HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHE. AMANI ABEID KARUME

KATIKA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MIAKA  38 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR TAREHE 12 JANUARI, 2002

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Benjamin William Mkapa,

 

Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr. Ali Mohammed Shein,

 

Makamo Mwenyekiti wa CCM Tanzania Visiwani na

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dr. Salmin Amour,

 

Makamo Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara

Mheshimiwa  John Samuel Malecela,

 

Waziri Mkuu, Mheshimiwa  Fredric Sumaye,

 

Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Mheshimiwa  Shamsi Vuai Nahodha,

 

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mzee Ali Hassan Mwinyi,

 

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,

 

Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Philip Mangula,

 

Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa,

Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi za Nje,

 

Ndugu Wananchi,

 

Mabibi na Mabwana

1.0     UTANGULIZI:

 

1.1       Kwanza naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu  kwa kutuwezesha kukutana hapa leo hii tukiwa wazima na wenye afya ili kwa pamoja tuadhimishe miaka 38 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika tarehe 12 Januari 1964.

 

1.2       Nachukua fursa hii pia kuwashukuru wananchi kwa jumla kwa kuienzi siku hii kwa kujitokeza kwa wingi ili tujumuike pamoja kwenye kilele cha maadhimisho haya.  Aidha nawapa shukurani nyingi wananchi wote wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuonesha busara na uvumilivu mkubwa kutokana na hali ngumu za maisha wakati wa kipindi kigumu cha uchumi duni.  Serikali yenu ya Awamu ya Sita imeanza kuchukua hatua za dhati za kuleta marekebisho kadhaa yenye lengo la kujenga misingi ya maendeleo kwa watu wote.  Shukurani pia ziwafikie wananchi wote kwa jumla kwa kudumisha utulivu, upendo, amani na usalama nchini mwetu.

 

1.3       Shukurani maalum kwa niaba yenu wananchi nazielekeza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kwanza kwa kujumuika nasi katika kilele cha maadhimisho haya siku hii ya leo.  Kuhudhuria kwako katika sherehe hii ni faraja kubwa kwetu.  Tunakushukuru Mhe. Rais kutokana na wewe mwenyewe binafsi kuwa karibu sana na watu pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nyakati zote ziwe za furaha au ziwe za shida.  Kwa nafasi zako mbali mbali ukiwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano, umeyafuatilia matukio na maendeleo ya Zanzibar kwa karibu sana kwa lengo la kuyafanya maisha ya Wazanzibari yawe tulivu na bora zaidi.

 

1.4       Tunakushukuru na kukupa pongezi Mheshimiwa Rais kwa ujasiri na uongozi wako wa busara, maamuzi na upeo mkubwa ambao umeiletea nchi yetu ya Tanzania sifa na heshima kubwa duniani.  Uongozi wako usioyumba umeweza kukuza umoja na upendo baina ya wananchi, amani na kupanuka kwa demokrasia ya kweli hapa nchini.

 

2.0     MAANA YA MAADHIMISHO YA LEO:

 

2.1       Ndugu Wananchi, tumejumuika kwa wingi leo kwa lengo la kuyakumbuka na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964, Mapinduzi yaliyojenga msingi wa ukombozi wa wanyonge wa nchi hii na ukombozi wa Wazanzibari wote kwa jumla.  Tunaikumbuka siku ya leo kwa sababu ni siku ambayo tofauti baina ya Wazanzibari, tofauti za rangi, asili, uzawa, kabila, imani na mali ziliondolewa na ni wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa tofauti hizo hazitorejea tena.

 

2.2       Aidha tunaitukuza siku ya leo kwa kuwakumbuka mashujaa wote walioshiriki kwa namna moja au nyengine katika Mapinduzi hayo, kuwaombea kwa Mola wale waliotangulia mbele ya haki na kuwatakia maisha mema wale ambao bado wako hai.  Ni siku ambayo tunawaenzi wale wote ambao kwa vipindi mbali mbali katika muda wa miaka 38 iliyopita wametoa nguvu zao katika kuyalinda, kuyaenzi na kuzitekeleza ahadi za Mapinduzi kwa maslahi ya wananchi wote.

 

2.3     Tunaiadhimisha siku hii ya leo kwa kuzikumbuka, kuzitafsiri na kuazimia kuendelea kuzilinda na kuzitekeleza ahadi zilizowekwa na waasisi wa Mapinduzi zenye lengo la kuinua hali za wananchi wote wa Zanzibar kuwa bora zaidi.  Aidha hatuna budi tuitumie siku ya leo kupima utekelezaji wetu wa ahadi hizo za Mapinduzi.

 

2.4       Wakati wa maadhimisho haya, na ikiwa ni matokeo ya Mapinduzi, tuna wajibu pia wa kuuzungumzia Muungano kati ya iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar - Muungano uliozaa Tanzania.  Tunauzungumza Muungano kwa madhumuni ya kuulinda na kuuenzi huku tukielewa kuwa bila ya Mapinduzi tusingelikuwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

2.5       Kadhalika, tunaiadhimisha siku hii ya leo, ili tuweze kutafakari yale tuliyofanikiwa kuyatekeleza, tufanye uchambuzi wa yale yaliyotutatiza na sababu zake na hatimae tupange mkakati wa kipi kifanyike ili tuweze kwa ufanisi zaidi kuziendeleza azma za Mapinduzi za kuinua hali za wanyonge na kulijengea heshima Taifa letu.

 

3.0 MAFANIKIO TULIYOYAPATA TANGU MAADHIMISHO YA MIAKA 37 YA MAPINDUZI

 

3.1       Ndugu Wananchi, leo ni mwaka mmoja tangu tuadhimishe miaka 37 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, na ni mwaka mmoja na kidogo tangu muiweke madarakani Serikali ya Awamu ya Sita ambayo mimi naiongoza.  Katika kipindi cha mwaka mmoja huo tumeweza kupunguza ukubwa wa Serikali Kuu na kuunda Serikali ndogo ya Wizara 12 tu.  Tumeunda Serikali ndogo ili kupunguza gharama za uendeshaji lakini bila ya kuathiri huduma za Serikali hiyo kwa wananchi.  Sambamba na marekebisho hayo ya muundo wa Serikali, baadhi ya mashirika na taasisi nyengine zilifanyiwa marekebisho kwa lengo la kuimarisha utendaji wake.

 

3.2       Pamoja na kufanya marekebisho kwenye muundo wa Serikali na vyombo vyake, tumejitahidi na tunaendelea kujenga nidhamu na uwajibikaji katika utendaji wa vyombo hivyo.  Katika kulitekeleza hilo, Serikali yenu imeidhinisha Sheria inayoongoza mambo ya fedha kwa lengo la kujenga udhibiti wa mapato na matumizi ya Serikali na vyombo vyake.  Pia Serikali yenu imeandaa Sheria ya Zabuni itakayosimamia taratibu zote za uagiziaji na ununuzi wa mahitaji ya Serikali.  Hatua hii ina lengo la kuondoa ubadhirifu wa rasilimali za Serikali na kuepukana na ununuzi wa mali holela na kwa bei zisizo za ushindani.  Aidha Serikali imesisitiza ununuzi wa mahitaji yake kutoka kwa wale wafanyabiashara wanaolipa kodi kihalali Serikalini watakaokuwa na namba maalum zinazowatambulisha.

 

3.3       Ndugu Wananchi, katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, Serikali yenu imeongeza juhudi za kuzishughulikia kero zinazowakabili wananchi walio wengi.  Kwa kipindi kirefu, wastaafu Serikalini na Mashirika ya Serikali, wamekuwa wakilalamika kwa sababu hawakulipwa haki zao.  Kwa taarifa yenu, hivi sasa Serikali imelishughulikia suala hili, na wastaafu wameanza kupata haki zao kwa utaratibu unaofahamika.  Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Serikali imeweza kuwalipa wastaafu 876 viinua mgongo vya jumla ya Shilingi 770 milioni.  Aidha Serikali imelipa pencheni za wafanyakazi zenye jumla ya Shilingi 784 milioni.

 

3.4       Suala la michango ya Serikali katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii pia lilikuwa ni tatizo kwa muda mrefu.  Baada ya kulifanyia uchunguzi, na kurekebisha kasoro zilizokuwepo, michango hiyo ya Serikali kwa niaba ya wafanyakazi sasa inalipwa kama kawaida, na mfanyakazi hana haja ya kuwa na hofu juu ya haki zake pale anapostaafu.  Katika kipindi cha mwaka mmoja  uliopita hadi kufikia mwezi wa Septemba, Serikali ilikwisha kulipa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii jumla ya Shilingi 258 milioni.

 

3.5       Ili kujenga msingi wa maendeleo endelevu, Serikali yenu imeandaa mpango utakaoongoza juhudi zake, na za wananchi katika kukabiliana na tatizo sugu la umasikini.  Kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Serikali yenu imetengeneza sera na mikakati ya utekelezaji kwa kila sekta ili kuongoza juhudi zetu katika kupambana na umasikini na kuzifanya hali za wananchi kuwa bora zaidi.  Mpango huu ambao ni tafsiri ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa Dira ya Zanzibar ya 2020 utakuwa ukitekelezwa katika vipindi vya miaka mitatu mitatu ambapo kila baada ya mwaka mmoja tathmini ya utekelezaji itafanyika na kufanya marekebisho yanayostahili kufanyika ili kuimarisha utekelezaji wa mwaka ujao.

 

3.6       Ndugu Wananchi, hatua nyengine ambayo Serikali yenu imeipa umuhimu mkubwa katika mwaka huu uliopita, ni ujenzi wa mazingira yatayopelekea kuondokana na migogoro ya kisiasa ndani ya jamii yetu na kujenga misingi mizuri zaidi ya demokrasia.  Kwa zaidi ya miaka sita sasa, nchi yetu imekuwa katika malumbano ya kisiasa baina ya vyama na wafuasi wa vyama vikuu vya kisiasa hapa nchini.  Malumbano na mivutano hiyo ilipelekea kuhatarika kwa amani na utulivu wa nchi na wananchi wake.  Aidha mivutano hiyo imezorotesha juhudi za maendeleo ya nchi yetu.  Jina la Zanzibar na Tanzania likaanza kuchafuka nchi za nje.

 

3.7       Ili kurekebisha hilo Serikali yenu ilitoa msamaha kwa wale wote waliokuwa na tuhuma za makosa yenye mwelekeo wa kisiasa.  Aidha Serikali yenu kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilitoa kila aina ya msaada kwa vyama vya CCM na CUF ili viweze kufanya mazungumzo yatakayotupeleka katika hatua mpya ya kujenga maelewano, kuaminiana na kudumisha amani na utulivu nchini.

 

3.8       Matokeo ya juhudi hizo ni kutiwa saini kwa muafaka tarehe 10 Oktoba 2001.  Kasoro za kiufundi zilizojitokeza katika utekelezaji wa muafaka huo, nazo zimeshughulikiwa kwa pamoja na hivi sasa utekelezaji unaendelea.

3.9       Ndugu  Wananchi,  juhudi  zote  hizi  za  jumla, zimeanza kujenga miongoni mwetu mioyo ya kuaminiana na hivyo kukuza ushirikiano na amani ndani ya nchi.  Kwa mataifa ya kigeni, nayo pia yameanza kurejesha imani juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Mazungumzo ya ushirikiano kati ya Serikali yenu na nchi za nje na mashirika ya kimataifa yanafanyika kila mara,  kama mnavyoona na kusikia kutoka vyombo vya habari.  Matumaini yetu ni kuukuza ushirikiano huo kwa faida ya pande zote.

 

4.0     HATUA MAALUM ZA UTEKELEZAJI -              KISEKTA:

 

4.1    Ndugu Wananchi, pamoja na mafanikio hayo ya jumla tuliyoyapata katika kipindi cha mwaka mmoja tangu maadhimisho ya miaka 37 ya Mapinduzi, yapo mambo mahsusi yaliyotekelezwa na Serikali yenu kwenye maeneo mbali mbali.  Nitatumia fursa hii kuelezea kwa ufupi baadhi ya hatua hizo ikiwa ni kipimo cha utekelezaji wa ahadi za Mapinduzi.

 

4.2      Usafiri na Usafirishaji:

 

4.2.1  Kwa lengo la kuimarisha huduma ya mawasilino na hivyo kuchochea maendeleo, Serikali yenu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imeweza kukamilisha ujenzi wa barabara zifuatazo Unguja na Pemba:

 

- Barabara ya Makunduchi - Mtende

- Barabara ya Kibuteni - Kizimkazi

- Barabara ya Kitogani - Paje

-        Barabara ya Kaebona - Kaepwani

-     Barabara ya Chake - Vitongoji

-  Barabara ya Chake - Wesha inaendelea kutengenezwa. 

-    Ujenzi wa Barabara ya Bambi nao umeanza na unaendelea.

 

4.2.2    Ndugu  Wananchi,  katika  kipindi  cha mwaka huu baada ya kumalizika ujenzi wa barabara nilizozitaja, kazi za ujenzi wa barabara zifuatazo zitaanza mara moja tukiwa na lengo la kuzimaliza kabla ya Januari 2003.

 

-     Barabara ya Mahonda - Donge - Mkokotoni

-     Barabara ya Mtuhaliwa - Chokocho

-     Barabara ya Kidimni - Kitope

-     Barabara ya Kilindini - Micheweni

 

4.2.3     Kwa upande wa sekta ya usafiri wa anga, mwaka huu wa 2002, Serikali ikishirikiana na Benki ya Dunia itaifanyia matengenezo barabara ya kurukia ndege Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Zanzibar.  Aidha katika sekta ya mawasiliano ya simu mpango wa kusambaza mtandao wa simu za mkono sehemu zote za Unguja na Pemba utakamilishwa.  Hali hiyo itawafanya wananchi wa visiwa hivi popote walipo waweze kuwasiliana na sehemu yoyote ile duniani.

 

4.2.4   Aidha  katika  kipindi  hicho,  Serikali  iliipeleka meli ya M.V. Mapinduzi ili ifanyiwe matengenezo makubwa.  Kazi hiyo iliyogharimu fedha nyingi imekamilika na meli hiyo imerejea na kuanza kufanya kazi.

 

4.3     Kilimo:

 

4.3.1   Kwa kutambua kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, Serikali katika mwaka uliopita ilipania kuimarisha upatikanaji wa uhakika wa zana za kisasa za ukulima.  Kwa madhumuni hayo, Serikali iliyafanyia matengenezo makubwa matrekta 16 ili yaweze kutoa huduma kwa wakulima Unguja na Pemba.  Aidha ili kuifanya huduma hii itosheleze, Serikali imeagizia matrekta mengine mapya 6 ambayo karibu yatawasili.

 

4.3.2    Kwa upande wa sekta ya uvuvi Serikali iliendelea na juhudi za kuwapatia wavuvi nyenzo muhimu kwa kazi zao kwa njia ya mikopo.  Napenda kuwakumbusha wananchi wote waliobahatika na mpango huo wazitumie vizuri nyenzo zao kwa uzalishaji bora.  Kwa wale waliokosa vifaa hivyo wakati huu wavute subira kwani Serikali tayari imeshaagiza vifaa ambavyo vinategemewa kuwasili wakati wowote mwezi huu.

 

4.3.3    Serikali pia iliendelea kuihudumia sekta ya ufugaji kwa kuwapatia wafugaji mafunzo ya utunzaji wa tembe wa kisasa.  Wafugaji 75 walipatiwa mafunzo hayo, na kati yao 23 wameshapatiwa mifugo hiyo kwa utaratibu wa kupewa na kurejesha ndama ili wafugaji wengine waweze kufaidika nao.

 

4.4     Elimu:

 

4.4.1  Kwa  upande  wa  sekta  ya  elimu,  Serikali imeendelea na juhudi za kuimarisha huduma za sekta hiyo.  Jumla ya madarasa 95 yalijengwa katika kipindi cha mwaka uliopita.  Aidha madawati 4,050 yalisambazwa maskulini.  Lengo ni kulimaliza tatizo la madawati hivi karibuni.

 

4.4.2    Kuhusu uandikishaji wa watoto wapya, jumla ya watoto 28,000 waliandikishwa ikiwa ni jumla ya watoto wote waliofikia umri wa kwenda skuli, na tutawaandikisha wale wote waliofikia umri wa kwenda skuli kwa mwaka huu.

 

4.5      Afya:

 

Utoaji wa huduma za afya na utibabu uliendelea kuimarishwa kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu.  Kwa wale wagonjwa waliohitaji uchunguzi zaidi au huduma za mabingwa, ama walipelekwa Tanzania Bara au baadhi yao walipelekwa nje ya nchi.  Watoto wenye matatizo ya ugonjwa wa moyo wamekuwa wakipelekwa Israel na India kwa matibabu zaidi.

 

Pamoja na juhudi hizo, bado hospitali zetu zina upungufu mkubwa wa madawa muhimu.  Kutokana na hali hiyo maandalizi ya kutafuta uwezo mzuri wa kuagiza madawa yanafanywa.  Lengo kubwa la Serikali ni kuirekebisha hali hiyo katika kipindi hiki ili wagonjwa wote waweze kupata huduma kamili ya matibabu na dawa.

 

Kwa upande wa majengo, Serikali imeweza kuyafanyia matengenezo majengo ya hospitali ya Mnazi mmoja pamoja na ujenzi wa ukuta wa hospitali ya wagonjwa wa akili.  Aidha nyumba ya kulelea watoto Forodhani, nyumba za matunzo ya wazee Dole, Mkwajuni na Kivunge zilifanyiwa matengenezo muhimu.

4.6 Maji:

 

4.6.1   Kwa lengo la kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji Serikali katika mwaka uliopita ilichukua hatua kadhaa za kuimarisha upatikanaji wa maji na usambazaji wake.

 

4.6.2  Maeneo ya Chwaka, Charawe, Bwejuu, Paje, Jambiani, Makunduchi, Bumbwisudi na Unguja Ukuu kwa upande wa Unguja sasa yanapata maji safi na salama.  Kwa upande wa Pemba, vijiji vya Vitongoji, Jamvini, Masipa, Kangani, Kionjo, Chunga na Konde vimewekewa mashine mpya za kusukumia maji.  Aidha Serikali imefunga jenereta mpya za kusukumia maji kwa ajili ya kijiji cha Weni - Wilaya ya Wete.  Kwa wastani hivi sasa karibu asilimia 60 ya watu wote wanapata maji safi na salama.  Hivi sasa Serikali inaelekeza juhudi zake katika kulimaliza tatizo la maji kwenye miji ya Unguja na miji ya Pemba.  Kiini cha matatizo hayo kwa kiasi kikubwa, ni uchakavu wa mtandao wa usambazaji maji, ujenzi holela, na kasi kubwa ya ongezeko la watu mijini Zanzibar.  Kutokana na gharama kubwa ya mradi huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeiomba Serikali ya Japan kusaidia lakini wakati huo huo juhudi zetu za ndani za kurekebisha hali hiyo zinaendelea.  Kwa hivyo nawaomba wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wawe na subira.

 

5.0     MATATIZO YALIYOTUKABILI:

 

Ndugu Wananchi, licha ya mafanikio mengi ya kupigiwa mfano ambayo nimeyaelezea, mafanikio hayo yamepatikana katika mazingira magumu ya kiuchumi.

 

5.1     Ufinyu wa Bajeti:

 

5.1.1  Moja ya matatizo hayo ni ufinyu wa bajeti ya Serikali kwa maana ya ukusanyaji mdogo wa mapato kulingana na mahitaji makubwa ya matumizi, hali inayoipunguzia Serikali uwezo wa utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.  Hali hii inasababishwa na vianzio duni vya mapato na matumizi yaliyopanuka kuliko uwezo uliopo.

 

5.1.2   Mapato ya Serikali kwa jumla kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja yalifikia wastani wa asilimia 59.3 tu ya lengo lililowekwa.  Kutokana na kuanguka kwa biashara, mapato yatokanayo na uagiziaji bidhaa toka nje yalifikia asilimia 55 tu.  Makusanyo ya kodi ya VAT yalifikia asilimia 50 tu ya lengo, ambapo makusanyo ya kodi za ndani kupitia Bodi ya Mapato yalifikia asilimia 67 tu ya lengo.

 

5.2     Gharama za Uendeshaji Serikali:

 

5.2.1 Tatizo jengine linaloikabili Serikali yenu, ni gharama za uendeshaji wake.  Licha ya kupunguza idadi ya Wizara, bado muundo wa utendaji Serikali ni mkubwa.  Serikali ina wafanyakazi wachache wenye uwezo wa kazi za kitaalam, na idadi kubwa ni ya watendaji wenye ujuzi wa kati na kati na wahudumu.  Ufanisi wa utendaji Serikalini bado ni mdogo.

 

5.2.2    Pamoja na tatizo la ukubwa wa Serikali, mapato ya wafanyakazi ni madogo na hayakidhi mahitaji yao.  Matokeo ni muda mwingi hutumika kujitafutia maslahi mengine kwa njia ambazo aghlab zinaambatana na udokozi na ubadhirifu.

 

5.2.3 Haya  ni  mambo  ambayo  yanahitaji kushughulikiwa kwa haraka.

 

5.3      Maendeleo ya Vijana:

 

5.3.1  Ndugu  Wananchi,  maendeleo  ya nchi yetu yanategemea sana nguvu za vijana.  Ili vijana waweze kutekeleza majukumu yao wanapaswa wajenge utamaduni wa kujituma na kupenda kufanya kazi.  Ingawa safari yetu ya kufikia maendeleo ni ndefu, lakini tunaweza kufanikiwa iwapo vijana watafanya kazi kwa bidii na maarifa huku wakipiga vita uzembe, uvivu na ubadhirifu.  Tunahitaji vijana wenye uwezo mkubwa wa kitaalam na maarifa.  Kama tulivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi, Serikali ya Awamu ya Sita, itaendelea na juhudi zake za kuongeza vyuo vya mafunzo ya amali, kwa lengo la kuwapatia vijana taaluma ya ufundi na hatimae kuweza kujiajiri wenyewe kwa wale watakaokosa ajira Serikalini.  Katika kutekeleza azma hii Wizara ya Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake na Watoto pamoja na Wizara ya Elimu, Utamaduni na Michezo na Wizara ya Fedha na uchumi zimesaini mkataba na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kuhusu uanzishaji wa vituo viwili vya Amali, Mkokotoni, Unguja na Vitongoji, Pemba.

 

5.3.2      Aidha Wizara hiyo inafanya utafiti kuhusu uwezo na mahitaji ya vifaa katika vituo mbali mbali vya Amali ikiwemo, Dole, Skuli ya Sekondari ya Mikunguni, Chuo cha Karume, Chuo cha Utalii, Dodeani na Chuo cha JKU, Mtoni.  Matokeo ya utafiti huu yataisaidia Wizara kujua mahitaji ya kila chuo ili itakapotoa msaada katika vyuo vya Amali ukidhi mahitaji yao halisi.  Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi, itaongeza nafasi za masomo ya juu mara baada ya kuzinduliwa rasmi Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar "State University of Zanzibar" (SUZA) hivi karibuni  kwa madhumuni ya kuongeza idadi ya wataalamu.

 

5.3.3  Kwa  upande  mwengine,  katika  juhudi  za kujiandaa na utekelezaji wa Mpango wa Dira ya Maendeleo ya 2020, Serikali yenu imewasiliana na vyombo vya fedha vya Kimataifa IMF na World Bank na kuwaomba utaalam na hata fedha ikiwezekana, utakaowasaidia wawekezaji kuanzisha ujenzi wa viwanda mbali mbali ndani ya Maeneo Huru vitakavyozalisha aina nyingi ya bidhaa zitakazosafirishwa nje ya nchi kwa kutegemea masoko ya Marekani,  Jumuiya ya Ulaya (EU),  Jumuiya ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Tukifanikiwa na utekelezaji wa  mpango huo, tatizo la ajira kwa vijana na wengine litamalizika kabisa na kugeuka historia.

 

5.3.4    Ndugu Wananchi, Serikali itaendelea na juhudi zake za kuimarisha mfumo wa uajiri Serikalini pamoja na kurekebisha mfumo wa mishahara ili uwe kivutio kwa vijana wenye taaluma nzuri katika fani zao.  Ili kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi wa Serikali analipwa malipo stahiki, Serikali itaendelea na zoezi la kutathmini na kuchunguza idadi halisi ya watumishi na taarifa zao kuwekwa vizuri katika kompyuta.  Zoezi hili litakapofanikiwa litaisaidia Serikali kupunguza matumizi ya mishahara na hatimaye fedha hizi zitumike katika miradi ya maendeleo.

 

5.4      Magendo ya Karafuu:

 

5.4.1   Ndugu Wananchi, tatizo jengine kubwa ambalo limeikumba nchi yetu katika miaka ya hivi karibuni ni magendo ya karafuu.  Kama tunavyofahamu karafuu ni zao ambalo nchi yetu inalitegemea sana kwa mapato yake ya fedha za kigeni.  Licha ya kwamba uzalishaji wake Zanzibar umepungua na wazalishaji duniani wameongezeka bado mauzo ya karafuu yanaipatia nchi yetu sehemu kubwa ya mapato yake ya fedha za kigeni zinazoisaidia nchi kununulia dawa za hospitali, vifaa vya maskuli, lami ya kujengea barabara, kusafirisha wagonjwa, ununuzi wa zana za kusukumia maji, kilimo na kadhalika.

 

5.4.2    Wimbi lililojitokeza hivi sasa la kusafirisha nchi jirani karafuu kwa magendo, linawadhulumu Wazanzibari walio wengi huduma hizo.  Serikali kwa msimu uliopita imejitahidi sana kuudhibiti usafirishaji huo wa magendo na jitihada hizi zitaendelea kwa nguvu zaidi.  Nachukua fursa hii kuvishukuru vyombo vyote vya ulinzi vilivyohusika katika zoezi hili la kupambana na magendo ya karafuu pamoja na wananchi wema waliosaidiana navyo.  Aidha nawapa shukurani za dhati wale wananchi wote waliofuata taratibu zilizowekwa katika uuzaji wa karafuu.  Serikali kama ilivyo kawaida yake, itajitahidi kila inapowezekana kuzirekebisha bei za ununuzi wa karafuu toka kwa wakulima pamoja na kuongeza huduma kwa wakulima hao.

5.5      Masuala ya Muungano:

 

5.5.1  Ndugu Wananchi, mwezi Aprili mwaka huu Muungano wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar utatimiza miaka 38 tangu uasisiwe.  Katika miaka 38 hiyo mafanikio mengi yamepatikana, kubwa ikiwa ni kudumu kwa Muungano wenyewe.

 

5.5.2  Muungano kama chombo chengine chochote kinachokutanisha watu na kuwaweka pamoja hakikosi misukosuko.  Katika maisha ya Muungano huu, imejitokeza misukosuko ya hapa na pale katika nyanja mbali mbali zikiwemo:-

 

-          Uwezo  wa  Zanzibar kufanya  mashauriano  na nchi za nje;

-          Uwezo wa Zanzibar kukopa nchi za nje;

-         Uwakilishi wa Zanzibar kama sehemu ya Tanzania kwenye vyombo vya nje na Jumuiya mbali mbali za kiuchumi;

-          Ugharimiaji wa kazi za Muungano

-          Sehemu ya Zanzibar katika misaada inayoingia Tanzania;

-       Gawio la mapato kutoka vyombo vya Muungano na kadhalika;

-     Uendeshaji wa biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara.

 

5.5.3      Haya na mengineyo ni baadhi ya masuala ambayo yamekuwa yakizungumzwa mara kwa mara kama kero za Muungano.  Hata hivyo kwa kupitia vikao vya mashauriano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ufumbuzi wa matatizo hayo hatua kwa hatua umekuwa ukipatikana.

 

5.5.4      Aidha,  Serikali zenu mbili zimeshaweka mikakati ya kuzishughulikia kero hizo kwa matayarisho ya kuunda Tume ya Pamoja ya Fedha itakayoshughulikia mambo yote yanayohusu mapato na matumizi ya mambo ya Muungano.  Kadhalika Kamati ya Wataalamu wa Fedha kutoka Serikali zote mbili imeshaundwa na hivi sasa itashughulikia matokeo ya siku hadi siku.

 

6.0       HATUA ZA USONI:

 

6.1        Ndugu Wananchi, nimejaribu kuyabainisha baadhi ya matatizo ambayo Serikali yenu imekabiliana nayo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.  Kuyataja matatizo si udhaifu, bali ni kujenga tabia ya ukweli na uwazi katika utendaji wa kazi zetu.  Kuyajua matatizo ndio mwanzo wa kupanga mikakati ya kutafuta ufumbuzi wake.

 

6.2    Serikali yenu katika mwaka ujao na siku za usoni imepanga kutekeleza mambo kadhaa ili kukabiliana na matatizo niliyoyataja, kupunguza kero zinazowakabili wananchi na kuendelea na kutekeleza ahadi za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya kuinua hali za maisha za watu wetu.

 

6.3       Katika  mwaka  ujao,  Serikali  yenu itaziendeleza kwa nguvu zaidi juhudi za uimarishaji wa mapato yake.  Serikali itaangalia vianzio vipya vya upatikanaji wa mapato, kuziba myanya ya uvujaji kwa sehemu mbali mbali na papo hapo kuimarisha udhibiti wa matumizi yake.  Katika kufanya hivyo Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaiimarisha  Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Zanzibar (TRA)  kiujuzi na vifaa ili ifanye kazi zake kwa ufanisi zaidi.  Aidha kwa mapato ya ndani, Serikali itauimarisha utendaji wa Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) ili iongeze uwezo wake wa ukusanyaji wa mapato na kupiga vita ukwepaji wa kodi.

 

6.4       Kuhusiana na ajira ya vijana Serikali ingependa kuwatanabahisha wananchi wake kwamba huko twendako, ajira itatokana na kuongezeka kwa harakati za sekta binafsi na Jumuiya za wananchi wenyewe.

 

6.4.1  Serikali kwa upande wake itaendelea na uhamasishaji wa wawekezaji kutoka nje kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.  Vitega uchumi vikiongezeka, ndivyo ajira itakavyoongezeka.  Ili kuwatayarisha vijana kwa ajira hizo, Serikali itapanua zaidi fursa zilizopo za mafunzo ya amali, ufundi na elimu mbadala.

 

6.4.2     Kwa upande wa wananchi, Jumuiya ya wananchi, Jumuiya zisizo za Kiserikali zitaendelea kuhamasishwa ili zipanue shughuli zao na hivyo kukuza uwezo wa ajira.

 

6.5    Muundo wa Utumishi Serikalini hivi sasa hauridhishi, gharama za  uendeshaji ni kubwa.  Serikali inaandaa hatua ya kuurekebisha muundo huo ili kuongeza ufanisi.  Serikali ina lengo la kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi wa kazi zao.  Kwa hiyo mafunzo kazini na nje ya kazi yatasisitizwa.  Nidhamu na uwajibikaji vitapewa umuhimu mkubwa.

6.6      Ili kukabiliana na tatizo la huduma za jamii kwa jumla, na kwa lengo la kuharakisha maendeleo, Serikali itaendelea na mipango yake ya kusaidia nguvu za wananchi katika kujijengea mabanda ya skuli, vituo vya afya, maji, umeme na kadhalika.  Sambamba na hatua hizo, Serikali kupitia Afisi ya Waziri Kiongozi itaendelea kuwahamasisha wananchi Mijini na Vijijini ili waweze kuutumia vizuri Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao umeshaanza kutumika na umetoa mchango mkubwa katika huduma za jamii. Aidha, kwa mwaka huu wa fedha Serikali itahakikisha kuwa jumla ya Shs. 150 milioni zilizotengwa kwa ajili ya miradi hiyo zitatolewa zote kama ilivyoahidiwa.

 

6.7     Nimeeleza hapo awali, kwamba moja ya fanikio kubwa tulilolipata katika mwaka uliopita ni kuandaa mpango wa kupunguza umasikini Zanzibar.  Kwa mwaka huu tuliouanza Serikali inaandaa mikakati ya kuanza kuitekeleza awamu ya kwanza ya miaka mitatu ya mpango huo.  Kipaumbele katika mkakati huo wa miaka mitatu ni kuelekeza nguvu zaidi kwenye sekta ya afya, maji, barabara, kilimo, elimu na utawala bora.  Serikali kwa kushirikiana na Mashirika ya Kimataifa ya UNDP na Benki ya Dunia yanaandaa mkutano wa mashauriano na wahisani wengine kuona jinsi gani wahisani hao wanaweza kutusaidia katika utekelezaji wa mpango huo wa kupunguza umasikini.

 

6.8    Ndugu Wananchi, mipango ya maendeleo inawahusu wananchi.  Ili kuwa na mipango mizuri ni vyema kujua idadi ya walengwa wanaokusudiwa.  Idadi ya watu wa Zanzibar inakadiriwa kufika milioni moja.  Uhakika wa idadi hiyo, imegawika vipi kimikoa, kijinsia, watoto na watu wazima, itafahamika wakati litakapofanyika zoezi la kuhesabu watu mwezi wa Agosti mwaka huu.  Maandalizi ya zoezi hili la sensa yapo mbioni kukamilika.  Zoezi la majaribio limefanyika na matokeo ni mazuri.  Ni haki na wajibu wetu sote kujitokeza bila ya kukosa wakati wa utekelezaji wa zoezi lenyewe.  Sensa ni jambo linalofanyika katika nchi zote duniani kila baada ya miaka kumi.  Madhumuni ni kuipa  Serikali uwezo wa kupanga vizuri mipango ya kuwahudumia watu wake.  Sensa haitafuti wakorofi, wala haitafuti majambazi.  Ni jukumu la watu wote na hasa viongozi kuwahamasisha wananchi washiriki zoezi hili kwa faida yetu sote.

 

6.9    Ndugu Wananchi, ongezeko la idadi ya watu linaambatana sana na uzito juu ya mazingira ya nchi.  Jinsi idadi ya watu inavyoongezeka ndivyo msongamano wa watu kwenye eneo dogo la ardhi unavyozidi.  Matokeo yake ni kuharibika kwa mazingira na kupungua kwa rasilimali za asili.  Inakadiriwa kuwa kwa wastani takriban hekta 1,000 za misitu ya asili hukatwa kila mwaka kwa ajili ya matumizi mbali mbali.  Ili kukabiliana na tatizo hili nchi haina budi iwe na mipango mahususi ya kuhifadhi mazingira ya asili.  Kila mwaka tumekuwa tukipanga siku maalum za upandaji wa miti hapa visiwani.  Kampeni hii ya upandaji wa miti haina budi iimarishwe na kuendelezwa kila mwaka.  Kutokana na haja hiyo, Serikali itasimamia kwa ukamilifu na kuwahusisha wananchi wote mijini na vijijini.

 

6.10     Ndugu Wananchi, mafanikio ya maandalizi yote ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake, yatategemea kuwepo kwa watu waliohai na wenye afya nzuri kwa kufanya kazi.  Wakati Serikali inayashughulikia hayo, ni wajibu wetu sote kuelewa vyema kwamba UKIMWI ni tatizo linaloathiri jamii yetu kwa kasi kubwa.   Hadi sasa watu zaidi ya 2,000 wameathirika na virusi vya ukimwi, na karibu watu 500 wameshapoteza maisha.  Makisio ni kwamba idadi ya walioathirika inafikia watu 7,000 au zaidi.

 

 

6.11    Ukimwi, tunaambiwa kwamba hadi sasa hauna tiba.  Kwa bahati nzuri kinga yake kubwa ni kujiepusha na tabia ya kufanya mapenzi nje ya ndoa.  Wakati umefika wa kuelimishana na kuhamasishana ili tuondokane na tabia zinazosambaza maradhi hayo.  Tuzungumze juu ya ukimwi kila tunapojumuika, kwenye mikutano ya kijamii, kisiasa, michezo, mikusanyiko ya kidini na kadhalika.  Tusione haya wala vibaya kuuzungumza ukimwi, kwani tukiuonea haya utatumaliza.

 

6.12     Kwa upande mwingine wapo wenzetu ambao tayari wameathirika na wengine wamekufa.  Tuwatunze walioathirika bila ya ubaguzi na tuwahudumie mayatima wa waliokufa kwa ukimwi kama watoto wetu.

 

6.13     Wale ambao wanashaka, wajitokeze, wapime damu zao na wapate ushauri nasaha ili waweze kuishi kwa matumaini.  Aidha, Serikali imo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa sheria ya kuanzishwa kwa Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZACAIDS).  Kazi kubwa ya Tume ya Ukimwi Zanzibar itakuwa ni kuhakikisha utayarishaji na utekelezaji wa mikakati na sera za kupambana na ukimwi pamoja na kuzuia kuenea kwa virusi na athari za ukimwi kwa jamii na kuwasaidia walioathirika na janga hilo.

 

6.14     Napenda kuitumia fursa hii pia kuvipongeza vyombo, mashirika na watu binafsi ambao wanajihusisha na kazi ya kupunguza kasi ya kuenea kwa ukimwi.  Jumuiya ya Umoja wa NGO - Cluster, ZACP, Africare, USAID, UNICEF, UNDP na wengineo ni baadhi ya vyombo tunavyosaidiana navyo katika vita hii.

 

6.15      Ndugu  Wananchi,  niliyoyataja  ni  baadhi ya mambo machache ambayo Serikali yenu imepanga kuyatekeleza katika mwaka ujao.  Mafanikio ya utekelezaji yatategemea sana mazingira ya kiuchumi na kijamii yatakavyokuwa.  Mipango ya kiuchumi imetayarishwa.  Kubwa ni kujenga mazingira ya kisiasa na kiutawala kuhakikisha utekelezaji mzuri.

 

 

6.16       Ndugu  Wananchi,  nchi  hii  ni  yetu  sote kila mmoja wetu ana haki na wajibu sawa na mwenziwe.  Tafauti zote zilizokuwepo huko nyuma ziliondoshwa tarehe 12 Januari, 1964,  siku ambayo nchi yetu ilipata uhuru wa kweli na jamhuri na ndio tunaisherehekea hivi leo.  Katika kipindi cha miaka 38, nchi yetu imeshuhudia mabadiliko mengi ya maendeleo yakiwemo maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kadhalika.

6.17     Kwa upande wa siasa tumepiga hatua kubwa zaidi kwa vile hivi sasa Taifa letu limefikia pahala ambapo tuna mfumo wa vyama vingi vya siasa unaosimamiwa na Katiba yenyewe na Sheria zinazohusika na kadhalika.  Hatua hii imetufanya Watanzania kuwa na utajiri mkubwa wa vyama vya siasa lakini sio utajiri wa uchumi.  Wamarekani wana vyama viwili tu vya siasa, Chama cha  "Democrats na Republican".  Wenzetu hao wana umasikini wa vyama vya siasa ukiwalinganisha nasi wenye zaidi ya vyama 12 lakini kwa upande wa uchumi wamepiga hatua kubwa kushinda nchi zote nyengine duniani.

 

 

6.18    Naamini wakati umefika kwa Watanzania kuutumia vizuri utajiri wetu wa vyama vya siasa kwa kuunganisha nguvu zetu na kuzielekeza kwenye juhudi za kutafuta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu na watu wake wote.  Kwa hivyo natoa changa moto kwa viongozi wa vyama, wafuasi wote na wananchi wote kwa jumla tuutumie wakati wetu vizuri kwa kujenga maisha yetu sote na vizazi vijavyo.  Inawezekana kila mmoja wetu atimize wajibu wake.

 

 

6.19     Tukijenga ushirikiano, na ushindani kwa misingi ya kuheshimiana na uzalendo tutaweza kudumisha umoja, utulivu, amani, upendo na maendeleo kwa watu wetu.

 

 

 

7.0     HITIMISHO:

 

7.1       Kwa kumalizia, naomba tena nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ujumbe wake kwa kuwa nasi siku hii ya leo.  Pia nawashukuru viongozi wengine wote wa Kitaifa kwa kuungana nasi katika kilele cha sherehe ya Mapinduzi mwaka huu.

 

7.2       Nawashukuru mabalozi wa nchi za nje, wahisani mbali mbali waliopo na wasiokuwepo hapa leo hii. Nazishukuru Serikali zote za nje zilizotusaidia wakati huu mgumu zikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa, Belgium, Sweden, India, Oman, Saudi Arabia, Kuwait, UAE, Egypt, Libya, Tunisia, Japan na kadhalika.  Shukurani maalum nazitoa kwa Serikali ya ndugu zetu wa China, kwa misaada ya hali na mali pamoja na msamaha wa madeni kwa Zanzibar na Tanzania.  Kadhalika nazishukuru taasisi za Kimataifa, World Bank, IMF, UNDP, UNESCO, UNIDO, WFP, FAO, ILO, WHO, ADB, OPEC, BADEA, KUWAIT FUND na SAUD FUND kwa mashirikiano mazuri tuliyonayo pamoja na misaada yao muhimu ya maendeleo kwetu.  Mwisho kabisa nawashukuru sana  wananchi wote kwa kunisikiliza kwa makini.

 

7.3       Nawatakieni nyote kheri za mwaka mpya.

 

Ahsanteni.

 

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR

MUNGU IBARIKI TANZANIA

MUNGU IBARIKI AFRIKA

 

MAPINDUZI  DAIMA