato na matumizi (baada ya ruzuku) - % ya GDPmp

3.3

0.2

0.8

-1.6

-1.2

-1.1

-1.7

-4.0

Ukuaji wa ujazi wa fedha (M2) - %

11.6

11.0

11.1

15.0

12.5

12.3

13.0

14.2

Wastani wa riba za amana  - %

11.0

10.0

7.9

7.1

4.2

3.5

3.1

3.9

Wastani wa riba za mikopo  - %

26.5

24.0

24.5

22.1

19.6

16.4

15. 7

13.8

Deni la nje (mil. USD)

6600.3

6435.8

6580.3

6538.3

6312.2

6559.7

6413.4

6730.8

Deni la Taifa (mil. USD) [3]

7578.5

7384.6

7669.7

7624.8

7482.1

7464.0

7268.17

7890.7

Chanzo; Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji

MCHAKATO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI YA MKAKATI WA KUPUNGUZA UMASKINI NA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2025

172. Mchakato wa ufuatiliaji na tathmini nchini una ngazi tatu ambazo ni wizara kuu, wizara za kisekta, na mikoa na serikali za mitaa. Katika kila ngazi, kuna viashirio muhimu vya ufuatiliaji na tathmini ambavyo vinaendana na vigezo na maana zilizowekwa katika ngazi ya wizara kuu ili kusaidia kuoanisha utaratibu katika ngazi zote. Katika ngazi ya serikali kuu, kuna programu mbalimbali ambazo serikali inatekeleza. Baadhi ya programu hizo zina utaratibu bayana uliowekwa wa kupima mafanikio dhidi ya shabaha. Yafuatayo ni mapitio ya mifumo ya ufuatiliaji, na tathmini kuhusu Mkakati wa Kupunguza Umaskini; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; na Bajeti.

Mkakati wa Kupunguza Umaskini na Mfumo Wake wa Ufuatiliaji
173. Mwaka 2001, Serikali ilianzisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya mwenendo wa hali ya umaskini, unaolenga kufuatilia na kutathmini kikamilifu maendeleo katika utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini nchini. Mfumo wa ufuatiliaji umaskini unatoa fursa ya kupata njia iliyo sahihi ya kupima matokeo katika juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya umaskini. Matokeo muhimu ya mfumo huu ni uchapishaji wa kila mwaka wa Taarifa ya Hali ya Umaskini na Maendeleo ya Watu; upatikanaji wa taarifa za tafiti; chunguzi na chambuzi mbalimbali; uchapishaji wa majarida na taarifa za elektroniki kupitia njia za kisasa kama vile mtandao wa tarakishi. Aidha, taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini zinaandaliwa kila mwaka ili kutathmini vipaumbele vya Mkakati vilivyowekwa.

174. Mfumo huu umeendelea kutekelezwa kama iilivyobainishwa katika Mpango Kamambe wa Ufuatiliaji mwenendo wa hali ya umaskini chini ya vikundi vya kitaalam vilivyoainishwa ndani ya mfumo huo. Njia zinazotumika ili kuhakikisha mchakato unafanyakazi vizuri ni utayarishaji na usambazaji wa taarifa mbalimbali, kama vile taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini; Taarifa ya Hali ya Umaskini na Maendeleo ya Watu; na usambazaji wa taarifa za tafiti na chunguzi mbali mbali. Taarifa hizi zinatoa na kuonyesha wazi mwenendo wa viashirio vinavyopimika na hufichua picha halisi juu ya kutekelezeka au kutotekelezeka kwa shabaha za Mkakati zilizowekwa, na kuona kama hatua za kurekebisha hali iliyojitokeza zitahitajika. Mambo muhimu katika mfumo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa hali ya umaskini ni pamoja na ufafanuzi wa taarifa zinazotakiwa; taratibu za kiasasi; njia za ukusanyaji wa takwimu na taarifa za kitakwimu ; vipaumbele vya utafiti, usambazaji wa taarifa; na kuongeza uwezo wa utendaji.

175. Tatizo kubwa katika mfumo huu ni pamoja na kutopatiwa fedha kwa wakati kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za mfumo, na uhaba wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ipasavyo. Changamoto inayojitokeza ni jinsi ya kuhuisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mfumo zinazoshabihiana. Aidha, kumejitokeza haja ya kuzingatia shughuli ambazo zinatekelezwa na sekta binafsi pamoja na kuimarisha uratibu wa mfumo na kuhakikisha ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuuwezesha mfumo kufanya kazi zake vizuri zaidi.

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025
176. Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 unahitaji kuwa na mchakato thabiti wa ufuatiliaji na tathmini ili kuiwezesha Tanzania ifanikiwe kuondoka kutoka katika kundi la nchi maskini sana na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati na hali bora ya maisha ifikapo mwaka 2025. Kama malengo yatafikiwa wakati huo Tanzania itakuwa na uchumi imara na wenye kuhimili ushindani; utawala bora; jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza zaidi; na amani, utulivu na umoja.

177. Katika mchakato wa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mpango wa Muda wa Kati wa kipindi cha miaka mitatu umebainishwa kama nyenzo muhimu ya utekelezaji. Ingawa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji katika Mpango wa Muda wa Kati haujaanza kutumika lakini ni muhimu kuwa na njia thabiti na sahihi za kufanya ufuatiliaji wa mabadiliko yanayotokea katika vipindi husika.

178. Ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mpango wa Muda wa Kati umeweka viashirio vyenye kupimika ambavyo vitatumika katika mchakato wote. Kuna viashirio vya vipindi vya muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi. Njia zitakazotumika katika mchakato ni pamoja na ukaguzi wa programu na miradi inayoendelea; ukaguzi kwa vipindi vya mara kwa mara wa programu, miradi na shughuli; kuchunguza kwa makini taarifa za utekelezaji halisi wa miradi na matumizi ya fedha na taarifa za mapitio ya mwaka, nusu mwaka, robo mwaka na mwezi. Kwa mfano, Kitabu cha Hali ya Uchumi kinachotayarishwa na serikali ni moja kati ya taarifa za mwaka ambazo zinaonyesha mapitio ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa mwaka uliopita. Vile vile, kutakuwepo na mpangilio wa kiasasi ambao unajaribu kuunganisha watendaji wote katika mchakato. Asasi zitakazoratibu mchakato huu zitakuwa zile zilizopewa dhamana ya kusimamia uchumi na mipango ya maendeleo; na fedha. Asasi mbili hizi zitafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wizara za kisekta pamoja na sekta binafsi.

Umuhimu wa Bajeti Katika Ufuatiliaji wa Mipango/Programu
179. Bajeti inaandaliwa na serikali kila mwaka ili kuelekeza rasilimali za fedha katika shughuli zilizobainishwa pamoja na kuainisha vyanzo vya rasilimali hizo (mapato). Ikizingatiwa kwamba rasilimali hazitosholezi mahitaji ya shughuli zote, kuna kila sababu ya kuchagua sekta za kipaumbele, ambazo zitapewa umuhimu wakati wa zoezi la kugawa rasilimali. Ubainishaji wa sekta za kipaumbele pekee hauwezi kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wa programu. Kwa maana hiyo, kunahitajika kuwepo na utaratibu wa udhibiti ili kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa programu hizo. Katika mchakato wa utayarishaji bajeti Tanzania, kuna nyenzo tatu za udhibiti, ambazo kwa namna moja au nyingine zinakuwepo kwa ajili ya kulinda na kusimamia utekelezaji wa programu mbalimbali (ikijumuisha sekta za kipaumbele). Nyenzo hizo ni Mapitio ya Matumizi ya Serikali, Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati, na Mfumo Usimamizi wa Fedha. Kila nyenzo hutoa taarifa mwishoni mwa mwaka wa fedha kubaini mafanikio ya mwaka ulioisha.

Mapitio ya Matumizi ya Serikali
180. Mapitio ya Matumizi ya Serikali ni utaratibu muhimu katika mfumo wa kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo, dhamira yake ikiwa ni kuongeza udhibiti wa matumizi ya serikali. Mapitio ya Matumizi ya Serikali yanalenga kutimiza madhumuni yafuatayo: -

  • Kuhakikisha kuwa mkazo unaendelea kuwekwa katika malengo ya msingi ya Mkakati wa Kupunguza Umaskini;
  • Kusaidia ushiriki wa wananchi katika upangaji wa rasilimali;
  • Kuendeleza taratibu nzuri za maamuzi ya matumizi kwa kuweka wazi vipaumbele;
  • Kuboresha uratibu wa maamuzi ya matumizi ili yaendane na upatikanaji wa rasilimali katika kipindi cha muda wa kati;
  • Kujenga mfumo wa bajeti unaokidhi mahitaji ya wananchi.

181. Kimsingi, Mapitio ya Matumizi ya Serikali yana malengo muhimu mawili ambayo ni kusaidia mchakato wa kuandaa bajeti na usimamizi wa bajeti, na kutoa mrejeshonyuma kwa serikali na wadau wengine kuhusu matumizi ya serikali na masuala ya usimamizi kupitia kwa wafanya tathmini wa nje ya serikali.

Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati
182. Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati ulianzishwa mwaka 1997 kuchukua nafasi ya Mpango Unaoendelea na Bajeti ya Upeo. Mfumo huu unazingatia masuala maalumu ya sekta zilizopewa kipaumbele na kuainisha gharama zake ikizingatia muktadha mzima wa upatikanaji wa rasilimali. Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati unatekelezwa sambamba na zoezi la kuendeleza mchakato wa Mapitio ya Matumizi ya Serikali. Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati na Mapitio ya Matumizi ya Serikali kwa pamoja vimewezesha kuimarika kwa mchakato wa bajeti, hususan, katika mazingira ya kuidhinisha matumizi sahihi ya serikali katika sekta za vipaumbele chini ya Mkakati wa Kupunguza Umaskini.

183. Uanzishwaji wa mchakato wa bajeti huanza kwa kuandaa rasimu ya mwongozo wa bajeti. Mwongozo wa bajeti kimsingi ndio chombo kikuu kinachotumiwa na serikali kushinikiza mkakati wa udhibiti wa mgawanyo wa rasilimali kwa kipindi cha Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati. Mwongozo unatoa kwa kifupi sera na malengo ya mikakati kwa mwaka unaofuata. Kwa kuzingatia madhumuni ya sera na uhaba wa rasilimali kwa ujumla, kikomo cha juu cha bajeti huwa kinawekwa. Kikomo hicho kinakuwa kama kiashirio cha ufuatiliaji.

184. Ugumu wa kufuatilia bajeti ya maendeleo unatokana na uwezo mdogo wa kukagua utekelezaji halisi wa miradi na kupima mafanikio katika kufikia malengo kabla na baada ya utekelezaji wa mradi. Pia, hakuna utaratibu wa kufanya mapitio ya kina, baada ya mradi kukamilika, ya miradi yote iliyokamilika, na inayoendelea ili kuweza kupata uelewa utakaoongeza ubora wa mradi. Tathmini inayofanyika baada ya mradi kukamilika inakuwa na manufaa zaidi iwapo itatanguliwa na tathmini, kabla ya kuanza miradi, inayobainisha malengo na gharama tarajiwa. Hii inawezesha pia kuweka msingi sahihi wa kuorodhesha kwa umuhimu wake miradi itakayoingizwa katika bajeti ya maendeleo

185. Tatizo la miaka mingi katika kupanga bajeti na taratibu za kuidhinisha matumizi ni jinsi ya kudhibiti upotevu wa fedha unaotokana na kujirudia kwa matumizi kutokana na kuingiliana kwa shughuli zinazofanana lakini zinafanywa na watekekelezaji tofauti. Kwa sasa takwimu za fedha za serikali ndizo zinazotumika kama utaratibu wa ufuatiliaji katika suala hili. Hii inawezesha kupunguza kujirudia matumizi katika vitu vinavyofanana ambavyo vinajitokeza katika programu tofauti au katika bajeti zote - ya maendeleo na ya kawaida.

Mapendekezo ya Mwelekeo wa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini
186. Kama ilivyoelezwa mwanzo, madhumuni ya kuanzisha mfumo wenye ufanisi wa ufuatiliaji na tathmini ni kuhakikisha kuwa utekelezaji wa programu/mpango unaendelea kufuatana na malengo yaliyobainishwa. Kwa sababu za kiufanisi, na baada ya kufanya marekebisho madogo, mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini, unaweza ukapanuliwa na kuwa utaratibu wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Kama ilivyo katika Mkakati wa Kupunguza Umaskini, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 nayo pia itakuwa na viashirio vya ufuatiliaji vitakavyoongoza utekelezaji wake katika kipindi cha muda wa kati. Tofauti na Mkakati wa Kupunguza Umaskini ambao viashirio vyake vya ufuatiliaji vinalenga katika umaskini, viashiria vya ufuatiliaji na tathmini katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 vitalenga katika kupima hatua zinazofikiwa katika kutekeleza malengo yote ya Dira.

Hitimisho.
187. Katika kuandaa utaratibu wa jumla wa utoaji wa takwimu za taarifa za ufuatiliaji wa utekelezaji mipango na programu za maendeleo ni muhimu kukumbuka kwamba misingi mizuri ya ufuatiliaji tayari imeshawekwa kutokana na mchakato wa kuleta mageuzi katika utendaji wa serikali ili kuboresha ufanisi wa huduma zake. Hatua kubwa imepigwa katika kuweka taratibu za kusimamia matumizi ya serikali ikiwa ni pamoja na utaratibu wa mapitio ya matumizi ya serikali, na Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati. Kwa upande wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini taratibu zilizowekwa ni thabiti. Taratibu hizi za kusimamia matumizi ya serikali na taratibu za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini hazina budi kuendelezwa na kupanuliwa ili kukidhi mahitaji ya ufuatiliaji na tathmini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

188. Mipango mingi ya serikali kuu ina mifumo ya ufuatiliaji na tathmini lakini haijionyeshi dhahiri. Ukiachilia mbali Mkakati wa Kupunguza Umaskini ambao una mfumo madhubuti wa ufuatiliaji, mipango mingine ya serikali kuu haijabainisha waziwazi taratibu na viashirio vya ufuatiliaji. Taarifa na takwimu za ufuatiliaji huwa zinatolewa kwa baadhi ya programu na kila moja ikilenga kutimiza lengo la programu husika. Hata hivyo, kuna haja ya kuwa na mfumo rasmi wa kuunganisha mifumo ya utoaji takwimu na taarifa za ufuatiliaji na tathmini kwa programu zote za serikali kuu, katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mkakati wa Kupunguza Umaskini.