HOTUBA
YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
Ndugu
Wananchi,
Naomba
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukutana kwa mara nyingine
tena na kuzungumza kwa mujibu wa utaratibu wetu mzuri wa kuzungumza kila mwisho
wa mwezi. Mwisho wa mwezi uliopita
hatukuweza kuzungumza kwa sababu nilikuwa
Siku
ya leo nataka kuzungumzia jambo moja tu, nalo ni Muswada wa Sheria ya Gharama
za Uchaguzi uliopitishwa na Bunge letu tukufu katika kikao chake
kilichopita. Hivi karibuni nitatia saini muswada huo kuwa
Sheria. Kwa sasa matayarisho ya shughuli
hiyo yanaendelea.
Ndugu
Wananchi;
Chimbuko
la kutungwa sheria hii ni mwenendo usiyoridhisha wa matumizi ya fedha katika chaguzi
zetu nchini. Kuna matumizi mabaya ya
fedha katika uchaguzi ndani ya vyama vya
siasa na baina ya vyama vya siasa katika chaguzi za kiserikali. Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge tarehe
30 Desemba, 2005, nilizungumzia kutokuridhishwa kwangu na hali hii na nilielezea
nia yangu ya dhati ya kutaka kuchukua hatua thabiti za kuweka utaratibu
utakaoongoza na kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi. Naomba ninukuu maneno niliyosema siku
ile:
“Jambo lingine linalonisumbua linahusu upatikanaji
na matumizi ya fedha na michango mingine kwenye Uchaguzi. Yameanza kujitokeza
mawazo, pamoja na kuanza kujengeka utamaduni kuwa uongozi unaweza kununuliwa
kwa fedha. [............] tusipokuwa waangalifu nchi yetu inaweza kuwekwa
rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za
kufanya hivyo. Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika
kufanikisha uchaguzi, kwa kila chama na kwa kila mgombea. Lakini, fedha
kutumika kununua ushindi si halali. Kwa maoni yangu hatuna budi kupiga vita
utamaduni huu kwa nguvu zetu zote. Ni vema sasa tuanzishe mjadala wa kitaifa na
hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea
kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali ulio wazi, wa chama au mgombea
kutumia fedha hizo. Na utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya
uchaguzi katika uchaguzi wa kiSerikali na ndani ya vyama vya Siasa.” Mwisho wa kunukuu.
Ndugu
wananchi,
Jambo
hili tumekuwa tunalifanyia kazi Serikalini tangu tuingie madarakani. Kwa vile ni jambo jipya na kwa nia ya kuepuka
kuanza vibaya, tumefanya utafiti wa kutosha na kujifunza kutoka mifano ya nchi
ambazo zina utaratibu wa aina hii.
Kadhalika, hapa nchini, tuliwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi
wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi zisizo za kiserikali, Tume ya
Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa na watu wengine wengi.
Ndugu Wananchi;
Matokeo ya
kazi hiyo nzuri ni kutengenezwa kwa Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ambao
uliwasilishwa katika kikao kilichopita cha Bunge kwa uamuzi. Kabla ya kupelekwa Bungeni, rasimu ya Muswada
huu ilijadiliwa kwa kina Serikalini.
Pale Dodoma Bungeni, muswada huu ulijadiliwa kwa siku kadhaa katika
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na kwenye vikao vya
Kamati za Vyama vya Siasa. Katika jamii
nako, Muswada huu uliibua mijadala iliyokuwa na hisia za namna mbalimbali na
wakati mwingine mijadala hiyo ilikuwa mikali.
Kwa ujumla, mijadala yote hiyo ilisaidia
kuboresha maudhui ya Muswada na hatimaye kupata ule uliopitishwa na Bunge letu
Tukufu tarehe 11 Februari, 2010.
Ndugu Wananchi;
Tumetunga
Sheria hii mpya kwa nia ya kupata majawabu kwa tatizo la matumizi mabaya ya
fedha katika shughuli za uchaguzi. Tunatambua kuwa matatizo haya si mageni, yamekuwepo
tangu miaka mingi huko nyuma na hata historia ya Bunge letu ina ushahidi wa
ushindi wa baadhi ya Wabunge kutenguliwa kwa makosa ya rushwa.
Lakini, siku hizi matatizo ya matumizi mabaya ya fedha yamekuwa makubwa
zaidi na yanakua kwa kasi inayotishia kugeuzwa kuwa ndiyo utaratibu wa kawaida au
utamaduni katika chaguzi zetu. Ni hali
ambayo haifai kuachwa kuendelea na kuzoeleka.
Hatuna budi kuchukua hatua za dhati kurekebisha mambo na kulirejesha
taifa katika mstari ulionyooka.
Ndugu Wananchi;
Tuliamua kuwa, hatua muafaka ya kuchukua ni hii ya kutunga sheria ya
kuongoza na kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi. Sheria hii ikitekelezwa ipasavyo itazuia
kugeuza uongozi kuwa ni kitu cha kununuliwa
Misingi ya Sheria
Ndugu
Wananchi,
Katika kufikiria na kutayarisha rasimu
ya muswada wa sheria hii, mambo saba ya msingi yalizingatiwa. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1.
Kuutambua kisheria mchakato wa uteuzi wa
wagombea ndani ya vyama vya siasa na kuusimamia kisheria.
2.
Kuweka utaratibu wa kisheria
utakaosimamia na kuratibu mapato na kudhibiti matumizi pamoja na gharama za
uchaguzi kwa vyama vya siasa na wagombea.
3.
Kuweka viwango
kwa matumizi na gharama za uchaguzi.
4.
Kuweka utaratibu utakaosimamia mapato
na matumizi ya vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na zawadi, misaada na michango
itakayotolewa na wagombea au wahisani wakati wa kampeni za uchaguzi.
5.
Kudhibiti michango na zawadi kutoka
nje ya nchi.
6.
Kuweka utaratibu na mfumo wa udhibiti
na uwajibikaji kwa mapato na matumizi ya fedha za uchaguzi kwa upande wa vyama vya siasa na wagombea.
7.
Kuainisha adhabu kwa watakaokiuka
masharti yatakayowekwa na Sheria hii.
Uteuzi
Ndani ya Vyama Umetambuliwa
Ndugu
Wananchi,
Katika
Sheria ya Gharama za Uchaguzi, mambo yote hayo ya msingi yamezingatiwa. Ni Sheria inayojitosheleza kwa kila hali
pamoja na ukweli kwamba ni mara ya kwanza tunakuwa na sheria ya namna hii.
Sheria
yetu mpya imezitambua rasmi gharama zinazotumika na vyama vya siasa na wagombea
kuanzia wakati wa mchakato wa uteuzi ndani ya vyama mpaka wakati wa uchaguzi
wenyewe. Sheria hii sasa inafafanua gharama za uchaguzi kuwa ni zile
zinazotumika na Vyama, Wagombea au Serikali wakati wa uteuzi ndani ya vyama, wakati
wa uteuzi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, wakati wa kampeni na hadi siku ya kupiga
kura.
Ndugu
Wananchi;
Kabla
ya Sheria hii kutungwa, matumizi mabaya ya fedha wakati wa uteuzi wa wagombea katika
vyama vya siasa yalionekana kuwa ni matatizo ya ndani ya vyama husika, hivyo yaliachiwa
vyama vyenyewe kushughulika nayo wajuavyo.
Kwa mujibu wa Sheria yetu mpya mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya
vyama umetambuliwa rasmi kuwa ni sehemu kamili ya uchaguzi, hivyo matumizi ya
fedha ya vyama na wagombea yametengezewa utaratibu wa udhibiti. Kwa hiyo, kuanzia sasa kuhonga au kuhongwa
katika mchakato wa uteuzi ndani ya vyama kutamulikwa kwa karibu na wahusika
wataadhibiwa na vyombo vya dola.
Uwazi wa Mapato na Matumizi
Ndugu
Wananchi;
Jambo lingine
muhimu katika Sheria hii ni kwamba, inaweka sharti la uwazi katika mapato na
matumizi ya vyama na wagombea kwa ajili ya uchaguzi
kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Sheria pia inaelekeza utaratibu wa kufuatwa
na vyama na wagombea katika kutoa taarifa zao za mapato na matumizi ya
uchaguzi. Kila mgombea, kwa mfano, atatakiwa
kutoa kabla ya uchaguzi, taarifa ya fedha alizonazo na makisio ya fedha
anazotarajia kupata kwa ajili ya kampeni na uchaguzi, ndani ya siku saba (7)
baada ya uteuzi wa wagombea kufanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Baada
ya uchaguzi atatakiwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi halisi siku tisini
(90) baada ya matokeo kutangazwa.
Ndugu Wananchi;
Vyama vya siasa,
navyo hali kadhalika, vitatakiwa kutoa taarifa ya mapato
Uwazi wa Michango
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa michango
ya hiyari na zawadi zinazotolewa kwa Chama na wagombea, Sheria inataka pawepo
na uwazi katika utoaji wake. Sheria inaelekeza
kwamba, kila chama cha siasa kilichopokea mchango unaozidi shilingi milioni
moja kutoka kwa kila mchangiaji binafsi au shilingi milioni mbili kutoka kwa
taasisi, kitoe taarifa kwa Msajili. Aidha, Sheria inataka fedha hizo zihifadhiwe
katika akaunti maalum itakayofunguliwa kwa ajili hiyo. Fedha hizo zitalipwa na
kutumika kutoka katika akaunti hiyo.
Naomba
ieleweke kuwa, si nia ya Sheria hii kuzuia wananchi kuchangia shughuli za siasa
au za kampeni za Chama wakipendacho au mgombea wanayempenda. Sheria inaruhusu michango ya aina yoyote
kutolewa kwa chama chochote au kwa mgombea yeyote ila inataka michango hiyo
itolewe kwa utaratibu ulio wazi. Kusiwe
na usiri au kificho cha namna yoyote.
Ndugu Wananchi;
Sheria pia inafafanua
utaratibu wa vyama au wagombea kupata misaada kutoka nje ya nchi. Sheria inazuia
michango na misaada hii isitolewe wakati wa kampeni. Inaruhusu vyama vya siasa au wagombea kupokea
misaada kutoka nje ya nchi siku 90 kabla ya Uchaguzi Mkuu au siku 30 kabla ya
uchaguzi mdogo. Pia, inataka kuwepo
uwazi na taarifa itolewe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Najua suala la
masharti yaliyowekwa kwa watu wa nje kuchangia vyama vya siasa na wagombea
nchini lilizua mjadala miongoni mwa wadau mbalimbali. Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya
vyama vya siasa kupinga masharti yaliyowekwa.
Naomba ieleweke kuwa, kwa kweli,
si jambo jema kwa Chama cha siasa au mgombea nchini kufadhiliwa na watu wa
nje. Wahenga wanasema “anayemlipa mpiga zumari huchagua wimbo”. Ipo hatari kwa kiongozi au chama kupokea amri
kutoka nchi za nje kwa kuwasikiliza wale watu wa nje waliowasaidia badala ya
kujali maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Uwajibikaji Kuhusu
Michango
Ndugu Wananchi,
Sheria pia
inaweka sharti la uwajibikaji wa vyama vya siasa, wagombea na washiriki wengine
kuhusu michango, mapato na matumizi katika uchaguzi. Sheria inaelekeza kwamba:-
1. Kila mchango
unaopokelewa na matumizi yatakayofanyika kwa ajili ya uchaguzi vifanywe na
Chama na siyo vinginevyo.
2. Chama cha
siasa kitawajibika kwa matumizi yote yatakayofanywa na chama au wagombea wake,
na kwamba matumizi yote yanatakiwa kuwa na risiti.
3. Kila mgombea atawekewa
mgawo wake wa matumizi ya kampeni na chama kitatoa taarifa ya fedha iliyokaguliwa
kwa matumizi hayo.
4. Chama
kitakachoshindwa kutunza taarifa hizo kitakuwa kimetenda kosa na kitastahili
adhabu.
5. Kila mgombea
atakayepokea mchango atapaswa kutoa taarifa kwa chama chake kuhusu mapato na
matumizi yanayohusu mchango huo.
6. Kila chama cha
siasa, taasisi ya kiraia, taasisi ya kidini au taasisi ya kijamii itakayohusika
katika kuchangia shughuli za uchaguzi, inayo wajibu wa kutunza taarifa za fedha zinazoelezea mapato
na matumizi
Mambo haya ni muhimu
Mambo Yaliyokatazwa
Ndugu Wananchi;
Sheria
imeainisha vizuri mambo yanavyokatazwa kwa upande wa matumizi ya fedha za
uchaguzi. Sheria inakataza, kwa mfano, vitendo vifuatavyo visifanyike pamoja na
matumizi ya fedha kwa ajili hiyo kuzuiliwa:
1. Kufanya malipo
kwa wapiga kura ili wamchague mgombea fulani;
2. Kuahidi kazi
au cheo au wadhifa kwa mpiga kura ili amchague mgombea;
3. Kutoa zawadi,
ahadi, mkopo, au makubaliano yoyote kwa mpiga kura ili amchague mgombea;
4. Kukubali
kurubuniwa kwa mambo yoyote yaliyotajwa hapo juu ili ampigie kura mgombea
yeyote;
5. Kufanya
vitendo vyovyote kati ya hivyo wakati wowote kabla au hata baada ya uteuzi wa
mgombea;
6. Kutoa malipo kwa
ajili ya takrima ya chakula, vinywaji au starehe yoyote kwa ajili ya
kuwashawishi wapiga kura wamchague mgombea;
7. Kuwasafirisha
wapiga kura ili wamchague mgombea. Hata hivyo Sheria inaruhusu wapiga kura
wenyewe kujilipia nauli kwenda kupiga kura au Serikali kuwasafirisha wapiga
kura pale ambapo kuna shida ya usafiri;
8. Kuweka mkataba
wowote ule wa pango kwa niaba ya wapiga kura ili wamchague mgombea;
Chama au
mgombea au mtu yeyote atakayetenda vitendo hivi nilivyovitaja atakuwa ametenda
kosa kwa mujibu wa Sheria hii na ataadhibiwa ipasavyo.
Viwango vya Gharama
za Uchaguzi
Ndugu Wananchi,
Sheria ya
Gharama za Uchaguzi inaweka utaratibu wa kudhibiti gharama za uchaguzi kwa
kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya uchaguzi kuweka viwango vya gharama za
uchaguzi. Waziri huyo atatangaza kiwango cha juu ambacho kila mgombea ataweza
kutumia katika kampeni na katika uchaguzi. Kiwango hicho cha gharama
kitazingatia tofauti ya majimbo, idadi ya watu, aina ya wagombea pamoja na
miundombinu. Chama au mgombea atakayevuka viwango vya mtumizi alivyowekewa bila
maelezo ya kuridhisha, atakuwa ametenda kosa na anastahili kuwajibishwa
ipasavyo.
Utaratibu huu ni
muhimu katika kujenga nidhamu na usawa miongoni mwa vyama na wagombea katika
uchaguzi. Hivi sasa kwa sababu ya
kutokuwepo ukomo, wako watu wenye pesa ambao wanafanya matumizi kupita
kiasi. Wapo wanaopitiliza au hata
kukufuru na kuwadhalilisha wenzi wao wasiokuwa na uwezo
Ndugu Wananchi,
Mimi naamini, hatua zilizomo katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi
zikitekelezwa, zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au hata kudhibiti kabisa vitendo
na hisia za rushwa katika uchaguzi. Mara
nyingi vitendo hivyo vinapofanyika, au hata kule kuwepo hisia tu kwamba
vinaweza kuwa vimefanyika, huwa ni chanzo cha manung’uniko na kukosekana
utulivu. Wakati mwingine huathiri taswira
ya demokrasia yetu na heshima ya uongozi uliochaguliwa hasa pale uhalali wa
matokeo ya uchaguzi unapotiliwa shaka. Tunachukua
hatua hizi ili kulinda hadhi ya chaguzi zetu nchini na kuzifanya kweli ziwe huru
na za haki na kufanya mfumo wa demokrasia uzidi kustawi. Hatima ya yote haya tufanyayo ni kusaidia
nchi yetu kuwa na viongozi wanaotokana na ridhaa ya wananchi.
Ndugu
zangu;
Demokrasia ya vyama vingi katika nchi yetu
bado ni changa. Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa nne tangu turudi kwenye mfumo
wa vyama vingi mwaka 1992. Ni muhimu
Mafanikio ya dhamira yetu njema yanategemea
Ndugu
Zangu, Wananchi Wenzangu,
Nimetumia muda wenu mwingi kuwadokeza
baadhi ya mambo ya msingi yaliyomo katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Nia yangu ni kufanya mambo matatu
muhimu.
Pili,
kuwathibitishia kuwa sisi wenzenu tuliopo katika Serikali tunatambua wajibu
wetu wa kuhakikisha kuwa Sheria hii inatekelezwa kwa ukamilifu.
Nimekwishaviagiza vyombo vya dola, ikiwemo TAKUKURU, kujipanga vizuri kuisimamia
Sheria hii na kuwabana ipasavyo wale wote watakaojihusisha na vitendo vya
rushwa kuanzia katika uchaguzi wa mwaka huu. Nawaomba wananchi mtoe ushirikiano
kwa vyombo vyote vinavyohusika na usimamizi wa Sheria hii ili vitimize kwa
ukamilifu malengo yake ambayo yana maslahi kwa nchi yetu na kwetu sote.
Tatu,
napenda kuwaambia kwamba, sisi
katika Serikali tunatambua wajibu wa kuhakikisha kuwa wananchi, wanachama na
viongozi wa vyama vya siasa wanaelimishwa vya kutosha ili waielewe vizuri
Sheria hii. Umuhimu wa kuielewa vizuri
Sheria hii hauhitaji kusisitizwa kwani watu wakiielewa vizuri inarahisisha
utekelezaji wake. Na, kwa vyama vya
siasa na wagombea, uelewa mzuri utasaidia kuepuka makosa ambayo yanaweza kuwa na gharama
kubwa ya wao kupoteza ushindi. Natambua kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa na Ofisi ya Waziri Mkuu wanajiandaa vizuri kwa ajili ya kutoa elimu kwa
umma kuhusu maudhui ya Sheria hii muhimu.
Nawaomba ndugu wananchi tusikilize kwa makini ufafanuzi watakaoutoa kwa
manufaa yetu na ya nchi yetu.
Ndugu
Wananchi;
Naomba
nimalize hotuba yangu kwa kuwashukuru kwa mara nyingine tena kwa kuendelea kuiunga
mkono Serikali yetu. Naomba tuendelee kushirikiana
katika utekelezaji wa Sheria hii muhimu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza
demokrasia katika nchi yetu. Nataka kuona
katika chaguzi zetu nchini tunajenga utamaduni wa kushindanisha sera za vyama na
uwezo wa wagombea kuliko kushindanisha uwezo wa kukusanya fedha za kampeni.
Asanteni
kwa kunisikiliza!
Mungu
Ibariki Afrika
Mungu
Ibariki