HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA WANANCHI KWA MWISHO WA MWEZI WA KWANZA, 31
JANUARY 2009
Ndugu
Wananchi,
Naomba nianze hotuba yangu, kama
ilivyo kawaida yetu, kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai na kutupa
fursa hii nyingine ya kuzungumza na taifa kwa kutumia utaratibu wetu wa kila
mwisho wa mwezi.
Napenda kuelezea faraja yangu kwamba
tumeuanza mwaka mpya vizuri, licha ya ajali kubwa kadhaa zilizochukua maisha ya
Watanzania wenzetu wengi. Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za ndugu
zetu hawa mahali pema peponi. Amin!
Napenda kuitumia nafasi hii kurudia wito wangu nilioutoa
kwenye salamu zangu za mwaka mpya wa kuwataka wenzetu wa Jeshi la Polisi kuwa
wakali na makini zaidi katika kusimamia sheria na kanuni za usalama barabarani.
Na, madereva nao wazingatie ipasavyo sheria na kanuni za usalama barabarani na wakati
wote watambue umuhimu wa kusalimisha roho za watu wanaowabeba kwenye magari
wanayoendesha.
Ndugu
Wananchi,
Nimeipokea kwa faraja kauli ya Inspekta Jenerali wa
Polisi, Ndugu Saidi Mwema, kuwa wanaendelea kutengeneza mikakati na mbinu bora
zaidi za kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani. Nawatakia kila la heri.
Ndugu
wananchi,
Leo ninayo mambo manne ambayo
ningependa kuyazungumzia: (1) Umoja wa Afrika; (2) Hali ya Mvua; (3)
Upatikanaji wa Matrekta, na (4) Uwezeshaji wa wananchi.
Umoja
wa Afrika
Ndugu
Wananchi
Wakati nazungumza nanyi, niko mjini Addis Ababa, Ethiopia,
kuhudhuria Mkutano wa Kawaida wa 12 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi
wanachama wa Umoja wa Afrika. Kama mjuavyo, katika kipindi cha mwaka mmoja
uliopita, tumepata heshima kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Kesho
au keshokutwa, panapo majaaliwa, tutakabidhi uongozi kwa kiongozi mwingine wa
nchi mwanachama tutakayemchagua.
Kwa niaba yenu, sina budi kuwashukuru viongozi wenzangu wa
nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa heshima hii kubwa walioipa nchi yetu
kupitia kwangu. Napata faraja kubwa kuona kuwa tumetumikia vyema Umoja wa
Afrika na kuna mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi chetu cha
uongozi. Lakini, pia yapo mambo kadhaa ambayo hatukuweza kuyamalizia ambayo
tunamwachia kiongozi ajaye kuyashughulikia.
Watanzania
wenzangu,
Pengine jambo la faraja kubwa kwangu wakati huu
ninapomaliza kipindi changu cha uongozi ni ajenda ya msingi ya kikao chetu cha
safari hii. Niliamua, na kuwaomba wenzangu, na wao wakanikubalia, kuwa katika
kikao hiki tuzungumzie suala zima la kuendeleza mioundombinu barani Afrika.
Nilifanya hivyo kwa kutambua kuwa umoja wa mataifa ya Afrika tunaoutaka
utafanikiwa na kustawi tu pale nchi zetu zitakapokuwa zimeunganishwa kwa njia
za uhakika za usafiri na usafirishaji, yaani barabara, reli na usafiri wa anga
na majini. Nafurahi hiyo ndiyo ajenda yetu kuu. Nina matumaini makubwa kuwa
mjadala na matokeo yake yatatufikisha mahali pazuri na kuchukua hatua muafaka
za kuwezesha kutimia kwa ndoto yetu hiyo.
Hali
ya Mvua
Ndugu Wananchi,
Hali ya
upatikanaji wa mvua nchini inazidi kutia mashaka. Taarifa za Mikoa yenye
upungufu wa mvua zinaongezeka, hasa ukanda wa kati. Hii inaashiria kwamba
huenda kukawa na tatizo kubwa zaidi la upungufu wa chakula katika baadhi ya
Mikoa mwaka huu.
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wanaendelea na
tathmini ya kina ya hali ya upatikanaji wa chakula nchini ilivyo sasa. Taarifa
yao itatupa sura kamili ya hali ilivyo na hatua za kuchukua kukabiliana na
tatizo. Naomba wananchi msiwe na hofu, tutalikabili tatizo hili kwa ukamilifu.
Upatikanaji
wa Matrekta
Ndugu
wananchi,
Jambo la tatu ambalo ningependa
kuliongelea ni suala zima la upatikanaji wa matrekta nchini na pembejeo muhimu
za kilimo.
Mtakumbuka kwamba katika hotuba yangu ya tarehe 31 Disemba
2008, ya kuuaga mwaka 2008 na kuukaribisha mwaka 2009, nilielezea dhamira ya
Serikali kuelekeza nguvu zake katika kuendeleza kilimo. Nilielezea nia yetu ya
kutoa msukumo maalum katika utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya
Kilimo nchini, maarufu kwa jina la ASDP. Miongoni mwa mambo ambayo tumeamua
kufanya kwa ajili hiyo ni kuongeza upatikanaji wa matrekta nchini. Kwa taifa
kama letu linalotegemea kilimo, hatuna budi kuongeza matumizi ya matrekta na
matumizi ya wanyama-kazi kulimia badala ya kuendelea kutumia jembe la mkono.
Serikali imekuwa inachukua hatua kadhaa za kuhimiza
uingizaji wa matrekta nchini. Miongoni mwa hatua hizo ni kufuta ushuru wa
forodha na kodi za ongezeko la thamani kwa matrekta, plau na kadhalika kutoka
nje ya nchi. Pia, baadhi ya Halmashauri za Wilaya nchini zimetumia sehemu ya
pesa za ASDP kununua matrekta na kuyauza kwa vikundi vya wakulima, SACCOS, na
hata mkulima mmoja mmoja.
Lakini, ukweli ni kwamba kiasi cha
matrekta yanayoingizwa nchini bado ni kidogo sana. Idadi hiyo haifanani na nchi
ambayo kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wake, na asilimia 80 ya watu wake
wanaishi vijijini wakitegemea kilimo. Hali hii haikubaliki na lazima ibadilike.
Ndugu
Wananchi,
Kwa nia ya kuongezea nguvu jitihada za kuongeza
upatikanaji wa matrekta nchini na pembejeo muhimu za kilimo, tumeamua kuwa
mwaka huu tuahirishe ununuzi wa magari ya Serikali, isipokuwa machache sana,
ambayo lazima yanunuliwe. Pia tutazuia semina, warsha, makongamano na mikutano
isipokuwa pale ambapo ni lazima ifanyike. Pesa hizo zitumike, badala yake,
kununulia matrekta ili kuongeza idadi ya yale yaliyonunuliwa na Halmashauri na
mengineyo yanayoletwa na sekta binafsi. Kadhalika, zisaidie kununulia pembejeo
muhimu za kilimo na ufugaji.Lengo letu ni kuona wakulima wetu wengi zaidi
wanatumia matrekta, hivyo kutoa fursa ya kupanua ukubwa wa mashamba yao na
kuongeza tija. Pia kuona mimea na mifugo yetu inahudumiwa vizuri zaidi.
Utaratibu mzima wa usambazaji na ugavi wa matreka hayo na
pembejeo utatolewa baadae na Serikali wakati wake utakapofika. Lakini,
tunachotaraji ni kwamba matrekta haya yatauzwa kwa vikundi vya wakulima kupitia
SACCOS au vyama vyao vya ushirika. Hii ni hatua ya mwanzo tu. Kuanzia mwakani
tutatenga fungu maalum katika bajeti la kununua matrekta kwa ajili ya wakulima
wetu.
Ndugu
Wananchi,
Wakati tunaendelea na mpango huu wa matrekta, kama
nilivyosema mwanzo, tutaendelea kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya
kuleta usasa katika kilimo chetu. Kwa ajili hiyo, tayari tumejiwekea mipango
kadhaa, ikiwemo ya kurahisisha upatikanaji wa mbolea, mbegu bora, na madawa ya
mimea na mifugo, pamoja na kuongeza huduma za ugani, kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji
maji, na kuhakikisha masoko na bei nzuri kwa mazao ya mkulima na mfugaji.
Azma yetu ni kwamba, katika kipindi cha miaka michache
ijayo, tuongeze uwekezaji zaidi kwenye kilimo na tuweke msukumo wa kipekee kwa
yale mambo makubwa ya kuboresha na kuleta usasa katika kilimo chetu. Tunapenda
kuona kilimo chetu kinabadilika: tunajitosheleza kwa chakula na maisha ya wakulima wetu nayo
yanabadilika na kuboreka. Naamini haya yanawezekana kabisa iwapo tutafanikiwa
kuyafanya haya na mengine tuliyoanza kuyafanya.
Uwezeshaji wa Wananchi
Ndugu
Wananchi,
Jambo la nne ninalopenda
kulizungumzia leo hii linahusu mabadiliko muhimu tuliyoyafanya mwaka jana
kwenye sheria zinazohusu masuala ya fedha na ardhi. Mabadiliko hayo yana lengo
la kuwezesha na kurahisisha utaratibu wa wananchi kupata nyumba za kuishi, kwa
upande mmoja; na, upande wa pili, kuwezesha na kurahisisha taratibu za wananchi
kupata mitaji na rasilimali za kuendesha shughuli zao za kiuchumi ili wapate
riziki ya kuendesha maisha yao.
Mikopo
ya Ukodishaji Rasilimali (Financial Leasing)
Ndugu Wananchi;
Kwa
muda mrefu sasa, Watanzania wengi wamekuwa wanashindwa kushiriki kwenye
shughuli za uzalishaji mali na kutoa huduma kutokana na ukosefu wa mitaji. Mfumo
wetu wa sasa wa mikopo kutoka mabenki na vyombo vingine vya fedha, ambao umekuwa
ukiandamana na kumtaka mkopaji kuweka dhamana ya mali yenye thamani
inayolingana na mkopo anaouomba, umekuwa kikwazo kikubwa.
Kwa sababu ya kukosa dhamana, wananchi wengi wameshindwa
kupata mikopo ili kutekeleza azma yao ya kuanzisha miradi na kujiongezea kipato
chao.
Ndugu
Wananchi,
Kwa nia ya kupunguza ukali wa tatizo hilo serikali ya
awamu ya tatu iliamua kuanzisha Mpango wa Kurasimisha Raslimali na Biashara za
Wanyonge Tanzania, yaani MKURABITA. Mpango huo sasa umekamilika na umeanza
kutumika kuwawezesha baadhi ya wananchi wenzetu wanaoishi kwenye maeneo
yasiyopimwa kupewa hati za kumiliki mali zao, na kuzitumia hati hizo kupata
mikopo kutoka kwenye mabenki na taasisi nyingine za fedha. Hata hivyo, napenda
kukiri kwamba Mpango huu haujaenea katika maeneo mengi nchini hivyo watu wengi
bado hawajanufaika nao. Tunaendelea kuueneza na ni dhamira yetu kuongeza kasi
ya utekelezaji ili watu wengi zaidi wanufaike.
Ndugu
Wananchi,
Aidha, kwa nia ile ile ya kukabiliana na tatizo la
upatikanaji wa mitaji, tulianzisha mpango wa mikopo ya wajasiriamali wadogo
wadogo yaani shilingi bilioni moja kwa kila Mkoa ambayo sharti la dhamana kwa
mkopaji halikuwepo. Mpango huu una matatizo mawili. Kwanza, pesa zenyewe ni
kidogo ukilinganisha na mahitaji. Tumeazimia kuziongeza. Tatizo la pili ni
kwamba mikopo hii haikukusudiwa kuwanufaisha wajasiriamali wakubwa, wa kati na
wadogo, yaani wale wanaohitaji mitaji mikubwa zaidi au wanaotaka kupata zana au
mitambo ya kufanyia kazi za uzalishaji mali, ambayo ni ghali. Imekusudiwa kwa wajasiriamali wadogo-wadogo
(yaani micro) na siyo wadogo (small), wala wa kati (medium) au wakubwa (large).
Ndugu Wananchi;
Kwa nia ya
kuwawezesha wajasiriamali wa kati na wakubwa kupata mitaji ya kupatia
rasilimali za kufanyia shughuli za uzalishaji mali na huduma, Serikali
ilipeleka Bungeni muswada wa sheria ya mikopo ya ukodishaji rasilimali
(Financial Leasing). Sheria hiyo
ilipitishwa na Bunge mnamo mwezi April 2008 na mimi kuirasimisha Julai Mosi 2008.
Kwa mujibu wa Sheria
hiyo, kama mtu anataka mkopo wa kununulia trekta au lori au mashine ya kukoboa
na kusagisha nafaka au zana na mitambo ya ujenzi wa barabara, na kadhalika, anaweza
kupata bila kulazimika kuweka dhamana nyumba yake au mali nyinginezo alizokuwa
nazo. Atapata mkopo wa zana, mitambo au kifaa anachotaka kufanyia shughuli zake
na hicho kifaa chenyewe ndicho kitakachokuwa dhamana ya mkopo huo. Iwapo
atashindwa kulipa deni, aliyemkopesha atamnyang’anya kile kifaa na kukiuza.
Kimsingi, ni utaratibu
wa kukopa zana na vifaa vya uzalishaji mali na huduma kwa mithili ya mtu
aliyekikodi. Ukimaliza kulipa deni, kifaa au zana hiyo inakuwa mali yako.
Ukishindwa kulipa, zana au kifaa hicho hurudi kwa aliyekukodisha.
Ndugu wananchi,
Kiutendaji na
kiutekelezaji, utaratibu huu unahusisha pande tatu, yaani muuzaji wa vifaa (supplier),
taasisi ya fedha inayokopesha fedha za kununulia kifaa (lessor) na
mkopaji (lessee). Mwananchi ambaye ni mkopaji huchagua zana au kifaa
anachohitaji kwa ajili ya shughuli zake za uzalishaji mali au utoaji huduma.
Kisha anawasiliana na benki au taasisi ya fedha ambayo hutoa mkopo wa kununulia
vifaa hivyo. Kutakuwepo na kutiliana saini mkataba wa mkopo kati ya asasi ya
fedha inayokopesha na mkopaji. Baada ya hapo, mkopaji hupata vifaa na kuendelea
na shughuli zake na kulipa mkopo kwa mujibu wa masharti waliyowekeana.
Zana na vifaa hivyo
hubakia kuwa mali ya taasisi ya fedha iliyomkopesha mpaka pale mkopaji atakapomaliza
deni lake kwa mujibu wa makubaliano. Akishindwa kulipa, zana na vifaa vyake
huchukuliwa na benki au taasisi ya fedha iliyotoa mkopo. Watauza ili kufidia
fedha zao walizokopesha.
Ndugu Wananchi,
Utaratibu huu unawarahisishia
watu kujiendeleza kimaisha kwa gharama nafuu. Unaondoa ugumu uliopo katika kupata
mikopo ya kawaida katika mabenki. Pia, Sheria hii mpya imeweka mazingira nafuu
ya ulipaji wa mkopo, yaani mkopaji kulipa mkopo kulingana na mtiririko wa
mapato yake (cashflow), huku akiendelea kuitumia rasilimali aliyokopa
katika uzalishaji.
Ndugu wananchi,
Utaratibu huu si
mgeni duniani na hata hapa nchini. Katika nchi zilizoendelea, inakadiriwa kuwa,
1/8 (moja ya nane) ya uwekezaji binafsi unagharamiwa kwa mikopo ya utaratibu
huu. Kwa mfano, katika mwaka 2005, dola za Kimarekani 582 bilioni zilitumika
kwa ajili hiyo. Hapa kwetu, utaratibu huo haujaenea, na pale kidogo unapotumika, haulindwi na sheria. Sheria hii
sasa inaondoa kasoro hiyo.
Natambua kwamba
tayari zipo baadhi ya taasisi chache ambazo zimekuwa zinatumia utaratibu huu,
lakini, kama nilivyosema, isivyo rasmi na bila kulindwa na sheria. Kwa mfano,
nimetaarifiwa na Benki Kuu kwamba shirika lisilo la kiserikali la SEROLEASE
limekuwa likiwawezesha wanawake kupata nyenzo za kufanyia kazi – kama vile
majiko ya kuokea mikate, vyerehani vya kushonea, matrekta madogo, mashine za
kusagisha nafaka, pikipiki, boti za uvuvi, na kadhalika. Wenyewe hubakia na
kazi ya kupata mitaji yao midogo kufanyia biashara (working capital).
Ndugu Wananchi,
Nimeambiwa kuwa Mpango
wa SEROLEASE umepata mafanikio mazuri. Vifaa
vyenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 9 vimekopeshwa na ajira 20,000
zimepatikana kutokana na miradi iliyoanzishwa. Mafanikio hayo yametokana na
wakopaji kuwa na nidhamu ya kurejesha mikopo yao.
Mimi naamini, kwa
kutumia kigezo cha mafanikio iliyopata Shirika la SEROLEASE, taasisi nyingi za
fedha, ndogo na kubwa, yakiwemo mabenki, zitashawishika kujihusisha na
utaratibu huu. Hata hivyo, mafanikio ya mpango huu yatategemea jinsi Watanzania
wenzetu, yaani wajasiriamali, watakavyokuwa waaminifu na kurejesha mikopo yao.
Wakifanya hivyo, tutakuwa tumefanikiwa. Wasipofanya hivyo, tutakuwa
tumeharibikiwa. Na, watakuwa wameniangusha
kweli kweli. Juhudi zangu zote zitakuwa zimepotea bure.
Ndugu zangu,
Tunafanya yote haya
kwa ajili yenu. Tunahangaika huku na kule, usiku na mchana, kutengeneza
mazingira mazuri ya kuwawezesha wananchi wa Tanzania kujiendeleza kiuchumi, waongeze
kipato chao ili wainue hali zao za maisha. Naona tusikubali nguvu zetu zipotee
bila ya kuzaa matunda tunayoyatajia sote. Sitegemei kuwa itakuwa hivyo.
Ndugu Wananchi,
Maisha bora kwa kila
Mtanzania hayatadondoka kama mvua, bali yatapatikana kwa kila mmoja wetu
kufanya kazi kwa bidii na maarifa. Wajibu wa Serikali ni kutengeneza mazingira
yatakayowasaidia watu wanaojituma kupata mafanikio na mapato yanayolingana na
jasho lao. Ilani ya Uchaguzi ya CCM
inaiagiza Serikali kuhakikisha kuwa wananchi walio wengi wanashirikishwa katika
shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuboresha hali zao za maisha. Hatua zote
zinazochukuliwa na Serikali, pamoja na hii, zina lengo la kutimiza wajibu huo.
Nawaomba Watanzania wenzangu na nyie mtimize wajibu wenu.
Ndugu Wananchi,
Kwa ujumla, kutungwa
kwa sheria hii ya mikopo ya ukodishaji wa rasilimali (financial leasing) kutaleta manufaa makubwa kwa wajasiriamali wa
Tanzania. Naomba tuitumie ipasavyo fursa hii kwa maslahi yetu.
Mabadiliko ya Mfumo na
Utaratibu wa Umiliki wa Nyumba
Ndugu
Wananchi;
Jambo la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia leo
linahusu mabadiliko katika mfumo na utaratibu wa upatikanaji wa mikopo na miliki
ya majengo na nyumba.
Mikopo
kwa ajili ya Ujenzi/Ununuzi wa Nyumba
Ndugu
Wananchi;
Suala la wananchi wa Tanzania kupata nyumba bora za kuishi
mijini na vijijini ni jambo tulilolipa umuhimu mkubwa Serikalini. Limesisitizwa
kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu na nililizungumzia kwenye hotuba yangu
ya kuzindua Bunge letu tukufu tarehe 30 Disemba 2005.
Kwa muda mrefu, maendeleo ya makazi nchini yamekuwa
yanarudishwa nyuma na kutokuwepo mfumo wa mikopo ya ujenzi au ununuzi wa nyumba
na majengo. Kwa ajili hiyo, mtu analazimika kujenga au kununua nyumba kwa
kutumia fedha yake mwenyewe. Uwezo wetu tunaujua wenyewe, hivyo kusababisha
ujenzi kuchukua muda mrefu. Pia huwafanya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu
kutumia njia zisizokuwa halali kujipatia hitaji hili muhimu kwa maisha ya
mwanadamu.
Ndugu
Wananchi,
Tuliahidi kulitafutia ufumbuzi tatizo hili la kutokuwepo
utaratibu wa mikopo ya kujenga au kununua nyumba. Katika kutimiza ahadi hiyo,
mwaka wa jana, 2008, tumetunga Sheria ya Upatikanaji wa Mikopo kwa ajili ya Uendelezaji
Nyumba [The Mortgage Finance (Special Provisions) Act, 2008].
Sheria hii inaboresha mazingira ya upatikanaji mikopo kwa
ajili ya ununuzi au ujenzi wa nyumba. Hivyo basi itasaidia wananchi kuweza
kukopa kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba na
kupata makazi bora ya kuishi. Manufaa mengine ya sheria hiyo ni kuongezeka kwa
uwekezaji katika sekta za Fedha na Ujenzi, fursa za ajira nchini, na kukua kwa
uchumi wa Taifa kwa jumla. Hivyo hivyo, mapato ya serikali yataongezeka kutokana
na kukua kwa sekta ya Ujenzi.
Umiliki wa Sehemu za Majengo (Unit Titles)
Ndugu
Wananchi,
Sheria nyingine tuliyoipitisha Bungeni mwaka jana, itakayosaidia
Watanzania kumiliki nyumba, ni ile ya Unit Titles Act, 2008. Kwa mujibu wa
sheria hiyo, watu wanaoishi au wenye ofisi katika jengo la ghorofa lenye fleti
au ofisi kadhaa wanaweza kununua na kupata hati za kumiliki fleti wanazoishi
ama ofisi wanamofanyia kazi.
Hivi sasa, jambo hilo haliwezekani kwa vile hati ya
kiwanja ni moja tu, yaani ya yule mwenye ghorofa. Kwa mujibu wa sheria hii
mpya, sasa unaweza kununua na kupewa hati ya kumiliki fleti uliyonunua. Tena
hati hiyo unaweza kuitumia kama dhamana kukopea katika mabenki. Aidha unaweza
kuuza fleti yako kwa mtu yeyote, na hati ikabadilishwa mmiliki na kuwa ya yule
mnunuzi mpya.
Ndugu
Wananchi,
Kuwepo kwa ile sheria ya mikopo ya
uendelezaji wa majengo kutatoa fursa kwa watu kupata mikopo ya kununua fleti
katika maghorofa wanayoishi sasa au hata mengine yatakayojengwa. Aidha Sheria
hizi mbili, zitasaidia kuchochea ujenzi wa majengo ya ghorofa kwa ajili ya
kuuza fleti zilizomo. Kwa kufanya hivyo, sheria hizi zitasaidia Watanzania
kupata makazi bora ya kuishi. Nawaomba Watanzania tuzitumie fursa zitakazotolewa na sheria hizi mbili kuinua
hali zetu za maisha.
Kutengeneza
Kanuni
Ndugu
Wananchi,
Kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, ili Sheria hizi tatu,
yaani Sheria ya Mikopo ya Ukodishaji Rasilimali (Financial Leasing Act, 2008),
Sheria ya Umiliki wa Sehemu za Majengo (Unit Titles Act, 2008) na Sheria ya
Mikopo ya Uendelezaji wa Nyumba [The Mortgage Finance (Special Provisions) Act,
2008] ziweze kutumika, ni lazima zitengenezwe Kanuni (Regulations) zitakazofafanua
jinsi Sheria hizi zitakavyotumika, kifungu kwa kifungu. Kanuni hizo
hutengenezwa na Wizara husika na kutolewa kwa amri ya Waziri anayehusika. Kwa
kawaida, amri hiyo hutangazwa katika Gazeti la Serikali.
Kazi ya utengenezaji wa kanuni za Sheria hizi tatu imekuwa inaendelea. Naambiwa inakaribia
kukamilika. Nimewasisitiza Mawaziri wahusika na masuala ya ardhi na fedha
kuongeza kasi ya kukamilisha kanuni hizo ili watu waanze kunufaika nazo. Hakika
tuko nyuma sana ya wakati.
Kadhalika nimewataka waanze kazi ya kuelimisha umma kuhusu
sheria hizo ili wananchi wazielewe na kuzitumia kuinua hali yao ya maisha.
Wakati huo huo, nimemtaka Waziri wa Fedha na Uchumi ashirikiane na Gavana wa
Benki Kuu kuyatayarisha mabenki na asasi za fedha nchini kuanza kujiandaa kutoa
mikopo. Nisingependa kuona tunachelewa baada ya Kanuni kutoka.
Hitimisho
Ndugu
Wananchi,
Leo nimeongelea jitihada za Serikali
kutengeneza fursa kwa wananchi kujiendeleza kiuchumi. Mwishowe ni jukumu la wananchi kuzitumia fursa
hizi. Tujiandae na kujipanga kutumia fursa zitakazotokana na mabadiliko haya.
Tutaendelea kuelimishana na kuelekezana namna ya kuzitumia fursa hizi. Napenda
kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kuhangaika kwa ajili yenu kubuni
mbinu na mikakati ya kuhakikisha kuwa tunajenga uchumi wa kisasa ambao
unawashirikisha wananchi walio wengi, kama ambavyo Ilani ya Uchaguzi ya CCM
inavyotuelekeza.
Mwisho kabisa, naomba niwashukuru
tena kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kuwaletea
maendeleo. Nawaomba tuendelee kushirikiana na kusaidiana. Aidha, tuendelee
kuipenda na kuitumikia nchi yetu kwa moyo wetu wote.
Mungu
Ibariki Afrika
Mungu
Ibariki Tanzania
Asanteni
kwa kunisikiliza!