HOTUBA YA MGENI RASMI, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI MHE. OMAR RAMADHAN MAPURI KWENYE SHEREHE YA KUADHIMISHA SIKU YA SILAHA UMOJA WA MATAIFA ‘UN ARMS DAY’ ITAKAYOFANYIKA VIWANJA VYA JANGWANI TAREHE 09/07/2004

 

 

·       Waheshimiwa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao katika maadhimisho haya.

 

·       Mheshimiwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa UNDP nchini Mhe. John Hendra.

 

·       Kamishna wa Polisi, Laurean Tibasana.

 

·       Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya kuratibu na kudhibiti silaha na Wajumbe wa Kamati ya kuratibu na kudhibiti silaha Mkoa wa Dar es Salaam.

 

·       Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la CEPEDE, Bw. Emanuel Mallya na Viongozi wa NGO zinazoshiriki.

 

·       Wawakilishi wa vyombo vya habari waliopo.

 

·       Washiriki wengine wote.

 

·       Mabibi na Mabwana.

 

 

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya wananchi wote kuwashukuru waandaaji wa sherehe hii muhimu ya kimataifa ya kuadhimisha Siku ya Silaha ya Umoja wa Mataifa (UN Arms Day) kwa uamuzi wao wa kuadhimisha siku hiyo hapa Mkoani Dar es Salaam.  Vile vile ninapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru waandaaji wa maadhimisho haya kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuwa Mgeni rasmi katika sherehe hizi.  Kwa hayo yote, nasema ahsanteni sana.

 

Uamuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi, asasi zisizo za kiserikali, wananchi na Serikali kwa ujumla wa kuamua kuadhimisha Siku ya Silaha ya Umoja wa Mataifa ni wa busara, hasa ukizingatiwa kuwa tatizo la uzagaaji wa silaha ndogo unaleta maafa na kuathiri shughuli za maendeleo kwa wananchi wetu kwa kiasi kikubwa.  Ni kweli kabisa kwamba hali ya uhalifu unaotokana na uzagaaji wa silaha ndogo ilivyo humu nchini mwetu haiwezi kulinganishwa na hali ilivyo kwenye baadhi ya nchi zinazotuzunguka zenye migogoro na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na hata kusababisha wakimbizi wengi kuingia nchini mwetu na silaha.  Lakini ukweli huo hauwezi kutupa faraja kutokana na fadhaa inayowapata Watanzania kila yanapotokea matukio ya uhalifu wa kutumia silaha.  Matukio mengi ya uhalifu kama vile kupatikana na silaha, unyang’anyi wa kutumia silaha, mauaji, shughuli za maendeleo ya wananchi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa jumla.  Tunaelewa kuwa silaha nyingi zilizoko kwenye mzunguko usio halali zimeingizwa nchini na wakimbizi; lakini vile vile vipo vyanzo vya silaha haramu humu humu nchini kama vile silaha zinazoibiwa kutoka mikononi mwa wamiliki halali.  Chanzo chengine ni utengenezaji haramu wa magobore.

 

Silaha hizi haramu ambazo zimo mikononi mwa majambazi zinaleta madhara makubwa kwa wananchi wetu na hivyo hazina budi kudhibitiwa.  Kumbukumbu zinaonyesha kwamba silaha nyingi haramu bado zimo mikononi mwa wahalifu.  Kwa mfano, takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2003, jumla ya silaha haramu 850 zilikamatwa nchini na watuhumiwa 838 walikamatwa, ambapo katika mkoa wa Dar es Salaam pekee zilikamatwa silaha 76 na watuhumiwa 89.  Kwa mwaka huu toka mwezi Januari hadi Mei, 2004 mkoani Dar es Salaam, jumla ya silaha 6 zilikamatwa sambamba na watuhumiwa 7.  Jumla ya silaha 71 ziliibiwa nchini katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2003, ambapo watuhumiwa 59 walikamatwa.  Kwa Dar es Salaam peke yake katika kipindi hicho, jumla ya silaha 21 ziliibiwa na idadi ya watuhumiwa waliokamatwa ni 16.

 

 

Ndugu washiriki wa sherehe hizi,

 

Matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha nayo bado ni mengi.  Matukio haya mbali ya kuleta maafa kwa wananchi wasio na hatia, pia yanasababisha uporaji wa mali na fedha za wananchi.  Nitatoa mfano vile vile wa mwaka 2003 ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kulikuwa na matukio 1,111 ya unyang’anyi wa kutumia silaha nchini ambapo mali yenye thamani ya Tshs.2,672,409,416 iliporwa na watuhumiwa 1,092 kukamatwa.  Kwa jitihada zilizofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na raia wema mali yenye thamani ya Tshs.285,892,718 kati ya hizo iliweza kuokolewa.

 

Matukio haya ya unyang’anyi wa kutumia silaha mbali na kwamba yanatokea katika mikoa mingine nchini, lakini ninasema kuwa mkoa wa Dar es Salaam unaongoza.  Hii inatokana na shughuli nyingi za kiuchumi zinazofanywa hapa Dar es Salaam.  Mfano katika kipindi cha kuanzia mwaka Januari hadi Mei 2004 takwimu zinaonyesha kuwa matukio yaliyotolewa taarifa Polisi ya unyang’anyi wa kutumia silaha mkoani Dar es Salaam ni 69 ambapo watuhumiwa 79 wamekamatwa na thamani ya mali iliyoporwa ni Tshs.138,048,100.

 

Ndugu washiriki wa sherehe hizi,

 

Hayo ni baadhi tu ya madhara yaletwayo na uzagaaji holela wa silaha ndogo nchini.  Kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa tatizo hili linapatiwa ufumbuzi.  Umefika wakati sasa kwa jamii na wananchi kwa jumla watambue kuwa jukumu la kukabiliana na hatimaye kutokomeza tatizo la uzagaaji na matumizi mabaya ya silaha si jukumu la Jeshi la Polisi pekee, bali jamii nayo inawajibika.

 

Waathirika wakubwa wa matukio mengi ya uhalifu utokanao na matumizi mabaya ya silaha ni raia wa kawaida tu.  Kwa hali hiyo wananchi wanapashwa kutoa ushirikiano na sio kuliachia Jeshi la Polisi.  Tunafahamu uwezo wa Jeshi hili ni mdogo kwa idadi ya watumishi wake, pamoja na vitendea kazi vyake duni ukilinganisha na idadi ya wananchi na ukubwa wa nchi yetu, hivyo hatuna budi kwa ujumla wetu kulisaidia Jeshi hili kukabili uhalifu nchini na hili naomba nilisisitize sana.  Pamoja na wito huo lakini, sina budi niwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao ambao sasa wanaonekana kuutoa kwa Jeshi la Polisi hivi siku za karibuni.  Lakini wapo wanaojitoa muhanga kukabiliana na wahalifu wakiwemo majambazi.  Matokeo ya ushirikiano huo wa wananchi ni kwamba sasa uhakika ni mkubwa wa kukamatwa kwa wahalifu kila linapotokea tukio la uhalifu.  Hata silaha zinazokamatwa, zinapatikana kutokana na taarifa za wananchi.

 

Napenda kutoa wito maalumu kwa waganga wa kienyeji waache kusaidia kisaikolojia wahalifu eti kuzindika silaha zao au kuwapa imani kwamba eti hawatoweza kuonekana watapokuwa wakifanya uhalifu.  Huo si aina ya uganga wa kienyeji tunaoutaka kwani unachochea uhalifu.  Nawaomba waganga hao kwamba wanapoendewa na wahalifu, watafute njia ya kuwaripoti Polisi.

 

Ndugu washiriki,

 

Kuna mipango ambayo inaandaliwa na Jeshi la Polisi kuhusisha wananchi hasa kwenye ngazi za kata, vijiji na serikali za mitaa ili kutoa mafunzo kwa askari mgambo, sungusungu na vikundi vingine vya ulinzi ili kufanyike operesheni za pamoja kwa kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali.  Vikundi hivi vya ulinzi pamoja na asasi zisizo za kiserikali baada ya kupewa mafunzo hayo ya awali watakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kushirikiana na vyombo vyetu vya dola katika kuwafichua wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na hatimaye kuwafikisha katika vyombo vya sheria.  Mkakati huo unaoandaliwa na Jeshi la Polisi ninauunga mkono na nina hakika kwa kufanya hivyo tutaweza kuboresha hali ya usalama wa nchi yetu.

 

-                     Kwa kuzishirikisha asasi zisizo za kiserikali ambazo zina nafasi kubwa ya kuwafikia wananchi wa kawaida walio wengi katika maeneo yao ya vijiji, tarafa, kata, wilaya na hatimaye mkoa nina uhakika Jeshi la Polisi litapata taarifa sahihi za majambazi yanayotumia silaha na yanayotuletea matatizo kila siku.

 

-                     Asasi hizi zisizo za kiserikali vile vile zinaweza kusaidia kutoa elimu kwa jamii ili jamii na wananchi kwa ujumla watambue kuwa jukumu la kukabiliana na uzagaaji na matumizi mabaya ya silaha si la Jeshi la Polisi pekee, bali nao wana nafasi kubwa ya kusaidia.

 

-                     Asasi zisizo za kiserikali vile vile zinaweza kusaidia kuanzisha au kuendeleza shughuli mbadala za kiuchumi ili kuweza kuwasaidia wale wachache wenye fikra potofu za kutegemea kufanya uhalifu waweze kuungana katika vikundi na kufanya shughuli za maendeleo.

 

-                     Tunategemea asasi zisizo za kiserikali kufanya harambee ya kuchangisha fedha zitakazosaidia kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kuratibu na Kudhibiti Silaha, hususani wakati wa kufanya operesheni za pamoja za kukamata silaha na wahalifu.

 

Ndugu washiriki nisingependa kuwachosha kwa kusema mengi, ila napenda kumalizia kwa kuwakumbusha kuwa maadhimisho haya yanalenga katika kutukumbusha sote madhara ya uzagaaji na matumizi mabaya ya silaha ndogo, na hivyo tuungane kwa pamoja ili tudhibiti na hatimaye kutokomeza kabisa tatizo hili.

 

Ninamalizia kwa kutoa wito kwa wananchi wote kwa ujumla kuendelea kushirikiana na vyombo vyetu vya dola ili nchi yetu na Ulimwengu kwa ujumla tuwe kwenye amani na utulivu.

 

Ahsanteni kwa kunisikiliza