MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI
 

Kilimo
Maliasili na Utalii
Madini
Viwanda na Biashara
Ujenzi wa Maendeleo ya Ardhi
Mawasiliano na Uchukuzi
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Nishati
Maji
Elimu na Mafunzo
Afya
Maendeleo ya Jamii

         
NISHATI
 

Mfumo wa Nishati

265. Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa asilimia 90 ya matumizi ya nishati nchini imetokana na tungamotaka (biomas), asilimia 8.0 hutokana na petroli, asilimia 1.2 hutokana na umeme. Vyanzo vingine vya nishati ikiwa ni pamoja na makaa ya mawe, mionzi ya jua na upepo huchangia pungufu ya asilimia 1.0. Tathmini inaonyesha kuwa Tanzania ina rasilimali kubwa ya vyanzo vya nishati ya umeme, gesi asilia, tungamotoka, makaa ya mawe na nishati inayojadidika. Hata hivyo, vyanzo vingi vya nishati bado havijaendelezwa kutokana na ukosefu wa mitaji na teknolojia ya kisasa. Aidha, juhudi na mikakati ya kuendeleza vyanzo hivi vya nishati ya gesi asilia, makaa ya mawe, umeme upatikanao kwa nguvu za maji na utafutaji mafuta ziliendelea mwaka 2004.

Umeme

266. Ukuaji wa sekta ya umeme ulipungua kutoka asilimia 5.0 mwaka 2003 hadi asilimia 4.9 mwaka 2004. Mchango wa sekta hii katika Pato la Taifa kwa mwaka 2004 uliendelea kuwa asilimia 1.4 sawa na mwaka 2003. Katika mwaka 2004, jumla ya umeme uliozalishwa ulikuwa ni saa za Gigawati 2,126.4 ikilinganishwa na saa za Gigawati 2,661.7 zilizozalishwa mwaka 2003, sawa na upungufu wa asilimia 20.1. Upungufu huo ulitokana na kuendelea kwa ukame ulioathiri uzalishaji wa umeme unaotokana na nguvu za maji.

267. Mwaka 2004, Gridi ya Taifa ilikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 518.6. Jumla ya umeme wa saa za Gigawati 2,046.4 ulizalishwa mwaka 2004, ikilinganishwa na umeme wa saa za Gigawati 2,585.1 uliozalishwa mwaka 2003, sawa na upungufu wa asilimia 20.9. Aidha, uwezo uliowekezwa wa kuzalisha umeme katika mifumo inayojitegemea ulikuwa Megawati 26.1. Kadhalika, katika mwaka 2004, umeme uliozalishwa na vituo mbalimbali vya mfumo wa kujitegemea uliongezeka na kufikia saa za Gigawati 79.8 ikilinganishwa na saa za Gigawati 76.6, zilizozalishwa mwaka 2003; sawa na ongezeko la asilimia 4.2.

268. Uwezo uliowekezwa kwa IPTL ni Megawati 100 na Kampuni ya Makaa ya Mawe ya Kiwira Megawati 4. Umeme unaonunuliwa kutoka Uganda ni Megawati 8 na kutoka Zambia megawati 5.

269. Mauzo ya umeme kwa matumizi ya viwanda na biashara yaliongezeka kutoka saa za Gigawati 1,190.0 mwaka 2003 hadi kufikia saa za Gigawati 1,232.3 mwaka 2004. Mauzo ya umeme kwa matumizi ya nyumbani yaliongezeka kutoka saa za Gigawati 1,058 mwaka 2003 hadi kufikia saa za Gigawati 1,162.7 mwaka 2004. Umeme uliopotea njiani uliongezeka hadi kufikia saa za Gigawati 841.2 mwaka 2004 kutoka saa za Gigawati 792.0 mwaka 2003. Kiasi cha umeme kilichouzwa Zanzibar kiliongezeka kutoka saa za Gigawati 145 mwaka 2003 hadi kufikia saa za Gigawati 160.9 mwaka 2004.

Petroli

270. Mwaka 2004, bei ya mafuta katika soko la dunia iliendelea kupanda na kufikia wastani wa dola 38 kwa pipa kutoka wastani wa dola 29 mwaka 2003. Bei ya rejareja ya mafuta nchini kwenye vituo mbalimbali mwaka 2004 ilikuwa wastani wa sh. 910 kwa lita ya petroli, sh. 835 kwa lita ya dizeli na sh. 700 kwa lita ya mafuta ya taa ikilinganishwa na sh. 672, sh. 639 na sh. 505 mwaka 2003, kwa mtiririko huo. Pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, ongezeko hilo la bei ya petroli lilisababishwa na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na bima kwa makampuni ya meli. Aidha, matumizi ya mafuta yatokanayo na petroli yaliongezeka kufikia tani za meta za ujazo 1.45 milioni mwaka 2004 ikilinganishwa na tani za meta za ujazo 1.35 milioni mwaka 2003. .

Jedwali Na.74(UWEZO WA MITAMBO YA UMEME NA KIASI CHA UMEME ULIOTENGENEZWA KWA VITUO)

Jedwali Na.75(MAUZO YA UMEME KWA WATUMIAJI MBALIMBALI)

Jedwali Na.76(MAUZO YA UMEME KWA MIKOA (GWH))

 
Back Top