HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA FREDERICK T. SUMAYE (MB)

WAKATI WA KUAHIRISHA BUNGE, TAREHE 9 APRILI 2003

 

        Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa hotuba yangu ninapenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kutoa salaam zangu za rambirambi kwa familia ya Jaji Mkuu Mstaafu Marehemu Francis Lucas Nyalali.  Marehemu Nyalali alikuwa mfano wa kuigwa kwa jinsi alivyosimamia kazi zake katika misingi ya haki.  Amekuwa Jaji Mkuu kwa miaka 23 na hivyo alikuwa kisima kikuu cha busara na hekima nchini mwetu.  Tunaiombea familia ya marehemu uvumilivu na subira katika wakati huu mgumu wa majonzi makubwa na tunamwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.  Amina.

        Mheshimiwa Spika, kazi zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge lako Tukufu zimekamilika.  Katika mkutano huu Waheshimiwa Wabunge wamepitisha miswada sita ya sheria na kuridhia maazimio matatu.  Aidha, Serikali imejibu maswali ya msingi 102 ya Waheshimiwa Wabunge na mengine mengi ya nyongeza.

 

        Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu Bunge lako Tukufu limepitisha miswada ya sheria yenye manufaa mbalimbali kwa maendeleo ya Taifa letu. Moja ya miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Nishati ya Atomiki ya mwaka 2003 inayoweka mazingira muafaka ya uendelezaji wa matumizi salama na ya amani ya nishati ya atomiki, teknolojia ya nyuklia na pia kuweka mfumo madhubuti wa kinga dhidi ya madhara ya mionzi.

        Matumizi ya nishati ya atomiki yatatuhakikishia kuwepo kwa nishati rahisi na yenye uhakika na hivyo kutuwezesha kuzalisha mali kwa haraka kwa gharama nafuu na kwa wingi.  Nchi yetu hivi sasa inategemea umeme unaotokana na maporomoko ya maji, mafuta na baadaye gesi ya Songo Songo.  Vyanzo hivi vya nishati hutupatia umeme ambao ni aghali na usioaminika sana kutegemeana na hali ya hewa na upatikanaji wa mafuta katika soko.  Nguvu ya nyuklia itatatua matatizo haya kwa kutupatia nishati ya uhakika na ya bei nafuu jambo ambalo litasaidia sana kukuza uchumi wetu.

 

        Mheshimiwa Spika, mbali na kuweka mazingira ya uendeshaji wa matumizi ya nishati ya atomiki, muswada huu unaweka pia masharti ya kulinda afya za wananchi kwa kudhibiti matumizi ya vyakula vilivyochafuliwa na mionzi na unaweka kinga dhidi ya madhara yote yanayotokana na mionzi kwa binadamu, wanyama, mimea na mazingira.

 

        Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limepitisha pia Muswada wa Sheria ya Ushindani wa Haki wa Mwaka 2003 (The Fair Competition Bill, 2003).  Katika dunia ya leo yenye uchumi huria na utandawazi, ushindani wa kibiashara mara nyingi sio wa haki kama haudhibitiwi.  Mara nyingi makampuni makubwa huweza kuunda vikundi vya kupanga bei, kufanya makubaliano ya kupunguza uzalishaji, kupanga bei ya zabuni, n.k. mambo ambayo huathiri mwenendo wa uchumi.  Aidha, baadhi ya wafanyabiashara wanayo pia tabia ya kudanganya kuhusu viwango vya ubora wa bidhaa zao na matumizi yake.

 

        Muswada huu ni muhimu sana kwa kuwa unaweka utaratibu muafaka wa kusimamia mashindano katika biashara, unalenga katika kudhibiti matumizi mabaya ya nguvu za soko na kuhakikisha kwamba maadili mema ya kibiashara yanafuatwa na kila mmoja na hatimaye kumlinda mlaji.  Moja ya maadili hayo ni pamoja na kuhakikisha kwamba taarifa muhimu zinaonyeshwa kwenye bidhaa kuhusu usalama wa bidhaa husika.  Masharti haya ya kusimamia ushindani halali wa biashara ni kigezo muhimu katika kuvutia biashara za kimataifa na uwekezaji kutoka nje.  Sheria hii itasaidia sana uchumi wetu katika nyanja hizi za uwekezaji.

 

        Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limepitisha pia Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Kuratibu Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2003 (The Tanzania Communications Regulatory Authority).  Madhumuni ya Muswada huu ni kuanzisha mamlaka mpya ya udhibiti wa sekta za mawasiliano.  Mamlaka hii itasimamia shughuli za watu na taasisi zinazoendesha biashara ya mawasiliano kwa njia ya simu, matangazo ya redio na televisheni, utoaji wa huduma za posta na teknolojia ya elektroniki.  Muswada huu unaweka mamlaka ya udhibiti ili kuwasimamia kwa karibu watoaji huduma hizi za mawasiliano.  Katika kuwasimamia, mamlaka hii imepewa uwezo wa kutoa leseni na kufuta leseni kwa wale watakaokwenda kinyume na viwango (standards) vya utoaji huduma vilivyowekwa na kusimamia upangaji wa bei (rates and charges) za huduma hizi kwa walaji na kuzingatia kuwa huduma hazileti athari kwa maadili ya jamii.

 

        Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limepitisha Muswada wa Sheria ya Kuifanyia Marekebisho Sheria ya Mikopo,  dhamana na Misaada ya Mwaka 2003 kwa madhumuni ya kusimamia vizuri zaidi ukopaji kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi kwa kuifanyia marekebisho Sheria ya Bunge namba 30 ya Mwaka 1974 iliyokuwa ikisimamia ukopaji huo.

 

        Muswada unalenga kuweka sheria ya kusimamia kwa karibu Deni la Taifa na kuandaa utaratibu mpya wa kusimamia madeni ya Taifa ili Serikali iweze kujua deni halisi la ndani na la nje kwa wakati wowote.  Muswada pia unampa Waziri wa Fedha mamlaka ya kisheria ya kukopa ndani na nje na kutoa dhamana kwa niaba ya Serikali na kupiga marufuku mtu mwingine yeyote kuiingiza Serikali katika madeni.  Katika kutekeleza wajibu wake, Waziri wa Fedha atakuwa anashauriana na Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Madeni.  Lengo ni kuweka udhibiti madhubuti katika kukopa, matumizi ya mikopo hiyo na matumizi ya fedha za misaada kutoka nje.  Muswada huu ni muhimu sana kwa uchumi wetu na kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi wetu.  Aidha, ni muswada muhimu sana kwa washiriki wetu katika maendeleo kwa sababu unaweka udhibiti mzuri katika ukopaji wa Serikali.

 

        Mheshimiwa Spika, Bunge pia limepitisha muswada wa sheria unaounda Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (Tanzania Civil Aviation Authority) ili kusimamia huduma zote za usafiri wa anga.  Lengo ni kuwa na mamlaka itakayosimamia na kuratibu shughuli hii muhimu na kuhakikisha kuwa usalama wa anga yetu hauathiriki wala usalama wa raia kudhurika.  Mamlaka hii ni muhimu kwa uchumi wetu kwa sababu biashara za mataifa zinategemea sana uwingi na usalama wa usafiri na usafirishaji katika nchi husika.  Bunge pia limepitisha Muswada wa Kufanya Marekebisho katika Sheria Mbalimbali kwa lengo la kuziboresha au kuendana na sheria zingine zilizotungwa.

 

        Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema mwanzoni, Bunge lako Tukufu limepitisha pia maazimio matatu.  Moja ya maazimio hayo ni lile linalohusu Kuridhia Mkataba wa Usafirishaji kwa Njia za Barabara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliotiwa saini tarehe 29 Novemba, 2001.  Mkataba huu ni muhimu sana katika kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa vile unahuisha (harmonize) mambo muhimu kama vile kodi, ada na ushuru vinavyotozwa mipakani, unaweka uwiano wa kisheria katika matumizi ya barabara, unaondoa ucheleweshaji wa mizigo mipakani na kurahisisha safari za wananchi kwenda nchi nyingine ya Jumuiya.

 

        Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limepitisha pia azimio la kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Afrika Mashariki kuhusu ushirikiano katika kuhakiki na kuthibitisha viwango vya ubora wa bidhaa na vipimo (Protocol on Co-operation in Standardization, Quality Assurance, Metrology and Testing).  Itifaki ya mkataba huu ilisainiwa tarehe 15 Januari 2001 na Mawaziri wa nchi zetu tatu ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Itifaki hii ni muhimu sana katika kuendeleza biashara baina ya nchi yetu, Kenya na Uganda kwa sababu inaondoa vikwazo vya biashara vinavyotokana na tofauti katika ubora wa viwango vya bidhaa, mizani na vipimo.  Maendeleo ya biashara mahali popote duniani yanategemea sana ubora wa bidhaa zinazozalishwa.  Bidhaa duni haziwezi kushindana kikamilifu na kupata bei nzuri katika soko la karne hii.

        Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limepitisha pia azimio la kuridhia Mkataba wa Ushirikiano wa kiuchumi, kisayansi na kiufundi baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Korea (Agreement on Economic, Scientific and Technical Co-operation between the Government of the Republic of Korea and the Government of Tanzania).  Mkataba huu ulitiwa saini na nchi hizi mbili huko Seoul, Korea tarehe 18 Desemba, 1998.  Mkataba huu ni muhimu sana kwa nchi yetu kwa kuwa unatupa fursa ya kukuza uwezo wetu wa kitaaluma na utafiti, kupata elimu ya juu na ile ya ufundi kutokana na kubadilishana wataalam, matokeo ya tafiti mbalimbali, majarida, habari za kitaalam na kushiriki katika semina, makongamano na mikutano mingine ya aina hiyo baina ya nchi hizi mbili.

        Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa ufafanuzi kwa kifupi wa yale tuliyofanyia kazi Bungeni kwa manufaa ya wananchi, naomba sasa nizungumzie maeneo mengine muhimu yafuatayo:

 

        Mheshimiwa Spika, hivi sasa kuna vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati kati ya Marekani na Washirika wake dhidi ya Iraq.  Matumaini ya kila mmoja wetu ni kuwa vita hivyo vitakwisha haraka ili visilete madhara makubwa kwa uchumi wa dunia.  Pamoja na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali yetu za kupunguza madhara yanayoweza kuletwa na vita hivi kama alivyoelezea Mheshimiwa Rais Mkapa katika hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi Machi, 2003, ni vema wananchi kwa upande wetu tukachukua tahadhari muhimu kwa maana hasa ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.  Kwa mfano, gharama za mafuta zinaonekana kupanda, tupunguze matumizi ya mafuta yasiyo ya lazima, n.k.  Bado hatujajua biashara itaathirika kiasi gani na hivyo kuathiri mapato ya Serikali kwa sababu athari hii hujitokeza polepole na kukaa kwa muda mrefu.  Hivyo, tunahitajika kuwa waangalifu sana katika matumizi ya fedha kwa sababu kama mapato yataathirika, kwa vyovyote vile matumizi pia yataathirika.

 

        Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Mkapa katika hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi niliyoitaja alizungumzia kwa kirefu sana juu ya athari za hali ya hewa inayotukabili nchini hivi sasa.  Sitaki kurudia yote aliyoyasema Mheshimiwa Rais lakini nasisitiza tu kuwa mvua alizotuasa Mheshimiwa Rais tuzitumie vizuri ndizo hizi zinazonyesha sasa katika baadhi ya maeneo nchini mwetu.  Tunachotakiwa ni kuzitumia mvua hizi kwa ukamilifu kadri inavyowezekana.  Hotuba ya Rais imeweka maelekezo mengi bayana katika suala hili.  Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wote watapelekewa nakala za hotuba hiyo kwa utekelezaji.  Hivyo, utekelezaji huo uanze mara moja kwa usimamizi wa matumizi ya mvua hizi zinazonyesha sasa na mengine yafuatie.  Kama nyongeza kwa maelekezo haya ya Rais, Wakuu wa Mikoa pia wamepelekewa maelekezo mengine kutoka kwa Waziri wa Kilimo na Chakula na kutoka kwa Waziri Mkuu.

 

Mheshimiwa Spika, leo mwezi Aprili 2003 ni mwaka wa saba na nusu wa uongozi wa awamu ya tatu yaani uongozi wa Rais Mkapa na mwaka wa pili na nusu wa kipindi cha pili cha awamu hiyo ya tatu.  Kipindi cha miaka saba na nusu sio haba lakini siyo kikubwa kwa maana ya uongozi wa nchi.  Katika vipindi mbalimbali vilivyopita na hata hivi sasa kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiandika makala mbalimbali katika vyombo vya habari, hasa baadhi ya magazeti kuilaumu Serikali ya Rais Mkapa na kwa mjumuiko Chama cha Mapinduzi kuwa hakuna lolote lililofanyika na hali za wananchi zimeendelea kuwa duni zaidi.  Inawezekana kabisa haya yanasemwa kwa sababu kipindi cha miaka saba na nusu kwa wengine ni kipindi kirefu sana na huenda watu wamesahau yaliyotokea tangu wakati huo hadi sasa.  Lakini pia inawezekana sana wengine hawana habari ni nini kimetokea katika miaka hiyo saba na nusu au hata katika hii miaka miwili na nusu ya kipindi hiki cha pili cha awamu ya tatu.

 

Mheshimiwa Spika, lengo langu siyo kulinganisha awamu zingine na awamu ya tatu, la hasha!  Kwanza awamu zote tatu zilikuwa chini ya CCM na mzazi wake CCM yaani TANU.  Aidha, kila awamu imeishi chini ya mazingira tofauti na nyingine na kila awamu imekuwa na mafanikio yake na matatizo yake pia.  Na muhimu zaidi, kwa vile zote zilikuwa chini ya CCM, kila awamu iliyopewa madaraka na wananchi iliendeleza yale yaliyofanywa au kuanzishwa na awamu iliyotangulia.  Nitataja tu baadhi ya vipengere ili kujibu baadhi ya hoja zinazojitokeza.

 

Hali ya Uchumi:

 

        Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi wetu imeendelea kukua.  Tangu awamu ya tatu ilipoingia madarakani ukuzaji wa uchumi umeendelea kwa kuendeleza marekebisho (reforms) katika sekta mbalimbali.  Marekebisho hayo yamefanyika katika vyombo vya fedha na mabenki, utumishi wa umma, sekta binafsi, mashirika ya umma na hata katika mfumo wa siasa.  Matokeo ya juhudi hizi zote ni mazuri kwani    uchumi wetu umekua kwa wastani wa asilimia 3 hadi kufikia zaidi ya asilimia 5.5.  Aidha, sekta binafsi imeweza kuchukua nafasi yake stahili ya kipaumbele katika kuendesha uchumi wetu.  Mapato ya fedha za kigeni nayo yaliongezeka na mfumuko wa bei uliteremka kutoka wastani wa asilimia 30 mwaka 1995 mpaka wastani wa asilimia 4.5 hivi sasa.  Kwa ajili ya kufanya vizuri katika kurekebisha na kuendesha uchumi wetu, nchi yetu ilifanikiwa kukubaliwa kuingizwa katika mpango wa nchi maskini zinazo samehewa madeni, yaani HIPC na kuwa moja ya nchi nne duniani kufanikiwa kuingia katika mpango huo. Mpango huu umekuwa na manufaa sana kwa nchi yetu kwa sababu tumeweza kuwa na uwezo zaidi wa kuhudumia huduma mbalimbali za jamii kwa sababu HIPC hutupatia unafuu wa fedha katika bajeti yetu, hutuwezesha kukopa fedha kwa miradi muhimu na husaidia kuwavutia wawekezaji kwa sababu ya kuwa na imani na jinsi uchumi wetu unavyoendeshwa.    Kuna watu wanaodhani kuwa kigezo cha kuingia HIPC ni umasikini.  Hiyo siyo kweli.  Kigezo muhimu sana ni jinsi unavyosimamia uchumi wako kwa umakini kwa kufuata misingi inayokubalika ya kiuchumi.  Tanzania tumefikia na kuvuka kigezo hicho.  Ninapenda kumpongeza sana Rais Mkapa kwa juhudi kubwa aliyoiweka katika kukuza na kusimamia uchumi wetu.

 

Mapato na matumizi ya Serikali:

 

        Mheshimiwa Spika, hali ya mapato ya Serikali mwaka 1995 ilikuwa ni duni sana.  Serikali yetu ilikuwa inakusanya wastani wa shilingi bilioni 27 hadi 30 kwa mwezi.  Hali hii hivi sasa imebadilika na wakati mwingine mapato yetu yanafikia shilingi bilioni 100 kwa mwezi.  Aidha, kabla ya mwaka 1996 nchi yetu ilikuwa imenyimwa misaada na mikopo kutoka nje kwa sababu ya mazingira ya uchumi tuliyokuwa nayo.  Hivi leo kwa sababu ya kufanya vizuri katika uchumi sasa tunapata misaada na mikopo.  Katika kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo hali yetu ya mapato bado ilikuwa ngumu hivyo matumizi yetu yalikuwa kwa misingi ya kutumia kile tunachopata, yaani Cash Budget.  Kwa hiyo, hatukuwa na fedha za maendeleo na wakati mwingine hata fedha za matumizi ya kawaida hazikupatikana kwa vipindi virefu hali iliyoathiri sana ufanisi katika utendaji wa Serikali.  Matumizi ya Cash Budget pia huathiri sana usafi wa taarifa za ukaguzi wa hesabu za Serikali.  Hii hutokana na kuwa fedha zinazopatikana katika siku au mwezi wa mwisho wa mwaka wa fedha wa Serikali, taarifa zake ni vigumu sana kuwahi ukaguzi hasa kama fedha hizo zimepelekwa katika wilaya za pembezoni.  Aidha, uduni wa mawasiliano kati ya mikoa na wilaya hizo na mikoa na Dar-es-Salaam huzidisha pia tatizo hili.  Kwa sababu hii, wapo baadhi ya watu ambao hutumia taarifa hizi kuishambulia Serikali kana kwamba fedha hizo zote zimeibiwa.  Baada ya taarifa za ukaguzi kutoka, maafisa wahasibu hujibu hoja mbalimbali za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali na kwa sehemu kubwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu ameridhika sana na majibu yanayotolewa na Serikali.

 

Huduma za Jamii na kupambana na umasikini:

 

        Mheshimiwa Spika, moja ya kigezo muhimu cha kupima hali ya umasikini ni jinsi huduma za jamii zinavyopatikana.  Penye umasikini uliokithiri huduma hizi huwa duni sana.  Lakini uboreshaji wa huduma za jamii nayo ni nyenzo muhimu ya kupambana na umasikini.  Kwa mfano, kama una taifa lenye elimu nzuri, lenye wananchi wenye afya nzuri, kuna njia nzuri za mawasiliano, n.k. ni nyenzo muhimu sana kwa taifa hilo kusonga mbele na kuachana na umasikini.  Kwa sababu ya umuhimu huo, Serikali ilitoa kipaumbele katika kuelekeza rasilimali chache ilizonazo katika sekta za huduma za jamii.  Kipaumbele hicho kilihusiana na fedha zetu wenyewe na fedha za washirika wetu katika maendeleo.  Kwa mfano, fedha za mfuko wa madeni na fedha za HIPC, sehemu kubwa zilielekezwa katika sekta za huduma za jamii kama mbinu za kupambana na umasikini.  Kwa sababu hiyo, kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta hizo kama nitakavyozielezea:


 

        ELIMU:

        (i)  Elimu ya Msingi

        Mheshimiwa Spika, ilani za uchaguzi za CCM ya mwaka 1995 na ya mwaka 2000 zote zimeweka msisitizo sana katika elimu ya msingi kama haki ya mtoto wa Tanzania.  Katika kutekeleza ilani hizo Serikali imefanya kila juhudi kufikia malengo yaliyokusudiwa.  Sote tunaelewa mapungufu makubwa yaliyokuwepo katika elimu yetu ya msingi.  Vyumba vya madarasa vya kutosheleza havikuwepo, na vilivyokuwepo vingi vilikuwa katika hali mbaya, nyumba za walimu, vyoo vya wanafunzi vilikuwa na upungufu mkubwa, vifaa vya kufundishia na vitabu vilikuwa havipo, n.k.  Ili kukabiliana na hali hii maamuzi muhimu ilibidi yachukuliwe na Serikali; kwa mfano:

 

·        Operation ya utengenezaji madawati nchi nzima;

·        Ujenzi wa majengo muhimu ya shule;

·        Ajira ya walimu wenye sifa;

·        Kuwafunza walimu waliokuwa kazini upya (upgrading courses);

·        Kuwaandikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule;

·        Kuondoa ada na michango kwa shule za msingi ili kusiwe na kisingizio cha watoto kutokwenda shule;

·        Kuanzisha mradi wa maendeleo wa shule za msingi (MMEM);

·        Kuendelea kuongeza bajeti katika sekta.

 

        Mheshimiwa Spika, juhudi hizi zimezaa matunda mengi na mazuri.  Hadi leo zaidi ya vyumba vya madarasa vya kisasa 40,000 vimekwishajengwa, nyumba za walimu zaidi ya 17,000 zimejengwa, madawati zaidi ya 880,000 yametengenezwa, idadi kubwa ya walimu wameajiriwa na vitabu na zana zingine za kufundishia kupelekwa shuleni.  Matokeo ya juhudi hizi ni kuwa hivi leo pamoja na alama za kufaulu mtihani wa darasa la saba kupandishwa, sasa tuna tatizo la watoto waliofaulu kubaki nyumbani tofauti na huko nyuma ambapo shule za sekondari zilikuwa zinakosa wnafunzi waliofaulu na hivyo kuchukua hata walio na alama za chini.

 

        (ii)  Elimu zingine

        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa hatua zingine zinazofuata za elimu hali ni hiyo hiyo.  Kumekuwepo na mafanikio makubwa sana.  Idadi ya shule za sekondari imeongezeka hasa zinazojengwa na wananchi na kukabidhiwa serikalini na zinazoendeshwa na taasisi, madhehebu au watu binafsi.  Jumla ya sekondari zaidi ya 450 zimejengwa katika kipindi hicho.  Aidha, elimu ya wasichana imetiwa mkazo katika ngazi zote.  Kwa upande wa mafunzo ya ufundi, vyuo vinavyotoa elimu hiyo vimeongezeka.  Zaidi ya vijana 20,000 wamefaidika na mafunzo hayo kati ya 1995 – 2000.  Kwa upande wa vyuo vikuu, kuna maendeleo makubwa na vyuo vikuu sasa viko zaidi ya kumi na vingine vinaendelea kuandikishwa.

 

        AFYA:

        Mheshimiwa Spika, utoaji wa huduma za afya ni muhimu ili kuwa na taifa lenye watu wenye afya.  Tangu mwaka 1995 juhudi kubwa zimefanyika kuboresha huduma hiyo.  Tutakumbuka kuwa hali ya huduma za matibabu haikuwa nzuri na ilikuwa ni vigumu hata kupata madawa ya kawaida katika hospitali za umma.  Vifaa vingine vya upasuaji havikuwepo na mara nyingi ilibidi mgonjwa au ndugu zake wavitafute.  Hali hiyo hivi sasa haipo.  Leo madawa muhimu yanapatikana katika hospitali zote mpaka zahanati za vijijini.  Wazee, wakina mama wajawazito kwa huduma za uzazi na watoto wadogo wanatibiwa bure.  Aidha, majengo ya kutolea huduma hizi za afya na vifaa muhimu vimeboreshwa.  Zahanati zaidi ya 1180 ama zimejengwa au kukarabatiwa, vituo vya afya 183 vimejengwa na hospitali kadhaa kujengwa ama kukarabatiwa.  Hali ni hivyo hivyo kwa nyumba za madaktari, waganga na watumishi wengine wa afya.  Uboreshaji wa huduma umeendelea kwa kununulia hospitali na vituo vya afya vifaa muhimu.  Kwa upande wa hospitali za wilaya na mikoa karibu zote sasa zina vifaa vya kisasa vya X-ray, Ultrasound machines, darubini za kisasa, vifaa vingine muhimu vya maabara, n.k.  Aidha, huduma muhimu za chanjo kwa watoto zimeendelea kutolewa kwa mafanikio makubwa, na vivyo hivyo kwa huduma zingine za kinga na tiba.  Aidha, matatizo ya milipuko ya magonjwa yameshughulikiwa mara yalipojitoleza.

 

        MAJI:

        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maji juhudi kubwa zimefanyika kuboresha utoaji wa huduma hiyo muhimu.  Visima vifupi na virefu zaidi ya 8,600 vimechimbwa, visima vingi vya zamani vimekarabatiwa, mifuko ya maji vijijini zaidi ya 2,200 imeanzishwa na bodi za maji safi na majitaka kuanzishwa katika karibu miji yote nchini.  Haya yote yameboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji kwa wananchi.

 

        BARABARA:

        Mheshimiwa Spika, sekta ya barabara ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi na upatikanaji wa huduma kwa wananchi.  Ili kuleta ufanisi katika eneo hili muhimu Serikali ilianzisha wakala wa barabara ili kusimamia ujenzi na ukarabati wa barabara kuu na kutumia halmashauri za wilaya, miji, na jiji kusimamia ujenzi wa barabara zilizoko chini ya milki yao kwa kupewa asilimia 30 ya fedha zinazokusanywa na mfuko wa barabara.  Barabara kuu ambazo zimejengwa au zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa kiwango cha lami ni kama, Ubungo-Mlandizi, Chalinze-Melela, Kawawa Road Dar-es-Salaam, Makuyuni-Ngorongoro Gate, Mutukula-Muhutwe-Kagoma, barabara za Mwanza mjini hadi Airport, Nyanguge-Mwanza, Bagamoyo-Wazo Hill, Mwanza-Mto Magogo, Songwe-Tunduma, Makutano-Butiama-Kiabakari, Tunduma-Sumbawanga, Nzega-Shellui, Ndundu Somanga, Morogoro-Dodoma, Dodoma-Manyoni,     Dar-es-Salaam – Kibiti, daraja la Mto Rufiji, barabara ya Kitonga escarpment, na nyingine nyingi fupifupi.  Aidha, barabara nyingi zimetengenezwa kwa viwango vya changarawe na udongo hasa kwa kutumia fedha zinazotolewa kwa Halmashauri za Serikali za Mitaa.

 

        Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kuwa kabla ya mwaka 1995 barabara katika manispaa zetu ikiwa ni pamoja na jiji la Dar-es-Salaam zilikuwa hazipitiki kabisa.  Mradi wa Urban Sector Rehabilitation Project ulikarabati barabara na mifumo ya maji safi na maji taka katika manispaa za Tanga, Moshi, Arusha, Morogoro, Iringa, Mbeya, Mwanza na Tabora.   Jiji la Dar-es-Salaam nalo lilishughulikiwa chini ya utaratibu tofauti na barabara hizo zote zimeboreshwa.  Hali ya manispaa zetu sasa zinapendeza.

 

 

 

        MASLAHI YA WATUMISHI:

        Mheshimiwa Spika, mwaka 1995 mshahara wa kima cha chini serikalini ulikuwa shilingi 17,500/= kwa mwezi.  Leo kima hicho kimepanda hadi shilingi 55,000/= kwa mwezi.  Bado kima hiki hakitoshelezi mahitaji ya mtumishi na familia yake, lakini kuna unafuu mkubwa na utumishi wa umma sasa una heshima ndani ya jamii.  Fedha hizi zimeleta unafuu hasa kwa vile mfumko wa bei (inflation) umeteremka sana.  Maslahi haya yataendelea kuboreshwa kadri uchumi wetu unavyokua.

 

        UBINAFSISHAJI, UWEKEZAJI NA AJIRA:

        Mheshimiwa Spika, sera ya ubinafsishaji na kuvutia wawekezaji ni sera ya msingi katika marekebisho ya uchumi.  Sera hii pia ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 1995 na ya mwaka 2000.  Katika sera hiyo na maelekezo ya ilani ya CCM, ubinafsishaji utaendelea kwa mashirika ya umma yaliyobaki ili yaweze kuchangia katika uchumi kwa ufanisi zaidi.  Hivi sasa idadi kubwa ya mashirika na makampuni ya umma yamebinafsishwa na zoezi hilo linaendelea. Kwa yale yaliyo binafsishwa, mengi yemeonyesha mabadiliko makubwa ya heri katika uzalishaji, na yapo yanayoendelea kutafuta mtaji wa kuwekeza.

 

        Mheshimiwa Spika, katika siku za karibuni kumekuwa na baadhi ya watu na hasa baadhi ya magazeti ambayo yamekuwa yakiandika kuwa ubinafsishaji umeleta umasikini zaidi hasa kwa kuondoa ajira kwa Watanzania.  Hii siyo kweli.  Kabla ya utekelezaji wa sera ya ubinafsishaji tujiulize mashirika yetu yalikuwa katika hali gani!  Ninatoa mifano michache tu.  Makampuni na mashirika yetu yaliyokuwa na ajira kubwa ni pamoja na viwanda vya nguo na mashamba makubwa.  Kwa upande wa viwanda, kiwanda cha Mwanza Textiles, Kilimanjaro Textiles, Musoma Textiles, Sungura Textiles, Mbeya Textiles, Morogoro Polytex na vinginevyo vilikwisha funga uzalishaji.  Hivi na hapo tulikuwa tunahesabu kulikuwa na ajira?  Nina hakika kama vyote hivi vingebinafsishwa mapema ajira nzuri, japo inaweza isiwe kubwa kama huko nyuma ingepatikana.

 

        Kwa upande wa mashamba, mashamba ya miwa ya Kilombero, Mtibwa na TPC (Arusha chini) yalikuwa yanazalisha kwa shida sana na mengine yalikuwa hayajawalipa wafanyakazi wao kwa zaidi ya miezi sita.  Mengine yaliwalipa wafanyakazi kwa kutumia sukari badala ya fedha.  Shamba la Kagera lilikwisha funga shughuli zake.  Leo viwanda hivi vinazalisha kwa zaidi ya mara mbili ya viwango vyake vya kabla ya ubinafsishaji na kutoa ajira na huduma ya bidhaa za uhakika kwa Watanzania.  Mashamba mengine ya umma kama mashamba ya Ngano – Hanang, mashamba ya Mahindi na Kahawa Mbozi, mashamba ya mpunga Mbarali, Ruvu, Dakawa na mengineyo ama hayazalishi kabisa au yanazalisha kidogo sana kwa kukodisha ardhi zao.  Watumishi waliokuwepo wanaishi kwa utaratibu wanaoujua wenyewe.  Hali hii wala haitofautiani sana ukienda katika sekta ya mahoteli.  Hoteli kama Kilimanjaro, Bahari Beach, Kunduchi Beach, Dodoma Hotel, Tabora Hotel na Moshi Hotel zilikwisha funga shughuli zao kabla ya ubinafsishaji.  Hali ni hivyo hivyo kwa mashirika kama Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), mashamba ya ng’ombe wa maziwa ya DAFCO, mashamba ya ng’ombe wa nyama, mashamba ya mkonge, mashamba ya chai na viwanda vyao.

 

        Mheshimiwa Spika, ningeweza kusema hivi kwa sekta zote na hali isingelikuwa tofauti sana.  Nakubali kuna mashirika yaliyokuwa yanaonekana yanafanya vizuri machoni pa watu.  Mashirika hayo yalipobinafsishwa, baadhi ya wafanyakazi walipunguzwa, na baadhi ya watu walilalamika.  Tukumbuke baadhi ya mashirika na makampuni hayo yalionekana hivyo kwa sababu yalikuwa yanafanya kazi katika mazingira ya ukiritimba.  Katika mazingira ya sasa ya ushindani mkali nina hakika hali ingelikuwa tofauti.  Katika hali ya ushindani mkali, wafanyakazi watakaoajiriwa ni wale tu wanaohitajika.

 

        Mheshimiwa Spika, siyo kweli kuwa ubinafsishaji umeua ajira.  Sehemu kubwa ya ajira yetu ilikwishajifunga.  Ubinafsishaji katika baadhi ya mashirika yaliyokuwa yanafanya kazi ni kweli imeua ajira isiyohitajika na umeboresha ajira inayohitajika katika uzalishaji.  Haya ni mambo mema kwa uchumi wetu na kwa watu wetu.  Tukitaka kupata ajira nzuri ya uhakika ni lazima kwanza, makampuni ya kutuajiri yawepo na pili, kampuni hizo zifanye kazi vizuri.  Ninaamini kabisa katika hili sera ya CCM na ilani ya CCM ni sahihi na utekelezaji wa Serikali ni makini.

 

        Mheshimiwa Spika, wapo wanaosema ubinafsishaji haufanywi kwa uwazi.  Tumeunda Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa Sheria ya Bunge na Tume inafanya kazi zake kwa uwazi kwa kutangaza katika magazeti yote mashirika yanayouzwa.  Barua za maombi hufunguliwa hadharani na baada ya hapo makamishna wa Tume hushughulikia ubinafsishaji na kuwasilisha mapendekezo yao kwa wizara husika ambayo huleta mapendekezo ya wizara serikalini kwa uamuzi.  Hivi hapo siri ipo wapi?  Napenda kuuthibitishia umma wa Watanzania kuwa hakuna siri yoyote katika ubinafsishaji wa mashirika na makampuni ya umma.

 

Kupambana na Kero Mbalimbali:

 

        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupambana na kero mbalimbali za wananchi zikiwemo za huduma za jamii kama nilivyokwishaelezea, kero za rushwa, kero za kutokuwa na chakula, ukosefu wa ajira, ukosefu wa mitaji, usalama wa raia, madhara yanayosababishwa na wakimbizi, n.k.  Kwa upande wa uboreshaji wa utawala na kupambana na tatizo la rushwa, juhudi kubwa pia zimechukuliwa.  Taasisi ya kupambana na rushwa imeimarishwa, hatua za kisheria na kiutawala zimeendelea kuchukuliwa dhidi ya wanaopatikana na rushwa, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekwisha undwa na utawala unaendelea kuimarishwa katika ngazi mbalimbali hasa kwa kuendelea kuimarisha maboresho katika mfumo wa Serikali za Mitaa.  Kwa upande wa kilimo, juhudi kubwa zimefanyika hasa kwa mazao ya chakula.  Kwa miaka mitatu mfululizo wakati hali ya hewa ilipokwa nzuri, nchi yetu siyo tu imejitegemea kwa chakula bali iliweza kuwasaidia chakula majirani zetu wa kusini waliokuwa na shida ya chakula.  Kwa muda sasa tumepata tatizo la bei kushuka sana katika masoko ya dunia kwa mazao yetu makuu ya biashara.  Hili ni tatizo nje ya uwezo wetu.  Hata hivyo, juhudi zinafanywa kupambana na tatizo hili kwa kuzalisha zaidi, kuongeza ubora na kusindika mazao kuongeza thamani kwa mazao hayo.

 

        Mheshimiwa Spika, baada maelezo haya mafupi kwa sekta hizi chache, sijui kama bado watakuwepo wanaosema Serikali ya Rais Mkapa haijafanya kitu.  Hata jana kuna makala katika gazeti moja yaliyosema “Tutarajie nini uchaguzi wa 2005?  Wananchi wanazidi kuwa fukara kila siku.”  Makala kama haya siyo ya kwanza wala hayako tu katika gazeti hili.  Lakini mimi ninataka kusema hivi sasa:

·        Watanzania hivi sasa wanakula vizuri zaidi kwa sababu kwa sehemu kubwa tunajitosheleza wenyewe kwa chakula.

 

·        Watoto wenye umri wa kwenda shule kwa kiwango kikubwa, zaidi ya asilimia 85 wanakwenda shule bila gharama ya mzazi moja kwa moja, na ifikapo mwaka 2005 watoto wote watakuwa wanasoma elimu ya msingi.

 

·        Huduma za afya ni nzuri zaidi na madawa yanapatikana hadi zahanati za vijijini.

 

·        Makundi yasiyo na uwezo yanahudumiwa matibabu bila kulipia.

 

·        Hali ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini ni nafuu sana.

 

·        Hali ya barabara zetu za vijijini na barabara kuu na hali ya mawasiliano mengine ni bora zaidi.

 

·        Elimu kwa ujumla imeboreka kuanzia ngazi za chini hadi chuo kikuu.

 

·        Mapato ya Taifa (GDP) yameongezeka na kiwango cha ongezeko la pato hilo kwa mwaka imekuwa ikiongezeka.

 

·        Mfumko wa bei umeshuka sana.

 

·        Pato la mwananchi limeongezeka kutoka kiasi cha US $ 120 mwaka 1995 hadi US $ 280 – 300 kwa mwaka hivi sasa (2003).

 

        Mheshimiwa Spika, hivi kwa haya yote bado kuna wanaoona Mtanzania sasa ana hali ngumu kuliko huko nyuma?  Labda tafsiri yao ya umasikini ni tofauti na tafsiri rasmi ya kitaalam.  Kama siyo tatizo la tafsiri, basi labda ni tatizo la watani wa jadi ambapo mtani anaweza tu akakataa kuwa marehemu hajafa na akajidai anaongea naye na kuchekeshwa sana na aliyoambiwa na marehemu.  Mimi ninaamini maisha ya Mtanzania yamekuwa bora zaidi na umasikini umepungua sana hasa kwa wale wanaojituma kufanya kazi.  Kwa wale wasiotaka kufanya kazi ni kweli umasikini utawaelemea kwa sababu wao wanaukumbatia!

 

        Mheshimiwa Spika, sikatai kuwa bado kazi ni kubwa mbele yetu na wala haitakuwa rahisi hata kama tungekuwa na pato la Mtanzania la US $ 2,500 ambayo tumepanga kuifikia mwaka 2025 kama Dira ya Taifa ya maendeleo inavyoelekeza.  Lakini tutaendelea kujitahidi kuboresha kadri tunavyopata uwezo wa kiuchumi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2000 ya CCM.

 

        Mheshimiwa Spika, kabla sijamalizia hotuba yangu naomba nikiri kuwa kuna maeneo mawili ambayo ni tatizo kwa ufanisi wa shughuli za Bunge na Wabunge.  Maeneo hayo ni ufinyu wa ukumbi wa Bunge.  Aidha, ukumbi huu kwa vile haukujengwa kwa ajili ya Bunge, haukidhi sana haja ya Bunge.                Bado tunakumbuka sakata iliyowapata Waheshimiwa Wabunge wakati wa dharura ya tetemeko la ardhi.  Serikali inaliangalia jambo hili kwa lengo la kulitatua.  Eneo la pili ni la Ofisi za Waheshimiwa Wabunge katika majimbo yao.  Hili nalo Serikali imelitolea maagizo mapya na taarifa rasmi zinatarajiwa ofisini kwa Waziri Mkuu mwishoni mwa mwezi huu ili hatua zinazoweza kuchukuliwa zichukuliwe.

 

        Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba nimalizie kwa kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika, Mheshimiwa Juma Jamaldini Akukweti, Mbunge wa Tunduru, Wenyeviti Mheshimiwa Eliachim Simpasa, Mbunge wa Mbozi Magharibi na Mheshimiwa Anne Makinda, Mbunge wa Njombe Kusini kwa uongozi wenu mzuri ambao umeliwezesha Bunge lako Tukufu kukamilisha kazi zote zilizopangwa katika     Mkutano huu.  Nawashukuru pia wafanyakazi wote wa Ofisi ya Bunge chini ya uongozi wa Mheshimiwa Kipenka Msemembo Mussa, Katibu wa Bunge, kwa huduma zao kwa Waheshimiwa Wabunge.

 

        Mheshimiwa Spika, baada ya mkutano uliopita ulizivunja Kamati za Kudumu za Bunge ili kuunda kamati zenye muundo na portfolio mpya za kiwizara.  Ninapenda kukupongeza wewe na wajumbe wako wa Tume ya Bunge na wajumbe wa Kamati ya Uongozi kwa uamuzi huo mzuri.  Hizi kamati sasa kwa vile zinahusiana na wizara, zitakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuzamia na kuweza kuishauri Serikali vizuri zaidi katika maeneo ya portfolio zao.  Ninapenda kuwapongeza sasa wenyeviti wapya waliochaguliwa kuongoza kamati hizo, nao ni:

 

1.                Mheshimiwa Pius Msekwa, Kamati ya Uongozi;

2.                Mheshimiwa Njelu M. Kasaka, Kamati ya Fedha na Uchumi;

3.                Mheshimiwa Athumani Janguo, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala;

4.                Mheshimiwa Dakta Amani W. Kabourou, Kamati ya Hesabu za Serikali;

5.                Mheshimiwa William Shellukindo, Kamati ya Uwekezaji na Biashara;

6.                Mheshimiwa Dr. William Shija, Kamati ya Mambo ya Nchi za Nje;

7.                Mheshimiwa Pius Msekwa, Kamati ya Kanuni za Bunge;

8.                Mheshimiwa Dakta John Malecela, Kamati ya Ulinzi na Usalama;

9.                Mheshimiwa Eliakim Simpasa, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge;

10.          Mheshimiwa Omar S. Kwaang’w, Kamati ya Huduma za Jamii;

11.          Mheshimiwa Sophia Simba, Kamati ya Maendeleo ya Jamii;

12.          Mheshimiwa Anne Makinda, Kamati ya Maliasili na Mazingira;

13.          Mheshimiwa Mgana Msindai, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa;

14.          Mheshimiwa Prof. Henry Mgombelo, Kamati ya Miundombinu;

15.          Mheshimiwa Eliakim Simpasa, Kamati ya Kilimo na Ardhi.

 

Mheshimiwa Spika, napenda niwashukuru sana Wenyeviti hao na Wajumbe wa Kamati zao waliopitia miswada ya sheria ya Serikali kwa ushirikiano wao na hoja mbalimbali walizozitoa katika kuboresha miswada hiyo. Serikali imepokea michango hiyo na pale ilipowezekana imeifanya kuwa sehemu ya marekebisho ya miswada husika.  Vikao vya Kamati vilianzia Dare-es-Salaam na baadhi kumalizikia Dodoma.

 

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanya kazi kubwa na nzuri katika kuhakikisha kwamba maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge ambao umekubaliwa umezingatiwa katika hatua za kupitisha miswada ndani ya Bunge lako Tukufu.  Naomba nimshukuru kwa dhati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Andrew Chenge (MB) na watalaam wa Ofisi yake kwa kazi yao nzuri.  Napenda pia kuwashukuru wafanyakazi wa Serikali na Mashirika ya Umma ambao wameiwezesha Serikali kujibu hoja mbalimbali na kutoa maelezo ya ziada ndani ya Bunge lako Tukufu.

 

Mheshimiwa Spika, napenda kwa niaba yenu na kwa niaba ya Serikali kuvishukuru vyombo vyote vya habari kwa kazi yao nzuri ya kutoa habari na kuwaelimisha wananchi kuhusu hoja zilizokuwa zinatolewa na Waheshimiwa Wabunge katika mkutano huu.

 

Mheshimiwa Spika, naomba katika majimbo yetu tukasaidiane na wananchi katika shughuli zao za maendeleo.  Jambo kubwa ambalo hatuna budi kulizingatia kikamilifu katika kipindi hiki ni kuwahamasisha wananchi kuzitumia vema mvua za masika katika maeneo ambayo mvua hizo zinanyesha kwa kupanda mazao yanayokomaa haraka ili taifa liweze kulikabili tatizo la uhaba wa chakula ikiwa litajitokeza.  Aidha, katika kipindi hiki tulizindua matumizi ya takwimu za sensa hapa Bungeni.  Tafadhali nawaomba Waheshimiwa Wabunge mkasaidie kuhimiza matumizi ya takwimu hizo katika mipango yetu ya maendeleo katika majimbo, kata na hata vijiji vyetu kwa sababu takwimu zipo hadi ngazi ya vijiji.

 

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 10  Juni 2003, siku ya Jumanne, saa 3.00 asubuhi litakapokutana hapa mjini Dodoma.

 

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.