TAARIFA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUKEMEA VITISHO VINAVYOFANYWA DHIDI YA WATANZANIA WENYE ASILI YA TANZANIA BARA

WANAOISHI ZANZIBAR

 

1.                Kule Zanzibar limezuka wimbi la uhuni wa kuwatisha Watanzania wenye asili ya Tanzania Bara wanaoishi huko.  Vitisho hivyo vinavyotolewa kwa njia za kauli na vipeperushi vinawataka Watanzania wenye asili ya Tanzania Bara waondoke Zanzibar kabla ya zoezi la uandikishaji wapiga kura kuanza vyenginevyo watadhuriwa.

 

2.                Napenda kuchukua fursa hii kukemea vikali vitendo hivyo ambavyo siyo tu ni vya kihuni na kihalifu, bali pia ni vya kuvunja Katiba zetu zote mbili; yaani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya 1984.

 

3.                Ibara ndogo ya kwanza ya ibara ya 17 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasomeka ifuatavyo:-

 

“17.-(1) Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano.”

 

4.                Aidha, ibara ndogo ya kwanza ya ibara ya 16 ya Katiba ya Zanzibar inasomeka ifuatavyo:-

 

“16.-(1) Hakuna mtu atakayenyimwa uhuru wake wa kwenda, na kwa madhumuni ya kifungu hiki uhuru uliotajwa humu maana yake ni haki ya kwenda popote katika Zanzibar, haki ya kuishi katika sehemu yoyote ya Zanzibar, haki ya kuingia Zanzibar, haki ya kuondoka Zanzibar na haki ya kutofukuzwa Zanzibar.”

 

5.                Vitendo hivyo vya kihuni vilivyojitokeza Zanzibar havina nguvu ya kisheria wala kimantiki kuweza kumkatiza mtu yeyote, Mtanzania na hata asiyekuwa Mtanzania, haki yake ya kuishi na kutofuzwa Zanziba; haki ambayo imetolewa kikatiba.

 

6.                Vitendo hivyo si vya kihuni tu bali pia ni vya kijinga, vya kipumbavu, vya ufinyu wa mawazo na si vya kuona mbali.  Hii ni kwa sababu si Watanzania wenye asili ya Bara tu ndio wanaoishi Zanzibar, bali wapo pia Wazanzibari kwa maelfu wanaoishi Tanzania Bara.  Vitisho dhidi ya Watanzania wa Bara wanaoishi Zanzibar vinaweza kabisa kuchochea vitisho dhidi ya Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara.  Hali hiyo haitokuwa kwa manufaa ya yeyote isipokuwa labda kwa maadui wa Muungano wetu.

 

7.                Vitisho dhidi ya “Wabara” vilikuwa vikisikika huko Zanzibar wakati wa mapambano ya kutafuta uhuru, na vilikuwa ni sera ya msingi ya chama cha Hizbu kilichokuwa kikitetea Usultani.  Pamoja na kwamba tulikuwa tunatawaliwa, vitendo kama hivyo vya vitisho havikuvumiliwa.  Iweje vivumiliwe na kuachiwa viendelee leo wakati tunajitawala na tuko huru?  Hiyo haiwezekani hata kidogo.

 

8.                Naliagiza Jeshi la Polisi kuvikomesha mara moja vitendo hivyo kwa nguvu zake zote za kisheria.  Na agizo hili nitalifuatilia kwa karibu.

 

9.                Kwa upande mwingine, nawataka Watanzania wote wanaoishi Zanzibar, Wazanzibari na wasiokuwa Wazanzibari, waishi kwa amani bila ya kubughudhiana kwa asili zao.  Wenye asili ya Bara Afrika, wenye asili ya Bara Arabu, wenye asili ya Bara Hindi na wengineo wote, wamekutana huko kwa matakwa ya historia.  Wapo waliopelekwa huko na harakati za kutafuta riziki kwa uvuvi; wapo walijikuta Zanzibar wakikimbia vita makwao; wapo waliopelekwa Zanzibar na biashara halali; wapo pia waliopelekwa huko na biashara haramu ya utumwa.  Leo wakianza kufukuzana nani atabaki?  Kwani, kama mwenye asili ya Bara Afrika hana haki ya kuishi Zanzibar, yule mwenye asili ya Bara Arabu au Bara Hindi ataipata wapi haki hiyo?

 

10.           Wakati wa kupigania uhuru, Wazanzibari wa asili zote walishirikiana.  Hivyo hivyo katika Mapinduzi ya 1964.  Iweje leo wabaguane kwa asili zao?

 

11.           Nawataka wananchi wote huko Zanzibar waendelee na shughuli zao bila ya hofu wala woga.  Wala wasikubali kutishwa kwani sera za vitisho zimekwisha pitwa na wakati.  Kila ataetishiwa atoe taarifa Polisi au hata kwa Sheha aliye karibu naye.  Nawataka Polisi na Masheha wazishughulikie taarifa hizo kwa uzito mkubwa tena bila ya ajizi.

 

12.           Daftari la kudumu la wapiga kura kamwe lisitumiwe kama kisingizio cha kuhalalisha vitendo vya kihuni na vya kutishia amani na utulivu.  Sheria za Uchaguzi zimeweka utaratibu mzuri wa kuweka pingamizi dhidi ya mtu asiyestahiki kuandikishwa kwa ajili ya kupiga kura.  Wala kustahiki au kutostahiki kupiga kura hakuambatani na kabila la mtu wala asili yake.

 

13.           Napenda kuwahakikishia Watanzania wote, Bara na Zanzibar, kwamba Jeshi la Polisi litasimamia haki za raia wote kwa uadilifu mkubwa.  Wakati wa uandikishaji katika daftari la wapiga kura, Jeshi la Polisi litasaidia kuhakikisha kwamba hakuna mwenye kustahiki ataenyimwa haki yake.  Natoa wito utapofika wakati, wote wenye kustahiki kisheria wakajiandikishe.  Kama kutakuwa na wasiotahiki wataojipeleka kujiandikisha, watashughulikiwa wakati huo kwa majibu wa sheria, na siyo hivi sasa kwa vitisho.

 

14.           Kuna tuhuma kwamba vitisho hivyo vinavyofanywa hivi sasa vinaendeshwa na chama fulani cha siasa.  Ni juu ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatilia hilo.  Lakini upande wetu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, vitendo hivyo si vya kisiasa na hivyo havistahiki hifadhi ya kisiasa.  Kwetu sisi hivyo ni vitendo vya kihalifu na tutavishughulikia kwa mtazamo huo.  Kwa hivyo tutapokuwa tunaviandama, hatutokubali lawana kwamba tunaandama chama cha siasa au tunaandama wanasiasa.  Kazi yetu ni kupambana na uhalifu popote unapofanywa na mtu yeyote anayeufanya.  Hatujali kama ni mwanasiasa, mkulima, mfanyabiashara, mhubiri wa dini, mweusi, mweupe, mwanaume au mwanamke n.k.

 

15.           Naomba ushirikiano wenu wote katika kuendeleza amani na utulivu nchini.

 

 

 

 

Omar R. Mapuri

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI

10 /2/2004