HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWA WANANCHI,

 31 OKTOBA 2005

 

 

Ndugu Wananchi:

 

            Katika wiki chache zilizopita nimepata fursa ya kuagana na makundi mbalimbali ya Watanzania, ndani na nje ya nchi yetu.

            Ninashukuru sana kwa zawadi nilizopewa.  Lakini zaidi sana nimefarijika na tathmini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu ambayo wananchi wamekuwa wakiifanya wanapoagana nami, na wengine kwa makala maridhawa wanazoandika magazetini.

            Leo napenda nichukue tathmini hizo hatua mbili mbele.  Hatua ya kwanza ni kuhakikisha kunakuwa na uendelevu wa sera, mipango, mikakati na mageuzi ambayo ninyi wananchi—achilia mbali wanasiasa—ambayo ninyi wananchi kwa tathmini yenu mnaona yana manufaa kwa sifa na maendeleo ya nchi yetu na maendeleo yenu wananchi.

            Hatua ya pili ambayo ndiyo nitaizungumzia zaidi leo ni kutafsiri mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tatu katika maisha bora kwa kila Mtanzania.  Maana, kwa maoni yangu, uhalali wa sera za Serikali, na uhalali wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa, ni maisha bora kwa kila mwananchi.

            Ahadi yangu kwenu wakati nawashawishi mkubali tufunge mikanda na kuanzisha au kuendeleza mageuzi ya kiuchumi ilikuwa kuwa mvumilivu hula mbivu.  Anayekunywa dawa, kwa kuzingatia masharti ya daktari, ndiye hupona, japo dawa yenyewe iwe chungu kiasi gani.

            Mwanadamu anapoumwa anatafuta tiba. Akipona, hapumziki kwa kudhani matatizo yake yamekwisha.  Kupona ni mwanzo wa kutumia afya na nguvu ya mwili iliyorejea kukabili matatizo yake mengine ya kimaisha na kimaendeleo.

            Na taifa letu la Tanzania hali kadhalika.  Miaka 10 iliyopita uchumi wetu ulikuwa katika hali isiyoridhisha kiafya.  Ikabidi tuvumilie machungu ya tiba iliyohitajika.  Tunachosifiwa nacho ni kuboresha afya ya uchumi wa kitaifa, na hivyo kuweka mazingira bora ya kukabiliana na matatizo yetu ya kimaendeleo, si kama Taifa peke yake, bali pia kama watu binafsi.

            Narudia.  Uhalali wa sera na mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ni maisha bora kwa kila Mtanzania.  Ni wajibu wa Serikali kudumisha afya bora ya uchumi wa kitaifa.  Ni wajibu pia wa Serikali kuweka mazingira bora ya kisera na miundombinu ya kiuchumi na ya huduma za jamii.  Lakini ni wajibu wa kila mwananchi kutumia fursa na mazingira hayo kujiendeleza ili kweli mageuzi yetu yajitafsiri katika maisha bora kwa kila Mtanzania.

            Tumekubaliana kitaifa juu ya sera na mikakati ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini.  Ni sera nzuri, na mikakati yake inao uhakika wa mafanikio ili mradi ubia uliopo baina ya Serikali na wananchi uendelee.  Serikali iendelee kusimamia vizuri afya ya uchumi wetu, na kuweka mazingira bora ya wananchi kujiendeleza.  Wananchi nao watumie mazingira hayo na fursa hizo kwa juhudi na maarifa zaidi, ili wanufaike na mageuzi yetu.

            Pamoja na ahadi zote za wanasiasa, maisha ya mkulima yataboreshwa kwa uzalishaji kwa wingi na ubora zaidi wa kila mkulima.  Vivyo hivyo kwa mfugaji na mvuvi.  Na kwa ujumla wao, wakulima, wafugaji na wavuvi ndio idadi kubwa zaidi ya Watanzania.  Vita dhidi ya umaskini lazima iwalenge hawa.  Lakini na wao wawe tayari kupokea na kutekeleza mawazo mapya, na wawe tayari kusikiliza ushauri ili kuboresha uzalishaji, tija na ubora wa mazao yao.

            Serikali ya Awamu ya Tatu imesifiwa, kwa haki, kwa ujenzi na ukarabati wa barabara kuu, barabara za mikoa na barabara za vijijini. Kazi hiyo ni mchango wa Serikali kurahisisha mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi yafike kwenye masoko ya miji mikuu na hata nje ya nchi kwa urahisi.  Lakini barabara hizi zisipotumika kwa ukamilifu; kama hakutakuwa na mazao ya kutosha, tutakuwa tumepoteza fedha bure na kupoteza fursa za kukuza uchumi na kuondosha umaskini.

            Serikali inaweza kutoa ruzuku za usafirishaji mbolea ili iwafikie wakulima kwa bei nafuu.  Vivyo hivyo kwa madawa ya mifugo.  Lakini wakulima na wafugaji wasipotumia mbolea hiyo na madawa hayo, hakutakuwa na faida yoyote na mazingira hayo bora yanayowekwa na Serikali yatakuwa hayana faida.

            Waziri wa Biashara na Waziri wa Mambo ya Nje wanaweza kufoka sana katika majukwaa ya kimataifa kudai haki ya kuuza mazao yetu kwa wingi zaidi, na kwa bei ya haki zaidi.  Lakini kama hatuna mazao bora ya kuuza, juhudi zao ni kazi bure, na maendeleo yatazidi kutupiga chenga.  Tena tunaweza kudhihakiwa na hao tunaowapigia kelele.  Maana tunadai haki ya kuuza bila kuwa na cha kuuza.

            Tumejitahidi kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwenye kusindika mazao yetu ya kilimo, ufugaji na uvuvi.  Mnaoishi maeneo yenye viwanda vya kusindika samaki mnaona faida yake.  Tunataka kupanua uwezo huo, na ule wa kusindika mazao ya kilimo na ufugaji.  Lakini juhudi hizo zitakuwa kazi bure iwapo hatutaongeza uzalishaji wa mazao ya kusindikwa.  Itakuwa aibu kubwa kwa kiwanda cha kusindika nyama nchini Tanzania kikose nyama ya kutosha, ya viwango vinavyotakiwa kwenye masoko ya nje.  Itakuwa aibu kubwa kwa kiwanda cha kusindika matunda na mbogamboga kukosa matunda na mbogamboga za kutosha kufanya kazi mwaka mzima katika nchi hii ambayo Mwenyezi Mungu ameijalia ardhi tele yenye rutuba na maji, ardhi ambayo wenzetu katika nchi jirani wanaitamani sana.

            Na tukubali ukweli wa dunia ya utandawazi.  Iwapo sisi wenyewe tutashindwa kuzalisha mazao ya kutosha, itabidi waje wawekezaji kutoka nje kufungua mashamba makubwa ya kutosheleza mahitaji yetu ndani ya nchi na kuuza nje.  Watanzania tungekuwa tunalima au kuvua kwa kiwango cha kutosheleza mahitaji hayo wawekezaji kutoka nje wasingevutiwa kuja kulima au kuvua huku kwetu.  Wanakuja kwa vile wanaona pengo kati ya mahitaji halisi kitaifa na kimataifa na uwezo wetu sisi wa uzalishaji.

            Tumeanzisha Mpango wa Kurasimisha Raslimali na Biashara za Wanyonge Tanzania ili, pamoja na mambo mengine, raslimali hizo zitumike kama dhamana ya mikopo ya kupanua uzalishaji na biashara kwa wananchi.  Aidha, tunatekeleza sera za kuendeleza uzalishaji na biashara ndogo na za kati, vijijini na mijini, ili kukuza uchumi, kuongeza ajira, na hivyo kupiga vita umaskini wa kipato.  Lakini juhudi zote hizo haziwezi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania iwapo kila mmoja wao hatajitokeza na kujituma kutumia fursa hizi kwa bidii na maarifa. Tusidhani Serikali itaweka fedha mfukoni mwa kila Mtanzania.  Badala yake Serikali itaweka fursa kwa kila Mtanzania kujiendeleza.

            Wapo wanaopinga mpango wa kurasimisha raslimali za wananchi, ati wananchi wakikopa kwa kuweka raslimali hizo kama dhamana watazipoteza pale watakaposhindwa kulipa.  Ninapokaribia kuhitimisha uongozi wangu naona upo umuhimu wa kuweka jambo hili wazi.

            Kwanza, ningependa wananchi muelewe kwamba mikopo ndiyo chanzo cha mitaji kote duniani, kuanzia kwa wawekezaji wadogo wanaokopa laki moja, hadi wawekezaji wakubwa wanaokopa mabilioni.  Hapa Tanzania wapo wananchi wengi ambao kupitia mifuko ya kuweka na kukopa wamejipatia mitaji ya kuboresha maisha yao.  Wapo pia waliokopa kwenye mifuko inayoanzishwa au kuungwa mkono na Serikali, na wengine wamekopa benki.  Msidanganywe wananchi.  Hata wawekezaji wakubwa, wakiwemo wanaokuja kuchimba madini hapa kwetu, wote wanakopa.  Tusiogope kukopa; tusipokopa hatuwezi kupanuka kiuwekezaji na kiuzalishaji.

            Lakini tukope kwa makini, kwa busara, baada ya kufanya upembuzi wa kutosha na kuridhika na faida ya mradi unaohusika.  Na baada ya kukopa tutumie kila senti ya mkopo kwa kilichokusudiwa.

            Juzi juzi nimetoka Afrika Kusini ambapo nilielezwa juu ya utaratibu mzuri sana wanaoutumia kukopesha wakulima.  Kwanza mkulima anatafuta soko la mazao anayotaka kuyalima.  Akishaingia mkataba wa manunuzi ya mazao atakayoyazalisha anakwenda benki kukopa ili azalishe mazao hayo ambayo tayari yana soko.  Benki haimpi fedha; inampa kila anachohitaji ili kuzalisha mazao hayo ambayo tayari yana soko.  Kama ni trekta, atakopeshwa trekta, si fedha taslim.  Kama ni kujenga mtandao wa kilimo cha unyweshaji, italetwa kampuni ya kumjengea mtandao huo.  Kama ni mbegu, atakopeshwa mbegu, si fedha.  Matokeo yake hakuna yale yanayotokea hapa kwetu ambapo mtu anakopa kwenda kulima, lakini badala yake anaoa mke wa pili, ananunua gari la kifahari, au anakwenda kutembea Ulaya.

            Badala ya kupinga wananchi kukopa kwa kuweka ardhi yao au raslimali yao kama dhamana, tutafute na sisi utaratibu wa kuhakikisha mikopo watakayopewa wananchi itatumiwa kwa makusudi ya mkopo na si vinginevyo. Lakini tusiwatishe wananchi kuwa ati ukikopa basi huo ni mwanzo wa kupoteza raslimali zako.

            Jambo la pili ambalo hapana budi Watanzania tulielewe ni kuwa kwa kadri unavyokopa, na kuweka rekodi nzuri ya kulipa, ndivyo unavyoaminiwa na benki, na ndivyo itakavyokuwa rahisi kukopeshwa, tena kwa riba nafuu.  Benki yoyote huwa na mashaka na mkopaji asiye na rekodi hiyo.

Ndugu Wananchi:

            Uchumi wa taifa letu sasa ni uchumi wa soko.  Uchumi wa dunia nao ni uchumi wa soko.  Na hii ni kanuni mojawapo ya uchumi wa soko.  Kukopa, kuzalisha, kuuza, kulipa.  Kukopa, kutoa huduma, kulipa.  Ni hapo tu Watanzania watakapoamka na kutumia vizuri utaratibu huu ndipo mageuzi ya kiuchumi yatakapojitafsiri katika maisha bora kwa kila Mtanzania.  Wananchi msikubali kulazwa usingizi na watu ambao mawazo yao yameganda katika miaka ya 1960 na 1970.

            Mojawapo ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tatu ni ongezeko kubwa la benki na taasisi nyingine za fedha.  Nitasikitika sana iwapo benki na taasisi hizo zitawanufaisha wageni tu, au kikundi kidogo cha Watanzania.  Nina uhakika Serikali ijayo itazidi kuhimiza mazingira bora ya ukopaji wa wananchi wa kawaida, na hivyo kuvutia benki hizi zitoke kwenye miji mikubwa kwenda miji midogo wakijua ipo biashara ya fedha huko.

            Narudia. Uchumi wa soko una kanuni zake.  Tusipozitambua na kuzifuata tutabaki kulalamika tukiona wivu Watanzania wenzetu wachache, na wageni, wakitumia fursa na kanuni hizo kutajirika.  Wakati wa Watanzania wengi zaidi nao kutajirika umefika; lakini tuwe wabunifu zaidi, tuwe makini zaidi, na tusiogope kuthubutu, kukopa, na kukuza ujasiriamali miongoni mwetu.

Ndugu Wananchi:

            Serikali pia imeanzisha Mpango Maalum wa Kuharakisha Maendeleo ya Tanzania kwa Kuzingatia Uzoefu wa Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (Tanzania Mini-Tiger Plan 2020).  Maandalizi yamekamilika na utekelezaji umeanza.  Utekelezaji huo unalenga kuiwezesha Tanzania kufikia haraka malengo yafuatayo ifikapo mwaka 2020:

 

1.                  Ukuaji wa uchumi uongezeke kutoka asilimia 6.7 kwa mwaka (2004) hadi asilimia 8 – 10;

 

2.                  Pato la Taifa liongezeke mara nne kutoka USD 10 bilioni mwaka 2004 hadi USD 40 bilioni;

 

3.                  Mchango wa sekta ya viwanda kwenye Pato la Taifa uongezeke kutoka asilimia 7 (2004) hadi asilimia 15 – 25 kwa mwaka;

 

4.                  Mapato ya fedha za kigeni yatokanayo na bidhaa zinazouzwa nje yaongezeke kutoka USD 1.3 bilioni (2004) hadi USD 20 bilioni;

 

5.                  Pato la Wastani la Mtanzania kwa mwaka liongezeke kutoka USD 286 hadi USD 1,000; na

 

6.                  Zipatikane ajira mpya milioni tatu ifikapo mwaka 2020.

 

            Ili kufikia malengo hayo, Serikali imeamua kutekeleza mikakati mikuu ifuatayo:

 

1.                  Kujenga mazingira mazuri zaidi ya kuvutia kwa wingi zaidi uwekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa kuanzisha Maeneo Maalum ya Uwekezaji, kwa Kiingereza Special Economic Zones – SEZs;

 

2.                  Kuzalisha bidhaa na huduma kwa kuzingatia kwanza mahitaji ya masoko;

 

3.                  Kuelekeza raslimali za ndani na nje ya nchi, ikiwemo Bajeti ya Serikali, misaada kutoka nje pamoja na uwekezaji wa moja kwa moja kwenye mpango huu;

 

4.                  Kuweka mfumo bora wa usimamizi utakaoweza kusimamia utekelezaji na kutatua haraka matatizo yatakayojitokeza;

 

5.                  Kuboresha masuala yanayohusu sheria na taratibu za utawala na nguvu-kazi; na

 

6.                  Kuongeza kasi ya kuvutia wawekezaji, ikiwemo kwa kutumia washauri wa kitaifa na kimataifa.

 

Ndugu Wananchi:

            Narudia tena.  Uhalali wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa; na uhalali wa sera za uchumi zinazotekelezwa na Serikali, ni maisha bora kwa kila Mtanzania.  Lakini Serikali haina uwezo wa kuweka fedha mifukoni mwa watu.  Kilichomo ndani ya dhamira na uwezo wa Serikali ni kuondosha vikwazo vya wananchi wajasiriamali wanaotaka kujiendeleza.  Kilicho ndani ya dhamira na uwezo wa Serikali ni kubuni sera sahihi na kuzisimamia, pamoja na kuweka mazingira bora ya uchumi mkuu na miundombinu ili Watanzania wanaojituma wafanikiwe.

            Kwa wale wasio tayari kujituma, na wale wanaoingojea Serikali iwafanyie kila kitu, hao wataachwa nyuma.  Hilo si lengo la Serikali na nina hakika hata Serikali ijayo itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha wengine hawaachwi nyuma.  Lakini kila mtu na ajitume na kujibidisha zaidi.

            Mimi karibu ninaacha uongozi.  Lakini kumbukeni kuwa hakuna nchi inayoweza kuendelea kwa kuilundikia Serikali madai na malalamishi.  Nchi inajengwa kwa ubia baina ya Serikali na wananchi, kila upande ukitimiza wajibu wake.  Umaskini unapigwa vita kwa Serikali kuweka mazingira bora, na wananchi kuyatumia kujiendeleza. Na tusisahau busara za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere.  We must run while others walk.  Wengine wakitembea sisi lazima tukimbie.

            Kwa pamoja tunaweza kufika mbali, na Tanzania ikawa mfano bora kwa wengine.

 

            Mungu Ibariki Afrika!

            Mungu Ibariki Tanzania!

 

            Ahsanteni kwa kunisikiliza.