MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI
   

Kilimo
Maliasili na Utalii
Madini
Viwanda na Biashara
Ujenzi wa Maendeleo ya Ardhi
Mawasiliano na Uchukuzi
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Nishati
Maji
Elimu na Mafunzo
Afya
Maendeleo ya Jamii

         
ELIMU NA MAFUNZO
Utangulizi

276. Katika mwaka 2004, Serikali iliendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya dini na watu binafsi katika utoaji wa elimu ya awali, msingi, sekondari, ualimu, na elimu ya juu. Kwa upande wa taasisi za umma, Serikali iliendelea kuimarisha ubora wa elimu kwa kutoa vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia; kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia; na kukarabati na kujenga madarasa mapya. Serikali iliendelea kutoa mafunzo kwa walimu ambao hawajahitimu, kuongeza uwezo kwa wale walioko kazini, na kuajiri walimu wapya ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM). Pia, Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) kwa kipindi cha 2004 – 2009 kwa lengo la kupanua na kuboresha utoaji wa elimu bora ya sekondari ili wanafunzi wengi watakaomaliza elimu ya msingi waweze kujiunga na elimu hiyo. Kamati za shule mbalimbali ziliendelea kuimarishwa kwa kuzishirikisha katika warsha za utawala, usimamizi wa fedha na vifaa na uandaaji wa mipango ya shule.

277. Serikali pia iliendelea kuongeza nafasi za masomo katika taasisi za elimu ya juu na ufundi, sambamba na kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike katika programu za sayansi na ufundi, na pia kuongeza uwiano wa wanafunzi wa kike katika taasisi hizo.

Elimu ya Awali

278. Katika mwaka 2004, Serikali iliendelea na mkakati wake wa kuwa na darasa la awali katika kila shule ya msingi ya Serikali na kuwashirikisha wadau na wabia wa elimu nchini katika kuanzisha shule za awali. Idadi ya shule za awali zilizosajiliwa zilikuwa 9,868, kati ya hizo 9,701 zilikuwa za Serikali na 167 zisizo za Serikali. Aidha, kulikuwa na jumla ya wanafunzi 554,635 ambapo 547,343 walikuwa katika shule za awali za Serikali na wanafunzi 7,292 katika shule za awali zisizokuwa za serikali. Kwa ujumla, wanafunzi wavulana walikuwa asilimia 50.4 na wasichana asilimia 49.6

279. Katika mwaka 2004, kiwango cha jumla kitaifa katika uandikishaji wanafunzi (GER) katika shule za awali kilikuwa asilimia 24.7 na kiwango halisi (NER) kilikuwa asilimia 23.7.

Elimu ya Msingi

280. Mwaka 2004 ulikuwa ni mwaka wa tatu wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) na mafanikio yameendelea kuonekana. Idadi ya shule za msingi iliongezeka kutoka 12,815 mwaka 2003 hadi kufikia 13,689 mwaka 2004. Pia, idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 6,562,772 mwaka 2003 hadi 7,083,063 mwaka 2004, kati yao wanafunzi 7,041,829 walikuwa katika shule za Serikali na 41,234 shule zisizokuwa za Serikali. Aidha, kati yao, wasichana walikuwa asilimia 49.9 na wavulana asilimia 50.1.

281. Katika mwaka 2004, kiwango cha jumla cha uandikishaji (GER) kitaifa kiliongezeka kutoka asilimia 105.3 mwaka 2003 hadi asilimia 106.3 mwaka 2004. Kiwango halisi cha uandikishaji (NER) kiliongezeka kutoka asilimia 88.5 mwaka 2003 hadi asilimia 90.5 mwaka 2004. Hata hivyo, viwango hivyo kimkoa vimetofautiana sana. Mkoa wa Mara unaongoza kwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha jumla ya uandikishaji (GER), yaani asilimia 126.4 na mkoa wenye kiwango cha chini zaidi ni Tabora wenye asilimia 79. Kwa upande wa viwango halisi vya uandikishaji, mikoa ya Mwanza na Mara imefikia lengo la asilimia 100, yaani watoto wote wenye umri wa kwenda shule katika mwaka 2004 waliandikishwa. Aidha, mkoa wa Tabora umekuwa na kiwango kidogo zaidi cha uandikishaji halisi, yaani asilimia 70.3.

Chanzo: Wizara ya Elimu na Utamaduni

 282. Hali ya viwango vya wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari (Kidato cha I) bado ni chini ya theluthi moja ya wanafunzi wote wanaofanya mitihani ya darasa la saba kwa mikoa yote ya Tanzania Bara. Wastani kitaifa ni asilimia 20 tu ndio wanaochaguliwa kujiunga katika shule za sekondari za Serikali. Mlinganisho kimkoa unaonyesha kwamba mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na kiwango cha juu zaidi, yaani asilimia 31.3 na Shinyanga ulikuwa na kiwango cha chini zaidi yaani asilimia 10.6.

283. Katika mwaka 2004, ujenzi ulifanyika wa madarasa 13,600; ofisi za walimu 498; nyumba za walimu 6,425; na vyoo vya shimo 11,780 na walimu wapya 6,888 waliajiriwa ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Walimu katika shule za msingi waliongezeka kutoka 114,660 mwaka 2003 hadi walimu 121,548 mwaka 2004, ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.

284. Wastani wa uwiano kati ya mwalimu na wanafunzi ulikuwa 1:58 mwaka 2004 ikilinganishwa na 1:57 mwaka 2003, ikiwa ni juu ya kiwango cha kimataifa cha 1:45. Uwiano kimkoa unaonyesha kwamba mkoa wa Kigoma ulikuwa 1:74, na Mwanza na Shinyanga ulikuwa 1:70 kila moja. Mikoa iliyokuwa na uwiano wa chini ni Dar es Salaam 1:48 na Kilimanjaro 1:43.

Elimu ya Sekondari

285. Katika mwaka 2004 kulikuwa na shule za sekondari 1,291 ambapo 828 zilikuwa za Serikali na 463 zisizokuwa za Serikali, kutoka shule 1,083 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 19.2. Idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne ilikuwa ni 248,963 katika shule za Serikali na 152,635 katika shule zisizokuwa za Serikali. Idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne iliongezeka kutoka 319,487 mwaka 2003 hadi 401,598 mwaka 2004, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.7. Aidha, uwiano wa wanafunzi wavulana kwa wasichana wa kidato cha kwanza hadi cha nne ulikuwa asilimia 52.9 kwa wavulana na asilimia 47.1 kwa wasichana.

286. Idadi ya wanafunzi wa kidato cha tano hadi cha sita iliongezeka kutoka 25,954 mwaka 2003 hadi 31,001 mwaka 2004. Uwiano wa wavulana kwa wasichana kwa wanafunzi wa kidato cha tano hadi cha sita ulikuwa asilimia 65.3 kwa wavulana na asilimia 34.7 kwa wasichana.

287. Katika mwaka 2004, kulikuwa na walimu 18,754, kati yao 11,320 walikuwa katika shule za Serikali na walimu 7,434 walikuwa shule zisizokuwa za Serikali. Hili ni ongezeko la asilimia 14.4 kutoka walimu 16,399 mwaka 2003. Aidha, uwiano kati ya walimu na wanafunzi kwa kidato cha kwanza hadi cha sita uliongezeka kutoka 1:20 mwaka 2003 hadi 1:23 mwaka 2004 kwa shule za sekondari za Serikali na kutoka 1:22 mwaka 2003 hadi 1:23 mwaka 2004 kwa shule zisizokuwa za Serikali.

Mafunzo ya Walimu

288. Katika mwaka 2004, idadi ya vyuo vya ualimu ilikuwa 45 ambapo 34 vilikuwa vya serikali na 11 visivyokuwa vya Serikali. Idadi ya walimu–wanafunzi daraja IIIA katika vyuo vya ualimu ilikuwa 24,873 katika vyuo vya Serikali na 1,248 katika vyuo visivyokuwa vya Serikali. Kati ya hawa, wanafunzi wanaume walikuwa 13,181 na wanawake 12,940. Uwiano kati ya walimu – wanafunzi wa kiume na kike ulikuwa asilimia 50.7 kwa wanaume na asilimia 49.3 kwa wanawake kwa vyuo vya ualimu vya Serikali na asilimia 46.2 kwa wanaume na asilimia 53.8 kwa wanawake katika vyuo visivyokuwa vya Serikali.

289. Kwa upande wa stashahada kulikuwa na walimu–wanafunzi 5,548, kati yao 5,079 walikuwa katika vyuo vya Serikali na 469 walikuwa katika vyuo visivyokuwa vya Serikali. Kati yao, idadi ya walimu–wanafunzi wa kiume walikuwa 3,389 na wa kike 2,159. Aidha, katika jitihada za kuongeza uwezo wa walimu, Serikali iliendelea kuendesha mafunzo ya kuinua viwango vya elimu vya walimu wa Daraja B na C kuwa Daraja la IIIA na pia iliendelea kulipia mafunzo ya wakufunzi na walimu waliojiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mwaka 2004.

Ufundi na Elimu ya Juu

290. Katika mwaka 2004, idadi ya wanafunzi katika vyuo vya ufundi vya umma imepungua kutoka wanafunzi 2,292 mwaka 2003 na kufikia wanafunzi 2,103, ikiwa ni sawa na upungufu wa asilimia 8.2. Hata hivyo, idadi ya wanafunzi wa kike wanaosoma ufundi imeongezeka kutoka 202 mwaka 2003 na kufikia 232 kwa mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 14.9.

291. Katika vyuo vikuu vya umma, idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 18,840 mwaka 2003 hadi kufikia 26,475 mwaka 2004, ikiwa ni ongezeko la asilimia 40.5. Idadi ya wanafunzi wa kike iliongezeka kutoka 5,126 mwaka 2003 hadi 7,213 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 41. Mwaka 2004, uwiano wa wanafunzi wa kike uliendelea kuwa Asilimia 27.2 ya wanafunzi wote kama ilivyokuwa mwaka 2003. Sababu zilizochangia ongezeko la wanafunzi katika taasisi za umma za elimu ya juu ni pamoja na: kuendelea kuboreshwa kwa miundombinu ili kuweka mazingira mazuri ya kusomea, mfano, vyumba vya mihadhara viliongezeka katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; kuanza kutumika kwa teknolojia ya kisasa katika kufundishia; na kuongezeka kwa wahadhiri wenye sifa, kwa mfano, kufikia mwaka 2003/04 Chuo Kikuu kishiriki cha Ardhi na Usanifu Majengo (UCLAS), kilikuwa na wahadhiri 34 wenye shahada za falsafa.

292. Mwaka 2004, kulikuwa na jumla ya taasisi 14 za elimu ya juu zisizo za serikali, kati ya hizo, 7 zilikuwa na hadhi ya chuo kikuu, na 7 zilikuwa na hadhi ya vyuo vikuu vishiriki. Idadi ya wanafunzi katika vyuo hivyo ilikuwa 2,543, kati yao, asilimia 37 walikuwa wa kike. Idadi ya wahadhiri katika vyuo hivyo ilikuwa ni 366, ikilinganishwa na 317 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 15.5

Jedwali Na.80(SHULE ZA SEKONDARI ZA SERIKALI: IDADI YA WANAFUNZI KWA KIDATO)

Jedwali Na.81(SHULE ZA SEKONDARI ZA BINAFSI: IDADI YA WANAFUNZI KWA KIDATO)

Jedwali Na.82(WANAFUNZI WATANZANIA KATIKA VYUO VIKUU VYA DAR ES SALAAM, SOKOINE NA CHUO KIKUU HURIA)

Jedwali Na.83(MUHTASARI WA TAKWIMU ZA ELIMU)

 
Back Top