MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2003/04

 

UTANGULIZI

 

Sura ya kwanza

Sura ya pili

Sura ya tatu

Sura ya nne

Sura ya tano

Sura ya sita

 

 

UTANGULIZI

Mpango wa maendeleo wa mwaka 2003/04 unalenga katika kuendeleza utekelezaji wa mikakati ya kupambana na umaskini pamoja na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Mikakati ya kupambana na umaskini na ufuatuliaji wake vilijumuishwa katika mfumo wa bajeti tangu mwaka wa fedha ulioishia Juni 2002.

 

Kwa kuzingatia mapitio ya mwenendo wa uchumi na bajeti ya mwaka 2002/03 pamoja na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ni dhahiri kwamba jitihada zaidi zitawekwa katika kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza umaskini na ukuaji wa uchumi. Mapitio na matarajio ya makubaliano kati ya serikali na wahisani mbali mbali pia yamezingatiwa katika kuandaa mpango huu wa maendeleo.

 

Ili kufanikisha malengo yaliyowekwa, vipaumbele vilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 vya uendelezaji rasilimali watu, usalama na uhakika wa chakula, kukuza ajira na kuongeza mapato ya fedha za kigeni vitaendelea kutekelezwa. Aidha, ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele hivyo, mkazo umewekwa katika kujenga mazingira mazuri ili wadau mbalimbali waweze kushiriki kikamilifu katika maeneo ya huduma za kijamii na kiuchumi na katika maeneo mengine yanayojumuisha, ardhi, utalawa bora, hifadhi ya mazingira, masuala ya jinsia na vita dhidi ya ukimwi.

 

Mgawanyo wa rasilimali kisekta umezingatia malengo yaliyotajwa hapo juu. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2003/04 kiasi cha sh 807,440,576,900 milioni zinatarajiwa kutumika katika mpango mzima. Fedha za hapa ni sh. 165,724,798,200 milioni na za nje sh 641,715,778,700 milioni.

 

SURA YA KWANZA

 

HALI YA UCHUMI KWA JUMLA

 

Ukuaji wa uchumi kwa jumla

Hali ya uchumi wa Taifa katika mwaka 2002 umekuwa kama ilivyotarajiwa, ambapo kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa uliongezeka, na akiba ya fedha za kigeni iliongezeka kutokana na kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi. Kasi ya upandaji bei pia iliendelea kupungua.

 

Pato la Taifa

Takwimu zinaonyesha kuwa Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.2 mwaka 2002 ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 5.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.7 mwaka 2001. Sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 5.0 na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Pato la Taifa. Sekta nyingine zilizokua na kuchangia kwa viwango vikubwa katika Pato la Taifa ni pamoja na biashara na hoteli ikijumuisha utalii (asilimia 7.0) na bidhaa za viwanda (asilimia 8.0), Mawasiliano na uchukuzi (asilimia 6.4) na huduma za kibiashara (asilimia 4.8)

 

Kasi ya Upandaji Bei

Kasi ya upandaji bei iliendelea kupungua na kufikia asilimia 4.2 mwezi Machi 2003 ikilinganishwa na asilimia 4.5 mwezi Juni 2002. Kupungua kwa mwenendo wa kasi ya upandaji bei kunatokana hasa na hali nzuri ya upatikanaji na ugavi wa chakula pamoja na sera za makusudi za kudhibiti mwenendo wa mapato na matumizi ya Serikali na ujazi wa fedha nchini.

 

Deni la Taifa

Katika kuimarisha usimamizi wa madeni ya nje na ndani, Mkakati wa Deni la Taifa ulizinduliwa mwezi Agosti 2002. Mkakati huu unabainisha mwongozo na maelekezo ya ukopaji nje, hususan, muundo wa usimamizi kiasasi, mamlaka ya kukopa na aina ya mikopo. Lengo kuu la Mkakati huu ni kuhakikisha kwamba mzigo wa madeni ya nje utakuwa stahimilivu (debt sustainability). Kwa upande wa madeni ya ndani ubadilishaji wa dhima za ndani zisizo na dhamana katika hawala zinazouzika unaendelea. Utaratibu huu umepanuliwa kufuatia kuzinduliwa hatifungani za hazina za miaka 5 na zilizoorodheshwa katika soko la Hisa la Dar es Salaam. Aidha, hatifungani za hisa za miaka 10 zimezinduliwa mwezi Oktoba 2002.

 

Mauzo na Uagizaji Bidhaa Nje

Thamani ya mauzo ya bidhaa nje kwa kipindi cha mwaka 2002 iliongezeka kwa asilimia 13.0 na kufikia dola 877.0 milioni ikilinganishwa na dola 776.4 kwa kipindi cha mwaka 2001. Ongezeko hilo la thamani ya mauzo ilichangiwa hasa na mauzo ya bidhaa zisizo asilia kama madini, mazao ya samaki na bidhaa za viwandani ambazo zilichangia asilimia 77.16 ikilinganishwa na asilimia 70.1 mwaka 2001. Kwa ujumla thamani ya bidhaa za asilia karibu zote zilishuka kutokana na kushuka kwa bei katika masoko ya dunia (kahawa, pamba, katani, korosho, karafuu). Kutokana na bidhaa za asilia kuendelea kushuka thamani zilichangia asilimia 22.8 tu ikilinganishwa na asilimia 29.9 mwaka 2001 kwenye Pato la Taifa. Thamani ya uagizaji bidhaa toka nje ilikuwa dola 1,511.3 milioni mwaka 2002 ikilinganishwa na dola 1,560.5 milioni mwaka 2001. Kupungua huko kulitokana na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa za mitambo na chakula.

 

Thamani ya Shilingi

Wastani wa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola moja ya Marekani ilipungua na kufikia Sh.966.6 mwaka 2002 ikilinganishwa na Sh. 888.9 kwa dola ya Marekani mwishoni mwa mwezi Juni 2001. Kupungua huku kwa thamani ya shilingi kulisababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa fedha za kigeni katika soko la fedha kulikosababishwa na kupungua kwa mauzo ya bidhaa nje na kuongezeka kwa mahitaji ya uagizaji bidhaa toka nje. Thamani hii iliendelea kupungua hadi kufikia shilingi 1040 kwa dola ya Marekani mwezi Aprili 2003.

 

 

 

 

Mapato

Uwezo wa serikali wa kukusanya mapato yake uliongezeka katika kipindi cha mwaka 2001/02 hasa kutokana na kutekelezwa kwa mikakati mbalimbali ya kukusanya kodi. Ongezeko hili hasa limetokana na ongezeko la makusanyo ya kodi za mapato pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Mapato ya serikali kwa mwaka 2001/02 yalikuwa asilimia 12.2 ya Pato la Taifa, ambayo yanalingana na ya mwaka uliopita. Mapitio ya miezi mitatu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2002/03 yanaonyesha kwamba makusanyo yamevuka na kuwa juu kidogo ya makadirio. Malengo ya muda wa kati wa sera ya kodi ni kuongeza uwezo wa serikali wa kukusanya mapato kwa kuongeza vyanzo vya kodi, kupambana na ukwepaji kodi, kudhibiti misamaha ya kodi pamoja na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa kodi.

 


SURA YA PILI

 

 

MUHTASARI WA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2002/03

 
Utangulizi

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2002/2003 Mpango wa Maendeleo uliidhinishiwa kiasi cha Sh 718,787,933 milioni kwa ajili ya kutekeleza programu na miradi mbalimbali. Kwa ujumla Mpango wa maendeleo ulilenga zaidi katika uboreshaji wa huduma za kijamii na uchumi; ukuzaji wa sekta ya kilimo, mifugo, viwanda, na biashara ya ndani; uimarishaji wa utawala bora na kukamilisha sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002.

 

MAENDELEO YA RASILIMALI WATU

 

 

SEKTA YA ELIMU

 

Utangulizi

Kutokana na Sera ya Elimu na Mafunzo pamoja na miongozo mbalimbali ya serikali, sekta ya elimu iliandaa Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Elimu (Education Sector Development Programme –ESDP) ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2001/02 kwa kuanzia na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM). Mpango wa MMEM unalenga katika kuongeza idadi ya uandikishaji watoto mashuleni, kuongeza ujenzi wa madarasa, kuajiri kwa awamu walimu na kuwapanga upya kulingana na mahitaji, kuinua ubora wa elimu kunakojumuisha mafunzo ya walimu walio kazini na tarajali, kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia; na kuinua uwezo wa uongozi na usimamizi wa uendeshaji wa shule.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Katika kipindi cha mwaka 2002/03, Serikali iliendeleza juhudi zake za kupanua na kuboresha elimu nchini kwa kutekeleza programu mbalimbali zenye lengo la kuboresha elimu. Programu hizi ni pamoja na uendelezaji elimu ya awali, elimu ya msingi, elimu ya sekondari, na elimu ya juu na ufundi. Hivyo mkazo uliwekwa katika:

-     Kuongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa kwa kuongeza idadi ya madarasa na walimu

-         Kuinua ubora wa elimu ya walimu kwa kuendesha mafunzo kazini na tarajali na utoaji wa vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunzia, na

-         Kuinua uwezo wa uongozi na usimamizi wa uendeshaji wa elimu katika ngazi zote.

 

Utekelezaji

a) Programu ya Uendelezaji Elimu ya Awali

Kutokana na serikali kuridhia mfumo wa elimu ya awali, shule za awali za serikali zimeongezeka toka shule 5,234 mwaka 2001 hadi kufikia shule 5,261 mwaka 2002. Kwa nchi nzima kuna jumla ya shule za awali 9,569 zikijumuisha shule za serikali na za watu binafsi. Ongezeko la shule za serikali na za watu binafsi limeongeza idadi ya wanafunzi toka 310,933 mwaka 2001 hadi wanafunzi 581,022 hapo Juni 2002. Hi ni sawa na ongezeko la asilimia 87.

 

b) Programu ya Uendelezaji Elimu ya Msingi

Kukamilika kwa mwaka wa kwanza (2002) wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (PEDP) unaonyesha ongezeko la uandikishaji wa wasichana na wavulana katika shule za msingi. Hadi mwezi wa Septemba 2002 wanafunzi 1,659,847 waliandikishwa ikilinganishwa na wanafunzi 1,100,312 mwaka 2001. Lengo lilikuwa kuandikisha wanafunzi 1,500,000. Kwa ujumla, idadi ya wanafunzi katika shule za msingi iliongezeka kutoka wanafunzi 4,842,875 mwaka 2001 hadi 5,972,077 mwaka 2002 sawa na ongezeko la asilimia 23. Uandikishaji wa watoto wote waliopo shuleni (GER) umefikia asilimia 98.6 wakati uandikishaji wa watoto wa rika ya Elimu ya msingi (miaka 7-13) walioko shuleni umefikia asilimia 80.7. Mafanikio mengine katika mwaka husika ni pamoja na kujenga madarasa mapya 8,817 (mengine 7,000 yalikuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi), kujenga nyumba za walimu 3,613 na kuajiri waalimu 7,277.

 

c) Programu ya Uendelezaji Elimu ya Sekondari.

Kwa upande wa elimu ya sekondari uwezo wa kuingia sekondari umeongezeka toka asilimia 19.5 mwaka 2001 hadi asilimia 21.7 mwaka 2002. Idadi ya wasichana wanaojiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kwa kiasi kidogo toka asilimia 49.9 mwaka 2001 hadi asilimia 50 mwaka 2002 na wale wanaojiunga na kidato cha tano toka asilimia 38 hadi asilimia 42. Ili kuimarisha uongozi na uendeshaji wa shule, waalimu wakuu wa shule za sekondari 120 walihudhuria mafunzo mafupi ya uongozi wa elimu (ADEM) na wengine 239 walifuzu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, shule 50 zilikarabatiwa na shule 530 zilipatiwa vitabu vya kiada na vifaa vya maabara.

 

Katika mwaka 2002 serikali chini ya Mpango wa Elimu ya Sekondari kwa Wasichana (GSES) iliwalipia ada wasichana 4,291 wa kidato cha I-IV na wasichana 76 wa kidato cha V-VI ambao wazazi wao hawakuwa na uwezo wa kuwalipia karo na mahitaji mengine.

 

d) Programu ya Uendelezaji Elimu ya Juu na Ufundi.

Katika ngazi hii ya Elimu kazi zilizofanyika ni pamoja na kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Vyuo Vikuu Vishiriki vya Ardhi na Muhimbili na vyuo vingine vya Elimu ya juu na vya ufundi. Mengine yaliyoendelea kufanyika ni pamoja na Baraza kuendelea na kazi ya kutathmini vyuo binafsi ili kusimamia ubora wa elimu itolewayo kwa kutoa ushauri na miongozo mbalimbali. Aidha, Serikali iliendelea na mpango wake wa kusaidia vyuo vya elimu ya juu vya binafsi kwa kuanzisha mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi katika vyuo hivyo.

 

SEKTA YA AFYA

 

Utangulizi

Katika mwaka 2002 serikali iliendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya na uboreshaji wa afya ya msingi kwa wananchi wote. Umuhimu mkubwa uliwekwa katika upatikanaji wa dawa, huduma za mama na mtoto na makundi mengine yanayoathirika zaidi.

 

Mapitio ya mwaka 2002/2003

Madhumuni na Malengo

Lengo Kuu la Sera ya Afya ilikuwa kuboresha afya za wananchi wa Tanzania ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kifamilia. Sera ya afya inahimiza yafuatayo:

-         Wananchi kushiriki kikamilifu katika mambo yanayohusu afya zao; na kipaumbele kutolewa kwa makundi ya watu wanaoweza kuathirika zaidi hususan, akinamama, watoto na jamii maskini zisizo na uwezo. Hii ni pamoja na kuzingatia usafi wa makazi ya watu na matumizi ya maji na vyakula salama.

-         Pia upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa katika vituo vya kutolea tiba, uendelezaji wa wataalam na watumishi wa afya pamoja na kuimarisha ubora wa majengo ya kutolea huduma ya afya.

 

Utekelezaji

Kwa mwaka 2002 sekta ya afya imeendelea kutekeleza programu ambazo zinalenga katika kuimarisha utoaji huduma bora za afya na uboreshaji wa afya ya msingi kwa wananchi wote. Kwa ujumla matokeo ya utekelezaji yamekuwa ya kuridhisha. Programu zifuatazo zilitekelezwa:

 

 

a)     Programu ya Kinga

Baadhi ya shughuli muhimu zilizotekelezwa ni pamoja na: huduma za chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano na akina mama waja wazito, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza hususan malaria, UKIMWI, kifua kikuu na ukoma; ununuzi wa dawa za magonjwa ya milipuko na ya kuambukiza na kutoa ruzuku kwa Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu na Taasisi ya Chakula na Lishe.

 

b)     Programu ya Tiba

Katika programu hii shughuli zilizofanyika ni pamoja na usimamizi na ununuzi wa dawa muhimu na vifaa vingine katika vituo vya kutolea huduma za tiba; uendeshaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Saratani Ocean Road, KCMC, Hospitali ya Bugando na Hospitali teule za wilaya; na kutoa ruzuku kwa hospitali za mashirika ya dini. Pia zilifanyika shughuli za matibabu ya wagonjwa wa rufaa nje ya nchi na uendelezaji wa mabadiliko juu ya mfumo wa uendeshaji hospitali za serikali.

 

c)     Programu ya Utawala na Maendeleo ya Watumishi

Pamoja na mambo mengine programu hii ilitoa mafunzo kwa wataalam wa afya na Kamati za Afya za Uendeshaji za mikoa na za wilaya juu ya mabadiliko ya sekta ya Afya. Aidha, yalifanyika mafunzo ya wataalam wa afya nje ya nchi; na ukarabati wa majengo ya vyuo 25 vya afya. Uimarishaji wa majengo ya ofisi za Wizara ya Afya, Wodi ya watoto Muhimbili, hospitali ya Rufaa Mbeya na hospitali ya Mirembe ulifanyika.

 

d)     Programu ya Huduma za Mipango, usimamizi Uhasibu na Udhibiti

Mapitio ya sera ya Afya ni mojawapo ya kazi muhimu zilizofanyika. Pia kulifanyika mapitio ya mipango na ripoti za fedha kwa halmashauri 113 za wilaya. Aidha, kulifanyika ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya zoezi la kutathmini matumizi ya fedha za serikali (Public Expenditure Review). Matayarisho ya Ulingo wa Muda wa Kati wa Matumizi ya Fedha za Serikali (MTEF) kwa mwaka 2003/04-2005/06 yalifanyika.

SEKTA YA MAJI

 

Utangulizi

Katika mwaka 2002/03 serikali ilikamilisha na kuridhia utekelezaji wa Sera mpya ya Maji ambayo inalenga katika kuchangia mkakati wa serikali wa kupunguza umasikini. Vidhihirishi vya kupungua kwa umaskini vilivyoainishwa kwenye sera ni pamoja na kutumia muda mchache katika shughuli ya kuteka maji mahudhurio mazuri shuleni, utumiaji wa muda wa ziada kwenye shughuli nyingine za uzalishaji mali, pamoja na ubora wa afya za wananchi. Sera ya Maji ya mwaka 2002 inaweka mkazo katika masuala yafuatayo:

-         Maji ni bidhaa muhimu na ina bei, kwa hiyo kama bidhaa zingine ni lazima inunuliwe

-         Vyanzo vya maji havinabudi kutunzwa na kuhifadhi mazingira yake na wadau wote hawana budi kushirikishwa katika utoaji wa huduma ya maji vijijini

-         Kubuni na kutumia tekinolojia nyepesi na yenye gharama nafuu ili kuwezesha watu wengi zaidi kupata maji kwa muda mfupi. Ukuzaji wa uvunaji wa maji ya mvua unapewa kipaumbele.

-         Ushirikishwaji wa sekta binafsi katika utoaji na usambazaji maji.

 

Mapitio ya Mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Kwa kipindi cha mwaka 2002/03 sekta ya maji iliweka mkazo katika maeneo yafuatayo:

-     Kuhakikisha kuwa mapitio ya Sera ya Maji ya 1991 yanafanyika ili kuboreshwa.

-     Kuboresha utoaji wa huduma ya maji safi, salama na ya kutosha kwa makundi mbalimbali ya kijamii mijini na vijijini.

-     Kuimarisha huduma ya mifumo ya uondoaji maji taka mijini.

-     Kuimarisha usimamizi na ugawaji wa rasilimali ya maji ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

-     Kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa lengo la kupunguza viwango vya uchafuzi.

-     Kuwa na wataalam wa kutosha wa kuimarisha na kuboresha maendeleo ya Sekta ya Maji.

 

Utekelezaji

Mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2002/03 yanaonyesha yafuatayo:

-         Miradi ya maji katika miji ya Morogoro, Tabora, Dodoma, Tanga, Arusha, na Moshi ilikarabatiwa;

-         Mamlaka ya maji safi na maji taka katika baadhi ya miji nchini iliimarishwa, kwa kupatiwa zana zinazohitajika;

-         Miradi 13 ya Maji Vijijini ilikarabatiwa na visima virefu (boreholes) vipatavyo 540 vilichimbwa katika vijiji mbalimbali nchini.

-         Idadi ya kamati za maji imeongezeka na vijiji 4,858 kati ya vijiji 6,767 vilivyoandikishwa vimeunda mifuko ya kuendeshea shughuli za maji; 

-         Halmashauri za miji 6 sasa zimeunda Mamlaka za Maji Safi na Majitaka kwa ajili ya usimamizi wa ugavi wa maji na kuondoa majitaka. Mamlaka hizo pia zimepewa uwezo wa kuwekeza kwenye huduma za maji na majitaka.

 

HUDUMA ZA KIUCHUMI

 

SEKTA YA ARDHI

 

Utangulizi

Ardhi ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya Taifa. Utunzaji na uhifadhi wa rasilimali ya ardhi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa. Ubora wa mipango ya matumizi bora ya ardhi, uelewekaji wa sheria za ardhi na vijiji na uimarishaji wa uwezo wa utekelezaji ni muhimu katika utunzaji na uhifadhi wa ardhi.

 

Mapitio ya Mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Katika kipindi cha mwaka 2002/03 malengo ya sekta ya ardhi yaliyowekwa ni pamoja na:

-         Kuongeza ubora na ufanisi katika kusimamia na kutoa huduma za ardhi.

-         Kuongeza ufanisi na ubora katika upimaji wa viwanja na uchoraji ramani.

-         Kuwa na usimamizi mzuri wa sera, mipango na programu.

-         Kuweka mazingira mazuri ya maendeleo endelevu ya makazi, ujenzi wa nyumba za bei nafuu na matumizi bora ya ardhi.

-         Kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi na maendeleo ya rasilimali  watu.

-         Kuweka utaratibu mzuri wa kukusanya na kusimamia mapato.

 

Utekelezaji

Sekta ya ardhi katika kipindi cha mwaka 2002/03 ilitekeleza majukumu yafuatayo:

-         Elimu kuhusu Sheria mpya za Ardhi ilifanyika pamoja na upembuzi yakinifu wa Mradi wa Viwanja 20,000 katika jiji la Dar es Salaam ulikamilika.

-         Mwongozo wa tathmini ya ardhi ulikamilika na kusambazwa pamoja na upimaji wa viwanja katika sehemu za Mbezi na Mbweni na hati 2,976 zilisajiliwa na maombi 190 yalikataliwa.

-         Upigaji wa picha za anga ulifanyika katika miji ya Mtwara, Lindi, Nachingwea, Ruangwa, Tandahimba, Masasi, Tunduru, Mahenge, Mbinga, Liwale na Newala.

-         Ripoti inayohusu tathmini ya mali 1,500 ilikamilika na kusambazwa ikiwa ni pamoja na sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya mwaka 2002 ambayo itaanzisha mabaraza ya ardhi na nyumba iliandaliwa.

-         Sera ya Taifa ya maendeleo ya makazi ilichapishwa na kusambazwa na utafiti wa taarifa zinazohusu vifaa vya ujenzi vya bei nafuu iliandaliwa na kuchapiswa.

-         Idara ya “Management Information System” ambayo inatumia teknolojia ya kisasa katika upatikanaji wa habari, takwimu na utunzaji wa kumbukumbu sahihi za ardhi ilianzishwa; na iliweza kubaini viwanja 76,000 vilivyopimwa na kutambua viwanja 33,000 ambavyo vina hati miliki.

 

SEKTA YA NISHATI

 

Utangulizi

Nishati ni nyenzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma za jamii na suala zima la kupambana na umaskini. Tanzania imedhihirisha kuwa na rasilimali kubwa ya vyanzo vya nishati ya umeme, gesi asilia,, tungamotaka, makaa ya mawe na nishati inayojadidika (renewable energy). Pamoja na kuwa na vyanzo vingi vya nishati bado havijaandelezwa licha ya shughuli za kukuza uchumi kuhitaji vyanzo hivi muhimu.

 

Mapitio ya Mwaka 2002/03

Madhumuni  na Malengo

Katika kipindi cha mwaka 2002/03 sekta ya nishati ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:

-         Kukamilisha mapitio ya sera ya nishati ya mwaka 1992, ili iende sambamba na sera za jumla za kiuchumi zinazotekelezwa hapa nchini

-         Kuendeleza matumizi ya vyanzo vya nishati kama mionzi ya jua, upepo, nishati inayojadidika (renewable energy) na makaa ya mawe

-         Usambazaji umeme vijijini na katika wilaya za Serengeti, Urambo na Ukerewe

-         Kuratibu na kusimamia biashara ya mafuta ya petroli nchini na kuendeleza utafiti wa mafuta pamoja na kukamilisha utekelezaji wa mradi wa gesi wa Songosongo

-         Kusimamia urekebishaji wa sekta ndogo ya umeme, kuimarisha utendaji katika shirika la TANESCO pamoja na ubinafsishaji wake

 

Utekelezaji

Pamoja na majukumu mengine sekta ya nishati ilitekeleza yafuatayo:

-         Kukamilisha mapitio ya sera ya nishati ya mwaka 1992 na kupitishwa rasmi na serikali

-         Kazi ya kumchagua Mkandarasi wa kutekeleza mradi wa Songosongo na kutiliana mkataba na kampuni ya “Larsen & Toubro Limited, India (L & T) “ imekamilika

-         Kazi ya kurekebisha Shirika la TANESCO ilikamilka na kuwekwa chini ya manejimenti mpya ya Net Group Solution kwa nia ya kuongeza ufanisi wa utendaji, hususan katika kukusanya mapato

-         Mikutano mbalimbali ilifanyika kwa kushirikiana na nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuweka mikakati ya kuendeleza nishati pia kutangaza maeneo yenye dalili za mafuta ya petroli na yanayoweza kuvutia wawekezaji

-         Takwimu za kasi ya upepo zinaendelea kukusanywa ili kuweza kuthibitisha kama kasi ya uepo huo inaweza kutosheleza kuzalisha umeme

-         Usambazaji umeme katika vijiji vya wilaya za Serengeti, Urambo, Ukerewe, Ngara na Biharamulo uliendelea. Aidha, serikali kwa kushirikiana na serikali ya Sweden iliandaa taratibu za kuanzisha asasi maalum, “Rural Energy Agency” ambayo itajihusisha na utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na “Rural Energy Fund” kwa ajili ya kutekeleza miradi ya nishati vijijini

 

SEKTA ZA BARABARA, MAWASILIANO NA UCHUKUZI

 
SEKTA NDOGO YA BARABARA

Utangulizi

Sekta ndogo ya barabara ni kati ya sekta muhimu katika uendelezaji na ukuzaji wa uchumi. Umuhimu wa sekta hii hujitokeza katika usafirishaji na uchukuzi wa abiria na mizigo toka sehemu moja hadi nyingine. Katika nchi yetu asilimia 70 ya uchukuzi wa mizigo hufanywa kwa njia ya barabara na asilimia 64 ya mizigo ya nchi za jirani. Katika kipindi cha mwaka 2002/03 sekta ya barabara imekuwa na maendeleo mazuri ambayo yametokana na kuanzishwa kwa mfuko wa Barabara (Road Fund), Wakala wa serikali wa Mamlaka ya Barabara (TANROADS) na Bodi inayosimamia uendeshaji mfuko wa barabara (Road Funds). Kutokana na mabadiliko hayo barabara zote kuu za mikoa na za vijijini zimeendelea kufanyiwa matengenenzo kama inavyopangwa. Aidha, sekta binafsi zimeendelea kushirikishwa zaidi katika sekta hii.

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na malengo

Madhumuni makuu ya sekta ya barabara ni kuwepo kwa mtandao wa barabara kote nchini zinazopitika katika kipindi chote cha mwaka na zenye muungano mzuri kati ya barabara kuu za mikoa na zile za vijijini.  Hii ni pamoja na kuwa na barabara kuu bora zenye kuunganisha nchi yetu na nchi jirani.

 

a) Ukarabati, Ujenzi na Matengenezo ya Barabara

Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2002/03 malengo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kuu yalikuwa:

-         Matengenezo maalum (Periodic maintenance) kilometa 165 za matengenezo ya kawaida (routine maintenance) kilometa 6,382 madaraja na “culverts” 1,279

-         Ukarabati wa barabara kuu kilometa 297, matengenezo ya dharura (emergency works) kilometa 377, “Backlog maintenance” kilometa 538 na madaraja makubwa 32

-         Kushirikisha sekta binafsi katika shughuli za ukarabati, ujenzi na matengenezo ya barabara ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kutoa mafunzo kwa makandarasi wazalendo

-         Utekelezaji wa mpango maalum wa ujenzi wa barabara kuu kwa viwango vya lami kwa kutumia fedha za ndani

 

b) Ukarabati, Ujenzi na Matengenezo ya Barabara Vijijini

-         Matengenezo ya kawaida (routine maintenance) kilometa 10,807, madaraja na “culverts” 1,351 pamoja na matengenezo ya dharura kilometa 699

-         Ukarabati wa kilometa 648.5 na madaraja makubwa 60

 

Utekelezaji

Katika kipindi cha mwaka 2002/03 utekelezaji wa malengo ya sekta ndogo ya barabara ulikuwa kama ifuatavyo:

-         Matengenezo ya kawaida kilometa 1,808 na madaraja 157 kwa upande wa barabara Kuu na kilometa 2,423 na madaraja 101 upande wa barabara vijijini kazi hizo zilifanyika

-         Ukarabati wa barabara kuu kilometa 121 zimekamilika ikiwa ni pamoja na kilometa 54.6 za barabara vijijini na daraja moja.

-         Maandalizi ya Sera ya Ujenzi yamekamilika na ipo katika hatua za mwisho kupitishwa na serikali. Pia kazi ya kuandaa mkakati wa ushirikishaji wa sekta binafsi kwenye shughuli za ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara imekamilika

-         Baraza la Taifa la Ujenzi (National Construction Council), Bodi ya Msajili wa makandarasi (Constractor Registration Board) na Tanzania Civil Engineering and Constructors Association (TACECA) wameendelea kutoa mafunzo kwa makandarasi wazalendo. Lengo kuu ni kujenga uwezo wa wazalendo ili washiriki kikamilifu katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara. Sambamba na kujenga uwezo wa makandarasi wazalendo Baraza la Ujenzi la Taifa kwa kushirikiana na wadau wake wameanzisha mfuko maalum wa kusaidia wakandarasi wazalendo kupata fedha za kununulia vifaa n.k

-         Kuhusu mpango wa kuwapa uwezo sekta binafsi ili ishiriki katika shughuli za ujenzi wa barabara kupitia mfumo wa (BOT) “Build Operate and Transfer” Wizara ya Ujenzi inaendelea na majadiliano na kampuni binafsi ya PRODECO kuhusu jinsi ya kuingia mkataba utakaoiwezesha kampuni hiyo binafsi kuanza na eneo walilopewa la ukanda wa kati. Hususani barabara za Itigi, Manyoni, Tabora na Kigoma.

 

Matatizo

Pamoja na mafanikio yalionekana katika kipindi cha mwaka 2002/03 kwenye sekta ya barabara yapo matatizo yaliyojitokeza ambayo ni pamoja na:

-         Pamoja na kuwepo kwa mfuko wa barabara bado fedha zinazopatikana hazijaweza kukidhi mahitaji halisi. Katika mwaka 2002/03 fedha za matengenezo zilizopatikana ni asilimia 30 ya mahitaji yote;

-         Uharibifu wa miundombinu unaosababishwa na uchukuzi wa mizigo usiozingatia viwango vilivyowekwa pamoja na uharibifu unaosababishwa na mvua; na

-         Makandarasi Wazalendo hawajaweza kushiriki kikamilifu katika kazi za matengenezo, ukarabati na ujenzi wa barabara. Sehemu kubwa ya kazi hizi zinafanywa na kandarasi za nje

 

SEKTA NDOGO YA MAWASILIANO NA UCHUKUZI

 

Utangulizi

Sekta za Mawasiliano na Uchukuzi zinalinganishwa na umuhimu wa mzungunko wa damu katika mwili wa mwanadamu. Kukwama kwa sekta hizi ni kielelezo cha kuanguka kwa shughuli za kijamii na maendeleo ya kiuchumi. Kwa kutambua umuhimu huo sekta hizi zinapewa kipaumbele katika mgao wa raslimali kitaifa na ushirikishwaji wa sekta binafsi. Aidha, serikali iliandaa pogramu maalum za ukarabati wa miundombinu ya sekta hizi. Programu hizi zilihusu ukarabati wa njia za reli, simu, barabara, posta na bandari. Ukarabati wa miundombinu kupitia programu zilizotanjwa hapo juu umesaidia kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta hizi; na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma.

 

 

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Katika mwaka wa 2002/03 malengo makuu ya sekta za mawasiliano na uchukuzi yalikuwa kama ifuatavyo:-

-         Kuratibu na kuhuisha sera, mikakati na sheria ili kuhakikisha kwamba huduma za mawasiliano na uchukuzi zinatolewa kwa ufanisi;

-         Kuratibu shughuli zote za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundo mbinu ya sekta za mawasiliano na uchukuzi;

-         Kujenga uwezo wa kiutendaji wa wafanyakazi wa taasisi zote zilizo chini ya sekta za mawasiliano na uchukuzi;

-         Kushirikiana na asasi za kitaifa na kimataifa kwa madhumuni ya kuendeleza na kuboresha huduma za mawasiliano na uchukuzi;

-         Kuweka taratibu nzuri zitakazosaidia uratibu wa usalama wa vyombo vya usafiri wa abiria ili kupunguza ajali;

-         Uratibu wa huduma za sekta za mawasiliano na uchukuzi ili kuhakikisha kwamba hazileti athari kubwa katika mazingira; na

-         Uboreshaji wa huduma za utabiri wa hali ya hewa.

 

Utekelezaji

Utekelezaji wa malengo ya sekta ya mawasiliano na uchukuzi kwa mwaka 2002/03 ni kama ifuatavyo:

-         Wizara imeandelea na kuhuisha sera za sekta za mawasiliano na uchukuzi. Sera ya uchukuzi imekamilishwa katika mwaka huu wa 2002/03 na kupitishwa na serikali. Mkakati wa utekelezaji wa sera hiyo unaendelea kukamilishwa. Sera ya Posta na ya “Information Communication Tecknology” zinaendelea kukamilishwa

-         Utaratibu wa shughuli za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya sekta za mawasiliano na uchukuzi zinaendelea vizuri. Kazi zilizopangwa za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya viwanja vya ndege, vituo vya hali ya hewa na mitandao ya simu zinaendelea vizuri

-         Mafunzo yenye lengo la kujenga uwezo wa kiutendaji (rasilimali watu) katika sekta za mawasiliano na uchukuzi yameendelea kutolewa kupitia vyuo vya mafunzo vilivyopo chini ya sekta hii pamoja na vingine kama chuo cha watumishi wa umma, vyuo vya elimu ya juu n.k

-         Sheria inayomtaka kila mwenye chombo cha usafiri kuwa na vifaa vyote muhimu vya kuokolea imekwishaandaliwa na ipo kwenye hatua za utekelezaji

-         Kuhusu kuboresha huduma za hali ya hewa, taratibu zakuendeleza sekta hii zinaendelea kitaifa na kupitia ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

HUDUMA ZA UZALISHAJI

 

SEKTA YA KILIMO

 

Utangulizi

Mchango wa sekta ya kilimo na chakula kwenye uchumi wa Taifa unabakia kuwa wa muhimu na wa kipekee kwani ndiyo chanzo kikuuu cha chakula na malighafi ya viwanda, nafasi za ajira na soko la bidhaa za viwandani.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Madhumuni na malengo ya sekta ya kilimo na chakula ya mwaka 2002/03 yaliendelea kulenga katika kutekeleza Sera ya kilimo na mifugo ya mwaka 1997 kupitia mkakati wa kuendeleza sekta ya Kilimo ya mwaka 2001 ambao unalenga katika masuala makuu yafuatayo:

-         Kuhakikisha upatikanaji na usalama wa chakula kwa wakati na kwa watu wote

-         Kuongeza kipato cha wakulima kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo, usindikaji na masoko imara

-         Kuongeza mapato ya fedha za kigeni kwa kuongeza wingi wa bidhaa zenye ubora unaokubalika kikanda na kimataifa na kuendeleza matumizi ya teknolojia sahihi na rahisi na yenye tija

-         Kutoa msukumo wa matumizi endelevu ya rasilimali za asili kama ardhi na maji pamoja na kuimarisha maingiliano ya sekta ya kilimo na sekta nyingine za kiuchumi

 

Utekelezaji

-         Jukumu la kutoa huduma shirikishi za ughani nchini kupitia National Agriculture Extension Project II (NAEPII) katika mikoa yote nchini zimehamishiwa kwenye Halmashauri za Wilaya kwa kuhamisha wataalam kutoka Wizara ya Kilimo na Chakula na kutayarishwa kwa uwiano wa majukumu ya Wizara ya Kilimo na Chakula na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

-         Jumla ya majaribio 114 yalifanyika katika mashamba ya wakulima na watafiti 80 walipatiwa mafunzo ya rejea ya utafiti husishi. Aidha, huduma za utafiti zinalenga katika kupata mbegu zinazo zaa kwa wingi, zinazostahimili ukame na kumudu kupambana na mashambulizi ya wadudu na magonjwa kwa kutumia mbinu shirikishi inayolenga matakwa ya wadau ambao huchangia sehemu kubwa ya gharama za utafiti. Matokeo ya tafiti shirikishi zilizofanyika ni kuwepo kwa mbegu mpya za mazao ya mahindi, maharage, mtama, pamba na ngano.

-         Mpango Kabambe wa Kilimo cha Umwagiliaji umekamilika na umeonyesha kuwepo kwa hekta 29.4 milioni zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kati ya hizo hekta 2.3 milioni zina uwezekano mkubwa, hekta 4.5 milioni zina uwezekano wa wastani na zilizobaki zina uwezekano mdogo. Baadhi ya mikakati ya kuhakikisha kuwa kilimo cha umwagiliaji maji kinaendelezwa ni: ufufuaji na uboreshaji wa miundo mbinu katika skimu za asili za umwagiliaji; kuanzishwa miradi mipya ya gharama ndogo ambayo wakulima watachangia nguvu na gharama za uendeshaji; kuongeza uvunaji wa maji ya mvua kwa kujenga mabwawa na kuchimba visima na kuwepo kwa mfumo mzuri wa usimamizi na uratibu wa kazi ya umwagiliaji.

-         Katika kuhakikisha kuwa uagizaji na usambazaji wa pembejeo unafanikiwa kwa kumpatia mkulima pembejeo kwa wakati unaofaa, kwa kiasi kinachohitajika na kwa bei nafuu Mfuko wa Pembejeo za Kilimo ulikopesha jumla ya shilingi 1.2 bilioni kati ya shilingi 1.5 bilioni zilizokuwa zimetengwa. Pia benki za ushirika zikiwemo Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCB) na Benki ya Ushirika wa Wakulima Kagera (KFCB) zilizokopesha jumla ya shilingi 19.81 bilioni kwa ajili ya kununulia na kusambaza zana na pemebejeo za kilimo.

 

SEKTA YA MIFUGO

 

Utangulizi

Sekta ndogo ya mifugo ni muhimu katika uchumi kwa vile huchangia upatikanaji wa chakula na lishe, nguvu kazi wanyama, usafirishaji, biashara na nishati.

 

Madhumuni / Malengo

-         Kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha na kuinua kiwango cha lishe kwa kudhibiti magonjwa ya mifugo;

-         Kuboresha uzalishaji, ubora na usambazaji wa mazao na pembejeo za mifugo;

-         Kuendeleza hali ya maisha vijijini kwa kuongeza kipato kitokanacho na uzalishaji, usindikaji na mauzo ya mazao ya mifugo;

-         Kuongeza mapato ya fedha za kigeni kwa kutoa msukumo wa uzalishaji na kuongeza mauzo ya mifugo na mazao ya mifugo nchi za nje ;

-         Kuendeleza na kutumia teknolojia za kisasa zinazoongeza uzalishaji wa mifugo, nguvukazi na ardhi;

-         Kuhakikisha matumizi na maendeleo endelevu ya malisho na maji ili kupunguza athari za  mazingira;

-         Kuendeleza rasilimali watu walioko katika sekta ili kuongeza tija, uwezo, hamasa na moyo wa kujituma;

-         Kuendeleza nguvukazi katika sekta ya mifugo kwa kuzingatia matakwa ya kijinsia ili kuongeza uzalishaji wa nguvukazi na uwiano wa kijinsia; na

-         Kuweka mazingira bora katika kutoa huduma kwa ufanisi.

 

 

Utekelezaji

Majukumu yaliyotekelezwa katika mwaka 2002/3 ni pamoja na:

-         Kuandaa mafunzo ya kanda ya magonjwa ya maumbikizo ya mifugo;

-          Kufanya mikutano kujadili sheria za mifugo;

-         Kufanya majaribio ya chanjo ya magonjwa ya mifugo kama vile New Castle;

-          Kuendesha mafunzo juu ya uzalishaji bora wa mifugo katika wilaya 36;

-          Ujenzi wa mabwawa ya mifugo;

-         Kukarabati Vituo vya Uchunguzi wa Mifugo na kuvipatia madawa muhimu;

-         Kuendesha mafunzo ya ukaguzi wa nyama na mifugo;

-         Kuratibu na kutathmini maendeleo ya mbuzi wa maziwa;

-          Kuanzishwa kwa vikundi vya ushirika wa wafugaji; na,

-         Kufanyika kwa mafunzo ya ughani kwa wafugaji 1000 na Maafisa wa Ughani 40.

 

SEKTA YA MALIASILI NA UTALII

 

Utangulizi:

Sekta ya Maliasili na Utalii inajumuisha sekta ndogo za Misitu, Nyuki, Uvuvi, Wanyamapori, Mambo ya Kale na Utalii. Katika kufanikisha majukumu yake, sera na sheria zinaendelea kuhuishwa na mikakati ya kutekeleza inaendelea kuandaliwa kwa nia ya kuhakikisha hifadhi, usimamizi na matumizi endelevu ya maliasili, na kukuza utalii pamoja na kulinda maeneo ya kihistoria na kutoa mchango mkubwa kwa pato la Taifa.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Sekta ya Maliasili ililenga kutekeleza yafuatayo:-

-         Kuongeza mchango wa sekta za maliasili na Utalii katika Pato la Taifa na katika kuongeza ajira na kuondoa umaskini nchini.

-         Kuhakikisha uhifadhi, usimamizi bora na matumizi endelevu ya maliasili zetu.

-         Kuboresha utendaji, uwezo wa kusimamia na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika shughuli zinazohusu sekta za maliasili na utalii.

-         Kuimarisha na kuendeleza utalii wa ndani na nje ya nchi.

-         Kuongeza mapato ya Serikali yatokanayo na sekta za maliasili na utalii.

-         Kuwezesha wananchi, sekta binafsi, vikundi vya kijamii na mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine wote kuweza kushiriki kikamilifu katika mipango yote inayohusu kulinda, kuhifadhi, kusimamia na matumizi endelevu ya maliasili na utalii.

 

Utekelezaji:

Ili kufikia malengo yaliyotajwa, utekelezaji kwa mwaka 2002/2003 ni kama ifuatavyo;

-         Wizara ilihuisha sheria na kuboresha kanuni zinazotawala Sekta ya Uvuvi.

-         Wananchi na sekta binafsi walishirikishwa katika kuandaa mipango ya hifadhi na usimamizi wa Misitu na Nyuki.

-         Utambuzi wa maeneo ya Hifadhi za Misitu na Nyuki ulifanyika katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Manyara.

-         Ili kuboresha mazao ya samaki ukaguzi ulifanyika katika sehemu mbalimbali hususani kwenye vyombo vya kuvulia samaki na viwanda vinavyotengeneza samaki.

-         Ukaguzi na tathmini ya maeneo yaliyotengwa na hifadhi za misitu zilifanyika.

-         Wizara iliandaa Mkutano wa Wawekezaji kwenye Sekta ya Utalii na ilishiriki katika Maonyesho ya Kibiashara na mikutano ya kimataifa inayohusu maliasili.

-         Utekelezaji wa mikakati ya kupambana na rushwa na uelimishaji wa wananchi katika kuhifadhi rasilimali za asili na utamaduni zilifanyika.

-         Jumla ya miche 9,256,289 ilikuzwa.

-         Jumla ya hekta 2,368 za ardhi ziliandaliwa na hekta 6,460 za mashamba ya miti na mashamba 16 ya miti yalitunzwa.

-         Ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika mashamba na maeneo ya uwindaji ulifanyika.

-         Ukaguzi na usimamizi wa uwindaji wa kitalii, wakala wa utalii na ukusanyaji wa mapato vilifanyika.

-         Kutangaza vivutio vya kitalii nje ya nchi na kukuza uwekezaji katika sekta ya maliasili.

-         Ukarabati wa majengo, sehemu za kihistoria, vifaa vya kufanyia kazi na ajira kwa wafanyakazi watakaoshughulikia uhifadhi na tathmini ya rasilimali za asili na utamaduni zilifanyika.

-         Programu na kampeni za kuzuia uvuvi haramu, ujangili na uchomaji moto ovyo wa misitu zilitekelezwa.

-         Programu ya hifadhi ya samaki katika ziwa Viktoria na Tanganyika zilitekelezwa.

 

SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA.

 

Utangulizi

Sekta ya viwanda na biashara katika mwaka 2002 ilikuwa na mafanikio ya kuridhisha. Majukumu makuu ambayo sekta imejiwekea ni kuweka mazingira mazuri ya uwekazaji ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa kuridhisha wa nyezo muhimu kama vile umeme na maji, na kuhakikisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa ili ziweze kuhimili ushindani wa ndani na nje.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03
Madhumuni/Malengo

Mwaka 2002/03 shughuli zifuatazo zilipangwa kutekelezwa:

-         Kuimarisha uwezo wa sekta katika kuhudumia wawekezaji na washikadau mbalimbali;

-         Uimarishaji wa taasisi za utafiti na teknolojia;

-         Kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma bora nchini;

-         Kuongeza uzalishaji na mchango wa sekta katika uchumi;

-         Kuwa na ushindani halali wa kibiashara, kumlinda mlaji na kuongeza mauzo ya bidhaa nje.

 

Utekelezaji

Hali ya utekelezaji wa shughuli zilizopangwa katika sekta hii ulikuwa mzuri ingawa kwa kiasi kikubwa uliathiriwa na ukosefu wa fedha.

-         Mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na upatikanaji wa nyezo muhimu kama vile umeme na maji umewahamasisha wawekezaji wengi kuendelea kufanya ukarabati wa viwanda na kuanza uzalishaji kwenye miradi mipya ya viwanda iliyokamilika

-         Wizara ilifanya ukaguzi wa viwanda katika mikoa mbalimbali kwa madhumuni ya kuhimiza maendeleo ya viwanda na kuelewa matatizo yanayokabili viwanda na pia kupata picha halisi ya ufanisi katika viwanda mbalimbali

-         Sekta ya viwanda na biashara ndogo imeendelea kutoa ajira na kuchangia Pato la Taifa. Inakisiwa sekta hii ilichangia kiasi cha 1/3 ya Pato la Taifa;

-         Katika hatua za kupambana na umaskini, mafunzo ya usindikaji wa vyakula yalitolewa kwa kina mama 1700 chini ya mradi wa UNIDO kupitia SIDO

-         Hadi kufikia Desemba 2002 mfuko wa wafanyabiashara wadogo ulitoa mikopo yenye thamani ya sh. 4.64 bilioni kwa wananchi;

-         Marekebisho ya “tariff” za umeme, urekebishaji wa viwango vya kodi na ukaguzi wa bidhaa ni hatua zilizochukuliwa na serikali ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kumudu ushindani wa bidhaa katika soko la ndani na nje.

 

Kutokana na utekelezaji mzuri wa sera na majukumu iliyojiwekea sekta ya viwanda kwa mwaka 2002 ilikua kwa asilimia 8.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.0 mwaka 2001. Sekta hii imeongoza kwa kuvutia wawekezaji wengi zaidi ikilinganishwa na sekta nyingine kwani miradi ya viwanda 103 yenye thamani ya shilingi 198,245 milioni iliidhinishwa mwaka 2002 ikilinganishwa na miradi 82 iliyopitishwa mwaka 2001. Aidha, miradi hii ina uwezo wa kutoa nafasi za ajira kwa watu 16,010.

 

Matatizo

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2002 bado sekta ya viwanda na biashara inaendelea kukabiliwa na matatizo kadhaa ikiwa ni pamoja na kodi kubwa, gharama kubwa za umeme, ushindani wa bidhaa kutoka nje, mitambo mibovu kwa baadhi ya viwanda na miundombinu hafifu hasa barabara za mikoani. Aidha, kwa upande wa viwanda vidogo matatizo makubwa yaliyoendelea kukwamisha ukuaji wake ni pamoja na tatizo la kupata mitaji, udhaifu wa huduma za kuendeleza biashara, na ushirikiano mdogo uliopo kati ya taasisi mbalimbali na sekta hii.

 

SEKTA YA MADINI

 

Utangulizi

Sekta ya madini ina mchango mkubwa katika pato la Taifa na mapato ya fedha za kigeni na pia sekta hii ni chanzo cha ajira katika sekta isiyo rasmi. Katika mwaka 2002/03 Serikali iliendeleza jitihada zake za kuweka mazingira bora ya kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi kuweka sera, sheria, taratibu, vivutio, huduma za ughani na ukusanyaji maduhuli ya Serikali. Aidha, mkazo uliwekwa pia katika kuendeleza wachimbaji wadogowadogo na uhifadhi wa mazingira katika machimbo ya madini.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03
Madhumuni/Malengo

Madhumuni na malengo kwa sekta ya madini kwa mwaka 2002/03 yalikuwa haya yafuatayo:

-         Kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa na fedha za kigeni;

-         Kuongeza ajira na kuchangia kuondoa umaskini kwa wananchi kwenye maeneo yenye migodi;

-         Kukuza na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uuzaji wa madini nchini na nchi za nje;

-         Kuendeleza na kuhamasisha uanzishaji na ukuzaji wa viwanda vitakavyoongeza thamani (value added) ya madini yanayochimbwa hapa nchini kabla ya kuyauza nje;

-         Kupunguza au kuzuia athari za uharibifu wa mazingira zinazotokana na uchimbaji madini kwenye maeneo mbalimbali nchini hasa kwenye machimbo; na

-         Kuimarisha usimamizi, udhibiti na uratibu katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji mapato.

 

Utekelezaji

Kazi zilizofanyika katika mwaka 2002/03 ni pamoja na: -

-         Kuanzishwa kwa kituo cha mafunzo ya uchongaji wa vinyago kwa kutumia miamba cha Arusha;

-         Kukamilika kwa uanzishaji wa kituo cha mafunzo ya teknolojia bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu huko Matundas Wilayani Chunya;

-         Kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu njia bora za uchimbaji wa madini (mfano dhahabu) na unaozingatia hifadhi ya  mazingira hususan matumizi bora ya zebaki;

-         Kukamilika kwa ukarabati wa nyumba na ofisi za kanda mbalimbali;

-         Kukamilika na kuanza kutumika kwa muundo mpya wa sekta ya madini unaotarajiwa kuimarisha usimamizi wa sera, sheria na taratibu. Katika muundo huo vitengo vya idara ya Jiolojia na maabara vimeundwa upya; na

-         Mtaala mpya wa mafunzo ya ufundi mchundo yalikamilishwa na kuanza kutumika katika chuo cha madini Dodoma.

 

 

 

SEKTA YA USHIRIKA NA MASOKO

 

Utangulizi

Ushirika na Maendeleo ya Masoko ni msingi imara wa kuongeza akiba na mitaji hivyo kuinua kipato na kupunguza umaskini kwa wananchi walio wengi hasa wale waishio vijijini. Aidha, uendelezaji ushirika na masoko unatoa fursa pana kwa wananchi hasa wanachama wa ushirika kuunganisha nguvu zao kwa pamoja na kupata bei nzuri ya mazao.

 

Wizara ya Ushirika na Masoko katika kutekeleza azma ya kufufua, kuimarisha na kuendeleza Ushirika nchini, imeendelea kusimamia jukumu la uwekaji wa mazingira ya maendeleo ya vyama vya ushirika endelevu vinavyomilikiwa na wanachama wenyewe pamoja na mfumo wa Masoko wenye ufanisi, kwa kutunga sera, sherie na taratibu za usimamizi.

 

Mapitio  ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

-         Kuweka mazingira mazuri katika kuendeleza sera, sheria na kanuni zinazohusiana na ushirika na masoko.

-         Kusimamia maendeleo endelevu na ya kiuchumi ya vyama vya ushirika na mfumo wa masoko ya mazao ya kilimo.

-         Kuratibu, kuimarisha na kusimamia shughuli zinazohusiana na ushirika na maendeleo ya masoko ya kilimo.

-         Kuweka mazingira mazuri na yenye ufanisi katika utoaji wa huduma na ushauri

-         Kuwapa uwezo wanachama wa Vyama vya Ushirika kuendesha vyama vyao kwa njia ya kidemokrasia

 

Utekelezaji

Katika kipindi cha mwaka 2002/03 Wizara ya Ushirika na Masoko ilitekeleza yafuatayo:-

-         Rasimu ya Sheria ya Vyama vya Ushirika, Mkakati wa Kuendeleza Ushirika na programu ya Marekebisho ya Ushirika viliandaliwa.

-         Tafsiri ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002 katika lugha ya kiswahili ilikamilika na kuanza kusambazwa kwa wadau.

-         Vyama vya ushirika 123-vinavyojumuisha wakulima, wavuvi, wanawake na wafanyabiashara wadogowadogo vilianzishwa.

-         Mafunzo ya kuanzisha na kusimamia vyama vya ushirika vya wakulima, wavuvi pamoja na vyama vya ushirika vya wanawake yalitolewa.

-         Ukaguzi wa vyama vya ushirika 16 katika mikoa ya Mbeya, Dodoma, Morogoro na Dar es salaam na ushauri wa jinsi ya kuviboresha na kuanzisha vingine ulitolewa.

-         Bei za jumla za mazao ya chakula na masoko ya mifugo zilikusanywa na kutangazwa.

-         Wasimamizi wa masoko 51 kutoka mikoa 10 walipewa mafunzo na takwimu zinazohusiana na tafiti za masoko ya mazao ya mifugo, pamba, pareto, sigara na vifaranga.

 

SEKTA YA UTAWALA, FEDHA NA MPANGO

 

Utangulizi.

Serikali inaendelea kutimiza jukumu lake kubwa la kulinda usalama wa raia na kuendeleza utawala bora. Hii ni kwa sababu maendeleo ya kiuchumi, kijamii au kiteknolojia yanategemea sana usalama wa raia pamoja na utawala bora. Aidha, uboreshaji na uimarishaji wa mfumo wa utendaji kazi, usimamizi thabiti pamoja na uendelezaji mahusiano na nchi zote ulimwenguni uliendelea kuimarika. Serikali pia iliendelea kutekeleza programu ya kurekebisha na kuboresha mfumo wa sheria hapa nchini kwa lengo la kutoa haki sawa kwa wote na kwa muda mfupi na kuimarisha nguzo za utawala bora.

 

 

 

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni/Malengo:

Utawala bora ni jibu la moja kwa moja katika kufikia uwajibikaji wa kijamii, uwazi na ushirikishwaji wa wadau wote. Kwa misingi hiyo, madhumuni na malengo ya sekta hii kwa mwaka 2002/03 yalikuwa:

-         Kuendelea na utekelezaji wa programu ya kurekebisha na kuboresha mfumo wa sheria (Legal Reform Programme) na kusimamia na kuendeleza utawala bora wa sheria na haki ili kujenga amani na utulivu, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi;

-         Kuimarisha idara ya Sheria na mifumo ya utendaji kwa lengo la kupunguza mlundikano wa kesi katika Mahakama na vyombo vingine vya sheria;

-         Kutayarisha na kuchapisha miswada 2,600 na sheria za Bunge 2,500;

-         Kuimarisha na kuhuisha mfumo wa upangaji na usimamizi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi;

-         Kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 pamoja na sera mbalimbali za kupambana na umaskini;

-         Kuendeleza ukusanyaji na uchambuzi wa Takwimu za kiuchumi na kijamii pamoja na kuchambua sera na kuwianisha masuala muhimu katika kusimamia uchumi; na

-         Kuratibu na kuhakiki mapato na matumizi ya rasilimali za Taifa.

 

Utekelezaji

Katika mwaka 2002/03 serikali iliweza kutekeleza malengo yaliyowekwa katika sekta hii ambayo ni pamoja na:

-         Sensa ya watu na makazi ilifanyika kwa mafanikio mwezi August, 2002. Aidha, takwimu muhimu zinaendelea kukusanywa na kuzalishwa kwa wakati ili ziweze kutumiwa na wadau mbalimbali;

-         Mikakati ya kuongeza uwazi, na nidhamu katika matumizi ya fedha na rasilimali za umma, inaendelea kuzingatiwa, kwa mfano matumizi ya mfumo wa sasa wa bajeti ya serikali, (Medium Term Expenditure Framework (MTEF);

-         Jengo la Mahakama Kuu lilifanyiwa ukarabati na ujenzi wa Mahakama Kuu Bukoba ulianza. Aidha, Mahakama za Mwanzo 2 zimeimarishwa katika mikoa ya Arusha na Manyara chini ya mradi wa Quick Start;

-         Wizara na Taasisi mbalimbali za serikali ziliendelea kutekeleza mikakati na ratiba za kazi za kupambana na rushwa;

-         Sekta ya sheria iliendelea kutoa ushauri wa kisheria kwa Wizara na Taasisi za Serikali;

-         Utaratibu wa kushirikisha asasi za vikundi vya jamii zisizo rasmi katika mfumo wa sheria ulianzishwa;

-         Wanasheria 6 walipata mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi. Aidha, Mahakimu 59 walipelekwa kuchukuwa mafunzo ya Stashahada ya sheria na 14 cheti cha sheria;

-         Huduma za mahakama zimeboreshwa kwa nia ya kupunguza msongamano wa kesi. Hii ni pamoja na kuimarisha kitengo cha Polisi na Magereza kwa kuwaongezea fungu la fedha na kuwapatia polisi vitendea kazi; na

-         Kutekeleza mfumo wa kisheria na utafiti, pamoja na programu ya urekebishaji wa sekta ya sheria.

 

MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

 

Utangulizi

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika kipindi cha mwaka uliyopita imeendelea kutekeleza majukumu mbalimbali iliyopewa kwa kutumia mikakati mbalimbali. Majukumu ya kiutendeji ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni pamoja na kuratibu na kusimamia tawala za mikoa ili ziweze pia kuzisaidia halmashauri katika kutekeleza wajibu na majukumu yake; kusimamia na kutayarisha sera za maendeleo vijijini; kuboresha miundo, hali ya watumishi na mifumo ya kazi ndani ya ofisi yenyewe, mikoa na halmashauri; na kusimamia taasisi na miradi inayotekelezwa chini ya ofisi.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Katika kipindi cha mwaka 2002/03, miradi iliyopangwa kutekelezwa chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni pamoja na:

-         Programu ya Uboreshaji mfumo wa Serikali za Mitaa (Local Government Reform Programme) na Programu ya uimarishaji huduma Mijini;

-         Programu ya ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya na Shirika la Elimu Kibaha;

-         Programu ya usafiri na usafirishaji vijijini na mfuko wa pamoja wa sekta ya afya (Health Sector Programm Support); na

-         Programu ya uboreshaji wa sekta ya Elimu pamoja na Programu ya uimarishaji wa sekretarieti za mikoa.

 

Utekelezaji

Katika kipindi cha mwaka 2002/03, kanuni za utumishi wa serikali za mitaa katika manispaa, halmashauri za miji na wilaya zimeandaliwa zikiwa katika lugha ya kiingereza na kiswahili na kusambazwa kwa wadau. Aidha, halmashauri 25 kati ya 38 zilizo katika awamu ya kwanza ya mpango wa kuboresha serikali za mitaa zimeandaa na kukamilisha mipango ya mikakati (strategic plans) ya halmashauri zao.

 

Hadi kufikia Septemba 2002, ukarabati wa miundo mbinu katika miji ya Arusha, Moshi, Morogoro, Iringa, Mbeya, Mwanza, Dodoma na Tanga ulikuwa umefanyika. Aidha, Utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya mikoa na halmashauri, umefikia hatua mbalimbali za kuridhisha ikiwa ni pamoja na ukarabati na ujenzi wa nyumba za serikali, madarasa, nyumba za walimu, zahanati/vituo vya afya na barabara; uimarishaji wa huduma za afya na maji; uendeshaji na usimamizi wa mfuko wa miradi ya kujitegemea n.k.

 

Matatizo

Kwa ujumla utekelezaji wa miradi mbalimbali umekabiliwa na matatizo ya kutokupatikana au kuchelewa kutolewa kwa fedha za maendeleo kama zilivyoombwa. Aidha, hata fedha za nje hazikuweza kupatikana kutokana na kukosekana kwa “counterpart fund”.

 

PROGRAMU MAALUMU

 

HIFADHI YA MAZINGIRA

 

Utangulizi.

Hifadhi na usimamizi wa Mazingira ni muhimu katika kuhakikisha kuwepo kwa maendeleo endelevu nchini. Hivyo katika mwaka 2002/2003 sera na mipango ya maendeleo iliendelea kuelekezwa katika kupambana na matatizo sugu sita ya mazingira nchini ambayo yamepewa kipaumbele katika Sera ya Mazingira ya mwaka 1998. Matatizo hayo ni uharibifu wa ardhi, kutopatikana kwa maji safi na salama kwa wananchi wengi wa mijini na vijijini, uchafuzi wa mazingira kwa jumla, upotevu wa makazi ya viumbe hai na bioanuwai, uharibifu wa makazi ya viumbe wa majini na uharibifu na uchomaji ovyo wa misitu. Azma hii inaendana na malengo ya jumla ya nchi ya kutengemaza uchumi, kuboresha afya na maisha ya wananchi na vilevile kuondoa umaskini.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Katika mwaka 2002/2003 malengo na madhumuni kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira yalikuwa ni:

-         Kuoanisha masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira na kuyazingatia katika maandalizi ya program, bajeti na mipango ya maendeleo ya kitaifa na ki-sekta.

-         Kuzuia na kudhibiti uharibifu wa ardhi, mimea na uchafuzi wa maji na hewa nchini.

-         Kuhifadi baioanuwai na kuhakikisha matumizi endelevu na sawa ya rasilimali zilizopo

-         Kukuza weledi kwa wananchi kuhusu masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira.

 

Utekelezaji.

Ili kufikia malengo yaliyotajwa juu ya hifadhi na usimamizi wa mazingira kwa mwaka 2002/2003 shughuli zifuatazo zilitekelezwa:-

-         Awamu ya pili ya kuelimisha na kuhamasisha viongozi wa  ngazi za juu wa Wilaya, Miji na Manispaa kuhusu Sera mpya ya Mazingira ilifanyika katika Halmashuri za Manispaa, Miji na Wilaya zipatazo 45.

-         Rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Hifadhi ya Bioanuwai na Mpango wake wa utekelezaji ulikamilishwa.

-         Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa miradi ya Hifadhi ya Ziwa Victoria na Tanganyika ilikamilika ambapo protocol/ convention za kuhifadhi maziwa haya zimekamilika. Zaidi ya hayo, na Wadudu milioni 10 wanaokula magugu maji walizalishwa na kusambazwa kwenye Ziwa Victoria na vilevile miti milioni moja ilipandwa na utekelezaji wa miradi kadhaa ulifanyika katika kipindi hicho katika maziwa haya.

-         Taasisi mbal imbali zilishiriki katika kukuza weledi kwa wadau mbalimbali na wananchi wote kwa ujumla kuhusu umuhimu wa hifadhi na usimamizi bora wa mazingira hapa nchini kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile semina, warsha, midahalo, makongamano, vipindi maalum kwenye vyombo vya habari (Redio, Television, magazeti, vipeperushi, n.k), na kuandaa mafunzo mbalimbali na upashanaji habari kwa kutumia mawasiliano na teknolojia ya kisasa.

-         Vyombo na asasi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali zilitoa mafunzo na kuwahamasisha wenye viwanda kuhusu matumizi ya teknolojia sahihi zenye kupunguza/kuzuia uzalishaji wa taka za viwanda na majumbani na zenye kuzingatia maendeleo endelevu ya viwanda.

-         Mikakati ya kitaifa inayohusu utekelezaji wa maazimio na mipango ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa kuhusu mikataba ya UNCCD, CBD, UNFCC na RAMSAR iliandaliwa na kutekelezwa.

 

-         Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira liliendelea na utekelezaji wa program zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na programu maalum ya kutunza mfumo ikolojia wa korongo la Kihansi unaolenga kuhifadhi bioanuwai iliyopo hasa vyura wa manyunyu.

 

PROGRAMU YA KUONDOA UMASKINI

 

Utangulizi

Utekelezaji wa malengo ya jumla ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kuhusu kuondoa umaskini uliokithiri nchini na kufikia ubora wa hali ya juu, unaofanywa na Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Umaskini (PRSP), umebainisha maeneo mbalimbali ya utekelezaji. Baadhi ya maeneo hayo yatatekelezwa na sekta za elimu, afya, kilimo, jinsia pamoja na maswala ya kijamii. Aidha, mkakati huu unaendelea kutekelezwa katika ngazi mbalimbali kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Katika kipindi cha 2002/03-malengo makuu yalikuwa yafuatayo:

-         Kuondoa umaskini uliokithiri miongoni mwa wananchi na kufikia ubora wa juu wa maisha ifikapo mwaka 2025

-         Kuimarisha taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uratibu wa mipango ya kuondoa umaskini.

-         Kuimarisha rasilimali watu, mawasiliano, ushirikiano na ushirikishwaji wa wadau wote wa ndani na nje katika mapambano ya kuondoa umaskini nchini.

-         Kuelimisha na kuhamasisha Sera za kupunguza umaskini.

 

Utekelezaji

Programu ya umaskini katika kipindi cha 2002/03 ilitekeleza yafuatayo:

-         Taarifa ya maendeleo ya Makakati wa Kupunguza Umaskini (PRS) ya mwaka 2001/02 ilitayarishwa na kusambazwa;

-         Taarifa ya hali ya umaskini na maendeleo (PHDR 2002) imechapishwa;

-         Taarifa za tafiti za matumizi kikaya (HBS 2000/01) na hali ya ajira (intergrated Labour Force Survey 2000/01) nchini imetayarishwa na kusambazwa;

-         Zoezi la kukusanya maoni kutoka vijijini yanayohusu uwiano wa idadi ya watu na mkakati mzima wa kuondoa umaskini lilifanyika (Participatory Poverty Assessment);

-         Mikutano na warsha mbalimbali iliyowahusisha wadau mbali mbali kuhusu umaskini, ikiwemo uendeshaji wa wiki ya Umaskini ilifanyika; na

-         Utayarishaji pamoja na usambazaji wa mwongozo wa kutathmini (Poverty Monitoring Master Plan) makakati wa kupunguza umaskini umefanyika.

 

 

PROGRAMU YA KUDHIBITI UKIMWI

 

Utangulizi

Tanzania inatambua athari kubwa inayokumba juhudi zake za maendeleo kutokana na janga la UKIMWI. Hali hii imefanya serikali kuchukua hatua madhubuti kwa kuhusisha sekta mabimbali ambazo zimekuwa zikifanya kazi kwa utaratibu wa pamoja. Pia mwitikio wa wananchi umepata nguvu zaidi kutokana na kujihusisha kikamilifu kwa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa katika kushughulikia janga hili.

 

Mapitio ya mwaka 2002/03

Madhumuni na Malengo

Katika kutekeleza Sera ya kudhibiti UKIMWI shughuli zifuatazo zilipangwa kutekelezwa katika kipindi cha mwaka 2002/03.

-         Kuzuia kuenea kwa UKIMWI kunatokana na tabia isiyo salama ya kujamiana

-         Kupunguza tabia ya kujamiana kama mkakati wa kuondoa umaskini

-         Kuhamasisha kukubalika kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ili kupunguza unyanyapaa

-         Kuhakikisha usalama wa huduma ya damu wanazopewa wagonjwa

-         Kutoa tiba ipasavyo kwa watu walioathirika kwa magonjwa ya zinaa

-         Kutoa elimu ya UKIMWI katika mashule yote na sehemu zote za kazi

-         Kuchukua hatua madhubuti za kuelimisha umma kuhusu kuachana na mila ambazo zinaendeleza kusambaa kwa UKIMWI

 

Utekelezaji

Katika kipindi cha 2002/03 Programu ya Ukimwi imetekeleza yafuatayo:

-         Uzinduzi na usambazaji wa nakala zaidi ya milioni 15 za Sera ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ambazo zimetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili kwa wadau mbalimbali

-         Kukamilishwa kwa wigo wa kitaasisi kwa ajili ya mkakati wa uongozi, kuratibu sekta mbalimbali, kufanya ufuatiliaji na tathmini kuhusiana na virusi vya UKIMWI (VVU/UKIMWI)

-         Kuhakikisha kuwa kila sekta na jumuiya zimejihusisha kikamilifu katika utengenezaji na utekelezaji wa mbinu za kupambana na VVU/UKIMWI

-         Kuchapisha vijitabu karibu 700,000 na kusambazwa mashuleni kama njia ya kuimarisha kampeni dhidi ya VVU/UKIMWI

-         Kutoa elimu ya afya kwa umma juu ya kinga dhidi ya UKIMWI pamoja na mbinu za huduma ya matibabu kwa wagonjwa

-         Kuhimiza wananchi kupima hali zao ya kiafya kwa hiari na kutoa ushauri nasaha wa kitaalam

-         Kuratibu utafiti kuhusiana na ugonjwa huu wa UKIMWI

-         Kuhakikisha usalama wa damu wanazopewa wagonjwa.

 

MASUALA YA JINSIA

 

Utangulizi

Madhumuni makuu ya serikali katika masuala ya Jinsia ni kuwa na sera ambayo inaleta usawa wa kinjisia pamoja na usawa katika mgawanyo wa rasilimali. Usawa unasaidia katika kusukuma ukuzaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa ujumla.

 

Kufuatana na sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agost mwaka 2002, Idadi ya Watanzania wote ni 34,568,609 millioni na kati ya hawa wanawake ni 12,558,530 millioni sawa na asilimia 51.1 na wengi wao wanaishi vijijini na ni wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula na biashara. Karibu asilimia 88 ya wanawake wote wanafanya shughuli mbalimbali ambazo hazina kipato kinachotambulika.

 

Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshughulikia masuala ya jinsia inaendelea kuhimiza uingizaji wa masuala ya jinsia katika sera, mipango na bajeti.

 

Mapitio ya Mwaka 2002/03

Madhumuni na malengo

Malengo makuu ya serikali kuhusu masuala ya jinsia kwa mwaka 2002/03 yalikuwa kama ifuatavyo:

-         Kuwa na mipango ya makusudi ya kuwapa uwezo wanawake waliopo katika utumishi wa serikali na mashirika yake fursa sawa za ajira na upandishaji wa vyeo

-         Kufundisha na kuelekeza wizara, Mikoa, na wilaya kuweza kupanga mipango na kuandaa bajeti zinazozingatia masuala ya jinsia

-         Kufanya utafiti wa kuwa na vitengo vya jinsia katika ofisi za serikali na mashirika ya umma

 

Utekelezaji

-         Wizara Mikoa na Wilaya zote zilipewa mafunzo ya jinsi ya kupanga mipango na bajeti zinazozingatia masuala ya jinsia sambamba na mafunzo ya Mfumo wa Bajeti wa Muda wa Kati (Medium Term Expenditure Framework-MTEF).

-         Utafiti wa kuwa na vitengo vya jinsia maofisini umekamilika (Gender focal points)

SURA YA TATU

 

MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2003/04

 

MISINGI YA MPANGO NA BAJETI

Katika mwaka 2003/04 shabaha ya mpango ni kuendeleza utekelezaji wa mkakati wa kupambana na umaskini pamoja na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Mkakati wa kupambana na umaskini pamoja na kufuatilia utekelezaji wake vilijumuishwa katika mfumo wa bajeti tangu mwaka wa fedha ulioishia Juni 2002.

 

Kwa kuzingatia mapitio ya mwenendo wa uchumi na bajeti ya mwaka 2002/03 ni dhahiri kwamba jitihada zaidi zinatakiwa ili kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza umaskini na kuongeza kiwango cha ukuaji wa uchumi. Aidha, mapitio na matarajio ya makubaliano kati ya serikali na wahisani mbali mbali yamezingatiwa.

 

Mpango wa mwaka 2003/2004 umezingatia vipaumbele vilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 vya uendelezaji rasilimali watu, usalama na uhakika wa chakula, kukuza ajira na kuongeza mapato ya fedha za kigeni. Ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele hivyo, mkazo umewekwa katika kujenga mazingira mazuri kwa wadau ikiwa ni pamoja na wawekezaji mbalimbali katika maeneo ya huduma za jamii na za kiuchumi na nyanja nyinginezo zinazojumuisha, ardhi, utawala bora, usalama na amani, hifadhi ya mazingira, masuala ya jinsia na vita dhidi ya UKIMWI.

 

Malengo ya jumla ya mpango na bajeti kwa mwaka 2003/04 ni kama ifuatavyo:

-         Kukuza uchumi kwa kiwango cha asilimia 6.3 mwaka 2003, hadi asilimia 7.4 mwaka 2006;

-         Kupunguza kasi ya upandaji bei kufikia kiwango cha asilimia 4.0 ifikapo Juni 2004 na kuendelea kulingana na viwango vya nchi tunazoshirikiana nazo kibiashara;

-         Kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ya serikali kwa kiwango cha asilimia 13.2 ya Pato la Taifa la mwaka 2003/04 asilimia 13.5 mwaka 2004/05 na asilimia 13.7 mwaka 2005/06;

-         Kudhibiti ujazi wa fedha (M2) kwa viwango vinavyowiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na kupunguza kasi ya upandandaji bei; na

-         Kuongeza akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi mitano.

 

Mwelekeo wa mpango na Bajeti:

Makadirio ya mapato na matumizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali yanaonyesha mwelekeo ufuatao:

Tsh (‘000’)

 

2001/02

Halisi

2002/03 Makadirio

2002/03

Mwelekeo

A.MAPATO YA NDANI

1,042,945

1,172,297

1,183,743

1.Mapato yatokanayo na kodi

938,478

1,066,899

1,097,643

 Ushuru wa Forodha

88,708

109,440

160,126

 Kodi za Mauzo ya nje na ndani

177,615

203,927

193,267

 Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)

351,893

394,300

409,564

  Bidhaa toka nje

208,674

243,505

241,009

  Bidhaa za ndani

143,219

150,794

168,555

  Kodi ya Mapato

219,852

240,920

298,289

  Kodi nyingine

100,410

118,313

36,397

2.Mapato yasiyotokana na Kodi

104,467

105,398

86,100

B.JUMLA YA MATUMIZI

1,462,767

2,106,290

1,844,160

  1.Matumizi ya Kawaida

1,118,156

1,386,163

1,401,423

  2.Matumizi ya Maendeleo

344,611

720,127

447,737

   Fedha za ndani

50,236

95,662

95,662

  Fedha za nje

294,375

624,465

347,075

  Mfuko wa Songosongo

-

-

-

C.NAKISI/SALIO (A-B)

-419,823

-933,993

-660,417

D. KUZIBA NAKISI

 

 

 

  1.Fedha kutoka nje

503,670

890,738

719,154

   Ruzuku

385,200

542,298

472,348

   Mikopo ya kibajeti (Programme/Budget Support Loan

33,171

110,801

134,566

   Mikopo ya miradi

154,184

340,561,

198,200

   Kulipia madeni ya nje (amortization)

-68,885

-102,922

-85,960

 2.Fedha za ndani

-83,849

43,254

-58,736

Mikopo isiyo ya mabenki

36,574

9,000

9,000

Mikopo ya mabenki

-59,181

21,254

21,655

Mapato ya Ubinafsishaji

0

18,000

0

Kulipa madeni ya nyuma (arrears)

-59,107

0

0

Kuongeza mitaji ya mabenki Mashirika

-

-

-

Marekebisho (Adjustment to Cash)

33,564

-

-

Kulipa madeni ya ndani (amortization)

-1,552

-10,000

-10,000

Expenditure float

-34,147

-

-79,391

Recovery of NBC Bond

-

5,000

-

 

 

Shabaha ya Mpango na Bajeti:

Shabaha kuu ya mpango na Bajeti ni kusaidia ufuatiliaji na utekelezaji wa mkakati wa kupambana na umaskini katika ngazi ya taifa na halmashauri. Aidha, Mpango na Bajeti wa mwaka 2003/04 unalenga katika maeneo yafuatayo:

-         Kudumisha haki na amani – kwa kuhakikisha kwamba vyombo vya sheria na usalama vimejumuishwa kikamilifu katika mipango na bajeti ili kupambana na uhalifu

-         Kutengemaza na kukuza uchumi – kwa kutumia sera madhubuti za uchumi ili kuzuia mfumuko wa bei, kuvutia wawekezaji na kushiriki kikamilifu katika ushindani wa kimataifa

-         Kuimarisha serikali za mitaa na halmashauri kwa kuzipa madaraka zaidi na kuziwezesha kuandaa na kutekeleza mipango na bajeti na kuweka taratibu zilizowazi za kutoa ruzuku kwa halmashauri hizo

-         Kukuza sekta binafsi – kwa kuweka mazingira mwafaka kwa kuzingatia marekebisho katika sera na taratibu, kuimarisha miundombinu na kuelekeza taasisi na vyombo vya fedha kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha watu kuweka akiba na kukopa toka vyombo hivyo

-         Kubuni mipango na bajeti ambazo ni kamilifu – kwa kuzingatia masuala ya usawa, mazingira, na kupiga vita rushwa

-         Mfumo unaofaa wa kufuatilia utekelezaji wa mkakati wa kupambana na umaskini – kuwa na vigezo bayana kuhusu maendeleo ya sekta ya vijiji, kilimo, ushirikishwaji wa wananchi na kupungua kwa umaskini katika ngazi za wilaya na halmashauri

-         Kuimarisha mageuzi katika sekta ya umma - kwa kuhakikisha uwajibikaji, kuendesha shughuli za serikali ki-uwazi na kushirikisha jamii pamoja na kupiga vita rushwa

-         Kuongeza mishahara ya wafanyakazi kwa awamu ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa jamii.

 

Sekta zilizopewa kipaumbele

Sekta zilizopewa nafasi muhimu kwa ajili ya kuchukua hatua za kisera na kupewa kipaumbele katika mgawanyo wa rasilimali ni pamoja na:

 

a)     Elimu – Kuboresha Elimu kwa kuongeza ubora na idadi ya shule za msingi na sekondari, matumizi bora ya rasilimali na kuijengea jamii uwezo wa kushiriki katika kuzihudumia shule

 

b)     Afya – Kukarabati miundombinu ya afya, kuhamasisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na kuboresha uongozi wa huduma za bima ya afya

 

c)     Ukimwi – Kutekeleza sera kamilifu ya kupambana na maambukizi ya ukimwi na kuboresha huduma za msingi za afya

 

d)     Maji – Kujenga, kukarabati na kuongeza skimu za maji, kuvuna maji ya mvua, kufanya utafiti juu ya rasilimali za maji na kutoa mafunzo maalumu kwa ajili ya wataalam katika sekta;

 

e)     Kilimo - Kuongeza tija na uzalishaji kwa kuboresha huduma za ugani, umwagiliaji, utafiti na masoko pamoja na kuboresha mazingira ili kuvutia ushiriki wa sekta binafsi

 

f)       Barabara - Kukarabati na kuboresha mtandao wa barabara, kuzifanyia ukarabati barabara za wilaya na mikoa pamoja na kuhamasisha jamii kushiriki katika uboreshaji wa barabara zao

 

g)     Utawala bora – Kuimarisha na kuboresha vyombo vya sheria na usalama, kutekeleza mikakati ya kupiga vita rushwa na kuboresha matumizi ya fedha za umma

 

h)     Takwimu muhimu – Kutoa takwimu sahihi na kwa wakati kwa ajili ya kuboresha sera, sheria, mikakati na mipango.

 

Maeneo mengine muhimu:

Ili kufanikisha juhudi za kupiga vita umaskini na kuimarisha ukuaji wa uchumi maeneo yafuatayo pia yatapewa kipaumbele:

 

a)     Nishati  - Upanuzi wa uzalishaji na usambazaji wa umeme, upanuzi wa matumizi ya umeme sehemu za vijijini pamoja na kuhamasisha matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati ikiwa ni pamoja na mionzi ya jua, upepo, makaa ya mawe, n.k.

 

b)     Viwanda – Kushawishi sekta binafsi kuwekeza katika usindikaji wa mazao, kuzalisha nishati, maji, mawasiliano, usafirishaji, utafiti (R&D) kwa kuzifanyia mapitio sheria na taratibu ili kuvutia uwekezaji wengi zaidi

 

c)     Ardhi - Kuweka mazingira yatakayohakikisha miliki ya ardhi na kuepusha matumizi mabaya ya ardhi ikiwa ni pamoja na ujenzi holela

 

d)     Madini – Kujenga uwezo wa wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mafunzo, teknolojia na taarifa za Masoko

 

e)     Utalii - Kuboresha na kukarabati miundombinu pamoja na kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo.

 

f)       Maendeleo Vijijini – Kuchukua hatua za kuhakikisha upatikanaji wa mikopo, masoko ya nje, kufufua viwanda vya kusindika mazao, kuondoa kodi mbali mbali ambazo ni kero kwa wakulima na wafugaji, kurahisisha biahsara na nchi jirani pamoja na kusambaza mbegu bora za mazao na mifugo kwa wakulima.

 

Muhtasari wa Bajeti ya Mpango:

Katika kipindi cha 2003/04 mpango na Bajeti ya Maendeleo umelenga katika kuimarisha mafanikio yaliyokwisha patikana katika kuongeza ukuaji wa uchumi na kuondoa umaskini uliokithiri.  Bajeti ya Maendeleo inakisiwa kufikia Tsh 807,440,576,900 kati ya hizo Tsh 165,724,798,200 zitapatikana toka vyanzo vya ndani na Tsh 641,715,778,700 ni za kutoka nje. Kwa upande wa fedha za ndani Tsh 771,949,619,700 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi na programu za wizara na Tsh 35,490,957,700 ni kwa ajili ya kutekeleza programmu na miradi mbali mbali ya mikoa na halmashauri za wilaya na miji.

 

MUHTASARI WA BAJETI YA MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2003/04  KWA SEKTA KUU

                                                                                                                        Tsh ‘000’      

 

Fedha za Hapa

Fedha za Nje

Jumla

HUDUMA ZA JAMII

 

 

 

Elimu

4,633,718.2

70,863,356.1

75,497,074.3

Afya

3,552,448.2

24,148,846.6

27,701,294.8

Maji na Mifugo

7,096,856

43,657,350

50,754,196

HUDUMA ZA KIUCHUMI

 

 

 

Barabara na Mawasiliano

46,369,000

104,201,683

150,570,683

Nishati na Madini

5,119,552.3

96,892,000

102,091,552.3

Ardhi

600,000

-

600,000

HUDUMA ZA UZALISHAJI MALI

 

 

 

Kilimo

6,436,433.2

25,081,541

31,517,964.2

Maliasili na Biashara

952,586,3

30,341,201.5

31,477,787.8

Viwanda na BiasharaI

200,000

1,620,469

1,820,469

UTAWALA

 

 

 <