Tanzania imetangaza Dira ya Maendeleo ya 2025. Chimbuko la Dira ya 2025 ni kwamba, ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa imepitia katika marekebisho ya kiuchumi na maendeleo yasiyoepukika ili kufikia hadhi ya pato la kati; likiwa na viwanda vya kisasa zaidi, ushindani, maisha bora, utawala wa sheria na kuwa na jamii iliyoelimika na inayopenda kusoma. Kwa usahihi zaidi, Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025 imeeleza kwa muhtasari matarijio ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa robo ya kwanza ya karne ya 21; kwa lengo la msingi la kufikia hadhi ya nchi yenye uchumi wa kati (MIC), yenye wastani wa pato la kila mtu la Dola za Marekani 3,000 (kwa makadirio tu) ifikapo mwaka 2025.
Dira ya 2025 ilipangwa itekelezwe kupitia mfululizo wa mipango ya maendeleo ya miaka mitano mitano. Serikali imeanzisha sera za uchumi kwa jumla na programu za maendeleo kwa lengo la kuwawezesha watu na kukuza ukuaji wa uchumi nchini. Sera na mikakati mbalimbali ilitungwa kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi Watanzania ili wamiliki, waendeshe na wanufaike na uchumi wao kufikia dira ya 2025.
Katika sehemu hii utapata taarifa kuhusu mipango ya maendeleo ya sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, elimu, afya, uvuvi, maji, usafirishaji, sheria,ardhi, utalii, nishati na madini. |