HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO
KIKWETE,
AKIAGANA NA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, UKUMBI WA
BUNGE, DODOMA, 16 JULAI, 2010
Mheshimiwa
Spika,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu aliyetujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kuishuhudia siku hii ya
kihistoria ambapo Bunge la 9
linamaliza kipindi chake cha miaka mitano.
Nimekuja hapa kutimiza wajibu wa Kikatiba wa kuhitimisha shughuli za
Bunge hili ili kufungua njia kwa mchakato wa uchaguzi wa kupata Wabunge na Rais
kwa kipindi kijacho kuanza rasmi.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kuagana na Wabunge wa Bunge lako
Tukufu, ambalo nami ni sehemu yake, ninayo mengi ya kushukuru, na ninao wengi
wa kuwashukuru na kuwapongeza. Wa kwanza,
ni Watanzania wenzangu wote, walionipa fursa hii adhimu ya kuwatumikia katika
nafasi hii ya juu kabisa ya uongozi wa nchi yetu. Nawashukuru kwa ushirikiano
wao mkubwa kwangu, kwa Serikali yangu na kwa Bunge letu tukufu katika kipindi
chote hiki cha miaka mitano. Nawashukuru pia kwa kutimiza wajibu wao wa kiraia
wa kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuijenga nchi yetu. Natambua na
kuthamini uvumilivu na uelewa wao wakati nchi yetu ilipokuwa inapita katika
vipindi vigumu. Nawashukuru sana kwamba hata wakati huo, Watanzania wenzangu
wameniunga mkono, wameiunga mkono Serikali yetu na kutusaidia. Asanteni sana.
Pili,
napenda kuwashukuru viongozi wenzangu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali na
mashirika yake. Napenda kuwatambua kwa
ajili hiyo, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt.
Ali Mohammed Shein; Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume;
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda; Waziri Mkuu aliyemtangulia Mheshimiwa
Edward Lowassa na Waziri Kiongozi, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha. Aidha, nawashukuru Mawaziri, Naibu Mawaziri,
Katibu Mkuu Kiongozi, Ndugu Phillemon Luhanjo, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu
Wakuu pamoja na watendaji wengine waandamizi na wafanyakazi wengine wa umma wa
ngazi zote. Msaada wao, ushirikiano wao
na uchapa kazi wao ndivyo vilituwezesha kupata mafanikio tunayojivunia leo.
Tatu,
Mheshimiwa Spika, natoa shukrani kwako na Wabunge wa Bunge lako Tukufu. Nakushukuru wewe kwa uongozi wako
mahiri. Nawapongeza Wabunge wote kwa
kazi nzuri mliyoifanya ya kuwawakilisha wananchi waliowachagua. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu na msaada
wenu kwangu na kwa Serikali yetu. Bunge
letu limekuwa kielelezo kizuri cha ustawi wa demokrasia nchini. Mmetoa hoja nyingi nzuri za kukosoa na kuishauri
Serikali. Ingawaje kuna baadhi ya
nyakati maneno yalivuka mipaka ya staha, lakini, napenda kuamini kuwa ilikuwa ni kwa nia
njema! Isitoshe elimu haina mwisho na
wakati mwingine kukosea ndiyo kujifunza.
Shukrani
zangu za mwisho lakini siyo mwisho kwa umuhimu, ziwaendee wakuu wa vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama na wanajeshi na
watumishi wote wa vyombo hivyo.
Tunamaliza nchi yetu ikiwa salama: mipaka iko salama na usalama wa
maisha na mali za raia ni wa uhakika.
Changamoto
na Mafanikio
Mheshimiwa
Spika,
Nilipokuja
kuzindua Bunge hili tarehe 30 Disemba 2005, nilielezea na kufafanua kwa kina
dira, mwelekeo na malengo ya Serikali ya Awamu ya Nne. Niliahidi kwamba
Serikali yangu ingeongozwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo
ilitoa majukumu mahsusi kwa Serikali kufanya. Kupitia kwenu, Waheshimiwa
Wabunge, niliwaahidi Watanzania mambo kumi yafuatayo katika miaka mitano ya
Serikali yetu. Naomba kwa ruhusa yako, Mheshimiwa Spika, niyakumbushe mambo
hayo:
1)
Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha
kuwa Amani, Utulivu na Umoja wa nchi yetu na watu wake vinadumishwa;
2)
Serikali ya Awamu ya Nne itadumisha na
kuendeleza mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi leo;
3)
Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza
vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, tena kwa ari mpya, nguvu mpya na
kasi mpya;
4)
Serikali ya Awamu ya Nne itatimiza
ipasavyo wajibu wake wa utawala na maendeleo, na itaendesha dola kwa misingi ya
utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za
binadamu;
5)
Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha
uwezo wake wa kulinda maisha na mali za raia wake. Tutapambana na uhalifu wa kila aina, na
majambazi hayataachwa yatambe yatakavyo;
6)
Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha
mipaka ya nchi yetu ipo salama.
Hatutamruhusu mtu au nchi yeyote kuchezea mipaka ya nchi yetu na uhuru wetu;
7)
Serikali ya Awamu ya Nne itafanya kila
iwezalo kuhakikisha Tanzania ina mahusiano mazuri na mataifa yote duniani,
pamoja na mashirika ya kimataifa na kikanda;
8)
Serikali ya Awamu ya Nne itajali sana
maslahi na mahitaji ya makundi maalum katika jamii kama vile wanawake, vijana,
watoto, wazee, walemavu na yatima;
9)
Serikali ya Awamu ya Nne itaongoza
mapambano mapya ya kuhifadhi mazingira ili vizazi vijavyo virithi nchi nzuri,
na msingi imara wa maendeleo endelevu; na
10)
Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza
michezo, na shughuli za utamaduni na burudani.
Mheshimiwa
Spika;
Leo,
naona fahari kusema kuwa tumepiga hatua kubwa katika kutekeleza malengo yetu
hayo. Tumefanikiwa pia mambo mengine
mbalimbali tuliyoahidi katika ilani ya Uchaguzi ya Chama tawala au kujitokeza
kwa nyakati au mahali mbalimbali. Viwango
vya mafanikio vinatofautiana kwa kila sekta, hata hivyo, tumesonga mbele kwa
kasi ya kuridhisha, japo bado tuna safari ndefu kuelekea kwenye maisha bora kwa
kila Mtanzania.
CHANGAMOTO
TULIZOKABILIANA NAZO
Mheshimiwa Spika;
Ninapoangalia
mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi hiki na kulinganisha na
changamoto tulizokabiliana nazo, huwa nastaajabu na kujiuliza tumewezaje? Mimi siyo Sheikh na wala siyo mwanazuoni wa
dini yangu. Ni mcha Mungu wa kawaida tu
hivyo naamini kuwa ni rehema za Mwenyezi Mungu ndizo zilizotuwezesha kupata
mafanikio tunayojivunia sote hii leo.
Kama mnavyojua tulianza kazi, nchi ikiwa
katikati ya ukame mkubwa wa aina yake kutokea tangu uhuru. Kukawa na upungufu mkubwa wa chakula,
takriban watu wapatao 3,776,000 walipatiwa chakula na Serikali. Ukame huo pia ulikausha maji katika mabwawa
yetu ya kuzalisha umeme hivyo kukawa na upungufu mkubwa wa umeme na tukalazimika
kukodi vinu vya kufua umeme kutoka nje.
Mheshimiwa
Spika;
Kuanzia katikati ya mwaka 2007, bei za
mafuta zilipanda kwa kasi sana na ilipofikia Juni, 2008 bei zilifikia kiwango
cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa duniani.
Mafuta yanagusa nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Hivyo gharama za usafiri, uchukuzi, uzalishaji
mashambani na viwandani na utoaji wa huduma mbalimbali zikapanda. Hali hiyo ilisababisha mfumuko wa bei na
gharama za maisha kupanda sana nchini.
Katika
nusu ya pili ya mwaka 2008, dunia ikakumbwa na tatizo jingine kubwa la
machafuko katika masoko ya fedha na mitaji yaliyosababisha kudorora kwa uchumi
wa dunia. Kudorora kwa uchumi wa dunia
kulisababisha bidhaa zetu tunazouza nje kukosa masoko na bei zake kuporomoka
sana na kuwatia hasara kubwa wazalishaji na wafanyabiashara wetu. Watalii kutoka nje wakapungua, wawekezaji
walioonyesha nia ya kuwekeza nchini waliahirisha kufanya hivyo. Utulivu wa uchumi wetu ulianza kuyumba. Ukuaji wa uchumi ukashuka, mfumuko wa bei
ukapanda sana, mapato ya Serikali yakawa chini ya lengo, n.k. Ili kulinusuru taifa, Serikali ikalazimika
kutengeneza mpango wa dharura wa kuunusuru uchumi ambapo shilingi trilioni 1.7
zilitumika. Hatua hiyo ndiyo iliyosaidia
kupunguza makali ya athari za kudorora kwa uchumi hapa nchini.
Mheshimiwa
Spika;
Wahenga walisema “kila msiba una mweziwe”.
Katika baadhi ya mikoa hasa ile inayopakana na Kenya miaka ya 2008 na
2009 ilikumbwa na ukame mkali uliosababisha hata mifugo na wanyama pori wengi kufa
na watu wake kuwa maskini na kukabiliwa na njaa kali. Serikali iliwapelekea chakula cha msaada na
sasa tunaangalia namna ya kuwasaidia waanze upya maisha. Kule Kilosa na Mpwapwa kwa sababu ya mvua
kubwa Mkoani, Dodoma, Desemba, 2009, sehemu nyingi za reli ya kati zikasombwa
na maji na ilituchukua miezi sita mpaka treni zilipoanza tena kazi.
Matatizo yote hayo niliyoyataja
yamekuwa na athari kubwa kwa ukuaji na ustawi wa uchumi wa nchi yetu. Umeturudisha nyuma kwa kiasi kikubwa kwani
kama athari hizo zisingekuwepo tungekuwa tumefikia malengo yetu mengi na hata kuyavuka. Hata hivyo, tumepata mafanikio ya kutia moyo
kwenye nyanja mbalimbali, jambo linalothibitisha kuwa sera zetu za uchumi ni
sahihi kwani uchumi wetu umeweza kujenga kiwango kizuri cha kuhimili misukosuko
mikubwa kama hii tuliyokumbana nayo.
HALI YA SIASA
Umoja
na Amani
Mheshimiwa Spika,
Tanzania imeendelea kuwa nchi tulivu,
yenye amani na usalama na watu wana umoja licha ya tofauti zao za dini,
makabila, rangi na ufuasi wa vyama vya siasa.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumejitahidi kadri ya uwezo
wetu kulinda, kuendeleza na kuimarisha sifa hii ya nchi yetu. Nawashukuru sana
Watanzania wote kwa kuelewa na kutambua kwa haraka na kuepukana na vihatarishi
vya amani na umoja wa nchi yetu. Nawashukuru na kuwapongeza kwa kuwapuuza wale
wanaotaka kuigawa nchi yetu kwa misingi ya udini, ukabila, Ubara na Uzanzibari
na Upemba na Uunguja.
Muungano
Mheshimiwa Spika,
Umoja
wa taifa letu una sura mbili. Kwanza,
ni umoja baina ya Watanzania wa makabila, rangi na dini zote. Pili, ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Muungano wetu umeendelea kuwa imara. Katika
miaka mitano hii tumechukua hatua mahsusi za kuimarisha Muungano na mshikamano wetu.
Tumeimarisha Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kumteua Waziri maalum katika ofisi
hiyo kushughulikia masuala ya Muungano. Tumeboresha taratibu za majadiliano ya
masuala ya Muungano kwa kumfanya Makamu wa Rais kuwa Mwenyekiti wa kikao cha
pamoja cha Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi cha kujadili masuala ya Muungano. Vikao
vitano vilifanyika na mambo mengi yalizungumzwa na kupatiwa ufumbuzi. Aidha vikao 75 vya ushirikiano kwa sekta
zisizo za Muungano pia vilifanyika.
Mpasuko
Zanzibar
Mheshimiwa
Spika,
Siku
ile ya tarehe 30 Disemba, 2005 nilieleza kusononeshwa kwangu na mpasuko wa
kisasa uliopo Zanzibar. Niliahidi
kufanya kila niwezalo ili hali hiyo ibadilike na Wazanzibari wawe wamoja, waishi
kwa upendo, amani na utulivu. Bila ya
shaka mtakubaliana nami kwamba tumefika mahali pazuri na ishara njema
zinaonekana. Napenda kuchukua fursa hii,
kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wenzangu wa Chama cha Mapinduzi na wenzetu
wa CUF kwa kukubali vyama vyetu vizungumze.
Nawashukuru na kuwapongeza kwa dhati
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi na Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF kwa
maridhiano yao ya tarehe 5 Novemba, 2009.
Maridhiano hayo yamefungua njia ya kuwezesha kutekelezwa kwa makubaliano
ya vyama vyetu. Nawapongeza kwa dhati
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kukubali kura ya maoni ifanyike ili
wananchi wa Zanzibar waamue kuhusu kuundwa kwa Serikali ya umoja wa kitaifa
baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Naendelea kuahidi ushirikiano wangu na msaada wangu pale
unapohitajika. Nawasihi ndugu zangu
Wazanzibari tuitumie vyema fursa hii ya kihistoria kuzika siasa za uhasama na
kushupaliana zilizowagawa wananchi katika makundi ya uadui, na badala yake
Wazanzibari wawe watu wamoja, wanaoishi kindugu na kwa kushirikiana.
Demokrasia Imestawi
Mheshimiwa
Spika,
Nchi yetu imeendelea kuwa
kielelezo kizuri cha utulivu wa kisiasa na ukomavu wa demokrasia barani Afrika.
Katika miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuhakikisha kwamba uhuru wa kisiasa,
uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kuabudu unaheshimiwa
na kulindwa. Tumehakikisha kwamba wanasiasa pamoja na vyama vya siasa, asasi
zisizo za kiserikali na wananchi wote kwa ujumla wanafaidi haki zao za msingi.
Tumefanya jitihada ya
kuhakikisha kwamba uwanja wa ushindani wa kisiasa unakuwa sawia zaidi. Kwa
ajili hiyo, tumefanya Marekebisho ya Sheria zetu za
Uchaguzi na tumetoa ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye madiwani kuanzia mwaka
2007. Sasa hivi chama kisichopata ruzuku ni kile tu ambacho kimeshindwa kupata
hata diwani mmoja. Hali hii imedhihirisha ukomavu wa kisiasa nchini.
Mapambano
Dhidi ya Rushwa na Maadili ya Uongozi
Mheshimiwa
Spika,
Ahadi
yangu ya kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma
na matumizi mabaya ya madaraka nchini tumeitimiza. Tumekemea vitendo vya kutoa
na kupokea rushwa na kuchukua hatua za kisheria na za kinidhamu kwa wahusika pale
ilipobidi kufanya hivyo. Tumetunga
Sheria mpya na kali zaidi na tumepitisha mkakati mpya wa kupambana na rushwa. Tumeunda
upya chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU). Sasa TAKUKURU ina ofisi
katika kila wilaya na tumeiongezea uwezo wa kibajeti na rasilimali watu na
vitendea kazi.
Juhudi hizo, zinadhihirisha
utashi mkubwa wa kisiasa tulionao wa kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya
madaraka. Kwa sababu hiyo, katika miaka mitano hii, tuhuma nyingi zimechunguzwa,
kesi nyingi zimefikishwa Mahakamani ikiwa ni pamoja na zile za rushwa kubwa. Mapambano bado yanaendelea. Katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita tumepeleka Mahamani kesi za rushwa 780. Idadi hii ni kubwa
kuliko kesi zote za rushwa zilizopata kupelekwa Mahakamani katika kipindi cha
miaka 20 kabla ya hapo, ambazo zilikuwa
543. Kati ya kesi hizo 780 Serikali
imeshinda kesi 160. Katika kipindi cha
miaka 20 kabl a ya hapo (yaani kuanzia
1985 – 2005) Serikali ilishinda kesi 58 tu.
Mapambano bado yanaendelea.
Mheshimiwa
Spika,
Katika miaka mitano hii Ofisi
ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeimarishwa kiutendaji
na kisheria. Mwaka 2008, Bunge lako tukufu
lilitunga Sheria mpya inayotoa uwezo na uhuru mkubwa zaidi wa kutenda kazi wa
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na ofisi yake.
Nilianzisha utaratibu mpya wa
viongozi na watendaji wakuu wa Wizara, Halmashauri za Wilaya na Miji, Idara za
Serikali na Wakala mbalimbali, kusoma na kujadili taarifa za kila mwaka za Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu maeneo yao na kuchukua hatua za
kurekebisha kasoro alizozigundua. Utaratibu huu unazifanya taarifa hizo ziwe na
thamani na imesaidia kuleta ufanisi wa hesabu za Serikali. Siku hizi wanaopata hati chafu wamepungua
sana.
Mheshimiwa Spika;
Nampongeza sana Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ofisi yake kwa kazi nzuri
wanayofanya. Nampongeza pia kwa uamuzi
wa kufanya ukaguzi wa thamani ya fedha kwa maana ya kulinganisha fedha
iliyotumika na kazi iliyofanyika. Hii ni
hatua muhimu itakayosaidia kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika vizuri na
kwa shughuli iliyokusudiwa.
Katika kipindi hiki pia
tumeanza utaratibu mzuri wa kuwawajibisha wale wote wanaohusika na wizi na ubadhirifu
wa fedha za umma mara unapogundulika na wakaguzi. Tofauti na zamani ambapo hatua husubiri baada
ya taarifa ya ukaguzi kuwasilisha Bungeni.
Hatua hii itasaidia kujenga
nidhamu na kunusuru fedha nyingi za umma zinazoibiwa na kutumiwa vibaya.
Tumejitahidi kusimamia vyema Sheria ya Manunuzi ili kupunguza mianya ya rushwa katika
manunuzi ya Serikali na hasa mikataba.
Tumefanya mapitio ya Sheria hiyo na kuainisha maeneo yanayohitaji
kufanyiwa marekebisho ili kuboresha usimamizi na kurahisisha upatikanaji wa
huduma katika sekta za umma. Nasikitika
kwamba kwa sababu ya ufinyu wa muda haikuwezekana Sheria hiyo kujadiliwa na
kuamuliwa katika Bunge hili. Ni
makusudio yetu kuiwasilisha mapema Bunge lijalo litakapoanza kazi.
Maadili ya Uongozi
Mheshimiwa
Spika,
Niliahidi
kulipa msukumo mpya suala la maadili ya uongozi. Tumeruhusu mijadala ya wazi
miongoni mwa wananchi, vyombo vya habari, taasisi zisizo za kiraia, na hata
hapa Bungeni, kuhusu maadili ya uongozi wa umma.
Tumeimarisha
Tume ya Maadili ya Viongozi, kwa kuijengea uwezo zaidi wa kisheria na kifedha. Tume
ya Maadili ya Viongozi sasa ina mamlaka siyo tu ya kupokea fomu za mali
walizojaza viongozi bali pia ina uwezo wa kuhakiki mali hizo ili kuthibitisha
ukweli wa taarifa zinazotolewa kila mwaka.
Tumebadilisha
utaratibu na kuamua kwamba mali za familia za viongozi nazo zijumuishwe kwenye
fomu na pia zikaguliwe. Kwa kufanya hivyo viongozi wasio waadilifu watapata
tabu kuficha mali zao. Naamini, tukiendelea na mwenendo huu, maadili ya
viongozi wetu yatakuwa yamejengewa msingi mzuri.
Mheshimiwa Spika,
Niliahidi
kwamba tutatafuta utaratibu wa kudhibiti mapato na matumizi ya fedha katika
uchaguzi ili uongozi usiwe bidhaa ya kununuliwa. Tayari Sheria ya Kudhibiti Gharama za Uchaguzi imepitishwa na Bunge
lako Tukufu na itaanza kutumika katika uchaguzi wa mwaka huu. Mimi naamini
kwamba, pamoja na upya wake itasaidia kupunguza na hata kukomesha vitendo vya
rushwa katika uchaguzi, iwe wa ndani ya vyama vya siasa au nje miongoni mwa
umma. Tuko tayari kufanya marekebisho
yoyote yatakayojitokeza katika utekelezaji kwa nia ya kuiimarisha. Aidha, mchakato wa kutenganisha shughuli za
biashara na siasa unaendelea na utakamilika mapema katika uhai wa Bunge lijalo.
Utawala Bora
Mheshimiwa
Spika,
Katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita tumefanikiwa kuimarisha utawala bora katika
utendaji kazi wa serikali. Tumeendesha shughuli za serikali kwa kuheshimu
mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mikuu ya dola, yaani, Bunge, Mahakama na Utawala. Sisi
katika Serikali tumeendelea kutimiza wajibu wetu wa uwezeshaji kwa mihimili
hiyo.
Bunge
Mheshimiwa
Spika,
Kama
mtakavyokumuka Mfuko wa Bunge tayari umeanzishwa kama yalivyo matakwa ya Katiba
ya nchi yetu. Bajeti ya Bunge tumendelea
kuiongeza na sasa ni mara mbili ya ile iliyokuwepo mwaka 2005. Maslahi ya Wabunge nayo yameboreshwa. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo umeanzishwa ili kuwawezesha
Wabunge kushughulikia matatizo madogo madogo yanayowakabili wananchi wao.
Mazingira bora
tuliyoyajenga yameliwezesha Bunge letu katika miaka mitano hii kufanya kazi zake
kwa uhuru, uwazi na ufanisi mkubwa zaidi na limekuwa kielelezo kizuri cha
ustawi na ukomavu wa demokrasia nchini mwetu. Katika kipindi hiki, changamoto
zilizojitokeza katika utendaji na mahusiano baina ya mihimili hii mikuu ya dola
tumezitatua kwa maelewano yanayozingatia maslahi ya taifa. Huu ni uthibitisho
kuwa demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria unaendelea kuota mizizi.
Mahakama
Mheshimiwa Spika,
Uimara na ufanisi wa
mahakama zetu na vyombo vingine vya kusimamia haki ndiyo msingi wa amani ya
nchi yetu. Ni, ukweli ulio wazi kuwa amani
na utulivu hustawi kama haki inatendeka na inaonekana kutendeka kwenye
jamii.
Tumetimiza ahadi yetu na
wajibu wetu wa kuiwezesha Mahakama kufanya shughuli zake kwa ufanisi zaidi. Mahakama
imendelea kuwa huru na kamwe Serikali haikuiingilia Mahakama katika kazi
zake. Tumeongeza idadi ya Majaji, Mahakimu na Mawakili wa
Serikali, na nafurahi kwamba tumezingatia uwakilishi wa kijinsia. Katika kipindi hiki pia nimeteua Majaji wapya
12 wa Mahakama ya Rufani kati yao 4 wakiwa wanawake na Majaji 51 wa Mahakama Kuu, wanawake wakiwa 24. Tumeajiri Mahakimu Wakazi 256 wanawake wakiwa 117 na Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo 394 kati yao 134 ni wanawake. Majaji na Mahakimu wanawake wamekuwa wengi
kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu. Hii ni kutekeleza
ahadi yangu na ya Ilani ya Uchaguzi ya kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi
za maamuzi. Kwa jumla kitaifa tumefikia
asilimia 31 kutoka asilimia 26 mwaka 2005.
Hii leo tuna wanawake wengi katika nafasi za Ubunge, Uwaziri, Wakuu wa
Mikoa na Wilaya, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Watendaji n.k. Nafurahi na kushukuru kwamba wanawake hawa
wengi hawajaniangusha. Wanachapa kazi
vizuri.
Mheshimiwa
Spika;
Tumeendelea kuboresha bajeti
ya Mahakama ingawaje bado kiasi kinachotengwa ni kidogo ukilinganisha na
mahitaji. Tumeboresha maslahi ya Majaji
na Mahakimu na tunakusudia kufanya zaidi siku za usoni. Hivi sasa tunaendelea na mchakato wa kuiwezesha
Mahakama nayo kuwa na Mfuko wake Maalum, kama inavyotaka Katiba ya nchi.
Utendaji
Serikalini
Mheshimiwa
Spika,
Ufanisi
wa utendaji wa Serikali unategemea kuwepo kwa rasilimali watu wenye ari ya
kuchapa kazi na wenye vitendea kazi stahiki. Katika hotuba yangu ya kufungua
Bunge Desemba 30, 2005 nilielezea pia kwamba tutachukua hatua za kuboresha
mishahara na maslahi yao kwa ujumla. Tuliunda Tume maalum ambayo ilitupatia
mapendekezo kadhaa. Tumekuwa tukiyafanyia kazi mapendekezo hayo na kuyatekeleza
kulingana na uwezo wetu wa kibajeti.
Katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita tumewapandisha vyeo watumishi 140,797 ambao hawakuwa wamepewa haki
yao hiyo kwa muda mrefu. Tumelipa fidia
ya stahili za watumishi kwa gharama ya shilingi bilioni 108. Aidha, Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 45.1 kulipia malimbikizo na madeni yote
halali ya walimu; walimu wa shule za msingi shilingi 32.2 bilioni na sekondari shilingi 12.9 bilioni. Kuna rufaa za
madai ya walimu yapatayo shilingi bilioni
6 ambazo zinaendelea kushughulikiwa na Kamati ya Maofisa wa Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Uchumi na Menejimenti ya
Utumishi wa Umma.
Katika kipindi hiki pia tumepandisha kima cha
chini cha mshahara ya watumishi wa umma kutoka shilingi 65,000 mpaka shilingi 135,000
sawa na ongezeko la asilimia 107. Ahadi ya kuendelea kuongeza iko pale
pale. Tumeboresha mafao ya uzeeni kwa
watumishi wa Serikali kwa kuhuisha ukokotoaji wa mafao ya LAPF na PSPF na
kuboresha ukokotoaji wa mafao ya Mfuko wa PPF.
Mheshimiwa
Spika;
Tumeboresha
utendaji wa Halmashauri zetu kimuundo, kifedha na kiutumishi ili ziweze kuchochea
kasi ya maendeleo ya watu wetu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita
tumeongeza ruzuku kwa Halmashauri kwa zaidi ya mara tatu kutoka shilingi bilioni 780 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 2,728 mwaka huu. Tumeajiri wahasibu 795;
wakaguzi wa ndani 447; maafisa kilimo
na mifugo 455; wahandisi wa maji 95; na watumishi wa kada mbalimbali za afya
6,437. Watumishi hawa na ruzuku
tunayotoa imechangia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Kazi ya kuboresha
utendaji wa Halmashauri bado ipo kubwa mbele yetu na hasa ile ya kuzuia wizi na
ubadhirifu. Tumeanza Awamu ya Pili ya
Maboresho ya Serikali za Mitaa na ni matumaini yangu kuwa suala hilo litapewa
uzito unaostahili.
Ulinzi
na Usalama
Mheshimiwa
Spika,
Ulinzi
na Usalama wa nchi yetu uliendelea kuwa agenda yetu kuu katika miaka mitano
iliyopita. Nilipokuja kulifungua Bunge letu mwaka 2005, niliahidi kwamba
Serikali ya Awamu ya Nne itajenga mazingira mazuri ya kazi kwa vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama. Kazi hiyo tumeifanya na tunaendelea nayo. Tumeviwezesha
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kifedha na kivifaa ili viweze kumudu
majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Tumeendelea
kuboresha makazi ya wanajeshi na askari wetu kwa kujenga nyumba bora kwa Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Polisi na Magereza. Kazi hiyo inaendelea. Bado kuna changamoto kubwa mbele yetu. Hata hivyo, tutaendelea kuimarisha vyombo vyetu ili viendelee kutekeleza
majukumu yake vizuri zaidi.
Mheshimiwa
Spika,
Niliahidi
kuwa tutaanza kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani duniani iwapo tutaombwa kufanya hivyo. Nafurahi kusema kuwa tumepeleka walinzi wa
amani huko Lebanon na Darfur. Vilevile, mwaka 2008 Jeshi letu liliongoza kwa
ufanisi mkubwa majeshi ya nchi za Umoja wa Afrika kukirejesha katika Umoja wa
Jamhuri ya Visiwa vya Comoro Kisiwa cha Anjouan kilichokuwa kikitawaliwa kwa
mabavu na kiongozi muasi Kanali Mohamed Bakar.
Umoja wa nchi hiyo umerejea na kuimarishwa.
Uhalifu
Mheshimiwa
Spika,
Uhalifu,
hasa wa kutumia silaha, bado ni changamoto kwa usalama wa watu wetu na mali
zao. Tulipoingia madarakani tulikuta wimbi kubwa sana la uhalifu, na nikaahidi
hapa Bungeni kwamba hatutawaacha majambazi watambe. Jeshi la Polisi lilifanya
kazi kubwa kututoa katika wimbi lile la uhalifu. Uhalifu upo, lakini sio kama ilivyokuwa
wakati ule.
Jeshi
letu linaendelea kudhibiti kuzagaa kwa silaha na kukusanya taarifa za uhalifu
na wahalifu na kuvunja mitandao yao. Hatuna budi kutambua kwamba uhalifu
unaozuiwa kwa jitihada za Jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika. Na, siku
hizi tofauti na mwaka 2005, tukio likitokea haichukui muda mrefu wahusika kutiwa
nguvuni na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria. Napenda kulipongeza Jeshi letu
la Polisi kwa kazi nzuri.
Wakimbizi
Mheshimiwa
Spika,
Mwaka
2005, niliahidi kwamba tutaongeza kasi ya kuwarudisha kwao wakimbizi waliopo
nchini mwetu. Ahadi hiyo tumeitimiza. Katika miaka mitano hii, tumewarejesha
kwao wakimbizi 483,804 na tumefunga kambi
12 za wakimbizi. Vilevile, kwa
kutimiza wajibu wetu wa kihistoria, tuliwapa uraia wa Tanzania wakimbizi 1,423 kutoka Somalia na 160,000 kutoka Burundi walioamua kuomba
uraia wa nchi yetu. Wengi wa ndugu zetu
hawa hawajui pa kwenda huko Burundi.
Mheshimiwa
Spika,
Niliahidi
pia kwamba katika kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu, tutaanza kutoa
vitambulisho vya uraia. Bahati mbaya hatukufanikiwa kuanza kutoa vitambulisho
hivyo, lakini tumefikia hatua nzuri. Ni matarajio yangu kwamba mapema kipindi
kijacho lengo hilo litatimizwa.
HALI
YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika;
Tuliwaahidi Watanzania kwamba katika
miaka mitano ya uongozi wetu, tutaendeleza jitihada za kukuza na kujenga uchumi
wa kisasa na ulio endelevu ili kupunguza umaskini na kuboresha hali zao zao za
maisha. Katika miaka mitano iliyopita tumeendelea kusimamia vizuri sera za
uchumi jumla (macro-economic policies).
Pia tumetunga na kuboresha sera za kisekta, na sheria mbalimbali ili
kurahisisha ushiriki wa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla katika shughuli za
kiuchumi.
Pato la Taifa liliongezeka kutoka shilingi 15.9 trilioni mwaka 2005 hadi shilingi 28.2 trilioni mwaka 2009
kwa bei za miaka husika. Kwa ajili hiyo pato la wastani la Mtanzania
limeongezeka kutoka shilingi 441,030
mwaka 2005 hadi shilingi 693,185
mwaka 2009. Kasi ya wastani ya ukuaji wa
pato la taifa ilikuwa asilimia 6.9 katika
kipindi hicho. Kasi ingekuwa kubwa zaidi
kama uchumi wetu usingekabiliwa na matatizo ya ukame, upungufu mkubwa wa umeme, kupanda sana kwa bei za
mafuta duniani na kudorora kwa uchumi wa dunia.
Kuharibika kwa reli ya kati kulikuwa pigo lingine kubwa kwa ustawi wa uchumi
wetu.
Pamoja na hayo hatuna budi kujipongeza kwani
uchumi wetu kukua kwa asilimia 6
mwaka 2009 na wastani wa asilimia 6.9
kwa miaka mitano hii ni mafanikio ya aina yake.
Ni kielelezo cha uimara na uhimilivu wa uchumi wetu na kuthibitisha kuwa
hatua tulizochukua kuuhami uchumi wetu zilikuwa sahihi. Mtakumbuka kuwa tulitumia shilingi trilioni 1.7 kwa ajili hiyo. Vile vile inathibitisha kuwa mageuzi ya
kiuchumi tuliyoendelea kuyatekeleza tangu miaka ya 1990 yamezaa matunda
tuliyoyatarajia.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
jumla uchumi uliendelea kuwa tulivu.
Karibu viashiria vyote muhimu isipokuwa mfumuko wa bei vilikuwa
imara. Mapato yetu ya fedha za kigeni kutokana
na mauzo ya bidhaa na huduma nchi za nje yaliongezeka kutoka dola milioni 2,994.9 mwaka 2005 hadi dola milioni 4,693.6 mwaka 2009. Akiba yetu ya fedha za kigeni iliongezeka
kutoka dola bilioni 2.21 mwaka 2005
hadi dola bilioni 3.55 mwaka 2009
ambazo zinatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa karibu miezi 6. Katika miaka mitano hii, kudhibiti mfumuko wa
bei ilikuwa changamoto kubwa hasa kuanzia mwaka 2007, ambapo bei za mafuta
zilipanda sana na bei za vyakula pia zilipanda kupita kiasi kwa sababu ya
upungufu uliosababishwa na ukame wa mwaka 2005, 2006 na wa 2009. Mfumuko wa bei ulipanda kutoka asilimia 5 mwaka 2005 hadi asilimia 12.1 mwaka 2009. Kutokana na juhudi tulizozifanya tukisaidiwa
na hali nzuri ya chakula mwaka huu, mfumuko wa bei unaonyesha dalili ya kushuka. Kwa mfano, mwezi Juni mwaka huu mfumuko wa bei
ulishuka na kufikia asilimia 7.2.
Kama hali ya upatikanaji wa chakula nchini na kwa majirani zetu itaendelea kuwa
nzuri na bei za mafuta hazitapanda sana mfumuko wa bei utashuka zaidi.
Mapato na Matumizi ya
Serikali
Mheshimiwa
Spika,
Katika miaka mitano hii, tumeongeza Mapato ya
ndani zaidi ya mara mbili kutoka wastani wa shilingi 177.1 bilioni kwa mwezi mwaka 2005/06 hadi shilingi 390.7 bilioni kwa mwezi mwaka
2009/2010. Hii imetupa uwezo wa kuongeza bajeti ya Serikali kutoka
shilingi trilioni 4.13 mwaka 2005/06
hadi kufikia shilingi trilioni 11.6
mwaka 2010/11. Aidha, tumeendelea kupunguza utegemezi wa wafadhili katika bajeti
ya Serikali kutoka asilimia 44 mwaka
2005/2006 hadi asilimia 28 mwaka
huu, 2010/2011. Hivyo safari ya kupunguza utegemezi tunaifanya kwa mafanikio
kama tulivyoahidi.
Nidhamu ya Matumizi ya
Fedha za Umma
Mheshimiwa Spika,
Mafanikio
kwenye kukusanya mapato ni jambo moja, lakini kuyatumia vizuri mapato hayo ni
jambo jingine. Kama nilivyoahidi, tumefanya jitihada kubwa katika kusimamia
ufanisi katika matumizi ya serikali. Nimeeleza awali hatua tulizochukua
kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuifanya
taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali isomwe na wahusika,
kuzungumzwa na kuifanyia kazi. Pia tumechukua hatua za kubana mianya ya
ubadhirifu na utekelezaji mbovu wa miradi ya Serikali. Nimeagiza kwamba
TAKUKURU na Polisi wahusike mara moja pale Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali anapogundua kuna wizi na ubadhirifu.
Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Mheshimiwa Spika;
Tulipokutana mara ya kwanza, tarehe 30 Desemba,
2005, niliainisha majukumu manane ya Serikali katika kutengeneza mazingira
mazuri kwa uchumi kukua na biashara kustawi. Tumeandaa sera mbalimbali
na kurekebisha baadhi ya sheria ili kuboresha mazingira ya uwekezaji, ukuaji wa
uchumi, na mfumo bora wa fedha. Pia, tumeweka mifumo bora ya kusuluhisha haraka
tofauti na migogoro baina ya wawekezaji au baina ya wafanyabiashara, au tofauti
za kibiashara baina ya mtu na mtu au kampuni na kampuni. Kwa ajili hiyo
tumeimarisha Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara. Aidha, tumeanzisha kitengo cha kusikiliza
malalamiko ya wawekezaji na kuyatafutia ufumbuzi haraka (Investors’ Complaints Bureau) chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu
Kiongozi. Ili kudhibiti na kusimamia viwango vya huduma na bidhaa tumeimarisha Tume
ya Ushindani wa Haki wa Kibiashara, Wakala wa Chakula na Madawa na Shirika la
Viwango Tanzania.
Mheshimiwa Spika;
Katika
kutambua ushiriki wa sekta binafsi katika masuala ya ubia, Serikali imeandaa Sera,
na jana Bunge lako Tukufu limepitisha
Muswada wa Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP).
Lengo ni kuweka bayana mfumo na taratibu zitakazowezesha kufikiwa kwa ufanisi
wa ubia kati ya sekta hizi mbili.
Vilevile, tumeendelea kuimarisha majadiliano kati
ya Serikali na Sekta Binafsi. Kama nilivyoahidi hapa Bungeni, Mabaraza ya
Biashara ya Mikoa na Wilaya yameshaundwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya
kufanya biashara na uwekezaji na kuibua fursa za uwezeshaji kiuchumi. Tunaendelea
kuchukua hatua za kisera na kisheria kwa lengo la kuboresha mazingira ya
uwekezaji na biashara nchini. Shabaha
yetu ni kuona kwamba uwekezaji unaendelea kuongezeka nchini kama ilivyotokea
kati ya mwaka 2005 na 2008 ambapo uwekezaji ulikua kutoka dola za Marekani 568 milioni hadi dola 744 milioni. Mwaka 2009 ulishuka na kuwa dola 550 milioni kutokana na
msukosuko wa uchumi duniani.
Uwezeshaji wa Wananchi
Mheshimiwa Spika,
Uwezeshaji wa wananchi ni moja ya dhima kuu za
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Tuliahidi kuwa Serikali itaendeleza
mifuko na fursa zilizopo na kuanzisha nyingine mpya kwa nia ya kuwawezesha
wananchi kiuchumi. Katika kutekeleza ahadi hiyo, tumeimarisha mifuko iliyopo kama
vile Mfuko wa Vijana, Mfuko wa Akina Mama, Mfuko wa Uwezeshaji wa Wajasiriamali
Wadogo (Small Entrepreneur Loan Facility –SELF), na Mfuko wa Dhamana wa Mikopo
kwa Wafanyabiashara Wadogo (SME Credit
Guarantee Scheme). Tumeanzisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
(Mabilioni ya JK). Kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, tumechangia
sehemu kubwa ya mtaji wa mwanzo wa uanzishaji wa Benki ya Wanawake ambayo
tayari tayari imeanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Mfuko wa Akina Mama umekopesha zaidi ya wanawake
300,000, hadi Mei 2010 Mfuko wa
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ulikuwa umekopesha shilingi 45.2 bilioni na wajasiriamali 67,000
wamenufaika. Halmashauri za Wilaya 128
zimekopesha vijana jumla ya shilingi
1.16 bilioni kutoka Mfuko wa
Maendeleo wa Vijana.
Mipango ya Serikali ya uendelezaji wa sekta
binafsi, uwekezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi imewezesha shughuli za
kiuchumi kupanuka na hivyo kuchochea ongezeko la ajira nchini. Hivyo,
utekelezaji wa ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuhusu kuzalisha ajira milioni
moja umeenda vizuri, kwani hadi kufikia mwezi Juni 2010, ajira 1,313,121 zilikuwa zimezalishwa nchini
kote.
Mheshimiwa Spika,
Vilevile, tumetimiza ahadi yetu ya kuimarisha ushirika
nchini kama nguzo kuu ya kuunganisha nguvu za wanyonge kujiletea maendeleo.
Chini ya uongozi wetu, idadi ya
Vyama vya Ushirika vya aina mbalimbali nchini imeongezeka kutoka 5,730 mwaka
2005 hadi 9,501 mwaka 2010. Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa mfano, vimeongezeka
kwa karibu mara tatu kutoka vyama 1,875
mwaka 2005 hadi 5,344 mwaka 2010. Aidha, akiba na amana za wanachama zimeongezeka zaidi ya mara tano kutoka Shilingi 31.4 bilioni mwaka 2005 hadi shilingi 174.6 bilioni mwaka
2010. Haya ni mafanikio makubwa.
Katika
kipindi hocho Serikali ilibebea mzigo wa madeni ya Vyama vya Ushirika
38 vilivyokuwa vinadaiwa shilingi 26.8 bilioni ili kuviwezesha kupata
mikopo kwenye mabenki. Kulipwa kwa
madeni hayo kunatoa fursa kwa wanachama wa vyama husika kuchukua hatua sahihi
za kuviimarisha Vyama vyao ili viweze kuwahudumia vizuri zaidi.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika,
Ahadi
tuliyoitoa ya kutoa kipaumbele cha juu kwa maendeleo ya kilimo tumeitimiza na matokeo
yake yanaonekana. Mara baada ya kuingia madarakani tukatengeneza na kuanza kutekeleza Programu
ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (Agricultural
Sector Development Programme - ASDP). Aidha, ili kuipa Programu hiyo
msukumo na kuwashirikisha kwa karibu wadau wa sekta binafsi mwaka 2009 tulibuni
mkakati ujulikanao kama Kilimo Kwanza ili kutoa msukumo zaidi wa kuleta
mapinduzi ya kijani nchini. Serikali
imeongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi 233.3
bilioni sawa na asilimia 5.8 ya
bajeti yote ya Serikali mwaka 2005/06 hadi shilingi 903.8 bilioni sawa na asilimia 7.8
ya bajeti yote ya Serikali mwaka 2010/2011. Ni dhamira yetu kuendelea kuongeza
bajeti ya kilimo hadi kufikia asilimia 10 ya bajeti ya Serikali au hata kupita.
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano
iliyopita, tumetimiza ahadi niliyoitoa hapa Bungeni ya kuhakikisha kwamba
upatikanaji na matumizi pembejeo kwa wakulima unaongezeka. Tumeongeza
fedha za ruzuku ya mbolea na pembejeo nyinginezo kutoka shilingi 7.5 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi
143.8 bilioni mwaka 2010/11.
Mbegu Bora
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki, tumefanya
jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora na hasa kutoka hapa nchini. Kwanza, tulichukua hatua za kuimarisha
vituo vya utafiti wa kilimo vinavyofanya uvumbuzi wa mbegu. Pili, tumechukua
hatua za kuongeza uwezo wa kuzalisha mbegu baada ya uvumbuzi wa mbegu
kufanyika. Miongoni mwa hatua hizo ni
kufufua mashamba ya mbegu ya Serikali na kuhusisha Jeshi la Magereza na Jeshi
la Kujenga Taifa. Kutokana na hatua
hizi, uzalishaji wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 10,477.17 mwaka 2005 hadi tani 16,144.79
Desemba 2009. Tatu, kuhakikisha kuea usambazaji wa mbegu bora unakuwa rahisi na
mbegu zinawafikia wakulima kwa bei nafuu. Aidha, tumeimarisha Wakala wa Mbegu (Agricultural Seed Agency - ASA) kwa
ajili ya kusimamia uzalishaji wa mbegu kwa wingi na kuhakikisha zinasambazwa
kwa urahisi na kuwafikia walengwa.
Zana za Kilimo
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii tumeanza kuchukua hatua thabiti
za kuhimiza matumizi ya zana bora za kilimo, hususan matrekta na ukulima wa
kisasa nchini. Tumeendeleza sera ya
kutokuwepo na ushuru wa forodha kwa matrekta.
Kwa sababu hiyo, idadi ya matrekta yaliyoingia nchini katika kipindi cha
2006-2009 ni 1,737; yakiwemo makubwa 362 na madogo (power tillers) 1,379.
Baadhi ya matrekta
yaliyoingizwa nchini yalinunuliwa kutokana na mkopo wa shilingi 16.3 bilioni kutoka Mfuko wa
Pembejeo. Kwa ujumla Mfuko wa Pembejeo
umeongeza utoaji wa mikopo ya zana na pembejeo za kilimo kutoka shilingi bilioni 4.9 mwaka 2005/06 hadi shilingi
30.1 mwaka 2009/2010. Vilevile, tunategemea kuongeza matrekta 3,000 madogo na makubwa kutokana na mkopo wa dola milioni 40 kutoka Serikali ya India.
Hii itafanya idadi ya matrekta yaliyoingia nchini kuwa kubwa kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya
nchi yetu. Tumeimarisha huduma za ugani kwa kuajiri watalaam 1,802 wa kilimo katika Halmashauri, ambao wanafanya kazi ya
kuwapatia wakulima mafunzo juu ya ukulima wa kisasa. Katika mwaka 2009/10 pekee, Halmashauri za
Wilaya zimenunua matrekta madogo 2,154
na makubwa 53. Serikali ilizitaka Halmashauri za Wilaya
kuwa chachu ya mapinduzi ya kilimo kwa kuagiza trekta na kuwauzia wakulima hasa
kwenye vikundi vya uzalishaji.
Mifugo
Mheshimiwa
Spika,
Kwa upande wa mifugo, dhamira yetu imekuwa ni kuboresha mifugo na
ufugaji wetu nchini ili wafugaji nao wafaidike na shughuli ya ufugaji tofauti
na ilivyo sasa. Shabaha hizo ni sehemu
kamili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo kwa upande wa mifugo. Kwa ajili hiyo, katika miaka mitano hii,
tumehimiza utumiaji wa madume bora ili kuongeza ubora wa mifugo yetu. Kwa vile si rahisi kupata madume ya kutosha,
tumehamasisha matumizi ya uhamilishaji.
Kituo cha Taifa cha Uhamilishaji kilichopo Usa River, Arumeru
kimeimarishwa na vituo vidogo vitano vya kusambaza mbegu vimeanzishwa Dodoma,
Mwanza, Lindi, Kibaha na Mbeya.
Tumeajiri maafisa ugani
1500 kusaidia kuelimisha wafugaji juu ya ufugaji bora na kusaidia kutoa huduma
na ushauri wa kusaidia kuboresha mifugo na ufugaji. Wafugaji nao wamenufaika na mpango wa ruzuku
ya pembejeo kwa kupata dawa za kinga na tiba.
Katika kipindi hiki ng’ombe 11,134,000 wamechanjwa kinga ya homa ya
mapafu na shilingi bilioni 13.5 zimetumika
kwa ajili dawa za majosho. Aidha,
majosho 543 yamejengwa, na juhudi zinaendelea za kujenga malambo, mabwawa na
visima ili kuipatia mifugo maji ya uhakika.
Vile vile, juhudi za kuimarisha ranchi za taifa zinaendelea kwa dhati
ikienda sambamba na ujenzi wa viwanda vya kusindika nyama katika maeneo
mbalimbali nchini. Katika juhudi hizi
sekta binafsi inatambuliwa, inashirikishwa na kusaidiwa pale inapostahili au
Serikali inapoombwa kufanya hivyo.
Kwa nia ya kutoa msisitizo
maalum kwa maendeleo ya mifugo nchini, mchakato wa kuanzisha Programu ya
Maendeleo ya Sekta ya Mifugo inayojitegemea umeanza.
Uvuvi
Mheshimiwa
Spika;
Niliahidi hapa Bungeni mwaka 2005 kwamba Serikali nitakayounda
itatoa kipaumbele kwenye sekta ya uvuvi.
Ahadi hiyo tumeitimiza. Niliunda
Wizara mpya ya Mifugo na Uvuvi ili kuupa uvuvi umuhimu unaostahili. Huko nyuma
uvuvi ulikuwa umefichwa chini ya sekta ya maliasili. Vile vile tumeondoa kodi ya zana za uvuvi
zikiwemo boti, nyavu, na injini ili kuwezesha wavuvi kupata zana za kisasa za
uvuvi. Aidha, katika kipindi hiki pia
juhudi za kupambana na uvuvi haramu ziliongezwa. Kati ya mwaka 2006 – 2009 tulivuna samaki
wenye thamani ya shilingi 783.3 bilioni na kuuza nje ya nchi samaki
wenye thamani ya shilingi 597.5 bilioni. Hivi sasa tumeelekeza nguvu zetu katika
kuendeleza ufugaji wa samaki.
Viwanda na Biashara
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii,
sekta ya viwanda iliendelea kustawi vyema.
Kasi ya ukuaji wa sekta hii ulikuwa mzuri na wa kutia moyo. Kati ya mwaka 2005 na 2009 sekta ya viwanda
ikihusisha ujenzi ilikua kwa wastani wa asilimia 8.8, wakati uzalishaji wa bidhaa za viwandani (manufacturing) uliongezeka kwa wastani wa asilimia 9.14.
Viwanda vilivyochangia sana kwenye mafanikio haya ni vile vya sementi,
vifaa vya umeme, vinywaji na usindikaji wa nafaka.
Tumechukua hatua thabiti za
kuchochea uwekezaji kwa ajili ya kuendeleza viwanda nchini. Tulianzisha Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji
kwa Ajili ya Mauzo Nje (Export Processing Zones Authority). Mamlaka hiyo imepewa dhamana ya kusimamia
shughuli za Maeneo ya Uzalishaji kwa Ajili ya Mauzo Nje (EPZ) na Maeneo Maalum
ya Kiuchumi (Special Economic Zones – SEZ).
Kati ya mwaka 2006 na 2008 viwanda 28
vya uzalishaji vimesajiliwa chini ya EPZ.
Mwezi Mei, 2010, Eneo Maalum la Kiuchumi la Benjamin William Mkapa
lilifunguliwa na tayari wawekezaji 12
wameshapatikana. Mauzo ya bidhaa kutoka
kwenye maeneo ya EPZ kwenda nje ya nchi yalikuwa dola za Kimarekani 235 milioni.
Mheshimiwa Spika;
Utaratibu wa EPZ na SEZ
utakuwa chachu ya kuchochea uwekezaji katika viwanda nchini. Ndiyo maana Mikoa na Wilaya zinahimizwa kutenga
maeneo yanayoweza kutumika kwa ajili ya kuanzisha EPZ na SEZ. Baadhi ya mikoa imefanya hivyo na mingine
bado. Nashauri wale ambao bado wafanye
hivyo haraka kwa maslahi ya mikoa yao na nchi kwa jumla.
Madini
Mheshimiwa Spika,
Madini ni
sekta muhimu sana hapa nchini. Ndiyo ya
pili baada ya utalii kwa kuingiza pesa nyingi za kigeni na inatoa ajira kwa
watu wengi. Thamani ya madini
yaliyosafirishwa nje ya nchi mwaka 2005 ilikuwa dola 720.49 milioni namwaka 2009 iklikuwa dola 1,219.06 milioni. Ajira katika uchimbaji mkubwa
iliongezeka kutoka wafanyakazi 7,000 mwaka 2005 hadi 13,000 mwaka 2008.
Hivyo,
kuendeleza sekta hii kwa maana ya uchimbaji mkubwa na mdogo ilikuwa miongoni
mwa vipaumbele vya juu vya Serikali yangu.
Miongoni mwa mambo muhimu niliyoamua kufanya ni kuitazama upya mikataba
ya madini, sera na sheria ya madini. Nia yetu ni kuhakikisha kuwa uwekezaji katika
sekta hii unakua na wawekezaji na wananchi wananufaika sawia.
Niliunda
Kamati chini ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini wakati ule Ndugu
Lawrence Masha, kuitazama upya mikataba ya madini. Kutokana na ushauri wa Kamati, niliagiza
kufanyike majadiliano kati ya Serikali na makampuni ya madini kuhusu kipengele
cha nyongeza
ya asilimia 15 kwenye mtaji wa awali
ambao haujarejeshwa (additional capital
allowance on unredeemed qualifying capital expenditure). Kuwepo kwa
kipengele hicho kulifanya makampuni yasilipe kodi ya mapato, hivyo kuifanya nchi
isipate chochote mpaka mwisho wa uhai wa mgodi.
Lengo letu lilikuwa kuondoa kipengele hicho ili makampuni husika yaweze
kulipa kodi ya mapato mapema inavyostahili.
Nafurahi kusema kuwa tulifanikiwa
katika mazungumzo yetu na makampuni makubwa manne ya uchimbaji madini hapa
nchini. Hivyo basi migodi ya Golden
Pride, Geita Gold Mines na Tanzanite One imekwishaanza kulipa kodi ya
mapato. Baadhi ya migodi ya Kampuni ya
Barrick itaanza kulipa kodi hiyo muda si mrefu kutoka sasa.
Jambo lingine ambalo tulilifanya ni kujenga uwezo wetu wa
ndani wa kukagua uzalishaji katika migodi mikubwa. Kazi hii ilikuwa inafanywa na Kampuni ya Alex
Stewart baada ya mkataba wao kuisha na tulipoamua tusiendelee nao, tukaunda
Wakala wa Kukagua Uzalishaji katika Migodi Mikubwa. Wakala unafanya kazi nzuri ya kubaini gharama halisi za uwekezaji na
shughuli zinazoendelea migodini ili kodi stahiki zilipwe kwa Serikali. Kutokana na hatua hizi mbili mchango wa sekta
ya madini kwenye mapato ya Serikali umeongezeka na utazidi kukua siku za usoni.
Kwa mfano, mwaka 2005 Serikali
ilipata shilingi 457.4 bilioni na mwaka 2008 illipata shilingi 840.0
bilioni.
Mheshimiwa Spika;
Novemba, 2007
niliamua nijumuishe watu wengine kutoka nje ya Serikali katika kazi iliyokuwa
inafanywa na Kamati ya Mheshimiwa Lawrence Masha. Ndipo, nikaunda Kamati ya Rais ya Madini
iliyoongozwa na Mheshimiwa Jaji Mark Bomani ili kuangalia kwa upana zaidi namna
gani tunaweza kuboresha shughuli za sekta hii muhimu kwa manufaa ya wawekezaji
na taifa. Kamati hiyo mbayo baadhi ya Wabunge
walishiriki, ilitoa mapendekezo mazuri ambayo yametusaidia kutengeneza Sera
Mpya ya Madini ya Mwaka 2009 na kutunga Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2010.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa
pongezi na shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Jaji Mark Bomani, Mheshimiwa
Masha na wajumbe wa Kamati zao kwa mchango wao adhimu uliosaidia kujenga
misingi mizuri ya kuwezesha taifa letu kunufaika na rasilimali yake iliyopewa
na Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Spika;
Katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Serikali imeanzisha na kutoa
leseni za uchimbaji mdogo (Primary Mining Licences), na kuwahamasisha waunde
vikundi vya ushirika ili kuweza kuwasaidia vizuri zaidi.
Utalii
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa Utalii, tumeendelea
na jitihada za kuiendeleza sekta hii muhimu na hasa kutangaza vivutio vya
utalii vya nchi yetu katika masoko makubwa duniani. Ni shughuli ya gharama, lakini faida yake ni
kuongezeka watalii na mapato kwa nchi yetu. Tumetunga Sheria ya Utalii ya
mwaka 2008 na Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 2009 kwa lengo la kuboresha huduma
za utalii na kuziba mianya ya uvujaji mapato yatokanayo na utalii. Tumeimarisha
pia miundombinu ya utalii kwa kuvutia uwekezaji katika ujenzi wa hoteli zaidi
za kitalii. Nafurahi kwamba hoteli mpya zimejengwa katika kipindi hiki.
Kutokana na jitihada hizo,
watalii wameongezeka na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola milioni 823.5 mwaka 2005 hadi dola
milioni 1,198.76 mwaka 2008. Mwaka 2009 mapato yalishuka kidogo na kuwa dola
milioni 1,162.8 kwa sababu ya kudorora
kwa uchumi wa dunia na kusababisha watalii kupungua na kukaa nchini kwa siku
chache. Sasa hali inaonekana kuanza
kurejea kuwa ya kawaida hivyo tutegemee kuongezeka kwa watalii na mapato ya
Serikali.
HUDUMA
ZA UCHUMI
Barabara
Mheshimiwa
Spika,
Hatuwezi kujenga mazingira mazuri ya
ukuaji wa uchumi, kuongeza uzalishaji mali, na kuboresha maisha ya Watanzania
kama miundombinu ya usafirishaji ni mibovu na haitoshelezi mahitaji.
Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka
2005 ilituagiza kwamba, ifikapo mwaka 2010, tuwe tumekamilisha kutekeleza
miradi 17 ya barabara kuu. Leo hii,
ninaposimama mbele yenu, kati ya miradi hiyo 17, tumekamilisha miradi 12 na miradi
5 iliyosalia ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Barabara
tulizozikamilisha ni: Singida
– Shelui (km 110), Shelui – Igunga – Nzega (km 108), Nzega – Ilula (km 138),
Muhutwe – Kagoma (km 24), Nangurukuru – Mbwemkuru – Mingoyo (km 190), Mkuranga
– Kibiti (km 121), Pugu – Kisarawe (km 3.6), Chalinze – Morogoro – Melela (km
129), Tunduma – Songwe (km. 71), Kyabakari – Butiama (km 11.4), Dodoma –
Morogoro (km 256), Dodoma – Manyoni (km 127), Buzirayombo – Kyamyorwa (km.120)
na Buzirayombo – Geita (km.100).
Mheshimiwa
Spika;
Ndani ya miaka hii mitano,
tumekamilisha ujenzi wa miradi ya barabara 26 zenye urefu wa kilomita 2,237. Sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa miradi ya barabara 28 zenye urefu wa kilomita 2,208. Kwa jumla lengo la kuiunganisha Mikoa yote ya
Tanzania kwa barabara za lami lina mwelekeo mzuri. Hivi sasa katika mikoa ya Mtwara, Lindi,
Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Tabora kuna kazi ya ujenzi wa barabara inayoendelea au
mchakato wa kuanza kazi hiyo umefikia hatua ya kuanza utekelezaji wake. Katika Barabara za Mikoa, kilomita 121 zimejengwa kwa kiwango cha lami; kilomita 1,979.4 zimefanyiwa matengenezo katika
kiwango cha lami na kilomita 3,114 zimefanyiwa
ukarabati kwa kiwango cha changarawe.
Katika
kipindi hiki, pia madaraja 8,385 yalifanyiwa matengenezo ya kuzuia
uharibifu na madaraja 660
kufanyiwa matengenezo makubwa. Aidha, Madaraja 53 yamejengwa likiwemo Daraja la Mpiji, Daraja la Ruvu na Daraja la
Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbiji.
Usanifu wa kina wa baadhi ya
madaraja umekamilika na kusubiri pesa zipatikane ili ujenzi uanze. Daraja la Mto Kilombero ni miongoni mwa
madaraja hayo. Tumenunua vivuko vipya 5 na kukamilisha ujenzi wa
vivuko 2. Nafurahi kwamba kero kubwa
zilizokuwepo Kigamboni, Busisi, Pangani na Kome sasa zimeisha.
Mheshimiwa Spika,
Pesa
nyingi tulizotenga katika mfuko wa barabara na kuzigawa kwenye Halmashauri za
Wilaya zimesaidia kuimarisha barabara za Wilaya na Vijiji. Kwa jumla, jitihada na hatua zote hizi
tulizochukua zimesaidia kuwezesha barabara nyingi nchini kupitika mwaka
mzima.
Reli
Mheshimiwa
Spika,
Nyote ni mashahidi kwamba tumehangaika sana na Reli
zetu mbili za TAZARA na Reli ya Kati katika kipindi hiki cha miaka mitano. Kwa
miaka kadhaa Reli reli zetu hizi zilikuwa na matatizo mengi na kusababisha
huduma za uchukuzi wa abiria na mizigo kuathirika. Kiini cha tatizo ni uendeshaji
usioridhisha. Kwa ajili hiyo, Serikali
ya Awamu ya Tatu iliamua kutafuta kampuni ya uendeshaji wa reli ije isaidie
kuendesha Reli yetu ya Kati. Hivyo
ikapatikana kampuni ya RITES ya kutoka India.
Wakati ule iliaminika kuwa kampuni hiyo ingesaidia kupata jawabu kwa
tatizo linaloisibu reli yetu. Bahati
mbaya matarajio yetu hayakuwa, ndiyo maana tumelazimika kufanya uamuzi
tulioufanya wa kuanza mazungumzo na wabia hao ili Serikali ichukue tena reli
hiyo na kutafuta namna nyingine iliyo bora ya kuiendesha reli yetu.
Kwa upande wa reli ya TAZARA, mazungumzo kati yetu
na Zambia yanaendelea kuhusu kupata ufumbuzi wa tatizo la uendeshaji wa reli
hiyo. Katika mazungumzo hayo pia na
marafiki zetu wa China waliotusaidia kuijenga reli hiyo tumewahusisha. Naamini baada ya muda si mrefu tutapata
ufumbuzi.
Nishati
Mheshimiwa
Spika,
Miaka mitano hii ilijawa na changamoto tele kwa upande wa
sekta nzima ya nishati. Tulikabiliwa na
tatizo kubwa la upungufu wa umeme kwa sababu ya ukame lililotufundisha
kupunguza utegemezi kupita kiasi kwa umeme wa maji. Tumeongeza uzalishaji wa umeme kutokana na
gesi asilia kwa megawati 145 pale Ubungo na Tegeta. Hivi sasa mchakato unaendelea wa kujenga
kituo kingine cha MW 100 Ubungo kitakachotumia gesi asilia na cha MW 60 Mwanza kitakachotumia mafuta ya
dizeli. Bahati mbaya mipango ya
kuzalisha MW 300 Mtwara kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay haukuweza kutekelezwa kwa
sababu wabia wetu walijitoa kutokana na msukosuko wa uchumi wa dunia. Umeme wa MW 200 kutokana na makaa ya mawe ya
Kiwira umecheleweshwa na taratibu za milki ambazo karibuni zitamalizika.
Tarehe 12 Juni, 2008, Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya
Umeme Na. 10 ya 2008 ambayo imetoa fursa pana kwa sekta binafsi kushiriki
katika uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini. Utaratibu huu mpya umepata
mwitikio mzuri. Nimeambiwa kuwa tayari wawekezaji
binafsi wanne (4) wameshafikia makubaliano na kuingia mikataba ya kuiuzia umeme
TANESCO. Naamini katika miaka mitano ijayo wawekezaji wengi binafsi
watajitokeza kuwekeza katika sekta hii, hivyo kupunguza hofu ya upungufu wa
umeme.
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano
iliyopita, tumefanikiwa kuyapatia umeme makao makuu ya wilaya za Serengeti,
Ukerewe, Mbinga, Simanjiro, Ludewa, Mkinga, Kilolo, Uyui, Kilindi na Bahi. Mipango
ya kuzipatia umeme Wilaya za Bukombe, Longido, Ngorongoro, Kasulu, Kibondo na
Nkasi ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Jitihada za kuunganisha mikoa
ya Ruvuma, Kigoma, Kagera na Rukwa kwenye gridi ya Taifa zinaendelea.
Mwaka 2007 Oktoba,
tulianzisha Wakala wa Nishati Vijijini ukiwa na jukumu la kuongeza kasi ya kupeleka
umeme vijijini. Tumepata mafanikio ya
kutia moyo kama inavyothibitishwa na kazi ya kupeleka umeme kwenye Makao Makuu
ya Wilaya. Aidha, tangu Wakala
ilipoundwa mwaka 2007 hadi sasa zaidi ya
vijiji 180 vimepatiwa umeme kwa gharama ya shilingi 9.4 bilioni. Kazi inaendelea.
Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mheshimiwa
Spika,
Kwa
upande wa ardhi na makazi nako tumepiga hatua. Kati ya Januari 2006 na Mei 2010
tumefanikiwa kupima na kutoa hati kwa jumla ya vijiji 6,129. Kwa sababu hiyo idadi ya vijiji vilivyopimwa na kusajiliwa vimefikia
10,682. Hii ni sawa na asilimia 97 ya vijiji 11,000
nchini. Mtakubaliana nami kwamba haya ni mafanikio makubwa.
Vilevile,
tumeendelea na mpango wa
matumizi ya ardhi, wa kupima mashamba ya wanavijiji na kutoa Hatimiliki za
Kimila. Jumla ya Hatimiliki za Kimila 54,393 zilitayarishwa na kutolewa kwa wananchi katika Wilaya za majaribio za
Mbozi, Babati, Bariadi, Namtumbo na Manyoni. Wananchi wameanza kunufaika kwa
kuzitmia hati hizo kama dhamana ya mikopo katika mabenki. Kwa mfano, hadi Desemba 2009, wananchi kadhaa
wa Mbozi waliweza kukopa shilingi bilioni
10.38 kutoka benki kwa kutumia hatimiliki hizo. Hii ni habari njema kwa
upande wa uwekezaji wa wananchi.
Mheshimiwa Spika;
Vilevile, kati ya Januari 2006 na
Mei 2010, tumepima viwanja
37,458
katika
maeneo ya miji mbalimbali. Ili kuharakisha utoaji wa hati za kumiliki ardhi, tumeanzisha
kanda 6 za ardhi nchini zenye mamlaka ya kutoa hati hizo. Vilevile, chini
ya Programu ya MKURABITA jumla ya nyumba 290,000 katika miji ya Dar es Salaam,
Mwanza, Dodoma, Tanga na Moshi zilitambuliwa na wamiliki kupewa leseni za
makazi ambazo wanaweza kuzitumia kama dhamana kuombea
mikopo katika taasisi za fedha. Huu ni
mfano mwingine wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia
Mheshimiwa
Spika,
Katika miaka mitano hii tumeboresha mazingira ya
kuendeleza sekta ya mawasiliano nchini.
Ujenzi wa mkongo wa taifa ulioanza Februari, 2009 unaendelea vizuri na
kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa, ifikapo Juni, mwakani, Makao Makuu
ya Mikoa na ya Wilaya zote yatakuwa yamefikiwa.
Katika kipindi hiki, watumiaji wa simu za mikononi wameongezeka kutoka milioni
3.5 hadi milioni 16. Watumiani wa simu za mkononi wataongezeka na gharama za simu
zitashuka baada ya kukamilika kwa ujenzi
wa mkongo kigae.
Mheshimiwa Spika;
Tumeanzisha mpango wa kutumia teknolojia ya habari
na mawasiliano kuendeleza elimu nchini.
Mpango uitwao Tanzania Beyond
Tomorrow au “Tanzania Baada ya Kesho” chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, una lengo la kufanya hivyo.
Katika mpango huo walimu na wanafunzi katika shule za sekondari watawezeshwa
kupata na kutumia kompyuta. Mpango huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi
yetu, hivyo tutafanya kila tuwezalo ufanikiwe.
HUDUMA
ZA JAMII
Maji
Mheshimiwa
Spika,
Mara
tulipoingia madarakani, ili kuhakikisha tunaongeza upatikanaji wa maji mijini
na vijijini tukaanzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inayotekelezwa kwa vipindi vya miaka mitano
mitano kuanzia mwaka 2007-2025. Utekelezaji wa Programu hii umetuwezesha
kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 53.7 mwaka 2005 hadi asilimia 60.1
mwaka 2010. Kwa mijini tumefikia asilimia 84
kutoka asilimia 74 mwaka 2005.
Katika kipindi hiki tumefanikiwa kukamilisha
ujenzi wa mradi mkubwa wa upelekaji maji katika miji ya Shinyanga na Kahama na
vijiji vinavyopitiwa na bomba hilo. Watu wapatao milioni moja wananufaika. Aidha, tumefanikiwa kuziwezesha Mamlaka za
Maji katika Manispaa 13 kati ya Manispaa 19 zilizopo kujitegemea kwa gharama zote za uendeshaji na matengenezo. Bado
tuko nyuma ya lengo la kufikia asilimia 65
vijijini na asilimia 90 mijini
ingawaje kazi itakayofanyika mpaka mwisho wa mwaka katika bajeti yetu ya tano
itatufikisha mahali pazuri kiasi.
Huduma
ya Afya
Mheshimiwa
Spika,
Maisha bora kwa kila Mtanzania
ni pamoja na watu kuwa na afya bora.
Katika kipindi hiki tulitengeneza Sera Mpya ya Afya na kutengeneza
Mpango wa miaka kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) kwa ajili ya kutekeleza
sera hiyo. MMAM una malengo makuu
yafuatayo:-
(a)
Kusogeza huduma ya afya karibu na
wanapoishi wananachi, hivyo zahanati na vituo vya afya vitajengwa vijijini na
kwenye kata. Hospitali za Wilaya na
Mikoa zitaboreshwa ili matatizo mengi ya afya yamalizikie huko.
(b)
Kuongeza wataalamu wa afya wa kada zote kwa maana ya kupanua fursa za
mafunzo na ajira.
(c) Kuboresha upatikanaji wa dawa,
vifaa tiba na mahitaji mengine.
(d)
Kuongeza nguvu katika kupambana na maradhi hasa yale yanayoua na kusumbua
watu wengi.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki bajeti ya afya imeongezeka
kutoka shilingi 271 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi 1,205.9 bilioni mwaka 2010/11, yaani kutoka asilimia 6 ya bajeti hadi asilimia 10.4. Zahanati 1,403,
vituo vya afya 167 na hospitali 24
zimejengwa. Hospitali zote za Wilaya
zimepatiwa X-ray na ultrasound isipokuwa wilaya 7 ambazo nazo zitapatiwa hivi
karibuni. Karibu hospitali zote za Mikoa
zina maabara za kisasa. Wanafunzi wa
taaluma mbalimbali za afya wameongezeka kutoka 1,059 mwaka 2005 hadi 4,422
mwaka 2010. Madaktari bingwa
wameongezeka kutoka 46 mwaka 2005
hadi 265 mwaka 2009. Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza kufundisha
madaktari na mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu kipya cha Tiba pale Mloganzila
karibu na Dar es Salaam umeanza.
Mheshimiwa Spika;
Mfumo wa upatikanaji wa dawa
umeboreshwa. Hivi sasa vituo hupata dawa
kulingana na mahitaji. Mapambano dhidi
ya malaria na UKIMWI yamezidi kuongezewa nguvu.
Kutokana na kuongeza upatikanaji wa vyandarua vilivyotiliwa dawa bure
kwa watoto wote wa chini ya miaka mitano na kwa hati punguzo kwa akina mama
wajawazito, na matumizi ya dawa mseto, vifo kutokana na malaria vimepungua
kutoka 80,000 – 100,000 kwa mwaka hadi
40,000 – 50,000. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika
kutokomeza malaria kwa maana ya kuua mbu wanaosababisha malaria. Kutokana na uhamasishaji wa kujikinga dhidi
ya maradhi ya UKIMWI na upimaji wa hiari, kiwango cha maambukizi kimeshuka
kutoka asilimia 7.7 mwaka 2005 hadi
aslilimia 5.6 mwaka 2009. Watu milioni 11 wamejitokeza kupima UKIMWI
tangu kampeni ya upimaji wa hiari tuliyoizindua Julai, 2007.
Tumeanza kupata mafanikio kwa upande wa kujenga
uwezo wetu wa ndani wa kupambana na maradhi ya saratani, moyo na figo. Juhudi zinaendelea kupanua uwezo huo na
kuendeleza kwa maradhi mengine.
Elimu
Mheshimiwa
Spika,
Katika
hotuba yangu ya kuzindua Bungeni hili nilisema kuwa “Hakuna taifa lililopata maendeleo bila kuendeleza elimu. Hivyo kuendeleza
elimu nchini itakuwa agenda muhimu ya serikali ya Awamu ya Nne.”
Mheshimiwa
Spika,
Nasimama
mbele ya Bunge hili nikiwa na faraja kubwa kutokana na mafanikio makubwa
tuliyoyapata kwenye sekta ya elimu nchini.
Tumepanua elimu ya awali na msingi.
Wanafunzi wa awali wameongezeka kutoka 638,591 mwaka 2005 hadi 825,465
mwaka 2010. Shule za msingi zimeongezeka
kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 15,816 mwaka 2010 na wanafunzi
wameongezeka kutoka 7,541,208 hadi
8,419,305 katika kipindi hicho. Upanuzi huu umewezesha asilimia 97 ya watoto wanaostahili kupata elimu
ya msingi wameandikishwa na uwiano wa kijinsia wa 1:1 umezingatiwa. Tumeajiri
walimu wapya 6,028 wa shule za awali
na 49,694 wa shule za msingi.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa
kushirikiana na wananchi, katika kipindi cha miaka mitano hii, tumeweza kujenga
shule za sekondari 2,171 ikilinganishwa
na shule 1,202 zilizojengwa toka
uhuru mpaka mwaka 2005. Lengo la sekondari moja kwa karibu kila kata
limetekelezwa na baadhi ya kata zina shule zaidi ya moja. Shule za sekondari za binafsi zimeongezeka
kutoka shule 531 hadi 856 katika kipindi hicho. Ongezeko hili
limewezesha idadi ya wanafunzi wanaosoma sekondari kuongezeka toka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,638,669 mwaka 2010. Aidha, idadi ya
wanafunzi wanaosoma kidato cha tano imeongezeka kutoka 9,710 mwaka 2005 hadi 33,169 mwaka 2010. Pia tumeajiri walimu
wapya wa Sekondari 14,329. Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010
tumejenga nyumba 15,343 za walimu,
ambapo nyumba za walimu wa shule za msingi ni 9,910 na nyumba za walimu wa
Sekondari ni 5,424.
Mheshimiwa
Spika,
Upanuzi huu mkubwa wa elimu ya
sekondari umezaa changamoto zake hasa za upungufu wa walimu, vitabu, vifaa vya
kufundishia, maabara na nyumba za walimu.
Kuna mipango thabiti inayoendelea kutekelezwa kukabili kila moja ya
changamoto hizo. Upanuzi wa mafunzo ya
walimu katika vyuo vikuu umeongeza walimu wanaohitimu kutoka 500 mwaka 2005 hadi 5,339 mwaka 2009. Kuna mpango kabambe wa kukabili upungufu wa
vitabu na vifaa vya kufundishia, maabara pamoja na uhaba wa nyumba za
walimu. Nyongeza kubwa ya bajeti ya
elimu kutoka shilingi 669.5 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi 2,045.3 bilioni mwaka 2010/11 ni ushahidi wa utashi wa kisiasa wa kuboresha
elimu nchini. Naamini katika miaka
michache ijayo matatizo yatapungua sana na mengine yatakuwa yameisha.
Mheshimiwa
Spika,
Katika
miaka mitano hii tumeshuhudia upanuzi mkubwa wa elimu ya juu nchini. Azma yetu ya kujenga chuo kikuu kipya
imetimia tena kwa mafanikio makubwa. Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza na ujenzi
wa majengo ya Chuo hicho unaendelea kwa kasi kubwa. Chuo hiki ni fahari ya nchi yetu kwani tumekibuni
wenyewe na kukijenga kwa kutumia fedha zetu wenyewe bila msaada kutoka
nje. Katika miaka mitatu ya mwanzo ya
Chuo hicho tayari kuna wanafunzi 15,000
na lengo la wanafunzi 40,000
litafikiwa.
Idadi
ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu vya umma na binafsi nchini
imeongezeka kwa karibu mara tatu, kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi 117,068
mwaka 2009. Katika kipindi hiki fedha za
mikopo ya wanafunzi zimeongezeka kutoka shilingi 56.1 bilioni mwaka 2005/06
hadi shilingi 197.3 bilioni mwaka 2009/10 na kuwa shilingi 237 bilioni mwaka 2010/11. Wanafunzi wanaonufaika na mikopo wameongezeka
kutoka 16,345 hadi 69,981.
Tumeanza kuchukua hatua za kurekebisha kasoro za utoaji wa mikopo hiyo.
Hifadhi
ya Mazingira
Mheshimiwa
Spika,
Niliahidi
kwamba tutafanya jitihada kubwa ya kuhifadhi mazingira kwa ajili ya maendeleo
endelevu ya nchi yetu. Niliunda Kamati ya Mazingira ya Baraza la Mawaziri chini
ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais,. Tulitoa
maelekezo kadhaa kuhusiana na uboreshaji wa mazingira kwa Wizara na Halmashauri
za wilaya na miji kutekeleza. Nafurahi maelekezo
hayo hususan yahusuyo mifuko ya plastiki na kutunza vyanzo vya maji
yametekelezwa na yanaendelea kutekelezwa. Kwa jumla mwamko wa watu wa kuhifadhi
mazingira unazidi kukua. Tumefanikiwa pia
kuiongezea Wizara inayohusika na Mazingira uwezo na mamlaka ya usimamizi.
Michezo, Burudani na Utamaduni
Mheshimiwa Spika,
Tuliahidi kuendeleza shughuli za michezo na
utamaduni. Tumerudisha michezo mashuleni ili tujipe fursa ya kubaini vipaji vya
watoto wetu na kuviendeleza. Nimetimiza ahadi yangu ya kumgharimia mwalimu wa
mpira wa miguu wa Timu ya Taifa Stars kutoka nje. Kocha Marcio Maximo kutoka Brazil aliajiriwa
na amesaidia sana kuinua kiwango cha
soka hapa nchini. Tanzania imepanda
kutoka nafasi ya 172 Desemba 2005
hadi nafasi ya 108 Aprili 2010. Mimi naamini kama tutaongeza juhudi
tupo karibu kufanikiwa zaidi.
Tumeshapata
makocha wa riadha na ngumi. Nimekubali
ombi la CHANETA kumlipia kocha wa mchezo wa netiboli. Hivi karibuni nilisaidia kugharimia kambi ya
mazoezi na posho za wachezaji wa Twiga Stars ili waweze kushiriki vizuri katika
mashindano ya soka la wanawake Afrika. Ushindi wao ni fahari ya nchi yetu.
Tutaendelea kuwasaidia ili waendelee kupeperusha Bendera yetu kwa mafanikio makubwa
zaidi.
Nafurahi kwamba kupitia Taifa Stars moyo wa uzalendo
umezidi kuongezeka miongoni mwa Watanzania.
Tofauti na ilivyokuwa zamani, ni jambo la kawaida kuwaona Watanzania
wakivaa jezi za timu yetu ya taifa au wakienda uwanjani wakiwa wanapeperusha
bendera yetu ya taifa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa wasanii hasa wa muziki, katika miaka
mitano hii tumeshuhudia kukua na kustawi kwa muziki wa kizazi kipya na uigizaji
wa filamu. Nasikitishwa sana na hali ya
wasanii kutokupata malipo ya haki kwa kazi zao.
Niliamua nijaribu kusaidia. Nilipokutana
na baadhi ya wana muziki wa kizazi kipya wakanieleza haja ya wao kuwa na mastering
studio yao ili waweze kumiliki kazi zao.
Nimeshawanunulia mtambo huo uliogharimu shilingi 50 milioni. Hivi sasa tumelipia
mtaalamu mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam asaidie kutengeneza njia
bora ya kusambaza kazi za wasanii wa muziki na filamu ili wapate malipo halali
kwa jasho lao. Mafanikio ya zoezi hili
yatatufundisha namna ya kuwasaidia wasanii wa fani nyingine pia.
Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa
Spika,
Katika
miaka mitano hii, tumepata mafanikio makubwa katika medani ya Kimataifa. Uhusiano wetu wa kiuchumi na kisiasa na
mataifa na mashirika ya kimataifa duniani umepanuka na kuimarika zaidi katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo tunaweza
kuiita adui. Nchi rafiki na mashirika ya
kikanda na kimataifa yameendelea kuunga mkono juhudi zetu za kujiletea
maendeleo. Tumepata misaada mingi ya maendeleo na kupata misamaha ya madeni tunayodaiwa
na hivyo kutupunguzia mzigo wa kulipa madeni hayo.
Uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umekuwa
ukiongezeka, wigo wa masoko ya nje umekuwa unapanuka kwa bidhaa zetu na watalii
kutoka nje wamekuwa wanaongezeka. Hakika
diplomasia ya uchumi imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Hadhi ya Tanzania katika medani za kimataifa
imepanda. Tunasikilizwa, tunaaminiwa, na
tunathaminiwa. Kwa upande wa ajira
katika mashirika ya Kimataifa, hakuna mafanikio makubwa kushinda yale ya dada
yetu Dkt. Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa. Ni heshima kubwa na fahari kwa
nchi yetu na wanawake wa Tanzania. Hakika
wanawake wakipewa fursa wanaweza.
Mheshimiwa
Spika;
Katika
kipindi hiki tulibahatika kutembelewa na wageni wengi mashuhuri na wengine ni
wa kihistoria kutembelea nchi yetu. Tulitembelewa na Rais George Bush wa
Marekani, Rais Hu Jintao wa China, Rais Abdullah Gul wa Uturuki, Rais wa
Ireland, Mary McAleese, ambaye alipata pia fursa ya kulihutubia Bunge hili,
Waziri Mkuu wa Zamani wa nchi hiyo Bertie Ahern, Rais Innancio Lula da Silva wa
Brazil, Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, Waziri Mkuu wa Canada, Bw. Stephen Harper, Waziri Mkuu wa
Norway, Jens Stoltenberg, Malkia wa Denmark, Margrethe II, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki-moon,
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa, Dkt. Asha-Rose Migiro na Gavana wa
Australia. Tumepokea Marais wengi wa Afrika kuja kututembelea. Yote haya yanadhihirisha kiasi gani
diplomasia ya Tanzania imefanikiwa.
Mheshimiwa
Spika,
Tanzania
imeendelea kushiriki vyema katika Umoja wa Afrika, SADC na Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Kwa upande wa Umoja wa Afrika
tumepata heshima kubwa mwaka 2008 ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja huo. Tuliifanya kazi hiyo vizuri kiasi cha kufanya
baadhi ya viongozi wenzangu kufikiria tuendelee kwa mwaka mmoja zaidi. Nilikataa kwa kusisitiza kanuni ya kila
kiongozi kuwa Mwenyekiti kwa muda wa mwaka mmoja.
Kwa upande wa SADC, tumeendelea kushiriki kwa
ukamilifu katika shughuli zote za Jumuiya hiyo ambayo inazidi kuimarika.
Kwa
upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika miaka mitano hii tumeshuhudia
utangamano ukizidi kuimarika na manufaa ya kiuchumi kwa Tanzania yakishamiri. Umoja wa Forodha umefikia hatua yake ya juu
Januari 1, 2010 baada ya bidhaa za kutoka Kenya nazo kuruhusiwa kuingia katika
masoko ya nchi wanachama bila ya ushuru.
Tarehe 1 Julai, 2010, Soko la Pamoja limeanza na matayarisho ya Umoja wa
Sarafu yameanza.
Mheshimiwa
Spika;
Jumuiya
ya Afrika Mashariki imekuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania kuliko
vile tulivyotazamia wote. Mwaka 2005 Tanzania
iliuza katika soko la Afrika Mashariki bidhaa zenye thamani ya dola za Kimarekani
milioni 161. Mwaka 2008 iliuza bidhaa za dola milioni 353.1, na mwaka 2009 mauzo
yalipungua hadi dola milioni 272.1 kutokana
na mtikisiko wa uchumi. Na, ukweli ni kwamba bado hatujatumia
ipasavyo uwezo wetu na fursa zilizopo.
Tuendelee kujipanga vizuri kuna manufaa makubwa zaidi mbele yetu.
Hitimisho
Mheshimiwa
Spika,
Nimezungumza
kwa muda mrefu, sasa naomba nifikie mwisho. Yapo mambo mengi muhimu ambayo
ningependa kuyazungumzia, mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokabiliana
nazo, lakini natambua kwamba wapo Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wanataka
kuwasha magari jioni hii hii na kuwahi majimboni.
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu, naomba kuwashukuru
kwa kipekee viongozi wa nchi yetu walionitangulia. Tumeendelea kuongoza nchi hii kwa mafanikio
makubwa kwa sababu ya misingi madhubuti iliyojengwa na waasisi wa nchi yetu: Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume. Pia, natambua mchango, ushirikiano na msaada
wa ushauri wanaonipa Marais Wastaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee
Benjamin William Mkapa ambao nao wakati wa uongozi wao liendeleza juhudi za ujenzi
wa taifa letu kwa umahiri mkubwa.
Aidha, ningependa kurudia shukrani zangu
za dhati kwa Watanzania wenzangu, kwenu Waheshimiwa Wabunge wote, kwa kazi
nzuri tuliyoifanya kwa kushirikiana katika miaka mitano iliyopita. Watanzania
hatuna hulka ya kuyashikia bango na kuyasheherekea mafanikio yetu. Lakini kwa
mafanikio tuliyoyapata katika miaka mitano iliyopita, ukizingatia mazingira
tuliyopitia, tuna kila sababu ya kujipongeza. Naamini wananchi watatambua na
kutuamini tena tuwaongoze.
Mheshimiwa Spika;
Wenzetu
katika mataifa mengine wanatuona kama mfano wa kuigwa barani Afrika na wako
tayari kutusaidia katika jitihada zetu. Hata hivyo, tusibweteke na sifa hizo.
Bado kazi kubwa ipo mbele yetu. Nina
imani kabisa kwamba kama Mwenyezi Mungu akiendelea kutujalia, na akituepusha na
majanga ya hali ya hewa na mengineyo, na akabariki kazi za mikono yetu na akili
zetu, tutapiga hatua kubwa zaidi na kwa kasi zaidi kuisukuma nchi yetu kwenye
neema tele na watu wake kwenye maisha yaliyo bora. La muhimu kwetu ni kudumisha
amani na utulivu, tuendelee kupendana sisi kwa sisi, tuipende nchi yetu na
tujenge umoja na mshikamano. Wote tufanye
kazi kwa bidii na maarifa kwani maisha bora hayatadondoka kama mana katika
Jangwa la Sinai.
Mheshimiwa Spika,
Tunaelekea kwenye uchaguzi. Wengi wenu
hapa mnaingia kwenye kinyang’anyiro. Nataka niwatakie kila la heri. Nami
mnitakie heri ili tukutane tena Bunge lijalo na kipindi kijacho. Wananchi sasa ndio wakati wao wa kuamua. Sisi
katika Serikali tumejiandaa na vyombo vyote husika vimejiandaa kwa uchaguzi huu
kuwa wa amani, huru na wa haki kama ilivyo sifa ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge,
Nawashukuru
sana kwa kunisikiliza!
Mungu
Ibariki Afrika.
Mungu
Ibariki Tanzania.