TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

UFAFANUZI KUHUSU AMRI YA KUPIGA MARUFUKU VYAMA VYA SIASA KUENDESHA MAFUNZO YA JUDO NA KARATE

 

1.                 Tarehe 25/3/2004 katika mkutano na waandishi wa habari huko Zanzibar, Mheshimiwa Capt. (Mst.) John Chiligati (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alitangaza amri ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya kupiga marufuku vyama vya siasa kuendesha mafunzo ya judo na karate.  Toka wakati huo Chama cha CUF kimekuwa kikitoa kauli kupitia taarifa kwa vyombo vya habari na hotuba za baadhi ya viongozi wake kwenye mikutano ya hadhara zikikejeli na kubeza tangazo hilo na kujaribu kuonyesha kana kwamba tangazo hilo lilikuwa la Mheshimiwa Chiligati mwenyewe tu na kwamba eti lilipingana na amri ya Waziri mwenyewe wa Mambo ya Ndani ya Nchi, yaani mimi.

 

2.                 Napenda kuthibitisha kwamba amri iliyotangazwa na Mheshimiwa Chiligati ni amri yangu ambayo niliitoa kimaandishi kwa Jeshi la Polisi toka tarehe 19/3/2004.  Ingawa amri hiyo inazungumzia vyama vya siasa kwa jumla, lakini niliitoa baada ya kupata taarifa kwamba Chama cha CUF kilikuwa kinayatumia mafunzo hayo kwa nia mbaya ya kuvuruga uchaguzi mkuu ujao na kuhatarisha amani na utulivu nchini.  Hofu hiyo imetokana na chama hicho kuendesha mafunzo ya siri ya karate na judo yenye mwelekeo wa kijeshi, wakiwa wamepuuza kabisa masharti yaliyoambatana na ruhusa niliyokuwa nimewapa ya kutoa mafunzo kwa vijana wao.

 

 

Ruhusa Ya Mafunzo na Masharti yake

3.                 Napenda nieleze kwa ufupi ruhusa niliyokuwa nimewapa CUF na mazingira niliyoitolea.

 

4.                 Muda mrefu huko nyuma tulikuwa tukipokea taarifa za kiintelejensia kwamba CUF ilikuwa ikifanya kwa siri  mafunzo ya kijeshi na kigaidi.  Wakati mwengine ilidaiwa kwamba mafunzo ya karate na judo yalitolewa hata katika baadhi ya misikiti, dai ambalo liliunganisha na tuhuma za udini zinazoelekezwa kwa CUF, haidhuru huwa inazikanusha.

 

5.                 Kwa bahati mbaya kila tulipozifuatilia taarifa kama hizo, hatukuweza kupata ushahidi wa kuwezesha kuchukua hatua za kisheria.

 

6.                 Tarehe 25/2/2003 Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Wilfred Lwakatare alikuja ofisini kwangu na kunieleza kwamba walikuwa wanakusudia kuandaa mafunzo kwa vijana wao wa Blue Guards na White Guards ili kuwaimarisha kisiasa na ulinzi wa viongozi na mali za chama chao.  Mimi nilizipokea taarifa hizo kwa furaha kwani sasa niliona fursa ya kuweza kuyajua na kuyafuatilia mafunzo hayo na kujua kwa uhakika nini kinafundishwa.  Hata hivyo, nilimwelezea kiongozi huyo juu ya tuhuma dhidi yao na zote alizikanusha.  Nilimfahamisha kuwa chama cha siasa kutoa mafunzo kwa wanachama wake si jambo geni, ila tu mafunzo yoyote yenye mwelekeo wa kijeshi hayakubaliki kwani jukumu la kuunda majeshi ni la Serikali pekee kupitia Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.  Alinihakikishia kwamba hilo analijua na chama chake hakina mpango kama huo.

 

7.                 Tarehe 4/12/2003, CUF waliniandikia barua kuomba rasmi ruhusa ya kutoa mafunzo katika mazingira hayo tuliyoelewana.  Nami niliwaruhusu kwa barua yangu ya tarehe 11/12/2003 kwa masharti yafuatayo:

 

(a)  Kabla ya kuanza mafunzo waliarifu Jeshi la Polisi ili lijiridhishe kwamba mafunzo hayo hayana mwelekeo wa kijeshi.

 

(b) Watakapofanya mafunzo baada ya kuruhusiwa na Polisi waliarifu Jeshi hilo mwahala na nyakati yatapofanyika mafunzo hayo, ili yaweze kufuatiliwa.

 

8.                 Kwa upande wa pili, nililielekeza Jeshi la Polisi liwape CUF ushirikiano kama wataonyesha nia njema na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao kama watavunja Sheria.

 

Kwa Nini Niliwaruhusu?

9.                 Niliwaruhusu kwa sababu zifuatazo:

 

(a)  Kwanza ni kwamba Serikali inavichukulia vyama vya siasa kuwa na nia njema hadi vinapodhihirika vyenginevyo.

 

(b) Pili, suala la chama cha siasa kutoa mafunzo kwa wanachama wake ni jambo la kawaida.  Tunazo taarifa za vyama vingi vinavyotoa mafunzo mbali mbali kwa wanachama wao katika mazingira ya uwazi na hatuna matatizo navyo.

 

(c)  Tatu, kwa dhamira ya Muafaka, nilitaka niwape CUF fursa ya kujisafisha na tuhuma dhidi yao kuhusiana na mafunzo ya kijeshi na kigaidi.  Niliwatarajia wadhihirishe nia njema katika mafunzo waliyoyaombea ruhusa  kwa kuyatolea taarifa na kuyafanya kwa uwazi kama yanavyofanywa na vyama vingine.

 

(d) Nne, nilitaka watoke mafichoni ili tuyafuatilie mafunzo hayo na kuyadhibiti yasichukue sura ya kijeshi kama ambavyo wamekuwa wakituhumiwa.

 

Walivyofanya CUF

10.             Wameyapuuza kabisa masharti niliyowapa ya kutoa taarifa za mafunzo yao Polisi na mwahala na nyakati yanamofanyika.  Badala yake, kila walipofumwa wakifanya mafunzo hayo wameitumia ruhusa yangu kujitetea.  Masharti yalikuwa wazi: watoe taarifa Polisi kabla ya mafunzo kuanza na kubainisha mwahala na nyakati yatamofanyika; na siyo kuanza mafunzo bila ya taarifa na kwa siri.

 

11.             Mbaya zaidi ni kwamba walimofumwa wamekutikana wakifanya mafunzo ya karate na judo yenye mwelekeo wa kijeshi na hayahusiani kabisa na siasa au itikadi isipokuwa labda kama fujo, vurugu na ugaidi ndiyo itikadi yao.  Wakati huo huo, baadhi ya viongozi wa CUF wamekuwa wakisikika katika mikutano ya hadhara wakitoa kauli za kuchochea vurugu kwa kuwahimiza wanachama wao wafanye mazoezi ya viungo kwa ajili ya kujiandaa kuingia Ikulu.  Lakini Ikulu hakuingiwi kwa mazoezi ya viungo bali huingiwa kwa sanduku la kura.  Kauli kama vile “kuna kazi nzito mbele” au “wapigeni Polisi” pia zimekuwa zikisikika kutoka viongozi wa CUF zikiashiria maandalizi ya kuleta vurugu katika uchaguzi mkuu ujao.  Zaidi ya yote, CUF wametangaza kuwa wanaunda kikosi eti cha kulinda kura.  Haya yote hayaashirii nia njema bali tu yanazidisha shaka, na kuthibitisha tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa CUF.

 

Kufutwa kwa Ruhusa

12.             Kutokana na hali hiyo iliyojitokeza ambapo CUF imevunja muamana, tarehe 19/3/2004 nilimwandikia Katibu Mkuu wa CUF kufuta ruhusa yangu niliyokuwa nimewapa awali ya kutoa mafunzo.  Aidha, nilimwarifu kwamba nimekwishaliamuru Jeshi la Polisi livisake vikundi vyote vinavyofanya mafunzo hayo na kuvishughulikia kwa mujibu wa Sheria.  Niliwataka CUF wavivunje wenyewe vikundi vyao kabla  havijafikiwa na mkono wa Sheria.  Na kama hawavivunji wenyewe, tutavivunja sisi kwa nguvu na wataokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.

 

13.             Jambo la kufurahisha ni kwamba katika kauli zao za kubeza tangazo la Mheshimiwa Chiligati, CUF wamekiri hadharani kwamba wanaendesha mafunzo ya karate na judo.  Hii ni tofauti na huko nyuma ambapo walikuwa wakijaribu kuvungavunga na kubabaisha.  Kukiri kwao huko sasa kumetuongezea uhalali wa kuvisaka vikundi vyao vinavyofanya mafunzo hayo kwani sasa tuna uhakika wa kuwa tunasaka kitu ambacho kipo kweli.  Ukweli tuliokuwa tunautafuta CUF sasa tumeupata na hapawezi tena kuwa na madai ya kusingiziwa.

 

14.             Hata hivyo, inasikitisha kwamba viongozi wa CUF inaelekea wanawaficha wafuasi wao kwamba hiyo ruhusa ya mafunzo nimekwishaifuta.  Badala yake wanawaambia wapuuze tangazo la Mheshimiwa Naibu Waziri.  Sielewi nia yao katika kufanya hivyo, lakini napenda kuwatahadharisha kuwa wanaweza kujikuta wanawauza watu wao.  Hii ni kwa sababu wote wataokutwa katika mafunzo hayo watakamatwa tu bila ya kujali kama wamearifiwa au la.

 

15.             Nasisitiza tena kwamba mafunzo ya judo na karate yamepigwa marufuku; na marufuku haya ni kwa vyama vyote ikiwemo na CCM.  Jambo la faraja ni kwamba amri hii haitokuwa na taathira yoyote kwa vyama vingine ukiondoa CUF, kwani katika programu zao za mafunzo vyama hivyo havina kipengele cha mafunzo ya judo na karate.

 

 

 

Wito

16.             Napenda kutoa wito kwa wafuasi wa CUF wanaohimizwa kujiunga na mafunzo ya karate na judo wasikubali kuuzwa na kuingizwa matatani.

 

17.             Aidha, napenda kutoa wito kwa raia wote wema kutoa taarifa Polisi kila watapoona dalili za mafunzo ya karate na judo ili hatua za kisheria zichukuliwe.  Mafunzo hayo hayana nia njema kwa jamii na yana lengo la kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu.

 

Indhari

18.             Kwa nia njema kabisa, napenda kuwaasa CUF wajihadhari sana na kauli na vitendo kama hivi ambavyo vinachafua hadhi yao ndani na nje ya nchi.  Mafunzo ya karate na judo yenye mwelekeo wa kijeshi yanayotolewa kwa siri yanaweza kwa urahisi kabisa kutafsiriwa kuwa yanaashiria mawazo ya ugaidi.  Hali hiyo ikitokezea haitakuwa kwa manufaa ya CUF wala ya Taifa kwa jumla.