MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI

Uendelezaji wa Sekta Binafsi
Masuala Maalum Yanayohusu Sekta Zote
Maendeleo ya Juhudi za Kupambana na Umasikini

   
MASUALA MAALUM YANAYOHUSU SEKTA ZOTE
UTAWALA BORA

145. Mwaka 2004, utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia unaonyesha kuwa, Tanzania ni nchi bora barani Afrika katika maendeleo ya utawala bora kati ya mwaka 1996 na 2004. Tanzania ni nchi pekee Afrika iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo katika viashirio vitatu vya utawala bora ambavyo ni sauti ya uwajibikaji ambacho kinapima haki za kisiasa, kiraia na kibinadamu; utendaji wa serikali inayopima ubora wa urasimu na utoaji huduma za jamii na udhibiti wa rushwa ambao ni uwezo wa serikali kutokomeza rushwa katika ngazi zote. Utafiti huu ulijumuisha vipimo 352 vya utawala bora kutoka vyanzo 32 vya utafiti wa miaka miwili (2003 na 2004) uliofanywa na asasi 30 za kimataifa kwa kusaili watu binafsi na taasisi mbalimbali katika nchi husika 209, na kati ya hizo, 47 zikiwa za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

146. Mwaka 2004, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika utoaji huduma kwa jamii. Maeneo yaliyohusika ni pamoja na kuimarisha utoaji haki sawa kwa wote, mfumo wa kurekebisha kanuni na sheria, upatikanaji wa taarifa kwa wakati kwa ajili ya uandaaji wa sera, mipango na mikakati ya kusimamia uchumi; na kampeni ya kupunguza rushwa chini ya Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa.

147. Serikali iliweka mkazo katika kuharakisha na kuongeza kasi ya kuendesha kesi mahakamani, kuboresha uwezo wa watendaji na kuinua kiwango cha utendaji kazi kwa watumishi wa idara ya sheria na mahakama. Juhudi zilifanyika katika kuwahamasisha wananchi wa ngazi zote juu ya haki za binadamu. Pia, tafiti zilifanyika kuhusu sheria mbalimbali kwa lengo la kuendeleza haki za binadamu, utawala bora na kuelewa mambo ya Katiba, shughuli za Kabidhi Wasii Mkuu, na kuboresha mazingira ya kazi na mafunzo.

148. Hadi mwaka 2004, Tume ya Haki za Binadamu ilishughulikia malalamiko 8,750 na kati ya hayo, malalamiko 3,212 yalikamilishwa. Katika kipindi cha mwaka 2003/04, malalamiko 2,458 yalipokelewa ikilinganishwa na 2,883 mwaka 2002/03. Tume hii ilisambaza vipeperushi 50,000 kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma, na ilikutana na viongozi wakuu 18, watendaji katika mikoa 20, na katika wilaya 27. Aidha, magereza 68 na vituo vya polisi 15 vilikaguliwa.

149. Ili kuimarisha vita dhidi ya rushwa serikali ilifanya mabadiliko katika Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKURU) kwa kuiongezea nguvu zaidi za kutafuta, kukamata, kuchunguza na kushitaki. Aidha, bajeti ya taasisi hiyo iliendelea kuongezwa na kufikia sh. 9.0 bilioni mwaka 2004/05, ikilinganishwa na sh. 6.0 bilioni mwaka 2003/04. Hadi mwaka 2004, TAKURU ilipanua wigo wake wa utendaji kwa kufungua ofisi katika ngazi ya mikoa na wilaya. Kwa upande wa mamlaka za Serikali za mitaa, juhudi zilifanyika katika kuandaa mwongozo uliotumika katika kuandaa mpango wa utekelezaji wa Mkakati wa Kupambana na Rushwa kwa kipindi cha mwaka 2005/06.

JINSIA

150. Tathmini ya utekelezaji wa ulingo wa Beijing inaonyesha kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika kuingiza masuala ya jinsia katika Sera, Programu, Mipango na Mikakati mbalimbali ya Taifa. Juhudi hizo zimezaa matunda ya kurekebisha Katiba ya nchi na kuongeza kipengele cha kuongeza uwakilishi wa wanawake kwa njia ya uwiano. Kumekuwa na ongezeko la Wabunge wanawake toka asilimia 17.5 mwaka 1995, hadi kufikia asilimia 22.5 mwaka 2004. Sheria za uchaguzi zimeendelea kurekebishwa ili kuwa na uwakilishi wa wabunge wanawake unaofikia asilimia 30. Vilevile, uwakilishi katika ngazi ya Serikali za Mitaa uliongezeka kutoka asilimia 25 mwaka 1995, hadi asilimia 33.3 mwaka 2004.

151. Mwaka 2004, chini ya Mpango wa Maboresho ya Utumishi wa Umma, serikali iliwafadhili watumishi wa umma wanawake 50 waliogharimiwa sh. 500 milioni katika vyuo mbalimbali hapa nchini, ikilinganishwa na wanawake 20 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 150. Vile vile, makatibu muhtasi 25 wengi wao kutoka ofisi za Makatibu Tawala wa mikoa na wilaya walifadhiliwa kozi ya tarakishi ikilinganishwa na 40 mwaka 2003.

152. Mwaka 2004, wanafunzi wanawake walioandikishwa kidato cha kwanza waliongezeka kutoka asilimia 48.2 mwaka 2003 hadi asilimia 49.5. Vile vile, walioandikishwa kidato cha tano waliongezeka kidogo kutoka asilimia 35.3 mwaka 2003 hadi asilimia 35.4. Aidha, programu maalum ya kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliwawezesha wasichana kufikia kiwango cha asilimia 33 mwaka 2004. Wanafunzi wanawake katika vyuo vya ufundi stadi walikuwa asilimia 24 na wanaume asilimia 76 mwaka 2004.

153. Mwaka 2004, idadi ya Makatibu Tawala wa mikoa wanawake iliongezeka hadi 5 ikilinganishwa na 4 mwaka 2003. Idadi ya wakuu wa wilaya wanawake iliongezeka kutoka 19 mwaka 2003 hadi 23 mwaka 2004. Kulikuwa na ongezeko kubwa la wakurugenzi wa wilaya wanawake kutoka 14 mwaka 2003 hadi 23 mwaka 2004. Pia, kulikuwa na ongezeko la wakurugenzi katika idara za serikali kutoka 29 mwaka 2003 hadi 30 mwaka 2004. Vile vile, idadi ya majaji wanawake ilifikia 7 mwaka 2004 kutoka majaji 6 mwaka 2003.

 Jedwali Na.8.1: Idadi ya wawakilishi katika ngazi ya maamuzi kuanzia 1997 – 2004

Ngazi

Idadi ya Wanawake

Idadiya Wanaume

Jumla

Asilimia wanawake

1997

2003

2004

1997

2003

2004

1997

2003

2004

1997

2003

2004

Mawaziri

3

4

4

24

23

24

27

27

28

11

15

15

Naibu Mawaziri

3

5

5

13

12

12

16

17

17

19

29

29

Wakuu wa Mikoa

1

2

2

19

19

19

20

21

21

5

10

10

Serikali za mitaa/Wakuchaguliwa

-

250

250

-

2287

-

-

2537

2537

-

10

10

Makatibu Tawala wa Wilaya

20

14

14

89

85

85

109

99

99

10

14

14

Makatibu Wakuu wa Wizara

4

6

7

21

19

18

25

25

25

16

24

28

Manaibu Katibu Wakuu wasaidizi

-

-

-

-

7

7

-

7

7

-

0

0

Makamishna

-

2

3

-

16

16

-

18

19

-

11

15

Mabalozi

1

1

1

29

34

34

30

35

35

3

3

3

Majaji Rufaa

-

-

1

-

-

8

-

-

9

-

-

11

Wakazi

-

33

33

-

82

82

-

115

115

0

29

29

Hakimu Wilaya

-

22

22

-

123

123

-

145

145

0

15

15

Hakimu Mwanzo

 

149

149

-

546

546

-

695

695

0

21

21

Chanzo: Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto

Jedwali Na.8.2: Uandikishaji wa wanawake katika sekta ya elimu mwaka 2002-2004 (Asilimia)

Kiwango cha Elimu

2002

2003

2004

Elimu ya msingi

Darasa la I

48.6

48.5

49.1

Darasa la VII

50.7

49.9

49.6

Darasa la I - VII

49.0

48.7

48.8

Elimu ya sekondari

Kidato cha I-IV

45.5

46.6

47.1

Serikali

44.7

44.6

46.0

Binafsi

46.7

40.4

48.9

Kidato cha I-VI

45.5

45.7

46.2

Serikali

44.7

43.9

45.5

Binafsi

46.7

48.2

47.4

Elimu ya Ualimu

Jumla

48.2

50.0

47.7

Serikali

41.7

53.2

34.8

Binafsi

48.3

49.9

48.1

Chanzo: Wizara ya Elimu na Utamadumi

 MAZINGIRA

154. Katika mwaka 2004, serikali iliendelea kuhamasisha asasi zisizo za serikali pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira. Vile vile, maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yalifanyika kitaifa Kigoma tarehe 5 Juni, 2004, ambapo programu mbalimbali za utekelezaji wa hifadhi ya mazingira ziliwasilishwa. Katika utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Upandaji Miti, mwaka 2004, miti 66,483,998 ilipandwa ikilinganishwa na 47,863,257 mwaka 2003, sawa na ongezeko la asilimia 38.9.

155. Katika mwaka 2004, serikali ilipitia miradi 7 ya asasi mbalimbali inayohusu mabadiliko ya hali ya hewa, ambapo baadhi ya miradi ilipewa fedha na kuanza utekelezaji. Serikali ilizifadhili asasi 8 zisizo za serikali na kutoa mafunzo kwa wakulima wa Mkoa wa Dodoma kuhusu njia bora za kupambana na kuenea kwa jangwa. Mpango wa Taifa wa mwaka 1999 unaohusu kuenea kwa jangwa na ukame ulifanyiwa marekebisho. Pia, mpango wa miaka mitano wa kituo kilichoanzishwa nchini cha Itifaki ya Basel kuhusu mafunzo na teknolojia, uliandaliwa.

156. Katika kufanikisha juhudi mbalimbali za kimataifa zinazohusu mazingira, Bunge lilipitisha ‘‘Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004’’. Vile vile, serikali iliendelea kuratibu miradi iliyo chini ya Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF), kwa kuzishauri asasi zisizo za serikali jinsi ya kuandaa miradi inayozingatia vigezo vya GEF. Miradi 20 ilipitishwa na serikali na kuwasilishwa GEF kupitia Shirika la Kimataifa la Mazingira, Benki ya Dunia, na Shirika la Kimataifa la Maendeleo.

157. Serikali iliridhia Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika, na miradi ya utekelezaji wa Mkakati wa Hifadhi ya mazingira ya ziwa na bonde, na mipango ya utekelezaji iliandaliwa. Aidha, Programu ya Hifadhi ya Ziwa Victoria na ukanda wa ziwa hilo iliendelea kutekelezwa.

UKIMWI

158. Utafiti uliofanywa Tanzania Bara na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI katika ngazi ya kaya, katika mwaka 2003/2004, unaonyesha kuwa wastani wa asilimia 7 ya watanzania wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 walikuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Utafiti huo unaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ni kikubwa kwa wanawake kuliko wanaume. Maambukizi ya UKIMWI kwa wanawake yalikuwa asilimia 7.7 ikilinganishwa na asilimia 6.3 kwa wanaume.

159. Asilimia 10.9 ya wakazi wa maeneo ya mijini wanakabiliwa na maambukizi ya UKIMWI, ikilinganishwa na asilimia 5.3 ya wakazi wa maeneo ya vijijini. Aidha, hali ya maambukizi ilikuwa inatofautiana baina ya mikoa. Mikoa ya Mbeya, Iringa na Dar es Salaam ilikuwa na viwango vya juu karibu mara mbili ya wastani wa watanzania wote wenye umri wa miaka 15 - 49. Mbeya ilikuwa na kiwango cha maambukizi cha asilimia 14, Iringa asilimia 13 na Dar es Salaam asilimia 11. Mikoa ambayo ilikuwa na kiwango cha chini cha maambukizi ni Manyara na Kigoma cha asilimia 2.

Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu

 

160. Katika kuboresha huduma ya tiba kwa wagonjwa wa UKIMWI majumbani, watoa huduma 814 walipata mafunzo na vifaa. Huduma hii hutolewa kwa kushirikiana na jamii na ndugu za wagonjwa kama sehemu ya tiba na matunzo kwa wagonjwa wa UKIMWI. Katika mwaka 2004, idadi ya vituo vya ushauri nasaha na kupima viliongezeka kutoka vituo 332 mwaka 2003 hadi 521. Hali hii ilichangia kuongezeka kwa idadi ya watu waliohudhuria katika vituo hivyo kutoka watu 139,972 mwaka 2003 hadi 227,972, sawa na ongezeko la asilimia 62.9. Vile vile, mafunzo kuhusu ushauri nasaha yalitolewa kwa watumishi wa afya 165 na kufanya idadi ya wataalam wa ushauri nasaha kufikia 12,000.

161. Katika mwaka 2004/05, wizara zote zilitengewa fedha katika Mpango wa Matumizi ya Serikali wa Muda wa Kati kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kudhibiti UKIMWI. Hii ni pamoja na kufanya tathmini ya athari za UKIMWI katika sekta husika, kuandaa mkakati wa kisekta wa kudhibiti UKIMWI, kuainisha udhibiti wa UKIMWI katika mipango ya wizara na kuwa na mpango shirikishi na endelevu ya kudhibiti UKIMWI sehemu za kazi. Aidha, Kamati shirikishi ziliundwa katika mamlaka za serikali za mitaa katika ngazi za halmashauri, kata, kijiji, mtaa na kitongoji ili kupanga na kutekeleza mipango ya kudhibiti UKIMWI kulingana na mazingira yao.

162. Katika mwaka 2004, serikali ilitekeleza mpango wa kuwapatia bure dawa za kurefusha maisha watu waishio na virusi vya UKIMWI. Vituo vya afya 32 katika mikoa 12 vilitoa huduma hiyo. Wataalamu 492 kutoka vituo 96 vya kutolea huduma za afya walipata mafunzo ya kutoa huduma ya utoaji wa dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa UKIMWI. Aidha, mashine 20 za “Facs count” zinazopima viwango vya chembechembe za “CD4” zilinunuliwa na kusambazwa katika hospitali zote za rufaa na baadhi ya hospitali za mikoa.

UTANDAWAZI WENYE HAKI

163. Teknolojia mpya ikisaidiwa na sera zilizo wazi imeunda dunia iliyounganishwa zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Hii imeanzisha mfumo wenye mabadiliko makubwa na ya haraka ambayo yanagusa kila taifa na kila mtu. Utandawazi umepanua wigo, siyo tu katika kupanuka kwa kutegemeana kiuchumi katika nyanja za biashara, uwekezaji rasilimali, fedha na kuzatiti mfumo wa uzalishaji mali kimataifa, bali pia mwingiliano wa kijamii na kisiasa miongoni mwa mashirika na watu binafsi duniani kote.

164. Mfumo wa sasa wa utandawazi unatoa matokeo yasiyo na uwiano sawa ndani ya nchi na kati ya nchi na nchi, hivyo, Tume ya Kimataifa kuhusu Masuala ya Kijamii katika Utandawazi iliundwa mwaka 2001 kutokana na uamuzi wa Baraza la Uongozi la Shirika la Kazi Duniani. Tume hiyo iliandaa taarifa maalum na shawishi kuhusu utandawazi katika nyanja za kijamii pamoja na mahusiano kati ya uchumi wa dunia na ulimwengu wa kazi. Mnamo Juni 2004, Tume iliwasilisha taarifa yake katika vikao mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kikao maalumu cha Shirika la Kazi Duniani huko Geneva, Uswisi. Taarifa hii ilijadiliwa katika vikao mbalimbali vya kimataifa ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, Umoja wa Afrika, na Umoja wa Mataifa. Tanzania na Burkina Faso ziliteuliwa kutekeleza mapendekezo ya Tume kwa majaribio na uzoefu utakaopatikana katika nchi hizi mbili utatumika kutekeleza mapendekezo ya Tume katika nchi nyingine.

165. Katika mwaka 2004, serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Utandawazi iliyojumuisha sekta mbalimbali, asasi na taasisi za elimu ya juu na zile za utafiti ili kuanza kutekeleza mapendekezo ya Tume. Kamati hii ilichambua mapendekezo ya Tume na kuandaa mpango wa utekelezaji wa muda wa kati na mrefu. Mpango huu unaendelea kujadiliwa na serikali pamoja na Shirika la Kazi Duniani. Aidha, Kamati hii ilitafsiri kwa lugha ya Kiswahili muhtasari wa taarifa ya Tume ili iweze kueleweka vizuri kwa walengwa wengi.

   
Back Top