PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT OF THE

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

 

 

 

                                                      

                                  The State House,

Tel: 255-22-2116539/2116913                                                      P.O. Box 9120 ,

Fax. No. 255-22 2113425                                                             DAR ES SALAAM.

 E-mail:  press@ikulu.go.tz                                                          TANZANIA .

              ikulupress@yahoo.com

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Rais Jakaya Kikwete amesema  maendeleo ya sayansi na teknolojia ndiyo mambo yanayozitofautisha nchi zilizoendelea na zinazoendelea. Na kwa sababu hiyo amesema anaunga mkono shule ambazo zinazitilia mkazo  ufundishaji wa masomo ya sayansi.

 

Ameyasema hayo  leo mara baada ya kufungua shule ya sekondari ya  wasichana ya Kandoto  inayofundisha masomo ya sayansi na kauli mbiu yake ni sayansi kwa maendeleo endelevu. Shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha sita inamilikiwa na  Kanisa Katoliki Jimbo la Same.

 

“ Baba Askofu Koda umenifurahisha sana, umenifurahisha kwa mambo mawili, moja ni hili la  upendeleo wa elimu kwa mtoto wa kike, na pili ni hili la kutilia mkazo masomo ya sayansi, yote  haya mawili  mimi nayaunga mkonoakasema Kikwete.

 

Akisisitiza  kuhusu umuhimu ya sayansi na teknolojia katika maendeleo ya nchi, Rais amewaeleza wananchi waliohudhuria ufunguzi wa shule hiyo, kwamba  hakuna maendeleo bila sayansi na teknolojia na kwamba kama Tanzania inataka kuendelea lazima itilie mkazo eneo hilo .

 

Ramli haziwezi kutuletea maendeleosayansi ndiyo itatuletea maendeleo na tofauti  zilizopo kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni maendeleo ya sayansi. Sayansi  ni elimu ya utambuzi  wa kanuni  zinazotawala  maumbile na mazingira na hivyo kutengeneza zana na vifaa ambazo ndiyo teknolojia ya kuleta maendeleoakafafanua.

 

Akizungumza upendeleo wa elimu kwa mtoto wa kike, Rais amesema mtoto wa kike lazima apate fursa ya kupata elimu, kwa kuwa kwa miaka mingi jamii imekuwa haitoi kipaumbele kwa mtoto wa kike.

 

Aidha ameainisha kwamba  katika utoaji wa fursa ya elimu kwa mtoto wa kike, ni vema pia akapata fursa ya kujifunza masomo ya sayansi, kama ambavyo Kanisa Katoliki Jimbo la Same lilivyofanya.

 

Amelipongeza Kanisa  Katoliki nchini kwa kuwa na heshima ya kutoa  mchango mkubwa  sana  wa elimu hapa nchini, na kuwanufaisha Watanzania wengi.

 

Amesema serikali itendelea kuyaunga mkono mashirika  ya dini na taasisi nyingine ambazo zinachangia juhudi za serikali katika kuendeleza sekta ya elimu hapa nchini.

  

Akitoa maelezo mafupi ya Shule hiyo y ya Sekondari ya  Kandoto, Askofu wa Jimbo la Same, Mhashamu Koda amemweleza Rais kwamba kanisa hilo limeamua kutoa kipaumbele cha elimu kwa mtoto wa kike, lakini na kutilia mkazo masomo ya sayansi kwa kuwa kanisa linatambua hakuna maendeleo bila elimu.

 

Askofu huyo amesema Kanisa Katoliki halitaacha kutekeleza wajibu wake wa kujenga na kuendesha shule za sekondari, msingi, ufundi na shule za awali  zitakazotoa elimu yenye ubora wa hali ya juu kabisa.

 

Akasema  “Mhe. Rais, Kanisa Katoliki litaendelea na kazi  yake ya kutilia mkazo elimu, kanisa litaendelea kutilia mkazo ubora wa elimu na ubora wa mazingira ya kusomea. Hata kama wenzetu wote watatilia mkazo ujenzi wa miradi yenye faida kubwa, sisi Kanisa Katoliki tutaendelea kukazania elimu.

 

Shule hiyo ya Sekondari ya Kandoto yenye kidato cha kwanza hadi cha sita ilianza kujengwa miaka  miwili iliyopita na jiwe lake la msingi liliwekwa na Rais Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

 

Shule hiyo ambayo imekamilisha ujenzi wa vyumba vya kisasa vya madarasa 18, ofisi za walimu 12,  na majengo mengine imegharimu shilingi milioni 420 na bado inaendelea  kujengwa.

 

Pamoja na kufungua shule hiyo ya Kandoto Rais  pia alifungua shule nyingine ya kisasa ya awali na msingi anayomilikiwa na masista wa Kanisa Katoliki kutoka Italia na imegharimu shilingi milioni 374.

 

Katika siku yake ya ziara yake ya siku saba mkoani Kilimanjaro, Rais Kikwete pia alifungua shule nyingine ya sekondari ya Alikachenje iliyoko katika kijiji cha Makanya inayomilikiwa na kuendeshwa na  Profesa  Mlacha.

 

Shule hiyo ya Alikachanje itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 na  tayari imeanza na wanafunzi 20 wa kidato cha kwanza na 20 wa sekondari.

 

Rais amempongeza Profesa Mlacha kwa kujenga shule inayoendana na karne ya 21 ikiwa na mazingira mazuri ya kusomea, majengo ya kutosha na mazuri, maktaba zenye vitabu va kutosha na maabara.

 

Rais pia amekagua mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Ndugu. Rais pia amewaeleza wananchi waliojitokeza kwa wingi kusalimiana naye katika vijiji mbalimbali kwamba serikali imeanza kazi ya utekelezaji wa ahadi alizoahidi wakati wa kampeni katika wilaya hiyo ya Same.

 

Baadhi ya ahadi hizo ni ujenzi wa barabara ya lami katika maeneo mbalimbali na tatizo sugu la maji kwa wilaya hiyo na vitongoji vyake. Ametumia fursa hii kuwashukuru wananchi  wa wilaya ya Same kwa kumpigia kura na kuichagua CCM.

 

Mwisho.

 

M. Mwingira

Same, Kilimanjaro.

 

3 Agosti, 2007