MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI |
|||||||||||||
| MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI | |||||||||||||
Kilimo |
|||||||||||||
AFYA |
|||||||||||||
Hali
ya Magonjwa kwa Jumla
293. Mwaka 2004, idadi ya wagonjwa iliendelea kuwa kubwa. Idadi ya wagonjwa wa kifua kikuu iliongezeka kutoka 63,211 mwaka 2003, hadi kufikia 64,665 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 2.3. Mikoa ambayo ilikuwa na wagonjwa wengi zaidi ni Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Arusha, Iringa na Mbeya. Ugonjwa wa malaria bado uliendelea kuwa tatizo. Utafiti wa ubora wa dawa za tiba ya malaria na dawa ya mseto uliendelea kufanyika katika vituo vya Masasi, Muheza, Kigoma, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Morogoro na Pwani. Matokeo ya tafiti yalionyesha kuwa usugu wa vimelea vya malaria uliongezeka na hivyo dawa mbadala (dawa ya mseto) kwa matibabu ya malaria inaendelea kufanyiwa utafiti zaidi. Serikali iliendelea kushirikiana na wadau wengine ikiwemo sekta binafsi katika kuhamasisha jamii kutumia vyandarua vyenye viuatilifu. Pia, mpango wa hati punguzo ulianzishwa ili kurahisisha upatikanaji wa vyandarua vyenye viuatilifu kwa ajili ya akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Juhudi nyingine zilizoendelea kufanyika katika kupambana na hali ya magonjwa ni pamoja na kutoa elimu ya afya, na kuweka msisitizo juu ya usafi wa mazingira na matumizi ya maji salama. UKIMWI 294. Mwaka 2004, janga la UKIMWI bado liliendelea kuwa tishio. Makisio yaliyofanywa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, yalionyesha kuwa watu 1,810,000 walikuwa wanaishi na virusi vya UKIMWI mwaka 2003. Hadi mwishoni mwa 2004, wagonjwa 4,200 walianzishiwa dawa za kurefusha maisha katika vituo vya afya 32, katika mikoa 12. Aidha, huduma ya tiba kwa wagonjwa wa UKIMWI majumbani ilianzishwa katika wilaya 65 na mafunzo kwa watoa huduma 814 yalifanyika na walipatiwa vifaa vya kuhudumia wagonjwa majumbani. Jumla ya wagonjwa 20,000 (wanaume 9,150 na wanawake 10,850) walikuwa wakipatiwa huduma hii. Elimu ya Afya kwa Wananchi na Afya ya Mazingira 295. Mwaka 2004, Sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali zitumikazo viwandani na majumbani iliendelea kutekelezwa. Sampuli za kemikali 3,934 zilichunguzwa na Mkemia Mkuu wa Serikali na kati ya hizo, asilimia 82 zilifikia viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa kwa matumizi ya binadamu na usalama wa mazingira. Pia, mitambo ya kisasa na vifaa vya maabara vilinunuliwa na elimu kwa umma kuhusu kemikali zilizopigwa marufuku duniani ilitolewa. Katika jitihada za kuwafikishia wananchi huduma karibu, maabara ilianzishwa Mwanza kwa ajili ya Kanda ya Ziwa. Afya ya Mama na Mtoto 296. Huduma za uzazi, mama na mtoto ziliendelea kutolewa bila malipo Mwaka 2004. Serikali ilianzisha mafunzo maalum ya stashahada ya juu ya fani ya ukunga na programu za kutoa huduma bora za uzazi. Aidha, mafunzo yalitolewa kwa wakufunzi 175 kuhusu Mikakati ya Kutibu Magonjwa ya Watoto kwa Uwiano. Wakunga wa jadi 112 kutoka maeneo ambayo hayana vituo vya kutolea huduma walipatiwa mafunzo ya huduma ya uzazi salama. Chakula na Lishe 297. Mwaka 2004, huduma za lishe ikiwa ni pamoja na utoaji wa matone ya vitamini A kwa wototo chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito, elimu kuhusu utunzaji na utumiaji wa vyakula vyenye vitamini A ziliendelea kutolewa. Vile vile, elimu ilitolewa kuhusu uboreshaji wa njia za asili za kuhifadhi mboga na matunda bila kupoteza vitamini A. Wazalishaji chumvi wakubwa na wadogo waliwezeshwa kwa kupatiwa vifaa, madini joto na mafunzo. Aidha, mashine za kupima madini chuma mwilini ziliwekwa kwenye baadhi ya hospitali. Mfuko wa Afya ya Jamii 298. Hadi mwishoni mwa mwaka 2004, Mfuko wa Afya ya Jamii uliendelea kutekelezwa katika wilaya 42 na nyingine 50 zilikuwa zinafanya taratibu za uanzishaji wa Mfuko huo. Mfuko huo uliwezesha kutatua tatizo la baadhi ya dawa na vifaa vya tiba katika vituo vya kutolea huduma. Vile vile, wananchi walipewa madaraka ya kusimamia na kutoa maamuzi juu ya matumizi ya Mfuko. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya 299. Mwaka 2004, Mfuko wa Bima ya Afya ambao unahusisha watumishi wa umma kuchangia matibabu yao na ya wategemezi wao kabla ya kuugua uliendelea kukua. Idadi ya wanachama wa Mfuko iliongezeka kutoka 242,508 mwaka 2003 hadi 248,343 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 2.4. Aidha, Mfuko ulikuwa na vituo 3,877 vya kuhudumia wateja vilivyosajiliwa mwaka 2004, ikilinganishwa na 3,551 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 15.5. Pia, Mfuko uliwaelimisha watoa huduma 47,643 kuhusu huduma bora kwa wanachama na pia wadau wa Mfuko walielimishwa kuhusu haki na wajibu wao. Vituo vya Kutolea Tiba 300. Mwaka 2003/04, zilijengwa zahanati 175 na vituo vya afya 25 kufikia jumla zahanati 3,037 na vituo vya afya 347. Vituo hivi vya kutoa huduma ya afya, vilijengwa na serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na vinaendelea kupatiwa dawa na serikali. Kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kutolea huduma ya afya kumesababisha kuongezeka kwa mahitaji ya dawa kwa asilimia 25, na gharama za vifaa vya matibabu kwa asilimia 30, ikilinganishwa na mwaka 2002/03. Pia, serikali iliongeza ruzuku kwa kitanda kwa hospitali za mashirika kutoka sh. 15,000 mwaka 2003/04 hadi sh. 30,000 mwaka 2004/05. Mafunzo ya Afya 301. Mwaka 2004, mafunzo ya kuimarisha Halmashauri za Wilaya kuzipa uwezo wa kupanga na kusimamia uendeshaji na utoaji huduma za afya yalitolewa kwa halmashauri 114. Kanda sita za mafunzo ziliimarishwa na kuboreshwa ili kutoa na kuratibu mafunzo mbalimbali katika ngazi za mikoa, wilaya na vijiji. Aidha, majengo ya vyuo 43 yalifanyiwa ukarabati na kupatiwa vitendea kazi. Wakunga na waganga Vijijini waliopo kazini waliendelezwa katika ngazi za Tabibu na Wauguzi wa Afya ya Jamii ili wawe na ujuzi unaokidhi mahitaji ya wateja. Jedwali Na.84(VYOMBO VYA AFYA NCHINI) Jedwali Na.85(WALIOFAULU MAFUNZO) Jedwali Na.86(MATUMIZI YA VYOMBO VYA AFYA) Jedwali Na.87(IDADI YA WATAALAM WA AFYA ) Jedwali
Na.87A(IDADI YA VITANDA KATIKA HOSPITALI ZOTE NCHINI - 2004) |
|||||||||||||