HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO
KIKWETE,
AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA
JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA,
30 DESEMBA 2005
Mheshimiwa Spika:
Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uhai na afya, na
akatukutanisha hapa. Ninamshukuru pia kwa Uchaguzi Mkuu wa amani, utulivu na
heshima kubwa kwa nchi yetu.
Nakishukuru sana Chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kwa heshima kubwa kilichonipa kwa kuniteua niwe mgombea wake wa nafasi ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ninawashukuru
wananchi kwa kunipa mimi na Chama changu ushindi mkubwa sana. Shukrani zangu
kwa Watanzania wenzangu—wana-CCM na wasio wana-CCM—ni ahadi ya kuwatumikia kwa
uwezo wangu wote.
Nawashukuru wapinzani kwa ujasiri wao mkubwa wa
kujitokeza kushindana na Chama Cha Mapinduzi.
Uchaguzi sasa umekwisha. Kauli ya
wananchi imedhihirika. Tuungane, tuwe kitu kimoja; tujenge na kuendeleza nchi
yetu.
Nawashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa kumkubali mteuliwa wa CCM kwa nafasi ya Spika,
Mheshimiwa Samuel John Sitta, Mb., na pia kwa kukubali uteuzi wangu wa Waziri
Mkuu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, Mb. Naomba mumpe Waziri Mkuu, pamoja na
Mawaziri na Naibu Mawaziri nitakaowateua hivi karibuni, ushirikiano mkubwa.
Wachangamsheni, lakini watendeeni haki na wapeni ushirikiano.
Mheshimiwa Spika:
Nawapongeza Wabunge wote waliochaguliwa. Ninyi,
Waheshimiwa Wabunge, ndio macho na masikio ya wananchi. Mmeaminiwa na kuheshimiwa. Naomba kila siku mnapoingia au kutoka katika Bunge
hili, mnapozungumza humu ndani au mnaposikiliza wengine wakizungumza, mnapokuwa
macho au mnapofumba macho kutafakari kwa kina, kila mara mkumbuke imani na
heshima hiyo kubwa mliyopewa na wananchi.
Nakupongeza sana wewe mwenyewe, Mheshimiwa Spika, kwanza
kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge, na pili kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge hili
Tukufu. Umepata kazi ya heshima kubwa
sana, yenye wajibu mkubwa sana. Unao uwezo na uzoefu wa kuifanya. Hivyo, sina
shaka utaimudu vema kazi hiyo, na utaliongoza Bunge hili kwa hekima na
busara, ukiwatendea haki Wabunge wote, na upande wa Serikali pia. Ninakutakia kila la kheri, na
ninakuhakikishia ushirikiano kamili katika kazi zako.
Mheshimiwa
Spika:
Ninampongeza Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Amani Abeid Karume,
kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Zanzibar.
Namhakikishia ushirikiano wangu na wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano.
Mheshimiwa
Spika:
Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi
kubwa na nzuri waliyoifanya ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa
kisiwa cha amani na utulivu wakati wote wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Wameonyesha uaminifu kwa Taifa na uzalendo wa
hali ya juu. Nawapongeza sana.
Mheshimiwa
Spika:
Wananchi wengi
wameelimika na kufuatilia mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu kutokana na kazi kubwa
na nzuri iliyofanywa na vyombo vya habari.
Nawashukuru na kuwapongeza.
Mheshimiwa
Spika:
Serikali ya Awamu ya
Nne ambayo nimepewa heshima ya kuiongoza, inaanza kazi wakati nchi ikiwa na
hali nzuri kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Mafanikio hayo yametokana na uongozi imara na thabiti wa Rais Mstaafu wa
Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.
Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri
aliyoifanyia nchi yetu. Kwangu binafsi,
amekuwa mwalimu na mwelekezi ambaye amenijengea uwezo na dhamira ya kuendeleza
kazi aliyoianza. Namtakia afya njema na
maisha marefu, yeye, Mama Mkapa, na familia yao.
Mheshimiwa Spika:
Nazipongeza Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na Tume ya
Uchaguzi Zanzibar, kwa kazi nzuri sana waliyoifanya katika chaguzi
zilizopita. Naomba waendelee kunoa
uwezo wao, maana Watanzania—Bara na Zanzibar—wanastahili uchaguzi mzuri. Kadhalika tunao wajibu wa kihistoria wa kuwa
mfano bora barani Afrika na hata kwingineko.
Siasa
Mheshimiwa Spika:
Chama Cha Mapinduzi kimerejeshwa madarakani kwa kura
halali za wananchi zilizotupa idhini ya kutawala, tena idhini kubwa isiyo na
shaka hata kidogo. Hatutaona aibu
kuitumia idhini hiyo, kupitia Bunge hili, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya 2005.
Kama
mwana-CCM nafurahia sana ushindi wetu. Lakini, nikiwa Rais, napenda
niwahakikishie wapinzani kuwa hatuna nia au sera ya kuua vyama vya
upinzani. Serikali ya Awamu ya Nne
itaendeleza, kwa dhati, mfumo wa siasa wa demokrasia ya vyama vingi. Ushauri wangu kwa vyama vya upinzani kwa
wapinzani ni kuwa wasiwe wepesi kutafuta mchawi kila wanaposhindwa uchaguzi.
Badala yake nawaomba wajiulize kwa nini Watanzania wamewakataa kiasi hicho. Nina uhakika watapata jibu.
Mheshimiwa Spika:
Ni kweli nchi yetu sasa ni ya
demokrasia ya vyama vingi. Lakini ni wazi bado utamaduni wa mfumo huu wa siasa
ni mchanga na kwa ujumla haujaimarika vya kutosha. Tutajitahidi kujenga
utaratibu na misingi ya mahusiano mema zaidi baina ya vyama vya siasa nchini Tanzania. Mimi naamini wakati umefika, kama alivyowahi
kusema Rais Mkapa, kuwa tuwe na maadili yatakayotawala shughuli za kisiasa,
ambayo hayategemei hiari ya viongozi wa kisiasa waliopo madarakani. Yanakuwa ni
maadili na miiko ya lazima, yanayobana kila chama cha siasa, wanachama na
viongozi wake, ikiwemo wale wa Chama Tawala.
Tusipofanya hivyo—na
dalili zimeanza kuonekana—wanaweza kujitokeza watu wakavuruga nchi yetu kwa
kisingizio cha uhuru wa kisiasa. Uhuru bila mipaka ni fujo, na siwezi kukubali
nchi mliyonikabidhi kuiongoza itawaliwe na fujo.
Mheshimiwa Spika:
Yameanza kujitokeza mawazo kuwa uongozi unaweza
kununuliwa kwa fedha. Kama ni kweli,
tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za
kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo. Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo
muhimu katika kufanikisha uchaguzi. Lakini, fedha kutumika kununua ushindi si
halali. Ni vema sasa tuanzishe mjadala
wa kitaifa na hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama
au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali, ulio wazi, wa chama
au mgombea kutumia fedha hizo. Na
utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya uchaguzi katika uchaguzi
wa kiserikali na ndani ya vyama vya siasa.
Katika mjadala huo suala la takrima nalo tuliangalie.
Majukumu ya Msingi ya Serikali ya Awamu ya Nne
Mheshimiwa Spika:
Tangu tupate Uhuru, kila awamu ya uongozi wa taifa
imekuwa na majukumu yake ya msingi.
Awamu ya Kwanza iliunda na kujenga taifa. Wakoloni hawakujenga hisia za utaifa, maana
mkakati wao wa kututawala ulikuwa kutudhoofisha kwa kutugawa ili tutawalike kwa
urahisi. Mwalimu Nyerere hakurithishwa
taifa na wakoloni. Alirithishwa
mkusanyiko wa makabila mbalimbali, na watu wa dini na rangi mbalimbali. Akatambua kuwa hata uchumi wa Tanzania
ungekua kwa kasi kubwa kiasi gani, iwapo hakuna misingi imara na hisia za dhati
za utaifa, baada ya muda tutasambaratika na uchumi huo utakuwa hauna maana. Kwa kushirikiana na hayati Mzee Karume
wakatujengea Taifa la Tanzania lenye umoja, pamoja na watu wake kuwa wa
makabila 120, rangi na dini mbalimbali.
Mwalimu aliongoza vita dhidi ya ujinga, umaskini na
maradhi. Mtandao mkubwa wa huduma za
jamii tunaojivunia leo ulianza na falsafa ya maendeleo ya Baba wa Taifa. Wengi wetu tuliomo humu ndani, wa makamo
yangu, tusingesoma na kufika hapa tulipo kama si kuona mbali na sera nzuri za
Baba wa Taifa. Tutamshukuru yeye na Mzee
Karume daima.
Awamu ya Pili chini ya Mzee wetu, Ali Hassan Mwinyi,
ilifungua milango na kupanua uwanja wa ushiriki wa wananchi kwenye uchumi na
siasa. Mzee Mwinyi ni muasisi wa mageuzi
ya kiuchumi na kisiasa Tanzania.
Alimaliza uhaba wa bidhaa na baadhi ya huduma muhimu uliodhalilisha
wananchi. Alipanua sana mipaka ya uhuru
wa raia katika maisha yao ya kiuchumi na kisiasa.
Nakumbuka siku moja
Mzee Mwinyi alielezea awamu yake kama wakati ambapo mtu anafungua madirisha ya
nyumba ili hewa safi iingie ndani.
Lakini, akasema, ukifungua madirisha ujue nzi, mbu na wadudu wengine nao
wataingia.
Hapo ndipo Awamu ya Tatu ya Rais aliyenitangulia,
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, ilipoanzia.
Ilibidi kushughulikia mbu, nzi na wadudu hao. Rais Mkapa alifanya kazi kubwa kurejesha
nidhamu kwenye ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali. Alipiga vita rushwa kwa nguvu zake zote. Alirejesha mahusiano mazuri na wahisani wetu
na washirika wetu kwenye maendeleo.
Aliweka mazingira bora ya uwekezaji, na ukuaji wa uchumi. Aliimarisha misingi ya uchumi mkuu. Bei za kuruka, na fedha za soksi zikaisha. Ameweka misingi imara ya kuwezesha wananchi
kujiendeleza kupitia miradi kama vile TASAF na MKURABITA chini ya mwavuli wa
MKUKUTA.
Alikarabati na
kupanua sana miundombinu ya elimu, afya, maji na umeme. Barabara na madaraja yamejengwa. Kutokana na juhudi za Rais Mkapa, Serikali ya
Awamu ya Nne inaanza bila mzigo wa madeni usiobebeka kama alivyoanza yeye. Tunaanzia mahali pazuri.
Mheshimiwa Spika:
Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa
Mwaka 2005 imetamka bayana majukumu mawili ya msingi ya Serikali ya Awamu ya
Nne:.
·
Kwanza, kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio
nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa taifa
linalojitegemea.
·
Pili, kuwashirikisha wananchi wote kwa njia ya uwezeshaji
katika ujenzi wa uchumi na kuutokomeza umaskini.
Mheshimiwa Spika:
Kwa kuzingatia majukumu haya ya msingi, na mbinu na
mikakati mbalimbali ya kuyatekeleza, Watanzania watarajie mambo kumi yafuatayo
katika miaka mitano ijayo:
·
Kwanza, Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa Amani,
Utulivu na Umoja wa nchi yetu na watu wake vinadumishwa;
·
Pili, Serikali ya Awamu ya Nne itadumisha na kuendeleza
mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi leo;
·
Tatu, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza vita dhidi ya
umaskini, ujinga na maradhi, tena kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya;
·
Nne, Serikali ya Awamu ya Nne itatimiza ipasavyo wajibu wake
wa utawala na maendeleo, na itaendesha dola kwa misingi ya utawala bora na
uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu;
itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ya woga wala kuoneana muhali.
·
Tano, Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha uwezo wake wa
kulinda maisha na mali za raia wake.
Tutapambana na uhalifu wa kila aina, na majambazi hayataachwa yatambe
yatakavyo;
·
Sita, Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha mipaka ya nchi
yetu ipo salama. Hatutamruhusu mtu au
nchi yeyote kuchezea mipaka ya nchi yetu na uhuru wetu;
·
Saba, Serikali ya Awamu ya Nne itafanya kila iwezalo
kuhakikisha Tanzania ina mahusiano mazuri na mataifa yote duniani, pamoja na
mashirika ya kimataifa na kikanda;
·
Nane, Serikali ya Awamu ya Nne itajali sana maslahi na
mahitaji ya makundi maalum katika jamii kama vile wanawake, vijana, watoto,
wazee, walemavu na yatima;
·
Tisa, Serikali ya Awamu ya Nne itaongoza mapambano mapya ya
kuhifadhi mazingira ili vizazi vijavyo virithi nchi nzuri, na msingi imara wa
maendeleo endelevu; na
·
Kumi, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza michezo, na
shughuli za utamaduni na burudani.
Umoja wa Kitaifa
Mheshimiwa Spika:
Umoja wa kitaifa wa Tanzania una pande mbili. Upande wa kwanza ni Muungano wetu; umoja wa
nchi zetu mbili huru zilizoungana kuunda Jamhuri ya Muungano. Muungano wetu sasa una zaidi ya miaka 41, ni
wa pekee barani Afrika. Pamoja na kuwepo
matatizo ya hapa na pale Muungano bado ni imara na ni wa kujivunia. Upande wa
pili wa umoja wa kitaifa ni umoja wa raia wenyewe, wanaojihisi wote ni
Watanzania kwanza, bila kujali tofauti zao za kabila, dini, rangi, jinsia au
eneo atokalo mtu.
Kazi mojawapo ya msingi ya Serikali
nitakayoiunda ni kulinda, kudumisha, kuendeleza na kuimarisha Muungano
wetu, kwa kufanya yafuatayo:
·
Kwanza, kwa jumla tutakuwa makini na wepesi katika
kushughulikia matatizo ya Muungano.
Tutayazungumza kwa uwazi na kuchukua hatua muafaka kwa wakati
muafaka;
·
Pili, nitampunguzia Makamu wa Rais majukumu ya kuondoa
umaskini ili apate muda wa kutosha wa
kushughulikia masuala ya Muungano;
·
Tatu, nitaimarisha taratibu zilizoanzishwa na Serikali
zilizopita za kujadili, kuainisha na kutatua matatizo ya Muungano; na
·
Nne, nitaangalia upya mchango wa Serikali ya Muungano katika
maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar, bila kuathiri haki na mamlaka
kamili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo ambayo si ya Muungano.
Mheshimiwa Spika:
Kwa upande mwingine, umoja wa Watanzania unahusu umoja
miongoni mwa wananchi. Ipo hofu ya kweli
miongoni mwa Watanzania kuwa bado wapo miongoni mwetu watu wanaotaka
kuturudisha tulikotoka, tuanze tena kuulizana na kubaguana kwa misingi ya
kabila zetu, rangi zetu, dini zetu, na maeneo tunayotoka. Nawasihi sana
wanaowania uongozi, kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ngazi ya kitaifa—uwe
uongozi wa kiserikali, uongozi wa kisiasa au uongozi wa kidini—wasitumie
ubaguzi wa aina yeyote ile.
Hawatavumiliwa na hawataachwa waigawe nchi.
Mheshimiwa Spika:
Nasononeshwa sana na mpasuko wa kisiasa kati ya Unguja na
Pemba. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2005
yamedhihirisha mpasuko huo ambao naamini chanzo chake ni cha kihistoria. Lakini
historia hiyo ni ya wanadamu, na wanadamu hawalazimiki kuwa wafungwa wa
historia yao. Iweje Wapemba hawa ambao
ni hodari wa kutumia fursa ya Muungano wetu kwa kuishi na kufanya biashara na
kuwekeza katika pembe zote za Jamhuri yetu wawe hao hao wanaojitenga kisiasa
kwa kiwango tulichoshuhudia kwenye Uchaguzi Mkuu?
Wakati umefika sasa
wa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko huo.
Nategemea ushirikiano mzuri kutoka kwa wanasiasa wa
Tanzania-Zanzibar. Natambua kuwa uamuzi
wa mwisho kuhusu hatma ya siasa na utawala Zanzibar ni wa Wazanzibari wenyewe.
Lakini, Jamhuri yetu ni moja, na yanayotokea Zanzibar yanatugusa sote. Pengine leo ni zaidi kuliko ilivyokuwa katika
historia wakati ulipokuwepo msemo kuwa
zumari likipigwa Zanzibar wanacheza mpaka bara. Hivyo, basi, nitakuwa tayari
kuanzisha, kuwezesha na kusaidia mjadala mpana juu ya mustakabali wa kisiasa
Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wabunge:
Serikali ya Awamu ya Nne inakusudia, miongoni
mwa mambo mengine, kuimarisha utaifa wetu kwa kufanya mambo kumi yafuatayo:
·
Kwanza, kutumia mfumo wa elimu kujenga na kuimarisha umoja wa
kitaifa, ikiwemo kutenga Shule za Sekondari za Kitaifa zitakazochanganya kwa
makusudi wanafunzi wenye vipaji mbalimbali kutoka pembe zote za Tanzania;
·
Pili, kuandaa mitaala ya somo la uraia itakayopanda mbegu za
uzalendo na umoja wa kitaifa katika ngazi zote za elimu;
·
Tatu, kuzipa changamoto shule za mashirika ya dini, isipokuwa
seminari, kupokea wanafunzi wa dini zote;
·
Nne, kuendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu
ya Tatu ya kufufua Jeshi la Kujenga Taifa;
·
Tano, kujenga muafaka baina ya vyama na makundi ya jamii juu
ya utambuzi wa, na kuheshimu, tunu za kitaifa kama vile haki, usawa, umoja na
mshikamano;
·
Sita, kutumia michezo, nyimbo na sanaa kuimarisha hisia za
utaifa na kujenga uzalendo na kuipenda nchi;
·
Saba, kueneza na kuruhusu matumizi ya alama za kitaifa kama
mambo ya kila raia kujivuna nayo na kuyaheshimu sana;
·
Nane, kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya dini, vyama vya
siasa na makundi mbalimbali ya jamii;
·
Tisa, kuteua Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais
atakayeshughulikia mahusiano kati ya vyama vya siasa, dini na makundi
mbalimbali ya jamii; na
·
Kumi, kuimarisha utaratibu wa mazungumzo ili kutatua mapema
migogoro katika jamii.
Amani na Utulivu
Mheshimiwa Spika:
Zipo sababu kwa nini nchi
yetu imekuwa, kwa kiwango kikubwa, kisiwa cha amani na utulivu katika bahari
iliyotibuka. Mojawapo ya sababu hizo, kama nilivyosema, ni sera ambazo kwa
makusudi zilijenga hisia za umoja, na hazikuwabagua wala kuwanyima haki
Watanzania kwa sababu za dini, rangi, kabila, jinsia au eneo wanakotoka. Nitawatarajia watakaokuwa kwenye Serikali
nitakayoiunda wasiwabague wananchi kwa sababu yoyote ile, na wawe watetezi thabiti wa haki za
binadamu. Ningependa pia tuwe na maadili na miiko ya kitaifa kuhusu
jambo hili.
Utawala Bora
Mheshimiwa Spika:
Serikali nitakayoiongoza itazingatia na kuendeshwa kwa misingi ya utawala
bora, uwazi na uwajibikaji. Tutaheshimu
utawala wa sheria, na tutazingatia na kuheshimu mgawanyo wa madaraka kati ya
mihimili mikuu ya dola, yaani Utawala, Bunge na Mahakama. Tutaheshimu uhuru wa Mahakama na Bunge;
tutatimiza ipasavyo wajibu wetu; na tutawezesha mihimili hiyo kufanya kazi zake
ipasavyo. Serikali ya Awamu ya Nne
itaimarisha utendaji Serikalini na kupambana na maovu katika jamii bila woga
wala kuoneana muhali.
Tutaongeza kasi ya kupambana na rushwa
kisayansi kwa kushambulia kiini chake, na kuziba mianya yake. Tutajitahidi kuongeza mishahara na kuboresha
maslahi ya watumishi wa umma ili kupunguza vishawishi vya rushwa. Tutaendelea
pia kuongeza uwazi katika maamuzi ya Serikali hasa katika manunuzi na mikataba.
Tutaimarisha uwezo wa kifedha na kiutendaji wa taasisi zilizo mstari wa mbele
kwenye vita dhidi ya rushwa, hususan Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Jeshi la Polisi
na Mahakama. Lakini yote hayo ni bure
iwapo wananchi hawatajitokeza kusaidia vyombo hivyo. Naomba ushirikiano huo kutoka kwa wananchi.
Katika harakati za
kupambana na rushwa yapo mambo mawili mengine ambayo tutayaangalia kwa
karibu. La kwanza ni mikataba. Tutaangalia upya taratibu za mikataba
mbalimbali inayoingiwa na Serikali, mashirika ya umma na idara zinazojitegemea
kwa nia ya kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Mikataba ni mwanya mkubwa wa rushwa hasa zile kubwa kubwa za wanaotafuta
utajiri.
Kadhalika, hatuna budi kuchukua
hatua thabiti za kuzuia watumishi wa umma kutumia nafasi zao kujitajirisha na
kujilimbikizia mali. Sisemi kwamba ni
haramu mtu kuwa tajiri au kuwa na mali.
Ninachosema mimi kuwa ni haramu ni kutumia nafasi yako ya utumishi au
uongozi wa umma kujipatia manufaa ya kujitajirisha au kujilimbikizia mali.
Jambo hili ndilo
linalokera sana watu kuona mtu ambaye hana chochote lakini miezi michache tu
baada ya kupata cheo anakuwa tajiri mkubwa. Ona majumba ya fahari, ona
madaladala, teksi bubu, anaishi maisha ya kifahari na kadhalika. Wananchi
wanayo haki kuhoji, na wanayo haki kupata majibu. Ndugu zangu, naomba tuwe waadilifu. Tusilaumiane. Nataka Tume ya Maadili ya
Viongozi isione haya kutuuliza jinsi tulivyozipata mali tunazosema tunazo.
Nitawasaidia kujenga uwezo wa kufanya hivyo kama tatizo lenu ni hilo.
Mheshimiwa Spika:
Dhana ya utawala bora ni pana sana; ni zaidi ya vita
dhidi ya rushwa. Tutahimiza utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ustadi, kwa
haraka na kwa ufanisi. Tunataka
watendaji wa Serikali wenye wawe waadilifu, na wanaowajibika; wawe na ari,
moyo, na msimamo wa dhati kuhusu utumishi wa umma na huduma bora kwa umma. Tabia ya “Njoo kesho” na nenda rudi tuache. Mwalimu alituasa linalowezekana leo lisingoje
kesho. Napenda huo uwe moyo wa utendaji
Serikalini.
Natambua tatizo na
malalamiko ya watumishi wa umma kuhusu mishahara na maslahi yao. Tutaliangalia. Tutalishughulikia. Nakusudia mapema iwezekanavyo niteue Tume ya
Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa Umma.
Naomba niwatahadharishe kutokana na matumaini ya miujiza. Tutafanya kinachowezekana kadri uwezo wa
Serikali unavyojengeka.
Mheshimiwa Spika:
Serikali nitakayoiunda, pamoja na kuheshimu uhuru wa
Mahakama, itatimiza ipasavyo wajibu wake na kuimarisha miundombinu ya kutoa
haki kwa kuongeza idadi ya watumishi, kuwaendeleza kitaaluma, kukarabati
majengo yaliyopo na kujenga mapya, na kupeleka huduma za utoaji haki karibu
zaidi na wananchi.
Mheshimiwa Spika:
Kusimamia vizuri mapato na matumizi
ya Serikali nayo ni sehemu ya utawala bora. Isitoshe, utekelezaji mzuri wa
jukumu hilo ndio unaipa Serikali uwezo wa kutekeleza mengine yote inayopaswa au
inayokusudia kuyatekeleza. Serikali ya Awamu ya Tatu, chini ya uongozi shupavu
wa Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, iliongeza mapato ya Serikali mara tano
sambamba na kuweka mfumo mpya na wa kisasa wa kudhibiti matumizi, na kuongeza
uwazi katika bajeti ya Serikali. Hatutalegeza
kamba hata kidogo. Hatutavumilia wanaokwepa kulipa kodi stahiki za Serikali au
wabadhirifu wa fedha na mali za umma. Sheria ya Fedha, na Sheria
ya Manunuzi ya Umma, lazima zifuatwe.
Watakaokiuka wachukuliwe hatua za nidhamu. Wasiorejesha masurufu ya
safari nao wasivumiliwe.
Mheshimiwa Spika:
Utawala bora ni
pamoja na Serikali kufanya vizuri kazi zake nyingine muhimu katika mazingira ya
uchumi wa soko. Jukumu la msingi la Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri
kwa uchumi kukua na biashara kustawi. Kwa sababu hiyo, Serikali ya Awamu ya Nne
itatekeleza mambo manane yafuatayo:
·
Kwanza, kuweka sera na mazingira bora ya kuvutia uwekezaji
kutoka ndani na nje ya nchi;
·
Pili, kuweka sera nzuri zinazowezesha ukuaji wa uchumi wa
kisasa;
·
Tatu, kuweka mfumo mzuri wa usimamizi wa mazingira ili
kulinda uhai wa binadamu na viumbe hai;
·
Nne, kuweka mifumo bora ya kusuluhisha haraka migogoro ya
kibiashara;
·
Tano, kuweka utawala mzuri wa sheria na wa haki;
·
Sita, kuwa na taasisi za kudhibiti na kusimamia viwango vya
huduma na bidhaa;
·
Saba, kuwa na sera nzuri za kifedha ili kuhamasisha uwekezaji
na uzalishaji; na
·
Nane, kutekeleza kwa dhati sera ya uwezeshaji wa wazawa.
Uchumi Endelevu wa Kisasa Unaokua
Mheshimiwa
Spika:
Serikali
ninayoiongoza itatoa kipaumbele katika kujenga uchumi endelevu, wa kisasa,
unaokua. Serikali ya Awamu ya Tatu
imefanya kazi kubwa katika eneo hilo, na kutuachia msingi imara ambao sisi
tutajenga juu yake. Hatutabomoa msingi
huo bali Serikali itatumia mafanikio hayo kama nyenzo ya kuongeza kasi ya
ukuaji wa uchumi wetu.
Mheshimiwa
Spika:
Sekta
binafsi ndiyo mhimili wa uchumi wa nchi yetu hivi sasa. Serikali ya Awamu ya Tatu imeweka mazingira
mazuri ya ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa Taifa. Aidha, Serikali ya Awamu ya Tatu imejenga
mahusiano mazuri na sekta binafsi ambayo sasa imepewa fursa ya kushirikiana na
Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza kazi
hiyo nzuri. Tutajitahidi kuwa karibu na
sekta binafsi kwa maslahi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika:
Kilimo ndiyo sekta
inayoajiri watu wengi na ndiyo inayotuhakikishia upatikanaji wa chakula, bidhaa
za kuuza nje na malighafi za viwanda.
Vilevile, uhai na maendeleo ya sehemu kubwa ya wananchi yanategemea
kilimo. Hivi sasa, Serikali inatoa ruzuku kwenye mbolea na vilevile unafuu wa
kodi kwenye pembejeo za kilimo na mifugo. Mpango huo utaendelezwa na
kuimarishwa zaidi.
Aidha, Serikali
itahakikisha kuwa Mpango Kabambe wa Umwagiliaji Maji unaongezewa fedha na
wataalam. Tutahakikisha kuwa utaalam wa
asili wa kilimo cha umwagiliaji unafufuliwa, pamoja na miundombinu yake. Huduma muhimu za ugani na masoko zitapewa
kipaumbele na msukumo maalumu.
Mheshimiwa Spika:
Tutachukua hatua za
dhati kuboresha ufugaji wetu. Hatuna
budi tutoke kwenye uchungaji wa kuhama-hama na kuwa wafugaji wa kisasa. Tutachukua hatua za kuboresha malisho na
huduma za madawa, majosho na minada.
Tanzania ina mifugo
mingi sana, na tukiboresha ufugaji, itatoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa
na maendeleo ya wafugaji. Serikali pia
itawawezesha wavuvi wengi iwezekanavyo kupata zana bora na vifaa muhimu vya
uvuvi wa kisasa ili waweze kutumia kwa ukamilifu eneo la bahari, maziwa na mito
ambalo tumejaliwa kuwa nayo.
Mheshimiwa Spika:
Katika maendeleo, uchumi wa taifa siku zote unaongeza
mchango na viwanda katika pato la taifa.
Nasi hatuna budi tufanye hivyo. Viwanda—vikubwa, vidogo na vya kati—vina
uwezo mkubwa wa kukuza uchumi, kutoa nafasi za ajira, lakini vilevile
vinasaidia kusindika mazao ya kilimo, kuyaongezea thamani na kuzuia
yasiharibike wakati wa mavuno. Serikali ya Awamu Nne itatengeneza mkakati
kabambe wa kutekeleza sera ya viwanda nchini.
Tutachukua hatua za makusudi za kukuza sekta ya viwanda nchini.
Serikali itaendeleza
na kuimarisha utoaji wa mikopo kwa viwanda vidogo na vya kati chini ya mpango
wa mikopo, na dhamana kwa mikopo, kwa sekta hiyo ambao unasimamiwa na Benki Kuu
ya Tanzania. Shirika la Viwanda Vidogo
nalo litapewa uwezo zaidi wa kumudu kazi za kutoa elimu, ushauri, uwezeshaji na
usimamizi.
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya
Nne itahimiza matumizi ya sayansi na teknolojia, na kuwekeza katika utafiti.
Aidha, Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kuwa fedha
zinapatikana kwa ajili ya taasisi na asasi mbalimbali zinazoshughulikia utafiti
wa kiteknolojia. Mfuko wa Taifa wa Sayansi na Teknolojia utaimarishwa kwa
kuongeza mchango wa Serikali na kuwahamasisha wadau wengine kuchangia.
Mheshimiwa Spika:
Teknolojia ya habari na mawasiliano imewezesha elimu, taarifa na habari kuvuka mipaka na
hivyo kusaidia kupunguza pengo la habari na elimu lililopo kati ya nchi
zilizoendelea na zile zinazoendelea.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, tutaongeza kasi ya kuandaa
mazingira yatakayotuwezesha kutumia teknolojia hii.
Uchumi
Unaoshirikisha Raia Wengi
Mheshimiwa Spika:
Mageuzi ya uchumi
yameongeza tofauti ya mapato miongoni mwa wananchi. Tofauti hizo zisiposhughulikiwa zinaweza kuwa
chanzo cha migogoro na mitafaruku katika jamii.
Jawabu si
kuwanyang’anya walio nacho na kuwagawia wasio nacho. Jawabu sahihi ni kuwasaidia wasio nacho
wajikwamue, na wainue hali za maisha yao.
Changamoto kubwa ni jinsi gani tunaongeza fursa kwa wasio nacho, na
kuchochea utayari wao kutumia fursa hizo.
Mheshimiwa
Spika:
Kurekebisha na kutengemaza uchumi ni hatua ya mwanzo tu katika safari
ndefu ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Serikali ya Awamu ya Nne itaendelea na hatua inayofuata ya kuongeza
ushiriki wa Watanzania walio wengi katika uchumi wa Taifa lao. Wakati wa
Serikali ya Awamu ya Kwanza juhudi zilikuwa kuwafanya wananchi wamiliki uchumi
wa Taifa lao kupitia mashirika ya umma. Leo tunataka kufikia lengo hilo hilo la
wananchi kumiliki sehemu kubwa ya uchumi wa Taifa lao, moja kwa moja, au
kupitia vyama huru vya ushirika.
Mheshimiwa Spika:
Kwa kifupi Serikali
ya Awamu ya Nne itaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa ajili ya
wafanyabiashara na wawekezaji wadogo wadogo,
kwa kuchukua hatua zifuatazo:-
·
Kwanza, kuandaa utaratibu mzuri zaidi wa kutoa leseni za
biashara;
·
Pili, kurekebisha mifumo ya udhibiti ili udhibiti usizuie
sekta binafsi kukua;
·
Tatu, kuandaa mazingira mazuri ya kufikisha taarifa muhimu
kuhusu masoko, kuhusu ubora wa viwango vinavyotakiwa, na kuhusu masharti
mengineyo kwa wafanyabiashara na hasa wafanyabiashara wadogo na wa kati;
·
Nne, kuitaka mikoa ianzishe vituo vya kufanikisha biashara na
uwekezaji mikoani, pamoja na Mabaraza ya Biashara ya Mikoa;
·
Tano,
kuboresha mazingira ya biashara na ujasiriamali, ikiwemo kutoa msaada na
upendeleo maalum kwa mikopo midogo midogo na ya kati hasa kwa vijana, wanawake
na Watanzania wanaohangaika kujikwamua kimaisha;
·
Sita,
kuboresha miundombinu inayogusa shughuli za wafanyabiashara wadogo na wa kati;
·
Saba,
kuhamasisha, kuhimiza na kutoa motisha kwa shughuli za usindikaji nchini ili
kuongeza thamani ya mauzo nje; na
·
Nane, kuhamasisha, kuhimiza na kutoa motisha kwa mafunzo ya
ufundi ili kuongeza tija na ufanisi.
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Nne itaongeza kasi ya kupambana na
umaskini. Tutawezesha Watanzania kwa
makundi. Kundi la kwanza ni la
Watanzania wasomi, walio ndani au nje ya nchi yetu. Zamani ilikuwa mtu ukitoka Chuo Kikuu, kazi
ya Serikali inakungoja. Leo hali si
hiyo. Wengi inabidi watafute kazi kwenye
sekta binafsi, au wajiajiri wenyewe.
Napenda leo nitoe changamoto na ahadi kwa wasomi wetu
hao, wenye fani mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, uvuvi, uhandisi, ubunifu
wa majengo, sheria, uhasibu na kadhalika.
Katika dunia ya utandawazi na ushindani unaoambatana nao, Watanzania
wasomi watabaki nje iwapo hawatakuwa wabunifu zaidi, wakaungana na kuanzisha
kampuni kubwa za wazalendo.
Lakini wakikubali
kuungana, na kuanzisha kampuni kubwa zinazoendeshwa kwa misingi halisi ya
kibiashara, na sio ubabaishaji, Serikali, kupitia vyama vya taaluma zao,
itawaunga mkono, itawasaidia na itawawezesha.
Serikali ya Awamu ya Nne itakaribisha mawazo kutoka kwa vyama vya
kitaaluma juu ya namna bora ya Serikali kufikia lengo hilo. Ninataka wasomi
wetu wawe kiini cha wajasiriamali wasomi na wakubwa nchini.
Kundi la pili la Watanzania tutakaowasaidia na
kuwawezesha ni la wenye miradi midogo sana, miradi midogo na miradi ya ukubwa
wa kati. Mazuri mengi yamefanywa na
Serikali ya Awamu ya Tatu, kama vile sera ya uwezeshaji wananchi, sera ya
uwekezaji mdogo na wa kati, na mfuko wa udhamini kwa mikopo ya mitaji midogo na
ya kati. Yote haya, na mengine mengi,
tutayaendeleza kwa jitihada kubwa.
Kundi la tatu ni la wakulima wadogo, wavuvi wadogo na
wafugaji wadogo. Hatuwezi kushinda
umaskini bila kuwasaidia watu wa kundi hili ambao ndio wengi zaidi. Nitahitaji kuona ubunifu wa hali ya juu kutoka
kwa nitakaowakabidhi kusimamia sekta hizi kufanikisha azma yetu hii.
Mheshimiwa Spika:
Yote haya yatawezekana tu iwapo Watanzania watabadili
mtazamo wao kuhusu nafasi yao, na nafasi ya Serikali, katika kukuza uchumi wa
Taifa na uchumi binafsi. Waswahili husema, ukibebwa na wewe shikilia. Maisha
bora hayaletwi na Serikali peke yake; yanaletwa kwa ubia kati ya Serikali na
wananchi. Naomba tuimarishe ubia huo katika Awamu ya Nne ya Uongozi wa Taifa
letu.
Ajira na Viwanda
Mheshimiwa Spika:
Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM tulijiwekea lengo la
kuongeza nafasi za ajira milioni moja katika kipindi cha miaka mitano
ijayo. Nafasi hizi za ajira zinatarajiwa
kupatikana Serikalini na katika sekta binafsi.
Upanuzi wa sekta za afya, elimu, kilimo, ujenzi wa nyumba na barabara,
usindikaji wa mazao na bidhaa asilia, samaki, na utalii ndilo tumaini kuu la
ajira. Aidha, matarajio mengine makubwa
ya ajira ni kutoka katika sekta isiyo rasmi, yaani ajira binafsi. Tunasisitiza ahadi yetu ya kuchukua hatua
thabiti za kuwasaidia vijana, wanawake na Watanzania kwa jumla kupata mikopo na
mitaji ya kuwawezesha kujiajiri. Lengo
letu ni kuwa kila raia awe na chanzo cha uhakika cha kipato, na kuibua maeneo
mapya ya kuwapatia ajira wananchi wengi zaidi.
Serikali ya Awamu
ya Nne itaendeleza pia juhudi za kuhimiza, na kuwezesha, uanzishwaji wa viwanda
vidogo, vya kati na vikubwa kama vile vya nguo na vya kuunganisha bidhaa za
matumizi ya nyumbani vyenye uwezo mkubwa wa kutoa nafasi za ajira. Serikali ya Awamu ya Tatu ilibuni mradi
uitwao Tanzania Mini-Tiger Plan 2020 ambao kwa kutumia maeneo maalum ya uchumi
utaongeza mauzo nje ya nchi, na kuongeza haraka nafasi za ajira. Serikali ya Awamu ya Nne itautekeleza mradi
huo kwa ukamilifu.
Mheshimiwa Spika:
Ushirika ni nguzo muhimu ya kuwawezesha wanyonge kuwa na
sauti na hivyo kuweza kupambana na umaskini.
Serikali ya Awamu ya Tatu imefanya kazi kubwa na nzuri ya kuunda upya
ushirika nchini kwa kuhuisha sera na sheria ili kuweka mazingira
yatakayochochea kujengeka kwa vyama huru vya ushirika vinavyomilikiwa na
kuendeshwa na wanaushirika wenyewe. Serikali ninayoiongoza itaendeleza juhudi
hizo pamoja na kuendelea kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kujiunga na
vyama hivyo.
Huduma ya Jamii
Kuendeleza huduma za jamii
kama vile elimu, afya, maji na kadhalika itaendelea kuwa kipaumbele cha juu cha
Serikali ya Awamu ya Nne.
Elimu
Mheshimiwa Spika:
Kazi kubwa ya
kupanua miundombinu ya elimu nchini imefanyika katika miaka kumi iliyopita
chini ya Serikali ya Awamu ya Tatu.
Uandikishaji wa wanafunzi, wa kike na wa kiume, katika ngazi zote za
elimu umeongezeka sana. Elimu itakuwa
agenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Nne, ambayo itafanya yafuatayo:-
·
Kwanza, kuendelea
kuandikisha watoto wote wa rika lengwa la kuanza shule;
·
Pili, kuboresha taaluma ili kuongeza viwango vya kufaulu;
·
Tatu, kuongeza ajira ya walimu wa elimu ya msingi na
sekondari;
·
Nne, kushirikiana na wazazi na wadau wengine wa elimu kujenga
vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo;
·
Tano, kuongeza ruzuku inayotolewa hivi sasa kwa ajili gharama
za kuendesha shule;
·
Sita, kuimarisha taasisi za kudhibiti ubora wa elimu
inayotolewa;
·
Saba, kutoa fursa na motisha kwa sekta binafsi, taasisi za
dini na mashirika binafsi yanayowekeza katika elimu;
·
Nane, kuimarisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili iweze
kutoa mikopo kwa wahitaji wengi zaidi;
· Kumi,
kuhakikisha kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanaendelezwa na kuimarishwa kama
mkakati wa kupambana na tatizo la ajira.
· Kumi
na moja, kuboresha maslahi ya walimu katika shule na vyuo hapa nchini.
Maji
Mheshimiwa Spika:
Tatizo la maji ndicho kilio kikubwa cha Watanzania
mijini na vijijini. Ndiyo kero nambari
wani. Serikali za awamu zote zimefanya
jitihada kubwa kukabiliana na tatizo hilo.
Serikali ya Awamu ya Nne inakusudia kulikabili tatizo hili kwa ari mpya,
nguvu mpya na kasi mpya.
Ni makusudio yangu
kuwa tuwe na Mpango Kabambe wa Maji kwa nchi nzima. Mpango ambao utajumuisha mikakati na mbinu
mpya za kutekeleza kwa kasi Sera ya Maji na kutatua tatizo la maji. Aidha, tutakamilisha miradi mikubwa ya
ukarabati na upanuzi wa Majisafi na Majitaka Dar es Salaam, na ule wa kupeleka
maji katika miji ya Kahama, Shinyanga na vijiji vitakavyopitiwa na bomba kutoka
Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Tatu imechukua hatua mbalimbali
kuboresha sekta ya afya, na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Tutaendeleza hatua hizo. Huduma ya afya
kwa kina mama na chanjo mbalimbali kwa watoto zitaendelea kutolewa na
kuboreshwa zaidi. Tunataka kila mtoto wa Kitanzania apate chanjo zote
zinazostahili.
Aidha, tutaimarisha mtandao wa kusambaza dawa katika
hospitali, vituo vya afya na zahanati, pamoja na kuendelea kuongeza bajeti ya
ununuzi wa dawa na vifaa vya tiba.
Ukarabati na ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati
utaendelea. Kwa kutambua kuwa kinga ni
bora kuliko tiba tutakazania pia elimu ya afya.
Mapambano dhidi ya malaria na kifua kikuu yatapewa msukumo maalum.
Mheshimiwa
Spika:
Nchi yetu inakabiliwa
na tatizo kubwa la UKIMWI. UKIMWI ni
janga la kitaifa na dunia kwa ujumla. Janga hili limekuwa likiathiri utendaji
na kupunguza nguvukazi ya Taifa. Tutaendeleza jitihada za kuhamasisha na kutoa
elimu ya UKIMWI kwa wananchi wote ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anao
uelewa sahihi wa janga hili. Aidha,
Serikali itatenga rasilimali zaidi, na kushirikiana na wadau mbalimbali,
kuongeza upatikanaji wa dawa za kurefusha maisha na kupunguza makali kwa watu
wengi zaidi walioathirika na UKIMWI.
Makundi Maalum
Mheshimiwa Spika:
Katika jamii yetu yapo makundi maalum ambayo Serikali
inao wajibu wa kuwasaidia. Kundi la
kwanza ni la watoto yatima. Tunahitaji
wadau mbalimbali wakae pamoja na kuandaa mipango endelevu ya kuwalea na kuwasaidia
watoto hawa. Watoto yatima wanahitaji
elimu, lishe bora, huduma za afya, makazi na upendo sawa na watoto wengine wa
Kitanzania. Serikali ya Awamu ya Nne
inaahidi kuwa yatima watapata elimu na huduma ya afya kwa kusaidiwa na
Serikali.
Mheshimiwa Spika:
Kundi jingine maalum ni lile la walemavu. Zipo hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa
kuwapa fursa walemavu kutumia vipaji vyao ili kujitegemea. Changamoto kubwa kwetu kama Taifa ni kuwa
tuache kuwanyanyapaa na tuwaone kuwa ni binadamu wenzetu. Serikali itachukua hatua za kuhuisha sera na
sheria ili kutoa upendeleo maalum kwa walemavu katika utoaji wa huduma
mbalimbali na vilevile katika kuweka mazingira yatakayowapa fursa ya kutekeleza
majukumu yao kwa jamii.
Mheshimiwa
Spika:
Lipo pia kundi la wazee wetu. Wazee ni hazina kubwa ya Taifa lolote. Jamii
yeyote iliyostaarabika inalo jukumu la kuwaenzi na kuwatunza wazee, tukianza na wanafamilia na wanajamii wa
karibu wa mzee anayehusika. Wasikwepe
jukumu hilo asilia, na la mila za Kiafrika.
Serikali itahakikisha kuwa kunakuwepo utaratibu na mipango
itakayowawezesha wazee kupata huduma muhimu kwa wepesi zaidi na kwa gharama
nafuu, kwa kuzingatia taratibu, mila na
utamaduni wa jamii zetu.
Mheshimiwa
Spika:
Serikali itazingatia nafasi ya wanawake katika maendeleo.
Tutaongeza, awamu kwa awamu, ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za
uongozi wa kisiasa, kiutendaji na nafasi nyingine za maamuzi. Kadhalika,
tutatekeleza ahadi ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Mheshimiwa Spika:
Serikali yangu inakusudia kuendeleza sekta ya utalii ili iongeze mchango
wake kwenye pato na maendeleo ya taifa letu. Tunapaswa kuboresha huduma
kwa watalii kama vile malazi, chakula, usafiri na bidhaa za kumbukumbu za
kuwauzia watalii. Tunapaswa kukaribisha
wawekezaji wa ndani na nje watakaojenga hoteli zenye hadhi ya kimataifa kuanzia
nyota nne hadi tano. Tunahitaji kujenga miundombinu ya kuwafikisha watalii
katika maeneo ya kitalii kwa urahisi.
Hifadhi
ya Mazingira
Mheshimiwa
Spika:
Serikali ya Awamu ya Nne itatoa msukumo maalum
kwa hifadhi ya mazingira kwani athari zake pale tulipopuuzia zinaonekana
wazi. Mvua haba, raslimali maji inazidi
kupungua, na ukame unaongezeka. Serikali
itaendelea kuthamini na kulizingatia suala hili, pamoja na kutoa elimu kwa
wananchi ili kuongeza uelewa wao kuhusu hifadhi ya mazingira. Tutaiongezea
Wizara inayohusika na mazingira uwezo na mamlaka ya usimamizi. Tutaendeleza
kampeni ya upandaji miti na kuhimiza tabia ya kutokata miti ovyo, au kuchoma
misitu ovyo. Ili kupunguza mahitaji ya
kuni na mkaa tutaendeleza matumizi ya nishati mbadala.
Miaka arobaini tu iliyopita,
Tanzania Bara ilikuwa bado na misitu mingi, chemchem na vijito vingi. Sehemu
kubwa ya ardhi yake ilikuwa imefunikwa na majani. Leo hali ni tofauti, na kwenye baadhi ya
maeneo hali inatisha.
Mheshimiwa Spika:
Uchomaji misitu na ukataji ovyo wa miti vimesababisha vyanzo vya maji kukauka, mito kupungua maji na baadhi ya viumbe kuathirika na kutoweka. Hatuwezi kuendelea kuwa watazamaji au washangaaji wa vitendo hivi vya hujuma dhidi ya misitu na uhai wa taifa letu. Na wala uhuru wa Mtanzania kuishi popote katika nchi yake haujumuishi pia uhuru wa kuharibu mazingira sehemu fulani na kuhamia sehemu nyingine.
Mheshimiwa
Spika:
Yapo maeneo
ambayo lazima zichukuliwe hatua maalum za kulinda na kuhifadhi mazingira kwani hali imeanza kuwa mbaya sana.
Eneo mojawapo ni Bonde la Mto Ruaha ambalo linahusisha vyanzo vya mito yote
mikubwa nchini. Tumeshuhudia hali ya
bwawa la Mtera inavyoendelea kuwa mbaya.
Aidha, mto Ruaha Mkuu umeanza kukauka katika baadhi ya maeneo. Itabidi uongozi wa Serikali katika ngazi zote
uwajibike zaidi kuhakikisha kuwa uharibifu wa mazingira unaosababisha hali hii
ya kutisha unakomeshwa.
Eneo jingine ni lile
linalozunguka Ziwa Victoria. Taarifa za kitaalamu zinaonyesha kuwa pamoja na
umuhimu wa ziwa hilo, uchafuzi wake unaongezeka. Serikali itahakikisha kuwa uongozi wa mikoa
yote inayozunguka ziwa hilo unashirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa na
wananchi kuhifadhi ziwa hilo linalotegemewa na idadi kubwa ya wananchi
wetu.
Uchumi Unaopaa
Mheshimiwa Spika:
Baada ya mafanikio
ya Awamu ya Tatu, haitarajiwi kuwa Serikali ya Awamu ya Nne italegeza kamba na
kupuuza misingi iliyotuletea mafanikio tunayojivunia. Najua mengi yamesemwa na
watu wanaodai wanamfahamu Jakaya Mrisho Kikwete na jinsi atakavyolegeza
mambo. Napenda kuwahakikishieni kuwa
watu hao wamepotea sana.
Wakati wa kampeni
wapo baadhi ya wapinzani waliothubutu, kwa kukosa shukrani, kusema ati Serikali
ya Awamu ya Tatu ilikuwa inatekeleza sera zinazobuniwa Washington. Serikali ya Awamu ya Nne haitaogopa kubuni na
kutekeleza sera na mikakati ya maslahi kwa ukuaji wa uchumi na maisha bora kwa
kila Mtanzania ati kwa vile zinaungwa mkono au kufadhiliwa na nchi tajiri na
mashirika ya fedha ya kimataifa.
Hatutafanya lolote lisilo na maslahi kwa taifa letu kwa
kuwaogopa au kutaka kujipendekeza kwa wakubwa hao. Lakini vile vile hatutaacha kufanya lolote la
maslahi kwa taifa na Watanzania kwa vile tu linaenda sambamba na ushauri wa
mashirika ya fedha ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika:
Mbali ya kusukumwa
na hoja ya kukuza uchumi haraka ili kupiga vita umaskini, tunasukumwa pia na
ukweli wa nguvu za utandawazi na ushindani mkubwa katika masoko ya kanda na ya
kimataifa. Hivyo basi, sote tuunganishe
nguvu zetu ili tuongeze uzalishaji, tuongeze uwekezaji, tuongeze mauzo nje,
tuongeze ubora wa mazao na huduma zetu na tuongeze kasi ya ukuaji wa uchumi
wetu ili upae.
Mheshimiwa
Spika:
Michezo ni furaha. Michezo ni muhimu kwa afya zetu. Watanzania wanapenda sana michezo, ila furaha imekuwa inawakwepa kwa timu zetu kutokufanya vizuri. Lazima tutoke huko na inawezekana. Tutahimiza maendeleo ya michezo shuleni na pale inapowezekana katika sehemu za kazi. Shule ziwe mahali pa kubaini vipaji vya sanaa na michezo na kuiendeleza.
Tutaviwezesha vyama mbalimbali vya michezo ili Tanzania iweze kuwa mshiriki vizuri, na siyo kuwa msindikizaji, katika mashindano mbalimbali ya michezo ulimwenguni. Pamoja na hayo nitaanzisha mjadala wa kitaifa wa kuendeleza michezo nchini. Wadau wote washiriki, na Watanzania, tukubaliane juu ya mstakabali wa michezo nchini mwetu.
Tutaendeleza sekta ya utamaduni na burudani kwa jumla. Miongoni mwa mambo ambayo tutayaangalia kwa karibu ni haki na maslahi ya wasanii ili kazi kubwa waifanyayo iwe na tija kwao.
Mheshimiwa Spika:
Lugha ya Kiswahili imeanza kupata umaarufu Afrika na duniani.
Mheshimiwa
Spika:
Kuendeleza miji ni jambo tutakalolipa uzito unaostahili
ili tuwe na miji mizuri, safi na salama. Sote tumeona jinsi ambavyo dhana ya
mipango miji inavyopuuzwa na kukiukwa na baadhi ya wananchi wetu, manispaa na
halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika:
Tusipozuia hali hiyo, miji yetu itakuwa kama pori la
majengo yasiyo na mpangilio wala huduma zinazohitajika. Serikali ya Awamu ya
Nne itazitaka Halmashauri zote zishughulikie jambo hili haraka inavyowezekana.
Tutaangalia uwezekano wa kuanzisha upya chombo cha fedha
kitakachotoa mikopo ya kujenga na kununua nyumba.
Kuendeleza huduma za kiuchumi za barabara, nishati, simu
na kadhalika itakuwa agenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Nne. Serikali za
Awamu zilizotangulia zilisimamia ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikijumuisha
barabara, vivuko na madaraja. Kwa kuzingatia hoja ya kuunganisha nchi na kuibua
maeneo mapya yenye uwezo wa kiuchumi, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza kwa
kasi upembuzi yakinifu, usanifu, na ujenzi wa barabara na madaraja yote
yaliyoorodheshwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005. Tutauimarisha Mfuko wa Barabara ili uendelee
kuwa nyenzo muhimu ya kuboresha huduma ya barabara nchini.
Mheshimiwa
Spika:
Nishati ni sawa na chembe za damu mwilini. Tutapanua wigo na aina ya vyanzo vya umeme na
nishati kwa jumla ili kuwa na nishati ya kutosha na yenye gharama nafuu kukidhi
mahitaji ya uzalishaji viwandani, utoaji wa huduma za kijamii, na matumizi ya
nyumbani. Tutayashughulikia kwa
kipaumbele cha juu matatizo ya sasa yahusuyo upatikanaji wa umeme nchini.
Mheshimiwa
Spika:
Ilani
ya CCM ya Uchaguzi wa Oktoba 2005 inasema wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Nne itaharakisha mradi wa kupata umeme kutoka makaa
ya mawe ya Mchuchuma. Na hivyo
ndivyo tutakavyofanya. Aidha, Serikali ya Awamu ya Nne itafufua mipango ya umeme wa Mto Rusumo na Stigler’s Gorge. Vile vile tutaharakisha upatikanaji wa umeme
kutoka gesi asilia ya Mnazi Bay.
Mheshimiwa
Spika:
Lengo la Serikali ya Awamu
ya Nne pia ni kuendeleza kazi ya kufikisha umeme katika miji mikuu ya wilaya
isiyo na umeme hivi sasa, kuongeza kasi ya kupeleka umeme vijijini kupitia
Mfuko wa Nishati Vijijini, na kuiunganisha Mikoa ya Kigoma na Ruvuma katika
gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika,
Awamu ya Kwanza ya uongozi wa nchi yetu iliweka misingi endelevu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Misingi hiyo ni ujirani mwema, ulinzi wa mipaka yetu, kuwasaidia wakimbizi na kuwa mtetezi wa wanyonge. Awamu zilizofuatia zimefanikiwa kuendeleza misingi hiyo. Serikali ya Awamu ya Nne nayo itaendeleza misingi hiyo pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje ambayo inalenga zaidi kwenye diplomasia ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika:
Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza kwa dhati mazungumzo ya kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki litakalotunufaisha sote sawia. Serikali ya Awamu ya Nne pia itaendeleza ushiriki wetu na uhusiano wetu na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizopo Kusini mwa Afrika (SADC).
Tutahakikisha pia kuwa Tanzania inaendelea kushiriki kwa ukamilifu na kuwa mwanachama mwaminifu wa Umoja wa Afrika, inaendelea kushiriki kwa ukamilifu katika utatuzi wa migogoro Barani Afrika, na hususan katika mchakato wa amani na maendeleo kwenye Kanda ya Maziwa Makuu.
Mheshimiwa Spika:
Tanzania itaendelea
kushiriki kwa ukamilifu kwenye shughuli za Umoja wa Mataifa. Hivi sasa nchi yetu ni mwanachama wa Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuanzia kesho kutwa, Januari 1, 2006,
Tanzania itashika nafasi ya Urais wa Baraza hilo kwa kipindi cha mwezi mmoja. Katika kipindi hicho Tanzania inatarajia kuleta
ajenda ya usalama na usuluhishi wa migogoro katika Eneo la Maziwa Makuu ili
lijadiliwe na Baraza hilo. Kadhalika,
tutaongeza ushiriki wa Jeshi letu katika Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa
Mataifa na Umoja wa Afrika.
Amani na utulivu wa nchi yetu ni moja ya agenda kubwa ya Serikali ya Awamu
ya Nne. Maendeleo ya uchumi pia
yanategemea sana utulivu wa nchi. Pamoja
na matukio ya hapa na pale nchi yetu kwa jumla imetulia, na ni wajibu wetu
kuuendeleza utulivu huu, kwa kufanya
yafuatayo:
·
Kwanza,
kujenga mazingira mazuri ya kazi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama;
· Pili, kuendeleza juhudi za kuwa na Majeshi ya Ulinzi na Usalama yaliyo imara yenye nidhamu ya hali ya juu na utii, na yenye utaalam na zana za kisasa;
·
Tatu, kuongeza uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama
kupambana na ujambazi na kuzagaa kwa silaha ndogondogo ambazo zinatumika
kufanyia uhalifu dhidi ya raia wema. Tatizo hili tutalivalia njuga.
·
Nne,
kuanzisha na kutoa vitambulisho vya uraia; na
·
Tano,
kuongeza kasi ya urejeshaji wa wakimbizi makwao.
Mheshimiwa
Spika,
Waheshimiwa
Wabunge:
Nimesema mengi.
Kwa leo inatosha. Ninamalizia kwa
kuwahakikishieni kuwa nafahamu vizuri sasa ukubwa wa heshima na uzito wa
majukumu niliyokabidhiwa na Watanzania wenzangu. Ninafahamu matarajio ya Chama changu, Chama
Cha Mapinduzi. Nitaongoza kwa dhati utekelezaji wa ahadi zetu kwa wananchi, na
kwa dunia. Ninayajua matarajio ya
Watanzania wenzangu walipoitikia wito wa ari mpya, nguvu mpya na kasi
mpya. Ninayajua matarajio ya nchi
jirani, bara la Afrika na dunia kwa Awamu ya Nne ya uongozi wa taifa letu.
Ninajua wahisani wetu na wawekezaji, wa ndani na nje, wananisikiliza kwa
makini, wakitaka kujiridhisha iwapo nitavijaza viatu alivyoniachia Rais wetu
mpendwa wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa. Nitajitahidi ingawa ni vikubwa kwangu.
Kwenu nyote, na kwao wote, naahidi kwa msaada wa Mwenyezi
Mungu, na kwa ushirikiano na Bunge hili na wananchi kwa ujumla, kuwa naweza
kutimiza matarajio ya kila mmoja.
Tanzania yenye neema tele inawezekana. Maisha bora kwa kila Mtanzania
yanawezekana. Kila mmoja wetu atimize
wajibu wake.
Mungu Ibariki Afrika.
Mungu Ibariki Tanzania.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.