MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI
 

Kilimo
Maliasili na Utalii
Madini
Viwanda na Biashara
Ujenzi wa Maendeleo ya Ardhi
Mawasiliano na Uchukuzi
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Nishati
Maji
Elimu na Mafunzo
Afya
Maendeleo ya Jamii

       
MAENDELEO YA JAMII
 

Elimu na Mafunzo

302. Katika mwaka 2004, vyuo vya maendeleo ya jamii viliendesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi ili kujenga uwezo wa wananchi kutambaua, kuamua, kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo. Mafunzo ya muda mfupi yalitolewa kwa wananchi 14,872 ambapo wanaume walikuwa 8,005 na wanawake 6,872. Mafunzo ya muda mrefu yalitolewa kwa wananchi 4,479, kati yao, wanawake walikuwa 1,334 na wanaume 2,745. Pia, mafunzo yalitolewa nje ya vyuo kwa wananchi 3,778 wakiwemo wanawake 1,779 na wanaume 1,999. Aidha, katika jitihada za kuwapunguzia wananchi mzigo wa kazi, “Kitita cha Teknolojia” ni kitabu kinachoonyesha aina na idadi ya Teknolojia zinazopatikana nchini kilichapishwa na nakala 8,000 zilisambazwa mwaka 2004.

Maendeleo ya Wanawake

303. Utoaji wa mikopo kwa wanawake ili kuwaimarisha kiuchumi uliendelea mwaka 2004 kwa kila wilaya kupewa sh 4.0 milioni za kukopesha wanawake kikiwa ni kiwango sawa na kilichokuwa kinatengwa na serikali miaka ya nyuma. Mgao wa mikopo hii hulingana na maombi yaliowasilishwa katika kamati za wilaya. Kwa jumla viwango vya mikopo inayotolewa huanzia sh. 50,000 hadi sh 500,000. Katika kuwawezesha wanawake kupanua uelewa wao kibiashara, wanawake 130 walishiriki maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa kuwezeshwa na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote. Pia, vikundi vya wanawake vilishiriki maonyesho ya Biashara Gaborone, Botswana ambapo kikundi cha Qualicloth Ltd. kilishinda tuzo kwa bidhaa zinazotokana na vitambaa (mavazi, vikoi na batiki).

Maendeleo ya Watoto

304. Taarifa ya utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Mtoto ilikamilika Agosti 2004 na kuwasilishwa Umoja wa Mataifa Geneva Septemba 2004. Taarifa hii ni ya pili kuandaliwa na serikali na inahusu utekelezaji wa kipindi cha mwaka 1998 – 2003. Msingi wa Mkataba huu ni kutobagua mtoto; mahitaji ya mtoto; haki ya kuishi na maendeleo ya mtoto; na kuheshimu mawazo ya mtoto. Baadhi ya mambo yaliokwisha tekelezwa chini ya mkataba huu ni kutungwa kwa Sheria ya Ajira na Kazi ya mwaka 2004; kuandaliwa kwa sheria moja inayozingatia masuala ya mtoto, yanayofafanua mtoto ni nani, kumkinga mtoto dhidi ya kunyanyaswa, kupuuuzwa na kunyimwa haki; na kuifanyia marekebisho Sheria ya Urithi na Ndoa ya mwaka 1971 ili kuhakikisha haki za mtoto zinazingatiwa. Aidha, Programu ya Elimu ya Idadi ya Watu na maisha ya familia imekamilika na masuala ya watoto yameingizwa katika mwongozo wa Bajeti.

Maendeleo ya Vijana

305. Mwaka 2004, jumla ya sh. 400,000,000 zilitengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana, ikilinganishwa na Sh. 370,000,000 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 8.1. Aidha, serikali iliweka utaratibu wa kuwa, Halmashauri itakayo rejesha kiwango cha mkopo cha sh. 3,089,756 ambacho ilipewa mwaka 2003 kwa asilimia 100, itapewa mara mbili ya kiwango hicho. Utaratibu huu uliwekwa kutokana na Halmashauri nyingi kutorejesha kiwango walichopewa kwa muda uliopangwa. Halmashauri ambazo ziliweza kurejesha kwa asilimia 100 na kupewa sh. 6,179,512 kila moja ni Geita, Kwimba, na Manispaa ya Arusha.

 
Back Top