MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI |
|||||||
| MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | |||||||
Hali
ya Uchumi wa Taifa |
|||||||
FEDHA
ZA SERIKALI |
|||||||
MAPATO
80. Sera za bajeti ya mwaka 2004/05, zililenga kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa 2025 na Mkakati wa Kupunguza Umaskini, na kutia chachu katika maendeleo ya Taifa. Serikali ilipanga kukusanya mapato ya ndani ya sh. 1,739,288 milioni, sawa na asilimia 14.4 ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na asilimia 13.3 mwaka 2003/04. Mapato ya kodi yalikadiriwa kuwa sh. 1,599,165 milioni na mapato yasiyo kodi sh. 140,122 milioni. Misaada na mikopo ikiwa ni pamoja na misamaha ya madeni chini ya Utaratibu wa Kuzipunguzia Madeni Nchi Maskini, yalikadiriwa kuwa sh. 1,233,578 milioni. Mapato ya Ndani 81. Mapato halisi ya ndani kwa kipindi cha Julai 2004 hadi Machi 2005 yalifikia sh. 1,314,523.8 milioni, ikilinganishwa na sh.1,089,261.9 milioni kipindi kama hicho mwaka 2003/04, sawa na ongezeko la asilimia 20.7. Mapato hayo ni sawa na asilimia 101.7 ya makadirio ya sh.1,292,843 milioni. Mapato yanayotokana na kodi yalichangia sh.1,205,492.8 milioni, sawa na asilimia 91.7 ya mapato ya kipindi hicho, wakati mapato yasiyotokana na kodi yalikuwa sh.109,031.0 milioni, sawa na asilimia 8.3 ya mapato ya kipindi hicho. 82. Katika kipindi cha Julai 2004 hadi Machi 2005, mwenendo wa mapato ya ndani ulikuwa ni wa kuridhisha kutokana na kuongezeka kwa ufanisi katika ukusanyaji wa kodi, hususan, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa za petroli na Kodi ya Mapato. Aidha, makusanyo ya kodi za ushuru wa forodha na bidhaa zinazozalishwa nchini yaliongezeka katika kipindi cha Julai 2004 - Machi 2005 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia kutokana na ongezeko kubwa la uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi katika kipindi hicho. Mwenendo wa mapato ya ndani ya serikali, unaonyesha kuwa hadi mwishoni mwa Juni 2005, jumla ya mapato halisi yanakadiriwa kufikia sh. 1,768,060 milioni, sawa na asilimia 101.7 ya makadirio ya mwaka 2004/05. Misaada na Mikopo ya Nje 83. Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2005, misaada na mikopo, ikijumuisha msamaha wa madeni chini ya Utaratibu wa Kuzipunguzia Madeni Nchi Maskini, ilifikia sh. 1,132,450 milioni. Kati ya hizo, misaada ilikuwa sh. 595,238 milioni, mikopo sh. 490,592 milioni, na msamaha wa madeni sh. 46,620 milioni. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ilifikia sh. 719,817 milioni katika kipindi hicho, sawa na ziada ya asilimia 23.0 ya makisio ya sh.585,375 milioni. Matumizi 84. Mwaka 2004/05, sera za matumizi ya serikali zililenga kuongeza ufanisi katika matumizi ili kufanikisha malengo ya Taifa ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini, kama yalivyoainishwa katika Mkakati wa Kupunguza Umaskini (MKU). Serikali ilipanga kutumia jumla ya sh. 3,347,538 milioni, sawa na asilimia 28.3 ya Pato la Taifa. Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida yalikadiriwa kuwa sh. 1,774,773 milioni na yale ya miradi ya maendeleo sh. 1,091,590 milioni, ikiwa ni uwiano wa asilimia 67.0 na asilimia 33.0, kwa mtiririko huo. Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, mishahara, sh. 551,159 milioni, sawa na asilimia 31.1, sekta za kipaumbele kama zilivyoainishwa katika Mkakati wa Kupunguza Umaskini zilitengewa sh. 374,358 milioni, sawa na asilimia 21.1 ya matumizi, na matumizi mengine yalitengewa sh. 849,256 milioni, sawa na asilimia 47.8. 85. Kati ya Julai 2004 na Machi 2005, jumla ya matumizi yalikuwa sh. 2,429,269 milioni, sawa na asilimia 97.5 ya makisio ya sh. 2,486,892 milioni katika kipindi hicho, sawa na upungufu wa asilimia 2.4. Matumizi ya kawaida yalifikia sh. 1,248,105 milioni, sawa na asilimia 51.4 ya matumizi yote na sh. 869,202 milioni zilitumika katika miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 35.8 ya matumizi yote. Matumizi kupitia Mfuko Mkuu (CFS) yalifikia sh. 311,962 milioni, sawa na asilimia 12.7 ya matumizi yote katika kipindi hicho. 86. Mwaka 2004/05, kiasi cha asilimia 7.8 ya bajeti kilitengwa kwa ajili ya sekta ya afya, ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2003/04. Sekta za kilimo, misitu, uvuvi na uwindaji zilitengewa asilimia 4.6, ikilinganishwa na asilimia 3.5 mwaka 2003/04. Bajeti ya utafiti wa kilimo ilikuwa asilimia 3.7 ya bajeti yote iliyoelekezwa katika kilimo. Mgao kwa sekta ya usalama ulipungua na kufikia asilimia 3.9 mwaka 2004/05, ikilinganishwa na asilimia 4.5 mwaka 2003/04. Sehemu ya bajeti iliyoelekezwa kwenye sekta ya huduma za uchumi (biashara, utalii, huduma za kazi nk) ilipungua kutoka asilimia 4.4 mwaka 2003/04 hadi asilimia 4.0 mwaka 2004/05. Mgao kwa sekta za madini, viwanda na ujenzi ulipungua na kufikia asilimia 5.4 mwaka 2004/05, kutoka asilimia 6.0 mwaka 2003/04, kulikotokana na kupungua kwa miradi ya ujenzi. Sekta ya ujenzi pekee ilichukua asilimia 83 ya jumla hii. Mgao kwa sekta ya elimu uliendelea kupungua na kufikia asilimia 11.8 mwaka 2004/05, kutoka asilimia 17.3 mwaka 2003/04. Kiasi cha bajeti iliyoelekezwa katika sekta ya usafirishaji na mawasiliano kilipungua na kufikia asilimia 7.8 mwaka 2004/05, kutoka asilimia 8.3 mwaka 2003/04. 87. Sekta ya nishati ilitengewa asilimia 3.0. Vile vile, kiasi kilichotengwa kwa sekta ya hifadhi ustawi na huduma za jamii ilipungua kutoka asilimia 1.6 hadi asilimia 1.0 mwaka 2004/05. Huduma nyingine za kijamii zilitengewa asilimia 0.1 mwaka 2004/05 kama ilivyokuwa mwaka uliotangulia 88. Mgao kwa huduma ya umma na shughuli nyingine za uchumi na jamii ilipanda kutoka asilimia 17.7 mwaka 2003/04 hadi asilimia 22.9 mwaka 2004/05. Deni la Taifa 89. Hadi Desemba 2004, deni la taifa lilikuwa dola 9,219.3 milioni, ikilinganishwa na dola 8,793.2 milioni Desemba 2003, sawa na ongezeko la asilimia 4.9. Kati ya deni hilo, dola 928.3 milioni lilikuwa la ndani, sawa na asilimia 10.1 na dola 8,291 milioni lilikuwa la nje, sawa na asilimia 89.9. Deni la Nje 90. Hadi Desemba 2004, deni la nje lilikuwa dola 8,291 milioni, ikilinganishwa na dola 7,890.7 milioni Desemba 2003, sawa na ongezeko la asilimia 5.1. Kati ya deni hilo, dola 6,990.6 milioni ilikuwa mikopo iliyotolewa na dola 1,300.4 milioni ilikuwa malimbikizo ya riba. Serikali ilipata mkopo wa dola 6,374 milioni sawa na asilimia 91.2 ya mikopo yote iliyotolewa, wakati mashirika ya umma na sekta binafsi yalikopeshwa dola 149.2 milioni (asilimia 2.1), na dola 467.4 milioni (asilimia 6.7), kwa mtiririko huo. Ongezeko la deni lilitokana na malimbikizo ya riba kwa madeni ambayo hayajapata msamaha, kuyumba kwa kiwango cha kubadilisha fedha za kigeni, na kutolewa kwa mikopo mipya kutoka kwa wahisani. 91. Hadi Desemba 2004, jumla ya ahadi za mikopo kutoka wahisani ilikuwa dola 8,740.3 milioni. Kati ya hiyo, dola 6,990.6 milioni ilikuwa imetolewa na kiasi cha dola 1,749.7 milioni kilikuwa hakijatolewa. Kati ya mikopo iliyotolewa na wahisani, dola 4,820.5 milioni (asilimia 69) zilitoka kwenye mashirika ya kimataifa, dola 1,520.1 milioni (asilimia 21.7) nchi wahisani, dola 401.7 milioni (asilimia 5.7) wakopeshaji wa kibiashara, na dola 248.2 milioni (asilimia 3.6) na wakopeshaji binafsi. Kiwango cha mikopo kutoka mashirika ya kimataifa kilikuwa cha juu ikilinganishwa na wakopeshaji wengine. Hii ilitokana na sera ya serikali inayosisitiza kukopa mikopo yenye masharti nafuu kutoka mashirika hayo. 92. Hadi Desemba 2004, asilimia 19.5 ya mikopo iliyotolewa ilikuwa kwa ajili ya kusaidia mizania ya malipo na nchi za nje. Sekta za miundombinu zilipata asilimia 16.2, kilimo, na nishati na madini zilipata asilimia 15.3 na 13.6 kila moja, kwa mtiririko huo. Mikopo iliyotolewa kwa sekta ya viwanda ilikuwa asilimia 6.0, wakati mikopo iliyotolewa kwa sekta za elimu, bima na utalii ilikuwa asilimia 5.0, 1.2 na 1.2 ya mikopo kutoka nje, kwa mtiririko huo. Asilimia 22.1 ya mikopo yote ya nje ilitolewa kwa sekta nyingine. Mpango wa Kuzipunguzia Madeni Nchi Maskini Zenye Madeni Makubwa - HIPC 93. Serikali iliendelea kupata misamaha ya deni la nje chini ya Mpango wa Kuzipunguzia Madeni Nchi Maskini Zenye Madeni Makubwa. Mwaka 2004, serikali ilipata misamaha ya deni la nje la kiasi cha dola 329.8 milioni, kutoka mashirika ya kimataifa ya fedha, kwa viwango vinavyooneshwa katika mabano kama ifuatavyo: Shirika la Maendeleo la Kimataifa (dola 205.1 milioni), Shirika la Fedha la Kimataifa (dola 65.6 milioni ), Benki ya Maendeleo ya Afrika (dola 37.2 milioni), Benki ya Uwekezaji ya Nchi za Ulaya (dola 8.3 milioni), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (dola 8.0 milioni) ), Mfuko wa Maendeleo wa Norway (dola 5.5 milioni), na Shirika la Maendeleo la Norway (dola 0.11 milioni). Jumla ya deni lililosamehewa na nchi wahisani ambazo ni wanachama wa Klabu ya Paris lilikuwa dola 858.7 milioni. Nchi zilizotoa misamaha hiyo ni pamoja na Austria, Ubelgiji, Canada, Ujerumani, Ufaransa, na Italia. Nchi nyingine ni Urusi, Japani, Uholanzi, Norway, Uingereza, na Marekani. 94. Mwaka 2004, msamaha wa madeni uliotolewa na nchi zisizo wanachama wa Klabu ya Paris ulikuwa dola 104.3 milioni. Nchi zilizotoa msamaha huo ni Bulgaria, India na Kuwait. Pia, Kuwait ilisogeza mbele ulipwaji wa deni lake la kiasi cha dola 31.8 milioni, wakati China ilitoa msamaha wa deni la dola 37.7 milioni nje ya utaratibu wa HIPC. Hata hivyo, serikali iliendelea kufanya majadiliano na nchi za Hungary, Libya na Abu Dhabi ili kupunguziwa deni lililokuwa linadaiwa na nchi hizo. Fedha zilizotokana na msamaha wa madeni zilitumika kwenye baadhi ya sekta zilizopewa kipaumbele katika Mkakati wa Kupunguza Umaskini, zikiwemo elimu, maji, afya, kilimo, barabara vijijini na utawala bora. Ulipaji wa Deni la Nje 95. Mwaka 2004, ulipaji wa deni la nje ulipungua kutoka dola 238.1 milioni mwaka 2003 hadi dola 149.9 milioni. Kupungua huko kulitokana na utekelezaji wa Mikataba ya Makubaliano ya Madeni na wanachama wa Klabu ya Paris chini ya mpango wa HIPC na msamaha wa madeni uliotolewa na nchi wahisani. Kati ya deni lililolipwa, dola 126.3 milioni, zililipwa kwa wakopeshaji wa mashirika ya kimataifa, wakati dola 4.1 milioni na dola 19.5 milioni zililipwa kwa nchi wahisani na wakopeshaji wa kibiashara, kwa mtiririko huo. Deni la Ndani 96. Hadi Desemba 2004, deni la ndani lilifikia sh. 968.2 bilioni, ikilinganishwa na deni la sh. 919.3 bilioni katika kipindi kilichoishia Desemba 2003, sawa na ongezeko la asilimia 5.3. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa uuzaji wa dhamana za serikali na hawala za Hazina. 97. Wanunuzi wakubwa wa dhamana za serikali na hawala za Hazina ni benki za biashara (asilimia 36.5), mifuko ya jamii (asilimia 35.5), Benki Kuu (asilimia 20.6) , taasisi zisizo za benki (asilimia 1.9), bima (asilimia 2.6), binafsi (asilimia 1.8), na mashirika mengine ya kiserikali na mifuko maalum ya Benki Kuu (asilimia 1.1). Jedwali Na. 25(MWENENDO WA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI)MWENENDO WA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALIl Jedwali Na. 26(MGAWANYO WA HUDUMA ZA SERIKALI ) |
|||||||