·
Kamishna Mkuu wa Magereza,
·
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya,
·
Mkuu wa Chuo,
·
Maafisa wa Majeshi mbalimbali,
·
Wahitimu wa Mafunzo,
·
Wageni Waalikwa,
·
Mabibi na
Mabwana.
Napenda kuchukua
fursa hii pia kuishukuru Jumuiya ya Chuo hiki kwa
ujumla kwa niaba ya waalikwa wote, kwa mapokezi mazuri tuliyoyapata tangu
tulipowasili hapa.
Aidha, napenda kuchukua fursa hii
kutoa shukrani na pongezi kwa wale wote waliohusika katika maonesho
mbali mbali yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha shughuli hii ya leo,
ikiwa ni pamoja na gwaride rasmi la kuhitimisha mafunzo, onesho la Watoto wa
Kituo cha Malezi, Kwaya, Brass Band, Shairi na Taarab. Mambo hayo yote yamefanywa kwa
ustadi mkubwa na kudhihirisha kwamba kulikuwepo na jitihada za hali ya juu
katika maandalizi ya shughuli hii ya leo.
Nawapongeza
Kabla ya kutekeleza jukumu lililonileta hapa la kuyafunga rasmi mafunzo
haya, napenda nizungumze machache kwa Wahitimu.
Suala hili la mafunzo endelevu kazini baada ya Mafunzo ya Awali lina
umuhimu wa pekee kwa chombo hiki kwa sababu, kazi ya
kuwatunza binadamu ni kazi inayohitaji maamuzi ya busara yanayozingatia mchanganyiko
wa sheria, taratibu na hali halisi inayojitokeza kwa wakati husika. Katika hali hii, ujuzi na
uzoefu wa muda mrefu ni hazina kubwa
Pamoja na suala hili la mafunzo endelevu,
napenda pia niwaase wahitimu kuhusu umuhimu wa kujiendeleza katika taaluma
nyingine zenye manufaa kwenye Jeshi hili.
Ni vyema muelewe kwamba, Jeshi hili linahitaji wasomi wa
taaluma mbali mbali ili kufanikisha majukumu yake kisayansi zaidi siku hadi
siku. Kwa sababu hii, mnayo fursa ya kujiendeleza katika nyanja
zinazohitajika Jeshini, hususan baada ya kukamilisha muda wa mwaka mmoja wa
kujijengea ujuzi wa kazi za msingi za Jeshi hili. Natoa wito kwenu kuhakikisha mnaitumia vyema
fursa hii ili mjihakikishie maendeleo kazini katika zama
hizi za sayansi na teknolojia.
Msibweteke na ajira hii mliyoipata na kusahau
kujiendeleza.
Jambo la pili ambalo ni vema mkalizingatia ni kuhusu
mwelekeo wa sasa wa kijamii na kisiasa nchini na duniani kote na jinsi
unavyoingiliana na shughuli za Jeshi lenu.
Nyote mnafahamu kwamba, ajenda za sasa duniani kote zimeegemea kwenye
utawala wa sheria, haki za binadamu na uendeshaji wa
shughuli za Serikali kwa uwazi na ukweli.
Mwelekeo huu umesababisha watu kutambua zaidi haki na
wajibu wao na hivyo kuleta hali ya uwajibikaji zaidi katika kazi za umma. Nyote mnafahamu pia kwamba vyombo vya
usimamizi na utekelezaji wa sheria yaani Polisi,
Mahakama na Magereza ndivyo vyenye nafasi kubwa zaidi katika kulinda na
kudumisha usalama katika jamii.
Ni kutokana na ukweli huu ninawajibika kuwaonya
kuhusu athari za kutozingatia kikamilifu sheria na taratibu za kazi wakati wote
na mahali popote mara mtakapofika kwenye vituo vyenu vya kazi. Napenda ieleweke kwenu na kwa watumishi
wengine wote kwamba, mnawajibika kufanya kazi zenu kwa kuzingatia sheria na
taratibu zilizopo na kwamba unyanyasaji wa wafungwa au ukiukaji wa maadili ya
kazi kwa njia yoyote ile ni marufuku.
Katika kuimarisha uwezo wa Jeshi hili wa
kuzingatia hali halisi iliyopo, Serikali ililiwezesha Jeshi kufanya kazi ya
kuziboresha kanuni za kudumu za Magereza, yaani “Prisons Standing Orders” ambazo ndizo mwongozo wa shughuli za kila
siku magerezani, vyuoni na kwenye ofisi zote za Magereza nchini. Kazi hii ilifanywa na
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP). Serikali inaamini kwamba, toleo jipya la “Prisons Standing Orders” ambalo ndilo
lilitumika kuendesha mafunzo haya yanayomalizika leo, litasaidia
katika kuliweka Jeshi hili kwenye mwelekeo mzuri zaidi kulingana na wakati
tulionao sasa.
Katika jitihada hizo hizo za kuboresha huduma za Jeshi hili serikali
imesimamia utolewaji wa chapisho la “Code of Conduct for Prisons Officers”
ambalo licha ya kuwekwa ndani ya “Prisons
Standing Orders”, limetolewa pia kwenye vijitabu vidogo vidogo
vinavyogawiwa kwa kila askari nchini.
Kijitabu hiki ni maelekezo mahsusi ya maadili
yanayopaswa kufuatwa na Askari Magereza ndani na nje ya kazi ili kumwezesha
kila askari kufanya rejea ya haraka pale anapohitaji kupata ufumbuzi kwa jambo
lolote. Nadhani ni
vyema nieleze hapa kwamba katika “Code
of Conduct for Prisons Officers” msisitizo mkubwa umewekwa
kuhusu uzito wa kosa la Trafficking,
yaani mahusiano yasiyostahili baina ya askari na mfungwa, ambao kimsingi ni
rushwa. Imeelezwa wazi kuwa askari
anapotenda kosa la Trafficking ni kwamba amesaliti kiapo chake cha uaminifu na utii moja
kwa moja.
Hatua hizi za serikali za kusimamia uboreshaji wa PSO na uchapishaji wa “Code
of Conduct for Prisons Officers” ni sehemu tu ya mpango kabambe wa serikali
wa kuimarisha utoaji huduma wa Jeshi la Magereza, pamoja na taasisi nyingine za
usimamizi na utekelezaji wa sheria hapa nchini, yaani Mahakama, Polisi na
Magereza. Katika mpango huo kwa upande wa Magereza, serikali tayari imekwishafanya tathmini
ya mahitaji ya Jeshi hili katika kuliwezesha kutekeleza majukumu yake kulingana
na viwango vinavyokubalika kimataifa.
Tathmini hiyo ilifanywa na wataalam wa
kimataifa walioteuliwa na Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la Mpango wa
Maendeleo (UNDP) na tayari baadhi ya
mapendekezo yaliyotolewa kwenye tathmini hiyo yameanza kutekelezwa na yako
katika hatua mbalimbali.
Mojawapo ya mapendekezo hayo ni umuhimu wa
Jeshi hili kuunda upya mfumo wake wa mafunzo ya watumishi na kuboresha vyuo
vyake, ili hatimaye kuwe na watumishi wenye uwezo unaotambulika kote duniani na
pia kuwa na vyeti vinavyokubalika kote duniani.
Tayari Jeshi limekwishaunda upya mfumo wa
Mafunzo ya Awali kwa kushirikiana na wataalam kutoka Kitivo cha Sheria, Chuo
Kikuu cha D’Salaam na Taasisi ya Technikon ya Afrika Kusini. Jitihada zinaendelea ili
mafunzo ya uongozi ya madaraja yote nayo yapitiwe upya. Tunategemea Jeshi hili litakuwa na watumishi wenye elimu ya ngazi ya vyeti (Certificates), Diploma na Shahada za
ngazi mbalimbali, katika taaluma ya “Correctional
Services”. Zote hizo zitatolewa hapa
nchini na kutambulika duniani kote.
Yapo mambo mengi katika mapendekezo hayo ya kuboresha hali ya Jeshi hili
lakini nadhani hili la uboreshaji wa mfumo wa mafunzo
na viwango vya taaluma kwa watumishi ndilo lenye umuhimu wa kuzungumziwa
hapa. Ni matumaini yangu kwamba mtakuwa
mmepata dira ya mwelekeo wa kazi hii mliyoamua wenyewe
kujiunga nayo. Kwa ufupi tu ni kwamba, katika muda mfupi ujao taaluma hii ya “Correctional Service” kwa hapa nchini
itapata hadhi ya kutambulika kimataifa na hivyo kuwapeni fursa za kuweza
kujinadi pale Umoja wa Mataifa unapotangaza nafasi za vikosi vya kulinda
usalama maeneo mbalimbali duniani. Vile
vile mtaweza kwenda kokote duniani na kuweza kupata
ajira kwa taaluma hii. Hii ni changamoto ambayo mnapaswa kuifanyia kazi tangu sasa kwa
kuzingatia nidhamu, uadilifu na ari ya kujiendeleza.
Napenda kutumia fursa hii pia kuzungumzia machache kuhusu matatizo
yaliyopo hapa chuoni
Serikali inatambua ukweli kwamba chuo hiki bado kipo katika ujenzi na hakijakamilika.
Shughuli za ujenzi wa chuo hiki zilikumbwa na
tatizo la kutokuwepo kwa fungu la maendeleo (yaani Development Fund) katika bajeti ya Jeshi la Magereza na hivyo kusimama
kwa muda mrefu. Kwa hali hiyo napenda
kuwathibitishia kwamba, serikali inafahamu kikamilifu upungufu uliopo chuoni
hapa na kuwa ina lengo la kuhakikisha kwamba, chuo
hiki kinakamilishwa kwa hadhi inayostahili utekelezaji wa majukumu yake
ipasavyo siku za usoni. Kwa kuwa tayari
Serikali imekwisharudisha fungu la maendeleo, utekelezaji wa
lengo
Ndugu Wahitimu, Mabibi na Mabwana, narudia tena
kuwapongeza kwa kufanikiwa kwenu kumaliza mafunzo haya salama na pia kuwapa
hongera wale wote waliofikia kutunukiwa tuzo za ubora katika maeneo mbali
mbali.
Baada ya kusema hayo, ninayo furaha kutamka kwamba Kozi
hii Namba 18 ya Mafunzo ya Awali ya Askari Magereza imefungwa rasmi.
Ahsanteni.