MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI |
||||||||
| MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | ||||||||
Hali
ya Uchumi wa Taifa |
||||||||
FEDHA
NA TAASISI ZA FEDHA |
||||||||
Ujazi wa Fedha na Karadha
98. Mwaka 2003/04, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) uliongezeka kwa sh. 297,542.3 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 19.1 kutoka sh. 1,558,784 milioni Juni 2003 hadi sh. 1,856,326.3 milioni Juni 2004. Ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) lilikuwa chini ya lengo lililopangwa la asilimia 20.2. Ongezeko hilo lilichangiwa zaidi na ongezeko la amana za hundi, amana za akiba na fedha zilizo katika mzunguko nje ya mabenki. Ongezeko la amana za muda maalum lilikuwa dogo zaidi ikilinganishwa na ongezeko la amana za aina nyingine. Kiwango cha ukuaji wa fedha zilizo katika mzunguko nje ya mabenki kiliongezeka kwa asilimia 24.6, ikilinganishwa na asilimia 10.3 mwaka 2002/03. Aidha, amana za hundi na amana za akiba ziliongezeka kwa asilimia 17.4 na 21.2 mwaka 2003/04 ikilinganishwa na asilimia 31.4 na 10.5 mwaka 2002/03, kwa mtiririko huo. 99. Katika kipindi cha Julai-Desemba 2004, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) uliongezeka hadi kufikia sh. 2,050,885.9 milioni, kutoka sh. 1,856,326.3 milioni Juni 2004, sawa na ongezeko la asilimia 10.5. Katika kipindi hicho, ujazi wa fedha ulichangiwa zaidi na fedha zilizo kwenye mzunguko nje ya mabenki ikilinganishwa na amana za akiba, hundi na muda maalum. 100. Mwaka 2003/04, karadha nchini iliongezeka kutoka sh. 858,204 milioni Juni 2003, hadi sh. 1,123,597.8, sawa na ongezeko la asilimia 31.0. Ongezeko hilo lilitokana na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Karadha kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 47.0 mwaka 2003/04, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 36.6 mwaka 2002/03. Jedwali Na. 27 linaonyesha mchanganuo wa ujazi wa fedha na karadha nchini na Jedwali Na. 28 linaonyesha viwango vya mabadiliko ya mchanganuo huo. Mikopo ya Benki za Biashara kwa Sekta Mbalimbali 101. Mwaka 2003/04, mikopo iliyotolewa kwa sekta mbalimbali iliongezeka kutoka sh. 658,524.6 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 965,985.9 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 46.7. Sekta zilizopata viwango vikubwa vya mikopo ni uzalishaji katika kilimo, biashara, na sekta nyinginezo. Mpango wa Kutoa Dhamana kwa Mikopo ya Kununulia Mazao ili Kuuzwa Nje uliendelea kuifanya sekta ya uzalishaji katika kilimo kuwa miongoni mwa sekta zilizopata viwango vikubwa vya mikopo. Serikali iliendelea kutekeleza Mpango huo ili kukuza uchumi, kuongeza ajira, na uuzaji wa mazao nje ya nchi. 102. Mwaka 2003/04, serikali iliendelea kuandaa mazingira mazuri ili kuziwezesha sekta mbalimbali kukopa zaidi. Aidha, serikali iliendelea kuweka muundo na taratibu za usimamizi wa benki zinazotoa mikopo midogo ili kuwawezesha wafanyabiashara wengi kupata mikopo hiyo. 103. Mwaka 2003/04, serikali iliendelea kukopa kwa kuuza dhamana zake. Jumla ya dhamana za sh. 375,500 milioni ziliuzwa, ikilinganishwa na sh. 347,166 milioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 8.2. Katika kipindi hicho, hawala za Hazina ziliongezeka kutoka sh. 190,446.1 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 205,111.9 milioni, wakati ambapo hawala za serikali ziliongezeka kutoka sh. 156,719.9 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 170,388.1 milioni. 104. Mwaka 2003/04, mikopo iliyotolewa na benki za biashara kwa sekta binafsi iliongezeka kutoka sh. 658,524 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 965,980.9 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 46.7. Kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi kulitokana na utekelezaji wa azma ya serikali ya kuacha kukopa kutoka benki za biashara, ili benki hizo ziweze kukopesha sekta binafsi zaidi. 105. Mwaka 2004, baadhi ya benki za biashara zilianza kutoa huduma mpya za mikopo, ambazo dhamana yake ni mazao ya kilimo, mshahara kwa wafanyakazi wa serikali na vifaa vya nyumbani. Amana katika Benki za Biashara 106. Mwaka 2003/04, jumla ya amana katika benki za biashara ziliongezeka kutoka sh. 1,732,190.4 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 2,012,493.8, milioni sawa na ongezeko la asilimia 16.2, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 26.6 mwaka 2002/03. Kupungua kwa kiwango cha ongezeko kulitokana na viwango vya riba za amana katika benki za biashara kubakia vya chini, hivyo kutowavutia wateja. Mchango wa amana za fedha za kigeni katika amana zote ulikuwa asilimia 37.1, hundi asilimia 29.6, akiba asilimia 19.9, na za muda maalum asilimia 13.4. Huduma Mpya katika Mabenki 107. Mwaka 2003/04, ushindani baina ya benki za biashara katika kutoa huduma za kibenki uliendelea kupanuka kama vile huduma ya kuweka fedha kwa kutumia mashine maalum. ATM, awali mashine hizo zilitoa huduma ya kuchukua fedha na kujua salio. Huduma nyingine mpya zilizoanzishwa ni pamoja na kujua salio la akiba kwa kutumia simu ya kiganjani, iliyoanzishwa na benki ya CRDB, kupelekewa fedha kwa wateja wakubwa, na kujua salio la akiba kwa kutumia tarakishi. Mwenendo wa Viwango vya Riba 108. Wastani wa riba zilizotolewa na benki za biashara kwa amana za akiba ulishuka kidogo kutoka asilimia 2.5 Juni 2003 hadi asilimia 2.4 Juni 2004. Hadi mwishoni mwa Desemba 2004, wastani wa riba uliongezeka kidogo na kufikia asilimia 2.6. Riba ya mikopo ya Benki Kuu kwa benki za biashara na serikali iliongezeka kutoka wastani wa asilimia 10.6 Juni 2003, hadi asilimia 12.6 Juni 2004. Hadi Desemba 2004, wastani ulifikia asilimia 14.4. Wastani wa riba za muda maalum uliongezeka kutoka asilimia 3.5 Juni 2003 hadi asilimia 4.4 Juni 2004. Hata hivyo, riba hiyo ilishuka hadi wastani wa asilimia 3.9 Desemba 2004. Wastani wa riba za hawala za hazina uliongezeka kutoka asilimia 5.9 Juni 2003 hadi kufikia asilimia 7.8 Juni 2004, na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 9.6 Desemba 2004. 109. Wastani wa riba zilizotozwa na benki za biashara kwa mikopo ya muda mfupi, zilipungua kutoka wastani wa asilimia 16.4 Juni 2003 hadi asilimia 15.7 Juni 2004 na kuendelea kushuka hadi asilimia 14.2 Desemba 2004. Mikopo ya muda wa kati na mrefu ilitozwa riba ya wastani wa asilimia 14.1 Juni 2004 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 13.5 Juni 2003, na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 14.5 Desemba 2004. Benki za biashara zilikuwa zikitoza riba tofauti kwa aina moja ya mkopo kwa wakopaji tofauti. Mwenendo wa riba katika benki za biashara, ulionyesha bado kulikuwa na tofauti kubwa kati ya riba za amana na za mikopo. Benki Kuu ya Tanzania 110. Mwaka 2003/04, amana za serikali katika Benki Kuu ziliongezeka kutoka sh. 248,382 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 254,779.2 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 2.6. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Katika kipindi hicho, amana za benki za biashara katika Benki Kuu nazo ziliongezeka kutoka sh. 117,100.2 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 156,390.1 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 33.5. 111. Mwaka 2003/04, jumla ya mapato yote ya Benki Kuu yalifikia sh. 192,133.7 milioni kutoka sh. 202,499.2 milioni mwaka 2002/03, sawa na upungufu wa asilimia 5.1. Shughuli za fedha za kigeni ziliingizia Benki Kuu mapato ya sh. 193,635.7 milioni sawa na ongezeko la asilimia 2.1, ikilinganishwa na sh. 189,710.6 milioni mwaka 2002/03. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa shughuli za wawekezaji wa nje. Mapato kutokana na shughuli za ndani yalipungua kutoka sh. 12,788.6 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. – 1,502 milioni mwaka 2003/04, sawa na upungufu wa asilimia 111.7. 112. Mwaka 2003/04, jumla ya matumizi ya Benki Kuu yalifikia sh. 64,593 milioni ikilinganishwa na sh. 64,667 milioni mwaka 2002/03, sawa na upungufu wa asilimia 0.1. Upungufu huo ulitokana na kumalizika kwa shughuli za utoaji wa noti mpya mwaka 2002/03. Shughuli za ndani ya nchi ziliigharimu Benki Kuu sh. 23,211.3 milioni, ikilinganishwa na sh. 10,440.7 milioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 122.3. 113. Kutokana na mwenendo huo wa mapato na matumizi ya Benki Kuu, faida iliyopatikana mwaka 2003/04 ilifikia sh. 17,749.2 milioni ikilinganishwa na sh. 20,004.7 milioni mwaka 2002/03, sawa na upungufu wa asilimia 11.3. Benki Kuu ilitoa gawio la sh. 5,086.8 milioni kwa serikali katika mwaka 2003/04, ikilinganishwa na sh. 5,004.0 milioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 1.7. Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) 114. Hadi Desemba 2004, makampuni 408 yalikuwa yamejiunga na Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma, ikilinganishwa na makampuni 362 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 11.9. Thamani ya vitega uchumi iliongezeka kutoka sh. 133.08 bilioni mwaka 2003, hadi sh. 178.36 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 34.0. 115. Uwekezaji katika hawala za hazina na dhamana nyingine za serikali na mashirika mbalimbali uliongezeka kutoka sh.20.8 bilioni mwaka 2003 hadi sh. 51.15 bilioni mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 145.9. Makusanyo kutoka kwa wanachama yaliongezeka kutoka sh. 33.7 bilioni mwaka 2003 hadi sh. 42.85 bilioni mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 27.2. Idadi ya wanachama ilipungua hadi 69,092, mwaka 2004, ikilinganishwa na wanachama 72,755 mwaka 2003. Kupungua kwa wanachama kulitokana na upunguzaji wa wafanyakazi katika mashirika ya umma yaliyobinafsishwa. Mafao yaliyotolewa kwa wanachama yalikuwa sh. 14.75 bilioni mwaka 2004, ikilinganishwa na sh 16.68 bilioni mwaka 2003. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) 116. Mwaka 2003/04, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii uliendelea kukusanya michango na kutoa mafao kwa wanachama wake. Michango kutoka kwa wanachama iliongezeka kutoka sh. 63,329.53 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 81,729.80 milioni mwaka 2003/04, sawa na ongezeko la asilimia 29.1. Kuongezeka kwa michango kulitokana na kuongezeka kwa waajiri na wanachama wapya katika kipindi hicho. Mwaka 2003/04, idadi ya wanachama ilifikia 353,835, ikilinganishwa na wanachama 327,609 mwaka 2002/03, wakati idadi ya waajiri iliongezeka kutoka 15,097 mwaka 2002/03, hadi waajiri 15,970 mwaka 2003/04. Kuongezeka kwa waajiri na wanachama katika kipindi hicho kulitokana na ufuatiliaji wa karibu katika kusajili wanachama wapya kutoka makampuni mapya na yaliyokuwepo. Jumla ya mafao yaliyotolewa kwa wanachama yalikuwa sh. 23,416.06 milioni mwaka 2003/04, ikilinganishwa na sh. 19,828.79 milioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 18.1. Kuongezeka kwa mafao yaliyotolewa kulitokana hasa na kupoteza ajira kwa baadhi ya wanachama. 117. Jumla ya thamani ya uwekezaji katika vitega uchumi ilifikia sh. 280,833.21 milioni mwaka 2003/04, ikilinganishwa na sh. 230,778.44 milioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 21.7. Ongezeko hilo lilitokana na kuendelea kupanuka kwa shughuli za uwekezaji uliokuwepo na uwekezaji mpya. Uwekezaji katika mitaji ya muda mrefu uliongezeka hadi sh. 236,778.01 milioni mwaka 2003/04, ikilinganishwa na sh. 183,839.59 milioni mwaka 2002/03. Ongezeko hilo lilitokana hasa na ongezeko kubwa katika uwekezaji wa mikopo ya muda mrefu, dhamana za shirika na za serikali. Uwekezaji katika mitaji ya muda mfupi ulipungua kutoka sh. 46,938.85 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 44,055.20 milioni mwaka 2003/04, sawa na upungufu wa asilimia 6.1. Kupungua kwa thamani ya uwekezaji kulitokana na kupungua kwa uwekezaji katika hawala za Hazina. Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) 118. Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma ulianzishwa kwa Sheria Namba 2 ya mwaka 1999 na kufuta sheria ya Pensheni sura 371 ya mwaka 1954. Wanachama wa Mfuko huu ni watumishi wa Serikali Kuu na Wakala wa Serikali ambao wameajiriwa katika masharti ya kudumu na malipo ya uzeeni. Mapato ya Mfuko huu yanatokana na michango ya wanachama, asilimia 5 ya mshahara wa kila mwezi wa mwanachama; mchango wa mwajiri asilimia 15 ya mshahara wa kila mwezi wa mwanachama; na faida inayopatikana kutokana na uwekezaji. Mfuko huu umewekeza katika hawala za Hazina na dhamana mbalimbali za serikali. Mafao yatolewayo na Mfuko huu ni malipo ya uzeeni, ulemavu, mirathi, malipo ya wategemezi, na msaada wa mazishi. Aidha, Mfuko unarejesha michango kwa mwanachama aliyeachishwa au kufukuzwa kazi. 119. Makusanyo kutoka kwa wanachama yaliongezeka kutoka sh. 53,010.09 milioni mwaka 2002/03 hadi sh.63,091.60 milioni mwaka 2003/04, sawa na ongezeko la asilimia 19.0. Idadi ya wanachama mwaka 2003/04 ilifikia 205,681 ikilinganishwa na wanachama 196,307 mwaka 2002/03. Mfuko ulianza kulipa mafao kwa wanachama wake kuanzia Julai 2004. Hadi Desemba 2004, Jumla ya mafao yaliyotolewa kwa wanachama ni sh. 9,519.85 milioni. 120. Uwekezaji katika hawala za Hazina na dhamana nyingine za serikali uliongezeka kutoka sh. 179, 305.20 milioni mwaka 2002/2003 hadi kufikia sh. 253,291.71 milioni mwaka 2003/2004, sawa na ongezeko la asilimia 41.3. Mapato yaliyopatikana kutokana na uwekezaji yaliongezeka kutoka sh. 8,697.86 milioni mwaka 2002/03 hadi sh. 15,172.71 milioni mwaka 2003/04. Faida iliyopatikana mwaka 2003/04 ilikuwa sh. 75,254.03 milioni, ikilinganishwa na sh. 59,520.15 milioni mwaka 2002/03, sawa na ongezeko la asilimia 26.4. Benki ya Posta 121. Mwaka 2004, amana za wateja ziliongezeka na kufikia sh. 50,391 milioni, kutoka sh. 49,651 milioni mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 1.5. Idadi ya wateja wenye amana katika Benki iliongezeka kutoka 1,104,954 mwaka 2003 hadi 1,117,844 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 1.2. 122. Mwaka 2004, Benki iliendelea kuwekeza katika hawala za hazina. Maeneo mengine ya uwekezaji ni akaunti za muda maalumu katika benki nyingine na kukopesha. Jumla ya uwekezaji ilipungua na kufikia sh. 42,124 milioni mwaka 2004, kutoka sh. 43,153 milioni mwaka 2003, sawa na upungufu wa asilimia 2.4. Vilevile, uwekezaji katika dhamana za serikali ulipungua kutoka sh. 26,359.5 milioni hadi sh. 24,043 milioni, sawa na upungufu wa asilimia 8.8. Uwekezaji katika mikopo uliongezeka kutoka sh. 8,932 milioni mwaka 2003, hadi sh.11,564 milioni mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 29.5. 123. Ingawa biashara ya Benki ilishuka kwa ujumla, mikopo kwa wateja iliongezeka zaidi. Kuongezeka huku kwa mikopo kwa wateja kulitokana na mikopo hiyo kuwa na uhakika wa marejesho na pia ni ya gharama nafuu. Idadi ya wateja waliokopa iliongezeka kutoka 5,518 mwaka 2003, hadi 10,633 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 92.7. Kiasi kilichokopwa kilifikia sh.8,032 milioni mwaka 2004, kutoka sh.7,039 milioni mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 14.1. Licha ya Benki kupata faida kwa kipindi kirefu, taarifa za awali za ukaguzi wa hesabu, zilionyesha kuwa Benki ilipata hasara ya sh.25 milioni mwaka 2004. Jedwali Na. 27(MWENENDO WA KARADHA NA UJAZI WA FEDHA - TANZANIA BARA) Jedwali Na. 28(VIWANGO VYA UKUAJI WA KARADHA NA UJAZI WA FEDHA - TANZANIA BARA) Jedwali Na. 29(MWENENDO WA VIWANGO VYA UBADILISHAJI KATI YA SHILINGI NA DOLA YA MAREKANI) Jedwali Na. 30(MIKOPO YA BENKI ZA BIASHARA KWA SEKTA MBALIMBALI) Jedwali Na. 31(MWENENDO WA AMANA KATIKA BENKI ZA BIASHARA) Jedwali
Na. 32( VIWANGO VYA WASTANI VYA RIBA) |
||||||||