HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UBINAFSISHAJI, MHESHIMIWA Dk. ABDALLAH OMARI KIGODA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI WA TAIFA KATIKA MWAKA 2002, NA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MUDA WA KATI NA MFUMO WA MATUMIZI YA SERIKALI KWA KIPINDI CHA MWAKA 2003/04-2005/06

 

UTANGULIZI

1.                 Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likae kama kamati ili liweze kupokea na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2002 na Mapendekezo ya Mpango wa Muda wa Kati na Mfumo wa Matumizi ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2003/04-2005/06.  Pamoja na hotuba hii nawasilisha Kitabu cha Hali ya Uchumi katika Mwaka 2002 na Kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2003/04.

 

2.       Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kutoa Taarifa nilizozitaja hapo juu napenda kutoa shukrani zangu kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa kwa mchango mkubwa iliotoa wakati ikijadili Muhtasari wa Hotuba hii ambao umetuwezesha kuboresha kazi yetu.  Aidha, napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani kwa viongozi na wafanyakazi wenzetu wa Wizara ya Fedha  pamoja na wadau wengineo ambao tumefanya nao kazi bega kwa bega kutayarisha Taarifa hii na Mpango wa Maendeleo.

 

3.       Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kutoa shukrani zangu kwa Dk. E. S. Bukuku, Katibu Mkuu, Mipango na Ubinafsishaji, Naibu Katibu Mkuu, Bwana O. M. S. Bendera, Wakurugenzi, Viongozi wa asasi na wafanyakazi wote wa Mipango na Ubinafsishaji ambao wamefanya kazi kwa bidii na kufanikisha utayarishaji wa Taarifa hii na mpango huu.

 

4.       Mheshimiwa Spika, sasa naomba kuchukua nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa majina kwa kushinda katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwezi Mei, mwaka huu. Mheshimiwa Abu Towagale Kiwanga (Mb.), CCM, Jimbo la Kilombero, Mhe. Nazir Mustafa Karamagi (Mb.), CCM, Jimbo la Bukoba Vijijini, Mhe. Ndeka E. Nziriye (Mb.), CCM, Jimbo la Kigoma Kusini, Mhe. Sumri Abdallah Salum Mohamed (Mb.), CCM, Jimbo la Mpanda Magharibi, Mhe. Karim Said Othman (Mb.), CUF, Jimbo la Chambani, Mhe. Masoud Abdalla Salim (Mb.), CUF, Jimbo la Mtambile, Mhe. Mohamed Juma Khatib (Mb.), CUF, Jimbo la Chonga, Mhe. Ali Said Salim (Mb.), CUF, Jimbo la Ziwani, Mhe. Shoka Khamis Juma (Mb.), CUF, Jimbo la Micheweni, Mhe. Salim Omar Ali (Mb.), CUF, Jimbo la Tumbe, Mhe. Mchande Salim Mchande (Mb.), CUF, Jimbo la Konde, Mhe. Khamis Ali Saleh (Mb.), CUF, Jimbo la Mgogoni, Mhe. Mohamed Ali Said (Mb.), CUF, Jimbo la Wingwi, Mhe. Khalifa Suleiman Khalifa (Mb.), CUF, Jimbo la Gando, Mhe. Khalifa Mohammed Issa (Mb.), CUF, Jimbo la Mtambwe, Mhe. Bakar Shamis Faki (Mb.), CUF, Jimbo la Ole, Mhe. Mwadini Abass Jecha (Mb.), CUF, Jimbo la Utaani, Mhe. Ali Said Juma (Mb.), CUF, Jimbo la Kojani; na, Mhe. Omar Juma Omar (Mb.), CUF, Jimbo la Pandani.

 

5.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji, imekua ikishughulikia na kufuatilia maeneo makuu matatu ya jumla:  Eneo la kwanza ni lile la kuona kuwa uchumi wetu unakua kwa viwango na kasi kubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita.  Tunaamini kuwa kama sharti moja la kupambana vyema na changamoto ya kupunguza umaskini ni viashiria vya uchumi jumla (macro economic fundamentals) kukua na kuwa tulivu.  Tunaelewa hili ni sharti la lazima ingawaje sio ufumbuzi pekee wa kuboresha maisha ya Mtanzania.  Katika eneo hili kama tutakavyoona tumepata mafanikio sio tu kwa ukuaji wa Pato la Taifa lakini takwimu zinatuonyesha pia ukuaji umetokea kwa karibu sekta zote.

 

6.       Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni ile changamoto ya kuhakikisha ni jinsi gani mafanikio haya tunayoyapata katika kutekeleza sera za uchumi jumla yanatiririka na kuwanufaisha wananchi hususan vijijini.  Hata hivyo jitihada na hatua za Serikali za utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini zimeonyesha dalili nzuri za kupunguza umaskini usio wa kipato baina ya wananchi. Aidha programu zilizopangwa kutekelezwa chini ya sekta ya kilimo; kwa mfano, Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo pamoja na taratibu za kuanzisha skimu za utoaji wa mikopo kwa wale wenye vipato vya chini (micro credit schemes); azma ya Serikali ya kutekeleza Sera ya Uwezeshaji pamoja na Urekebishaji wa Utendaji kazi wa Halmashauri zetu za Wilaya; vitasaidia sana kupunguza umaskini wa kipato baina ya watu hasa vijijini.  Changamoto kubwa ni kwa kila mwenye uwezo wa kufanya kazi afanye kazi kwa bidii, tija na ufanisi na Serikali itimize majukumu yake ya utawala bora na uwekaji wa mazingira bora.

 

7.       Mheshimiwa Spika, eneo la tatu pamoja na lile la kuratibu mipango Kitaifa, ni lile la Uwekezaji na Ubinafsishaji.  Tunaamini uwekezaji utasaidia sana katika kukuza ujenzi wa mtaji wa taifa na hivyo kukuza uchumi wetu.  Mazingira tuliyojiwekea ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje yatabidi yawe endelevu, pamoja na kuimarisha taratibu za kutoa upendeleo wa makusudi kwa Watanzania wazalendo.  Takwimu za uwekezaji kama tutakavyoziona zinaonyesha kutuelekeza kwenye upendeleo huo.  Zoezi la ubinafsishaji linalenga katika urekebishaji wa utendaji wa viwanda na mashirika yetu.  Mafanikio yamepatikana na vile vile yapo matatizo mbali mbali ambayo bado yanabakia ni changamoto kwa Serikali.  Medani za uchumi zinaelekeza kuwa zoezi la ubinafsishaji ni asilimia ndogo tu ya hatua za urekebishaji uchumi zinazochukuliwa na nchi.  Hivi sasa nchini Tanzania zoezi hili linakaribia hatma, ila changamoto tuliyonayo ni vipi tutahakikisha kuwa mafanikio yaliyokwishapatikana katika zoezi hili yanakuwa endelevu.  Ipo haja kwa Serikali kuendelea kuweka mazingira bora ya sera ya fedha (monetary) na sera za kodi (fiscal) ili kuwezesha wamiliki kufanya kazi zao kwa tija na ufanisi.  Takwimu zinatuonyesha kuwa kati ya viwanda vilivyobinafsishwa, karibu asilimia 51 vinamilikiwa na Watanzania.

 

8.       Mheshimiwa Spika, hata hivyo tumegundua kwamba kwa baadhi ya Watanzania makini (serious) wanaomiliki viwanda hivi wamekumbwa na matatizo yafuatayo:  Kwanza, mtaji mkubwa wa kifedha unaohitajika kubadilisha mitambo na mashine zilizopitwa na wakati zilizokuwa katika viwanda wanavyomiliki ni mzigo mkubwa.  Mzigo huu unawafanya wasianze kufanya kazi kwa kuendana na teknolojia ya kisasa hivyo kushindwa kumudu ushindani wa soko.  Pili, gharama kubwa za uzalishaji zinazotokana au na madeni yaliyorithiwa au na gharama za uendeshaji hasa zinazotokana na bei kubwa za umeme.  Tatu, udhaifu katika menejimenti na ujuzi.  Mwisho, udhaifu tuliorithi wa kutohimili utamaduni mpya wa Watanzania wazawa kumiliki viwanda na ule wa kushindwa kutayarisha michanganuo yakinifu ya miradi ambayo inaweza kupata mikopo kutoka mabenki.  Inawezekana kabisa ipo haja ya makusudi kwa Serikali kutafuta sasa taratibu za kuwapunguzia mizigo hii, hususan wawekezaji Watanzania ili waweze kuvifufua viwanda hivi kwa ukamilifu ili vifanye kazi, hasa kwa wale wawekezaji Watanzania ambao ni makini.  Kwa hiyo, ipo haja ya msingi kwa Serikali kutafakari na kubuni njia na taratibu zinazoweza kuchukuliwa ili kuwapunguzia wawekezaji Watanzania: bei ya manunuzi ya mashirika hayo; kufuta madeni yanayowasibu; kuwaongezea muda wa kulipa madeni yao na mwisho kuwapa uwezo wa kupata mikopo kutoka mabenki au taasisi nyinginezo za fedha ili kuendeshea na kutekelezea mipango yao ya uwekezaji na biashara.

 

9.       Mheshimiwa Spika, nilipowasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2001 na Mapendekezo ya Mpango wa Muda wa Kati na Mfumo wa Matumizi ya Serikali kwa Kipindi cha mwaka 2002/03 – 2004/05, nililitaarifu Bunge lako Tukufu juu ya malengo ya uchumi jumla kwa mwaka 2002/03 kama ifuatavyo:

·        Pato la Taifa halisi kukua kwa asilimia 5.9 mwaka 2002 na asilimia 6.3 mwaka 2003;

·        Kuwa na kiwango cha kasi ya upandaji bei kisichozidi asilimia 4.2 ifikapo Juni, 2003;

·        Kuongeza mapato ya ndani ya Serikali kwa uwiano wa Pato la Taifa wa asilimia 12.3 mwaka 2002/03;

·        Kukidhi ujazi wa fedha (M2) kwa viwango vinavyowiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na kupunguza kasi ya upandaji bei; na,

·        Kuongeza akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

 

MAPITIO YA HALI YA UCHUMI KWA JUMLA

Ukuaji wa Uchumi

10.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vigezo na viashirio vya msingi vya uchumi jumla (macro economic fundamentals) Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.2 mwaka 2002, ikilinganishwa na asilimia 5.7 mwaka 2001. Ukuaji huu wa uchumi ni zaidi ya lengo lililowekwa la asilimia 5.9 kwa mwaka 2002. 

 

11.     Mheshimiwa Spika, kiwango tulichofikia cha ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia 5.6 kwa miaka mitatu iliyopita ukilinganisha na kile cha asilimia 3.4 kwa wastani kwa nchi za Afrika kinatia moyo.  Hata hivyo ukuaji huo bado ni mdogo mno kuweza kukidhi mahitaji yatokanayo na ongezeko la idadi ya watu la asilimia 2.9 kwa mwaka na kutoa ufumbuzi wa matatizo yetu kama vile ukosefu wa ajira na umaskini.  Njia kuu ya kuinua kiwango cha kukua kwa uchumi wetu ni kuongeza juhudi, maarifa na ubunifu katika ngazi zote za jamii.  Serikali itaendelea kuweka mazingira bora, lakini tegemeo kuu la kukua kwa uchumi wetu ni pamoja na: kuongeza kiwango cha uwekaji akiba; kuongeza kasi ya ongezeko la mitaji; kuongeza kasi ya mauzo nje; na, wananchi wenyewe kufanya kazi kwa bidii.

 

Kasi ya Upandaji Bei

12.     Mheshimiwa Spika, kasi ya upandaji bei iliendelea kupungua na kufikia   asilimia 4.3 mwezi April 2003, ikilinganishwa na asilimia 4.5 mwezi Juni 2002.   Kupungua kwa mwenendo wa kasi ya upandaji bei kunatokana hasa na hali nzuri ya upatikanaji wa mapato, mazao na usambazaji wa chakula, pamoja na sera za makusudi za kudhibiti mwenendo wa mapato na matumizi ya Serikali na ujazi wa fedha nchini.

 

13.     Mheshimiwa Spika, kushuka kwa kasi ya upandaji bei kutoka asilimia 30 mwaka 1995 na kufikia asilimia 4.3 kumetuletea manufaa makubwa kama vile kutengemaa kwa uchumi; kuvutia wawekezaji, na kuboresha ufanisi wa sekta ya fedha.  Kutokana na ongezeko katika ubora wa bidhaa zetu sasa tunaweza kuuza nje baadhi ya bidhaa kama vile saruji, nyaya na transfoma za umeme, bia, sigara, na mablanketi.  Hata hivyo, kutokana na kutokuwepo kwa ongezeko linaloridhisha la pato halisi (disposable income) kwa wananchi walio wengi vijijini na mijini, kushuka kwa kasi ya upandaji bei hakujaleta manufaa makubwa kwa wananchi wengi.  Kazi kubwa ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa na utoaji huduma mbali mbali pamoja na uwezo wa wananchi wa kununua bidhaa na huduma hizo.

 

Ujazi wa Fedha na Karadha

14.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Juni – Desemba 2002 ujazi wa fedha kwa maana pana (M2) uliongezeka kwa asilimia 13.0 ikiwa karibu sawa na kiwango cha lengo la asilimia 12.0 katika mwaka 2002/03.  Katika kipindi hicho mikopo kwa Serikali iliongezeka kwa asilimia 30.4, ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 11.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2001. Mwenendo huo ulitokana na ongezeko la mauzo ya dhima za Serikali. Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 18.4, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 6.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2001.  Wastani wa riba za mikopo zinazotozwa na mabenki ya biashara ulipungua kidogo na kufikia asilimia 15.7 mwezi Desemba 2002 kutoka asilimia 16.4 mwezi Juni 2002.  Wastani wa riba inayotolewa kwa amana ulipungua na kufikia asilimia 3.1 mwezi Desemba 2002 kutoka asilimia 3.5 mwezi Juni 2002.

 

15.     Mheshimiwa Spika, kiwango cha ujazi wa fedha kilichofikiwa katika mwaka 2002 cha asilimia 13.0 kinaashiria  kwamba uchumi wetu unakaribia kuanza kuwa na nguvu za kujirekebisha wenyewe na kufanya kazi ipasavyo; yaani uchumi ambao ujazi wake wa fedha unaendana na ongezeko la uzalishaji na viwango vya huduma zinazotolewa nchini, mabenki yanayotoa mikopo kwa riba za kadri, sekta za uzalishaji zinazofanya kazi kwa ufanisi na fedha yenye thamani ndani na nje ya nchi.

 

Akiba ya Fedha za Kigeni

16.     Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni iliongezeka kwa asilimia 32.3 na kufikia dola 1,529.9 milioni mwaka 2002 kutoka dola 1,156.6 milioni mwaka 2001.  Kiasi hiki ni sawa na uwezo wa kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 8.9 ikilinganishwa na miezi 6.3 mwaka 2001.

 

Thamani ya Shilingi

17.     Mheshimiwa Spika, thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola moja ya Marekani ilipungua kwa asilimia 7.6 kutoka Sh. 888.9 kwa dola ya Marekani mwishoni mwa Juni 2001 hadi Sh. 956.8 kwa dola ya Marekani mwishoni mwa Juni 2002.  Thamani iliendelea kupungua kwa kasi hadi kufikia shilingi 1040 kwa dola ya Marekani mwezi Mei 2003.  Kupungua huku kwa thamani ya shilingi kulisababishwa kwa kiasi kikubwa na kasi ndogo ya mauzo nje na kuendelea kushuka kwa bei za bidhaa asilia katika soko la dunia.  Njia kuu ya kuimarisha thamani ya shillingi ni kuongeza mauzo nje.

 

          BAJETI YA SERIKALI

Mapato

18.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2001/02 makusanyo ya mapato ya ndani kupitia kodi za mapato, ushuru wa forodha, kodi ya ongezeko la thamani (VAT), na mapato kutokana na vyanzo vingine yalikuwa asilimia 12.2 tu ya Pato la Taifa, ambayo yanalingana na ya mwaka 2000/01.  Malengo ya muda wa kati ya sera ya kodi kuendelea ni kuongeza uwezo wa Serikali wa kukusanya mapato kwa kuongeza vyanzo vya kodi, kupambana na ukwepaji kodi, kudhibiti misamaha ya kodi pamoja na kuimarisha usimamizi ili kufikia kiwango cha asilimia 13.2 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2003/04.

 

Matumizi

19.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/02 matumizi makubwa ya Serikali yalielekezwa katika kupunguza umaskini na kukuza uchumi.  Sekta na maeneo yaliyopewa kipaumbele yaligawiwa fedha karibu zote zilizokuwa zimekadiriwa.

 

Deni la Taifa

20.     Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa Desemba 2002, deni la taifa lilikuwa dola za Marekani 8.9 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 7.2 ikilinganishwa na deni la dola 8.3 bilioni mwishoni mwa mwaka 2001. Kati ya fedha hizo, deni la nje ni dola za kimarekani 8.0 bilioni au asilimia 89.9, na lile la ndani ni dola 0.9 bilioni sawa na asilimia 10.1.  Ongezeko la deni linatokana hasa na kupevuka kwa madeni ya nyuma.

 

21.     Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Deni la Taifa unaolenga katika kuimarisha usimamizi wa madeni ya nje na ndani ulizinduliwa mwezi Agosti 2002. Mkakati huu unabainisha mwongozo na maelekezo ya ukopaji nje, ukiwa na lengo la kuhakikisha kwamba mzigo wa madeni ya nje utakuwa stahimilivu (debt sustainability).

 

22.     Mauzo na Uagizaji Bidhaa Nje

Mheshimiwa Spika, thamani ya mauzo ya bidhaa nje mwaka 2002 iliongezeka kwa asilimia 16.25 na kufikia dola 902.55 milioni, ikilinganishwa na dola 776.4 milioni mwaka 2001.  Ongezeko hilo lilichangiwa hasa na mauzo ya bidhaa zisizo asilia kama vile madini, mazao ya samaki na bidhaa za viwandani ambazo zilichangia asilimia 77.16, ikilinganishwa na asilimia 70.1 mwaka 2001.  Kwa ujumla thamani ya bidhaa asilia karibu zote zilishuka kutokana na kupungua kwa bei katika soko la dunia na hivyo kuchangia asilimia 22.8 tu ya jumla ya mauzo nje, ikilinganishwa na asilimia 29.9 mwaka 2001.  Thamani ya uagizaji toka nje ilikuwa dola 1,511.3 milioni mwaka 2002, ikilinganishwa na dola 1,560.5 milioni mwaka 2001. Kupungua huko kulitokana na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa za mitambo hususan kwenye sekta ya madini na chakula.

 

Mkakati wa Kuongeza Mauzo Nje

23.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002 mwenendo wa mauzo na uagizaji bidhaa nje umeendelea kuonyesha nakisi katika urari wa biashara ya nje japokuwa imepungua.  Ili kupunguza nakisi serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga katika kukuza mauzo ya bidhaa nje.  Itakumbukwa kwamba mnamo Julai 2002, Bunge lilipitisha sheria ya kuanzisha maeneo huru ya uzalishaji bidhaa kwa ajili ya kuuza nje (EPZ).  Baada ya sheria hiyo kupitishwa na Bunge, Serikali ilikamilisha utayarishaji wa kanuni zinazoongoza uanzishaji na usimamizi wa maeneo hayo.  Kutokana na jitihada hizi Kiwanda cha nguo cha NIDA-Tabata, Dar-es-Salaam kimepata usajili wa EPZ na kuzinduliwa.  Aidha viwanda vya Nguo vya Urafiki na kile cha Ubungo Millennium vinaendelezwa ili kusajiliwa.  Ili kukuza mauzo nje ni muhimu kuendelea kutekeleza kwa dhati mkakati wa kukuza mauzo nje kwa kuboresha miundo mbinu, ujuzi, masoko, utangazaji wa bidhaa, ubora wa viwango, n.k.

 

SEKTA YA NJE

HALI YA UCHUMI DUNIANI NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Ukuaji wa Uchumi:

24.     Mheshimiwa Spika, licha ya misukosuko mingi duniani, pato la dunia lilikua kwa asilimia 3.0 katika mwaka 2002, ikilinganishwa na asilimia 2.3 katika mwaka 2001.  Kwa nchi zilizoendelea pato lilikua kwa asilimia 1.8 mwaka 2002 ikilinganishwa na asilimia 0.8 katika mwaka 2001. Nchi zinazoendelea pato lake liliongezeka kwa asilimia 4.6, kutoka ongezeko la asilimia 3.6 mwaka 2001 wakati ongezeko la pato la bara la Afrika lilipungua kutoka asilimia 3.6 mwaka 2001, hadi asilimia 3.4 mwaka 2002.  Aidha, katika baadhi ya nchi za Afrika, kutozingatiwa kwa suala la usimamizi mzuri wa uchumi; migogoro ya kisiasa katika nchi nyingi za Afrika, tatizo la magonjwa na ukame wa 2002 vilichangia kulegalega kwa uwekezaji na shughuli za kiuchumi barani Afrika.

 

Mwelekeo wa Ukuaji wa Uchumi Duniani katika Kipindi cha Mwaka 2003/04

25.     Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa ukuaji wa uchumi duniani kwa kipindi cha muda mfupi ujao siyo wa kuridhisha kutokana na matatizo ya kiusalama na afya kwa maana ya kuongezeka kwa wasiwasi wa ugaidi, machafuko ya kisiasa katika maeneo ya Mashariki ya Kati, Bara la Afrika na baadhi ya nchi za Amerika Kusini; na kuongezeka kwa athari za UKIMWI na kuibuka kwa ugonjwa wa Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS).  Matatizo haya mawili yanaweza kuathiri biashara yetu ya utalii na uwekezaji.  Serikali inachukua hatua zinazostahili ili kukabiliana na matatizo haya na kutoa taarifa sahihi ndani na nje ya nchi.

 

          Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

26.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002, Jumuiya ya Afrika Mashariki iliendelea na: maandalizi ya itifaki ya ushuru wa pamoja wa forodha ambayo imepangwa kukamilika mwezi Novemba 2003; jitihada za kukuza biashara na uwekezaji rasilimali; na, taratibu za kufungua masoko ya mitaji na mizania ya malipo na nchi za nje hususan kwenye masoko ya mitaji ya Dar es Salaam, Nairobi na Kampala. Rasimu ya Sera na Mkakati wa Sekta ya Kilimo na Maendeleo Vijijini ilikamilishwa kwa lengo la kuendeleza ushirikiano katika kilimo, usalama na uhakika wa chakula na mchanganuo wa fursa za Bonde la Ziwa Victoria kama Eneo Maalum la kukuza Uchumi ulikamilishwa (Economic Growth Zone).  Katika mpango wa muda wa kati maeneo haya yataendelea kupewa kipaumbele.

 

JUMUIYA YA MAENDELEO YA NCHI ZA KUSINI MWA AFRIKA (SADC)

27.     Mheshimiwa Spika, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wa SADC uliofanyika Zanzibar mwezi Februari, 2002 ambao pamoja na mambo mengine uliazimia kufanyika kwa mkutano wa kutathmini fursa za uwekezaji vitega uchumi kusini mwa Afrika unaotarajiwa kufanyika mjini London Uingereza mwezi Julai, 2003.

 

28.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002, SADC ilikamilisha rasimu ya kwanza ya Mkakati wa Mpango wa Maendeleo ya Ushirikiano (Regional Indicative Strategic Development Plan – RISDP).  Mpango huu unalenga: kuondoa umaskini; ushiriki sawa wa maendeleo; utandawazi; maendeleo endelevu; pamoja na, masuala yanayohusu jinsia ili yapatiwe ufumbuzi wa pamoja.

 

29.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Azimio na Mkataba wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (Declaration and Treaty) mwaka 2002, Serikali ya Tanzania iliridhia itifaki zinazohusu Maendeleo ya Utalii; Afya; Kulinda na Kuhifadhi Wanyamapori; Siasa na Ushirikiano katika Ulinzi; Udhibiti wa Silaha Ndogo Ndogo; pamoja na itifaki ya Taratibu za Kuendesha shughuli za Jumuiya. Aidha, kwa mwaka 2003/04 SADC itakamilisha zoezi la muundo wake kulingana na majukumu yake mapya.

 

 

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SEKTA MUHIMU

 

SEKTA ZA UZALISHAJI

Sekta ya Kilimo

30.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ukuaji kisekta (sectoral growth) katika mwaka 2002, sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 5.0 ikiwa ni pungufu kidogo, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.5 mwaka 2001.  Ukuaji huo ulitokana zaidi na ukuaji katika sekta ndogo ya mifugo (asilimia 3.5), misitu na uwindaji (asilimia 3.0) na uvuvi (asilimia 6.5). Sekta ndogo ya mazao ya kilimo, ilikua kwa asilimia 6.2 mwaka 2002 ikiwa ni chini ya ukuaji wa asilimia 7.3 mwaka 2001.

 

31.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2002/2003 Serikali iliendelea kuweka msingi utakaowezesha sekta ya kilimo kuongoza katika kukuza uchumi, kuongeza nafasi za ajira na kupunguza umaskini nchini kupitia:-

·        Kukamilisha programu ya kutekeleza mkakati wa kuendeleza sekta ya kilimo;

·        Mpango kamambe wa kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini uliokamilishwa mwezi Oktoba, 2002.  Ili mpango huu uwe wa manufaa hapana budi kuziwezesha wilaya, kata na vijiji kuandaa mipango shirikishi ya utekelezaji katika ngazi hizo ili kujenga dhana ya umiliki (ownership);

·        Kuainisha mfumo wa kodi wa Serikali kuu na Serikali za mitaa kwa nia ya kupunguza kodi wanazotozwa wakulima;

·        Kukarabati barabara na madaraja vijijini yaliyopewa kipaumbele chini ya mkakati wa kupunguza umaskini, ili kupunguza gharama za uzalishaji katika sekta ya kilimo;

·        Kueneza kwa mtandao wa simu katika vijiji vingi mwaka 2002 kwa lengo la kurahisisha mawasiliano kwa wakulima wanapotafuta masoko kwa ajili ya mazao yao, pembejeo na zana za kilimo;

·        Kuelimisha wawekezaji juu ya kufutwa kwa malimbikizo ya madeni ya kodi ya ardhi iliyokuwa inatozwa kwa shillingi 600 kwa ekari hapo awali ikilinganishwa na kiwango cha sasa cha shilingi 200 tu kwa ekari;

·        Taasisi za kifedha zimehimizwa kutoa mikopo kwa wakulima wakubwa na wadogo nchini na kuhamasisha wananchi kuungana ili kuanzisha benki za ushirika na jamii.  Aidha azma ya Serikali, ni kuhamasisha uanzishaji wa Benki ya Maendeleo itakayohudumia kilimo;

·        Kuongeza bajeti kwa ajili ya kukusanya takwimu muhimu katika sekta ya kilimo, kwa hiyo kuwezesha kufuatilia mwenendo wa sekta.

 

32.     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2003/04 ni azma ya Serikali kuendelea na jitihada zake za kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha taifa kufanya mageuzi katika kilimo. Lakini ni dhahiri kwamba jitihada pekee zinazofanywa na Serikali haziwezi kuongeza tija na kuleta mageuzi yanayotarajiwa katika kilimo.  Ninaamini tunaweza kufanikiwa katika kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo kwa muda mfupi iwapo wadau katika sekta ya kilimo watatimiza wajibu wao kikamilifu.  Serikali kwa upande wake itaendelea kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya kilimo kwa kuimarisha ugani, kuainisha na kupunguza kodi, kuhimiza taasisi za kifedha kutoa mikopo, kutoa motisha, kusaidia wakulima kupata masoko na kurahisisha upatikanaji wa zana na pembejeo; na kwa upande mwingine kama mabenki na taasisi za kifedha zitatoa mikopo; wakulima wataanzisha vyama vya ushirika vitakavyorahisisha upatikanaji wa pembejeo kwa bei nafuu; sekta binafsi zitaanzisha viwanda vidogo vya kusindika mazao ya wakulima; mikoa na wilaya zitasimamia kikamilifu utayarishaji na utekelezaji Mipango ya Maendeleo ya Sekta ya kilimo; na Mashirika yasiyo ya kiserikali na madhehebu ya dini na yatahamasisha wananchi kwa bidii kwa nia ya kubadilisha fikra zao kuhusu kilimo.

 

Sekta ya Viwanda

33.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2002 sekta ya viwanda ilikua kwa asilimia 8.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.0 mwaka 2001. Kufufuliwa kwa baadhi ya viwanda na ongezeko la uzalishaji na tija ni miongoni mwa sababu za ukuaji huu.

 

34.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002 sekta ya viwanda iliongoza kwa kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje ikilinganishwa na sekta nyingine ambapo jumla ya miradi ya viwanda 103 iliidhinishwa na Kituo cha Uwekezaji yenye thamani ya shilingi 195,072 milioni, ikilinganishwa na miradi 82 iliyopitishwa mwaka 2001 yenye uwezo wa kutoa nafasi za ajira kwa watu 15,685.  Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa sekta binafsi nchini inakua na kuwekeza kwani kati ya miradi ya viwanda iliyoidhinishwa miradi 35 ilikuwa ya wawekezaji binafsi wa ndani, miradi 42 ya wawekezaji wa nje na miradi 26 ikiwa ni ya ubia ya wawekezaji wa ndani na nje.

 

35.     Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kwa mwaka 2003/04 kutekeleza Sera ya Viwanda Vidogo na vya Kati ili kuongeza nafasi za ajira; kuboresha mazingira ili kuvutia wawekezaji kwenye viwanda vinavyoongeza thamani ya bidhaa na mauzo nje hususan kwenye sekta ya nguo, ngozi na usindikaji wa matunda na mboga na vifungashio.

 

Sekta ya Madini

36.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002 sekta ya madini ilikua kwa asilimia 15.0, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 13.5 katika mwaka 2001.  Mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa mwaka 2002, uliongezeka na kufikia asilimia 2.7, ikilinganishwa na asilimia 2.5 mwaka 2001.  Katika mpango wa muda wa kati na mrefu Sekta ya madini inatarajiwa kuongeza nafasi za ajira, mapato zaidi kwa Serikali, kuendeleza sekta ya viwanda, kuchangia katika Pato la Taifa na upatikanaji wa fedha za kigeni, na hatimaye kuchangia katika kupunguza umaskini.

 

37.     Mheshimiwa Spika, mauzo ya madini nchi za nje mwaka 2002 yalifikia kiasi cha dola 372.8 milioni, ikilinganishwa na dola 302.2 milioni mwaka 2001, sawa na ongezeko la asilimia 23.3. Mchango mkubwa wa zaidi ya asilimia 88.5 ulitokana na mauzo ya dhahabu ambayo yameongezeka kutokana na wawekezaji wengi wa nje na ndani wenye mitaji na teknolojia ya kisasa.

 

38.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2003/04 sekta ya madini itaendelea na jitihada za kutekeleza sera ya madini ya mwaka 1997, na sheria ya madini ya mwaka 1998 vyote vikilenga katika kutoa nafasi za ajira na kuongeza uzalishaji wa madini.  Aidha, Serikali itahakikisha kwamba amani na utulivu kati ya wawekezaji wakubwa na wadogo vinadumishwa, na kuwa jamii zilizopo karibu na migodi ya madini zinafaidika na miundo mbinu na huduma za kijamii muhimu kama vile barabara, shule, huduma za afya, maji, na umeme. Serikali pia itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma muhimu za uchimbaji na uuzaji wa madini kwa wachimbaji wadogo.

 

Sekta ya Biashara na Utalii

39.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002 sekta ya uuzaji jumla, reja reja na mahoteli ikijumuisha utalii ilikua kwa asilimia 7.0, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.7 mwaka 2001. Ongezeko hili limetokana na maendeleo ya kuridhisha ya upatikanaji wa bidhaa hapa nchini. Aidha, hali ya biashara ya utalii nayo ilichangia kwa kiasi kikubwa kwenye ongezeko hili hasa kutokana na jitihada za utangazaji wa vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi. Pia, Serikali iliandaa kongomano la kwanza kimataifa la wawekezaji kwenye sekta ya utalii mwezi Oktoba, 2002.

 

40.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2003/04 Serikali itaendelea kuweka mkazo katika utangazaji wa vivutio vya utalii ndani na nje katika masoko asilia na mapya, ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwekezaji katika sekta ya utalii, kuboresha huduma za utalii, kuimarisha miundo mbinu muhimu ya utalii na kudumisha usalama wa wageni na mali zao.

 

MIUNDOMBINU

          Sekta ya Ujenzi

41.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002, sekta ya ujenzi ilikua kwa asilimia 11.0, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 8.7 mwaka 2001.  Ukuaji huu ulitokana na ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara kuu na za vijijini, madaraja madogo, ujenzi wa majengo ya nyumba za kuishi na ya biashara na majengo ya shule za msingi na kukamilika kwa daraja la mto Rufiji.

 

          Barabara na Madaraja

42.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2002 Serikali ilikamilisha na kuanza utekelezaji wa sera ya ujenzi pamoja na mpango kamambe wa miaka kumi wa maendeleo ya sekta ya barabara nchini. Aidha, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi mingi ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara kuu kwa kiwango cha lami kwa kutumia zaidi fedha zake za ndani. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kwamba Mheshimiwa Rais William Benjamin Mkapa hivi karibuni amefungua miradi hiyo ikiwemo barabara za Mtukula – Muhutwe – Kagoma (136 km), Songwe – Tunduma (70 km), Shelui – Nzega ( 108 km), Chalinze _ Melela (129 km), Mkuranga – Kibiti (60 km), Somanga – Masaninga (33 km) na daraja la mto Matandu.

 

43.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara za vijijini, jumla ya madaraja 180 na kilometa 3,780 zilifanyiwa matengenezo mwaka 2002 ikilinganishwa na madaraja 73 na kilometa 3,573 zilizofanyiwa matengenezo mwaka 2001. Pia, Serikali ilikamilisha maandalizi ya taarifa ya mkakati wa utekelezaji wa barabara za Jumuiya Afrika Mashariki mnamo mwezi Novemba, 2002, na kuiwasilisha kwenye mkutano wa wahisani uliofanyika Arusha tarehe 29 Aprili, 2003. Tanzania itafaidika sana na programu hii ambayo zaidi ya asilimia 75 ya barabara zilizopewa kipaumbele zipo nchini. Mfano, barabara kuu ambazo zipo katika mpango huu ni :

 

44.     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2003/04 Serikali itaendelea kuweka mkazo katika ujenzi, matengenezo na ukarabati wa madaraja na barabara kuu na zile za vijijini zilizopewa kipaumbele chini Mkakati wa Kupunguza Umaskini na wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Utekelezaji wa shughuli hizi utaishirikisha sekta binafsi kwa kiwango kikubwa.

 

Sekta ya Mawasiliano na Uchukuzi

45.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002 sekta ya mawasiliano na uchukuzi ilikua kwa kiwango cha asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 6.3 mwaka 2001.  Viwango hivi vinaonyesha kuanza kuimarika kwa huduma za mawasiliano kwa njia ya simu na uchukuzi kwa njia za barabara na anga ambazo sasa zinamilikiwa kwa kiwango kikubwa na sekta binafsi hivyo kufanya utoaji wa huduma kuwa wa ufanisi.  Hali hii imechangia kuongezeka kwa mchango wa sekta hii katika Pato la Taifa kutoka asilimia 5.4 mwaka 2001 hadi asilimia 5.5 mwaka 2002.

 

46.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2003/2004 sekta hii itaendelea kuboresha usafiri wa abiria na uchukuzi wa mizigo kwa pande zote za  mijini na vijijini. Aidha, usafiri kwa njia za reli na majini na taratibu bora za usalama kwa usafiri wa vyombo vyote  utaimarishwa.

 

Sekta ya Nishati

47.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002 Serikali iliendelea kufanya marekebisho ya kisera na urekebishaji wa muundo na uendeshaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Aidha, Serikali itaendelea na jitihada za kuendeleza na nishati mbadala ambazo zinaendelea kutumika na kufanyiwa utafiti zaidi za micro-hydro, upepo tungamotaka, bayogesi, mionzi ya jua na makaa ya mawe.

 

48.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ndogo ya gesi, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na wahisani wengine imekamilisha makubaliano ya uendelezaji wa Mradi wa Gesi ya Songosongo.  Utekelezaji wa Mradi huu ulioanza mwezi Oktoba 2002 utajenga mtambo na bomba la kupitisha gesi kutoka Songosongo hadi Dar es Salaam.  Mradi huu utakamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka 2004.

 

HUDUMA ZA JAMII

49.     Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali za kuhakikisha kuwa mafanikio ya ukuaji wa uchumi jumla yanatiririka kwa wananchi wengi vijijini, imeanzisha kwa makusudi Mpango wa Kupunguza Umaskini kupitia uboreshaji wa huduma za jamii.  Lengo la Serikali ni kupunguza umaskini usio wa kipato, pamoja na ule wa kipato.

 

            Sekta ya Elimu

50.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2002/03 Serikali iliendelea kuimarisha mazingira ya elimu kwa kushirikisha asasi mbalimbali. Aidha, mashirika na watu binafsi wamejitokeza zaidi katika kujenga na kutoa elimu ya awali, elimu ya msingi, sekondari na elimu ya juu.

 

51.     Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) mwaka 2002, madarasa 15,991 yalijengwa kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na wananchi na kupita lengo lililopangwa la madarasa 13,868. Uandikishaji wa watoto wote walioko shuleni umefikia asilimia 98.6 na watoto wa rika ya elimu ya msingi (miaka 7-13), walioko shuleni umefikia asilimia 80.7 ikiwa inakaribia lengo la asilimia 85 lililowekwa kwa mwaka 2003. Aidha, takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya wanafunzi katika shule za msingi za Serikali na za binafsi iliongezeka kwa asilimia 23, kati yao waliokuwa wanasoma shule za binafsi waliongezeka zaidi ya mara tatu.  Ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi, shule za Serikali ziliongezeka kwa asilimia 4.8 na walimu nao kwa asilimia 5.8.

 

52.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu ya sekondari uwezo wa kuingia sekondari umeongezeka toka asilimia 19.5 mwaka 2001 hadi asilimia 21.7 mwaka 2002. Idadi ya wasichana wanaojiunga na kidato cha tano pia imeongezeka toka asilimia 38 hadi asilimia 42 na Serikali chini ya Mpango wa Elimu ya Sekondari iliwalipia ada wasichana 4,367 wa kidato cha I-VI ambao wanajiweza kimasomo lakini wazazi wao hawana uwezo wa kulipa karo.  Aidha, kazi zilizoendelea kufanyika katika ngazi ya elimu ya juu na ufundi, ni pamoja na kuboresha utoaji wa mafunzo mbalimbali katika vyuo vya elimu ya juu na kuvipandisha hadhi baadhi ya vyuo.

 

53.     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2003/04, mpango wa maendeleo katika sekta ya elimu utaendelea kuweka mkazo katika kuimarisha mazingira ya kutoa elimu na mafunzo katika ngazi zote. Jitihada zaidi zitawekwa katika kuongeza uandikishaji wa wanafunzi unaoenda sambamba na kujenga na kukarabati madarasa na nyumba za walimu na kuajiri walimu wapya.

 

Sekta ya Maji

54.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002 Serikali iliridhia utekelezaji wa sera mpya ya maji yenye lengo la kupatikana maji kwa urahisi ili wananchi wapate   muda wa kujishughulisha na uzalishaji maji ili kuboresha maisha yao na hivyo kupiga vita umaskini.

 

55.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2002, jumla ya  vyanzo vya kuchepua maji 4849 vilitambuliwa katika mabonde ya mto Rufiji, Mto Pangani na Ziwa Victoria.  Kati ya hivyo 1773 vimetolewa hati, na 3076 havijapata hati za haki ya kumiliki maji.  Aidha, hadi Desemba, 2002 jumla ya visima virefu 369 vilichimbwa katika maeneo mbalimbali nchini, na vyombo 1278 vya kuchimba na kutafuta maji viliundwa.

 

56.    Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi waishio vijijini katika mwaka 2002 ulifikia asilimia 53 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3 ikilinganishwa na mwaka 2001. Huduma ya majisafi mjini iliongezeka na kufikia asilimia 73 ikilinganishwa na asilimia 70 ya mwaka 2001. Ongezeko hili linatokana na kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa mji wa Dodoma ambao ulizinduliwa Desemba 2002 pamoja na utekelezaji wa mradi wa dharura wa maji wa mji wa Shinyanga.  Pia, ukodishaji wa DAWASA umekamilika chini ya Kampuni ya Dar es Salaam City Water Services kwa kipindi cha miaka kumi na inatarajia kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2003. 

 

57.     Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi, Serikali itaendelea kuhamasisha mashirika ya kitaifa na kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, watu binafsi na wananchi wenyewe kuchangia, na kushiriki katika ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji vijijini. Lengo la sekta ya maji ni kutoa huduma ya maji safi, salama na ya kutosha kwa sehemu za mijini na vijijini ili kuongeza idadi ya watu wanaopata maji toka asilimia 50 mwaka 2002/03 hadi asilimia 55 mwaka 2003/04.  Sekta ya maji pia inalenga kuimarisha na kulinda vyanzo vya maji.

 

Sekta ya Afya:

58.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2002/03 Serikali ilifanya mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 1990 na kwa nia ya kuandaa sera mpya.  Sera inalenga katika kutoa huduma za afya bora na madhubuti kwa Watanzania wote hasa walio na kipato cha chini. Sera hii imejumuisha mapendekezo ya mabadiliko ya Sekta ya Afya (1994), Dira ya Taifa ya Mandeleo 2025, Mkakati wa Kupunguza Umaskini, uainishaji wa masuala ya Jinsia na UKIMWI.

 

59.     Mheshimiwa Spika, Mafanikio yaliyopatikana katika sekta hii ni pamoja na kuongeza idadi ya wilaya zilizoingizwa kwenye Programu ya huduma ya uendeshaji wa pamoja wa tiba za magonjwa ya watoto kutoka wilaya 31 hadi 92; na kuongezeka kwa asilimia ya watoto waliopata chanjo kutoka 74 mwaka 2001 mpaka 79 mwaka 2002. Aidha, kutokana na janga la UKIMWI, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wamewezesha kuwepo kwa hospitali 110 zinazotoa ushauri nasaha. Kwa upande mwingine, Serikali kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali inaendeleza juhudi za upatikanaji wa madawa na vifaa vya matibabu katika vituo vyote vya kutoa tiba.

 

60.     Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2003/04 sekta ya afya itaanza kutekeleza mpango wa pili wa Mkakati wa Sekta ya Afya.  Mpango huu unalenga katika kuboresha utoaji wa huduma, na umuhimu utawekwa katika kukarabati vituo vya afya, kutoa tiba na kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wanapata kwa urahisi zaidi wa huduma za afya ya msingi.  Pia mkazo utaendelea kuwekwa kwenye kutoa huduma za mama, watoto na watu wasiojiweza pamoja na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza na milipuko.

 

UKUAJI WA SEKTA BINAFSI NA UWEKEZAJI

61.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002/03 Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Rasilimali imeendelea kuhamasisha na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kuzidi kujenga mazingira bora ya uwekezaji na kuboresha huduma mbali mbali kwa wawekezaji kwa mtindo wa “One stop Centre”.  Aidha katika kipindi cha mwaka 2002 Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji na kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) kilianzisha mpango maalumu wa kuwawezesha wawekezaji wa ndani (Domestic Investors Capacity Building) kuboresha nyaraka za mipango ya biashara (Bankable Business Plans) na kuinadi kwa wawekezaji wa ndani na nje ili waweze kupata aidha mikopo, wabia au teknolojia.  Kwa sasa zaidi ya miradi 60 ya wawekezaji wa ndani inatangazwa duniani kote kwa ajili hiyo.

 

62.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake ya kuwapatia wawekezaji ardhi kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 20 cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Kituo cha Uwekezaji na kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Makazi na Maendeleo Mijini kimeainisha ardhi inayofaa kwa uwekezaji.  Tayari ekari milioni 4 zimepatikana  na uhakiki wa aina ya umilikaji wa maeneo hayo unaendelea kufanywa na maafisa wa Serikali katika mikoa yote ya Tanzania bara.  Napenda kusisitiza ya kwamba hakuna Mtanzania atakayenyang’anywa ardhi ili apewe mgeni bali Mtanzania husika ndiye atakayeitumia ardhi hiyo kumwezesha kuwekeza.

 

63.     Mheshimiwa Spika, Aidha katika mwaka 2002 Kituo cha Uwekezaji kiliandikisha miradi 311 yenye thamani ya Sh. 1,024.5 milioni.  Kati ya miradi hiyo, 126 ni ya wawekezaji wa ndani, 104 ni ya wawekezaji wa nje, na 81 ni wawekezaji wabia.  Vile vile, katika kipindi hicho (2002) idadi ya wawekezaji waliohudumiwa kwa kupatiwa vibali mbali mbali ni 260 kwa masuala ya kodi, 243 kwa masuala ya uanzishaji makampuni na 214 leseni za biashara, 926 walipatiwa vibali vya kufanya kazi nchini (Resident Permit Class “B”), 976 walipatiwa vibali vya kuishi nchini na 61 kwa masuala ya ardhi.

 

64.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Mkakati wa kukuza ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi Serikali kwa mwaka 2002/03 ilishughulika na:-

 

65.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2002/2003, Serikali kwa kushauriana na sekta binafsi chini ya Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) imepitia sera na sheria mbalimbali za kibiashara na uwekezaji.  Masuala yaliyoshughulikiwa ni pamoja na:-

§         Kuandaa mapendekezo ya kurekebisha Sheria za Ardhi ili kurahisisha utolewaji wa mikopo;

§         Kuanzisha mfumo wa Hazina ya Ardhi (Land Bank) ili kukuza uwekezaji katika kilimo;

§         Kuhuisha Sheria za Ajira;

§         Kurekebisha mfumo wa kodi ili kuondoa adha ya utozaji wa kodi nyingi na kupunguza kero kwa wazalishaji; na,

§         Kupunguza urasimu katika kutoa leseni na kushirikisha sekta binafsi katika majadiliano ya mikataba ya kimataifa inayohusiana na biashara na uwekezaji.

 

66.     Mheshimiwa Spika, kiwango cha uwekezaji rasilimali kimeongezeka kutoka asilimia 14.8 ya Pato la Taifa mwaka 1997, na kufikia asilimia 17.4 mwaka 2002. Hata hivyo, uwekezaji rasilimali nchini bado ni mdogo ikilinganishwa na mahitaji ya ongezeko la haraka la ukuaji wa uchumi.  Uwiano unaohitajika wa uwekezaji akiba na Pato la Taifa kwa nchi changa kama Tanzania ili ipate kuendelea kwa kasi zaidi ni asilimia 25.  Kwa mwaka 2003, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na taratibu zitakazowezesha shughuli ndogo ndogo za uzalishaji na biashara zipate mikopo.

 

          Uwekaji Akiba

67.     Mheshimiwa Spika, licha ya ongezeko dogo la uwekezaji rasilimali nchini, bado maendeleo yetu kwa ujumla ni madogo kutokana na ukosefu wa utamaduni wa kujiwekea akiba. Uwiano kati ya uwekaji akiba nchini na Pato la Taifa kwa mwaka 2002 ni asilimia 11.1 tu, ambapo katika nchi nyingine kama  Kenya ni asilimia 17, Uganda asilimia 14.7, Nigeria na Afrika Kusini asilimia 18, Korea na China zaidi ya asilimia 30. Ni wajibu wetu Waheshimiwa Wabunge, kuhamasisha wananchi kwenye Majimbo yetu kujiwekea akiba na kuanzisha vitega uchumi vitakavyowawezesha kuondokana na umaskini.  Aidha ni wajibu wetu pia kuwahamasisha wananchi kujenga utamaduni na nidhamu katika kukopa, kutumia vizuri na kurejesha mikopo hiyo.

 

UREKEBISHAJI NA UBINAFSISHAJI WA MASHIRIKA YA UMMA

68.     Mheshimiwa Spika, hadi Machi 2003 mashirika ya umma yaliyobinafsishwa, yakijumuisha 47 yaliyopelekwa LART ni 266.  Kati ya mashirika hayo mashirika 134 yamenunuliwa na Watanzania kwa asilimia 100, mashirika 16 yamepata wawekezaji wa nje kwa asilimia 100 na mashirika 116 yamebinafsishwa kwa njia ya ubia kati ya wawekezaji wa nje na wawekezaji wa ndani. Mashirika 16 kati ya mashirika yaliyonunuliwa na Watanzania yamebinafsishwa kwa njia ya kuwauzia wafanyakazi wa mashirika husika. Hali kadhalika mali nyinginezo (Non-core-assets) 265 ziliuzwa.

 

69.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2002, kazi zaidi ilielekezwa katika kuandaa mikakati mbalimbali ya kubinafsisha au kurekebisha mashirika ya miundombinu na huduma yakiwemo DAWASA, ATC, TANESCO, THA, TRC, NIC na NMB.  Hadi Februari 2003 Serikali iliweza kubinafsisha shirika la Ndege la Tanzania (ATC) kwa njia ya ubia na DAWASA kwa njia ya ukodishaji.

 

70.     Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti mashirika makubwa yanayotoa huduma na ya miundombinu, Serikali imechukua hatua ya kuanzisha mamlaka nne za udhibiti: Mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji – EWURA, Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini - SUMATRA, Mamlaka ya udhibiti wa mawasiliano na utangazaji – TACRA, na Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa anga - TCAA.  Aidha, kwa mwaka 2003/04 Serikali itaendelea na ubinafsishaji wa mashirika makubwa ya huduma na miundombinu na mashamba makubwa ya kilimo na mifugo. Serikali pia itaendelea kufuatilia mashirika yaliyobinafishwa kuhakikisha kuwa mashirika hayo yanafanya kazi kwa ufanisi kulingana na mikataba ya mauzo.

 

          MASUALA MENGINEYO YA KITAIFA

Mkakati wa Kupunguza  Umaskini

71.     Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa takwimu na taarifa zilizotokana na tafiti za mapato na matumizi ya kaya (HBS 2000/01) na tafiti za nguvukazi (ILFS 2000/01) umebainisha kuwa hali ya umaskini wa kipato na maendeleo ya jamii (elimu, afya, maji, ajira, nyumba) haijabadilika sana.  Matokeo ya tafiti hizo yanaonyesha kuwa asilimia 19 ya watu wana umaskini uliokithiri (food poverty) mwaka 2000/01, ikilinganishwa na asilimia 22 mwaka 1991/92. Vile vile, asilimia 36 ya watu ni maskini kutokana na kukosa mahitaji muhimu (basic needs poverty) mwaka 2000/01 ikilinganishwa na asilimia 39 mwaka 1991/92.  Bado lindi la umaskini liko vijijini.  Aidha, tofauti ya kipato imeongezeka sana Dar es Salaam. Utekelezaji wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini umeanza kuonyesha mafanikio hasa katika sekta ya elimu na katika baadhi za viashirio katika sekta ya afya, maji mijini, na barabara vijijini.

72.     Mheshimiwa Spika, changamoto iliyoko mbele yetu katika suala zima la kupunguza umaskini ni:-

 

Idadi ya Watu na Maendeleo

73.     Mheshimiwa Spika, sensa ya watu na makazi ilifanyika kuanzia tarehe 25 Agosti 2002 hadi 4 Septemba 2002 kama ilivyopangwa.  Ripoti ya kwanza ya jumla ilitolewa rasmi mwezi wa Januari, 2003.  Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya jumla, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa na idadi ya watu wapatao 34.6 milioni iliyoongezeka kwa asilimia 2.9 kwa mwaka kati ya mwaka 1988 na 2002.  Katika jumla hiyo karibu watu 17.7 milioni ni wanawake na watu 16.9 milioni ni wanaume.  Aidha katika jumla yote watu milioni 33.6 walikuwapo Tanzania Bara (wakiwemo wanawake 17.2 milioni na wanaume 16.4) na watu 985,000 walikuwepo Tanzania Visiwani (wakiwemo wanawake 502,000 na wanaume 483,000).  Matokeo ya sensa pia yamedhihirisha kwamba Tanzania Visiwani ina kiwango kikubwa cha ukuaji wa idadi ya watu wa asilimia 3.1 kwa mwaka kuliko Tanzania bara ambayo kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu kilikuwa ni asilimia 2.9 kwa mwaka. 

 

74.     Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2002, kumetokana na ushirikiano wa hali ya juu pamoja na juhudi za viongozi wote kwenye ngazi mbali mbali za Serikali, taasisi, wafadhili na wananchi wote kwa jumla.  Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, Watanzania wote, na wafadhili wetu UNFPA, DFID, UNDP, USAID, SIDA, na Serikali ya Japan kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia zoezi la sensa.  Kwa mwaka 2003/04, Serikali itaendelea kukamilisha ripoti 11 zenye takwimu na taarifa mbali mbali za sensa na kuhakikisha kuwa zinawafikia watumiaji katika ngazi na nyanja mbali mbali.

 

Nguvukazi na Ajira

75.     Mheshimiwa Spika, matokeo ya Utafiti wa Nguvukazi wa mwaka 2000/01 yanaonyesha kuwa kati ya watu 17.8 milioni wenye uwezo wa kufanya kazi, walioajiriwa kwa tafsiri ya kitaifa walikuwa 15.5 milioni. Tafsiri hii inazingatia mazingira ya ajira katika Tanzania ambapo sehemu kubwa ya watu wanafanya kazi za kujiajiri badala ya kuajiriwa, na kazi nyingi ni za msimu kwenye sekta ya kilimo na sekta isiyo rasmi. Kati ya hao walioajiriwa, watu 13.0 milioni walikuwa katika kilimo cha asili, 0.9 milioni katika sekta isiyo rasmi, 0.6 milioni katika sekta binafsi, 0.5 milioni katika kazi za nyumbani, 0.4 milioni Serikalini na 0.1 milioni katika mashirika ya umma.

 

76.     Mheshimiwa Spika, watu wasio na kazi walikuwa 2.3 milioni, sawa na asilimia 12.9 kwa nchi nzima. Kati ya hao, wanawake walikuwa 1.3 milioni na wanaume 1.0 milioni. Karibu nusu ya wasiokuwa na kazi walikuwa wakiishi mijini. Katika Jiji la Dar es Salaam peke yake, asilimia 46.5 ya wenye uwezo wa kufanya kazi walikuwa hawana kazi, ambapo katika miji mingine ni asilimia 25.5 na vijijini asilimia 8.4. Pia, matokeo yameonyesha kuwa ukosefu wa ajira unawaathiri zaidi vijana wenye umri kati ya miaka 10 na 34. Kijinsia vijana wa kike ndio wanaoathirika zaidi kuliko wanaume.

 

77.     Mheshimiwa Spika, matokeo haya yanabainisha wazi kuwa sekta ya kilimo, sekta isiyo rasmi na sekta binafsi ndizo zinazoajiri watu wengi zaidi. Hivyo juhudi za Serikali zitaendelea kulenga katika kuboresha kilimo na kuwezesha uwekezaji katika viwanda vya kusindika mazao ili kuyaongezea thamani.  Aidha, Vyuo vya Majaribio ya Ufundi vitahimizwa kutoa mafunzo yanayohitajika katika soko la ajira.  Kwa kuwa viwanda vya nguo vina fursa ya kuajiri watu wengi, Serikali itaendelea kutoa motisha kwa viwanda kama hivyo vitakavyoajiri watu wengi.

 

 

 


JINSIA

78.     Mheshimiwa Spika, sensa ya watu na makazi ya mwezi Agosti/Septemba 2002 ilibainisha kwamba idadi ya wanawake nchini ni 17,156,905 sawa na asilimia 51.1 ya watu 33,584,607 waishio Tanzania Bara. Kwa kuzingatia mchango mkubwa unaotolewa na wanawake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo, Serikali ikishirikiana na taasisi isiyo ya kiserikali ya mtandao wa jinsia nchini (TGNP) katika mwaka 2002 ilishughulikia masuala yafuatayo:-

·        Kuhakikisha kwamba masuala ya jinsia yanazingatiwa katika utayarishaji na utekelezaji wa mipango na katika usimamizi wa uchumi katika ngazi zote;

·        Kutathimini idadi ya wanawake walio katika ngazi ya uongozi katika ngazi zote za wizara, mikoa na Serikali za mitaa kwa lengo la kuleta usawa; na,

·        Kutoa mafunzo kwa wanawake katika nyanja mbali mbali.

 

79.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi kijacho, Serikali ikishirikiana na taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya jinsia itaendelea na zoezi la kujenga uwezo wa kitaalam wa kuandaa, kuchambua na kutekeleza mipango kwa kuzingatia masuala ya jinsia katika ngazi mbalimbali.

 

 KUDHIBITI KUENEA KWA UKIMWI

80.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2002 idadi ya wananchi walioambukizwa, iliendelea kuongezeka na kufikia watu 2.2 milioni.  Idadi hii ni sawa na asilimia 6.5 ya wananchi wote. Kati ya idadi hiyo ya watu walioambukizwa, theluthi moja ambayo ni zaidi ya watu 700,000 tayari ni wagonjwa.  Kinachotisha zaidi ni kwamba kasi ya maambukizi hayo haijapungua kutoka ile ya mwaka jana ambayo ni asilimia 7 hadi 10 kwa maeneo ya mashambani na asilimia 20 hadi 24 katika sehemu za mijini. Takwimu zinazonyesha kwamba maambukizi mijini yako juu.  Mwaka 2002 pia umeshuhudia utekelezaji wa sera na Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI pamoja na kupanua mtandao wa wadau katika vita dhidi ya UKIMWI.

 

81.       Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2003/04 Serikali itaendelea kusisitiza na kulifanya suala la kupambana na UKIMWI kuwa agenda ya kudumu katika sehemu zote za kazi ili kupunguza athari ya kuangamia kwa nguvukazi nchini.

 

MATARAJIO KWA MWAKA 2003/04

Misingi na Malengo ya Mpango na Bajeti

 

82.     Mheshimiwa Spika, malengo ya uchumi jumla katika mwaka 2003/04 – 2005/06 yatakuwa kama ifuatavyo:-

·        Pato la Taifa halisi litakua kwa asilimia 6.3 mwaka 2003, asilimia 6.6 mwaka 2004, asilimia 7.0 mwaka 2005, na asilimia 7.4 mwaka 2006;

·        Kasi ya upandaji bei itapungua hadi asilimia 4.0 ifikapo Juni 2004 na baadaye kupungua kulingana na viwango vitakavyokuwepo katika nchi tunazofanya nazo biashara kubwa;

·        Kuongeza mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa kwa bei husika wa asilimia 13.2 mwaka 2003/04, asilimia 13.5 mwaka 2004/05 na asilimia 13.7 mwaka 2005/06;

·        Kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) litakalowiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na kasi ya upandaji bei; na

·        Kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje kwa kipindi kisichopungua miezi mitano.

 

SHABAHA NA MAENEO YATAKAYOPEWA KIPAUMBELE KATIKA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2003/04

 

83.     Mheshimiwa Spika, shabaha kuu ya mpango na bajeti ya mwaka 2003/04 ni kutekeleza Mkakati wa Kupunguza Umaskini, kuendeleza mafanikio ya uchumi jumla yaliyopatikana hadi sasa, kukuza sekta binafsi na kuimarisha Serikali za Mitaa kwa kuzipatia madaraka na rasilimali zaidi.  Ili kufikia malengo ya uchumi jumla na ya kisekta Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na:- 

·        Kukuza uzalishaji na uboreshaji huduma katika sekta za viwanda, madini, utalii na sekta isiyo rasmi;

·        Kutolegeza sera ya udhibiti wa ujazi wa fedha;

·        Kukuza na kuendeleza sekta binafsi ili iweze kuchangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa;

·        Kuweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa kuimarisha sera pamoja na taratibu mbalimbali; na

·        Kuwepo kwa mpango wa kusimamia na kutekeleza mkakati wa kuondoa umaskini katika ngazi ya Wilaya na kijiji.

 

84.     Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopewa kipaumbele katika Mpango na Bajeti ya Mwaka 2003/04 ni pamoja na:-

 

i)                   Kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha Miundombinu  Sekta zilizopewa kipaumbele ni:- Elimu, afya, maji, barabara na madaraja vijijini na huduma za ardhi;

 

ii)                 Kilimo

Mkazo umewekwa kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kufufua skimu za asili za kisasa za umwagiliaji wa wakulima wadogo wadogo na uvunaji wa maji ya mvua na kutekeleza kwa nguvu mikakati yote ya kuendeleza kilimo;

 

iii)               Mipango ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo

Hadi sasa malengo ya mikakati ya kitaifa kama vile Mkakati wa Kupunguza Umaskini, Mkakati wa Kuboresha Kilimo na Mkakati wa Maendeleo Vijijini haujaweza kutafsiriwa katika ngazi ya Wilaya.  Ili kuliwezesha Taifa kufikia malengo ya mikakati hiyo ambayo kwa kiwango kikubwa yanalenga katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini, Serikali imeona ni vyema kila wilaya kutayarisha na kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati utakaotungamanisha na kutafsiri malengo ya mikakati mbalimbali ya kitaifa katika ngazi ya wilaya;

 

iv)              Utawala Bora

Sheria, Mahakama, jinsia na vita dhidi ya rushwa; na,

 

v)                Ulinzi na Usalama

Hivi karibuni kumekuwepo na wimbi la uhalifu kwa kiwango cha kutishia amani na kuvuruga jitihada za kuleta maendeleo nchini. Katika kukabiliana na hali hii, Serikali imeandaa mikakati inayolenga katika kuhamasisha wananchi na kuimarisha vyombo vya ulinzi katika vita dhidi ya uhalifu.

 

MAJUMUISHO

85.     Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kusisitiza kwamba licha ya dalili kadhaa za mafanikio kuonekana kama vile: uchumi wetu kukua kwa asilimia 6.2 katika mwaka 2002; kasi ya upandaji bei kushuka hadi kufikia asilimia 4.3; akiba ya fedha zetu za kigeni kuongezeka na kutosha kulipia bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita; na kiwango cha uwekezaji rasilimali kuongezeka na kufikia asilimia 17.4 ya Pato la Taifa mwaka 2002; bado uchumi unakabiliwa na changamoto na matatizo mbali mbali ambayo hatuna budi kuyatatua.  Matatizo yanayokabili uchumi wetu hivi sasa ni pamoja na Bajeti tegemezi, umaskini vijijini na mijini, ukosefu wa utamaduni wa kujiwekea akiba, uwekezaji mdogo wa rasilimali, ukosefu wa ajira, miundombinu hafifu na huduma duni za kijamii.

 

86.     Mheshimiwa Spika, ili tuweze kuondokana na matatizo niliyoyataja, hatuna budi kutekeleza yafuatayo:-

 

(i)      Kubaini fursa zote za kuongeza ukusanyaji wa aina mbalimbali za mapato katika ngazi zote ili kupunguza utegemezi na kutuwezesha kugharamia maendeleo yetu wenyewe kwa kiasi kikubwa;

 

(ii)      Kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo yetu. Hivyo, Taifa, kila kijiji, kata, tarafa, Wilaya hadi ngazi ya mkoa, walenge katika kubainisha yale wanayoweza kuyafanya kwa kutumia fursa na rasilimali zilizoko katika maeneo yao;

 

(iii)     Kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba ambayo itawezesha wananchi kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kuzalisha mali na kutoa huduma. Suala la uhamasishaji wa wananchi kujiwekea akiba ni la msingi;

 

(iv)     Kuelekeza juhudi katika kujenga na kuendeleza shughuli ndogo ndogo za uzalishaji na biashara zinazojumuisha usindikaji wa bidhaa asilia, viwanda vidogo na vya kati na utoaji wa huduma mbalimbali.  Ili kufanikisha azma hii, hapana budi kuanzishwa vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali, kuvisaidia kupata mikopo na kujenga na kuendeleza ujasirimali;

 

(v)      Kuboresha mazingira ya uwekezaji wa sekta binafsi wa ndani na nje pamoja na kuweka mkakati thabiti wa kuuza nje bidhaa zilizosindikwa na zisizo asilia kwa kutumia fursa zote zilizopo kama vile AGOA, EBA na New Canadian Initiative ; na,

 

(vi)     Serikali itaendelea na utaratibu wa kuboresha mfumo wa ushuru na kodi mbali mbali kwa Wakulima Vijijini ili kuwaondolea kero na usumbufu ili wajizatiti zaidi katika uzalishaji na kuongeza viwango vya ubora ili kuongeza viwango vya mapato yao.

 

87.     Mheshimiwa Spika, kama Waheshimiwa Wabunge wajuavyo, azma ya Serikali ni kujenga na kudumisha ushirikiano mzuri na wenye manufaa kwa maendeleo ya Taifa letu na nchi zote pamoja na mashirika na taasisi za kimataifa.  Zipo nchi, mashirika na taasisi za kimataifa ambazo tumeendelea kushirikiana nazo na zinastahili pongezi zetu.  Hivyo, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wote walioshirikiana nasi na kutusaidia.  Baadhi ya nchi na mashirika ya kimataifa yanayostahili pongezi zetu ni pamoja na:- Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Mashirika mbali mbali ya Umoja wa Mataifa kama vile UNDP, UNESCO, UNFPA, UNHCR, UNICEF, UNIFEM, FAO, IFAD, WFP na WHO, Jumuiya ya nchi za Ulaya (EU), mfuko wa fedha wa nchi wanachama wa uzalishaji mafuta (OPEC Fund), Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD), Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), Shirika la Maendeleo la Finland (FINNIDA), Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA), Shirika la Maendeleo la Japan, Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Serikali za Uswisi, Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Hispania, China, Afrika ya Kusini, Japan, Kuwait, Italia, Ireland na nchi nyingine marafiki na mashirika mbali mbali ya Kimataifa yasiyo ya kiserikali (NGOs).  Tumeendelea kupata mchango mkubwa sana katika maendeleo yetu kutoka nchi hizo na mashirika hayo.  Napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa nchi Wahisani na mashirika na taasisi mbali mbali za kimataifa zinazotusaidia katika harakati zetu za maendeleo.  Tunawaomba waendelee kushirikiana nasi na kutusaidia katika juhudi zetu za kujenga uchumi imara na kuboresha maisha na maendeleo ya wananchi wetu.  Aidha, mashirika hayo na nchi hizo, zinakubaliana na azma yetu na dhana ya kujenga national capacity and local ownership katika uandaaji sera, mipango, mikakati na miradi.  Napenda pia nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ushauri na ushirikiano wao wanaoendelea kutupatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji.

 

88.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.

 

 


Jedwali Na. 1: Mwenendo kwa Baadhi ya Vigezo vya  Kiuchumi

Vigezo

1995

1996

1997

1998

1999

2000

2001

2002

Ukuaji Halisi wa Pato la Taifa (%)

3.6

4.2

3.3

4.0

4.7

4.9

5.7

   6.2

Mfumuko wa bei 

27.1

21.0

16.1

12.9

7.8

6.0

5.2

    4.5

Kiwango cha wastani cha kubadilisha Sh/Dola

574.8

580.0

612.1

664.7

744.8

808.4

876.4

978.9

Mauzo ya nje ya  bidhaa (mil. US$) 

682.9

763.8

752.6

588.5

543.3

663.3

776.4

877.0

Uagizaji wa bidhaa (mil. US$) 

1340.5

1212.6

1148.0

1382.2

1497.9

1366.3

1560.5

1506.5

Uwiano wa mauzo nje/ uagizaji bidhaa (%)

50.9

63.0

65.6

42.6

39.7

49.6

52.0

58.7

Uwiano wa uwekezaji rasilimali /Pato la Taifa (%)

19.7

16.5

14.7

16.0

15.4

17.5

17.2

-

Akiba ya fedha za kigeni (Miezi ya Uagizaji Bidhaa)

1.6

2.4

3.8

3.0

4.1

5.6

6.3

8.9

 

1995/96

1996/97

1997/98

1998/99

1999/00

2000/01

2001/02

2002/03

Nakisi ya Bajeti kabla ya ruzuku (% Pato la Taifa)

0.1

-1.7

-2.3

-2.3

-5.8

-4.6

-6.6

 

Wastani wa riba za Amana za akiba

12.0

11.0

10.0

7.9

7.1

4.2

3.5

3.1

Wastani wa riba za mikopo

28.0

26.5

24.0

24.5

22.1

19.6

16.4

15. 7

 

Chanzo: Ofisi ya Rais, Mipango na ubinafsishaji; Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania

 

 


Jedwali Na 2: Ukuaji Halisi wa Pato la Taifa Kisekta na Malengo 1996 – 2006

 

Sekta

1996

Halisi

1997

Halisi

1998

Halisi

1999

Halisi

2000

Halisi

2001

Halisi

Kilimo

3.9 %

2.4 %

1.9 %

4.1 %

3.4 %

5.5 %

Uchimbaji wa Madini na mawe

9.6 %

17.1 %

27.4 %

9.1 %

13.9 %

13.5 %

Bidhaa za Viwandani

4.8 %

5.0 %

8.0 %

3.6 %

4.8 %

5.0 %

Umeme na Maji

11.1 %

2.2 %

5.5 %

3.9 %

5.9 %

3.0 %

Ujenzi

7.6 %

35.5 %

-12.3 %

8.7 %

8.4 %

8.7 %

Biashara , Uuzaji Jumla, Rejareja na Mahoteli

3.5 %

5.0 %

4.7 %

6.0 %

6.5 %

6.7 %

Mawasiliano na Uchukuzi

1.1 %

-16.1 %

32.8 %

5.8 %

6.1 %

6.3 %

Fedha, Bima na Huduma za Kibiashara

0.4 %

7.7 %

5.6 %

4.1 %

4.7 %

3.3 %

Uendeshaji Serikali na Huduma Nyingine

1.6 %

3.2 %

2.7 %

3.5 %

3.6 %

3.5 %

Ukuaji wa Pato la Taifa kwa mwaka unaohusika

4.2 %

3.3 %

4.0 %

4.7 %

4.9 %

5.7 %

Mwaka wa Fedha

1995/96

1996/97

1997/98

1998/99

1999/00

2000/01

Ukuaji wa Pato la Taifa kwa Mwaka wa Fedha

3.9%

3.7%

3.7%

4.4%

4.8%

5.3%

Ukuaji wa Pato la Taifa kwa Mwaka wa Fedha

3.9%

3.7%

3.7%

4.4%

4.8%

5.3%

 

Linaendelea


Jedwali Na 2: Ukuaji Halisi wa Pato la Taifa Kisekta na Malengo 1996 – 2006 – (linaendelea)

Sekta

2002

Halisi

2003

Malengo

2004

Malengo

2005

Malengo

2006

Malengo

Kilimo

5.0 %

5.3 %

5.5 %

5.4 %

5.7 %

Uchimbaji wa Madini na mawe

15.0 %

11.1 %

10.2 %

9.6 %

9.5 %

Bidhaa za Viwandani

8.0 %

6.9 %

7.1 %

8.1 %

9.0 %

Umeme na Maji

3.1 %

6.9 %

7.1 %

8.1 %

7.9 %

Ujenzi

11.0 %

4.8 %

5.3 %

6.7 %

8.0 %

Biashara , Uuzaji Jumla, Rejareja na Mahoteli

7.0 %

8.9 %

9.6 %

10.4 %

10.8 %

Mawasiliano na Uchukuzi

6.4 %

7.9 %

8.3 %

9.2 %

9.9 %

Fedha, Bima na Huduma za Kibiashara

4.8 %

6.3 %

6.6 %

7.0 %

7.4 %

Uendeshaji Serikali na Huduma Nyingine

4.1 %

4.1 %

4.2 %

4.2 %

4.6 %

Ukuaji wa Pato la Taifa kwa mwaka unaohusika

6.2 %

6.3 %

6.6 %

7.0 %

7.4 %

Mwaka wa Fedha

2001/02

2002/03

2003/04

2004/05

2005/06

Ukuaji wa Pato la Taifa kwa Mwaka wa Fedha

6.0%

6.1%

6.5%

6.8%

7.2%

 

Chanzo:  Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ofisi ya Rais Mipango na Ubinafsishaji

 

 

 


Jedwali  3:  Thamani ya bdhaa za asili na zisizo za asili zilizouzwa  nje ya nchi

 

Bidhaa

1999

2000

2001

2002

Badiliko 2001/02

Bidhaa Asilia

 

 

 

 

 

 

Kahawa

76.63

83.7

57.05

35.14

-38.4%

Pamba

28.46

38

33.7

28.15

-16.5%

Katani

7.26

5.6

6.68

6.65

-0.4%

Chai

24.65

32.7

29.03

29.35

1.1%

Tumbaku

43.44

38.4

35.69

50.50

41.5%

Korosho

100.89

84.4

56.58

46.26

-18.2%

Karafuu

19.86

10

12.32

5.40

-56.2%

Jumla ndogo ya Bidhaa asilia

301.18

292.8

231.05

201.46

-12.8%

Bidhaa zisizo asilia

 

 

 

 

 

Madini

73.26

178.2

302.23

372.78

23.3%

Bidhaa za Viwandani

30.05

43.4

56.17

67.10

19.5%

Samaki na Bidhaa zake

56.75

76.3

96.77

116.76

20.7%

Mazao ya mboga na Maua

8.88

9.7

11.01

10.86

-1.4%

Bidhaa nyinginezo

72.74

62.9

79.34

108.09

36.2%

Jumla ndogo ya bidhaa zisizo Asilia

241.67

370.5

545.52

675.58

23.8%

Jumla ya Mauzo ya Bidhaa Nje

542.85

663.3

776.37

877.04

12.9%

 

 

Chanzo: Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji

 


Jedwali Na. 4. Mizania ya Malipo na Nchi za Nje

USD  mill.

 

1995

1996

1997

1998

1999

2000

2001

2002

 

Halisi

Halisi

Halisi

Halisi

Halisi

Halisi

Halisi

Makisio

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Urari wa biashara

-657.6

-448.8

-395.4

-793.7

-954.6

-703.1

-784.1

-629.46

     Bidhaa zilizouzwa

682.9

763.8

752.6

588.5

543.3

663.2

776.4

877.04

     Bidhaa zilizonunuliwa

1340.5

1212.6

1148.0

1382.2

1497.9

1366.3

1560.5

1506.5

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Urari wa Huduma

-216.9

-278.8

-317.9

-463.1

-158