DIBAJI | MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUM KIMAENDELEO|MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI |
||||
Utangulizi Historia ya kutayarisha takwimu za Pato la Taifa Tanzania Bara ilianza mwaka 1954. Toka wakati huo, maboresho yameendelea kufanyika katika njia zinazotumika kutayarisha takwimu hizo. Vigezo muhimu vilivyotumika kutayarisha takwimu za Pato la Taifa kwa miaka ya nyuma, vilizingatia zaidi dhana na mifumo ya takwimu za Pato la Taifa ya Umoja wa Mataifa ya miaka ya 1953, 1968 na 1993. Marekebisho ya kwanza ya takwimu za Pato la Taifa yalifanyika kwa kutumia bei za mwaka 1966, makisio ambayo yalitumia mfumo wa takwimu za Pato la Taifa wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1953. Marekebisho ya pili yalifanyika kwa kutumia bei za mwaka 1976 kwa kutumia mfumo wa takwimu za Pato la Taifa wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1968. Marekebisho ya tatu yalifanyika kwa kutumia bei za mwaka 1992, makisio ambayo yalitumia mfumo wa takwimu za Pato la Taifa wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1968 na kwa kiasi fulani, yalifuata mfumo wa mwaka 1993. Marekebisho ya sasa ya takwimu za Pato la Taifa yametumia bei za mwaka 2001 na mfumo wa takwimu za Pato la Taifa wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1993. Kusudio la kubadilisha mwaka wa kizio na marekebisho ya takwimu za Pato laTaifa Mwaka wa kizio ni ule ambao bei zake zinatumika katika kutayarisha makisio. Kwa mfano, Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2001, hapa mwaka 2001 ndiyo unaoitwa mwaka wa kizio. Sababu za kuchagua mwaka wa kizio kuwa 2001 ni kwa kuwa mwaka huo ulikuwa na takwimu za kutosha toka vyanzo mbalimbali ambazo hazikuwahi kujumuishwa katika mfumo uliopita wa takwimu za Pato la Taifa. Marekebisho ya takwimu za Pato la Taifa yalihusisha kukadiria makisio ya mwaka wa kizio na miaka ya nyuma na ya mbele ya mwaka wa kizio. Marekebisho ya mwaka wa kizio na makisio ya takwimu za Pato la Taifa yalitayarishwa kutokana hasa na sababu zifuatazo: i. Takwimu zilizokuwepo kwa bei za mwaka 1992 zilikuwa zimepitwa na wakati na hazikuwa zikionyesha mabadiliko halisi ya muundo wa uchumi uliokuwa umetokea nchini kwa kipindi hicho; ii. Kujumuisha mabadiliko ya muundo wa uchumi uliojitokeza hususani katika uzalishaji, matumizi na uwekezaji katika uchumi; iii. Kuzingatia mabadiliko ya mahusiano ya bei za bidhaa mbalimbali yaliyojitokeza ndani ya kipindi hicho; iv. Kuboresha orodha ya bidhaa na huduma kadri maendeleo na ubunifu unavyosababisha ongezeko la bidhaa na huduma mpya katika soko wakati ambapo bidhaa na huduma zinazopitwa na wakati hutoweka; v. Kujumuisha taarifa na takwimu zote mpya katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kutokana na tafiti mpya zinazofanyika kama vile tafiti za kaya binafsi; na vi. Kujumuisha mahitaji na maelekezo mapya kulingana na mfumo wa kimataifa wa takwimu za Pato la Taifa wa mwaka 1993. |
||||