HOTUBA YA WAZIRI WA UJENZI MHESHIMIWA JOHN P. MAGUFULI (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO WA MAENDELEO NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2001/02
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha wa 2001/02.
2. Mheshimiwa Spika, wakati Bunge hili la Bajeti likiendelea, nchi yetu ilipatwa na msiba mkubwa usiotarajiwa kufuatia kifo cha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Omar Ali Juma. Napenda kuchukua nafasi hii kuungana na Watanzania wote kumwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Aidha, nawapa pole ndugu na jamaa wa Waheshimiwa Wabunge waliotutoka katika kipindi cha 2000/01. Naomba Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi.
3. Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kulielezea Bunge lako Tukufu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa sera na majukumu mbali mbali ya Wizara ya Ujenzi katika mwaka wa fedha wa 2000/01 na mpango wa Wizara kwa mwaka 2001/02, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Frederick T. Sumaye (Mb) kwa kuchaguliwa bila kupingwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Hanang na kuteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu. Hii inaonyesha imani kubwa waliyonayo wananchi wa Hanang na Mheshimiwa Rais juu yake. Aidha, ninampongeza kwa dhati na kumshukuru kwa hotuba yake ya Bajeti ambayo imesisitiza na kutoa upeo wa majukumu ya Serikali katika kipindi kijacho. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Wizara ya Ujenzi itazingatia na kutekeleza maelekezo hayo ya Serikali katika kipindi cha mwaka 2001/02.
4. Mheshimiwa Spika, ninaomba pia nitumie nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango) Mheshimiwa Abdallah Kigoda, Mbunge wa Jimbo la Handeni na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Basil Mramba, Mbunge wa Jimbo la Rombo kwa hotuba zao ambazo zimechambua na kuweka bayana sera, mafanikio, matatizo na mikakati ya Serikali katika kuendeleza uchumi wetu pamoja na kuweka mwelekeo wa mapato na matumizi katika kipindi kijacho cha 2001/02.
SERA NA MAJUKUMU YA WIZARA YA UJENZI
5. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi ikiwa msimamizi mkuu wa Sekta ya Ujenzi imetayarisha bajeti hii kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya 2000-2005 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo - 2025. Aidha, misingi na mikakati ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi inazingatia mfumo wa jumla wa sera za Taifa za kukuza uchumi na kuboresha maendeleo ya jamii ambapo lengo kuu ni kuondoa umaskini, kuongeza pato la Taifa, utawala bora unaozingatia sheria na ukuzaji wa demokrasia nchini. Kutokana na sera hizo, majukumu ya Wizara ya Ujenzi yameelekezwa katika kuendeleza miundo mbinu ili iwe kichocheo cha kuleta ufanisi zaidi na kujitosheleza katika nyanja za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara na madaraja kwa ujumla hapa nchini na kutoa huduma za majengo, ugavi, ufundi na umeme Serikalini.
6. Mheshimiwa Spika, majukumu ya Wizara ya Ujenzi kwa sasa yanalenga katika mambo
yafuatayo:-
7. Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha majukumu haya Wizara yangu imejiwekea mikakati ifuatayo:-
8. Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu haya, Wizara ya Ujenzi imefanya mapitio ya mfumo wa utendaji ili shughuli za kiutendaji zifanywe na taasisi zinazojitegemea (Wakala) na Wizara ibaki na majukumu yake ya msingi ya uandaaji wa sera na mikakati inayolenga katika ukuzaji na uimarishaji wa sekta ya ujenzi, kusimamia utendaji na kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mikataba unazingatia viwango vya ubora na utendaji vilivyowekwa na ambavyo vinakubalika. Hadi sasa Wizara yangu imekwishaanzisha Wakala wa Barabara (TANROADS) na inaendelea na maandalizi ya kuanzisha Wakala wa Nyumba. Aidha, hatua mbalimbali zinachukuliwa ili Idara za Ufundi na Umeme na Ugavi na Huduma nazo ziwe Wakala katika kipindi cha mwaka 2001/02.
9. Mheshimiwa Spika, katika kubinafsisha Mashirika ya Umma yaliyoko chini ya Wizara yangu, Serikali imetoa kibali rasmi kuwa Shirika la Mwananchi Engineering and Contracting Corporation (MECCO) liuzwe kwa Kampuni ya Sisi Construction Company Limited (SISICOL) ambayo ni kampuni inayoundwa na wafanyakazi wa MECCO ya zamani kwa kushirikiana na wawekezaji wa kizalendo. Katika makubaliano ya uuzaji, SISICOL itakuwa na asilimia 75 ya hisa na Serikali itabaki na asilimia 25 ya hisa. Aidha, Wizara inaendelea na taratibu za ubinafsishaji wa kampuni ya Plant and Equipment Hire Company (PEHCOL).
MPANGO WA TAIFA WA KUENDELEZA MTANDAO WA BARABARA
10. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka wa fedha wa 1999/00 Wizara inaendelea na maandalizi ya mpango wa miaka kumi wa kuendeleza mtandao wa barabara hapa nchini. Mpango huo utatumika kama mwongozo katika uteuzi wa barabara kuu na za vijijini za kujengwa na kufanyiwa ukarabati kwa kipindi cha miaka kumi ijayo. Rasimu ya mapendekezo ya mpango wa miaka kumi wa maendeleo ya sekta ya barabara itakamilishwa katika kipindi cha mwaka 2001/02.
11. Mheshimiwa Spika, uzoefu tulioupata katika miaka michache iliyopita umetudhihirishia kuwa Serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu. Ushirikiano wa dhati na sekta binafsi ni wa lazima. Nchi yetu imeingia katika milenia mpya ikiwa na malengo makubwa ya kukuza maendeleo kama ilivyo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa hadi mwaka 2025. Mchango wa dhati wa sekta hii ni muhimu sana katika kutekeleza Dira hiyo. Kwa kuwa ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara na madaraja hugharimu fedha nyingi kuliko uwezo wa Serikali, hatuna budi sasa kutafuta vyanzo vingine vya fedha za kugharamia miradi ya barabara na hasa vile vyenye misingi ya kujitegemea kwa kushirikisha sekta binafsi.
12. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendeleza mazungumzo na Wawekezaji binafsi walioonyesha nia ya kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa barabara za Manyoni - Itigi - Tabora - Nzega katika Ukanda wa Kati na Mtwara - Masasi - Songea - Mbamba Bay katika Ukanda wa Kusini. Aidha, ujenzi wa daraja la Kigamboni ni moja ya miradi ambayo inatafutiwa wawekezaji chini ya utaratibu wa Jenga-Endesha-Rejesha (Build - Operate & Transfer - BOT).
USHIRIKIANO NA NCHI ZA KIAFRIKA
13. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya nchi yanapatikana kwa haraka, na yanawiana na yale ya wenzetu tunaofanya nao biashara kwa wingi, nchi yetu imeelekeza juhudi zake katika jumuia mbali mbali za ushirikiano wa kiuchumi ambazo ni Jumuia za Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Ushirikiano wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC). Katika sekta ya ujenzi na usafirishaji, juhudi zinaendelea kufanywa katika kuunganisha miundo mbinu, kuainisha na kuwianisha sera, sheria na mifumo ya pamoja ya kitaasisi na taratibu za utendaji katika nchi zetu.
JUMUIYA YA NCHI ZA KUSINI MWA AFRIKA (SADC)
14. Mheshimiwa Spika, miradi ambayo inahusika chini ya ushirikiano wa Jumuia ya SADC ni pamoja na ile inayotekelezwa kupitia ukanda wa Maendeleo wa Mtwara ambao unajumuisha nchi za Tanzania, Msumbiji, Malawi na Zambia. Katika Tanzania, ukanda huu unajumuisha mikoa minane ambayo ni Mtwara, Lindi, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Rukwa, Pwani na Morogoro.
15. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ndiyo mratibu wa shughuli za Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Wizara yangu inaendelea kuwasiliana na wawekezaji wa nje ambao wameonyesha nia ya kuwekeza katika miradi kadhaa katika sekta za miundo mbinu, nishati na madini pamoja na utalii. Kwa wakati huu, miradi mama (Anchor Projects) imekwishabainishwa. Miradi hiyo ni pamoja na ule wa kuzalisha umeme kutokana na makaa ya mawe ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 400, mradi wa miundo mbinu unaohusu ujenzi wa barabara ya Mtwara - Masasi - Songea - Mbamba Bay pamoja na bandari za Mtwara na Mbamba Bay.
16. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Fedha na Washika dau wengine tumefikia hatua nzuri ya makubaliano na wawekezaji kuhusu Mtwara Development Corridor. Makubaliano ya awali (Agreement of Intent) ya mradi wa umeme wa Mchuchuma - Katewaka yaliwekwa saini kati ya wawekezaji na Serikali tarehe 2/7/2001. Hii ni hatua kubwa katika kufanikisha mradi huu.
17. Mheshimwa Spika, katika kutekeleza majukumu ya ukanda huu, nchi wanachama zinaandaa mfumo wa kisheria ambao unakubalika na kutoa nguvu ya kisheria katika kutekeleza ushirikiano huu wa kiuchumi. Rasimu ya Mkataba wa Maelewano (Memorandum of Understanding) inaandaliwa na itawekwa saini na wakuu wa nchi wanachama itakapokuwa tayari.
USHIRIKIANO WA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI (EAC)
18. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wizara yangu imeendelea na utekelezaji wa miradi ya barabara ambayo imepangwa kutekelezwa kupitia Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki kama ilivyoorodheshwa kwenye Kiambatanisho Na. 1. Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kongamano la wafadhili wa kugharamia miradi ya barabara lililofanyika mwezi Mei 1998, Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki inaandaa kongamano jingine la Wafadhili ili kupata ahadi zao na ushauri wa jinsi ya kuboresha mtandao wa barabara.
BODI YA MFUKO WA BARABARA
19. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mfuko wa Barabara (Road Tolls Amendment No. 2 Act, 1998) ilianzisha Bodi ya Mfuko wa barabara ambayo pamoja na mambo mengine iliimarisha Mfuko kwa kuzuia matumizi nje ya yale yaliyokusudiwa na iliruhusu uundaji wa Bodi ya Mfuko wa Barabara ambayo inajumuisha wawakilishi kutoka Serikalini na sekta binafsi hususan watumiaji wa barabara.
20. Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mfuko wa Barabara ilizinduliwa rasmi mwezi Agosti 1999 na imepewa pamoja na mambo mengine, majukumu makuu yafuatayo:-
21. Mheshimiwa Spika, tangu ilipoanzishwa, Bodi hii pamoja na mambo mengine imefanya yafuatayo:-
22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/01, hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi Juni 2001, Bodi ya Mfuko wa Barabara ilipokea na kugawa jumla ya Shilingi 41,400 milioni ambayo ni asilimia 87.8 ya lengo la mwaka ambalo ni Shilingi 47,100 milioni. Kati ya fedha hizo, Shilingi 2,900 milioni zimetolewa kwa Wizara ya Ujenzi, Shilingi 25,600 milioni kwa TANROADS, Shilingi 600 milioni kwa ajili ya matumizi ya Bodi yenyewe na Shilingi 12,300 milioni kwa Serikali za Mitaa.
23. Mheshimiwa Spika, katika kutelekeza majukumu yake, Bodi ya Mfuko wa Barabara imepanga kutekeleza yafuatayo katika mwaka wa fedha 2001/02:-
24. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2001/02 malengo ya Mfuko wa Barabara ni kukusanya jumla ya Shilingi 50,790 milioni ambazo zitagawanywa kwa TANROADS Shilingi 31,390 milioni, Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa Shilingi 15,240 milioni, Wizara ya Ujenzi Shilingi 3,490 milioni na Bodi ya Mfuko wa Barabara Shilingi 670 milioni. Kutokana na ukweli kuwa chanzo kikuu cha mapato ya Mfuko wa Barabara ni kodi ya mafuta ya dizeli na petroli, Serikali itaendeleza vita dhidi ya biashara haramu ya mafuta haya ili kuongeza mapato ya Mfuko wa Barabara.
WAKALA WA BARABARA (TANROADS)
25. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya mwaka jana katika Bunge hili la Bajeti, nilielezea hatua zilizokuwa zinachukuliwa na Wizara yangu kuanzisha Wakala wa Barabara kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Utekelezaji (Executive Agencies Act, No. 30 ) ya 1997 na Sheria ya Mfuko wa Barabara (Road Tolls Amendment No. 2 Act, 1998). Nafurahi kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Wakala wa Barabara (The Tanzania National Roads Agency) kwa kifupi TANROADS ulianzishwa rasmi tarehe 1 Julai, 2000 ili kutekeleza jukumu la usimamizi wa kazi za Barabara Kuu na Barabara za Mikoa zenye jumla ya kilometa zipatazo 35,000.
26. Mheshimiwa Spika, kuanzishwa kwa TANROADS kunakamilisha mgawanyo wa majukumu ya usimamizi wa sera, taratibu na sheria kama kazi ya msingi ya Serikali kwa upande mmoja, na jukumu la utekelezaji wa kazi za barabara kupewa TANROADS kwa upande mwingine. Katika utekelezaji wa kazi zake taasisi hii mpya itakuwa na mikataba ya utendaji kazi (Performance Agreements) na Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara. Pia TANROADS itakuwa na mikataba na Wizara ya Ujenzi kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
27. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ianzishwe, TANROADS imekamilisha kuunda mfumo wa utawala katika ngazi za Makao Makuu, Kanda na Mikoa. Muundo huu unazingatia kufanya kazi kwa mfumo wa kibiashara na kutoa madaraka ya utekelezaji kazi kwa mikoa na kanda. Katika kipindi cha mpito, Wizara iliamua kuwa wafanyakazi wote wa barabara waliokuwa chini ya zilizokuwa Ofisi za Wahandisi wa Mikoa na baadhi ya wafanyakazi waliokuwa Makao Makuu ya Wizara waazimwe kwa muda wakati TANROADS ikiendelea na taratibu za kuajiri wafanyakazi wake kwa njia ya ushindani.
28. Mheshimiwa Spika, TANROADS pia wamefanikiwa kutayarisha “Business Plan" na kuingia mkataba na Bodi ya Mfuko wa Barabara (Performance Agreement) kwa mujibu wa sheria. Aidha, Wizara imekwishakabidhi baadhi ya miradi ya maendeleo kwa TANROADS kwa ajili ya utekelezaji. TANROADS itaendelea na utaratibu wa kutumia Makandarasi kwa ajili ya kazi za barabara na madaraja. Tangu TANROADS ianzishwe hadi Juni 2001 imekwishatoa kandarasi 1455 katika mikoa yote 20 ya Tanzania kama ilivyoonyeshwa kwenye Kiambatanisho Na. 2.
29. Mheshimiwa Spika, mwito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi wa Mikoa na Wilaya ni kuzipa taasisi hizi mbili mpya (TANROADS na Bodi ya Mfuko wa Barabara) ushirikiano wa karibu ili ziimarike na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Aidha, ushirikiano wenu utahitajika katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na haya yafuatayo:-
· Katika vikao vya Bodi za Barabara za Mikoa, Waheshimiwa Wabunge ni Wajumbe. Hivyo mna jukumu la kuishauri Wizara katika utendaji kazi wa TANROADS.
· Kujadili kwa makini taarifa za utekelezaji ikiwa ni pamoja na taarifa za matengenezo ya barabara na matumizi ya fedha.
· Ni muhimu pia wananchi waelimishwe juu ya jukumu lao kubwa la kutunza barabara zao na wale wanaohusika waache tabia mbaya ya kuvamia na kujenga katika maeneo ya barabara. Pia ni muhimu wananchi wajue kuwa kila barabara imetengewa eneo lake kisheria. Hivyo kabla mwananchi hajajenga katika maeneo yaliyo karibu na barabara hana budi kupata maelezo sahihi ya eneo la barabara. Serikali haipendi kulazimishwa kuwabomolea wananchi wake, lakini vile vile Serikali haitasita kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinafuatwa na kila raia.
UTEKELEZAJI WA KAZI ZA BARABARA KWA MWAKA 2000/01 NA MATARAJIO YA MWAKA 2001/02
25. Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo kuhusu sera na majukumu ya sekta ya ujenzi pamoja na mtazamo katika siku zijazo, naomba sasa nieleze kuhusu utekelezaji wa mpango wa mwaka 2000/01 na matarajio ya mwaka 2001/02.
26. Mheshimiwa Spika, ningependa kuelezea mambo ya jumla yaliyoathiri utekelezaji wa miradi katika mwaka 2000/01 kuwa ni pamoja na:-
· Upungufu wa fedha za ndani za kugharamia miradi.
· Ufanisi duni wa baadhi ya makandarasi katika kutekeleza kazi za barabara.
· Upungufu wa mitambo ya kuwawezesha makandarasi wazalendo kumudu utekelezaji wa kazi za barabara.
· Baadhi ya wahisani kuchelewa kutoa fedha kufuatana na ratiba iliyowekwa.
· Ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi kwa muda uliokubaliwa katika mikataba.
32. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itachukua hatua za dhati za kuyatatua baadhi ya matatizo ambayo yako ndani ya uwezo wetu. Baadhi ya hatua zinazokusudiwa kuchukuliwa na Wizara yangu katika mwaka 2001/02 ni kama ifuatavyo:-
· Kuongeza ufanisi wa makandarasi kwa kuimarisha utoaji wa mafunzo na usimamizi wa kazi.
· Kuimarisha huduma ya ukodishaji mitambo kwenye Karakana za Barabara (Road Workshops) zilizoko katika mikoa ya Mbeya, Tanga na Morogoro.
· Kuhakikisha Bodi ya Mfuko wa Barabara inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
· Kuhakikisha TANROADS inafanya kazi inazopewa na Wizara kwa gharama inayokubalika na kwa ubora na wakati unaotakiwa.
· Kuhamasisha watu na makampuni binafsi kumiliki na kuanzisha shughuli za ukodishaji zana na mitambo ya ujenzi ili kuongeza upatikanaji wake.
· Kuhamasisha watu, mashirika na makampuni binafsi kujenga barabara, madaraja na vivuko kwa utaratibu wa kulipia (Toll Roads and Bridges).
· Kuendelea kuwafutia usajili na hata ikiwezekana kuwachukulia hatua kali zaidi kwa mujibu wa sheria makandarasi watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao kama sheria namba 17 ya mwaka 1997 inavyoelekeza.
· Kuendelea kutumia sheria Na. 15 na 16 za mwaka 1997 katika kudhibiti mwenendo wa kitaaluma wa Wahandisi, Wahandisi Washauri, Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi.
BARABARA KUU
MIRADI YA MAENDELEO YA BARABARA KUU
33. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kutekeleza miradi ya ukarabati na ujenzi mpya wa barabara kuu katika mfumo wa kanda kuu za usafirishaji. Kanda hizo pamoja na barabara zake zimeorodheshwa katika Kiambatanisho Na. 3. Utaratibu huu una lengo la kuhakikisha kwamba barabara zote za kila ukanda zinapitika na kutoa mtiririko wa usafiri wenye uhakika kati ya kanda moja na nyingine.
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/01 Wizara yangu ilipanga kutekeleza jumla ya miradi 24 ya ujenzi, ukarabati na usanifu wa barabara kuu. Muhtasari wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi, ukarabati na usanifu wa barabara kuu umeonyeshwa kwenye Kiambatanisho Na. 4.
35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi 91,799.0 milioni zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo shilingi 16,554 milioni ni fedha za hapa na shilingi 75,245.0 milioni ni fedha za Kigeni. Aidha Wizara imetengewa jumla ya shilingi 3,488 milioni toka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kwa hiyo jumla ya fedha za hapa zitakazotumika kwa shughuli za maendeleo kwa mwaka 2001/02 ni shilingi 20,042.0 milioni. Muhtasari wa Mpango huu umeonyeshwa katika Kiambatanisho Na. 5 na maelezo ya kina ya mradi kwa mradi ni kama yalivyotolewa kwenye aya zinazofuata.
MRADI MAALUM WA KUJENGA BARABARA KUU (SPECIAL PROJECT)
36. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara nchini, Serikali imeanzisha mpango maalum wa kutekeleza miradi ya barabara kwa kutumia fedha za ndani kama Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 5 wa 2001 unavyoelekeza. Katika mpango huu Serikali itakuwa inatenga Shilingi 1,840 milioni kila mwezi kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Wizara yangu imepanga kutekeleza miradi ifuatayo kuanzia mwaka wa fedha wa 2001/02 mpaka 2005/06 kupitia mpango huu maalum:-
· Barabara ya Somanga-Masaninga na Daraja la Matandu (km. 33)
· Barabara ya Nangurukuru-Lindi (km 165)
· Barabara ya Lindi-Mingoyo (km 25)
· Barabara ya Dodoma-Manyoni (km 127)
· Barabara ya Manyoni-Singida (km 118)
33. Mheshimiwa Spika, chini ya mpango huu maalum, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Wizara yangu imepanga kuteua mkandarasi na kuanza ujenzi wa barabara ya Somanga-Matandu kwa kiwango cha lami na Daraja la Matandu. Kazi za usanifu katika sehemu hii ya barabara zimekamilika mwezi Juni 2001 na ujenzi unategemewa kuanza mwanzoni mwa mwezi Septemba 2001. Fedha za usanifu zimetolewa na Serikali ya Denmark. Wizara yangu pia imepanga kufanya usanifu, kuitisha zabuni na kuanza ukarabati kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Lindi-Mingoyo. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Wizara pia imepanga kufanya usanifu, kuitisha zabuni na kuanza ujenzi wa sehemu za Nangurukuru-Lindi, Dodoma-Manyoni na Manyoni-Singida.
34. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi mitano iliyotajwa hapo juu kwa kutumia fedha za ndani pamoja na miradi mingine inayotekelezwa kwa kutumia misaada na mikopo kutoka kwa Wafadhili mbalimbali utatuwezesha kuwa na barabara ya lami yenye kilomita 1,720 kutoka Mtwara mpaka Mwanza kupitia Dar es Salaam ifikapo mwishoni mwa mwaka 2005/06.
BARABARA KUU YA TANZAM (KM 925) SH 14,746 MILIONI.
35. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kufanya ukarabati wa barabara ya TANZAM kwa kuanzia na sehemu zilizoharibika zaidi. Aidha, sehemu ambazo hazijaharibika sana zitaimarishwa kwa kuongeza tabaka la lami. Utekelezaji wa mradi huu ulianza 1988/89 na hadi sasa jumla ya kilomita 356 zimefanyiwa ukarabati.
36. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2000/01, Shilingi 250 milioni za ndani na Shilingi 11,808 milioni za kigeni zilitengwa kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa mradi huu. Kazi ambazo zilipangwa kufanyika ni kukamilisha ukarabati wa sehemu ya Dar es Salaam-Mlandizi yenye urefu wa kilomita 56, kuitisha zabuni na kuanza ukarabati wa sehemu ya Songwe-Tunduma (km 70) na kukamilisha usanifu wa sehemu ya Chalinze-Melela (km 129) na kuitisha zabuni. Kazi ya ukarabati wa barabara ya Dar es Salaam-Mlandizi inatarajiwa kukamilika katika mwezi huu wa Julai 2001. Mkandarasi wa sehemu ya Chalinze-Melela aliteuliwa Desemba 2000 na ameanza maandalizi ya kazi. Mkataba wa Mhandisi Mshauri kwa sehemu ya Songwe - Tunduma ulisainiwa tarehe 12 Juni, 2001 na zabuni kwa upande wa makandarasi zimeitishwa mwezi Mei, 2001 na zitapokelewa mwezi huu wa Julai 2001.
37. Mheshimiwa Spika, malengo ya mwaka wa fedha wa 2001/02 ni kuendelea na ukarabati wa sehemu ya Chalinze-Melela chini ya ufadhili wa Serikali ya Denmark na kuanza ukarabati wa sehemu ya Songwe-Tunduma chini ya ufadhili wa Serikali ya Norway. Aidha, kazi ya usanifu na maandalizi ya ujenzi kwa ajili ya upanuzi wa kilomita kumi (10) eneo la mlima Kitonga katika sehemu ya Msimba-Igawa (km 365) imepangwa kufanyika katika mwaka wa fedha wa 2001/02 kupitia msaada kutoka Japan. Jumla ya Shilingi 150 milioni za ndani na Shilingi 14,596 milioni za kigeni zinahitajika katika mwaka wa fedha wa 2001/02 ili kutekeleza kazi zilizotajwa hapo juu.
BARABARA YA SINGIDA-SHELUI (KM 110) SH 300.0 MILIONI
38. Mheshimiwa Spika, mradi huu ni sehemu ya barabara ya Singida-Shelui-Nzega yenye jumla ya urefu wa kilomita 218 ambao usanifu wake ulianza mwaka 1994/95 chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Mnamo Januari, 1998 Benki ya Dunia ilikubali kugharamia ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya barabara ya Singida-Shelui. Katika mwaka 2000/01 kazi zilizopangwa kutekelezwa zilikuwa kufanya mapitio (updating) ya usanifu wa sehemu ya Singida-Shelui, kuandaa nyaraka za zabuni na kulipa fidia ya mali zitakazoathirika na ujenzi wa barabara hii. Jumla ya Shilingi 205 milioni za ndani na Shilingi 562 milioni za kigeni zilitengwa kwa ajili ya kugharamia kazi hizi. Kazi ya mapitio ya usanifu imeendelea katika mwaka wa fedha wa 2000/01 na inatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa 2001/02.
39. Mheshimiwa Spika, malengo ya mwaka wa fedha wa 2001/02 ni kukamilisha mapitio ya usanifu na kuandaa nyaraka za zabuni, kuitisha zabuni, kuanza maandalizi ya ujenzi na kulipa fidia ya mali zilizopo katika eneo la barabara. Jumla ya Shilingi 300 milioni za ndani zinahitajika katika mwaka wa fedha wa 2001/02 kwa ajili ya fidia ya mali.
BARABARA YA SHELUI-NZEGA (KM 108) SH. 6,432.0 MILIONI
40. Mheshimiwa Spika, mradi huu ni sehemu ya barabara ya Singida-Shelui-Nzega yenye jumla ya urefu wa kilomita 218 ambao usanifu wake ulianza mwaka 1994/95 chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Katika mwaka wa fedha wa 2000/01 mradi huu ulitengewa Shilingi 500 milioni za ndani na Shilingi 1,720 milioni za kigeni kwa ajili ya kulipa fidia, kuitisha zabuni na kufanya maandalizi ya kazi ya ujenzi. Sehemu kubwa ya mali zitakazoathirika na ujenzi zimefidiwa. Zabuni za ujenzi zimekwishapokelewa kutoka kwa makandarasi na uchambuzi kukamilika. Aidha, kibali cha Bodi ya Tenda kilitolewa katika mwezi Juni 2001 na maandalizi ya kusaini mkataba yanaendelea.
41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 450 milioni za ndani na Shilingi 5,982 milioni za kigeni zinahitajika kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, usimamizi na fidia ya mali nyingine zitakazoathirika kutokana na ujenzi wa barabara hii.
BARABARA YA MWANZA-NZEGA/ISAKA (KM 269) SHS. 11,276.0 MILIONI.
42. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kujenga barabara ya lami kati ya Mwanza na Nzega/Isaka (km 269) kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 1994/95 inahusu sehemu ya barabara kati ya Mwanza na mpaka wa Mwanza/Shinyanga (Ilula) yenye urefu wa kilomita 101 kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia. Awamu ya pili inahusu ujenzi wa barabara kati ya Ilula na Nzega (km 133) na Tinde hadi Isaka (km 35). Mradi huu unagharamiwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU).
43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/01 sehemu ya Mwanza-Mto Magogo (km 54) ilitengewa Shilingi 800 milioni za ndani kwa ajili ya kuweka tabaka la pili la lami kwenye kilomita 6 zilizobaki pamoja na ujenzi wa kingo za madaraja (protection works). Kazi hizi zilipangwa kusimamiwa na Mhandisi wa Mkoa wa Mwanza. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2000/01 Shilingi 50 milioni za ndani na shilingi 10,000 milioni za kigeni zilitengwa kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu, uandaaji wa nyaraka za zabuni, kuitisha zabuni na kufanya maandalizi ya ujenzi wa sehemu ya Ilula-Tinde-Nzega na Tinde-Isaka (km 168). Uwekaji wa tabaka la pili la lami kwenye kilomita 6 pamoja na ujenzi wa kingo za madaraja katika sehemu ya Mwanza-Mto Magogo haukufanyika katika mwaka wa fedha 2000/01 kutokana na ukosefu wa fedha. Hata hivyo, kazi hizi zimepangwa kufanyika katika mwaka wa fedha wa 2001/02. Kazi ya mapitio ya usanifu na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya Ilula-Tinde-Nzega na Tinde-Isaka imekamilika katika mwaka wa fedha wa 2000/01. Aidha, zabuni za ujenzi wa sehemu ya Ilula-Tinde-Nzega na Tinde-Isaka zinatarajiwa kuitishwa mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa 2001/02.
44. Mheshimiwa Spika, malengo ya mwaka wa fedha wa 2001/02 ni kuweka tabaka la pili la lami kwenye kilomita 6 zilizobaki pamoja na ujenzi wa kingo za madaraja sehemu ya Mwanza-Mto Magogo. Aidha, kazi ya ujenzi kwa kiwango cha lami itaanza katika sehemu ya Ilula-Tinde-Nzega na Tinde-Isaka. Shilingi 350.0 milioni za ndani na Shilingi 10,926 milioni za kigeni zinahitajika katika mwaka wa fedha wa 2001/02 kwa ajili ya kazi zilizotajwa hapo juu.
BARABARA YA MUTUKULA-MUHUTWE-KAGOMA (KM 136) SHS. 5,779.0 MILIONI.
49. Mheshimiwa Spika, mradi huu ni sehemu ya barabara ya Mutukula-Bukoba-Biharamulo-Lusahunga yenye urefu wa kilomita 294 ambayo usanifu wake ulikamilika mwaka 1996. Usanifu huu uligharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika ambapo ujenzi wake ulipangwa kufanyika kwa awamu. Mnamo mwaka 1997 Benki ya Maendeleo ya Afrika ilikubali kutoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami sehemu ya Mutukula-Bukoba-Muhutwe yenye urefu wa kilomita 112. Aidha, mfuko wa fedha wa OPEC umetoa mkopo wa dola za Kimarekani milioni 6 ili kuiwezesha awamu hii ya kwanza iishie katika mji mdogo wa Kagoma ambao ni kilomita 24 kutoka mji mdogo wa Muhutwe.
50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2000/01 jumla ya Shilingi 1,200 milioni za ndani na Shilingi 2,940 milioni za kigeni zilitengwa kwa ajili ya ulipaji wa fidia, kuanza ujenzi wa sehemu ya Mutukula-Muhutwe na kukamilisha nyaraka za zabuni, ulipaji wa fidia na kuitisha zabuni ya ujenzi wa sehemu ya Muhutwe-Kagoma. Mkandarasi wa sehemu ya Mutukula-Muhutwe amekwishateuliwa na anaendelea na maandalizi ya kuanza ujenzi. Aidha, zabuni ya ujenzi wa sehemu ya Muhutwe-Kagoma inatarajiwa kuitishwa mwezi huu wa Julai 2001.
51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 jumla ya Shilingi 1,000 milioni za ndani na Shilingi 4,779.0 milioni za kigeni zinahitajika kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Mutukula-Muhutwe pamoja na kuanza ujenzi wa sehemu ya Muhutwe-Kagoma.
BARABARA ZA MWANZA MJINI, MWANZA MJINI-UWANJA WA NDEGE NA MWANZA-NYANGUGE (KM 58) SH. 8,557.0 MILIONI.
52. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kukarabati kilomita 13 za barabara za Mwanza mjini na kilomita 10 za barabara iendayo uwanja wa ndege wa Mwanza kwa kiwango cha lami. Aidha, mradi huu unahusisha pia kujenga upya kilomita 35 kwa kiwango cha lami katika sehemu ya Mwanza-Nyanguge. Mradi huu unagharamiwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya pamoja na mchango wa Serikali ya Tanzania. Katika mwaka wa fedha wa 2000/01, Shilingi 150 milioni za ndani na Shilingi 4,500 za nje zilitengwa kwa ajili ya kulipia fidia ya mali na kuanza ukarabati wa barabara zilizotajwa hapo juu. Mkandarasi amekamilisha maandalizi na ameanza kazi za ukarabati wa barabara hizi mwezi Mei 2001.
53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 50 milioni za ndani na Shilingi 8,507 milioni za kigeni zinahitajika kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa barabara za Mwanza Mjini, Mwanza Mjini-Uwanja wa Ndege na Mwanza-Nyanguge.
BARABARA YA DAR ES SALAAM-KIBITI-LINDI-MINGOYO (KM 508) SHS. 11,608 MILIONI.
54. Mheshimiwa Spika, mradi huu una lengo la kujenga na kukarabati barabara hii yenye urefu wa kilomita 508 kati ya Dar es Salaam hadi Mingoyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kilomita 13.5 za tuta la barabara na daraja la mto Rufiji, na madaraja mengine katika sehemu hii ya mradi. Utekelezaji wa mradi huu unakwenda kwa awamu ambapo jumla ya kilometa 74 za barabara ya lami zimekamilika sehemu ya Kibiti-Ikwiriri na sehemu ya Kilwa Masoko-Matandu. Katika mwaka wa fedha wa 1995/96 kazi ya ukarabati wa sehemu ya Dar es Salaam-Kibiti ilianza kwa kutumia fedha za Serikali ya Tanzania na mkopo kutoka Benki ya Dunia na Mfuko wa Fedha wa Kuwait ambapo tayari jumla ya kilomita 53 zimefanyiwa ukarabati. Aidha, hivi karibuni Serikali ilipata mkopo mwingine wa dola za Kimarekani 20 milioni kutoka Mfuko wa Fedha wa Kuwait na mkopo wa dola za Kimarekani 7 milioni kutoka Mfuko wa Fedha wa OPEC kwa ajili ukarabati kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Mkuranga (Kitonga)-Kibiti (km 79) na ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Ndundu-Somanga (km 60).
55. Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Somanga-Matandu-Nangurukuru-Lindi-Mingoyo (km 223) utatekelezwa chini ya Mpango Maalum wa Uboreshaji wa Barabara Kuu wenye lengo la kuboresha barabara nchini kwa kutumia fedha za ndani. Kukamilika kwa barabara ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi-Mingoyo kutaharakisha maendeleo ya mikoa ya kusini hasa Lindi na Mtwara kwa kurahisisha usafiri wa abiria, usafirishaji wa mazao, pembejeo za kilimo na bidhaa nyingine. Pia kukamilika kwa barabara hii kutawavutia watalii kwenda kutembelea mbuga za wanyama za Selous na mji wa Kilwa, kukuza biashara kati ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam, na kurahisisha utekelezaji wa mradi wa gesi wa Songosongo.
56. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2000/01 Shilingi 2,633 za ndani na Shilingi 2,780 milioni za kigeni zikiwa ni mkopo kutoka Mifuko ya Fedha ya Kuwait, OPEC na Saudi zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya kuendelea na kazi ya ukarabati wa sehemu ya Dar es Salaam (Kisemvule)-Mkuranga (km 16) kwa kiwango cha lami, kuendelea na ujenzi wa daraja la mto Rufiji pamoja na barabara ya lami katika bonde la mto Rufiji, kukamilisha ujenzi wa sehemu ya Njenga-Masaninga, kutangaza zabuni ya ukarabati kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Mkuranga (Kitonga)-Kibiti (km 79) na kufanya usanifu na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya sehemu ya Ndundu-Somanga (km 60). Kazi ya ukarabati wa sehemu ya Dar es Salaam (Kisemvule)-Mkuranga ilikamilika katika mwaka wa fedha wa 2000/01 kama ilivyopangwa. Ujenzi wa daraja la mto Rufiji na barabara ya lami katika bonde la mto Rufiji hautakamilika katika mwaka wa fedha wa 2000/01 kama ilivyokuwa imepangwa awali kutokana na matatizo ya fedha za nje yaliyosababisha Mkandarasi kusimamisha kazi kati ya mwezi Aprili na Agosti 2000. Aidha, awamu ya pili ya mradi wa daraja la Rufiji inayojumuisha uwekaji lami kwenye barabara ya Ikwiriri-Ndundu na ujenzi wa kingo (protection works) za madaraja na tuta la barabara ilichelewa kuanza kutokana na kuchelewa kusainiwa kwa mkopo kutoka Mfuko wa Fedha wa OPEC kwa ajili ya kuchangia gharama za kazi hizi.
57. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa daraja la Rufiji kwa hivi sasa unaendelea vizuri ambapo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 70% na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2001/02. Ujenzi wa sehemu ya Njenga-Masaninga unatarajiwa kukamilika kabla ya mwishoni mwa Julai 2001. Aidha, kazi ya usanifu kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Somanga-Matandu pamoja na daraja la mto Matandu (km 33) inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Julai 2001 chini ya msaada kutoka Serikali ya Denmark. Aidha, zabuni kwa ajili ya ukarabati wa sehemu ya Mkuranga (Kitonga)-Kibiti pamoja na usanifu wa sehemu ya Ndundu-Somanga hazikuweza kuitishwa kama ilivyopangwa kutokana na kuchelewa kupata maoni na kibali kutoka Mfuko wa Fedha wa Kuwait kuhusu nyaraka za uteuzi wa Wahandisi Washauri na Makandarasi zilizoandaliwa na Wizara. Kazi hizo sasa zitaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2001/02.
58. Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kufanyika katika mwaka wa fedha wa 2001/02 ni kukamilisha ujenzi wa daraja la Rufiji na barabara ya lami kwenye bonde la mto Rufiji, kuitisha zabuni na kuanza ukarabati kwa kiwango cha lami, sehemu ya Mkuranga (Kitonga)-Kibiti na kufanya usanifu na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, sehemu ya Ndundu-Somanga. Jumla ya Shilingi 1,227 milioni za ndani na Shilingi 10,381 milioni za kigeni zitahitajika katika mwaka wa fedha wa 2001/02 ili kutekeleza kazi zilizotajwa hapo juu. Malengo ya mwaka wa fedha wa 2001/02 katika sehemu ya Somanga-Matandu, Nangurukuru-Lindi na Lindi-Mingoyo yameelezwa kwenye Mpango Maalum wa Uboreshaji wa Barabara Kuu.
BARABARA YA DAR ES SALAAM (WAZO HILL)-BAGAMOYO (KM 43) SHS. 1,382.0 MILIONI
59. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kujenga barabara yenye urefu wa kilometa 43 kati ya Wazo Hill na Bagamoyo kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara hii utaimarisha utalii wa sehemu za kihistoria za Bagamoyo na pia hoteli za kitalii zilizoko kwenye ufuko wa bahari ya Hindi. Mradi unagharamiwa kwa pamoja kwa msaada wa Serikali ya Italia na Jumuiya ya Nchi za Ulaya. Serikali ya Tanzania inagharamia fidia zote za mali zilizoathirika kutokana na utekelezaji wa mradi huu.
60. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/01 Shilingi 800 milioni za ndani na Shilingi 4,173 milioni za kigeni zilitengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara hii. Utekelezaji wa mradi huu unaendelea na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2001/02. Aidha, jumla ya Shilingi 100 milioni za ndani na Shilingi 1,282 milioni za kigeni zitahitajika katika mwaka wa fedha wa 2001/02 ili kukamilisha mradi huu.
MADARAJA YA BARABARA KUU SH. 7,500.0 MILIONI
61. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kutathmini, kufanya usanifu, na kukarabati madaraja yaliyoharibika kwenye barabara kuu ya TANZAM, Tanga-Horohoro na Tunduma-Sumbawanga kwa kutumia mkopo kutoka Benki ya Dunia. Katika mwaka wa fedha 2000/01 Shilingi 600 milioni za ndani na Shilingi 3,200 milioni za kigeni kutoka Benki ya Dunia zilitengwa kwa ajili ya kukamilisha uandaaji wa nyaraka za zabuni, kuitisha zabuni na kuanza ukarabati wa madaraja 22 katika barabara kuu zilizotajwa hapo juu. Zabuni za Wahandisi Washauri na Makandarasi ziliitishwa na uchambuzi wa zabuni za Wahandisi Washauri umekamilika. Aidha, uchambuzi wa zabuni za Makandarasi ulikamilika katika mwezi Juni 2001.
62. Mheshimiwa Spika, malengo ya mwaka wa fedha wa 2001/02 ni kuanza ukarabati wa madaraja 22 yaliyotajwa hapo juu. Mradi huu utahitaji Shilingi 300 milioni za ndani na Shilingi 7,200 milioni za kigeni katika mwaka wa fedha wa 2001/02.
BARABARA YA MAKUYUNI-LANGO LA NGORONGORO (KM 77) SHS. 4,400.0 MILIONI.
63. Mheshimiwa Spika, barabara ya Makuyuni-Lango la Ngorongoro yenye urefu wa kilomita 77 ilifanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 1988/89. Hapo awali mategemeo ya kupata msaada kutoka kwa wafadhili ili kufanya usanifu yalishindikana kutokana na suala la mazingira. Hata hivyo, Serikali ya Tanzania ilichunguza na kuhakikisha kuwa ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami hautakuwa na madhara kwenye mazingira, hivyo ikaamua kugharamia usanifu kwa kutumia uwezo wake wa ndani. Aidha, hivi karibuni Serikali ya Japan iliamua kugharamia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
64. Mheshimiwa Spika, malengo ya mwaka wa fedha 2000/01 yalikuwa kukamilisha kazi ya usanifu na kuandaa nyaraka za zabuni. Shilingi 100 milioni za ndani zilitengwa kwa ajili ya malipo ya mwisho ya Mhandisi Mshauri. Usanifu wa barabara hii umekamilika na zabuni ya ujenzi itaitishwa katika mwaka 2001/02. Ujenzi wa barabara hii unatarajia kuanza katika mwaka wa fedha wa 2001/02 ambapo Shilingi 100 milioni za ndani na Shilingi 4,300 milioni za kigeni zitahitajika kwa ajili ya kulipia fidia pamoja na gharama za ujenzi.
BARABARA YA MAKUTANO-KYARANO (KM 12) SH. 240.81 MILIONI.
65. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kujenga barabara ya lami kati ya Makutano na Butiama (km 12) mkoani Mara. Usanifu wa barabara hii ulikamilika katika mwaka wa fedha wa 1992/93 na nyaraka za zabuni kutayarishwa. Hata hivyo, ujenzi wa barabara hii ulichelewa kuanza kutokana na ukosefu wa fedha. Kutokana na kuchelewa huko, usanifu na nyaraka za zabuni zilihitaji mapitio (updating) ili kuzingatia hali halisi ya barabara hii kwa sasa na kuwezesha kuitisha zabuni ya ujenzi. Katika mwaka wa fedha wa 2000/01 mradi huu ulitengewa Shilingi 150 milioni za ndani kwa ajili ya kukamilisha usanifu, kuitisha zabuni na kuweka makalvati thelathini (30). Kazi ya usanifu imekamilika na maandalizi ya kuitisha zabuni ya kuweka makalvati 30 yanaendelea. Aidha, uitishaji wa zabuni ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utafanyika katika mwaka wa fedha wa 2001/02.
66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 240.81 milioni za ndani zitahitajika kwa ajili ya kuitisha zabuni, kulipa fidia ya mali zilizopo katika eneo la barabara na kufanya maandalizi ya ujenzi.
BARABARA YA NELSON MANDELA - (KM 16.8) SH. 1,272.0 MILIONI.
67. Mheshimiwa Spika, barabara ya Nelson Mandela ilijengwa katikati ya miaka ya sabini na kwa sasa hivi ni moja ya barabara zenye msongamano mkubwa wa magari hapa nchini. Sensa ya karibuni ya magari iliyofanyika katika barabara hii inaonyesha kuwa barabara hii inatumiwa na magari yapatayo 20,000 kwa siku ambapo kati ya hayo asilimia 50% ni magari ya biashara. Malengo ya mradi huu ni kuimarisha barabara hii kwa kuongeza tabaka la lami. Kazi nyingine zitakazofanyika sambamba na uimarishaji wa barabara hii ni kuboresha mfumo wa mifereji pamoja na taa za barabarani na zile za kuongozea magari (street lighting and traffic lights). Aidha, mizani ya kupimia uzito wa magari itawekwa nje ya lango la kutokea bandarini ili kudhibiti uzito wa magari ya mizigo yanayotoka bandarini. Mradi huu utagharamiwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya pamoja na mchango wa Serikali ya Tanzania.
68. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 50 milioni za ndani na Shilingi 1,222 milioni za kigeni zinahitajika kwa ajili ya kuitisha zabuni na kuanza ukarabati wa barabara hii.
BARABARA YA MOROGORO-DODOMA (KM 256) SH. 4,940.0 MILIONI.
69. Mheshimiwa Spika, barabara ya Morogoro-Dodoma (km 256) ilijengwa hadi kufikia kiwango cha lami mwanzoni mwa miaka ya themanini. Hata hivyo, kutokana na barabara hii kukosa matengenezo ya muda maalum (periodic maintenance) kwa wakati unaotakiwa kwa sababu ya ufinyu wa bajeti, ilibidi ifanyiwe matengenezo ya dharura mwaka 1999 baada ya kuharibika sana. Ingawa barabara hii kwa sasa inapitika kwa urahisi, hali ya barabara katika sehemu ya Morogoro hadi njia panda ya Dakawa na kwenye bonde la Wami sio nzuri.
70. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kujenga upya sehemu zilizoharibika zaidi na kuimarisha sehemu zilizobaki kwa kuongezea tabaka la lami. Mradi huu utagharamiwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya pamoja na mchango wa Serikali ya Tanzania. Katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 70 milioni za ndani na Shilingi 4,870 za nje zinahitajika kwa ajili ya kuitisha zabuni na kuanza ukarabati wa barabara hii.
DARAJA LA MPIJI SH. 100.0 MILIONI.
71. Mheshimiwa Spika, daraja la Mpiji lipo katika barabara ya Dar es Salaam (Wazo Hill) - Bagamoyo ambayo ujenzi wake unaendelea. Daraja la sasa la Mpiji ambalo lina urefu wa meta 42.2 na upana wa meta 3.2 haliruhusu magari kupishana. Aidha, katika mradi wa barabara ya Dar es Salaam (Wazo Hill)-Bagamoyo fedha zilizotolewa na Wafadhili zilikuwa ni kwa ajili ya kulifanyia matengenezo tu daraja hili. Malengo ya mradi wa daraja la Mpiji ni kuanza usanifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja jipya la Mpiji linalotarajiwa kuwa na urefu wa meta 60 na upana utakaowezesha magari mawili kupishana. Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa kutumia fedha za ndani. Katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 100 milioni za ndani zinahitajika wa ajili ya usanifu na kuitisha zabuni kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili.
BARABARA YA MBEYA - MAKONGOLOSI (KM 125): SHS. 80 MILIONI
72. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara kati ya Mbeya na Makongolosi kupitia Chunya kwa kiwango cha lami. Mradi huu ulikuwa utekelezwe katika kipindi cha 1999/00 lakini kutokana na uhaba wa fedha za miradi ya maendeleo kazi za mradi huu hazikufanyika. Kutokana na sababu hii, mradi huu ulipangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2000/01. Katika mwaka wa fedha wa 2000/01 Shilingi 100 milioni za ndani zilitengwa kwa ajili ya kazi ya kuitisha zabuni za Wahandisi Washauri na kufanya upembuzi yakinifu wa barabara hii. Uchambuzi wa zabuni za Wahandisi Washauri umekamilika na kazi ya upembuzi yakinifu inatarajiwa kuanza Agosti 2001. Kati ya fedha zilizotengwa, Shilingi 20 milioni zitatumika kwa ajili ya malipo ya awali kwa Mhandisi Mshauri ambaye amekwishateuliwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 80 milioni za ndani zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu.
BARABARA YA TUNDUMA-SUMBAWANGA (KM 231): SH.420 MILIONI.
73. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia. Malengo ya kazi katika mwaka wa fedha wa 2000/01 yalikuwa kuitisha zabuni kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu wa barabara hii. Aidha, kazi ya upembuzi yakinifu ilipangwa kuanza mara baada ya kukamilika kwa kazi ya uchambuzi wa zabuni. Zabuni za Wahandisi Washauri zimepokelewa na uchambuzi unaendelea. Kazi ya upembuzi yakinifu inatarajia kuanza na kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2001/02. Jumla ya Shilingi 20 milioni za ndani na Shilingi 400 milioni za kigeni zinahitajika kwa ajili ya kufanya na kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu wa barabara hii.
BARABARA YA MAKUYUNI – OLDEANI – LALAGO.
74. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu lilikuwa ni kufanya upembuzi yakinifu wa sehemu ya Makuyuni – Oldeani – Lalago kupitia Kusini mwa Ziwa Eyasi kwani kuanzia Lalago hadi Lamadi hakukuwa na athari kubwa za mazingira. Katika mwaka wa fedha 2000/01, Mhandisi Mshauri alikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na kuwasilisha taarifa ya mwisho ya upembuzi yakinifu mwishoni mwa April, 2001. Wizara inapitia na kutafakari taarifa hiyo kwa madhumuni ya kuendelea na hatua zinazofuata katika utekelezaji wa mradi huu. Wakati Serikali inaendelea kutathmini mapendekezo ya Mhandisi Mshauri, Wizara kupitia Wakala wa Barabara itaendelea kuzifanyia matengenezo sehemu za Karatu - Mbulu - Haydom na Mwanhuzi - Lalago za barabara hiyo pamoja na kuboresha matengenezo ya madaraja ili iweze kupitika kirahisi.
BARABARA YA MTO WA MBU – LOLIONDO.
75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/01 kazi ya upenguzi yakinifu wa barabara hii ilikamilika na Mhadisi Mshauri kuwasilisha taarifa ya matokeo ya upembuzi yakinifu mwezi Oktoba, 2000. Matokeo ya utafiti yalibaini kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 209.4 kwa kiwango cha changarawe ungegharimu jumla shilingi 26 bilioni. Hata hivyo, tathmini ya kiuchumi inaonyesha kuwa barabara hiyo kwa sasa haikidhi vigezo vya kiuchumi vya kuiwezesha kujengwa kwa kiwango cha changarawe. Pamoja na barabara hiyo kutokidhi vigezo vya kiuchumi vya kuiwezesha kujengwa kwa kiwango cha changarawe, Serikali imebaini faida ambazo zitaweza kupatikana kama barabara hiyo itajengwa. Faida hizo ni pamoja na:-
· Kufunguka kwa maeneo itakamopita barabara kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ujumla,
· Kuwepo kwa mawasiliano na Makao Makuu ya Wilaya,
· Kuimarika kwa hali ya usalama katika Wilaya,
· Kufungua eneo kwa shughuli za kilimo, na
· Kulifungua eneo kwa shughuli za kitalii.
76. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia faida zilizotajwa hapo juu, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) itaendelea kuhudumia barabara hiyo kwa kuweka makalvati kwenye baadhi ya sehemu, kuweka changarawe kwenye sehemu muhimu ili kuiwezesha barabara hiyo kupitika kwa kipindi kirefu cha mwaka. Kazi hizo zinatarajia kugharimu jumla ya shilingi 282.4 milioni. Katika mwaka wa fedha 2001/02 kazi hizi zitatekelezwa kama sehemu ya mpango wa matengenezo ya barabara za vijijini katika Mkoa wa Arusha.
BARABARA YA KANDA YA KATI (CENTRAL CORRIDOR BOT ROAD PROJECT) NA MTWARA CORRIDOR SH. 100.0 MILIONI.
77. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwashirikisha Wawekezaji Binafsi katika kutekeleza miradi ya ujenzi/ukarabati wa barabara. Utaratibu huu unalenga katika kutafuta vyanzo vingine vya fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya barabara. Tayari baadhi ya Wawekezaji wameonyesha nia ya kuwekeza katika miradi ya barabara na Serikali inaendeleza mazungumzo na wawekezaji ambao wameonyesha nia ya kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa barabara za Manyoni - Itigi - Tabora - Nzega katika Ukanda wa Kati na Mtwara - Masasi - Songea - Mbinga - Mbamba Bay katika Ukanda wa Kusini kupitia Mtwara Corridor.
78. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02, Wizara yangu itaendeleza majadiliano na wawekezaji pamoja na kutafuta wawekezaji kwa ajili ya miradi mingine. Jumla ya Shilingi 100 milioni zimeombwa ili kuendelea na kazi za uratibu wa Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara na pia kuanzisha na kuratibu kanda nyingine za maendeleo. Aidha, wakati tunaendelea kujadiliana na wawekezaji kwa ajili ya barabara za Manyoni - Itigi - Tabora na Mtwara - Masasi - Songea - Mbinga - Mbamba Bay, Wizara yangu itaendelea kuzifanyia matengenezo barabara hizo wakati tukisubiri kukamilika kwa majadiliano na wawekezaji.
BARABARA YA UVINZA-ILUNDE-MALAGARASI-KALIUA (KM 194) SH. 100.0 MILIONI.
79. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kufanya usanifu na ujenzi wa barabara kati ya Uvinza na Kaliua (km 194) pamoja na ujenzi wa daraja la mto Malagarasi. Kazi ya usanifu na ujenzi wa daraja la chuma katika mto Malagarasi ilikamilika katika mwaka wa fedha wa 1999/00. Aidha, kazi ya usanifu wa sehemu ya Ilunde-Malagarasi (km 28) ilikamilika katika mwaka wa fedha wa 2000/01. Malengo ya mwaka wa fedha wa 2001/02 ni kuitisha zabuni kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya Ilunde-Malagarasi (km 54) kwa kiwango cha changarawe. Jumla ya Shilingi 100 milioni za ndani zimetengwa katika mwaka wa fedha wa 2001/02.
BARABARA YA USAGARA-CHATO-KYAMYORWA (KM 326) SHS. 400.0 MILIONI.
80. Mheshimiwa Spika, lengo la mradi huu ni kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Usagara-Chato-Kyamyorwa yenye urefu wa kilomita 326. Katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 400 milioni za ndani zinahitajika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa barabara hii.
BARABARA YA MARANGU-TARAKEA (KM 52) SH. 100.0 MILIONI.
81. Mheshimiwa Spika, barabara ya Marangu-Tarakea (km 52) ilifanyiwa upembuzi yakinifu na wataalam wa Wizara mwaka 1998 na ikakidhi mahitaji ya kiuchumi ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Lengo la mradi huu ni kufanya usanifu kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Shilingi 100 milioni za ndani zinahitajika kwa ajili ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu wa barabara hii.
MATENGENEZO YA BARABARA KUU
82. Mheshimiwa Spika, Matengenezo ya barabara kuu yamepangwa kugharimu jumla ya shilingi 38,887.7 milioni zikiwa ni shilingi 16,790.1 za Mfuko wa Barabara na shilingi 22,097.6 milioni kutoka kwa wahisani mbalimbali.
Matengenezo ya Kawaida
83. Mheshimiwa Spika, chini ya mpango wa matengenezo ya kawaida ya barabara kuu kwa mwaka 2000/01, jumla ya kilometa 3,658 za lami na kilometa 2,266 za changarawe zilipangwa kufanyiwa matengenezo ya kawaida. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2001, jumla ya kilometa 5,057 zilikuwa zimefanyiwa matengenezo ya kawaida.
84. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02, jumla ya kilometa 3,964 za barabara kuu za lami na kilometa 3,337 za barabara kuu za changarawe katika mikoa yote 20 ya Tanzania zitafanyiwa matengenezo ya kawaida kwa gharama ya Shilingi 6,796 milioni zinazotokana na Mfuko wa Barabara pamoja na Wahisani.
Matengenezo ya Muda Maalum
85. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2000/01, jumla ya kilometa 99 za barabara kuu zinazohusisha uwekaji wa tabaka jipya la lami kilometa 77 na tabaka jipya la changarawe kilometa 22 zilipangwa kufanyiwa matengenezo ya muda maalum. Hadi mwezi Juni 2001, kilometa 97 zilikuwa zimefanyiwa matengenezo ya muda maalum.
86. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02, jumla ya kilometa 79 za barabara kuu zitafanyiwa matengenezo ya muda maalum, kazi ambayo itagharimu jumla ya shilingi 5,617 milioni za Mfuko wa Barabara na wahisani mbalimbali.
Matengenezo Makubwa, ya Sehemu Korofi na ya Dharura
87. Mheshimiwa Spika, malengo katika mwaka wa fedha 2000/01 yalikuwa kuendeleza na kukamilisha matengenezo ya dharura katika barabara zilizoharibiwa na mvua za El-Nino, pia kufanya matengenezo kwa barabara kuu zilizokosa matengenezo kwa muda mrefu. Jumla ya kilometa 830 zilipangwa kufanyiwa matengenezo. Hadi mwezi Juni 2001, jumla ya kilometa 780 zilikuwa zimefanyiwa matengenezo ya dharura na ya sehemu korofi.
88. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2001/02 jumla ya kilometa 16 za barabara kuu za lami zitafanyiwa matengenezo ya sehemu korofi kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara na jumla ya Shilingi 840 milioni zitatumika. Aidha kilometa 338 za barabara kuu zisizo za lami zitahusika katika matengenezo ya sehemu korofi kwa gharama ya Shilingi 4,239.3 milioni toka katika Mfuko wa Barabara na wahisani mbalimbali. Kuhusu matengenezo makubwa (backlog maintenance), jumla ya Shilingi 16,166.9 milioni za Mfuko wa Barabara na wahisani mbalimbali zitatumika kwa matengenezo ya kilometa 1054. Aidha, jumla ya Shilingi 3,976.8 milioni za Mfuko wa Barabara zimepangwa kutumika kwa matengenezo ya dharura yatakayojitokeza.
Matengenezo ya Madaraja
89. Mheshimiwa Spika, takwimu za madaraja tulizonazo zinaonyesha kuwa kuna madaraja 4,010 yanayohudumiwa na Wizara yangu ambapo madaraja, 1,904 yamo katika barabara za vijijini na madaraja 2,106 yamo katika barabara kuu. Aidha, hali ya madaraja 220 katika barabara hizo ni mbaya. Katika mwaka wa fedha wa 2000/01, madaraja na makalvati 2,009 katika barabara kuu yalipangwa kufanyiwa matengenezo. Mpaka kufikia mwezi Juni 2001, madaraja na makalvati 230 yalikuwa yamefanyiwa matengenezo.
90. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 jumla ya Shilingi 602.70 milioni kutoka katika Mfuko wa Barabara zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kuyafanyia matengenezo ya kawaida madaraja na makalvati yapatayo 2,009 katika barabara kuu. Aidha, zaidi ya madaraja 19 yaliyopo katika barabara kuu yatafanyiwa matengenezo makubwa kwa gharama ya shilingi 648.4 milioni za Mfuko wa Barabara na wahisani. Muhtasari wa makisio ya kazi zote za matengenezo ya barabara katika mwaka wa 2001/2002 yameonyeshwa kwenye Kiambatanisho Na. 6 na kazi zote hizi zitasimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS).
91. Mheshimiwa Spika, mpango wa matengenezo ya barabara kuu uliofafanuliwa hapo juu unajumuisha pia matengenezo ya barabara za Itigi - Rungwa - Mbeya, Sumbawanga - Kigoma - Kasulu - Nyakanazi (Kiambatanisho 6h), Mwandiga - Manyovu (Kiambatanisho 6e) na Minjingu - Babati - Dodoma - Iringa ambazo ni barabara muhimu katika mtandao wa barabara za Ushirikiano wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
BARABARA ZA VIJIJINI
MAPITIO YA MPANGO WA MWAKA 2000/01
92. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/01, kwa upande wa barabara za vijijini malengo ya kazi yalikuwa kama ifuatavyo:
· Kukarabati barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 641
· Ujenzi wa madaraja 8 katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro
· Ukarabati na uboreshaji wa gati ya kivuko cha Kigamboni mkoani Dar es Salaam upande wa Kigamboni.
· Kufanya matengenezo ya Kawaida (Routine & Reccurent maintenance) kwa barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 10,256 pamoja na madaraja 1,500 katika mikoa yote 20.
· Kufanya matengenezo ya Muda Maalum (Periodic Maintenance) kwenye barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 281.5 katika mikoa yote 20.
· Kufanya matengenezo ya sehemu korofi (Spot Improvement) na ya dharura (Emergency Works) kwenye barabara zenye jumla ya kilometa 8,392 katika mikoa yote 20.
93. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Juni 2001 ukarabati wa kilometa 476 za barabara za vijijini ulikuwa umekamilika, ujenzi wa madaraja 4 umekamilika na madaraja mengine 2 yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Aidha, ukarabati na uboreshaji wa gati ya kivuko cha Kigamboni upo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji. Pia matengenezo ya kawaida kilometa 3,730, matengenezo ya dharura na sehemu korofi kilometa 5,357 na matengenezo ya madaraja 180 yamefanyika. Muhtasari wa taarifa ya utekelezaji ni kama ilivyoonyeshwa katika Kiambatanisho Na. 4
MPANGO WA MATENGENEZO YA BARABARA ZA VIJIJINI KWA MWAKA 2001/02
94. Mheshimiwa Spika, lengo la mpango wa matengenezo ya barabara Vijijini kwa mwaka wa fedha 2001/02 umefafanuliwa kwenye Kiambatanisho Na. 6 na kwa kifupi ni kama ifuatavyo:-
· Kufanya matengenezo ya kawaida kwa barabara za changarawe/udongo zenye urefu wa jumla ya kilometa 8,352 kwa gharama ya Shilingi 3,880.13 milioni na za lami zenye urefu wa kilometa 159 kwa gharama ya Shilingi 84.95 milioni pamoja na kufanya matengenezo makubwa kwenye madaraja 28 katika mikoa yote 20 kwa gharama ya Shilingi 828.80 milioni; fedha zote hizo zikiwa ni za Mfuko wa Barabara na michango ya wahisani mbalimbali.
· Kufanya matengenezo ya kawaida ya madaraja 1,463 kwa gharama ya Shilingi 438.90 milioni za Mfuko wa Barabara.
· Kufanya matengenezo ya muda maalum kwenye barabara za lami zenye urefu wa jumla ya kilometa 19 kwa gharama ya shilingi 672 milioni za Mfuko wa Barabara.
· Kufanya matengenezo ya sehemu korofi kwenye barabara za changarawe/udongo zenye jumla ya kilometa 553 katika mikoa yote 20 kwa gharama ya Shilingi 6,587.68 milioni za Mfuko wa Barabara na wahisani mbalimbali.
· Kufanya matengenezo ya dharura yatakayojitokeza kwenye barabara. Jumla ya Shilingi 2,366.98 milioni za Mfuko wa Barabara zimepangwa kwa ajili ya kazi hizo za dharura.
MIRADI YA MAENDELEO YA BARABARA ZA VIJIJINI KWA MWAKA 2001/02
95. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02, Wizara yangu imepanga kuzifanyia ukarabati barabara zenye jumla ya kilometa 77.7. Miradi ya ukarabati itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2001/2002 imeonyeshwa katika Kiambatanisho Na. 7. Miradi hiyo ni ukarabati wa kilometa 16 za barabara ya Ubena - Ngerengere - Kiganila iliyopo mkoani Morogoro, ukarabati wa kilometa 35 za barabara ya Makofia - Mlandizi na ujenzi kwa kiwango cha lami urefu wa kilometa 2.7 za barabara ya Pugu - Kisarawe zilizopo mkoani Pwani na ujenzi wa daraja la Kyabakoba mkoani Kagera. Miradi hii itagharamiwa na fungu la bajeti ya maendeleo. Vilevile fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund) zitatumika kugharamia ukarabati wa kilometa 10 za barabara ya Mvuha-Mgeta Kafa mkoani Morogoro na kuchangia ukarabati wa kilometa 14 za barabara zinazokwenda kwenye mahoteli ya kitalii yaliyoko kwenye ufukwe wa bahari mkoani Dar es Salaam.
MATUMIZI YA TEKINOLOJIA YA NGUVU KAZI
96. Mheshimiwa Spika, mradi huu una lengo la kuendeleza teknolojia inayohusu matumizi ya nguvu kazi (Labour Based Technology) katika ukarabati, matengenezo na ujenzi wa barabara. Katika mwaka wa fedha wa 2000/01, Wizara yangu iliendelea kutumia teknolojia hii katika kazi za barabara pale ilipowezekana. Aidha, Wizara imefanikiwa kutoa nakala 500 za vitabu vya miongozo na maelekezo ya matumizi ya teknolojia hii (Labour Based Technical Manuals) na mpaka sasa zaidi ya vitabu 435 vimesambazwa kwa watumiaji na watendaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wahandisi wa Mikoa, Wahandisi wa Wilaya, Makandarasi na Wahandisi Washauri.
97. Mheshimiwa Spika, Wizara ilipanga kukiimarisha chuo kinachotoa mafunzo ya matumizi sahihi ya teknolojia hii (Appropriate Technology Training Institute – ATTI) kilichopo Kiwira mkoani Mbeya. Tathmini ya kina imefanyika kwa kutumia Mtaalam Mshauri (Consultant) ambapo imebainika kuwa chuo hiki kinaweza kujiendesha chenyewe kama Wakala endapo kitapewa uwezo kifedha, kitaaluma na kimaamuzi. Wizara yangu inayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Mshauri huyo kwa lengo la kuhakikisha chuo kinaanza mapema iwezakanavyo kutoa mafunzo tena kwa walengwa ambao ni Wahandisi, Wasimamizi na Wajenzi wa barabara kutoka sekta za umma na binafsi.
98. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02, Wizara yangu ina mpango wa kuendelea kutoa miongozo na maelekezo ya utumiaji wa teknolojia hii kwa walengwa wote na kutathmini mwenendo mzima wa utekelezaji katika kazi za barabara. Wizara itakamilisha kutathmini mapendekezo yaliyotolewa na Mtaalam Mshauri na kuanza kuchukua hatua za kukiendeleza chuo cha ATTI ili kiweze kutoa mafunzo kwa walengwa wote kwa ufanisi zaidi. Wizara yangu pia itaendelea kufanya utafiti katika nyanja za vifaa bora vinavyohitajika pamoja na mbinu mbalimbali za kiutendaji ili kuimarisha na kuendeleza ubora wa kazi zinazofanyika kwa kutumia teknolojia hii.
USHIRIKISHWAJI WA WANAWAKE
99. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekuwa ikiendelea kuhamasisha na kuelimisha wanawake ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi katika kazi za barabara tangu mwaka 1992/93. Juhudi hizi zimeleta mafanikio, kwani katika baadhi ya mikoa tayari asilimia 20 hadi 35 ya nguvu kazi ya kazi za barabara ni wanawake. Mbinu zilizotumika katika kufanikisha kazi hii ni pamoja na kuielimisha jamii kuhusu suala hili, kuwaelimisha wanawake wenyewe na kutoa mafunzo ya matengenezo ya barabara.
100. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2000/01, Wizara yangu ilipanga kuhakikisha kuwa ajira ya nguvu kazi ya wanawake na ushiriki wao katika kazi za barabara nchini unaongezeka. Mafunzo ya uhamasishaji kwa wasichana wa shule za sekondari yaliendelea kutolewa ili wapende masomo ya Sayansi na Ufundi ambayo ni masomo ya msingi kwa Wahandisi au Mafundi Mchundo. Wizara yangu kupitia Kitengo cha Wanawake iliweza kutoa mafunzo kwa watumishi wanawake Serikalini 30 ambao watatumika kuhamasisha wasichana waliopo kwenye shule za sekondari ili wapende zaidi masomo ya Sayansi na Ufundi kwa lengo la kuwa Wahandisi au Mafundi Mchundo hapo baadaye.
101. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Chama cha Wahandisi, Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi Wanawake (WEQA); Kitengo cha Wanawake na kwa msaada wa Serikali ya Denmark kupitia Shirika lake la DANIDA imefanya kongamano la wanawake Wahandisi, Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi wapatao 150 ambapo pamoja na mambo mengine waliweka mikakati ya kumwendeleza mwanamke katika sekta ya ujenzi kuanzia ngazi ya juu hadi vijijini.
102. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Wizara yangu imepanga kutoa mafunzo ya upangaji mipango na bajeti yenye mtazamo wa ushiriki wa kijinsia kwa watendaji katika ngazi ya Wizara na Mikoa ili kujenga msingi imara wa ushirikishwaji wanawake katika sekta ya ujenzi. Aidha, kitengo hiki kwa kushirikiana na vyombo vingine kitaendelea kuhamasisha wanawake katika mikoa yote ili waweze kuunda vikundi vya ukandarasi kwa lengo la kufaidika na zabuni za barabara na kuongeza ajira ya nguvu kazi kwa wanawake.
KITUO CHA UENEZAJI WA TEKINOLOJIA
103. Mheshimiwa Spika, Kituo hiki cha uenezaji wa teknolojia (Tanzania Technology Transfer Centre (T2 Centre)) katika sekta ya usafirishaji kilianzishwa mwaka 1997 kutokana na juhudi za Wizara yangu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na msaada wa Mamlaka ya Barabara ya Marekani (US Federal Highway Administration); madhumuni yake ikiwa ni kuimarisha na kuboresha miundo mbinu ya usafirishaji kwa kutumia mbinu ya uenezaji wa teknolojia. Kwa kuanzia kituo kinajihusisha na uenezaji wa teknolojia inayohusu miundombinu ya sekta moja ya usafirishaji ambayo ni barabara.
104. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/01, Wizara yangu kwa kupitia kituo hiki iliendelea kueneza teknolojia katika sekta ya usafirishaji wa barabara hapa nchini kwa kuendesha semina ya kuhamasisha washikadau katika sekta hii kuhusu mikakati ya uenezaji wa teknolojia, kuendesha kozi moja ya kufundisha wakufunzi juu ya usalama barabarani kwenye sehemu za ujenzi na matengenezo ya barabara na kuanza kutekeleza mradi wa TRAC (Transportation and Civil Engineering) ambao unahamasisha wanafunzi wa shule za sekondari kuchukua masomo ya sayansi katika shule za sekondari za Jangwani, Mzizima na Azania zilizoko jijini Dar es Salaam.
105. Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Mei, 2001 kituo kiliandaa kongamano la kwanza la kimataifa Barani Afrika kuhusu uenezaji wa teknolojia katika masuala ya sekta ya barabara. Kongamano hilo lilifanyika mjini Arusha na lilihudhuriwa na washiriki wapatao mia mbili kutoka nchi za Afrika, Marekani, Ulaya na Asia. Pia kituo kiliendelea kutekeleza mpango wa kutembeleana na nchi/taasisi tunazoshirikiana nazo ili kujifunza na kubadilishana uzoefu katika sekta ya usafirishaji, kimeanzisha njia ya kisasa ya upashanaji habari na nyaraka mbalimbali za kitaalam kupitia mtandao wa kompyuta (Website), kimeboresha huduma ya maktaba ya kituo na kuimarisha huduma za kituo kwa ujumla kwa kununua vitendea kazi mbalimbali.
106. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2001/02, Wizara yangu ina mpango wa kukiendeleza kituo hiki ili kiendelee na mpango wake wa uenezaji wa teknolojia katika sekta ya barabara kwa kufanya yafuatayo:-
· Kuandaa warsha ya washikadau katika sekta ya usafirishaji na kutayarisha mpango wa muda mfupi na mrefu kuhusu uenezaji wa teknolojia hapa nchini.
· Kuandaa kozi zinazohusu sekta ya usafirishaji.
· Kuendeleza utekelezaji wa mradi wa kuhamasisha wanafunzi wa shule za Sekondari kuchukua masomo ya sayansi na teknolojia (TRAC Programme).
· Kuendelea kutekeleza mpango wa kutembeleana na nchi na taasisi tunazoshirikiana nazo ili kujifunza na kubadilishana uzoefu katika sekta ya usafirishaji.
· Kuendelea kuboresha njia ya kisasa ya upashanaji habari na nyaraka mbalimbali za kitaalamu kupitia mtandao wa kompyuta (Website), na
· Kuboresha zaidi huduma ya maktaba na kukiimarisha zaidi kituo kwa kununua vifaa mbalimbali na kukarabati ofisi.
USALAMA BARABARANI NA UDHIBITI WA UZITO
107. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ongezeko kubwa la ajali za barabarani katika miaka ya karibuni ambako kumesababishwa na ongezeko la magari. Kwa mfano, katika mwaka 1999 zilitokea ajali za barabarani 15,370 ambapo watu 2,897 walifariki na wengine 10,786 kujeruhiwa. Hasara iliyotokana na ajali hizi inakadiriwa kufikia Shilingi 30 bilioni, mbali na simanzi, majonzi na kupotea kwa nguvu kazi nyingi kwa Taifa na familia kutokana na walioathirika na kufariki katika ajali hizo. Utafiti uliofanywa na Wizara yangu kwa kushirikiana na jeshi la polisi umebaini kuwa ajali nyingi za barabarani husababishwa na uendeshaji mbaya, uzembe wa madereva na watumiaji wengine, ubovu wa magari, barabara mbaya, elimu duni kwa baadhi ya watumiaji wa barabara na ukiukwaji wa sheria ya kudhibiti uzito na viwango vya vipimo vya magari yanayotumia barabara zetu.
108. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua athari za kijamii na kiuchumi zinazotokana na ajali za barabarani pamoja na uzidishaji uzito, wizara yangu imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zinazolenga kupunguza ajali pamoja na uharibifu wa barabara unaotokana na uzidishaji uzito. Baadhi ya hatua zinazochukuliwa ni kama ifuatavyo:-
· Kuanzisha mpango mpya wa kukusanya, kutunza na kuchambua kumbukumbu za ajali za barabarani ujulikanao kama Microcomputor Accident Analysis Package (MAAP5).
· Kuandaa mitaala ya kufundishia elimu ya usalama barabarani kuanzia shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo vya ualimu.
· Kuandaa mfumo mpya wa ukaguzi wa magari unaoendana na mapendekezo ya nchi za Jumuia ya SADC.
· Kuandaa mfumo mpya utakaoainisha viwango (Standards) vya shule za madereva, mitaala ya kufundishia madereva na taratibu za kutahini na kutoa leseni za udereva utakaotumika kwa nchi nzima.
· Kutoa elimu kwa umma inayohusu usalama barabarani na matumizi bora ya miundo mbinu
· Kuandaa mfumo wa ukaguzi na uhakiki wa vipengele vya usalama barabarani (Road Safety Audit System) utakaotumika kukagua barabara zote nchini. Sambamba na mkakati huo wizara pia itakamilisha maandalizi ya kanuni za matumizi ya barabara (Highway Code) na miongozo ya uendeshaji bora wa magari (Drivers' Training Manual).
109. Mheshimiwa Spika, lengo la muda mrefu ni kuanzisha mpango wa kuboresha hali ya usalama barabarani unaolenga kuongeza ufanisi katika kupunguza ajali za barabarani ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya sheria zilizopo.
110. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2000/01 Wizara yangu imetoa mafunzo kwa askari polisi wa usalama wa barabara 77 na wahandisi 14 kutoka taasisi mbalimbali juu ya uwekaji na uchambuzi wa takwimu za ajali kwa kutumia MAAP5. Aidha, Wizara yangu imechambua takwimu mbalimbali za ajali na kufanya usanifu wa hatua za kupunguza ajali kwenye sehemu mbaya (black spots). Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani imeifanyia marekebisho sheria inayohusika na uzito wa magari ili kuridhia makubaliano ya SADC na hivyo kuongeza viwango vya uzito unaokubalika katika barabara zetu kutoka tani 52 hadi 56. Ili kudhibiti uzito na kuondoa tatizo la rushwa, Wizara yangu kupitia kwa Wakala wa Barabara, imewashirikisha washika dau wote ili kuhakikisha kwamba mizigo inayoagizwa na kusafirishwa katika barabara zetu inakuwa katika viwango vinavyoruhusiwa na hivyo kupunguza mianya ya rushwa.
111. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kuwaelemisha Wananchi juu ya utumiaji salama wa barabara zetu kupitia vyombo mbali mbali vya habari pamoja na kushiriki kwenye wiki ya Nenda kwa Usalama. Aidha, majukumu mengine ambayo Wizara yangu inatarajia kuyatekeleza katika mwaka 2001/02 ni kama ifuatavyo:-
· Kufanya penguzi yakinifu mbalimbali kwa kutumia wahandisi washauri kwa madhumuni ya kuboresha hali ya usalama barabarani na kudhibiti uzito.
· Kushirikiana na washika dau mbalimbali katika ujenzi wa vizuizi vya ajali (counter measures) kwenye sehemu mbaya.
· Kuendelea kusimamia majaribio ya elimu ya usalama barabarani katika baadhi ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
· Kuendelea kutoa mafunzo kwa askari wa Usalama barabarani na Wahandisi mbali mbali juu ya uingizaji wa takwimu za ajali kwenye kompyuta na uchambuzi wa vyanzo vya ajali.
· Kukamilisha rasimu za kanuni za barabara, miongozo ya udereva na ukaguzi wa magari pamoja na mfumo wa ukaguzi wa magari.
· Kuandaa rasimu ya mfumo wa shule za udereva, upimaji na utoaji wa leseni kwa madereva.
112. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na wafadhili mbali mbali inakusudia kujenga mizani mitatu ya kisasa katika mikoa ya Morogoro, Mbeya na Shinyanga pamoja na kununua mizani mipya ya kuhamishika. Aidha, Wizara yangu itaandaa mfumo wa kisasa ujulikanao kama "Computerized Vehicle Overload Management System" kwa ajili ya usimamizi na uendeshaji wa shughuli za mizani pamoja na mfumo utakaowezesha mambo ya usalama barabarani kuzingatiwa katika kila hatua ya ujenzi wa barabara. Wizara yangu itaendelea kutoa mafunzo ndani na nje ya nchi kwa watumishi ili kuwaongezea ujuzi katika majukumu yao ya usalama barabarani na udhibiti uzito. Aidha, Wizara yangu itaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria watumishi wote watakaojihusisha na rushwa katika mizani.
IDARA YA UFUNDI NA UMEME
113. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2000/01 Idara ya Ufundi na Umeme iliendelea kutekeleza majukumu yake ya kuratibu, kuthamini, kusajili, kufuta, kukodisha na kufanya matengenezo ya magari na mitambo ya Serikali; uendeshaji wa vivuko na mitambo ya kusaga kokoto; kutoa ushauri wa kitaalam; usimamizi wa miradi; usimikaji (commissioning) na matengenezo ya mitambo ya umeme, mabarafu, viyoyozi na vifaa vya elektroniki.
114. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma zinazotolewa na Idara hii hapa nchini, Wizara yangu katika mwaka 2000/01 ilitekeleza kazi zifuatazo:-
· Ukarabati wa Kivuko cha M.V. Kome huko Mwanza na wa Pantoni ndogo yenye uwezo wa tani 15 katika Kivuko cha Kilombero. Aidha, vivuko vya M.V. Rufiji, M.V. Kigamboni, M.V. Alina na M.V. Sengerema vimefanyiwa matengenezo ya kawaida.
· Utengenezaji wa injini ya mtambo wa kokoto uliopo kijiji cha Uchira mkoani Kilimanjaro.
· Ukarabati wa Mtambo wa kokoto wa Lilondo–Madaba mkoani Ruvuma ulikamilika na mtambo ulianza kufanya kazi tangu Oktoba 2000.
· Kivuko kipya cha tani 45 kilichonunuliwa kutoka Ujerumani kwa msaada wa Shirika la Benedictine, Ndanda kimewasili na sasa kinaunganishwa kwenye eneo la Kilambo kwenye mto Ruvuma. Kivuko hicho kitarahisisha usafiri kati ya Mtwara na Msumbiji.
· Uboreshaji wa huduma inayotolewa na kitengo cha ukodishaji wa magari (GTA) na ukarabati wa magari pamoja na kuwapatia mafunzo madereva.
· Ukarabati wa mtambo wa uyeyushaji na umiminaji wa chuma (Foundry) katika Karakana ya Ufundi Dar es Salaam.
· Ukarabati wa umeme kwenye majengo mbalimbali ya Serikali na taasisi zake yakiwemo ya chuo cha ufundi Mbeya na jengo la Bunge, Dodoma.
· Uwekaji wa “Fire Detectors and Alarm System” kwenye ukumbi wa Bunge.
115. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2001/02 Idara inalenga kutekeleza kazi zifuatazo:-
· Kuzifanyia upembuzi yakinifu pantoni za M.V. Kigamboni (DSM), M.V. Sengerema (Mwanza), Kilombero (Morogoro), Pangani (Tanga) na Rufiji/Ndundu (Pwani) chini ya mpango wa ukarabati wa dharura wa barabara (Urgent Road Rehabilitation Project) na kwa kutumia mkopo wa fedha toka IDA.
· Kuendelea na jitihada za kuweka vifaa vipya na vya kisasa vya kufanyia kazi na kuimarisha huduma ya utengenezaji wa magari na mitambo katika karakana za Idara ya Ufundi na Umeme zilizopo Dar es Salaam pamoja na zile za mikoani na kuendelea kujitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kutafuta wateja zaidi wa huduma za idara hii.
116. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha utendaji kazi Serikalini, Wizara yangu inaendelea kukamilisha taratibu za kuifanya idara hii kuwa Wakala kwa lengo la kuiwezesha kutoa huduma bora.
IDARA YA NYUMBA NA MAJENGO YA SERIKALI
117. Mheshimiwa Spika, Idara ya Majengo ina majukumu ya kusimamia na kuendesha kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya majengo na nyumba za Serikali, kuchora michoro ya majengo ya Serikali, kusimamia na kushiriki katika utengenezaji wa samani za maofisi ya Serikali na kutoa ushauri kuhusu vifaa vya ujenzi vilivyo bora katika ujenzi na matengenezo ya nyumba za Serikali. Kama nilivyosema katika hotuba yangu mwaka 2000/01 Wizara yangu bado inaendelea kuboresha taratibu za kumiliki nyumba na majengo ya Serikali ili kukabili tatizo la uhaba uliopo.
118. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/02, Idara ya Majengo imepanga kuendelea na kazi ya kuondoa tatizo la muda mrefu la uvamizi wa viwanja na maeneo ya nyumba za Serikali, kwa kutambua upya mawe ya mipaka kwa viwanja vilivyopimwa na kuanza kupima vile ambavyo bado. Katika mwaka 2001/02, idara imepanga kupima viwanja 1,056 kati ya viwanja vya nyumba 6,000 za Serikali katika mikoa 20 ya Tanzania. Aidha, zoezi kama hilo linaendelea kwa mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Ruvuma ambako kazi ya kutayarisha ramani za viwanja vyote vyenye nyumba za Serikali imekamilika kwa asilimia sitini (60%). Kazi ya kuzithamini nyumba za Serikali imekamilika kwa mkoa wa Dares Salaam na itaanza katika mikoa mingine mara baada ya kukamilika kazi ya upimaji wa viwanja vyenye nyumba za Serikali, kwa kutegemea upatikanaji wa fedha. Katika kipindi cha mwaka 2001/02 Idara ya Majengo itakuwa Wakala na hivyo kujiendesha kibiashara.
IDARA YA UGAVI NA HUDUMA
119. Mheshimiwa Spika, Idara ya Ugavi na Huduma ina majukumu ya kusimamia sera ya ununuzi; utunzaji na usambazaji wa vifaa na upatikanaji wa huduma na kazi mbalimbali kwa ajili ya shughuli za Serikali (Procurement and Supply Management). Aidha, Idara ya Ugavi na Huduma inasimamia taratibu za ugomboaji na usafirishaji wa shehena za Serikali (Clearing and Forwarding). Idara pia inasimamia shughuli za uendeshaji wa Bohari Kuu za Serikali.
120. Mheshimiwa Spika, majukumu yaliyotajwa hapo juu yanalenga katika kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuhakikisha kunakuwepo mfumo thabiti wa utendaji wa kazi za ugavi unaolenga katika matumizi bora ya fedha za umma. Takwimu kutoka vyanzo mbalimbali zinaonyesha kwamba kati ya asilimia 60 hadi 70 ya matumizi ya Serikali hutumika katika ununuzi wa vifaa, kazi na huduma (goods, works and services). Serikali pia hutumia fedha nyingi katika kugomboa shehena zake kutoka nje ya nchi zinazoletwa kupitia bandari, viwanja vya ndege na mipakani.
121. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2001/02 Wizara yangu, itahakikisha kwamba muundo na sheria zinazosimamia shughuli za Idara ya Ugavi na Huduma zinaboreshwa ili kuleta ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa kazi hizi. Aidha, Wizara itaweka utaratibu wa kusimamia shughuli za ununuzi katika Wizara, Mikoa na Taasisi zote za Serikali ili kuhakikisha kwamba kila shilingi itakayotumika katika ununuzi italeta huduma bora. Hali iliyopo inaonyesha kuwa baadhi ya Wizara, Idara, Mikoa na Taasisi za Serikali, hazitumii ipasavyo huduma zinazotolewa na idara hii. Wizara yangu inaangalia pia uwezekano wa kutumia Idara ya Ugavi na Huduma katika kuhudumia miradi ya maendeleo ambayo inagharamiwa na Wafadhili ili kupunguza gharama.
122. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza uboreshaji wa utendaji kazi Serikalini katika kipindi cha 2001/02 Idara hii itafanyiwa marekebisho chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali. Wizara yangu inaamini kuwa Wizara na Idara za Serikali zitaendelea kutumia huduma za Bohari Kuu.
BARAZA LA TAIFA LA UJENZI
123. Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Ujenzi lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 20 ya mwaka 1979 kwa lengo la kuendeleza sekta ya ujenzi nchini ambayo ilikuwa nyuma sana. Baraza linatekeleza jukumu hili kwa kutoa ushauri kuhusu mipango, sera na mikakati ya kukuza sekta, ushauri wa kiufundi, mafunzo, takwimu, upashanaji habari wa shughuli za sekta na utoaji miongozo ya kiufundi ikiwa ni pamoja na kanuni za zabuni.
124. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2000/01 Baraza lilitoa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa makandarasi 63 wa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Singida, Tabora, Lindi na Mtwara. Aidha, mafunzo juu ya kanuni na mikataba ya ujenzi na usimamizi wa miradi yalitolewa kwa washiriki wapatao 506 wakiwemo Wakurugenzi wa Wilaya, Maafisa Mipango wa Wilaya, Waweka Hazina wa Wilaya, Wahandisi wa Wilaya na Madiwani kutoka mikoa ya Rukwa na Ruvuma, Wahandisi wa kilimo na Mafundi Mchundo wa TANROADS. Pia Baraza lilitoa mafunzo ya kiujumla kuhusiana na tathmini za zabuni (tender evaluation) na mambo ya kisheria yahusuyo zabuni na mikataba kwa washiriki wapatao 51.
125. Mheshimiwa Spika, Baraza limetengeneza majarida na miongozo ya kiufundi kama vile: Taratibu za mikataba za majengo (Agreement and Schedule of Conditions of Building Contract); Taratibu za mabadiliko ya bei (NCC Price Fluctuation Formula); Kitabu cha takwimu za ujenzi (Construction Basic Economic Statistical Data) na rasimu za taratibu za zabuni na mikakati kwa ajili ya mradi wa “Agricultural Sector Programme Support” wa Wizara ya Kilimo na Chakula.
126. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ushauri kuhusu sera na mikakati ya kuendeleza sekta, Baraza liliratibu upatikanaji wa maoni kuhusu matatizo ya kodi kwa washikadau na mswada wa shughuli za zabuni (public Procurement Bill) na kanuni zake. Pia lilitoa huduma za ushauri zipatazo 20 na usuluhishi wa migogoro (4) minne. Aidha kwa kushirikiana na Wizara yangu Baraza liliandaa warsha kuhusu mikakati ya kuziba mianya ya rushwa katika sekta ya ujenzi iliyofanyika katika Ukumbi wa Karimjee na kushirikisha washikadau wapatao 241.
127. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2001/02, na kama ilivyokuwa mwaka jana, Baraza linalenga kutoa msukumo katika uanzishwaji wa Mfuko wa Fedha (Construction Industry Trust Fund) na ukamilishaji wa Sera ya Taifa ya Ujenzi. Pia, kipaumbele kitatolewa kwa malengo na mikakati inayolenga kuondokana na matatizo makuu ya sekta ya ujenzi ambayo ni uwezo mdogo, tija ndogo na ubora hafifu wa kazi. Vile vile Baraza litaendelea na shughuli za mafunzo kwa makandarasi, washauri, watendaji wakuu wa serikali katika mambo ya ujenzi, kuboresha upatikanaji wa takwimu za shughuli za ujenzi, utayarishaji wa miongozo ya kiufundi, huduma ya ushauri, ukaguzi wa miradi na usuluhishi wa migogoro.
BODI YA TAIFA YA USIMAMIZI WA VIFAA
128. Mheshimiwa Spika, Bodi ya Taifa ya Usimamizi wa vifaa (National Board for Materials Management – NBMM) ni Taasisi ya Serikali yenye jukumu la kukuza na kuendeleza taaluma ya ugavi na utunzaji vifaa nchini iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na. 9 ya mwaka 1981. Bodi hii ina jukumu kubwa la kutoa mafunzo, ushauri wa kitaalamu, utoaji wa miongozo ya taaluma ya ugavi, utaratibu wa mafunzo na uendeshaji wa mitihani ya Taaluma ya Ugavi. Pia husimamia mienendo ya wanataaluma kwa njia ya usajili, ambapo mpaka Juni 2001 wataalamu wapatao 1,197 wamekwishasajiliwa na Bodi.
129. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa 2000/01 Bodi imetoa mwongozo wa miiko na tabia za maafisa ugavi (Ethical Code of Conduct) ambayo hutumiwa kuwaelimisha wataalamu hao juu ya maadili mema ya kazi. Pia Bodi imesajili wataalamu wapya wapatao 66 na kutahini watahiniwa wapatao 1,706 katika ngazi mbalimbali za taaluma. Aidha hadi kufikia Juni 2001 jumla ya wataalamu 9,011wamefuzu mitihani yao katika ngazi mbalimbali sawa na 42.5% ya watahiniwa wote. Mahitaji ya Taifa yanakadiriwa kuwa idadi ya wataalamu 15,046 katika ngazi mbali mbali.
130. Mheshimiwa Spika, Bodi hii imeweka majukumu yafuatayo kwa ajili ya utekelezaji katika kipindi cha mwaka wa 2001/02.
· Kuendelea kutoa mafunzo na elimu yenye ubora wa juu ambapo itahusisha matumizi ya kompyuta hivyo kutambulika kimataifa hasa wakati huu soko huria na utandawazi.
· Kufuatilia na kukamilisha taratibu muhimu za kufanya marekebisho kwenye baadhi ya vifungu vya sheria Na. 9 ya 1981.
· Kuendeleza kitengo kitakachoshughulikia ushauri na utafiti wa kitaaluma (Research and Consultancy Unit) ili kuendelea kuzishauri Wizara, mashirika ya umma na sekta binafsi juu ya umuhimu wa fani hii katika harakati za kuinua uchumi na kutokomeza rushwa hasa katika wakati huu wa soko huria na utandawazi.
· Kuwaendeleza wataalamu waliopo hadi kufikia ngazi ya juu ya Shahada ya Taaluma ya Ugavi (CSP - Certified Supplies Professional) na kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara kwa kwa njia ya semina na makongamano kwa lengo la kuboresha huduma hii kwa umma na kuziba mianya ya rushwa.
131. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2001/02 Bodi inatarajia kusajili wataalamu wapya 80 katika ngazi mbali mbali, kutahini watahiniwa 2,500 kwa ngazi mbali mbali pamoja na kutoa ushauri na mafunzo ya kujiendeleza (Continued Professional Development) kwa wanataaluma wa fani ya ugavi.
132. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Sheria Na. 9 ya mwaka 1981, waajiri wote nchini wanaohitaji huduma za ugavi wanatakiwa kuajiri wanataaluma wa ugavi waliosajiliwa na Bodi na kuruhusiwa kufanya shughuli za ugavi kwa mujibu wa sheria. Kuruhusu watu wasio wataalamu kufanya kazi holela ni kukiuka sheria na taratibu zinazopelekea Serikali kupata hasara kubwa kama anavyoelezea Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali katika ripoti yake kila mwaka. Bodi itachukua hatua za kisheria zinazostahili dhidi ya wahalifu watakaobainika kukiuka sheria ya ugavi
BODI YA USAJILI WA MAKANDARASI
133. Mheshimiwa Spika, Bodi ya Usajili wa Makandarasi (Contractors Registration Board) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 17 ya mwaka 1997. Aidha, Bodi inazo Sheria ndogo ndogo (By laws) za kudhibiti mwenendo wa Makandarasi. Madhumuni makubwa ya kuanzisha Bodi hii ni kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za Makandarasi katika soko huria. Katika kutekeleza azma hiyo Bodi imepewa majukumu yafuatayo:-
· Kusajili makandarasi wa aina zote,
· Kuratibu shughuli na mwenendo wa makandarasi wote, na
· Kujenga uwezo wa makandarasi wa Kitanzania.
134. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2000/01, Bodi ilisajili makandarasi 398 wa fani mbalimbali. Jumla ya makandarasi wote waliosajiliwa hadi Juni 2001 ni 2,210. Bodi ilifuta makandarasi 859 kwa kushindwa kutimiza masharti ya sheria ya usajili. Aidha, kampuni 14 zilipelekwa Mahakamani kwa kufanya kazi za ukandarasi bila kusajiliwa. Katika kipindi hiki Bodi ilikamilisha zoezi la kupitia upya makandarasi 243 waliosajiliwa na Bodi ya zamani kwa lengo la kuwapanga katika madaraja kulingana na sheria mpya. Katika kuwasaidia makandarasi wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika miradi inayogharamiwa na wafadhili wa nje, Bodi ilifanya mazungumzo na mashirika na Balozi mbalimbali za nje zinazofadhili miradi ya ujenzi hapa nchini ili kuwezesha makandarasi wetu wa Kitanzania kupata kazi.
135. Mheshimiwa Spika, Bodi itaendelea kusajili, kuratibu na kujenga uwezo wa makandarasi kwa kufuata sheria. Lengo ni kuwa na Makandarasi Watanzania wenye uwezo kimitambo, ujuzi na wanaozingatia usalama na kufanya kazi nzuri kwa muda uliopangwa. Kwa mwaka 2001/02, Bodi imeweka malengo yafuatayo:-
· Kusajili makandarasi wapya 347.
· Kutathmini upya kulingana na sheria mpya uwezo wa makandarasi 849 waliosajiliwa na Bodi ya zamani.
· Kutoa mafunzo kwa makandarasi 120.
· Kusaidia makandarasi wadogo kupata dhamana za mikataba (Bonds and Guarantees) kutoka katika mabenki.
· Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya ujenzi (construction sites) yapatayo 120.
· Kuchukua hatua kwa makandarasi wazembe/wakorofi ikiwa ni pamoja na kuwafuta.
· Kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Makandarasi Na. 17 ya 1997 ili kuipa Bodi nguvu ya kisheria ya kutekeleza vyema majukumu yake.
BODI YA USAJILI WA WAHANDISI
136. Mheshimiwa Spika, majukumu ya Bodi hii ni pamoja na kusajili, kuendeleza ubora na kudhibiti mwenendo wa kitaaluma wa wahandisi. Aidha, katika kipindi cha mwaka wa 2000/01 Bodi ya Usajili wa Wahandisi imetekeleza yafuatayo:-
· Bodi ilisajili wahandisi 290 na makampuni ya ushauri wa kihandisi 6, hivyo kufanya idadi ya wahandisi waliosajiliwa nchini kufikia 4,005 na makampuni ya ushauri ya Kitanzania 45 na makampuni 15 ya kigeni.
· Bodi ilitembelea mikoa ya Lindi, Mtwara, Iringa, Ruvuma na Mbeya na kukagua shughuli za kihandisi viwandani, kwenye miradi na mashirika ya umma.
· Kuanzia Julai 2000, Bodi ilianza kupambana na rushwa katika sekta ya uhandisi. Hii ni pamoja na kutoa maadili ya utendaji wa kazi za kihandisi na kufuatilia kwa karibu utendaji wa kazi za kihandisi. Bodi imeshiriki pia katika warsha ya kuzuia rushwa iliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi.
· Kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi, Vijana na Michezo na Idara ya Uhamiaji, Bodi iliendelea kuangalia na kudhibiti ajira ya wahandisi wa kigeni wanaoingia nchini.
137. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2001/02 Bodi inakusudia kufanya yafuatayo:-
· Kuhakikisha kuwa wahandisi ambao bado hawajasajiliwa wawe wamekwisha sajiliwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2002.
· Kuendelea kukagua kazi za kihandisi nchini ili kuondoa wahandisi bandia na kuhakikisha kuwa kazi za kihandisi zinafanywa na wahandisi waliosajiliwa kwa kufuata maadili ya kazi za kihandisi.
· Kwa kushirikiana na Wizara yangu, Bodi itaanzisha utaratibu wa mafunzo ya vitendo kwa wahandisi wanaomaliza masomo yao vyuoni.
· Kuwezesha kuanzishwa kwa kampuni za ushauri wa kihandisi mikoani.
· Kufanya sensa ya wahandisi waliomo nchini ili kujua idadi yao, mahali walipo na kazi wanazofanya. Hii itaiwezesha Bodi kufuatilia kwa karibu kazi zote za kihandisi nchini.
BODI YA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI
138. Mheshimiwa Spika, majukumu ya Bodi hii ni kusajili, kuratibu mwenendo wa kitaaluma na kuendeleza wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi kulingana na Sheria Na. 16 ya mwaka 1997. Bodi pia ina jukumu la kudhibiti ubunifu wa majengo na usanifu wake ili kupata mazingira bora ya ndani na nje ya majengo na kuendeleza ubora wa makazi ya watu na shughuli zao katika miji na vijiji.
139. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2000/01, Bodi ilifanya ukaguzi (site inspections) kwenye maeneo 462 ambapo ujenzi wa majengo ya huduma za jamii na biashara ulikuwa unaendelea na kubaini kuwa kwenye maeneo mengi Wabunifu Majengo (Architects) hawakushirikishwa. Hali hii inapelekea kukosekana kwa muwajibikaji endapo maafa yatokanayo na utaratibu usiozingatia Sheria Na. 16 ya mwaka 1997 yatatokea. Aidha, Bodi iliendesha mitihani mara mbili na kusajili wataalamu wapya 20 waliohitimu.
140. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2001/02 Bodi inakusudia kutekeleza yafuatayo:-
· Kuendelea kuimarisha ukaguzi katika maeneo ya ujenzi ili kuhakikisha kwamba shughuli zote katika sekta ya majengo zinawashirikisha wabunifu wa majengo na wakadiriaji majenzi wanaotambuliwa na sheria namba 16 ya mwaka 1997 na hivyo kupunguza hadi kuondoa kabisa utendaji wa watu wasiotambulika kisheria katika sekta hii.
· Kuendelea kuhamasisha watu katika maeneo yote ya jamii waone umuhimu wa kupata huduma zao kwa kutumia Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi.
· Kushirikiana na Serikali za Mitaa, Bodi nyingine pamoja na Taasisi mbalimbali katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoathiri utendaji bora wa wataalam na hivyo kuendelea kuwachukulia hatua wataalamu wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
MAENDELEO YA WATUMISHI
141. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2000/01 watumishi 454 wa kada mbalimbali wamepandishwa vyeo, na Wizara yangu itaendelea na zoezi hili kwa watumishi watakaostahili kutokana na miundo ya Utumishi ya kada zao.
142. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2000/01 watumishi 22 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu, kati ya hao 8 walihudhuria mafunzo nje ya nchi na 14 humu humu nchini. Pia watumishi 217 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi katika fani za Usimamizi wa Miradi ya Barabara na Madaraja, Mikataba ya Ufundi, Uhandisi, Huduma na Ugavi, Kompyuta, Jinsia, Usimamizi wa Fedha na Uongozi. Lengo la kuwapatia mafunzo watumishi ni kuwaongezea ujuzi na ufanisi katika kazi zao. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2000/01 watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo, Wahandisi, Makandarasi, Wabunifu Majengo, Wakadiriaji Majenzi, Wahandisi Washauri, Wahasibu na kadhalika walihudhuria semina juu ya kupiga vita rushwa katika sekta ya Ujenzi. Mwishoni mwa semina hiyo, wajumbe walitoa maazimio ya mikakati ya kupiga vita rushwa katika sekta ya ujenzi ambayo Wizara yangu inayafanyia kazi. Wizara itaendelea na juhudi za kuwapatia mafunzo zaidi wafanyakazi wake katika mwaka wa fedha 2001/02.
HITIMISHO
143. Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaeleza hapo awali, Wizara yangu inatekeleza malengo yake kwa kushirikiana na wananchi pamoja na misaada ya Serikali na mashirika mbali mbali ya kigeni. Napenda nitumie nafasi hii kuzishukuru Serikali za nchi za Denmark, Finland, Italia, Japan, Kuwait, Marekani, Norway, Saudi Arabia, Switzerland, Uholanzi, Uingereza na Ujerumani ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia sana sekta ya Ujenzi. Pia nayashukuru Mashirika ya Kimataifa ya ADB, EU, IDA na Mfuko wa Maendeleo wa OPEC kwa kuendelea kusaidia sekta ya ujenzi. Jitihada zao wote zimechangia katika mafanikio na maendeleo ya Wizara yangu. Tunawashukuru sana kwa msaada wao.
144. Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii pia kuishukuru Kamati ya Bunge ya Miundo Mbinu chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Prof. Daimon Mwaga, Mbunge wa Kibakwe, kwa ushauri mzuri waliotupa katika kuandaa bajeti hii. Nawashukuru viongozi wenzangu katika Wizara ya Ujenzi ambao ni Naibu Waziri, Mheshimiwa Hamza Abdallah Mwenegoha (Mb), Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Katibu Mkuu, Wakurugenzi, Bodi mbalimbali zilizo chini ya Wizara pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa juhudi zao katika kutekeleza majukumu yetu katika mwaka uliopita. Aidha, napenda nimshukuru sana Mhe. Anna Abdallah, (Mb) Mbunge wa Jimbo la Lulindi na Waziri wa Afya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi kabla yangu. Napenda kukiri mafanikio yanayoonekana sasa katika Wizara ni matokeo ya juhudi kubwa na kazi nzuri aliyoifanya wakati akiwa Waziri katika Wizara hii, ninamshukuru sana. Ninawashukuru pia Mawaziri wote kwa ushirikiano walionipa katika kutatua hoja mbalimbali za Wizara ya Ujenzi. Aidha, napenda niwashukuru Wabunge wote na Bodi za Barabara mikoani kwa ushauri na maelekezo yao yaliyosaidia kufanikisha haya machache yanayoonekana.
145. Mheshimiwa Spika, naona nitumie nafasi hii pia kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo langu la Biharamulo Mashariki. Nawashukuru sana kwa heshima waliyonipa ya kuwa mwakilishi wao Bungeni kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
146. Mheshimiwa Spika, mwisho ninakushukuru wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti na wasaidizi wako wote kwa jinsi mnavyoliendesha Bunge hili kwa uwezo na ufanisi mkubwa.
MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA
147. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza majukumu na malengo yake kwa mwaka 2001/02, Wizara yangu inatarajia kutumia jumla ya shilingi 167,508,471,600. Kati ya fedha hizo, shilingi 64,745,589,600 ni za hapa na shilingi 102,762,882,000 ni za nje. Fedha za nje zinajumuisha shilingi 75,245,000,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi 27,517,882,000 kwa ajili ya kazi za matengenezo ya barabara kuu na za mikoa. Aidha, fedha za hapa zinajumuisha:-
148. Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge lako Tukufu lijadili na hatimaye liidhinishe Makadirio haya ya Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2001/02.
149. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.