DIBAJI | MAENDELEO YA UCHUMI JUMLA | UENDELEZAJI WA SEKTA BINAFSI | SUALA MAALUM KIMAENDELEO| MAENDELEO KATIKA SEKTA MBALIMBALI |
||||
UTEKELEZAJI WA SERA YA KUPELEKA MADARAKA KWA WANANCHI |
||||
Dhana na Chimbuko la Sera ya Kupeleka Madaraka kwa Wananchi 179. Mfumo wa Serikali za Mitaa nchini ulianza kutekelezwa tangu mwaka 1961, ambapo Halmashauri za wilaya na miji zilianzishwa kama njia ya kuharakisha maendeleo. Halmashauri za wilaya na za miji ziliendelea kutekeleza majukumu yao ya kisera katika maeneo yao. Hata hivyo, uhaba wa rasilimali ulisababisha kupungua kwa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu. 180. Mwaka 1972, Halmashauri zilivunjwa na madaraka ya kutekeleza majukumu yao yalibaki katika uangalizi wa Serikali Kuu. Hali hii ilisababisha kupungua na kuzorota zaidi katika utoaji wa huduma za jamii katika ngazi za Serikali za Mitaa, kwani Halmashauri hazikupewa madaraka kamili ya kupanga na kufanya maamuzi ya kisiasa, kiutawala na rasilimali fedha. Aidha, ilikuwa ni vigumu kwa Serikali Kuu kusimamia na hivyo kuonekana umuhimu wa kurejesha Halmashauri za Serikali za Mitaa mwaka 1984. Pamoja na mabadiliko yaliyotokea, mfumo wa utoaji huduma ulibakia kuwa chini ya Serikali Kuu kwani wizara ziliendelea kusimamia rasilimali fedha na watu kwa kutoa maagizo kwa Halmashauri kupitia tawala za mikoa. Hata hivyo, utekelezaji wa majukumu katika ngazi ya Serikali za Mitaa kwa kutegemea maagizo kutoka Serikali Kuu haukuleta matokeo yaliyotarajiwa, yaani utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utoaji huduma kwa ufanisi. 181. Mwaka 1996, Serikali iliamua kuanzisha Mpango wa Maboresho wa Serikali za Mitaa kwa lengo la kuimarisha mfumo wa mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kupitia Sera ya Kupeleka Madaraka kwa Wananchi (Decentralization by Devolution - D by D). Madhumuni ya kupeleka madaraka kwa wananchi ni kutekeleza azma ya Serikali ya kuwashirikisha wananchi katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao wenyewe, na kuoanisha na dhana za uwezeshaji, utawala bora na vita dhidi ya umaskini. Mchakato wa utekelezaji wa Sera hii uko katika maeneo matatu ambayo ni: siasa, utawala na rasilimali fedha. 182. Siasa: Katika eneo hili Sera inalenga kuwapa wananchi au wawakilishi waliowachagua kwa njia ya kidemokrasia, uwezo wa kupanga na kufanya maamuzi ya mambo yanayohusu maendeleo ya kiuchumi na kijamii kulingana na vipaumbele vyao. 183. Utawala: Katika eneo hili, Sera inalenga kuhamisha majukumu ya kutoa huduma kwa jamii kutoka Serikali Kuu na kupeleka Serikali za Mitaa. Hii inajumuisha usimamizi wa watumishi hao kuwa chini ya Serikali za Mitaa ili kuimarisha kiwango cha uwajibikaji kwa wananchi wanaowahudumia. 184. Rasilimali Fedha: Baada ya mchakato wa kuhamisha majukumu katika maeneo ya utawala na siasa, rasilimali fedha, zinahamishwa kulingana na majukumu yaliyoainishwa kupelekwa Serikali za Mitaa. Serikali za Mitaa zimepewa madaraka ya kupanga matumizi ya fedha hizo kulingana na vipaumbele vilivyowekwa kwa kuzingatia mahitaji na mazingira yao. Mchakato wa Kupeleka Madaraka kwa Wananchi 185. Mipango na bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa huandaliwa kwa kuzingatia maamuzi na Sera ya Serikali ya Kupeleka Madaraka kwa Wananchi. Dhana hii imejidhihirisha kufuatia uamuzi uliofanywa na Serikali wa kuhamisha majukumu na rasilimali kutoka katika usimamizi wa wizara husika na kwenda katika ngazi ya Serikali za Mitaa. 186. Katika mwaka 2006 Serikali ilifanya tathmini katika wizara sita kuhusu uzingatiaji wa zoezi la kupeleka madaraka kwa wananchi. Wizara hizo ni: Kilimo, Chakula na Ushirika; Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Afya na Ustawi wa Jamii; Maendeleo ya Miundombinu; Maji na Umwagiliaji; na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambazo ndizo zinazoonekana kuwa na shughuli nyingi zinazoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye suala zima la upelekaji madaraka kwa wananchi. Kufuatia zoezi hilo, mwaka 2007/08 jumla ya sh. 216.2 bilioni zilihamishwa kwenda kwenye Halmashauri kutoka katika kasma za wizara kwa lengo la kugharamia utekelezaji wa shughuli zilizohamishwa. Kiwango cha fedha kilichopelekwa kwenye Halmashauri kiliongezeka kutoka sh. 858.4 bilioni mwaka 2006/07 hadi sh. 1,074.6 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 19.7 la bajeti ya Halmashauri kwa mwaka 2007/08. 187. Kwa upande mwingine, tathmini iliyofanyika ilibaini kuwa katika Wizara ya Miundombinu, baadhi ya shughuli zilihamishiwa kwenye Wakala za Serikali zilizoanzishwa chini ya wizara hiyo. Tathmini ya wakala hizo zitabainisha miradi na shughuli zinazostahili kuhamishiwa kwenye Mikoa na Halmashauri ili zitekelezwe kwa ufanisi zaidi. 188. Halmashauri zimepewa mamlaka ya kusimamia ajira na kuendeleza wafanyakazi kulingana na matakwa ya Halmashauri husika kwa kuzingatia utawala bora. Aidha, Serikali imeweka vigezo vya upimaji wa utawala bora kwenye Halmashauri. Vigezo hivyo ni demokrasia; ushirikishwaji wa jamii; utawala wa sheria; uadilifu wa viongozi na watendaji; uwazi na uwajibikaji; ufanisi katika utendaji; uzingatiaji wa jinsia; utaratibu wa upangaji mipango; stadi za upangaji mipango; na matumizi ya takwimu katika mipango. Aidha, kila Halmashauri ina mamlaka ya kuainisha vyanzo vya mapato na kupanga matumizi kwa njia shirikishi. 189. Mwaka 2008, tathimini nyingine imefanyika ili kuainisha majukumu ambayo utekelezaji wake unasimamiwa katika ngazi ya wizara wakati majukumu yenyewe yako katika Halmashauri. Wizara nyingine nane zimefanyiwa tathimini na kuainisha shughuli zitakazohamishiwa kwenda kwenye Halmashauri. Wizara hizo ni: Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; Maendeleo ya Mifugo na Umwagiliaji; Maliasili na Utalii; Nishati na Madini; Viwanda, Biashara na Masoko; na Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana. 190. Pamoja na kubainika kuwa baadhi ya majukumu ya wizara hizo nane yanafaa kupelekwa katika Halmashauri, imeonekana kuwa ni vyema ifanyike tathimini katika wizara sita za awali zilizoanza kutekeleza sera ya kupeleka madaraka kwa wananchi ili kubaini kasoro zilizojitokeza. Aidha, imeonekana kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kujenga uwezo katika Halmashauri ili ziweze kutekeleza majukumu yatakayo hamishiwa huko. Hitimisho 191. Katika kipindi kifupi hiki cha utekelezaji wa Sera ya Kupeleka Madaraka kwa Wananchi, dalili za kuongezeka kwa ufanisi zimeanza kujitokeza hasa katika nyanja za elimu, maji na afya ambapo wananchi wanashirikishwa na hivyo utoaji huduma za jamii umeanza kuboreka. Hata hivyo, utekelezaji wa baadhi ya majukumu yaliyohamishwa kutoka wizarani na kupelekwa kwenye Serikali za Mitaa umekuwa na tatizo la upungufu wa wataalamu wa kutekeleza majukumu husika na rasilimali fedha kuendelea kubakia katika wizara. Changamoto zinazojitokeza ni pamoja na kujenga uwezo wa Halmashauri ili ziweze kutekeleza kwa ufanisi majukumu yaliyohamishwa; kuboresha utoaji wa huduma; kuhakikisha shughuli zote zinazohamishwa zinapewa mgao wa rasilimali za kutosha; na kuoanisha na kurahisisha njia mbali mbali zinazotumika kupeleka fedha kwenye Halmashauri. Katika kipindi cha muda wa kati Serikali itahakikisha kuwa watumishi na vitendea kazi kwa shughuli zilizohamishwa kutoka serikali kuu vinapelekwa kwenye Serikali za Mitaa. Aidha, wizara zimeelekezwa kupanga na kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Serikali za Mitaa zinajengewa uwezo wa kiutekelezaji. |
||||