HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA

TANZANIA, MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA

WANANCHI, TAREHE 31 MEI, 2006

 

UTANGULIZI

 

Ndugu Wananchi;

 

          Katika hotuba zangu za kila mwisho wa mwezi, kwa Taifa, nimekuwa nazungumzia masuala muhimu ya Kitaifa na wakati mwingine ya Kimataifa yenye maslahi kwa nchi yetu.  Kuna baadhi ya mambo nimekuwa nikiyazungumzia mara kwa mara kama vile upungufu wa chakula, matatizo ya umeme, bei kubwa ya mafuta na ujambazi.

 

          Nimekuwa nafanya hivyo kwa sababu ya unyeti wa masuala hayo na kwamba jitihada za kuyatafutia ufumbuzi zilikuwa zinaendelea.  Kila wakati nimekuwa nikiwafahamisha hatua mbalimbali ambazo Serikali imekuwa inachukua au inajiandaa kuchukua katika kukabiliana na matatizo yote hayo.

 

Ndugu Wananchi;

 

          Kwa vile matatizo hayo bado yapo, hata leo pia nimeonelea nitumie fursa hii kuyazungumzia ili nanyi muweze kuelewa hali halisi ilivyo hivi sasa. Aidha, nitawafahamisha hatua tunazoendelea kuchukua katika kukabiliana na matatizo hayo yote.

 

 

 

 

 

 

Shukrani

 

Ndugu Wananchi;

 

          Sina budi kuwashukuru sana kwa mara nyingine tena kwa uvumilivu wenu, utulivu wenu na uelewa wenu wa matatizo yanayotukabili sote kama taifa.  Moyo wenu mnaounesha wa kutambua ukweli kuhusu matatizo yanayotukabili unanipa nguvu mimi na wenzangu serikalini kuwatumikia kwa uwezo wetu wote.  Nawashukuruni nyote.  Ahsanteni sana!

 

Hali ya Chakula Nchini

 

Ndugu Wananchi;

 

          Naomba nianze na suala la chakula.

Kwa jumla, hali ya upatikanaji wa chakula nchini bado ni tatizo kwani bado Wananchi wenzetu wengi wanaishi kwa kutegemea chakula cha msaada kutoka Serikalini na kwa wafadhili wengineo.

 

          Hivi sasa Serikali inaendelea kuwahudumia wananchi wenzetu wenye shida.  Kwa ajili hiyo tunaendelea kusambaza tani 42,000 za chakula cha msaada kwenye maeneo yenye upungufu.  Kwa mujibu wa hali ya mvua ilivyokuwa msimu huu kuna dalili kwamba huenda mavuno yakawa mazuri kwa sehemu kubwa ya nchi yetu.  Yatakuwepo maeneo machache yatakayokuwa na upungufu ambao hautakuwa kero kubwa.  Matumaini yetu ni kwamba mgawo wa sasa wa chakula cha msaada utakuwa ndio wa mwisho ulio mkubwa kutoka Serikalini kabla ya mavuno.

 

 

 

Ndugu zangu;

 

Wananchi Wenzangu;

 

          Tatizo la uhaba wa chakula lililoikumba nchi yetu msimu huu limetufundisha mengi, na hasa yapo mafunzo makubwa mawili. Kwanza; kwamba kuwa na Hifadhi ya Taifa ya Chakula yenye akiba ya kutosha ni jambo la msingi na muhimu sana. 

 

          Nimekuwa najiuliza kama tungekuwa hatuna akiba ya kutosha ya chakula katika hifadhi ya Taifa ya Chakula hali yetu ingekuwaje mwaka huu.  Naamini ingekuwa mbaya sana lakini, hifadhi ya taifa ya chakula imetuepusha na balaa hilo.  Hivyo basi ni lazima wakati wote tuwe na akiba ya kutosha ya chakula ambayo tunaweza kuitumia pindi tunapokuwa na dharura au maafa kama haya ya ukame.  

 

          Hivyo basi, katika msimu ujao wa mavuno tutahakikisha kuwa tunanunua chakula cha kutosha na kukihifadhi kwenye maghala ya Hifadhi ya Chakula ya Taifa (SGR) yaliyoko sehemu mbalimbali hapa nchini.   Utaratibu huu umetufaa sana safari hii hivyo tutafanya kila tuwezalo kuudumisha na kuuendeleza.

 

          Nafurahi kusema kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika ameshaanza kuchukua hatua kuhakikisha kuwa Hifadhi ya Taifa ya Chakula inayo akiba ya kutosha.  Nia yetu ni kuwa na akiba ya chakula ya kutosha wakati wote bila kujali kama tumepata mvua za kutosha ama la.

 

 

 

Ndugu Wananchi;

 

          Jambo la pili kubwa tulilojifunza linahusu hali ya kilimo chetu.  Ni jambo lililo wazi kuwa kilimo chetu bado ni duni na hakina tija ya kutosha.  Hali hii inasababisha matatizo kila tunapokosa mvua hata kama kwa msimu mmoja kama ilivyokuwa safari hii.  Bado kilimo chetu hakituwezeshi kuhimili dharura kama hii ya ukame.

 

          Tumedhamiria kuchukua hatua za dhati kuboresha kilimo chetu.  Kwa ajili hiyo tuko mbioni kukamilisha mkakati kabambe wa kuendeleza kilimo nchini.  Naamini tukifanikiwa katika utekelezaji wa programu zake tutakuwa tumejenga ngome kubwa ya kupambana na upungufu wa chakula.

 

 

Hali ya Umeme

 

Ndugu Wananchi;

 

          Tatizo la umeme bado halijaisha ingawa kumekuwepo na unafuu katika siku za hivi karibuni ikilinganishwa na miezi ya nyuma.  Bado hali ya maji katika bwawa la Mtera ni mbaya ingawaje kina kimepanda kwa mita tatu tu hadi kufikia mita 690 tangu msimu wa mvua uanze.  Kina hicho ni pungufu kwa mita nane (8) na msimu wa mvua ndiyo umefika ukiongoni.  Kutokana na hali hii ni dhahiri basi kwamba tutalazimika kuendelea na mgao wa umeme mpaka hapo hatua za dharura za kuongeza uzalishaji wa umeme utokanao na gesi zitakapokamilika.

 

 

Watanzania Wenzangu;

 

          Naomba tuendelee kuwa na subira wakati ambapo mipango ya kupata ufumbuzi wa muda mfupi, wa kati na muda mrefu inaendelea kushughulikiwa.  Tena kwa taarifa nilizopewa mipango hiyo inakwenda vizuri.  Tayari utaratibu wa kuipatia TANESCO mitambo mipya ya megawati 100 itakayofungwa pale Ubungo umekamilika.  Uagizaji wa mitambo hiyo utafanyika wiki chache zijazo baada ya  kukamilisha taratibu za manunuzi. 

 

          Pia, inatarajiwa wiki hii TANESCO na Serikali zitakamilisha mazungumzo kuhusu uagizaji toka nje wa mitambo ya kukodisha ya megawati 100.  Wakati huo huo maandalizi ya awali ya mradi wa umeme wa Kinyerezi na ule wa makaa ya mawe kule Kiwira yanaendelea vizuri.

 

Wananchi Wenzangu;

 

          Napenda kurudia kauli yangu ya huko nyuma kwamba: Naamini kuwa mara baada ya kukamilisha miradi yote hii nchi yetu itapata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la umeme ambalo limekuwa ni kero kubwa kwa miaka kadhaa sasa.

 

Ndugu Wananchi;

 

          Katika hotuba zangu za nyuma nimekuwa nikielezea tatizo la bei kubwa ya mafuta duniani.  Nilipolizungumzia mara ya kwanza mwezi Januari mwaka huu kwenye mkutano wangu na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, nilielezea hofu ya tatizo kuzidi kuwa kubwa.

 

           Nilielezea ukweli kwamba ni tatizo ambalo hatuna uwezo nalo kulizuia kwani hatuna mafuta hapa nchini na uchumi wetu hauwezi kuhimili kutoa ruzuku ya bei ya mafuta.  Nimekuwa nawasihi wananchi wenzangu kuutambua ukweli huo na kwamba tujitahidi kuwa waangalifu na wabanifu katika matumizi ya mafuta. Na leo napenda kusisitiza tena ombi hilo kwenu. 

 

Ndugu Wananchi;

 

          Tatizo la kupanda sana kwa bei za mafuta ni la dunia nzima.  Linaziathiri nchi zote na sisi tukiwemo.  Tanzania pekee haina uwezo nalo.  Naomba sote tulielewe hivyo na tuendelee kama nilivyosema kuwa waangalifu na wabanifu katika matumizi ya mafuta.  Kama tutapata mwanya wowote wa kupunguza makali ya bei ya mafuta tutautumia.

 

          Aidha napenda kuitumia nafasi hii kuwaonya watu wenye tamaa ya utajiri iliyokithiri wasitumie fursa hiyo kudhulumu.  Si sawa,  si haki na ni kukosa utu kufanya hivyo.  Kwa kweli si jambo jema hata kidogo kwa mtu au kampuni kutumia shida za wananchi kupata utajiri wa haraka haraka.  Naziomba mamlaka zinazohusika na nishati (EWURA) na usafiri (SUMATRA) hapa nchini kusimamia ipasavyo masuala ya bei za mafuta na nauli za mabasi na vyombo vingine vya usafiri ili kuhakikisha kuwa taratibu zinazingatiwa ipasavyo.

 

Ujambazi

 

Ndugu Wananchi;

 

          Mapambano dhidi ya ujambazi na majambazi yanaendelea kwa nguvu, ari na kasi ile ile.  Hatutalegeza uzi hata kidogo.  Tayari tumewanyima majambazi fursa ya kutamba kama ilivyokuwa siku za nyuma na kila siku tunazidi kuwabana zaidi na kupata ushindi.

 

          Napenda kuwahakikishia Wananchi wenzangu, kuwa tutaendelea kupambana nao hadi ushindi kamili.  Mwelekeo wa ushindi ni mzuri na sasa tunakaribia kuuvunja uti wa mgongo wa ujambazi.  Navipongeza sana vyombo vyetu vya usalama kwa kazi nzuri waifanyayo na wananchi kwa ushirikiano wenu mkubwa.

 

          Tuendeleze ushirikiano huo mzuri ili tupate ushindi mapema.  Kwa upande wake Serikali itaendelea kuviimarisha vyombo vya usalama kwa nyenzo na utaalamu ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu na kwa ufanisi mkubwa zaidi.

 

MAMBO MAPYA

 

Ziara Nchi za Nje:

 

Ndugu Wananchi;

 

          Katika miezi ya hivi karibuni nimekuwa nikifanya ziara za kujitambulisha kwa nchi rafiki na majirani. Majuzi nimemaliza  ziara ya nchi za Falme za Kiarabu, Ufaransa, Marekani na Uingereza.  Pamoja na kujitambulisha kama kiongozi mpya wa Taifa letu, madhumuni makubwa ya ziara hizi za nje ni matatu.

         

1.    Kwanza, ni kudumisha, kuendeleza na kuimarisha uhusiano mzuri na majirani zetu, mataifa mengine duniani na mashirika ya kimataifa;

 

2.    Pili, ni kudumisha na kuendeleza maslahi ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiusalama ya nchi yetu miongoni mwa mataifa na mashirika ya kimataifa; na

 

3.    Tatu, kuipatia nchi yetu marafiki wapya na kudumisha waliopo katika jumuia ya kimataifa.

 

Hii ndiyo kazi niliyokuwa naifanya katika ziara zangu za nchi za nje.  Ziara hizo zimekuwa za mafanikio makubwa na tumefikia malengo yetu.  Nitaendelea nazo siku za usoni kwa mataifa mengine rafiki ambayo sijayatembelea.  Wakati huo huo pia tutawaalika viongozi toka mataifa rafiki duniani waje kututembelea na kutimiza malengo yetu hayo hapa hapa nyumbani.

 

Mwelekeo wa Bajeti ya Serikali 2006/2007

 

Ndugu Wananchi;

 

          Jambo la mwisho ninalotaka kulizungumzia ni Bajeti ijayo.  Tarehe 15 mwezi ujao Serikali itawasilisha Bungeni bajeti yake kwa mwaka 2006/2007.  Bajeti hiyo itakuwa ndiyo ya kwanza kwa Serikali ya Awamu ya Nne.  Ni mwanzo wa safari ya miaka mitano ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na masuala mengine muhimu kitaifa.  Tutaanza kuchukua hatua za kuongeza kasi ya kukuza uchumi na kupambana na umaskini wa kipato wa Watanzania.

 

          Kadhalika tutaanza kuchukua hatua za kukuza ajira na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii.  Pia tutaanza safari ndefu ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.  Bahati mbaya bajeti hiyo imeandaliwa wakati uchumi wa nchi yetu umetikishwa na matatizo ya ukame, upungufu wa chakula, umeme na bei kubwa za mafuta.

 

          Ni dhahiri kwamba hali hii inaweza kuwa na athari kwa mwenendo mzima wa bajeti ya mwaka ujao, ukuaji wa pato la taifa, na hasa kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo na viwandani.  Pia inaweza kuathiri akiba ya pesa za kigeni, mapato ya Serikali na hivyo kupunguza kwa kiasi fulani uwezo wetu wa kutekeleza mipango na mikakati ya maendeleo tuliyoibuni.  Hata hivyo, ni dhamira yetu kuhakikisha kuwa tunajitahidi kuchukua hatua mbalimbali ili kupunguza makali ya athari hizo.

 

WAJIBU WETU

 

Ndugu Wananchi;

 

          Sisi sote tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba uchumi wetu unaendelea kukua licha ya matatizo niliyoyaeleza hapo juu.  Kila mmoja wetu anao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na maarifa pale alipo.  Aidha, sote tunawajibika kuchangia katika kukuza mapato ya serikali.  Kadhalika, tuongeze juhudi za kuvutia mitaji toka ndani na nje na kuongeza misaada toka nje ili kujijengea uwezo mkubwa zaidi wa kuleta maendeleo yetu na ya nchi yetu.

 

Ndugu Wananchi;

 

          Mwisho, napenda kuwashukuru tena nyote kwa uelewa wenu mkubwa wa hali inayoikabili nchi yetu kwa sasa.  Nawashukuru pia kwa uvumulivu wenu, ushirikiano na mshikamano wenu. 

 

          Nawaombeni tuendelee kushirikiana, kushikamana na kusaidiana. 

 

          Daima tukumbuke msemo wa wahenga kuwa, Umoja ni nguvu, Utengano ni udhaifu. Na, Silaha ya Mnyonge ni Umoja.  Hima tushirikiane, tuwe kitu kimoja.  

 

Kwa pamoja tutashinda!

 

          Mungu Ibariki Afrika!

          Mungu Ibariki Tanzania!

          Ahsanteni kwa Kunisikiliza.