HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWA WANANCHI,

 31 JULAI 2004

 

 

Ndugu Wananchi,

 

            Juzi nimerejea nyumbani kutoka Gaborone, Jamhuri ya Botswana, ambapo nilikwenda kutembelea Makao Makuu ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kukagua kazi za Jumuiya, na kuzungumza na viongozi na wafanyakazi kwa wadhifa wangu wa Mwenyekiti wa SADC.  Nilipata pia fursa ya kufanya mazungumzo na Rais wa Botswana, Mhe. Festus Mogae na viongozi wengine wa nchi hiyo.

            Mojawapo ya mambo niliyoyafuatilia ni mipango ya SADC kuhusu sekta ya afya, hususan UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, magonjwa ambayo yanaleta matatizo makubwa ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo katika nchi zetu.

            Leo napenda nizungumze nanyi kuhusu ugonjwa wa malaria.  Nafanya hivyo kwa sababu tumezoea mno kuishi na malaria kiasi kwamba hatuoni au kuzingatia vya kutosha hatari kubwa sana inayoletwa na malaria.  Tunayo kila sababu kuongeza nguvu kwenye kupambana na UKIMWI, lakini tunayo kila sababu pia kuongeza nguvu kwenye kupambana na malaria.  Ningependa takwimu zifuatazo zinazoelezea hali ya malaria na athari zake kwenye nchi za SADC, na pia kwetu Tanzania, zituzindue kuhusu hatari iletwayo na malaria.

Ndugu Wananchi,

            Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa kwa nchi wanachama wa SADC, kwa ujumla wao, malaria ni chanzo cha pili kwa kuua watu wengi, baada ya UKIMWI.  Watu kati ya 300,000 – 400,000 hufa kila mwaka.  Asilimia 30 ya wagonjwa wa nje katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, wanasumbuliwa na malaria.  Asilimia 40 ya wanaolazwa wanaugua malaria.  Hawa ni watu ambao hawafanyi kazi za familia na za kujenga nchi kwa vile wanaumwa.  Hiyo ni hasara kubwa kwa familia zao na kwa mataifa yao.  Fikiria pia gharama kubwa kwao wenyewe, na kwa Serikali zao, ya kuwatibu.

            Hali ni hiyo hiyo hapa kwetu Tanzania; tena sisi malaria ndiyo huua watu wengi zaidi kuliko UKIMWI.  Tanzania  tunaongoza kwa vifo vya malaria katika nchi zote za SADC. Lakini tunaogopa UKIMWI zaidi kwa vile ni ugonjwa mpya kuliko malaria, ugonjwa ambao tumekuwa nao kwa karne na karne.  Tunaogopa UKIMWI kwa vile hauna tiba, na hatuogopi malaria kwa vile yana tiba japo yanaua watu wengi kuliko UKIMWI. Na wengine wanahalalisha mazoea ya malaria kwa kusema lazima ukiishi hapa uwe na kiasi fulani cha vimelea vya malaria mwilini wakati wote.  Ombi langu ni kuwa tusiseme hivyo kwa maana ya kupuuzia hatari ya malaria; tuseme hivyo kwa kujikumbusha wakati wote kuwa kama vile ambavyo vimelea vyake viko nasi wakati wote, malaria inapaswa kuwa ajenda ya kudumu katika kaya zetu na jamii zetu.

Ndugu Wananchi,

            Hebu tafakarini takwimu zifuatazo. 

            Kila mwaka Watanzania karibu milioni 18 wanaugua malaria.  Maana yake ni kuwa karibu kwa kila Watanzania wawili, mmoja anaugua malaria kila mwaka. Takwimu za mwaka 2002 zinaonyesha kuwa matukio ya malaria yaliyoripotiwa kwenye sehemu za huduma za afya yalikuwa mara tano zaidi ya matukio ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Surua na Ukoma kwa pamoja.  Malaria huua wastani wa Watanzania 100,000 kila mwaka, yaani sawa na kuua mtu mmoja katika kila dakika 5.  Na wote hao hawana sababu ya kufa, maana malaria ni ugonjwa unaozuilika kwa gharama ndogo, na kwa kiasi kikubwa unatibika ukiwahiwa. Lakini bado kwa kuzoea malaria, hatutaki kukubali ukweli kuwa ugonjwa huu ni hatari kubwa kwa uhai, maendeleo na ustawi wa taifa letu, na ni sababu mojawapo kubwa ya kutupunguzia sana maksi za maendeleo ya kijamii tunapolinganishwa na nchi nyingine.

            Kinachosikitisha zaidi ni kuwa wengi wa wanaougua na kufa kwa malaria ni watoto wetu wadogo wenye umri wa chini ya miaka 5.  Kitakwimu, tangu nimeanza kuzungumza nanyi, dakika tano zilizopita, watoto zaidi ya 300 wameambukizwa malaria na wanaweza kufa. Kila mwaka tunapoteza watoto 70,000 wanaokufa kwa malaria.  Yaani, kwa kila vifo 10 kutokana na malaria, 7 ni vya watoto hao chini ya umri wa miaka 5.

            Narudia.  Malaria huathiri zaidi kina mama wajawazito na watoto wadogo chini ya miaka 5. Kipindi kinachoongoza kwa maambukizo ya malaria ni Oktoba-Desemba, na Februari-Aprili.  Kwa hiyo, kwa uchungu mkubwa, naomba kuanzia mwaka huu tukubaliane kitaifa kuibua upya nia na moyo wa ushupavu wa kupambana na malaria ili kuokoa watoto wetu tunaowapenda sana.

 

Ndugu Wananchi,

            Leo napenda nipendekeze kwenu hatua zifuatazo ambazo mimi naziona ni muhimu sana katika kupambana na malaria.

 

·        Kwanza, kila mmoja wetu atambue na kukubali kuwa malaria ni tatizo kubwa sana. Tusilipuuze wala kulifanyia mzaha.

 

·        Pili, kila mmoja wetu akubali yeye mwenyewe kuwa askari katika mapambano dhidi ya malaria.  Mzigo huu ni wetu sote, Serikali na kila mwananchi.

 

·        Tatu, kila mmoja wetu ajiandae kwa mapambano hayo kwa kujifunza mbinu zake, kuzielewa na kuzizingatia.  Kila mtu, mkubwa kwa mdogo, ajue malaria inavyoenea, inavyoweza kuzuiliwa, na inavyoweza kutibiwa.

 

·        Nne, wenye wajibu wa kuelimisha jamii, kuanzia Wizara ya Afya, Asasi Zisizokuwa za Serikali, Halmashauri na Serikali za Mitaa katika ngazi zote, na hata viongozi wa kijamii, wote waongeze kasi na usahihi wa elimu ya afya kuhusu kuzuia na kutibu malaria.

 

·        Tano, tujenge ushirikiano na ushirikishwaji miongoni mwa wadau wote, kwenye ngazi zote.  Ugonjwa wa malaria utadhibitiwa vizuri zaidi kila mwanajamii akishiriki.  Haisaidii sana, kwa mfano, kwa kaya moja kuharibu mazalio ya mbu, kama jirani zao nao hawafanyi hivyo.

 

·        Sita, wanasiasa na viongozi wa dini watumie majukwaa yao kuelimisha jamii na kuhimiza utekelezaji wa mikakati ya kupambana na malaria, si UKIMWI peke yake.

 

·        Saba, watoto wadogo, chini ya miaka 5, na akina mama wajawazito, wapewe kipaumbele cha pekee kwenye kuzuia na kutibu malaria.

 

·        Nane, tusisahau kuwa kinga ni bora na nafuu zaidi kuliko tiba.  Serikali imeondoa kodi kwenye vyandarua na dawa za kuzuia malaria. Tanzania imesifiwa sana kwa hatua hizo. Lakini sifa hizo hazitakuwa na maana iwapo wananchi hawataongeza sana matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa.

 

·        Tisa, tiba ni muhimu na inabidi iwe ya haraka kwa wagonjwa.  Kila mtu, na hasa kila mzazi, ajue vizuri dalili za malaria, na afanye nyumba yake kuwa kituo cha kwanza cha kutibu malaria.  Upatikanaji wa dawa bora za malaria nyumbani unaweza kuokoa maisha ya mtoto wako mpendwa.  Maeneo yote yanayotoa huduma za afya yaimarishe uwezo wa kupima haraka na kwa usahihi vimelea vya malaria na kutibu.  Wafanyao kazi hapo wachukulie malaria, si kama kitu cha kawaida, bali kama jambo la hatari kwa uhai wa mgonjwa husika, hasa mgonjwa mwenyewe akiwa mtoto mdogo.  Watoto wadogo wengi hufa katika muda wa saa 48 tu iwapo hawatapata tiba haraka na sahihi tangu waonyeshe dalili za kwanza za malaria.

 

·        Kumi, tiba asilia zilizokubalika na wataalam kuwa zinatibu malaria zitumike, lakini kamwe tusidanganyike kuwa degedege ni ugonjwa; degedege ni dalili za homa kali ya malaria.  Ugonjwa ni malaria.  Degedege ni dalili. Tusipoteze muda kupambana na degedege ambayo ni dalili badala ya kumkimbiza mtoto hospitali ili ugonjwa wenyewe, ambao ni malaria, utibiwe haraka.  Na kama lipo tatizo lingine litabainika hospitalini, si kwa mganga wa kienyeji, au kwa kutafuta mchawi. Tupambane na malaria kisayansi, si ki-imani.

 

Ndugu Wananchi,

            Serikali yenu itajitahidi kuongeza matumizi ya fedha kukabiliana na magonjwa kama haya ya malaria. Lakini yapo mengi yanayoweza kufanywa katika ngazi ya familia ili kujikinga na malaria, na kuyatibu.  Tusingoje Serikali kila mara.

            Uwezo wa Serikali nao ni mdogo.  Ndio maana tunawashukuru wahisani wote – Serikali za nje, mashirika ya kimataifa, na Asasi Zisizokuwa za Serikali, wanaotusaidia katika kupambana na malaria.  Nawashukuru sana.  Lakini kazi bado ni kubwa.  Utafiti wa chanjo ya malaria lazima uendelee, tena kwa kasi kubwa zaidi maana huo utakuwa ufumbuzi wa kudumu.  Nafurahi kuwa Tanzania imo mstari wa mbele katika utafiti huo, kwa kushirikiana na wengine. Nawapongeza sana watafiti wetu ambao wanasifiwa sana duniani, na ninawatia shime.

Dawa mpya, zenye uwezo wa kudhibiti usugu wa vimelea vya malaria, nazo lazima zitafitiwe, na zipatikane kwa bei nafuu.  Duniani,  fedha nyingi zaidi hutumika kutafiti magonjwa na dawa kwa magonjwa yanayosumbua wakubwa, yaani matajiri.  Magonjwa yanayoshamiri kwenye nchi maskini, na ambayo yanazidisha umaskini wetu kama malaria, hayafanyiwi utafiti wa kutosha, ati kwa vile hata dawa mpya zikipatikana hatuna uwezo wa fedha wa kununua dawa hizo.  Matokeo yake fedha zinazotumika duniani kote kutafiti malaria kwa mwaka ni chini ya sh.100 bilioni, ambazo hazitoshi kununua hata ndege moja tu aina ya Jumbo Jet! Fedha zinazohitajika kudhibiti malaria kwa mwaka ni sh.300 bilioni, ambazo ni sawa na gharama ya kujenga barabara ya njia nne ya urefu wa kilometa 24 tu katika nchi tajiri.  Nusu ya vifo vyote barani Afrika husababishwa na magonjwa yanayozuilika na kutibika kama ilivyo malaria.  Barani Ulaya ni asilimia 2 tu ya vifo husababishwa na magonjwa hayo.

            Lazima sasa dunia iamue:  ama sisi wote ni binadamu sawa, tunaohitaji haki ya msingi ya kuishi na kuwa na afya bora, au sivyo.

Ndugu Wananchi,

            Wakati tukisubiri wakubwa watafakari swali hilo, naomba sisi wenyewe tusisahau kamwe kuwa malaria inaua watoto wa Kitanzania 70,000 wenye umri chini ya miaka 5 kila mwaka, au karibu watoto 200 kila siku. Lakini dawa ya chandarua ya sh.300/= tu inaweza kuokoa uhai wa mtoto wako.  Kumwahisha hospitali mtoto wako kunaweza kuokoa maisha yake.  Namwomba kila baba, na kila mama, ahakikishe mtoto wake analala ndani ya chandarua kilichotiwa dawa, na auguapo ahakikishe anamfikisha mara moja kwenye zahanati, kituo cha afya au hospitali iliyo karibu.  Kuchelewa, hata kwa siku moja tu, kunaweza kugharimu uhai wa mwanao.  Shirika la Kimataifa la UNICEF linakadiria kuwa mambo haya mawili:  kulala ndani ya chandarua chenye dawa, na kuwahi hospitali, yanaweza kupunguza malaria kwa asilimia 60, na kupunguza vifo vya watoto kwa asilimia 20!  Na hizi si takwimu tu, ni maisha ya watoto wetu wa Kitanzania ambayo tunaweza kuyaokoa.

            Naomba tusisahau kamwe kuwa malaria inazidisha umaskini wetu.  Malaria hufikia kilele chake wakati wa msimu wa mvua, ambao ni wakati wa kilimo.  Hivyo malaria ni adui wa kilimo tunachokitegemea kwa chakula na mapato kwenye ngazi ya kaya na taifa.  Malaria hupunguza kipato cha wakulima kwa karibu asilimia 40 kwa familia zenye wagonjwa wa malaria.  Kwa wastani, familia ya Kitanzania inatumia asilimia 20 ya mapato yake kutibu malaria. Kupambana na malaria ni kupambana na umaskini.  Tusilegeze kamba maana sasa malaria inanyemelea hata maeneo ambayo zamani yalikuwa hayana ugonjwa huu.

            Naomba tusisahau kuwa malaria hupunguza kasi ya kukua kwa uchumi wa taifa na maendeleo yetu.  Tanzania inapoteza sh.122 bilioni kila mwaka kutokana na ugonjwa wa malaria.  Hiyo ni hasara kubwa kwa nchi maskini kama yetu.  Na inawezekana kupunguza sana hasara hiyo kama tukizingatia yote niliyoyaeleza leo.

            Namalizia kwa kukuombeni sana, Ndugu Wananchi, kila mmoja, kila kaya, kila jamii, tutoe kipaumbele kipya kwenye vita dhidi ya malaria.  Watoto wetu wengi wanakufa bila sababu; vifo vyao vinazuilika tukiamua hivyo. Taifa linapata hasara kubwa, inayoepukika.  Mapato ya familia yanaathirika, na si lazima iwe hivyo.

            Mwaka mpya wa fedha umeanza.  Naomba Wizara ya Afya, wahisani mbalimbali, asasi zisizokuwa za kiserikali, Halmashauri za Miji na Serikali zote za Mitaa, na kila mwananchi, tushirikiane upya kuongeza kasi ya vita dhidi ya malaria.  Inawezekana.  Okoa watoto wako.  Jiokoe mwenyewe.  Okoa uchumi wa familia na taifa.  Timiza wajibu wako.

 

            Mungu Ibariki Afrika!

            Mungu Ibariki Tanzania!

 

            Ahsanteni kwa kunisikiliza.