HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO  WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA HAFLA YA KUKABIDHI HATI IDHINI KWA VYUO VIKUU NA VYUO VIKUU VISHIRIKI,  IKULU, DAR ES SALAAM TAREHE, 18 AGOSTI, 2010

 

Mheshimiwa Jumanne Maghembe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;

Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi;

Katibu Mtendaji wa Tume;

Wakuu wa Vyuo Vikuu;

Viongozi Wenzangu;

 Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana:

          Nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunishirikisha katika hafla hii ya kukabidhi Hati Idhini za kuviidhinisha rasmi vyuo vikuu 09 kutoa elimu ya juu hapa nchini.  Hafla hii ni kielekezo dhahiri cha mafanikio tuliyoyapata katika maendeleo ya elimu ya juu hapa nchini.  

          Napenda kuchukua nafasi hii kuvipongeza vyuo vyote ambavyo leo nimevikabidhi Hati Idhini za kuviruhusu rasmi kutoa elimu ya juu.  Hongereni sana.  Hii ni hatua kubwa katika maendeleo ya vyuo vyenu na maendeleo ya elimu nchini.  Ni jambo la fahari kubwa kwetu sote na ni jambo la kutia moyo kwamba dhamira yetu ya kuwawezesha vijana wetu wengi kupata elimu ya juu ina mwelekeo mzuri.  Wahenga waliosema elimu ni ufunguo wa maisha hawakukosea, kwani sisi kama nchi mwelekeo wetu sasa ni kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na watu wengi wenye elimu nzuri ili kufungua milango ya kuliletea taifa maendeleo ya haraka.  Dira ya Maendeleo inalenga nchi yetu kutoka kuwa nchi maskini na kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka wa 2025.  Lakini hatutafika huko kama hatutafanikiwa kuwapata Watanzania wenye elimu nzuri tangu ya msingi mpaka elimu ya juu. 

Mheshimiwa Waziri na Wageni Waalikwa;

           Mtakubaliana nami kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumepata mafanikio makubwa katika kupanua elimu.  Tumefanya upanuzi mkubwa wa elimu katika ngazi zote, kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na mpaka elimu ya juu.  Vile vile, Elimu ya Watu Wazima na Elimu Maalumu nazo zimepewa msukumo mkubwa. Mafanikio haya makubwa yamepatikana kwa kushirikisha wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo ya elimu kama vile MMEM, MMES na MEMKWA.

Ndugu Wageni Waalikwa;

          Kwa upande wa maendeleo ya elimu ya juu pia tumepata mafanikio ya kutia moyo.  Tumeongeza idadi ya vyuo vikuu kutoka 26 mwaka 2005 hadi 33 mwaka 2009 ambapo kwa sasa vyuo vikuu vya binafsi vipo 21 na vya Serikali 12.  Ongezeko hili la vyuo vikuu nchini limewezesha idadi ya Wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu kuongezeka kutoka 55,296 mwaka 2005 hadi 118,000 mwaka 2009. 

          Tumefanikiwa kufikisha idadi hiyo kubwa ya wanafunzi katika vyuo vikuu kutokana pia na ufadhili unaotolewa na Serikali kwa wanafunzi. Serikali iliongeza fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kutoka shilingi 56.1 bilioni mwaka 2005 hadi shilingi 243 bilioni mwaka 2010. Ongezeko hili la fedha limewezesha idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo kuongezeka kutoka wanafunzi 16,345 mwaka 2005 hadi wanafunzi 69,250 mwaka 2009. Pamoja na juhudi za kuwezesha wanafunzi wengi kupata mkopo hiyo, hapana budi hatua zaidi zichukuliwe kuyapatia ufumbuzi malalamiko yahusuyo utaratibu wa kukubaliwa kupata mkopo na uchelewashaji wa malipo. Nilishaagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Fedha na Bodi ya Mikopo kushirikiana kumaliza matatizo hayo.  Naamini tutaanza mwaka mpya wa masomo na mambo mapya mazuri.  Aidha, ofisi yangu kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi itafuatilia kwa karibu mchakato huo. 

Ndugu Wageni waalikwa

          Sisi serikalini tumejipanga vyema kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu (MMEJU) ambao tumeanza kuutekeleza. Ni mategemeo yetu kuwa utekelezaji wa Mpango huo utasaidia kuimarisha na kuboresha elimu ya juu kwa kiwango kikubwa.      Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itasimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu (MMEJU) ili malengo yake yaweze kufikiwa. Chini ya mpango huu tunategemea kufanya yafuatayo:

1.    Kukarabati, kupanua na kuimarisha miundombinu ya vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki ili viweze kuhimili ongezeko kubwa la wanafunzi watakaomaliza elimu ya sekondari.

2.    Kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya elimu ya juu na           kuhamasisha wanafunzi wa kike idadi ifikie asilimia 40 ya wanavyuo         wanaodahiliwa kila mwaka.

3.    Kuandaa wahadhiri wa kutosha na wenye sifa za kufundisha kwenye vyuo vya elimu ya juu.

4.    Kuunganisha vyuo vikuu na taasisi za utafiti kwenye mtandao mmoja ili kuimarisha utafiti wa pamoja, kupanua elimu katika kiwango cha uzamili na uzamivu.

5.    Kuratibu na kusimamia utoaji wa Elimu ya Juu iliyo bora na kufanyika kwa utafiti ili ziweze kutatua matatizo ya kijamii na kiuchumi.

6.    Kuimarisha mazingira ya utoaji wa Elimu ya Juu na maslahi yanayoendana nayo ili wahadhiri wavutiwe kujiunga na kubaki katika vyuo vya Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu.

7.    Kuimarisha utoaji wa Elimu ya Juu kwa njia ya Masafa na Elimu Mtandao.

8.    Kuimarisha uwezo wa watendaji katika usimamizi na menejimenti ya programu za elimu katika ngazi zote.

          Tukitekeleza malengo haya, kama taifa tutakuwa tumepiga hatua kubwa. Ni mategemeo yangu kwamba vyuo na taasisi husika vitajipanga vyema katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango huu wa maendeleo ya elimu ya juu.

Mheshimiwa Waziri na Ndugu Wakuu wa Vyuo;

          Upanuzi wa elimu ya juu umeleta changamoto zake kama ilivyo kwa sekondari na msingi.  Kubwa kati ya changamoto hizo ni uhaba wa wakufunzi wenye sifa stahiki wa kufundisha katika vyuo hivyo.  Natambua na kuwapongeza kwa jitihada kubwa mnazozifanya za  kukabiliana na changamoto hii kubwa.  Napenda kutumia nafasi hii kurudia ushauri wangu nilioutoa siku za nyuma kuwa vile vyuo vyetu vyenye Wahadhiri na Maprofesa wa kutosha katika fani mbalimbali kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro, na Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili,  wapanue,  waimarishe na waboreshe programu zao za uzamili na uzamivu.  Kwa kufanya hivyo tutapata wahitimu wengi wenye sifa stahiki za kufundisha kwenye vyuo vyetu vikuu.

          Naomba niwakumbushe na kusisitiza umuhimu wa vyuo vikuu kujikita katika masuala ya utafiti. Sifa moja nyingine kubwa ya Chuo Kikuu zaidi ya ile ya kufundisha ni kufanya utafiti.  Naomba vyuo vikuu kuhakikisha kwamba vinatoa kipaumbele cha juu kwa shughuli za utafiti.  Vyuo viwe na mikakati maalum na mipango kazi mizuri ya kufanya tafiti za namna mbalimbali zitakazonufaisha vyuo kitaaluma na kuliwezesha taifa letu kusonga mbele kimaendeleo. 

Kwa kutambua umuhimu wa utafiti na kwa nia ya kusaidia kuendeleza shughuli za utafiti, sisi katika Serikali tumetenga shilingi bilioni 30 kwa ajili ya utafiti katika maeneo mbalimbali. Huu ni mwanzo tu, tutaendelea kuongeza fedha hizo hatua kwa hatua mpaka tufikie lengo letu la kutenga asilimia moja ya bajeti ya Serikali kwa ajili ya shughuli za utafiti. Ni jukumu lenu sasa kujipanga vizuri  ili muweze kutumia fursa hiyo kwa manufaa ya vyuo vyenu na taifa.

Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wageni Waalikwa

          Kabla sijamaliza hotuba yangu, napenda nichukue nafasi hii kuipongeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania kwa jinsi inavyokabiliana na changamoto mbalimbali katika kuboresha elimu ya juu katika nchi yetu.   Nafurahi kusikia kwamba mmekamilisha mfumo wa kutambua viwango vya elimu na taaluma mbalimbali, ziwe za ndani au nje ya nchi unaojulikana kama National Qualifications Framework.  Nawapongeza kwa kuanza kutumia mfumo wa mtandao kudahili wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu nchini. Natambua mwanzo ni mgumu, kutakuwepo na mapungufu yake.  Kinachotakiwa ni kuondoa kasoro hizo na kuuboresha.    Ni matumaini yangu kuwa mahitaji maalum ya kujali makundi mbalimbali katika jamii yatazingatiwa.  Si busara kuwa na mfumo ambao hautajali mazingira maalum ya jamii na nchi yetu na kusababisha makundi fulani kukosa fursa ya elimu ya juu. 

Nimefarijika sana kusikia kuwa mmeweza kutoa mafunzo mbalimbali kwa viongozi wa vyuo vikuu ili kuwajengea uwezo wa kuweza kuvisimamia na kuviendeleza vyuo vyao ili kukidhi mahitaji ya Taifa kielimu.  Nawasihi muendelea na juhudi zenu  hizo maradufu.  Katu msirudi nyuma na wala msikubali kukatishwa tamaa.   Uboresheni mpango huu na kama hapana budi siku za usoni tuangalie uwezekano wa kufanya mafunzo haya kuwa sharti la kupewa nafasi ya uongozi katika vyuo au kuendelea nao.

Mheshimiwa Waziri, Wakuu wa Vyuo  na Wageni Waalikwa;

          Mwisho kabisa, nachukua fursa hii kwa mara nyingine, kuwashukuru wenzetu wa sekta binafsi kwa jinsi walivyoitikia wito wa kuanzisha vyuo vya elimu ya juu nchini.  Mmeonyesha mfano mzuri kwa kuiunga mkono Serikali katika kuendeleza elimu hapa nchini. Napenda tu nitoe tahadhari kwamba mjiepushe kusukumwa na tamaa na kupata faida kubwa bali kutoa huduma kwa jamii.  Elimu ikigeuka biashara ya kumpatia mtu faida nono itakuwa hatari. Viwango vyetu vya ada vitakuwa vikubwa mno na havitaendana na hali halisi ya uwezo wa wananchi wengi kumudu kuipata.  Elimu kuwa kwa wachache ni hatari kwa jamii kwani hata Serikali itashindwa kuwasaidia wengi kupitia Bodi ya Mikopo.  Kama suala la viwango vya ada lipo kenye mamlaka ya TCU basi lisimamamieni ipasavyo na, kama halina chombo cha kulisimamia, nadhani wakati umefika litafutiwe chombo.  Lazima tufanye hivyo, vinginevyo tutakosa mwelekeo mzuri katika masuala ya elimu, kitu ambacho ni hatari kwa maendeleo yetu kama taifa.

Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na wageni waalikwa

          Baada ya kusema hayo, naomba kuwatakia kila la heri katika shughuli zenu za kutoa na kusimamia elimu.

 

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA