MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI

Uendelezaji wa Sekta Binafsi
Masuala Maalum Yanayohusu Sekta Zote

Maendeleo ya Juhudi za Kupambana na Umasikini

     
    UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI    
UWEKEZAJI

Uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC)

132. Katika mwaka 2004, Kituo cha Uwekezaji Rasilimali Tanzania, kiliendelea kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza na kushiriki katika juhudi za serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. Kituo kilishiriki kikamilifu katika Programu ya Uimarishaji wa Mazingira ya Biashara Tanzania, na katika midahalo baina ya sekta za umma na binafsi inayosimamiwa na Baraza la Biashara la Taifa.

133. Katika mwaka 2004, Kituo kiliwahudumia wawekezaji kwa idadi ifuatavyo: masuala ya TRA, 1405; uandikishaji wa makampuni, 174; na leseni za biashara, 278; ikilinganishwa na 272, 196, na 218 mwaka 2003, kwa mtiririko huo. Vibali 1,845 vya kufanya kazi nchini vya daraja B vilitolewa ikilinganishwa na 473 vilivyotolewa mwaka 2003. Maombi 1,951 ya kufanya kazi nchini yalipokelewa na kupitishwa na Wizara ya Kazi mwaka 2004 ikilinganishwa na maombi 1,298 mwaka 2003.

134. Kituo kiliidhinisha miradi 454 yenye thamani ya sh. 1,246,040 milioni iliyotarajiwa kutoa nafasi za ajira 56,057 mwaka 2004, ikilinganishwa na miradi 272 yenye thamani ya sh. 1,6694,000 milioni na nafasi za ajira 198,458 mwaka 2003. Kupungua kwa ajira katika mwaka 2004 kulichangiwa na makampuni mengi kuajiri wafanyakazi wachache kutokana na kuwepo na miradi inayotumia teknolojia ya kisasa zaidi kuliko nguvu kazi. Miradi 269 kati ya hiyo ilikuwa mipya, ambapo miradi 185 ilikuwa ya ukarabati na upanuzi wa shughuli zilizopo. Mchanganuo wa umiliki wa miradi unaonyesha kuwa 208 ilikuwa ya wawekezaji wa ndani, 119 ya wawekezaji wa nje na 127 ya ubia. Sekta ya viwanda ilivutia wawekezaji wengi zaidi, ikiwa na miradi 151. Sekta nyingine zilizovutia wawekezaji ni pamoja na utalii miradi 110, ujenzi 57, usafirishaji 49, kilimo na ufugaji 30, uendelezaji wa rasilimali watu 17, maliasili 14, miundo mbinu ya kiuchumi 9, taasisi za fedha 8 na mawasiliano 5. Sekta za nishati na huduma hazikupata wawekezaji. Jedwali Na. 34 linaonyesha miradi kisekta iliyopitishwa na Kituo katika mwaka 2001 – 2004.

135. Mgawanyo wa miradi iliyoandikishwa kimkoa unaonyesha kuwa mkoa wa Dar es Salaam uliongoza kwa kupata miradi 262, ukifuatiwa na Arusha 79. Mikoa mingine iliyopata wawekezaji ni pamoja na Kilimanjaro miradi 21, Mwanza 20 na Tanga 4. Mtwara ilipata miradi 9 wakati Shinyanga miradi 8. Mikoa ya Morogoro, Mbeya na Iringa ilipata miradi 7 kila mmoja; Pwani, Lindi na Mara ilipata miradi 5 kila mmoja; Dodoma, Kigoma na Tabora ilipata miradi 2 kila mmoja; na Kagera, Rukwa na Manyara ilipata mradi 1 kila mmoja, wakati Ruvuma na Singida haikupata mradi wowote. Miradi mingine ina matawi zaidi ya mkoa mmoja.

Uhamasishaji wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi

136. Kituo kilifungua Ofisi ya Kanda ya Kaskazini mjini Moshi Septemba, 2004. Ofisi hii inashirikisha Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida. Vilevile, Kituo kilifanya semina maalum kwa Makatibu Tawala wa Mikoa, kwa madhumuni ya kuwakumbusha umuhimu wa uwekezaji, kuondoa kero wanazokutana nazo wawekezaji na kuwaelekeza maafisa walio chini yao namna ya kutoa huduma kwa wawekezaji. Aidha, Kituo kilifanya semina ya uhamasishaji kwa kundi la vijana mikoa ya Mwanza na Tabora.

137. Kituo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilihamasisha wawekezaji kutoka Botswana. Uhamasishaji huu umewezesha kuvutia kampuni ya GH Group, kuwekeza dola 80 milioni katika mradi wa “Mlimani City”.

Uwekezaji wa Mitaji ya Kigeni ya Moja kwa Moja (FDI)

138. Thamani ya Mitaji ya Kigeni ya Moja kwa Moja iliongezeka hadi dola 260.2 milioni mwaka 2004, ikilinganishwa na dola 247.8 millioni mwaka 2003. Jedwali Na. 7.1 linaonyesha mwenendo wa mitaji ya kigeni ya moja kwa moja katika kipindi cha mwaka 1998 – 2004.

 

Jedwali Na. 7.1: Uwekezaji wa Mitaji ya Kigeni ya M oja kwa M oja, 1998-2004

Mwaka

Thamani ya Mitaji iIiyowekezwa ( Dola Milioni)

1998

172.2

1999

516.7

2000

463.4

2001

327.4

2002

240.4

2 003

247.8

2004

260.2

Chanzo: Benki Kuu ya Tanzania

 
Uboreshaji wa Mazingira ya Uwekezaji

139. Kituo kiliendelea kuwahudumia wawekezaji wa ndani kwa kushirikiana na sekretariati za Mikoa kwa lengo la kupata idadi ya wajasiriamali nchini. Katika zoezi hili wajasiriamali 200 waliorodheshwa kwenye “data bank” ya Kituo kama wajasiriamali endelevu. Kituo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, kilifanya uchambuzi na kupata miradi bora 40. Miradi hiyo iliwekwa kwenye tovuti ya Kituo na kunadiwa kwa wawekezaji wenye teknolojia.

140. Katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini, serikali iliendelea kutekeleza Programu ya Kuimarisha Mazingira Bora ya Biashara Tanzania, inayotekelezwa na Kitengo cha Taratibu Bora za Biashara kilichopo chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji. Kitengo kilishiriki kikamilifu katika kuwezesha marekebisho ya Sheria ya Ardhi na Kanuni zake, Sheria ya Ajira ya mwaka 2004, na Sheria ya Taasisi za Kazi ya Mwaka 2004.

141. Mwaka 2004, Baraza la Taifa la Biashara liliendelea na mpango wake wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa njia ya mashauriano kati ya sekta ya umma na binafsi, kwa lengo la kuongeza mitaji ya ndani na nje na kukuza uchumi. Baraza lilifanya mikutano miwili iliyowajumuisha wajumbe toka serikalini na sekta binafsi, mabalozi na mashirika ya kimataifa. Katika mikutano hii, Baraza lilitoa taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya mikutano ya mwaka 2002 na 2003, ambapo serikali ilitekeleza kwa kiwango kikubwa. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na Kurekebisha Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 kwa kuifanya iwe dhamana ya mikopo; na kupitishwa kwa sheria ya kodi ya mwaka 2004 kwa madhumuni ya kuboresha uwekezaji. Vile vile, sekta binafsi, serikali na wabia kutoka nje wameanzisha mfuko wa kuendeleza rasilimali watu unaojulikana kama ‘Çhief Executive Officers Scholarship Fund’. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mfuko huu itakuwa ya miaka mitano na itagharimu dola 6.3 milioni.

UREKEBISHAJI NA UBINAFSISHAJI WA MASHIRIKA YA UMMA

142. Hadi kufikia Desemba 2004, jumla ya mashirika 312 yalikuwa yamebinafsishwa na mali za mashirika zipatazo 499 kuuzwa, ikilinganishwa na mashirika 295 na mali za mashirika zipatazo 328 mwaka 2003. Katika mwaka 2004, jumla ya mashirika 17 yalibinafsishwa na mali 172 ziliuzwa, ikilinganishwa na mashirika 22 na uuzaji wa mali za mashirika zipatazo 75 mwaka 2003. Mashirika hayo yamebinafsishwa kwa Watanzania na kwa wawekezaji kutoka nje kwa utaratibu wa kuuza hisa, kuuza mali, na kukodisha.

143. Mwaka 2004, juhudi kubwa zilielekezwa katika kukamilisha uundaji wa mamlaka za udhibiti kwa ajili ya mashirika ya miundombinu na huduma, na kufanya marekebisho ya sheria za sekta zinazolengwa kudhibitiwa. Mamlaka zilizoundwa na kuanza kufanya kazi ni Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Mamlaka ya Udhibiti ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), na Mamlaka ya Udhibiti ya Mawasiliano ya Anga (TCAA). Taratibu za kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Tume ya Ushindani wa Haki (FCC) na Mahakama ya Ushindani wa Haki (FCT) hazikukamilika.

144. Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma iliongezewa muda wa utendaji kisheria kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia Januari, 2004. Ubinafsishaji wa NMB, Shirika la Bima la Taifa, Shirika la Ugavi Umeme (TANESCO), Vitengo vilivyosalia vya Mamlaka ya Bandari, mashamba ya NAFCO ya Ruvu na DAKAWA, na viwanda vya korosho vilivyosalia, uliendelea kushughulikiwa. Aidha, taratibu za ukodishaji wa Shirika la Reli (TRC) zinaendelea.

Jedwali Na.34(KITUO CHA UWEKEZAJI TANZANIA (TIC): MIRADI ILIYOPITISHWA)

Back Top