HOTUBA
YA WAZIRI WA MAWASILIANO NA UCHUKUZI MHESHIMIWA
PROF. M.J. MWANDOSYA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO WA MAENDELEO NA
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2001/2002
1.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kisekta inayohusu Wizara yangu, naomba kutoa hoja kwamba
Bunge lako Tukufu, sasa likubali kupitisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya
Mawasiliano na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2001/2002.
2.
Tarehe 4 Julai, 2001 tulipokea kwa majonzi makubwa kifo cha Kiongozi wetu
mpendwa Dr. OmarAli Juma. Natoa
salaam za rambirambi kwa Mheshimiwa Rais, mjane wa marehemu, familia yake
na Watanzania wote. Mola aiweke
roho ya marehemu mahala pema peponi, “Amin”.
3.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbuka wenzetu ambao wameitwa mbele ya
haki. Marehemu Nyanda; Marehemu Mgeja, Marehemu Haule, Marehemu
Bhiku na Marehemu gulamali. Mwenyezi
Mungu aziweke roro zao mahali pema peponi, Ameni.
4.
Aidha, nampongeza Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kwa kuchaguliwa tena
kuwa Rais. Pia, nampongeza
Mheshimiwa Amani Abeid Karume kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
5.
Mheshimiwa Spika, tumepokea uteuzi wa Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein kuwa
Makamu wa Rais kwa furaha kubwa. Tunampongeza
sana. Tunaahidi kumpa ushirikiano mkubwa.
6.
Vile vile, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Frederick Sumaye kwa
kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.
7.
Mheshimiwa Spika, nakupongeza sana wewe binfasi kwa kuchaguliwa kwako.
Nawapongeza vilevile Naibu Spika na Wevyeviti wa Bunge kwa kuchaguliwa
kukusaidia kuendesha shughuli za Bunge
8.
Pongezi zangu za mwisho, lakini si kwa umuhimu, ni kwa
Wabunge wote kwa kuchaguliwa/kuteuliwa kwao kwa kipindi hiki cha miaka
mitano.
9.
Naishukuru, Kamati ya Kisekta ya Miundombinu, chini ya Uenyekiti wa
Mheshimiwa profesa Daimon Mwaga, Mbunge wa Kibakwe, kwa kuyachambua kwa undani
na kwa kina, makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka
2001/2002. Naahidi kwamba maoni,
maelekezo na ushauri wa Kamati utazingatiwa katika kuendeleza sekta na katika
utekelezaji wa majukumu ya Wizara na taasisi zake.
UTENDAJI
KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2000/2001
10.
Mheshimiwa Spika, utendaji
katika sekta kwa kipindi kilichopita uliongozwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM,
Dira ya Maendeleo ya taifa, sera ya
kuondoa umaskini, usimamizi wa mazingira pamoja na sera za sekta.
Rasimu ya Sera ya Uchukuzi na ile ya sera ya huduma za Posta,
zimekamilika.
11.
Februari, 2001 Serikali iliuza hisa asilimia 35 za Kampuni ya Simu (TTCL)
kwa Kampuni za MSI ya Uholanzi na Detecon ya Ujerumani.
Kufuatana na malengo tuliyompa mbia huyo njia za simu zitaongezeka
kufikia zaidi ya milioni mwaka 2005, ongezeko la zaidi ya asilimia 340.
12.
Serikali imeunda Kampuni iitwayo SIMU 2000.
Kampuni hii itakuwa na dhamana na kusimamia, mali zote zisizohamishika za
TTCL, ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo ya simu.
Aidha, kampuni hii itakuwa na jukumu la kulipa mafao, ya waliokuwa
wafanykazi wa Shirika la Posta na Simu, la iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
waliostaafu, na ambo bado walio kazini. Kampuni
hiyo tayari imeanza kazi. TTCL
anayo imeunda kampuni tanzu, SIMUNET ili kutoa huduma za “internet”.
Kuanzishwa kwa SIMUNET kutapunguza sana gharama za huduma hii mikoani.
13.
Serikali imelifuta Shirika la uchukuzi la Taifa (NTC) ili kutoa nafasi
kwa sekta binafsi kufanya kazi zilizokuwa zinafanywa na shirika hili.
Waliokuwa wafanyakazi wa NTC, wamejiunga pamoja na kuunda kampuni binafsi.
Kampuni hii inaitwa Transport Resource Centre.
Kampuni inatarajia kutoa huduma za ushauri katika sekta ya uchukuzi.
Naahidi Serikali itawewezesha wazawa hawa, na MEBO nyingine.
14.
Wizara pia inasimamia Mamlaka ya Usalama na Usafiri wa Anga, Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege, na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Wizara yangu imeendelea kusimamia shughuli za Idara ya Ndege za Serikali.
15.
Aprili 2001, Bunge lako Tukufu lilipitisha sheria ya kuanzisha mamlaka
iitwayo SUMATRA, ambayo itasimamia ushindani wa kiuchumi katika shughuli za
uchukuzi. Chombo hiki kitahakikisha wananchi wanapata huduma bora na
kwa ufanisi zaidi.
16.
Tunatambua pia umuhimu wa kuzingatia usalama na ubora wa vyombo vya
uchukuzi. Serikali imeona ni vyema
ikatenganisha udhibiti wa kiuchumi na wa usalama.
Ajali za vyombo vya uchukuzi zinazongezeka.
Wizara yangu inaanda chombo cha udhibiti wa usalama na uchukuzi.
17.
Wizara pia imeendelea kusimamia shughuli za Mkataba wa Utendaji wa
Shirika la Posta. Juhudi zimelengwa katika kulifanya Shirika lijiendeshe
kibiashara, kuboresha mtaji, na kubadili mfumo, ili kuongeza tija.
18.
Wizara imekamilisha rasimu ya mbinu za kutunza mazingira itakayotumika
wakati wa kutayarisha, kutekeleza, miradi ya Mawasiliano na Uchukuzi.
MWELEKEO
NA MPANGO WA MWAKA 2001/2002
19.
Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza kwa ujumla hali ya utendaji wa sekta
ya mawasiliano na uchukuzi mwaka 2000/2001, sasa nazungumzia utendaji, mkakati,
malengo na mwelekeo kwa mwaka 2002/2002.
USAFIRI
NA UCHUKUZI KWA NJIA YA BARABARA
20.
Kuhusu usafiri wa barabara, sekta binafsi imechangia kwa kiasi kikubwa
katika kutoa huduma mjini na vijijini. Wasafirishaji
wameungana na kuunda vyombo vyao.
Vyombo hivyo ni pamoja na vya wenye kumiliki mabasi, magari ya mizigo, na
ya mafuta. Hatua hii itasaidia
mawasiliano kati ya watoa huduma, wateja, na vyombo vya udhibiti.
21.
Kuhusu Jiji la Dar es Salaam, sekta binafsi imeendelea kuwa tegemeo kubwa
la huduma ya usafiri. Shirika la
UDA nalo limeborasha huduma kwa wastani. Aidha,
jitihada za kurekebisha Shirika ili livutie wawekezaji, zinaendelea.
Mshauri naanagalia jinsi ya kurekebisha mfumo wa utoaji huduma kwa mkoa
wa Dar es Salaam.
22.
Bado wapo baadh ya madereva ambao hawataki kuzingatia sheria na taratibu.
Ajali nyingi hutokea na maisha ya watu yamepotea.
Natoa wito kwa wote wanaohusika na usimamiaji wa sheria na taratibu,
kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa.
23.
Kati ya Julai 2000 na Machi 2001, Mamlaka Kuu ya Leseni ilitoa leseni
8,400 ikilinganishwa an leseni 7,400 zilizotolewa kipindi kama hicho mwaka
uliopita. Mafanikio haya yametokana na ukaguzi wa mara kwa mara wa
leseni. Mamlaka pia imesogeza
huduma zake kwa wananchi kwa kufungua ofisi ya Kanda Moshi, Mwanza, Dodoma na
Mbeya.
24.
Mwaka 2002/2002, Mamlaka itaimarisha ofisi za Kanda, itanunua vitendea
kazi vya kutosha, itaweka kwenye vibwebweto kumbukumbu zake, itaendeleza utafiti,
na mafunzo ya wafanyakazi.
USAFIRI
NA UCHUKUZI KWA NJIA YA RELI
25.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2002, Wizara ililenga kurekebisha mifumo ya
utoaji wa huduma za mashirika ya reli ili yaweze kujiendesha na kujiimarisha.
TRC itarekebishwa kwa njia ya kukodishwa.
Lengo ni kukamilisha zoezi la ukodishaji ifikapo Juni 2002.
Aidha, TAZARA itarekebishwa baada ya Serikali za Tanzania na Zambia
kukubaliana juu ya mkakati utakaofaa. Katika
zoezi hili tutakuw ana mawasiliano na marafiki zetu wa China.
Hata hivyo, kwa mashirika yote mawili utendaji katika kipindi cha 2000
ulikuwa wa kuridhisha ikilinganishwa na ule wa mwaka 99.
26.
Mwaka 2000, Shirika la Reli Tanzania lilisafirisha mizigo tani milioni
1.2 na abiria 630,000. Shirika
lilikusanya shilingi bilioni 48.1. Malengo
yaliyokusudiwa hayakufikiwa kutoka na kuw ana mtaji mdogo.
Matatizo mengine ni, uchache na uhafifu wa mabehewa na injini,
uliosababishwa na kukosekana kwa vipuri kwa ajili ya maetengenezo.
27.
Mwaka 2002 Shirika litatekeleza mradi wa njia ya mawasiliano na mradi wa
mabehewa ya mifugo. Aidha, Shirika
litanedelea kufanya matengenezo ya reli kati ya Manyoni na Singida, Kaliau na
Mpanda, na litatekeleza miradi ya maji kwenye kambi zake.
28.
Kwa mwaka 2001, Shirika litasafirisha jumla ya abiria 700,000 na shehena
zenye uzito wa tani 1,300,000. Aidha,
mapato yatafika shilingi bilioni 54.1 na matumizi ya shilingi bilioni 48.3.
29.
TAZARA inakabiliwa na uhaba wa fedha za uendeshaji.
Uhaba huo umeathiri ukarabati wa miundombinu na umeongeza uchakavu wa
vifaa. Kumekuwa na wizi wa nyaya za
simu na matufa, hasa katika maeneo ya Mbeya na Dar es Salaam.
Tatizo la wizi wa nyaya za simu na mafuta limekithiri pia, katika maeneo
ya reli ya Shirika la Reli Tanzania hasa Mkoa wa Tanga.
Kitendo hiki ni uhujumu wa uchumi. Wananchi
tushirikiane kuondoa tatizo hili linaloturudisha nyuma.
30.
Mwaka 2001/2002 TAZARA itaendelea kukarabati njia, kubadilisha teknolojia
ya mawasiliano, kukarabati vifaa na kununua vipuri, kwa msaada wa dola za
Kimarekani miloni 12.3 kutoka China. Mkataba
wa msaada huu umesainiwa Dar es Salaam tarehe 19 Julai 2001.
USAFIRI
NA UCHUKUZI KWA NJIA YA MAJI
31.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2000, Serikali ilikodisha kitengo cha kontena cha
Mamlaka ya Bandari, kwa kampuni binafsi. Hivi
sasa Serikali inafanya upembuzi wa kuhusisha sekta binafsi katika kutoa huduma
kwenye vitengo vya Bandari vilivyobaki. Mamlaka
itaendelea kumiliki bandari zote zilizo chini yake.
32.
Mwaka 2001/2002, Mamlaka itahudumia tani milioni 6.2 katika bandari zake
na hivyo kupata shilingi bilioni 57.8 na kutumia shilingi bilioni 53.4.
Mamlaka itaimarisha bandari za Tanga, Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Kilwa
na Pangani. Aidha itashirikiana na
sekta binafsi katika ujenzi wa gati ndogo ya Mafia.
33.
SINOTASHIP inamilikiwa kwa pamoja kati ya Tanzania na China.
Ni kampuni pekee nchini inayoshiriki katika biashara ya usafirishaji wa
kimataifa kwa njia ya bahari. Kampuni
ina meli tano, nne kati ya hizo ni mali yake na moja ya kukodisha.
Meli hizo ina uwezo wa kubeba jumla ya tani 77,100 kwa wakati mmoja.
Mwaka 2000 meli zilifanya safari 35 ikilinganishwa na 23 za kipindi
kilichopita. Jumla ya tani 402,000 za shehena zilisafirishwa.
34.
Mwaka jana wizara yangu ilitoa taarifa kwamba, utekelezaji wa majukumu
mapya ya TCFB ya usimamizi na udhibiti wa usafirishaji majini, ungeanza mwezi
Julai, 2000. Kazi hizo zimeanza. Shirika
limefanikiwa kuunda Baraza la Mawasiliano.
Baraza linajumuisha washikadau katika usafirishaji majini.
Hata hivyo, baada ya kuundwa kwa SUMATRA, kazi za udhibiti za Shirika
zitahamishiwa kwenye chombo hicho.
35.
Mwaka 2000/2001, uchukuzi wa meli mwambao na visiwani ulikuwa ufanisi wa
wa wastani. Kuna ongezeko meli kutoka meli tatu, mwaka 2000, hadi tano
mwaka 2001.
36.
Hata hivyo kuanzia Januari 2001 meli nne tu zinatoa huduma.
Hii inatokana na matatizo yaliyoikumba MV Zahara, tarehe 22 January,
2001. Tumeagiza meli hiyo ifanyiwe
matengenezo makubwa. Aidha,
niliahidi katika Bunge lako tukufu kulishughulikia
suala la MV Zahara. Mkaguzi
wa meli amesimamishwa. Wizara yangu
imemteua Mkaguzi wa meli wa muda. Kutokana
na uzito wa suala hili, na kwa kutumia mamlaka niliyonayo chini ya sheria ya
‘Merchant Shipping Act’ ya mwaka 67, nimeteua Tume ya Uchanguzi wa Ajali.
Tume hii inaoongozwa na Mheshimiwa Jaji Seven Ihema wa Mahakama Kuu ya
Tanzania. Tume imeanza kufanya kazi.
37.
Marine Services, kampuni tangu ya TRC, imeendelea kutoa huduma katika
Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Aidha,
wamiliki binafsi wa vyombo vya majini nao wameendelea kushirikiana na Kampuni
katika kutoa huduma ya uchukuzi.
38.
Nawahimiza wenye vyombo vya usafiri majini, kufuata sheria na kanuni za
usalama. Vyombo vikaguliwe mara kwa
mara. Wawe na vifaa vya kutosha vya
usalama. Watoe mafunzo kwa abiria
jinsi ya kutumia vifaa hivyo. Kwa
upande wa sekta binafsi, tayari mabaharia wameunda chama
ambacho kitaangalia suala zima la usalama wa abiria, mizigo na meli.
USAFIRI
NA USAFIRISHAJI UKANDA WA MAGHARIBI
39.
Mheshimiwa Spika, uendelezaji wa uchukuzi hutekelezwa kutumia dhana ya
Kanda. Maendeleo ya uchukuzi kwa
Kanda ya Mtwara yamefafanuliwa vizuri na Waziri wa Ujenzi.
Umuhimu wa usafirishaji katika Ukanda wa Magharibi, unayounganisha mikoa
ya Mbeya, Rukwa, Tabora, Kigoma, Kagera, Mwanza na Shinyanga, tunauelewa.
40.
Bado wananchi katika maeneo haya, wanapata matatizo makubwa ya
mawasiliano, kutokana na ubovu wa barabara, na uduni wa huduma za reli na meli.
Juhudi za wananchi wa maeneo hayo katika kujiletea maendeleo yao
zinakwama. Wanashindwa kusafirisha
mazao ya ziada. Ukanda huu ni njia
mbadala na fupi zaidi, ya kuunganisha nchi za SADC na zile za Burundi, Rwanda na
Uganda. Taifa linaweza kuendeleza
ukanda huu wa usafirishaji na kuinua uchumi wa nchi.
41.
Wizara yangu inatayarisha mpango kabambe wa sekta ya uchukuzi.
Mpango huo utabaini maeneo, na kiasi cha uwekezaji kinachohitajika,
katika kutatua matatizo yaliyopo hasa katika ukanda huu na kanda nyingine.
USAFIRI
NA USALAMA WA ANGA
42.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2001/2002 Mamlaka ya Usalama wa Anga itabadilisha
mitambo chakavu ya kuongoza ndege katika uwanja wa Dar es Salaam.
Mamlaka itafanya upenguzi wa kuanzisha kituo cha kuongoza ndege katika
anga za juu katika eneo la SADCC. Mamlaka
itafaanya upenguzi wa kuanzisha kituo cha kuongoza ndege katika anga za juu
katika eneo la Afrika Mashariki. Miradi
hii itagharimiwa kwa mikopo nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya.
43.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inaendesha viwanja 62 kama ilivyoainishwa
kwenye Sheria Na.1 ya mwaka 74. Wizara
yangu imefanya uchambuzi wa kubaini njia mbali mbali zinazofaa, katika kuhusisha
sekta binafsi, katika uendeshaji wa baadhi ya viwanja hivi.
44.
Mamlaka iliendelea na matengenezo madogo madogo ya viwanja 58 na
kuboresha mitambo na miundo mbinu ya viwanja vinne.
Mamlaka pia ilifanya ukarabati mkubwa wa viwanja vya Mwanza na Arusha.
Mwaka 2001/2002, Mamlaka itavifanyia matengenezo na kuboresha viwanja
hivi na vingine 11.
45.
Serikali imeona umuhimu wa kuboresha huduma za Viwanja vya Nyanda za juu
Kusini. Serikali imeamua kujenga
uwanja wa ndege wa Songwe – Mbeya. Kwa
kuanzia kiasi cha shilingi milioni 400 zimetengwa katika bajeti ya 2001/2002.
Uongozi wa Mkoa na Halmashauri ya Manispaa ya Mbeya washirikiane na TAA
kufanikisha ujenzi wa kiwanja hiki muhimu.
Kiwanja hiki kitakapokamilika kitakua ni lango kwa nchi za Malawi,
Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na nchi nyingine za SADC.
46.
Kuhusu ukodishaji wa kiwanda cha Kilimanjaro kwa KADCO, Wizara yangu, kwa
kushirikiana na Idara nyingine za Serikali, tumefanya mapitio ya kina ya Mkataba
Mkuu, na Mkabata wa Pango na kubaini vipengele vyote ambavyo havina manufaa kwa
Taifa. Nimeteau time ya majadiliajo
ya kupitia upya mikataba hii. Katika
mapitio haya tutazingatia maoni na ushauri uliotolewa na waheshimiwa Wabunge.
47.
Mwaka 2002/2001 utendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania ulikuwa bado si
wa kuridhisha. Shirika lilipata hasara ya shilingi milioni 460 mwaka 2000.
Hali hii ilitokana na gharama kubwa za ununuzi wa vipuri pamoja na
matengenezo ya ndege. Ilipofika mwezi Desemba, 2000 ilibidi Serikali ichangie jumla
ya shilingi bilioni 1.8. Lengo ni
kuliwezesha Shirika liwe katika hali ya unafuu tunapotafuta mwekezaji.
Mategemeo yetu ni kwamba Shirika litakuwa limebinafsishwa ifikapo Desemba
2001.
48.
Hisa za Serikali katika AJAS zimeuzwa kwa kampuni binafsi, infra Invest
Limited. Kampuni hii ni ya
wafanyabiashara wa Tanzania. Aidha, kampuni hii imeungana na kampuni binfasi ya Uganda
iitwayo DAIRO na kuanzisha Shirika la pamoja ili kutoa huduma za usafiri wa anga
zinazofanana na zile za Alliance Air.
49.
Wizara yangu imeendelea kusimamia na kuratibu shughuli za Idara ya Ndege
za Serikali ambayo itabadilishwa kuwa Wakala wa Serikali 2001/2002.
SEKTA
YA MAWASILIANO
Usimamizi
wa huduma za Mawasiliano
50.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2000/2001 Tume ya Mawasiliano ilitoa leseni ya
mdahalishi (Internet) kwa Shirika la Posta, na kutoa leseni 14 kwa wakandarasi
wa ukarabati na ufungaji mitambo ya redio na simu.
Tume ilitoa leseni nne za wasafirishaji wa vifurushi/mizigo.
Vile vile, Tume ilifanikiwa kutoa leseni 396 za masafa ya redio.
51.
Tume, kwa kushirikiana na Kampuni za Posta na Uholanzi na New Zealand,
walikagua ubora wa mtandao wa Shirika la Posta.
Ukaguzi huo ulifanyika mikoa 14. Mikoa
11 iliyobaki itafanyiwa ukaguzi mwaka huu wa fedha.
52.
Aidha, Tume ilikagua kampuni zote za simu katika mikoa yote.
Tume pia ilikagua watumiaji wa masafa ya redio kwa mujibu wa Sheria Na.18
ya mwaka 93.
53.
Katika juhudi za kuiimarisha Tume, Serikali inatarajia kupata msaada wa
Sweden kiasi cha Kronor milioni 10. Mkataba
utasainiwa hivi karibuni.
54.
Suala zima la udhibiti na ugawaji wa masafa, liko chini ya usimamizi wa
Tume. Masafa ni rasilimali muhimu
ya Taifa. Itumiwe kiuangalifu na
kikamilifu pale inapogawiwa. Wizara
yangu inaliangalia kwa undani suala hili kwa nia ya kutoa haki, kuleta usawa, na
kuwezesha ushindani ili kuongeza mawasiliano chini.
Huduma
za Simu
55.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2000/2001 TTCL, ilikamilisha programu kubwa ya
kurekebisha mfumo wa siku (TRP), iliyoanza mwaka 94 na kugharimu shilingi
bilioni 125. Madhumuni ni kuboresha
na kupanua njia za simu ili kukidhi mahitaji ya wateja.
Mikoa 15 imefaidika na mradi huo.
56.
Mradi wa simu bila waya ulianza kutekelezwa mwaka 98 katia mikoa 13.
Mradi uligharimu shilingi bilioni 25.
Njia za simu 300,000 zimesambazwa. Mradi
mwingine, wa uwekaji mtambo wa utoaji ankara za simu kwa wateja, pia umekamilika,
na hivyo kuhitimisha mradi wa TRP. Miradi hii imekuwa na matatizo ya hapa na pale ya kiufundi.
TTCL inajitahidi kurekebisha mapungufu hayo.
57.
TTCL imekuwa ikitekeleza mradi unaohusu uhamishaji wa mitambo ambayo
uwezo wake ni mdogo, ukilinganisha na mahitaji ya watumiaji, kwenda kwenye
maeneo mengine. Mikoa nane imefaidika na mradi huu. Aidha, mitambo ya simu za kisasa imewekwa Mkoa wa Kagera.
TTCL imeweka mitambo mipya maeneo mbali mbali katika mikoa nane.
58.
Licha ya hatua iliyofikiwa katika sekta ya mawasiliano ya simu nchini,
nakiri kuwa bado hali ya mawasiliano ya simu kwa mikao ya Kusini hairidhishi.
Upo uchakavu mkubwa wa mitambo ya simu, na sehemu kubwa ya mikoa hii
haina mawasiliano kabisa. Mitambo
iliyowekwa imekwisha muda wake na imekuwa vigumu kuwa na simu za uhakika.
Zipo Wilaya ambazo bado huduma za simu, hata zile za kukoroga hazipo.
Wilaya hizi ni Tandahimba na Liwale.
Mtambo wa Mtwara umejaa na wateja wengi wanasubiri.
59.
Tayari upembuzi wa kubadili mfumo wote wa simu Mtwara na Lindi,
umefanyika. Wizara imewasiliana na
mwekezaji mpya wa TTCL ili atoe kipaumbele kwa mikoa hii.
Mwekezaji ameahidi kufanya hivyo. Aidha,
wawekezaji wa simu za mikononi nao wameona umuhimu wa kufika mikoa hiyo. Mobitel na Vodacom wametaarifu kuhusu nia yao ya kufikisha
huduma Mtwara katika kipindi cha 2001/2002.
60.
Ifikapo Septemba 2001 TTCL itaanzisha huduma ya simu za mkononi, huduma
ambayo wamepanga kuitoa katika maeneo ya kanda zote za mawasiliano nchini.
Tayari TTCL imeanzisha kampuni tanzu iitwayo ‘CELTEL’.
61.
Hadi Juni 2001 Mobitel iliyoanza kutoa huduma zake hapa nchini mwaka 94
ilikwishaunganisha wateja 100,400. Kampuni
ya Tritel iliyoanza shughuli zake mwaka 96 imeunganisha wateja 18,000, Kampuni
ya Vodacom iliyoanza shughuli zake mwaka 2000 imeuganisha wateja 102,000 na
Zantel iliyoanza shughuli zake mwaka 2000 imeunganisha wateja 6,800.
62.
Pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na TTCL na kampuni nyingine katika
maendeleo ya simu nchini, bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kueneza
mtandao hasa vijijini. Aidha, changamoto nyingine katika utoaji wa huduma hiyo ni
kwa TTCL kupunguza malalamiko, na kero kubwa kwa wananchi kuhusu ankara za
malipo ya simu sizizo sahihi, na wizi wa simu unofanyika kiufundi.
Changamoto kubwa pia ni kwa kampuni zote kupunguza bei za huduma za simu
ambazo ni za juu sana ukilinganisha na majirani zetu.
Tekinolojia
ya Habari na Mawasiliano nchini (ICT)
63.
Mheshimiwa Spika, katika karne hii tumejionea mabadiliko makubwa katika
sekta ya habari na mawasiliano, kutokana na maendeleo makubwa na ya haraka ya
teknolojia (ICT). ICT inasaidia
sana katika maendeleo ya sekta kama vile afya, elimu, kilimo, hali ya hewa,
usafiri, n.k. Huduma hizi ni pamoja
na zile za mawasiliano ya simu za kawaida na mikononi, mtandao wa vibwebweto (comptuers),
mdahalishi (internet), tovuti (website), baruapepe (e-mail) na nukulishi (fax).
Huduma nyingine ni zile za utangazaji habari kwa njai ya redio,
televisheni, video, magazeti, vitabu na vipeperushi.
64.
Napenda kujulijusha Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imepewa jukumu
la kusimamia maendeleo ya ICT nchini. Lengo
letu ni kuedeleza, kuboresha na kukuza mawasiliano na teknolojia za habari.
Tayari Wizara yangu imeunda Kamati maalum ijulikanayo kama “Tanzania
DOT Force”, itakayotoa mapendekezo kuhusu sera na mikakati ya kuendeleza
matumizi ya teknolojia za mawasiliano. Kamati
hii inahusisha sekta binafsi, wanataaluma, na Serikali.
Kamati hii inaongozwa na Profesa Mathew Luhanga, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam. Japan, Sweden, UNDP na USAID wameonyesha nia ya kutusaidia.
Huduma
za Posta
65.
Mheshimiwa Spika, Aprili 2001, Benki ya Dunia na Umoja wa Posta Duniani
wametoa ripoti ya maendeleo na mabadiliko ya sekta ya Posta duniani.
Nafurahi kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa Shirika la Posta ni mojawapo
ya mashirika kutoka nchi zinazoendelea yaliyosifiwa.
Mashirika mengine ni kutoka nchi za Indonesia, Costa Rica na Trinidad na
Tobago.
66.
Mwaka 2001/2002, Shirika la Posta litapanua huduma kwa kutumia dhana ya
Vituo vya kusambazia barua, na kununua vyombo vya usafiri ili kuongeza kasi ya
kusambaza barua. Shirika
litaanzisha mawasiliano kitakwimu, kwa njia ya kompyuta, kwa wateja wake.
Aidha, Shirika litakamilisha Mradi wa teknolojia mpya ya mawasiliano,
katika kaunti za Posta katika Posta kuu zote za kanda na mikoa.
Shirika litahamasisha ufunguzi wa wakala wa Posta vijijini.
Aidha, Shirika litajenga posta zenye hadi za ki-wilaya kwenye makao makuu
ya wilaya.
HUDUMA
ZA HALI YA HEWA
67.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2000/2001, Mamlaka ya Hali ya Hewa iliendelea
kutoa taarifa za hali ya hewa, kwa kupitia vyombo vya habari, kuwaelimisha
wananchi juu ya hali ya hewa kila siku. Taarifa
hizi huwasaidia wananchi katika kupanga shughuli zao za kimaendeleo na kijamii. Mwaka 2001/2002, Mamlaka itaweka vifaa vya kupimia hali ya
hewa, katika viwanja vya ndege vya kimataifa.
Mamlaka itafufua vifaa vya kupima anga za juu, kuviboresha vituo vya
kupima mvua, na kuongeza idadi yake. Serikali
itaisaidia Mamlaka katika juhudi za kupata ofisi zenye hadi na ubora unaotakiwa
kuwawezesha kumudu majukumu waliyopewa.
MAFUNZO
NA MAENDELEO YA WAFANYAKAZI
68.
Mwaka 2001/2001 Wizara yangu itaendelea kutoa mafunzo kupitia vyuo
vilivyo chini yake. Vyuo hivyo ni
Chuo cha Bandari, Chuo cha Ubaharia, Chuo cha Usafirishaji, Chuo cha Usalama wa
Anga, Chuo cha Simu, na Chuo cha Hali ya Hewa.
Wizara inakusudia kukamilisha kuwasomesha wafanyakazi wake wote masomo ya
kompyuta katika kipindi cha 2001/2002.
69.
Chuo cha Ubaharia (Dar es Salaam Martime Institute), ndio pekee chenye
sifa na uwezo wa kufundisha masomo ya ubaharia katika nchi za Afrika Mashariki
na kati. Jumuiya ya Afrika Mashariki imekitambua chuo na kukipa hadhi
ya kuwa moja ya taasisi zitakazotoa huduma katika Jumuiya nzima.
70.
Wizara yangu imeanza kutekeleza mpango maalum juu ya kujikinga na ukimwi.
Wafanyakazi wanaelimishwa namna ugonjwa huu unavyopatikana na
unavyosambazwa. Mashirika na
taasisi zetu nao wametakiwa kuandaa mipango thabiti juu ya suala hili, kwa
kushirikiana na Kitengo cha Udhibiti wa Ukimwi, cha Wizara ya Afya.
HATIMISHO
71.
Nimejitahidi kueleza hali lilivyokuwa katika kipindi kilichopita, juhudi
zilizofanyika, na mwelekeo wa shughuli za Mawasiliano na Uchukuzi kwa ujumla.
Natarajia kuwa Waheshimiwa Wabunge hawatasita kutukosoa, kutuweka sawa
tulipoteleza, na kuwapongeza wafanyakazi wa sekta hii pale wanapofanya vizuri.
SHUKRANI
72.
Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wote
walioshirikiana nasi katika kufanikisha malengo tuliyojiwekea.
Aidha, shukrani zangu za dhati ziende kwa Nchi, Mashirika na Taasisi za
kimataifa na wahisani mbali mbali waliotusaidia.
73.
Nitakuwa mnyimi wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wenzangu katika
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi. Naanza
na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dr. Maua Abeid Daftari (Mb), Katibu Mkuu, Ndugu
Salim Himid Msoma, pamoja na watendaji wote wa Wizara, Mashirika yaliyo chini ya
Wizara yangu. Wamenipa ushirikiano
mkubwa katika jitihada za kuendeleza sekta ya mawasiliano na uchukuzi. Hapana shaka, kwamba bila mchango wao mkubwa, kazi yangu ya
kuongoza sekta hii, ingekuwa ngumu sana na pengine isingewezekana kabisa.
Nawashukuru.
74.
Lazima nikiri, na kwa unyenyekevu mkubwa, kwamba nasimama mbele ya Bunge
lako Tukufu kutokana na dhamana na heshima kubwa waliyonipa wananchi wa Rungwe
Mashariki kunichangua, bila kupingwa, katika uchanguzi wa mwaka 2000.
Wananchi wote wa Rungwe Mashariki: kutoka Ikubo mpaka Kapula Mpunguti;
kutoka Bujingijila mpaka Kisegese nawashukuru sana kwa imani yao.
MAKADIRIO
YA BAJETI YA WIZARA
75.
Mheshimiwa Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na malengo
yake kwa mwaka 2001/2002, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishwe jumla ya
Shilingi bilioni kumi na saba, milioni mia nane themanini na tisa, mia
moja sabini na mbili elfu na mia saba (17,889,172,700).
Kati ya hizo, shilingi bilioni kumi, milioni mia tatu ishirini na
mbili, sabini na mbili elfu, na mia saba (10,322,072,700) ni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida. Shilingi bilioni
saba, milioni mita tano sitini na saba, na laki moja (7,567,100,000)
ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati
ya fedha hizo za maendeleo shilingi milioni mia nne (400,000,000) ni
fedha za hapa nchini na shilinig bilioni saba, milioni mia moja sitini
na saba, na laki moja (7,167,100,000) ni fedha za kigeni toka kwa wahisani
mbali mbali.
76.
Mwisho kabisa, naomba nikushukuru wewe binafsi, pamoja na Waheshimiwa
Wabunge kwa kunisikiliza.
77. Meshimiwa Spika, kwa heshima kubwa, naomba kutoa hoja.